Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Makame Kassim Makame (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MAKAME KASSIM MAKAME: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa tukiwa na afya njema. Pia sina budi kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutumbua majipu na kuongeza mapato, kwa hili hongera sana. pia napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kwa kazi nzuri ya kuwasilisha hotuba ya bajeti iliyo nzuri kabisa na yenye muamko kwa Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hii napenda niishauri Serikali kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Ingawa ceiling hairidhishi lakini naomba fedha za mikopo ya wanafunzi zigawiwe angalau 40% zipelekwe kwa wanafunzi walioko Zanzibar ili na wao wafaidike na mkopo huo na waweze kuinua kiwango cha elimu kwa sababu wanafunzi walio wengi ni maskini na wana uwezo mkubwa na kusoma vyuo vikuu lakini wanashindwa kuendelea kusoma kutokana na kikwazo hicho cha ukosefu wa fedha na hatima yake wanabaki mitaani kuzurura ovyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Wizara/Serikali ilizingatie hili ili tuandae wataalamu watakaoweza kuendesha uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuweka mfumo mzuri wa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi hususan shule za kule Zanzibar ambao hivi sasa wanasoma mpaka darasa la sita. Kwa kweli nashauri utaratibu huu urekebishwe au urejeshwe ule ule utaratibu wa zamani kwa sababu mwanafunzi anayemaliza darasa la sita bado ni mdogo mno hatimaye wanakosa elimu ya kutosha na wanafeli na kubaki kuzurura. Nashauri urejeshwe utaratibu wa zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.