Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Juma Kombo Hamad (9 total)

MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-
Serikali imekuwa ikiendeleza zoezi la bomoa bomoa katika maeneo tofauti hapa nchini. Zoezi hili limekuwa likiwaathiri wananchi kiuchumi na hata kisaikolojia kwa kuwaacha wakiwa hawajui waelekee wapi:-
Je, kwa nini Serikali isiwafidie wananchi hawa ukizingatia kwamba wakati wanajenga, Serikali ilikuwa inawaona, lakini haikuchukua hatua stahiki?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali namba 109 la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Mwingwi, kama ifuatavyo:-
SPIKA: Wingwi. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali namba 109, naomba kutoa maelezo yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, suala la bomoa bomoa katika maeneo tofauti hapa nchini limesababishwa na sababu zifuatazo:-
(1) Ni wananchi kuvamia kwenye maeneo hatarishi na oevu kinyume cha sheria;
(2) Ni kuvamia maeneo au viwanja vya watu wengine au maeneo ya wazi na ya umma bila kufuata utaratibu;
(3) Ni kujenga ndani ya hifadhi ya barabara, misitu, mbuga, mikoko, fukwe, kingo za bahari na mito; na
(4) Ni kujenga majengo kwenye maeneo yaliyopangwa bila kufuata taratibu.
Mheshimiwa Spika, mambo yote manne niliyotaja hapo juu na mengine yanayofanana na hayo yanasimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 na Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, bila kuathiri maana iliyopo katika Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya 2004, Kifungu cha 55 na 57 cha Sheria hii, vimeeleza wazi na kutoa katazo la kutoruhusu mtu yeyote kufanya shughuli zozote za kibinadamu za kudumu ndani ya mita 60 ambazo zinaharibu au kwa asili yake inaweza kuathiri ulinzi wa mazingira ya bahari au kingo za mito, mabwawa au miamba ya asili ya ziwa.
Aidha, Sheria hii pamoja na mambo mengine, imekataza shughuli zozote zinazohusisha kuchepusha au kuzuia mto, ukingo wa mto, ziwa au mwambao wa ziwa, ufukwe au ardhi oevu kutoka mkondo wake wa asili au kukausha mto au ziwa. Vile vile imeeleza wazi kuwa mtu yeyote anayekiuka masharti hayo anakuwa ametenda kosa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na sheria tajwa hapo juu, Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007 inaeleza na kufafanua kwa upana namna bora ya kusimamia ardhi yote ya Mijini kuwa, ―Sheria itaweka utaratibu wa maendelezo endelevu ya ardhi katika maeneo ya Mijini, kulinda na kuboresha huduma pamoja na kutoa vibali vya uendelezaji wa ardhi na kudhibiti matumizi ya ardhi katika masuala yanayohusiana na hayo.‖
Mheshimiwa Spika, wananchi wote watakaovunjiwa nyumba zao kwa sababu ya kutofuata sheria au kuvunja sheria au sababu nilizozitaja awali, hawatalipwa fidia.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-
Ni muda mrefu sasa Kikosi cha Polisi Marine Pemba hakina boti ya doria hali inayopelekea polisi kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
(a) Je, Serikali inatambua hilo?
(b) Kama inalitambua, je, ni lini Serikali itakipatia Kikosi cha Polisi Marine Pemba boti za doria ili kuwawezesha polisi hao kufanya kazi zao kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inalitambua tatizo la Polisi Wanamaji Pemba kukosa boti ya doria. Serikali itawapatia Polisi Wanamaji Pemba boti pale uwezo wa kibajeti utakapoongezeka kwani boti zilizopo haziwezi kuhimili mkondo wa maji uliopo Nungwi kuelekea Pemba.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-
Kumekuwa na mgongano mkubwa wa Katiba kati ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar unaosababisha ongezeko la Kero za Muungano na mgongano wa kimamlaka baina ya Serikali mbili:-
Je, ni lini Serikali ya Muungano italeta mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ili kuondoa changamoto zilizomo ndani ya Katiba hizo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kikatiba hakuna mgongano mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar unaosababisha ongezeko kubwa la Kero za Muungano wala mgongano wa kimamlaka baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka utaratibu mahsusi wa kushughulikia tafsiri ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano au utekelezaji wake inayobishaniwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Hadi sasa hakuna upande wowote baina ya Serikali hizi mbili ambao una tafsiri tofauti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano au utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa, hakuna mgongano wa Katiba kati ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar, Serikali haina sababu ya kuleta Mapendekezo ya Mabadiliko ya Katiba ili kuondoa changamoto hiyo ambayo haipo.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-
Je, Zanzibar ina nafasi gani katika Jumuiya za Kimataifa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na mabadiliko yake, masuala ya Mambo ya Nje yapo chini ya mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikihakikisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashiriki kikamilifu kwenye masuala yote ya kimataifa. Masuala hayo ni pamoja na ziara za viongozi na mashirika mbalimbali ya kimataifa zinazofanyika nchini, ziara zinazofanywa na viongozi wa Kitaifa kwenye nchi mbalimbali, mikutano ya mashirika na Taasisi za Kimataifa na Kikanda na mikutano ya pande mbili (bilateral) na Zanzibar kuwa mwenyeji wa mikutano na makongamano ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, aidha, viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamekuwa wakiongoza ujumbe wa nchi kwenye mikutano mbalimbali ya kimataifa. Kwa mfano kwa mwaka 2017/2018, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshiriki katika mikutano ipatayo 11 ya mashirika na taasisi mbalimbali za kimataifa; imeshiriki katika ziara nne za viongozi mbalimbali wa mashirika na taasisi waliofanya ziara hapa nchini; imekuwa mwenyeji wa mikutano na warsha zilizosimamiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na kunufaika na miradi ya miundombinu, afya, kilimo na maji safi inayofadhiliwa na mashirika ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, miradi hiyo ni kama vile ujenzi wa barabara mbalimbali zikiwemo barabara za Mahonda – Mkokotoni Kilomita 31, Fuoni-Kimbeni kilomita 8.6, Pale – Kiongole kilomita 4.6 na Matemwe - Muyuni kilomita 7.6 inayotekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Kadhalika, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Chakula na Kilimo (FAO), linatekeleza miradi mbalimbali ya kilimo na lishe Zanzibar, ukiwemo mradi wa aquaculture.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-
Mfumo wa ulipaji kodi za kusafirisha bidhaa kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu kwamba unakwaza na kuvunja harakati za biashara Zanzibar na hivyo kusababisha uchumi wa Zanzibar kushuka:-
Je, Serikali ipo tayari kuunda Kamati kwa ajili ya kushughulikia mfumo wa ulipaji kodi za mizigo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, chimbuko la malalamiko ya kodi wakati mizigo inaposafirishwa kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara linatokana na kuwepo kwa mifumo tofauti ya kuthamini bidhaa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara. Hali hiyo inasababishwa na viwango tofauti vya ushuru wa forodha vinavyopaswa kulipwa kwa bidhaa ya aina moja kutoka nje ya nchi na kusafirishwa kwenda sehemu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, mfumo wa uthaminishaji bidhaa zote zinazoingia Tanzania Bara unafanyika kwa kutumia mifumo ya TANCIS na Import Export Commodity Database ikiratibiwa na kituo cha Huduma za Forodha kilichopo Dar es Salaam. Hata hivyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitumii mifumo hiyo na hivyo kusababisha kuwepo na tofauti ya kodi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, kutokana na utofauti wa mifumo inayotumika, bidhaa zote za nje zinazoingia Tanzania Bara, kupitia Zanzibar hufanyiwa uhakiki licha ya kuwa zimethaminiwa Zanzibar. Iwapo uthamini wa Tanzania Bara utakuwa sawa na ule uliofanywa Zanzibar, hakuna kodi itakayotozwa Tanzania Bara. Ikiwa kodi iliyolipwa Zanzibar ni kidogo, Mamlaka ya Mapato hukusanya tofauti ya kodi iliyozidi.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kukusanya tofauti ya kodi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara kwa kutumia mifumo ya IECD na TANCIS haina lengo la kuua biashara Zanzibar, hatua hiyo inalenga kuleta usawa wa gharama za kufanya biashara na ushindani hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kujadiliana ili kuona kuwa suala hili linapatiwa ufumbuzi wa kudumu. Aidha, kwa kuwa Serikali zetu mbili hazijashindwa kutatua changamoto hii, ni dhahiri kabisa kuwa hakuna sababu ya kuunda Kamati ya kushughulikia mfumo wa ulipaji kodi kwa mizigo inayotoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara. Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63(2), Bunge lako Tukufu ni Mhimili unaojitegemea na hivyo Serikali haina mamlaka ya kuunda Kamati ndogo ya Bunge kwa ajili ya jambo hili au jambo lolote lile.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-

Vitendo vya utekaji kwa watu wasio na hatia na kuwatesa, kuwahujumu na hata kuwaua vinaendelea kukithiri nchini:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzuia, kulinda na kuhakikisha inakomesha vitendo hivyo haraka sana?

(b) Je, hadi sasa ni watu wangapi ambao wamekamatwa na kuchukuliwa hatua kutokana na uhalifu huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, lenye Sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, jukumu la msingi la Serikali ni kuhakikisha raia wake wanakuwa salama wakati wote na wanaendelea na shughuli za uzalishaji mali na shughuli nyingine za kijamii kwa amani na utulivu pasipokuwa na hofu. Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwenye taarifa za utekaji, utesaji ama mauaji zinapotolewa lengo likiwa ni kuwabaini, kuwachukulia hatua za kisheria watu ambao wanajihusisha na vitendo hivyo.

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutumia taarifa za kiitelijensia imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ya kudhibiti mipango ya wahalifu kwa kufanya operesheni na doria mbalimbali kwa lengo la kuzuia na kukomesha vitendo vya aina hii ambapo hadi sasa mtuhumiwa mmoja amekamatwa kwa makosa ya utekaji nyara.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-

Watu wanaoishi na VVU wanapata shida sana katika kupata lishe bora na matibabu ya uhakika:-

(a) Je, Serikali imejipangaje katika kuwapa mikopo itakayowasaidia kuendesha maisha yao kupitia vikundi mbalimbali?

(b) Je, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kutenga sehemu ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya kundi hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inatoa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kwa wagonjwa wote wanaoishi na VVU ili kuimarisha afya zao na kuwakinga na magonjwa nyemelezi. Aidha, kwa kuwa watu wanaoishi na VVU wanashiriki kama kawaida katika shughuli za ujenzi wa Taifa, Serikali inawanashauri waendelee kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na taasisi za kifedha ikiwemo pamoja na Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na VICOBA.

Mheshimiwa Spika, Serikali inashauri na kusisitiza watu wanaoishi na VVU kuitumia fursa ya mikopo inayotolewa kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi na jumuishi yatakayonufaisha makundi yote kiuchumi wakiwemo watu wanaoishi na VVU.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-

Zanzibar inategemea sana biashara katika kuendeleza uchumi wake na uvuvi wa Bahari Kuu unaweza kukwamua uchumi wa Zanzibar na kwa sababu suala la Bahari Kuu ni jambo la Muungano:-

Je, Serikali haioni ni busara sasa kuondoa suala hilo kwenye orodha ya mambo ya Muungano ili kuisaidia Zanzibar kujiendesha yenyewe na kuweza kusaidia uchumi wa Zanzibar?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya Territorial Sea and Exclusive Economic Zone Act, 1989 iliyoanzisha maeneo ya Bahari yaitwayo Bahari ya Ndani (Inner Sea), Bahari ya Kitaifa (Territorial Sea) na Eneo la Uchumi la Bahari (Exclusive Economic Zone – EEZ). Chimbuko la Sheria hii ni Sheria ya Kimataifa ya Bahari (The United Nations Convention on the Law of the Sea) ya mwaka 1982 inayotoa fursa sawa kwa nchi duniani kugawana rasilimali za bahari zilizopo kwenye maji (water column) na pia kwenye sakafu ya bahari (sea bed).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania iliridhia na kuanza kuitekeleza Sheria hii mwaka 1985. Hivyo, jukumu la kusimamia shughuli za uvuvi kwenye maji yaliyo katika Bahari ya Ndani (inner sea) na Bahari ya Kitaifa (Territorial Sea) ya Tanzania Bara hutekelezwa kupitia Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003, na upande wa Zanzibar Sheria ya Uvuvi (Na. 7) ya mwaka 2010. Ili kutekeleza sheria ya mwaka 1989 hususan katika kusimamia rasilimali za uvuvi zilizopo kwenye eneo la ukanda wa uchumi wa bahari ya Tanzania lenye ukubwa wa kilomita za mraba 223,000, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zilikubaliana kwa pamoja kuunda Taasisi Mamlaka ya Muungano yenye wajibu wa kusimamia uvuvi wa eneo hilo la Uchumi la bahari na pia Bahari Kuu kwa meli zenye kupeperusha bendera ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhitimisha suala hili, ninapenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, uvuvi wa Bahari Kuu unatambulika Kimataifa kupitia Sheria ya Kimataifa ya Bahari ya mwaka 1982 hata katika mikutano mbalimbali ya Kimataifa Tanzania huwakilishwa kama nchi.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-

Ni muda mrefu Serikali ilikuwepo kwenye mchakato wa kupata Vazi la Taifa.

(a) Je, Serikali imefikia hatua gani ya mchakato huo?

(b) Je, ni lini Watanzania wategemee kuwa na Vazi la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa Vazi la Taifa ulianza mwaka 2003/2004 na kufufuliwa tena mwaka 2011 baada ya kuona mitindo iliyopatikana haikukidhi haadhi ya kuwa na Vazi la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2011 Kamati ya Kukamilisha Mchakato wa Kupata Vazi la Taifa iliteuliwa ambapo upatikanaji wa Vazi la Taifa ulipitia jatika hatua kadhaa ambazo Wizara ilishirikisha wabunifu na wanamitindo kwa lengo la kushirikisha wadau wa fani hizo ili kupata Vazi la Taifa litakalotambulisha Taifa letu.

Baada ya kamati kumalizia kazi yake ilikabidhi Wizarani taarifa na mapendekezo kuwa Vazi la Taifa litokane na aina ya kitambaa na siyo mshono.Aidha, aina ya vitambaa kwa vazi hilo ilipendekezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Baraza la Mawaziri iliagiza kwamba jamii iachiwe huru kuchagua aina ya vazi ambalo litatokana na mageuzi ndani ya jamii yenyewe na isiwe uamuzi wa Serikali. Wizara ilitoa taarifa kwa maamuzi yaliyofikiwa na Serikali kwenye vyombo vya habari na tovuti ya Wizara ili wananchi wajadili na waamue wenyewe kuhusu Vazi la Taifa ambalo litapendekezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya changamoto zilizojitokezakwa kipindi hicho ni uhamasishaji hafifu wa uvaaji wa Vazi la Taifa. Aidha walitarajia kupokea vazi na siyo kuoneshwa kitambaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya agizo la Waziri Mkuu la kuandaa Tamasha la kupata sura ya Vazi la Taifa ifikapo 30 Desemba, 2018, mchakato ulianza upya ambapo utaratibu wa ukusanyaji wa michoro, picha ya vazi au mavazi halisi kutoka kwa wabunifu kwa kila mkoa uliandaliwa kwa kuwaandikia Makatibu Tawala wa Mikoa yote, kuwapa taarifa kuhusu mchakato wa kupata Vazi la Taifa kwa kushirikiana na Maafisa Utamaduni kuhamasisha wabunifu ili waweze kuandaa, kuwasilisha michoro, picha au mavazi waliyobuni yanayoendana na asili ya mkoa husika. Aidha, Wizara imeweka mkakati maalumu kwa kushirikiana na Maafisa Utamaduni ili kuweza kupata Vazi la Taifa.