Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Nassor Suleiman Omar (3 total)

MHE. NASSOR SULEIMAN OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Serikali ilitoa kauli kwa wale wote walioathirika na zoezi hili kimakosa; Je Serikali imeshawarejesha?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna wale ambao walioathirika kimakosa na wako karibu na kustaafu; je Serikali ina kauli gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba baada ya zoezi hili yalitokea manung’uniko na vilevile zilitokea rufaa mbalimbali za watumishi ambao walidhani kwamba wameonewa. Serikali ilifanya uchambuzi wa kina, wale ambao walionekana kwamba kulikuwa na makosa katika mchakato huo wamesharejeshwa kazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ameuliza swali lingine kwamba wale ambao walikuwa wanakaribia kustaafu Serikali imewaangalia namna gani? Ukweli ni kwamba kwa makosa ambayo walikuwa wameyafanya walitakiwa wapelekwe Mahakamani, lakini Serikali ilisema tuwasamehe mambo ya kuwapeleka mahakamani kwa makosa ya kughushi na wao wasilete madai mengine.

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kwanza kupongeza majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini napenda tu kuongezea kuhusiana na idadi ya waliokata rufaa na kurudishwa kazini, jumla ni watumishi 1,907. Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.(Makofi)
MHE. NASSOR SULEIMAN OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa wakulima wa zao hilo hapa nchini kwetu wamekuwa wengi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwatafutia soko la uhakika wa bidhaa hizo?
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa kuna ongezeko la uzalishaji wa spices hapa nchini na sisi kama Serikali, kama nilivyoeleza kwenye majibu ya swali la msingi, tunayo mikakati ya kusaidia wakulima wetu wa spices kuongeza uzalishaji; sanjari na hilo kuwasaidia kupata masoko ya uhakika. Azma ya Serikali ni kuhakikisha mazao yote ambayo yanatuingia fedha za kigeni tunawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kuwasaidia masoko ili waweze kusaidia kwenye pato la Taifa na kuingizia Taifa fedha za kigeni.
MHE. NASSOR SULEIMAN OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Utamaduni una maana pana ikiwemo mazishi na mavazi. Je, ni lini Serikali itatangaza rasmi vazi la Taifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuridhika na majibu ambayo yametolewa na Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na swali lake la msingi ambapo ametaka kujua ni lini sasa Serikali itakuja rasmi na mchakato wa kutangaza vazi rasmi la Taifa, mara nyingi tumekuwa tukijibu swali hili ndani ya Bunge na sisi kama Wizara ambao ndiyo tunasimamia masuala mazima ya utamaduni ikiwemo lugha pamoja na vazi la Taifa, tupo kwenye mchakato wa kuhakikisha kwamba tunaleta vazi la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato unaoendelea sasa hivi ndani ya Wizara ni kuhakikisha kwamba tunakusanya mavazi yote kutoka kwenye mikoa kwa sababu tunajua kabisa vazi la Taifa siyo kitu ambacho tunaweza kukipata kutoka kwenye jamii moja. Tunachotaka kukifanya sasa hivi ni kuhakikisha mikoa na wilaya zote na wadau wote wa sanaa pamoja na wabunifu wa mavazi wanashiriki kwenye mchakato huu wa kupata vazi la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi mchakato huo utakapokamilika sisi kama Wizara tutakuja rasmi na vazi la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.