Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mussa Bakari Mbarouk (67 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, labda na mimi niungane na wenzangu katika kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa alivyotuwezesha kutupa afya njema tukaweza kuwemo katika Bunge letu leo hii siku ya tarehe 27 Mei, siku ya Ijumaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara nyingine nirudie kuwapongeza wapigakura wa Jimbo langu la Tanga Mjini. Kama nilivyosema kwa kubadilisha historia ya Tanzania na kuweza kumleta Bungeni Mbunge kutoka Kambi ya Upinzani kwa mara ya kwanza. Lakini vilevile niseme kwamba katika Wizara ya Elimu naunga mkono hoja iliyotolewa na Kambi ya Upinzani asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo nianze kuchangia kama ifuatavyo; moyo na engine ya nchi ni elimu na ndio maana wanataaluma wakasema education is a life of nation. Lakini vilevile nimnukuu aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini Mzee Nelson Mandela, alisema kwamba education is the most powerful weapon which you can use to change the world yaani elimu ni silaha nzito ambayo inaweza ikaibadilisha dunia lakini sisi Tanzania imekuwa ni kunyume na ninasema hivyo kwa sababu leo ukienda katika Wizara ya Elimu kuanzia elimu ya nursery kuna matatizo, ukienda katika elimu ya msingi kuna matatizo, elimu ya sekondari kuna matatizo, ukienda kwenye vyuo vikuu ndio kabisa, sasa tujiulize hivi kweli miaka 55 baada ya Uhuru mpaka leo sisi Watanzania tunajadili madawati!
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano wenzetu nchi ya India baada ya kupata Uhuru miaka 40 tayari Wahindi walikuwa wanaweza kutengeneza pikipiki aina ya Rajdoot, tayari walikuwa wanaweza kutengeneza magari aina ya Mahindra, tayari walikuwa wanaweza kutengeneza matreni, tayari wahindi baada ya miaka 40 waliweza kutengeneza vyombo vinavyokwenda aerospace katika anga za juu. Lakini leo Tanzania twajadili madawati, twajadili matundu ya vyoo, mashuleni vyakula hakuna it is a shame. Hii ni aibu, nchi kama Tanzania yenye rasilimali zote ambazo Mwenyenzi Mungu ametujalia lakini tumeshindwa kuisimamia vizuri elimu, tumeshindwa kuiweka misingi mizuri ya kielimu matokeo yake Tanzania tunakuwa na wa mwisho katika nchi tano za Jumuiya ya Afika Mashariki na kama sio ya mwisho basi labda tutakuwa tumeishinda Southern Sudan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunashindwa na Burundi, Rwanda,Uganda na Kenya. Leo Burundi waliokuwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe wakauana watu milioni mbili lakini wana system ya one child onelaptop,sisi Tanzania ambao tunajisifi tuna eneo kubwa la nchi, tuna uchumi imara lakini tumeshindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi niseme na niishauri Serikali tusichanganye siasa na elimu. Tunaposema elimu bure basi iwe bure kweli, lakini kama tunawacheza shere Watanzania Mwenyenzi Mungu atakuja kutuhukumu kesho. Leo tumesema elimu bure, lakini hivi ni kweli elimu ni bure?
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda shule za msingi leo hata maji ya kunywa watoto hakuna, kama pana nyumba ya jirani wakimbilie nyumba ya jirani kwenda kunywa maji. Leo watoto wa kike Ashakum si matusi anapokwenda kujisaidia lazima apate maji, shule zimekatwa maji, wanategemea kwenda katika nyumba za jirani, kama kuna muhuni, mvuta bangi huko mtoto wa kike ndio anaenda kubakwa huko huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wenzetu hamuoni kwamba haya ni matatizo. Sisi wapinzani tuna akili gani na ninyi wenzetu wa Chama Tawala mna akili gani. Miaka 55 baada ya Uhuru leo, tunajadili matundu ya vyoo, na ukiangalia hata katika matangazo ya Haki Elimu, mwalimu anakwenda kwenye choo na wanafunzi wamepanga mstari wanasukumana, choo hakina bati, hakijapauliwa, mwalimu anakanyaga mawe, lakini tunaambiana hapa ukitaka kuwa Rais lazima upitie kwa mwalimu, ukitaka kuwa Mbunge lazima upitie kwa kwa mwalimu, ukitaka kuwa Waziri Mkuu upitie kwa mwalimu. Tuna wacheza Watanzania shere, tuwaambieni ukweli kama tumeshindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme kitu kimoja tu kwenye suala la elimu ya nursery, Mheshimiwa Waziri lazima ukasimamie vizuri kwa sababu elimu ya nursery tumeweka utaratibu kwamba mtoto haanzi standard one mpaka apite nursery school, lakini hivi Serikali imeangalia ufundishaji na mitaala ya kwenye nursery school? Hakuna kitu kila mwenye nursery school yake ana mitaala yake ana utaratibu wake wa kufundisha. Hii ni hatari kwa sababu mwingine anaweza akawa ana uwezo mzuri wa kufundisha, mwingine hana uwezo mzuri matokeo yake sasa wazazi wanapoteza fedha lakini watoto wakitoka huko kwa sababu msingi sio mzuri hakuna kitu wanapofika standard one.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi kwenye elimu ya msingi, hapa pana matatizo makubwa. Kwenye elimu ya msingi katika nchi yetu kumekuwa na utaratibu kwamba kwanza watoto wanakwenda shuleni wakati mwingine hata chakula mtoto hajapata nyumbani. Sasa matokeo yake mtoto anakwenda na njaa, na mtu mwenye njaa hafundishiki, matokeo yake mimi nilikuwa naishauri Serikali ikibidi lazima tupeleke bajeti ya chakula katika shule zetu za msingi, hata na sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mtoto anapotoka nyumbani, anapokwenda shuleni na njaa hata mwalimu afundishe namna gani anakuwa haelewi. Amesema mwanafalsafa mmoja anaitwa Bob Marley, the hungry man is angry man, kwamba mtu mwenye njaa anakuwa na hasira, haelewi. (Makofi)
Kwa hiyo, mimi niseme tupeleke bajeti kubwa ya chakula katika shule za msingi na sekondari na vyuo. Hata wale wanaotu-supply vyakula katika vyuo vyetu na shule zetu basi walipwe kama alivyotangulia kusema msemaji aliyetangulia, kwa sababu wengine wanapelekwa mahakamani, wametoa zabuni za vyakula Serikali haijawalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine kwenye sekondari kuna matatizo makubwa, kuna suala zima la ukosefu wa walimu wa sayansi. Hakuna walimu wa mathematics, biology, physics na chemistry. Matokeo yake mtoto anamaliza form four hata ukimuuliza what is bunsen burner hajui, ukimuuliza what is test tube hajui, na matokeo yake wanakosa katika theory na practical zote wanakosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimtake Waziri ahakikishe maabara zinazojengwa zinaambatana pamoja na vifaa. Tusiseme tu kisiasa kwamba tunajenga maabara kumbe vifaa hakuna na matokeo yake hata wanaokuwa wanachukua masomo ya sayansi, kwa mfano wanaosoma PGM ndio hao tunaotegemea kwamba watakuja kuwa marubani. Lakini kwa ukosefu wa vifaa sasa tunakosa ma-pilot katika ndege zetu, matokeo yake tunaajiri wageni tunapeleka ajira katika nchi nyingine, mimi niseme lazima tujikite katika elimu iliyo bora kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda kwenye suala zima la vyuo vikuu. Vyuo vikuu kuna matatizo, na matatizo ni hayo ya mikopo, lakini hata na matatizo na uwezo wa wanafunzi wenyewe wengine wanaopelekwa. Lakini hata baadhi ya walimu pia nao uwezo wao sio mkubwa sana, matokeo yake sasa wanafunzi wetu wa vyuo vikuu wamekuwa nao elimu yao ikishindanishwa na nchi nyinine inakuwa sio bora.
Pia yupo Makamu Mkuu wa Chuo kimoja alisema, hata wanafunzi wa chuo kikuu hawawezi kuandika barua ya kuomba kazi, kwa kiingereza kwa sababu msingi ulikuwa ni mbovu, leo mtoto anakwenda shule ya msingi na njaa, leo mtoto anakuwa hana chakula, matokeo yake anateseka na njaa mpaka mchana, anatoka shule hana alichoelewa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia mambo kama manne hivi, nitazungumzia kwanza suala la road licence na motor vehicle, lakini nitazungumzia pia udhaifu na uchakavu wa fedha zetu, vilevile udhaifu wa EFD receipts na utozwaji kodi mara mbili pale unaposhusha mizigo Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema nikaweza kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Fedha. Vilevile niungane na wenzangu kuwatakia waislamu wenzangu wale ambao tunafunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani na wasiofunga pia Mwenyezi Mungu awafanye wavae vizuri kusudi tuweke swaumu zetu sawa. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Baada ya kusema hayo niseme tu kwamba palikuwa na utaratibu hapo zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa taarifa ya makusanyo ya fedha kila mwezi, lakini mpaka sasa hivi hatujui utaratibu umepotelea wapi. Hili tunaliona ni tatizo, namshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha utaratibu ule uendelee, kila mwezi TRA inapokusanya fedha tupewe taarifa za mapato ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia road licence, hii ni kodi ambayo inalipwa kwa vyombo vinavyotumia barabara. Baada ya wananchi kulalamika tulibadilisha tukaletewa motor vehicle lakini sasa kinachotushanganza motor vehicle inakuwa inalipwa hata kwa vyombo ambavyo vimeshakufa zamani au vimepata ajali na havipo barabarani kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali motor vehicle badala ya kushikwa katika vyombo ambavyo hata vimekufa au havipo barabarani basi sasa hivi motor vehicle tuiingize kwenye mafuta ili iwe chombo kinachotumia mafuta moja kwa moja kiwe kinalipa kodi ya Serikali, lakini kulipisha kodi chombo ambacho pengine kama ni gari limeshakufa au lipo garage miaka mingi au limeshatengenezwa majiko ya kupikia huko lakini bado linatozwa kodi, hii ni dhuluma ya mchana kweupe. Kwa hiyo, naishauri Serikali tuingize kodi ya motor vehicle kwenye mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna kodi nyingine naishukuru Serikali kwamba imeondoa motor vehicle katika pikipiki, lakini cha kushangaza pikipiki imewekewa kuna kitu kinaitwa fire extinguisher.Ukienda TRA unalipishwa shilingi 10,000 unapotoa shilingi 10,000 kwanza unaelekezwa ukalipie Max Malipo, risiti unapewa Max Malipo lakini hupewi hiyo fire extinguisher yenyewe. Sasa hii nayo ni dhuluma ya Serikali kwa wananchi wa Tanzania. Kwa hiyo, ndugu zangu wa bodaboda na wamiliki wa pikipiki nafikiri mtaona jinsi gani Wabunge tunavyowatetea katika Bunge letu hili. Kwa hiyo, naishauri Serikali fire extinguisher katika pikipiki nayo iondolewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia kuzungumzia suala hili la motor vehicle na road licence jirani zetu Kenya hapa hawana. Kenya unalipia insurance ime-contain vitu vyote, lakini Tanzania kuna kodi lukuki mpaka tunawachanganya Watanzania, tunawachanganya wafanyabiashara. Naomba ikibidi hili suala la motor vehicle viondolewe pia. Vilevile pia tuige kwa wenzetu kwa sababu kama ikiwa kumbe unapolipa insurance unaweza ukawa umelipia vitu vyote na sisi tungeiga mfano wa wenzetu Kenya kwa sababu ni jirani zetu na katika baadhi ya mambo ni kama walimu wetu. Kwa hiyo, nafikiri hilo litakuwa limeeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa kuzungumzia ni suala la wafanyabiashara kulipishwa kodi kabla hawajafanya biashara, hii nayo mimi naona ni dhuluma ya wazi. Ilikuwa kwanza Watanzania kuna kitu unataka kufanya biashara unaambiwa ufanyiwe assessment, wakati kodi inatakiwa ulipe baada ya kupata faida, Watanzania walipolalamika wakaletewa kitu kinaitwa hiyo assessment lakini unailipa kabla hujafanya biashara. Sasa wenzetu Kenya unapewa tax holiday ya karibu miezi sita, ina maana ufanye biashara, uwe umejiweka vizuri lakini wakati huo huo unapitiwa katika vitabu vyako, na sisi tuombe Tanzania tuwaige wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiingii akilini mtu kabla hajafanya biashara unamlipisha kodi, hii ni dhuluma vilevile kwa wafanyabiashara. Kwa hiyo, naiomba Serikali iwaache wafanyabiashara pale wanapotaka kufanya biashara kwanza wafanye biashara, baadaye Maafisa waTRA wakakague vitabu vyao ndiyo watoze kodi, lakini Tanzania tunakwenda kinyume kabisa, matokeo yake biashara nyingi zinafungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi hapa tulisikia taarifa ya Wizara ya Fedha, kwamba kuna biashara zaidi ya 300 Dar es Salaam zimefungwa, yaani katika mafanikio ya Wizara ya Fedha ni pamoja na kufungia biashara 300 ambazo hazilipi kodi. Mimi nasema haya sio mafanikio, haya ni matatizo. Hizi biashara zinapofungwa zimeondoa Watanzania wangapi katika ajira, zimewafanya watu wangapi maskini? Hata mfanyabiashara mwenyewe anakuwa hana kipato tena, ina maana unahatarisha maisha yake kwa kumkosesha kupata mkate wake wa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya wananchi kulalamika sana, kuna kitu kililetwa kinaitwa presumptive tax. Hii TRA waliiweka kwamba yeyote anayeuza kuanzia shilingi milioni nne mpaka shilingi milioni saba na nusu anatakiwa alipe shilingi 150,000 kwa mwaka, na anayeuza shilingi milioni 16 mpaka shilingi milioni 20 alipe shilingi 862,000. Sasa mtu analipaje fedha zote hizi kabla hajafanya biashara? Naishauri Serikali, kwanza tuwaache wafanyabiashara wafanye biashara halafu ndiyo tushike hizi kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine pia twende mbali zaidi, hizi assessment zinakuwa ni kubwa sana, naishauri Serikali tungetumia ile third law of demand, in the high price low demanded, in the low price high demanded. Sasa sisi hatuendi huko, matokeo yake tunakosa fedha nyingi katika makusanyo ya kodi kwa sababu kodi zetu sio rafiki kwa wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka kuzungumzia ni EFD machines. Mashine hizi kwa kweli ni utaratibu mzuri, lakini hapa kwetu Tanzania utaratibu huu tumeukosea. Kwanza, haioneshi kuwa mfanyabiashara aliuza kwa mkopo kwa mteja au anaporudishiwa mali endapo ina dosari risiti ile inamsaidiaje, mwisho wa mwaka anapofanya mahesabu inakuwa ni usumbufu na matatizo makubwa. Vilevile EFD machines zinafutika haraka, sio za madukani tunaponunua bidhaa wala kwenye ATM unapokwenda kutoa fedha benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi ambao tunatunza vitabu vyetu vya mahesabu ikiwa risiti ndani ya siku nne mpaka saba imefutika, mimi nasema huu ni sawasawa na utapeli, kwa sababu kama inavyosemekana kwamba unapokuwa una risiti ndiyo unajua pia takwimu zako za makusanyo zikoje, sasa sisi risiti zetu mbovu. Niliwahi kuwauliza wataalam wa TRA wakasema quality ya zile karatasi za risiti zipo grades tatu, sasa kwa nini tuweke grades tatu kama sio utapeli huu, kwa nini tusiweke grade moja tu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, risiti za EFD machines ikibidi zibadilishwe ziwe za plastic material kwa sababu zitakuwa hazifutiki, kama vile ambavyo fedha ya Msumbiji ilivyo, ni ya plastic, hata uichovye kwenye maji haifutiki. Kwa hiyo, nashauri EFD machine receipts ziwe za plastic. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu udhaifu wa fedha zetu, fedha zetu za Tanzania zinatia aibu, nchi kama sisi wenye historia kubwa na pana duniani lakini ukishika shilingi 50, ukishika shilingi 100 ya coin, ukishika shilingi 500 ya noti, ukishika shilingi 1,000, ukishika 2,000 aibu tupu. Pesa ya noti ikipita kwa muuza mkaa, ikaenda kwa muuza samaki, ikiingia kwa muuza juisi hapo ndipo wabillahi taufiq na mchezo umekwisha! pesa imeoza, haifai hata kumzawadia mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, narudi tena, tuitazame dola material yake ilivyo, tuitazame Riyal ya Saudi Arabia jinsi ilivyo, lakini pia tuiangalie pesa ya nchi kama Msumbiji ambayo tumechangia katika kuitetea kupata uhuru, leo wana fedha bora kuliko fedha yetu ya Tanzania, hii ni aibu. Kwa hiyo naishauri Serikali, tuboreshe material ya fedha zetu tunazotumia kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba nizungumzie suala la mafao ya wazee wetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki atakapokuja Mheshimiwa Waziri atuambie, deni la wastaafu wa Afrika Mashariki litakwisha lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunisikiliza.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia kukutana ili tuzungumze masuala ya nchi yetu. Vilevile nichukue fursa hii nikiungana na wenzangu waliotangulia kuchangia Kamati ya LAAC na PAC.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kukumbusha tu kwamba Serikali za Mitaa zipo kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni. Hata hivyo, taarifa ya Kamati pamoja na kuandikwa vizuri kuna baadhi ya maeneo kuna upungufu. Labda nisema katika Halmashauri zetu kumekuwa matatizo ya matumizi mabaya, lakini Kamati imetupa taarifa ya baadhi ya maeneo yaliyochambuliwa kwa mfano katika uchambuzi wa taarifa ya CAG kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 na 2014/2015 na kuonesha hesabu zake zina matatizo katika baadhi ya maeneo. Kwa mfano, katika matumizi yasiyozingatia Sheria za Manunuzi, hapa kuna upungufu mkubwa kwa sababu Sheria za Manunuzi hazifuatwi na matokeo yake baadhi ya bidhaa au huduma zinazotolewa katika Halmashauri zinakuwa chini ya kiwango au nyingine haziridhishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, mfumo uliopo sasa hivi katika Halmashauri zetu ambapo Madiwani wametolewa katika ile Tender Board na kuachwa watendaji peke yao ndiyo wanaofanya shughuli za manunuzi, naona huu ni upungufu, naishauri Serikali iliangalie upya suala hili kwa sababu watendaji wanapobaki peke yao huku tukiambiwa kwamba Madiwani ndiyo jicho la Serikali katika Halmashauri, wao wanafanya wanavyotaka, wanatoa zabuni kwa watu wanaowataka, matokeo yake sasa ama bidhaa au huduma zinazotolewa zinakuwa chini ya kiwango.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna upungufu katika kutekeleza mapendekezo ya Kamati kwa kipindi kilichopita na pia kutojibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Lingine kuna usimamizi mbovu katika kupeleka au kutokukamilika kwa miradi au miradi inakuwa chini ya kiwango. Vilevile katika Halmashauri kuna taratibu zilizofanyika za kuzinyang‟anya Halmashauri makusanyo ya property tax.
Kwa maoni yangu naona hili ni tatizo kubwa sana kwa sababu Halmashauri zilikuwa zikitegemea sana property tax kama chanzo chake kikubwa cha mapato. Leo Halmashauri zimenyang‟anywa kukusanya property tax imepelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA). Kwa mfano, hata Halmashauri yetu ya Jiji la Tanga ilikuwa na nyumba za kupangisha (quarters) pia zimeingizwa katika ukusanyaji wa TRA. Mimi naliona hili ni tatizo au Serikali itueleze kama imeamua kuziua Halmashauri kwa kifo cha kimya kimya (silent killing). (Makofi)
Mheshimwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo? Leo Halmashauri zinahudimia wananchi ikiwa ni moja ya majukumu yake, kuna zahanati, shule, barabara, mifereji na usafi wa miji, unapozinyang‟anya vyanzo vya mapato shughuli hizo zitafanyikaje bila fedha?
Mimi nashauri ikibidi Halmashauri zirudishiwe kufanya mapato au kama Serikali imeona property tax ni chanzo ambacho inastahili kupata Serikali Kuu basi irudishe vyanzo vingine ambavyo ilizinyang‟anya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwenye suala la Serikali za Mitaa, Serikali nayo inahusika moja kwa moja kuziwezesha Halmashauri ili ziweze kutenda shughuli zake vizuri lakini Halmashauri zimenyang‟anywa uwezo wake. Hata katika kitabu chetu hiki kuna miradi ambayo imefanywa chini ya kiwango au haijatekelezwa. Kwa mfano, mradi wa maji katika Kijiji cha Kayanze, Jijini Mwanza wenye thamani ya shilingi 618,704,554 haujatekelezwa. Pia kuna mradi wa maji wenye thamani ya shilingi 5,049,000,000 katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji nao pia haukutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kusema miradi ya maji itekelezwe.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza hotuba ya Kambi ya Upinzani ya pamoja na Serikali kufanya warsha, makongamano na mjadala mbalimbali ya kushughulikia kero za Muungano lakini kwa kuwa Muungano unahusu binadamu (watu) lazima kero zitaendelea kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika moja ya kero ya Muungano ni kitendo cha kupeleka Wanajeshi, Polisi, Mgambo, pamoja na silaha nzito na nyepesi wakati wa uchaguzi, hili jambo ni kero kwa wale wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waishio Zanzibar, nahoji je, hata Visiwa vilivyopo katika Ziwa Victoria navyo vinapelekewa vikosi na silaha kama Zanzibar?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri hadi kufikia hapo, wanaona ni kero na vitisho. Naishauri Serikali iache kupeleka vikosi na silaha toka Bara na kupeleka Zanzibar ili kuifanya demokrasia ya Tanzania ichukue mkondo wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bidhaa zinazoingia Zanzibar, zote zinalipwa kodi lakini cha kushangaza mwananchi yoyote akinunua hizo bidhaa na kuja nazo Tanzania Bara anatakiwa alipe upya ushuru wa forodha kupitia TRA. Naishauri Serikali kulipia mara mbili ushuru ni udidimizaji ushuru, bidhaa zinazoingia Bara zisilipishwe forodha mara mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira yanazingatia uwanda mpana na pia baadhi ya watu hawafahamu mazingira ni nini? mfano katika Jiji langu la Tanga yapo mambo mengi ya utunzaji wa mazingira mfano, open space (Viwanja vya wazi, viwanja vya michezo, Bustani za kupumzikia lakini mengi ya hayo maeneo yanasimamiwa na Halmashauri zetu, lakini sasa yameporwa na itikadi za vyama vya siasa. Naishauri Serikali ifute usia wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini William Mkapa kuwa viwanja vyote vya michezo , viwanja vya wazi na bustani zimilikiwe na Halmashauri (TAMISEMI).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Mipango Miji maeneo mengi katika Halmashauri zetu wanashindwa kupanga miji yetu, wanamilikisha viwanja vya wazi, michezo na bustani kwa kupima viwanja na kuwauzia kwa uroho wa kupata fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali Afisa Mipango Miji/Ardhi atakayefanya umilikishaji ardhi hovyo awajibishwe mara moja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kusimama hapa na kuchangia katika taarifa za Kamati hizi mbili. Labda niseme tu kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, vilevile nilikuwa kwenye Kamati Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuchangia kuhusu Serikali za Mitaa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya LAAC kuna maeneo ambayo yamezungumzia kuhusiana na kukaimu kwa Wakuu wa Vitengo au Wakuu wa Idara kwa muda mrefu. Naungana na wale wanaosema kwamba hili ni tatizo, kwa sababu unakuta Mkuu wa Idara anakaimu nafasi zaidi ya miezi sita inafika mpaka miaka mitatu wakati mwingine. Hii inapunguza uwezo wa kujiamini kwa Mkuu wa Idara pia anakuwa hana mamlaka kamili ya kusimamia au kutoa amri na maelekezo katika baadhi ya mambo. Kwa hiyo, naishauri Serikali katika hili baadhi ya taratibu zifuatwe ili wanaokaimu wasikaimu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu wapo watu wengi ambao wanazo sifa za kuwa Watumishi au Wakuu wa Idara kamili lakini kwa muda mrefu wanakaimu, hivyo hilo naomba lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia ni ucheleweshwaji wa ruzuku kutoka Serikali Kuu. Nashauri kwamba hakuna haja ya kuchelewesha ruzuku kwa sababu Halmashauri hasa ukizingatia baada ya kunyang’anywa baadhi ya vyanzo vya mapato zimekuwa hazina fedha, Kwa hiyo ruzuku inayotoka Serikali Kuu ndiyo inayofanyiwa kazi na Halmashauri zetu hivyo isicheleweshwe ili Halmashauri zikamilishe miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia ni unyang’anywaji wa property tax na mabango ya biashara kwa Halmashauri zetu. Kwanza napenda niseme tu kwamba Serikali za Mitaa nazo ni Serikali, kwa sababu kwa ufahamu wangu najua kuna Central Government na Local Government, sasa hizi Serikali za Mitaa zina majukumu ya kutoa huduma na kutimiza wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi, sasa tumezinyang’anya property tax pia tumechukua na mabango ya biashara, yote yamekwenda TRA. Nashauri kwamba turudishe property tax, turudishe mabango ya biashara katika Halmashauri zetu ili ziweze kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mingi ya maendeleo kama vile vituo vya afya, kuna zahanati pia kuna miradi ya madarasa na mambo mengine kadha wa kadha ambayo kama tutazirudisha property tax na mabango ya biashara Serikali za Mitaa zitaweza kufanya kazi kwa ukamilifu na kuwapa huduma bora wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni matumizi mabaya ya fedha za umma ambapo katika Halmashauri inabidi zisimamiwe kikamilifu. Pamoja na kupeleka fedha bila ya kuzisimamia ipasavyo itakuwa ni sawa na kazi bure. Kama wataalam wanavyosema the power without control is nothing. Kwa hiyo, lazima tunavyopeleka pesa tuzisimamie. Tuhakikishe kwamba zinafanyiwa ukaguzi na wale ambao wanapata hati chafu na hati zenye mashaka nao wajieleze kwa nini wanapata hati hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia katika Serikali za Mitaa ni mikataba ya upimaji wa viwanja. Mara nyingi upimaji wa viwanja umekuwa unatumia fedha nyingi lakini haukamiliki kwa wakati. Sasa tutoe maelekezo kwa Wizara kwamba wahakikishe pale ambapo Halmashauri inataka kupima viwanja, viwanja vipimwe kwa wakati na wananchi wauziwe bei nafuu ili kila mmoja aweze kupata kiwanja na ajenge nyumba bora ya kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie sasa katika Kamati ya PAC. Katika Kamati ya PAC kuna taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo imeishia tarehe 30 Juni 2016, taarifa hii imeeleza upungufu mwingi. Miongoni mwa upungufu uliojitokeza ni utekelezaji wa miradi iliyofanyika bila ya tija na kusababisha hasara kwa Serikali. Pia kuna dosari zilizojitokeza katika usimamizi wa miradi, kutokuwepo kwa nyaraka za malipo kwa baadhi ya taasisi na Wizara na Mashirika ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna upungufu wa kutokuzingatiwa kwa Sheria za Manunuzi ipasavyo, dosari katika usimamizi wa mikataba na ufanisi mdogo wa mabenki ya umma ukilinganisha na mabenki binafsi pia kuna kutokuzingatiwa kwa Sheria ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka kulizungumzia ni taarifa ya kwamba hadi Juni 30, 2015 kuna Maazimio nane tu ambayo ni sawa na asilimia 64.2 kati ya maazimio 14 ambayo ndio yametekelezwa, lakini kuna mengine Sita ambayo ni sawa na asilimia 35.8 haya bado hayajatekelezwa. Nafikiri ipo haja Serikali kuhakikisha maazimio haya yanatekelezwa yale ambayo yamebaki ili kuweza kuisimamia Serikali, Bunge linapotoa maelekezo kutokana na maelezo ya taarifa za Kamati, basi maelekezo yale yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ipo taarifa kwamba Serikali kutokulipa kwa wakati madeni ambayo imechukua au imekopa kutoka katika Mifuko ya Jamii. LAPF wanaidai Serikali shilingi bilioni 243.43, WCF inaidai Serikali shilingi bilioni 26.6, PPF inaidai Serikali shilingi bilioni 139.5, PSPF inaidai Serikali bilioni 623. 93, NSSF inaidai Serikali bilioni 519.05, NHIF inaidai Serikali bilioni 43.8 jumla ya madeni haya yote ni takribani trilioni 1.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa Mifuko ya Kijamii ambayo jana tu tumepitisha sheria hapa kwamba iunganishwe kwa pamoja, lakini sasa kama fedha hizi hazitalipwa au zitakaa kama deni kwa Serikali kwa muda mrefu, hii Mifuko itajiendeshaje? Matokeo yake ndio tunaposababisha watumishi wanapostaafu kukaa kwa muda mrefu wakisubiri mafao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niishauri Serikali katika hili, haraka iwezekanavyo ilipe madeni haya ya Mifuko ya Jamii, au kupitia kikao hiki Serikali ituambie baada ya jana kupitisha sheria ya kuunganisha Mifuko hii ya kijamii hadi lini Serikali itakuwa imelipa deni hili la shilingi trilioni 1.59. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naliona ni kutoanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Fund) nao pia Serikali ituambie, kwa sababu hii ilikuwa ni katika mapendekezo na maazimio ya Bunge letu ni lini Serikali itaanzisha hii Public Investment Fund.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni hali ya kifedha ya Mfuko wa PSPF kutoimarika ipasavyo. Hii nafikiri kwa upeo wangu ni ile kutokana na kuikopesha Serikali na Serikali kutolipa kwa wakati. Kwa hiyo nashauri Serikali ilipe madeni haya kwa wakati. Kingine pia ni usimamizi duni wa mikataba katika Wizara na Mashirika ya Umma. Mikataba yetu imekuwa na matatizo mengi na yote hii ni kwamba tuonawapa mamlaka na tunaowapa dhamana wanaona labda kwa sababu si mali yao, siyo taasisi zao binafsi ndiyo maana hawasimamii ipasavyo. Naishauri Serikali pale mtu anapofanya uzembe katika Idara yake au katika Wizara yake kama kuna mkataba mbovu mtu huyo awajibishwe moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ninalotaka kulizungumzia ni kutokukamilika kwa uzingatiaji wa Mfumo wa Kihasibu (IPSAS) accrual basis, hili ni tatizo, kwa sababu kama tunashindwa kusimamia mifumo na kuikamilisha tutasababisha ufisadi mwingi katika Halmashauri zetu. Ni bora hii mifumo tuisimamie lakini mifumo hii pia tuhakikishe inakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kulizungumzia ni baadhi ya Taasisi za Umma kutofuata Sheria za Manunuzi, ndiyo maana katika taasisi zetu za umma kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha za Serikali. Kwa mfano hata katika ununuzi wa samani tu kwa sababu hatusimamii vizuri, kwa sababu hatufuati Sheria za Manunuzi matokeo yake imekuwa kila mwaka tunabadilisha samani au kila mwaka rasilimali au vyombo vya Serikali vimekuwa havina ubora unaostahili na tunaagiza vyombo vipya, tukijua ni matumizi makubwa na matumizi mabaya ya fedha za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kulizungumzia ni dosari katika mkataba wa Mlimani City na Mlimani Holdings Limited. Katika taarifa iliyosomwa hapa na Mwenyekiti wetu Mama Naghenjwa Livingstone Kaboyoka ameeleza upungufu mwingi sana katika Mkataba huu. Nami niungane na mchangiaji aliyesema kwamba, takribani miaka 17 sasa imepita, ubadhirifu unaendelea, miradi haikamiliki lakini watu walikuwa wako kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama inafika mahali wanaingia mkataba mbovu kama huu, tutegemee nini? Kwa sababu katika Vyuo ndiko wanapotoka wasomi ambao ndiyo wanaokuwa Makatibu Wakuu wa Wizara, wanakuwa Makamishna, lakini leo hapohapo ndipo pana ubadhirifu na kumeingiwa mkataba mbovu. Sijawahi kuona katika mradi kama huu mkubwa kwamba eti Mwekezaji anatakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 inatakiwa Mwekezaji aoneshe mtaji wa namna gani anaweza kuendesha ule mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mradi wa Mlimani City Mwekezaji ameonesha Dola za Kimarekani 75 ambazo ni sawasawa na shilingi 150,000 lakini mkataba huo ukaingiwa. Sasa huu siyo wizi wa mchana kweupe? Bahati mbaya haya yametokea Serikali iko kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC kama nilivyosema, tumeanza kupigia kelele haya tangu mwaka jana na tukawaita baadhi ya Maafisa wa Chuo Kikuu vilevile tukatoa taarifa kwamba mkataba wa Mlimani City una upungufu, tulikitegemea tangu
kipindi hicho angalau wangefanya marekebisho. Hadi leo hii nazungumza hakuna kilichofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kwamba katika mradi au mkataba wa Mlimani City pamoja na Mlimani Holdings bado Serikali inatakiwa kufanya kazi kubwa katika hili na kupitia Bunge hili tutoe maelekezo kwamba waliohusika na mkataba ule Serikali iwachukulie hatua za kisheria haraka na mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumza ni ukiukwaji wa malipo ya land rent ambapo UDSM ilitakiwa ipate asilimia 10 ya pango kwa mapato ghafi, badala yake UDSM inalipwa baada ya kutoa gharama, wao wanalipwa asilimia 10 wakati walitakiwa walipwe kabla ya kutoa gharama. Kwa hiyo, ukiuangalia kwa undani mkataba huu wa Mlimani City na Mlimani Holdings pana uchafu mkubwa umejificha hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza CAG kwa kuibua uchafu na ubadhirifu katika mkataba ule, lakini kama CAG ndio jicho letu Wabunge anatuletea taarifa na Serikali haichukui hatua, itafika mahali tutamchosha CAG. Serikali imwezeshe kwa kumpa bajeti anayotaka kwa asilimia 100 lakini yale anayotuletea tusioneane haya, Waswahili wanasema ukicheka na nyani utavuna mabua. Kupitia Bunge hili nataka waliohusika wote katika mkataba ule wachukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe ni funzo na fundisho kwa wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mradi wa Dege Kigamboni au Dege Eco Village, kuna taarifa kwa kweli zinatia kichefuchefu, kuambiwa kwamba kuna kiwanja Kigamboni kinachoweza kufikia milioni 800 cha makazi ya kawaida. Hili naona halitakiwi kufumbiwa macho. Katika hili kwa kutokana na muda ni kwamba mkataba wa NSSF wana asilimia 45 ya hisa na hawa AHER au Azimio Holdings…

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha, naomba umalizie sentensi yako.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Nimalizie kwa kusema kwamba mkataba wa Dege Eco unatakiwa ufanyiwe kazi lakini vilevile pia kupitia Bunge hili, taarifa ya mabaya yote yaliyoibuliwa katika taarifa ya PAC na LAAC Bunge lako lichukue hatua za kinidhamu na lichukue hatua za kisheria. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia niwashukuru wapigakura wangu wa Jimbo la Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu nitaanza na hotuba ya bajeti ya Utumishi. Sekta ya Utumishi ni sekta muhimu na vile vile katika kila nchi basi sekta hii inakuwa na changamoto, lakini kwetu niseme imezidi. Kwa nini nasema hivyo; kwa sababu kwanza kuna tabia ya kuwacheleweshea watumishi wetu michango yao ya Mifuko ya kijamii katika NSSF, LAPF, WCF, GEPF na kadhalika. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi suala hili ili hii michango iwe inapelekwa mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pale wafanyakazi au watumishi wanapostaafu kumekuwa kuna tabia ya kucheleweshewa mafao yao. Sasa wale wanaohusika na malipo ya mafao wajijue na wao pia kwamba ni wastaafu watarajiwa, kwa hiyo wanavyowafanyia wenzao na wao wakija wakistaafu wajue watakuja kufanyiwa hivyo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, miongoni mwa changamoto ni kwa wale ambao walifukuzwa kazi. Katika Bunge hapa tumeambiwa kwamba Serikali imesema watarudishwa kazini, lakini mara tu jambo lolote linapotoka juu likienda kule chini kuna tabia unaambiwa kwamba waraka bado haujafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano hai katika mambo mbalimbali; kwa mfano mwaka jana tulipitisha hapa kwamba road license isamehewe, lakini ukienda ukafanya transfer kule unalipishwa na TRA, ukiwauliza wanakwambia kwamba bado waraka haujafika. Jambo likiwa la kuwasulubu wananchi hawaulizi waraka, moja kwa moja linafanyiwa kazi, kwa hiyo hii tabia nayo naomba iachwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale wafanyakazi ambao waliachishwa kazi kwa kisingizio cha vyeti feki au hawana vyeti vya darasa la saba; kuna wengine wameachishwa kazi wakiwa tayari katika QT, wamefanya mitihani na wanasubiri vyeti vile vya form four, lakini wameachishwa kazi. Sasa hili la kuwarudisha ni jambo jema lakini pasiwe na kisingizio cha kwamba waraka haujafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni vibali vya ajira katika halmashauri. Zoezi hili pia limetuathiri katika baadhi ya vituo vya afya, zahanati na maeneo mengine ya huduma muhimu, watu wamefukuzwa kazi; matokeo yake vituo vya afya havina manesi, hata baadhi ya Madaktari hakuna. Hata katika halmashauri tumepata tatizo kubwa la kuwa na watendaji ambao wanakaimu kwa muda mrefu; hili la kukaimu nalo pia lifanyiwe kazi. Mtu kukaimu zaidi ya miaka miwili inakuwa sio vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri yetu ya Jiji la Tanga tuna mitaa 181, lakini watumishi waliopo ni 123, na tuna upungufu wa watendaji wale wa mitaa 58. Pia tunazo kata 27, tuna watendaji 13 tu, bado tuna upungufu wa watu 14 kama watendaji kata. Kwa hiyo hilo naomba lifanyiwe kazi. Ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba vibali vya ajira pia vipelekwe katika halmashauri ili tuweze kujaza nafasi za wale watendaji ambao hawapo, hiyo ni kwenye utumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye suala zima a TAMISEMI sasa. Kabla sijaanza, najua TAMISEMI inaendana na shughuli nyingi, ni idara au ni taasisi pana ambayo inabeba mambo ya watu wengi. Pamoja na yote katika suala zima la utawala bora kuna kipengele kimeeleza kwamba mazingira ya utulivu na amani ni fursa adhimu katika kujenga uchumi imara na endelevu katika nchi yoyote ile. Sasa sisi bado kuna baadhi ya maeneo yamekuwa yanatupa shaka kidogo; huu mpango wa watu kukamatwa halafu hawajulikani walipo lakini familia zao zinahangaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kuna tatizo lililotokea tarehe 3, Aprili, 2018 kule Pemba kuna vijana sita walikamatwa, watatu wameachiwa ambao walikuwa ni; Juma Abdallah Kombo (miaka 16), Abdallah Hamisi Abdallah (miaka 19) na Said Shaabani Mohamed (miaka 16), hawa waliachiwa. Bado kuna wengine watatu hawajulikani walipo, mmoja wapo ni Thuwein Nassoro Hemed (miaka 30), Hamisi Abdallah Mattar (miaka 25) na Khalid Hamisi Abdallah (miaka 30). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kuna mambo mengine, kama alivyozungumza mzungumzaji mmoja jana, kuna baadhi ya mambo yakifanyika ni kama kuitia doa Serikali. Ni bora wale vijana huko walipo wakaachiwa…

T A A R I F A . . .

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, taarifa nimeipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwenye suala la Serikali za Mitaa, nianze kwa kumshukuru na kumpongeza Waziri wetu wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo, lakini Mheshimiwa Kapteni Mkuchika sijamsahau, ukizingatia alikuwa ni Mkuu wetu wa Mkoa wa Tanga; nampongeza, lakini haya niliyoyasema ayafanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika TAMISEMI naanza kwenye elimu. Wanafalsafa mmojawapo, bwana Nelson Mandela, amesikika akisema; education is the most powerful weapon which we can use to change our world; lakini pia wapo wengine waliosema education is the key of life. Sasa kwa nini natoa mfano huu; Mheshimiwa Jafo katika elimu yetu Tanzania tumekuwa na mitihani mingi sana, bado kuna matatizo ya ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi kama biology, chemistry, physics na mathematics.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile pia bado kuna uhaba wa matundu ya vyoo. Mwaka jana nilisema hapa kwamba kuna tangazo la Haki Elimu linaonesha kwamba mwalimu na wanafunzi wanasukumana kuingia chooni, choo ambacho kiko wazi juu hakina paa, kumejaa maji machafu, wanakanyaga kwenye mawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado inahitajika bidii kubwa ya Serikali kuwekeza. Kama vile tulivyonunua magari ya maji ya kuwasha, basi tuhakikishe tunapeleka hata vile vyoo vya bei nafuu katika shule zetu ili kuepukana na tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mitaala yetu ya kielimu; tumekuwa na matatizo ya mitaala kuanzia kwenye nursery schools, primary schools, secondary schools, colleges na universities; bado kuna matatizo makubwa ya hii mitaala. Kwa mfano katika nursery kila mtu anafundisha anavyojua mwenyewe, yaani Serikali haikuweka mtaala maalum, kwamba nursery wanatakiwa wafundishwe kupitia nyanja hizi, hakuna hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi naishauri Serikali kwamba ni lazima tuwe na utaratibu mzuri. Haiwezekani katika nchi zote za Afrika Mashariki sisi Watanzania mfumo wetu wa elimu, mimi kwa maoni yangu naona tumepitwa na wenzetu wote. Kwa sababu ukienda Rwanda na Burundi leo ni one child one laptop. Ukienda Kenya kwa wenzetu wametangaza kwamba elimu bure lakini ni kuanzia standard one mpaka university, tena hakuna mambo ya mikopo ya wanafunzi wala hakuna matatizo, wanafunzi kazi yao ni kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa kwetu kwa sababu mifumo yetu imekuwa ikiingiliana na mambo mbalimbali, matokeo yake kumekuwa na migomo ya mara kwa mara, wazazi wanashindwa kulipa ada kwa baadhi ya watoto wa familia za maskini. Tumetangaza elimu bure lakini kisiasa, kwa mantiki hiyo wengi wana akili, wamefaulu lakini wanabaki nyumbani. Naamini Wabunge wenzangu ni mashahidi hapa; kama hawakufuatwa na watoto 20 basi 30, kila mtoto amefaulu lakini hana school fees, hana viatu, hana madaftari na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali, kama tunasema elimu bure basi angalau kidogo tuwaige wenzetu wa Kenya ili watoto wetu wapate elimu. Unakuta mtoto ananyongeka, yeye amefaulu amefanya kazi ya kusoma lakini familia haina uwezo, mtoto anakaa nyumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, juzi tarehe 11 Rais Uhuru Kenyatta amesaini sheria kwamba wanafunzi wote wa kike Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Kenya itakuwa inawapa taulo za kike (pads) bure, free, no charge. Sasa najiuliza; ukiitazama Kenya Mbuga ninazozijua mimi ni Tsavo na Maasai Mara. Sisi tuna mbuga za wanyama, tuna bandari tatu, Kenya wana bandari moja, tuna Mlima Kilimanjaro Kenya hawana, tuna mkonge, katani, pamba, pareto, alizeti na mambo mengine… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema pia naendelea kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga kwa kunichagua na nawaahidi kuwatumikia kwa utumishi na uwakilishi uliotukuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, education is the most powerful weapon which we can use to change the World (By Nelson Mandela Madiba) education is the key of life.

Mheshimiwa Mwenyekiti, semi zote hizi zimetumiwa na Wahenga wetu zikiwa na maana kubwa sana. Katika miaka ya 1970, Tanzania ilikuwa katika level moja ya kiuchumi au hata sarafu yetu ilikuwa na thamani kuliko sarafu ya nchi za Singapore, Malaysia, Indonesia, China, Vietnam na Kenya lakini leo hii 2018, nchi zote hizi zimetuacha kiuchumi na kielimu na sababu kubwa wenzetu hawa waliwekeza katika elimu kuanzia nurseries, primaries, secondaries, colleges and universities.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi za East African Communities tunaishinda Southern Sudan tu, nchi nyingine zilizobaki zimetuacha nyuma. Nchi nilizozitaja zimefikia uchumi wa dunia ya kwanza na dunia ya pili sababu waliwekeza katika elimu, hiyo ndio siri ya mafanikio. Kenya walipoamua elimu bure waliamua kwa dhati ya moyo wa Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri, Serikali iwekeze katika elimu ili tuepuke shida na matatizo yaliyopo katika elimu ya Tanzania kuanzia mitaala, chakula mashuleni, mikopo vyuo vikuu. Tanzania uchumi wake ukue practically badala theoretically kama nchi nilizozitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana 11 aprili 2018 Rais wa Kenya Uhuru Kenyata alisaini sheria kwa niaba ya Serikali kuwapatia huduma ya taulo za kike kwa wanafunzi wote wa kike nchini Kenya kupatiwa huduma hiyo bure (free of charge).

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure bado katika ngazi za chini haieleweki na Walimu wetu wamechanganyikiwa maji na umeme vinakatwa, walinzi hakuna na shule zinaibiwa vifaa mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya, naipongeza Serikali kwa kutoa katika halmshauri mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Tanga kutupatia shilingi 1.4 bilioni kwa ajili ya Vituo vya Afya vifuatavyo:-

Makorora 500 milioni, Mikanjuni 400 milioni na Ngamiani 500 milioni na shughuli za ujenzi sasa hivi zinaendelea katika vituo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga hatuna hospitali ya Wilaya, katika bajeti ya halmashauri, Baraza la Madiwani tumetenga shilingi milioni300, regardless shilingi milioni 400 ambazo zimeshajenga administration block ambapo kwa sasa baadhi ya vyumba vinatumika kutoa huduma kwa wananchi kama zahanati. Naiomba Serikali itupatie shilingi bilioni 1.6 ili tuweze kujenga Out Patient Department (OPD). Kwa kufanya hivi tutaipunguzia mzigo mkubwa wa wagonjwa toka Wilaya zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Bombo ni hospitali ya rufaa ambayo ina upungufu mkubwa wa vifaa tiba, Madaktari Bingwa lakini hata miundombinu, lift ina muda mrefu zaidi ya miaka mitatu ni mbovu na old model inahitajika lift mpya Bombo.

Mheshimiwa Mwenyekitim, nimefanya utafiti na ufuatiliaji katika kampuni maarufu ya lift ya OTIS- FRANCE zinahitajika euro 126,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 400 kuweza kupata lift mbili mpya kwa ukubwa wa jengo la lift lililopo. Naiomba Serikali itoe hizi euro 126,000 ili kutatua tatizo la lift na kuondoa adha ya mabaunsa kubeba wagonjwa na pia tunaomba Madaktari Bingwa wa mifupa, vichwa na magonjwa ya akinamama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo, nawapongeza wakulima wote Tanzania. Tanzania miaka 57 baada ya uhuru bado kilimo chetu ni cha jembe la mkono 80% na bado kilimo kipo katika propaganda za kisiasa na misamiati kibao. Kilimo cha ushirika, kilimo cha kufa na kupona, kilimo kwanza, kilimo cha bega kwa bega, lakini Serikali bado haipo serious na hata pale wakulima wanapofanya bidii ya kulima na kupata mazao ya kutosha kwa chakula na biashara wanakatazwa kuyauza kwa soko wanalotaka wenyewe. Mfano, zao la mahindi, Mbaazi na zao la Karafuu Zanzibar. Baada ya Bunge kuchachamaa mahindi ruksa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri, Tanga City Council, tunazalisha muhogo na matunda kwa wingi katika Kata za Kirare, Tongoni, Mabokweni, Pongwe, Mzizima na Chongoleani lakini hakuna soko la uhakika. Ni aibu kwa Tanzania kuagiza juice za orange, mango, guava, mastafeli tena tunaagiza kwa fedha za kigeni kutoka nchi za Saudi Arabia, South Africa na Kenya juice za Ceres na tropical. Serikali ijenge viwanda vya kusindika (processing) matunda Tanga kulingana na wingi wa matunda yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo; ufugaji katika Tanzania imekuwa ni balaa wafugaji wanateseka wao na mifugo yao, hawaruhusiwi kuchunga mifugo yao katika mapori ya hifadhi wala ranchi za Serikali kwa kisingizio kuwa wanavamia hifadhi za Taifa. Mifugo ni uchumi na biashara, nchi kama Botswana, Swaziland na Ethiopia zinafaidika kiuchumi na kutumia fedha hizo katika miradi ya maendeleo. Tanzania wafugaji wetu wananyang’anywa mifugo yao na kutiwa umaskini hali inayosababisha wafugaji kukimbia familia zao kutokana na umaskini baada ya kunyanga’anywa mifugo yao. Wananyang’anywa mifugo ng’ombe 500, 700 hadi 2,000 habaki na hata ng’ombe mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuweka alama kwa moto, huu ni ukatili wa kupindukia kwa kuwa chuma cha moto ni maumivu makali kwao. Waziri wa Mifugo anazindua uwekaji alama kwa kumchoma mnyama kwa moto. Ushauri Serikali itoe elimu ya ufugaji wa kisasa kwa kuweka pin masikioni badala ya moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi na zana za kisasa, wavuvi wamesahauliwa na kubwa kwao ni kulipishwa ushuru wa samaki, kunyang’anywa nyavu na boti zao. Hii sio haki inahitajika elimu na replacement za vifaa vinavyokubaliwa kisheria na sio kuchoma moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA (Tanzania Rural and Urban Road Agency); katika Bunge la mwaka jana bajeti tulipatiwa taarifa na kupitisha TARURA, tunajua nia njema ya Serikali lakini TARURA haijafahamika kwa Wabunge na Madiwani hata kidogo. Tuliomba Serikali itufanyie semina Wabunge, kisha Madiwani lakini hadi leo ni mwaka bado hakuna semina. Ushauri wangu, Wabunge tupatiwe semina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za vijana na akinamama asilimia kumi; kila halmashauri inatakiwa kutenga 10% za vijana na akinamama, lakini kutokana na vyanzo vya mapato vya property tax na mabango kuporwa na Serikali Kuu (TRA), halmashauri kwa sasa zina hali mbaya kifedha. Hii ni moja ya sababu za kutotengwa kwa fedha hizi. Ushauri wangu ni kwamba, naomba Serikali irudishe vyanzo vya property tax na mabango ya biashara ili makusanyo haya yaweze kuziwezesha halmashauri kutenga fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Utumishi ni sehemu muhimu katika nchi yetu ambayo ina changamoto nyingi ikiwemo watumishi na wafanyakazi kucheleweshwa michango yao katika Mifuko ya kijamii kama vile NSSF, LAPF, GEPF na kadhalika. Miongoni mwa changamoto nyingine ni mtindo wa kuwahamasisha Walimu toka sekondari kuwarudisha kufundisha shule za msingi bila ya kuwalipa stahiki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni tatizo na tunaona ni jambo jema kwa kisingizio cha kuboresha tatizo la upungufu wa Walimu katika shule za msingi, lakini hili ni tatizo ambalo Walimu hawa wanafanya mgomo wa kimya kimya na matokeo yake wanaoathirika ni wanafunzi kwa kuwa Walimu hawafundishi kwa moyo, wanafunzi wanafeli na ushahidi wa hili shule zinazoongoza kwa ufaulu ni za private.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vibali vya ajira kukosekana katika halmashauri, kufuatia zoezi la uhakiki wa vyeti feki watumishi waliokosa vyeti vya form four pamoja na Serikali kutangaza kuwa walioathirika na zoezi hili warudishwe kazini, lakini kuna tabia kule chini likitoka agizo la Serikali katika utekelezaji wanasema hatujapokea waraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba, waraka huo ushushwe ngazi za chini immediately, wale ambao wamefariki kufuatia pressure na mshtuko ingawaje kufuatia zoezi hili pia athari zimepatikana katika sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya, Madktari na wauguzi baadhi wamekosekana na vituo, zahanati zimekosa watumishi na ajira mpya vibali havitolewi bila ya kuelezwa sababu zenye kueleweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu, bado kuna upungufu mkubwa sana katika sekta ya Walimu (shule za msingi, shule za sekondari na vyuo). Mfano, Mamlaka ya Maji Tanga wafanyakazi wengi wamefukuzwa katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, tunazo kata 27 na mitaa 181; Watendaji wa Mtaa katika mitaa 181 waliopo 123 na pungufu ni 58. Watendaji Kata katika kata 27, waliopo ni watendaji 13, pungufu ni 14. Pia kuna mitaa ambayo kuna makaimu ni zaidi ya miaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, vibali vya ajira vitolewe haraka ili kuondoa upungufu wa watumishi katika sekta mbalimbali ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MUSSA BAKARI MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha na mimi leo kusimama hapa kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Vilevile nitakuwa ni mchoyo wa shukrani kama sikuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo langu la Tanga Mjini ambao kwa mara ya kwanza wamebadilisha historia ya Tanzania kwa kupatikana Mbunge wa Upinzani katika Jimbo la Tanga iliyokuwa ngome kuu ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia viwanda, biashara na ubinafsishaji. Kwanza nisema bila umeme wa uhakika basi Tanzania ya viwanda itakuwa ni ndoto za alinacha. Nasema hivi kwa sababu nchi yetu imekuwa kama nchi ya kufikirika. Baada ya kugundulika gesi na makaa ya mawe tumekuwa tukiambiwa kwamba umeme kukatikakatika utakuwa kama historia ya vita ya Majimaji iliyopiganwa mwaka 1905 lakini leo umeme umekuwa hauna uhakika, humu humu ndani ya Bunge pia umeme unakatika, sasa sijui Tanzania ya viwanda itakuwa ni Tanzania ipi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba viwanda, biashara, reli na barabara ni vitu vinavyoambatana. Imefika mahali sisi Tanzania tumekuwa tunafanya vichekesho, kwa nini? Leo reli inayotoka Tanga kuja kuungana na reli ya kati imekufa, lakini vilevile pia viwanda vingi, hakuna asiyejua kwamba Tanga ulikuwa ni mji wa viwanda. Tulikuwa na Kiwanda cha Chuma – Steel Rolling Mills, tulikuwa na kiwanda cha Sick Saw Mill, tulikuwa na Kiwanda cha Mbolea, tulikuwa na Kiwanda cha Kamba – Ngomeni, tulikuwa na NMC, tulikuwa na karakana kubwa ya reli, vyote hivyo vimeuliwa chini ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, kutokana na kufa viwanda hivi, leo Mji wa Tanga umekuwa hauna ajira. Tukumbuke Tanga ulikuwa siyo mji wa mazao ya vyakula, ilikuwa ni mashamba ya mkonge nayo pia yamekufa. Sasa imefika mahali Tanga umekuwa kama mji ambao ulikuwa na vita kama Baghdad vile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kuuliwa viwanda vya Tanga matokeo yake sasa miaka 55 baada ya uhuru Tanzania leo tunaongoza kwa kilimo cha pamba lakini nepi za watoto wachanga made in China. Sindano ya kushonea kwa mkono made in China! Vijiti vya kuchokolea meno (tooth pick) made in China! Miti ya kuchomea mishikaki pia made in China! Basi hata handkerchief pia! Bado tukikaa humu ndani tunajisifu kwamba sisi tuna viwanda na tunataka kuifanya Tanzania ya viwanda, mimi sikubaliani na suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema kama tunataka kuifanya Tanzania ya viwanda kwanza tufufue vile viwanda vingi vilivyouliwa katika mji wa Tanga! Hakuna asiyejua, ukienda Tanga, Muheza ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya matunda hususan machungwa lakini leo tunanunua packet ya juice kutoka Saudi Arabia kwa shilingi 5,000. Hakuna asiyejua kwamba ukienda maeneo ya Hale na Korogwe kuna maembe ya kutosha lakini hakuna hata viwanda vya ku-process matunda hayo tukaweza kuuza sisi katika nchi nyingine. Leo matunda na juice zote zinatoka nje wanaoleta huku wanachukua pesa zetu za kigeni wakaenda kununulia. Unapokuwa una-import zaidi kuliko ku-export maana yake unajikaribishia umaskini lakini wenzetu hilo hawalioni! Anayezungumza hapa ataanza kupongeza, ataanza kusifu Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini yanapoharibika hasemi kwamba ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi ndiyo inayoharibu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi nashangazwa, mbona nchi nyingi duniani zinafanya maendeleo lakini hawataji ilani za chama! Kenya shule zinajengwa, maabara zinajengwa, ukienda Malawi barabara zinajengwa na maendeleo mengine yanafanyika lakini watu hawataji Ilani ya Chama! Mimi naona tatizo hapa ni Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, lazima tubadilike, Serikali yoyote inayokusanya kodi kazi yake ni kurudisha kodi hiyo kwa kuwapelekea wananchi maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye suala la biashara, Watanzania leo wamekuwa wakihangaika hususan akina mama, ukienda katika kila nyumba sasa hivi katika mikoa yetu na miji yetu mikuu, kila nyumba ina frame za maduka kwa sababu ajira hakuna na viwanda hakuna. Leo akina mama ndiyo wanaolea familia, wanahangaika wanafungua biashara lakini cha kushangaza sheria ya biashara ya Tanzania ni tofauti na sehemu nyingine. Kawaida ya biashara, mfanyabiashara anapoanza biashara upya lazima apewe tax holiday ili ajiweke vizuri aweze kupata faida alipe kodi. Hata hapa ndiyo sheria inavyosema kwamba usilipe kodi kabla ya kupata faida lakini Tanzania mtu anakwenda TRA akishapata TIN Number anafanyiwa assessment, analipa kodi kabla hajafanya biashara! Matokeo yake sasa akina mama wanaokopa mikopo katika taasisi za kifedha kama BRAC, Poverty Africa na wengine wamekuwa wakichukuliwa vyombo vyao, wamekuwa wengine wakijinyonga na wengine wamekuwa wakikimbia familia zao kwa kuogopa madeni wanayodaiwa na taasisi za fedha. Sasa kwa nini Serikali yetu haiwasaidii wananchi wake katika biashara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Rwanda na Burundi anayekuwa na nia ya kufanya biashara baada ya mtaji aliokuwa nao Serikali inamuongezea fedha na kuambiwa kwamba tunakuongezea fedha uajiri Waburundi wenzako au Warwanda wenzako wawili usaidie kukuza ajira katika nchi yetu lakini Tanzania ni kinyume. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, nakuomba ulizingatie hili, Tanga viwanda vingi vimeuliwa, hususan reli. Panazungumzwa hapa reli ya kati itajengwa katika kiwango cha standard gauge, lakini Waswahili wana usemi wao wanasema, mwiba uingiapo ndiyo unapotokea hapo hapo. Reli ya kati ilianza kujengwa na Wajerumani katika miaka ya 1905 na ilianzia Tanga, vipi leo twataja reli ya kati ijengwa kuanzia Dar es Salaam! Tumesahau kwamba mwiba uingiapo ndio utokeapo? Mimi naomba kama reli ya kati inataka kufanyiwa ukarabati basi ianzie Tanga, Bandarini pale ambapo ndio reli ilipoanzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nalotaka kusema, tumeambiwa hapa na wazungumzaji wengi kwamba viwanda vilifanyiwa ubinafsishaji na vingine kuuzwa. Amesema Mheshimiwa Lijualikali kwamba kule kwake kuna mbuzi katika kiwanda cha sukari lakini hata Tanga kwenye kiwanda cha chuma! Cha kushangaza walikuja wawekezaji wa Bulgaria, wakaja Wajerumani wakataka kiwanda kile cha chuma lakini matokeo yake wakanyimwa, wakapewa wawekezaji waliotakiwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Matokeo yake sasa kiwanda kile imekuwa ndani kunafugwa mbuzi napo kama vile ilivyokuwa Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha chuma cha Tanga kilikuwa kinazalisha two products same time, kulikuwa pana misumari bora kabisa katika Afrika Mashariki na nondo zinazozalishwa Tanga zilikuwa ni bora. Sasa na mimi najiuliza, chuma bado kinahitajika siku hadi siku katika ujenzi wa maghorofa, katika ujenzi wa madaraja lakini hata katika body za magari, inakuwaje kiwanda cha chuma kipate hasara mpaka kife? Huu ni ushahidi kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshindwa kusimamia viwanda vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme Mheshimiwa Waziri, hoja yako siiungi mkono naunga mkono hoja iliyotolewa na Upinzani lakini kwanza iangalie Tanga! Katika viwanda vingine usisahau viwanda vya matunda, Tanga ni mji unaozalisha matunda kwa wingi, tunahitaji viwanda vya matunda navyo vijengwe Tanga ili Tanga iweze kurudia hadhi yake kama zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nikumbushe historia kidogo, hata ukiangalia jina la nchi hii kabla ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar ilikuwa inaitwa Tanganyika. Sasa hebu angalia Tanga ilivyokuwa na umuhimu katika nchi hii, Tanga na nyika zake ndio tukapata hii Tanganyika lakini bado watu wamesahau historia kwamba Tanga imechangia mchango mkubwa katika kuleta uhuru wa nchi hii, leo Tanga imekuwa imeachwa kama mtoto yatima! Hata ukiangalia bajeti ya mwaka huu 2016/2017, Tanga tuna mambo mengi ambayo tumeachwa, tutakuja kuzungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata vilevile pia katika huo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar palikuwa pana mahusiano mazuri sana kati ya watu wa Zanzibar na watu wa Tanga na hususan katika masuala ya kibiashara. Mpaka leo watu wanaingiliana katika biashara, watu wanawekeza upande wa Bara na Visiwani, lakini Serikali imekuwa haitii nguvu kwa hawa wafanyabiashara ambao ni wazalendo.
Vilevile pia tumeacha sasa kuikumbuka na kuisaidia Tanga kwamba ndio yenye historia ya uhuru wa nchi yetu, lakini tunaomba Mheshimiwa Waziri asisahau kwamba hata yeye yawezekana akawa ana jamaa zake na ndugu zake Tanga, kwa nini? Kwa sababu Tanga ulikuwa ni mji wa viwanda, uliweza kukusanya makabila yote ya Tanzania 122 lakini hata nchi jirani kutoka Burundi, tunao Warundi wengi kule, kutoka Malawi tunao watu wanaitwa Wanyasa kule, kutoka Kenya, Uganda, Zambia watu walikuja kufuata ajira Tanga, sasa inakuwaje viwanda vya Tanga vife. Mimi naomba kama Waziri una nia ya kweli ya kuifanya Tanzania ya viwanda hakuna haja ya kujenga viwanda vipya, tukifufua viwanda vya Tanga peke yake na maeneo mengine ya Tanzania kweli tutakuwa Tanzania ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa kabisa tusisahau kwamba bila ya umeme wa uhakika viwanda vitakuwa ni kama vile mchezo wa alinacha. Lazima kwanza tuwe na umeme wa uhakika, iwe tuna dhamira ya kweli kwamba kweli tumegundua gesi, tumegundua makaa ya mawe lakini hata upo umeme pia wa upepo lazima tushirikishe umeme wote huo. Wenzetu wa baadhi ya nchi kama Ujerumani pamoja na ukubwa wake wanatumia solar power system na sisi kwa nini hatuna mpango wa muda mrefu wa Serikali wa kujenga mtambo mkubwa wa umeme wa kutumia solar power system? Kama tuki-fail katika hydro-electric power twende katika gesi, Kama kwenye gesi tumeshindwa, tungekwenda katika solar power. Sasa Waziri unapozungumzia viwanda bila ya kutuhakikishia kwanza kwamba tuna umeme wa uhakika, mimi hapo inakuwa sielewi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri, hakuna haja ya kujenga viwanda vipya, tufufue viwanda vingi zaidi ya 70 vilivyokuwa Tanga ambavyo vimekufa lakini tufufue na viwanda vingine ambavyo vya zamani kama alivyotaja Mheshimiwa mmoja kiwanda cha Nyuzi Tabora na vinginge ili tuweze kufikia maendeleo ambayo Watanzania wanayatarajia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hotuba ya Bajeti ya Wizara yako kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la maliasili ni pamoja na Hifadhi za Taifa (TANAPA), bahari, mito, misitu na mbuga za wanyama au hifadhi. Tanga tunazo mbuga au hifadhi kama Mwalajembe, Kalalani, Mkomazi na Saadani, lakini bado hazijatangazwa katika medani za kitaifa, kiasi kikubwa cha kutosha. Naiomba Wizara yako ihakikishe inazitangaza mbuga za Mkomazi, Mwakijembe, Kalamani na Saadani katika viwango vya kimataifa ili ziweze kujulikana na kutembelewa na watalii wa ndani na nje na kuingiza mapato ya fedha za kigeni (foreign currency).
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapokuja watalii ajira zinaongezeka, kutajengwa hoteli, zitaajiri wahudumu pia wasafirishaji maliasili, pamoja na misitu. Napenda kuzungumzia utunzaji wa misitu ya nchi kavu na baharini pembezoni mwa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ambayo kuna shughuli za utalii au maliasili na ikiwa kuna mapato yanaingia asilimia 20 zirudi katika eneo husika. Ikibidi isiwe fedha, ziwe samani au vifaa kama madawati, ujenzi wa zahanati na kadhalika. Naomba Tanga Mjini isikose madawati ya TANAPA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumezuka tabia ya kuibiwa wanyama pori wetu, ndege wetu na viumbe hai na kupelekwa nchi mbalimbali za Ulaya, Marekani na Asia, je, ni akina nani wanaofanya biashara hii haramu? Lazima nchi idai rasilimali zake na itunze viumbe hai hawa na anayehusika akipatikana hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia kwa maandishi bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuboresha majengo ya ofisi zetu za Balozi za Tanzania nje ya nchi, zinatia aibu kwa majengo kuwa machakavu hata rangi hayabadilishwi. Naishauri Serikali, pale ambapo baadhi ya nchi zinatupatia viwanja kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kudumu ya Ubalozi mfano Oman, tuyajenge haraka iwezekanavyo ili kuepuka kunyang‟anywa viwanja hivyo na kupewa nchi nyingine kama ilivyotokea Oman; kiwanja chetu kupewa nchi ya India ambayo tayari wameshajenga jengo la kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafungu ya fedha yapelekwe mapema katika Balozi zetu za nje ili kuboresha utendaji bila kusahau kuboresha mishahara na elimu zao na kuwashughulikia Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi ambao wanapata matatizo katika ajira zao au shughuli mbalimbali za kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamekuwepo na tatizo la vyeti vya baadhi ya vyuo vyetu (certificates) kutotambulika katika nchi za nje, hali ambayo inasababisha usumbufu katika ajira kwa Watanzania waliopo nje. Mfano, Dar es Salaam Maritime Institute Certificates, hazitambuliwi Kimataifa kwa mujibu wa taarifa nilizopata toka kwa Watanzania, mabaharia wanaofanya kazi katika nchi za ng‟ambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ihakikishe inavitangaza vyuo vyetu Kimataifa kwa kufuata taratibu za Kimataifa ili vitambulike katika medani za Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali yetu kufanya taratibu ya kuondoa visa na kutumia entry katika nchi za Nordic United Arab Emirates, United Kingdom, German and Northern America. Hii itasaidia Watanzania wengi kupata fursa za kibiashara na kielimu, hali itakayowezesha Watanzania wengi pia kupata ajira na wale wenye vipaji vya michezo mbalimbali. Pia wataweza kuionesha dunia kuwa Watanzania wanaweza na wao pia watapata ajira. Mfano, wachezaji wa basketball, football, golf, tennis, athletics na kadhalika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema. Naanza kwa kuchangia Wizara hii ambayo inahusiana na Katiba na Sheria ambavyo vyote ndio msingi wa haki. Mfano; katika kitabu cha Hotuba ukurasa wa 36 kipengele cha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora:-
(i) Kukuza na kutetea haki za binadamu hususan makundi yenye mahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno haya yameandikwa lakini hayafanyiwi kazi na ushahidi kuna mahabusu na wafungwa wengi ambao wamefungwa bila kupatiwa haki za kisheria kwa kutetewa na wanasheria wa Serikali, kutojua haki zao lakini pia kwa kesi za kubambikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo akinamama wajawazito wanaojifungulia Magerezani na pia wapo wanaotiwa hatiani wakiwa na watoto wachanga ambao bado wananyonya maziwa ya mama zao na hawawezi kuishi bila ya mama zao, wanakuwa wafungwa bila hatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu; Serikali itafute adhabu mbadala kuwaepusha watoto kuwa wafungwa bila hatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Katiba na Sheria nimeishangaa kwa kutoweka katika Bajeti yake Fungu la Fedha kwa ajili ya kuendeleza mjadala wa Katiba mpya ambayo ndio haja ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria itenge fedha kwa ajili ya mwendelezo wa mjadala wa Katiba mpya ili kuondoa kiu ya Katiba mpya kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakimu kukaa katika Vituo vyao kwa muda mrefu wanazoeleka na wanazoea na kuwa wepesi kuweza kupokea rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakimu waongezewe mishahara ili kuwaepusha katika suala zima la kupokea rushwa.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujaalia afya njema na kuweza kuendelea na shughuli zetu za Bunge kama kawaida. Pili, wakati wote sitaacha kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo langu la Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa maendeleo wa Taifa, naanza na viashiria vya uchumi kama vilivyoelezwa katika kitabu alichotusomea Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Kwa mujibu wa takwimu ambazo tumezipata au Taarifa ya Fedha kupitia Shirika la Fedha Duniani (IMF) imezungumza kwamba uchumi wa dunia unakua kwa asilimia 3.9 na kwa upande wa Afrika Mashariki, Nchi yetu ya Tanzania na Rwanda ndizo zinazoongoza kwa uchumi wake kukua kwa asilimia 7.2 dhidi ya asilimia 7.1 ya mwaka uliopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua tu kwamba katika hili, mara nyingi wananchi wamekuwa wakituuliza sisi viongozi tunapopewa takwimu hizi za kukua kwa uchumi lakini mbona tukiangalia sisi wananchi hali kila siku inakuwa afadhali ya jana? Nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, pamoja na mipango mizuri aliyokuwa nayo ya kukua kwa uchumi lakini uchumi usikue kwenye makaratasi na makabrasha, uchumi ukue mpaka mifukoni kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu mfumuko wa bei kila siku unapanda. Kwa mfano, mwaka jana sukari kilo moja ilikuwa ni kati ya Sh.1,500 mpaka Sh.1,800 lakini sasa hivi mfumuko wa bei umependa ni Sh.2,600. Ukienda kwenye petroli kwa sisi watumiaji wa vyombo vya moto bei haishuki inaendelea kupaa. Jana bei imepanda tena kwa hapa Dodoma ni takribani Sh.2,445, bei inapanda. Sasa tunapoambiwa uchumi umekuwa hata sisi Wabunge inatushangaza. Naomba hii mipango ya Serikali ifike mpaka kwa wananchi nao waone kwamba kweli uchumi umekua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nalotaka kuzungumzia ni kuhusu hili sual la mikopo na madeni. Kwenye kitabu humu imeandikwa kwamba kuna mikopo tuliyoipata kutoka nje takribani shilingi trilioni 7.05. Kati ya hizo kuna deni la ndani na la nje, deni la nje ni takribani shilingi trilioni 1.35, lakini deni la ndani ni karibu trilioni 5.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe katika madeni haya, maneno yale tunayosema kwamba deni ni himilivu kwa kweli tunawadhuru na kuwafilisi wazabuni wanatoa huduma mbalimbali kwa Serikali. Kuna watu wanadai mpaka miaka mitano hawajalipwa, wamepeleka huduma mbalimbali katika sekta mbalimbali za Serikali. Naomba katika mipango yetu hii tuwalipe. Wengine wanapelekwa Mahakamani, wengine mali zao zinapigwa minada hali ya kuwa wameihudumia Serikali yetu. Kwa hiyo, naishauri Serikali iwalipe, kwanza asilimia kubwa ni maskini, wana-tender tu hizo za Serikali lakini wanafanya kazi katika mazingira magumu walipwe madeni yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo kwenye kitabu alichotusomewa Waziri hapa iko ukurasa wa 12. Nianze na ufuaji wa umeme wa maji (hydro-electric power). Tunashukuru Serikali juhudi inazofanya kila siku miradi kuja lakini miradi mingine inakuwa inaishia njiani. Huu mradi wa Stiegler’s Gorge, naishauri Serikali na kuiomba kwamba iwekeze fedha huu mradi ukamilike isije ikawa kama ule mradi wa gesi wa Mtwara ambao umeanza mpaka umefikia mwisho tunaambiwa watumiaji wa gesi ni asilimia 6 tena ambayo ni TANESCO peke yake hali ya kuwa gesi ni kitu kinachohitajika sana katika shughuli mbalimbali duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nishauri Serikali mradi wa Stiegler’s Gorge ufanikiwe kwa asilimia 100 ili hii Tanzania ya viwanda tunayoisema viwanda bila umeme haviwezi kwenda. Tunaanzisha reli ya Standard Gauge ambayo itakuwa ni treni inayotumia umeme kama umeme wetu utakuwa sio wa uhakika iko siku treni itakujaishia katikati ya mbuga ya wanyama ya Mikumi na hapo sasa abiria wajiandae kuliwa na simba. (Makofi)

Mheshimiwe Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali tunapoanzisha miradi tuihakikishe inakamilika kwa asilimia
100. Nashauri umeme uwe wa uhakika ili wawekezaji wa viwanda watakapokuja wasiwe na matatizo ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine katika huu umeme, bei ya umeme Tanzania ni kubwa kuliko nchi zote. Haya siyo maneno yangu hata Mheshimiwa Rais aliwahi kusema hivi na akaiomba TANESCO ipunguze bei ya umeme kusudi wananchi wetu waweze kutumia umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nikupe mfano, Watanzania ndiyo tunaoongoza kwa matumizi ya kuni na mkaa chini ya Jangwa la Sahara. Unaposafiri kati ya mji mmoja kwenda mji mwingine ni Tanzania peke yake ndiyo utakuta pembeni kulia na kushoto mwa barabara kuna magunia ya mkaa na kuni. Tunataka tuondoe matumizi ya kuni na mkaa tutumie umeme na gesi ili tuweze kuokoa misitu yetu ambayo itatuletea mvua za uhakika na tuweze kupata umeme wa kutosha unaotokana na maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumzia ni suala la utalii. Kwenye utalii hapa naona kama tunafanya mchezo au tunafanya masihara kwa sababu haiingii akilini Tanzania tuna vivutio vingi sana vya utalii, tuna mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro, Mapango ya Amboni ya Tanga, Tongoni Ruins na mambo mengine ya kiutalii lakini hatutangazi, ndiyo tatizo letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana hapa ilipitishwa bajeti ya shilingi bilioni 2 kama sikosei, mmoja wa Wabunge akatoa mfano Kenya wenzetu wanatumia shilingi bilioni 70 kwa matangazo. Ukiangalia hata matangazo katika ligi za Ulaya katika viwanja vya mipira wenzetu wengine wanatangaza lakini sisi Tanzania kuna tangazo moja ambalo lipo katika EPL, ligi ya Uingereza. Kwa nini tusitangaze katika Bundesliga ya Ujerumani, La Liga ya Spain na katika maeneo mengine ambayo yanakusanya watu wengi ili tukaweza kuingiza watalii wengi ambapo sekta ya utalii ni chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali yote duniani kama utasimamiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali tutangaze utalii wetu, tuna vyanzo vingi vya utalii lakini hatuvifanyii kazi.

Kuna mbuga pekee ya Saadan lakini haitangazwi kama inavyotakiwa kutangazwa. Nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama kweli tunataka mapato kwenye utalii tutumie fedha nyingi sana kwenye matangazo, matangazo ya biashara ndio yanayovutia wateja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye uvuvi bahari kuu. Kazi yetu kubwa kama Serikali ni kuanzisha operesheni na operesheni ile ilikuja mpaka ndani ya Bunge samaki wakaja wakapimwa kwa rula hapa canteen lakini tumeacha meli kubwa zinazovua katika bahari kuu. Wavuvi wadogo wadogo wa kwenye maziwa na bahari tunakamatana nao, nyavu zinakamatwa zinachomwa, nyumba za wavuvi zinachomwa moto na mashua zao zinachomwa moto na kupigwa mashoka, lakini tunaacha meli kubwa zinazovua katika bahari kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano hai wa hili, miaka michache iliyopita palipatikana samaki wakawa wanaitwa samaki wa Magufuli. Sasa hebu fikiria ikiwa meli moja tu inaweza kuwa na tani 60,000 za samaki wakagaiwa magezani na taasisi mbalimbali za Serikali, je, meli zaidi ya 300 zinazovua sasa hivi tunavyozungumza kwenye bahari yetu na TRA hawachukui kodi hata shilingi moja tunapoteza kiasi gani? Kwa nini tuwakamate wavuvi wadogo hali ya kuwa kumbe bahari peke yake ni uchumi kama tutaisimamia vizuri itaweza kutuingizia mapato makubwa? (Makofi)

Mheshimiwe Mwenyekiti, kwenye Kamati yetu tumewahi kupata taarifa kwamba kuna shilingi bilioni 3 za feasibility study ambapo inatakiwa ikafanyike uchunguzi tu katika bahari kuu kuona tunawezaje kuwekeza kwenye bahari kuu tuweze kukusanya mapato. Kwa hiyo, naishauri Serikali kama tumeamua kufanya uvuvi katika bahari kuu tununue meli za uvuvi, ndege tulizonunua zimetosha sasa twende kwenye meli za uvuvi ili tuweze kukusanya mapato yanayotokana na bahari yetu. Japan, Singapore, Vietinum, Thaiwan na China ndiyo wanaonufaika na bahari yetu sisi wenyewe tunaenddelea kuwa maskini. Kwa hiyo, naishauri Serikali tununue meli za uvuvi tuanze kuvua katika bahari kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulisema ni suala zima la bandari. Katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 50 -51 limezungumzwa suala la bandari na reli kwamba kutakuwa na ujenzi wa bandari ya Mwambani Tanga. Mimi naishauri Serikali bandari ile ya Mwambani ijengwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zitengwe ili tuweze kujenga bandari ile ambayo nayo itakuwa ni kichocheo cha uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho siisahau barabara ya Pangani. Barabara ya Pangani nayo itatuokoa kwanza kuokoa muda wa usafiri lakini pia wakazi wa Tanga watatumia muda mfupi sasa kutoka Tanga hadi Dar es Salaam kwa sababu barabara ya Pangani ni njia ya shortcut.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nasema nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujaalia afya njema na kuweza kukutana kuzungumza mambo mbalimbali ya nchi yetu. Pili niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga Mjini ambao wameniwezesha nirudie mara kwa mara kuwa Mbunge wa kwanza wa Upinzani kufika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, vilevile pia niwashukuru wazazi wangu kwa namna walivyonilea mpaka nikakubalika.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, hebu ili taarifa zetu zikae vizuri, wewe ni Mbunge wa kwanza wa Upinzani, au Mbunge wa kwanza wa Upinzani kutokea Tanga? Ili taarifa zikae vizuri kwenye Taarifa zetu Rasmi za Bunge.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mbunge wa kwanza wa Upinzani katika Jiji la Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nianze kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nachangia katika bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nianze kwanza na suala la vijana. Vijana kuna usemi unaosema kwamba ni Taifa la kesho, lakini mimi niseme vijana ni Taifa la leo. Kwa nini nasema hivyo? Nina mifano ya kutoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi nyingi duniani katika masuala ya maendeleo, katika masuala labda ya michezo, katika masuala ya uzalishaji mali kwa mfano ajira viwandani, wanaoajiriwa kwanza ni vijana. Hata hapa tulipofikia leo sisi Tanzania, vijana ndio wanaokuwa ni nguvukazi, wana nguvu ya kufanya mambo ambayo yanaweza kuipeleka nchi mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, muda siyo mrefu tulizungumzia masuala ya vilabu vyetu, ukitazama kwa mfano Klabu ya Simba, vijana wale wa kikosi kipana cha Simba, ndio waliowezesha kuifanya Simba ifanye vizuri kuweza kuipiga JS Saoura, kuifuga AS Vita kuzifunga Al-Ahaly kwa sababu ni vijana wana nguvu. Pia kwa Taifa Star. Taifa Star wamefanya vizuri kuipiga Uganda bao tatu bila kwa sababu ni vijana wenye nguvu ambao wameandaliwa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nami naishauri Serikali yetu vijana tuwaandae vizuri ili tuweze kuwatumia katika nguvu kazi ya Taifa letu. Kwa mfano, leo Tanzania tuna maeneo mengi sana ya mapori ambayo hayajatumika, ajira zimekuwa zikikosekana. Kama Serikali itaweka mipango mizuri ya kuweza kuwatumia vijana, tukaweza kuwawezesha kwa vifaa, mitambo na mashine mbalimbali pamoja na mitambo hii ya irrigation, tunaweza kabisa kujizalishia chakula ambacho kitaweza kututosheleza nchi yetu na nchi jirani tutaweza kuwauzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa imekuwa kuna tatizo kidogo ambalo mimi naliona. Kwa mfano, kwenye masuala ya Kambi za JKT vijana zamani walikuwa wakimaliza Darasa la Saba asilimia kubwa wanapelekwa kwenye Kambi za JKT. Sasa hivi kuipata nafasi ya kuingia JKT imekuwa ni shughuli. Lazima pawe na mipango ya chini kwa chini, pawe na undugunaizesheni, pawe na ujamaa ndiyo mtu ataweza kuingia katika Kambi za JKT.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hili siyo sawa hata kidogo. Wale wengi ambao wanashindwa kufaulu mtihani wa Darasa la Saba, kwenda Form One, wale ambao wanashindwa kufaulu mtihani wa Form Four kwenda Form Five, Form Six, naamini kama tungewawekea mazingira mazuri, tukawapeleka katika Kambi zetu za JKT wakajifunza huko uashi, ufundi umeme, kilimo cha kisasa, mechanics na aina mbalimbali ya ufundi hata kuchomelea (welding) na mambo mengine, tungekuwa na jeshi kubwa la vijana ambalo lingeweza kuwa la uzalishaji mali. Sasa hivi imekuwa ni kinyume. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba tuiangalie upya taratibu za kujiunga na JKT.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, kwenye Sekta ya Walemavu; Tanzania tunao walemavu. Naishukuru Serikali kwamba angalau tunajitahidi sasa katika makusanyo ya kila Halmashauri, 2% ya kati ya zile 10% inakwenda kwa walemavu; 4% kwa akina mama, 4% kwa vijana. Hivi tukiulizana hapa Waheshimiwa Wabunge, ni kweli hizi fedha zinapelekwa huko kwa walemavu hizo 2%? Ni kweli zinapelekwa kwa vijana hiyo 4%? Kidogo angalau kwa akina mama, lakini kwa vijana bado. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba hizi asilimia za mapato, lazima Halmashauri tuzisimamie vizuri tuhakikishe kwamba hizi fedha zinakwenda; vijana na akina mama na walemavu wapatiwe hizi fedha. Kwa sababu kama watapatiwa hizi fedha, Watanzania wana upeo wa kuelewa mambo haraka. Kama watawezeshwa, wataweza kuzitumia vizuri, zitaweza kuwasaidia katika maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo walemavu wengine ambao ni mafundi viatu, wengine ni mafundi vyerahani tena wanawaajiri na wenzao, lakini mitaji wanakuwa hawana. Sasa niseme tu kwamba tuwawezeshe...

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mussa Mbarouk, kuna taarifa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Ahsante.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge wa Tanga kwamba Bunge lililopita ziligawiwa hapa Kamusi za Kiswahili na lugha sahihi ya kutumia hapa ni kwamba ni watu wenye ulemavu, sio watu lemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Ahsante. Naibu Waziri

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeipokea. Watu wenye ulemavu, sio walemavu, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niombe tuwasaidie hawa wenzetu kwa sababu, sisi tuliokuwa wazima hatukuwa na mipango na Mwenyezi Mungu kwamba tuwe wazima na wale wenzetu waliokuwa wenye ulemavu sio kwamba kuna kitu wamekosea. Kwa hiyo, tuwaangalie kwa jicho la huruma na tuwasaidie pale inapobidi kihalisia, siyo iwe kimaneno maneno tu, kwamba tukija humu tunaambiana maneno, lakini ukirudi huko unamkuta mlemavu anakwambia Mheshimiwa Mbunge kama ungenipatia mashine ya cherehani, ungenipatia na ngozi na uzi ningewaajiri vijana wenzangu hapa wenye ulemavu wanne, watano. Sasa tuwasaidie kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la wazee. Sote sisi hapa ni wazee watarajiwa lakini cha kushangaza, ukienda kwa wazee unaambiwa watatibiwa bure. Wameandaliwa vitambulisho, wamelipa shilingi elfu elfu lakini ama akienda hospitalini au kwenye Kituo cha Afya, ataishia kuandikiwa tu dawa aambiwe hizi kanunue. Mzee huyu kipato chake kimeshakuwa kidogo kwa sababu hizo pensheni zenyewe pia wanazopewa hapewi moja kwa moja hiyo shilingi 66,000/= analimbikiziwa baada ya miezi mitatu ndiyo apewe. Kwa hiyo, hana uwezo hata wa kununua ile dawa anayoandikiwa. Niseme, hawa wazee kama tumeamua watibiwe bure, akina mama wajawazito na watoto basi iwe wakienda wanapata dawa zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC tumekwenda kutembelea bohari la madawa MSD Dar es Salaam, tumekuta kuna madawa mengi mpaka yanafikia ku-expire kwa sababu hayafikishwi kule kunakohitajika. Tulipowahoji wataalam wetu, wanasema Madaktari wa Wilaya, na wa mikoa dawa nyingine hawaziombi. Kwa mfano, dawa za nyoka, dawa za mambo mengine, sukari na nini haziombwi, kwa hiyo, zinakaa mpaka zina- expire. Tungezipeleka kule ili hawa wazee na akina mama na watoto wanaotakiwa kutibiwa bure, zi-expire huko huko kwenye Vituo vya Afya sio zi expire pale MSD. Kwa hiyo, nasema wazee wetu watibiwe bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta amekwenda labda mzee, mwanamke ana cheni ya dhahabu. Daktari anamwambia ah, wewe unataka kutibiwa bure, mbona una cheni ya dhahabu? Sasa kwani cheni ya dhahabu ni dhambi? Si Sera ya Taifa kwamba wazee watibiwe bure? Ama amekwenda na gari, au amekwenda na taxi, sera inasema atibiwe bure.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Taarifa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, lingine niende kwenye hali ya kiuchumi. Kwenye kitabu cha Waziri Mkuu ukurasa wa 11.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mussa Mbarouk, kuna taarifa. Sasa kengele ya pili imeshagonga. Nitakuongezea dakika moja ili umalizie.

Mheshimiwa Ummy, Taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Mussa Mbarouk kwamba, sera kuhusu matibabu bure kwa wazee ni kwa wazee wasio nauwezo na sio kila mzee anatakiwa kupata matibabu bure, ni mzee asiye na uwezo. Niliona nitoe taarifa hiyo.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mussa Mbarouk unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MUSSA MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenda suala la kiuchumi, pato la Taifa limekuwa kwa 6.7% mwaka 2018 na 6.2% kwa mwaka 2017, lakini niseme linakuwa katika makaratasi lakini kihalisia ukiwatazama watanzania huko nje wako hoi bin taabani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya njema na kuweza kuwepo hapa tukaendelea na shughuli zetu za Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pia niwapongeze wananchi kwa namna walivyojitokeza kujiandikisha katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na kwamba baadaye hili zoezi lilikuja kuvurugwa, nitazungumza hapo mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Wizara ya Kilimo. Mara nyingi Watazania tumekuwa tukisema kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu lakini tumekuwa tunasema kwa nadharia siyo kwa vitendo. Kwa nini nasema hivyo? Kilimo cha Tanzania kimekuwa katika misamiati ya kisiasa, tumeanza na Kilimo cha Ushirika, Kilimo cha Bega kwa Bega, Kilimo cha Kufa na Kupona, Kilimo Kwanza na kadhalika lakini ukikitazama kilimo chenyewe kimekuwa kila siku kinarudi chini badala ya kwenda juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatokana na nini? Kwenye bajeti ya kilimo fedha zilizotengwa, kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017 zilitengwa shilingi bilioni 100.52 lakini mpaka Machi 2017, fedha iliyotolewa ilikuwa ni bilioni 2.25 tu ambayo ni sawasawa na asilimia 2.2 kwa maana ya kwamba asilimia 98 haikutekelezwa. Je, hapo tunaweza kusema kwamba tuko serious na kilimo kweli! Jibu ni kwamba hatuko serious.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukiangalia kwenye mwaka 2017/2018, tulitenga shilingi bilioni 150.235 lakini mpaka mwezi Machi, 2018, fedha iliyotoka ni shilingi bilioni 16.52, ambayo ni sawasawa na asilimia 11, ina maana asilimia 89 haikutekelezwa. Hatuishii hapa, hata kwenye mwaka 2018/ 2019, tulitenga shilingi bilioni 98.119 lakini mpaka mwezi Machi ikapokelewa shilingi bilioni 41.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa napata tabu kidogo kuona kwa nini tunatenga bajeti ambazo hatuwezi kuzitekeleza. Badala ya kuweka shilingi bilioni 100 basi angalau tungeweka shilingi bilioni 50 halafu tukipeleka shilingi bilioni 39 au 40 tunakuwa tumeweza kufikia angalau asilimia 50 lakini hili jambo limekuwa ni la kila mwaka. Wakati mwingine ndiyo tutazidi kusema bajeti zetu zinakuwa ni kama vile za copy and paste kwamba tunapeleka hivyo hivyo tu. Yanatokea matatizo lakini haturudi nyuma kujiuliza kwa nini hatukufikia asilimia hii ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukienda kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mwaka 2016/2017 ilitengwa bajeti ya shilingi bilioni 4, lakini mpaka mwezi Machi, 2017 zilimepelekwa Wizarani shilingi milioni 130 ambayo ni sawasawa na asilimia 3.25. Mwaka uliofuata 2017/2018, bajeti ilikuwa ni shilingi bilioni 4 kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi lakini mpaka mwezi Machi, 2018 haijapelekwa hata senti 10! Sasa hapa tunakwendaje? Hii mipango tunayoipanga halafu haitekelezeki inakuwaje? Ndiyo ile if you fail to plan, you plan to fail.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niseme tu tutayarishe au tuandae mipango ambayo inatekelezeka. Wananchi wetu sasa hivi wanafuatilia na wanaona katika nchi za wenzetu mipango wanavyoipanga na wanaona na sisi jinsi tunavyopanga mipango yetu ambayo haitekelezeki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wa Tanzania wanajitahidi sana kwenye kilimo. Pamoja na hiyo misamiati inayosemwa kuna kama asilimia 10 ambao wanalima kilimo cha kisasa kutumia matrekta na dawa na kadhalika. Kuna kama asilimia 30 wanaolima kutumia wanyama kazi kwa maana ya mifugo hii na plau lakini asilimia 60 ni wakulima wa jembe la mkono ambao hawa ndiyo haohao wakulima wanaolima mbaazi, korosho, njugumawe na mhogo ambapo mwisho wake kwenye mavuno wananchi wanakuwa hawana masoko, tunawakatisha tamaa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuelewe kwamba tunapopanga hii mipango tujue kwamba tunawapaingia mipango wananchi ambao wanasikiliza Serikali yao inawapangia nini ili waweze kutekeleza. Tukumbuke kwamba hawahawa wakulima ambao tunawakwamisha kwenye masoko ndiyo hawahawa ambao wanasomesha watoto vyuo vikuu na English Medium Schools, tunapowakwamisha kwenye masoko ndiyo hapohapo sasa wanafunzi wanapobaki nyumbani kwa sababu wazazi wanakuwa hawakuuza mazao, hawana fedha, hawawezi kulipa ada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi mwishoni mwa wiki nilirudi Tanga, amekuja kijana na mzazi wake ananiambia Mheshimiwa sisi tuna shamba letu la mihogo Kirare, Kirare ni Kata moja Tanga ambayo ni mashuhuri kwa kilimo cha mhogo, wanasema lakini mhogo kawaida miezi sita unavuna kama kuna soko, sasa tuna mhogo una miezi nane haujavunwa, hatuna soko, carry nzima ya mhogo unauza Sh.60,000. Matokeo yake mzazi yule ana watoto wawili wamefaulu, mmoja anatakiwa aende chuo Mbeya mwingine Iringa, mzazi hana fedha, mazao ambayo ni mhogo yako shambani, afanye nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, inabidi tuhangaike sasa kutafuta wafadhili, mfadhili wa kumsaidia mtoto kusoma itategemea na anavyojisikia na anavyojua umuhimu wa elimu. Je, kama mhogo ungekuwa na soko la uhakika kwa nini mzazi yule asingeenda kukopa hata benki kwa dharura halafu akatumia fedha ile kuwalipia watoto wake ada? Huu ni ushahidi kwamba Serikali tunasema maneno mengi sana, tunaandika sana, lakini ukirudi kwa wananchi hali zao ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, hii mipango ambayo kila mwaka tunaitayarisha, tunaitangaza, tunaipitisha halafu haitekelezeki, inawakatisha tamaa wananchi. Matokeo yake sasa wakati mwingine mtu anaona bora aachane na shughuli za kilimo. Akienda kwenye biashara nako anakutana na kodi kubwa huko biashara inamshinda, duka anafunga, hajui afanye nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine wengine wanafikia hata kujinyonga, maana yake mtu anadaiwa school fees za watoto, ana biashara kwenye frame anadaiwa, ana gari huku labda bovu, huku ana watoto wengine wanasoma shule za msingi, huku anadaiwa bili za umeme na maji, afanye nini? Inafika mtu anachukua maamuzi magumu ya kufikia kujinyonga, maisha yamekuwa magumu kila kukicha. Waheshimiwa Wabunge wenzangu ukitaka kujua kama maisha magumu turudini mitaani hali ni mbaya sana, milo mitatu tuliyoizoea hailiki sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu sasa hivi wanakunywa cha saa tano asubuhi, chakula cha mchana kinaliwa saa kumi na moja, ndiyo imetoka watu wameua winga mpaka siku ya pili. Kwa nini Tanzania ambayo ina rasilimali nyingi, Mwenyezi Mungu ametujalia bahari, madini ya aina zote (tanzanite, almasi, dhahabu mpaka uranium), kwa nini Watanzania washindwe hata kula milo mitatu kwa siku? Ni kwa sababu mipango yetu tunaipanga vizuri kwenye makaratasi lakini kwenye utekelezaji inakuwa ni asilimia chache sana. Kwa hiyo, naomba tubadilike Mheshimiwa Waziri tunapopanga mipango basi mipango hiyo itekelezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nije kwenye masuala ya mipango ya uchukuzi, nagusa Kitengo cha Bandari. Watanzania tuna Bandari kubwa ya Dar es Salaam lakini tusisahau tuna bandari nyingine kama Tanga, Mtwara na Zanzibar. Mimi nitazngumzia huu upande wa Bara kwa sababu Zanzibar angalau inafanya kazi vizuri inachukua mizigo yote ya Unguja na Pemba lakini Tanzania Bara mizigo yote tunaisukumiza Dar es Salaam, matokeo yake sasa Bandari ya Dar Salaam imezidiwa, makontena na meli ni nyingi, zinashindwa kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwenye hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nishukuru baadhi ya kilio changu kusikilizwa na Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Bandari ya Tanga sasa ipo meli pale inayoongeza kina (inachimba) na vilevile pia tumepata vifaa vipya, kama ile crane ya forty, fifty containers imepatikana na nyingine ndogondogo lakini kama cranes zile tumepeleka na kina kinaongezwa halafu hakuna meli za mizigo zinazokwenda, faida ya kutumia fedha zote hizo takribani shilingi bilioni tatu na milioni mia saba Mheshimiwa Waziri umetenga kwa mwaka huu wa fedha itakuwa ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari ni lango kuu la biashara duniani. Nashauri tufanye categories za mizigo, bandari ya Dar es Salaam ichukue mizigo ya Dar es Salaam yenyewe, Pwani na Morogoro lakini Bandari ya Tanga ichukue mizigo ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Msoma na Bukoba na nchi za jirani kama vile Rwanda na Burundi mizigo yao ipitie kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye Bandari ya Mtwara, tunayo Mtwara Corridor, kwa nini Bandari ya Mtwara basi isichukue mizigo ya Mtwara yenyewe, Lindi, Mbeya, Sumbawanga, Katavi, Kigoma, Zambia na Malawi. Hapo tutakuwa tumezitendea haki bandari zetu lakini Bandari ya Dar es Salaam tumeibebesha mizigo yote, bandari nyingine kama Tanga ukienda sasa hivi watu wanacheza draft. Hivi kweli bandarini unaweza ukacheza draft au karata?

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani tunaambiwa na wazee wetu linapitishwa tangazo kwamba jamani vijana wa mjini kuna kazi bandarini, meli ya Spain, Ujerumani, China na German zote zimekuja kwa wakati mmoja zinahitaji vibarua wakafanye kazi lakini leo unaweza ukakaa kwa mwezi zinakuja meli mbili au moja, matokeo yake tunawekeza fedha nyingi kwenye bandari zetu lakini mizigo inayoingia na kutoka haipiti katika bandari zetu. Kwa hiyo, nashauri Serikali tufanye categories za mizigo, bandari zetu zote ziwe zinafanya kazi, tushindane na nchi jirani ya Kenya ambayo imekuwa kimbilio la wafanyabiashara wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie kuzungumzia suala la demokrasia.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante lakini ujumbe umefika.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya njema na uhai tukaweza kukutana hapa tukaweza kuzungumza mambo mbalimbali yanayohusu Bunge letu na nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwanza kwenye suala zima la bajeti, bajeti ni makadirio ya mapato na matumizi kwa Serikali au taasisi yoyote ile kwa mwaka au kwa mwezi au vyovyote vile viwavyo. Mara nyingi tumekuwa tunapitisha bajeti ambazo hazitekelezeki, tunapitisha bajeti lakini kwenye upelekaji wa fedha sasa inakuwa kiwango kilichohitajika katika bajeti hizo hakitekelezeki. Vilevile pia, kumekuwa na ucheleweshaji wa fedha katika miradi, kwa mfano miradi inayosimamiwa na halmashauri fedha unakuta inapelekwa katika robo ya mwisho ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake sasa zikifika katika halmashauri kwa sababu wanaogopa usije mwaka wa fedha ukaisha fedha ile ikarudi Hazina, matokeo yake inapitishwa miradi ya haraka haraka, miradi inakuwa iko chini ya kiwango, miradi haikaguliwi ipasavyo na matokeo yake sasa fedha zile zinakuwa kama tumekwenda kuzitupa. Nashauri Serikali ipeleke fedha mapema pale ambapo imekusudia kupeleka fedha za miradi katika halmashauri zetu na miradi yoyote ile ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni katika halmashauri kuzipora nazo vyanzo vya mapato. Kwa mtazamo wangu naona kama vile Serikali Kuu sasa imeamua kuziua Serikali za Mitaa kwa sababu hapa mwanzo tulichukua property tax ikapelekwa TRA lakini baadaye tena ilipokuja TARURA tukaambiwa parking, mabango na bus stands na mapato mengine yote yanapelekwa TARURA. Ukipatazama hapa TARURA imepewa mamlaka ya kukusanya mapato lakini taa za barabarani, usafishaji wa mifereji bado uko kule kule kwenye halmashauri. Halmashauri watapata wapi fedha ya kununua luku au ya kulipia umeme wa taa za barabarani? Nasema hapa tunaziua Serikali za Mitaa (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nashauri, hebu tuziache vile vyanzo vilivyobaki navyo sasa tuache halmashauri iendelee kukusanya mapato. Tumekuwa tukiwang’ang’ania kwamba nyingine zinakuwa zinakusanya chini ya kiwango na kwa mfano jana hapa wakati tulipokuwa tunapitisha taarifa za PAC na LAAC imefika mahali kwamba halmashauri zitakazoshindwa kukusanya mapato kwenye uvuvi inaambiwa waziri atazipoka mamlaka ya kukusanya mapato hayo. Sasa tujiulize halmashauri zitapelekwa vipi! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasemaji wengi waliozungumza wamesema mpaka madiwani sasa wanakaa vikao bila kulipwa posho zao za mwezi wala hizi sitting au posho zao za vikao. Nasema halmashauri kama tumeamua kuziua tuseme wazi, tuweke wazi yaani tusifichefiche kwa sababu hizi halmashauri ndiyo Local Government, ndiyo Serikali za wenyeji, ndiyo zinazofikia kero zaidi za wananchi kuliko Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo zinazojenga madarasa, ndiyo zinazojenga barabara, ndiyo zilikuwa zinajenga labda shule, mifereji, maji taka na kadhalika lakini tunapora kila uchwao. Nina wasiwasi ipo siku tutakuja kuchukua vyanzo vyote tuwaambie wajitegemee watafute vyanzo vingine au wananchi tuwachangishe sasa kama vile kodi ya kichwa, hii itakuwa siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri hapa halmashauri ikibidi tuzipelekee fedha kwa wakati lakini pia miradi ambayo wameikusudia kuitekeleza ipelekwe fedha ambayo inatosha tusipeleke fedha pungufu. Tunapopeleka fedha pungufu miradi inakuwa imedumaa, utakuta majengo yamekaa muda mrefu hayaezekwi, zahanati zimekaa muda mrefu hazifanyi kazi, kwa hiyo, hapa nilikuwa nashauri fedha zipelekwe kwa mpango maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kusema ilikuwa ni kwenye suala zima hili la kodi kubwa kuwaua wafanyabiashara au kukimbiza wawekezaji. Nchi yetu tunasema tunataka Tanzania ya viwanda lakini ukitazama. Kwa maoni yangu naona kama tunasema hapa mdomoni tu. Hao wawekezaji wanapokuja katika nchi yetu adha wanayoipata wengine wamekuwa wanahama wanakimbilia nchi jirani. Ipo mifano mingi kwa mfano katika Jiji letu la Tanga tulikuwa na mwekezaji pale ana kiwanda cha kusaga unga wa ngano kinaitwa Pembe, Pembe Wet Flower Mill Co. Ltd. Ile iliajiri zaidi ya vijana 1000 pale Tanga lakini cha kushangaza sasa hivi imefungwa tangu mwaka jana mwezi wa tano kwa sababu ya kodi kubwa wanayotozwa na TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walikuwa na kiwanda tanzu cha kutengeneza vifungashio au visalfet inaitwa Bajeber Packaging Co. Ltd, nao pia wametozwa kodi kubwa wote kwa pamoja wamefunga viwanda, vijana wamekosa ajira sasa hivi ndiyo nasikia kama Tanga mmekuwa mkisikia kuna watoto wa ibilisi. Ni walewale vijana waliokuwa wakifanya kazi Pembe, wakifanya kazi CIC, wakifanya kazi viwanda vingine ambavyo vimefungwa hawana kipato, anategemewa na familia yake, anategemewa na wazazi wake, yeye mwenyewe anataka kutumia hana fedha matokeo yake wamejiita jina la ibilisi. Watoto wa ibilisi wamekuwa wanapora simu, wanawavizia akinamama wanapokwenda kwenye sherehe za harusi simu zinakwenda, cheni za dhahabu, viatu, fedha, vitu vyote wananyang’anya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kama kweli tumekusudia kuwa Tanzania ya viwanda, wawekezaji wanapokuja tuwanyenyekee, tuwape ushirikiano tuwapunguzie kodi ili waendeshe shughuli za kibiashara, walipe kodi ya Serikali lakini pia waajiri vijana wetu. Kama itakuwa mpango ni huu ni sawasawa na kumkamua ng’ombe maziwa bila ya kumpa malisho matokeo yake sasa maziwa yakiisha tutakuwa tunakamua damu. Tunajisifu tu kwamba TRA wamekusanya sasa hivi trilioni 1.9 kwa mwezi, ni jambo zuri lakini tunajua hii 1.9 trillion inavyopatikana. Leo Dar es Salaam katikati ya Jiji Kariakoo ukitaka fremu pia unapata kwa sababu kodi zimekuwa ni kubwa wafanya biashara wameshindwa wanakimbilia nchi jrani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, hata wafanyabiashara wa malori sasa taarifa tulizonazo ni kwamba wengine malori yao wameyahamisha Tanzania wameyapeleka Kenya, wengine wamekwenda kuyasajili Zambia, wengine wamekwenda kusajili Burundi, wengine wamekenda kusajili Malawi kwa sababu kodi tunazowatoza ni kubwa na tuna utaratibu ambao haupo dunia nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo dereva wa lori pia aambiwa awe EFD mashine, kwamba akipeleka mzigo wa cement labda Mwanza au Arusha akirudi akipakia hata magunia mawili au matenga kumi ya nyanya lazima alipe kwenye EFD. Wakati gari ikiharibika anatakiwa alizibe pancha, alipe njiani, alipe ma-tan boy na kadhalika, sasa wanaona imekuwa ni adha kubwa. Niseme baada ya kuhamisha usajili Tanzania wakapeleka nchi nyingine mapato yanaingia katika nchi hizo, naomba hapa Serikali ipaangalie upya, hebu tupunguze baadhi ya masharti kusudi tukaribishe kweli wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kulisema, kuna matumizi mabaya ya fedha za Serikali na vilevile pia, hii inatokana na kutofata demokrasia ambayo ni ya vyama vingi kama ilivyokusudiwa. Labda hapo nitoe mfano, kwenye jiji letu la Tanga kuna madiwani wamerudi kwenye Chama Cha Mapinduzi, ninavyojua na ndiyo utaratibu, kanuni na sheria ilivyo kwamba kiongozi wa kisiasa akihama chama kimoja kwenda chama kingine amepoteza sifa ya kuwa na nafsi hiyo aliyoitumia. Sasa inakuwa madiwani hawa wameshahama kutoka CUF wamehamia CCM wanaingia kwenye vikao vya Kamati ya Fedha, wanaingia kwenye Baraza la Madiwani na wanalipwa posho za vikao na fedha ya mwisho wa mwezi. Haya ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbarouk ahsante sana.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iliangalie jambo hili kwa makini kwa sababu huu mchezo ukiendelea itakuwa sasa kama sheria na kanuni tulizozitunga na kuapa kuziheshimu na kuzitekeleza hazina maana yoyote. Ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Naomba nichangie kwa maandishi katika Mpango wa 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, mizigo kupungua Bandari ya Dar es Salaam; mizigo imepungua kutokana na urasimu au wizi wa mizigo ya wafanyabiashara na kodi kubwa kuliko thamani ya mizigo tofauti na bandari ya Mombasa - Kenya; Beira Port - Mozambique; Durban Cape town na Port Elizabeth za Afrika ya Kusini. Bandari nne za Tanzania ni sawa na mapato ya bandari ya Mombasa, Kenya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri; Mamlaka ya Bandari (TPA) isifanye kazi kimazoea (business as usual) ifanye kazi kiushindani, iondoe urasimu katika utoaji mizigo; mizigo iweze kutolewa katika muda mfupi (min – 24 hours – max 72 hours).
Mheshimiwa Naibu Spika, ili bandari zote za Tanzania zifanye kazi kwa viwango vinavyokusudiwa, mizigo ifanyiwe classification. Aina ya mizigo ya Mikoa; Kanda ya Kaskazini- Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mara, Mwanza na Kagera, mizigo ishushe katika bandari ya Tanga. Mizigo ya Mikoa ya Kanda ya Kati- Dodoma, Morogoro, Dar es Salaam, Tabora, Singida, Shinyanga na Kigoma, mizigo ishushwe katika Bandari ya Dar es Salaam; meli nyingi zinatumia muda mrefu katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, mizigo ya Mikoa ya Kanda ya Kusini (Southern Regions) Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Rukwa, na Katavi, mizigo ishushwe katika bandari ya Mtwara. Hii iangalie pia shehena ya mizigo ya Kimataifa na izingatie hali ya kijiografia (Geographical Conditions). Mfano, mizigo ya Burundi, Rwanda, Uganda na Sudan Kusini ishushwe bandari ya Tanga na mizigo ya Malawi, Zambia na Congo, ishushwe bandari ya Mtwara na Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, inatia huzuni kuona au kusikia kuwa katika Bank Economic and Investment Report kuwa, katika nchi 140, Tanzania inashika nafasi ya 120 huku tukiwa na rasilimali na malighafi nyingi tofauti na nchi nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, TRA na Mapato; pamoja na taarifa ya ukusanyaji mkubwa wa mapato unaofanywa na TRA, lakini wafanyabiashara wanakamuliwa sana, wanafanyiwa makisio (assessment) makubwa kuliko faida inayopatikana katika biashara zao. Matokeo yake, wafanyabiashara wengi wanafunga biashara zao au viwanda vyao. Wengine wanadiriki kuhamia nchi jirani za Burundi, Rwanda, Mozambique, Uganda, Kenya na Sudan Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati TRA inaongeza mapato ya Serikali, lakini inaua biashara na kuzorotesha uchumi wa nchi yetu. TRA inakamua ngo‟mbe maziwa hadi anatoa damu bado TRA inakamua tu! Nashauri TRA ifanye utafiti na uchambuzi ili ijue kwa nini wafanyabiashara wanailalamikia TRA na ikibidi itumie Demand Law System.
Mheshimiwa Naibu Spika, Third Law of Demand; in the high price low demand and in the low price high demands. Maana yake, kodi ikiwa kubwa walipaji watakuwa kidogo na kodi ikiwa ndogo walipaji watakuwa wengi. Wahindi wanasema, „dododogo bili shinda kubwa moja‟.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupeleka property tax kukusanywa na TRA ni kuzuia Halmashauri zetu nchini. Je, Mheshimiwa Waziri Mpango, Serikali imeamua kuziua Halmashauri kwa kuwa vyanzo vyake vikuu vyote vinatwaliwa na TRA? Tanga City Council imenyang‟anywa hadi nyumba za kupangisha! Naomba Serikali irudishe property tax itwaliwe na Halmashauri zetu. Tanga City Council irudishiwe nyumba zake na kupangisha. Zipo Serikali za aina mbili, Central Government and Local Government hivyo, tusizinyong‟onyeze Local Government.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ya Viwanda; viwanda vinahitaji umeme wa uhakika, vingi vimekufa au kuuzwa na Serikali. Ushauri; Serikali ifufue viwanda vilivyokufa kwa kuweka mitambo mipya. Mfano, Steel Rolling Mills, Sikh Saw Mill, Kamba Ngomeni na kadhalika katika Mkoa wa Tanga; General Tyres - Arusha; na Kiwanda cha Nyuzi, Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kilimo, Mifugo, Michezo na Uvuvi vyote vinahitaji kuboreshwa na kutekelezwa kwa vitendo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunijaalia afya njema na kuweza kuchangia Wizara hii. Pia nawatakia Watanzania Ramadhani Kareem. Naunga mkono hotuba/ maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuchangia kwa kuipongeza Wizara kwa kupata hati safi za ukaguzi wa mahesabu kasoro Ofisi moja tu ya Ubalozi wa Tanzania nje ya nchi. Ni vema wakati Waziri akifanya winding up aitaje ofisi hiyo ni ya Ubalozi wa Tanzania iliyo katika nchi gani na hatua gani zimechukuliwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kutaka Serikali yetu kusaidia Watanzania wanaoishi na kufanya kazi nchi za nje (diasporas) kupata haki na stahili zao, kuondoa manyanyaso kwa Watanzania lakini pia wabaki na passport zao katika baadhi ya nchi ambazo Watanzania wananyang’anywa passport zao na Serikali za nchi hizo. Kwa ufahamu wangu passport ni document halali inayotakiwa kumilikiwa na raia wa nchi husika. Je, inakuwaje katika baadhi ya nchi duniani Watanzania wakiajiriwa wanaporwa passport zao na Serikali za nchi hizo wanazofanya kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu demokrasia na haki za binadamu, kufuatia uchaguzi wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015 ambapo matokeo yake yalibatilishwa kimazingaombwe hali iliyopelekea uchaguzi ule kurudiwa na Chama cha CUF na vyama vingine vya mageuzi kuususia na kuleta sintofahamu kwa wananchi, taarifa za International Observers nazo ziliweka wazi kuwa mshindi katika Uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015 alikuwa ni mgombea wa chama cha CUF, Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sakata hili imepelekea Taasisi ya MCC (USA) imefunga ofisi zake na kusitisha kutoa shilingi trilioni 1.06. Je, fedha hizi shilingi trilioni 1.06 sawa na US$ milioni 472.8 zingeendesha miradi mingapi ya maendeleo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kama ifuatavyo:-

(i) Waziri aeleze kuna mikakati gani ya kufanya mazungumzo ya kutatua jambo hili ili MCC irudishe ofisi dar es Salaam na tuweze kurejeshewa shilingi trilioni 1.06 ambayo ni sawa na US$ milioni 472.8.

(ii) Je, hatutafanya makosa ya kuwekewa vikwazo vya kiuchumi kimataifa kwa kukandamiza demokrasia? Naomba Waziri afafanue.

(iii) Serikali ianzishe utaratibu Watanzania wanaoishi nje na kufanya kazi (diasporas) waruhusiwe kupiga kura wakati wa Uchaguzi Mkuu kama zinavyofanya nchi nyingine duniani.

(iv) Kuna nchi tulizopewa viwanja, majengo na rasilimali nyingine na tumeshindwa kuvijenga (Oman na Mozambique) lakini pia katika ofisi 35 baadhi ya majengo yamechakaa sana, zifanyiwe ukarabati.

(v) Mabaharia wa Tanzania waliosomea katika Chuo cha Bandari - Temeke Dar es Salaam wanasumbuliwa kuwa vyeti vyao havitambuliki kimataifa. Serikali ichukue hatua zinazostahili ili vyeti vya chuo hiki vitambulike kimataifa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami kwanza nichukue fursa hii kushukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia na nitaanza na TAMISEMI. Kwa mujibu wa taratibu zilizopo Serikali zipo za aina mbili, kuna Central Government na Local Government, lakini sasa kuna kitu au utaratibu ambao umeanzishwa wa kuondoa makusanyo ya property tax ambacho kilikuwa ni chanzo cha mapato katika Halmashauri zetu tumekipeleka katika Serikali Kuu kwa kukusanywa na TRA. Naona hili ni kama kuzizika Serikali za Mitaa, kwa hiyo nakumbusha kwamba Serikali za Mitaa ndizo zinazoziba aibu ya Serikali Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na miradi mingi ambayo inatekelezwa na Serikali za Mitaa, kwa mfano uchongaji wa barabara za vijijini, miradi ya maji vijijini, pamoja na kwamba inapelekewa fedha na Serikali Kuu lakini bado wenye mamlaka ya kusimamia ni Serikali za Mitaa. Sasa kuzinyang‟anya Serikali za Mitaa chanzo hiki cha property tax ni kuziua Serikali hizo. Kwa hiyo, nashauri kwamba ikibidi property tax irudishwe katika Serikali za Mitaa kama kweli tunataka miradi ya wananchi inayofika moja kwa moja katika Halmashauri zetu iweze kusimamiwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala zima la mapato, leo ukienda kwenye Halmashauri zote zipo hoi kimapato, baada ya kunyang‟anywa chanzo kile zimekuwa kama zimechanganyikiwa, zimekuwa zikitegemea tu kupata ruzuku kutoka Serikali Kuu ambayo nayo inacheleweshwa, inaletwa katika robo ya mwisho ya Mwaka wa Fedha wa Serikali, matokeo yake sasa inafanywa miradi kwa kukurupuka, miradi mingi inakuwa chini ya viwango na hapohapo pia ndipo watu wanapopiga „dili‟. Nashauri bado tuzitazame sana Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tukumbuke pia Serikali za Mitaa kama alivyotangulia kusema mmoja imekuwa ni kama jalala, mizigo yote imesukumwa kwenye Serikali za Mitaa; elimu ya msingi na sekondari zinasimamiwa na Serikali za Mitaa, miradi ya maji vijijini inasimamiwa na Serikali za Mitaa na miradi mingine ya afya bado inasimamiwa na Serikali za Mitaa. Hata hivyo, tukija kwenye elimu kwa mfano, elimu kwa mujibu wa utaratibu siyo biashara ni huduma, lakini kuna utaratibu ambao umeanzishwa tena wa kukusanya mapato kutoka kwenye hizi English Medium Schools, matokeo yake sasa wamiliki wa shule nao kwa kuwa wanatozwa fedha nyingi, wanaongeza ada matokeo yake wananchi au wazazi wanashindwa kuwapeleka watoto katika hizi shule za English Medium. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, ikibidi tuondoe hii tozo ya kodi katika hizi shule za English Medium, vilevile pia hata kwenye sekondari. Tunasema hapa elimu bure lakini ukiangalia, kwa mfano katika sekondari kumesamehewa sh. 20,000 tu ya ada, vikorombwezo vyote bado mzazi anatakiwa kulipia, tena baya zaidi kunatakiwa counter books, counter book moja sh. 5,000 mtoto anatakiwa atumie zaidi ya counter books 12, hapohapo tena kuna nguo za michezo, kuna uniform, viatu pair mbili, majembe, tumewasaidia tu kuondoa hilo suala la madawati baada ya fedha iliyobaki katika Bunge kuingiza fedha hiyo kwenye madawati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Halmashauri napo labda nimpongeze tu Mheshimiwa Rais kwa hili suala la kumaliza tatizo la madawati lakini bado elimu bure siyo bure. Katika baadhi ya shule wanashindwa hata kulipa walinzi, wanashindwa hata kulipa maji, wanashindwa hata kulipa umeme! Hebu fikiria watoto wanashinda kutwa nzima lakini maji yamekatwa, yote hii inatokana na kutamka kwamba elimu itakuwa bure lakini siyo bure kwa asilimia mia moja. Nashauri Serikali kama tumeamua elimu iwe bure basi iwe bure kwelikweli kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kingine pia naishauri Serikali, TAMISEMI haina uwezo wa kulipia maji na umeme katika shule zetu za sekondari, sasa ikibidi shule za sekondari, shule za msingi, taasisi za kidini kama makanisa na misikiti, hili naona pia tungeondoa kabisa hilo suala la kuzichaji masuala ya bili ya umeme na maji tusiwe tumependelea, ili taasisi na shule hizi ziwe zinatumia maji pasipo malipo, tutasaidia kupunguza mzigo kwa wazazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni kawaida kwamba hata inapotokea kukiwa na majanga tunatumia viongozi wetu wa kidini kumwomba Mwenyezi Mungu aisalimishe nchi yetu na majanga na matatizo mengine sasa je, tunasaidiaje taasisi za kidini. Nashauri kupitia shule za msingi na sekondari pamoja na taasisi za kidini hizi tuondoe haya masuala ya malipo ya maji na umeme ili kama tunasema elimu bure iwe elimu bure kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika elimu natoa ushauri hata shule za private za sekondari tumekuwa tunawatoza kodi kubwa sana, matokeo yake na wao wanaongeza school fees ambayo imekuwa sasa ni kilio kwa wananchi. Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakuwa ni mashahidi, kila Mbunge hapa ana orodha ya watoto siyo chini ya 20, wote wamefaulu wazazi hawana uwezo unatakiwa Mbunge uchangie, utachangia watu wangapi? Naishauri Serikali elimu iwe bure kama katika baadhi ya nchi za wenzetu, wenzetu wanawezaje sisi tushindwe, upo usemi unaosema wao waweze wana nini, sisi tushindwe tuna nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala zima la Katiba na Sheria; mimi niliipitia taarifa hii lakini kuna baadhi ya maeneo naomba yafanyiwe marekebisho kidogo, kwa mfano, Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakuwa mashahidi, sote katika Wilaya zetu kuna Magereza, ukiwa ni mwenyeji wa kutembelea Magereza utakuta kuna akinamama ambao wana watoto wachanga wananyonyesha. Mama ndiye amefanya kosa labda ameiba, labda amefanya kosa lingine huko ametiwa hatiani, lakini mtoto mchanga anayenyonyeshwa ambaye hawezi kuishi bila mama yake inabidi naye ageuke mfungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naishauri Serikali, kwa wale akinamama ambao wengine ni wajawazito wanajifungulia kule gerezani, lakini na kwa wale akinamama wote ambao watakuwa wana watoto wachanga, hawa watoto dini zote zinaamini kwamba mtoto mdogo kuanzia miaka 14 kuja chini ni malaika, kwa nini tumtese malaika huyu akae gerezani hali ya kuwa yeye hakufanya kosa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, kama mama ana mtoto mchanga basi ama asamehewe apewe kifungo kile cha kufanya kazi za kijamii kama kusafisha hospitali, ofisi ya Mkuu wa Mkoa au Mahakama, lakini kitendo cha kuwafanya watoto wachanga wawe wafungwa, hawapati haki za watoto za kucheza na watoto wenzao, hawapati muda wa kujinafasi, lakini pia mama zao wanakuwa wanyonge wanaona kwamba mimi nimekosa, mtoto wangu naye anafungwa amekosa nini. Naishauri Serikali tuangalie mtindo mwingine wa kuwafikiria hawa watoto ambao mama zao wamekuwa wafungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la Sheria na Katiba kuna kipengele hiki tumekipitisha hapa cha kwamba wasaidiwe wale wasiokuwa na uwezo. Mimi naomba hili jambo kwa mujibu wa utaratibu wa kisheria tuliangalie vizuri, kwa sababu ni watu wengi ambao wana kesi hawana uwezo wa kuweka Mawakili, vilevile pia kuna suala zima la ajali. Nchi nyingi zilizotuzunguka inapotokea ajali wahanga wa ajali wanaokufa ama wanaopata vilema vya maisha, utaratibu katika baadhi ya nchi Mawakili wa Kujitegemea wanakwenda hospitalini au wanakutana na familia za wale wahanga wanaweka makubaliano, kwamba kwa sababu mtu wenu amefariki, ameacha wajane na watoto yatima, sisi tutaisimamia kesi ya compensation, kwamba huyu mtu alipwe fidia ili aweze kusomesha watoto wake ambao wamebaki yatima au kama ana mjane au wagane waweze nao kupata haki yao ya malipo yanayotokana na insurance, lakini nchini kwetu…………
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza mimi nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia leo kuwa na afya njema na kuweza kuchangia Hotuba hii ya Wizara ya Ujenzi. Vilevile pia nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Tanga kwa kazi waliyonipa ya kuja kuwawakilisha katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano. Tatu naanza kwa kuunga mkono Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, mimi sitapongeza sana, lakini niseme tu sisi watu wa Pwani tuna kawaida tunajua kwamba baba ndio mlezi wa familia na anapotimiza majukumu yake ametimiza majukumu hakuna haja ya kumsifu, ndiyo kazi yake hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza moja kwa moja kuchangia sekta ya barabara. Kwa muda mrefu tumetoa kilio watu wa Tanga kwa barabara ya Tanga – Pangani – Bagamoyo. Barabara hii ni ya kihistoria, barabara hii imepita katika majimbo matatu, kuanzia Tanga Mjini, Pangani hadi Bagamoyo na pia Muheza na ina Wabunge watatu au wanne, lakini kwa muda mrefu imekuwa haikufanyiwa matengenezo lakini safari hii tunaambiwa imetengewa shilingi bilioni nne ambayo ni sawasawa na asilimia 15 ya mradi mzima wa barabara.
Mimi kwanza niiombe Serikali ikamilishe asilimia 100 kabisa ili barabara ile iweze kutumika kwa wakati wote. Kwa sababu tukumbuke barabara ya Pangani imepita ahadi za Marais wanne waliopita, Rais Nyerere, Rais Mwinyi, Rais Mkapa na Rais Kikwete, wote waliahidi kujenga katika kiwango cha lami lakini ilishindikana. Tunaomba safari hii barabara ile ijengwe kwa kiwango cha lami na tusije tukaambiwa fedha bado hazijapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ninachoiombea barabara ya Pangani kujengwa, kuna Mbuga ya Saadani ambayo ni mbuga pekee duniani ukifika time za jioni kama hizi utakuta wanyama wote wamekusanyika beach kama vile binadamu. Kwa hiyo, hiyo nayo ni hali tunayoitaka barabara ya Pangani ijengwe itakuwa ni chanzo cha uchumi lakini pia itaboresha utalii wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala linguine ninalotaka kuzungumzia ni suala zima la reli. Kuhusu reli ya kiwango cha standard gauge niliwahi kusema mwaka jana kwenye bajeti kama hivi kwamba waswahili wanasema mwiba uingiapo ndipo utokeapo. Reli ya Tanzania au Tanganyika wakati huo ilianza kujengwa Tanga kuanzia mwaka 1905 ikaanzia Tanga ikaenda mpaka Moshi ikafika mpaka Arusha baadaye ikagawanywa ikapita Dar es Salaam ikaingia Morogoro hadi kufika Kanda ya Ziwa, lakini leo tunaona wenzetu katika standard gauge mnatutenga watu wa Tanga. Tunataka tuwaambie watu wa Kanda ya Ziwa sisi Tanga ndio walimu wenu, kwa hiyo, nataka reli ya standard gauge, Serikali pamoja na kwamba wanataka kuianzisha Dar es Salaam, lakini Tanga msije mkaisahau kwa sababu Moshi, Tanga yote hiyo ndiyo reli ya kwanza ilianza kujengwa.
Kwa hiyo, tunapenda keki hii ya Taifa igawanywe kwa usawa ambao hautaleta manung’uniko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu usafiri wa majini, nashukuru kwamba kampuni ya Bakhresa imetuletea meli kubwa inayofanya usafiri kati ya Pemba na Tanga na sasa ajali zitakuwa zimepungua. Kama mtakumbuka Januari, 09 ilitokea ajali kubwa kabisa ya boti ikaua zaidi ya watu 15.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfanyabiashara binafsi amejitolea kuleta meli, lakini bado kuna siku na siku; tunataka Serikali nayo ituwekee meli pale ili hata kama mfanyabiashara anaweza kuamua wakati wowote akiona hapati faida akaamua kuondoa meli yake, lakini ya Serikali itakuwa inahudumia wananchi wake. Kwa hiyo, mimi nakutaka Mheshimiwa Naibu Spika na Mheshimiwa Waziri mhakikishe Serikali nayo ilete meli katika bandari ya Tanga itakayotoka Tanga kwenda Pemba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote Tanga zimekuwa zikitokea ajali za mara kwa mara. Nimekusikia Mheshimiwa Mbarawa asubuhi ukisema kuna kikosi kazi cha uokoaji, lakini kikosi kazi kile hakina zana za kufanyia kazi, na hata pale wanapokuwa na zana za kufanyia kazi hawana mafuta. Iliwahi kutokea ajali moja, mimi na Mheshimiwa Khatib, wakati huo mimi ni Diwani, tukakubali kutoa hata mafuta ili wakaokolewe ndugu zetu ambao boti ilikuwa inawaka moto, lakini ikawa pia tunaambiwa mpaka Meneja wa Bandari atoe go ahead ndipo chombo kianze kutoka, kwa hiyo, hili ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kikosi cha uokoaji kama kipo kweli Mheshimiwa Waziri akiimarishe kiwe na helikopta, kiwe na boti, kisisaidie tu kuokoa maisha ya watu wanaopata ajali baharini, lakini hata zinapotokea ajali za magari. Leo imetokea ajali Daraja la Wami au barabarani watu wengine wanapoteza maisha kwa sababu hakuna usafiri wa haraka unaoweza kuwafikisha katika hospitali zetu.
Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri katika bajeti yako uongeze fungu ambalo litasaidia kupata hata helikopta za uokoaji zisaidie kuwahisha majeruhi katika hospitali zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu usafiri wa anga. Usafiri wa anga Tanga imekuwa kuna kizungumkuti kidogo, uwanja ni uleule wa tangu mkoloni. Tunahitaji Tanga kutokana na uwekezaji mkubwa unaokuja tupate kiwanja cha ndege cha kimataifa (Tanga International Airport) kwa sababu pana uwekezaji wa bomba la mafuta, Tanga kuna utalii, vile vile Tanga pia kuna Tongoni Ruins, Amboni Caves na mambo mengine pamoja na Amani Research Institute, zote hizo zinatakiwa tuweke uwanja wa ndege wa kisasa ili tuweze kupata mafanikio ya uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine katika hicho kikosi pia pawe na divers. Tumeona wakati wa ajali ya MV Bukoba watu walishindwa kuokolewa kwa sababu hatuna divers, tumeagiza divers kutoka Mombasa - Kenya, hii ukiangalia inatutia udhaifu kidogo nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhsu suala la Daraja la Wami. Nimekuwa nikisema Daraja la Wami ni link yaani kiunganishi kati ya Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na hata nje ya nchi kama Kenya kupitia Nairobi mpaka Ethiopia huko. Lakini daraja lile ni la tangu mkoloni, daraja lile lina single way hayawezi kupita magari mawili kwa wakati mmoja, hivi Serikali inashindwa kujenga Daraja jipya la Wami? Nimeona kwenye taarifa ya bajeti yako umetenga fedha, lakini nasema iwe ni kweli. Daraja la Wami limekuwa likipoteza maisha ya watu na mali zao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, naomba Daraja la Wami lijengwe daraja kubwa na jipya la kisasa kama lilivyokuwa la Kigamboni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Bandari ya Tanga. Bandari ya Tanga imekuwa ikikimbiwa na wafanyabiashara kwa sababu kuna tofauti kubwa na usumbufu mwingi unaotokea katika Bandari ya Tanga na uliwahi kutoa taarifa kwamba Bandari ya Tanga imekuwa inafanya kazi kwa hasara, inafanya kazi kwa hasara kwa sababu wafanyabiashara wanaikimbia. Mfanyabiashara yuko radhi apitishe mzigo wake Bandari ya Mombasa, Kenya azunguke Holili, Kilimanjaro ndipo aje Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu cha kodi ni kimoja katika mipaka yetu yote ya Tanzania kwa nini watu wanaikimbia Bandari ya Tanga? Ni kwa sababu pana usumbufu na vilevile pana dosari za hapa na pale. Si hivyo tu hata border ya Horohoro kuna matatizo, wafanyabiashara pia wanakimbia na sasa hivi Serikali imeanzisha utaratibu kwamba kuna watumishi wa TRA ambao wapo Mombasa, Kenya wanafuatilia makontena huko huko, ukija Horohoro tena ushushe mzigo tena, ni usumbufu kwa wafanyabiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda nimshauri Mheshimiwa Waziri, aboreshe Bandari ya Tanga pasiwepo na usumbufu, mizigo itoke kwa muda mfupi ili wafanyabiashara waweze kuitumia vizuri Bandari ya Tanga, lakini pia tuongeze mapato ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala zima la ununuji wa ndege. Tunashukuru kuwa Bombardier zimepatikana, zifike Tanga, lakini ndege zile…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia afya njema na kuniwezesha kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya ndiyo utajiri mkubwa kuliko utajiri wowote na hospitali, vituo vya afya, zahanati hizi zote ndizo ambazo tunaweza kuzisema garages za binadamu. Lazima pawepo na vifaa vya aina zote (apparatus) ili ziweze kuwarahisishia utendaji kazi madaktari na wahudumu wetu wa afya (nurses) ambao kwa kweli wanafanya kazi katika mazingira magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto za vituo vya afya; katika maeneo ya vijijini kuna kero ya kufunga vituo vya afya na zahanati saa 8:30 mchana, hili ni tatizo. Mfano katika Jimbo langu la Tanga Mjini, vituo vifuatavyo ni miongoni mwao; Kituo cha Afya Pande (Kiomoni), Kirare, Manungu, Chongoleani, Mabokweni, Tongoni na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri/ombi langu ni kuwa hivi vituo vikifanya kazi 24 hours kuna tatizo gani? Naishauri Serikali yangu sikivu iwatumie madaktari 258 waliokuwa waende kufanya kazi nchini Kenya wakati wa mgomo na ambao Mheshimiwa Rais Magufuli ameshatangaza kuwaajiri, tupatiwe madaktari 70 kati yao waende katika vituo vya afya na zahanati zetu za Jiji la Tanga pamoja na vitongoji na viunga vilivyopo maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Tanga lilianzisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tanga ili kuweza kupunguza msongamano katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo. Halmashauri ilishaanzisha ujenzi wa Administration Block (Jengo la Utawala) kwa gharama ya shilingi milioni 400 katika mwaka 2013/2014. Kwa sasa mpango wa Halmashauri ya Tanga 2017/2018 tumetenga shilingi 300,000,000.00 ili kujenga jengo la OPD (Out Patient Department).

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu naiomba Serikali iunge mkono juhudi za Jiji la Tanga kwa kuipatia fedha takribani bilioni 1.2 ili iweze kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa, theatre, sehemu za tiba ya macho, moyo, mifupa na kadhalika; lakini pia gari la wagonjwa (ambulance). Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tukifanikiwa kuikamilisha Tanga District Hospital tutasaidia kuboresha afya za wananchi wa Jiji la Tanga na Watanzania lakini pia tutaipunguzia Bombo Regional Hospital msongamano wa wagonjwa wanaotoka Wilaya zote nane na Halmashauri tisa za Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira za madaktari/ wahudumu, naomba pia wahudumu (nurses) wengi wanaosoma katika Vituo vya Hospitali Teule za Tanga, Matc na Eckenforde Nursing Training waajiriwe katika hospitali yetu ya Wilaya tunayoitarajia pamoja na vituo vyetu vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la dawa MSD, medicine supply chain iwekwe wazi. Naomba kwa kuwa Jiji la Tanga tayari tunao mpango na utekelezaji wa Hospitali ya Wilaya, mgao wa dawa za MSD ungepelekwa katika zahanati na vituo vya afya vilivyopo (ama msaada au kwa kununua ili kupunguza upungufu wa dawa katika Jiji la Tanga).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hospitali ya Mkoa ya Bombo Hospital, naiomba Serikali (Wizara) kuingilia Hospitali ya Mkoa wa Tanga (Bombo Regional Hospital) ambayo imepandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa lakini haina hadhi hiyo kwa kuwa haina:-

(i) Madaktari Bingwa wa kutosha;
(ii) Vifaa tiba vya kutosha (oxygen machine, x-ray, ultra sound, CT Scan;
(iii) Intensive Care Unit ina mapungufu mengi;
(iv) Barabara za ndani za hospitali mbovu kupita kiasi;
(v) Lift ya Bombo imekufa zaidi ya miezi 36 iliyopita (paundi 126,000 zinahitajika); na
(vi) Gari za wagonjwa mbovu inayofanya kazi ni moja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri na maombi yangu kwa Serikali (Wizara) ni kwamba Serikali iangalie kwa jicho la huruma Hospitali hii ya Mkoa ya Bombo kwa mapungufu yote kuanzia (i) – (vi) na namkumbusha Mheshimiwa Ummy (Waziri) kwamba charity begins at home.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma za ustawi wa jamii, ukurasa wa 57; nawazungumzia walemavu wa akili. Serikali itenge fedha kila Halmashauri ili kuwepo kitengo cha kuwatunza walemavu wa akili (vichaa) ili kuwapatia nguo, kuwakata nywele, kucha na kuwatibu kwa kufuatilia chanzo cha maradhi yao, kama ni matumizi ya dawa za kulevya, mtindio wa akili na kadhalika, watibiwe kwa kuwa nao ni Watanzania wenzetu. Inatia aibu kuwaona vichaa watu wazima wanatembea uchi mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za watoto, wajawazito na wazee; naiomba Serikali iangalie katika eneo hili kwa sababu kuna maneno kuliko vitendo. Akina mama, wazee na watoto wanalipa, naomba Wizara itoe vifaa vya kujifungulia na dawa za wazee bure.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuweza kunijaalia kuchangia. Naunga mkono Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani na pia nawapongeze Mawaziri kwa kazi .

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ni kwamba, hapo zamani za kale Tanzania hapakuwepo na migogoro ya ardhi hususan ya wakulima na wafugaji, lakini siku za karibuni migogoro ipo kila kona ya Tanzania. Sababu kubwa watu wamejua thamani ya ardhi kuwa ni mali. Ardhi ni rasilimali muhimu ambayo pia ni urithi na utajiri wa asili toka kwa Mwenyezi Mungu. Naishauri Serikali, ardhi yetu ipimwe, ipangiliwe isiwe nchi nzima ni viwanda, barabara, makazi na maeneo ya vijijini tu ndio mashamba. Ardhi ipimwe na imilikiwe na wananchi kama ilivyo kwa South Africa, Kenya na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mashamba ya Mkonge (Amboni Company Limited). Halmashauri ya Jijiji la Tanga lina mashamba makubwa ya Mkonge ya Amboni Company Limited sasa (COTAIL) ambayo imechukua nafasi ya Amboni Limited. Naipongeza Kampuni ya Cotail Limited kwa kuipa Halmashauri ya Jiji la Tanga ardhi kwa ajili ya shughuli za maendeleo yenye ukubwa wa takriban heka 400.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamejitokeza matatizo baada ya Halmashauri kupata mwekezaji wa China anayetaka kujenga Kiwanda cha Cement. Kuna wakulima ambao wanalalamika kuwa wamepunjwa fidia, hivyo naomba, Mheshimiwa Waziri tukatembelee eneo husika ili kutatua kero ndogo ndogo na kuweza kufanya mradi mkubwa wa Kiwanda cha Cement uanze bila malalamiko ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mashamba ya Marungu na Kwamkembe. Sheria inaelekeza kuwa majiji hayana mashamba yenye zaidi ya 50 hectors, lakini Jijji la Tanga katika Kata ya Marungu kuna mashamba tajwa hapo juu ambalo siku za karibuni wameuziwa na wamiliki wenye Hatimiliki, wameondoa wananchi waliokuwa wakilima mazao ya chakula na biashara, yaliyowezesha kupata kipato cha kila siku na kulipia ada za watoto. Waliahidi kuwakatia wakulima baadhi ya maeneo kwa ajili ya kilimo (mashamba yana zaidi ya ekari 2000 – 4000). Namwomba Mheshimiwa Waziri hili pia alishughulikie na kupata ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha miaka 21-Tanga. Hili ni eneo lililotwaliwa kinyume na taratibu. Nashauri, Mheshimiwa Waziri, Ofisi yake ilirudishe Halmashauri ya Manispaa ya watu wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Ngamiani Kusini Kati na Kaskazini. Eneo hili ni katikati ya mji kuanzia Barabara 1- 21, kuna nyumba zaidi 10,000 na ni eneo la kihistoria lakini wamiliki wake hawana hatimiliki wana Hati ndogo (offers) tu. Ushauri, naomba Wizara ya Ardhi isaidie katika kupima au kutoa Hatimiliki (99 years) ili wananchi waweze kutumia katika shughuli za maendeleo kama kukopa mabenki kwa ajili ya biashara na kilimo. Tukumbuke wananchi hawa wanalipa property tax.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu 30% ya makusanyo, naiomba Wizara irudishe 30% ya mapato ya ardhi katika Halmashauri ili zitumike kwa shughuli za Maendeleo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kuhusu hali ya utalii nchini. Sekta ya utalii ni moja kati ya sekta ambazo huliingizia Taifa mapato makubwa na pia hutupatia fedha za kigeni. Pamoja na umuhimu wake bado bajeti yake ni ndogo, lakini pia Serikali haijakuwa na mipango mizuri kiasi kwamba ushindani kati yetu na nchi jirani unakua siku hadi siku. Kwa kukosa mipango mizuri, imefikia leo Tanzania pamoja na mbuga nyingi na kubwa, mapango, maporomoko, maziwa, wanyama wengi, ndege, wadudu na samaki, mapato yetu bado hatuifikii Kenya, Ethiopia, Botswana, Zambia, South Africa, Rwanda na kadhalika, bado mapato yetu ni madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara ya Maliasili na Utalii ishirikishe wadau mbalimbali katika kutoa mchango wa mawazo katika sekta ya utalii ili yatapatikane mawazo mengi yenye manufaa na yataisaidia Serikali. Kwa mfano, advertisements (matangazo), bado Tanzania hatujatangaza utalii wetu katika mataifa ya nje kiasi cha kutosha ukilinganisha na washindani wetu Kenya, Uganda, Malawi, Namibia, Rwanda na kadhalika. Tuwatumie Watanzania wanaoishi nje (diaspora) washirikiane na Mabalozi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunadhani utalii ni wanyamapori na hoteli tu, sivyo. Katika ukurasa wa 12 – 59 wa hotuba ya Waziri anazungumzia wanyamapori tu. Je, Makumbusho, Olduvai Gorge, Tongoni Ruins, Amboni Caves, Michoro ya Kondoa Irangi, Magofu ya Pangani, Amboni Sulphur Bath, yote haya tunayaacha bila ya kuyatangaza. Nashauri sasa tufanye matangazo ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Tanga na utalii; Tanga ni mji wa kihistoria, una majengo mengi ya kihistoria, una bandari, railway na hata makazi ya kale, kuna visiwa vilivyokuwa na magofu na makaburi yaliyodumu kwa zaidi ya miaka 200. Hivyo, naishauri Serikali itenge eneo la Posta na Uhindini kuwa eneo la kihistoria kama lilivyo eneo la Stone Town, Zanzibar. Tanga tunayo Mapango ya Amboni (caves), Tongoni Ruins na Amboni Sulphur Bath.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sports tourism kama football, basketball, netball, golf, cricket, etc ni michezo ambayo nchi za wenzetu wanaitumia na kuingiza mapato kwa kufanya mashindano ya kimataifa, mfano Dubai Open, golf umekuwa ni mchezo mkubwa unaoingiza fedha nyingi katika sekta ya utalii na pia surf (swimming and fishing) ni michezo ambayo tukishirikiana na sekta binafsi tutaweza kufanya vizuri kwa kuwa wenzetu wa nchi za Kenya, South Africa na Mauritius wanafanya vizuri, tusibaki nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mali kale na makumbusho, hadi leo mjusi wa Tanzania dinosaur yupo Ujerumani na anaiingizia fedha za kigeni nchi ya Ujerumani. Kwa nini asirejeshwe kama fuvu la Mkwawa na awekwe katika Makumbusho ya Taifa? Tunahitaji mjusi wetu arejeshwe Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna 1424km3 za bahari kuanzia Jasini (Mkinga District - Tanga) hadi Msimbati (Mtwara), amegundulika samaki kisukuku (coelecanthy) ambae alikosekana zaidi ya miaka 80 iliyopita, Tanga – Kigombe (Muheza) amepatikana. Taasisi za kimataifa kupitia Mradi wa Coast Zone wameweka kambi na wanaendelea na kukusanya taarifa zake. Je, Wizara wana habari? Habari ndiyo hiyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpira wa miguu na udhamini wa Serikali, Mpira wa miguu katika nchi yetu ya Tanzania ni mchezo unaopendwa lakini kwa bahati mbaya tumeshindwa kuwekeza katika michezo ipasavyo. Mfano katika Academy tupo nyuma sana, vilabu havina academies na shuleni hakuna mipango (mission wala vision) na hata ikiwepo dhaifu. Angalau tungeweza kuviandaa vilabu vyetu viwe na academies zao, hili nashauri vilabu vyote vilivyo katika VPL – Vodacom Premier League vielekezwe kuanzisha academies na Wizara ichangie. Vilabu vya Simba na Yanga kupewa mabasi na vilabu vingine kuachiwa huu utaratibu mbaya, vilabu vyote vinavyoshiriki VPL, vipatiwe usafiri (Buses).

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu wachezaji kukatwa kodi ya mapato. Wachezaji wa vilabu vyetu kukatwa kodi ni utaratibu mzuri lakini bado tuko mbali sana, kipato chao ni kidogo. Pawe na utaratibu wa kiwango fulani cha malipo na kwa muda maalum ukifika ndio wachezaji hawa wakatwe kodi. Mfano, mchezaji anayekuwa na mkataba unaoanzia Tsh. Milioni 100 kwa miaka mitatu mfululizo huyu akatwe kodi angalau asilimia tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vya kisasa vya michezo, Jiji la Tanga lipo eneo la uwanja wa kisasa unaotaka kujengwa kwa ufadhili wa FIFA, hadi leo hakuna hata uzio na matokeo yake uwanja unaanza kuvamiwa na wajenzi holela. Je, Serikali katika ujenzi wa uwanja huu na udhamini wa FIFA inawaeleza Watanzania, mikataba ikoje, lini uwanja utaanza kujengwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo ya Kimataifa; mchezo wa boxing ndiyo mchezo pekee ambao unadiriki kututoa kifua mbele, lakini mchezo huu Wizara (Serikali) imeutupa, katika mikoa na wilaya ambazo mchezo huu unaendelea kuchezwa wapatiwe vifaa vya kisasa na vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uibuaji vipaji shuleni, nashauri Serikali itilie maanani masuala ya michezo ya aina zote kuanzia primaries, secondary’s hadi Universities, Serikali ianze kuwekeza kwa dhati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo ya Wabunge; pamekuwepo na mashindano ya Wabunge wa Afrika Mashariki, lakini maandalizi na stahiki za Wabunge wa Tanzania hazieleweki, wanadai kuanzia mashindano ya Mombasa (Kenya) hadi ilivyofanyika Dar es Salaam (Tanzania). Ushauri, namwomba Waziri atulipe Wabunge.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutujalia afya njema na kuweza kuendelea na shughuli zetu za Bunge. Vilevile nitoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Kamati kwa taarifa zao walizowasilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Hii Wizara ni nyeti na imebeba au imeshikilia maisha ya Watanzania, lakini ukiangalia changamoto zilizokuwemo katika Wizara hii ni kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mzungumzaji aliyepita hapa amezungumza kwamba gharama za matibabu zimekuwa juu sana. Huu ni ukweli usiofichika. Ushahidi wa hili ni pale Mtanzania anapokuwa na maradhi kwa sababu ya ukali wa maisha, kwa sababu ya umasikini anakwenda katika vyombo vya habari kama ITV Television au Channel Ten anakwenda kujidharirisha kuomba, kwamba naomba wasamaria wema wanichangie. Mimi hili jambo linaniuma kweli kweli, kwa sababu huyu ni Mtanzania, tunajifaragua na kujidai kwamba tunakusanya 1.9 trillion kwa mwezi, lakini kwa nini Mtanzania aende akajioneshe pengine ana maradhi ya aibu, anachukuliwa na moving camera anaonyeshwa namna hii yale maradhi yake. Huu ni udhalilishaji! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetembea katika baadhi ya nchi, najua hata baadhi ya Waheshimiwa Wabunge humu mmetembea, Naibu Spika, umetembea. Kwa mfano, nchi kama Qatar au Saudia, Denimak, Norway, Finland, kwa wenzetu matibabu hakuna mtu anayekufa kwa sababu hana fedha ya matibabu. Serikali imeweka utaratibu kwamba elimu ni bure na matibabu ni bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mtanzania, hata mtoto mchanga, watoto waliozaliwa wameungana, bila aibu tunaenda kuwaonyesha kwenye television kwamba watoto hawa wanahitaji wasamaria wema wawachangie. Hili pato la Taifa tunalokusanya kupitia mamlaka ya mapato, shughuli yake ni ipi? Kazi yake ni kununua silaha peke yake? Kazi yake ni kutulipa mishahara sisi Wabunge na Watumishi wa Serikali peke yake? Hawa Watanzania wakimbilie wapi?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali mambo mengine ni aibu!

MHE. AMINA S. MOLELL: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: …na kwa bahati mbaya sana, vyombo vyetu vya habari sasa hivi vinaonekana Kimataifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk, kuna taarifa. Mheshimiwa Amina Mollel.

T A A R I F A

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda tu kumpa taarifa Mheshimiwa Mbarouk kwamba moja ya kazi za vyombo vya habari ni pamoja na kuihabarisha jamii. Katika kuihabarisha jamii ni pamoja na kuishirikisha katika mambo mbalimbali ikiwemo pia matatizo mbalimbali yaliyopo katika jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni utaratibu wa kawaida kabisa unaotumika na vyombo vya habari, anapokwenda mtu mwenye tatizo kuweza kutaka kuwasilisha tatizo lake kwa jamii na kwa sababu kwenye jamii wapo watu ambao wanaguswa na kuweza kusadia. Kwa hiyo, asione kwamba ni aibu bali ni utaratibu uliopo katika vyombo vya habari. Ndiyo maana katika vipindi mbalimbali pia watu wanaweza kwenda na kushiriki katika hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo taarifa siipokei. Namwomba Amina Mollel aichukue mwenyewe taarifa yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumzia aibu maana yake, kwa mfano tangu majuzi inarushwa clip, kuna mtoto ana matatizo ya figo, tumbo lake limekuwa kubwa kabisa. Ukimtazama mama yake yupo kwenye television analia, maana yake hana uwezo wa kwenda kumtibu yule mtoto wake India. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine labda niutoe, mimi na Waziri wangu wa Afya pale Mheshimiwa Ummy Mwalimu, sote ni watu wa Tanga, yupo dada mmoja wa Kwanjeka, ana maradhi ya mguu kama tende hivi. Tumejitahidi tukampatia Bima ya Afya, lakini Bima ya Afya kumbe nayo kuna baadhi ya package hazihusiki kwamba labda mtu kupelekwa nje. Sasa mtu anadhalilika na maradhi mpaka anakufa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani ndugu yenu mnamwangalia huyu ndio anakwenda zake sasa, lakini hamna cha kumfanya. Mbona kwenye Serikali za wenzetu wanaweza? Kutibiwa na masuala ya elimu ni bure. Kwa nini sisi inashindikana wakati sisi Mwenyezi Mungu ametujalia rasilimali bila ya kumpa rushwa? Ametujalia madini, ametujalia bahari, ametujalia mazao, ametujalia wanyama, vyote hivyo Serikali inapata pesa, lakini inashindwa kuwatibu wananchi wake. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mashimba Ndaki.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Hizi taarifa zinakula muda…

T A A R I F A

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa msemaji ayezungumza kwamba yeye ni Mbunge. Kipindi cha kupitisha bajeti hapa mwezi Juni alikuwepo. Mambo anayoyazungumza alikuwa anayajua, lakini hajayaleta mbele ya Bunge lako ili kwamba bajeti iweze ku-consider jambo hilo. Sasa anakuja kusema kipindi hiki ambacho hata hatupangi mipango kama hiyo anayosema, sasa anayewahurumia watu hao ni yeye au anapenda tu kujisemea? Ahsante. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk, jitahidi utumie lugha ya Kibunge maana hapo umezungumza mambo mengine. Kwanza umemwambia Mheshimiwa Amina Mollel aichukue mwenyewe taarifa, hairuhusiwi kikanuni. Wewe unajibu kama unaipokea ama huipokei, unaendelea na utaratibu.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, basi taarifa siipokei.

NAIBU SPIKA: Taarifa hiyo unaipokea?

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, hii pia siipokei. Labda niseme, Mheshimiwa aliyesema kwamba eti tunapitisha bajeti; bajeti ndiyo tunapitisha, lakini kwa mfano jana mchangiaji mmoja alizungumza hapa, nami niliwahi kuzungumza huko nyuma, tunapitisha bajeti labda ya Wizara ya Kilimo kwamba wapewe asilimia 100 ya fedha, wanapewa asilimia 11, ni bajeti isiyotekelezeka. Hata mimi najua dada yangu Mheshimiwa Ummy hiyo bajeti tunayompelekea pia haimtoshelezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naizungumzia Serikali kwa ujumla wake sasa kwa sababu ndiyo inayokusanya mapato yote ya Serikali. Ni wajibu wa Serikali kuwatibu wananchi wake hasa pale wanapokuwa katika maradhi ambayo hawayamudu kugharamia kwa matibabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niseme, kwa mfano Sera ya Taifa ni kwamba Wazee, Watoto na Akinamama Wajawazito Watibiwe Bure, lakini ukienda katika hospitali zetu hawa akina mama kwenye hizo delivery kit pia unakuta katika baadhi ya maeneo wanachangishwa, wanaambiwa walipie, siyo kwamba ni bure. Mtu anaambiwa alipie hiyo delivery kit, lakini pia kuna vitu vingine ambavyo anatakiwa alipie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, akina mama Wabunge humu ni mashahidi, labda kama watakuwa wanapendelewa kwa upendelo kwa hadhi waliyokuwa nayo, lakini akina mama wengi hususan maeneo ya vijijini, akienda kujifungua lazima delivery kit alipie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kusema, hata watoto ndiyo huo mfano ninaoutoa kwamba watoto chini ya umri wa miaka mitano wameambiwa watibiwe bure, sasa huyu mtoto ambaye anapelekwa kwenye television wakaombwa wasamaria wema, matibabu bure yako wapi hapo? Huyu ni Mtanzania, tena ni mtoto mchanga, malaika wa Mungu, basi sisi hata hatumwonei huruma? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, tunaposema matibabu yawe bure, basi yawe bure; akina mama wapate delivery kits zile free no charge, wazee watibiwe bure. Tena kwa bahati mbaya, anakwenda mzee labda kutaka matibabu, anaambiwa wewe si una watoto? Sera ya Taifa haikusema kwamba mtu akiwa na watoto asitibiwe bure. Imesema “mzee.” Au anafika hospitalini au Kituo cha Afya mzee anaambiwa, lete kitambulisho cha uzee. Sura yake ukimtazama, si unamwona ni mzee huyu, kitambulisho cha nini? Mtu unamwona kabisa huyu ni mzee, lakini anaambiwa atoe kitambulisho cha uzee.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naona huku ni kuwanyanyasa. Kama tumeshindwa kuwatibu bure watu wetu, naomba tuwaambie basi hakuna matibabu bure, kuliko tunawapa moyo, mtu anajua anaumwa anakwenda kutibiwa bure halafu akifika kule anakatishwa tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua umenilindia muda wangu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni watoto wa mitaani. Wizara inazungumza kwamba itahudumia maendeleo ya jamii, lakini watoto wa mitaani wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku kwa sababu hatushughuliki nao, hatuna center tunazowaweka tukawapatia labda elimu, tukawapa mafunzo; matokeo yake wale wale ndio wanaogeuka kuja kuwa vibaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, tukiachilia mbali watoto wa mitaani, hata vichaa; unakuta kichaa anatembea uchi sokoni au anapita maeneo ya shule; yaani watoto wadogo wanajua kumbe mtu akishakuwa mtu mzima, ana vitu hivi na hivi! Kichaa hana mtu wa
kumwangalia, hana hata nguo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikari iweke vituo maalum kama baadhi ya nchi za wenzetu. Watu wenye kichaa tunawachukua, tuhakikishe na wao wanaoga, wanabadilishwa nguo na wanapewa chakula. Wengine wanakufa kwa njaa tu. Mtu ni kichaa, amekaa sehemu hana akili hata ya kujua kwamba muda huu natawakiwa nile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali, watoto wa mitaani na vichaa lazima tuwawekee utaratibu, tuhakikishe kwamba kwanza watoto wa mitaani wanapata elimu, lakini hata hawa vichaa isiwe ni aibu sasa mitaani. Wawekewe maeneo maalum. Hebu fikiria wewe usipooga kwa muda wa siku moja tu unajisikiaje? Sasa kichaa miezi tisa hajaoga, unafikiri anajisikia vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali, hawa nao ni Watanzania, wanahusika kabisa na pato la Taifa au keki ya Taifa ambayo inakusanywa na Serikali nao iwahudumie kwenye mavazi, chakula na hata hali ya kimazingira ya afya zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho labda nizungumzie kwenye masuala ya huduma; huduma ziko katika maeneo mengi sana. Sasa hivi tuzungumze hata kwenye huduma hizi kama za maji, labda na umeme, tunashukuru kwenye umeme wamejitahidi, lakini kwenye masuala ya maji bado wenzetu wa vijijini wana matatizo makubwa ya huduma hii ya maji. Maji wanayotumia kwa kweli yanawasababishia maradhi kwa sababu siyo safi na salama. Tuishauri Serikali sasa, katika ile miradi ya vijiji kumi kila Halmashauri, wahakikishe wananchi wa Vijijini nao wanapata maji kwa usalama wa afya zao, lakini kwa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka kuzungumzia ni suala la maiti. Kumekuwa na tabia sasa maiti imekuwa ni dili au nacho ni chanzo cha mapato ya Serikali. Huyu mtu ameshatangulia mbele ya Mungu, amesamehewa. Kwa mfano sisi Waislamu, mtu akishakufa, amesamehewa kuswali, amesamehewa kufunga, maana yake huyu amerudi mikononi mwa Mwenyezi Mungu, lakini Serikali yetu ya Tanzania, maiti anachajiwa akikaa mortuary. Hii mimi nasema ni aibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tuhakikishe kwamba sasa hawa maiti isiwe dili, wasamehewe kama walivyosamehewa na Mwenyezi Mungu. Kuna baadhi ya familia hazina uwezo; mtu anaambiwa shilingi milioni tano, ndiyo hayo sasa aliyosema Mheshimiwa Sugu hapa, kwamba mtu anajitokeza mbele ya Mkutano wa Rais anaomba shilingi milioni tano akakomboe maiti. Hivi Rais huyu kwa nini tunamlundikia mizigo ya kazi nyingine ambazo hata hazimuhusu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri tena, maiti kwenye nchi yetu ya Tanzania wasichajiwe. Wakiwekwa mortuary, siku hizi kuna mawasiliano mengi tu, ifahamishwe familia yake waje wachukue maiti yao wakazike, lakini kumdhalisha maiti kumweka katika mortuary kwa muda mrefu, hilo nalo pia sio haki. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda tayari.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante. Labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya njema, tukaweza kukutana na kuendelea na shughuli za Bunge letu. Pia niungane na wenzangu katika kuipongeza Wizara, pamoja na kwamba upo upungufu mchache, lakini wanapofanya vizuri lazima tuseme wamefanya vizuri, lakini pale kwenye matatizo basi hatuna budi kushauriana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema tu kwamba, ardhi ni mali, lakini kwa bahati mbaya ardhi sasa haiongezeki, lakini sisi binadamu na shughuli zetu tumekuwa tukiongezeka. Sasa tatizo linalokuja ni kwamba kwa kuwa ardhi haiongezeki na kila mmoja sasa hivi amekwishajua kwamba ardhi ni mali ndiyo pale panapotokea migogoro ya mara kwa mara. Sasa nishauri tu kwamba Mheshimiwa Waziri aendelee kufanya kazi, lakini asiwe anafanya kazi yeye na Naibu Waziri tu, pamoja na watumishi wa Wizarani, lakini hata wale Maafisa Ardhi wa kwenye Halmashauri, Maafisa Mipango Miji na Maafisa wengine nao waige mfano wa Mawaziri wetu hawa wawili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo? Kwenye Jimbo letu la Tanga pamekuwa na migogoro ya hapa na pale, kwa mfano ipo migogoro ambayo Mheshimiwa Waziri amekwishajaribu kuishughulikia, lakini bado haijakaa vizuri sana. Nitoe mfano, labda kuna mgogoro huu wa JWTZ na maeneo ya Mwahako pamoja na wananchi. JWTZ waliwalipa pale wananchi kumi tu, lakini baada ya kulipa wananchi kumi wanasema eneo lote lililobaki ni eneo la Jeshi.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sasa, wakati mwingine majeshi nayo yanakuwa na sheria ngumu, baada ya kuchukua umiliki wa lile eneo basi imekuwa hakuna ruhusa hata kupita kwa miguu katika maeneo hayo. Ikumbukwe baadhi ya maeneo hata kama tuna majiji lakini bado kuna vitongoji au kuna maeneo ambayo ni ukiyatazama ni maeneo ya vijiji kwa sababu kuna mashamba, kuna wafugaji na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa namwomba kwanza Mheshimiwa Waziri, pale ambapo Jeshi liko karibu na wananchi pawe na mahusiano mazuri. Kwanza, ukilitazama jina lenyewe la Jeshi ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Sasa linapokuwa jeshi hapatani na mwananchi, hapo napata tabu kidogo kuelewa. Kwa hiyo naomba awaelekeze washirikiane na wananchi.

SPIKA: Haya Taarifa Mheshimiwa Laizer.

TAARIFA

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa, kwamba ni Jeshi la Wananchi...

SPIKA: Ngoja zima kwanza, Mheshimiwa Mbarouk, endelea…

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, taarifa ninayotaka kumpa ni kwamba tulichofanya sisi Monduli, kwa sababu ni Jeshi la Wananchi tuliwapa ardhi bure, tukawa na ujirani mwema; tatizo la wananchi wengi wanataka walipwe fidia, lakini warudi kutumia ardhi hiyo hiyo ambayo alishalipwa fidia. Kwa hiyo tujenge utaratibu wa mashirikiano na jeshi.

SPIKA: Anakushaurini tu kwamba, ukilipwa fidia maana yake uondoke jumla.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, sasa baadhi ya watu hawajalipwa, kuna wananchi 112 hawajalipwa na wamekuwa wakifuatilia malipo yao wamekuwa wanahangaishwa na wao kikubwa wanasema kwa nini wanadai fidia? Ni kwa sababu hata kama eneo hilo limechukuliwa na Jeshi, wanasema Sheria Na.4 ya mwaka 1999 nafikiri Waziri anaijua vizuri ile inayosema: “whether you have tittle deed or not so long you have been there for a long time, customary law recognize you as the owner of the land.” Sasa wananchi wanapoitumia sheria hii ndiyo wanapoona kwamba ni haki yao.

SPIKA: Nani alikuwa anasema Mussa Mbarouk hajui Kiingereza? Si mnaona ameteremka vizuri kabisa jamani? Endelea Mheshimiwa Bwana. (Kicheko)

MHE. MUSSA B. MBAROUK: …inaeleza kwamba hata kama kuna mradi wa maendeleo lakini lazima kwanza akae mwekezaji, ikae Serikali kwa maana ya Wizara ya Ardhi na wananchi; sasa wakati mwingine wananchi wanakuwa wanasumbuliwa kulipa malipo ambayo wanastahili na ni haki yao; na siyo hapo tu; kwa mfano; nashukuru kwamba Serikali Waziri Kamwelwe hapo amesema Uwanja wetu wa Ndege Tanga umepatiwa fedha takribani bilioni 36 ili ufanyiwe upanuzi na uwe wa kisasa zaidi; hususani kutokana na uwekezaji mkubwa unaokuja. Hata hivyo kuna nyumba zimefanyiwa evaluation tangu mwaka 2008, wananchi wale hawajalipwa, nyumba 38. Sasa hivi ili uwanja uwe mkubwa zaidi pana nyumba 802 maeneo ya Masiwani Shamba ambayo ni kata mpya zinahitajika kuondoka. Sasa wananchi wanasema hatukatai kuondoka lakini kwa Sheria ile Namba Nne tulipwe kwanza fidia hatukatai maendeleo.

Mheshimiwa Spika, mimi nashauri, Mheshimiwa Waziri, wananchi wale wa mwaka 2008 wa maeneo ya Masiwani Shamba walipwe fidia zao, lakini hata hizi nyumba 802 ambazo ni za kisasa ziondoke lakini wananchi wakabidhiwe fidia zao. Kwa sababu, mtu wa kawaida anaweza akajenga nyumba labda miaka mitatu mpaka miaka 10 lakini inapokuja shughuli za maendeleo likitolewa tu tamko ujue utaondoka; sasa hawa nao ni Watanzania wakimbilie wapi? Kwahiyo mimi naishauri, Serikali pamoja na maendeleo, maendeleo nayo yana gharama zake Wananchi wetu lazima wafidiwe.

Mheshimiwa Spika, kama hilo halitoshgi, kuna mgogoro wa eneo pia la kwa Ramsing, nafikiri Mheshimiwa Waziri hili ulilisikia. Wapo wazee ambao ni wenyeji wa maeneo hayo, lakini kuna huyo Ramsing ambaye alikuwa ni Singasinga alikuwa analima miwa na kutengeneza sukari wakati huo. Baada ya kuondoka na shamba lile kutaifishwa na Serikali, kwa bahati mbaya sana lile eneo lilirudishwa kwenye Halmashauri. Sasa baada ya Halmashauri nayo kushindwa kulisimamia vizuri pakatokea UVCCM wakasema lile eneo ni la kwao.

Mheshimiwa Spika, wale wazee hawakatai, wanasema kuna eneo la UVCCM lakini kuna eneo la wenyeji. Sasa limechukuliwa eneo lote limekuwa la UVCCM, wazee wale wanasema sisi tutakwenda kulima wapi na sisi tuna warithi wetu ambao ni watoto wetu? Kwahiyo naomba pia Mheshimiwa suala hili ulishughulikie ili tuondoe migogoro isiyokuwa ya lazima; na kama wachangiaji wengi wanavyokusifu, kwamba ni kinara wa kutatua migogoro, basi nakuomba na migogoro hii iliyoko Tanga nayo uitatatue.

Mheshimiwa Spika, lakini kama hili halitoshi kuna suala la EPZ maeneo ya Mwahako vilevile; jambo hili lina karibu miaka nane watu wa maeneo ya mbugani; miaka nane imeanzishwa EPZ lakini watu bado hawajalipwa na wamezuiwa kuendeleza majengo yao. Wanasema tunavyojua sisi sheria na taratibu za evaluation ikipita miezi sita lazima ifanyike upya kwa bei ya soko iliyokuwepo ya ardhi ya wakati huo; sasa hawa wananchi mpaka leo hawajui waende wapi. Nakuomba nalo Mheshimiwa Waziri hili ulishughulikie lipate ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, lakini lingine nikija kwenye gharama za upimaji; vifaa vya kupimia umetuambia na kupongeza kwa hili, kwamba Halmashauri zetu zikachukue vifa vya kupimia kwenye Kanda, lakini sasa kupitia Bunge hili uwatamkie wananchi kwamba gharama za kupima kiwanja kimoja ni shilingi ngapi. Kwasababu wenzetu wa kwenye Halmashauri wanatoza gharama kubwa utafikiri kile kifaa labda ni chaki kwamba ukiandikia inakwisha, kumbe kifaa kile ni kuweka battery kwenye charge ukaenda ukakitumia kinakuwa kinaendelea kudumu.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hilo, eneo la Ngamiani Kati, Ngamiani Kaskazini na Ngamiani Kusini ambayo ndiyo kioo cha Mji wa Tanga; eneo lile lilipimwa zamani enzi za wakoloni watu wakapewa offer lakini hawana hizi hati kubwa za kisasa. Sasa nilikuwa naishauri serikali, kwa gharama zake, kwasababu pale asilimia kubwa nyumba zile ni za mirathi, wengine wameuza, wengine hawaelewi taratibu; kwahiyo napo Serikali ingepima eneo la kuanzia barabara ya kwanza mpaka barabara ya 21 ili na wananchi wale wapatiwe hatu ambazo zitawasaidia katika matumizi yao ya kila siku.

Mheshimiwa Spika, kama hili halitoshi, kuna mgogoro mkubwa sana sasa hivi kati ya Halmashauri na wananchi wa maeneo ya Mabokweni na Kirare na maeneo ya Amboni Cross Z. Tunajua kuna Kampuni ya Amboni ilikuwepo. Kamouni ya Amboni wakati huo, Waziri wa Kilimo na Mifugo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Wataalam wa Afya Shirikishi wa Mwaka 2016
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia leo kukutana katika Bunge letu hili ili tuzungumzie masuala mbalimbali ikiwemo suala hili la Sheria ya Madaktari wa Meno na Wataalam wa Afya Shirikishi (The Medical Dental and Allied Health Professionals Act, 2016).

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile pia niunge mkono Kambi Rasmi ya Upinzani katika hotuba yao, pamoja na kuunga mkono na mimi nina yangu machache kuhusu mchango wangu kwenye jambo hili. Madaktari ni watu muhimu sana katika maisha ya binadamu na tunaweza kusema kwamba madaktari ni sawa na mainjinia wa miili ya binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nikubali kwamba kweli madaktari wetu wanafanya kazi ngumu na ukiangalia pia mishahara yao siyo sawa na wale waliopo katika nchi nyingine. Kwa mfano, nimewahi kipindi fulani kuishi Swaziland nimekuta madaktari wengi wanatoka Tanzania na Kenya, madaktari ambao wanafanya kazi vizuri, lakini wameona maslahi yao wanapokuwa katika nchi zetu hizi za Afrika Mashariki ni madogo wakaamua kwenda katika nchi za Kusini mwa Afrika huko. Kwa hiyo, niwashawishi tu madaktari kwamba kazi yao ukiangalia historically imetokana na kazi ya wito wa kumuhudumia binadamu basi pamoja na maslahi lakini waangalie pia ule ubinadamu na wawe na uzalendo wa kufanya kazi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kusema ni kwamba madaktari wanatakiwa wawe na huruma kwa wagonjwa wetu, pia wajaribu kutumia ubunifu wao na weledi wao katika kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma nzuri za kidaktari.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli kama tunavyojua tunatumia gharama nyingi sana kupeleka wagonjwa wetu nje ya nchi. Serikali inatumia gharama nyingi hali ya kuwa kumbe wao kama watatulia na kama wataeleza shida zao kwa Serikali wataweza kusaidiwa hata kwa kiwango ambacho kitakuwa labda ni asilimia 50 ya vile wanavyotaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema hapa ni kwamba pamoja na kuwa madaktari ni watu muhimu kwetu, lakini kinachohitajika zaidi ni kwanza waishauri na wao Serikali pale wanapoona kuna baadhi ya mambo yanawakwaza. Kwa mfano, kumekuwa na gharama kubwa katika vifaatiba, kwa mfano, CT Scan, MRI, Ultra Sound Machine na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine ukiangalia gharama hizi katika nchi yetu zinakuwa ni kubwa, kwa sababu tunakuwa tunarundika au tunaweka kodi kubwa katika vifaa hivi. Kwa mfano, kwa wenzetu wa Kenya ambao tunapenda kutoa mfano sana kwao, utakuta vifaa kama hivi siyo lazima viwepo katika hospitali kubwa kama Muhimbili, Bugando labda na KCMC hata hospitali za kawaida za madaktari binafsi wanavyo. Kama unavyojua, kitu chochote kikiwa kwa wingi bei inapungua, lakini Watanzania bahati mbaya hizo CT Scan, MRI na mashine nyingine zinakuwa zina masharti magumu kwanza kuziingiza lakini pia zipo katika hospitali kubwa tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano wa mwananchi mmoja katika Jimbo langu ambae alikuwa na tatizo juu ya kipimo hiki cha MRI na hii CT Scan; yeye alifika Dar es Salaam, gharama za hiki kipimo kilikuwa takribani fedha za Kitanzania shilingi 400,000 lakini bahati nzuri akawa ana jamaa yake Kenya. Baada ya kumpa hii taarifa ya ugonjwa kutaka msaada akamshauri aende Kenya, alipoenda Kenya akakuta gharama ya vipimo hivi ni shilingi 12,000 ya Kenya ambayo ni takribani shilingi 60,000 ya Kitanzania. Hii inasababisha madaktari wetu vifaa hivi vinakuwa ni vichache, wanashindwa kufanya kazi zao kwa nafasi, sasa nitoe wito kwamba hivi vifaa vipunguzwe bei kusudi madaktari wetu sasa waweze kuvitumia, waoneshe ujuzi walio nao na wawasaidie wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika ukurasa wa tano wa sheria hii imeelezwa kwamba sheria inayopendekezwa kutungwa inalenga kufuta Sheria ya Madaktari na Madaktari wa Meno Sura ya 152 na kutunga Sheria ya Madaktari wa Meno na Wanataaluma, lakini mwisho wake utakuta ni kwamba lengo kubwa itasaidia kuongeza ufanisi kwa watendaji kwa kuongeza viwango vya ubora wa wahitimu na fani hizi nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna kipengele kingine pia kimezungumzia hapa kwamba lengo kubwa ni kutoa huduma bora kwamba pawe na huduma bora kwa wananchi wetu, sasa naamini kwamba sheria hii inapitishwa ili kuwapa uwezo madaktari wetu wa kufanya kazi kwanza kwa kujiamini lakini pia kuna maelezo ambayo yalielezwa hapa kwamba madaktari wetu hawa kuna sheria iliyokuwepo imeshindwa kukidhi hali ya mabadiliko na ongezeko la wahitimu wa taaluma hizi ikiwemo kutotoa nafasi kwa Baraza la Taaluma kushauri juu ya mitaala ya elimu, wanataaluma na utendaji wa kazi za kitaaluma pamoja na utatuzi wa migogoro kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda mimi niseme tu kwamba, lengo la sheria hii tunayoipitisha ni kuwafanya madaktari wetu sasa waweze kufanya kazi zao kwa nafasi, wito wangu kidogo kwa madaktari ni kwamba kwanza, nimpongeze hii hatua ya kwamba Mwenyekiti sasa wa Baraza la Madaktari atateuliwa na Waziri mwenye dhamana. Mimi ninashukuru kwamba kwenye nchi yetu mara nyingi Mawaziri wetu wa Afya wanakuwa nao ni madaktari, wanakuwa wanaelewa wale wanaowateua kwamba watakuwa ni watu wa namna gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nitoe wito kwa madaktari pia kuna tabia ya madaktrai kuzungumza kama anafanya kazi katika hospitali ya Serikali, unakwenda pale wewe ni mgonjwa anakuambia kwamba mimi katika hospitali hii ninakuwa sina muda mzuri wa kutibu, lakini ukija kule kwenye hospitali yangu kule nina muda mzuri sana wa kukutibu. Ninatoa wito kwa madaktari wasiseme maneno haya, anapofanya kazi katika hospitali ya Serikali bado ni daktari wa nchi hii, lakini hata anapokwenda kwenye hospitali yake bado ni daktari pia wa nchi hii, kwamba anayemtibu na anayemsaidia kumpa huduma ni Mtanzania mwenzie, kwa hiyo amhudumie kwa roho ya upendo na atumie elimu aliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kufanikisha matibabu ya yule mgonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine pamekuwa na tabia moja kwa madaktari kuthamini zaidi maslahi. Anamuona labda mgonjwa huyo amekuja hana uwezo, lakini anashindwa kutumia huruma, kwa sababu mimi najua daktari ana uwezo wa kutumia mamlaka yake aliyonayo kumuandikia mtu hata msamaha. Lakini mtu amekuja hapa pengine hana uwezo wa kununua dawa, anaachwa mpaka mtu anakuwa na hali mbaya au hata kupoteza maisha kwa sababu tu pengine hana shilingi 150,000 au 200,000. Mimi nawaomba madaktari watumie nafasi watakayokuwa wamepewa lakini pia watumie sheria hizi vizuri ili lengo kubwa iwe ni kutoa huduma bora kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwa madaktari wetu wawe na uchu wa kujifunza, wawe na wivu wa kimaendeleo, waone kwamba kwa nini wagonjwa wengi wa Tanzania wanatumia gharama kubwa kwenda nje wakati kumbe wao nao wangekaa kwenye hilo Baraza la Madaktari wafanye utaratibu wa magonjwa yale ambayo yatakuwa yanasumbua sana. Ni bora kuleta hata madaktari kutoka nje wakaja wakawafundisha madaktari wetu hapa Tanzania gharama zile kubwa za kutoka Tanzania kwenda katika baadhi ya nchi kufuata tiba watibiwe hapa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa Hospitali ya Moyo ya Dar es Salaam, wamejitahidi sasa hivi operation zinafanyika hapa nchini. Sasa isiwe kwa ugonjwa wa moyo tu, hata magonjwa mengine yawe yanatibiwa hapa. Mimi najua madaktari wetu wana uwezo mkubwa sana, najua wana elimu ya kutosha lakini kubwa ninaloliona linaloshindikana ni kwamba kwanza wamekuwa hawafanyi kazi as a team. Kama madaktari wa hospitali za private, madaktari wa hospitali za government watakaa pamoja na kufanya kazi pamoja, ninaamini maradhi yanayotusumbua ambayo yameibuka kama cancer ambayo iko katika hali ya juu sana, magonjwa kama ya kisukari, pressure ambayo sijui kwa nini magonjwa haya katika miaka ya sasa hivi yameibuka sana lakini madaktari nao pia wako kimya. Hawatuambii nini kinachosababisha magonjwa haya yakaendelea kwa muda mrefu. Kama watakaa pamoja kwa muda mrefu na kufanya tafiti ambazo watakuwa wanatoa matokeo yake mimi naamini wataweza kufikia katika hatua ambayo wataepusha wananchi wetu kwenda nje kwa matibabu.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho niseme kwamba, kumekuwa na tabia ya kwamba madawa na tafiti nyingi tunategemea kutoka nje, madaktari wetu sasa wanategemea labda mpaka wasikie aina fulani ya matibabu imetoka labda Marekani, imetoka Ulaya au Asia. Mimi natoa wito, madaktari wetu na wao wawe wabunifu wa huduma ambazo watatoka watu kutoka Ulaya na Marekani nao waje wajifunze kutoka huku kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nasema ahsante kwa kunisikiliza.
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kupata nafasi ya kuzungumzia Muswada huu ambao tunaujadili sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala zima la taulo za kike. Kwa hesabu za haraka haraka kutokana na kutokumudu gharama za ununuzi wa taulo za kike, mtoto wa kike hukosa masomo kwa mwezi kati ya siku tatu mpaka sita na ukipiga mahesabu kwa mwaka anaweza kukosa kati ya siku 36 au siku 72 kwa mwaka. Sasa hatumtendei haki kwa sababu tu ya kukosa taulo za kike kwa vile anapokuwa katika mazingira hayo anakuwa hayuko huru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha kusema kwamba eti baada ya kupewa punguzo la VAT kwa asilimia 25 walionufaika ni wafanyabiashara, hili sikubaliani nalo. Kama vile tunavyopiga marufuku bidhaa nyingine, kwa mfano, tulivyopiga marufuku mifuko ya plastic, tumeweza, Serikali yetu imejitahidi imepunguza mpaka matatizo ya dawa za kulevya, tumeweza, inakuwaje wafanyabiashara watushinde baada ya kuwasamehe asilimia 25 wawe wanafaidika zaidi kuliko Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu ushauri kwamba kwa kuwa taulo hizi zinatumiwa na watoto wetu, dada zetu, shangazi zetu, mama zetu na wake zetu ikibidi kodi hii iendelee kuondolewa. Mwaka jana wakati nikichangia nilitoa mfano, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisaini sheria kwamba wanafunzi wote nchini Kenya wapatiwe taulo za kike bure na Serikali inafidia. Sasa ukiitazama Kenya haina resource nyingi kama sisi Tanzania, sisi tuna Mlima Kilimajaro, mbuga za wanyama nyingi kuliko Kenya, madini ya aina zote, gesi, tuna dhahabu, almasi, kwa nini tushindwe na Kenya? Nashauri Serikali yetu itoe taulo za kike bure kwa watoto wa kike ili wapate uhuru wa kujinafasi katika masomo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua na wewe ni mwanamke hili linakuhusu, huoni ambavyo umepata elimu wewe mpaka leo umekuwa Naibu Spika na inshaallah Mwenyezi Mungu akijaalia pengine kipindi kijacho utakuwa Spika, basi na wewe utusaidie kupiga debe tuhakikishe kwamba watoto wa kike wanapatiwa taulo za kike bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala zima hili la kupata tax holiday kwa wafanyabiashara. Kilio hiki kwa kweli Wabunge tumekisemea sana lakini tunashukuru kwamba Serikali imeweza sasa kutoa ile tax holiday ya miezi sita kwamba mfanyabiashara wa Tanzania naye awe kama mfanyabiashara wa Kenya, Burundi au Uganda apate kujiweka sawa kwenye biashara yake, ajihakikishie biashara yake inakwendaje kuangalia faida na hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoshauri, mara nyingi tunavyopitisha mambo hapa ukifika kule chini unaambiwa Waraka bado haujafika. Kwa mfano, suala la msamaha wa kodi ya vyombo vya usafiri tulipitisha hapa tukaipeleka kwenye mafuta lakini pia suala la kufanya transfer kwenye vyombo hivi vya usafiri kukawa kuna tatizo unaambiwa Waraka haujapelekwa chini. Naiomba Wizara na Serikali kwa ujumla, tunapopitisha mambo hapa basi Waraka haraka upelekwe kule kwa wananchi kwa sababu jambo likiwa la kumnufaisha mwananchi Waraka unachelewa lakini jambo likiwa la kumbana mwananchi likitamkwa tu hapa Bungeni, kesho asubuhi linaanza kufanyiwa kazi. Sasa tunaomba hizi tozo na kodi mbalimbali ambazo zinasamehewa basi Waraka ushuke kule chini ili wananchi wetu wasiweze kusumbuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala zima la vitambulisho hivi vya wajasiriamali. Sasa hivi tunaona jinsi Wabunge wanavyopiga kelele hapa lakini sasa ni kweli kwamba vimepitia kwa Wakuu wa Mikoa na ma-DC, imekuwa mpaka bodaboda naye pamoja na kwamba analipia license, TRA, sticker kwenye Halmashauri na malipo mengine kadha wa kadha lakini bado anaongezewa mzigo sasa wa kulipa kitambulisho kile cha ujasiriamali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyosema wenzangu, kwanza havina ubora kwa sababu hakina picha, hakielezi aina ya biashara lakini bodaboda na yeye ni dereva kama alivyo dereva tax kwa sababu ana license, kama alivyo dereva wa basi na kama alivyo dereva wa gari ya private. Sasa kama tunamshushia Sh.20,000 ya kitambulisho cha ujasiriamali bodaboda maana yake sasa madereva wa Wabunge nao watalipa Sh.20,000 ya kitambulisho, madereva wa mabasi watalipa kitambulisho na madereva wa tax watalipa. Mimi naona bodaboda tuwaache waendelee kulipa SUMATRA, TRA, sticker katika Halmashauri na walipie vile vituo vyao vya bodaboda ule ujira ambao wamepata kulipa katika kila kituo cha bodaboda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bodaboda huyu tuumbuke pikipiki sio ya kwake, yeye ameajiriwa. Kwanza apeleke hesabu kwa tajiri halafu apate fedha za kujihudumia yeye na familia yake, kwa kweli tunawatwisha mzigo mkubwa bodaboda. Mimi naomba tuliondoe suala hili kwa bodaboda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwenye suala zima hili za kuongeza kodi katika vifaa vya ujenzi. Nimeona kwenye kitabu kwamba ipo katika East African Common Tariff lakini tujiulize sisi Watanzania kwanza ni soko kubwa sisi la bidhaa za plastic za Kenya, pili tunapoongeza kodi kwenye bati, nondo, fito za plastiki, mabomba ya plastiki, tujue tunaongeza gharama za ujenzi. Mtu wa kawaida nyumba anaweza akajenga kwa miaka saba au nane, leo tena badala ya kumshushia gharama za ujenzi, tunamuongezea. Mimi naona kwenye hili wale wawakilishi wetu, Waziri wa Fedha mnapokutana katika vile vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki mjaribu kututetea sisi Watanzania ili na sisi tupate manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninaloshauri katika hili, hizi bidhaa pamoja na kuongezewa kodi, mimi naomba ziondolewe, lakini zitakapoondolewa kodi pia pawe na nembo maalum ya ubora kwa sababu wananchi wa kawaida labda wa vijijini hawezi kujua kwamba nondo hii inatoka Kenya au hii imezalishwa kwenye kiwanda cha ndani. Hawezi kujua plastiki hii inatoka Kenya au plastiki hii inatoka kwenye viwanda vya ndani. Mimi nafikiri ni vyema tuhakikishe vinakuwa na nembo ya ubora ambayo itasaidia sasa wafanyabiashara wale wasije wakatufanya kama kwenye taulo za kike…

T A A R I F A

MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk, kuna taarifa.

MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni jana tu nilitaka nimpe taarifa msemaji aliyekuwa akichangia, Wabunge wengi wa upande wake ikiwemo na yeye ni miongoni mwa Wabunge walioikataa bajeti ya shilingi trilioni 33 isipite.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Twendeni taratibu tu, daktari akichelewa kazini na akakutibu, twendeni taratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sisi tulijipanga na bajeti yetu ya shilingi trilioni 33 na wao wakaikataa, sasa kile anachokichangia tuondoe ushuru kwenye maeneo mbalimbali angetueleza mbadala wake utakuwa ni nini? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk, malizia mchango wako.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sipokei taarifa yake. Kwanza huyu ni mtoro, anazungumza kusudi asije akatajwa kama alivyotajwa mara ya kwanza kwamba ni mtoro. (Makofi)

MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Kuhusu utaratibu

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea, lingine, kwenye mitambo ya kuchimba visima, naamini unajua kwamba kama unavyosema kwamba likizungumzwa suala la maji….

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk kuna kanuni inavunjwa.

MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni taratibu za kawaida unapopewa taarifa either uikubali ama uikatae, anakubali taarifa yangu ama anakataa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niendelee kusema kwamba….

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk. naomba ukae kidogo.

Waheshimiwa Wabunge huwa nawakumbusha mara kadhaa, Kanuni ya 68(8), unapotoa taarifa, ni kwamba anayezungumza amekuwa amezungumza jambo ambalo wewe unataka kuongezea hapo.

Kwa hiyo, hoja ya mimi kuuliza kama taarifa mtu anaipokea ama haipokei, ni mpaka iwe taarifa, kwa muktadha wa kanuni zetu na tusome, kanuni ya 68(8). Mheshimiwa Mbarouk malizia muda wako.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nililopenda kuzungumzia ni kwenye mitambo ya kuchimba visima, nashukuru kwamba, hili nalo tumelizungumza, lakini niombe kwamba, kodi nayo ipunguzwe kwenye mitambo ya kuchimba visima kwa sababu, watu wengi au Wabunge wengi linapozungumzwa suala la maji hapa wanakuwa wanachangia sana, kila mmoja analalamika kwamba, maji kwake hakuna, lakini ikiondolewa kodi kwenye mitambo hii ya kuchimba visima, wachimbaji watapunguza gharama za uchimbaji na vilevile wataisaidia Serikali katika kumtua mwanamke ndoo kichwani. Kwa hiyo, naomba suala hili nalo liangaliwe, ili watu hawa waweze kusamehewa kodi katika mitambo ya visima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho, nimalizie sekta ya uvuvi, kwenye suala la uvuvi, tumeona kwamba, baadhi ya wavuvi ni sehemu ya mapato ya nchi yetu, lakini kwa mfano, baada ya kuchomwa nyavu, lakini wapo wavuvi wengine mashine zao zilichukuliwa kama bond kwao. Sasa niombe, wale wavuvi waliokuwa wamechukuliwa mashine zao kwa mfano kule Tanga, warudishiwe kusudi waendelee na shughuli za uvuvi ili waweze kulipa kodi na kuchangia pato la taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia kuwa na afya njema na kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Maji. Vile vile nami niungane na Wabunge wenzangu na Watanzania kwa ujumla kutoa pole kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki ambao watoto wao wamefariki katika ajali kule Mkoani Arusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo pia natoa nyingine kule kule Arusha, kama tulivyoona katika vyombo vya habari kuwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mti umeanguka na msiba mwingine umetokea wakiwemo watoto wamefariki. Pia nitumie fursa hii kutoa pole za dhati kabisa kwa wananchi wangu wa Jimbo la Tanga kwa mafuriko makubwa yaliyotokea ambapo yamesababisha uharibufu wa mali, maisha na vile vile pia madaraja yamekatika na kukata mawasiliano kati ya mji wa Tanga na Pangani na vilevile Lushoto na Tanga Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nianze kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitabu cha Mwenyenzi Mungu cha Qurani kwenye Surat Anbiyaa aya ya thelathini Mwenyezi Mungu anasema wajaalna minal-mai kul shaiyn hai; kwamba ametujalia sisi binadamu kwamba maji ni uhaki kwa kila kitu. Utaoa ni namna gani Mwenyezi Mungu mwenyewe ametoa umuhimu kwa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji hayana mbadala, umeme ukikatikaunaweza ukaweka kibatari, lakini maji yakikatika hakuna mbadala. Kwa hiyo, naitaka Serikali ijue kwanza umuhimu wa maji kwa maisha ya binadamu. Vile vile mahitaji ya si kwa binadamu tu, wanyama, wadudu, ndege na kadhalika na kadhalika wote wanahitaji maji; mpaka vyombo vya moto tunavyovitumia pia vinahitaji maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inashangaza Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya maji na mifugo kupunguza bajeti ya maji kutoka Shilingi za Kitanzania bilioni mia tisa thelathini na tisa na kurudi chini hadi bilioni 623, hilo jambo haliingii akilini hata kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nami niungane na Mheshimiwa Zitto Kabwe na Waheshimiwa Wabunge wengine waliosema kwamba bajeti hii irudi ili ikarekebishwe iongezwe; kwamba kutoka shilingi milioni mia sita za mwaka 2017/2018 ipande. Haiingii akilini kwamba ikiwa maji yanamhusu kila mtu lakini bajeti tunaipunguza wakati ndiyo sehemu muhimu katika maisha ya binadamu. Kwa hiyo naungana na wale wote waliosema kwamba bajeti hii irudi na ikongezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, siishii hapo. Jambo lingine kwenye suala zima la maji, sasa hivi maji katika baadhi ya mikoa kwa mfano katika jimbo langu bei ya maji sasa hivi imekuwa ghali kuliko umeme; na wananchi wanahitaji maji kwa shughuli za kimaendeleo lakini maji yamekuwa hayapatikani kama yanavyokusudiwa. Pia katika jimbo langu siku za karibuni maji yamekuwa ni machafu kuliko maelezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namtaka Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa; nilitoa mwongozo siku moja akasema alikuwa hana habari; sasa nataka pia anijibu kupitia majibu yake kwamba amegundua nini mpaka Tanga iliyokuwa na historia ya maji safi kabisa leo yanatoka machafu kama chai ya maziwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka kulizungumzia ni miradi ya maji vijijini. Miradi ya maji vijijini Serikali imepata ufadhili wa Benki ya Dunia, sasa kinachotushangaza Benki ya Dunia wametoa fedha kwa nini miradi ile haikamiliki? Kwa mfano mimi nina miradi ya vijiji kumi, kuna mradi unaoelekea kaskazini na kuna mradi unaelekea kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi wa Kaskazini maji yameishia sehemu moja inaitwa Mabokweni ambayo ndiyo jina la kata vile vile; lakini mradi unatakiwa ufike mpaka Kata ya Chongoleani kwenye Vijiji na Vitongoji vya Mpirani, Kibafuta, Mchanga Mweupe, Mchana Mwekundu, Putini, Helani hadi Chongoleani kwenyewe na kufikia Bagamoyo; lakini mradi kule Mkandarasi ameondoa mpaka vifaa anasema anaidai Serikali na hajalipwa fedha zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napata kigugumizi hapa kujiuliza, fedha tunaambiwa zimeletwa na benki ya dunia kwa nini mradi haukamiliki na wananchi wanapata shida? Wameeleza wengi hapa; akinamama kule Tanga wamekuwa na vipara kama wanaume kwa kubeba ndoo za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa Mawaziri nao ni watoto waliozaliwa na mama, binadamu wote wamezaliwa na mama, kwa nini basi hata kama wao hawana huruma, wangewaonea huruma hawa akinamama ambao ndio waliotuleta sisi hapa duniani. Maji ni bidhaa muhimu katika maisha ya kila siku ya binadamu. Kwa hiyo, namtaka Mheshimiwa Waziri, hili la kwamba bajeti irudi ili iongezwe alizingatie.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine linahusu miradi ya maji vijijini; baadhi ya contractors wa miradi ile ya maji wamefikishwa mahakamani kwa sababu na wao wamekopa materials ili wakaendeleze ile miradi, hawajalipwa na Serikalini kwa kwa muda mrefu kumekuwa kuna ubabaishaji hapa. Naomba hilo pia Mheshimiwa Waziri atueleze kwa nini wakandarasi wale wa maji hawalipwi na ikiwa fedha za World Bank zimetoka na wao kwa kuisaidia Serikali yao lakini wanapelekwa mahakamani kwa kuwasaidia wananchi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Maji Taka. Wamesema wazungumzaji wengi hapa kwamba hata mifumo ya maji taka katika mikoa yetu, majiji yetu na manispaa zake si mizuri na lazima tujue tukiwa na mfumo mbaya wa maji taka ndicho kinakuwa chanzo kikubwa cha malaria. Kwa sababu kama utakuwa na mfumo nzuri wa maji taka maji yatakakuwa hayasimami, hayatuami, yatakuwa yanakwenda ambapo mbu hawatoweza kuzaliana.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji taka yanayotuama na kumwagika hovyo kwanza yanaharibu mandhari ya miji yetu lakini pia harufu na pia kusababisha magonjwa ya milipuko kama kuhara na kutapika. Kwa hiyo, lazima wizara inayohusika ihakikishe inatilia nguvu ama kwa kutafuta wafadhili au kupeleka fedha pia katika miradi ya maji taka.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo wananchi wanahitaji kuwekewa mfumo wa majitaka kwa mfano katika jiji letu la Tanga lakini Mamlaka ya Majisafi na Majitaka hawana uwezo, wanasema tu tuna uwezo wa kukarabati si kuanzisha miradi mipya ya mifumo ya majitaka. Naitaka Wizara pia ipeleke fedha katika Mamlaka ya Majisafi na Majitaka kwa Jiji la Tanga ili iweze kuweka mfumo wa maji taka na hivyo tuondokane na maradhi ya milipuko pia na masalia ya mbu yanayosabisha malaria.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia katika suala la maji ni kwamba maji katika Halmashauri ya Tanga ilikuwa ni historia. Halmashauri nyingi na Waheshimiwa Wabunge watakuwa ni mashahidi hapa walikuja kujifunza ku-treat maji kutoka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka ya Tanga. Leo wananchi wanapata tabu mpaka maji yanatoka machafu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile pia nimuulize Mheshimiwa Waziri kupunguza bajeti haoni kwamba hili ni tatizo? Leo tuna miaka 56 ya uhuru maji wanayokunywa wanyama wa porini ndiyo hayo hayo maji wanayokunywa binadamu. Yapo baadhi ya maeneo unakuta watu wanachota maji kwenye madimbwi ya barabarani au kwenye mifereji pembeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii hali ni mbaya, haiingi akilini nchi kama Tanzania iliyojaliwa raslimali lukuki lakini tunashindwa kusimamia hata maji; mimi nasema hili jambo ni la aibu sana. Lazima Mheshimiwa Waziri aliyepewa dhamana utuletee mfumo mpya; pamoja na kurudi na bajeti lakini ukija uje na mikakati mipya ya kuwasaidia wananchi wetu wa vijijini. Sote hapa tunatokea vijijini lakini kama vijijini kutakuwa hakuna maji safi na salama ina maana watu wote watazidi kuathirika na maradhi yataongezeka.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Nami nichukue fursa hii, kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tupo katika enzi ya viwanda na uchumi wa kati, lakini kiukweli kabisa ni kwamba yanahitajika maandalizi thabiti. Sasa ni maeneo mengi ambayo tumekusudia kuyafanyia kazi. Jambo la kwanza kabisa ili tuwe na viwanda vya uhakika, ni lazima vilevile pia tuwe na umeme wa uhakika. Sasa ni mara nyingi tumekuwa na tatizo la umeme. Mheshimiwa Waziri atakapokuja naomba atuthibitishie, ni kweli tutakuwa na umeme wa uhakika? Kwa sababu viwanda bila umeme inakuwa ni kama kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Tanzania sisi ni wa tatu wa idadi kubwa ya mifugo; kama sikosei, baada ya Ethiopia na Botswana ni sisi tunaofuatia Tanzania. Ukiangalia wenzetu wa Botswana, ng’ombe anapoingia katika kiwanda cha kuchakata nyama, hakuna kinachotoka. Ngozi ina shughuli yake, nyama ina shughuli yake, pembe ina shughuli yake na kwato zina shughuli yake. Sisi Watanzania pamoja na mifugo tuliyokuwa nayo, bado hatujaweza kuitumia mifugo vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, tutafute wawekezaji wenye uwezo wa kujenga viwanda vya kusindika nyama. Vilevile pia wenzetu wa Ethiopia, kwa mwaka 2016, wamepata takriban Dola 186,000 kutokana na ngozi peke yake. Wanatarajia mwaka 2017 kupata vilevile Dola za Kimarekani kuongeza idadi ya Dola 90,000,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo, mpaka 2017 ikimalizika watapata zaidi ya Dola 276,000,000. Sisi Watanzania badala ya kuitumia mifugo vizuri, imekuwa tunazalisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine iliwahi kutokea hapa kwamba Maafisa wa Wanyamapori, wakagombana na wafugaji, ng’ombe wakapigwa risasi, wafugaji wale wakadhalilishwa, hadi kupelekea baadhi ya Mawaziri kujiuzulu katika Serikali ya awamu iliyopita. Kwa hiyo, naishauri Serikali tutumie mifugo vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Watanzania tumekuwa tunashindwa na baadhi ya nchi ambazo zimekuwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe. Tukumbuke Ethiopia waliwahi kuwa na vita na Djibout, lakini baada ya kumaliza vita, wamekaa wamepanga mambo mazuri namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, ng’ombe pia wanazalisha maziwa, lakini Watanzania tumeshindwa kuyasindika. Matokeo yake tunaagiza maziwa ya kopo kutoka nje. Tunaagiza Nido, Lactogen, Nan; hali ya kuwa maziwa ya ng’ombe yangepakiwa vizuri, yangeweza kuwasaidia wananchi wetu. Kwa hiyo, naishauri Serikali itafute wawekezaji wa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye suala zima la viwanda; tuna matunda. Kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Tanga, Lushoto ni wazalishaji wa matunda na mboga mboga za aina nyingi. Muheza kuna kilimo kikubwa cha machungwa, lakini pia unakuta tunaagiza juice za Ceries kutoka South Africa na Saud Arabia ambayo ni nchi iko jangwani. Inakuwaje sisi ambao tunazalisha machungwa by nature lakini tunashindwa kuyachakata tunaagiza juice kutoka nje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali tutafute wawekezaji wa uhakika. Tusizungumze suala la viwanda kisiasa; tuwe na dhamira ya dhati na ya kweli. Viwanda hivyo vitakapojengwa wananchi wetu watapata ajira lakini vilevile Serikali pia itapata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nililotaka kuzungumza, moja ya matatizo yanayofanya wawekezaji wasije Tanzania, ni mifumo mibovu ya kodi, umeme usiokuwa wa uhakika, lakini vilevile pia kuna kitu kinaitwa urasimu. Mtu akitaka kuwekeza kiwanda Tanzania, atahangaishwa, itafika miaka miwili. Wenzetu Uganda ndani ya masaa 48 ukitaka kuwekeza unapata kila aina ya msaada unaotaka na Serikali inakwambia, kama unataka kuongezewa mtaji pia iko tayari, lakini Tanzania hilo hatulifanyi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe kwanza inaweka miundombinu rafiki, mifumo mizuri ya kodi, lakini tuondoe urasimu. Vilevile pia nataka kuiambia Serikali…

(Hapa kengelee ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema. Pia nawatakia Waislam wote Tanzania na duniani kwa ujumla Heri na Baraka ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahusiano ya Kimataifa; Tanzania bado ni nchi inayotambulika kuwa bado amani na utulivu unapatikana, lakini kadri siku zinavyokwenda mbele Tanzania inapoteza heshima na umuhimu tunaopewa na dunia. Mfano, moja, demokrasia inaminywa kwa kutoruhusiwa mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbili, maiti zinazookotwa katika mito na fukwe za bahari na mito na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani, Waziri Mwigulu Nchemba anajibu bila shaka hao maiti ni wahamiaji haramu. Napata shaka dunia itatuelewaje Watanzania? Je, wahamiaji hawatakiwi au tumepitisha sheria ya kuwaua hao wahamiaji haramu?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri Mheshimiwa Dkt. Mahiga alijibu Bunge na kutoa tafsiri sahihi kwa kuwa badala yake Watanzania waishio nje ya nchi (Diasporas) wanaweza kudhuriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania waliofungwa nje; katika nchi nyingi duniani, Watanzania katika kutafuta maisha, wanapatikana na hatia mbalimbali kama vile:-

(a) Kuishi bila ya “Permit” au “overstay” baada ya VISA kuisha na kufungwa magerezani.

(b) Wanaotuhumiwa kujihusisha/kushirikiana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Mfano, familia ya Tanga iliyokamatwa China na mtoto wao wa miaka mitatu kurudishwa nchini kutokana na tuhuma za dawa za kulevya.

(c) Wanaokwenda kutafuta ajira za viwandani, mashambani na majumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali, je, Serikali ina mpango gani wa Kidiplomasia wa kubadilishana wafungwa ili warejeshwe Tanzania kuhukumiwa kwa Sheria zetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanja vya Ubalozi tunavyovitelekeza; kwa masikitiko makubwa, natoa hoja hii nikiwa bado nashangaa kuwa Serikali ya Kifalme ya Oman imetupa Kiwanja “Low Density” huko Muscat, lakini mpaka leo tumeshindwa kukijenga. Nashauri Serikali itafute fedha na kujenga na kuondoa aibu hii inayochafua Taifa letu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuweza kuchangia bajeti ya Wizara hii. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja hatua ya Kambi Rasmi ya Upinzani. Tanga ulikuwa ni mji wa viwanda na biashara pamoja na kilimo cha zao la mkonge (palikuwepo mashamba 72).

Mheshimiwa Naibu Spika, Viwanda vya Zamani. Tanga ina bandari na reli ambavyo viliweza kusafirisha bidhaa zinazozalishwa viwandani, wakati ule katika miaka ya 1970 -1990 ambapo pia ajira zilipatikana kwa wingi. Viwanda vingi vimelenga kwa ama kubinafsishwa na kupewa (kuuziwa) watu wasio na uwezo wa kuendesha aina za viwanda hivyo. Mfano Tanga, Steel Rolling Mill (chuma) kimekufa, hali ya kuwa chuma bado kinahitajika na kina soko kubwa katika ujenzi wa madaraja, nyumba, mabodi ya magari na bidhaa nyingine za chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Kamba Ngomeni Tanga kilikuwa kikizalisha kamba zitokanazo na zao la katani ambazo kwa sasa, mkonge umepata soko kubwa katika Soko la Dunia na kwamba bidhaa zitokanazo na katani zinahitajika sana kwa matumizi mbalimbali. Zana/ bidhaa za mkonge zina soko na mahitaji yake ni ndani na nje ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni mategemeo yangu kuwa kutokana na soko kuwa kubwa Serikali itawekeza upya au kutafuta wawekezaji makini na wenye uwezo wa kuendesha viwanda vya korona na viwanda vya kamba kwa lengo la kutoa ajira kwa Watanzania, lakini pia kuiwezesha Serikali kupata kodi na kuongeza mapato ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanga kulikuwa na viwanda vya sabuni kama Foma, Mbuni, Gardenia, mafuta ya nazi (nocolin) na kadhalika. Viwanda vyote nilivyovitaja vimekufa katika zoezi la ubinafsishaji mbovu lakini pia ukosekanaji wa umeme wa uhakika; vile vile kodi kubwa zilizopo. Hivyo nadhani kwa sababu nilizozitaja nimeeleweka. Ushauri wangu; viwanda vyote vilivyokufa au vilivyoshindwa kuendeshwa na wawekezaji wanavyovimiliki, vifufuliwe kwa kupewa wawekezaji wapya lakini pia Serikali ihakikishe kunapatikana yafuatayo:-

(i) Umeme wa uhakika na bei nafuu;

(ii) Mfumo wa kodi uwe rafiki kwa wawekezaji (VAT/CUSTOMs DUTY);

(iii) Vivutio vya kibiashara (Tax Holiday et cetera); na

(iv) Sheria ziwe rafiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Viwanda Vipya vya Nyama na Ngozi. Tanzania ni nchi ya tatu Afrika kwa kuwa na mifugo mingi lakini nchi yetu haipati/haifaidiki na mifugo hiyo ukilinganisha na nchi kama Ethiopia na Botswana. Vile vile mifugo (ng‘ombe) hutoa maziwa ambayo pia tunashindwa kuyasindika na kusimamia na hatimaye tunaagiza nyama za kopo (beaf tin) na maziwa ya kopo ya Lactogen, NIDO, NAN, Kerrygold, kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ethiopia imepata USD milioni 186 (2016) kwa mazao ya ngozi na inatarajia kuongeza US $ milioni 90 (2017) na kufikia USD 276 (2017). Je Tanzania inapata USD ngapi kwa 2015 – 2020? Zaidi ni migogoro ya wakulima na wafugaji, Maafisa Wanyamapori kuwapiga risasi ng’ombe na wafugaji na kashfa ile na kusababisha Mawaziri kujiuzulu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili (scandal) ya Wizara ya Maliasili na Utalii ilisababisha baadhi ya Mawaziri kujiuzulu. Ushauri wangu, (Serikali itafute wawekezaji wakubwa kuboresha sekta ya mifugo ili viwanda vya nyama na ngozi vijengwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vya kusindika mboga/matunda. Tanzania imejaaliwa na Mwenyezi Mungu katika mikoa na kanda aina mbalimbali za matunda na mboga mboga. Pia Tanzania inayo mito na maziwa yenye maji ya kutosha na kama tukifanya Irrigation scheme for fruits and vegetables tunaweza kupata mapato kwa wananchi (kujiajiri wenyewe). Serikali za mitaa zitapata mapato na Serikali kuu pia itapata mapato kutokana na kodi baada ya kulifanyia kazi kikamilifu eneo hili la kilimo cha matunda na mboga mboga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mazao ya Matunda na Mboga Mboga Katika Mkoa wa Tanga. Mkoa wa Tanga unazo wilaya nane (8) na kati ya hizi zipo ambazo ni wazalishaji wakubwa wa mazao husika na wilaya hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Muheza ni Wilaya inayozalisha matunda aina ya machungwa, machenza, madalanzi, malimao, mashuza, mafenesi na mapera, ambayo ikiwa Serikali itatafuta wawekezaji wa viwanda vya kusindika matunda ajira na mapato yatapatikana. Lushoto, ni wazalishaji wakubwa wa aina zote za mbogamboga na matunda (nyanya, vitunguu maji/saumu, cabages, spinaches, matango pamoja na pilipili hoho. Aina zote hizi zina soko kubwa katika Soko la Dunia (Europe na America) Serikali ilete wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda bila umeme ni sawa na gari bila mafuta. Umeme ndio Enquire kuu za viwanda, bila ya umeme wa uhakika, wataalam waliobobea na wenye weledi na uzalendo hata tujenge viwanda vingi kama utitiri baada ya muda vyote vitakufa tena. Ushauri, Serikali inahitajika kuhakikisha kwamba umeme wa uhakika unapatikana, mifumo ya kodi iwe rafiki na tuondoe urasimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuniwezesha kuchangia. Naunga mkono hoja ya hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani katika kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kupitia Waziri Kivuli, Mheshimiwa Cecilia Paresso.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Kamati ya Kilimo katika maoni na ushauri ilioutoa katika kitabu chake ukurasa wa tatu. Inashangaza kuona wafadhili wanatoa fedha nyingi kufadhili kilimo kuliko Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ili tuendelee tunahitaji mambo manne; moja, ardhi – kilimo, ujenzi, ufugaji, viwanda, barabara na kadhalika; pili, watu – wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara; tatu, siasa safi - kwa kuwa haipo; nne, uongozi bora – hakuna sababu. Uongo na mipango isiyotekelezeka. If you fail to plan, you plan to fail.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tupo hapa kwa kuwa plans zetu zote tume-fail na tunapeleka mambo kisiasa ili kuvutia wapiga kura. Asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima. Wizara hii ni nyeti na ni uti wa mgongo wa Taifa letu, inachangia 29% ya pato la Taifa letu na inatoa ajira 75% ya watu wetu. Kwa masikitiko makubwa, bajeti iliyotengwa ni 3.0%. It is the shame, hapa Serikali inafanya utani na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zilizotengwa katika bajeti; wafadhili 78%, fedha zetu 21%. Fedha zilizotengwa katika bajeti, shilingi bilioni nne mifugo, shilingi bilioni mbili uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mkanganyiko/ ugumu katika taasisi za fedha; wakulima ni wachangiaji na wazalishaji wakubwa katika uchumi wa Taifa letu, lakini ndio wanadharauliwa mno na Serikali haina mission wala vision. Wakulima katika benki wamewekewa masharti magumu, pamoja na kuwa na hatimiliki za ardhi, nyumba na vyombo vya moto. CRDB (Co-operative and Rural Development Bank) enzi za Mwalimu (by definition) ilikuwa ndiyo benki yao wakulima. Je, leo CRDB ni ya wakulima? Ni ya wafanyabiashara na wawekezaji. Yamewekwa mazingira na dhana kuwa wakulima hawakopesheki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni kizungumkuti, Tanzania haijaamua kutoa kipaumbele katika kilimo (first priority) kwa kuwa kilimo kinaendeshwa kisanii kwa matambo na misamiati mingi na siasa kibao:-

(i) kilimo cha kufa na kupona;

(ii) kilimo cha ujamaa na kujitegemea;

(iii) kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa letu,

(iv) kilimo cha bega kwa bega; na

(v) kilimo kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kwa misamiati hii ndiyo tutavuna mahindi, mpunga, viazi, mtama, ngano, alizeti, pamba na karafuu? Serikali ijipange na tusiwe wababaishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tumbaku na soko la nje, kilogramu 32,000 ni sawa na 3.2 tonnes iliyouzwa Uturuki kutoka Tanzania. Nchi nyingine wanaolima tumbaku wameuza tumbaku kilogramu 939,000,000, Uturuki (Europe). Hii inadhihirisha namna gani Serikali haiko serious katika mambo ya kiuchumi tofauti na nchi za jirani, Mozambique, Rwanda, Kenya, Uganda, na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga na zao la mihogo na matunda. Tanga ni wazalishaji wakubwa wa mihogo hususan katika maeneo ya vijijini. Mfano, maeneo ya Kirare, Mapojoni, Pongwe, Kisimatui, Marungu, Mkembe, Mpirani, Mabokweni, Putini, Bwagamoyo na kadhalika. Mihogo ya Tanga ni mihogo bora, mitamu na haina sumu ukilinganisha na mihogo ya maeneo mengi katika Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mihogo ya Tanga haina soko la uhakika ndani na nje ya Tanzania. Siku za karibuni China walitoa tangazo (tender) kwa kutaka zao la muhogo katika mitandao/media. Je, Serikali ya Tanzania, Mheshimiwa Waziri anatuambie? Wamelifuatilia soko hilo vipi? Wamefikia hatua gani ya majadiliano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu uvuvi na siasa za Tanzania. Norway ni nchi tajiri na mfadhili mkubwa katika miradi mingi ya kimaendeleo Tanzania na Afrika nzima. Utajiri wao unatokana na uvuvi ambao wameamua kuwekeza, kutafiti na kushughulika kikamilifu. Tanzania tunazo 1,400 cubic kilometres (Indian Ocean) kutoka Jasini – Mkinga – Tanga hadi Msimbati – Mtwara; ni bahari tupu na kuna samaki wa kila aina. Humo Indian Ocean kuna gesi pia, lakini Watanzania (Coastal zone are very poor people), ndio maskini wa kutupwa. Badala ya Serikali kuwasaidia, vyombo na nyavu zao zinachomwa moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba Serikali ithamini watu wa Ukanda wa Pwani katika Mikoa ya Pwani, Tanga, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Unguja, Pemba na Mafia kwa kutafuta wawekezaji (investors) wa viwanda vya kusindika samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijengwe vyuo vya uvuvi kwa ajili ya elimu ya uvuvi wa kisasa. If you fail to plan, you plan to fail. Jambo lolote likifanywa kitaalam (kielimu) linakuwa na manufaa makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi (registration fees 20,000 under 20mt boat); Serikali iondoe tozo/kodi ambazo ni kero kwa wavuvi. Tukiachilia mbali kodi iliyoondolewa kwa vyombo vyenye urefu chini ya mita 20, lakini bado Halmashauri inatoza tozo na Serikali Kuu inatoza tozo ya leseni kwa kila baharia. Leseni alipe nahodha tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, katika vyombo vingine kama bus, anaulizwa leseni dereva na siyo conductor wala turn boy? Kwani wavuvi ni wote?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika meli meli/ferry boat anahojiwa captain tu. Kwa nini wavuvi wanatozwa leseni? Samaki wao wanatozwa ushuru na vyombo vyao registration fees na kodi ya mapato (revenue). Matrekta hayana kodi, lakini mashua zina kodi kubwa. Badala ya kukamata vyombo na nyavu za wavuvi wadogo na kuzichoma (hasara), wazuie utengenezaji wa nyavu ndogo katika viwanda vyetu na iache kuchukua kodi na itoe vipimo vya nyavu (size) zinazohitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba kwa kuwa mara kwa mara wakati wa kaskazi ajali nyingi hutokea, hivyo Serikali iwe na Rescue Team Department isaidie kuokoa ajali zinapotokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mifugo, kuna usafirishaji katili, wanyama wengi wanateswa/kufa katika usafirishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna gharama kubwa za dawa kwa ajili ya kilimo na mifugo. Wanyama hawatendewi haki Tanzania kwa sababu hakuna chama cha kutetea haki zao. Wanyama kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku wanasafirishwa katika vyombo vidogo na wanabanana na kuumia hadi kufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba Wizara iliangalie suala hili kwa umakini kwa kuwa hata wanyama wetu wanakosa soko bora kwa kuwa nyama yao huwa na dosari.
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba (Intergovernmental Agreement – IGA) baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamuhuri ya Uganda kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East Africa Crude Oil Pipeline – EACOP) kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nianze kuunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya kusema hayo, nami nina yangu machache ya kuzungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya njema na kuweza kukutana katika Kikao chetu hiki cha Bunge na hatimaye kuipitia taarifa hii ya Intergovernment Agreement Between the United Republic of Tanzania and the Republic of Uganda Concerning the Pipeline System of the East African Crude Oil Pipeline Project.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nami nina yangu ya kushauri. Kwanza, nishukuru kwamba mradi huu umekuja kwenye Jimbo letu la Tanga ambayo itakuwa ndiyo last destination. Vilevile niwashauri wale ambao mradi huu utapita katika maeneo yao, katika mikoa nane, wilaya 24 na vijiji takribani mia moja na ushehe.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kwanza tushirikishe wananchi wetu katika suala hili lakini vilevile na Serikali nayo itoe maandalizi maalum kwa sababu wananchi wengi huu mradi wamekuwa wakiusikia juujuu, lakini hapa nishukuru kwamba Kamati yetu ya Nishati na Madini imelifanyia kazi vizuri na imetoa baadhi ya tahadhari na hata Kambi Rasmi ya Upinzani katika baadhi ya maeneo ambayo nikipata nafasi nikayataja huko mbele, imetoa tahadhari, lakini makubwa zaidi ninayoona ni haya yafuatayo.

Kwanza, Serikali iwe makini katika kila hatua kuepuka tabia ya kusaini mikataba ambayo baadaye inakuja kuonekana kuwa mikataba mibovu kama ilivyosemwa na Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu malipo ya fidia, yazingatie bei ya soko la ardhi iliyopo sasa na pasiwe na visingizio. Kwa mfano katika eneo la Chongoleani wananchi kule wamelipwa eka moja kwa thamani ya shilingi milioni mbili na baadhi walikuwa wakitaka ufafanuzi zaidi kujua kwa nini wanalipwa pesa hiyo kwa sababu wapo watu ambao walikuwa wamenunua, ule ni Ukanda wa Pwani kabisa, wapo watu waliokuwa wamenunua eka moja kwa zaidi ya hata milioni 10, lakini baada ya kutaka ufafanuzi tukaenda kwa Mkuu wa Mkoa wakaitwa wataalam wa ardhi wao wakasema tu moja kwa moja kwamba bei ya milioni mbili iliwekwa kabla hapajawekwa miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo kwa kweli lilileta taabu kidogo kwa sababu binafsi kwa maoni yangu niliwahi kuwaeleza kwamba lazima mjue wakulima hawa maeneo yao ambayo yalikuwa ndiyo chanzo chao cha mapato yanachukuliwa. Zao kubwa katika maeneo ya Chongoleani ni minazi, mihogo, midimu, milimao, michungwa na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nikueleze tu, ndimu katika maeneo ya Chongoleani imekuwa na faida kubwa sana kwa sababu mdimu mmoja unaweza kutoa visalfeti viwili na kila kiroba cha ndimu kikifikishwa katika soko la Dar es Salaam ni sawasawa na Sh.40,000. Kwa hiyo, mti mmoja wa mdimu unaweza kutoa katika zao la awamu moja Sh.80,000 ya Kitanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niliiomba Serikali kwamba kwa kuwa wananchi wale maeneo yao yanachukuliwa basi watafutiwe maeneo mbadala. Vilevile pia kama tunavyojua kwamba kuna thamani ya ardhi na thamani ya mimea, kwa hiyo, yote hayo niliitaka Serikali iyazingatie. Sasa nawashauri Waheshimiwa Wabunge wengine ambapo mradi huu utapita wawe makini na hilo ili tusije tukawarudisha wananchi wetu katika lindi la umaskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tujue kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu. Kwa kuwa Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Uganda tunaamua kuchukua maeneo yale ya wananchi, basi lazima wananchi wale tuwatafutie maeneo mbadala kwa ajili ya shughuli zao za kilimo. Kwa mfano, katika eneo la Chongoleani lipo shamba la mkonge linalomilikiwa na Kampuni ya Amboni Limited ambayo sasa hivi imebadilisha jina inaitwa Cotel Company Limited. Shamba lile limekuwa haliendelezwi, kwa hiyo, naiomba Serikali hususan Mheshimiwa Rais alifutie hati shamba lile la Amboni ambalo liko eneo moja linaitwa Mwanyungu na wananchi wale ambao maeneo yao yamechukuliwa wapewe maeneo ya Mwanyungu sasa katika shamba la mkonge ili waendelee na shughuli zao za kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba maeneo yamechukuliwa lakini fedha waliyolipwa haikidhi kwenda kununua mashamba au ardhi maeneo mengine. Wale ambao nyumba zao zimepitiwa na mradi pamoja na kwamba ni nyumba za tope lakini kwa fedha waliyopewa labda mtu anaweza akawa ana eka nne amepata labda shilingi milioni nane na fidia ya mimea labda amepata shilingi milioni nne, shilingi milioni 12 leo huwezi ukajenga nyumba yenye hadhi na ya kisasa, kwa sababu lengo letu ni kwamba wananchi wetu waishi katika maisha bora na nyumba ambazo zina huduma zote za kibinadamu. Kwa hiyo, mimi niombe tu kwamba Serikali iwe makini katika kufidia wananchi wetu lakini pia kuwapatia maeneo mbadala ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusiana na suala zima la first priority kwa wale wakazi ambao wanapitiwa na mradi. Kwa mfano, zimetajwa ajira hapa takribani 10,000 ambazo zitajitokeza katika mradi, lakini kutakuwa na zile ajira ambazo ni permanent takribani 1,000. Sasa hatukuchanganuliwa hapa katika hizi ajira 1,000 labda zitagawanyika vipi ki-percentage, kwamba katika 1,000 asilimia kadhaa itatoka Uganda, asilimia kadhaa itatoka Tanzania. Tuwe makini hapa, tusije tukakuta zile ajira 1,000 zote zinatoka kwa wananchi wa Uganda.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tena viongozi wa ngazi mbalimbali ambao wanapitiwa na maeneo ya mradi kuanzia Waheshimiwa Wabunge, Madiwani, hata Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji wawe wanashirikishwa kwa karibu katika zoezi zima la mradi huu. Kwa sababu lengo ni mradi huu uwe na manufaa kwa Watanzania isije ikawa tena mradi umekwishaanza panaanza manung’uniko ya hapa na pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nashukuru katika Jimbo langu nimeshiriki kwa asilimia kadhaa au kwa asilimia takribani 70 katika haya masuala yote ya mradi, ndiyo maana umeona pia hata Tanga hapakutokea manung’uniko mengi kuhusiana na mradi huu. Kwa hiyo, naishauri Serikali kule ambapo mradi huu utapita wananchi, Viongozi wa Vijiji, Mitaa, Madiwani, Waheshimiwa Wabunge washiriki kikamilifu. Waelewe in and out katika kila kinachoendelea katika mradi huu ili baadaye tusije tukaja tukabeba lawama.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile pia nawakumbusha Waheshimiwa Wabunge, mtakaposhiriki kikamilifu katika mradi huu tukawatetea wananchi wetu itakuja kuwa ni sababu mojawapo ya wewe kurudi tena humu Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana katika Bunge letu hili tukajadili mambo ya nchi yetu na hususani Mpango huu wa Maenedeleo wa 2018/2019. Baada ya hapo vilevile pia bado niendelee kushukuru chama changu kwa nafasi niliyoipata. Lakini mimi nianze kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba Serikali yetu imekuwa na mipango sana. Lakini katika mipango hii mingi imekuwa haina tija, na nianze kwa kutoa mfano, tulikuwa na mpango wa MKUKUTA One, Two and Three lakini mpaka leo hatujui mpango ule umeashilia wapi. Umetajwa hapa asubuhi MKURABITA bado una matatizo, lakini pia palikuwa na Big Result Now hatuelewi imeishia wapi, lakini palikuwa na Kilimo Kwanza, watu wakakopeshwa matreka leo hii taarifa tulizozipata kwenye Kamati yetu imebidi baadhi ya matrekta yakamatwe kwamba watu wameshindwa kulipa.

Lakini pia palikuwa na mpango wa shilingi milioni 50 za vijana kila Wilaya hatujui umeashilia wapi, lakini vilevile palikuwa na mabilioni ya JK nayo haya tukiulizana sijui nani aliyepata. Lakini kama hilo halitoshi bado palikuwa na Mpango wa MMEM wa ujenzi wa shule za msingi na sekondari MMES, lakini bado palikuwa na mpango wa kujenga vituo vya afya kila kijiji nao hatujui umeashia wapi. Sasa napata taabu nkuona hii mipango tunayoipanga yote kwanini haina tija Watanzania wanatuelewa vipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nilikuwa nashauri tu Serikali ni bora iwe na mpango mmoja ambao utakuwa unafuatiliwa na kufanyiwa tathimini kila baada ya mwaka mmoja na nusu kuona kwamba faida iliyopatikana kutokana na mpango huo ni ipi na kama hakuna faida basi mipango tuiache, lakini jambo lingine tumekuwa kukisema kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu na 75% ya Watanzania wanaishi vijijini wamejiajiri wenyewe kupitia kilimo, lakini tujiangalie kama Taifa ni kweli tunathamini kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu? Haiingii akilini kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Tifa letu lakini ni theoretically sio practically. Kwa hiyo, mimi niseme tu lazima kama kweli tumeamua kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa tujue vilevile kwamba kilimo ndio kitakachotoa material ya kwenda katika Tanzania ya viwanda. Sasa kama kilimo chenyewe tumekipuuza leo tunajadili hapa masuala ya mahindi kukosa bei. Wananchi wameweza kufanya kazi kubwa sana bila ya kuwezeshwa na Serikali kwa mfano katika Mkoa ninaotoka mimi hatutumii pembejeo sisi tunalima kutokana na ardhi ambayo ipo na ina rutuba by nature. Lakini leo mahindi yamerundikana hayana bei wananchi wameshindwa kusomesha watoto wao, wananchi wanashindwa kuendeleza nyumba zao za kisasa. Serikali ndio inayozuia mahindi hasiuzwe nje ya nchi, sasa tujitazame tunafanana na nchi za wenzetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahindi yana soko kwamba yanahitajika Southern Sudan, mahindi yanahitajika Kenya, mahindi yanahitajika maeneo ya Ethiopia huko, lakini sisi bado tunazuia mahindi yasiuzwe. Mimi niishauri Serikali tuondoe kikwazo kwa uuzaji wa mahindi, kama Serikali wakala wake wa chakula ameshindwa kununua mahindi haya tuwaache wafanyabiashara wenye uwezo, wanunue mahindi wauze katika nchi za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hilo halitoshi pia vilevile mazao kukosa bei mi naweza nikasema ni Serikali haikutaka kutafuta bei ya soko la mahindi. Kwa hiyo, lazima wananchi waache watafute soko wenyewe, haiingii akilini kwa sababu kwa mfano yupo mfanyabiashara mmoja wa mabasi anaitwa Sumry ameamua kuachana na biashara ya mabasi imeingia kwenye kilimo. Sasa hivi kweli anaweza akaamua kulima mahindi ya kula yeye mwenyewe binafsi, kwa ekari ya zaidi 10,000 au 15,000 alizokuwa nazo! Ni wazi anaamua kuingia kwenye kilimo afanye kilimo cha biashara, amevuna mahindi wanamwambia asiyauze, hapa hukumsaidia bali unamrudisha nyuma katika umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hilo halitoshi, ushauri wangu niseme pamoja na kuwaachia wananchi kutafuta masoko ya mahindi lakini basi tuwawezeshe kama tunaweka vikwazo hivi angalau tuwape mashine za kusaga unga sasa badala ya kupeleka mahindi ghafi, makapi ya mahindi yapaki kuwa vyakula vya mifugo kama ng’ombe wa maziwa lakini wauze unga angalau tumekuwa tumewasidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, laini lingine nije katika suala loa uvuvi bahari kuu. Mimi ninatoka Tanga, Tanga tuna bahari kuanzia Jasini karibu na Kenya mpakani huko mpaka Kipumbwi karibu na Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumejaaliwa bahari kutoka Jasini mpaka Msimbati lakini ukiwatazama wavuvi wa ukanda wa Pwani ni maskini wa kutupwa hohehahe. Badala ya Serikali kuwasaidia imewarundikia kodi lukuki na ushuru mbalimbali, mimi niseme tu wavuvi tuwasaidie kwanza kwa kuwaondolea hizi ushuru na kodi mbalimbali, kwa mfano, mashua moja inachukua wavuvi 25 mpaka 30 lakini wavuvi hawa 30 kila mmoja anatakiwa awe na leseni ya uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini kwenye basi anayekuwa na leseni dereva peke yake turn boy hana leseni wala kondakta hana leseni, kwa nini kwenye vyombo vya uvuvi isiwe mwenye leseni nahodha peke yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tuulizane Waheshimiwa Wabunge katika meli kubwa zinazokukuja kutoka nje kwa mfano ile meli iliyokamata na samaki waliyoitwa samaki wa Magufuli hivi wale watu wa mazingira waliwakamata wakawauliza mpaka mabaharia kwamba walikuwa na leseni ya uvuvi, kwa nini tunawaacha watu wa nje wanufaike tunawakandamiza Watanzania wazalendo wenzetu wadhalilike na waendelee kuwa maskini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naishauri Serikali iondoe...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Kamati kwa taarifa iliyosheheni maelekezo, mapendekezo na ufuatiliaji katika mambo mbalimbali yanayohusu ardhi, maliasili na utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefarijika kuona Kamati imefanya ziara katika maeneo mbalimbali katika tasnia ya ardhi, maliasili na utalii na kujionea physically badala ya kukaa katika kumbi na kujadiliana bila kutembelea maeneo husika na mara nyingine hata Mahakama huhamia eneo la tukio. Ningeshangaa kama Kamati isingetembelea na kujionea hali halisi ya sekta ya ardhi, maliasili na utalii hali iliyopelekea kuishauri vema Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imejaaliwa mapori na mbuga nyingi za wanyama, lakini ni Watanzania wenyewe wanajihusisha na ujangili na uharibifu wa maliasili zetu. Ushauri wangu, ni vema Serikali ikatoa elimu ya ufahamu kwa wananchi. Wananchi wakipata elimu na uelewa kuwa hata nchi zilizoendelea zilikuwa na wanyamapori na maliasili nyingine lakini kutokana na matumizi mabaya (ujangili) leo nchi hizo wananchi wao wanalazimika kuja Afrika na Tanzania kujionea wanyamapori na vivutio vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo natoa wito kwa Serikali kuwapatia elimu ya ufahamu na waelewe pato linalotokana na utalii linachangia pato la Taifa. Mfano, ni vivutio vilivyopo katika Mkoa na Jiji la Tanga kama Hifadhi ya Amani, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Fukwe (Beaches) zilizopo Pangani, Magofu ya Tongoni na Amboni Sulphur pamoja na Amboni Caves. Niungane na mapendekezo ya Kamati lakini nashauri kwamba Amboni Caves iongezewe uwekezaji mkubwa pamoja na kupatiwa umeme na tochi zenye mwanga mkali na barabara pia iboreshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iendeleze mpango wa Kata Mti Panda Mti na iandae utaratibu wa kufanya mashindano ya kupanda miti mijini na vijijini kama inavyofanya nchi ya Malaysia. Nashauri maeneo ya mjini kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini zipatiwe miche ya miti ya matunda ambayo itatoa vivuli, itabadilisha mandhari za miji na itatoa matunda na itatoa kipato kitakachopatikana kutokana na zawadi zitakazotolewa kwa watunzaji wa miti hiyo pia itatoa matunda na wananchi watafaidika na matunda hayo kiafya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi za Taifa kuvamiwa na wafugaji. Ni vema Serikali ikajipanga vizuri katika jambo hili kwani imekuwa ni tatizo la Kitaifa kwani wafugaji nao ni Watanzania wanafuga na wanauza mifugo hiyo ndani na nje ya nchi na kuingizia kodi Serikali. Wafugaji wanatoa kodi na tozo mbalimbali katika minada kwenye Halmashauri zenye wafugaji. Serikali itoe elimu kwa wakulima na wafugaji na kuwapangia maeneo ya kulishia mifugo na maeneo kwa ajili ya kilimo. Pia maeneo yenye Hifadhi na Mapori Tengefu, yawekewe alama maalum na zitambulishwe kwa wananchi wetu (wakulima na wafugaji). Tukumbuke ardhi haikui na watu wanaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi mijini/ vijijini. If you fail to plan, you plan to fail. Katika Halmashauri zetu nchini 98% kuna migogoro ya ardhi, mingine ni kwa wananchi kutokufahamu lakini mingine inasababishwa na wataalam wa ardhi katika Halmashauri kwa interest zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kutoa shinikizo la kila Halmashauri kuwa na ukanda wa EPZ (Exporting Processing Zone), ardhi za wananchi zimetwaliwa na ama kulipwa fidia ndogo ama kucheleweshwa hadi leo fidia zao hawajalipwa. Mfano, ni katika Halmashauri ya Jiji la Tanga kuna Kata za Donge, Mabawa na Tangasisi na Masiwani Shamba, wananchi bado wanasumbuliwa katika fidia zao. Nashauri Serikali iwalipe wananchi fidia zao kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na.5 ya mwaka 1999.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa ujenzi wa uwanja ndege. Katika mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege Tanga kuna mgogoro wa nyumba kuvunjwa. Zipo nyumba 208 zilizofanyiwa evaluation mwaka 2008 hadi leo fidia haijalipwa. Pia zipo nyumba 802, nazo hazijalipwa fidia lakini zinatakiwa zivunjwe. Hivi ni kwa nini katika miradi lazima tuwatie wananchi hasara. Nashauri Serikali iwe na vision na mission na tulipe fidia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia mimi na Watanzania wote afya njema. Na pia nawatakia waislam wa Tanzania na duniani kwa ujumla mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, JWTZ na JKT ni majeshi yetu ya ulinzi wa nchi yetu ya Tanzania na kwa muda mrefu yamekuwa yakifanya kazi katika mazingira magumu katika kutekeleza majukumu yao. Kwa kuwa Tanzania bado ni nchi maskini na bajeti yetu haijitoshelezi na tunategemea sehemu ya bajeti yetu toka kwa nchi wafadhili ambapo fedha haziletwi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi letu pia linatumika vizuri wakati wa majanga mbalimbali kama mafuriko, tetemeko la ardhi, ujenzi wa madaraja na barabara wakati wa athari za mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya ardhi kati ya JWTZ na wananchi; jina la Jeshi letu linajieleza kuwa ni la wananchi wa Tanzania lakini katika siku za karibuni kumekuwa na migogoro ya ardhi kati ya Jeshi na wananchi, na katika kitabu cha hotuba ya Waziri imezungumzia ukurasa wa 29 hadi 30 imeeleza kuwa limedhibiti maeneo ya Jeshi kwa kuboresha mazingira kwa kupanda miti na kusimika nguzo na pia kulipa fidia maeneo ya Ras Mshindo (Lindi) shilingi 3,005,697,801.00 na Kakonko (Kigoma) shilingi 550,000,000.00, napongeza hatua hii. Lakini katika Jiji letu la Tanga upo mgogoro wa Jeshi na wananchi katika Kata za Masiwani Shamba na Tangasisi, naiomba Wizara imalize mgogoro huu kwa kulipa fidia wananchi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ardhi Na. 4 (1999) inasema; “whether you have title deed or not so long you have been there for long time, customary law recognizes you as the owner of the land.” Naomba kupitia sheria hii na Wizara wawalipe wananchi fidia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikiano na majeshi mengine duniani; napongeza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Jeshi letu na majeshi mengine katika nchi za Bara la Afrika, Ulaya, Marekani na Jumuiya za Kimataifa kama NATO na United Nations. Vyema tukatoa kila aina ya ushirikiano katika mafunzo na mazoezi mbalimbali kwani Jeshi letu pia huvuna uzoefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafao kwa wanajeshi wastaafu; kumekuwa na tabia wanajeshi wetu wanapostaafu au wanapopandishwa vyeo kucheleweshewa malipo yao ya kustaafu na malipo ya kupandishwa vyeo. Naiomba Serikali ihakikishe wanajeshi wanalipwa stahiki zao kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora; katika Jeshi linazungumzwa suala la utawala bora lakini mara kadhaa Jeshi linahusishwa na mambo ya kisiasa kwa kuegemea upande wa Chama Tawala (CCM). Nashauri Jeshi letu lisijihusishe na masuala ya kisiasa kabisa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ikisemwa mara nyingi kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu na 75% ya ajira inapatikana katika kilimo na 100% ya chakula Tanzania inatokana na kilimo lakini Serikali bado haijawekeza katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa 80% ya wakulima wetu wanatumia jembe la mkono ambapo mazao yanayopatikana ni machache ukilinganisha na wakulima wanaotumia zana bora na za kisasa katika nchi za wenzetu. Hivyo inahitajika Serikali yetu iwekeze katika kilimo kwa kuwapatia wakulima zana bora za kisasa na pembejeo na kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Serikali ianzishe utaratibu wa kuwalipa fidia wakulima pale inapotokea majanga kama ukame, wadudu/wanyama waharibifu, mafuriko au mvua zinazoangamiza mimea mfano mvua za mawe na bei inaposhuka. Kwa kufanya hivi itawasaidia wakulima kupunguza hasara wanayopata kutokana na majanga haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Serikali iweke matawi ya benki katika kila wilaya ambazo zinajishughulisha na kilimo. Kwa mfano, katika Jiji la Tanga ziwekwe benki katika maeneo yenye wakulima na wafugaji kama Kata za Tongoni, Kirare, Mzizima, Mabokweni, Chongoleani na Kiomoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, kilimo cha umwagiliaji. Katika miradi ya kilimo cha umwagiliaji (irrigation schemes) imekuwa ikifanya kazi pale inaposimamiwa na wafadhili lakini wafadhili wakiondoka tu, miradi hii yote inakufa au kuwa na hali mbaya. Serikali iangalie kwa umakini miradi hii kwa kuitengea fedha za kutosha ili hata pale wanapoondoka wafadhili, miradi hii iendelee kuwa na tija na faida kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, maji ni uhai na ni nyenzo muhimu katika shughuli za maendeleo kama kilimo, lakini hata mashine nazo zinahitaji maji. Miradi ya maji vijiji 10 kila Halmashauri inakwenda kwa kusuasua, fedha za miradi zinacheleweshwa sana na ni kidogo. Wito wangu ni kama ifuatavyo:-

(i) Serikali ipeleke fedha kwa wakati;

(ii) Katika miradi ya maji ipite/itumie Mamlaka za Maji zilizopo kwa kuwa wanaweka mitambo ya maji kwa uzoefu waliokuwa nao na wanategemea mtandao wa maji kama chanzo chao cha mapato kila mwezi kwa kupitia bili za kila mwezi; na

(iii) Serikali ianzishe miradi ya visima virefu na vifupi katika maeneo yenye ukosefu wa maji hususani katika vijiji ambavyo havikubahatika kupitiwa na miradi ya maji vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, uvuvi ni sekta ambayo imeajiri Watanzania wengi katika maeneo/mikoa yenye maziwa na bahari. Tanzania ina ukanda mrefu wa bahari kilometa 1,425 kutoka Jasini, Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga. Wavuvi hawaelimishwi juu ya uvuvi bora na wa kisasa bali mara kwa mara wavuvi wanasulubiwa kwa kisingizio cha uvuvi haramu, wananyang’anywa mashua na majahazi, nyavu na vifaa vingine vya uvuvi na vinatangaziwa kuharibiwa/kuangamizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa kama nyavu vinatengenezwa katika viwanda vya hapa nchini na pia vinaingizwa kupitia mipaka na bandari zetu na Serikali inakusanya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta hii nashauri mambo yafuatayo:-

(i) Serikali itoe elimu kwa wavuvi juu ya nyavu zinazofaa na ipige marufuku nyavu zisizohitajika kuingizwa nchini;
(ii) Serikali isiangamize/kukamata wavuvi na mali zao na kufanya replacement ya vifaa haramu dhidi ya vifaa halali ili tusijenge uadui kati ya wavuvi dhidi ya Askari wa JWTZ na Coastal Zone;

(iii) Serikali ianzishe vipindi vya redio na televisheni kutoa elimu ya uvuvi na mazingira; na

(iv) Serikali ianzishe Benki ya Wavuvi kama ilivyo Benki za Wakulima.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuweza kuchangia. Pia, nachukua fursa hii kuwatakia Waislam wote Tanzania na duniani kote mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Madini Tanzania, madini ni sekta muhimu katika uchumi wa nchi yetu Tanzania na inachangia katika Pato la Taifa kwa kiasi kikubwa hususan tangu imeingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano. Cha kushangaza katika bajeti ya mwaka jana taarifa zinasema fedha ya miradi ya maendeleo iliyopokelewa na Wizara ni chini ya asilimia moja. Hili ni jambo la aibu kwa kuwa sekta hii inaingiza fedha nyingine katika Hazina ya Serikali. Sasa ikiwa Wizara imeomba Sh.19,620,964,000.00 badala yake, hadi Februari, 2019 Wizara ilipatiwa 100,000,000 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha ni jinsi gani Serikali yetu haijawa tayari kuendeleza Sekta ya Madini ukilinganisha na nchi za Botswana, Malawi, South Africa, Rwanda na Burundi ambao tumewazidi kwa rasilimali ya madini tuliyonayo Tanzania. Miongoni mwa nchi nilizozitaja zina aina chache mno ama aina moja tu ya madini. Tanzania tunayo aina mbalimbali zikiwemo, almasi, dhahabu, tanzanite, ruby radolite, alexanderlite, blue sapphire, pink sapphire, red sapphire, white sapphire, red gainet, green tomoline, green gainet, rose acquamarine, chuma (iron) shaba, uranium. Aina hizi za madini ni ushahidi tosha kuwa Tanzania yetu ina utajiri wa kutosha na mkubwa katika Sekta ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, Serikali ihakikishe Sekta ya Madini inaboreshwa kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo na fedha za matumizi ya kawaida angalau kwa asilimia 80 badala ya kupeleka asilimia 0.5, tuoneshe seriousness katika madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wachimbaji wadogo, ni ukweli usiofichika kuwa wachimbaji wadogo ndio chanzo/waanzilishi wa machimbo ya madini ya aina zote hapa Tanzania na maeneo mengine katika nchi mbalimbali. Nchini kwetu Tanzania wachimbaji wadogo wakishagundua madini, Serikali inawaita wavamizi na wanapelekewa Jeshi la Polisi (FFU) na kupigiwa, kunyanyaswa na kubambikiwa kesi za uvamizi au uhujumu uchumi, mahali pengine wachimbaji wanapigwa risasi na kufa ama kujeruhiwa. Mfano, ni maeneo ya Kalalani, Korogwe, Tanga; Dalini, Korogwe, Tanga; Ngombeni, Korogwe, Tanga; Mwakijembe, Mkinga; Kigwase, Mkinga na Uimba River Mkinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya Serikali kuwaita wachimbaji wadogo, wavamizi, wangepatiwa elimu ya kutosha mitaji ya mitambo ya kuchimbia kama diggers na excavators, pamoja na kuwawezesha kupata mikopo ya masharti nafuu kutoka katika taasisi zetu za fedha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Naomba pia nami nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa maisha ya binadamu. Pia sichelewi kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jiji la Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kuipongeza Serikali kwa kuweza kupokea bilioni moja na milioni mia nne kama mpango wa Serikali wa kuboresha vituo vya afya kwa ajili ya mama na mtoto. Labda katika hilo niseme tu kwamba nimepokea milioni mia tano kwa Kituo cha Afya cha Makorora, milioni mia tano kwa Kituo cha Afya cha Mikanjuni, lakini pia milioni mia nne kwa Kituo cha Afya cha Ngamiani, kwa hilo nashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizi naomba Waziri wa Afya anisikilize kwa makini. Tanga ni Manispaa ya kwanza Tanzania tangu mwaka 1951, lakini mpaka leo miaka 57 baada ya Uhuru hatuna hospitali ya wilaya. Halmashauri tumejitahidi kidogo tukaweza kujenga jengo la administration block katika Kata ya Masiwani Shamba, kata mpya ili tuweze angalau kujikongoja tuweze kupata hospitali ya wilaya, lakini bado haijatosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya halmashauri mwaka huu tumetenga takribani shilingi za kitanzania milioni mia tatu. Kwa hiyo namuomba Waziri wa Afya atutafutie angalau bilioni mbili, tukichanganya na milioni mia tatu hizi angalau tunaweza tukapata jengo la OPD ili wananchi wetu waweze kupata huduma za hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, kuna upungufu mkubwa katika Jiji letu la Tanga katika sekta ya afya. Kuna upungufu wa watumishi, nikiwa na maana ya Wauguzi na Madaktari Bingwa. Kwa hiyo, Waziri napo kama wanavyosema wataalam the good charity beginning at home. Sasa naomba atupe upendeleo maalum ahakikishe katika hospitali yetu ya wilaya hiyo ambayo tunakusudia kuijenga tujiandae na Madaktari Bingwa na Wauguzi wa kutosha lakini hili la upungufu wa watumishi limepelekea sasa siku za weekend vituo vingi vya afya na zahanati kufungwa saa nane na nusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo nafikiri Wabunge wenzangu mtakuwa ni mashahidi; huu ni utaratibu ambao upo nchi nzima. Sasa inasababisha wananchi wetu kupata shida. Wananchi wanahoji sisi Watanzania tuna mkataba na Mungu? Kwamba kuumwa mwisho saa nane na nusu? Kama hatuna mkataba huo basi vituo vyetu vya afya na zahanati vifanye kazi masaa 24 ili wananchi wetu waweze kupata huduma bora na huduma ambazo zimekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kuizungumzia Hospitali yetu ya Rufaa ya Bombo. Bombo ni hospitali kongwe nchini Tanzania ambayo ilijengwa na wakoloni na ilikuwa hospitali iliyokamilika idara zote katika wodi na vifaa tiba; vile vile hata katika miundombinu ya lifti. Huu ni takribani mwaka wa nne Bombo hatuna lifti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri, najua nilifika kwake nikamweleza kwamba kuna utafiti mdogo nilioufanya katika kampuni ya lifti inayoitwa OTC ya Ufaransa wameeleza kwamba ili tupate lifti mpya za kisasa wanahitaji Euro 126,000 ambazo ni takribani shilingi za kitanzania milioni mia nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua, kama Serikali itaamua kwa dhati tutaweza kuzipata milioni mia nne kama tulivyoweza kupata fedha za kununulia ndege na mambo mengine. Kwa hiyo, naomba kupitia Bunge hili Mheshimiwa Ummy hata kwa kutafuta wafadhili tuwe tayari kushirikiana lakini tuipate lifti ya Bombo, Tanga. Wananchi wanapata shida, wagonjwa wanaangushwa; mtu anatoka operation amebebwa na baunsa. Kuna utaratibu pale, kuna mabaunsa wako special, mtu akitoka operation kupandishwa ghorofani huko lazima abebwe na mabaunsa familia ilipe. Sasa hii ni aibu kwa nchi yenye rasilimali kama Tanzania kukosa lifti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia, Tanga pia kuna ukosefu wa vitu kama CT Scan. Hospitali ya Rufaa ya Bombo haina vifaa hivyo; lakini kuna taarifa kwamba Watanzania wenzetu wenye asili ya kiasia, Mabohora wametoa mashine ya MRI kama sikosei na CT-Scan, lakini Serikali imeshindwa kujenga jengo la kufitisha mitambo hii. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri na Serikali, tusingoje mpaka wale Mabohora Watanzania wenye asili ya Kiasia wakaamua vinginevyo, mashine ile ikapelekwa mji mwingine. Tunaomba mashine ile Serikali iweze kujenga jengo pale ili tuweze kupata faida ya kutumia mashine ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kusema pia, nchi za wenzetu kama Kenya wameondoa ushuru katika mashine kama hizo za MRI, CT Scan, Ultra Sound na nyinginezo, hali inayopelekea hiyo huduma gharama yake kuwa ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitoa mfano mwaka jana na leo nautoa tena. Yupo mtu mmoja wa Tanga alikuwa na mke wake mgonjwa, alimpeleka Dar es Salaam kupata vipimo hivyo na aliambiwa ni laki nane. Jamaa yake wa Kenya alimwita, na alipofika Mombasa ikawa gharama ni sh 12,000 za Kenya, sawasawa na Sh.60,000/= za kitanzania. Kwa hiyo Serikali iondoe kodi katika vifaa tiba hivi kama MRI, CT Scan na nyinginezo ili gharama za matibabu ziwe nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi Madaktari Bingwa wa mifupa na vichwa kwa Tanga bado tuna tatizo kubwa. Kama tunavyojua kwamba watumiaji wa boda boda na vyombo vya usafiri wa miguu miwili ni wengi na kwa hiyo ajali ni nyingi. Anapoumia mtu lazima akimbizwe MOI Dar es Salaam au apelekwe KCMC Moshi na kwa sababu hiyo gharama zinakuwa kubwa. Hata hivyo, kama Serikali kupitia Wizara ya Afya itatuletea Madaktari Bingwa wa mifupa na vichwa pamoja na magonjwa ya akinamama tutaweza kuhudumia watu wetu pale Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu taulo za akinamama. Nilizungumza juzi kwamba juzi Rais Uhuru Kenyata alisaini sheria kwamba Serikali ya Kenya itawapatia bure taulo za kike wanafunzi wote wa Kenya. Sasa nikitazama Kenya hawana rasilimali nyingi kama Tanzania, wao waweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini? Kama tumeweza kununua Bombadier tunawezaje kushindwa kugawa taulo za kike kwa wanafunzi wetu nchini Tanzania? Mheshimiwa Waziri naomba hili ulifanyie kazi, ikibidi na sisi Tanzania isainiwe sheria kwamba wanafunzi wote wa kike wapewe taulo za kike free, no charge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni wenzetu hawa wa Tanzania ambao wana upungufu wa akili au vichaa. Hawa nao katika maendeleo ya jamii ni jamii ya Watanzania, wao wananufaika vipi na pato la Taifa? Nashauri Serikali itenge fedha na kuipeleka katika kila halmashauri ili wenzetu hawa ambao wana upungufu wa akili waweze kusaidiwa. Leo mtu mzima mwenye upungufu wa akili anatembea uchi wa nyama bus stand, sokoni na watu hawajali, huu ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nashukuru kwa Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema katika kuchangia bajeti ya Wizara hii ambayo ni muhimu katika maendeleo ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, niseme tu kwamba kwa ufahamu wangu, Bunge siyo rubber stamp, ni kwamba kinacholetwa hapa kinatakiwa kijadiliwe halafu tukubaliane kwa pamoja. Kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali. Sasa siyo lazima kila kinacholetwa hapa tuunge mkono hoja tu, hapana. Wakati mwingine kama kuna marekebisho, lazima yafanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, niseme tu, jana kuna mchangiaji mmoja hapa alitoa taarifa kidogo ambayo nami naungana naye. Kama sikosei alikuwa ni Mheshimiwa Silinde. Alizungumza akasema kwamba kuna barabara hewa ambazo zimetumia shilingi bilioni 252, lakini barabara hizi hazijulikani zimejengwa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, tupate maelezo ya shilingi bilioni 252 barabara zake zimejengwa wapi? Kama hilo halitoshi, nami ni Mjumbe pia wa PAC, tutakuja kuangalia huko katika vitabu tuone hiyo value for money.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine imezungumzwa pia kwamba tunaboresha Shirika la Ndege, lakini ili lifanye kazi vizuri, lazima liwe na routes, lisafiri sehemu mbalimbali, ndani na nje ya nchi. Sasa hapa naiomba Serikali kwamba pamoja na kwamba tunanunua ndege, lakini tujitayarishe katika kushindana na mashirika mengine makubwa ya ndege ili ndege hizi zisije zikaitia hasara Serikali kwa sababu Watanzania wana matatizo mengi sana, lakini hatukuyaangalia hayo, tumeona kwanza tuanze na ndege. Hilo pia bado taarifa ya CAG haipo na hii taarifa ya Shirika la ATCL hailetwi Bungeni kujadiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nianze kuchangia mchango wangu. Nataka kuizungumzia kwanza barabara ya Pangani. Kwa maoni yangu ni kama barabara ya Pangani ni mfupa uliomshinda fisi. Kwa nini nasema hivyo? Hii barabara imepita Marais wanne. Ameanza Mwalimu Nyerere akaweka ahadi; akaja Mheshimiwa Rais Mwinyi, akaweka ahadi, akaja Mheshimiwa Mkapa akaweka ahadi, amekuja Mheshimiwa Kikwete naye ameweka ahadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbarawa namheshimu sana pamoja na wasaidizi wake, lakini mwaka 2017 walituambia kwenye bajeti kwamba wametenga shilingi bilioni nne kwa ajili ya upembuzi yakinifu (feasibility study) na mambo mengine. Asubuhi pia nilimpelekea ki-memo kutaka kujua ufafanuzi, hii inayozungumziwa katika ukurasa 271 ndiyo hiyo barabara ya Pangani? Naona ile pesa imepungua! Sasa kila siku gharama za ujenzi zinakwenda mbele lakini bajeti ya barabara ya Pangani inapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja anijuze na anishibishe ili nitakaporudi Tanga niwaambie watu wa Tanga kwamba safari hii barabara ya Pangani itajengwa au haijengwi? Kwa sababu tumechoka na ahadi zisizotekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amekuja Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, hata alipokuja kufanya ziara Tanga ya kuweka jiwe la msingi la bomba la mafuta nilimgusia suala hili na akaahidi kama ataijenga, lakini kwenye bajeti siioni. Sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aniambie hii barabara itajengwa au haitajengwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namkumbusha kwamba barabara hii ina Wabunge wanne au watano; imeanza Tanga Mjini, inapita sehemu ya Kigombe ambayo ni Muheza kwa Mheshimiwa Adadi Rajabu, inaingia Pangani kwa Mheshimiwa Juma Aweso, lakini inaingia vilevile Chalinze kwa Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete. Kwa hiyo, Wabunge watano wote tumekuwa tukiizungumzia hii barabara, lakini inaonekana kama tunatwanga maji ndani ya kinu. Sasa tunataka kujua, hii barabara itajengwa au haijengwi? Kama haijengwi pia utupe jibu, kwa sababu tumechoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara ina historia ndefu. Nafikiri wakati wa miaka ya nyuma, wakati wa enzi za kupigania uhuru, wapo wapigania uhuru ambao waliitumia njia hii, lakini mpaka leo barabara nyingine za karibuni hapa zimejengwa. Hakuna barabara iliyokuwa ndefu kama kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza, imejengwa. Sasa inakuwaje kipande kidogo hiki cha Tanga – Pangani - Bagamoyo mpaka Dar es Salaam kishindwe kujengwa? Marais wanne wote wametoa ahadi mpaka leo barabara hii haijengwi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja anieleze hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme, kama hakuna fedha, tuitafute ilipo ile 1.5 trillion ili tuiingize katika barabara ya Pangani tuweze kujenga barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niizungumzie Bandari ya Tanga. Bandari ya Tanga ni bandari kongwe, ndiyo bandari ya kwanza kujengwa katika Afrika Mashariki na Kati, lakini bandari hii inapuuzwa. Tarehe 28 mwezi wa Pili nilialikwa katika Kikao cha Bodi ya Bandari wakawepo wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga na mikoa ya jirani pamoja na uongozi wa bandari, lakini ukisikiliza wafanyabiashara wanalalamika, viongozi wa bandari wanalalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari ile haina vifaa vya kisasa vya kushusha na kupakia mizigo. Kwa mfano, crane ya kubeba forty feet container haifanyi kazi, ni mbovu. Hata wakiomba fedha kwa ajili ya ukarabati pia haufanyiki. Sasa itakuwaje tuwe na bandari lakini haina vifaa vya kushushia mizigo, wakati tunaagiza mizigo kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo pia nitataka nijibiwe, linawezekana au haliwezekani? Ikibidi basi itafutwe fedha au Bandari ya Tanga nayo iingizwe katika bandari ambazo zinapelekewa vifaa vya kisasa na vya kutosheleza kupakia na kupakua mizigo. Kwa sababu Bandari ya Tanga inasemwa, inafanya kazi kwa hasara. Haifanyi kazi kwa hasara, haina vifaa. Hata muwe wengi vipi, hamwezi kubeba kontena la forty feet kwa mikono. Kwa nini bandari isifanye kazi kwa hasara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini huu ni mpango wa kuiua makusudi Bandari ya Tanga kwa sababu haiingii akilini kwamba leo bidhaa zetu zote tuziingize katika Bandari ya Dar es Salaam hali ya kuwa Bandari ya Dar es Salaam yenyewe imefanyiwa ziara za kushtukiza. Mheshimiwa Waziri mwenyewe amefanya, Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya na Mheshimiwa Rais amefanya, lakini pana matatizo hayamaliziki. Kwa nini hawabadilishi bandari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie, hata alipokuja Mheshimiwa Rais Tanga katika bomba la mafuta nilipata nafasi ya kuzungumza nikasema lazima tufanye categories za mizigo. Haiingii akilini, Bandari ya Mtwara imelala, Bandari ya Tanga imelala, ifanye kazi Bandari ya Dar es Salaam peke yake. Nikaishauri Serikali kwamba baadhi ya mizigo iwe inateremka katika kila bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mikoa ya Ruvuma, Mtwara kwenyewe, Katavi, Rukwa na Sumbawanga huko pamoja na nchi za Zambia na Malawi mizigo yao ingeshuka Bandari ya Mtwara kwa sababu pana Mtwara Corridor. Bandari ya Tanga ishughulikie mizigo ya Tanga yenyewe, Moshi, Arusha, Manyara, Simanjiro na Musoma pamoja na nchi za Uganda labda na Rwanda mizigo yake ingekuwa rahisi kwa gharama kuishushia Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali mnayoisema sikivu, sijui usikivu huo uko wapi? Kwa sababu tunakubali sasa bandari moja ya Mombasa mapato yake kwa mwaka inazishinda bandari nne za Tanzania. Bandari ya Zanzibar, Dar es Salaam, Mtwara na Tanga, mapato yake ukiyajumuisha vyote kwa pamoja hayafikii Bandari ya Mombasa. Kwa nini? Wenzetu wameamua kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalozungumzia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuweza kuchangia Wizara hii muhimu katika nyanja mbalimbali za maendeleo, hususan katika uchumi, mawasiliano na usafiri wa anga, baharini, reli na barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Pangani ni kongwe na ya kimkakati (East Africa and Southern Roads Projects). Barabara hii kama itajengwa kwa kiwango cha lami itainua hali ya uchumi wa Mikoa na Majimbo ya Tanga, Muheza, Pangani, Bagamoyo na maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, mwaka jana barabara hii ilitengewa shilingi bilioni nne, naomba ziongezwe na barabara tuambiwe itaanza kujengwa lini? Barabara hii ni ya kihistoria na tayari ilishaahidiwa na Marais wanne waliopita akianzia Mheshimiwa Mwalimu Nyerere, Mheshimiwa Ally H. Mwinyi,
Mheshimiwa Benjamin Mkapa na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege wa Tanga ni wa kizamani lakini tangu umeachiliwa na wakoloni haujafanyiwa ukarabati mkubwa wa maana. Nimezungumza katika bajeti mwaka 2016/2017, 2017/2018 na leo hii 2018/2019 nimeona shilingi bilioni 7.6; naomba fedha hizi zifanye kazi ya kubadili sura na hali ya uwanja, pia nataka nijue fedha hizi ni pamoja na fidia ya nyumba tatu zilizofanyiwa tathmini (evaluation) 2008 na nyumba 802 ambazo nazo zinatakiwa kubomolewa, zote hizi naomba wamiliki wake wafidiwe kuepuka mgogoro unaoweza kusababisha kesi mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali kufuatia miradi mikubwa ya bomba la mafuta toka Hoima - Uganda hadi Chongoleani - Tanga viwanda vya saruji vipya vya Kilimanjaro na Sinoma China chenye thamani ya shilingi trilioni saba. Naomba Tanga tujengewe uwanja wa ndege wa kisasa wa Kimataifa. Naomba pia huduma za bombadier kupitia ATCL zifike Tanga kwa kuwa Tanga kuna shughuli nyingi za kiuchumi, ukiwemo utalii, viwanda, uvuvi na bandari.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia mipaka ya uwanja wa ndege wa Tanga iwekwe wazi na Waziri utaje vipimo vyake kwa kuwa kuna mgogoro ambao unasumbua wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirikia la Ndege ATCL pamoja na ununuzi wa ndege sita, lakini naiomba Serikali inunue ndege tano na fedha za ndege mbili zinunue ambulance, helicopter mbili ambazo zitasaidia kuokoa maisha ya wananchi wetu pindi zinapotokea ajali barabarani au katika vyombo vya usafiri. Ndege hizi zipatiwe routes za nje na ndani ili shirika lijiendeshe kwa faida na lisijiendeshe kwa hasara kama ilivyokuwa Air Tanzania. Shirika letu la ndege liajiri wataalamu na watumishi wenye weledi na ubunifu ili kuweza kufanya competition na mashirika mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya standard gauge katika bajeti ya mwaka 2017/2018 nililieleza Bunge na Serikali kuwa reli ya Tanganyika ilianza kujengwa mnamo mwaka 1905 ikianzia bandari ya Tanga hadi Kilimanjaro, Kigoma na hatimaye kufika Mwanza. Baada ya kuja standard gauge Tanga imeachwa, nashauri kama wasemavyo wanafalsafa kuwa mwiba unapoingilia hutokea hapo hapo, hivyo naomba standard gauge ifike Tanga ili uchumi wa Tanga nao uweze kukua kwa kasi kwani uchumi wa Tanga unategemea reli, barabara, bahari na anga.

Mheshimiwa Naibu Spika, bandari ya Tanga ni miongoni mwa bandari kubwa nne za Tanzania (Dar es Salaam, Tanga, Zanzibar na Mtwara) na kihistoria bandari ya Tanga ndiyo ya kwanza katika East Africa. Katika enzi za sayansi na teknolojia, bandari ni lango kuu la biashara, lakini bandari zetu zilizoko katika Bahari ya Hindi hazitumiki vizuri, ukilinganisha na bandari moja ya Mombasa nchini Kenya. Serikali yetu imeelekeza shughuli nyingi katika bandari ya Dar es Salaam na zingine za Tanga na Mtwara hazitumiki vizuri na kusababisha kujiendesha kihasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto katika bandari ya Tanga tarehe 28 Februari, 2018 nilialikwa katika kikao cha Bodi ya Bandari na wadau wa bandari, wafanyabiashara, wajasiriamali na kadhalika. Katika kikao hiki zilizungumziwa changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa zana mkononi, hakuna cranes za kubeba kontena za 40 fts, magari ya kutosha, urasimu ni mkubwa, pamoja na udokozi katika bidhaa zinazoingizwa toka nje, kina cha bandari ni kifupi, meli haziwezi kukaa longside na kusababisha gharama kubwa katika ushushaji mizigo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali bandari ya Tanga ipatiwe vifaa vya kisasa kama cranes, matishari, malori, fire department, waletwe watumishi wenye kujituma kuondoa urasimu, wazalendo/weledi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali ianzishe categories za mizigo ambapo kila bandari ingepangiwa utaratibu wa kupokea na kusafirisha mizigo kama ifuatavyo; Bandari ya Tanga ingepokea ama kusafirisha mizigo ya Arusha, Kilimanjaro, Simanjiro, Manyara, Musoma, Bukoba, nchi za nje, Uganda, Rwanda, Burundi na Congo DRC. Bandari ya Mtwara ingepokea ama kusafirisha mizigo ya Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Katavi, Rukwa, Sumbawanga, Kigoma na Tabora, nchi za nje mizigo ya Malawi, Zambia, Zimbabwe na Mozambique na Bandari ya Dar es Salaam ingepokea ama kusafirisha mizigo ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora na Mwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nchi za nje mamlaka ikiona ipo haja baadhi mizigo ya baadhi ya nchi zipitie Dar es Salaam lengo kuu liwe bandari zote zifanye kazi kwa kiwango kinachofanana na faida.

Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu ni kuwa together we build our nation.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi nishukuru kwa kunipatia nafasi hii.

Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuweza kukutana na kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Lakini mara zote nimekuwa nikisema katika michango yangu kwamba Watanzania sijui tumekumbwa na balaa gani. Kwa sababu hapa viwanda vinazungumzwa kinadharia ziadi, lakini ukienda katika uhalisia mimi nasema hakuna kitu kwa sababu gani? Viwanda vilikuwepo, tulikuwa na viwanda vingi tu kwa mfano katika Jiji letu la Tanga tulikuwa na Kiwanda cha Mbolea, tulikuwa na Kiwanda cha Chuma (Steel Rolling Mills), tulikuwa na Gapex, tulikuwa na Kiwanda cha Sabuni (foma), tulikuwa na Amboni plastic, tulikuwa na CIC, tulikuwa na Kiwanda cha Mafuta ya Nazi (Nicoline), tulikuwa na Viwanda vya Sabuni Gardenia pamoja na railways. Tujiulize vitu vyote hivi viko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nimuweke sawa mchangia aliyechangia Mheshimiwa Devotha Minja katika historia ya Tanzania Tanga ndio ulikuwa mji wa pili kwa shughuli za kimaendeleo kwa sababu ulikuwa ni mji wa viwanda na uliweza kukusanya makabila yote Tanzania mpaka tukaweza kuingiza majirani zetu kama watu kutoka Malawi, kutoka Rwanda na Burundi, Uganda na Kenya wamekuja kufanya kazi Tanga lakini viwanda vyote vile vimekufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo kubwa ambalo naliona kwanza hatuna umeme wa uhakika, lakini pia umeme ni ghali kuliko dunia nzima na hayo si maneno yangu nafirikiri katika siku za karibuni Mheshimiwa Rais pia aliwahi kuzungumza kwamba Tanzania gharama za umeme ni kubwa ndio maana wazalishaji au wenye viwanda wanashindwa kuja. Hata hivyo hata kama una fedha unataka kuweka kiwanda umeme unakatika mara kwa mara utaajiri watu wakae-shift masaa manane mazima, masaa manne umeme hakuna, hilo haliwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nasema kwanza tupate umeme wa uhakika, lakini pili tupunguze utitiri wa kodi. Tanzania kodi zetu sio rafiki wa wafanyabiashara na wazalishaji na wenye viwanda. Kwa hiyo, lazima Serikali hapo ijitathimini na ijilinganishe na nchi majirani zetu. Kwa nini wawekezaji wengi wanakwenda Kenya, wanakwenda Rwanda, wanakwenda Msumbiji sasa hivi wanakwenda Uganda. Kwetu kuna matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda lingine ninaloweza kulizungumzia sisi ni wakulima wakubwa wa pamba, lakini tujiulize kwa nini Tanzania hadi leo tunaongoza kwa kuvaa mitumba, tena bahati mbaya zaidi hata leo kulikuwa na mjadala katika redio ya Clouds, kwamba kwanini Watanzania mpaka nguo za ndani, chupi, sidiria, soksi, gloves pia tunaingiza za mitumba wakati baada ya Sudan katika Afrika tunaoongoza kwa uzalishaji wa pamba ni sisi. Sasa lazima Serikali ijiangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwijage, usivitaje tu viwanda kinadharia, leo hata vijiti vya kuchokolea meno hizi toothpicks pia zinatoka China, handkerchief made in China sijui mijiti ya kuchomea mishikika pia made in China miaka 57 baada ya uhuru. Sasa tunaposema Tanzania ya viwanda tusizungumze kinadharia na tusizungumze kimisamiati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama Singapore, Malaysia, Vietnam hata China katika miaka ya 1970 huko tulikuwa angalau tunalingana lingana nazo. Kwa nini sasa hivi wenzetu wametuacha kiasi hiki? Kwa sababu hatuko serious, sisi katika kila jambo tunaingiza siasa na hapa ndiyo tunapoharibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kama tunataka viwanda kweli tumejaza magofu ya viwanda wengine wanafugia mbuzi, wengine wamegeuza ma- godown, kuna viwanda vimebinafsishwa kwa watu binafsi, tujiulize hawa tuliobinafsishia viwanda hivi wanafanya shughuli gani sasa hivi? Wameweka yamekuwa ni ma- godown wengine wanafungua mashine zilizokuwa ni vyuma vya pua wanakwenda kuzalisha vyuma vipya au wanatengeneza scraper. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali iko wapi? Na pia tujiulize hivi viwanda baada ya kubinafsishwa hizi fedha zilizopatikana zimefanya shughuli gani? Nashauri ni vyema viwanda vile ambavyo vimekufa vikafungwa mitambo mipya ya kisasa tukapata umeme wa uhakika ili viwanda vyetu viweze kufanya kazi. Lakini pia tunapotamka viwanda tusifikirie kwamba itakayojenga hivyo viwanda ni Serikali maana yake hapa tunalolichukulia ni suala la viwanda kama vile Serikali ndiyo inayojenga viwanda. Tuweke mazingira mazuri ya kodi iwe rafiki kwa wawekezaji, lakini tuwe na umeme wa uhakika, na vilevile pia tuwe na attraction kwa hawa wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema hapa Mheshimiwa Kuchauka kuwa leo mtu akitaka leseni au akitaka kibali cha kujenga anasumbuliwa kuna urasimu wa jambo la saa moja Tanzania litachukua siku nne lakini akienda Kenya au Uganda jambo la saa moja ndani ya dakika 20 keshapata kibali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kuweza kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya kilimo Tanzania, leo ni miaka 57 baada ya uhuru bado Tanzania kilimo kimekuwa cha kusuasua na kimejaa siasa na misamiati kibao. Kwa kifupi bado nchi yetu haijawa serious na kilimo kwa kuwa bado wakulima asilimia 70 wanategemea jembe la mkono na asilimia tatu wanatumia wanyama kazi na asilimia tatu ndiyo wanaotumia zana za kisasa za kilimo kama matrekta na mitambo mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo chetu tumekiingiza kwenye siasa na misamiati ya maneno badala ya vitendo. Yapo maneno siasa ni kilimo, kilimo cha bega kwa bega, kilimo cha kufa na kupona, kilimo cha ushirika, kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu, kilimo ni uhai na kilimo kwanza. Je, nchi jirani wanayo hii misamiati katika kilimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kudharauliwa kwa bajeti ya Wizara ya Kilimo, pungufu asilimia 23. Bajeti ya mwaka 2017/2018 ilipelekwa asilimia 18 na bila shaka itapungua hadi asilimia tatu, hii ni hatari, hatujui kipaumbele ni kipi na kipi kisubiri, kuna mambo namna tatu, moja umuhimu haraka sana, mbili muhimu lakini siyo haraka, tatu muhimu kawaida. Bajeti ya Kilimo ni asilimia 0.52 ya Bajeti Kuu, namtaka Waziri atakapokuja katika winding up atueleze vipaumbele katika Wizara yake. Bajeti haitoshi ni bado tunasema kilimo ni uti wa mgongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kizungumkuti cha mawakala, bajeti ya mwaka 2015/2016 ilikuwa shilingi 35 bilioni na deni wanalosema wanadai ni shilingi bilioni 67. Maswali ya kujiuliza Waziri uje na majibu ama shilingi halali yangu kuishika. Kwa nini shilingi bilioni 67 inatoka wapi?, kwa nini vocha zilizidi hata bajeti iliyotengwa ni vocha za thamani gani zilirudi kutoka Mikoa yote? Kwa nini zilitengenezwa vocha nyingi zaidi ya bajeti iliyotengwa, ni fedha shilingi ngapi zilitumika kutengeneza vocha hizo? Baada ya vocha kurudi deni halisi ni shilingi ngapi? Je, Serikali ipo tayari kuwasikiliza mawakala ili watoe hesabu halisi? Hakuna ofisi iliyovunjwa na vocha kuibiwa kwanini kuna tofauti ya deni ya shilingi bilioni 35 na shilingi bilioni 67? Waziri uje na majibu sahihi na uchunguzi ufanywe na Serikali ili kubaini waliohusika na hatua zichukuliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyama vya ushirika ni matatizo kwa wakulima. Zamani miaka ya 1950 – 1960 vyama vya ushirika kama KNCU - Kilimanjaro na KNCU - Kagera, Nyanza na Tanga - TARECU, vyama hivi viliwasaidia wakulima kwa kukata shilingi moja hadi mbili na kisha waliwalipia ada wanafunzi ambao leo ni madaktari, wachumi, maprofesa, engineers, pilots lakini pia bado vyama vya ushirika viliwasaidia wakulima katika kuendeleza kilimo, leo vyama vya ushirika kazi kubwa ni kuwaibia, kuwadhulumu na kuwatapeli wakulima mazao yao na bahati mbaya mnaihusisha Ilani ya CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha mbolea Tanga - Tanzania Fertilizer Company (TFC). Tanga ilikuwa ni mji wa viwanda, miongoni mwao ilikuwa ni Kiwanda cha Mbolea. Kiwanda kilifanyiwa hujuma na kikafa kwa maksudi ili pafanyike biashara ya kuagiza mbolea kama urea, sulphur/DAP bei juu, kisha eti kikajengwa Minjingu lakini vifungashio made in Kenya. Wakati Kiwanda cha Mbolea Tanga kinafanya kazi hakijauliwa kwa makusudi tatizo la mbolea halikuwepo na wala issue ya mbolea ilikuwa haijadiliwi Bungeni kwa ghadhabu na hasira kama ilivyo leo. Tujiulize tatizo nini na liko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kwa jina la Mwenyezi Mungu bila ya kuimarisha na kuboresha kilimo kinachotoa raw materials za viwanda tutabaki na hadithi za paukwa pakawa hapo zamani za kale, bajeti ya kilimo ni asilimia 18 kwa mwaka 2018, nashauri Serikali iongeze bajeti kwa mwaka 2018/2019 angalau ifikie asilimia 35 kwa kuwa kilimo kinaajiri Watanzania asilimia 75 angalau kilimo kitaimarika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wakulima kukosa masoko; Tanga ni wazalishaji wakubwa wa zao la muhogo katika Kata za Kirare, Mzizima, Tongoni, Pongwe na Kiomoni lakini tatizo kubwa ni soko la uhakika kiasi kikubwa cha muhogo hutegemea soko la Tanga Mjini na Dar es Salaam. Masoko hayatoshelezi na kusababisha muhogo kuporomoka bei, zimekuwepo tetesi kuwa Wachina wanahitaji muhogo, Tanzania Chamber of Commerce iko katika mazungumzo ili kujua kwa mwaka China itahitaji tani ngapi kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri, Waziri wa Kilimo wakati wa majibu ni vyema akaeleza ukweli na uthibitisho wa taarifa hii ili kuweza kuwatoa shaka wakulima wa muhogo wa Tanga na Tanzania kwa ujumla. Masoko ya mazao mengi yamekuwa mashakani na mazao hayo ni mbaazi, mtama, miwa, machungwa, mahindi, ufuta na kadhalika. Serikali iwe na mipango ya muda mrefu ya utafutaji wa masoko, Serikali ifuate mfano wa nchi za India, Brazil, Rwanda, Burundi na Uganda kutafuta masoko ya mazao ya wakulima wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo kwa wakulima katika mabenki; mikopo katika mabenki ya nchi yetu ni haki kwa kila Mtanzania atakayekamilisha taratibu zilizopo. Serikali ilianzisha hatimiliki za kimila na moja ya manufaa ya hati hizi ni wakulima kuweza kuzitumia katika mabenki na kuweza kupata mikopo, kitu cha kushangaza wananchi wengi waliotaka kuzitumia hatimiliki za kimila kutaka mikopo katika benki za NMB, NBC na CRDB. Hati hizi hazitambuliki na wakulima wanashindwa kuelewa kati ya mabenki na Serikali nani ni mkweli au nani ni muongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri kwa Serikali, isiwadanganye wakulima inawakatisha tamaa, wakulima wamejitahidi kupata hatimiliki za kimila lakini hazina maana yoyote. Serikali itafute njia mbadala kuwawezesha wakulima wa Tanzania kuweza kupata mikopo katika mabenki yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo cha Mkonge Tanga. Tanga imefahamika na kupata umaarufu katika Afrika Mashariki, Afrika na dunia kutokana na zao la mkonge kuanzia katika miaka 1886, zao hili lililetwa na Wagiriki na Wajerumani, Serikali ya United Kingdom, walikuja kuliboresha na kuliimarisha kwa kuwa walipata kodi kubwa katika mkonge. Mkonge katika Tanzania upo katika Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Lindi. Mkoa wa Tanga pekee ulikuwa na mashamba 72 yaliyoajiri wafanyakazi 40,000 na vibarua 32,000. Serikali baada ya kuimarisha mashamba ya mkonge iliamua kuzibinafsisha Mamlaka ya Mkonge (Tanzania Sisal Authority) na hapo ndipo mkonge ulipoanza kufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati njema sana dunia imeamua kutumia bidhaa za mikonge kwa kuwa mkonge hauchafui mazingira, lakini mkonge katika Tanzania haupo mikononi mwa Serikali, mamlaka na udhibiti ipo kwenye taasisi na watu binafsi ambao hawawezi kuendesha mkonge. Nashauri Serikali iamue kwa makusudi kulifanyia kazi na kulithamini zao la mkonge kama inavyofanya kwa mazao ya korosho na pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hitimisho Maafisa Ugani wasikae ofisini waende mashambani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, nami kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kukutana na tukajadili mambo ya nchi yetu, lakini jambo lingine niwatakie heri ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani Waislam wote Tanzania na duniani kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza kwa kuzungumzia hali ya uvuvi Tanzania katika kitabu cha Wizara ukurasa wa 82 ambapo pana takwimu zimetolewa hapa kwamba Ziwa Victoria kwa mwaka kuna tani 2,143,248; Ziwa Tanganyika tani 295,000; Ziwa Nyasa tani 168,000; Bahari ya Hindi tani 100,000 maji ya Kitaifa ambapo ninavyoamini ni katika ule ukanda unaoanzia Jasini karibu na Kenya mpaka Msimbati ambapo ni kilometa 1,425 na mabwawa madogo madogo yanazalisha tani 30 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, takwimu hizi sikubaliani nazo. Haiwezekani ikawa Ziwa Victoria litoe samaki tani 2,143,000 lakini ukanda wote wa bahari wa maji ya Kitaifa utoe tani 100,000 tu! Naomba Waziri atakapokuja atupe takwimu sahihi au labda niwe nimeelewa vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nizungumzie hali ya uvuvi katika nchi yetu kwa ujumla. Wataalam wanasema if you fail to plan, you plan to fail, hapa ndiyo ninapoona pana tatizo, kwa sababu haiingii akilini kwamba Wizara badala ya kukaa na wavuvi kuwaelimisha elimu ya uvuvi wa kisasa, nyavu zinazotakiwa kisheria, vilevile pia kuwapa elimu ya madhara ya uvuvi haramu sasa kazi yetu imekuwa ni kuanzisha operation. Operation haitengenezi jambo na waswahili wanasema kosa siyo kutenda kosa, kosa ni kurudia kosa.

Mheshimiwa Spika, huko nyuma kulikuwa na Operation Tokomeza, ikaleta balaa kubwa katika nchi yetu. Wafugaji waliuawa, ng’ombe wakapigwa risasi na hali ikawa mbaya katika nchi. Sasa inakuwaje Waziri Mpina sasa naye badala ya kurekebisha makosa anarudia makosa anatuletea operation! Naona hapa haliko sawa sawa.

Mheshimiwa Spika, nimtake atakapokuja, hivi katika fikra zake zote kama Waziri aliyeaminiwa na Rais Magufuli, hana plan ya kufanya ni lazima aendeshe kwa operation. Wavuvi hawataki operation, naamini kwamba wavuvi ni watu ambao ni waelewa, wavuvi wamejaribu kuunda vyama vyao vidogovidogo lakini hata katika kanuni ambazo zinaanzishwa za uvuvi hawashirikishwi.

Mheshimiwa Spika, jana tulikuwa na baadhi ya wavuvi hapa, malalamiko yao ni hayo. Wameandika barua tarehe 25 Julai, 2017 wakaambiwa kwamba wataitwa na Waziri, watakaa naye kikao ili warekebishe mambo, matokeo yake mpaka bajeti inaletwa hapa, Waziri hajawaita. Kama hilo halitoshi, katika hiyo Operation Sangara, kuna kitu ambacho mpaka sasa hivi sielewi. Nilisikia kwenye taarifa ya habari kwamba hata mama lishe wanahusishwa na uvuvi haramu.

Mheshimiwa Spika, mama lishe kazi yake ananunua samaki, amewapikia chakula wavuvi, mama anaambiwa atoe faini shilingi milioni mbili halafu banda lake la mama lishe linachomwa moto. Najiuliza sasa, huyu Waziri Mpina anayefanya ukatili huu ni kweli amezaliwa na mama? Kwa sababu ni lazima akina mama tuwaonee huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kwa taarifa yako akina mama baada ya kukosa ajira, ndiyo wanaolea familia. Sasa leo matokeo yake mama lishe wanachomewa mabanda yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kuwachomea wavuvi nyavu. Kwetu baharini na hata kwenye maziwa, Tanga kuna dagaa wale wadogo wadogo wanaitwa uono, Mwenyezi Mungu ndiyo alivyowaumba hivyo kama hivi binadamu kuna wengine warefu, wengine wanene, wengine wafupi; uono, dagaa wa Mwanza na dagaa wa Kigoma yale ndiyo maumbile yao. Sasa unapomwambia mvuvi avue na nyavu ya nchi nne au nyavu ya nchi mbili atamvuaje dagaa yule? Hebu watutafutie njia mbadala, mnapowakataza Watanzania wasivue, ujue unahatarisha ajira ya zaidi ya asilimia 36 ya Watanzania ambao utawafanya wasiwe na ajira.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mpina atakapokuja hapa ku-wind up atueleze ni nyavu zipi zinazoweza kuvua uono, dagaa wa Mwanza na dagaa wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hilo halitoshi, Operation Jodari. Hii operesheni katika ukanda wetu wa Pwani imekuwa ni balaa, ni tatizo. Wavuvi wanalishwa samaki wabichi, wavuvi wanalishwa pweza wabichi, sijui kama unamjua pweza alivyo akiwa mbichi anavyokuwa. Mtu analazimishwa amle mbichi, hivi Mheshimiwa Waziri kama ni yeye angeweza kula pweza mbichi? Kwa nini tuwafanyiwe wavuvi ukatili kiasi hiki? Kwa sababu uvuvi unaingiza asilimia mbili ya Pato letu la Taifa. Ilikuwa ni kiasi cha kukaa nao na kuwaelimisha ili tupate mapato mazuri kwa Serikali lakini matokeo yake ni kuwapiga, wengine wanapigwa risasi.

Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Tongoni Tanga yupo mvuvi amepigwa risasi kwa sababu eti ni mvuvi haramu! Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje atupe njia mbadala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la leseni, leseni kila baada ya miaka miwili inapandishwa bei, kwa nini chombo kimoja kina wavuvi zaidi ya 25 wote wawe na leseni? Ninavyojua mtumbwi ni sawasawa na basi au gari. Anatakiwa kepteni awe na leseni, wale wengine ni kama Wasaidizi wa kuvuta nyavu za jarife na kutupa mishipi, kwa nini kepteni awe na leseni, wavuvi wawe na leseni, chombo kiwe na leseni, samaki walipishwe ushuru, huu ni uonevu. Tunamtaka Waziri aondoe leseni kwa wavuvi, leseni ibaki kwa kepteni peke yake kama ilivyo leseni kwa dereva wa basi, kondakta hana leseni na tanboy vilevile hana leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali, tuwape elimu wavuvi wawe wavuvi bora na wa kisasa. Amesema msemaji mmoja hapa kama sikosei Mheshimiwa Bashe kwamba katika Katiba ya CCM Ibara ya 7 inazungumzia majukumu ya CCM ni kulinda haki na kuhakikisha kila mtu anapata haki yake kutokana na kazi anayoifanya. Ninawashauri wavuvi mpo hapa, kama mtaona haki yenu hamuipati tishieni kama vile wenzenu wanavyofanya kurudisha kadi za CCM. Sasa hivi operation zitasimamishwa na ninyi mtabaki salama, lakini mkiendelea kuwa kimya, operation zitaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika sekta ya mifugo, Tanzania ni ya pili kwa mifugo katika Bara la Afrika, lakini tujiulize ni wananchi wangapi wanakula nyama? Kama hilo halitoshi kwenye suala la upigaji chapa, tunatumia gharama kubwa lakini ni kuharibu ngozi.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kuendelea na shughuli za Bunge letu. Nawatakia Waislam wote heri ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Spika, operatation tokomeza na wafugaji/wakulima. Kama kuna wakati Serikali ilikosea ilikuwa ni katika kipindi cha operatation tokomeza, kwa kuwa ulifanyika ukatili na unyama wa kutisha kwani wanyama katika hifadhi walikuwa na thamani zaidi ya binadamu na mapori tengefu nayo pia yalikuwa na thamani kuliko mifugo na binadamu katika maeneo yaliyo karibu na mapori hayo. Cha kushangaza, hawa wananchi walikuwa toka enzi za kabla na baada ya ukoloni ndio waliokuwa walinzi na rafiki wa wanyama, kwa mfano, Wamasai, Wahadzabe na Wasandawe.

Mheshimiwa Spika, Serikali badala ya kuwaelimisha ili wajue faida zipatikanazo na utalii, Serikali inawatumia askari wa wanyamapori (game rangers) kuwapiga, kuwatesa na hata kuwaua kwa risasi kwa kisingizio cha uvamizi wa hifadhi na mapori tengefu, lakini pia wawindaji haramu. Hii si sawa na ni kinyume cha haki za binadamu. Ni vyema Serikali ikatoa elimu na kuwashirikisha wananchi wa maeneo yaliyo karibu na hifadhi, mapori tengefu na mbuga zetu ili wajue kwamba mbuga za Serikali ni mali yao na wajulishwe faida zinazopatikana kutokana na utalii.

Mheshimiwa Spika, migogoro ya ardhi katika mbuga/ hifadhi na wakulima; migogoro haitaisha katika mbuga na hifadhi kwa kuwa watu wetu (wakulima na wafugaji) hawapangiwi mipango shirikishi ambayo ingeweza kugawa maeneo machache ya kulisha mifugo na maeneo mengine yabaki kuwa ya hifadhi. Ukipatikana ushirikiano wa pamoja ungeleta mafanikio kwani hifadhi/mbuga na mapori tengefu ni mali ya Watanzania, ni mali yetu. Tabia ya kuwanyang’anya ng’ombe iachwe.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali; watu huongezeka, ardhi haikui; Serikali ijue wazi wananchi wakiamua kugoma watalii wasipite katika miji yao, wakiamua kufanya hujuma dhidi ya utalii, hakutakuwa na utalii. Hivyo ni vyema Serikali ikawapa elimu na ushirikiano na iache kuwafanyia ukatili wakulima na wafugaji ili Wizara hii iendelee kuwa chanzo cha mapato ya Serikali ambayo ni 17.6% Pato la Taifa (GDP) = USD 2.3 billion per year.

Mheshimiwa Spika, unyang’anyi unaofanywa na game rangers katika utalii kwa Watanzania (wakulima/ wafugaji) kuwapiga ng’ombe mnada kisha fedha inayopatikana ni shilingi ngapi, iko wapi na inafanya nini? Je, hii ndiyo Serikali ya wanyonge au ni Serikali ya kuwaonea wanyonge?

Mheshimiwa Spika, wosia wangu kwa Serikali, rasilimali tulizonazo tumezipata kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu, lakini badala ya kuwaneemesha Watanzania imekuwa ni NAKAMA, hivyo Serikali ijitathmini, ishirikishe wananchi zaidi, badala ya wageni.

Mheshimiwa Spika, utalii kimataifa (cultural tourism) (Sukuma, Makonde, Ngoni, Bondei, Digo). Zipo kabila katika nchi yetu, ni utalii kwa kutumia mavazi yao (Wamasai), ngoma mbalimbali, taarab (Zanzibar) pamoja na picha za kuchora. Vyote hivi wanapokuja watalii wa nje huzinunua na kuzifurahia, lakini tujiulize makabila haya yananufaika vipi kutokana na utalii? Hawanufaiki zaidi ya mifugo yao na wao wenyewe kupigwa na kufungwa magerezani.

Mheshimiwa Spika, matangazo kimataifa; yapo matangazo katika ligi ya Uingereza (England Premier League) peke yake ambayo hayakidhi haja, ni vyema tungekuwa na matangazo katika Bundesliga (German) Laliga (Spain), Series A (Italy), French-League na kadhalika. Pia CNN, BBC, Sky News, Reuters, DW – Deutsche Welle, Aljazeera, kote tutangaze nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, hata katika World Weather Condition Tanzania majiji yetu hayaonekani, tunaona tu Cape Town, Johannesburg, Cairo, Kampala, Kigali, Nairobi, Bujumbura lakini huoni Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Mbeya na Mwanza, kwa nini?

Mheshimiwa Spika, utalii wa bahari (ocean tourism), Tanzania tumejaaliwa ufukwe wa bahari wenye urefu wa kilometa 1,425 kutoka Jasini – Mkinga (Tanga) hadi Msimbati (Mtwara) lakini tunapata mapato kidogo ukilinganisha na mapato ya Kenya ambao ufukwe wao hauzidi kilometa 180 kutoka Mombasa – Vanga (Kenya). Tujiulize tunakwamia wapi?

Mheshimiwa Spika, fishing tourism & surfing; upo utalii wa kuvua samaki wakubwa na kuogelea kwa vidani pamoja na mashindano ya ngalawa (boat). Mashindano haya yanafanyika katika nchi za Dubai, Mozambique, Kenya, South Africa, kwa nini Tanzania tusifanye ambapo watalii wanapokuja wanakaa kwenye hotels na wanatumia huduma mbalimbali zinazotolewa na wenyeji, hii ni ajira, lakini tunashindwa kuweka vivutio (attractions).

Mheshimiwa Spika, VAT na tozo nyingi katika utalii Tanzania; Tanzania tumejaliwa mbuga, mapori, mito, maziwa, vijito na bahari; vyote hivi vipo na Mwenyezi Mungu ametaka tuvitunze na tuvitumie vizuri, vinahitajika vitupatie pia manufaa kwa Serikali na wananchi. Katika nchi sita za Afrika Mashariki, Tanzania ni ya kwanza kwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii, lakini kimapato, kimipango, kitaratibu na mazingira tunashindwa na nchi jirani zetu. Hata kwa watalii wengi kuja katika mbuga tunashindwa. Tunazo mbuga ambazo ni unique. Kwa mfano mbuga ya Saadani (Saadani National Park) ni mbuga pekee inayopakana na bahari na watalii wanapenda kuja kuitembelea lakini kodi zimezidi mno. Kwa mfano VAT, Kenya imeondolewa hali ambayo imekuwa ni kivutio kwa watalii kwenda Kenya zaidi kwa kuwa gharama ni nafuu. Hivyo na Tanzania tuondoe VAT/kodi lukuki

Mheshimiwa Spika, maliasili za misitu, katika nchi zote za SADC ni Tanzania pekee ndiyo pembezoni mwa barabara kumekuwa na magunia ya mkaa na kuni ambayo ni biashara iliyoshamiri.

Mheshimiwa Spika, kwa nini biashara hii imeshamiri? Ni kwa sababu Tanzania ndiyo nchi ambayo umeme na gesi ni bei ghali kuliko nchi zote duniani. Kama tunavyojua asilimia 75 ya Watanzania ni wakazi wa vijijini (wakulima na wafugaji). Je, hivi wakulima na wafugaji wanaweza kumudu kununua umeme wa luku na gesi kwa ajili ya kupikia?

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali ipunguze bei ya umeme, iondoe VAT na pia iondoe utitiri wa kodi, kuokoa muda na kuvutia watalii na pia kuwanufaisha Watanzania katika maisha yao ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi lakini kwanza niwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jiji la Tanga ambao nitaanza kwanza kwa kuwazungumzia katika suala zima la bomba la mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hilo nisije nikasahau kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kunipa afya njema na kuweza kuzungumza katika Bunge lako hili.

Mheshimwa Mwenyekiti, Tanga itakuwa ndiyo last destination ya bomba la mafuta na patakuwa na refinery nyingi ambapo itakuwa ndiyo mitambo ya kuingiza kwenye meli, mitambo ya kusafisha crude oil na mambo mengine. Kwa hiyo, kama walivyosema wasemaji wengine niishauri Serikali kwamba pale ambapo mradi utakuwa umepita kipaumbele cha kwanza katika ajira wapewe watu wa eneo hilo. Kwa hiyo, nawaombea watu wa Tanga wale ambao wana taaluma mbalimbali wapewe kipaumbele cha kwanza katika ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, nizungumzie suala zima la umeme wa REA. Sisi ambao tuko kwenye Majiji umeme wa REA sasa umekuwa kama unatugeuka kwa sababu tuliambiwa kwanza hakutarukwa kijiji hata kimoja lakini pia shule zote za msingi na sekondari ambazo hazina umeme watawekewa umeme wa REA. Nitaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze mpaka sasa hivi ni shule ngapi za msingi zimewekewa umeme wa REA na shule ngapi za sekondari zimewekewa umeme wa REA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, kwenye umeme wa REA, kuna baadhi ya vijiji waliomba umeme wa TANESCO baada ya kuja hii neema ya MCC ambayo ilileta REA I, II na III wakaomba sasa waingizwe katika mradi ule ambao utakapokuwa umefanya wiring unalipia Sh.27,000. Hata hivyo, TANESCO inawalazimisha walipe gharama ile ile ya TANESCO ya Sh.370,000. Mfano upo katika Jiji langu la Tanga kwenye Kata za Kiomoni kwa maeneo ya Pande Mavumbi, Pande Muheza, Pande Marembwe, vilevile katika Kata ya Pongwe maeneo ya Kinangwe na Kisimatui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, hata kwenye Kata ya Kirare kule kunakozalishwa sana muhogo, maeneo ya Mapojoni na maeneo ya Mtakuja, bado umeme wa REA huko haujafika lakini wananchi pia wamekuwa na huko wanakizungumkuti wakiuliza wanaambiwa kwa sababu mmekuwa Jiji ninyi hampaswi kupata umeme wa REA. Kuna kitu kipya sasa hivi pia nimeambiwa kinaitwa para urban, kwamba kuna kitengo kipya kinaanzishwa, huu itakuwa kama ni ujanja wa kuwakwepa wananchi. Kama tumeamua kuwasaidia wananchi tusianze kuleta visingizio vidogo vidogo tuwapelekeeni umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiambiana hapa kwamba asilimia 75 ya Watanzania wanaishi vijijini lakini tangu tupate Uhuru mpaka leo ni asilimia 10 tu ya Watanzania wanaofaidi umeme. Sasa kwa nini tunataka wazalishaji wawe wa vijijini lakini tukifika kwenye umeme tunaanza kupanga mipango tofauti. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuhakikishie ni kweli vijiji havitarukwa au lah! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna baadhi ya vijiji walipelekewa nguzo chache. Wanakijiji wako 1,000 wanaomba nguzo1,000 wanapelekewa nguzo 500 au nguzo 400, wengine wanakosa kupelekewa huduma ya umeme. Wako tayari kulipia kama vile ambavyo unalipa umeme
TANESCO lakini unasubiri miezi sita, hata kwenye REA watu wapo tayari kulipia lakini hawapatiwi umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ichukue utaratibu wa kuandaa kampuni ya TANESCO iwe kama vile kampuni za simu, pawe na ushindani kwa sababu disadvantage of monopoly kwa TANESCO ndiyo inawafanya wajione kwamba wao wako zaidi. Tuanzishe kampuni za umeme kama kampuni za simu iwe mwananchi ana uhuru wa kuchagua kampuni anayotaka. Simu leo wanashindana kupunguza bei ya muda wa maongezi kusudi wapate wateja. Kama kungekuwa na shirika lingine la umeme Tanzania, Waziri nakuhakikishia TANESCO labda ingebaki na Taasisi za Serikali, kwa sababu kuna usumbufu, kuna urasimu, na rushwa imejaa huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua, ufisadi wote unaopita Tanzania TANESCO hawatoki. Mheshimiwa Waziri tunaomba hili uliweke sawa. Kwenye umeme wa REA tunataka wananchi wetu wapate umeme wa vijijini na kama ni Sh.27,000 mtu akishafanya wiring iwe Sh.27,000 kweli, siyo Serikali inatangaza Sh.27,000 akifika TANESCO anaambiwa aaah, hizo ni kauli za wanasiasa tu, hili jambo linaichafua Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la bei ya umeme. Bei ya umeme ndiyo inayosababisha watu watumie mkaa kwa wingi, ndiyo inayosababisha watu watafute vishoka kwa ajili ya kuwaunganishia umeme. Sasa tushushe bei ya umeme ili wananchi wetu wafaidi umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Afrika Mashariki na Kati …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuweza kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Fedha. Pili, ninawashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga kwa ushirikiano ambao wananipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza kuchangia kwenye Mpango. Katika kitabu cha mpango, ukurasa wa tisa, limeelezwa kwamba pato halisi la Serikali limefikia trilioni 50 vilevile pia ni ongezeko la karibu trilioni 3.35 ukilinganisha na mwaka 2016.

Sasa hapa naona kuna marekebisho kidogo kwa sababu ukipiga hesabu vizuri, mgawanyo wa pato la Taifa kwa kipato cha kila Mtanzania kupata shilingi 2,275,601,000 kutoka shilingi 2,086,168,000 za mwaka 2016 naona panahitaji marekebisho kidogo. Namuomba Waziri alifanyie marekebisho hili ili kusudi hesabu hizi zikae sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la mfumuko wa bei. Katika Mpango ukurasa wa 12 kwenye kitabu kimeeleza kwamba mwenendo wa mfumuko wa bei ulikuwa tulivu. Sasa ukisema kwamba mfumuko wa bei ulikuwa tulivu wakati tuna mifano hai katika mwezi Mtukufu tu wa Ramadhani uliopita juzi ambapo leo ni siku nne tangu umemalizika, naona sio sawasawa. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu ukiangalia bei ya kio moja ya tambi kutoka shilingi 1,800 ilipanda mpaka shilingi 2,500 vilevile pia sukari kutoka kilo moja shilingi 2,000 ilipanda mpaka shilingi 2,500, ngano kutoka 1,200 ilipanda mpaka shilingi 1,800, vilevile pia mafuta ya kula kutoka shilingi 2,200 kwa lita yalipanda mpaka shilingi 3,000. Sasa tukisema kwamba eti mfumuko wa bei ulikuwa tulivu naona hilo haliko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza katika kitabu chetu hiki cha Mpango ni katika ukurasa wa 55 kuna ubia kati ya Sekta ya umma na sekta binafsi. Nimeona kwamba wamezungumzia zaidi katika masuala ya viwanda kwamba sekta ya umma ishirikiane au iwe na ubia na Serikali lakini kuna vyanzo vingine ambavyo vingeweza kuisaidia Serikali kimapato. Kwa mfano, kama Serikali ingeweza kuingia ubia na sekta binafsi na kuweza kujenga viwanja vya michezo kama vile michezo ya football, basketball, golf na tennis, angalau pia tungekuwa hapo tumeweka mazingira mazuri kati ya Serikali na sekta binafsi na ingeweza kutupatia kipato kwa sababu katika mipango hiyo sikuiona katika kitabu, sasa nashauri mipango hiyo nayo iingizwe katika Mpango wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni uandaaji wa wachezaji wetu. Nchi za wenzetu nyingi zimekuwa zinanufaika baada ya wachezaji wao kuwa wanacheza katika nchi za Ulaya. Kwa mfano, nchi kama Nigeria, Senegal, Mali, Tunisia, Algeria na nyinginezo, wameweza kukusanya mapato, hata Brazil Serikali inakusanya kodi kutoka kwa wachezaji kwa sababu kunakuwa na maandalizi maalum, lakini katika kitabu hiki sijaona kama kuna mpango wa kuiendeleza sekta ya michezo kupitia hivyo viwanja hata kwa wachezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kulizungumzia sasa niende moja kwa moja kwenye bajeti yetu. Katika bajeti kuna kitu ambacho ninakiona hakiko sawa, kwa mfano, katika bajeti ya Wizara ya Kilimo tumeona hapa kuna upungufu wa karibu asilimia 23 ambayo ni sawasawa na karibu kwa mfano katika fedha za korosho kuna pesa ambazo zilikuwa ni shilingi bilioni 211 za Mikoa ya Kusini, hizi zimeleta mkanganyiko, hazijapelekwa na hazijulikani ziko wapi.

Sasa atakapokuja Waziri hapa atueleze pia kwanini ninagusa kwenye zao la korosho kwa sababu na sisi Tanga katika baadhi ya maeneo korosho zinalimwa. Sasa ikiwa imeguswa Mikoa ya Kusini maana yake na Tanga pia imeguswa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni katika kupunguza kodi kwa taulo za kike. Mimi naipongeza Serikali kwamba imepunguza kodi, lakini katika siku za karibuni mimi nilichangia nikatoa mfano wa nchi ya Kenya. Rais Uhuru Kenyatta alitia saini sheria ambayo Kenya watazitoa taulo bure badala ya kusema wanapunguza kodi. Kwa nini ninalisema hili? Kenya wameondoa kodi lakini wakaamua pia zitolewe bure, hapa katika viwanda ambavyo vinazalisha hizo taulo za kike, baadhi ya viwanda vimepunguziwa tu kodi, lakini baadhi ya kodi zipo. Kwa hiyo, tufikirie wale watoto wa kike ambao wako maeneo ya vijijini, hiyo taulo ya kike iliyokuwa inauzwa shilingi 3,500 hata ikiuzwa shilingi 1,500 bado kwao itakuwa ni tatizo kwa sababu hawana njia za kipato ambazo zitawawezesha kulipia taulo hizo za kike. Kwa hiyo, naishauri Serikali badala ya kuondoa kodi, zitolewe bure kwa watoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kulichangia ni kuhusu wastaafu. Serikali yetu kwanza katika kipindi cha miaka miwili hii tumeshindwa kuongeza mishahara ya wafanyakazi. Sasa bado pamoja na kushindwa kuongeza mishahara, kuna tatizo la wastaafu, wale waliokuwa watumishi wa Serikali waliongezewa kutoka shilingi 50,000 mpaka shilingi 100,000 tena wanalipwa kila mwezi, lakini wale waliokuwa watumishi wa mashirika ya umma bado wako pale pale katika kiwango cha shilingi 50,000 na wanaendelea kulipwa shilingi 50,000 tena kwa malimbikizo baada ya kila miezi mitatu.

Kwa hiyo, naishauri Serikali kwanza hawa wastaafu waliokuwa katika Mashirika ya Umma nao waongezewe wafikie shilingi 100,000 lakini walipwe kila mwezi na isiwe wanalipwa kila baada ya miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ninalopenda kulizungumza ni deni la ndani tumeambiwa ni himilivu, lakini bado kuna wazabuni ambao wana-supply vyakula katika magereza, katika shule na taasisi nyingine ambazo zinahitaji vyakula kama vile hospitali. Wazabuni hawa wengine wanapelekwa mahakamani, wanadaiwa kwa muda mrefu na kila mwaka imekuwa inatolewa ahadi tu kwamba wataanza kulipwa.

Kwa hiyo, nashauri Serikali ituambie hapa/Waziri atakapokuja atuambie ni lini wataanza kuwalipa wazabuni ambao wanaidai Serikali. Kwa mfano, katika Jiji letu la Tanga wapo wazabuni wengi tu ambao wanadai ambao wame- supply vyakula magerezani, hospitalini na shuleni, lakini nimeshuhudia wengine wanataka kufilisiwa, walichukua mikopo kwenye benki, wanashindwa kulipa mikopo ile lakini Serikali inaendelea kuwapa ahadi. Naitaka Serikali ijibu kwamba ni lini wazabuni wale watalipwa fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni katika miradi. Miradi bado inapelekewa fedha kwa kuchelewa na fedha hizi zinakuwa hazitoshi na bahati mbaya mara nyingi zinapelekwa katika robo ya mwisho ya mwaka wa fedha wa Serikali matokeo yake sasa miradi baada ya kuwa fedha zimeshafika Wakurugenzi, wataalam na wanaohusika wengine inapelekwa haraka haraka matokeo yake inakuwa chini ya viwango. Kwa hiyo, naishauri Serikali iendelee kupeleka fedha mapema lakini pia namtaka Waziri wa Fedha Tanga katika Halmashauri yetu tumetenga shilingi milioni 300 kwa jengo la Hospitali ya Wilaya na tulikwishaanza kipindikilichopita (mwaka jana) tukajenga administration block kwa takriban shilingi milioni 400 lakini sasa hatujapata fedha kwa ajili ya kuweka hii OPD, kwa hiyo naiomba Serikali ituongezee fedha ili tuweze kujenga jengo la OPD.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ni kuhusu wastaafu wanaotarajiwa kustaafu, kama Serikali imeshindwa kuwalipa wafanyakazi au kuwaongezea mishahara katika miaka miwili hii, je hawa watakaostaafu mwaka huu, Serikali ina fedha za kuwalipa? Naomba atuthibitishie Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwamba hata watakaostaafu waweze kulipwa fedha zao. Kwa nini nalisema hili? Naogopa kwamba Watanzania wataendelea kuwa maskini na mtu baada ya kustaafu anakuwa hana umri mrefu, anapoteza maisha kwa sababu anakuwa hana kipato. Kwa hiyo, ninamtaka Waziri atakapokuja hapa aje atuambie kwamba wamejiandaa vipi kuwalipa wastaafu wanaotarajiwa kwa sababu watumishi wengi wa Serikali ni wastaafu watarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuweza kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Fedha. Pili, ninawashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga kwa ushirikiano ambao wananipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza kuchangia kwenye Mpango. Katika kitabu cha mpango, ukurasa wa tisa, limeelezwa kwamba pato halisi la Serikali limefikia trilioni 50 vilevile pia ni ongezeko la karibu trilioni 3.35 ukilinganisha na mwaka 2016.

Sasa hapa naona kuna marekebisho kidogo kwa sababu ukipiga hesabu vizuri, mgawanyo wa pato la Taifa kwa kipato cha kila Mtanzania kupata shilingi 2,275,601,000 kutoka shilingi 2,086,168,000 za mwaka 2016 naona panahitaji marekebisho kidogo. Namuomba Waziri alifanyie marekebisho hili ili kusudi hesabu hizi zikae sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la mfumuko wa bei. Katika Mpango ukurasa wa 12 kwenye kitabu kimeeleza kwamba mwenendo wa mfumuko wa bei ulikuwa tulivu. Sasa ukisema kwamba mfumuko wa bei ulikuwa tulivu wakati tuna mifano hai katika mwezi Mtukufu tu wa Ramadhani uliopita juzi ambapo leo ni siku nne tangu umemalizika, naona sio sawasawa. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu ukiangalia bei ya kio moja ya tambi kutoka shilingi 1,800 ilipanda mpaka shilingi 2,500 vilevile pia sukari kutoka kilo moja shilingi 2,000 ilipanda mpaka shilingi 2,500, ngano kutoka 1,200 ilipanda mpaka shilingi 1,800, vilevile pia mafuta ya kula kutoka shilingi 2,200 kwa lita yalipanda mpaka shilingi 3,000. Sasa tukisema kwamba eti mfumuko wa bei ulikuwa tulivu naona hilo haliko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza katika kitabu chetu hiki cha Mpango ni katika ukurasa wa 55 kuna ubia kati ya Sekta ya umma na sekta binafsi. Nimeona kwamba wamezungumzia zaidi katika masuala ya viwanda kwamba sekta ya umma ishirikiane au iwe na ubia na Serikali lakini kuna vyanzo vingine ambavyo vingeweza kuisaidia Serikali kimapato. Kwa mfano, kama Serikali ingeweza kuingia ubia na sekta binafsi na kuweza kujenga viwanja vya michezo kama vile michezo ya football, basketball, golf na tennis, angalau pia tungekuwa hapo tumeweka mazingira mazuri kati ya Serikali na sekta binafsi na ingeweza kutupatia kipato kwa sababu katika mipango hiyo sikuiona katika kitabu, sasa nashauri mipango hiyo nayo iingizwe katika Mpango wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni uandaaji wa wachezaji wetu. Nchi za wenzetu nyingi zimekuwa zinanufaika baada ya wachezaji wao kuwa wanacheza katika nchi za Ulaya. Kwa mfano, nchi kama Nigeria, Senegal, Mali, Tunisia, Algeria na nyinginezo, wameweza kukusanya mapato, hata Brazil Serikali inakusanya kodi kutoka kwa wachezaji kwa sababu kunakuwa na maandalizi maalum, lakini katika kitabu hiki sijaona kama kuna mpango wa kuiendeleza sekta ya michezo kupitia hivyo viwanja hata kwa wachezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kulizungumzia sasa niende moja kwa moja kwenye bajeti yetu. Katika bajeti kuna kitu ambacho ninakiona hakiko sawa, kwa mfano, katika bajeti ya Wizara ya Kilimo tumeona hapa kuna upungufu wa karibu asilimia 23 ambayo ni sawasawa na karibu kwa mfano katika fedha za korosho kuna pesa ambazo zilikuwa ni shilingi bilioni 211 za Mikoa ya Kusini, hizi zimeleta mkanganyiko, hazijapelekwa na hazijulikani ziko wapi.

Sasa atakapokuja Waziri hapa atueleze pia kwanini ninagusa kwenye zao la korosho kwa sababu na sisi Tanga katika baadhi ya maeneo korosho zinalimwa. Sasa ikiwa imeguswa Mikoa ya Kusini maana yake na Tanga pia imeguswa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni katika kupunguza kodi kwa taulo za kike. Mimi naipongeza Serikali kwamba imepunguza kodi, lakini katika siku za karibuni mimi nilichangia nikatoa mfano wa nchi ya Kenya. Rais Uhuru Kenyatta alitia saini sheria ambayo Kenya watazitoa taulo bure badala ya kusema wanapunguza kodi. Kwa nini ninalisema hili? Kenya wameondoa kodi lakini wakaamua pia zitolewe bure, hapa katika viwanda ambavyo vinazalisha hizo taulo za kike, baadhi ya viwanda vimepunguziwa tu kodi, lakini baadhi ya kodi zipo. Kwa hiyo, tufikirie wale watoto wa kike ambao wako maeneo ya vijijini, hiyo taulo ya kike iliyokuwa inauzwa shilingi 3,500 hata ikiuzwa shilingi 1,500 bado kwao itakuwa ni tatizo kwa sababu hawana njia za kipato ambazo zitawawezesha kulipia taulo hizo za kike. Kwa hiyo, naishauri Serikali badala ya kuondoa kodi, zitolewe bure kwa watoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kulichangia ni kuhusu wastaafu. Serikali yetu kwanza katika kipindi cha miaka miwili hii tumeshindwa kuongeza mishahara ya wafanyakazi. Sasa bado pamoja na kushindwa kuongeza mishahara, kuna tatizo la wastaafu, wale waliokuwa watumishi wa Serikali waliongezewa kutoka shilingi 50,000 mpaka shilingi 100,000 tena wanalipwa kila mwezi, lakini wale waliokuwa watumishi wa mashirika ya umma bado wako pale pale katika kiwango cha shilingi 50,000 na wanaendelea kulipwa shilingi 50,000 tena kwa malimbikizo baada ya kila miezi mitatu.

Kwa hiyo, naishauri Serikali kwanza hawa wastaafu waliokuwa katika Mashirika ya Umma nao waongezewe wafikie shilingi 100,000 lakini walipwe kila mwezi na isiwe wanalipwa kila baada ya miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ninalopenda kulizungumza ni deni la ndani tumeambiwa ni himilivu, lakini bado kuna wazabuni ambao wana-supply vyakula katika magereza, katika shule na taasisi nyingine ambazo zinahitaji vyakula kama vile hospitali. Wazabuni hawa wengine wanapelekwa mahakamani, wanadaiwa kwa muda mrefu na kila mwaka imekuwa inatolewa ahadi tu kwamba wataanza kulipwa.

Kwa hiyo, nashauri Serikali ituambie hapa/Waziri atakapokuja atuambie ni lini wataanza kuwalipa wazabuni ambao wanaidai Serikali. Kwa mfano, katika Jiji letu la Tanga wapo wazabuni wengi tu ambao wanadai ambao wame- supply vyakula magerezani, hospitalini na shuleni, lakini nimeshuhudia wengine wanataka kufilisiwa, walichukua mikopo kwenye benki, wanashindwa kulipa mikopo ile lakini Serikali inaendelea kuwapa ahadi. Naitaka Serikali ijibu kwamba ni lini wazabuni wale watalipwa fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni katika miradi. Miradi bado inapelekewa fedha kwa kuchelewa na fedha hizi zinakuwa hazitoshi na bahati mbaya mara nyingi zinapelekwa katika robo ya mwisho ya mwaka wa fedha wa Serikali matokeo yake sasa miradi baada ya kuwa fedha zimeshafika Wakurugenzi, wataalam na wanaohusika wengine inapelekwa haraka haraka matokeo yake inakuwa chini ya viwango. Kwa hiyo, naishauri Serikali iendelee kupeleka fedha mapema lakini pia namtaka Waziri wa Fedha Tanga katika Halmashauri yetu tumetenga shilingi milioni 300 kwa jengo la Hospitali ya Wilaya na tulikwishaanza kipindikilichopita (mwaka jana) tukajenga administration block kwa takriban shilingi milioni 400 lakini sasa hatujapata fedha kwa ajili ya kuweka hii OPD, kwa hiyo naiomba Serikali ituongezee fedha ili tuweze kujenga jengo la OPD.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ni kuhusu wastaafu wanaotarajiwa kustaafu, kama Serikali imeshindwa kuwalipa wafanyakazi au kuwaongezea mishahara katika miaka miwili hii, je hawa watakaostaafu mwaka huu, Serikali ina fedha za kuwalipa? Naomba atuthibitishie Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwamba hata watakaostaafu waweze kulipwa fedha zao. Kwa nini nalisema hili? Naogopa kwamba Watanzania wataendelea kuwa maskini na mtu baada ya kustaafu anakuwa hana umri mrefu, anapoteza maisha kwa sababu anakuwa hana kipato. Kwa hiyo, ninamtaka Waziri atakapokuja hapa aje atuambie kwamba wamejiandaa vipi kuwalipa wastaafu wanaotarajiwa kwa sababu watumishi wengi wa Serikali ni wastaafu watarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami niungane na wenzangu kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa na afya njema na kuweza kuchangia katika Wizara hii muhimu. Vilevile pia nami nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri ambao wapo sasa hivi katika Wizara hii, lakini tutashauri na kueleza upungufu uliopo, wauchukue na kuweza kufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo nawatakia ndugu zangu Waislamu wote Tanzania na duniani kwa ujumla mfungo mwema wa mwezi wa Ramadhani. Pia natoa pole kwa Bunge letu kwa kuondokewa na Mbunge mwenzetu Mwalimu Bilago, Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema. Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, nitoe tu nami shukurani zangu vilevile kwa Wizara, lakini naona kuna upungufu kidogo, kwa sababu najua vipo vyama vya wachimbaji wadogo hususan wachimbaji wanawake, lakini sikuona au hawapo kama ilivyozoeleka kwa Wizara nyingine ambapo wahusika wanakuja kama tulivyoona katika uvuvi na kilimo. Kwa hiyo, nieleze kwanza upungufu au changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa la mashine za kukata madini katika nchi yetu au hizi wanazoziita mineral cutters, zipo chache. Sasa nazungumzia hili kwa sababu hili tatizo la utoroshwaji wa madini kwa uchunguzi ambao kwa maoni yangu nimeufanya unasababishwa na foleni kubwa ambapo unapokata madini, madini labda ya gram moja yanaweza yakatumia kukata kareti kwa muda wa saa nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa madini yanayochimbwa Tanzania ni mengi, matokeo yake sasa kunakuwa na foleni kubwa katika utakataji madini kama vile ilivyo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwenye Wizara ya Afya ambapo specimen moja inaweza ikachukua miaka miwili. Sasa inawezekana hii nayo ikawa ni sababu mojawapo ya kutoroshwa kwa madini yetu kwa sababu teknolojia tuliyonayo Tanzania ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Wizara na Serikali kwamba tuondoe au tupunguze kodi kwenye mashine za kukata madini ili ziwepo kwa wingi ili Watanzania sasa waweze kukata madini kwa muda mfupi baada ya kuwapeleka nchi jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naliona, ni ushauri wangu kwa Serikali kwamba Chuo cha Madini kinafanya kazi vizuri, lakini ama kipo kimoja au vipo vichache.

Sasa tulipofanya ziara na Kamati yetu ya PIC, tulipofika Shinyanga VETA tulikuta nao wana kozi ya ukataji wa madini. Naishauri Serikali, kwa kuwa Shinyanga VETA imewezekana, basi naamini katika VETA nyingine napo kozi zile zinaweza kuendeshwa. Kwa hiyo, naishauri Serikali iweke kozi za kukata madini katika Vyuo vya VETA. Kwanza, tuzalishe wataalam wengi wa madini ambao watakwenda kuwasaidia wachimbaji wadogo ili wawe wachimbaji bora, waepuke uchimbaji wa kubahatisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, itakuwa ni ajira kwa watu wetu ambao baada ya mafunzo yale naamini Wizara itaweza kuwaajiri na kuwapa shughuli ya kwenda kuwatembelea au kwenda katika maeneo ambayo yanachimbwa madini na kuweza kuwafanya wachimbaji wetu wawe wa kisasa kuepuka kufukiwa na vifusi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naishauri Serikali, Wizara haina rescue team. Tumeshuhudia mafuriko yaliyoporomoka ndani ya machimbo ya Mererani, mwaka 2016 kama sikosei, walikufa watu wengi tu. Ni kwa sababu kama pangekuwa pana zana za kisasa za uokoaji na kungekuwa na rescue team ambayo ina vifaa vya kisasa, tungeweza kuokoa maisha ya watu wale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata katika upasuaji wa mawe, kwa mfano, katika kware zilizopo Tanga ilitokea ajali pale, kuna mtu mmoja alilaliwa na jiwe. Kama kungekuwa na Helcopter Ambulance naamini angeweza kuchukuliwa akafikishwa Muhimbili Dar es Salaam angeweza kuokolewa maisha yake. Kwa hiyo, Wizara pia ijitahidi basi iwe na japo Ambulance Helcopter ambayo itaweza kuokoa maisha ya watu wetu pale itakapotokea ajali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni mabenki kutokuwaamini au kutokuwathamini wachimbaji wadogo. Imezungumzwa hapa kwamba Serikali imeanzisha uwezeshaji wa wachimbaji wadogo na kama sikosei katika kitabu cha Kamati imeeleza kwamba kuna wachimbaji ambao walikuwa wanawezeshwa U$ Dollar 50,000 ambayo ni sawasawa na milioni 100 hadi U$ Dollar 100,000 ambayo ni sawasawa na milioni 200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika Mkoa wangu wa Tanga napo kuna madini kule ya aina nyingi tu ya vito ambayo nitayataja baadaye. Ningetaka kujua, vigezo vinavyotumika kuwawezesha wachimbaji wadogo hawa kupata Dollar 50,000 na Dollar 100,000 ili na wale wachimbaji walioko Tanga waweze kupatiwa msaada huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulijua pia ni idadi ya wale wachimbaji wadogo ambao wamewezeshwa hasa ile Dollar 50,000 na 100,000 ni wangapi; na ni maeneo gani ya machimbo katika Tanzania yetu? Ili tuweze kujua na tunapoulizwa na baadhi ya wachimbaji tuweze kuwapa elimu, wafuate vigezo waweze kupatiwa msaada huo wa Dollar 50,000 na Dollar 100,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile yametajwa madini mengi sana hapa, kwa mfano madini ya jasi, yametajwa almasi, dhahabu, tanzanite lakini kuna madini mengine ya thamani ya vito. Kwa mfano, kama vile uranium pia hapa sikusikia ikitajwa taarifa yake, lakini kuna rubby kuna rhodolite, kuna green-garnet kuna green tourmaline na kadhalika. Yangechambuliwa katika takwimu ya mapato tujue kwamba green garnet kwa mwaka huu imeiingizia Serikali kiasi gani? Green tourmaline imeingiza kiasi gani? Rhodolite imeingiza kiasi gani? Rose imeingiza kiasi gani? Sapphire imeingiza kiasi gani? Ingekuwa ni takwimu bora zaidi kwa faida ya vizazi vijavyo na pia kwa faida ya Taifa kujua kwamba, kumbe madini tuna faida nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nasikitishwa kidogo na hii taarifa ya madini ya bati. Tanzania tulikuwa hatuna sababu ya kuwa na nyumba zilizoezekwa kwa majani, matembe, lakini pia kununua mabati kwa bei ghali. Sasa pana taarifa hapa imeeleza kwenye ukurasa wa 18 kwamba kuna masikitiko yaliyoelezwa na Kamati nami nayaunga mkono kwamba imekosekana fedha za kununua mtambo wa kuchakata bati na vilevile kukosa hati ya uasilia (ICGLR) yaani Certificate of Origin.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nauliza, Wizara inakuwaje ishindwe kupata fedha za kununua mtambo wa kuchakata bati wakati bati ni bidhaa ambayo kwanza ina soko wakati wote? Mabati yanatumika katika ujenzi wa nyumba, lakini pia kwa sasa hivi kwa sheria za ujenzi, kabla ya kujenga lazima uzungushe mabati; na yana soko kubwa ambapo Serikali kama ingekuwa na mtambo huo ingeweza kukusanya fedha nyingi tu ambazo zingesaidia katika matumizi ya masuala mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, je, ni lini Wizara sasa itanunua mtambo wa kuchakata bati? Vilevile, huu mpango mpaka tukashindwa kununua huu mtambo wa kuchakata bati, siyo hujuma za wenye viwanda vya mabati kwamba wanatufanyia hujuma kusudi waendelee kuuza mabati kwa bei ghali? Hilo nalo nitataka jibu lake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niliona katika taarifa hapa, kuna wanafunzi wa Chuo cha Madini Dodoma. Nafikiri vikwazo vingi na changamoto nyingi katika vyuo ni bajeti kuwa ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iongeze bajeti ya fedha katika Chuo cha Madini Dodoma ili wanafunzi wale waweze kujifunza kwa nafasi, lakini pia wasiwe na upungufu na usumbufu katika mafunzo yao. Watakapoingiziwa fedha kwa wakati, naamini wataweza kusoma vizuri na tutazalisha wartaalam bora zaidi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumshukuru Mungu kunijalia afya njema na kuweza kuchangia katika Wizara ya Madini. Niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga kwa kunituma kuja kuwasemea katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nitoe pole kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kuondokewa na Mbunge mwenzetu marehemu Mwalimu Kasuku Samson Bilago, Mbunge wa Jimbo la Buyungu Kigoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe masikitiko yangu kidogo kwa kuwa leo ni siku ya Bajeti ya Wizara ya Madini lakini sijawaona wawakilishi wa wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzania, hususani Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Wanawake na Chama cha Wachimbaji Wadogowadogo wa Madini Tanzania. Ushauri wangu kwa Serikali, katika bajeti ya mwakani, Wizara itoe mwaliko kwa wadau wa madini, wachimbaji wadogo, vyama vyao na kampuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa wachimbaji wadogo na Serikali. Wachimbaji wadogo duniani kote ndiyo wagunduzi wa kwanza wa madini na baadaye ndipo hupatikana wachimbaji wakubwa (wawekezaji) na kuingia mikataba na Serikali na kulipa kodi za Serikali zinazojulikana kama mrabaha. Niwape pole kwa kuwa wanagundua madini kisha Serikali wanakuja kuwafukuza na kuwaweka wawekezaji wageni (matajiri). Jambo hili si sawa kwa kuwa wachimbaji ndiyo wagunduzi wa kwanza, Serikali ingewathamini na wageni wangewathamini, ikibidi wenye migodi waingie ubia na wenyeji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali badala ya kuwapelekea FFU (Field Force Unit) na kuwafukuza kwa mabomu ya machozi (tear gas), iwawekee utaratibu wa kuwaelimisha na waweze kuona madini ni mali ya Taifa. Vilevile wachimbaji wadogo wapewe ajira katika kampuni za uwekezaji kutoka nje na wachimbaji wapewe mikopo na benki. Watanzania wazawa wakiajiriwa wanaweza kuwa ni askari kanzu (inteligency unit) kujua wawekezaji wabaya (bad investors) ambao wanatorosha madini yetu na kuweza kutoa taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, madini ya tanzanite na madini ya vito. Tanzania tumejaliwa madini ya thamani ya aina nyingi mno kama vile tanzanite yanayopatikana Tanzania tu, ruby, sapphire (pink, white and red), rhodolite, alexandrite, rose, change colour, green garnet, red garnet, green tourmaline, ammolite, moonstones. Madini yote haya yana thamani na ni ajira kwa vijana wa Kitanzania, endapo patafanyika mipango ya makusudi ya kuanzisha viwanda vya kuchakata madini (mines cater center). Pia madini haya tungepata taarifa zake kwamba kila aina imeingiza/ inaingiza kiasi gani kwa mwaka na iwepo data base ya precious stone.

Mheshimiwa Naibu Spika, madini ya tanzanite yanapatika nchini mwetu tu, duniani kote hakuna. Hivyo ni vyema yakafanyiwa matangazo ya kutosha kwani itakuwa ndiyo symbol ya nchi yetu kama ilivyo Mount Kilimanjaro kwa kuwa dunia nzima ipo Kilimanjaro moja tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, majanga katika uchimbaji madini. Katika migodi mikubwa na midogo duniani kuna changamoto kubwa ya ajali za moto, kufukiwa na vifusi, kuishiwa hewa ya oxygen, tetemeko la ardhi na mafuriko. Katika nchi za wenzetu kwa kuwa madini ni uchumi wamewekeza fedha nyingi lakini zipo rescue teams za uhakika ili kuweza kuokoa wachimbaji pale inapotokea dharura za ajali kama nilivyozitaja. Nashauri Serikali iweke utaratibu wa kuwa na rescue teams katika migodi yote mikubwa na midogo nchini Tanzania. Serikali inunue ambulance/helcopter ambayo itasaidia kuokoa maisha ya wachimbaji kwa kuwawahisha watakaokutwa na ajali katika hospital zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini madini yanatoroshwa? Madini yanatoroshwa kwa sababu mbalimbali kama: Foleni zinazosababishwa na uchache/ muda/teknolojia ndogo zinazosababisha wafanyabiashara wa madini kuyatorosha nje kwa kuwa ukataji unatumia muda mwingi kukata madini machache; technology iliyopo Tanzania ni ya kizamani na pia imepitwa na wakati; na mashine (mineral cutters machines) zipo chache mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nashauri Serikali yafuatayo:-

(i) Iwekeze katika vyuo vya madini ili vyuo vizalishe wataalam watakaosaidia wachimbaji wadogo.

(ii) Ianzishe course za masomo ya ukataji wa madini na aina za madini katika vyuo vyetu vya VETA. Kwa mfano, katika ziara ya Kamati ya PAC Shinyanga tulikuta course ya ukataji madini katika Chuo cha VETA Shinyanga. Ada ya course hizi ziwe kiwango cha chini kuwavutia wanafunzi.

(iii) Mashine za ukataji madini ziwekewe kodi ndogo ili kufanya bei ya ukataji iwe ndogo na kuweza kuongeza thamani ya madini yetu baada ya kukatwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, benki kutowaamini wachimbaji. Benki na taasisi za fedha haziwaamini wachimbaji wadogo kwa kuwa haziwakopeshi na ama kuna masharti magumu mno. Nashauri Serikali kama ifuatavyo:-

(i) Iweke mpango wa kuwakopesha vifaa (mitambo) wachimbaji wadogo kwa ajili ya uchimbaji badala ya fedha.

(ii) Mpango wa kuwawezesha wachimbaji wadogo US$50,000 (Sh.100,000,000) hadi US$100 (Sh.200,000,000) uwekwe wazi na vigezo vinavyotumika, wachimbaji waelimishwe ili wajue na kuweza kufaidika na mpango huu.

(iii) Benki zote zipewe maelekezo na namna ya kuwakopesha wachimbaji wadogo mitambo/fedha na uwepo uwazi.

(iv) Wizara itoe takwimu za wachimbaji wadogo wote waliowezeshwa na maeneo walipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, madini ya ujenzi/viwandani. Wizara katika taarifa yake haijatoa takwimu za madini ya uranium yanayotumika katika utengenezaji wa silaha za nuclear. Naomba tupatiwe taarifa kwa hapa nchini yapo maeneo gani na yapo kwa ujazo wa kiasi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, madini ya bati, ni madini ambayo Serikali kama ingetilia maanani kwa kununua mtambo wa kuchakata bati, wananchi wetu wasingekuwa na sababu ya kuishi katika nyumba za nyasi, tembe na bei isingekuwa kubwa. Naiomba Serikali inunue mtambo wa kuchakata bati kwa manufaa ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri afanye ziara katika maeneo yenye madini katika Jiji na Mkoa wa Tanga katika maeneo yafuatayo ili kutambua kero za wachimbaji.

Na. Eneo la Mgodi Sehemu Ulipo Aina ya Madini
1 Kalalani / Kigwase Tarafa Daluni - Korogwe Madini ya Vito
2 Ng’ombeni, Umba “
3 Amboni Kata ya Mzizima - Tanga Kokoto/ Mawe/ Chokaa
4 Maweni Kata ya Maweni Jiji la Tanga Kokoto na Mawe ya ujenzi
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujaalia afya njema tukaweza kuzungumza masuala mbalimbali ya nchi yetu. Pili, asubuhi wakati Mheshimiwa Baba Paroko Joseph Selasini akizungumza hapa kuna maneno aliyasema, niongezee kidogo katika yale aliyoyasema, nimuombe Rais wetu msikivu, kwa heshima na taadhima, haya yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, kupitia kwa DPP wetu ambaye ana dhamana basi waweze kuwapatia dhamana Waheshimiwa Wabunge wenzetu ambao tumewakosa katika Bunge hili; Mheshimiwa Freeman Mbowe na Mheshimiwa Esther Matiko ili Bunge lijalo tuweze kujumuika nao. Pili, kupitia nafasi hiyohiyo, nimwombe tena Mheshimiwa Rais wale Mashekhe wetu ambao hawajapata dhamana mpaka leo nao wapatiwe dhamana ili waweze kuhudumia jamii yetu katika huduma za kiroho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine niipongeze TAMISEMI kwa kumaliza mgogoro wetu wa Hospitali ya Wilaya kule Tanga ambapo sasa ujenzi unaendelea. Vilevile pia nishukuru kwa Vituo vyetu vya Afya vya Makorora, Mikanjuni na Ngamiani navyo kwa kupatiwa fedha takribani shilingi bilioni 1.4 na hali inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwenye mchango wangu nizungumzie Serikali za Mitaa. Najua tunazo Serikali za namna mbili, tuna Central Government (Serikali Kuu) na tuna Local Government ambazo ni Serikali zetu za Kienyeji au Serikali za Mitaa. Mimi nilikuwa najua kazi ya Serikali za Mitaa kwanza ni kukusanya kodi, kutoa huduma bila ya kusahau kutengeneza ajira kwa wananchi wa eneo husika. Hata hivyo, sasa hivi Serikali zetu za Mitaa zimepokonywa vyanzo vya mapato kama property tax hata mabango ya biashara, imekwenda sasa wananyang’anywa mpaka uwakala wa barabara za vumbi, ukarabati na ujenzi wa mifereji lakini hata huduma za taa za barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu shughuli hizi sasa zinapelekwa TARURA (Wakala wa Barabara) basi TAMISEMI ingefanya utaratibu ufuatao; hizo gharama za usafi wa mifereji na taa za barabarani nazo zingepelekwa TARURA ili kuzipunguzia Halmashauri zetu mzigo. Kwa sababu Halmashauri zinafanya shughuli kubwa sana, zinashughulika na masuala ya afya, elimu na masuala mengine ya huduma za kijamii. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba TARURA ibebe mzigo wa huduma za usafi wa mifereji na taa za barabani lakini enough is enough hivi vyanzo vya mapato vya Halmashauri visichukuliwe vingine.

Mheshimiwa Spika, hata hili suala la uvuvi, Halmashauri zinapokea mapato katika uvuvi kutokana na ushuru wa samaki. Kwa bahati mbaya sasa katika hiyo operesheni, kumekuwa na tatizo kwamba wavuvi wanapokamatwa na nyavu ambazo haziruhusiwi wanatozwa faini mpaka shilingi milioni 2 kwa nyavu moja lakini cha kushangaza, nina mfano wa risiti hapa ambazo wametozwa wavuvi, navyojua mapato ya Serikali sasa hivi yanakusanywa kwa EFD machine, hizi risiti ukizitazama zimeandikwa kwa mkono. Nina mashaka inawezekana mapato haya yakavuja na ikawa ni mianya hii ya kutengeneza masuala ya rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nalotaka kulizungumza ni kwenye uteuzi wa Wakurugenzi. Baadhi ya Wakurugenzi siyo wote wamekuwa wababe na wakati mwingine wanakuwa na kiburi. Nitoe mfano wa Mkurugenzi wa Jiji langu la Tanga, mimi upande mwingine ni Diwani wa kuchaguliwa katika Kata yangu lakini ameniandikia barua kwamba eti nimepoteza sifa ya kuwa Diwani kwa kukosa Ward Council sita. Naamini Mkurugenzi anajua Kanuni za Halmashauri, moja ya sifa za Diwani kupoteza sifa ni kutohudhuria vikao vitatu vya Mabaraza ya Madiwani (Full Council) bila taarifa siyo Ward Council sita. Nimeiandikia barua Wizara ya TAMISEMI lakini mpaka leo sijapata majibu. Vilevile Mkurugenzi hata kuniita labda akaniambia Bwana hili jambo ulilifanya kimakosa kwa sababu Kanuni hazisemi hivyo imeshindikana. Mimi niitake TAMISEMI kwanza inipe majibu ya barua yangu lakini Wakurugenzi nao tuwasimamie waweze kutoa ushirikiano mzuri kwa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mungu, mwingi wa rehema na wakati wote nitaendelea kuwashukuru wazazi na wapigakura wangu wa Jiji la Tanga kwa kuniwezesha kuwa Mbunge wao. Nitaendelea kuwawakilisha katika kufikisha kero zao katika Bunge letu ili ziweze kufanyiwa kazi na kuwapelekea wananchi maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya vijana; vijana wote ndio engine ya maendeleo na nguvu kazi katika sekta zote iwe ajira, michezo, kilimo, uvuvi, viwanda na kadhalika, mfano, vijana wana nguvu ya kusukuma mbele shughuli za kiuchumi. Ajira viwandani wanaajiriwa viwanda kwa kuwa wana nguvu ya kuendesha mashine kubeba na kutengeza mashine na kupakiwa bidhaa na kupeleka maeneo mbalimbali ya nchi. Hivyo nadiriki kusema vijana Taifa la leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zamani wanafunzi walikosa nafasi kuendelea na masomo kidato cha kwanza na kidato cha tano na sita, walikuwa wanajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na waliweza kupata mafunzo ya ufundi umeme, uashi, seremala na vifaa vya kielektroniki kama computer, magari na kadhalika. Baada ya kufuzu mafunzo yao, waliweza kujiajiri na kuweza kupata kipato cha kujikimu kimaisha. Nashauri vijana walioondolewa masharti magumu kujiunga na JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walemavu, nichukue fursa hii kumpongeza agizo la Serikali na pia kusisitiza kuwa utaratibu wa kutenga 10% ya mapato ya Halmashauri zote nchini kwa magawanyo zifuatao 2% watu wenye ulemavu, 4% vijana, 4% akina mama. Nashauri mgawanyo huu usimamiwe kikamilifu na fedha zitolewe kwa wakati ili kufikia malengo tuliojiwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya kiuchumi ukurasa II, pato la Taifa lilikuwa kwa 6.7 mwaka 2018 badala ya 6.2 mwaka 2017 ukiangalia wananchi watanzania mitaani wamechoka wako hpi bi taaban mzunguko wa fedha ni mdogo, benki hazikopeshi, masharti ya mikopo ni magumu sana, hali inayopelekea wananchi kukopa katika VICOBA, BRAC, SEDA, Poverty Africa, FINCA na kadhalika ambazo zinatoza riba kubwa sana kiasi kupelekea wakopaji kunyang’anywa vyombo vyao, nyumba zao kupigwa mnada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, thamani ya shilingi kuporomoka; thamani ya shilingi ya Tanzania kila kukicha imekuwa ikiporomoka/kushuka kwa thamani (inflation), lakini tunaambiwa uchumi unakua, naomba ufafanuzi katika hili kwa faida ya Watanzania. Mfano, mwaka 2018 USD moja ilikuwa sawasawa na shilingi 2226 mpaka mwaka 2019 USD moja ni sawasawa na Sh.2400. Mwaka 2018 pound moja ilikuwa sawasawa na shilingi ….. mpaka mwaka 2019 pound moja ni sawasawa na shilingi…. Mwaka 2018 shilingi moja ya Kenya ilikuwa sawasawa na shilingi 20 mpaka mwaka 2019, shilingi moja ya Kenya sawasawa na shilingi 220. Mwaka 2018 S/Rand moja ilikuwa sawasawa na shilingi…mpaka mwaka 2019 S/Rand moja ni sawasawa na shilingi ….. Katika hali hii ambapo shilingi ya Tanzania inashuka uchumi unakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumuko wa bei, ulipungua kwa wastani 4.0%, mwaka 2018 hadi 3.0 mwaka 2019 mwezi Januari. Sasa nataka nipate ufafanuzi kwa kuwa naona ipo tofauti katika taarifa kwa mfano ufuatao:-

(i) Mwaka 2018 Juni – Sukari kilo moja ilikuwa shilingi 2,100 lakini mwaka 2019 sukari kilo moja ni shilingi 2,500;

(ii) Mwaka 2018 Juni –Maharage kilo moja yalikuwa Sh.1,700, lakini mwaka 2019, maharage kilo moja ni Sh.2,400;

(iii) Mwaka 2018 Juni –Tambi zilikuwa kilo moja Sh.1,800, mpaka mwaka 2019, tambi kilo moja ni Sh.2,500;

(iv) Mwaka 2018 Juni – mafuta yalikuwa lita moja ni Sh.1,100, mpaka kufikia 2019, mafuta lita moja Sh.2,000; na

(v) Mwaka 2018, petrol lita moja ilikuwa Sh.1,600, lakini mpaka kufikia mwaka 2019, petrol lita moja ni Sh.2,206.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu hii hapo juu mfumuko wa bei Tanzania umeshuka au umezidi? Waziri atoe ufafanuzi kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya elimu na sintofahamu kwa wazazi, Katika sekta ya elimu kuna sintofahamu hasa baada ya Serikali kutangaza elimu bure darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Wazazi wanaelewa kuwa bure ni free no charge, hivyo hawalipii maji, umeme, mlinzi, uji na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaeleza kwa kila mwezi inatoa fedha katika sekta ya elimu Sh.… kwa mwezi, wananchi wanajua fedha za Serikali ni nyingi na zipo. Hali imepelekea umeme na maji kukatwa shuleni (mkumbuke Mheshimiwa Rais aliwaambia TANESCO, penye deni la umeme kata na pia ulinzi hakuna na vifaa shuleni vimeanza kuibwa. Ushauri, naomba Serikali itolee ufafanuzi elimu bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Jamii NSSF, LAPF, LPF, PSPF, PPF na wafanyakazi. Mifuko hii inakusanya mapato kupitia makato yanayokatwa katika kipato cha watumishi mbalimbali Serikalini na sekta binafsi na Mfuko mmoja PSSF lakini bado kuna tatizo pale wastaafu wanapodai mafao yao baada ya kustaafu kuna usumbufu mkubwa sana. Kama tunavyojua ukistaafu mategemeo ni akiba yako (mafao ya kustaafu). Hivyo nashauri na kuomba Waziri aeleze usumbufu huu chanzo chake nini na usumbufu huu utakwisha lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo utaratibu umefanyika wa kuwaongezea pension waliokuwa watumishi wa Serikali toka Sh.50,000 hadi Sh.100,000 lakini kwa waliokuwa watumishi wa Mashirika ya Umma (SU), bado watumishi wa SU wanaendelea kulipwa pension ya Sh.50,000 kwa malimbikizo ya malipo baada ya miezi mitatu (3). Tukumbuke wastaafu ni watu wenye umri mkubwa na wana shida na matatizo mengi. Ushauri wangu ni kwamba, waliokuwa watumishi (SU) waongezewe na wao toka Sh.50,000 hadi Sh.100,000 na walipwe kila mwezi bila malimbikizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya kisiasa nchini ni ngumu na demokrasi inahitaji kuboreshwa na kuimarishwa. Kitendo cha kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano kumepelekea msisimko wa kisiasa na uelewa wa siasa kwa wananchi kurudi nyuma au kupunguza hamu na ladha ya siasa hadi kupelekea baadhi ya wanasiasa kupotea katika ramani ya siasa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapomzuia mwanasiasa asifanye mikutano ya hadhara, asifanye maandamano, ni sawa na kumzuia mkulima asiende shambani, mvuvi asiende baharini, mchezaji asiende uwanjani au mfanyakazi asiende ofisi, kwa kuwa mwanasiasa ofisi yake ni jukwaa la mikutano au mkutano. Ushauri ni kwamba, naiomba Serikali katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu hali hii ingeangaliwa upya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kuwa na afya njema na kuweza kukutana katika kikao chetu hiki cha Bunge na kuzungumzia mambo mbalimbali ya nchi yetu. Pia nishukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga bila kukusahau wewe kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuchangia TAMISEMI, labda nami niwe miongoni mwa wale ambao tunashukuru kwa ule mpango wa kujenga vituo vya afya 300. Kwenye Jimbo langu la Tanga tumepata vituo vya Makorola, Mikanjuni na Ngamiani. Tumepata takribani shilingi bilioni moja na milioni mia nne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pia nisisahau kwamba tulikuwa mgogoro wa Hospali ya Wilaya ijengwe sehemu gani. Baada ya kuwasiliana na Mheshimiwa Waziri hapo mambo yamewekwa sawa na sasa ujenzi unaendelea. Nishukuru kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye suala la elimu hususani elimu bure. Elimu bure mimi niseme imepigiwa debe sana lakini wananchi na wazazi bado hawajaielewa vizuri na hata badhi ya Wabunge nafikiri hawajaielewa vizuri kwa saabu unaposema kitu bure ni ile free no charge sasa wazazi kufuatia suala hilo wamekuwa wazito kuchangia masuala ya umeme na maji, fedha ya mlinzi na hata akuchangia vifaa. Unapowahoji wanakwambia kwamba tumeambiwa elimu bure na ndiyo maana watoto wameongezeka sana katika shule zetu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niitake Serikali sasa, kwa sababu watoto tumekuwa kama tunawaadhibu katika baadhi ya shule maji yamekatwa kwa sababu kufuatia kauli ya Mheshimiwa Rais ile anayosema maneno ni mawili ‘Kata’ kwamba panapodaiwa maji na umeme kata. TANESCO na Mamlaka za Maji sasa hivi hazitoi huduma zinafanya biashara matokeo yake umeme na maji katika shule yamekatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake tunawaadhibu watoto. Wanafunzi hawa masikini ya Mungu, malaika wa Mungu hawana hata maji ya kunywa shuleni wanalazimika ama kubeba chupa za maji katika mabegi yao wanayoweka madaftari au kama wako shule basi pana nyumba ya jirani karibu waende wakaombe maji ya kunywa katika nyumba za jirani. Naiona hii ni hatari kwa sababu katika baadhi ya nyumba kuna watu wengine siyo wema, mathalani watoto wa kike tunaweza kuwahatarisha maisha yao kwa kubakwa na kupata maradhi ya UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isiongeze fedha katika ule mpango wa kupeleka capitation na fedha za matumizi katika shule tukaweza kulipia maji na umeme kwenye shule zetu? Au kwa nini Serikali isisamahe kwenye shule za msingi na sekondari lakini nifike mbali zaidi hata kwenye Misikiti na Makanisa kule ambako Mwenyezi Mungu tunamwomba nchi iendelee kuwa amani tuweke huduma ya maji na umeme iwe bure? Kwa hiyo, naishauri Serikali lifanyiwe kazi suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa nini pia tusiwape umeme wanafunzi wakaweza kutuumia katika kujifunza kwa sababu kuna mambo mengi. Sote tumepitia elimu ya msingi panakuwa na umeme mnajifundisha mambo mengi, sote tumeyaona haya. Kwa hiyo, naiomba Serikali hilo walifanyie kazi na tuliambiwa kwenye bajeti ya mwaka jana kwenye Wizara ya Nishati na Madini kwamba kwenye huu umeme wa REA watahakikisha kuwa shule zote nchini zinawekwa umeme, naliomba suala hilo liharakishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nalotaka kulizungumzia ni suala la dawa. Tumeona dawa zilitengewa takribani shilingi bilioni 531 lakini fedha iliyopokelewa ilikuwa ni shilingi milioni 81, pana tofauti ya takribani shilingi bilioni 450. Kama ikiwa tunatenga fedha kubwa halafu fedha tunayopeleka ni kidogo hatuwasaidii wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hakuna haja ya kuweka kasma kubwa halafu tunapelekea asilimia ndogo ya fedha. Kama tumepanga shilingi milioni 5312 basi angalau kungepelekwa shilingi milioni 400 hapo ingekuwa tumewasaidia lakini katika shilingi bilioni 531 kupeleka shilingi milioni 81 tu tunawakwaza ama madaktari na watumishi wetu wa Idara ya Afya. Kwa hiyo, naiomba Serikali pale inapopanga bajeti ihakikishe fedha inapatikana na inapelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye Mfuko wa Maji, Tanga tunayo miradi ya maji ya ile vijiji 10 kila Halmashauri lakini kwa masikitiko makubwa niseme upande wa Kusini tulifanikiwa, maji yanatoka kuelekea upande wa Marungu, Kirare, Tongoni na wananchi sasa hivi wanaomba huduma ya maji ipelekwe mpaka kwenye nyumba zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika mradi wa Kaskazini wa Mabokweni, Kibafuta, Mpirani na Chongoleani mpaka leo kuna kizungumkuti, maji hayatoki na wananchi wana shida ya maji na mimi mwenyewe nimefika nikashuhudia. Nitamwomba tu Mheshimiwa Waziri wa Maji au Naibu wake mara baada ya Bunge hili tutembelee ili tujue kikwazo kwa nini maji hayatoki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mradi huohuo wa maji, Kamati PAC ambayo nipo tumetembelea mradi wa maji ule wa Chalinze na maeneo mengine naona kuna hitilafu kidogo kwa sababu fedha zilizoahidiwa katika mkopo ilikuwa ni takribani shilingi bilioni 158 mpaka sasa hivi zimetumika shilingi bilioni 93 lakini kuna shilingi bilioni 65 bado hazijatumika. Hata hivyo, kuna masharti ambayo katika miradi ile vifaa vyote hadi bolt lazima itoke kwa yule mtu ambaye mmeingia naye mkataba kwamba awakopeshe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ule mradi unafadhiliwa na India sasa basi hata mipira, bolt, nati za kwenye mradi lazima zitoke India! Tunasema tunalinda viwanda vya ndani, tunalindaje viwanda vya ndani kwa miaktaba mibovu kiasi hiki? Ina maana watumishi sasa baadhi ya ma-expert ambao wapo hata Watanzania wanashindwa kulipwa sawasawa na wale ma-expert wa Kihindi, naona hiyo ni dosari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie utawala bora. Ukitazama Katiba, Ibara ya 146(1)(2)(c) kinaeleza hapa kwamba, madhumuni ya kuwepo Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi na vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa ujumla. Ukienda kwenye kipengele (c) inasema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mbarouk.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ndiyo uliozaa jina Tanzania na ni wa kihistoria Afrika na duniani kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo nchi zinataka kufanya Muungano kama huu lakini zimeshindwa na pia zipo nchi ziliungana na baadaye muungano huo ulivunjika na sasa zinafanyika bidii za kujiunga upya na mfano ni Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977 na sasa bidii na juhudi zinafanyika kuunda upya muungano huo (East Africa Community) kwa nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Southern Sudan. Ni mategemeo yangu Muungano wa watu wa pande hizi (Tanganyika na Zanzibar) utadumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida, changamoto na mustakabali; Watanzania kwa miaka mingi wamekuwa na umoja na mshikamano katika nyanja mbalimbali ambapo kwa kutekeleza haya ndiyo tunapata neno Muungano. Kihistoria tokea miaka mingi iliyopita tangu dunia iumbwe, makabila na watu wa maeneo mbalimbali katika Tanganyika, wamekuwa na ushirikiano na mahusiano ya karibu. Mfano ni katika harakati za kuondoa uonevu, ukandamizaji na ubaguzi uliokuwa ukifanywa na Wakoloni Wajerumani mnamo mwaka 1905 hadi mwaka 1907.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Vita ya Minonge katika maeneo ya Ukanda wa Pwani Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Zanzibar, mikoa hii makabila yake yalishirikiana kuondoa uonevu hali iliyopelekea kutokea Vita ya Kwanza ya Dunia (1st World War 1914-1918). Hii yote ni kuonesha namna muungano ulivyokuwa na umuhimu na faida kwa jamii. Hivyo, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulianzia miaka mingi na hadi katika Mapinduzi ya Zanzibar 1964. Mchango mkubwa ulitokea Tanganyika (Tanzania Bara) na kufanikiwa kuondoa ukandamizaji uliokuwa ukifanywa na Wakoloni wa Kiarabu katika Visiwa vya Unguja na Pemba (Zanzibar).

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi na ushauri; Serikali izifanyie kazi kero zote za Muungano na kuzipatia ufumbuzi wa haraka; Sera ya kulinda viwanda vya ndani ifanye kazi pande zote za Muungano, mfano Kiwanda cha Sukari Mahonda kiruhusiwe kupata soko la sukari na bidhaa zake upande wa Tanzania Bara. Magari yaliyosajiliwa Zanzibar yaruhusiwe kutumika Tanzania Bara bila vikwazo vyovyote; kero na changamoto zinazofanyiwa kazi, taarifa zake ziwekwe wazi na isiwe siri; gawio la Pato la Taifa, deni la TANESCO, suala la FIFA, Exclusive Zone katika Bahari Kuu yafanyiwe kazi na yaishe; suala la mafuta ya gesi, zote hizi ni sekta ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi na kupata ufumbuzi. Mfumo wa Serikali tatu (Serikali ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Shirikisho ndio ufumbuzi wa kudumu).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ni neno lenye maana pana sana ambalo bado Watanzania wengi hawajalielewa maana yake na bahati mbaya bado Serikali haijatoa elimu ya kutosha kwa kutumia vyombo vya habari, vipeperushi na Taasisi zake katika jamii ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira katika Tanzania yanaingiliana sana na shughuli za uzalishaji mali (kutafuta riziki) kwa wananchi wake kama vile kilimo, uvuvi, ufugaji na shughuli za viwandani. Sheria nyingi na Kanuni zinatungwa bila kuwashirikisha wananchi ili wazielewe na kuzifanyia kazi, badala yake Sheria zinatumika kuwakandamiza wananchi na pale wawakilishi wao tunapotetea (Wabunge, Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa) tunajibiwa ignorance of laws is not a defence na inaonekana Serikali inatumia makosa yanayofanywa na wananchi kujipatia faini (fedha) na kuwa chanzo cha mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji, wakulima na wawindaji wamekuwa wahanga wakubwa katika suala zima la mazingira, hivyo Serikali katika hili ifanye kazi ya ziada kwa kutoa elimu ya kutosha. Sheria ya kuacha mita 60 ya vyanzo vya maji katika shughuli za uzalishaji mali ni mpya, iwekwe vizuri na itolewe elimu ya kutosha ili kuondoa mkanganyiko uliopo hususan pale ambapo sheria imekuta mwananchi ameshaanza kufanya kazi (kabla Sheria kuanzishwa), Serikali imfidie kwa eneo litakalotwaliwa na sheria hii katika ngazi za Serikali za Vijiji, Serikali za Mitaa, Halmashauri za Manispaa na Halmashauri za Majiji kwa thamani ya fedha katika soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira inatengewa fedha ndogo sana na mfano katika bajeti ya 2018/2019, bajeti iliyotengwa hadi mwaka wa fedha unaoishia ni shilingi bilioni 1.7 tu ndiyo iliyopokelewa hali inayoonesha Serikali haitilii maanani suala la Mazingira.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia kukutana katika kikao chetu hiki tukaweza kuzungumzia masuala mbalimbali ya nchi yetu. Sitaacha kuwakumbuka na kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko katika kupitisha bajeti ya Wizara ya Sheria na Katiba. Kwanza nianze kwa masikitiko kidogo kwa sababu sheria nyingi Tanzania bado ziko katika utaratibu ule ule wa kikoloni labda niseme kwa sababu zinaandikwa katika lugha ambayo kwa Watanzania siyo lugha mama kwao. Matokeo yake wengi hawaelewi na wanapata kigugumizi na wakati mwingine wanafanya makosa kwa sababu sheria hawazitambui na hawazifahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kutoa ushauri kwa Serikali, sheria zetu ziandikwe katika lugha zote mbili iwe lugha ya Kingereza lakini pia katika lugha ya Kiswahili ambayo our mother tongue.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu nimeshuhudia kwa sababu mara nyingi…

MWENYEKITI: Eeh, umesemaje? Hebu rudia tena. (Kicheko)

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi nimeshuhudia sheria zetu hizi kutokana na kuandikwa Kingereza matokeo yake wengine wanakuwa hawazifahamu. Kwa hiyo, niseme tu kwamba kama tunavyotayarisha vipeperushi mbalimbali hasa kwa wenzetu wa vijijini au kuzifanya ziende katika makala mbalimbali za magazeti kuwe na kurasa ambazo zinatafsiriwa sheria mbalimbali ili wananchi waweze kusisoma na kuzielewa. Kwa sababu lugha inayozungumzwa katika Mahakama zetu unakuta wananchi ama washtakiwa au washitaki wengine hawaelewi na mwingine anakuwa hana Wakili wa kumuwakilisha katika kesi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulipitisha sheria hapa kuwapatia Watanzania usaidizi wa kisheria kwa maana kuwapata Mawakili wa Serikali. Labda Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze ni kesi ngapi Watanzania wamepatiwa hawa Mawakili wa Serikali kuwasaidia kuwatetea katika kesi hizo? Kwa sababu mpaka leo bado kuna tatizo kubwa la uwakili na wananchi wetu asilimia kubwa hawana uwezo gharama za uwakili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua kesi ni gharama na Mawakili wana gharama kubwa. Labda niipongeze Serikali kwa ile azma nzuri ya kutoa usaidizi wa kisheria kwa wananchi lakini mpaka leo hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kwamba wananchi kadhaa kesi zao zimesimamiwa na Mawakili wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri na kuweka msisitizo kwamba Serikali itumie fedha na iongeze bajeti kuhakikisha sheria zinatafsiriwa katika lugha ya Kiswahili. Pia hizo tafsiri ziwe katika vipeperushi au majarida mbalimbali ili ziende mpaka kwa wananchi. Kwa sababu wakati mwingine mtu hana usaidizi lakini amefanya kosa na utetezi hauwezi na katika sheria tunaambiwa ignorance of law is not a defense, hii ndiyo kubwa inayofanyika lakini watu wanaendelea kufungwa, kuwekwa mahabusu na wanaendelea kufanya makosa kwa sababu hawaelewi tafsiri ya kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna sehemu imesemwa hapa kwamba Tanzania tumeridhia Mkataba wa Afrika kuhusu suala la demokrasia lakini leo ni mwaka wa sita sisi bado hatujaweka saini. Naomba Waziri atakapokuja hapa aeleze ni kwa sababu zipi mpaka leo sisi hatujasaini lakini tulishiriki katika kuridhia mkataba huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu hiki kuna kipengele kinasema kwamba hivi sasa miaka sita imepita tangu Tanzania ishiriki na kupitisha Azimio kuhusu masuala ya demokrasia, chaguzi na utawala bora lililopitishwa na Umoja wa Afrika ambapo Tanzania ni mwanachama. Mkataba huo ulipitishwa na Umoja wa Afrika wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Serikali za Umoja wa Afrika 30 Januari, 2007. Lengo la mkataba huu ni kuzitaka nchi wanachama kuzingatia na kutekeleza utawala bora utawala wa sheria na haki za binadamu kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 3 na 4 ya mkataba huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu hili suala linatutia aibu kama Tanzania. Tanzania kama tunavyosema sisi ni kisiwa cha amani na Tanzania katika mambo mengi ndiyo mfano wa kuigwa vipi tuna kigugumizi katika suala hili la kutia saini huu Mkataba wa Demokrasia, Utawala Bora pamoja na Haki za Binadamu? Hili ni jambo kubwa na zito katika Afrika na dunia kwa ujumla, sasa Waziri atuleleze kwa nini mpaka leo miaka sita imepita bado hatujasaini mkataba huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala hili la kupiga marufuku mikutano na maandamano. Jambo hili lipo katika sheria ya nchi sasa inakuwaje tunapiga marufuku mikutano, maandamano hali ya kuwa ni jambo ambalo limo ndani ya sharia? Inakuwaje wananchi wakose haki yao ya kikatiba kwa sababu Katiba ndiyo sheria mama na ndiyo iliyotoa ruhusa hiyo kwa nini tuzuie mikutano ya hadhara, maandamano hali ya kuwa tunaona katika nchi za wenzetu kupitia maandamano na mikutano hata inapokuwa wananchi hawamkubali Rais anajiondoa. Kwa mfano, Rais wa Algeria, wananchi, Jeshi na wanafunzi wamefanya maandamano na hapakuwa na umwagaji damu kumetokea mapinduzi baridi Rais yule ameondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika baadhi ya nchi wananchi wanapokuwa hawaridhishwi basi wanapoandamana wanakuwa wamepeleka ujumbe wa jambo fulani. Kwa mfano, baadhi ya nchi bei ya mkate inapoongezeka au fedha yao kupungua thamani au mfumuko wa bei kuzidi wanafanya maandamano ya amani ambapo hauliwi hata sisimizi na matokeo yake Serikali inakubali na inafanya marekebisho na mambo yanakwenda vizuri. Kwa hiyo, mimi niseme suala hili la kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano tujitanzame upya ili tuweze kutoa ruhusa na ukiangalia tunaelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Mimi napenda Tanzania ionekane ni mfano wa kuigwa katika mambo mengi hasa haya ya demokrasia pamoja na utunzaji wa haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni dhamana. Katika Bunge lililopita niliwahi kuzungumza hapa nikaiomba Serikali, tena nilimwomba Mheshimiwa Rais kupitia kwa huyu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kumtaka kwamba wale Wabunge wenzetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika kumi tayari?

MWENYEKITI: Ndiyo.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Naona umeweka tano.

MWENYEKITI: Hapana, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Namnukuu Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela; “Education is the most powerful weapon which we can use to change our World”

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno haya yanaonesha jinsi gani elimu ilivyo na umuhimu katika maisha ya mwanadamu ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la uhaba wa madarasa; kufuatia kuongezeka kwa wanafunzi wa shule za msingi kuanzia STD I – STD VII, ufaulu umeongezeka (2019 – 17% primary schools) wanafunzi wameongezeka lakini bajeti inayotengwa haiongezeki. Hali hii imepelekea wanafunzi wa Kidato cha I (Form one) kukosa madarasa ya kutosha na kupelekea wanafunzi wengine kuchelewa kujiunga na masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kupeleka fedha za ujenzi wa madarasa, bado fedha zinahitajika, bajeti iongezwe na Serikali ihakikishe kila mwanafunzi aliyefaulu anaingia darasani, kwa kujenga madarasa ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga ilibahatika wakati wa Ukoloni wa Ujerumani ilijengwa Shule ya kwanza Afrika Mashariki na Kati, shule iliyozalisha pia Walimu waliopelekwa katika nchi jirani, hali iliyopelekea Tanzania kuwa na historia iiyotukuka katika maendeleo ya elimu. Kwa sasa Halmashauri ya Jiji la Tanga inazo shule za Sekondari, High Schools, vyuo lakini hatuna Chuo Kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru Wizara kutupatia Tsh. 1.8 bilioni kwa ukarabati wa Tanga Technical School, lakini Tanga hakuna Chuo Kikuu cha Serikali. Naomba Serikali yangu iwaeleze wananchi ni lini itajenga Chuo Kikuu Tanga? Kama itakuwa tatizo ni fedha, mwaka jana niliomba kuipandisha Daraja Galanos High School kwa kuwa inazo “facilities” zote na nyongeza kidogo kuwa Chuo Kikuu. Je, kutoka mwaka jana 2018 hadi leo, Wizara inasemaje kuhusu kuipandisha Galanos High School?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo ambalo Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu (3) Benjamini Mkapa atakumbukwa ni uanzishaji wa Capitation Grants, wa Tsh 12,000 – 10000 kwa kila mwanafunzi kwa mwezi. Kwa sasa kila muda unavyokwenda Capitation Grants inapungua. Naiomba Serikali ilieleze Bunge tatizo ni nini?

Kwa masikitiko makubwa Tanzania imepata taswira mbaya katika medani za elimu katika Afrika na Duniani kwa ujumla kufuatia matukio yafuatayo:-

(a) Mwalimu Mkoani Kagera kumpiga hadi kumuua mwanafunzi wa darasa la tatu bila hatia;

(b) Mwanafunzi wa kidato cha kwanza wiki mbili baada ya mauaji ya mwanafunzi STD III alipigwa hadi kupoteza fahamu;

(c) Mwalimu Mkoani Mbeya amemfunga mwanafunzi miguu juu kichwa chini, amempiga hadi amemvunja mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa matokeo hayo hapo juu ni kielelezo kuwa tunao Walimu ambao hawana sifa ya ualimu bali walitakiwa wawe Field Force Unit (FFU). Naiomba Serikali iliambie Bunge, ina mkakati gani wa kusafisha sekta ya ualimu kwa kuwaondoa Walimu makatili? Zamani wanafunzi wakati tukisoma tulipenda tutakapomaliza shule tutakuwa kama Walimu wetu waliokuwa wakitufundisha, lakini siku hizi imekuwa kinyume, wanafunzi hawapendi kuwa Walimu kwa sababu, Walimu siku hizi wamekuwa wajasiriamali, mwalimu anaenda kazini (shule) amebeba deli la ice cream, chupa ya ladu, kashata, chipsi za mihogo, ubuyu na binjra. Yote hiyo Mwalimu anataka kuongeza kipato kwa kuwa mishahara midogo, wanasomesha watoto, wanahitaji kodi ya nyumba, bili ya maji na umeme. Hivyo naitaka Serikali iongeze mishahara ya Walimu na itamke ni lini itaanza kuongeza mishahara na lini itamaliza kulipa madeni ya Walimu?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Labda nami niungane na wenzangu katika kutoa pole kwa Watanzania wote baada ya kuondokewa na mzee wetu, Reginald Mengi. Namkumbuka tu Tanga, baada kuanzishwa kwa ITV alituletea television kubwa sana pale katika uwanja wa Tangamano ikawa wananchi wa Tanga wanapitia taarifa na burudani mbalimbali kupitia katika television hiyo. Mwenyenzi Mungu amweke mahali panapostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba katika taarifa ya Kamati iliyotolewa, kuna upungufu ulielezwa kwamba Kamati ilivyotembelea miradi, miradi mingi ilikuwa haijapelekewa fedha za kutosha. Vile vile hata ukingalia katika bajeti, nayo inakuwa imetekelezwa kwa 16% badala ya 100% na 84% bado haikuweza kutimizwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwape pongezi Mheshimwia Waziri na Naibu wake wa kufanya kazi katika mazingira magumu. Pamoja na hivyo, naitaka Serikali nayo sasa iangalie kwamba Wizara ya Afya ndiyo kitengo au Wizara muhimu katika maisha binadamu, kwa sababu binadamu bila kuwa na afya bora hapawezi kukawa na uzalishaji mali, hapawezi pakawa na Jeshi ambalo lina ngumu kamili, lakini pia sekta mbalimbali zinaweza kufeli kama watumishi watakuwa hawana afya bora. Kwa hiyo, pamoja na mazingira magumu, lakini endeleeni kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwamba wakati mwingine lazima Serikali yetu nayo inapopanga bajeti, basi ihakikishe kwamba bajeti inapelekwa. Kuna jambo lingine gumu ambalo naliona katika bajeti zetu, mafungu makubwa ya fedha tunategemea katika fedha za wahisani. Wakati mwingine wahisani nao ama hawatuletei fedha kwa wakati ama wanatoa visingizo na matokeo yake fedha hizo zinakuwa haziji na matokeo yake mambo hayakamili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niende katika hotuba hii ya Kambi Rasmi ya Upinzani, kuna eneo limesema kwamba kwa mwaka wanakufa akina mama wajawazito 11,000,000, sawa na akina mama 30 kila siku kutokana na vifo vya uzazi. Kwa nchi kama Tanzania ambapo kuna Madaktari wasomi wakubwa, ina rasilimali nyingi; kushindwa kulishughulikia suala hili kwa kweli naona ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika akili za kawaida, kila siku kuna akina mama 30 wanapoteza maisha kutokana na vifo vinavyotokana na uzazi. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze, wana mkakati gani wa kupunguza vifo hifo hivi? Kwa sababu Watanzania 30 kupoteza maisha kutokana na vifo vya uzazi, hii idadi ya ni kubwa sana. Kwa mwaka watu 11,000,000. Hili siyo jambo dogo. Yakipangwa majeneza hapa 30 kwa siku au kwa mwaka kwamba ni watu 11,000,000 ni idadi kubwa sana. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze wana mpango gani kuhakikisha jambo hili linakwisha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine limezungumzwa hapa kwamba katika Mkoa wa Tabora kuna Wakunga wanaozalisha kwa kutumia mifuko ya rambo au mifuko ya plastiki. Serikali imeshapiga marufuku mifuko ya Rambo, sijui Wakunga huko Tabora watatumia vitu gani katika kuzalisha akina mama? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais alipokwenda Malawi, amepata taarifa moja ilinifariji, kwamba Malawi wameweza kuanza kutoa chanjo ya Malaria. Malawi ndiyo nchi ya kwanza Barani Afrika kuanza kutoa chanjo ya Malaria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind-up naomba atueleze, nasi Tanzania tuna mpango gani wa kutoa chanjo ya Malaria ili nasi tuwe nchi ya pili Barani Afrika kwa kutoa chanjo ya Malaria? Tukumbuke kwamba kila dakika tano, Tanzania Malaria inaua Mtanzania mmoja. Sasa hili nalo naomba tuje tuelezwe, tuna mpango gani na sisi kuwa nchi ya pili kutoa chanjo ya Malaria?

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nirudi kwenye…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujaalia afya njema ya kukutana katika Bunge letu hili na kuzungumza masuala ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda baada ya kusema hapo kwanza nitoe shukrani kwa Wizara yetu ya Ujenzi kwa taarifa ambazo walinipa kwenye Bandari yetu ya Tanga, kwamba kuna fedha zilitengwa na zimekwishafika kwa ajili ya kuongeza kina cha maji ya Bandari yetu ili Meli ziweze kufunga a long side nishukuru sana kwa hili takribani shilingi bilioni 1.8 kama sikosei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo jingine nipende kuzungumzia Bandari yetu ya Tanga; Bandari yetu ya Tanga ni Bandari ya muda mrefu na ya kihistoria lakini bado inafanyakazi chini ya kiwango. Sasa niiombe na kuishauri Serikali, Bandari ile pamoja na kuongeza kina, pamoja na pia taarifa nyingine kwamba baada ya ile green ya forty foot container kupata mpya lakini bado inahitaji ifanyekazi kama ilivyokuwa zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanini nasema hivyo? Zamani Bandari ya Tanga ilikuwa ikisafirisha mizigo mingi sana ya Kahawa, ya Pamba, ya Katani, Alizeti na vitu vingine sasa, sasa hivi Bandari ile imekuwa inafanyakazi chini ya kiwango. Niseme hata alipokuja Mheshimiwa Rais katika kuweka jiwe la msingi la uzinduzi wa bomba la mafuta nilimuomba basi angalau bandari zetu hizi zifanye kazi kwa kiwango angalau japo kukaribiana, kwa sababu gani nasema hivyo? Kama unakwenda Zanzibar ama kwa ndege, ama kwa meli utakuta kuna msururu wa meli zimekaa zinasubiri zamu ya kuingia Bandarini kupakua mizigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme tu, kanini basi tusifanye category hizi za mizigo kwa mfano, Bandari yetu ya Tanga ichukue mizigo yetu ya Tanga, ichukue mizigo ya Moshi, Arusha, Manyara lakini hata Musoma na Bukoba na Nchi kama Rwanda na Uganda angalau ingekuwa inafanyakazi hivyo ingekuwa imerudia kufanya kazi katika kiwango chake kama ilivyokuwa zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Bandari nyingine pia labda ya Mtwara tuseme ingechukua nayo mizigo labda ya Mtwara yenyewe, Mbeya, Sumbawanga, Katavi huko, Malawi na kwingineko ingekuwa Bandari inafanyakazi. Sasa tumekuwa kama wafanyabiashara ya mayai ambao mayai yote tumeyatia katika chombo kimoja ukijikwaa tu ni kwamba umeshapoteza mtaji. Nashauri Serikali ifanye categories za mizigo; mizigo iwe kwa Kanda fulani, Bandari fulani itumike, Kanda fulani, Bandari fulani itumike lakini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo pia, zipo Bandari Bubu hatuwezi kukataa na hatuwezi kuepuka Bandari Bubu kwa sababu wananchi wetu ama wawe wavuvi au wasafirishaji wa vyombo vidogo vidogo wanazitumia. Mfano, Bandari ya Kipumbwi, mfano Bandari ya Kigombe hizi nasema zingeboreshwa zikajengwa kama ilivyojengwa Bandari ya Pangani pakajengwa Gati, pakawa pale na majengo kwa ajili ya kuchukua ushuru wa forodha, wakawepo wafanyakazi wa TRA tukakusanya mapato. Lakini kuendelea tu kuzitamka tu Bandari Bubu, Bandari Bubu hatuwezi kuziepuka. Ni vyema tungeweka Maafisa wa forodha pale wakawa wanapokea bidhaa zinazotoka Zanzibar kwa sababu hizo ndiyo ambazo mara nyingi tumekuwa tukizilalamikia kwamba zinapitishwa katika Bandari Bubu na kuikosesha Serikali mapato. Kwa hiyo, hilo nilikuwa nashauri Bandari ya Kipumbwi, Bandari ya Kigombe zifanyekazi na pia zitaongeza ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo jingine nipende kuizungumzia barabara ya Pangani; barabara ya hii ni barabara ya kihistoria. Iliwekewa ahadi na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Nyerere, Rais wa Awamu ya Pili, Rais Mwinyi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na sasa imeingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano. Kwa maneno ambayo yamekuwa yakisemwa mara kwa mara kwamba hii Serikali ya Awamu ya Tano ni sikivu na tumeona kwenye Bajeti fedha nyingi zimepelekwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namuomba Mheshimiwa Magufuli autafune ule mfupa uliomshinda Fisi, kwanini? Barabara ya Pangani kama itajengwa itakuwa ni kichocheo kwanza cha kiuchumi kwa sababu gani? Wanaotoka nchi jirani kama Kenya kupitia Mombasa na sisi watu wa Tanga tutaokoa muda wa kufika Dar es Salaam, kama tunavyoijua Dar es salaam ni Jiji la kibiashara na biashara nyingi zinafanywa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa leo kusikia kupitia Bunge hili, pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri tumekwishanong’ona kidogo kaniambia fedha zimekwishapatikana, Mkandarasi amekwishapatikana, hiyo feasibility study ilikwishafanyika. Basi Serikali itoe nneo, itoe tamko ili ionekane kwamba lini barabara ya Pangani inaanza kujengwa rasmi. Naamini tamko litakalotoka hapa leo, Mheshimiwa Waziri utaona watu wa Tanga watakavyoshangilia, watakavyokuombea dua na vilevile pia watakavyonipongeza Mbunge wao ambae niliyekuwa naizungumzia mara kwa mara. Kwa hiyo, hapa nategemea kupata tamko la Serikali kwamba rasmi lini barabara itajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, hata wale ambao walizuiwa ama kuendeleza mashamba yao au kuendeleza nyumba zao ambao wako pembezoni mwa barabara wamekuwa wakihoji kuhusu fidia pia nilitaka leo Serikali itoe tamko lini watu wale wataanza kulipwa fidia zao kwa sababu wamekubali kutokuendeleza mashamba na majengo kwamba wanataka barabara ijengwe ili tuweze kusogeza maendeleo ya wananchi. Kwa mfano, barabara ya Pangani kama itajengwa kuna mazao ya nazi, kuna mazao ya muhogo maeneo ya Kirare lakini kuna mazao mengine pia kama ya Matikitimaji n.k yataweza kusafirishwa kwa urahisi kupelekwa katika soko la Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine, barabara…

MWENYEKITI: Ahsante muda wako umekwisha.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: …naomba nazo pia changarawe zifanyiwekazi kwa sababu sikuona humu katika kitabu. Naomba mtakapokuja Mawaziri basi mtuelezee barabara za changarawe nazo zinajengwa lini kama vile kutoka Mabokweni kwenda hadi Daluni, Maramba na Korogwe. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na pia kuwatakia Waislamu wote Tanzania na duniani kwa ujumla, Mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Pangani ni miongoni mwa barabara za kimkakati na ni miongoni mwa barabara inayounganisha Mikoa na Wilaya. Pangani road inaanza Mkoa wa Tanga na kupitia Wilaya za Muheza, Pangani na Chalinze Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam. Pia barabara hii inaunganisha nchi za Afrika Mashariki kwa barabara kuu itokayo Mombasa - Kenya kupitia Tanzania na hadi Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.

Mheshimiwa Spika, barabara hii imewekewa ahadi na Marais wanne ambao sasa ni wastaafu ambao Julius K. Nyerere, Mzee Ally Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete. Pamoja na fedha kupatikana (bajeti) upumbuzi yakinifu tayari na mkandarasi ameshapatikana, naiomba Serikali itoe tamko ni lini barabara ya Pangani itaanza kujengwa rasmi?

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara kwa changarawe. Barabara zifuatazo katika kitabu cha bajeti na sijaziona, naomba zitengewe fedha:-

(i) Barabara ya Mabokweni-Maramba-Daluni-Korogwe;

(ii) Barabara ya Kirare-Mapojoni-Mkembe;

(iii) Barabara ya Amboni-Mleni-Rubawa-Pangarawe;

(iv) Barabara ya Pongwe-Marungu-Geza; na

(v) Barabara ya Fuweni-Mondura-Mwarongo.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iongeze fedha katika bajeti hii ili barabara hizi ziweze kupitikana wakati wote wa mwaka.

Mheshimiwa Spika, Bandari ya Tanga ni miongoni mwa bandari za kihistoria duniani. Kama tunavyojua, bandari ni lango kuu la biashara lakini haitumiki ipasavyo pamoja na kufanyiwa ukarabati wa shilingi bilioni 1.8 na crane ya 40Ft mpya bado kuna upungufu wa vifaa vingi.

Mheshimiwa Spika, nashauri bandari hii ipatiwe fedha za kutosha kwa ajili ya vifaa bora na vya kisasa. Serikali na Mamlaka ya TPA ifanye utaratibu wa kupanga aina za mizigo (categories) kwa kila mandarin. Bandari ya Tanga ichukue mizigo ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Musoma na Bukoba bila kusahau mizigo ya Uganda, Rwanda na Burundi. Bandari ya Mtwara (Mtwara Corridor) ichukue mizigo ya Mtwara, Mbeya, Sumbawanga, Katavi, Kigoma, Iringa bila kusahau mizigo ya Zambia, Malawi na Congo DRC. Bandari ya Dar es Salaam ni kuipa mizigo mikubwa sana. Dar es Salaam Port kwa kuifanya ishughulikie mizigo yote inayotoka nchi za nje matokeo yake meli zinasubiri muda mrefu sana na kuwa ni sababu ya baadhi ya makampuni ya meli kuikimbia Bandari ya Dar es Salaam na kushushia mizigo Mombasa port, Beira na Maputo. Hivyo, naiomba Serikali ifanye categories za mizigo na Bandari zote za Tanga, Zanzibar, Dar es Salaam na Mtwara zifanye kazi kwa faida.

Mheshimiwa Spika, Bandari Bubu ziboreshwe. Bandari Bubu Tanzania ni jambo lisiloepukika kwa kuwa Watanzania wanafanya kazi za usafirishaji kupitia maji (bahari, mito, maziwa). Bila kuathiri huduma hii kwa wananchi ni vyema Bandari Bubu zikafanyiwa tathmini na zinazokidhi vigezo zikarasimishwa (kuboreshwa) na kuwa chanzo cha mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Tanga tunazo Bandari Bubu katika maeneo ya Moa, Jasini, Monga, Tongoni, Mwarongo, Marungu (Tanga Mjini), Kigombe (Muheza), Kipumbwi na Mkwaja. Nashauri Bandari Bubu za Kigombe (Muheza) na Kipumbwi (Pangani) ziboreshwe kwa kujengewa majengo bora ya TRA, TPA kwa ajili ya kukusanya mapato ya Serikali ya forodha na kodi mbalimbali. Bandari hizi zikiboreshwa zitaongeza mapato ya Serikali na pia itaongeza ajira na kuongeza mzunguko wa fedha kwa wananchi (wafanyabiashara) wa maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, minara ya simu/mawasiliano. Moja ya vigezo vya maendeleo ni mwasiliano ya uhakika. Yapo maeneo katika Jimbo/Jiji la Tanga hakuna mawasiliano ya uhakika. Unapotaka kuongea na simu lazima upande ju ya mti, kichuguu au katika maeneo maalum hali inayopelekea wananchi kupata shida ya mawasiliano hususani katika kipindi cha dharura yoyote inapotokea au hata katika shughuli za biashara. Maeneo hayo baadhi ni Kata za Marungu, Tongoni, Mzizima, Mabokweni, Kiomoni na Maweni. Naishauri Serikali kwa kushirikiana na Makampuni ya simu (Tigo, Airtel, Zantel, TTCL na Vodacom) kuongeza minara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuwepo Bungeni leo na kuchangia Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuiomba Serikali yetu sikivu kutoa msamaha (exemption) au kuruhusu taasisi ambazo wameagiza tende kama chakula kwa kutoa msaada kwa watu masikini wenye mahitaji. Naamini ombi langu litakubaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie biashara katika Tanzania. Wafanyabiashara nchini Tanzania ni sawa na wale wanaofanya biashara katika nchi nyingine; na kazi ya biashara ni kununua na kuuza, pamoja na kulipa kodi katika idara husika, mfano TRA. Wafanyabiashara wa Tanzania wamekuwa kila mara wakilalamikia mifumo ya kodi ambayo siyo rafiki kwa wafanyabiashara wenyewe na biashara zao. Tanzania kuna utitiri wa kodi. Utitiri huu wa kodi unasababisha wafanyabiashara kujiona wanaifanyia kazi Serikali kwa kuwa katika mapato. sehemu kubwa ya mapato inabidi kulipia kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe wafanyabiashara kote duniani wanafanya biashara ili wapate faida baada ya kulipia gharama za uendeshaji kama mishahara ya wafanya kazi, gharama za umeme na maji, kodi na tozo mbalimbali (Serikali Kuu na Halmashauri), michango mbalimbali katika taasisi, fremu ya biashara ilipo biashara yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mfanyabiashara kuona hana anachopata katika biashara, anachobaki nacho anaona bora afunge biashara kwa kuandika barua ya kufunga biashara kwenda TRA ili wasiendelee kutozwa kodi.kufuatia jambo hili, mapato ya Serikali yanapungua na hatimaye wafanyabiashara wanahamia nchi jirani ambapo wanaona kuna masharti nafuu ya kufanya biashara. Mfano wafanyabiashara ya nguo, wanaona ni nafuu kufanya biashara nchini Uganda, wanaanzisha maduka ya jumla na rejareja kisha wafanyabiashara wadogo wanakwenda kufuata nguo Uganda.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni bidhaa kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara. Pamekuwepo na sintofahamu ya hali ya juu kwa bidhaa kutoka Zanzibar kwa kulipiwa kodi mara mbili. Kwa mfano, ukinunua sukari Kiwanda cha Mahonda ukija nayo Tanzania Bara unatakiwa uilipie tena kodi. Swali; je, nikinunua sukari Mtibwa Sugar, Kilombero, Kagera Sugar au Kilimanjaro TPC, kwa nini hailipiwi ushuru? Au tatizo ni kuvuka bahari?

Mheshimiwa Naibu Spika, bidhaa zinazotoka Zanzibar zinasaidia kupunguza ukali wa mfumuko wa bei na pia bei rahisi na hupunguza baadhi ya kero ya upungufu kwa baadhi ya bidhaa. Hivyo, bidhaa za Zanzibar ziwe huru. Hata sera ya kulinda viwanda vya ndani bado itafanya vizuri na haitaathirika kwa bidhaa toka Zanzibar. Ni ajabu hata redio na TV moja pia inabidi ilipiwe kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanga ulikuwa ni Mji wa viwanda tokea katika zaa za ukoloni, lakini hata katika miaka ya 1970 mwanzoni mwa uhuru hadi miaka ya 1993 ndipo mambo yalipoanza kuharibika, hususan baada ya kuanza kubinafsisha (privatization) mashirika na makampuni ya Serikali. Tanga kulikuwa na viwanda vifuatavyo: Steel Rolling Mill (chuma), Foma Detergent, Amboni Plastic, Sikh Saw Mills, Tanganyika Blanket, Mkumbara Cheapboard, TIP Soap Company, Tanga Dairy, Kiwanda cha Kamba Ngomeni, Tanzania Fertilizer Company, Tanga Nicolln (coconut oil production) na CIC Textiles.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vyote hivi vimekufa, vimeuliwa kwa kuwauzia wafanyabiashara ambao hawana uwezo wa kuviendesha. Tujiulize, viwanda hivi viliajiri Watanzania wengi mno, leo Watanzania (wafanyakazi) wako wapi? Kutofanya kazi kwa viwanda hivi ni dhahiri mzunguko wa fedha, ajira na maisha ya watu wa Tanga yameathirika sana. Nataka kujua, Serikali (Wizara) imejipangaje kufufua viwanda hivi au kuvichukua kwa wawekezaji walioshindwa kuviendeleza viwanda hivi?

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni upatikanaji wa vibali/leseni. Ni rahisi kwa ngamia kupenya kwenye tundu la sindano kuliko kuanzisha viwanda Tanzania, kwa sababu kuna vikwazo na vipingamizi na visingizo vingi unapotaka kuanzisha kiwanda Tanzania. OSHA, TBS, TFDA, NSSF, EWURA, NEMC na SUMATRA, hivi vyote ni vigingi vinavyowaudhi/kusumbua wafanyabiashara wanaotaka kuanzisha viwanda Tanzania. Nashauri, hebu viondolewe na zibaki taasisi mbili tu badala ya utitiri wote huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni biashara ya usafirishaji mabasi. Jana, tarehe 14 Mei, 2019 wasafirishaji wa mabasi na madereva wameandaa mgomo wa kutosafirisha abiria nchi nzima kupitia vyama vyao kuwa kuanzia leo, tarehe 15 Mei, 2019 hawatafanya safari kwa mabasi yao na madereva hawataendesha mabasi. Hii ni kutokana na kero ya Traffic Police kuwatoza faini zaidi ya mara tatu kwa safari moja ya Tanga – DSM, Tanga – Arusha na mikoa mingine nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu ni kwamba Serikali itambue kuwa wenzetu hawa (wasafirishaji) wanaisaidia Serikali kuwahudumia Watanzania, hivyo waondoe faini/vikwazo visivyo na ulazima.

Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya boda boda nayo ni miongoni mwa biashara zinazotoa huduma kwa Watanzania katika Sekta ya Usafirishaji. Ni moja ya sehemu ambapo imeweza kuondoa kero maeneo ya mijini na hasa vijijini. Changamoto ya biashara hii nayo inawekewa vikwazo na vikorombwezo vingi kama zilivyo biashara nyingine na kufanya mazingira ya biashara kuwa mabaya. Wamewekewa SUMATRA, TRA (mapato), Halmashauri na traffic sticker. Vyote hivi inabidi bodaboda alipie kodi na tozo. Ukiangalia kwa kina, nayo inaonekana ni usumbufu. Ingetakiwa walipe sehemu moja tu kama SUMATRA au TRA tu na kuondoa ukiritimba uliopo.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante; na mimi niungane na wenzangu kwanza kuunga mkono kuridhia nchi yetu kujiunga na itifaki hizi ambazo zilizotajwa hapa ambazo ni FAO na masuala ya umeme wa jua yaani solar power. Mimi nianze kuzungumzia kwenye suala hili la mkataba wa FAO.

Mheshimiwa Spika, wazungumzaji waliopita wamezungumza lakini ni ukweli usiofichika; ni kweli kwamba meli nyingi za nje zinavua katika bahari yetu bila sisi wenyewe kufaidika, na hili tuliligundua tulipokuwa kwenye ile Kamati Maaluma. Tukaona kwamba kuna meli zinakuja zinatumia bendera yetu lakini wanavua halafu mapato sisi hatupati kodi wala hatupati hao bycatch wanaotajwa.

Mheshimiwa Spika, labda Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa Kamati hakuifafanua vizuri hiyo bycatch. Ni samaki wale ambao wanaovuliwa hasa kuna Kanuni za kiuvuvi kwamba lazima katika ile nchi ambayo mmevua mpeleke samaki kwa ajili ya lishe kwa matumizi mbalimbali, labda kwa mfano kama kwenye watoto au shule au magereza ni Kanuni inatakiwa samaki wale washushwe hapo, na wasiuzwe.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa kama alivyose aliyekuwa Mwenyekiti wetu; wamekuwa wakishushwa hapa; kwanza hatuna bandari ya uvuvi, kwa hiyo wanaposhushwa wajanja wachache wananufaika wanawachukua wale samaki halafu wanawuza; sasa hili Wizara nalo iliangalie. Mimi, si kwa kujipendelea, lakini niseme hii bandari ya uvuvi ni vizuri ikajengwa haraka na nilikuwa napendekeza basi kama kuna sehemu ya kujengwa basi ingejengwa Tanga kwa sababu hakuna msongamano mwingi kwa masuala ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo mimi niseme tu kwamba tu kwamba tumeona kwamba katika masuala mazima ya uvuvi…

SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk ijengwe Tanga sio Kongwa? (Kicheko)

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, Kongwa hakuna bandari, kwa hiyo hili jambo ni vyema tukalifanya.

Mheshimiwa Spika, pia tumeona faida zinazopatikana kutokana na kuridhia hii mikataba tumeona kumbwa tunapata fedha za mafunzo za kujenga uwezo lakini tunapata pia misaada ya vifaa vya doria. Kwenye nchi zetu tumejifunza kwamba nchi kama Seychelles, Mauritius na kwingineko wanazo meli za doria, sisi hapa hatuna. Sasa Serikali nao baada ya kuridhia hili jambo la uvuvi lakini iangalie namna ya kupata hizi meli za doria ambazo tukijiunga tutapata misaada lakini na sisi wenyewe pia tujipange kuwa nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine hata meli za uvuvi zitatusaidia tutapata ajira kwa vijana wetu lakini na Serikali itapata fedha za mapato mengi kutokana na uvuvi wa bahari kuu. Kama alivyosema msemaji mmoja, kwamba kama tukisimamia uvuvi wa bahari Kuu vizuri tunaweza tukapata fedha nyingi kuliko kwenye dhahabu na almasi; hili sasa tulifanyie bidii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo napenda kulishauri Bunge letu na Serikali kwa ujumla; kwa wale wenzetu ambao wamefanikiwa katika masuala haya, Serikali isione tabu katika kutumia fedha, kwa mfano ama kupeleka Waheshimiwa Wabunge kwenda kujifunza ama kupeleka wataalam wetu wakajifunze. Wanafarsafa wanasema, ukitaka kula lazima uliwe, kwa hiyo na sisi tuhakikishe kwamba tunapeleka watu wetu kwa kutumia fedha zetu ili tuweze kukusanya mapato vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nikija kwenye suala hili la umeme, nimeona hapa kwenye huu mkataba wa Solar kuna mambo mengi ambayo sisi Tanzania tunaweza kusema sio kisiwa. Wenzetu wengi wamefanikiwa kutokana na umeme wa solar kwa sababu kwanza ni umeme wa bei rahisi, lakini hata bidhaa za viwandani zinashuka bei kwasababu gharama za uzalishaji zinakuwa ni ndogo na umeme wa solar ndio umeme wa bei rahisi zaidi duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, niseme tu kwamba Serikali isisite kutoa elimu hii ya manufaa ya umeme wa solar kwa sababu wengine wanatia dosari, wanasema umeme wa solar kama ni fridge la futi tano haligandishi vizuri, umeme wa solar kwenye nyumba hauna nguvu vizuri, sijui kwenye welding haufanyi vizuri; kumbe tumeona baadhi ya nchi wanautumia huu umeme katika kila jambo.

Mheshimiwa Spika, nilibahatika kwenda Denmark, tukakuta wenzetu wanautumia umeme wa solar, wametega kila maeneo wameweka panel zinachukua umeme unakwenda magerezani, viwandani, shule, na kwenye vyuo. Wenzetu wananufaika, sasa sisi sasa kwa hili naomba na sisi tusibaki nyuma, tutumie umeme wa solar kuendeleza maslahi ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, kuna mwekezaji mmoja kule Kigoma, yeye huyu anazalisha umeme wa megawatt tano; kuna sehemu inaitwa Kisenzi. Sasa TANESCO watu kama hawa iwasogeze karibu, iwe inasaidia, kwa sababu TANESCO haiwezi ikasambaza umeme nchi nzima bila kuwa na washirika. Sasa watu kama hawa nao watumike kuwasaidia maeneo ya vijijini kuwasambazia wananchi wetu umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho niseme tu, napo hata hapa katika masuala ya umeme wa solar tujitahidi sasa katika vyuo vyetu kama VETA, katika mafundi wetu hawa wanaotumia umeme huu wa TANESCO, nao wapewe elimu kwa ajili ya kujifunza kutumia umeme wa solar ili kuepusha gharama za umeme, na ili kuyafanya maisha ya wananchi wetu yawe rahisi zaidi. Ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na tukawezesha kuendelea na shughuli zetu za Bunge kama kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la TAMISEMI. Kwenye TAMISEMI kuna jambo ambalo limetokea katika jiji letu, hususan katika Halmashauri yetu ya Jiji la Tanga. Kuna Madiwani wamehama kutoka chama kimoja kwenda chama kingine. Ufahamu wangu unanielekeza kwamba moja ya sababu za kupoteza Udiwani ni ikiwa Diwani atahama kutoka chama chake alichochaguliwa nacho kwenda chama kingine; ikiwa Diwani atafungwa zaidi ya miezi sita; na labda akifanya biashara na Halmashauri bila kutangaza interest. Hizo ni baadhi ya sifa za kupoteza Udiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Madiwani wamehama chama kutoka CUF kwenda Chama cha Mapinduzi, lakini cha kushangaza sasa, sheria haifuatwi. Madiwani wale bado wanaingia katika vikao vya Madiwani, wanalipwa posho na wanalipwa pesa ya mwisho wa mwezi na wanapitisha mpaka bajeti. Sasa je, wakitokea wasamaria wema, wakaenda wakafungua kesi kwamba bajeti hiyo iliyopitishwa siyo halali, si ina maana tutawaathiri wananchi wa Tanga? Kwa sababu itabidi Halmashauri isimamishwe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu kuishauri Serikali. Hili jambo siyo mara ya kwanza. Kipindi cha nyuma kutoka mwaka 2014 kuja 2015 yupo Diwani alifanya mchezo huo huo na akatangazwa na Mkurugenzi kwamba ataendelea kuwa Diwani mpaka mwisho wa kipindi utakapofika na atapewa kiinua mgongo. Sasa najiuliza, sisi hapa kwa imani zetu tunaapishwa hapa…

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Tunaapishwa, tunashikishwa misaafu Waislamu, Wakristo wanashikishwa Biblia…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mussa, taarifa. Mheshimiwa Susan Lyimo.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mussa, taarifa hiyo?

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii nimeipokea kwa mikono miwili. Nataka niseme kwamba, narudia tena; Wabunge wote humu ndani kila mtu ana imani yake ya dini. Tunapoapishwa kushika vitabu vya Mwenyezi Mungu, halafu kumbe tunamdhihaki Mwenyezi Mungu kwamba tutaiheshimu, kuitii na kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano pamoja na sheria zake, kumbe sisi ni waongo. Tunafikiri Mwenyezi Mungu atatuchukulia hatua gani kwa mambo… (Makofi)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mwacheni amalizie. Malizia Mheshimiwa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, wale Madiwani kwa sababu wameshapoteza sifa kwa mujibu wa sheria na Katiba, basi wasihudhurie vikao vya Halmashauri na wasilipwe posho wala wasilipwe kiinua mgongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kulisema ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kuna mikoa mitano ilitangazwa isifanye uchaguzi wa Serikali za Mitaa kabisa, ukiwemo Mkoa wetu wa Tanga. Athari yake imeanza kujitokeza. Jana wakati tunaangalia taarifa ya habari huu Mkoa wa Dodoma, kipo kijiji wamemkataa Mwenyekiti, wanasema sio chaguo letu.

Sasa je, hatuoni kwamba tunakwenda kuitia hasara Serikali? Kama wananchi wamemkataa ina maana pale lazima uchaguzi urudiwe. Je, likifanyika jambo hilo nchi nzima itakuaje? (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, ikibidi uchaguzi wote wa Serikali za Mitaa urudiwe, tutende haki tuwape Watanzania haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Waitara, nusu dakika. Haya, Mheshimiwa Waitara.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

T A A R I F A

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yake mimi siipokei, lakini tu niseme kwamba majibu ya taarifa anayonipa ni kwamba waliharibu uchaguzi makusudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema ina maana kwa maelezo ya Mheshimiwa Waitara wameharibu makusudi ili wananchi waje waandike barua sasa za kuomba eti ifanyike mikutano ya hadhara halafu waangalie asilimia. Huo siyo utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashawishi Wabunge wenzangu, hasa wa Upinzani, tutakaporudi kwenye Majimbo yetu tuwahamasisheni wananchi wawakatae Wenyeviti wote waliopita bila kupingwa. Nami nawaambia, kama uchaguzi utafanyika haki bin haki, bila ya dhuluma, hakuna Mwenyekiti hata mmoja wa CCM atakayepatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tufanyeni haki, tuwaache wananchi wachague Wenyeviti wanaowataka. Sasa hivi Wenyeviti hawajulikani na wengine wameanza kulalamika kwamba tumepewa nafasi ambazo wananchi hawatutambui. Huu siyo utaratibu.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mussa, umefahamika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante labda na mimi nianze kwa kumshukuru Mwenyezi mungu kwa kutujaalia kuwa katika Bunge letu hili tukiwa na afya njema.

Mimi niseme tu kwamba pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, lakini bado hali yetu ya maisha Watanzania ni ngumu hususan ukiangalia hali ya kiuchumi kila siku inaendelea kuwa ngumu na maisha katika Tanzania kila ni afadhali ya jana na hii inatokana na nini kwanza mazingira kibiashara na kodi sio rafiki na hili nalisema kwa sababu ukiangalia tuna tofauti kubwa na wenzetu.

Sisi watanzania unaanza kulipa kodi kabla hujafanya biashara, ukitaka kufungua biashara kwanza upate TIN Number, uende TRA wakufanyie assessment, kabla ya hili halijafanyika unaanza kulipa sasa inakuwa ni taabu na hususan niende kwa akina mama, akina mama wengi ni wafanyabiashara wadogo wadogo, wajasiriliamali, wenye maduka ya nguo, wenye maduka ya vyakula, lakini wanapata tabu hali ya kuwa kwanza hata mikopo wanapochukua msharti ni magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hili naliona ni tatizo kubwa kibiashara ukinagalia baadhi ya nchi jirani kama Kenya, labda Rwanda au Uganda wenzetu wafanyabiasha wanapaanza wanapewa tax holiday ya karibu miezi sita angalau wajiimarishe waweze kujua faida wanapata vipi na aangalie mtiririko wa biashara unaendaje, lakini kwetu ni tofauti. Sasa nashauri Mheshimiwa Waziri jambo jema huigwa, hebu tuige wenzetutuwasidie wafanyabiasha wetu wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yamesemwa maneno mengi hapa na wenzangu, lakini kiukweli hata ukija kwenye mfumuko wa bei tunasema tu kwamba mfumuko wa bei umepungua kwa 3.9%. Lakini h ivi tuulizane Wabunge ni kweli mfumuko wa bei umepungua? Twende kwenye petrol na diesel tunayoitumia mwaka jana ilikuwa takribani shilingi 1800 leo shilingi 2290. Hapa mfumuko wa bei umepungua au umepanda? Wale tunoafunga tunajua mwaka jana bei ya kilo moja ya tambi ilikuwa shilingi 1800 leo shilinig 2500. Maharage yalikuwa kilo moja shilingi 1700 leo shilingi 2400, sukari ilikuwa shilingi 1900 au shilingi 2000 leo shilingi 2500. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mwananchi wa kawaida unapomwambia kwamba mfumuko wa bei umepungua hakuelewi hata tukienda kwenye shilingi yetu ta Tanzania kila kukicha thamani ya shilingi ina shuka. Tujilinganishe na Kenya, tujilinganishe na dola ya Marekani hela yetu inazidi kupungua thamani kila uchao, lakini tunasema uchumi unakuwa pato na Taifa linaongeza, lakini mwananchi wa kawaida mtaani ukimtanzama amechoka hohe hahe, hajielewi kabisa yaani haelewi somo.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi niseme tunaponzungumza mambo mengine tuwafikirieni hawa watanzania wenzetu ambao asilimia kubwa wapo vijiji na mijini na ambapo wengine hawana hata ajiri unapomwambia mtu uchumi umekuwa hata hakuelewi. Kwa hiyo, niseme hebu tuwaeleze ukweli lakini vilevile pia tuwaweke mazingira rafiki ya biashara kwa sababu wafanyabiashara wengi sasa hivi wanalalamika.

Mheshimiwa Spika, juzi hapa nilikuta Katibu wa Chama cha Biashara Mkoa wa Tanga ananiambia Mheshimiwa kutokana na ukali wa kodi nina barua 60 za wafanyabiashara ambao wanataka kufunga biashara wanaandika barua TRA ili wasidaiwe tena kodi. Sio Tanga tu, Dar es Salaam leo ukitaka frame katikati ya Jiji Kariakoo leo unapata. Kwa sababu gani watu wanashindwa kufungua biashara, mzunguko wa fedha umekuwa ni mdogo biashara zinafungwa na mwaka jana nilishauri hili Mheshimiwa Waziri alisema katika moja ya mafanikio Wizara ni kwamba wamefunga biashara takribani 300 kwa Dar es Salaam. Na nilisema kufunga biashara sio mafanikio kwa sababu kila biashara moja uliyoifunga pana wafanyakazi labda hao kwenye duka ua kampuni hao wanategemewa na watu 11 mgongoni, sasa unaposema umefunga biashara kwanza tunakosa mapato, lakini pili tunateketeza familia za Watanzania.

Kwa hiyo mimi niseme kufunga biashara kodi kubwa sio mafanikio ni matatizo watu hawana ajira Tanzania wanakimbilia kwenye biashara. Kwenye biashara napo kodi kubwa wakienda kwenye kilimo ndio hivyo, kwenye korosho kuna matatizo, sasa tunaelekea mpaka kwenye mahindi.

Mheshimiwa Spika, amezungumza hapa Waziri wa Kilimo kwamba wenye mahindi mengi wampe taarifa. Lakini watakapokuwa wemeleta hiyo taarifa kodi itapungua? Hawawezi kutoa taarifa kwa Waziri wa Kilimo kwa sababu wanajua nikisema nina tani 50 za mahindi tayari TRA watanikalia benet, hawawezi kukupa, lazima tupunguze kodi nafikiri wajua katika commerce kuna the law of demand.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mbarouk.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, kwamba the low price, high demand and the high price, low demand. Tuweke mazingira hayo angalu tuwasaidie wafanyabishara. Wafanyabiasha hasa sisi wa mikoa ya karibu na mipakani wananchi wetu wanakwenda Kenya, Uganda na Congo kuchukua bidhaa ili waweze kuuza wajipate kipato cha kila siku, ahsante. (Makofi)
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa Mwaka 2017
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Mimi kwanza nishukuru kwa kupata nafasi hii, lakini vilevile niunge mkono asilimia 100 Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, hata hivyo na mimi nina ya kwangu machache.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la dawa za kulevya ni tatizo la kimataifa, lakini moja ya changamoto zinazojitokeza katika nchi yetu, bado ipo mianya mingi ambayo inasababisha dawa za kulevya ziingizwe nchini. Kwa mfano katika viwanja vya ndege bado ni mwanya ambao unatumika mara nyingi sana kuingiza dawa za kulevya nchini mwetu. Jambo lingine pia katika viwanja vya ndege hivyo hivyo kuna mbinu mpya ambayo wasafirishaji wanaitumia sasa hivi ambayo ni ya kupitisha watu kama wagonjwa katika wheel chairs.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati mwingine inapofikia hatua hiyo hapo hapo inatolewa taarifa kwamba lift hazifanyi kazi, hapo ndio wanapopenya waingizaji wa dawa za kulevya na wakatumia mwanya huo kufanya biashara hiyo ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, mimi naishauri Serikali katika viwanja vyetu vya ndege tuwe makini sana na tuwe macho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dawa za kulevya ni biashara kubwa, kama alivyoseme mtangulizi wangu Mheshimiwa Mnadhimu Ally Saleh, kwamba hii biashara kubwa, imewahi kufanywa hata na baadhi ya Marais. Tuliona ugomvi kati ya Rais Manuel Antonio Noriega na Rais wa Marekani aliyemaliza muda wake kipindi cha nyuma bwana George Bush.

Sasa haya yalikuwa ni mapambano ya biashara, kwa hiyo na sisi tusije tukafikiri kwamba tunapozungumza biashara ya dawa za kulevya tunazungumzia kitu rahisi. Hili ni tatizo kubwa la kimataifa. Na jambo lolote ambalo linaingiza fedha binadamu anatafuta kila aina ya mbinu, kila aina ya nyenzo kuhakikisha kwamba, biashara hiyo inafanyika. Kwa hiyo, mimi nashauri tu Serikali iwe makini.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulisema ni kwamba kuna mkanganyiko sasa katika nchi zetu za Afrika Mashariki. Ukienda Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda na Southern Sudan mirungi ni kitu kinachotumika kama uraibu au kama ulevi wa kawaida, lakini Tanzania kwetu peke yake mirungi ndiyo haramu. Sasa hapa lazima Serikali tulifanyie kazi kwa kina suala hili kwa sababu leo nguvu kazi ya Taifa kwa maana ya vijana kwa mfano katika Jimbo langu la Tanga wengi wako magerezani, hawapewi dhamana. Na wakati mwingine kuna watu wanatiwa hasara ya umaskini, mimi ni tajiri nimemkabidhi dereva gari au kondakta, anapakiza bidhaa mimi sijui, lakini gari likikamatwa linataifishwa hali ya kuwa mimi sikuhusika katika biashara hiyo, kwa hiyo, hili nalo Serikali pia iliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo pia lazima tufanye utafiti wa kina. Haiwezekani katika gari dereva turnboy na conductor wote wakawa wanalijua hilo tatizo. Kwa sababu pana biashara ya magendo yawezekana akawa anajua mtu mmoja tu, kwa hiyo, wengine wanapata adhabu bila ya kuhusika katika biashara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulisema, kuna dawa kama valium. Valium ni dawa inayotumika katika kupata usingizi, lakini watumiaji wa dawa za kulevya, hasa wanapokosa dawa za kulevya wanatumia valium. Anakwenda hospitali anasema yeye anaumwa anapewa valium anaitumia kama dawa ya kulevya. Sasa Serikali napo hapa hili italishughulikia vipi suala hili la kutumia valium kama dawa za kulevya?

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni katika sober house, Serikali bado haijajikita hasa katika kuwatibu wanaotumia dawa za kulevya. Katika sober house unakuta inaanzishwa na mtu binafsi au mtu anayejisikia uchungu kuona nguvukazi ya Taifa inapotea.

Mimi naishauri Serikali ihakikishe kwamba, inazisaidia sober house kwa kuwapa vifaa kama chakula na nyenzo nyingine ambazo zinahitajika katika vituo hivi vya kuwafanya watu waache kutumia dawa za kulevya. Pamoja na hivyo pia, kuna dawa za aina nyingi ambazo zinatumika katika kuwatibu hawa watu wanaotumia dawa za kulevya, ziwe zinapatikana kiurahisi, ikibidi ziondolewe kodi, ili jamaa zetu, ndugu zetu waweze kutibiwa warudi katika hali zao za kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nalisema kuhusiana na masuala ya dawa za kulevya ni katika masuala ya wanafunzi. Mwaka jana tulipata taarifa hapa kwamba Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) pana wanafunzi wamekamatwa na misokoto ya bangi. Sasa inakuwaje wanapata fursa ya kuweza kufanya biashara ya misokoto ya bangi ndani ya Chuo Kikuu kama Dodoma?

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mimi naiomba Serikali napo iwe macho…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia kuweza kukutana na kuzungumza masuala ya nchi yetu katika Bunge letu hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwanza niseme nadhani jambo hili lilitakiwa lifanyike muda mrefu sana kutoka 1973 mpaka leo ni miaka mingi imepita. Sasa sijui labda kikwazo kilikuwa ni nini mpaka leo ndiyo tunahamia Dodoma na kupitisha sheria hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalosema, ni kweli Serikali inahamia Dodoma, lakini ukiangalia baadhi
ya vigezo vya kuwa Makao Makuu ya nchi bado havijatimia. Sasa naishauri tu Serikali kwamba ijue ina kazi kubwa na safari bado ni ndefu. Kwa mfano, wamesema waliosema, lakini mimi nasema sasa hivi hata bus stand imekuwa ni shida, ndiyo kwanza inaanza kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata uwanja wa ndege wa kisasa hatuna na tunategemea kwamba baadhi ya Mabalozi au Viongozi kutoka nchi mbalimbali, kwa kuwa Serikali itakuwa imehamia hapa, nao watatakiwa kuja hapa. Sasa kitendo cha kwamba, atue Dar es Salaam halafu afanye connection nyingine ya usafiri kuja Dodoma, huo bado ni upungufu katika uanzishwaji wa Makao Makuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, bado Dodoma ilitakiwa iwe na masoko ya kisasa, iwe vilevile na community centre, masuala ya tourism and information centre na mambo kadha wa kadha. Pamoja na hayo, bado hata huduma zile za kijamii ambazo zinahitajika kama vile maeneo ya masoko, hata hizo community centres bado hazipo. Kwa hiyo, naona ilikuwa Serikali ifanye haraka kuweka mioundombinu ambayo itasadia kurahisisha hizo huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulisema ni mpangilio wa maofisi yanavyojengwa. Moja ya sababu zilizosababisha Dar es Salaam kuwa na foleni nyingi ni huduma nyingi za Serikali kuwekwa upande mmoja. Sasa nashauri, maofisi haya ya Serikali pamoja na Wizara yasiwekwe katika eneo moja tu; yanapowekwa katika mtindo huo, ndiyo foleni zinapokuwa nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza wafanyakazi wanapotoka kwenda katika ofisi zao, lakini pia hawa wananchi wanaotaka huduma nao watakuwa wanasababisha foleni zisizokuwa na sababu. Kwa hiyo, miundombinu au ofisi zijengwe kutokana na hali nzima ya kijiografia. Pawe na usambazaji wa ofisi ili huduma zipatikane maeneo tofauti watu wasielemee upande mmoja. Hata huo usalama pia ni vizuri ikiwa hizi Ofisi za Serikali zimesambazwa kutokana na hali ya kijiogafia ya Mji wa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naliona, tumeona kwamba hata hizi huduma za Serikali au shughuli za Kiserikali ama hizi sikukuu za Kitaifa; kwa mfano, hakuna uwanja ambao umeandaliwa hapa wa shughuli za Kiserikali au Sikukuu za Kitaifa. Sasa utakuta shughuli zote zinazofanyika tunafanyia katika Uwanja wa Jamhuri, uwanja ambao original yake ni uwanja wa michezo ya mpira. Kwanza tunafanya uharibifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri basi tungekuwa na eneo maalum la uwanja ambao utakuwa unajulikana kwamba hapa panafanyika shughuli za Kiserikali na kuondoa uharibifu wa kiwanja kile ambacho ni cha michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, amezungumza msemaji aliyepita hapa, ameitaja Katiba Ibara ya (4), lakini ni kweli ukiangalia Tanzania ni Muungano wa nchi mbili. Inapokuwa nchi mbili zimeungana, basi kweli lazima haki itendeke. Ukienda katika hii preamble kwenye ukurasa wa tatu hapa, kwenye application, pana sehemu namba mbili imesema: “This Act shall apply to Mainland Tanzania as well as in Tanzania Zanzibar.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirudi kwenye kitabu cha Kamati sasa, wametajwa wadau hapa. Nafikiri ingekuwa ni vyema kweli kama kwenye hawa wadau napo angalau japo NGOs moja nayo kutoka Zanzibar ingetoa maoni, lakini hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wametajwa hapa wadau kwamba ni Chama cha Wanasheria, Tanganyika Law Society, kimetajwa Kituo cha Sheria cha Haki za Binadamu Legal and Human Right Centre, imetajwa Taasisi ya Twaweza, Kimetajwa Chuo cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa Hombolo, ametajwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, lakini ukiangalia wadau kutoka Zanzibar hawapo. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niseme pamoja na kwamba yanazungumzwa kwamba kwenye Kamati watu walijadili…

T A A R I F A . . .

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa kwa sababu, hapa imetajwa kwamba ni Tanganyika Law Society haikutajwa Tanzania. Sasa hiyo taarifa siipokei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachosema ni kwamba mambo mengine yanapofanyika hakuna haja ya kutetea jambo ambalo kila mtu anaona wazi kwamba hii ni dhuluma. Wakati mwingine tunajitia doa bila ya sababu. Kila mchangiaji anayesimama, hakuna anayepinga kuhamishiwa Makao Makuu Dodoma, lakini tusitoe mwanya wa watu wengine kulalamika kwa sababu hili jambo tunaona ni dogo, lakini linaweza kugeuka kama tone la mafuta ya taa juu ya meza. Tone moja tu la mafuta ya taa, moja tu ukiliangusha juu ya meza usiku, asubuhi unakuta meza yote imelowa. Hilo nimetoa kama ushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye suala zima la fidia. Ni kweli kwamba Makao Makuu yanahamia Dodoma, lakini wapo wananchi ambao wana mashamba, wapo ambao wana maeneo, lakini maeneo yao yanachukuliwa. Ukienda katika Sheria Na. 4 ya Mwaka 1999 inasema: “whether you have a title deed or not, so long you have been there for a long time customary law recognise you as the owner of the land.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa wananchi maeneo yanachukuliwa kwa kisingizio tu kwamba Makao Makuu inahamia Dodoma na ardhi ni mali ya Serikali. Hii sheria inakiukwa. Ametaja mzungumzaji mmoja hapa, lakini wapo watu wengine ambao maeneo yao yamechukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yupo bwana mmoja anaitwa Gilbert, kuna bwana mwingine anaitwa Msafiri na kuna dada anaitwa Anna na mwingine Mariam, hawa ni watu ambao niko nao, ni majirani zangu kidogo. Maeneo yao yanachukuliwa na Sheria Na. 5 inasema hakuna ardhi ya bure hata kama kuna mradi wa maendeleo ya Serikali, lazima Serikali mwenye eneo lake na taasisi inayotaka kuleta maendeleo watu wakubaliane kwanza. Hata hivyo, kinachotokea wananchi wetu wanadhulumiwa, wanachukuliwa maeneo hali ya kuwa wengine wanaambiwa watapelekwa Mtumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sehemu hiyo wanayochukuliwa na ukifikiria huko Mtumba anakwenda kukabidhiwa kiwanja wakati yeye ameshakuwa ni mtu mzima, hajiwezi tena, hana kipato cha kuweza kujenga makao. Kwa hiyo, nashauri kwanza hata kama unataka kupitishwa mradi wa maendeleo, wananchi wa eneo hilo walipwe fidia yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulisema ni suala zima la miundombinu. Kwa mfano, barabara, kweli barabara zinajengwa, lakini hazina vivuko vya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri basi, hata hapa kwenye Bunge, jana katika briefing lilizungumzwa na baadhi ya Wabunge wenzetu wameshapata ajali pale. Kwa nini basi halijengwi daraja kama lile la Manzese au la pale Buguruni? Isiwe Bungeni tu, hata maeneo mengine ambayo ni barabara kubwa kwa wananchi yajengwe ili kuepusha ajali na kuokoa maisha ya Watanzania.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha tukutane kwenye Bunge letu hili na kuweza kuzungumzia leo Sheria ya Vyama vya Siasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimjibu mzungumzaji aliyemaliza kuzungumza sasa kwamba akisema vyama vyetu havina demokrasia yawezakana kwao ni zaidi. Nimuulize swali moja tu, swali moja la kumuuliza hawa Wabunge waliotoka CHADEMA na CUF wakaenda CCM ni vikao vipi vilivyokaa vikawapitisha. Kwa hiyo kama ni demokrasia huko hakuna zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine linalotaka kulisema ni kwamba, nishukuru kwamba leo tunapitisha Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa na asubuhi hapa tumesikia wakitajwa, yupo Balozi wa Marekani na yupo Balozi wa Sweden ambao ni wafadhili wetu wakubwa, najua wamekuja makusudi kuja kuangalia namna gani tunavyojadili Muswada huu. Sasa nawapa tahadhari tu kwamba, sheria tunayopitisha hii yawezekana kama ni nzuri itadumu miaka hamsini ijayo, lakini kama mbaya yawezekana hata isifike 2020 mambo yakavurugika. Kwa hiyo niwambie ipo siku CCM itakuwa chama cha upinzani sheria hii itawahusu na ushahidi wa hilo, juzi Kongo nani alijua kuwa wapinzani watachukua uongozi katika nchi ya Kongo. Nani alijua kwamba Zambia itaongozwa na upinzani, nani alijua kwamba Malawi itaongozwa na upinzani, kwa maoni yangu naamini sisi wanyonge Mungu atatupa haki yetu.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nitangulie kusema kwamba, anayejua 2020 ni Mwenyezi Mungu na naamini kulinga na mambo yanavyokwenda wananchi wa Tanzania wanalisikiliza Bunge hili hata iwe usiku linaooneshwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naanza na kifungu cha 5 hiki kinachosema kwamba kutoa taarifa ya mafunzo ndani ya siku 30 na kutoa taarifa ya vifaa, wahusika, aina ya mafunzo na kadhalika kama ni yule RC ya Tabora ningesema kifungu hiki fyekelea mbali. Kwa sababu gani nasema hivi? Hiki kifungu haiwezekani sisi leo mpaka tuzungumze tukatumia maker pen, tupeleke orodha ya wanaotaka kupewa mafunzo, tupeleke Walimu wa hayo mafunzo, wakati vyama vyetu vina vyama rafiki nchi za nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano sisi CUF kuna chama ambacho kipo Ujerumani inaitwa FNF hawa tunafanya nao mafunzo mbalimbali, lakini hakuna mafunzo yoyote mabaya waliyoyatoa kwa vyama vyetu na mafunzo yanayotolewa yametusaidia kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliopita mwaka 2015. Pia kwenye nchi ya Denmark kuna chama kinaitwa Radikale Venstre nacho kimesaidia kutupa mafunzo ambayo yametuwezesha mpaka tumekuwa viongozi bora katika chama yetu cha CUF. Sasa watakapoona kwamba kuna masharti magumu kama haya, ulete orodha ya mafunzo aina na vifaa itakuwa ni sharti ambalo halina msingi wowote. Kwa hiyo kifungu hiki cha tano 5A(1) fyekelea mbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kuwa, kuvinyima vyama vya kisiasa vikosi vya ulizi ambavyo havitumii silaha hawana hata kiwembe, ni mikono tu yamezidi mafunzo ya kareti, naona kama itakuwa sio sawa na kwa nini tunatetea hivi vikundi vya ulinzi? Kwa sababu tumeona uchaguzi unapofika wenzetu wa Zanzibar kwa maana ya Unguja na Pemba kuna watu wanaitwa Janjawid wanatesa watu, wanapiga watu, wanaua watu na hata ikitolewa taarifa Polisi, wale wanalindwa badala ya kuchukuliwa hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kifo cha Mheshimiwa Mawazo kilipotokea katika uchaguzi, haya yamefanywa na vikundi ambacho ni vya baadhi ya vyama. Sasa na sisi vyama vya upinzani ni lazima tuwe na vikundi vya ulinzi. Vikundi vyetu havitumii silaha, vikundi vyetu vitatumia tu taaluma ya mikono, kwa hiyo mimi nataka vyama vyetu vya siasa viruhusiwe kuwa na vikundi vya ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la kuzuia ruzuku kwa vyama pale itakapoonekana kuna dosari; tukukumbuke vyama vinaendeshwa kwa fedha, vyama vina magari, vyama vina ofisi, vyama vinatumia maji, vyama vinatumia umeme. Sasa inapotokea imetokea kosa dogo unavinyima vyama ruzuku ni kuviua vyama vya siasa na kuitukana demokrasia.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya njema na kukutana katika Bunge letu hili.

Pili, nachukua fursa hii kuwatakia Wabunge wenzangu wote pamoja na wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga, heri ya mwaka mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme, maji ni kitu muhimu. Hata katika kitabu chetu sisi Waislam katika Quran Mwenyezi Mungu anasema Wajaalna-l-mai kullu shaiyn haiy (kwamba nimejalia maji kuwa ni uhai wa kila kitu). Maji hayana mbadala. Umeme ukikatika, unaweza ukatumia mshumaa, lakini maji kama hakuna, inakuwa ni tatizo kubwa. Kwa hiyo, naomba kwa heshima na taadhima kwamba Muswada huu uzingatie sana kuhakikisha miradi yote ya maji inakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nianze moja kwa moja kwenye Kifungu cha 30. Kifungu hiki kinapendekeza utolewaji wa leseni ya biashara katika shughuli za usambazaji maji safi na unyonyaji wa majitaka, kwamba leseni iwe miaka kumi. Nashauri tu kwamba leseni ile ingekuwa miaka 15; pili, pia pawepo na bei elekezi, kwa sababu katika Mamlaka ya Maji, kunakuwa na tofauti kubwa lakini maji yamekuwa yakipandishwa bei mara kwa mara kiasi kwamba Watanzania wanyonge wanashindwa kutumia maji kutokana na bei ghali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Wajumbe wa Bodi. Naungana na wale wanaosema kwamba tuzingatie gender katika Wajumbe wa Bodi. Kwenye Mabaraza ya Madiwani, Wakurugenzi wanakuwa ni Wajumbe, lakini hata Wajumbe wengine kwa Madiwani mara nyingi anakuwa anapelekwa Mstahiki Meya. Sasa wakati mwingine Meya anakuwa na shughuli nyingi hahudhurii na hatoi kilio cha watu wake katika hiyo Halmashauri kwenye kero ya maji. Kwa hiyo, napendekeza wawe Madiwani wa kawaida, wasiwe Mameya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kwenye kifungu cha 6 na cha 7, pana sehemu inasema, “the responsibility of Minister responsible for Local Government,” lakini pia kuna Responsibility of Regional Secretariat, Cap No.
97. Sasa majukumu ya huyu Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa na majukumu ya RAS yanafanana. Nashauri majukumu yangeachwa kwa Waziri wa Serikali za Mitaa, kwa sababu yeye ana mamlaka ya hizo kuzisimamia Halmashauri za Serikali za Mitaa ambazo nazo zinahusika na miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye kifungu cha 65 kuna neno linazungumza tu “misuse,” lakini halikutolewa uchanganuzi au ufafanuzi wa kina kwamba hiyo “misuse” ni nini? Kuna maneno kwamba wengine wanasema hata
ukikutwa unaosha gari kwa kutumia maji nje ya nyumba yako ni misuse, au labda mwingine ameweka pump ananyweshea labda bustani ya mboga mboga ni misuse. Sasa tunataka Mheshimiwa Waziri anapokuja afafanue hiyo “misuse” ni nini? Kwa sababu kuna faini zinazopigwa ambazo vilevile pia ni kubwa. Kwa mfano, mtu anapigwa faini ya shilingi milioni tano kwenye Kifungu cha sita hiki. Sasa shilingi milioni tano kwa mtu wa kawaida ni adhabu kubwa sana. Nami siamini kwamba kutoa adhabu kali itakuwa eti kuwafanya watu wawe na nidhamu ya kutumia hayo maji. Ninachoshauri, tuweke adhabu ndogo lakini elimu itolewe, ikibidi hii sheria yenyewe itafsiriwe kwa Kiswahili lakini wapelekewe hata watu wa vijijini ambao ndio watumiaji wakubwa wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye kifungu cha 66, imezungumzwa tu kwamba watumiaji wakubwa wa maji ni wananchi, lakini vilevile na faini nayo pia ni kubwa. Tuzingatie kwamba unapoweka faini ya kutoka shilingi 50,000 mpaka shilingi milioni moja, hii haitawasaidia sana wananchi wetu hali ya kuwa wao uwezo wao wa kulipa hizo faini ni mdogo lakini maji wanahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nitoe mfano. Kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, ukitupa takataka au ukichafua mazingira faini ni shilingi 50,000, haipandi. Kwa sababu watu wamekuwa na dhamira na wameeleweshwa usafi wa mazingira, mpaka leo ni zaidi ya miaka saba Halmashauri ya Manispaa ya Moshi inashinda katika zawadi ya usafi wa mazingira. Siyo kwa sababu ya faini, elimu ambayo imetolewa imekuwa inasaidia sana. Kwa hiyo, nizungumzie hilo kwamba faini tuzizingatie na hali ya wananchi wetu ambao ni masikini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali katika suala zima la maji, nimezungumza suala la bei elekezi, lakini kuna baadhi ya maeneo mpaka leo wanatumia ile average scale kwamba bili za maji zinakuwa sawasawa, lakini katika baadhi ya maeneo mengine bili za maji zinakuwa ni kubwa, wananchi wanashindwa kumudu kulipa hizo bili za maji, lakini vile vile kwenye Halmashauri hizo wananchi hawashirikishwi pale mamlaka zinapokaa na wadau katika kuchangia mawazo au kuchangia namna gani huduma za maji ziweze kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wajumbe wa Bodi ya Maji watakapokuwa wamepatikana, lakini washirikishwe pia na wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda jambo lingine ninalotaka kulizungumzia kwenye suala zima la maji ni suala zima la utumiaji wa wenzetu wa maji vijijini. Katika baadhi ya sheria zimetaja kwamba unapokuwa umetumia maji kinyume na utaratibu, upigwe faini. Mimi nasema ikiwa sheria haikutafsiriwa vizuri, ikiwa sheria haitambuliki na sisi Waheshimiwa Wabunge tunaipitisha hapa, ambapo inakwenda kwa wananchi wetu, lazima tujiangalie na sisi kuna kipindi tutakuwa sio Wabunge, sheria hii inaweza ikaja ikatukwaza. Ni vyema tukazingatia sheria ambazo zitakuwa ni nyepesi kwa wananchi wetu, zitakuwa zinaweza kutekelezeka, lakini zitawasaidia pia wananchi hawa kuweza kumudu matumizi ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho katika mchango wangu niombe tu pia kuwatakia salamu za mwaka mpya Wabunge wenzetu ambao wako...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)