Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mbarouk Salim Ali (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mheshimiwa Spika, uwazi ni nyenzo muhimu ya Utawala Bora. Mtawala yeyote, ambaye utendaji wake ni wa kifichokificho, huwa anatiliwa shaka kwamba kuna jambo ambalo halistahili analofanya kwa siri na mtawala wa aina hiyo huwa haaminiki na wale walio chini yake.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya CCM imevunja kanuni muhimu ya utawala bora ambayo ni uwazi (transparency) katika uendeshaji wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa Mbunge katika Bunge la Kumi na namshukuru Mungu nimerudi tena katika Bunge hili la Kumi na Moja. Kwa miaka yote mitano ya uhai wa Bunge la Kumi suala la kukosekana kwa uwazi katika Mikataba mikubwa ya uwekezaji katika sekta za nishati, madini na uvunaji wa maliasili nyingine limeitia doa Serikali hii ya CCM kwamba pengine ina ajenda ya siri ya kuwaibia wananchi kupitia mikataba hiyo ndiyo maana mara zote haikubali kuweka mikataba hiyo wazi ili wananchi waijue.
Mheshimiwa Spika, Wabunge humu walishapendekeza kwamba mikataba yote ambayo Serikali inaingia na wawekezaji katika nchi yetu iletwe Bungeni ili ijadiliwe kwa uwazi ili kuliepusha Taifa na hasara kubwa inayotokana na wizi wa hila unaofanyika kwenye mikataba inayosainiwa kwa siri.
Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa Bunge la Kumi lilimaliza muda wake bila kutuletea Mkataba hata mmoja Bungeni. Bunge la Kumi na Moja limeanza, Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani mambo ni yale yale, hakuna uwazi katika mikataba mikubwa ya uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, binafsi napata shida kuelewa Serikali inapata wapi ujasiri wa kutumbua majipu ya watu wengine wakati kuficha mikataba ya uwekezaji nalo ni jipu tena lililoiva? Nafikiri kama Serikali iko serious kukomesha ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma ingeanza kujitumbua yenyewe kwa kushindwa kuweka wazi mikataba hiyo ambayo inasadikiwa kulinyonya Taifa na kuliacha hoi kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, nataka Serikali ijue kwamba kitendo cha kukosekana kwa uwazi katika Mikataba, kinaiondolea sifa ya utawala bora.
Mheshimiwa Spika, natambua kwamba katika utendaji wa Serikali kuna masuala fulani fulani ambayo huwa ni siri. Masuala hayo ni yale yahusuyo Menejimenti ya Rasilimali Watu ili kuhifadhi taarifa binafsi za Watumishi, lakini hakuna usiri katika masuala yahusuyo miradi au mikataba inayotekelezwa kwa kutumia fedha za umma.
Mheshimiwa Spika, unapoweka usiri katika masuala hayo, harufu ya ufisadi na ubadhirifu inaanza kusikika. Kwa hiyo, kitendo cha Serikali hii kutokuwa na uwazi, kunaifanya ikose mamlaka ya kimaadili (moral authority) ya kusema kwamba inapambana na ufisadi wakati ufisadi wenyewe umejificha kwenye mikataba hiyo ambayo Serikali inafanya kwa siri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, sheria za udhibiti katika tasnia ya uchimbaji madini. Mwezi Julai, 2015, Bunge hili lilipitisha kibabe Miswada mitatu ya sheria za udhibiti katika tasnia ya uchimbaji. Miswada hiyo ilikuwa ni ya Sheria ya Petroli, Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi ya mwaka 2015 na Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika tasnia ya uchimbaji Tanzania ya mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote wa upinzani hatukuunga mkono namna Miswada hiyo ilivyoletwa Bungeni na namna ambavyo mijadala ya Miswada hiyo ilivyokuwa ikiendeshwa. Kwanza, Miswada yote mitatu ililetwa kwa hati ya dharura na pili mijadala yake iliendeshwa kwa pamoja na uamuzi wake ulifanyika kwa pamoja kinyume kabisa na kanuni na taratibu za kibunge za utungaji wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja za Wabunge wa Upinzani kwa wakati huo na mpaka sasa ni kwamba kulikuwa na uharaka gani wa kuleta Miswada hiyo katika hati ya dharura na kuendesha mjadala wa Miswada hiyo haraka bila Wabunge kupata nafasi ya kutosha ya kupitia na kuelewa maudhui ya vifungu vya Miswada hiyo? Ni nini kilikuwa kinafichwa katika Miswada hiyo hadi kufanya mambo haraka haraka namna hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi na Wabunge wote wa Upinzani hatukuridhishwa na namna Miswada hiyo ilivyopitishwa. Hii ni kwa sababu sheria nzuri inapatikana ikiwa kuna maridhiano miongoni mwa Wabunge katika kupitisha Miswada mbalimbali ya sheria. Kwa maoni yangu, kitendo cha Serikali kutumia jeuri ya wingi wa Wabunge wa CCM kupitisha sheria mbovu kwanza ni kuudhalilisha mhimili wa Bunge lakini pia kunaiondolea Serikali sifa ya utawala bora kwa maana ya utawala wa sheria kwa kuwa sheria hizo zinakuwa mbovu na au za kulinda maslahi ya mafisadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ilivyokuwa wakati ule presha ilikuwa kubwa sana kwa sababu Serikali ya Awamu ya Nne ilikuwa inamaliza muda wake na inasemekana kuwa ilikuwa imeshaingia mikataba na makampuni makubwa ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta na kwa hiyo ilitaka kutunga sheria haraka haraka ya kuwalinda kabla haijaondoka madarakani ili isije ikaingia Serikali nyingine halafu ikatengua mikataba hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hofu kubwa ilikuwa ni uwezekano wa chama cha upinzani kushinda uchaguzi mkuu wa 2015 na kufuta mikataba yote ya kinyonyaji ambayo Serikali ya CCM iliingia na makampuni makubwa ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta. Kwa kuwa Rais John Pombe Magufuli ameonekana dhahiri kuwa hapendi ufisadi wala mikataba ya kinyonyaji inayolikosesha Taifa letu mapato, atumie madaraka yake na kuagiza iletwe Miswada mingine ya sheria ya kuifuta ile iliyopitishwa kibabe ili Waheshimiwa Wabunge wapate nafasi ya kuipitia na kuiridhia kwa maslahi ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya umeme na gesi. Baada ya ugunduzi wa gesi katika nchi yetu, wananchi walitegemea kuwa bei ya umeme na gesi kwa matumizi ya majumbani ingeshuka kwa kiasi kikubwa ambapo wananchi wengi wenye kipato cha chini wangeweza kumudu gharama ili waweze kunufaika na huduma hiyo. Bei ya mtungi wa gesi wa kilogramu 15 ni Sh. 45,000/=. Bei hii ni kubwa kwa wananchi wa kipato cha chini kiasi kwamba hawawezi kununua gesi kwa matumizi ya nyumbani na kwa maana hiyo wanaendelea kumaliza misitu yetu kwa ajili ya kutafuta nishati ya kuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali ipunguze bei ya gesi hadi kufikia angalau Sh. 20,000 kwa mtungi wa gesi wa kilogramu 15 ili wananchi wa kipato cha chini waweze kununua. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumewavutia wananchi wengi kutumia nishati mbadala na hivyo kuhifadhi misitu yetu ambayo ina maana kubwa sana katika utunzaji wa mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika kwenye umeme. Ikiwa gesi yetu inazalisha umeme, Serikali iiagize TANESCO unit moja ya umeme iuzwe Sh.50 ili Watanzania wanufaike na hii rasilimali ya gesi asili iliyogunduliwa katika nchi yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MABROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia fursa hii ya kuweza kuchangia katika hoja hii ya bajeti ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kiongozi wangu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa ziara ambazo anaendelea kuzifanya za kuimarisha chama katika visiwa vya Unguja na Pemba na Tanzania kwa ujumla. Lakini pia nimpongeze kwa hotuba yake ya tarehe tisa pale Lamada hotel Dar es Salaam kwa kweli ilikuwa hotuba nzuri sana, nampongeza sana Mwenyezi Mungu amjalie na amfanyie wepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba Inna-Lillahi Wainna-Ilayhi Rajiun na nasema hivyo kwa sababu mwelekeo wa nchi yetu kwa kweli unasikitisha sana. Unasikitisha kwa sababu inawezekana tunacheza na Mungu; binadamu hatakiwi kucheza na Mungu, tunacheza
na Mungu na kwa sababu mwanzoni katika kipindi cha kampeni tulikuwa tunaomba sana dua tunawaomba Watanzania watuombee dua na Watanzania wamefanya hivyo na viongozi wa dini wote wamefanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unapomwomba Mwenyezi Mungu akusaidie na akakusaidia, lakini badala yake ukarudi sasa ukafanya mambo ya kimaajabu ajabu ya kutesa watu, kunyanyasa watu na kudhulumu watu kwa kweli hapo Mwenyezi Mungu anakuwa hayupo. Kwa hiyo, hili
jambo la kucheza na Mungu ni baya sana na hili halitotupeleka pazuri Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana kwamba hakuna linalokwenda, hali ya uchumi ni mbaya, hakuna ajira, kila linalopangwa halienda na hapa tulifanya fanya tu kidogo kwa sababu kulikuwa na pesa za kuokota za madawati ndio ikaonekana kwamba tulijitahidi tukafanya kidogo lakini hakuna lolote ambalo linafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye issue ya Muungano; Waziri Mkuu katika hotuba yake amesifu sana vikao vinavyofanyika baina ya SMT na SMZ kuhusu kero za Muungano. Niseme tu kwamba kwa kweli tumechoka na kuona idadi ya vikao; wananchi wameona idadi ya vikao vinavyofanyika baina ya SMT na SMZ lakini hatuoni matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Muungano sio wa viongozi, sio wa Mawaziri; waasisi wa Muungano walikusudia kwamba Muungano ni wa watu wa Zanzibar na watu wa Tanganyika. Sasa inapotokea kwamba kuna vikao vinakaa lakini haijulikani linalotatuliwa wala linalozungumzwa hilo ni
tatizo na hatuwezi tukaenda hivyo kwa sababu kero zipo pale pale. Kila siku vikao 13, 16, 20 lakini huoni jambo ambalo linatatuliwa, kwa hiyo hili ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kusikitisha zaidi ni kwamba hata zile mamlaka ambazo zinahusika na zile kero ukienda wanakwambia sisi hatujui, kama wametatua, wametatua wao juu. Sasa wanasiasa tunatatua kero lakini watendaji hawajui; kwa hiyo kero zinabaki zipo pale pale. Kwa hiyo, hili kwa kweli halitendeki vizuri hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni kuhusu Msajili. Kwa kweli hatuwezi kuidhinisha pesa kwa ajili ya kwenda kufanya au kutumia mtu anavyotaka. Kama hatukupata maelezo mazuri ya Ofisi ya Waziri Mku ya pesa milioni 369 zilivyotumika kwa kweli hapa patachimbika, hatuwezi kuruhusu hiyo kitu, kwa sababu tunakaa hapa tunaidhinisha pesa kwa matumizi ambayo tunakubaliana halafu anatokea mtu tu wakati yeye mwenyewe ameshaandika barua kumpelekea Katibu Mkuu wa CUF kwamba Chama cha Wananchi CUF kwa sababu ya mgogoro tunakizuia ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa iweje tena urudi uipitishe ruzuku kwa mtu ambaye ameshafukuzwa, sio mwanachama lakini pia ruzuku hiyo hiyo ikatembea mpaka kwenye akaunti za watu binafsi, hatuwezi kufanya upumbavu wa aina hiyo. Kwa kweli hatukubali; hii ni lazima tupate
maelezo ya kutosha na vinginevyo hatuwezi kupitisha hii bajeti, lazima pachimbike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni kuhusu Mfuko wa Jimbo hususan kwa sisi Wazanzibari. Pamoja na kwamba Mfuko wa Jimbo bado pesa ni ndogo sana yaani pesa ambazo zilikuwa zinatolewa kwa idadi ya watu kidogo sana ndio zile zile mpaka leo haubadiliki; nafikiri kuna mjumbe mwenzangu aliwahi kusema hilo. Lakini tatizo kubwa la Zanzibar hizi pesa zinachelewa sana; ile Serikali yenu ya Zanzibar inazikopa pesa kwa sherehe za Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila zikitolewa Disemba wanazichelewesha mpaka Juni ndio pesa tunazipata. Tunashindwa kufanya mambo ambayo tumeahidi kufanya sasa naomba patafutwe utatuzi wa tatizo hilo, sio mara moja mara mbili wala mara tatu, kila siku pesa hizi zinachelewa.
Wenzetu huku wanatumia pesa wanamaliza sisi bado kule tunaulizia kila siku; tumechoka kuja kuulizia pesa hii. Hili jambo hebu litafutiwe ufumbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nataka nizungumzie kidogo kuhusu Bandari ya Wete. Bandari ya Wete pana kaofisi kidogo kabanda tu; hicho hicho wanatumia wavuvi na hilo hilo wanatumia wasafiri na hilo hilo wanatumia Ofisi ya Uhamiaji. Kwa kifupi ni kwamba pale pana movement kubwa sana ya wasafiri baina ya Pemba na Mombasa Kenya lakini kuna tatizo kubwa hakuna Ofisi ya Uhamiaji, forodha wala Ofisi yoyote. Kwa hivyo, inawezekana kuna upotevu mkubwa wa mapato. Namwomba Waziri Mkuu hili jambo tuliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika awamu iliyopita ilisemekana kwamba pesa za ujenzi wa Ofisi pale tayari zilishatoka kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini la kusikitisha mpaka leo hatujaona lolote ambalo limetendeka. Hili Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba tulipatie majibu sijui
limefikia wapi. Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia leo hii kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii. Niseme tuu kwamba this is a noble chance for me kwa sababu nimeomba Wizara karibu tano, lakini hii ni Wizara yangu ya mwisho ambayo niliomba na ndio mwanzo kupata leo. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Waziri pamoja na Naibu wake pamoja na watendaji wote wa Wizara, kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana. Niseme tu kwamba Wizara hii ina changamoto nyingi sana na ni Wizara ambayo ni ngumu sana kwa sababu ardhi ni rasilimali ya Watanzania wote na kila mtu anategemea ardhi kufanya shughuli zake. Sasa kama hatukupata watu, watendaji kama Waziri na Naibu waliopo hivi sasa, basi kwa kweli hayo malengo ambayo tunategemea kuyafikia tunaweza tusiyafikie kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata mashaka makubwa sana, kwamba ule uchumi ambao malengo ya Serikali ya awamu hii tumekusudia kufikia, uchumi wa kati na uchumi wa viwanda, huenda hatutoufikia kutokana na matatizo ya ardhi. Matatizo ya ardhi bado ni makubwa mno na Serikali inashindwa kwa kweli Serikali inashindwa kutatua migogoro mingi ya ardhi ambayo ipo. Ukilinganisha labda Mheshimiwa Waziri atatuambia; hii migogoro kwa sisi watu wa nje tunavyoona ni kwamba badala ya kupungua, inazidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna migogoro mingi kati ya wakulima na wafugaji; kuna migogoro mingi kati ya wafugaji na watu wa hifadhi; kuna migogoro mingi hata katika taasisi za Serikali. Sasa, sitegemei au hatutegemei kwamba huko ambako tumelenga kufikia tunaweza tukafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni kitu kimoja, kwamba kama ardhi ni tegemeo la watu wote nina wasiwasi kwamba kunakosekana coordination, coordination ya Taasisi za Serikali hakuna, kwamba kila taasisi inawania kipande hicho hicho cha ardhi lakini hakuna mtu ambaye ana-coordinate matumizi hayo ya ardhi. Sasa hili ni tatizo na inawezekana hili ndilo jambo ambalo linatusababishia migogoro mingi katika matumizi yetu ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa tunafuata utaratibu mzuri wa matumizi ya ardhi, kuna mbinu nyingi nyuma ambazo zimeweza kutumika/kuanzishwa ambazo zingeweza kutusaidia katika utatuzi wa migogoro ya ardhi. Kwa mfano, kuna mambo ya mbinu hizi za agro-forestry ambazo ni matumizi bora ya ardhi, tuliianzisha lakini utekelezaji wake unaonekana kama ni wa kusuasua. Pia kuna conservation agriculture ambacho ni kilimo kinachotumia ardhi vizuri, kinaonekana kwamba kimeanzishwa lakini uendelezaji wake ni wa kusuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mambo kama haya ambayo labda tungewaweka watumiaji wa ardhi kwenye eneo dogo tu wakaweza kutumia kwa pamoja, tukapunguza migogoro; sasa tunaanzisha halafu tunaacha. Tafiti zinaonesha kwamba haya mambo tukiyatumia vizuri kwa kweli tunaweza tukaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa niligusie ni kuhusu bajeti. Bajeti ya Wizara hii inaonekana kwamba kila mwaka inashuka. Sasa bajeti inashuka; pamoja na kwamba bajeti ni ndogo lakini kile kima ambacho kinakisiwa pia hakitoki kikawaida. Kwa kweli ni jambo ambalo tunaifanya Wizara hii ishindwe kutekeleza kazi zake kama ambavyo imepanga kufanya. Napata mashaka makubwa kwamba utendaji wa Wizara hii unaweza ukawa mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni kuhusu Programu ya Land Tenure Support, ambayo ni nzuri na imeonekana kwamba inafanya vizuri. Hata hivyo, kwa sababu ya mfumo tu wa Serikali inaonekana kwamba hatuiendelezi. Ingawa Waziri ameigusia gusia katika kitabu chake lakini kuna technology inaitwa MAST…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.