Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Bahati Ali Abeid (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. BAHATI ALI ABEID: Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanazozifanya. Mheshimiwa Waziri mna kazi kubwa ya kusimamia Taifa letu kuhakikisha mnajitahidi sana ili mila na desturi za nchi yetu na utamaduni wetu uendelee kubaki. Nasema hivi kwa kuona vijana wetu wanajiajiri kwa kuanzisha sanaa ya muziki huu wa kizazi kipya ambao baadhi yao hasa vijana wa kike huwa wanacheza wakiwa wana nguo ya ndani tu.

Mheshimiwa Spika, hivi Baraza la Sanaa la Taifa linaangalia maudhui ya nyimbo tu kama maneno yaliyotumika siyo au linawangalia kundi lote hata wachezaji? Kwani vijana wa kike baadhi yao wanatutia aibu sana. Mheshimiwa Waziri Wanawake tunadhalilika sana wakati mwingine unashindwa kuangalia TV ukiwa na watoto wako wa kiume kuogopa itatokea hiyo nyimbo yenye vijana waliovaa vibaya, Watanzania sio Wazungu hata kama tunataka muziki ukue siyo hivi. Namwomba Waziri akemee vikali kwani mila na desturi za Watanzania ni hazina kubwa aliyotupa Mwenyezi Mungu, tusiwaachie watu watuharibie.

Mheshimiwa Spika, michezo ni jambo ambalo linalitangaza Taifa letu na Tanzania, kwa kweli tunajitahidi ila viwanja vya michezo Tanzania Bara ni kidogo. Ni muhimu kila vinapopimwa viwanja tukumbuke viwanja vya mpira kwani vipaji vya michezo vinaanzia vijijini Wizara ikishirikiana na Wizara ya Ardhi jambo la kutengwa viwanja vya michezo linawezekana.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. BAHATI ALI ABEID: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na miradi ya umwagiliaji; maeneo mengi ya nchi yetu haijamalizika na miradi mingi haikuwa kwenye kiwango chenye kuonesha kuwa hata ikimaliza haitanufaisha Watanzania na hasa ile miradi iliyosimamiwa na Kanda. Kanda hizi kwa asilimia kubwa, miradi waliyoisimamia haikumalizika, ilikuwa ni tatizo. Hivi ni kweli walikuwa ni wataalam waliosimamia miradi hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai kwa viumbe vyote. Ni vema Serikali tukipanga vipaumbele vyetu, ni lazima maji tuipe bajeti kubwa na siyo kuipunguzia bajeti. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia kuongeza hiyo sh.50/= ili bajeti iongezeke. Hivi zile pesa za msaada wa India zimefikia wapi na hata kule Zanzibar?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. BAHATI ALI ABEID: Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara iondoe kodi na tozo ya mitambo na vifaa vya miradi ya gesi ili miradi hii iweze kuendelea na utekelezaji wake kama ilivyopangwa kwani wakati mwingine miradi hii huwa ina mitambo mizito na mikubwa. Kama TANROADS huwa wanataka sheria iliyowekwa kwa ajili ya tozo hizi ziendelee kama zilivyo. Ni sawa, lakini miradi hii au mashine hizi ni za muda mfupi, siyo za kila siku. Naomba tuondoe tozo hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. BAHATI ALI ABEID: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia ingawa ni kwa dakika tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri, Naibu Waziri pamoja na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa sana wanayoifanya ya kumshauri Mheshimiwa Rais kwa kuleta maendeleo ya nchi yetu, pia napenda sana niwapongeze Marais wangu wawili kwa kazi kubwa sana wanazozifanya kwa kutekeleza Ilani ya CCM kwa viwango kabisa.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mbunge wa muda mrefu, nimeona Ilani mbalimbali zinavyotekelezwa lakini miaka hii ambayo Mheshimiwa Rais wangu John Pombe Magufuli amekamata madaraka kwa kweli haijawahi kutokea, ni miradi mikubwa tunaiona inayotekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini naona miradi mikubwa ya umeme inayoendelea kwa kweli tumefanikiwa kuanza kuzima mitambo inayoendeshwa kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta. Hii ni habari nzuri sana naamini mitambo yote inayozalisha umeme kwa kutumia mafuta itaendelea kuzimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwenye hiyo Nishati. Kwa kweli nimeona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mpango na kitabu hiki kimeandaliwa vizuri na kwa kweli Waheshimiwa Wabunge niseme uwe mtaalam kweli kweli wa kukipinga kitabu hiki, ni kitabu kizuri sana, kimejifafanua, kina miradi mingi mikubwa ya maendeleo. Naamini miradi hii ikipitishiwa pesa kama tutakavyozipitisha hapa naamini miradi hii itatekelezwa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimechangia kwa muda mrefu juu ya umeme wa Zanzibar, Umeme wa Zanzibar kwa kweli ZECO tuliomba sana wapunguziwe bei ya umeme na hatukupata jibu hadi leo, Serikali ilisema inaenda kukaa na itaangalia hilo ingawa nipongeze na nishukuru sana kwa ile VAT iliyoondoshwa ni jambo jema sana, lakini kama miradi mizuri inaendelea kutekelezwa na kwa nini ZECO wamejenga mitambo yao wenyewe na mitambo hii TANESCO wameunganisha wafanyabiashara mbalimbali na hakuna pato lolote wanalowapa ZECO.

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. BAHATI ALI ABEID: Kwa nini haiwi sababu basi ya kuona sasa wawapunguzie…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mattar sijui kama una fursa ya kuchangia, maana kila Mbunge akisimama kuzungumzia ZECO wewe una taarifa, sijui kama umeizingatia ile Kanuni yetu inataka useme nini. Mheshimiwa Mattar.

T A A R I F A

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kumpa taarifa Dada yangu Mheshimiwa Bahati, kuna vitu vikikugusa unatakiwa lazima uwe unatoa taarifa ili viende vizuri sana. Nimpongeze Mheshimiwa Bahati lakini suala la…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mattar taarifa ni kwa ajili ya ufafanuzi wa jambo ambalo analizungumza Mbunge mwingine sasa naona unaanza kwa kumpongeza sasa pongezi tena Mheshimiwa?

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpe taarifa Dada yangu Mheshimiwa Bahati kuhusu suala la umeme, ZECO wanauziwa umeme KV Moja ni shilingi 16,500 lakini ZECO wanauza umeme shilingi 13,500, kwa hiyo ukiangalia tunauziwa umeme ghali lakini ZECO wanakwenda kuuza umeme rahisi na tukiangalia hii ni Tanzania moja kwa hiyo tumuongezee Mheshimiwa Bahati tuweze kupungziwa bei ya umeme ili tuweze kwenda vizuri ili wananchi wetu waweze kupata maslahi mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU SPIKA: Sasa Mheshimiwa Mattar, Mheshimiwa Bahati ndicho alichokuwa anazungumza kwa hiyo wewe umekichukua chake kimekuwa Taarifa sasa yeye anatakiwa azungumze nini sasa? Ndiyo maana nasema taarifa ni kwamba unamsikiliza Mbunge amalize hoja yake Je, wewe unatakiwa kuchangia kwenye hicho, kwa sababu la sivyo unauchukua ule mchango wa Mbunge anayesimama ndiyo maana nilikuambia namna hiyo. Mheshimiwa Bahati na kengele imegonga hivyo ninakupa dakika moja malizia muda wako.

MHE. BAHATI ALI ABEID: Mheshimiwa Naibu Spika, utakuwa umenionea huyu amenichukulia muda wangu. Mheshimiwa Mattar hiyo taarifa unatakiwa uwe na subira unisikilize kidogo ingawa naipokea. Kwa kweli amenionea muda wangu ameuchukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Mpango atakapokuja hapa hebu atupe ufafanuzi juu ya umeme huu wa ZECO, miundombinu yao wenyewe na miundombinu hiyo wameunganishwa na wateja wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la kumalizia ni wafanyabiashara wa Zanzibar, wenzangu wamelisema sikutaka kurejea jambo hili. Zanzibar ni Kisiwa na uchumi wake unaeleweka. Kama wafanyabiashara hawa wananyanyasika naamini uchumi wa Zanzibar utaendelea kushuka. Wazanzibar au Tanzania nzima wanategemea kuvuna pato la biashara yao kipindi cha Mwezi wa Ramadhani, lakini wafanyabiashara hawa wengi wamekosa kuuza nguo zao Mwezi wa Ramadhani, nguo ziko huko Mombasa.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa muda uliokuwa umeongezewa pia umekwisha. Waheshimiwa Wabunge nilikuwa nimemtaja Mheshimiwa Bhagwanji lakini kabla hajasimama wapo wageni ambao hawakutangazwa.

MHE. BAHATI ALI ABEID: Mheshimiwa Naibu Spika, samahani, naunga mkono hoja. (Makofi)