Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Muhammed Amour Muhammed (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema mwenye kurehemu. Pia nampongeza Mheshimiwa Spika, yeye binafsi kwa kuwa makini sana kusimamia Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika meneo yafuatayo: maslahi duni ya Walimu, kubadilisha syllabus pasi kushauriana na Wizara ya Elimu Zanzibar; NECTA; kutolipatia stahiki somo la dini ya Kiislam mashuleni kuhusiana na ufaulu wa wanafunzi; shule za binafsi; mikopo ya elimu ya juu; kufuta mfumo wa GPA na kurejesha divisions; na elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na maslahi duni ya Walimu. Hapa ndipo hasa penye matatizo makubwa sana katika kada ya elimu. Walimu wanalipwa mishahara duni. Hii inapelekea sana Walimu kufanya kazi bila ya utulivu kwa sababu umasikini ni mwingi, wanashindwa hata kujikimu. Ingekuwa vyema maslahi ya Walimu yakaangaliwa upya. Mwalimu wa Tanzania amekuwa kama mshumaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubadilisha syllabus bila kushauriana na kupeana taarifa kwa wakati stahiki inasumbua sana. Wizara ya Elimu Zanzibar haishirikishwi wakati wa kubadilisha syllabus hasa kwa madarasa ya Kidato cha Kwanza hadi cha Nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie chombo cha NECTA. Naomba nipatiwe majibu, Zanzibar inashiriki vipi katika chombo hiki? Ni vyema pangejengwa Ofisi ndogo basi ya NECTA kule Zanzibar ili kuzuia kwenda Dar es Salaam kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu ambao wanachaguliwa kusimamia mitihani ya CSEE wengi wao hawana sifa na kwamba masharti yanayotakiwa hayazingatiwi. Hii hupelekea kuwepo na matatizo mengi sana wakati wa kufanya mitihani hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ubadilishaji wa mitihani (matokeo) kutoka GPA kwenda Division ni vyema ukaangaliwa tena kwa utafiti wa kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye shule binafsi. Shule ni nzuri na mimi binafsi ninakubaliana nazo sana. Ila ni vyema Serikali nayo ikazifanye shule zake ziwe na uwezo angalau kama hizi. Maabara za shule za Serikali ni vituko! Walimu wazuri wote wamepotelea katika shule za binafsi, matokeo mazuri yako ndani ya shule binafsi. Kuna nini hapo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasadikika kwamba somo la dini halipatiwi stahiki zake katika ufaulu wa kuendelea Kidato cha Tano. Naomba hapa nipatiwe jibu, ni kweli au la? Kama ni kweli, ni kwanini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu ni vipi Zanzibar inapatiwa gawio lake na kwa wakati upi? Pia dhana ya elimu bure haijaeleweka ipasavyo? Ni vyema ikaelezwa vizuri sana na ikaonekana kiutendaji, naomba kuwasilisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ni vema nikamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye rehemu. Ninakupongeza pia Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kulisimamia Bunge hili Tukufu kwa umakini mkubwa. Pia nitoe shukrani zangu za dhati kwako kwa kunipatia fursa na mimi kuchangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie hapa “kufufua viwanda” na kufanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Ingekuwa busara kama kwanza tungefanya utafiti wa kina hadi tukaelewa chanzo cha kufa viwanda vyetu hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema kwanza tukaandaa miundombinu itakayowezesha Tanzania kuwa ni nchi ya viwanda kweli. Umeme bado ni tatizo, umekuwa siyo wa uhakika unakatika hovyo hovyo, maji pia ni tatizo ni vema tungeboresha miundombinu hii kwanza.
Mheshimwia Spika, ni vyema viwanda vyetu vikaanza na sekta hii ya kilimo kwani ni rahisi kupata malighafi. Tungetumia zana za kisasa sana pamoja na mbolea hata mbegu za kisasa ili kupata tija baadaye tukipeleka kwenye viwanda vyetu. Nyanya zipo kwa wingi, miwa ya kutosha na matunda mengine. Hata mpunga kama tutalima kisasa tutavuna vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenda kwenye viwanda vya general tyre. Mimi hapa napata mashaka kidogo, sidhani kama tutaweza kumudu soko vizuri.
Bahari yetu pia ina samaki wengi wa aina tofauti, samaki hawa wanavuliwa na wageni, ni vyema viwanda pia vikaangaliwa kushindika samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema Tanzania ya viwanda tunayotaka ikaangalia mapema kuimarisha bandari zetu zote ambazo zitaweza kutuunganisha vizuri, tuweze kuuza vizuri mali zetu zitokanazo viwandani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema kabla ya kuanzisha viwanda tukaandaa mpango mkakati wa kuvilinda viwanda hivyo. Lakini pia ni vema kukawa na maelewano ya karibu sana baina ya Wizara ya Kilimo, Miundombinu, Biashara, Viwanda na Uwekazaji wakatengeneza “unit” ili wakafanyakazi kwa pamoja, kwa baadhi ya wakati ikawa ni rahisi sana njia za mawasiliano na kukamilisha kwa wepesi lile lililopangwa mashirikiano baina ya Wizara hizi yanahitajika ili tupate Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuwa hai, mzima na kunipatia nguvu ya kuweza kuchangia mada ambayo ipo hewani sasa. Pia napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Spika kwa namna ambavyo analiongoza Bunge hili kwa upendo na umahiri pia na uvumilivu mkubwa anaouonyesha ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia mambo sita yafuatayo:-

Moja, UKIMWI; Taifa letu sasa linahujumika kwa maradhi haya na wengi wao ni vijana ambao ndio manpowers ya Taifa. Naomba hapa Wizara husika iendelee kutoa elimu ndani ya nchi yetu namna unavyoambukizwa bila ya kuona haya, hali inatisha. Kwa upande mwingine ni vyema hizo dawa za ARV zikawekwa maeneo mengi zaidi tena kwa waziwazi pasi na kuficha.

Pili, malaria; nikienda kwenye malaria, haya ni maradhi bado yapo ijapokuwa yamepunguka. Jitihada za makusudi za kuyamaliza maradhi haya zinahitajika. Malaria ni maradhi ambayo huenezwa zaidi na mbu, mbu hawa kama tukiweka mikakati ya kusafisha maeneo, kupiga dawa za kuulia wadudu (insecticides) nchi nzima hasa kwenye mitaro ya maji machafu utapungua ama kwisha kabisa. Pia malaria ina kina, ni vyema tukaangalia zaidi kuwapatia watu wetu chanjo ya malaria.

Tatu, Madaktari na Wahudumu wengine wa Afya; ni vyema wakaongezewa mishahara kwani kazi ambazo wanafanya ni kubwa sana na maslahi bado ni duni kwa watumishi hawa. Nikiendelea kuchangia mada hii ni kwamba kwenye hospitali zetu na vituo vya afya bado watumishi ni haba, hawatoshi. Niombe Serikali kwa heshima zote iongeze watumishi katika sekta hii.

Nne, vituo vya afya; naomba Serikali iangalie tena upya namna ya kuboresha vituo vya afya hasa vilivyoko vijijini kwani havitoshi kulingana na mahitaji.

Tano, vifaa vya kisasa; hapa ndipo penye matatizo makubwa. Hospitali zetu hasa za Serikali hazina vifaa vya kisasa vya kutosha. Niiombe Serikali kwa heshima zote iliangalie suala hili kwa huruma sana, tunahitaji X-ray, Ultra- sound, CT Scan na vifaa vingine maana ni vichache sana.

Sita, maradhi yasiyo ya kuambukiza. Maradhi haya kama pressure, sukari yanazidi kuendelea kuwaumiza watu wetu. Kwa heshima zote niiombe Serikali/Wizara husika itoe elimu ya kutosha juu ya kujilinda na maradhi haya nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi kuchangia mada iliyopo hewani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uhaba wa muda nitaenda moja kwa moja na ajenda yangu. Awali ya yote nitapenda kuzungumzia ufaulu mbaya kabisa wa wanafunzi wa form four. Mwenzangu ameenda Chuo Kikuu moja kwa moja huko kwenye masters, mimi nitakuja hapa kwenye vijana wetu hawa wa form four.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukijigamba sana Watanzania kwamba tunafanya vizuri sijui tuko vizuri, tumepata sijui wanafunzi hamna, sana sana tuko below 30 percent ya wanafunzi wote wanaofanya mitihani. Kwa wakati huu na kwa ukubwa wa nchi hii na kwa wataalam tulionao ndani ya nchi hii, hii ni aibu, kwamba tunafanya mitihani ya Taifa wanaofaulu below 30 percent nchi nzima ni aibu, sana ni private schools ndiyo zinajikakamua kidogo, lakini hizi za kwetu hizi I mean government school hamna kitu. Ukiangalia matokeo acha shule hizi za vijijini ukiachia labda hizi za mijini kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza pengine na Zanzibar pale mjini, huko vijijini “F” zinatafunana pale. Unaweza ukafikiria labda…

T A A R I F A . . .

MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba uniachie tu niendelee nimuachie na hayo yake kwa sababu tunajua kwamba wajenga shule ni sisi Watanzania, lakini hiyo ni lugha ya kiswahili na yeye ni mswahili anafahamu hiyo lugha maana yake nini. Kwa hiyo, naomba unilindie muda wangu niendelee na kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tungeangalia hapa form four kuna tatizo gani hapa, shule zinazofanya vizuri zaidi ni za private, narejea tena hizi za kwetu bado. Kwa hiyo, kwanza tungeangalia yawezekana kuna matatizo kidogo kwa walimu wetu hawa, yawezekana there are some of the topics zinawasumbua, ni vema tungefanya research tukatumia ile Idara ya Ukaguzi shuleni, tukafanya research through countrywide, tukazungumza na walimu wetu wanaofundisha madarasa haya ya form three na form four, watasema hawa zile topics ambazo zinawasumbua zile tukatengenezea module, tukaandaa in service training kwa walimu wetu ili kuwa upgrade waweze kufundisha grade ile ya form three na form four. Kwa kufanya hivyo ninaamini kwamba hizi “F” nyingi kabisa zingepungua. Huo ulikuwa mchango wangu wa mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa pili, sayansi inakufa mashuleni, kwenye shule za sekondari hizi ukiangalia matokeo ya wanafunzi wa form four hata form six hawa wanaenda form six zaidi ya asilimia 70 wanasoma arts, hata wale wengine ambao form four walisoma sayansi. Kwa hiyo, kwa kipindi sasa hizi subject za sayansi zinaendelea kufa na zinakufa kifo kibaya. Sasa tutafute namna hapa ya kuweza kuwasaidia hawa vijana na hizi science subject. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye shule zetu hizi na ni-declare interest mimi mwenyewe ni mwalimu wa sayansi na nimefundisha zaidi ya miaka 25 katika shule hizi za Serikali, kwa hiyo, kuna matatizo tunayaelewa. Kuna uhaba mkubwa sana wa laboratory, achilia mbali hata vile vifaa vya kuviweka. Lile jengo angalau tukipata at least tube moja tuweke tunakosa hizi laboratory, sasa huwezi kufundisha sayansi without laboratory. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, saa nyingine mwalimu mwenyewe, kuna wakati mmoja alikuja mwalimu pale katika shule ananiuliza hii variable mass ndiyo ikoje, yeye ni mwalimu lakini kwa kuwa ni mwalimu mgeni na hakupata vizuri practical wakati akiwa anasoma kwa hivyo anashindwa hata baadhi ya terminology zinazotumika kule maabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali itafute namna ya kuweza kuziboresha hizi laboratory zetu ili tuihuishe sayansi. Huko tunapokwenda kwenye nchi ya viwanda, viwanda vinahitaji wasomi waliosoma sayansi baadae wapelekwe kwenye kusoma ufundi, baada ya kufaulu vizuri katika kiwango cha form four na form four six, kama hii sayansi itaendelea kulemazwa hivi sijui itakuwaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli mbaya tunayopenda sana kuitumia Watanzania kwamba kilimo kwanza, mimi siyo muumini wa kauli hii, mimi nasema elimu ni mwanzo. Juzi moja nilikuwa nasoma gazeti wenzetu Afrika ya Kusini hivi karibuni tu kama hawajarusha watarusha satellite moja kubwa sana… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ni vema nikamshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na ardhi, mwingi wa rehema. Pia nakupongeza wewe binafsi kwa jinsi ulivyokuwa makini katika kulisimamia Bunge letu na kwa umakini mkubwa sana. Ninaomba kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu ufaulu mbaya na usiofurahisha kwa wanafunzi wa kidato cha nne na cha sita. Kwa kweli asilimia ndogo ya ufaulu wa chini ya asilimia 30 siyo mzuri, ni vyema Wizara ingepanga haraka utaratibu mwingine kuhusiana kuongeza taaluma kwa walimu (in service training) kwa mada ambazo baada ya utafiti zingebainika kama zina matatizo kwa walimu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni National Examination Supervision, kumekuwa na kero zilizoambatana na masikitiko ya kwamba ni walimu gani wenye sifa za kusimamia hii mitihani? Kuna wakati walimu wa chekechea pia hawapewi fursa kusimamia mitihani ambapo ni kinyume na utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu nyongeza ya mishahara ya walimu. Idadi ya wanafunzi inaendelea kuongezeka na walimu wamekuwa wakiendelea kufundisha katika mazingira magumu sana na kipato chao kinaendelea kushuka na kuonekana walimu nchini ni watu dhaifu sana na maskini. Ni vyema bajeti ya elimu iwe ni pamoja na kuwaongezea mishahara walimu. Hili liangaliwe sana ili kuwalinda walimu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nakushukuru kunipatia fursa ya kuchangia bajeti ya Serikali ya mwaka 2019/2020. Kwanza nitoe pongezi kwa hotuba nzuri sana kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni jinsi ilivyosheheni ushauri mzuri sana kwa Serikali. Pia kabla sijaendelea na mchango wangu naomba niikumbushe Serikali ile ahadi tuliyotoa kwamba tutawapatia wana vijiji wetu milioni 50 kila kijiji katika Tanzania hii ule wakati wa kutoa ndiyo huu. Watanzania wana msemo wao wanasema, ahadi ni deni kwa muungwana na muungwana ni kitendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo nianze rasmi, kwanza nitaanza na elimu, elimu ndiyo mwanzo kuliko kila kitu na hapa nataka kuzungumzia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na ucheleweshwaji mkubwa sana wanaopatiwa vijana wetu hawa wanaoanza chuo. Wale vijana wanaomba mikopo baada ya kuomba na kupata uhakika wa kujiunga na vyuo. Wanapoomba mikopo kwenye Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nao wanaarifiwa kwamba mkopo umepata lakini inafika wakati wanaenda chuo ile mikopo bado hawajapata. Wanakaa wiki tatu, mwezi mmoja; sasa je, muda ule wote watapata wapi fedha ya kujikimu?

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hatari kwa maslahi ya hao vijana wetu, mimi niiombe Serikali kwa heshima zote ifikirie tena wale vijana once wakiripoti tu pale chuoni basi siku ya kwanza, ya pili, sana sana ya siku ya tatu basi zile akaunti zao ziseme. Ile mikopo yao wapewe ili waweze kuwa na utulivu wasome vizuri pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia vizuri sana kitabu cha bajeti lakini bajeti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano siyo sensitive kwa Zanzibar, haitaji kabisa Zanzibar. Naomba uniongeze dakika mbili, tatu labda turudi kwenye historia tuangalie kwani hii Tanzania ni nini? Na Tanzania ni akina nani hasa? Kwa kipindi kirefu hakukuwa na Taifa linaloitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni two Independent Sovereign State ndizo zilizokuja kwenye shirikisho zikaunda Tanzania United Republic of. Jamhuri ya watu wa Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Tanganyika wakaungana pamoja wakatengeneza Jamhuri ya watu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mbele ya hii Jamhuri ya watu wa Tanzania kuna Mamlaka tatu hapa separately. Kwanza Zanzibar na Tanganyika walikubali kusalimisha baadhi ya mamlaka yao wakayaweka pamoja wakasema haya ndiyo mambo tutakayoshirikiana katika Muungano, Nataka kuzungumzia haya. Pia kuna mambo mengine yakabaki Tanganyika, wao watafanya peke yao lakini still yatasimamiwa na Serikali ya Muungano, hayo ni ya kwao peke yao Tanganyika. Kwa upande wa Zanzibar wao watasimamia yale mambo yaliyokuwa si ya Muungano kwa upande wa Zanzibar yatasimamiwa na SMZ. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kuzungumza hiki kikapu cha pamoja hiki, hapa ndiyo bajeti haiku sensitive na Zanzibar. Ukienda bandarini pale Zanzibar, nianzie hapa Dar es Salaam kwanza, ukienda pale kuna maboresho mengi sana kabisa ya bandari yanafanywa, ni Union meter ile. Ni jambo jema, zuri nalipongeza kwa kweli, tulikuwa tunapendelea tuone kwamba na Zanzibar mambo kama yale yanafanywa. Ukienda uwanja wa ndege Dar es Salaam the reserve holl room, ukienda uwanja wa ndege Zanzibar umeachwa kama kwamba wenyewe hawapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wapi tunakwenda watanzania, Baba wa Taifa alisema hapa, umoja na nguvu na utengano ni udhaifu. Kwa hivyo mnatutenga, narudia kusema hapa miradi mingi sana ya kimaendeleo hata yale ya Muungano yanafanywa upande mmoja tu wa muungano na upande wa pili unaachwa kama kwamba wao siyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tu Waziri wa fedha kule Zanzibar anawasilisha bajeti yake kwenye Baraza la Wawakilishi kalitamka hili, kwamba wenzetu wametukalia pabaya kwenye uchumi, tunapotaka kuomba mikopo wanakataa kutupa loan guarantee. Juzi hapa kuna Mbunge mmoja alichangia akakuletea hii document ambayo Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Mpango alikataa kusaini na akamwambia yule mjumbe hapa, Mheshimiwa Dkt. Mpango una roho mbaya sana alimwambia hivyo. Sasa siweze kusema hivyo lakini kama utaratibu utakuwa ndiyo huu na nyingine tunayo hapa kama hiyo ya mwaka 2014. Wakati ule sijui Waziri wa Fedha alikuwa nani, naye alikataa kusaini, sasa kama trend itakuwa ndiyo hii hata ile sifa ya kuambiwa Waziri Mpango una roho mbaya itakuwa haikutoshi, labda tufikirie msamiati mwingine tukupatie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo niseme naiomba Serikali kwa heshima zote, kwa heshima zote, kwa heshima zote. Najua Mheshimia Waziri Dkt. Mpango wala huna roho mbaya ni mtu mzuri, kule Zanzibar kuna ndugu zako kule na wewe unaelewa hilo. Kwa hivyo nikuombe ukae na Waziri mwenzako wa SMZ mfikirie namna gani itapatikana mikopo ya namna kama hii mnakaa pamoja, mnazungumza ili ile mikopo Zanzibar nayo ipate. Au mtataka wale watu kule wafe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende 4.5 ambayo Zanzibar inapata kutoka Serikali ya Muungano. Wakati East Africa Currency Board inavunjika Zanzibar ilikuwa inachangia karibu asilimia 11, tukatengeneza BoT, BoT kule sisi kuna mtaji wetu Zanzibar, tukakubaliana tupewe 4.5 siyo mbaya. Kwa hiyo, wakati ule ilikuwa inatosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivi sasa demand ni kubwa sana, population inaongezeka kwa kiasi kikubwa sana kule Zanzibar nadhani na hata huku Bara viwanda vya kutengeneza watoto Alhamdulillah. Sasa watu wanaongezeka kwa kiasi kikubwa sana sana kabisa. Kwa hivyo 4.5 haitoshe kwa mahitaji hayo ya sasa ya Zanzibar. Sasa niiombe Serikali kwa heshima zote kabisa, mkae tena mjadili angalau tutoke kwenye 4.5% tuende 9% angalau Zanzibar nayo ikaweze kujitutumua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kauli ya Serikali kwamba uchumi wa Taifa umepanda kwa asilimia 7. Hapa napa pana matatizo kidogo ila sitaki kupingana na Serikali wala sitaki niishutumu vibaya Serikali kwa sababu wao ndiyo wenye mandate ya kuweka hizi data na kuzitangaza kwa watu wote nchini. Hii 7.5 tunaweza kui-transform vipi hii from the digital form kwenye paper in to our everyday life, hili swali sasa, how we can verify this? Siyo tunasema tu kwamba 7.1%, Je, tunajenga Standard Gauge? Ukiangalia uchumi katika nchi yetu sasa katika yearly practice ni vigumu mtanzania wa kawaida kukubali hili hakubali kirahisi. Mifuko kidogo imetoboka, korosho ndiyo hivyo Nchi is going a stun

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda uwekezaji umeshuka nearly 40%, uzalishaji nao mtihani mtupu, wafanyakazi na watumishi wengine Serikalini hawaongezwi mishahara. Sasa kama uchumi umepanda, wapi unasema? Kwa sababu inabidi mfanye mipango tuone maana yake ni kweli huu uchumi umepanda really practice. Kuna watu wakati fulani walikuwa wanaishi kwa milo miwili, hivi sasa hata huo mmoja kidogo ni mtihani. Sasa niombe sana sana sana kwa heshima zote, Serikali jaribuni ku-transform hii data 7.1 muilete in to our everyday life tuone kwamba ni kweli uchumi sasa umepanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nije kwenye Mfuko wa Jimbo, hapa kwa kweli kuna matatizo makubwa. Nia njema ya Serikali kutoa Mfuko wa Jimbo kwa Wabunge wote wa Majimbo Tanzania nzima is a good approach, kwa kweli naipongeza. Sasa swali langu liko hapa; mnapohakiki, mnafanya uhakiki, mnahakikisha vipi kwamba hii fedha imewakuta walengwa na wameitumia kama vile inavyotakiwa. Naheshimu uwepo wa Waziri Kiongozi wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Shams Vuai Nahodha na naheshimu uwepo wa Waziri Mkuu ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Amour Kengele ya pili imeshagonga, ahsante sana shukrani sana. Ahsante Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika mbili naomba.

NAIBU SPIKA: Dakika moja!

MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge wako sijapata Mfuko wa Jimbo wa mwaka uliopita. Sasa kama Serikali kuna watu mliwapa waje watupe, mimi bado. Ni hilo sasa, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa wazima wa afya zetu na tunaendelea na harakati zetu vizuri. Pia ninapenda nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwako wewe kwa namna unavyosimamia Bunge hili kwa umakini na umahiri mkubwa kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nichangie Wizara hii ya Afya kwa mambo yafuatayo; malaria, UKIMWI, maradhi ya figo na maradhi yasiyo ya kuambukiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba malaria yameshuka nchini kwa kiasi cha afadhali, lakini kwa namna Serikali ilivyojisahau uwezekano wa kurudi tena kwa kasi upo. Hivyo basi ni vyema Serikali ikafikiria tena namna ya kupambana na malaria. Ni vyema Watanzania wakawekwa mbali na malaria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Taifa linaelewa sana jinsi athari za UKIMWI zinavyoweza kupunguza nguvukazi ya Taifa, ni vyema Serikali ingeongeza juhudi zaidi katika kuwaelimisha watu wetu. Lakini pia hizi dawa za ARV ni vyema ikawa ni rahisi zaidi kupatikana katika kila eneo la nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa nitoe pongezi kwa Wizara kuhusiana na kadhia hii, Taifa limeweza kulipa fedha nyingi sana kwa kuwatibu watu wetu nchini. Kwa namna ya pekee, ninapenda niishauri Serikali iendelee kufunza zaidi wataalam wa fani hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee naomba niishauri Serikali kutoa taaluma ya kutosha kuhusiana na vipi Watanzania wataweza kujilinda na maradhi haya, yakiwemo pressure, sukari na kadhalika. Kwa kasi ya kutisha maradhi haya yanajitokeza kwa watu wetu na pia namna ya kuwatibu haijakuwa maridhawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala hili la vifaatiba, bado kabisa Taifa letu lina tatizo kubwa sana. Ukienda hospitali zote za rufaa utawakuta wagonjwa wengi wamepanga mistari wakiwa wanasubiri kupata huduma za x-rays, CT-scan, ultra sound na vifaa vingine. Mimi ninadhani huu sasa ndiyo wakati wa kuacha porojo na kufanya kazi kubwa ya kujenga afya zetu kwa kuvitafuta vifaa hivi na kuvieneza katika hospitali zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu usambazaji wa dawa; hapa napo pana uzembe mkubwa. Hivi inakuwaje Serikali inanunua au inatengeneza dawa kwa maslahi ya Watanzania wakati wa kuzisambaza dawa hizi eti kuna maeneo hazifiki, zinapelekwa wapi na nani? Ninaomba hapa Waziri atakapofanya majumuisho atoe majibu ya swali hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na utumishi wa Wizara, ni ukweli usiofichika kwamba Wizara hii ina uhaba mkubwa wa watumishi, yawezekana ndiyo maana utendaji wa Wizara hii unasuasua, siyo mzuri, malalamiko ni mengi, wagonjwa wanarundikana mahospitalini, watabibu ni haba. Ni vyema Serikali ikafikiria vizuri na ikaajiri vijana kwa lengo la kuziba hii mianya.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhaba wa hospitali; bado kabisa hospitali ni haba sana kulingana na ukubwa wa nchi yetu. Tanzania ya sasa inahitaji hospitali kama za Muhimbili angalau 10 katika Mikoa yote mikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenye - Enzi – Mungu, mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuchangia hapa hoja iliyopo mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ninapenda nikupongeze wewe mwenyewe kwa namna unavyosimamia Bunge hili kwa umakini mkubwa sana. Ninaomba nizungumzie mambo yafutayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mazao ya mahindi na mbaazi, msimu huu mazao haya yamepatikana kwa kiasi kikubwa, ni hawa wakulima wetu wamelima kwa ajili ya mahitaji tofauti kama kujikimu, kusomesha, kutibu watoto, kujenga na kadhalika, hivyo inakuwaje wananchi wanazuiliwa kuuza mazao yao nje ya nchi? Si jukumu lao wananchi kuhakikisha kwamba nchi ina chakula cha kutosha, huu ni wajibu wa Serikali. Hivi sasa mbaazi zinauzwa shilingi 100 hadi 150 kwa kilo moja, wapi tunakwenda? Mahindi nayo hayana soko, hayatakiwi. Ni vyema Serikali ikafikiri zaidi kuhusu suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuje kwenye zao la kahawa, ni vyema tungeongeza nguvu kwenye zao hili, tulikuwa tukipata fedha za kigeni. Ni vyema Serikali ingesimamia kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ya kuweka pembejeo na mawakala, mawakala wa pembejeo wametiwa umaskini na Serikali bado imekaa kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu korosho, mpaka sasa hatujawa na soko la uhakika la korosho. Ni vyema Serikali ingehangaika ili kuhakikisha kwamba tunapata masoko ya uhakika kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kusimamia wakulima, ni vyema Serikali ikasimamia kwa umakini mkubwa kuhusu wakulima, si waachiwe walime tu. Ni vyema wakasimamiwa ili waweze kulima na tija iwe kubwa zaidi, matumizi ya ardhi kuhusiana na kilimo bado yako chini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema Serikali ikahangaika kutafuta masoko ya kuuzia bidhaa zetu ndani na nje ya nchi yetu. Wakulima wamekuwa wanavuna mazao yao kwa wingi ila hawana pa kuyauza, yanawaozea mikononi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si vyema Serikali kubaki na maneno tu. Watu wanaumia, hawana pa kuuza mazao yao. Ni hatari, yanawaozea mikononi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru wewe binafsi kwa kunipatia nafasi ya kuchangia mada iliyopo hewani. Naomba kuchangia namna wavuvi wanavyotozwa na kudhalilishwa na Wizara ya Uvuvi nchini.

Kwanza kuchomwa kwa nyavu zao. Kumekuwa na utaratibu mbaya sana wanaofanyiwa wavuvi wetu, wanaokamatwa na nyavu za aina fulani kwa kuchomewa moto, dau lake ni moto na kila kitu moto. Hivi kweli ni haki wananchi kufanyiwa hayo katika nchi yao? Kwani hapa Tanzania hakuna Mahakama?

Mheshimiwa Spika, lingine ni leseni ya wavuvi. Kumekuwa na manyanyaso makubwa hapa kwamba ni watu wa aina ipi katika chombo cha uvuvi wanaopaswa kuwa na leseni. Ni chombo, nahodha, mabaharia au vipi? Matatizo haya huletwa hasa na JWTZ na kusababisha madhara makubwa, vipigo na mara nyingine JWTZ huwanyang’anya wavuvi samaki wao baharani eti kwa kuwa hawana leseni ilivyo sahihi. Wakati mwingine wavuvi kutoka Zanzibar hulazimishwa kukata leseni ya kutoka Zanzibar na wakifika Bara haitakiwi wakati mwingine. Usahihi ni upi?

Mheshimiwa Spika, katika mitungi ya gesi hapa napo pana matatizo. Kwa kipindi kirefu wavuvi wamekuwa wakinyang’anywa mitungi yao. Kimsingi hakuna sababu.

Wao wamenunua mitungi kwa ajili ya kuvulia na leo wananyang’anywa. Kama wametenda kosa, sheria ichukue nafasi yake, siyo kuwaonea.

Mheshimiwa Spika, lingine ni mifugo, hivi ni kweli vifaranga vile vilivyotiwa moto ilikuwa ni sahihi? Naomba Mheshimiwa Waziri atapokuja kutoa maelezo, anipatie majibu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi, mwingi wa rehema. Pia nakushukuru kwa kupata fursa hii ya kuchangia kwa maandishi hoja iliyopo mezani sasa. Napenda kuzungumzia Vitambulisho vya Uraia; pigwapigwa inayofanywa Zanzibar na Vikosi vya SMZ wakati huohuo Polisi wanawalinda wapigaji na kuwekwa ndani Mashekhe kwa kipindi kirefu bila kujali sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na vitambulisho. Kuhusu suala hili japo halijakaa sawa kabisa, bado kuna Watanzania wengi hawajapatiwa vitambulisho ilhali tayari wameshatimia umri wa miaka 18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pigapiga inayofanywa kule Zanzibar na Vikosi vya SMZ inatisha. Baya zaidi Askari Polisi ambao wao ndiyo wenye dhamana ya kulinda raia na mali zao huwa wao Polisi wanawalinda hawa wapigaji ambao ni Vikosi vya SMZ. Kama kuna makosa yoyote yanayofanywa kwa mujibu wa sheria basi watu hawa wapelekwe Mahakamani. Haya wanayoyafanya Vikosi vya SMZ hawana mamlaka ya kuyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Zanzibar limekuwa ni jambo la kawaida kupigwa, kutekwa, kupotezwa na hata kutupwa vichakani. Baya zaidi kuna mtu amepigwa nyumbani kwake usiku na Polisi na baadaye akakimbizwa hospitali na baada ya siku kama ya tatu mzee yule akafariki. Tunakwenda wapi Watanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusu Mashekhe waliowekwa ndani kwa miaka kadhaa sasa. Hivi ni upelelezi wa aina gani hadi leo ushahidi haujakamilika? Inashangaza sana. Wabakaji, wahuni, walawiti watoto, wote hawa ushahidi umethibitika lakini kwa Mashekhe ambao kimsingi hawana makosa yoyote mpaka leo bado.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote ni vyema nikamshukuru Mwenyezi Mungu wa rehema kwa kunipatia afya njema na busara ya kuweza kuchangia mada iliyopo hapa mezani. Pia, nikushukuru kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa homa ya matumbo ya kuendesha, imekuwa ni tabia ya kawaida kila baada ya miongo ya mvua hutokea maradhi ya milipuko ya matumbo. Ni vyema Serikali ingefikiria zaidi namna ya kuwalinda wananchi wetu ili kuzuia maafa haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala ya maambukizi ya UKIMWI, ni hali yenye kutisha, mazingira ya kupambana na UKIMWI hayajaridhisha kabisa, bado vijana wetu hawajakuwa na hadhari ya kutosha na maambukizi bado yanaendelea kutisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kuhusiana na maradhi yasiyo ya kuambukizwa. Kumekuwa na hadhari kubwa kuwaeleza wananchi kufanya mazoezi na timu mbalimbali zimeanzishwa ili kukidhi haya mahitaji lakini je, Serikali ina mkakati gani mahususi wa kulisimamia hili na kulipigia debe kwa wananchi wote hasa vijijini?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye medical instruments kama ct-scan, ultra sounds, x-rays tube. Hivi vyombo ni muhimu na ni bado havijaenea nchini, bado vijijini hizi zana hazijafika. Niombe sana Serikali kwa namna ya pekee ieneze hizi zana kwa haraka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu wa rehema kwa kunipa uhai na uzima na pia kuniwezesha kuchangia mada iliyopo hewani kwa lengo la kulipaisha Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nianze na Bandari ya Bagamoyo. Ni vyema Serikali ingefikiria zaidi kujenga Bandari ya Bagamoyo. Hii itasaidia kuimarisha uchumi wa maeneo hayo na pia kuongeza Pato la Taifa. Bandari ya Bagamoyo kama itajengwa, hata hii Reli ya Kati nayo ndiyo itaweza kufanya kazi vizuri, mizigo itapatikana kutoka nchi tofauti kuletwa hapa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, usajili wa simu; kwa masikitiko makubwa sana, TCRA haionekani kutoa mashirikiano mazuri na Zanzibar (SMZ). Kwa upande wa Zanzibar ZAN – ID ndiyo kila kitu, ndimo yalimo maisha ya Wazanzibari. Ni vyema basi kama ZAN – ID nayo ikatumika katika usajili wa simu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bandari ni masuala ya Muungano, kule Zanzibar bandari zake zimekuwa hovyo sana na zimeachwa kama hazina mwenyewe, je, Serikali ya Muungano ina mpango gani kuhusiana na maboresho ya bandari za Zanzibar?

Mheshimiwa Spika, wizi wa mitandaoni; kumekuwa na wizi mkubwa wa wananchi katika miamala ya fedha. Kwa mfano kama utamtumia fedha mdogo wako na kwa bahati mbaya usipate wakati wa kumuarifu, baada ya muda basi anapigiwa simu na mtu mwingine kama yeye ndiye aliyemtumia fedha na azirejeshe na namba ya kurejesha anatoa na hii inarudi kwa mwizi. Zikitakiwa namba zilizotumika ninazo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MUHAMED AMOUR MUHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ni vyema tukamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa uhai na uzima na kuniwezesha kuchangia mada iliyopo mezani ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Nianze kwa kuzungumzia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia kuhusu maeneo yaliyochukuliwa na JWTZ kutoka mikononi mwa wananchi; kwa miaka mingi sasa baadhi ya maeneo hayo wananchi hawajafidiwa, kwa mfano kule Zanzibar sehemu inayoitwa Kiongwe Jeshi limechukua eneo ambalo wananchi walikuwa wakilima na kufugia wanyama wao, lakini pia hili eneo ni mali yao. Kwa miaka mingi tunavyozungumza wananchi hawajapata fedha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali iwaonee huruma wananchi hawa kukatwa fedha katika mafao yao baada ya kustaafu. Kupitia awamu hii askari wastaafu wamekuwa wakikatwa asilimia 20, hii ni hatari, niiombe Serikali ifikirie tena hali ya kuwabakishia wastaafu hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kitengo cha Bahari, hapa napo pana mazonge makubwa, JWTZ linatumia force kubwa sana ya kutisha kupambana na wavuvi wetu ambao pia ni raia wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, suala la license haieleweki dhahiri hasa ni license ya aina gani inayotakiwa na hapa wavuvi kutoka Zanzibar wamekuwa wakisumbuliwa kwa aina ya license inayohitajika. Aidha, baadhi ya nyakati hupigwa na kuumizwa vibaya. Niiombe Serikali iliangalie hili kwa huruma sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Spika, Awali ya yote inapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutupatia uhai na uzima na kuwa tunaendelea na harakati zetu kama kawaida. Pia kwa namna ya pekee napenda kukushukuru wewe binafsi kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia mada iliyopo hewani. Katika mchango wangu naomba nizungumzie mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kupigwa nyavu moto, Wavuvi kunyang’anywa zana zao za uvuvi na kupigwa Wavuvi na JWTZ; kumekuwa na utaratibu kwa kipindi kirefu, wavuvi wetu kunyang’anywa nyavu zao na kutiwa moto. Ni vyema watu hawa wakapelekwa Mahakamani, Mahakama ikaamua kuliko kuamuliwa maamuzi ya aina kama hii.

Mheshimiwa Spika, niongee vipigo wanavyopata Wavuvi; kumekuwa na utaratibu mbaya sana wa kupiga wavuvi kwa visingizio mbalimbali. JWTZ Kitengo cha Navy kimekuwa kikipiga wavuvi, hatari sana kabisa inatisha, inaumiza lakini pia inasikitisha sana.

Mheshimiwa Spika, niombe kwa heshima zote, Serikali ione umuhimu wa kutatua hili kwani linazidi kuleta changamoto kwa wavuvi na kwa Taifa kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuchangia kuhusiana na kunyang’anya wavuvi zana zao; kumekuwa na tatizo hili kwa kipindi kirefu sana, wavuvi wetu wamekuwa wakinyang’anywa zana zao kama nyavu, mashine, mitungi ya gesi. Kwa nini baada ya kunyang’anywa vifaa hivyo hawapelekwi kwenye sheria Mahakamani, matokeo yake vifaa hivyo vinabaki kwa wale waliokamata hadi lini? Tunaweza kusema wananyang’anywa na hawapewi vifaa vyao?

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. MOHAMMED AMOUR MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye rehema zote. Pia napenda kukushukuru wewe kwa kunipatia fursa ya kutoa mchango wangu kwa njia hii ya maandishi. Napenda kuzungumzia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusajili Walimu wote, kwa njia na nia nzuri ni vyema kazi ya usajili ingefanywa kwa Kanda ili kudhibiti msongamano wa Walimu, hii itapelekea kuwadhibiti Walimu na kubaki maeneo ya kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoa leseni za kufundishia kwa Walimu, ni jambo jema ila haijafahamika kama nia hii inaonekana kama kwamba kuna lengo nyuma baya ambalo linakuja kuwabana baadhi ya Walimu. Kwa mfano, Walimu watapewa leseni bure, lakini baadaye watalipia kodi leseni hizo. Kwa hiyo baada ya kuwasaidia Walimu, badala yake Walimu wanamalizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna nyingine lesseni hii inakuja kuwakandamiza Walimu kushiriki na kutumia haki yao ya msingi ya kidemokrasia na kuingia kwenye Chama cha Siasa. Wale wote watakaopenda siasa za upinzani wadhibitiwe na kutishwa hata kunyang’anywa leseni hizo. Kwa hiyo, leseni huenda zikawa zinaleta kudhoofisha demokrasi nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Walimu tu? Kwa nini Watumishi wengine wa Serikali na wao hawapatiwi leseni isipokuwa kwa Walimu tu? Kuna namna nyingine hapa nje ya pazia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.