Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mussa Bakari Mbarouk (13 total)

MHE. SAUMU H. SAKALA (K.n.y. MHE. MUSSA B. MBAROUK) aliuliza:-
Awamu zote za Serikali zilizopita Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne ziliahidi kujenga barabara ya Tanga – Pangani – Saadani hadi Bagamoyo kwa kiwango cha lami:-
(a) Je, ni lini Serikali itaamua kujenga barabara ya Tanga – Pangani kwa kiwango cha lami?
(b) Kupitia Bunge la Kumi na Moja, je, Serikali inaahidi nini kuhusu ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini, lenge kipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Tanga – Pangani – Saadani hadi Bagamoyo, yenye urefu wa kilometa 178 ni sehemu ya mradi wa Kikanda wa barabara ya Malindi – Mombasa – Lungalunga – Tanga hadi Bagamoyo. Mradi huu wa Kikanda unaratibiwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani – Bagamoyo kwa kiwango cha lami ilianza mwezi Januari, 2011 na kukamilika mwezi Novemba, 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kutoka kwa washirika wa maendeleo. Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), tayari imeonesha nia ya kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa barabara hii. Taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa barabara hii ya Tanga – Pangani – Saadani hadi Bagamoyo zitaanza baada ya kupatikana kwa fedha za ujenzi. Aidha, zoezi la uhakiki wa taarifa za uthamini wa mali za wananchi watakaoathirika na ujenzi wa barabara hii linaendela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imedhamiria kuijenga barabara hii ya Tanga – Pangani – Saadani hadi Bagamoyo kwa kiwango cha lami.
MHE. MBONI M. MHITA (K.n.y. MHE. MUSSA B. MBAROUK) aliuliza:-
Daraja la Mto Wami ni miongoni mwa daraja la muda mrefu na jembamba (single way). Aidha, daraja hilo limesababisha ajali za mara kwa mara na kusababisha wasafiri kupoteza maisha na mali zao:-
Je, ni lini Serikali itajenga daraja jipya katika Mto Wami hasa ikizingatiwa kuwa daraja hilo ni kiunganishi kati ya Dar es Salaam na Mikoa ya Kanda ya Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbaruok, Mbunge wa Tanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbarouk kuwa daraja la Mto Wami ni miongoni mwa madaraja ya muda mrefu ambayo yamejengwa kwa muundo ambao hupitisha magari kwa mstari mmoja yaani (single lane).
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kujenga upya daraja hili ili kukidhi ongezeko la magari yanayopita katika eneo hilo. Kwa hivi sasa kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina zinaendelea ambapo tayari ripoti ya awali ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina imeshakamilishwa na inafanyiwa mapitio kabla ya kukamilisha ripoti ya mwisho. Baada ya kukamilisha kazi ya usanifu wa kina wa daraja la Wami, Serikali itatafuta fedha za ujenzi wa daraja hilo.
MHE. KHATIB SAID HAJI (K.n.y. MHE. MUSSA BAKARI MBAROUK) aliuliza:-
Kwa muda mrefu hakuna usafiri wa uhakika kati ya Pemba na Tanga hali inayopelekea vyombo vya usafiri vya kienyeji kupata ajali mara kwa mara na kupoteza maisha ya watu na mali zao:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kununua meli ya kisasa na ya uhakika ili kuokoa wasafiri wa Tanga – Pemba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa kuanzia tarehe 29 Januari, 2017 Kampuni ya Azam Marine imeanza kutoa huduma ya usafiri wa abiria na mizigo kati ya Pemba na Tanga kwa kutumia meli ya Sealink 2 yenye uwezo wa kubeba abiria 1,650 na mizigo tani 717.
Mheshimiwa Spika, tarehe 31Januari 2017 Meli ya Sealink 2 ilizindua safari ya kutoka Tanga saa 3.00 asubuhi kwenda Mkoani Pemba hadi Unguja. Sealink 2 itafanya safari zake mara moja kwa wiki baina ya Pemba na Tanga hadi pale idadi ya abiria na mizigo itakapolazimu kuongeza safari nyingine.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bunge lako Tukufu inapenda kutumia fursa hii kuipongeza kampuni ya Azam Marine kwa kuitikia wito wa kuanzisha huduma ya usafiri majini baina ya Tanga, unguja na Pemba na kuendelea kutoa wito kwa wawekezaji wengine kuleta vyombo vya usafiri majini vya kisasa ili kuongeza huduma ya usafiri katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto hiyo.
Mheshimiwa Spika, pia tunaomba wananchi wanaosafiri kati ya Pemba na Tanga kutumia huduma za meli salama na kuachana na vyombo visivyo salama vinavyohatarisha maisha na mali zao. Aidha, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Tanga na Pemba kuendelea kuhamasisha wananchi kuachana na vyombo visivyo salama ili kulinda maisha na mali zao.
MHE. MUSSA B. MBAROUK aliuliza:-
Bandari ya Tanga siku hadi siku inafanya kazi chini ya kiwango:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza kina, kuipanua na kuifanya bandari ya kisasa ili kuvutia wafanyabiashara kushusha mizigo yao na wasikimbilie Mombasa Kenya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuvutia wafanyabiashara kushusha mizigo yao na kutokukimbilia bandari ya nchi jirani, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ina mpango wa muda mfupi na wa kati wa kuboresha bandari ya Tanga kwa kutekeleza mradi wa kuimarisha gati namba mbili (2).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kuboresha Bandari ya Tanga ulianza Februari, 2016 na unatarajiwa kukamilika Juni, 2017. Mradi huu unatekelezwa na Kampuni ya Ukandarasi ya COMARCO kutoka Kenya. Maboresho ya bandari yanayofanyika katika mradi huu ni pamoja na kuongeza kina cha gati kwa kuchimba (dredging) kiasi cha mita 1 na kufanya kina cha gati kufikia mita 4.5; kuimarisha gati na kuweka mfumo wa kuzuia kutu katika nguzo (cathodic protection).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ukikamilika utasaidia kuongeza uwezo wa bandari kuhudumia meli zenye wastani wa ukubwa wa tani 1,200 kuingia bandarini. Aidha, Serikali kupitia TPA ina mpango wa muda mrefu wa kujenga bandari katika eneo la Mwambani ambayo ina kina kirefu na uwezo wa kuhudumia meli kubwa. TPA tayari inamiliki ardhi yenye ukubwa wa hekta 92 katika eneo la Mwambani.
MHE. MUSSA B. MBAROUK aliuliza:-
Tanga kuna uwekezaji wa bomba la mafuta toka Hoima - Chongoleani, viwanda mbalimbali vya saruji, vivutio vya utalii vya Amboni Caves, Magofu ya Tongoni na Saadani National Park:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kiwanja cha ndege kikubwa na cha kisasa katika Jiji la Tanga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini ambaye anapendwa sana na wapiga kura wake kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwaja cha ndege cha Tanga ni miongoni mwa viwanja 11 nchini vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kugharamiwa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa Transport Sector Support Project. Viwanja vingine vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ni Lake Manyara, Musoma, Iringa, Songea, Kilwa Masoko, Lindi, Moshi, Njombe, Simiyu na Singida.
Mheshimiwa Naibu Spika, usanifu huu ulikamilika mwezi Juni, 2017 na ulihusisha usanifu wa miundombinu ya viwanja hivi kwa ajili ya upanuzi na ukarabati ili kukidhi mahitaji ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza majadiliano na Benki ya Dunia ili kupata mkopo wa kugharamia ukarabati na upanuzi wa baadhi ya viwanja hivi kwa kuzingatia mapendekezo ya report ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao ulizingaia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukuaji wa shughuli za uchumi, utalii na mahitaji ya usafiri wa anga. Katika upembuzi yakinifu na usanifu wa kina huo, kiwanja cha ndege cha Tanga ni miongoni mwa viwanja vilivyopewa kipaumbele kwa mahitaji ya ukarabati hivyo katika majadiliano ya awali, Benki ya Dunia imeonesha nia ya kugharamia ukaratabi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unaopendekezwa utahusisha mradi wa barabara ya kuruka na kutua ndege pamoja na barabara ya kiungio kwa kiwango cha lami. Ukarabati wa maeneo ya maegesho ya ndege, ujenzi wa jengo kubwa la kisasa la abiria pamoja na miundombinu yake, usimikaji wa taa pamoja na mitambo ya kuongozea ndege. Baada ya ukarabati unaopendekezwa kiwanja kitakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege aina ya ATR 72 yenye uwezo wa kubeba abiria 70 au ndege za kufanana na hiyo na kitaweza kutumika kwa saa 24.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa majadiliano kati ya Serikali na Benki ya Dunia yanaendelea yakiwemo mapitio ya awali ya report za miradi inayopendekezwa pamoja na maandalizi ya taarifa mbalimbali zinazohitajika kabla ya mkataba wa mkopo kusainiwa na baadae kutangazwa zabuni.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y. MHE. MUSSA B. MBAROUK) aliuliza:-
Kwa kuwa usafiri wa majini, mizigo na watu havifanyi usajili na vipimo.
Je, kwa nini Serikali isianzishe utaratibu wa kupima mizigo na usajili wa abiria katika vyombo vyote kama wanavyofanya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCCAA) ili kuepusha ajali za mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuna utaratibu wa aina mbili unaotumika kupima mizigo na usajili wa abiria katika vyombo vinaavyotumika majini. Kwanza usajili na uorodheshaji wa mizigo wakati wa ukataji wa tiketi za abiria na upakiaji wa mizigo kama inavyoainishwa katika passenger or Cargo Manifests and Crew List. Pili, uhakiki wa upakiaji kabla ya chombo kuruhusiwa kuanza safari, kwa kuhesabu abiria wakati wa kuingia kwenye chombo na kuhakiki kuwa alama ya Loading Mark haivukwi. Aidha, matumizi ya Port Clearance Forms huwezesha kudhibiti kiwango cha upakiaji abiria na mizigo kwenye chombo na kuacha taarifa za safari.
Mheshimiwa Spika, Serikali hufanya udhibiti huo, kupitia mamlaka ya udhibiti usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA) na mamlaka ya usimamizi wa bandari TPA ambazo husimamia utaratibu wa upakiaji bandarini na kudhibiti usalama wa vyombo vya usafiri majini. Taratibu hizi hufanywa au hatakiwa kufanywa kwenye bandari na mialo yote iliyosajiliwa.
MHE. MUSSA B. MBAROUK aliuliza:-
Tafiti zinaonesha Watoto njiti Tanzania wanapoteza maisha wakiwa chini ya miaka mitano:-
(i) Je, Serikali inachukua hatua gani mahsusi kupambana na tatizo hili na kuhakikisha Watoto njiti walio hai wanakua bila matatizo?
(ii) Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu kwa Watanzania juu ya sababu zinazosababisha watoto kuzaliwa njiti?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa nchini Tanzania asilimia 17 ya watoto huzaliwa kabla ya muda wa mimba kukomaa. Watoto hawa huwa katika hatari zaidi ya kupoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kushindwa kupumua kutokana na kutokomaa kwa mapafu, kupoteza joto la mwili kwa haraka, kupata uambukizo wa bakteria, kushindwa kunyonya na kupata manjano, hivyo huhitaji huduma maalum.
(a) Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara imefanya na inaendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kuboresha huduma kwa watoto hawa na ili kuepusha vifo hivyo kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwemo:-
(a) Kuwapatia wajawazito dawa ya kusaidia mapafu ya mtoto kukomaa haraka iwapo mama anatarajiwa kujifungua kabla ya wakati.
(b) Kuanzisha huduma ya Mama Kangaroo katika ngazi ya hospitali ili watoto njiti ambao hawana changamoto nyingine za kiafya watunzwe kwa utaratibu wa ngozi kwa ngozi na wazazi wao ili watunze joto mwilini. Kuanzia mwaka 2009 mpaka sasa jumla ya hospitali 63 zinatoa huduma ya Mama Kangaroo nchini.
(c) Kununua na kusambaza vifaa vya kuwahudumia watoto njiti ambao wana matatizo ya kiafya. Vifaa hivyo ni pamoja na mashine za Oksijeni, mashine za kutibu manjano yaani phototherapy machines, mashine za kufuatilia hali ya mtoto akiwa kwenye matibabu, mashine za kuongeza joto na vipima joto vya chumba cha kutibia watoto hawa.
(d) Kuendelea na mafunzo ili kuwajengea uwezo watoa huduma za afya juu ya namna ya kumhudumia mama anayetarajia kujifungua mtoto njiti kama vile mama mwenye ujauzito wa watoto pacha, mama mwenye shinikizo la damu wakati wa mimba na wenye upungufu wa damu.
(b) Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii, ili waweze kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya afya ya uzazi na mtoto, ikiwemo dalili za hatari wakati wa ujauzito, sababu zinazopelekea kuzaliwa kwa watoto njiti na umuhimu wa kuhudhuria kliniki mapema ili jamii iweze kuhamasika na kuchukua hatua stahiki na kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, vilevile Wizara inaendelea kuwahamasisha wajawazito kumeza vidonge vya kuongeza damu, kumeza dawa za kuzuia malaria pamoja na kuwasisitiza wajawazito kupata muda wa kutosha wa kupumzika na kulala kwenye vyandarua vyenye dawa.
MHE. MUSSA B. MBAROUK aliuliza:-
Kumekuwa na sintofahamu kwa baadhi ya wafanyabiashara na TRA kuhusu mashine za EFDs hususani bei za mashine na aina za mashine.
(a) Je, bei halali ya mashine ya EFD kulingana na aina na ubora wake ni shilingi ngapi?
(b) Kwa kuwa mashine za EFDs zinafanya kazi kwa niaba ya TRA, je, kwa nini Serikali isitoe mashine hizo bure kwa wafanyabiashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Spika, kuna aina tano za mashine za EFD kwa ajili ya kutunza kumbukumbu na kutoa risiti za mauzo. Mfanyabiashara anaweza kununua aina mojawapo ya mashine hizo kulingana na mahitaji yake. Aidha, ubora wa mashine zote ni lazima uthibitishwe na Mamlaka ya Mapato Tanzania kabla mashine hizo hazijaingia sokoni na kuanza kutumika. Bei ya kila mashine ni kama ifuatavyo:-
i. Rejista za Kielekroniki za Kodi - mashine hizi hutumiwa na wafanyabiashara wasiotumia mifumo ya kompyuta au mifumo ya kihasibu na bei yake kwa sasa ni shilingi 590,000.
ii. Mashine za kielektroniki zinazoweka alama au saini (Electronic Signature Devices) - mashine hizi hutumiwa na walipakodi wanaotumia mifumo ya kompyuta na mifumo maalum ya kihasibu na bei zake ni kati ya shilingi 1,000,000 na 1,200,000.
iii. Printa za Kielektroniki za Kodi (Electronic Fiscal Printers) - mashine hizi hutumia mfumo maalum wa kompyuta kufanya mauzo na bei zake ni kati ya shilingi 1,500,000 na 1,700,000.
iv. Printa za Pampu za Mafuta ya Petroli na Dizeli - mashine hizi hutumiwa na wafanyabiashara wanaouza mafuta ya petroli na dizeli kwa kutumia pampu na bei zake ni shilingi 6,000,000 ikijumuisha gharama za ufungaji na uunganishaji kwenye pampu za mafuta.
v. Printa za Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni - bei za mashine hizi ni shilingi 2,150,000 ikiwa ni pamoja na programu ya mfumo (software).
b) Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara wanaponunua mashine za EFD hulipa gharama za ununuzi wa mashine hizo na baadaye Serikali hurejesha gharama hizo kama ifuatavyo:-
i. Wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye VAT; kwa mujibu wa jedwali la saba chini ya Kanuni ya 54(2) za Sheria ya Usimamizi wa Kodi za mwaka 2016, mashine zilizonunuliwa kwa mara ya kwanza zinagharamiwa na Serikali kwa kumruhusu mfanyabiashara kujirejeshea fedha zake kwa utaratibu wa input – output tax kwenye return yake ya mauzo ya mwezi husika.
ii. Kwa wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani hurejeshewa gharama za mashine kama ifuatavyo:-
Mosi, wanaoandaa hesabu za mizania; kundi hili linaruhusiwa kujirejeshea gharama za ununuzi wa mashine kwa kuziingiza gharama husika kama gharama za kuendesha biashara kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 11(2) cha Sheria ya Kodi ya Mapato.
Pili, wafanyabiashara wasioandaa hesabu za mizania (presumptive cases) kwa mujibu wa Kanuni ya 54(2) ya Kanuni za Sheria ya Usimamizi wa Kodi za mwaka 2016 kundi hili la wafanyabiashara wanajirejeshea gharama za mashine kwenye kiasi cha kodi walichokadiriwa kwa mwaka husika. Kama hawatakuwa wamejirejeshea kwa asilimia 100 basi kiasi kilichobakia kitasogezwa mwaka unaofuata.
MHE. MUSSA B. MBAROUK aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali isianzishe utaratibu wa kupima mizigo na usajili wa abiria katika vyombo vyote vya majini kama inavyofanyika Airport ili kuepusha ajali za mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inao utaratibu wa kupima mizigo na usajili wa abiria katika vyombo vya usafiri kwa njia ya maji na utaratibu huo hutekelezwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ambapo kwa hivi sasa utekelezaji wake unadhibitiwa na Wakala wa Meli Tanzania (TASAC).
Mheshimiwa Spika, vyombo vyote vya majini husajiliwa na kupewa vyeti vya ubora (Sea Worthiness Certificate) ambayo huonesha uwezo wa chombo husika kubeba mizigo au abiria. Aidha, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imeipa dhamana Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kutoa kibali cha kuondoa chombo bandarini (Clearance Certificate) kutoka bandari moja kwenda nyingine baada ya kujiridhisha kuwa chombo husika kimebeba abiria au shehena kulingana na viwango vya usalama vilivyokusudiwa kwa shughuli ambazo chombo husika kimesajiliwa kufanya.
Mheshimiwa Spika, kwenye kibali cha kuondoa chombo bandarini hujazwa takwimu kama vile; idadi ya wafanyakazi wa chombo (crews), idadi ya abiria (passengers) idadi ya mizigo (cargo) na huambatanishwa na majina ya abiria (passenger manifest) na idadi ya mizigo (cargo manifest) kwa ajili ya ukaguzi, ukamilishaji wa miamala ya kibiashara, ufuatiliaji pindi ajali inapotokea na kumbukumbu za ofisi. Hivyo, vyombo vyote hubeba shehena au kupakia abiria kulingana na uwezo wake na hivyo kuepusha ajali zisizo za lazima.
Mheshimiwa Spika, napenda nitoe wito kwa Watanzania wenzangu hususani wanaoishi katika mwambao wa Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Tanganyika na Ziwa Nyasa kuacha kutumia vyombo vya usafiri visivyosajiliwa na SUMATRA au TASAC, hususan vinavyotoa huduma katika bandari zisizo rasmi (bandari bubu) kwa upande wa Bahari Kuu na mialo kwa upande wa maziwa makuu ili kuepusha ajali za mara kwa mara na hivyo kunusuru maisha ya watu na mali zao.
MHE. SONIA J. MAGOGO (K.n.y. MHE. MUSSA B. MBAROUK) aliuliza:-

Wakazi wa Kata ya Kirare, Tongoni, Mzizima, Chongoleani, Mabokweni na Pongwe Wilayani Tanga Mjini ni wazalisaji wakubwa wa zao la muhogo lakini hawana soko la uhakika:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kutafuta soko la uhakika wa zao la muhogo ndani na nje ya nchi?

(b) Zipo mashine za kuchakata muhogo lakini bei zake ni kubwa na hivyo wakulima hawana uwezo wa kununua; je, Serikali haioni haja ya kuondoa kodi katika mashine hizo?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, imeweka vipaumbele vitatu ambavyo ndivyo tunavyoviwekea msisitizo wa uwekezaji kwenye sekta ya viwanda. Vipaumbele hivyo ni viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ili kuongeza thamani sambamba na kulinda jasho la mkulima; viwanda vya kutengeneza bidhaa za majumbanii kama vyakula, nguo, mafuta ya kula, samani na kadhalika na bidhaa tegemezi kwenye sekta ya ujenzi kama sementi, mabati na kadhalika ili kuharakisha ubora wa maisha na maendeleo; viwanda vinavyoajiri watu wengi kwa ajili ya kuhakikisha ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la muhogo ambalo ni maarufu kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara na maeneo mengi ya nchi hadi Kigoma kwa sasa limepewa kipaumbele maalum duniani. Kutokana na ukweli kwamba muhogo hausindikwi kutengeneza unga wa ugali au uji au mkate au biskuti peke yake bali unga wa muhogo unatumika kwa sasa kwenye uunganishaji wa chuma, mbao, kutengeneza gundi na matumizi mengine mengi sana. Soko la muhogo Ulaya, Marekani na China ni kubwa sana kwa sasa. China peke yake inahitaji tani milioni mbili na nusu za muhogo kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ukweli huo, kasi ya ujenzi wa viwanda vya kusindika muhogo ni kubwa. Mwaka huu peke yake ukiacha viwanda vitano vinavyonunua muhogo wa mkulima kwa sasa kikiwemo kile kilichopo Handeni, viwanda viwili vipya vitakuwa vimefunguliwa kabla ya Juni, 2019 kimoja Lindi na kingine Pwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bei kubwa za mitambo kutoka nje, nawashauri wawekezaji wa ndani watembelee SIDO na TEMDO kwanza maana ni taasisi za ndani ambapo miongoni mwa majukumu yake ni kubuni na kutengeneza mitambo na mashine za kusindika mazao zenye gharama nafuu. Endapo italazimika kuagiza nje ya nchi, italazimu kufuata Sheria ya Fedha iliyopo au kusubiri mapendekezo yaliyopelekwa kwenye Kikosi Kazi cha kutathmini mapendekezo ya marekebisho ya kodi yatakayojadiliwa wakati wa kujadili rasimu itakayoletwa na Serikali Bungeni Juni, 2019.
MHE. MUSSA BAKARI MBAROUK aliuliza:-

Tanzania ina jumla ya Majiji sita likiwemo Jiji la Tanga; katika Majiji hayo kuna maeneo ambayo yako nje ya Jiji ambayo ni Mitaa, Vitongoji na Vijiji (Perry Urban); Kitengo cha Perry Urban kimekabidhiwa jukumu la kusambaza umeme wa REA III katika Majiji:-

Je, ni lini Perry Urban itaanza kusambaza umeme katika Jiji la Tanga?
WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na utekelezaji wa miradi ya umeme iliyopo katika vijiji, vitongoji na maeneo mbalimbali kandokando ya miji na vijiji yaani Perry Urban. Awamu ya kwanza ya utelelezaji wa mradi huu umeanza katika Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa Pwani na kwa upande wa Dar es Salaam katika Wilaya ya Kigamboni. Utekelezaji wa mradi huu utakamilika mwezi Aprili, 2020. Baada ya kukamilika kwa mradi huu, Serikali itaanza kutekeleza mradi huu katika Mikoa yote nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jiji la Tanga Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na kubainisha kuwa miradi wa kupeleka umeme maeneo ambayo yako kandokando ya Jiji la Tanga unahusisha ujenzi wa njia ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 15, ufungaji wa transfoma 15 kati ya hizo transfoma 4 ni za KVA 200, transfoma sita za KVA 100 na 5 za KVA 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi ya Perry Urban katika Jiji la Tanga pia utahusisha ujenzi wa njia ya Msongo wa kilovoti 11 yenye urefu wa kilomita 48.8, ufungaji transfoma 35; na kati ya hizo transfoma nane ni za 200KVA, 20 za 100KVA na saba za KVA 50. Kazi nyingine ni kuvuta laini ndogo ya kV 0.4 yenye urefu wa Kilomita 200. Wateja wa awali watakaonufaika na mradi huu katika Jiji la Tanga ni 5,125 ambao wanatarajiwa kupata umeme katika maeneo hayo. Utekelezaji wa mradi huu utaanza mwezi Julai, 2020 na kukamilika mwezi Machi, 2021. Gharama za mradi huo ni shilingi bilioni 7.5.
MHE. MUSSA B. MBAROUK aliuliza:-

Katika Vijiji vya Kigombe Wilayani Muheza na Kipumbwi Wilayani Pangani kuna bandari bubu zinazotumika kwa uvuvi na kusafirisha abiria na bidhaa:-

Je, ni lini Serikali itarasimisha bandari hizo kwa kujenga gati pamoja na kituo cha forodha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ina taarifa ya uwepo wa bandari bubu yaani bandari zisizo rasmi katika Mwambao wa Pwani pamoja na changamoto za kiusalama, kiulinzi na kiuchumi zinazoletwa na bandari hizo.

Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti matumizi ya bandari hizo, mamlaka zinazohusika zimeelekezwa kushirikiana na kuweka mikakati ya pamoja ya kudhibiti matumizi ya bandari hizo. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kutambua bandari zenye umuhimu kwa wananchi kiuchumi na kijamii ili kuzirasimisha kwa kuziweka chini ya uangalizi wa vijiji vilivyo kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza maelekezo hayo, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilikamilisha zoezi la kukusanya taarifa za bandari Tanzania Bara na kubaini kuwa kuna bandari zisizo rasmi 208 katika Mwambao wa Bahari ya Hindi. Baada ya zoezi hilo, TPA iliainisha bandari ambazo zinafaa kurasimishwa.

Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifa Bunge lako Tukufu kuwa Bandari za Kigombe na Kipumbwi Wilayani Muheza na Pangani ni miongini mwa bandari 24 zenye umuhimu kwa wananchi kiuchumi na kijamii na zimeorodheshwa kwa ajili ya kurasimishwa.

Mheshimiwa Spika, hatua inayoendelea hivi sasa kuhusu bandari hizo ni kuzipanga katika madaraja (classification) ili kubaini zile ambazo zitachukuliwa na TPA moja kwa moja kwa kuziendesha baada ya kuboreshwa na kuendelezwa kwa miundombinu yake ikiwemo kujenga gati pamoja na kuweka kituo cha forodha, zile ambazo zitaendeshwa kwa mkataba na zile ambazo zitawekwa chini uangalizi wa halmashauri kwa maeneo husika. Kazi hii inatarajiwa kukamilika kabla ya kumalizika kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Spika, baada ya urasimishaji huo, usimamizi wa sheria na udhibiti wa maeneo hayo utafuata.
MHE. MUSSA B. MBAROUK aliuliza:

Tarehe 12 Septemba, 2019 katika Mkutano wa Kumi na Sita wa Bunge yamepitishwa Marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma ili kumpa Katibu Mkuu Kiongozi Mamlaka ya mwisho ya uhamisho wa watumishi wa umma.

Je, kwa kumpa Mamlaka ya Mwisho Katibu Mkuu Kiongozi hakutasababisha ukiritimba katika uhamisho wa Watumishi wa Umma?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298, imefanyiwa marekebisho katika Kifungu cha 4(3) kupitia Kifungu cha 69 cha Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 13 ya Mwaka 2019 kwa kumpa Katibu Mkuu Kiongozi Mamlaka ya Mwisho ya Uhamisho wa Watumishi wa Umma kwa kuzingatia Mamlaka yake kama Mkuu wa Utumishi wa Umma kwa mujibu wa Kifungu cha 4(2) cha Sheria hii.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Mamlaka hayo, Kifungu cha 8(2) cha Sheria hiyo kinampa Katibu Mkuu (Utumishi) Mamlaka ya kuwa Msaidizi Mkuu wa Katibu Mkuu Kiongozi. Hivyo, katika kutekeleza majukumu ya Katibu Mkuu Kiongozi, Kifungu cha 8(3)(h) cha Sheria husika kinampa Katibu Mkuu (Utumishi) Mamlaka ya kuhamisha Watumishi wa Umma kutoka Taasisi moja kwenda nyingine Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, Katibu Mkuu (Utumishi) amekasimu Mamlaka yake kwa Katibu Mkuu (TAMISEMI) ili aweze kuhamisha Watumishi wa Umma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Vilevile, Katibu Mkuu (Utumishi) amekasimu Mamlaka yake kwa Makatibu Tawala wa Mikoa ili waweze kuhamisha Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Mikoa yao. Pamoja na kukasimisha Mamlaka yake, Katibu Mkuu (Utumishi) anaweza kuhamisha Watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa yeye mwenyewe pale inapobidi.

Mheshimiwa Spika, Ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa marekebisho yaliyofanyika katika Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298, yamempa Katibu Mkuu Kiongozi Mamlaka ya mwisho ya uhamisho wa Watumishi wa Umma ili kuwezesha uhamisho unaofanywa naye kutopingwa au kutotenguliwa na Mamlaka nyingine. Hata hivyo, Mamlaka hayo yatatumika kwa kuzingatia masilahi mapana katika Utumishi wa Umma au pale ambapo Katibu Mkuu Kiongozi hakuridhika na uhamisho uliofanywa na Mamlaka nyingine zilizopewa au zilizokasimiwa madaraka hayo kama ilivyoelezwa.