Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Salum Mwinyi Rehani (31 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE: SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii adhimu kwangu ya kuchangia bajeti hii ya Ofisi ya Makamu wa Rais na nitaomba tuchangie na sisi wengine tutachangia kitaalam zaidi kuliko kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana wananchi wa Jimbo langu la Uzini, walioniwezesha leo hii kuweko hapa ili kutoa mchango wangu huu katika Ofisi ya Makamu wa Rais na hasa kwenye upande wa Mazingira. Hali ya Tanzania ni tete, bado hakujawa na mikakati ya utekelezaji wa Sera na miongozo mbalimbali, kwa ajili ya kuhami mazingira yaliyopo. Nchi hii miaka 20 na miaka 10 iliyopita sivyo ilivyo leo, kila siku zikienda nchi inakwenda na maji na kama hakutakuwa na uthubutu wa udhibiti wa mazingira tuliyonayo baada ya miaka 10 hapa tutakuwa hatuna tofauti na wale wenzetu wa Ethiopia na nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la uharibifu wa mazingira lakini vilevile na kuondoka kwa uoto wa asili kwa maeneo mbalimbali tuliyonayo katika nchi yetu, miaka 20 iliyopita katika mabonde ya Usangu, ukija mpaka Mlimba na Iringa, yalikuwa ni mabonde ambayo yanaitwa ni mabonde chepe, leo hii maeneo yale yameharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hali ni mbaya zaidi katika Kanda ya Ziwa, hali ya hewa imebadilika, joto limepanda, miti hamna, hali imekuwa ni ngumu zaidi. Ushauri wangu kwa Wizara hii ni kwamba kuwepo na mkakati maalum wa kurudisha uoto wa asili na hasa kwa maeneo yale ya Kanda ya Ziwa na Mikoa ya Kati hapa. Nakuomba Waziri na Waziri Mkuu, uwepo mkakati wa kupanda miti, kwa Watanzania wote, angalau miti minne kwa kila Mtanzania kwa kila mwaka. Mkakati huu ukiwekwa sahihi, tutaweza kuwa na uhakika wa kurudisha hali ya mazingira tuliyonayo. Pia kuweko na aina maalum ya miti ambayo inaweza kuongeza kiwango kikubwa cha uzalishaji wa carbon katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeelezwa katika taarifa iliyoletwa hapa na Waziri kwamba uharibifu uliopo uko wa asilimia mbili, latest information na hasa ile taarifa iliyotoka Durban iko zaidi ya hapo. Kila siku tunapokwenda Ozone Layer inazidi kumomonyoka na ndiyo maana joto linapanda na linashuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka mitano iliyokwisha Dodoma kipindi hiki tulikuwa na baridi leo hii tuna joto na hatuna uhakika kwamba itafika mwezi wa saba baridi itarudi kama vile ilivyokuwa, nchi inakwenda na maji!
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu nataka kuunganisha na ule Mfuko aliousema Waziri wa Mazingira, ule ndiyo ukombozi wa nchi hii. Mheshimiwa Waziri nikushauri kitu kimoja, tuanzishe kwa maksudi Mfuko huu na upitie kwenye simu zetu. Kila Mtanzania mwenye simu angalau achangie nusu shilingi katika Mfuko wa Mazingira. Kwa kila sh. 1,000 itaweza kutusaidia utekelezaji wa mbinu mbalimbali za kuweza kuokoa maeneo yale ambayo yameathirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ni kwamba, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana urudi kwenye mkakati ule uliotengenezwa na NEAP ambao ulikuwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais. Ule Mpango Mkakati na action plan ya NEAP itaweza kututoa kuhakikisha kwamba tunakuwa na mfumo mzuri wa ufugaji, mfumo mzuri wa kilimo, mfumo mzuri wa viwanda na mfumo mzuri wa kuhakikisha kwamba, kila idara inaweza kushiriki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira, Wizara zote ni wadau, suala la mazingira ni mtambuka, hivyo kila Wizara inastahili kuweka fungu maalum kuchangia katika Mfuko wa Mazingira. Wizara ya Madini maeneo mengi yanayochimbwa mashimo ya madini hakuna mpango mkakati wa kuyarudisha kama yalivyokuwa, basi isiwe kurudisha lakini kuweza kuyafanya yale maeneo kutumika kwa shughuli nyingine. Mfumo wa Kilimo tunaolima unasababisha ardhi iondoke rutuba, uoto wa asili unapotea na hali ya hewa inazidi kuwa disturbed, uzalishaji kila siku unaendelea kuwa chini. Hofu yangu kama hakutakuwa na nia thabiti ya kudhibiti mazingira haya, Tanzania itafika mahali itaomba chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika kuangalia suala zima la uharibifu wa mazingira katika bahari, Tanzania imezungukwa upande mmoja na bahari, lakini kule Zanzibar tumezungukwa na bahari kila pembe. Bado sijaona udhibiti au mkakati maalum wa kuvinusuru visiwa vile na kuinusuru hii nchi upande wa bahari na hali ya mmomonyoko unaokwenda siku hadi siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zilizopo za utafiti, kila mwaka bahari inasogeza nusu mita mpaka mita moja juu ya ardhi, kwa hiyo eneo tulilonalo linazidi kupungua, ukiangalia miaka 20 ijayo maeneo mengi ambayo sasa hivi yanakaliwa na watu yatakuwa yamehamwa na maji yatakuwa yamechukua nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi zetu za NEMC na zile zinazofanya impact assessment za kutoa vibali vya ujenzi wa mahoteli na vitu mbalimbali katika maeneo yetu ya bahari, zimekuwa nazo zinatumika kuchangia uharibifu wa mazingira badala ya kunusuru. Nitoe mfano mmoja, tumekuwa na kawaida mahoteli mengi ya Waitaliano yanajengwa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango ambayo yamewasilishwa leo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Nishukuru Mpango umeeleza mambo mengi na umejikita kwenye mambo mengi makubwa zaidi. Inawezekana yakawa size ya uwezo wetu kama nchi au yakawa zaidi ya uwezo wetu kama nchi kwa sababu projections zilizopo kwenye Mpango huu ni kubwa kiasi fulani.
Mimi nataka kujikita zaidi katika kutoa ushauri ushauri kuhusiana na mwelekeo mzima wa huu Mpango ulivyo na mbele tunakokwenda. Mchango wangu zaidi utajielekeza kwanza kwenye sekta ya kilimo, lakini na uanzishaji wa viwanda kwa bidhaa zinazotokana na kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu ulitakiwa zaidi uoneshe mwelekeo sahihi kwenye kilimo na hasa kwenye uzalishaji ili tuweze kupata dira na mwelekeo wa kuelekea kwenye viwanda. Tunajua kwamba kutakujakuwa na udadavuaji wa baadhi ya mambo lakini kwa hivi ilivyoelezwa ndani ya huu Mpango iko too brief na hapa ndipo penye roho ya uchumi na maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza katika hili, mpango haujaeleza mkakati mzima wa udhibiti na uendelezaji wa maeneo yale ambayo mazingira yake yameathirika. Miaka kumi iliyopita Tanzania ilikuwa zaidi inategemea mikoa minne kwa upatikanaji wa mvua ya uhakika, lakini sasa hivi hiyo mikoa minne tuliyokuwa tunasema ina mvua ya uhakika imeshapoteza mwelekeo. Tulikuwa tunaiangalia zaidi Kigoma, Kagera, Katavi, Njombe pamoja na Iringa. Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa maeneo haya yamekumbwa na uharibifu wa mazingira na unapoweka mpango kama huu ambao unataka kutengeneza mazingira ya uzalishaji, vitu hivi lazima viwe na mtazamo maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yetu tumeyaharibu, tukiangalia eneo kubwa tulilokuwa tunalitegemea, tunaliita eneo chepe la mabonde ya Usangu mpaka Ruaha leo hii imekuwa ni mbuga ya kufugia ng‟ombe tu. Hata tukienda maeneo yale ya Kagera, Karagwe, Misenyi na Biharamulo nayo vilevile tumeyaachia huru as if nchi yetu haina mpango mkakati wa udhibiti wa uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo langu, turudi kwenye kuweka mkakati maalum wa udhibiti wa uharibifu wa mazingira katika maeneo hayo ili kurudisha uoto wa asili na hali nzuri ya unyeshaji wa mvua katika maeneo yale. Sambamba na hilo, ule mkakati uliokuwa umeanzishwa Dar es Salaam wa upandaji miti, tunarudia tena, uweze kusambaa nchi nzima kuwe na mkakati kama ule vinginevyo hatma ya nchi hii ndani ya miaka kumi tutakuwa kwenye mtihani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, ni lazima nchi iwe na mkakati wa kuhakikisha kwamba kunakuwa na uzalishaji. Kwa kipindi hiki sasa mkakati mkubwa uelekezwe kwenye umwagiliaji maji. Bado mpango haujaonesha kiwaziwazi mkakati wetu wa ujengaji ama mabwawa au miundombinu yoyote ya umwagiliaji maji kwa kutumia rasilimali ya mito na maziwa tuliyonayo hapa nchini. Tanzania tumejaliwa, lakini mpaka tunajiuliza sijui tumerogwa wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano tuliokuwa nao sisi wengine tuliopata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya nchi za wenzetu, mwezi uliokwisha kulikuwa na kikao cha wataalam wa kilimo cha SADC pale Angola, Wamisri walikuja kutoa taarifa na uzoefu wao tu, kwa kutumia maji ya Mto Nile, ile Suez Canal, wenyewe wanaita Suez Belt, wana uwezo wa kuzalisha pamba tani milioni tano kwa miaka miwili. Sisi tuna Ziwa Victoria lakini uzalishaji wetu kwa Kanda ya Ziwa ambayo ndiyo maarufu kwa ajili ya uzalishaji wa pamba tunasuasua kwenye tani 300,000, wenzetu wanazungumzia kuongeza kutoka milioni tano kwenda kwenye milioni nane sisi tunaangalia 300,000 tutai-maintain vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ili uwe smart uangalie raw material zinazotokana na uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo. Hata hivyo, mwelekeo wetu uwe kwenye irrigation ili na sisi kama wananchi tupate fursa ya kutumia maji na mito ambayo ipo ndani ya maeneo yetu, kitu ambacho bado hakijatendeka vilivyo. Maji tunayo yanaishia baharini kama wengi walivyosema. Nikuombe Mheshimiwa Waziri tukafanye restructuring kwa baadhi ya mambo tuelekeze nguvu kwenye umwagiliaji maji ndipo tutakapokomboka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ni usalama wa chakula, tuwe na mipango ambayo itatuwezesha kuwa na uhakika wa usalama wa chakula hapa nchini. Kwa kweli bado na mimi nasema ni aibu nchi hii kulalamika njaa wakati fursa za vyanzo vya maji tulivyonavyo ni nyingi sana lakini bado hatujajiweka sawa, mipango yetu haijajielekeza kuhakikisha kwamba watu hawa wanalima kwa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mmoja, kama tutaweza kujenga mabwawa yakawa yanatumika kwa kilimo na mifugo, tukaweza kuendeleza hekta 50 tu kila Mkoa kwa yale maeneo yenye uwezekano wa kutengeneza yale mabwawa tuna uhakika wa reserve ya tani 500,000 kila mkoa kwa kila mwaka. Hii ni akiba nzuri lakini hiki ni chanzo cha raw material ya viwanda ambavyo tunategemea tuvianzishe na maeneo mengine yatumike kwa ajili ya chakula na mambo mengine. Tuwe na mkakati na muono wa mbele wa kuona kwamba nchi inakuwa na uhakika wa ile reserve iliyokuwa tunaisema tu lakini kuweka reserve ya chakula kwa kutegemea mvua ambazo hazina uhakika bado hatujaenda vizuri na hatujawa stable. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri tuzingatie kuyafanyia marekebisho baadhi ya mambo, mtuite tuwape mawazo ambayo yataweza kutujenga. Kinachotia uchungu ni kwamba tunatumika katika nchi za wenzetu kutoa mawazo ambayo wao wanayafanyia kazi na wanaweza kupiga hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea mwezi uliokwisha, wenzetu wa Malawi baada ya kupata tatizo kubwa la ukame mtazamo wao sasa hivi ni huo. Haya maelezo ambayo mmeyatoa hapa katika page number 16 ya mpango tuliokuwa nayo ni mkakati ambao EU kwenye agricultural sector ndiyo waliokuwa nao, AU ndiyo waliokuwa nao na SADC wame-copy and paste huohuo.
Kwa hiyo na sisi tusiwe tunauweka kimaandishi, tuuweke kivitendo uwe practical na siyo tunachukua mipango kama hii na maelekezo ambayo wenzetu wameyaweka sisi kwetu baadaye yanaishia kwenye shelf. Nimuombe sana, tusipozingatia na tukaelekeza nguvu zetu kwenye kilimo tumewamaliza Watanzania na tutakuwa na ndoto tu ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mpango bado haujatuambia kwenye uvuvi tunafanya nini. Tumepata maelezo na baadhi ya watu wameeleza lakini katika eneo kubwa ambalo tutaweza kuajiri watu wengi kabisa ni sekta ya uvuvi. Tukijipanga vizuri katika eneo hili, wenzetu wametoa mawazo pale kwamba tutafute angalau meli moja tu ya uvuvi ina uwezo wa kutuanzishia viwanda viwili lakini ina uwezo wa kutoa ajira kwa watu mpaka 3,000. Kwa sababu kazi zilizopo kupitia sekta ya uvuvi ni nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tutengeneze mazingira ya pale bandarini kuwepo na port dock ambayo itawalazimisha wale wanaovua katika maeneo mengine yote ile kuchakata wale samaki na process nyingine zifanyike katika maeneo yetu, tutatengeneza pesa ya kutosha. Taarifa zilizopo sasa hivi duniani, Tanzania baada ya kuzuia leseni za uvuvi katika uvuvi wa bahari kuu, demand ya samaki katika soko la dunia imepanda mpaka tani 230,000, soko lipo wazi, nafasi hii ndiyo pekee ya kuitumia. Nimuombe Waziri wetu wa Kilimo azuie kutoa vibali vya uvuvi wa bahari kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaofuatilia haya mambo na tunayajua, ukiikodi meli moja ya uvuvi Philippines au Thailand wanakodi kati ya dola milioni tano mpaka milioni saba, catchment yake kwa wiki tatu mpaka miezi miwili ina thamani ya dola milioni 40.
Kwa hiyo, kwa wale wanaokodi, kwa wenzetu wanafanya deal kwamba akikodi meli mara moja harudi tena baharini kapata utajiri wa maisha anafanya mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utafiti unavyoonesha samaki wale wengi wanawatoa katika maeneo yetu na wakija katika maeneo yetu haya hawavui jodari tu peke yake, wanavua kamba, pweza, ngisi na samaki mbalimbali na baadaye wanakwenda kufanya uchambuzi katika maeneo yao sisi tunabaki kama tulivyo. Ile ni bahati, ni riziki Mungu katupa tujipange vizuri tuitumie vizuri ilete manufaa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linajieleza hapo, tutakapoweza kuwa na eneo la kuweza kushusha samaki, tukaweza kuanzisha maeneo ya majenereta ya kuhifadhia vizuri samaki, tutaweza kuongeza ajira kubwa kwa sababu wenzetu Ulaya wanachotaka ni minofu. Hivi sasa biashara kubwa iliyojitokeza maeneo ya Kongo ambao wanakuja kuchukua dagaa kwa wingi sana Zanzibar, Mwanza na Kigoma wanakwenda kutengeneza raw material ambayo wanapeleka Ulaya kama ni fish meal, demand yake sasa hivi ndani ya soko la dunia kubwa. Sisi tukiwa na meli hiyo pale zile by products zilizotokana na kutoa zile nyama za samaki tunatengeneza fish meal kwa kiwango kikubwa sana ambapo soko ndani ya eneo la soko la dunia ni kubwa sana. Fursa nyingine ni hizo, pale hutupi kitu, hata ule mwiba wa katikati wa samaki bado ni bidhaa adimu kabisa kwa sababu ile calcium iliyomo mle ni bora zaidi na inahitajika katika maeneo mengi sana kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali na dawa.
Kwa hiyo, mimi wito wangu na wazo langu ni kuiambia Serikali hili eneo la uvuvi lina fursa kubwa sana, kuliko kuwaita Wachina kuja kuweka soko pale la bidhaa zao mbalimbali, hapa pana pesa za waziwazi, tujikite jamani katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kuzungumza ni kwenye mazao ya biashara bado kama nchi tunaendekeza ukiritimba fulani hivi ambao hauleti maana. Leo hii kutengeneza rustan coffee mpaka twende Moshi, Arusha? Gharama za kuchukua kahawa iliyoko Mbinga ambapo kule tunafanya process ya mwanzo tu ya catchment uisafirishe uipeleke Moshi ni kubwa. Wakati mwingine unachukua kahawa kutoka Manyovu au Kigoma iende Moshi, very unfair! Tutengeneze viwanda ambavyo tutaweza kutengeneza kahawa ambayo itaweza kwenda kuuzwa katika soko la nje moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa yetu ni ya nne duniani, bado tuna nafasi kubwa. Kwa ubora hatujawapita Ethiopia, Rwanda lakini tumewapita Uganda, Burundi na Kenya. Kahawa yetu ni bora kuliko ya Brazil, bado tuna nafasi katika soko la dunia. Hata hivyo, utaratibu wa makampuni yanayoshughulika na zao la kahawa ni wa kujitengenezea faida wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi hiyohiyo ipo kwenye tumbaku. Tumbaku kilichotokea pale ni ukiritimba tu wa yale makampuni ya kujifanya wao ndiyo wao wakati bado kuna fursa kubwa ya ile tumbaku katika soko la dunia. Mnunuzi mkubwa wa tumbaku ni China. Sasa hivi China baada ya kuona bureaucracy ya Afrika anatenga hekta karibu milioni mbili azalishe tumbaku nchini mwake, lakini mbegu ya tumbaku kutoka China sisi tunayo hapa. Sasa lile tishio la yale makampuni la kusema kwamba sisi hatununui wanasema wanatisha bwege ni ili sisi tuweze kujiachia hawanunui tupunguze uzalishaji ili wao …
MWENYEKITI: Ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia katika Mpango huu wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri na Menejimenti yote ya Wizara kwa kuleta huu Mpango ambao tunataka tuone ni dira ambayo inaweza ikatuondoa tulipo na kuelekea kwingine ambako tutakuwa na taswira mpya ya kuifanya Tanzania hii iwe ni nchi ya uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi nataka nizungumzie maeneo yale ambayo tunayaita economic tools ambapo tukiyatumia tunaweza kufikia kwenye huo uchumi wa kati mbali na miundombinu na miradi ya kimkakati ambayo inatekelezwa na Taifa. Sina tatizo na miradi yote ya Serikali iliyokuwa imeipanga ya kimkakati, ile miradi mikubwa kwamba itakuwa ni sehemu ya kuifanya Taifa hili liweze kuelekea huko kwenye uchumi wa kati lakini napenda zaidi niishauri Serikali kwani kuna maeneo lazima tutoe lawama kwa kitu ambacho hakijafanyika ili Serikali wasikilize ushauri ambapo utasaidia kutoka kuliko kuendelea kubaki kama tulivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekta ya mifugo, Tanzania mbali ya kuwa ni nchi ya pili kwa mifugo lakini bado sekta hii haijafanikiwa. Nimepitia Mpango huu hapa sijaona maeneo thabiti ambayo tunaweza kufaidika na mifugo lakini na fursa ya ufugaji hapa nchini. Kuchunga tunakochunga hakutusaidii chochote hardly pengine tunakwenda kwenye 2% or 3%. Tunataka tuone Wizara ya Mifugo imejikita katika kuhakikisha kwamba inapeleka mfumo wa artificial insemination vijijini ili kubadilisha aina ya ufugaji kwanza, ili kubadilisha ng’ombe waliokuwepo kule ambao wana uwezo wa kutoa nusu lita na lita moja ya maziwa na waende kuwa ng’ombe ambao wanatoa zaidi ya lita 20 na kuendelea, hilo linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tunataka kuona maziwa haya ambayo yanaweza kuzalishwa ndani ya nchi yanafaidisha nchi. Biashara ya maziwa wenzetu wa Zimbabwe ni sehemu ya uchumi wao mkubwa sana na kwa kipindi kile ilikuwa unachangia zaidi ya asilimia 12 lakini sisi Watanzania tumekuwa ni sehemu ya wanunuzi wakubwa wa maziwa kutoka maeneo ya Zimbabwe na sehemu nyingine wakati ndani ya nchi hapa tunaweza kuzalisha maziwa na kuuza na kuyatumia kwa matumizi yetu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali na Wizara ya Mipango tuwe na Mpango madhubuti na maalum wa kuhakikisha kwamba tunaweza ku-handle maziwa ambayo yako zaidi ya lita milioni mbili kwa siku yanayozalishwa yageuzwe kuwa bidhaa ambazo zinatumika katika maeneo yetu mbalimbali. Mimi niseme wazi nasikitika sana na mfumo wa biashara ya kupokea maziwa mengi sana kutoka kwa majirani zetu kuingizwa ndani ya nchi kuliko maziwa yanayozalishwa hapa nchini. Ni kitu gani ambacho kinatushinda kuweza kuwa na viwanda ambavyo vinaweza kuchakata maziwa ambayo yako hapa nchini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu handling yake ni gharama, sasa Serikali pamoja na miradi mikubwa ambayo inaifanya ielekeze nguvu sasa katika eneo hili ambapo raw material yake ipo ndani ya nchi ya kutosha na tuache mfumo huu uliopo sasa. Nafikiri iwekwe kodi maalum kubwa ya kudhibiti uingizwaji wa maziwa kutoka nje ili watu waweze kutumia maziwa yaliyoko hapa nchini. Mkiwauliza watu wa Mifugo, hata jana nilionana na Profesa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo bado anasema hakujawa na engagement ya fedha ambazo zinakwenda kutengeneza mitamba ya kutosha ambapo tutaisambaza katika maeneo yetu mbalimbali na kubadilisha taswira ya ufugaji kuwa wa kisasa zaidi kuliko kuendelea kuchunga ambapo tunasababisha ugomvi wa wakulima na wafugaji uliokuwa hauna sababu wakati njia rahisi ya kutumia teknolojia ya kisasa ya ufugaji ipo na hatujaitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, vilevile nilikuwa naangalia Mpango Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa mara ya tatu niseme kwamba bado hatujatumia bahari iliyokuwepo ndani ya nchi hii. Katika dunia hii watu wote wanatushangaa, Mheshimiwa Dkt. Mpango kinachoniuma zaidi nilipata fursa ya kwenda Comoro kama miezi mitatu iliyopita. Comoro wao kama kisiwa wameanza kufaidika na blue sea sisi kwetu bado.

Tuna suffer na 0.4 imekimbiza meli zote, tuna fursa ya kuifanya SUMATRA iweze kukusanya karibu shilingi milioni 40 kwa kila meli iliyokuja kufanyiwa inspection ya kwenda kwenye uvuvi wa bahari kuu na zaidi ya meli 200 hapa duniani zinataka kuja kuchukua leseni lakini kuna kikwazo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niombe Serikali badala ya kuelekeza nguvu zaidi katika maeneo ya uwekezaji wa reli, umeme na uwekezaji mwingine wowote mkubwa i- engage pesa maalum kwa ajili ya blue sea. I will promise Bunge hili ndani ya miaka miwili break even ambayo itapatikana kutoka katika bahari hakuna sehemu yoyote ya uchumi ambayo itaweza ku-compete. Fedha ziko nyingi na ziko nje nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunachosema hapa demand inaendelea kuongezeka na kinachofanyika duniani tunatengenewa artificial fish siyo samaki halisi tunaoletewa kwenye makontena hapa na Watanzania tunakula wakati tuna bahari ya kutosha na bado tumeomba kuongezewa eneo la nautical miles 150 la nini sasa kama hatuwekezi? Kama tumeomba tuongezewe eneo basi tuiombe Serikali iwekeze katika bahari ile tuoneshe kwamba na sisi tunayo potential ya kuitumia bahari hii iliyokuwepo hapa na Mungu aliyotujalia tuweze kuleta mabadiliko chanya na tuende kwenye uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana kama wanavyoweza kufaidika watu wa Namibia kwa zaidi ya asilimia 11 ya uchumi wao GDP wanategemea samaki ambao wanapenya tu katika mlango mmoja wa Mozambique Current kwenda katika eneo la Namibia na wanaweza kupata fedha ambazo zinaweza kuongezea GDP zaidi ya asilimia 11. South Africa pamoja na uchumi wao mkubwa lakini 8% wanapata fedha kutoka bahari, tunachoshindwa Tanzania ni nini? Mimi nimeuona Mpango halisi huu hapa lakini sijaona mkakati ambao tunaelekea kwenye bahari kuu na kuifanya nchi hii ni sehemu ya nchi ambazo zinauza samaki nchi za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala zima la kilimo. Nchi hii tumejaliwa kuwa na maeneo mengi mengi ya kilimo lakini pamoja na kuwepo na miradi ya SPDII ambayo mpaka sasa hivi hatujaona uendelezwaji wake na kufanya kazi katika maeneo ambayo yanaweza kuleta mabadiliko hayo chanya. Bado mwendo wake nauona unasuasua ingawaje mradi sasa hivi umeshafikia miaka miwili. Ushauri wangu uko hapa, Serikali inatakiwa iwekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niombe Serikali kitu kimoja, mfumo uliopo hivi sasa wa kujenga canal irrigation hautusaidii kitu, unakula fedha nyingi na unachukua muda kumalizika na wakandarasi ndiyo sehemu ambayo wanaweza kupata pesa bila ya sababu.

Kwa ushauri wangu mimi tuzuie fedha zote zinazokwendwa kwenye canal irrigation ambapo tunaweza tuka-save zaidi ya asilimia 70 kwa kutumia pipe irrigation ambazo unaweza kuwekeza kwa muda mfupi tu. Wiki mbili tu unajenga zaidi ya hekta 200 au 100 kwa kutandika mabomba ukaweza kuhifadhi maji na akatumia maji ambayo hayawezi kupotea. Tukitumia mfumo huo tuaweza ku-control ile wanaita Evapo-transpiration lakini vilevile contamination ya wadudu, maradhi, magugu na vitu vingine vyote tutaepuka. Hiyo ndiyo teknolojia tunayotaka twende na dunia huko ndiko iliko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuendelea kujenga mitaro kwa mawe na saruji ambayo baada ya muda wakandarasi wanapiga hiyo pesa na hakuna kinachoendelea, niseme wazi kwamba huko sioni kama kuna tija na hakuwezi kutufikisha. Tutumie njia rahisi ambapo tutaweza kuzalisha na kuyatumia maji effectively kuliko hivi sasa. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali katika mipango yetu yote hizi billions of money zinazokwenda kwa ajili ya kutengeneza canal za irrigation tuelekeze kwenye pipe irrigation ambacho ndicho kilimo cha kileo zaidi kuliko huku tunakokwenda.

MWENYEKITI: Muda wako umeisha Mheshimiwa.

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE: SALUM M. REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana na mimi niipongeze Serikali kwa kuleta muswada huu ambao kusema ukweli umechelewa kwa sababu ni muda mrefu nchi ilikuwa inakwenda katika muelekeo ambao kwa kweli hakuna mdhibiti, yaani hakuna eneo lile ambalo lina mwenyewe hasa katika eneo hili la maabara. Naomba nizungumzie katika baadhi ya maeneo ambayo nahisi yanaleta ukakasi, yanaji-contradict.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niungane na mwenzangu aliyemaliza tunapozungumzia jina kamili la hii maabara yenyewe, ni Government Chemical Laboratory Authority. Tukitia authority hapa tunakusanya na maabara nyingine zilizokuwa nje ya hii ya chemistry kwa sababu moja. Kemikali zinazotumika ndani ya nchi ziko za aina nyingi, na kila maabara inatumia kemikali. Sheria hii inahusiana na maabara za kikemikali tu peke yake, lakini tukija kwenye laboratory za mifugo tunatumia kemikali za aina nyingi na humu hazijaguswa wala hazijazungumzwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye maabara za kilimo, zinatumia kemikali za aina tofauti. Ni-declare interest sisi watafiti kazi zetu hazimaliziki shambani, zinakwenda kwenye maabara. Utakapokwenda kwenye maabara unatumia aina mbalimbali za kemikali. Sasa sijui sheria hii inaweza ikasema nini ili kuwadhibiti wale wote wanaotumia kemikali ndani ya nchi kuwa katika mfumo unaoeleweka. Kinachohitajika hapa ni consistence ya matumizi ya kemikali ambazo zinakuja ndani ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nililoliona ni suala zima la uingizaji wa kemikali na watumiaji hapa nchini. Tuna maabara binafsi nyingi. Zipo zinazofanya shughuli ambazo nyingine hata huelewi, ili mradi tu mtu anasema kwamba mkono unaenda kinywani. Sasa hapa kwenye sheria hii sijaona pahala ambapo tunaweza kuwakamata hawa ambao kwanza waagizaji, wanaagiza bidhaa au kemikali hizi kwa sheria ipi na nani atakuwa anawasimamia. Je, ni huyu Chief Government Chemical Laboratory au kuna mamlaka nyingine ambayo itaweza kuwakamata hawa? Naomba Mheshimiwa Waziri pale tupate clarification hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mwongozo wa matumizi ya hizi kemikali kwa watu mbalimbali, kwa matumizi mbalimbali bado kumeonekana kuna uhuru mkubwa ambao hauna udhibiti wa matumzi ya hizi kemikali; na ndiyo maana hapo nyuma kukajitokeza wimbi kubwa la watu kutengeneza mabomu, kutengeneza vitu mbalimbali vya kemikali na acid nyingine zikawa zinatumika bila ya kuwa na mdhibiti maalum. Sasa kama sheria hii inakwenda kujibu hoja hii niliyokuwa nimeitoa hapa naomba ijielekeze au kuwepo na vipengele ambavyo vitaweza kueleza straight, kwamba hawa wanatakiwa ili kuweza kufanya matumizi yao wapite njia hii na kibali chao kitapatikana katika ofisi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nilitaka kuzungumzia suala zima la research on toxicity and food toxic. Hapa napo pana shida kwa sababu kuna sheria tofauti na mamlaka tofauti zinafanyakazi katika eneo hili. Mamlaka ya udhibiti wa chakula, TBS wote wanafanyakazi katika eneo hili. Lakini hapo hapo tunapokwenda kuangalia insurance of quality and service nao vilevile sheria inaji-contradict, kwa sababu kuna mamlaka chungu nzima ambazo zinafanyakazi katika eneo hilo. Sheria hii inabidi iwe specific au iwe na mamlaka ya kugusa hawa wote na wawekwe katika kapu moja na tuwe tunazungumza sauti moja kama Serikali ili kuweza kuonekana kwamba msimamo wa Serikali kwa wote ambao wanakuwa wananasibishwa na matumizi ya kemikali basi wanaeleweka na kunakuwa na mfumo unaotambulika.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nililotaka kuzungumzia ni kwenye suala la directory, zone unit and section; hapa panahitaji clarification. Kwa sababu tunaposema kwamba tuna-establish set number of directory zone, unit, section with pre-describe function as the board determine, bado hapajakaa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtazamo uliokuweko kwamba, je, hizi zone, unit zitakuwa kwa kanda zetu kimikoa au kulingana na institutional entity ya pahala fulani? Inabidi tuweze kujua kwa undani zaidi zone hizi na unit hizi ni za aina gani na set yake inakuwaje, tupate clarification na function zake zitaweza kufanyakazi vipi na wata-flow kwa nani? Kwenye act hii au watakuwa na watu wengine? Kwa sababu hao watu wanaosimamia vitu hivyo kwa hivi sasa kila mmoja ana-play, wanasema kwa yule ambaye anaweza kumpa tonge, yule anayeweza kukufadhili ndiyo mtu anaweza ku-play katika maeneo hayo. Tumezikuta baadhi ya laboratory zinafanya shughuli tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tunaloweza kulisema hapa, kuna kundi moja kati ya hizi directory units kuna watu wa pathology wanahitajika wawemo katika eneo hili na wanafanya shughuli hizi, ambao ni biologist hao, hawamo na hawakuonyeshwa, lakini wanatumia kemikali, wanafanya shughuli za maabara ambazo zinafanana na maeneo haya, lakini hakuna mwongozo ambao unaosema kwamba hawa wako wapi. Tuwaweke kwamba hawa ma-pathologist wako kwenye health tu pake yake au wako wenye agriculture au mifugo peke yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano; kuna maeneo ambayo linatokezea tatizo ambalo linawakutanisha hawa watu wote. Kuna kichaa cha mbwa katika maeneo yetu mbalimbali ya nchi yetu hii. Kichaa cha mbwa kinapotokea nani mwenye ku-play ile role? Je, maabara za mifugo au ni Maabara hii ya Mkemia Mkuu ndiyo inayoweza ku-sound na kusema kwamba mwongozo uliokuweko sasa hivi utumike labda drugs aina hii au uthibiti uweko hivi? Kwahiyo tunahitaji tupate clarification katika hayo maeneo, na hao watu ambao tunahisi kwamba wako nje ya hii taasisi waweze kuingizwa na tuweze kuwajua wanafanyaje.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka nilizungumze ni suala zima la uchunguzi. Kwanza nilitaka kuzungumza kwenye suala zima la Bodi. Bodi imeelezwa hapa vizuri kwenye hii Part Three, Administration and Institutional Arrangement, lakini haya mamlaka ya huyu Mtendaji Mkuu ambaye ndiye Katibu wa Bodi. Nahisi upande mmoja yako makubwa zaidi kuliko uwezo wake, lakini upande mwingine namhisi kwamba hana mamlaka ya kuingilia baadhi ya maeneo. Kwa mfano, dhana yangu mimi ningefikiri, Bodi hii ingekutanisha na wale ma-director ambao wanatumia laboratory nyingine; kwa mfano wale wanaotumia maabara za mifugo, wale wa pale Mikocheni.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna maabara nyinginezo kama za Muhimbili. Maabara nyingine zilizo kubwa ni za SUA; lakini kuna maabara nyingine za chemistry ambazo watu wako nje ya institutions za Serikali, nao ni sehemu ya Bodi ambayo wangeweza kuchangia sana kutoa muelekeo sasa wa laboratory hii ili kuwa na maamuzi ya kikemia zaidi kuliko kuchukua watu ambao wako ndani ya taasisi moja au Wizara tu peke yake ukatengeneza bodi na wengine ukawaacha; kwa hiyo, wale wengine wanakuwa hawana role ya ku-play. Tukifanya hivyo angalau tutaweza kuwakutanisha na wao wataweza kupangiwa majukumu yao kulingana na mwongozo wa act hii. Sasa suala la uchunguzi linatakiwa kuweko na ile wanaita advisory committee, hii iwe ina-prove kwa zile kesi zilizo kubwa zinazojitokeza, zinazofanyiwa uchunguzi na si ni kazi ya huyu chief peke yake kuweza yeye ku-authorise kila kitu. Ushauri wangu ulikuwa hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna pahala ambapo nimehisi kwenye hii function and power of the board; kuna eneo naona kwamba linaji-contradict linahitaji kuwa na clarification; ya mwanzo, kwenye ile namba 8(b); “ approval registration, suspension or councilation of Industry chemical, consumer chemical or chemical dealers.”
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa panahitaji paongezwe na non-industrial chemical kwa sabaabu hawa kwa muktadha huu wametolewa na wanahitaji wawepo, na ndio hao wanaotengeneza aina mbalimbali za kemikali katika maeneo yao; kama alivyokwishakuwataja hapa ndugu yangu Waitara wengine wanatengeneza mpaka gongo zinazotumika kwa vitu vinginevyo na spirit kwa hiyo hao nao waweze kuwemo ili tuweze kuwatambua. (Makofi)
Lakini vilevile nilitaka kuangalia suala zima la disposal of articles, chemicals and chemical products. Hii hapa inakuwa na shida. Shida iliyokuweko kwenye maabara hii kuu ya Mkemia panatawaliwa zaidi na rushwa. Na rushwa inatokezea kwasababu kila mmoja anayepeleka sampuli zake pale anahitaji kuwa na positive results. Na ili aweze kupata positive results anatengeneza mazingira ya kupata positive results. Nafikiri ni pahala ambapo pa kuweza kuangalia vizuri. Wale ambao wanaambiwa kwamba hii bidhaa iende ikawe disposed nyingine nyingi zinafika njiani zinageuzwa na zinaingizwa mtaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja ya kwamba kunakuwa na Askari wanao-escort lakini tushashuhudia bidhaa nyingi nyingi ambazo tunaambiwa hizi aidha zime-expire au zimekuwa condemned zikawe disposable lakini baada ya wiki moja, mbili unazikuta ziko mtaani pengine zimehamishwa Mkoa mmoja na kupelekwa Mkoa mwingine. Nafikiri hapa kungekuwa na sheria yenye adhabu kali inayoweza kuoneka ya kuweza kuwadhibiti hawa watu ambao bidhaa zao zimeshakuwa condemned au zimeshaambiwa hizi zikawe disposable na ziweze kuwa disposable; lakini wasimamizi wa hapa waweze kueleweka. Hii technical committee (advisory board) ndiyo inayotakiwa ifanye usimamizi wa zile bidhaa ambazo zinakuwa disposable.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nimeliona kwamba lina mkanganyiko, tuna maeneo ambayo tumeyaona kwamba ni kazi za bodi lakini siyo kazi za bodi. Ni kazi za Chief huyu wa Government Chemical Laboratory, yeye ndiyo anaweza kuzifanya na zisiingizwe kwenye bodi, ni shughuli ambazo ni nyepesi za kuingizwa huko. Kwa mfano; take the sample of laboratory test imo kwenye moja ya function ya power of the board, haihusiki hapa. Tuitoe na tumuachie Mtendaji Mkuu hiyo kazi anaweza kuifanya na ikamalizika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nyingine hata hii tuliyosema conducting inspection of premises of service regularly by the authority, hii hapa nayo vilevile haina haja ya kuweko kwenye bodi, ni kazi ambayo inaweza kufanywa na chief na hiyo kazi ikaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nililiona ambalo linahitaji kufanyiwa marekebisho ni power of inspection. Kwenye power of inspection article ya 15 hii hapa…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nilitaka nitoe shukrani kwa uwasilishaji wa hotuba hii ya Waziri kuhusu bajeti ya elimu. Nilikuwa na mambo ambayo yananisikitisha na hasa kuhusiana na mfumo mzima wa elimu unavyokwenda hapa Tanzania. Kwa kiufupi kusema ukweli, hakuna consistency ambayo tunaiona inatolewa kwa elimu yetu katika level zote. Tuchukulie mfano kule Zanzibar, safari hii wamesema wameanza kufanya mitihani ya Darasa la Sita. Ukitoka Darasa la Sita unaaza Form One.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto hawa wanaoanza shule miaka minne, miaka mitano anaanza Darasa la Kwanza, akifika Darasa la Sita, ana umri gani? Halafu arukishwe aende Form One. Mtu huyo huyo anatakiwa afanye Common Exam Form Four, ambayo inasimamiwa na NECTA. Huku Tanzania Bara Darasa la Saba, lakini Form Four wanafanya Common Exam. Sasa hizi elimu tunaiga mifumo ya nje ambayo kwa kweli haijafanyiwa uchunguzi na utafiti wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya utafiti katika Jimbo langu la Uzini na nilikuwa naandaa strategic plan. Preliminary survey niliyokuwa nimeifanya matatizo niliyoyakuta ndani ya lile Jimbo, kuna tofauti kubwa baina ya shule na shule ndani ya Jimbo, achilia mbali ndani ya Wilaya. Tofauti nyingine iliyokuwepo, ni baina ya shule za private na shule za Serikali, there is no common syllabus. Kila mmoja anaangalia mazingira ya uboreshaji wa elimu kwa eneo lake.
Sasa kwenye Serikali unajiuliza, tofauti ya syllabus hii ya Serikali inatofautiana baina ya shule moja na shule nyingine, lakini kubwa linatokana na kwamba hakuna monitoring, ufuatiliaji haupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakaguzi ndio wanaoweza kupita katika zile shule wakaweza kuhakikisha kwamba syllabus inayofundishwa pale ni sahihi. Shule zetu nyingi nyingine zinatumia mitaala inayotoka Cambridge, nyingine zinatumia mitaala ya Kenya nyingine zinatumia mitaala waliyotengeneza wenyewe kulingana na mazingira yao; ndiyo maana unakuta level ya upasishaji inakuwa tofauti baina ya eneo moja na lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kama tuna Common Exam, lazima tuwe na mtaala mmoja na flow iwe inaeleweka kutoka chini kuja juu. Flow yetu iliyokuwepo ndiyo kitu kinachotutesa. Kila mmoja anakwenda njia yake. Nchi hii hatutafika kwa kila mmoja kwenda vile anavyoona yeye. Leo ukienda St. Mary‟s na shule nyingine za mission zina miongozo na mitaala yao na kiwango chao cha elimu kinachotolewa ni tofauti kabisa na shule nyingine za private, lakini halikadhalika shule nyingine hizi za vipaji maalum zina miongozo yake na mitaala yake mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba tukae pamoja, kama ni NECTA na wadau wake wengine ili kuweza kutoa common syllabus itakayoweza kufuatwa, lakini vilevile ile consistency ya madarasa tukubaliane, kwa sababu wale Wazanzibari wanasema wao wakiona flow imekwenda vizuri mwakani nao Tanzania Bara inataka kuanza mwisho Darasa la Sita, haieleweki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoamua jambo, tujiandae kwanza, tufikiri hawa wanafunzi kweli tunataka kuwapa kitu gani na kwa level gani? Mtoto akimaliza Shule ya Msingi, Darasa la Sita, huyo anamaliza Form Four bado mdogo sana na uwezo wa kukabili mtihani wa Form Four unakuwa haupo. Sasa nashauri kwamba mkutane viongozi wa elimu wa sehemu hizi mbili ili kuwe na mustakabali mzuri wa kuweza kuendesha hizi shughuli na mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linakwaza kwenye elimu ni suala zima la ukosefu wa Walimu husika kwa masomo husika. Shule zetu nyingi Walimu wamekuwa wanabambikiziwa masomo ambayo hawana ujuzi nayo. Mwalimu amesomea arts kwa vile hakuna Mwalimu wa science, anapewa science anaambiwa bwana utaziba kiraka.
Vilevile Mwalimu amesoma science sekondari, pengine Form Two au Form Three, lakini leo ndiyo unamweka Mwalimu huyo aweze kufanya practicals za chemistry na physics kwa wananfunzi wa Form Four. Sasa kwa kufanya hivi, tunaziba viraka. Hii siyo elimu ambayo tunategemea kwamba itaweza kuwasaidia Watanzania. Kuwepo na utaratibu maalumu wa kuajiriwa Walimu wapelekwe katika maeneo maalum ili kuwe na uwiano wa utoaji wa elimu. Vinginevyo bado tutaendelea hapa kuhangaika na kutengeneza bajeti na kushauri lakini hakuna kinachoendelea. Elimu inaporomoka kwa mfumo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kinachotofautiana, shule nyingi zimejenga maabara, lakini tatizo la vifaa vya maabara limekuwa sugu na haviko katika shule chungu nzima. Na leo tuna lengo la kuhakikisha kwamba tunainua elimu ya sayansi katika nchi hii. Watu wale waliokuwa wamejenga maabara pengine inawezekana kwa shinikizo, kwamba lazima iwepo maabara pale, hapana walimu, vifaa vile hata kama wanavipeleka walimu waliokuwepo hawana uwezo wa kufanya zile practical. Kwa hiyo, mtu anakuwa na majengo na vifaa ambavyo havitumiki. Nakuomba Mheshimiwa Waziri hili nalo ukae na timu yako …
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami kupata fursa ya kuchangia katika hoja iliyokuwepo sasa hivi Mezani ya Bajeti ya Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishukuru Serikali, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha hapa taarifa yake nzuri. Vile vile naishukuru sana taarifa ya Kamati ya Bajeti, imeshauri mambo mengi ya msingi, Namwomba Mheshimiwa Waziri aiangalie kwa jicho la aina yake. Nina mambo kadhaa ambayo napenda niishauri Serikali kuweza kuyaangalia na ikiwezekana kuyafanyia marekebisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza nataka kuzungumza juu ya suala zima la tozo ya bidhaa za mbogamboga za kilimo na hasa kwa wafanyabiashara wale ambao wanatoka Bara kwenda Zanzibar na wale ambao wanatoka Zanzibar kuja Tanzania Bara. Mheshimiwa Waziri hili linarudisha tena kidonda cha kero za Muungano; isitoshe, suala hili halijaangaliwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar hivi sasa ina zaidi ya mahoteli 450 ya utalii. Asilimia 70 ya vyakula ambavyo ni mboga mboga na matunda vinatoka Tanzania Bara. Mazao haya ni very perishable, yaani hayana uwezo wa kustahimili kwa muda mrefu. Leo ukichukua nyanya Ilula, ukifika Dar es Salaam, umemaliza siku moja au siku moja na nusu; robo ya ile bidhaa tayari imeshaharibika. Unangoja meli uyasafirishe kufika Zanzibar, nusu yake nyingine tayari imeshaharibika; lakini bado unatoa pale uyapeleke Kiwengwa au Nungwi ambako ndiko kwenye ulaji wa yale matunda. Mfanyabiashara yule atakwenda mara mbili mara tatu, biashara ile imemshinda. Hapa hatujengi. Tunawavuruga hawa wafanyabiashara na mwisho wake badala ya kwenda mara tatu, mara nne, biashara hii imemalizika. Hakuna biashara itakayokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utafiti tulioufanya mwaka 2014 kwa mwezi mmoja, biashara ya mboga mboga na matunda ni zaidi ya tani 160,000 kwa mwezi mmoja zinasafirishwa kutoka Bara kwenda Zanzibar. Biashara hizo zinaingiza zaidi ya shilingi bilioni 2.6, fedha zinazunguka kila siku kutoka Bara kuja Unguja; yaani eneo hili tunalivuruga. Lazima tuwe makini na tupate maelezo yaliyo sahihi kuhusiana na mazao haya kutozwa tozo hizo ambazo zimependekezwa na Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka kuzungumza suala zima la makato au tozo za Waheshimiwa Wabunge. Ni eneo ambalo kwa kweli limemgusa kila Mbunge aliyekuwemo ndani ya Bunge hili. Siyo hivyo tu, hasa wale Wabunge ambao wanatoka katika Majimbo waliyogombea; hali ni ngumu Mheshimiwa. Sms zaidi ya 300 kwa siku, kati ya hizo sms 200 zote zinaomba hela. Leo Mbunge huyu unakwenda kusema unamkata kile kiinua mgongo chake unategemea nini? Atarudi vipi hapa? Ni wazi kabisa huo ni mkakati wa kuwadhibiti kwamba hapa wasirudi mwaka 2020 au 2021. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo tu athari yake haitokani na hapo, athari hiyo itatokana vilevile na ile miradi ambayo ilionekana kwamba Mbunge huyu angeweza kusaidia kuleta maendeleo katika maeneo yake. Kwa mtazamo ninaouona, katika watu wenye hali ngumu hivi sasa ni Waheshimiwa Wabunge. Waonewe huruma! Waangaliwe kwa jicho ambalo litaweza kuwafanya Wabunge hawa, hasa wengi wa CCM, warudi katika miaka mitano ijayo. Vinginevyo, wanakwenda na maji kama eneo hili halikufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumza vile vile suala zima la zile shilingi milioni 50. Naomba nishauri kwamba fedha hizi tusiangalie kuzipeleka kwenye SACCOS, ziangaliwe kuboresha mazingira ya vijiji ambavyo vinapelekewa hii fedha, kwa sababu, kuna mahitaji mengi ya msingi; hospitali hazijamalizika, zahanati, shule zimekaa magofu na zilizomalizika hazina vitendea kazi, hazina madawati, hazina vitu mbalimbali; maji hamna na barabara ni mbovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi fedha ni muhimu sana, lakini ziangalie kujenga maendeleo ya vile vijiji, viwe bora zaidi na watu wanahitaji kuishi maisha bora zaidi kuliko hali ilivyo sasa hivi. Kila mmoja anatamani fedha ile iende katika eneo lake kwa ajili ya kuboresha vijiji vilivyokuwa na hali mbaya katika maeneo husika. Naomba kasma ikatwe kwa ajili ya kuangalia vikundi vya akinamama na hizo SACCOS, lakini zaidi fedha hizi zielekezwe kuangalia miradi ya maendeleo katika kila kijiji ili kuboresha mazingira yaliyokuweko kule na kuwafanya watu wawe na maisha bora zaidi kwa kila Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania bado tuna fursa nyingi ambazo Serikali kama itaweza kusimamia vizuri, tunaweza kutengeneza maeneo mengine ya mapato kuliko vyanzo ambavyo sasa hivi vimeainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Fursa iliyokuweko katika corridor ya Mtwara na hasa kwenye yale maeneo ya uchimbaji wa makaa ya mawe na chuma…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kujikita zaidi kwenye suala zima la kilimo. Bajeti haikumtazama mkulima, haikutazama kilimo kwa ujumla wake. Mimi kilichonisikitisha zaidi, bajeti ya mwaka uliopita pembejeo zilitengewa karibu zaidi ya shilingi bilioni 50, lakini mwaka huu ambao tunajiandaa kuwa Tanzania ya viwanda pembejeo haikuzidi shilingi bilioni 20. Sasa tunaposema kwamba tuna lengo la kuongeza uzalishaji au kupata mazao kwa ajili ya viwanda, mazao haya yatapatikana vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia tathmini ya pembejeo zilizotoka miaka iliyopita siyo zaidi ya asilimia 10 kwa wale wasambazaji wa pembejeo, wakulima walikuwa wanapata pembejeo hizo katika maeneo yao. Hali hii mwaka huu tunaitazama kwa jicho gani? Obvious, uzalishaji utashuka. Hakuna njia ya mkato, uzalishaji utashuka kwa sababu hakuna pembejeo ambazo zitatosha kwa ajili ya kuwafanya wakulima hao waweze kuzalisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili litaathiri maeneo mengi, litaathiri kwanza wazalishaji wenyewe, litaathiri zile Taasisi na Mamlaka tulizoweka kwa ajili ya kununua mazao katika maeneo yao mbalimbali na hasa kwa zile taasisi ambazo tumeziweka zinunue chakula kwa ajili ya chakula cha akiba na kile cha ruzuku, hakutakuwa na chakula cha kutosha kwa hali inavyokwenda. Vilevile athari nyingine iliyojitokeza hapa ni kufungua milango kwa private sector au waleta pembejeo binafsi kuweza kuleta hizi pembejeo na kuziuza kwa bei ya juu sana kwa sababu ndiyo mahali pekee panapopatikana hizi pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliona kwenye ripoti au taarifa ya Kamati ya Bajeti na tulilipeleka kama Wajumbe wa Kamati ya Kilimo suala hili liongezewe fedha na lipewe msukumo maalum ili kuwafanya wananchi wa nchi hii waweze kuzalisha kwa uhakika na ile surplus itakayopatikana iweze kupelekwa kwenye hivyo viwanda ambavyo tunataka tuvianzishe. Wasiwasi wangu, mpango mzima wa kuanzisha viwanda katika maeneo haya hasa kwa kutumia raw materials za kilimo utaweza kuathirika na vinginevyo usiweze kufanyika kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kuzungumza kwenye suala zima la kilimo cha umwagiliaji maji. Bado Serikali hapa haijawa na kipaumbele. Tanzania hii ya leo iliyokuwa imeathirika na mazingira na hali ya hewa katika maeneo mbalimbali vyazo vingi vya maji vimepotea, hata yale unayochimba sasa hivi unayochimba katika urefu mkubwa sana kwenda chini, water table imeshuka. Njia pekee ya kulima ni kutumia umwagiliaji. Scheme zetu zilizokuweko nyingi zimechoka zimetengenezwa zamani na zile zinazotengenezwa sasa hivi speed ya utengenezaji wa hizo scheme mpaka kuwafanya wakulima waweze kulima kwa kutegemea maji ni ndogo, lakini fedha vilevile zilizotengwa kwa ajili ya masuala mazima ya umwagiliaji maji ni kidogo sana. Sasa nina wasiwasi nia ya kweli ya dhati ya Serikali ya kuhakikisha kwamba wakulima hawa wana uhakika wa kulima iko wapi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba Waziri wa Fedha aangalie sana, tuwe na mpango maalum wa kuhakikisha kwamba tunaongeza maeneo ya umwagiliaji angalau asilimia kumi kila mwaka ili tuwe na uhakika wa uzalishaji wa mazao mbalimbali na kuweza kuwafanya wakulima wetu wawe na uhakika wa uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine katika hilo ni suala zima la utafiti. Nchi yoyote katika eneo ambalo linatakiwa liwe na kipaumbele utafiti ni eneo mojawapo kwa sababu ndipo mahali ambapo unapata hizo facts. Nina-declare interest kwamba na mimi niluwa mtafiti kwa zaidi ya miaka nane, ninajua machungu, adha na taabu za utafiti kama hakuna fedha zinazotikawa. Leo hakuna msukumo wa fedha ambazo zinakwenda kwa watafiti moja kwa moja wakati watafiti wale tayari wameshaanza kazi kubwa ya miaka mitatu, miaka minne kutafiti aina mbalimbali, aidha, mbegu, au maradhi mbalimbali au dawa au ufumbuzi wa tatizo ambalo limekabili katika eneo fulani. Leo hii kama hakuna fedha ambazo zinapelekwa katika maeneo haya ya utafiti kwa kweli tunaanzisha kitu ambacho kitawavunja moyo watafiti na hatutakuwa na maendeleo thabiti kwa sababu hatutakuwa na uhakika wa kile ambacho tunakifanya, tutakuwa tunakwenda kwa kubahatisha. Niombe sana kuwepo na msukumo maalum katika eneo hili la utafiti na zipelekwe fedha ili hawa watafiti wengine wamalize research zao na wengine waweze kuanzisha zile research ambazo zitaleta manufaa na mwelekeo mpya wa Tanzania hii ya viwanda tunayokwenda nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti uko katika kila eneo, hata hivyo viwanda ambavyo tunataka kuvifanyia kazi au kuvianzisha lazima kuwe na tafiti za kutosha kuona kwamba zinaweza zikafanya kazi vipi. Kuna material au kuna malighafi za kutosha za aina gani na ubora wa hizo malighafi ambazo zitatumika katika hivyo viwanda tulivyokuwa navyo. Niombe sana tuziangalie taasisi zetu za elimu ya juu, lakini tuangalie Taasisi za Utafiti ili ziwe na kazi na kuleta mabadiliko ya kweli hapa nchini. (Makofi)
Nizungumzie eneo lingine ambalo nimeona bado mkazo wake siyo mkubwa. Tuna mifugo mingi Tanzania, lakini bado eneo hili halijawa productive kwa nchi yaani zile revenue hazijaonesha kwamba kweli inaisaidia hii nchi kupunguza umaskini na kuwaongezea kipato, siyo kwa wananchi wenyewe lakini siyo kwa Serikali vilevile. Eneo hili linahitaji tafiti, lakini inahitaji kutiliwa mkazo ili tuweze kuwa na mifugo iliyo bora na kuwa na ufugaji wa kisasa zaidi. Bado mifugo yetu tunaendelea kuendeleza ufugaji ule tunauita indigenous ufugaji wa kizamani sana, kiasi kwamba mifugo yetu inakosa bei lakini inakosa vilevile kustahimili mazingira yaliyokuwepo hivi sasa matokeo yake ng’ombe, mbuzi na wanyama wengine wanakufa kwa wingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitishwa na kitu kimoja ambacho Serikali inapoteza pesa nyingi sana. Utafiti tulioufanya kuna ng’ombe wengi wanavushwa kimagendo hasa katika mpaka wa Arusha kwenda Kenya. Wakenya wanatarajia kupokea ng’ombe 2,000 karibu kila wiki kutoka Tanzania, lakini ng’ombe wale wakishachinjwa na kufanyiwa process nyinginezo miguu na zile kwato tunaletewa Tanzania kwa ajili ya viwanda au kwa ajili ya ku-pack na kupeleka katika maeneo ambayo watu wanaweza kuifanyia bidhaa. Sasa tunajiuliza…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuunga hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii kwa uchache nizungumze yale ambayo nilikuwa nimepanga niweze kutoa kama ushauri kwa Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwe mbali saa nyingine kwa baadhi ya maelezo ambayo wenzangu wameyatoa, moja hasa likugusa kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka huu. Ni lazima tukubali ukweli kwamba tumepitisha bajeti ambayo siyo practicable, haifanyi kazi ile bajeti ni ndogo na hasa tukizingatia kwamba kwa kiwango kikubwa tumepunguza pembejeo kutoka kuwahudumia wakulima 999 mpaka kuwahudumia wakulima 300, hapa hatujawatendea haki wakulima wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zimeelekezwa katika maeneo mengine lakini pembejeo zimeshuka sana, sasa tuna ukame ambao umekabili nchi yetu, tulichokuwa tunatakiwa ni kuongeza nguvu kwa yale maeneo ambayo yamepata mvua ili wananchi wale waweze kuzalisha kwa wingi kuweza kufidia maeneo ambayo yalikuwa yamekosa mvua kwa kipindi hiki, ingeweza kuiweka nchi yetu kuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii ya ukosefu wa mvua bado katika Ukanda wetu wote wa SADC unazikabili nchi zote hizi na ukosefu wa mvua.
Kwa hiyo, ukame utaendelea na ukosefu wa chakula utaendelea. Nchi pekee wanayoitegemea ni Tanzania, Tanzania yenyewe uzalishaji wake umekuwa wa kusuasua, tunakimbilia wapi, hapo ndipo pa kujiuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba bajeti ijayo tukubaliane Waheshimiwa Wabunge tuhakikishe kuna maeneo lazima yawe ya kipaumbele na tuhakikishe Serikali inasikiliza kilio chetu. Tulipendekeza kwa nguvu zote kwamba bajeti ya pembejeo ipande tukapendekeza fedha wapewe NFRA waweze kununua chakula kwa msimu uliokuwepo, NFRA hawanunui chakula wanangoja bajeti ya Serikali, chakula wananunua walanguzi na watu wengine wakianza kununua wao bei zimeshapanda.
Kwa hiyo, tuwatake NFRA wanunue chakula mwezi wa tano kwa yale maeneo yenye uzalishaji ili kuwepo na chakula cha akiba kujihami kwa hali ambayo inaweza kujitokeza huko mbele tunapokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kusisitiza ni kwamba nchi hii hakuna kitu ambacho kimeonesha mwelekeo mzuri kama Mfuko wa Maji na tozo ya shilingi 50, tuliishauri Serikali msimu uliopita kwenye bajeti ipandishwe iwe shilingi 100, leo hii miradi yote iliyofanyika inaonekana katika Majimbo yetu ni kwa shilingi 50 ambayo imeweza kutengeneza zaidi ya bilioni 75 ambazo zimekwenda katika maeneo yetu mbalimbali. Kwa hiyo, nitoe wito wa Waheshimiwa Wabunge, bajeti ijayo tuiombe Serikali hiki kilio itusikie, ipandishe hadi shilingi 100 ambapo tutakuwa na uhakika kwa mwaka zaidi ya shilingi bilioni 300 na miradi yote ya maji itaweza kufanya kazi au itaweza kumalizika kwa wakati pasi na kutegemea tu pesa kutoka Serikalini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba fedha zaidi ziangaliwe maeneo ya utafiti, Tanzania tuna matatizo ya kupata mbegu ambazo zinatumika katika maeneo yetu, asilimia 70 sasa hivi ya mbegu tunaagiza nchi za nje. Tatizo kubwa ni zile tozo za wale watafiti au wale wazalishaji mbegu wa hapa nchini, lakini ukizalisha mbegu nchi za nje au nje ya Tanzania unakuwa na duty free. Hivyo, makampuni ya uzalishaji mbegu yamekimbilia Zambia, Malawi, Zimbabwe, yanazalisha halafu yanaleta Tanzania kwa sababu kuingiza Tanzania ni bure. Kwa hiyo, kitendo hiki kinawavunja moyo watafiti, kinavunja moyo makampuni ya uzalishaji mbegu, hivyo basi kila mmoja anaona bora akazalishe nje au aende akanunue mbegu Belgium na afunge Tanzania halafu auze ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kinacholeta athari zaidi ni baadhi ya mbegu zinazotoka katika nchi hizo hazifanyiwi uchunguzi, matokeo yake zinaleta athari za maradhi kwa watu mbalimbali na hasa kwenye ugonjwa wa kansa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine linaloleta athari hapa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Rehani.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kazi za Ubaharia wa Shirika la Kazi Duniani na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Vitambulisho vya Mabaharia Na. 185 wa Mwaka 2003 wa Shirika la Kazi Duniani
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata muda huu wa kuchangia kwenye mawasilisho haya. Kwanza nipongeze kuletwa huu Mkataba ambao utaweza kusaidia kurekebisha kasoro nyingi zinazotokea kwenye sekta hii ya marine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujielekeza hasa kwenye mambo machache kwa sababu ya muda, hasa suala zima la Mabaharia ambao wanasafiri na vyombo ambavyo vya kuchukulia hasa mizigo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara na vile vingine vinaenda Mafia na vingine vinaenda mpaka Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mabaharia hawa hawana mikataba rasmi, lakini vyombo vile vinakaguliwa na SUMATRA, vinapewa leseni ya kusafirisha mizigo, lakini uhalali wa ufanyajikazi wao katika zile meli haupo. Mtu unaweza kuingia leo kazini kesho ukasimamishwa, ukakoseshwa mshahara na mambo mengine ambayo hayastahiki kufanyiwa wafanyakazi hasa wa meli.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile suala zima la vyombo ambavyo vinasafirisha abiria hasa katika bandari zile ndogo ndogo mfano Mkokotoni kuja Tanga, Kipumbwi nao vilevile wale Mabaharia wanaofanya kazi ndani ya vyombo vile zile fiber, boti ndogo ndogo hakuna mikataba ya ufanyaji kazi katika meli zile au boti zile ambazo zinakwenda katika maeneo yale. Linapotokezea lolote Baharia yule anakuwa hatambuliki, anayetambulika pale ni mwenye chombo au Nahodha kwa kiasi kidogo sana. Naomba vilevile hili Waziri aje atupe maelezo hatua gani SUMATRA itazichukua kudhibiti hali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwenye hili ni suala zima la wanafunzi ambao wanasoma katika Chuo cha Marine kile kilichopo Dar es Salaam, wanafunzi wale wanapata nafasi ya kwenda kufanya kazi katika meli za nje, lakini ikifika muda kutaka kuja ku-renew zile leseni zao, pale kwenye kile chuo wanatakiwa wasome tena...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba hii ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa taarifa yake na hotuba yake ya bajeti hii ambapo angalau tunaona mwelekeo kidogo ukisimamiwa mambo yataweza kwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile niwashukuru Mawaziri ambao wamo ndani ya Wizara hii Ofisi ya Waziri Mkuu, swahiba yangu pale dada Mheshimiwa Jenista, lakini vilevile na kaka Mheshimiwa Mavunde kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujielekeza kwenye mambo matatu makubwa ambayo nahisi kama nchi tunaweza tukaleta mabadiliko. La mwanzo niombe ofisi yako na tuiombe Wizara ya Kilimo na Serikali kwa ujumla ili nchi hii kuinusuru na janga kubwa la njaa ambalo linatokea katika maeneo mbalimbali ambalo hasa linasababishwa na tatizo la hali ya hewa lazima tuwe na kilimo cha umwagiliaji maji, hatuna njia ya mkato. Mataifa yote ya wenzetu wengine mkakati uliokuwepo ni kuwa na kilimo cha umwagiliaji maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Novemba mwaka jana tulishiriki kwenye Agriculture Council ya SADC nchi zote zinazotuzunguka tamko lao limejielekeza kwenye umwagiliaji maji. Napenda kutoa rai tufanyaje katika hili ili tuweze kupata mlango wa kutokea. Niombe Serikali kwa ujumla iridhie kuufufua Mfuko wa Umwagiliaji Maji uwe unachangiwa kama inavyochangiwa mifuko mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfuko huu ni muhimu na ndiyo dawa ya kuweza kukomboka na kuwa na miundombinu ya umwagiliaji maji. Hesabu ya haraka haraka kama tutakuwa na wachangiaji wa shilingi 50 tu, tukiwa na wapiga simu au wamiliki wa simu milioni 20 ambao kwa Tanzania tunafika idadi hiyo, pesa ile kwa mitandao mitano iliyokuweko ndani ya nchi tunaweza kuwa na zaidi ya shilingi bilioni 144. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi tunaweza kuwa na maeneo maalum ya kimkakati na mazao ya kimkakati, kila eneo tukaweza kuchimba visima vinane, tukaweza kuwa na zaidi ya hekta 1200, tayari tuna uhakika wa reserve ya tani 300,000 za chakula kwa mwaka. Hivyo, tishio la NFRA na mazao yale mchanganyiko ya kusema tutanunua wapi chakula, wale watanunua kwa hawa ambao wamewekeza kwenye umwagiliaji maji hivyo Taifa litakuwa na uhakika wa akiba ya chakula na tatizo kubwa la njaa litakuwa halipo katika maeneo yetu, hiyo ni rai yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka kumuomba Waziri Mkuu, kazi nzuri aliyoifanya kwenye Bodi ya Korosho ahamishie kazi ile kwenye bodi nyingine za Wizara ya Kilimo. Kuna matatizo na hakuendi vizuri kwenye Bodi ya Pamba, kuna matatizo na hakuendi vizuri kwenye Bodi ya Kahawa, kuna matatizo kwenye Bodi ya Chai, chai kama kaachiwa limekuwa shamba la bibi tu hamna anayemuuliza mtu. Tulikuwa na Bodi ya Pareto, leo hii tumeanzisha vilevile Bodi
ya Maziwa, bodi hizi zinatakiwa zipitiwe, zifuatiliwe, utendaji wao wa kazi ujulikane lakini vilevile yale makato wanayowakata lazima yajulikane yanatumika vipi. Hali ilivyo sasa hivi kama hakuna anayesimamia bodi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Waziri Mkuu mkakati zaidi ulioufanya kwenye Bodi ya Korosho ambapo umewakomboa wakulima na wamerudisha imani wakulima wa korosho tuhamishie kwenye bodi nyingine hizi ili kurejesha imani ya wakulima wa kahawa ambao wengi
wao wameacha kulima kahawa kutokana na makato na mazingira mabaya yaliyokuweko kwenye kahawa. Hali kadhalika, tuangalie pamba inakuwaje, chai inakuwaje lakini tusisahau na pareto vilevile. Tulikuwa ba Bodi ya Pareto ambayo sasa hivi hata haizungumzwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala kubwa linalotukabili kwenye kilimo ni kutokutilia maanani suala zima la upatikanaji wa pembejeo. Kilimo bila pembejeo hatuna kilimo, ardhi yetu tumeshaitumia imechoka. Serikali kadri tunavyoishauri kuhusiana na pembejeo linaonekana suala lile kwamba ni jepesi na halina uzito wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka juzi nchi ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 250 kwa ajili ya pembejeo, zikapatikana zaidi ya shilingi bilioni 120, mwaka jana tumekwenda na shilingi bilioni 20, hali imekuwa tete. Tumetoka kwenye wakulima waliopewa ruzuku ya pembejeo 99,000 sasa hivi tumekuja kwenye wakulima karibu 350, hali ni ngumu. Niiombe Serikali hili suala iliangalie kwa jicho la maana, bila pembejeo utazalishaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito wangu kwamba, Kamati ya Bajeti na Wizara ya Fedha hili jambo iliangalie kwa jicho la huruma. Wakulima hawa wana nia ya kuzalisha, pamoja na ukata na hali ngumu ya hali ya hewa lakini ukosefu wa pembejeo nao vilevile unachangia kudumaza
maendeleo yao. Hili tulitilie maanani na tuweze kuwasaidia wakulima katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuzungumza ni la mifugo. Nikushukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu umeshughulikia vizuri suala zima la mifugo hasa maeneo ya Loliondo. Wafugaji wale wa Loliondo bila Kamati ile wangefikia pabaya, sasa hivi wangekuwa wameshafukuzwa na hawaelewi pa kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, wale wafugaji kule wako zaidi ya 64,000 ukiwaondoa pale wana ng’ombe zaidi ya 500,000 wale wanakwenda maeneo ya Morogoro na wanakwenda maeneo ya Kusini kitu ambacho kinakwenda kuchochea machafuko baina ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu, suala hili tuweze kuli-handle vizuri kwa sababu bado Wamasai wale wana uwezo wa kufuga ng’ombe na wakatunza zile rasilimali zilizokuwapo pale za hifadhi bila kuathiri na maisha yakaweza kuendelea baina ya wanyama wa porini na wanyama wa kufugwa. Wito wangu, Kamati iendelee na uchunguzi na mkakati wake, lakini ifike mahali uwekwe utaratibu mzuri wa kufuga pasiwe na wazo la kuwafukuza watu wale. Kwa sababu kuondoka kwao sio kama watachinja wale ng’ombe wao, watahama maeneo na
hivyo tutaongeza tatizo la ugomvi baina ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia Bodi ya Maziwa. Bodi hii ina malengo mazuri, imesema mwaka huu inataka kuimarisha ng’ombe wa maziwa angalau wafike milioni moja na laki tano. Ushauri wangu tuanzishe cowshed au vijiji vya ufugaji ili kuweza kuwapelekea huduma hawa wafugaji ambao watapewa hawa ng’ombe wa maziwa. Tutakapoanzisha cowshed hizi itakuwa rahisi kuweza kuwapelekea elimu ya ugani kwa wale wafugaji ambao
wataanzisha mabanda haya kwa pamoja lakini vilevile tutaweza kuweka zile collection centre. Bado Tanzania inaathirika na maziwa ambayo yanatoka nje, ni aibu jamani! Tanzania hatuna kiwanda cha maziwa ya unga tunashindwa na Zimbabwe walau wana kiwanda cha maziwa ya unga. Tatizo letu ni kwamba maziwa yetu hayana viwango na ng’ombe tulionao hawana uwezo wa kutoa maziwa ya kutosha tukaweza kuanzisha hivyo viwanda tulivyokusudia. Kwa hiyo, kama hatukujipanga kuweza kusambaza ng’ombe wa kutosha katika nchi hii… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nashukuru kwa kupata nafasi hii adhimu ili niweze kuchangia katika taarifa hii ya bajeti ya Wizara ya Habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kasi aliyoanza nayo katika Wizara hii na kuonesha nia kweli kuleta mabadiliko yaliyoachwa na mtangulia wake kwa Wizara hii ya Habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo nataka nitoe shukrani ya dhati kabisa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha Zanzibar kuweza kupata nafasi ya kuwa mwanachama wa CUF au Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CUF), nafasi ambayo ilikuwa imetafutwa kwa miaka mingi na kilio kikubwa kwa Wazanzibari kuweza kupata nafasi hiyo, nao kushiriki kama nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupata nafasi hiyo, bado naomba Wizara hii kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania TFF na kile cha Zanzibar ZFA kuendelea na jitihada hizo katika kutafuta nafasi ya FIFA ili nayo iwe mwanachama kama ilivyo Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nilichokuwa nakiomba, ushirikiano uliokuwepo baina ya ZFA, TFF na Wizara zetu mbili hizi za Michezo za Tanzania Bara na ile ya Zanzibar uweze kuendelezwa katika mtazamo wa kuisaidia Zanzibar au ZFA ili nayo timu zake zinazoshiriki katika mashindano hayo ya Afrika ziweze kuwa na nguvu, kwani kwa hivi sasa timu nyingi zilizokuweko kule Zanzibar, kwa mfano, ndani ya Jimbo langu nina zaidi ya timu 60, lakini nina wachezaji ambao tumechukua Tanzania Bara wanaweza kufika hata 300. Kwa hiyo hii fursa ya ushirikiano huu iliyokuwa imepatikana isikatikatishwe kwa vile Zanzibar sasa hivi imepata kuwa mwanachama wa CUF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninachotaka nikione kwamba kinaendelezwa ni suala zima la michezo hasa kwa vijana wadogo. Tuna mashindano ya Coca Cola na kuna mashindano mengine mbalimbali ya NSSF ambayo yanashirikisha timu kutoka Zanzibar na hizi Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli timu hizi au mashindano haya yanaleta chachu ya ushindani na kuibua vipaji vingi vya wachezaji mbalimbali kuonekana wale wa Zanzibar wanapata nafasi ya kuja kucheza timu za Tanzania Bara, lakini na wale wa Bara wanapata nafasi ya kuja kucheza kule Zanzibar. Naomba fursa hii iweze kusimamiwa na Wizara na kuwe na mashindano ya ushindani kweli ambayo yataweza kuwanufaisha pande zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumza ni programu zima ya kuendeleza vijana wetu. Zanzibar miaka ijayo tunategemea nasi kuanza maandalizi ya vijana kwa ajili ya AFCON kama ilivyo Serengeti Boys, mkakati ambao unatakiwa uungwe mkono pande zote mbili na kuwe na programu za kushirikiana ambazo zitaziwezesha kuwa na timu ambayo itaweza kufanya vizuri na kupata nafasi kama ilivyopata nafasi Serengeti Boys.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi hizi zinataka ziungwe mkono na wanachama wote, Wabunge, wadau mbalimbali wa ndani na nje ili leo hii tuione kwamba Serengeti Boys inavuka hapa tulipo na inatimiza lengo ambalo ilikuwa imetuahidi na iliyomwahidi Makamu wa Rais kwamba safari hii italeta kombe la Afrika la Vijana Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri akae na mwenzie, Mheshimiwa Waziri yule wa Zanzibar waangalie mkakati ukoje, kwa miaka mingine mitatu ijayo timu zetu hizi tutaweza kuziinua na kutengeneza timu ambazo zitaweza kuonesha ushindani na kupandisha kiwango cha mpira hapa Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi hapa tarehe mosi kulikuwa na maadhimisho ya siku ya habari ambayo yalifanyika kule Mwanza. Waziri alitoa kauli kali kidogo, nami kama mdau wa habari vilevile niliguswa na ile kauli. Sasa sijui iko vipi? Kauli ambayo ilipiga marufuku uchambuzi wa magazeti katika vyombo vyetu vya habari. Sasa tunauliza; Mheshimiwa Waziri, siyo Watanzania wote ambao wanaweza kuwa na uwezo wa kununua gazeti, lakini siyo Mtanzania yeyote anaweza kufikishiwa magazeti haya. Leo tutakapopiga marufuku uchambuzi ule wa habari, wengi wao tumewanyima haki ya kupata habari Watanzania. Kwa sababu Magazeti yale au uchambuzi ule wengi wetu tulikuwa tunasikiliza kupitia redio, kwa hiyo, hata vile wengine kununua…

T A A R I F A...

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nimeipokea hiyo taarifa. Naomba kuisherehesha. Fursa hii ya uchambuzi wa magazeti ndiyo sauti ya Watanzania wengi, inaweza kuwaambia kwamba ndani ya dunia hii au ndani ya Tanzania hii kuna taarifa hizi, hizi na hizi kwa leo; na kesho kuna taarifa hizi na hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aweze kulitathimini agizo lake hili, kwa kweli linawakosesha fursa kubwa Watanzania kupata habari ambazo zinapita katika vyombo vyetu vya habari hivi hasa asubuhi kwa uchambuzi wa magazeti mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mwenzetu alivyosema, kundi hilo la wasioona na kuna makundi mengine mengi tu ambao uwezo wa kununua gazeti hawana, lakini wanazihitaji taarifa. Hili lipitiwe tena upya na Mheshimiwa Waziri atoe kauli ili kuweza kuwapa fursa Watanzania kupata habari kama walivyokuwa wanapata habari hivi sasa. Nitamsikiliza kwenye majibu yake ili tuone kitu gani ambacho ataweza kutuambia Watanzania katika hili eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kuzungumza suala zima la Wasanii. Tanzania hii wanapozungumzwa Wasanii wanadhaniwa kwamba ni Wanamuziki na wale watu wa Filamu; lakini kuna kundi kubwa la wafinyanzi, wachongaji, waandishi wa vitabu mbalimbali, sijaona jicho la Mheshimiwa Waziri au Wizara yake kuweza kuangalia kundi hili na vipi wanavyoweza kuwasaidia kuinua vipaji vyao, lakini watu hawa wanaitangaza Tanzania katika Sanaa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kisiwa cha Brunei ni mteja mkubwa wa bidhaa za vinyago ambazo zinachongwa Tanzania. Taarifa nilizonazo, kwa miaka mitano iliyopita wamenunua bidhaa hizi zaidi ya Dola milioni 600, zinanunuliwa katika maeneo mbalimbali na yeye kule wameweka ma-shop mall ya vinyago hivi ambavyo vinachongwa katika maeneo yetu mbalimbali.

Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, eneo hili nalo jicho lake liweze kuelekea. Wakurugenzi au Wizara iwe na mpango maalum wa kuwatambua kwanza, lakini siyo kuwatambua tu kama ilivyokuwa wanatambuliwa wanamuziki ambao mpaka leo hawana walichokipa kutokana na mirahaba inayopatikana waweze kupewa support na Serikali na zile bidhaa zao zitangaze utalii wa nchi yetu na sanaa iliyokuwepo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba BASATA, bado haijafanya kazi ya kuwasaidia wanamuziki na wacheza filamu wa Tanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nachukua fursa hii kwanza kupata nafasi hii. Niishukuru Wizara kwa kuwasilisha bajeti hii ya mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa haraka haraka nilitaka kuzungumza mambo mawili, moja, suala zima la bajeti. Ni kweli bajeti imeshuka lakini bajeti iliyokuwepo ndio uhalisia. Si vema kuwa na bajeti kubwa isiyoweza kufikia malengo, ni vema kuwa na bajeti ambayo kweli tutaweza kuisimamia na kuweza kupata kile ambacho tulichokuwa tumekikusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niungane na wenzangu wote kuitaka Serikali kwamba suala la shilingi 100 katika Mfuko wa Maji hili si la kuweka kigugumizi, kwa sababu imekuwa ni kila siku, suala hili limezungumzwa sana mwaka wa jana. Kama fedha hizi zingelipatikana tungelikuwa na zaidi ya shilingi bilioni mia tatu na sitini kwa mwaka na miradi mingi ingeweza kutekelezeka mbali na kutegemea fedha kutoka Serikalini moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti ,kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuungane, kwa hili suala la shilingi 100 kama Serikali haitakubali kuongeza basi tuchukue hatua zinazofaa; kwa sababu Serikali haliigharimu chochote, Serikali ni kukubali tu shilingi 100 zikatwe kwenye mafuta, haina gharama yoyote. Niiombe sana Serikali hapa ilizingatie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili tunakabiliwa na changamoto kubwa ya uzalishaji wa mazao mbalimbali kupitia kilimo cha irrigation. Kwenye eneo la irrigation fedha hazikwenda kabisa. Tuna miradi mingi na maeneo mengi ya Tanzania tunahitaji tuweze kuwa na kilimo cha umwagiliaji maji. Mimi langu ni kutoa rai kwa Serikali na Wizara hii na hasa Makatibu Wakuu na Kamisheni ya Umwagliaji Maji tuzingatie rai nitakayoitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo langu mimi nilisema tokea kipindi kile cha nyuma kwamba Mfuko wa Umwagiiaji Maji ufufuliwe. Upo siku nyingi lakini hauna fedha hata shilingi, hautengewi fedha. Nilitoa wazo kwamba fedha hizi sisi tunaweza kuzipata kupitia mashirika ya simu. Tukatoa tu kiwango cha watu milioni 20 ambao wanamiliki simu hapa Tanzania wakikatwa shilingi 100 tu kila muamala wa shilingi 1,000 kwa siku 30 tu unazalisha zaidi shilingi bilioni 600.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi tayari unaweza kutengeneza zaidi ya hekta 2400; hekta ambazo zitaweza kukuzalishia zaidi ya tani 330,060 kwa mwaka kama wakulima wataweza kulima mara mbili, kiwango ambacho kwa kweli ni full security ya nchi hii. Lakini ni chanzo cha uzalishaji wa viwanda mbalimbali katika nchi yetu. Tatizo letu liko wapi? Wenzetu wengine wametoa mawazo hapa wamesema watu wanakunywa bia kwa wingi, kwa nini tusikate shilingi 100 au shilingi 200 tukaweza kufufua huu mfuko na tukaweza kupunguza matatizo ya ukame na ukosefu wa maji katika maeneo yetu mbalimbali kwenye uzalishaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali tuzingatie haya, mengine tutakuwa tunapiga tu blabla kwa kusema kwamba tupate fedha moja kwa moja kutoka Serikali kuingizwa kwenye umwagiliaji maji si rahisi. Tuangalie Mifuko ya NSSF, PPF na mashirika mengine tukate kiwango kidogo kidogo. Mimi nimetoa mfano mdogo kwa siku 30 tu watu wangapi wanatumia shilingi 1,000 kwa miamala ya simu?

Tukifanya miezi sita nchi yote hii tumeifanya kuwa umwagialiji maji na tutakuwa na uhakika wa uzalishaji wa chakula nchini mwetu na ile dhana nzima ya Tanzania ya viwanda itatimia kupitia huko. Nafikiri tufunue mawazo tuangalie kwa upana zaidi kuliko hali ilivyo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nilichokuwa nimekiomba ni kwamba Serikali iangalie maeneo yale kame zaidi. Wazo la kuwasaidia hasa wafugaji katika maeneo mbalimbali kuepusha ile wanaita migration, movement ya wanyama kutoka eneo moja kwenda lingine kwa ukosefu wa maji. Suala la ujengaji wa mabwawa katika maeneo mbalimbali ndilo mkombozi wa suala hili, na litaunguza sana migogoro ya wafugaji na... (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Rehani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Vilevile niungane na wenzangu wale ambao walimpongeza ndugu yetu Sugu kwa kuweza kurudi hapa Bungeni, baada ya kutoka kifungoni kule Mbeya. Pia tumshukuru Rais kwa kuliona hilo na kuweza kuleta tafifu ya kumrudisha hapa na leo tunaye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nataka kusema kwa haraka haraka kulingana na muda suala la kwanza, Tanzania ndani ya tasinia ya Afrika mashariki. Kila tunapokwenda bado hakujawa na mikakati chanya ya kuweza kukabiliana na ushindani iwe wa uchumi, elimu, hata utamaduni. Tunahitaji Wizara ieleze kwa undani ni mikakati gani ambayo itaweze kutufanya sisi kama nchi kuweza kukabiliana na tasinia ya ushindani ndani ya East Africa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona wenzetu kila siku wanafungua fursa nyingi za kiuchumi katika maeneo yao, lakini bado pamoja na harakati ya miradi ambayo iliyoko ndani ya nchi ya Tanzania haionyeshi competitive advantage ya kuweza kushindana na wenzetu ambao wako katika maeneo yetu wakati sisi tuna rasilimali nyingi ambazo zinaweza kutupaisha haraka zaidi kuliko wao. Kwa hiyo, nimwombe Waziri aje atupe maelezo hapa mkakati gani tunao ndani ya utengamano huu wa East Africa, kukabiliana na ushindani wa kibiashara, ushindani wa kielimu lakini vilevile na kiutamaduni baina ya nchi zetu hizi sita zilizo katika mtengamano huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nataka kulizungumza ni suala zima la Balozi zetu zilizo nchi za nje. Bado uwezo wa Mabalozi kuona output katika nchi hii ni mdogo. Tegemeo la kupewa post hizi hawa Mabalozi tunategemea waitangaze hii nchi kwa vivutio mbalimbali vya kiuchumi, kiutamaduni na teknolojia vilivyoko ndani ya nchi hii. Hata hivyo, tumeona tu wenzetu Wafaransa juzi balozi amechangamka na kuweza kuleta delegation hapa ya Wafaransa kuja kuangalia fursa za uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, na sisi Tanzania tunahitaji kuona tunatoa delegation mbalimbali zinakwenda katika nchi mbalimbali kuangalia fursa. Siyo hao tu wafanyabiashara hata nao Wabunge pia wapewe fursa za kwenda nje kuangalia fursa mbalimbali za kiuchumi, kiutamaduni na teknolojia ili waweze kuisemea nchi hii na kuleta matunda ambayo yataweza kuisaidia hii nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna vitu vingi ambavyo tunaweza kufanya uwekezaji, lakini tuna miradi mingi ya kimkakati ambayo inaweza kuitoa nchi hii, lakini tunasema miradi hii tumeifungasha sisi wenyewe tu. Wazo langu tuitoe, tuitangaze kama tunaanzisha mradi mkubwa wa Stiegler’s Gorge, tuutangaze duniani utapata support, watu wanahitaji kuuona na kuujua, ziletwe ripoti za hii miradi ili tuweze kuona miradi hii inapata ufadhili, lakini vilevile inapata…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi kupata fursa hii adhimu. Kwanza niunge mkono hoja hii ya kuanzisha Commission hii ya Bonde la Mto Songwe ambayo kimsingi, the highly potential area kwa nchi yetu, kwa uchumi wa nchi hii, lakini vilevile kwa mustakabali wa wananchi wale wa Wilaya zile tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba mimi kwa bahati nzuri nimeusoma huu mkataba vizuri na nimeuelewa madhumuni yake. Ikiwa dhumuni kubwa ni kuhifadhi, kuendeleza na kuondoa athari za maji ambayo yanasababisha mto ule uweze kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine na tishio la athari ya wananchi ambao wanakaa pembezoni mwa mto ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, fursa hasa za kuangalia kitu gani ambacho kitaweza kutusaidia kama nchi, eneo lile la Mto Songwe kwa Tanzania ni belt ya uzalishaji wa mazao mbalimbali. Kinachotakiwa baada ya kuridhiwa Kamisheni hii; Kamisheni itengeneze mpango mkakati ambao utaweza kuridhiwa na pande zote mbili kwa sababu yale yote yaliyoainishwa katika Kamisheni hii, kila mmoja yanamgusa hasa kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango mkubwa pale wa kuanzisha mabwawa matatu yale ya Songwe Juu, Songwe Kati na Songwe Chini, kwa kweli kwa Tanzania ni fursa kubwa kwanza kwa upatikanaji wa maji hasa ya mvua. Ile dhana ya rainfall harvesting pale ndipo itakapotimia. Tutakapoweza kuyavuna yale maji, tutaweza kuu-shape ule mto uweze kwenda kwa mujibu wa mwelekeo tunaoutaka sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mto ule unafungua uwanja mpana wa kuanzisha maeneo ya umwagiliaji maji kwa eneo lile la Kyela. Tutaweza kuzalisha mpunga kwa kutumia yale mabwawa kama wanavyozalisha Moshi Chini na Moshi Juu. Tufanye uwekezaji wa maana ili nchi ionekane kwamba kuanzisha ile Kamisheni imeleta manufaa na isiwe Kamisheni tu kama nyingine ambazo baada ya miaka mitano, kumi tukija kutathmini, hakuna kilichofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Mawaziri watakaosimamia, pawe na uwekezaji ambao utaleta fursa kwa kila sekta. Tukizungumza Sekta ya Kilimo, zaidi ya hekta 15,000 pale tunaweza kuzifanya zote kuwa za umwagiliaji maji na zikaweza kutuzalishia zaidi ya tani laki tatu za mchele. Hilo linawezekana, suala ni kujipanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika eneo lile kuna mazao ya biashara, kuna ndizi ambalo ni zao kubwa katika maeneo yale ya Tukuyu na Kyela. Fursa ya uzalishaji kwa kutumia irrigation ipo, kutumia mabwawa yatakayoanzishwa kule. Tuhamasishe wananchi wajipange kwenye uzalishaji wa tija kuliko uzalishaji wa kutegemea mvua ambao hauna uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo yale, bado unaweza kuzalisha mahindi kwa mpango maalum na nchi ikaweza kunufaika na kuondokana na tishio la njaa linalotokana na ukosefu wa maji wa kila siku. Isitoshe, kazi kubwa inayotaka kufanywa pale ni kuhifadhi mazingira ya vyanzo vya mto ule toka vinavyotokea huko kwenye zile chemchemi za kutilia maji katika eneo lile, kwa sababu maji katika eneo lile ni mwaka mzima. Hiyo siyo kwamba yanavunwa yale ya mvua, lakini maji yanatoka kwenye chemchemi ambazo ziko katika maeneo mbalimbali na ndiyo maana tunapata fursa na nguvu ya kuanzisha yale mabwawa ya kuzalisha umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale panategemewa kuzalishwa umeme zaidi ya megawati 180, kitu ambacho tunafikiria tu kwamba mgawanyo uwe nusu kwa nusu. Nasema, bwana, kila mwamba ngoma huvutia kwake vilevile. Asilimia kubwa ya ule mto na eneo kubwa ni letu siye, lakini na zile infrastructure ambazo zinahitajika kujengwa katika eneo lile ziko kwetu. Nafikiri hao watakaoenda kukaa; Mawaziri na watu wengine, waangalie uwiano wa kugawana na siyo tu kwa kujenga mahusiano ya kusema kwamba tunaridhiana nusu kwa nusu, hapo tupaangalie kwa undani zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nitachangia katika hii Kamisheni ni uanzishwaji wa viwanda. Tuhamasishe maeneo yale ambayo yanazalisha kokoa katika maeneo mbalimbali ya Kyela, basi kuwepo na kiwanda ambacho kitaweza kuzalisha Chocolate na vitu vingine kuanzishia wananchi wetu ajira na fursa nyingine mbalimbali za kiuchumi zitakazokuwepo kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo vilevile inafungua corridor ile kuweza kuwa na mpango wa kujengwa reli kutoka huko Mchuchuma mpaka Lindi lakini ikaunganisha mpaka kwenye reli ya TAZARA. Itazidi kufungua fursa kubwa za kiuchumi na kulifanya eneo lile kuwa moja katika eneo, wanaita economic zone. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili kwa nchi yetu limekuwa likitumika isivyo na faida; yaani likitumika kikawaida. Hii sauti ya kuanzisha Kamisheni ilianza miaka mingi, lakini tushukuru Mungu sasa hivi Serikali imefika mahali pa uamuzi wa kuianzisha na kuanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wataalam mbalimbali wa Wizara zote zinazohusika na Kamisheni hii kukaa na kuanzisha miradi ambayo itaweza kuwasaidia wananchi kushiriki nao hasa kwenye uhifadhi wa mazingira ya eneo lile, kwa sababu kila eneo mto unapopita mazingira yanakuwa ni mazuri, lakini kutokana na kazi na shughuli za kibinadamu, mazingira yale yanaharibiwa kwa njia moja au nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu niombe hasa Wizara ya Kilimo kupitia mifugo, eneo hili lilindwe na lisiingizwe mifugo. Tutalimaliza! Tutauua ule mto na matokeo yake maji yale yatashindwa kutiririka kama yanavyotiririka hivi sasa. Haya ni mambo ya msingi. Tunaweza kuanzisha mambo mazuri, lakini kuna lingine tukalisahau ambalo linaathiri mazingira ya pale. Kwa hiyo, nawaomba sana wahusika wa Mikoa, Wilaya na maeneo mengine kuweza kuepuka uingizwaji wa ngombe wengi katika maeneo yale pale ambayo yanatumika kwa kilimo sasa hivi kikubwa. Kule Zanzibar wanasema mchele wote unaoletwa kutoka Mbeya ndio wenye soko kubwa. Kwa hiyo, nawaomba wazalishaji na viongozi walioko katika maeneo yale tuweze kutilia mkazo sana uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nimeliona kwamba ni fursa kubwa, zile meli za bandari za Itui, Itumbi na sehemu nyingine, pale sitaweza kufanya kazi vizuri zaidi, kwa sababu ufungukaji wa ile Kamisheni itaanzisha fursa kubwa ya wafanyabiashara, lakini na wenzetu wa Malawi watapata fursa kubwa ya kuleta mizigo yao katika maeneo yale na hasa kwa kutumia ile meli mpya iliyoundwa hivi sasa iliyokuwa inaanza kazi kuwa na manufaa zaidi kuliko vile ambavyo tulivyokuwa tumetegemea.
Itifaki ya Nagoya ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo Sahihi wa Faida zitokanazo na Matumizi ya Rasilimali za Kijenetiki.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi nashukuru kuweza kupata nafasi hii, ninakushukuru kwa kuweza kupewa haya makabrasha na maazimio haya yote matatu wakati mmoja kuweza kuyapitisha, tatizo moja tu lililokuwepo kwamba uelewa wa Wabunge wengi katika haya Maazimio ndiyo kitu kidogo kinachoonekana ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina-declare interest kwamba nimefanya kazi kwenye Marine Conservation kwenye Mradi wa MACEP chini ya World Bank miaka mitatu, naelewa haya maazimio yaliyokuwa yamepita huku nyuma. Lakini nilitaka kutoa ushauri tu sijui kama muda utatosha katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja katika maazimio ambayo yalipendekezwa miaka mingi kwa nchi yetu hii imegeuka dampo la kutupwa takataka nyingi kutoka nchi za nje. Wenzetu Kenya waliridhia mapema, baadae baada ya kuridhia wakawa wanachukua bidhaa kutoka viwandani mwao, zile by products zilizomalizika wanakuja kutupa katika bahari yetu kwa sababu tumeshindwa kuridhia mkataba huu, kwa hiyo shamba hili limekuwa kila mmoja anaweza kutupa na kufanya anavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili katika bahari kuna mambo mengi, moja katika vitu vinavyokuwa disturbed ni bioanuai iliyopo katika bahari. Mazingira yetu ya bahari yanachafuliwa kwa vitu vingi, hali ya hewa inachangia, lakini mtiririsho wa bidhaa za kikemikali kutoka kwenye viwanda umekuwa ni mkubwa na hasa Watanzania wenyewe tunaufanya. (Makofi)

Mheshikiwa Mwenyekiti, tuna viwanda vingi katika belt hii ya bahari ambayo Wahindi na wengineo wanaomiliki viwanda vile wanatiririsha maji ambayo yana sumu na kemikali kutoka kwenye viwanda vyao, hawana mifumo ya kuhifadhi maji machafu na ya kemikali ambayo wanatengeneza bidhaa mbalimbali. Sasa sheria hii au Azimio hili liende likawabane hawa wote wenye viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua wazi kwamba wengi wao wanawahonga wale watu wa mazingira wanaokwenda kufanya impact assessment katika maeneo yao na kusababisha uchafuzi wa mazingira uongezeke. Bahari yetu, beach zetu, kila siku, kila mwaka inaongezeka zaidi ya mita moja, bahari inalika kutokana na destruction ambazo zinafanyika za uchafuzi wa mazingira katika maeneo haya, ninaiomba Serikali hili tuweze kulisimamia. (Makofi)

Mheshikiwa Mwenyekiti, jingine ambalo linachangia, tumeweka uwekezaji wa mahoteli, tumezuwia wenye mahoteli kujenga ndani ya bahari, lakini yapo mahoteli wamejenga migahawa ndani ya bahari kitu ambacho vilevile kinachangia kuharibu fukwe na kuharibu ule uoto wa asili wa bahari uliokuwemo katika maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingi za nje zinatumia eneo lile la bahari kuu kupitisha na kumwaga bidhaa mbalimbali katika maeneo hayo. Mfano mdogo nilionao ni meli nyingi zilizokuwa zimezuiliwa kipindi kile na Al-Shabab zilikaa na bidhaa zile kwa muda mrefu zikiwa zimezuiliwa katika maeneo yao na bidhaa zile zilimwagwa katika ukanda huu wa bahari yetu sisi.

Kwa hiyo, athari iliyotokea samaki wengi waliokuweko katika maeneo yale waliathirika, lakini watu ambao walitumia wale samaki walipata matatizo ya ngozi na wengine walipata matatizo ya cancer. Haya matatizo imekuwa sasa kwetu bila kuridhia mikataba kama hii au maazimio kama haya hatutaweza kuweza kufanya usimamizi wa mazingira yetu. (Makofi)

Mheshikiwa Mwenyekiti, lingine lililokuweko katika nchi pamoja na rasilimali nyingi tulizokuwanazo katika eneo letu lakini hakuna doria ambazo zinakwenda kuangalia kitu gani kinafanyika katika ukanda wa bahari kuu, kitu ambacho kila mmoja ana uwezo wa kufanya anachokitaka, mpaka silaha mbalimbali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Usimamizi wa Mazingira kwa ajili ya Maendeleo Endelevu (The Southern African Development Community SADC – Protocol on Environmental Management for Sustainable Development)
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kunipa nafasi hii niweze kuzungumza kidogo. Na mimi naunga mkono Itifaki hii ya Kigali, lakini napenda kuishauri nchi katika eneo hili kwenye mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, Tanzania tumetangaza kwamba sera yetu ni Uchumi wa Viwanda. Ila moja kati ya vitu ambavyo vinaleta athari ya hizo emission katika ozone layer ni aina ya viwanda ambavyo vinatoa carbonmonoxide kwa kiwango kikubwa. Sasa sijui katika ile blueprint yetu na huo mkakati wa uchumi wa viwanda tumejiandaaje kukabili kiwango kikubwa cha emission ambazo zitakuja kuzalishwa hapa ndani ya nchi, pengine nasi kama Tanzania tukatakiwa tutoe fidia kwa uharibifu wa mazingira ya ozone layer. Sasa hilo natoa angalizo la mwanzo kabisa kwa nchi, tunapokwenda huko tuwe na tahadhari hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, bado ndani ya nchi vile vile hakujawa na mikakati thabiti. Hapo nyuma tuliandaa mpango mkakati unaitwa REDD (Reduce, Emission, Degradation of Deforestation) kwa ajili ya kunusuru emission zote ambazo zinaweza kutokea, iwe kupitia kwenye madawa na kemikali mbalimbali za viwandani, lakini vilevile kwa carbon monoxide ambayo haivunjiki kutokana na miti tuliyonayo kidogo haiwezi kunyonya au kuvuta hewa yote ya carbon monoxide.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine vilevile, ndani ya nchi bado mkakati wa kuwadhibiti watu wenye magari mabovu yanayotoa moshi mwingi njiani na sehemu nyingine haujawekwa na tukaweza kuona kwamba kuna una udhibiti kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi ninaloliona, hata viwanda viwanda vyetu vile vya Wazo, hata ile Songwe vile vya saruji vinatoa moshi mkubwa. Ile ni pure carbon monoxide ambayo kuvunjika kwake kunataka kuweko na emission nyinginezo ambazo zinaweza kusaidia kuvunja. Sisi tumeviacha vile viwanda, hatuvishauri katika mazingira haya tuliyokuwanayo. Kwa hiyo, tunachangia na sisi katika uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wito wangu nafikiri Wizara inahusika, ikae na wahusika, tuweke mpango thabiti sasa ambao utaweza kudhibiti huo uharibifu wa mazingira kwa hilo eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi nashukuru kuweza kupata nafasi hii adhimu ya kuchangia kwenye Mpango huu wa mwelekeo wa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia mpango katika nchi hii lazima uwe na vyanzo ambavyo vitawezesha utekelezaji, lakini vile vile utawezesha upatikanaji wa mapto ya nchi hii; lakini vile vile utaonesha taswira ya mabadiliko ya maendeleo. Mimi sina tatizo na mipango iliyokuwemo kwenye masuala ya miundombinu, iko vizuri na tunakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mpango mkubwa ambao unatazamiwa uweze kuleta mabadiliko chanya katika nchi yetu ni wa uanzishwaji wa viwanda mbalimbali, na hasa hivi ambavyo vimetangazwa na Waheshimiwa Mawaziri katika kila mkoa. Navyo vimejikita kwenye uzalishaji wa kilimo na mazao mbalimbali ambayo tunategemea tuweze kuyachakata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hivi vitabu vyote viwili, mwelekeo na mpango wenyewe uliopo bado kama nchi hatujaonesha mwelekeo thabiti kwenye uzalishaji wetu ukoje. Hakuna projections sahihi ambazo tunalenga kwamba mwaka huu tutaweza kuzalisha mazao kiasi fulani. Kwa baadhi ya mambo tayari tumeshatoa maelekezo na ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tulikuja tukaishauri hapa Wizara ya Kilimo na Serikali ijikite kwenye uanzishaji wa mbegu mpya za pamba. Leo mikoa ya Kusini tumetoa maelekezo na tunatarajia kama kweli wataweza kufanikisha ule mpango tuliokuwa tumewapa wa uzalishaji wa hekta zile zilizokuwa zimeshatengwa, tutaweza kupata mpaka marobota kwenye 600,000; kitu ambacho kwa uzalishaji uliokuwepo nyuma kilikuwa ni ndoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukija kwenye upande wa mazao ya mahindi, bado Serikali haijaweza kusaidia katika eneo hili. Mahindi kwetu ndicho chanzo kikuu cha kila kitu; chakula na viwanda ambavyo vimo ndani ya maeneo yetu. Lakini leo bado nchi haijaweza, kuanzia kwenye mbegu tu ambazo tungeweza kuwapa wakulima wetu wakazalisha katika kiwango ambacho kinastahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takiwimu za kitafi zinaonesha kuwa asilimia 75 ya wakulima Tanzania waliozalisha mazao mbalimbali wanazalisha chini ya asilimia 30 ya mazao ambayo wangetarajia kuyapata ya asilimia 100. Nina maana gani? Maana yangu ni kwamba kwamba kila wakulima 100 kama ingeweza kuzalisha gunia 40; kwa eka moja mkulima huyu uwezo wake anazalisha gunia 12. Sasa hapa bado hatujajipanga, wakulima wanatumia nguvu zaidi mbegu bora haipatikani, mbolea bora haipatikani lakini vile vile na pembejeo za viuatilifu hazipatikani kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatakiwa ijipange itie msukumu zaidi kwenye uzalishaji wa mbegu bora, kwenye uzalishaji wa kuhakikisha kwamba tunazalisha mbolea katika nchi yetu. Lakini vilevile Serikali iweze kuhakikisha kwamba viwanda vile vya viuatilifu vilivyokuwa vimeanzishwa hapa nchini vizalishe viuatilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi nchi inatakiwa iweze kuwa na maono, kuwe na teknoloji ambayo ndiyo itaweza kututoa katika uzalishaji mdogo kwenda kwenye uzalishaji mkubwa hatimaye kupata bidhaa au raw materials kwa ajili ya viwanda tunavyotaria kuvianzisha. Tuna uzalishaji mkubwa wa chai katika maeneo yetu lakini ndani ya masoko ya nje Tanzania ni nchi ambayo inazalisha kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii chai sisi tunazalisha kati ya tani 35,000 lakini wenzetu Kenya wao wako kwenye tani zaidi ya 400,000, lakini hizo 400,000 Tanzania sisi tunachangia kuwapa Kenya bidhaa. Mimi niipongeze Wizara ya Kilimo kwa uwamuzi thabiti wa kuanzisha mnada wa chai ndani ya nchi, na hii itawasidia sana Watanzania kile kidogo cha pesa za nje zinazopatikana ziweze kutumika ndani ya nchi. Ile chai iliyopo maeneo ya Iringa, Mbeya, Njombe na maeneo mengine kule Arusha na sehemu nyingine itaweza kusaidia sasa kuanzisha soko la minada ya chai kama tunavyofanya kwenye minada ya kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo kama nchi tutaweza kuwashawishi wenzetu wa Malawi, Waburundi Warwanda kuunga katika huu mnada ambao tuliokuwa nao hapa hivyo kuhakikisha kwamba tunapandisha bei ya chai kutoka shilingi 600 kwenda kwenye 1000 na zaidi. Wito wangu ni kwamba Serikali ijikite kwenye vile vyanzo ambavyo tutaweza kuongeza mapato zaidi kuliko kuangali kwenye mambo ya miundombinu tu peke yake. (Makofi)

Kuhusu mifugo, Tanzania tunazaidi ya ng’ombe milioni 28 lakini kwa kweli katika uzalishaji wa maziwa hatumo kwenye ramani ya uzalishaji wa maziwa; tunazalisha watani wa lita milioni mbili tu ambazo vile vile hazina takwimu sahihi. Lakini Tanzania nchi moja ambayo inaagiza maziwa mpaka kutoka Zimbabwe, hii kwa kweli ni aibu. Kitu gani tunachoweza kushindwa kukifanya ndani ya nchi hii kuweza kukauka maziwa na kutengeneza maziwa ya unga? Tukichukua hao indigenous breed tuliokuwa nao hatoi lita moja moja tu kwa ng’ombe milioni nane , lita milioni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi yangu. Nami nashukuru kupata fursa ya kuchangia kwenye bajeti hii kuu nikiwa nataka kujielekeza kwenye mambo manne ambayo nahisi yanaweza kuisaidia Serikali lakini kumsaidia Waziri sasa kuweza kujipanga zaidi katika kuhakikisha anapata mapato ya kutosha kutokana na vyanzo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwanzo ninalotaka kuzungumza ni suala zima la bandari bubu na magendo yanayofanyika kwa bandari zetu kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara. Biashara kubwa inayofanyika hapa ni mafuta ya kupikia. Hii biashara imekuwa ni kubwa na kama nchi hakujawa na utaratibu mzuri wa kudhibiti hizi bandari lakini kudhibiti zile bidhaa zinazoingia pale Zanzibar na kutawanywa katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara hii inafanyika kupitia bandari ndogo ndogo mbalimbali na kushushwa katika bandari ndogo ndogo hapa Dar es Salaam na bidhaa nyingi zinazosafirishwa ni mchele, mafuta, sukari, mafriji yale used, redio, mipira used kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kinaikosesha Serikali mapato. Hii imetokana na mfumo mzima ule wa ukusanyaji mapato kule Zanzibar, double tax, ndicho kitu kinachosababisha wafanyabiashara kukimbia kulipa kodi mara mbili katika bandari yetu ya Dar es Salaam. Kwa sababu wao wanaleta bidhaa pale Zanzibar wakishashusha kwenye makontena wanalipishwa ushuru, TRA wanachukua chao na ZRB wanachukua chao, lakini mtu yule yule akisafirisha mzigo ule kuuleta bandari ya Dar es Salaam analipa tena kodi mara mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie wazi Mheshimiwa Waziri, kiwango kikubwa cha bidhaa zile au mafuta yanayoingia Tanzania Bara asilimia 80 yanapitia Zanzibar. Hiyo ni taarifa rasmi naomba aifanyie kazi na si hivyo tu, mipira used na vifaa vingine used vinavyoletwa kutoka nje vinashushwa tu Zanzibar lakini vinaishia Tanzania Bara na maeneo mengine kwa njia za panya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni jukumu la Serikali kujipanga sasa kuhakikisha hii kero inayotajwa kila siku kwamba tumemaliza tatizo la tozo ya ushuru wa mara mbili kwa biashara au kwa bidhaa zilizoko Zanzibar zinazoingia Bara bado halijamalizika na imekuwa maneno ya kila siku. Hili nimwombe Waziri ulifanyie kazi na tufike mahali iwe mwisho wa hili suala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia eneo lingine ambalo Serikali bado ina nafasi kubwa ya kuwekeza na kuweza kujipatia mapato mengi. Nimeangalia bajeti vya kutosha lakini bado wito wetu tunaoutoa na kulia kila kwenye suala zima la uvuvi wa bahari kuu na uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata samaki halina kipaumbele. Nimwombe Waziri hesabu za haraka haraka, sasa hivi duniani mpaka juzi nilivyokuwa natembea kwenye mitandao ndani ya soko la dunia kuna mahitaji ya tani 271,000 kwa mwezi za samaki ambazo zinahitajika zikiwa processed ambao ni cane fish.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kama nchi ingeweza kuwa na hii tunaita pot fish moja tu au mbili zinaweza kutengeneza ajira zaidi ya watu 30,000 kwa kila meli inayo- land kwa kipindi cha miezi mitatu watu wale wanafanya kazi lakini pato linalopatikana kwa meli moja tumeshawaeleza mara nyingi pale ile process nzima ya meli moja ni zaidi ya dola 85,000, pesa zile zinakuwepo ndani ya nchi, zinasaidia Watanzania na watu wengine. Vilevile bahari yetu tumeshaeleza mara nyingi jamani, hivi sasa pamoja na mazingira mengine yaliyoko katika maeneo mengine current ya maji katika maeneo yetu ni very conducive kuliko maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Namibia current imechafuka, Mozambique current imechafuka, Tanzania current ni conducive. Kwa hiyo, stock kubwa ya samaki imekusanyika katika maeneo yetu na ndiyo maana meli nyingi za nje zinakimbilia kuvua katika maeneo yetu kwa sababu kuna mazingira rafiki ya kuishi. Si hivyo tu, wenzetu wa Philippine na Mataifa mengine ya nje yanakuja kumwaga vyakula katika maeneo ya Tanzania ili kuwavuta samaki kuwepo kwa wingi na kuvuna samaki wale kwa njia ya kirahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu nyingine tuendeleze uvuvi mpya unaoingia hivi sasa wa kutengeneza uvuvi wa kutumia cadge. Utafiti tayari umeshafanyika na cadge fishing imeonekana kuwa na mafanikio makubwa. Leo hii wavuvi wetu wengi walikuwa wanavua majongoo kwa kutumia gesi lakini leo baada ya kufanyika utafiti, wavuvi hawa wanaweza kuvua kwa kutega cadge tu ndani ya deep sea na cadge moja ina uwezo wa kuingiza mpaka milioni 24 kwa mvuo mmoja tu wa kipindi ambacho utaweza kufuga wale samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini kusiwe na mipango mahsusi kuwawezesha wananchi hawa, wakawa na vyombo vya kisasa wakaweza kwenda kuweka cadge zao katika deep sea, wakavua kwenye deep sea na tukaweza kupata samaki wa kutosha lakini tukaanzisha viwanda vya kuchakata samaki na kufunga na kusafirisha nje, wakati soko sasa hivi linatafuta bidhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulisema ni kwamba bado tuna tatizo kwenye kilimo. Tunasema kilimo tumekipa kipaumbele lakini bado sijaona mikakati halisi ya kusaidia kilimo cha Tanzania kikaweza kuonesha mafanikio na kuwasaidia wakulima wengi katika nchi yetu. Nitoe mfano mmoja wa kahawa bado kuna urasimu katika soko la kahawa, soko la kahawa lazima uende Moshi, lakini tuna kiwanda kipo Mbinga kilianza kuchakata na kutengeneza Mbinga Instant, kahawa ile ikawa imepata soko kubwa tu katika nchi mbalimbali zikiwemo Ulaya hata Zanzibar na maeneo mengine lakini bado Serikali haikutoa msukumo wa kufanya eneo lile likaweza kuzalisha na kufanya canning ile kahawa iliyoko katika maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungeweza kukianzisha kile kiwanda cha Mbinga kingehamasisha kilimo cha kahawa katika maeneo yote yale ya Mikoa ya Ruvuma lakini hata maeneo ya Mikoa ya Lindi na Mtwara yale ambayo yanakubali kahawa ingeweza kuzalishwa, lakini Njombe ingepata fursa kubwa zaidi ya kuzalisha kahawa na ikaingia katika ramani ya maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa wa kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe vitu kama hivi Serikali itie mkono wake si tu kuiachia pengine kampuni au Halmashauri na wananchi wenyewe wakaweza kufanya kitu kama kile, lakini ile ile ingesaidia urasimu wa kutoa kahawa Mbinga kuipeleka sokoni Moshi. Vilevile ungesaidia urasimu wa kutoa kahawa Mbozi ukaipeleka Moshi, tunapoteza gharama kubwa ya uzalishaji bila ya sababu wakati huku tunasema Serikali inaondoa tozo lakini tunaanzisha tozo nyingine ambazo tunaweza kuzipunguza na... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa kwa mara ya kwanza leo hii kuweza kuchangia katika bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza ninalotaka kuchangia ni suala zima la fidia katika maeneo yetu mbalimbali ya Jeshi la Ulinzi Tanzania. Kwa kweli hili limekuwa dondandugu na nimwombe sana Waziri wa Fedha, Jeshi limeshaomba bilioni 20.9 zaidi ya miaka mitatu hazijapatikana. Kuna mizozo mikubwa inaanzishwa na inakuzwa kutokana na kutokulipwa fidia katika maeneo mbalimbali ya Jeshi letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata kuzunguka katika kila eneo unapouliza juu ya fidia unaambiwa, tulipokwenda Mtwara tumeambiwa, Songea kuna madai mengi tu ya maeneo ya wananchi, Bukoba, Mbeya, Zanzibar, kila eneo kuna madai haya. Kwa hiyo, niombe Waziri wa Fedha hili liwe moja kati ya vipaumbele vya kumaliza migogoro baina ya wananchi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nataka kuzungumza suala la Jeshi kuongeza maeneo ya shughuli zao. Niwaambie tu kwamba kwa hali ilivyo sasa hivi, it’s too late. Kwa sababu maeneo ambayo wanataka kuyaongeza tayari wananchi wameshakaa na wananchi walikaa zamani sana wao wanalijua hilo. Sasa leo kitendo cha kwenda kuwaondoa wananchi wakasema tunaongeza sehemu hii wakati eneo lile hata kama wataongeza itakuwa wao wenyewe wameshajiingiza ndani ya wananchi ni kujitengenezea migogoro isiyokwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawasihi sana, yale maeneo ambayo tunataka kuyachukua ambayo yalishachanganyika na wananchi kwa kiasi kikubwa sana, ni bora kuyasamehe na kuweka uzio katika eneo ambalo litakuwa salama zaidi kufanya shughuli zao kuliko kujichanganya na wananchi ambapo matatizo mengi baadaye yanaweza kuzuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo linanasibishwa na mfano wa eneo ambalo liko katika Jimbo langu la Uzini, eneo la Kambi ya Ubago, eneo la Kidimni, eneo ambalo wananchi wamekaa toka miaka ya sitini wako pale, lakini juzi wanakuja kuibuka viongozi wa Jeshi na kupiga X kuanza kuwatisha wananchi na kuwaambia kwamba wahame katika eneo lile wakati eneo lile lilikuwa la Wizara ya Kilimo, nami najua mpaka makubaliano waliyopewa wananchi na Wizara ya Kilimo kukaa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naliomba Jeshi sana na nalisihi sana, kwa eneo lile it is very sorry kwa sababu wamechelewa, wananchi wameshakaa pale na kwenda kuwahamisha wananchi wale ni kuongeza fidia nyingine wakati hizi za nyuma bado hazijalipwa. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri katika majibu yake tupate kauli ya Serikali na ya Wizara juu ya eneo ambalo linataka kuchukuliwa na Jeshi wakati wananchi wameshakaa katika eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa hakuna uendelezaji wowote unaofanywa katika eneo lile kwa sababu kumepigwa X na Wanajeshi wale ambao wanapita kila siku kuwatisha wananchi, wengine wanapigwa, wengine wanazuiliwa kufanya shughuli zao, naomba wapate uhuru wa kufanya shughuli zao na Jeshi mipaka waliyokuwa wameiweka toka miaka ya 1975 na 1980 na mwisho 2005 iheshimiwe na waweze kufuata ile mipaka ya zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumza ni suala zima la Jeshi kuanza uwekezaji sasa hivi. Tuondokane na mawazo ya zamani kwamba Jeshi kazi yake ni kushika bunduki, kulinda mipaka na shughuli nyingine za Kijeshi. Majeshi mengi sasa hivi duniani yanakwenda kwenye mtindo wa kisasa kuweka uwekezaji na kujiendesha yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahali pekee Jeshi linaweza kufanya uwekezaji ni suala la kuweka dry dock ile ambayo iko kule Mtwara, eneo lile litaweza kufungua pato kubwa ndani ya Jeshi la Wananchi kwa sababu naamini wazi kama tutaweza kujenga ile bandari, niiombe Serikali, tutafute fedha tulipe fidia, bilioni 3.6, lakini isitoshe, tutafute fedha tukope tuwekeze pale. Tukiweza kuweka dry dock pale ya samaki, kwa mfano bandari ya uvuvi ikiwekwa pale, meli zote zinazotaka kufanyiwa fishing inspection zitakwenda pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, meli moja kuifanyia inspection ni dola 6,800, lakini meli moja ikija pale kuchukua mzigo tu wa kuweza ku-feed wavuvi ambao watakaa ndani ya bahari kwa muda wa miezi mitatu, ni zaidi ya milioni 45 hadi milioni 60, hicho ni kipato kikubwa! Kwa nini, tukatafute fedha nyingine, kwingine za Serikali wakati vyanzo vya kupata pesa vipo?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pale panahitajika pawekwe karakana ambapo kama kuna kifaa kinahitajika kuchongwa kichongwe na Wanajeshi wetu, JKT watapata nafasi. Pia kiwanda cha chumvi katika eneo lile ndiyo penyewe, kwa hiyo fursa zipo nyingi. Niwaombe sasa hivi waanze kubadilika na wawe na mtazamo chanya wa maendeleo zaidi wa kujiwekeza kwenye uzalishaji pamoja na shughuli za ulinzi zikiwa zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuchangia katika eneo hili, ni suala zima la makazi ya Wanajeshi wetu. Bado kuna tatizo kubwa katika maeneo yetu, Wanajeshi kweli wanakaa katika nyumba ambazo bado hali zake ni mbaya na nyingine zimejengwa toka miaka
ya sabini, hazina ukarabati, hazina miundombinu yoyote, zimechoka. Kwa hiyo, niombe kwa kweli Kitengo hiki cha JKT kisiwe tu kinajenga katika maeneo mengine lakini kiwezeshwe fedha za kujenga au kufanya ukarabati katika maeneo ambayo wanakaa Wanajeshi wetu ili na wao waishi kama maafisa wengine wa ngazi mbalimbali wanavyoweza kufanya shughuli zao kwa raha na wajisikie kama kweli wako kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Waziri hili nalo alitilie mkazo na atoe kauli kwamba sasa hivi mwelekeo wao ukoje katika ukarabati na ujenzi wa nyumba za Wanajeshi wetu katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni suala zima la muda wa kuondoka kazini Wanajeshi wetu. Suala hili kuna manung’uniko mengi ya Wanajeshi wetu, muda wanaoondoka ni mwingi na wanataka kujua sheria gani ya utumishi inawafanya kuingia kazini saa 12 asubuhi na wakatoka saa 12 jioni. Kwa hiyo, hili lazima Mheshimiwa Waziri atupe maelezo ili na wao waweze kuridhika, kwa sababu wao hawana mahali pa kusemea, wanatuma wawakilishi wao waweze kuwasemea, katika hili tupate maelezo kitu gani kipo huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, nataka kuzungumzia juu ya maendeleo ya SUMA JKT na shughuli wanazozifanya na vijana ambao wanakwenda katika maeneo yale. Wenzetu wengine wamelidokeza kwamba bado vijana ambao wanatoka katika maeneo yetu ni wachache, vilevile ile recruitment inayofanyika kwa kweli inakuwa ina figisufigisu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza vijana hawa kuweza kupatiwa skills maalum za kuweza kujiendeleza kule wanakokwenda. Hii ni kwa sababu siyo wote wanaokwenda kule wanafaa kuwa Askari, wengine wana vipaji mbalimbali na kazi mbalimbali za mikono, wanaweza kwenda kuwekeza. Kwa hiyo, wazo langu ni kwamba, JKT iweze kuwa na skills maalum kwa vijana ambao wanakwenda kule wakitoka pale waweze kwenda kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba ikiwezekana watoke pale basi wengine wapewe kits za kuweza kwenda kuanza maisha katika maeneo yao na siyo kwenda pale kila mmoja kutegemea kwamba apate ajira ya Jeshi au Polisi au Magereza au kazi nyingine. Wale vijana kule wakikusanyika mambo mengi wanaweza kuyabuni, wakaweza kuyafanyia kazi na wakaweza kutoka pale na ujuzi wa aina yake wakalisaidia Taifa hili kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SALUM M. REHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye hotuba hii ya Bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza mimi baada ya kuipitia bajeti ningeanza kwanza kujikita kwenye tasnia ya tafiti ndani ya nchi. Baada ya kupitia vitabu na maelekezo ambayo Serikali imesema kimaelezo tu itasaidia na kuhakikisha kwamba inatoa msukumo kwenye tafiti mbalimbali ili kufanya nchi iwe na vitu ambavyo vinaendana na uhalisia.

Mheshimiwa Spika, kitu cha kwanza ambacho ninachokiona kwa kweli kimevunjisha moyo, Serikali haielekezi fedha kwa ajili ya taasisi za utafiti zilizopo nchini, pesa zinatengwa lakini haziendi. Sasa kama fedha haziendi matokeo yake yanakuwa haya; moja, kwenye upande wa kilimo suala zima la uletaji wa mbegu kutoka nchi za nje ndiyo unaotawala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa inakuwa kama ni mpango maalum wa kuwawezesha makampuni ya nje yakawa yanaleta mbegu nchini kufanya biashara hizo na kuwaacha wazawa hapa ambao wana uwezo wa kuweza kuzalisha hizo mbegu kwa ajili ya mazingira ya nchi yetu wakishindwa kufanya chochote katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona katika vituo ambavyo vinazalisha mbegu za mahindi tafiti zimeganda zaidi ya miaka miwili sasa hivi wale ambao walitaka kumaliza utafiti wao umekwama, lakini tunaona tatizo kubwa lililopo kwenye suala zima la mbegu za alizeti. Mbegu za alizeti tulizonazo ndani ya nchi hazifai, lazima tuseme ukweli. Ni asilimia 12 tu ya mafuta ambayo yanatoka ndani ya zile mbegu, kwa wenzetu mbegu hizi tunaziita ni makapi.

Mheshimiwa Spika, ukienda nje; leo hii kuna mbegu ambayo ipo Belgium ina uwezo wa kuzalisha mafuta mpaka asilimia 67, kitu ambacho kingeweza kutuongezea mapato lakini kingeweza kutuongezea mafuta mengi ya uzalishaji kama tungeweza kuwekeza katika haya maeneo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niiombe Serikali, katika hayo mazao ambayo ya mkakati ambayo yamekudiwa kuweza kuyawezesha maeneo ya kanda ya kati kuwa ni maeneo ya uzalishaji wa alizeti na kuwa ni sehemu ya mazao ya uchumi, kungekuwa na mtazamo wa aina yake. Kuiwezesha alizeti ya nchini inayozalishwa katika maeneo yetu hapa kutoa mafuta na si kuweza kutoa makapi au mashudu kama ilivyo hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiweza kuwekeza hapa sasa hivi, tukifanya tafiti za kuzalisha mbegu ambazo zinatoa uwezo mkubwa wa mafuta itaweza kutusaidia kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pili, tunahitaji kuzalisha mawese. Mawese tuliyonayo katika nchi hakujawa na mwendelezo wa aina yoyote; Wizara ya Kilimo ipo, watafiti wapo na watu wamesema lakini mbegu zile za mawese za kwetu hizi kutoka Kigoma zimetumiwa kama mother stock kwa nchi mbalimbali duniani ambazo sasa hivi zinaleta mafuta ya mawese katika nchi yetu hii hapa. Kwa hiyo, sisi kama Watanzania tuliotoa zile mother stock tunaletewa mafuta nchini hapa na yanauzwa katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, niwaombe Wizara ya Fedha na Waziri husika, atie msukumo kwenye research ambazo zitaweza kubadilisha tasnia ya uzalishaji wa mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la mbegu za mboga mboga Tanzania imekuwa ni soko kuu la kampuni za Belgium, Uingereza, Switzerland na nchi nyinginezo, hata Kenya, kutuletea mbegu za aina mbalimbali hapa, nyingine zikiwemo za GMO ambazo zinahatarisha na kuongeza kiwango cha kansa kwa mazao ambayo wanakula wananchi wetu hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wito wangu ni kwamba tuondokane na hii hali, tuweze kuwa na uwezo wa kuzalisha mbegu ambazo zitakubaliana na mazingira yetu na mbolea na udongo tuliokuwa nao na kuwafanya Watanzania waweze kufaidika na kilimo kilichopo nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye utafiti safari hii Tanzania tumeathirika karibu hekta 30,000 kwa American worm au viwavijeshi vya Amerika tunakiita. Hiki kiwavi jeshi kipya kilichokuja hivi karibuni na matokeo yake kuingia tu Tanzania, tumeona athari katika maeneo ya Chemba, Mikoa ya Dodoma, Manyara, Kaskazini kote kwa ujumla, Tanga na maeneo mengine. Sasa wadudu wale au wale viwavijeshi wa aina ile tusifikiri kwamba wamemalizika. Wale sasa hivi mayai wametaga yapo, kama safari hii tulipata athari ya hekari 30,000 mwakani tutarajie zaidi ya hekari laki moja ziaathirika na American worm wale.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wito wangu ninachokiomba tuiwezeshe TFDA na taasisi hizi ambazo zinaweza kushughulika kwanza na udhibiti, upatikanaji wa dawa na mafuta kwa ajili ya kuweza kuwaangamiza hawa wadudu; ziwepo fedha standby ili ikitokea outbreak ya kile kitu tuweze ku-harm kwa nguvu zote kuliko kwamba mnamtafuta Waziri wa Kilimo baada ya athari kuwa imeshatokea, wale wadudu wakiingia siku moja, mbili tatu tayari wameshamaliza maelfu ya heka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wito wangu ni kwamba tuwezeshe taasisi hizi za utafiti ambazo zinaweza kututengenezea dawa maalum, maana mpaka hivi sasa dawa tunazochukua tunachanganya tu. Hatujawa na dawa maalum kwa ajili ya kuangamiza viwavijeshi vya aina hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, uwezo wa kutengeneza hizo dawa tunao, wapewe wataalam hiyo kazi tuingie maabara ili tutengeneze dawa ambayo itaweza kuwasaidia Watanzania na kuondokana na hili janga. Safari hii athari kubwa imeonekana kwenye mahindi lakini wadudu wale wanakula miche au majani ambayo yana siku kuanzia nne, saba mpaka 25. Vile vile wanakula mpaka ile stem, ule mmea wenyewe wanatoboa ndani katikati pale.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, uwezo wake ni mkubwa tofauti na viwavijeshi wale wa zamani ambao tunaita African worm ambao wale uwezo wao kula hawazidi majani ya siku saba. Kwa hiyo, mazao kama maharage, njegere, kunde na hata mazao mengine madogo madogo ya mtama tujiandae kwamba yanaweza kuangamia kama hatukuchukua tahadhari ya mapema tuka-harm hiyo hali na kuinusuru nchi na kupata janga la njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wito wangu kwa kweli hizi fedha zilizokuwepo ziwekwe standby kwa kusaidia eneo hili na fedha hizi zilizokuwa allocated ziende, zisiwe nadharia tu za kila siku.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusu suala zima la soko la bidhaa zetu. Sisi Tanzania tunazalisha na safari hii projection ya uzalishaji tunaweza kuwa na excess ya mazao zaidi ya tani milioni saba, hayo yamo ndani ya maeneo yetu. Hata hivyo sijaona katika mpango huu kwamba nchi imejipanga vipi kukabiliana nah ii ziada ya mazao ambayo yatakuwa katika maeneo yetu; lengo ni kuwasaidia wakulima wetu. NFRA pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko uwezo wake ni mdogo wa kununua haya mazao na tumeona athari iliyotokea mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki na nchi nyinginezo za SADC watu wamezalisha, kwa hiyo yale masoko ambayo tulikuwa tumeyatamani kwamba tungeweza kuwapelekea majirani zetu hayapo. Kwa hiyo nchi kama nchi ijiandae sasa kukabiliana na surplus ambayo itatokea katika uzalishaji ambao watu wamezalisha ili tuweze kupeleka mazao yetu nje zaidi na kutanua wigo wa kuwaongezea kipato wakulima wetu hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami naunga mkono hoja. Naomba nichangie na nishauri Serikali katika mpango huu, nikimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha maoni yake. Nami naomba niwasilishe maoni ambayo naona yanaweza kuisaidia Serikali hii kuiondoa hatua moja kwenda hatua nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa la mwanzo ambalo nataka kuanza nalo ni suala zima la uwekezaji katika bahari kuu. Nchi zote za visiwa na nyingine zilizozungukwa na bahari suala hili limekuwa kipaumbele na wenzetu limewatoa na ndiyo nguzo ya uchumi wao. Tanzania hatufaidiki hata asilimia moja katika maeneo ya uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni huu, kama tumeweza kununua ndege, kwa nini tushindwe kununua long vessels mbili tu ambazo zitaweza kuongeza mapato zaidi ya shilingi bilioni 7.8 kwa kila bamvua. Wale wenzangu wa Pwani wanaelewa bamvua ni kipindi kile cha uvuvi tu kwa kila long vessel moja. Kwa hesabu za haraka nilizozipiga ni kwamba tukiwa na long vessels mbili tunahitaji wataalam katika mchakato mzima wa uwekezaji wa viwanda vya samaki na uvuvi wa bahari kuu karibu 3,640; lakini tunahitaji hard labor katika eneo hilo karibu wafanyakazi 48,000 wakati mmoja na hawa watakuwa wanafanya kazi kwa pamoja ambapo meli moja inakwenda Pwani, meli moja inapakua mzigo kutoka baharini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia sasa hivi ina mahitaji zaidi ya asilimia 67 ya samaki. Tuna demand kubwa in the world wa samaki aina ya tuna katika soko la China, Nordic countries, Japan. Sasa hivi samaki aina ya tuna wamepanda kutoka dola 8,000 kwa tani mpaka dola 18,000 kwa tani. Hiyo demand haijawahi kutokea duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni sehemu ambayo sisi kama nchi tunakiwa tuiangalie. Nami nashangaa Doctor, kwa nini hili lisiwemo katika mpango wa sasa hivi? Tumechelewa sana, kwa sababu uwekezaji uliokuwepo hapa, input na output haziko sambamba, ni only two percent ya input, lakini una output ya 98% kwenye total production ambayo tunaweza tukaifanya katika maeneo hayo. Wewe ni mchumi na unaelewa hapa ni kitu gani tunachokizungumza. Naomba tufanye restructuring tuhakikishe kwamba tunakuwa na uwekezaji katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika eneo hilo, tutaanzisha viwanda ambavyo vitaweza kuchakata hawa samaki. Tukiianzisha bandari moja ya uvuvi hapa nchini ambayo mwenzangu ameshaidokeza pale, inaweza kutuingizia mapato mengi sana. Kwa mfano, ukaguzi wa long vessel moja tu ambayo tutaipa leseni sisi kama Tanzania ni dola 40,000. Ndani ya nchi kwa mwaka mmoja tunaweza kusajili zaidi ya meli 40 au 100, ni kiasi gani ambacho nchi itaweza kuingiza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kila meli moja inayokuja kukagua lazima ichukue vyakula ndani ya nchi, inaanzia tani 10 mpaka 17. Hizi ni fursa ya soko la bidhaa ambazo tunazalisha wananchi hapa, wakulima watakuwa wamepata sehemu ya soko na vyakula mbalimbali vitaweza kuuzwa kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hicho tu, niliwaambia watu, maji haya ya kawaida ambayo yanatiwa katika vile vyombo, kila meli moja tungeiuzia zaidi ya shilingi milioni mbili au shilingi milioni nne. Mbali na upande wa mafuta, tutaweza kufanya biashara kubwa kabisa ya uwekezaji katika maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti,katika kitu ambacho kinaweza kututoa ni hili suala la uwekezaji katika uvuvi wa bahari kuu. Kwa sababu meli, hii long vessel ndogo ya kawaida ina uwezo wa kuvua kuanzia tani 42,000 mpaka 105,000 na tunaweza kuinunua meli hii kwa dola za Kimarekani 450,000 na hizi mbili au zile kubwa zaidi tukainunua kwa dola 700,000 kitu ambacho kinawezekana kwa nchi. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijielekeze huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda nishauri ni eneo ambalo bado kama nchi uwekezaji wake hatujaufanya. Wenzetu nchi za nje na nchi nyingine ambazo ziko ndani ya eneo la Sahara zinawekeza kwenye research. Namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango aangalie suala hili la research. Nchi yoyote duniani haipigi hatua kama haikuwekeza kwenye research. Research hupotezi, ndiyo mwongozo utakaokupelekea kufikia yale malengo uliyokusudia. Tuna tatizo katika uwekezaji katika eneo hili, tunazungumza sana na kama Doctor kazi yako kubwa na wewe ilikuwa ni research lakini priority za maeneo ya research hazijakuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mmoja kati ya Wajumbe wa Baraza na hayo malalamiko yapo katika kila eneo la research unaambiwa kwa kweli fedha katika maeneo hayo zinazokwenda kwa kiwango kidogo sana. Siyo tu kwenye research kwenye maeneo ya kilimo na mifugo lakini hata maeneo ya elimu na viwanda, huko kwenye viwanda bado hatujafanya utafiti wa kutosha tukagundua viwanda gani tunahitaji kama nchi? Tuwekeze kitu gani tuweze kutoka hapa? Je, tuwekeze kwenye viwanda vya chuma ambavyo vinapatikana ndani ya nchi au tuwekeze kwenye viwanda vya aina gani? Nafikiri hili nalo lionekane katika huu mpango, kuna vipaumbele katika maeneo hayo na litatutoa katika kipindi kifupi tu kijacho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo nataka kulizungumzia ni suala zima la utalii. Bado kama nchi sisi tunapata tip tu, hatufaidiki na fee zinazotokana na utalii. Wanaoshughulika na tasnia ya utalii wanaelewa, nchi yoyote ili ifaidike na utalii unatakiwa uwe na link ambayo itakuunganisha kutoka mtalii anapotoka na aweze kulipa ndani ya nchi. Watalii wetu wengi wanalipa kwao, wanalipa kwenye makampuni yao, wanakuja na travelling card ndani ya nchi hapa, hatufaidiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala hili liangaliwe upya. Kwa kweli kiwango tunachokipata hapa nchini ni kidogo sana, tungeweza kupata zaidi ya mara 20 au 50 ya pato ambalo wanapata wenzetu na tungeweza kwenda kujifunza Mauritius na Seychelles, nchi ndogo watu wachache, lakini kipato chake kinachotokana na utalii ni kikubwa. Leo mtalii nchini kwetu mpaka kufika hapa, mchakato wote ule anatoa dola 15 lakini akiingia Seychelles kufanya utalii, mtalii yeyote lazima atoe dola karibu 160 za mwanzo hizo. Ni entry fee ambazo wao wamezitengenezea mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba twende tukafanye utafiti kwa wenzetu, tukae nao, watupe ujanja na mbinu tuweze na sisi kuwekeza katika hayo maeneo. Vivutio tulivyokuwanavyo vinalipa. Leo hii watalii ambao wanakuja katika maeneo yetu, kwa mfano, Ngorongoro ukiwazuia, kwa kweli yatakuwa maandamano makubwa. Sasa kama vivutio hivi potential viko nchini na tunaweza kuvi-control wenyewe, tuwe na usimamizi mzuri tupandishe kipato ambacho kitaweza kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuzungumza kidogo suala la mbegu ambazo tunasema kwamba tunataka tuzizalishe ndani ya nchi, tuna tatizo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue fursa hii kukushuruku kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuzungumza mambo mtatu ambayo zaidi ni kushauri katika Jeshi letu hili na hasa kwenye upande wa JKT. JKT kwa sasa tunaweza kusema kwamba ni moja kati tegemeo na nguzo mahiri kabisa ambayo inaweza kututolea vijana ambao wanaweza kushiriki harakati mbalimbali Jeshi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kubwa zaidi tunachotaka hapa ni kuweza kutolewa mafunzo yale ya ueledi zaidi katika Jeshi letu hili la JKT na hasa yale ya kuwafanya vijana wale wakitoka pale waende wakajitegemee. Pamoja na mafunzo yanayotoka sasa hivi, lakini bado hayawajengi wale vijana na kuwapa ile confidence ya kumaliza JKT na kuweze kwenda kujitegemea na wengi wao wanakwenda kwa mawazo kwamba hawapati ajira kitu ambacho Serikali haiwezi ku-afford kuwapa ajira watu wote ambao wanaweza kwenda katika maeneo haya ya JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wito wangu kwa nini kusianzishwe programu maalum ndani ya JKT ambazo zitawafanya vijana wale waweze kuwa mahiri hasa kwenye upande wa kilimo, mifugo na uvuvi. Tuna mahitaji mengi vitu sasa hivi katika nchi yetu lakini tuna matishio ya hali mbalimbali za hali ya hewa ambazo zinakabiri mazingira yetu kama tungeweza kuliimarisha Jeshi hili la JKT hasa kwa kuzalisha kwenye kilimo cha umwagiliaji maji wakaweza kuzalisha mazao mengi kabisa hasa na tatizo hili la upungufu wa chakula au tishio la ukame ambalo linatokea katika maeneo yetu mbalimbali tungeweza kulikabili na hii ingekuwa ni sehemu moja ya kuwa na food reserve kuliko hali inavyokwenda sasa hivi. (Makofi)

Kwa hiyo, wito wangu zaidi ni kulitaka jeshi hili lijitengeneze upya na kuweza kujitegemea hasa kwa ajili ya chakula na mimi maoni yangu binafsi ningependelea wangeweze kuwa kama walivoambiwa Magereza na wao JKT waweze kujitegemea kwa chakula na sio Serikali iweze kuwalisha siku zote wakiwa makambini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika eneo hili ningeomba JKT kupitia Shirika lake lile SUMA na mashirika mengine yaliyoko katika Jeshi la Kujenga Taifa, Jeshi la Wananchi kuweza kujenga ile bandari ya uvuvi. Jeshi limeweze kulipa eneo lile Ras Mshindo, eneo ambalo ni sahihi kabisa kwa ajili ya kujega bandari ya uvuvi. Bandari ile haitaumika kwa sababu ya uvuvi lakini itatumika kama ni sehemu ya karakana meli mbalimbali ambazo zitakuwepo pale ziwe za kijeshi, ziwe za wananchi, ziwe za nje, za sehemu nyingine mbalimbali ambazo zitatengeneza mazingira mazuri ya fedha na kulifanya Jeshi kuwa na mitaji na miradi ya mikakati zaidi kuliko hali inavyokwenda hapa.

Lakini vilevile itadaia katika eneo lile kuweza kulinda mazingira sasa ya bahari kuliko sasa hivi maeneo yetu ya bahari umekuwa ni mkubwa, lakini Wizara inayohusika na taasisi nyinginezo hazina doria wala udhibiti wowote wa mazingira ya bahari tunalitegemea jeshi hili liweze kuzunguka katika maeneo yetu ya bahari yaweze kuyalinda, lakini kudhibiti uchafunzi ambao unafanyika hasa sasa hivi ulioingia utupaji wa takataka za kemikali katika bahari zetu na maeneo yetu mbalimbali ya uzalishaji. Kwa hiyo, ningeomba zaidi Jeshi hili lingejikita katika mwelekeo huo na kuweza kujiimarisha zaidi katika maeneo yetu ya bahari ambayo yana fursa kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilitaka nilizungumze ni suala zima ya kuimarisha vikosi vyetu hasa kwenye mambo ya michezo kuna fursa kubwa kupitia Jeshi hili la JKT na Jeshi la Wananchi kuimarisha michezo kama ilivyokuwa zamani inavyoonekana sasa hivi ule mwendelezo hasa na makakati uliokuwepo umepungua nguvu. Kwa hiyo, nimkumbushe Waziri lakini nimkumbeshe CDF na wenzake ya kuweza kuimarisha michezo na kulifanya Jeshi kuonekana kwamba ndio ramani sasa ya michezo Tanzania kama wanavyotumia wenzetu kwa sababu ukiangalia Marekani, Uingereza na maeneo mengine wanajeshi ndio wanakuwa wameshika hatamu hasa michezo na inakuwa ndio dira na nembo ya Taifa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningemuomba CDF kuangalia mbinu na njia gani ya kuimarisha sekta hii ya michezo katika Jeshi ambavyo inaweza kutusaidia kuwafanya wanajeshi wetu kuwa mahiri lakini vilevile na kutunza afya zao kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nakushuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kupata muda wa kuchangia. Nataka kuiomba Wizara itoe taarifa rasmi hapa kuhusiana na suala zima la Mradi huu wa SPD II utaanza lini na kama umeanza, umeanza wapi na vipi hatuelewi chochote mpaka leo zaidi ya miaka miwili sasa hivi toka umezinduliwa hakuna tunachokiona kinaendelea katika eneo hilo, kwa hiyo, tunaomba Serikali au Wizara itupe maelezo ya SPD II na ile mipango iliyokuwepo katika ule mradi inakwendaje.

Mheshimiwa Spika, la pili vilevile kuitaka Wizara hasa kwenye kile kitengo chake cha Early morning iweze kuwa inatoa maelezo sahihi kitu ambacho niseme wazi kwamba kimesababisha hasa wakulima wa mikoa zaidi ya nane ndani ya nchi hii kuweza kupata na janga la njaa kidogo yaani upungufu wa mazao kwa sababu kimeshindwa kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa au hali ya mvua inavyonyesha au ukame utakavyotoka, kitu ambacho kwa kweli hawatutendei haki kama Watanzania. Kitengo kile kipo kina taarifa ambazo wanazipata kutoka meteorological agent lakini hawatoi taarifa wamekaa kimya watu wanalima hawajui hatima yao na watu wanategemea mvua. Kwa hiyo, tunataka utupe maelezo kipi kilichosababisha kwamba mpaka wakashindwa kutoa maelezo safari hii watu mikoa mingine ikaweza kupata upungufu wa mvua.

Mheshimiwa Spika, lakini jingine nilitaka kulizungumza kwamba Serikali au Wizara kwa ujumla wake imeondoa mkono wake kutoka SAGCOT zile shughuli ambazo tulikuwa tunaziona ambazo zinasadia wananchi kuwekeza katika kilimo hasa mikoa ile ambayo ya Kusini ina mfumuko mkubwa wa uzalishaji lakini leo hii SAGCOT tunaiona inaanza kuelekea kulikokuwa siko. Kwa hiyo nitoe angalizo kwa Serikali pale ilipokuwa inaona kwamba imekosea irudi kwenye mstari SAGCOT ndio mkombozi ilikuwa kwa maeneo ya mikoa ya Kusini lakini imeelekea sasa hivi mikoa ya Pwani na mikoa mingine tunaihitaji SAGCOT irudi kwenye progress hali inayokwenda sasa hivi sivyo, hilo lazima tulizungumze. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jingine ambalo tulitaka kuona kwamba Serikali ijikite kwenye mbegu bado Tanzania tumekuwa jalala la mbegu feki mpaka leo kiwango ambacho nchi inaweza kutoa mbegu ndani ya nchi ni asilimia 12,15 mbegu zote zinatoka kwa Belgium, zinatoka South Africa, zinatoka nchini Kenya na nchi nyinginezo kitu ambacho watu wanatumia nafaasi hiyo kuingiza mbegu feki. Makampuni haa ambayo tunayaita yako hapa nchini ya KIBO, SIDCO sjui mengine ambayo yako Arusha hayazalishi mbegu yanafungasha mbegu ambazo inakaa miaka chungumzima huko kwao na zikiletwa hapa ile variability inakuwa imeshapotea kwa hiyo, hazioti na zinawatia hasara wakulima. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Salum Rehani.

MHE.SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kupata nafasi hii ya kuchangia kwenye itifaki hii. Kwanza niseme kwamba naunga mkono na ninaomba Wajumbe mbalimbali tuweze kuiridhia itifaki hii ya FAO ambayo sasa inatupeleka na sisi kutuunga miongoni mwa nchi ambazo zinanufaika katika itifaki hii kwa wale waliokuwa wameanza kuridhia. Sisi tumechelewa.

Mheshimiwa Spika, hasara ya mwanzo ambayo inatokana na kutokuridhia kwetu, Tanzania imekosa siyo chini ya dola za Marekani 184,000 ambazo zilikuwa ni fedha maalum za nchi ambazo zinapitiwa na bahari upande wa mashariki na hasa zile ambazo zinatumika kupitishia meli kubwa zinazomwaga dawa na sumu mbalimbali katika eneo letu. Kwa hiyo, eneo letu limekuwa linaathirika sana na watu ambao wanafanya biashara ya kutupa uchafu mbalimbali hasa wa sumu katika eneo letu, lakini sisi kwa kutokuridhia mkataba huu, tumeshindwa kutetewa au kulindwa kwa pamoja na wale waliokuwa wameridhia mkataba huu.

Mheshimiwa Spika, la pili, tunaingia miongoni mwa nchi ambazo zitakuwa zina ule mpango, routine research na monitoring ya meli zile ambazo zinaingia katika mkumbo wa meli ambazo zinaitwa za eneo la Indian Ocean and Pacific, ambapo tutakuwa tunapata takwimu sasa za fish stock karibu kila baada ya miaka mitatu katika eneo letu hili la bahari kuu.

Mheshimiwa Spika, lingine mabalo linanufaisha; Tanzania pamoja na kuwa na ukubwa wa eneo la mita za mraba laki mbili, tulizoziongeza hizo la uvuvi wa uvuvi wa bahari kuu, lakini tumeomba tena eneo lingine tuongezewe la zaidi ya nautical miles 150,000. Kwa hiyo, tunakwenda kuwa na eneo kubwa zaidi la uvuvi wa bahari kuu au eneo la bahari kuu ambalo tunatakiwa sisi wenyewe tuweze kulilinda, tuweze kulitumia na litunufaishe kama ni sehemu ya rasilimali.

Mheshimiwa Spika, sasa huwezi kuwa na eneo kubwa kama hili halafu ukasema kwamba wewe huungi mkono wenzako ambao wanatumia vyombo mbalimbali kuweza kulilinda eneo hilo. Kwa hiyo, tukiridhia, hizo ni moja kati ya faida ambazo tutazipata.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo linakwenda kutupeleka sasa hivi, ni kwamba Serikali na mtazamo wa watu mbalimbali, tumeomba hapa kwamba, nchi hii iwekeze kwenye uvuvi wa bahari kuu. Tukiwekeza kwenye uvuvi wa bahari kuu na sisi sasa tunakuwa miongoni mwa nchi ambazo zinaingia kwenye ile wanaita Tuna World Market; Soko lile la Japani, kuna Soko la China na Soko lile la Norway, ambapo nasi tutapata fursa ya kuweza kuuza samaki wetu katika masoko ya nje.

Mheshimiwa Spika, faida nyingine ambayo imejitokeza hapa, ni kwamba zile meli ambazo tutazikamata zikichafua mazingira katika eneo letu la bahari kuu, tutaweza kupiga faini au kuweza kuzilipisha faini za uchafuzi wa mazingira pale kisheria, kuliko kusema kwamba tunatumia sheria zetu za ndani, kitu ambacho wale wanaotumia sheria za nje, hatuwezi kuwabana na baada ya kufanya huo uchafuzi wanakwenda zao, kwa sababu hakuna kitu au hakuna mkono wa sheria unaowakamata na kuweza kuwaadhibu kwa vitendo ambavyo wanatufanyia.

Mheshimiwa Spika, la mwisho katika faida ambazo zinapatikana, ni kulindwa katika ile wanaita Ocean Biological Weapons, ambapo katika eneo letu la bahari kuu huweza kutumika kwa uhalifu wa kibiolojia. Katika njia mbalimbali ambazo wenzetu nchi za nje zinatumia uharamia huo, eneo letu litakuwa linalindwa na vifaa maalum, zile VMS, maalum za Kimataifa kupita satellites na chochote kitakachopita katika eneo hilo kwa nia ya kufanya uhalifu wa kibiolojia, kisheria zitaweza kuchukua mkondo wake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawamba Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, turidhie, kwa sababu tukiridhia na sisi tutapata faida ya kuwemo miongoni mwa hao watu ambao ni wanufaika wa mkataba huu.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, nawaomba Serikali kwa upande mwingine, tuweze kushiriki baadhi ya mikutano na makongamano ambayo yanakwenda kutunufaisha na miradi mbalimbali ya kimazingira katika eneo letu. Bado tu tuendelee kuwakumbusha Watanzania kwamba, asilimia 67 ya tuna ambao wanaliwa duniani au wanaoingia katika Soko la Dunia, wanatoka katika belt hii ya Tanzania ambapo ni eneo lile la Kizimkazi mpaka Kitutio kule Mafya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, fursa hii iliyokuweko duniani mwote, tunaweza kusambaza samaki duniani, tuweze kuilinda na kuitunza. Ni kitu ambacho kwa kweli hakiwezi kupatikana, yaani faida yake haiwezi kupatikana kwa miradi mingine yoyote. Bado tuikumbushe Serikali kwamba eneo hili tukiwekeza, hakuna cha dhahabu, hakuna cha bidhaa nyingine yoyote itakayoweza kuishinda hii blue sea kwa kipato. Kwa hiyo, nawataka wadau mbaimbali, wawekezaji mbalimbali, waje tukae na Serikali, tuangalie uwezekano wa kuwekeza katika eneo hili la uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, fursa nyingine ambayo tunaipata sasa Tanzania, baada ya kuondoa ile 0.4, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hatua kubwa aliyoifanya na kuridhiana na wenzie wa Zanzibar na kuweza kumaliza tatizo lile la 0.4, sasa tunakwenda kurudisha leseni za uvuvi wa bahari kuu, na kuifanya Mamlaka ile ya Uvuvi wa Bahari Kuu kuwa na kipato cha ajabu sasa hivi. Kwa sababu, pending ya meli ambazo zinakaa zinagoja kufanya uvuvi wa bahari kuu ni zaidi ya 200 zinangoja leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, issue ilikuwa ni 0.4, Serikali imesikia kilio cha wadau, imekiondoa kwa muda hivi. Nami nasema kwamba, tukiweke pembeni, ili tuweze kupata faida ya meli zile ku-land katika maeneo yetu au kubaki katika maeneo yetu, ambapo kila meli itaweza kuacha zaidi ya shilingi milioni 40, ikija kutua katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, vilevile tusisahau; tujiandae sasa na kufaidika na by-catch ambazo zitakuja katika maeneo yetu, ambazo zitaziba gap lile la upungufu wa samaki, ambao wanahitajika kwa kupunguza lishe na utapia mlo uliokuweko hapa nchini. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kupata fursa hii japokuwa muda ni mchache. Napenda kuchangia zaidi, eneo la kwanza ni eneo la mbegu. Bado nchi yetu na Wizara hasa hatujawa serious kwenye mbegu. Nchi inapoteza fedha nyingi kwa ajili ya uagizaji mbegu.

Mheshimiwa Spika, taarifa zilizopo sasa hivi, tulitarajia na Waziri alikuja kutuambia hapa tunategemea kwamba tungeweza kujitosheleza kwa mbegu kwa asilimia 20 mpaka 30, lakini hali ilivyo kwa nchi yetu tumeweza kutoa mbegu siyo zaidi ya asilimia 19. Hivyo nchi imetumia zaidi ya trilioni 1.8 kuagiza mbegu kutoka nje. Maeneo tunayo, watafiti wapo, vituo vipo, tatizo hatujaamua kuwekeza katika eneo hilo. Namwomba Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla iangalie katika eneo ambalo tunapoteza pesa nyingi wakati uwezo wa kuzikabili hizo changamoto upo.

Mheshimiwa Spika, kingine katika eneo hilo, kuna tafiti ambazo zinahitajika ziweze kuendelea. Ile mbegu ya pamba tunayoendelea nayo mwaka huu ni wa mwisho, tunatakiwa tuwe tumetoa mbegu nyingine ambayo itachukua mbadala wake, kwa sababu ikiendelea kuzalishwa ile, huko mbele haitakuwa na mavuno yoyote, itakuwa imeshamaliza muda wake wa uzalishaji. Sasa sijui Wizara na Bodi ya Pamba ina mkakati gani katika eneo hilo. Naiomba Wizara tuangalie zaidi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala zima la pareto. Hapa kuna changamto hasa kwenye Bodi ya Pareto. Viongozi ni tatizo kubwa na ndiyo maana Sekta ile haiendi mbele. Bado tumewaruhusu baadhi ya watu ambao wananunua zile pareto zinakwenda kuchakatwa nje ya nchi, wakati mikataba ya kununua pareto tunataka kuiona ile crude oil inatoka hapa na kunufaisha watu wetu ndnai ya nchi wapate ajira lakini tupate raw material ambayo tunaweza kuitumia kwa uzalishaji wa vitu mbalimbali. Sasa leo mchakato wa umalizaji wa pareto unaenda kufanywa Kenya kwa sababu ipi?

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri hapa aje na majibu, atueleze sababu ni zipi wakati mikataba haiko hivyo? Ni kiwanda kimoja tu ambacho kinachakata hiyo crude oil na inapatikana hapa na tunauza na kuweza kupata faida na kodi zinatozwa. Kwa hiyo, tunaona tatizo ni Bodi ya Pareto na usimamizi wake bado umekuwa ni tatio kubwa.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kwa sababu ya muda, bado tunarudia tena kwenye Sekta ya Uvuvi, hatunufaiki. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuifanyia kazi 0.4, kule Zanzibar imeanza kuleta matunda. Juzi tu baada ya mwezi mmoja na nusu baada ya kuruhusu ile 0.4 ambayo ni probation period, zaidi ya meli 27 zimeshasajiliwa na tunatarajia meli nyingine zaidi ya 60 zitaweza kusajiliwa, hivyo kuifanya ile Mamlaka ya Uvuvi iweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi lililokuwepo, kuna akiba kubwa ya samaki ambao sasa hivi wanahitaji kuvuliwa. Ni eneo la buffer zone ambalo lipo baina ya Msumbiji na Mtwara. Eneo lile lina samaki wasiopungua zaidi ya milioni 50 wa tuna wazee walioko kwa miaka zaidi ya minne, mitano, wanahitaji kuvuliwa kwa percent maalum ambazo sisi kama nchi tungeingiza pesa nyingi tukaingia udau na wale ambao watavua kwa sababu sisi hatuna vyombo vya kuvulia. Samaki wale sasa hivi wanakula samaki wadogo wanaozaliwa katika eneo lile. Tunahitaji tuweze kujiwekeza katika eneo hilo, tuwavue.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili ni ombi. Wenye meli kubwa wakitaka kuleta ombi hilo kwa kuvua, tuwaruhusu kwa sababu akiba tuliyokuwa nayo katika eneo letu hilo la mazalio ya samaki kutoka Kizimkazi, Kitutio Mafia mpaka Mtwara ni zaidi ya milioni 70 ya samaki wako katika eneo lile, wanatosheleza kabisa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Rehani.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. SALUM MWINYI REHANI - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru kwa kuweza kunipatia muda tena wa kuja kuhitimisha hoja yetu tuliyoanza nayo asubuhi, lakini kwa makofi mengi yaliyopigwa hayo yanaanshiria kwamba sasa hivi niko ki-diplomatic zaidi. (Vicheko)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wamepata fursa ya kuchangia kwenye Wizara zetu hizi tatu, na mimi niseme wazi kwa dhati kabisa nimechukua maoni yote na mawazo waliyokuwa wametushauri. Yako ambayo yametolewa ufafanuzi na baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri na yako ambayo sisi kama Kamati tutakwenda kuyafanyiakazi. Hata hivyo na mimi nilitaka niyaweke sawa tu baadhi ya mambo ambayo yamejitokeza na kuahisi kwamba haya tutakwenda kuyafanyiakazi.

Mheshimiwa Spika, lilikuja suala zima la Sera na Sheria ya Ulinzi binafasi; hili lazima tukubali ukweli katika eneo hili watu wengi wameajiriwa na hatuwezi kutaacha kundi la watu zaidi ya 250,000 wasiwe na sera na sheria inayoweza kuwaongoza. Makampuni mengi kama tulivyokwishasema ni ya kurithiwa tu. Wazee wao walianzisha wao wakarithi watoto na hakuna sheria inayoweza kuwasimamia. Kwa hiyo hilo bado tutarudi kuweza kuhakikisha kwamba Wizara inaitekeleza na kuiwasilisha hapa Bungeni ili kuweza kupata sheria itakayoweza kuwalinda na kuweza kuwa na Mashirika au Kampuni ambazo zinajiendesha kwa sheria iliyo thabiti.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo limezungumzwa ni suala la NIDA; bado kwetu kama Kamati tumeliona kama ni donda ndugu. Watanzania wengi hawajapata fursa ya kupata Vitambulisho vya Taifa na bado wengine wako waliokuwa hawajaandikishwa. Sisi kama Kamati tumeshalizungumza lakini tunasema wazi kwamba bado tunakwenda kulikalia na kuhskikisha kwamba mitambo iliyokuwa imewekwa kuweza kutoa vile vitambulisho kwasababu tulikuwa na ahadi ya vitambulisho milioni 20 Disemba mwaka jana, ahado ambayo kwa mitambo iliyokuwepo haikuweza kufikiwa; kwahiyo tunakwenda kusimama na mitambo mipya kuhakikisha kwamba ahadi hiyo Watanzania wanapata vitambulisho vyao mapema na kila mmoja atakuwa anatambulika kihalali.

Mheshimiwa Spika, lingine dogo lilidokezwa na Mheshimiwa Masele; suala la uwekezaji kwenye sekta ya ulinzi; nalo hili tumelichukua na bado tutaendelea kuisgauri Serikali iweze kuwekeza kwenye suala zima la ulinzi wa nchi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Bobali aliligusia suala la mipaka; ni kweli kabisa Tanzania ina mipaka mirefu sana na hasa upande huu wa. Mimi nilipata fursa ya kuwa mwangalizi katika uchaguzi ule wa Msumbiji, maeneo yale ya Tunduru ukiangalia mipaka zaidi ya kilometa 70 na ina Panya road zaidi ya 300 na zaidi. Kwahiyo, hili nalo ni suala ambalo linatakiwa tujipange zaidi kuhakikisha kwamba haipitishi wahalifu katika maeneo yale.

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi linalojitokeza hapa, wenzetu, hasa wa ule upande wa Kusini wa Msumbiji wamekuwa wakijiegesha au wanasema kwamba wanatoa fursa ya kuolewa kwa wingi Tanzania ili kuweza kupata uraia wa Tanzania na hivyo kutumia fursa hiyo ya ile mipaka kuweza kujipenyeza na kuishi huku isivyohalali lakini baadaye wanakuwa halali kwasababu wengi wao wanaomba kuwa raia wa nchi hii.

Mheshimiwa Spika, suala la Magereza tumelichukua.

Mheshimiwa Spika, lingine lililozungumzwa hapa ni suala la Diplomasia. Mimi niseme wazi kwamba tunakwenda vizuri kwasbabu Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi, Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi kwa kweli tuseme wazi kwamba tumepata hazina nzuri, ni nguzo ya Nchi yetu, ana uwezo mzuri wa kuisemea Tanzania ndani na nje ya nchi. Katika eneo hili haogopi kitu na amekuwa akisimama kizalendo kuhakikisha kwamba thmanai na hadhi ya Tanzania inaweza kutambulika na kuweza kupewa hadhi inayostahili ndani ya sura ya Dunia. Nimpongeze sana na nishukuru kwa uzalendo na nguvu ambayo anaitumia kuhakikisha kwamba nchi hii haiweze kuonewa wala haiweze kudhulumiwa kwa njia nyingine yoyote ile. Sisi kama Kamati tuseme wazi kwamba tutashirikiana naye kwa karibu zaidi kuona kwamba tunaweza kufanikiwa kwa kila ambalo tumekuwa tukilipanga.

Mheshimiwa Spika, lakini hata lile ambalo tunasema kwamba halikuguswa, la maradhi ya Corona kule China tuseme wazi kwamba sisi kupitia Wizara hii tumezungumza kwenye Kamati na Mabalozi wetu wanafnya uratibu wa watu wetu ambao wako katika nchi mbalimbali duniani kuhakikisha wkamba Watanzania hawawezi kuathirika. Lolote litakalotokea nchi yetu itatoa taarifa kupitia viongozi hawa wa Mabalozi pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje kuijulisha hali ilivyo kwa maradhi haya lakini na maradhi mengine.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile nimdokeze Dada yangu Salome, kwamba nchi haijajitoa kwenye suala zima la ICC, bado maelezo yaliyokuwepo ya kwamba nchi imejotoa si kweli na tunajua msimamo wa Tanzania ulivyo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo tumeweza kulishughulikia kama Kamati ni suala zima la kuhskikisha kwamba diplomasia ya uchumi kwa Mabalozi wetu inafanyakazi; na ndiyo maana kipindi hiki cha karibuni wameletwa Mabalozi hapa nchini kuja kuona vivutio na fursa zilizopo ndani ya nchi na kujua kwamba wakienda kule wanakokwenda waweze kuitangaza Tanzania kwenye diplomasia ya uchumi. Wameona miradi mikubwa ya umeme, reli ya mwendokasi, Bandari pampja na utayari wa Watanzania tulivyoweza kujipanga kwenye suala zima la utalii. Moja ya task ambayo wamepewa ni kuhakikisha kila Balozi analeta watalii ndani ya nchi hii na kuongeza Pato la Taifa lakini kuongeza watalii ambao wanaitembelea nchi yetu hii ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache ambayo tumeweza kuyaangalia na kuyatolea ufafanuzi niseme wazi kwamba yale ambayo yaliyokuwa hayakuguswa au wale Wabunge ambao hawakuguswa mawazo yao yote tumeyachukua sisi kama Kamati tutayafanyia kazi na tutayaleta majibu yake kwa maandishi kwa wahusika ambao wanayahitaji hayo majibu.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo mimi nikushukuru na niombe tena kutoa hoja ili niweze kukamilisha hoja yangu hii ya report hii ya nusu Mwaka 2019/2020 kwa awamu hii ya pili.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi kupata fursa hii kuchangia hoja ya Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilitaka niunge pale ambapo mchngiaji amemaliza. Tanzania takribani tumekosa kwa wastani, tungeweza kupata, kwa mwaka huu, zaidi ya meli 54 ambazo zingeweza kutuingizia si chini ya bilioni zaidi ya 20 mpaka 30 za pesa ambazo zingeweza kuingia kwa tozo ile ya 0.4. Kwa kweli lazima tuseme ukweli kile ni kikwazo na hakuna mtu ambaye atakaekuja kwa ile 0.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili wenzetu Comoro tu hapo safari hii wamesajili meli 31 kwa kutumia gape hilihili, kwamba sisi tumeshindwa kuweza kutoa hiyo fursa ya kuondoa hiyo tozo, imetu-cost. Wao wanasema hawajawahi kupata mapato mengi yatokanayo na uvuvi kama mwaka huu kwa vile sisi tumeshindwa kutoa hiyo tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ndani ya maeneo yetu ya bahari tuna zaidi ya maili 360 zinavua katika ukanda wa Tanzania katika meli za mraba zile zaidi ya mia mbili na ishirini na tatu elfu zinavuliwa, watu wanavua; na hayo ni mataifa ya nje; na ndiyo maana ikapatikana ile takwimu ya asilimia 67 ya mapato wanayochukua nje yanatokana katika ukanda wetu wa uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, tunapoteza kiasi kikubwa na hii sekta tuseme ukweli bado haijafanya vizuri. Mimi nakataa kuniambia takwimu ya kwamba, samaki walioko katika Ziwa Victoria ni wengi zaidi kuliko walioko katika ukanda wa bahari, hiyo data mimi siikubali. Naomba tupate reference iliyo ya uhakika zaidi; kwa sababu meli za mraba zaidi ya 1,400 ukaseme kwamba eneo la Ziwa Viktoria ndio samaki wengi? Si kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, stock fishing imefanyika juzi baada ya miaka zaidi ya 20 na meli ile ya ki-Norway, taarifa rasmi hazijaja. Kwa hiyo Waziri utupe taarifa zilizokuwa sahihi zaidi kuhusiana na eneo hili. Bahari yetu bado ni potential, ina samaki wakutosha, lakini bado hatujafanya uwekezaji ulio sahihi tukaweza kuvuna samaki ambao wako katika maeneo yetu matokeo yake tunawafaidisha watu wengine ambao hawako Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jingine nililotaka kulizungumza ni kwenye sekta ya mifugo. Sekta ya mifugo pamoja na maelezo mengi na mazuri ambayo umeyatoa ya kukusanya maduhuli, lakini bado sekta ya mifugo inakabiliwa na changamoto nyingi; kwanza kwenye ngozi yenyewe. Kitendo kile cha kupiga chapa kimesababisha ngozi yetu ikose thamani na imejazana kwenye magodauni, hainunuliki popote sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ng’ombe wengi wamepigwa chapa, uchinjaji uliofanyika holela, hakuna viwanda vya kuchakata samaki matokeo yake ng’ombe wetu wanakosa thamani ya ubora katika viwanda mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi sasahivi umejitokeza mtindo kwamba wenzetu wa Nigeria wanakuja kuchukua zile ngozi kwa ajili ya chakula na si kutumia kwa ajili ya kuchakata kwenye viwanda mbalimbali. Kwa hiyo nafikiri tunahitaji tujitathmini na sheria zetu na kanuni zetu ili kuona kwamba suala hili ili liweze kuboresha mazingira tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa na watu wale wa kiwanda kile cha Magereza cha Luanda, bado wanasema ngozi zetu haziendani na thamani ya viatu ambavyo wanavitengeneza. Wakati mwingine wanalazimika kuchukua ngozi nje ya Tanzania kwa ajili ya uendeshaji wa viwanda vyetu. Tunahitaji tuone tunafaidika na rasilimali tulizonazo ndani ya nchi na si vinginevyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye suala zima la maziwa na hasa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Bado Serikali au sekta hii ya mifugo haijawekeza kwenye dairy farm. Tunahitaji kuwa na ng’ombe wa maziwa na si kuchunga ng’ombe. Watanzania wanachunga ng’ombe sana, lakini hawafugi ng’ombe inavyotakiwa, matokeo yake sasa tunashindwa kuweza kuingia katika soko la maziwa na sisi kuwa ni dampo la kuletewa maziwa kutoka nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zimbabwe imekuwa Tanzania ndio soko lake kubwa, Malawi sasahivi ndio soko lake vilevile, Uganda wanatuletea, Kenya wanatuletea, lakini sisi tunajisifu kwamba ni wa pili sijui wa tatu kwa kuwa na ng’ombe wengi hapa Tanzania, haileti maana kwa kweli. Tunataka tuone restructuring ya maana katika sekta ya mifugo na si hivi tunavyokuwa tunaelezwa kila siku, hatujafanya vizuri katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tunalolisema ni kwamba tunahitaji kuona kwamba viwanda vile vya maziwa vya hapa vinatengeneza bidhaa ambazo zinakubalika katika masoko. Tatizo letu bidhaa za viwanda vyetu haziingii kwenye soko la utalii. Sisi kule Zanzibar wale wanaoleta maziwa zaidi ya tani 40 kila mwezi zinashushwa pale na zinasambazwa katika ukanda wa hoteli za kitalii. Maziwa yale yangekuwa ya Watanzania pato lile lingerudi likaingia Tanzania, lakini maziwa yale unayaona ni ya Wakenya, Waganda, Wazimbabwe na Afrika Kusini, this is not fair. Tunataka tuone mabadiliko chanya sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Rehani, muda umeisha.

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nilikuwa na mambo mawili matatu lakini nitachangia japo moja atleast nami niweze kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ulikuwa kwenye suala zima la Madaktari, katika hiki kifungu cha 219 cha Veterinary Act Cap No. 319 Ibara 59 ambayo inatoa usajili wa Madaktari kwa mtu ambaye aliweza ku-attend course pengine au mafunzo ya mwaka mmoja. Neno Udaktari ni professional, sasa mtu ambaye ame-attend course ya mwaka mmoja leo tunampa usajili wa cheti cha Daktari it is not realistic. Tuwe realistic!
Mheshimiwa Naibu Spika, huu Udaktari wa Mifugo uliokusudiwa hapa, una nyanja nyingi. Mtu huyu inawezekana amekwenda kule ameshiriki course inayoitwa An Animal Production; leo unampa cheti cha Udaktari, ataua mifugo! Kesho mwingine anashiriki course ambayo inaitwa Animal Breeding, siyo Daktari. Angalau yule mtu ambaye ameshiriki Animal Health au Veterinary. Ukizungumza veterinary ni wale waliopata course ya miaka mitano ya Udaktari.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii nafikiri iangaliwe kwa jicho lingine, hawa watu bado hawajawa na capacity ya kula Daktari.huyu ni livestock attendance, ambaye yeye anaweza kwenda kule akatoa ushauri wa mifugo kwenye kada hii ya matibabu, lakini hawezi kuwa anatibu wala kupewa hii certificate au cheti ya kwamba yeye anaweza kutibu mifugo. Kwa sababu hapa unamwingiza kwenye kada ambayo anaweza kufanya mambo mengine makubwa zaidi. Anaweza kukuta kesi ya kutakiwa kuzalisha ng‟ombe katika maeneo mbalimbali au mbuzi; amekwama mtoto wa ng‟ombe au mbuzi, anaweza ku-attend course kama hiyo na kama ana cheti, basi hata kama akiua yule kiumbe pale, atajitetea kwamba yeye ana cheti cha kufanya vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri hili tuliangalie kwa jicho la ukubwa zaidi. Professional izingatiwe zaidi katika kipengele hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nataka kueleza kuhusiana na suala zima la adhabu hizi za viboko kwa hawa wanafunzi. Adhabu ya viboko bado naona kama ni nyepesi, haitoshi. Kwa wengine waliozoea, ni suala tu la kumlea. Kuna watu hata viboko haviwaingii ndani ya mwili wao; anaweza akapigwa hata kama ni viboko 30, akiingia, 30 akitoka, kesho yake unamkuta mtaani na anafanya jambo lile lile. Bado itafutwe adhabu ambayo itaweza kuwasaidia hapa, apate funzo huyu ambaye amepewa adhabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sawa ni watoto, tunasema kwamba tunachukua tahadhari kwa utoto wao, lakini kwa age zetu na mazingira yetu hapa, kijana wa miaka 18 anaweza akafanya uhalifu wa kuua, anaweza kufanya uhalifu mwingine wowote ule au akashirikiana na wahalifu kufanya jambo ambalo linakuwa kubwa zaidi.
Kwa hiyo, adhabu ya kiboko bado haijawa ni adhabu ambayo inaweza kumfanya yule mtoto aweze kujifunza kwa kosa alilolifanya au wengine kuweza kuwafanya waweze kujifunza kwa kosa walilolifanya. Hapa panataka pakaziwe, kidogo, kuwepo na adhabu ambayo kweli itaonekana hii amejifunza na imeonekana kwamba ni adabu kwa wengine waweze kujifunza kwa kosa ambalo anaweza kulifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliangalie kwa undani zaidi, tusichukulie kwamba labda huyu ni mtoto pengine labda ni miaka 12, 13 basi ukimtia bakora anaweza kujifunza, lakini wengine hawa bado unaweza kumpa njia akaweza kuendelea kufanya mengine zaidi. Hata hivyo, kwa wale ambao wanaweza kuweza kufungwa jela nao vile vile bado mimi nilikuwa na wazo lile kwamba kuna maeneo yale yalikuwepo kipindi cha nyuma, yanaitwa maeneo ya kuwafunza vijana, maalum kwa ajili ya vijana watukutu kama hawa, yangeweza kuimarisha maeneo hayo na ikawa adhabu mbadala kuliko kusema kwamba unampiga viboko, baadaye anaendelea kuweko mtaani, bado hajaweza kujifunza.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kupata fursa hii ya kuchangia hii miswada miwili iliyo mbele yetu. Kwanza nishukuru Mungu kwamba Serikali imeshtuka na kuweza kujitambua katika eneo hili. Na mimi ni-declare interest kwamba na mimi ni mtafiti na nimefanya hii kazi kwa muda wa miaka tisa, najua machungu na najua kazi inayotakiwa kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaloweza kusema la mwanzo, sheria hii ndiyo roho ya nchi ya uhai wa chakula cha nchi hii ya Tanzania. Dunia yoyote bila ya kuwa na utafiti/watafiti haiwezi kupata maendeleo. Tanzania tumekuwa siku zote watafiti kama watoto waliokuwa yatima; kila mmoja anafanya shughuli zake kwa mujibu wa anavyoona yeye na kwa mujibu wa fedha alikozipata. Lakini kuweko na sheria hii utaweza kuifanya nchi kuwa na mwelekeo na kuratibu hizi tafiti mbalimbali ambazo zimeshafanywa, na nyingine ambazo zinahitajika kufanywa katika utaratibu ambao wa kuleta maendeleo au tunaita research impact. Act hii imeweza kutuonesha mwelekeo sasa vipi tuweze kuelekea na vipi tuweze kujipanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo tulilokuwa nalo ndani ya nchi hii watafiti wamekuwa hawana coordination ya kuweza kujua kwamba huyu mtafiti anatakiwa afanye utafiti huu kwa ajili gani. Matokeo yake siku zote tunapata tatizo kubwa la asilimia 80 ya mbegu ambazo tunatumia katika mazao yetu tunaagiza nje au mbegu hizo zinatumika zile ambazo zilikuwa zimeshatumika miaka mitatu ama minne nyuma, yaani wakulima wetu bado wana ule utamaduni wa kutumia mbegu wanazoweka katika moshi; zikapigwa na moshi kwa muda wa mwaka mzima baada ya mwaka unaofuata zikaenda shambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa utafiti huu kutaweza sasa kuratibu utaratibu mzuri wa upatikanaji wa mbegu katika vituo vyetu mbalimbali vya uzalishaji mbegu lakini vile vile itawasaidia watafiti na Sheria ile ya Breeding Act kuweza kkujitambua na kutoa mbegu hizi kwa mujibu wa mahitaji ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi itawasaidia wajasiriamali mbalimbali waliohusiana na utafiti kuweza kupata soko la uzalishaji wa mbegu ambazo zitaweza kutumika nchini na kupunguza tatizo la upatikanaji wa mbegu mbovu, zisizo na viwango na zisizotoa mazao ambayo yanalingana na uzalishaji kwa eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linajitokeza, sheria hii itaweza kuisaidia nchi kuanza sasa kupata fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali vya taasisi vya utafiti duniani. Kuna mashirika manne makubwa duniani ambayo wao kazi yao kubwa kusaidia taasisi za utafiti. Kwa hiyo, kuanzishwa kwa mfuko wa utafiti utasaidia mashirika yale kuitambua nchi hii kwamba ina sheria ya utafiti na kuweza kuleta fedha zao ambazo zitawasaidia watafiti kwa kiasi kikubwa kufanya shughuli zao na kuleta mabadiliko chanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si hilo tu, hata kwenye vyuo vyetu vikuu ambavyo kwa kiasi kikubwa ndizo zinazoratibu na kufanya tafiti nyingi ambazo hazichukuliwi zikafanyiwa kazi. Sheria hii itaweza kuvifanya vile vyuo zile tafiti zao zitambulike na ziweze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa lililokuwepo ni database ya utafiti haipo, kila mmoja amekusanya data zake kwa mujibu wa vile alivyokuwa nazo yeye mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kubwa linalotakiwa hapa ni kuwepo na uratibu mzuri wa Mkurugenzi huyu wa TARI kuweza kukusanya taarifa za tafiti mbalimbali katika vituo mbalimbali na kuweza kuzi-publish lakini nyingine kuanza kuzifanyia kazi kama zilivyopendekezwa katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sasa hivi ni msimu wa kilimo katika maeneo yetu mbalimbali, Tanzania hii mikoa minne tu ndio yenye uhakika wa kupata mvua ya milimita 800 kwa mwaka, mikao iliyobaki mvua zake ni za kubahatisha; zipo chini ya milimita hizo 700 na wakati mwingine zinanyesha katika mazingira tofauti kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa utafiti kila Mkoa utaweza kusaidia sasa watu hawa wanatakiwa wapande zao gani, kwa wakati gani na kiwango gani ambacho cha mazao kinachoweza kutoka katika yale mashamba kulingana na uwezo wa uzalishaji na nyenzo zile alizozipata za kuzalishia. Lakini vilevile itaisaidia Serikali kuweza kuweka nguvu katika ile Mikoa ambayo ina uhakika wa uzalishaji, ili kupeleka mbolea na pembejeo nyingine kwa wakati unaofaa na kuwa na uhakika wa uzalishaji kuliko hali ilivyo sasa hivi, kila mmoja anakwenda kulingana na mazingira yanayomkabili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nimeliona na nililotaka kuchangia ni suala zima la kazi za hizi taasisi. Taasisi ina kazi nyingi na ni za msingi. Kwa bahati na mimi ni mjumbe wa Kamati hii, nilichangia mengi katika Kamati lakini yapo yale ambayo nilikuwa nataka kukazia tu. Moja kati ya kazi ambayo nlitakiwa kuhakikisha ina-coordinate ni kukusanya database ya utafiti iweze kuwa alive, iweze kuwa strong na kuwe na mfumo mzima wa upashanaji habari; hiki ndicho kitu kitakachoweza kutusaidia. Kwa sababu wavumbuzi ni wengi, wanavumbua vitu vingi lakini hakuna taarifa zinazotangzwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, juzi kulikuwa na kikao cha wavumbuzi waliokuwa wamefanya tafiti za kuzalisha miche bora ya kahawa ambayo inakubali katika mazingira ya baridi kama maeneo ya Arusha, Moshi, Mbeya na maeneo mengine ambayo yana baridi ambayo inafikia mpaka degree 18 na miche ile inafanya uzalishaji ulio mzuri. Taarifa zile ni nzuri, miche ile inakomaa au inazaa kwa muda mfupi lakini vile vile inastahamili yale magonjwa ambayo yanasababisha miche ile ieweze kufa. Kwa mfano leaf mina ni tatizo kubwa, coffee stem borer, wale ambao wana athiri katika maeneo yale, wamefanyia utafiti mzuri, wamepata tiba ya kuweza kuhakikisha kwamba miche ile imekuwa resistance na mazingira yetu. Kinachotakiwa sasa hivi ni kuwepo uhakika sasa wa kuisambaza kwa wakulima. Lakini vilevile kuwepo na taaluma ambayo itatolewa na mabwana shamba na mabibi shamba katika maeneo mbalimbali ili uzalishaji uweze kubadilika baada ya miaka mitatu. Miche mingi tuliyokuwanayo sasa hivi inazaa hasa kuanzia miaka mitano, lakini hii ya sasa hivi iliyokuwa imegunduliwa na vituo vyetu vya utafiti vya Arusha na KCU wameweza kutoa miche ya miaka mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hivyo tu kuna tafiti ambazo zinafanywa siku nyingi na bodi ya korosho, kule Naliendele, mpaka tafiti zile hazitangazwi, mpaka leo tafiti zile hazijaleta matunda. Kunachohitajika ni kupata mikorosho ambayo itazaa kwa muda mfupi, njia za kufanya hivyo zipo. Kumepatikana njia za kuweza kufanya grafting ya mikorosho ambayo itaweza kuzaa kwa muda wa miaka mitatu na ikifika miaka mitano tumeshafikia pick ya production na kuweza kupata matunda kwa muda mfupi, lakini yaliyo bora na yanayoweza kustahamili ukungu kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamefanya utafiti watu wengi lakini tafiti zile bado zipo kwenye makabati; tunahitaji zitoke, tunahitaji ziwasaidie wakulima waweze kuzalisha mazao kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine linalokuwa linaleta ukakasi ni suala zima la tafiti zinazofanyika hasa kwa nzi wa maembe au wadudu ambao wanaathiri matunda mbalimbali. Tanzania ilikuwa ni moja kati ya nchi ambayo inasafirisha matunda nje kwa kiasi kikubwa sana. Lakini kutokana na tatizo la kupatikana na hawa nzi wa maembe ambalo limekuwa ni tatizo kubwa hapa nchini tumeshindwa kabisa kuweza kuingia katika hayo masoko ya nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zipo za kugundua tiba ya hawa nzi wa maembe lakini vilevile tiba ya nzi ambao wanasababisha matunda mbalimbali kuweza kuharibika, lakini bado zimefungiwa kwenye makabati. Lakini watu tayari wameshachukua Ph.D kwa tafiti hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hii timu ya watafiti au huyo director aweze kukusanya hizi taarifa mbalimbali za tafiti na kuzitangaza ili watu ambao wanaweza kusaidia kutoa ufadhili wa kutengeneza hizo dawa au kununua hizo dawa nje ya nchi ziweze kuja, ziweze kutusaidia ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia katika Muswada huu. Nina mambo machache ya kuweza kushauri kwenye Bodi hii ya Kitaalam ya Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naona ili Bodi iweze kujengwa lazima ichukue majukumu ya taasisi na bodi nyingine zilizopo ndani ya Wizara ya Elimu ili iweze kujijengea sasa misingi ya kuweza kufanya kazi. Kwa sababu inasimamia elimu, lazima baadhi ya mambo yaliyokuwepo pengine NECTA, Chama cha Walimu au kwingine kokote ambayo yanahusiana na taaluma yaweze kusimamiwa na Bodi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi hii inatakiwa kwanza iwe na meno, kitu ambacho kwa kweli inabidi Waziri aje atueleze structure nzima itakuwa vipi mpaka kuweza kuijenga vizuri ili iweze kuwa na meno ya kufanya kazi hii ya kitaaluma. Kwa sababu hapa pana tatizo. Isipokuwa na meno bodi hii itashindwa kutekeleza majukumu yake na kitakuwa ni chombo tu cha Serikali kama vilivyo vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo tunaliona ni kwamba hapa Bodi hii inatakiwa isimamie na maadili ya walimu. Maadili yanakuwaje sasa? Wenzangu wameweza kuzungumza hapa ni kwamba maadili yanaendana na maslahi vilevile, yaweze kuwa sambamba ili kuweza kusimamia hayo maadili yenyewe. Kwa mfano, tofauti iliyopo kwa walimu wa vyuo na wale walimu wanaofundisha shule za msingi na sekondari inakwaza. Kwa sababu ukimchukua mwalimu mwenye degree moja au master’s akiweko chuoni anakuwa ni Assistant Lecturer, lakini akiwa shuleni anakuwa mwalimu tu wa kawaida na mshahara wanatofautiana. Kule pengine akianza kwenye chuo huyu mtu anaweza kuanza na Sh.1,800,000 lakini huku sekondari au shule ya msingi pamoja na master’s yake mtu huyu anakuwa anapata na Sh.800,000 na Sh.700,000. Kwa hiyo, hapo hakujawa na consistency ya taaluma hasa. Kwa hiyo, Bodi hayo ndiyo mambo inayotakiwa ijikite iweze kueleza na ichanganue madaraja ya walimu ili kuweza kuonekana hayo maadili yanayotakiwa kila mmoja anatekeleza wajibu wake kwa nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Bodi hii kwa mujibu wa maelezo ya Waziri hapa nilivyoipitia inataka kuangalia hawa walimu ambao wapo tu hapa nchini na hawatambuliki. Mimi nakubaliana na usajili wa walimu kwani unatusaidia kwanza kupembua wale walimu halisi kwa qualification na uajiri wao ulivyokwenda sahihi kabisa Serikalini na wale makanjanja ambao wamejipandikiza tu pengine labda amefukuzwa kazi, ametafuta sehemu ya kufundisha basi amepata amejiingiza katika hiyo tasnia. Wengine tunawaajiri, anafukuzwa huku anahamia mkoa mwingine anatengeneza mazingira anaajiriwa tena, tunajua hayo yanafanyika. Hivyo, usajili utasaidia kuweza kuwatambua hawa walimu, huyu ni nani na taarifa na qualifications zake. Hii siyo haifanyiki hapa tu, dunia nzima ndiyo iko hivyo, lazima kuwepo na usajili wa walimu na leseni lazima zilipwe, hakuna usajili wa bure, hivyo ndivyo ukweli ulivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika usajili huu tuweze kuwajua, ambao siyo wetu waondolewe. Kama tulivyoweza kuwaondoa wale wenye vyeti feki na vitu vingine, hawa wasio na qualifications nao basi tuweze kuona kwamba Bodi imesimamia na wanaondoka katika hii tasnia tubaki na ile cream ambayo tunaihitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tunataka kuona kwamba Bodi hii inashughulika na taaluma za walimu hasa huku chini. Kwa sababu duniani au huko kwa wenzetu, walimu qualification na vetting kubwa inafanywa kwa shule za msingi na nursery na ndiko kunakopatikana walimu wenye uwezo kabisa wa kujenga wale wanafunzi ambao juu wataweza kwenda kufanya vizuri. Tofauti na kwetu inavyoonekana mwalimu akishakuwa na diploma na degree hataki kufundisha chini, lakini inawezekana mwalimu huyu hajaiva.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wale walioiva taaluma iweze kufanya kazi kwa kuiva kwako tukupeleke utujengee foundation kwa wanafunzi wetu ili wakija juu tuwe tunapata urahisi kwa wanafunzi ambao wamejengeka vizuri. Hizo ndizo kazi tunazotaka tuione Bodi hii ina meno na kusimamia hili na isiwe inaridhia kila mtu anayekwenda, kwamba ameshakaa kule chini miezi mitatu anaomba akafundishe juu ameruhusiwa, amekwenda zake juu kwa mujibu wa taaluma yake. Kwa wenzetu Ulaya mpaka ukifika kukubaliwa kufundisha pengine nursery au primary School, umefanyiwa vetting ya kutosha. Naomba Bodi hii iweze kuwa na uwezo wa kupembua walimu ambao wataweza kujenga foundation nzuri na kujenga watoto ambao wanaweza kuja kufanya vizuri huku mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia taaluma hizi zina migawanyiko mbalimbali, baadaye Bodi hii iweze kutuwekea madaraja na taaluma mbalimbali. Kwa mfano, tuweze kuwa na Walimu wa Arts na madaraja yao; Walimu wa Sayansi na madaraja yao; Walimu wa Hisabati na madaraja yao; Walimu wa Fizikia na madaraja yao, ili sasa tuwe na cream ya walimu ambayo tunasema tukiwa na package ya walimu wa Fizikia ni hawa, wa Kemia ni hawa, wa Baiolojia ni hawa na masomo mengine tutaweza kuwa na mgawanyo mzuri wa hizi resources katika maeneo yetu na hasa yale maeneo ambayo tunahisi kwamba yana upungufu wa Walimu wa Sayansi au Walimu ambao wanahitajika, hasa wa Hisabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi Bodi hii naomba iwepo lakini vilevile naomba ikae pamoja na Mabaraza mengine ambayo yameshaundwa hapa nchini ili sasa iweze kujijengea uwezo. Wasiwasi wangu ni mmoja tu, hii Bodi itakapoundwa, hawa Wajumbe wa Bodi wanavyoweza kupatikana, niombe sana hapa siasa isitumike. Tunaunda Bodi ya Wataalam siyo Bodi ya Wanasiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hili lazima tulizungumze kwa uwazi. Tunapozungumzia taaluma, it is a special case, hatuhitaji siasa hapa. Kama mtu anapelekwa kwenye kuteuliwa na Rais awe professional. Kule kwenye Baraza la Watafiti tunasema kwamba lazima uwe on boat, kama haupo on boat hustahili. Tusichukue mtu tu ambaye ame-retire kwenye u-engineer au kwenye mambo yake mengine huko tunamleta hapa kwa sababu ana PhD au ana kitu gani, hapana! Tuwe na mtu ambaye yupo kwenye tasnia na anaweza kusimamia masuala haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia kwenye Mswada huu wa Fedha. Kwanza niishukuru Serikali na Wizara ya Fedha kwa wazo hili la kuweza kuondoa tozo hii ya vilainishi vya ndege (lubricants) ambavyo vinatumika kwenye ndege zetu mbalimbali. Hii tozo mbali tu kwamba itasaidia kuzifanya ndege zetu kuwa na huduma rahisi zaidi kuliko zinavyoweza kujihudumia sasa hivi kutokana na hii tozo. Vilevile, tutahamasisha sasa nauli za ndege katika maeneo mbalimbali kwa sababu gharama za uendeshaji zitapungua kidogo, tuna imani vilevile hata gharama za tiketi na mambo mengine zitaweza kuangaliwa kwa jicho la huruma zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo kwa kweli limenigusa moja kwa moja, ni tozo hizi za uingizaji wa haya majokofu. Hiki ni kitu muhimu zaidi kwa sababu sasa hivi kuingiza jokofu na kuwa nalo, yaani ukiwa na cooled storage katika eneo lako unatakiwa ulipe; kule kwetu sisi tunalipa karibu Sh.880,000. Inawezekana umeingiza mzigo kuhifadhi, inawezekana hujaingiza mzigo, lakini cost hizi ni kubwa sana na kwa kweli haziko friendly.

Kwa hiyo suala la kusamehewa haya majokofu yakishaingizwa basi zibaki zile tozo mbalimbali ambazo zinakuwa za kuingiza mzigo na kuweka lakini zile ambazo za kuingiza ziondolewe. Hiki kwa kweli ni kitu kimoja cha faraja na kitasaidia sasa kuweza kuchechemua wawekezaji mbalimbali na sekta binafsi kuanza kuwekeza katika eneo hili. Tanzania ni moja kati ya nchi ambayo kwa kweli ina tatizo kubwa la post-harvest. Asilimia 40 ya mazao yetu sisi yale ambayo tunasema mazao ambayo hayawezi kustahimili kukaa kwa muda mrefu yanapotea. Aidha, wakati wa kuvunwa, wakati wa kusafirisha lakini wakati wa kuhifadhi, kwa hiyo kupata punguzo hili au kuondolewa punguzo hili itawafanya watu mbalimbali wawekeze hivi vitu katika maeneo yetu ya mashamba na hivyo sasa kuwafanya wakulima kuweza kuhifadhi mazao yao na kupunguza ile post harvest loss kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo linaweza kuchachamua uchumi ni suala zima hili la vifaa vya plastic. Tunachokihitaji kwamba tuweze kuwa na viwanda ambavyo vitaweza kutengeneza hapa vifaa vya plastic hasa vinavyohusu kilimo. Kwa mfano drip irrigation kits, lakini pipe hizi ambazo tunatumia kufanya irrigation katika mashamba yetu. Utamaduni wa sasa hivi au mfumo wa sasa hivi wa umwagiliaji maji unategemea pipe irrigation. Plastic tools ndivyo vitu vinavyotumika kwa ajili ya kuweza kufanyia hiyo installment ya irrigation katika mashamba yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunachokihitaji kwamba, viwepo viwanda ambavyo vitaweza kutengeneza hizi bidhaa hapa nchini, mimi sina tatizo na bidhaa ambazo zinatoka nje na kutozwa kiwango kikubwa. Kwa mfano sasa hivi balton kit moja ya drip irrigation katika eka moja inagharimu karibu 2,400,000. Kitu ambacho wakulima wengi wanashindwa kuweze ku-afford na kuweza kununua na kuweza kutumia katika mashamba yao. Hali ya hewa tunaona tatizo tulilokuwa nalo hakuna uhakika wa mvua, lakini utakapopatikana unafuu huu wakulima wengi wataanza kulima kwa kutumia mipira hii ya maji, kwa hiyo hicho kitu kitaweza kusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo tunaliona kwamba litaweza kusaidia ni vifaa vya ukaushaji. Tuna tatizo Tanzania ukaushaji tunatumia jua na wengine wanatumia kuni kwa kiasi kikubwa sana hasa ndugu zangu wa kule Kanda ya Pwani na kwenye maziwa wanaovua dagaa. Ndiyo maana dagaa zetu kwa kiasi fulani nyingine zinakosa ule ubora wa food process inavyotakiwa ifanyike hasa kuzianika mpaka zikawa katika; wenyewe wanasema ziwe zimenyooka kama alifu, haziwezi kupatikana katika hali hiyo kutokana na methods ambazo tunatumia kwenye uanikaji.

Kwa hiyo tutakapopata hili punguzo watu wengi au wawekezaji wengi wataleta vile vifaa, watakuwa wanaanika kwa kukodisha hivi vifaa na kuweza kuipata hii bidhaa ambayo tutaweza kuisafirisha nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo tutaweza kusaidia ni vifaa kama vya green house, vitakavyoletwa hapa na kuondolewa hizi tozo itahamasisha kilimo hiki na watu wengi watalima kwa uhakika zaidi. Leo green house kit moja inauzwa kwa zaidi ya 8,000,000 ile wanaita 20 x 10. Tutakapopata punguzo hili itashuka na hivyo kipato cha mkulima kitapanda kwa sababu green house moja ukiitunza inakuletea 15,000,000. Kwa hiyo tukipata punguzo hili una uhakika wa kutengeneza 20,000,000 na una uhakika wa kuhakikisha kwamba mkulima umemkomboa na umemwongezea kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naliona kwamba litaweza kusaidia ni suala zima la huu ukaushaji kuweza kutengeneza viwanda vya ku-grind. Tunahitaji sana tomato powder ndani ya nchi, demand ni kubwa lakini hakuna viwanda ambavyo vinajitokeza kutengeneza tomato powder. Wenzetu Ulaya nchi kama Israel na nyinginezo tomato haiuzwi, hatuli tomato fresh kama tunavyokula sisi hapa. Tunakula powder ambayo unatia tu kama bizari kama mchuzi biashara imekwisha. Sasa hiyo biashara itaweza kuwa chachu sasa ya viwanda vidogo vidogo katika maeneo yetu tukipata hii tozo kuondolewa na kuhamasisha uchumi na kilimo kwa upande wa nchi yetu. Tutaweza kukausha tomato, tutaweza kukausha vitunguu, tutaweza kukausha vitunguu maji na bidhaa nyinginezo mbalimbali ambazo zipo katika maeneo yetu. Hata tangawizi tutaweza kuuza, tangawizi ya powder ambayo kwa kiasi kikubwa sasa hivi sisi tunaingiziwa ndani ya nchi kutoka nchi nyingine.

Kwa hiyo chachu ya viwanda vidogo vidogo katika maeneo yetu ya uzalishaji itakuwa kubwa zaidi kama hizi tozo zitaondolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, niishukuru Serikali kwa kulikubali wazo hili. Niombe kwamba sasa sekta binafsi uwanja na mlango umefunguliwa wazi, tuwekeze katika hilo eneo na tutaifanya Tanzania kweli kuwa ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)