Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ahmed Juma Ngwali (14 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii japo kwa ghafla.
MWENYEKITI: Niichukue hiyo nafasi nimpe mwingine?
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Aah okay, aah usimpe! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, lakini kabla ya kuchangia Mpango kuna jambo naomba niliweke sawa, japo nilitamani sana Mwanasheria Mkuu angekuwepo tukaenda sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya (1) naomba niisome, inasema: “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.” Kwa hiyo, sisi hapa kama Wazanzibari tumo ndani ya Tanzania na ni Watanzania. Hakuna Mzanzibari kwa mujibu wa Katiba kwa sababu Tanzania ni dola moja tu, wala Zanzibar siyo dora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaposema Wazanzibari wakatatue matatizo yao, huo ni ubaguzi ambao umekatazwa na Katiba. Haiwezekani tatizo linatokea Arusha, mkasema kwamba tatizo hilo ni la Waarusha tu, haliwahusu watu wa maeneo mengine; linawahusu Tanzania nzima. Kwa hiyo, hili naomba niliweke sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili watu wanasema kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haihusiki kabisa na masuala ya Zanzibar, lakini naomba niisome Katiba ya Zanzibar… nani kaikimbiza tena! Aah! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niisome. Ukisoma Katiba ya Zanzibar Ibara ya 119… imechukuliwa bwana! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 119(14) inasema kwamba; “Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar itashirikiana na Tume ya Taifa katika kuendeleza shughuli zao za uchaguzi.”
Sasa ikiwa Tume ya Uchaguzi ya Taifa ambayo ni ya Jamhuri ya Muungano inashirikiana na Tume ya Zanzibar, kwa hiyo, hata uchaguzi uliofutwa, Tume ya Taifa imeshiriki katika kufuta uchaguzi ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu kimoja cha busara sana; tumetoka mbali sana na Taifa hili, tuna maingiliano ya muda mrefu; tuna maingiliano toka karne ya 16 na nyuma huko, tumeishi kwa udugu sana, tumeishi kwa mapenzi, tumeishi kwa furaha wala hakuna tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na matatizo mengi yanayojitokeza madogo madogo, lakini yamekuwa yanapatiwa ufumbuzi na mambo yanakwenda. Leo isifike wakati Mpango huu ukawa hautekelezeki kwa sababu ya mtu mmoja tu peke yake. Nikimtaja mtu anayeitwa Jecha Salum Jecha, mseme laanatullah, kwa Kiswahili “laana za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi mbalimbali ambao wanaitakia mema nchi hii, naomba nimtaje kwa heshima kubwa Komredi Salim Ahmed Salim, alisema kwamba lazima tatizo la Zanzibar lipatiwe ufumbuzi, lakini pia Mheshimiwa Bernard Membe aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Awamu ya Nne, kwa ufasaha kabisa alisema tatizo hili lazima tulipatie ufumbuzi. Vilevile Jaji Warioba, watu hawa ni watu wenye heshima kubwa katika nchi hii, ni watu ambao tunawaheshimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tatizo lisichukuliwe kama ni tatizo dogo tu. Niwaambie kitu kimoja; tunapanga mipango hapa, hata Kenya na Burundi wana mipango wanapanga, inakuwa sasa? Mara Garissa limelipuka! Mara hapa, mara pale, kwasababu mnaonea watu waliokuwa hawana silaha. Watu waliokuwa hawana silaha, wanatafuta namna.
Kwa mfano, Waziri Mkuu aliyepita alikaa pale wakati Mheshimiwa Mama Asha Bakari, Marehemu, Mungu amrehemu, alipokuwa akisema nchi hii haipatikani kwa vikaratasi. Sasa ukisema nchi hii haipatikani kwa vikaratasi, maana yake ni kwamba, huo ni ugaidi, tutafute utaratibu mwingine. Hata Mheshimiwa Lukuvi naye aligusagusa sana kwenye swali hili, mtu mbaya sana yule! Tuendelee lakini. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme kwa busara kabisa, viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakae pamoja tuone namna gani wanalishughulikia tatizo la Zanzibar na uchaguzi usifanyike. Uchaguzi kwanza ukae pembeni, usifanyike tuone ni namna gani Serikali hii inatatua tatizo letu hili, kwa sababu mkiacha uchaguzi ule ukifanyika, na sisi tumetangaza rasmi kuwa hatushiriki kwenye uchaguzi ule; ninyi mnaona ni busara hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnaona ni busara, endeleeni na uchaguzi, lakini niwaonye kitu kimoja, Serikali mnanisikia vizuri sana, mpo hapo. Haya makundi yote yaliyojitokeza kama Islamic State, Al-shabab, Boko Haram yalitokana na kudhulumiwa haki zao. Haya hayakuwa bure! Hayakujitengeneza tu, yalijitengeneza baada ya kudhulumiwa. Sasa msije mkatuharibia nchi yetu kwa kumlinda mtu mmoja tu. Serikali ya Muungano mmewabeba sana Serikali ya Zanzibar! Mmewabeba mwaka 2000… (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ngwali!
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Naam!
MWENYEKITI: Huo mfano ulioutumia, chimbuko la hayo makundi uliyoyataja wewe, una ushahidi kwamba misingi yake ndiyo hiyo?
MWENYEKITI: Unaweza ukatuthibitishia hapa?
MWENYEKITI: Mimi nakusihi sana, ufute tu hiyo kauli yako, tusifike mbali.
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafuta kauli yangu, haina shida. (Kicheko/Makofi)
MBUNGE FULANI: Taarifa, Mheshimiwa Mwenyekiti.
MWENYEKITI: Taarifa! Keti tu Mheshimiwa Ngwali, muda wako umekwisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Spika, mimi jina langu naitwa Ahmed Juma Ngwali, siitwi Ahmed Ali Ngwali.
Mheshimiwa Spika, sihitaji makofi wala sihitaji vijembe. Nimekuja hapa na nimesimama hapa nina jambo langu ambalo naiomba Serikali inisikilize kwa umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna Sheria ya Wakfu, (Commission Ordinance) ya mwaka 1953, Sheria hiyo ikafanyiwa marekebisho mwaka 1956. Ilikuwa Sheria namba 7 na ikafanyiwa marekebisho ikawa Sheria Namba 9. Jambo la kushangaza, sheria hiyo mpaka leo ipo, Sheria hiyo inahusu Wakfu ya Waislamu. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Nyerere akaiacha hiyo commission hakuwahi kuiunda pia Mheshimiwa Rais Mwinyi akapita hiyo commission haikuundwa, akapita Rais wa Tatu Mheshimiwa Benjamin Mkapa pia hiyo commission haikuundwa na Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Jakaya Kikwete commission haijawahi kuundwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo mali za waislamu zimekuwa zikiibiwa. Hiyo commission ni muhimu sana kwa ajili ya maslahi ya waislamu na mali zao.
Kuna Sheria ya Mirathi ambayo ndani ya Sheria ya Mirathi sasa imeingizwa sehemu ya Sheria ya Wakfu ambayo imeeleza mambo mengi. Inashangaza sana! Sheria ya Wakfu ipo halafu ikatiwa ndani ya Sheria ya Mirathi.
Mheshimiwa Spika, mirathi na wakfu ni mambo mawili tofauti, hayafanani!
SPIKA: Mheshimiwa Ngwali, neno moja dogo tu….
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Naam.
SPIKA: Umesema mali za waislam zinaibiwa tukashtuka, ni kitu gani? Unaweza ukafafanua kidogo?
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Tunakwenda, tulia…
SPIKA: Ni jambo kubwa hilo!
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Spika, tulia!
Mheshimiwa Spika, nirudi hapo ambapo unapotaka sasa, kwasababu tu hii commission ya kusimamia mali za waislamu….
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Spika, Taarifa!
SPIKA: Mheshimwa Ngwali pokea Taarifa.
TAARIFA....
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Spika nimepokea vizuri na muda wangu nilindie.
Mheshimiwa Spika, tunachosema sasa ni kuiomba Serikali, hii commission ya Wakfu ianze kufanya kazi, kwa sababu sheria tayari ipo na kila kitu kipo, waislamu wengi wanapata shida na kuchelewa kwa Serikali kuanzisha wakfu hii kumesababisha mali za wakfu zilizowekwa waislamu hawajui ni kiasi gani zilikuwepo, kiasi gani zilizopo sasa, zilizouzwa na zilizofanyiwa mambo mengine. Kuna waislamu wengi wanataka kuweka mali lakini kwa sababu commission bado haijaundwa ni shida sana wanaogopa mali zao kupotea, hata mimi nataka kuweka wakfu.
Mheshimiwa Spika, katika hili tunaiomba Serikali kwa nia njema kwa sababu Serikali ina nia njema, hii sheria ipo, hawajaifuta, siyo tu kwamba hawajaifuta, wameitengenezea utaratibu mwingine mzuri ili kupitia katika Sheria ya Mirathi waislamu waweze kufaidika na hiyo Sheria ya Mirathi.
Mheshimiwa Spika, ikiwa Wakoloni mwaka 1953 walikuwa na sheria hii, wala jambo hili siyo la dini, jambo hili ni la kisheria. Wakoloni ndiyo waliokuja na dini, wao ndiyo waliokuwa na dini, kwa nini waliweka utaratibu kwamba watu hawa waisalmu waishi hivi na watu hawa wa dini nyingine waishi hivi, hivyo tunaiomba Serikali kwamba kama Rais hajateua au kama kateua atuambie hao watu aliowateua katika hiyo commission ni akina nani na kwa mujibu wa ile sheria Rais anayo mamlaka ya kuchagua siyo chini ya watu nane na katika hao watu watano watakuwa waislamu, pia Rais atachagua Mwenyekiti atateua na Katibu. Vilevile Rais atachagua kwa mapenzi yake anayoyaona na Tume ile inaweza kukaa kwa muda ambao Rais atapenda. Katika hali hiyo tunaiomba Serikali hii Tume ianzishwe.
Mheshimiwa Spika, suala la pili, nataka kuzungumzia Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo. Sheria hii inafanya kazi vizuri sana kwa upande wa Tanzania Bara lakini kwa upande wa Zanzibar hii sheria ni tatizo.
Kwa mfano, fedha zikitoka Hazina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinakwenda katika Ofisi ya Makamu wa Rais, zikitoka Ofisi ya Makamu wa Rais zinakwenda Hazina Zanzibar, zikitoka Hazina Zanzibar zinakwenda kwa Makamu wa Pili wa Rais, zikitoka kwa Makamu wa Pili wa Rais zinakwenda kwenye ofisi ya Haji Omar Kheir, Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, zikitoka hapo ndiyo ziingie katika Halmashauri za Majimbo. Sasa hii inashangaza sana, huo mlolongo hata hizo fedha zikifika inakuwa ni muda mrefu sana.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine baya zaidi ni kwamba pesa zile hazikaguliwi kwa sababu Mdhibiti na Mkaguzi wa Mahesabu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano hawezi ku-cross over akaenda kukagua Hazina ya Zanzibar. Kwa hiyo, kwa miaka mitano fedha zile au kama ushahidi kuna mtu alete ushahidi kama upo, miaka mitano fedha zile hazijakaguliwa! Mwisho wa siku wanakuja watu kutoka katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na karatasi zao eti wanakagua fedha ambazo zinatoka katika Hazina ya Jamhuri ya Mungano na ni fedha za Muungano. Wala sheria haijasema mahali popote kwamba mwenye mamlaka ya kwenda kukagua zile fedha ni mtu fulani kwa hivyo zile fedha za Serikali zinapotea, Serikali yenyewe ipo na haina habari! Naomba Serikali kwenye jambo hilo walitazame vizuri na sisi tutaweka input zetu katika kuleta maerekebisho ya sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nataka kuuliza ambalo ni dogo tu, ile Mahakama ya Kadhi imefikia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali tunataka mtuambie tu kwamba ile Mahakama ya Kadhi imeshindikana, haipo ama vipi kwa sababu ile mimi naithamini sana kwa sababu iliahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010-2015 ikasema kwamba ile ni moja katika mkakati wa Chama cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba Mahakama ya Kadhi inasimama.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki nijihuzishe sana na mazungumzo yaliyopita, naomba nijielekeze kwenye hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia hoja hii niliamua kwanza nipitie Sheria ya Baraza la Michezo, Sheria Namba 12 ya mwaka 1967 ikafanyiwa marekebisho na Sheria Namba 6 ya mwaka 1971 pamoja na Kanuni za Michezo na Kanuni za Usajili Namba 442 ya mwaka 1999.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipitia hii sheria, ukistajabu ya Musa utayakuta ya Firauni, bahati nzuri sana Mwanasheria Mkuu yupo, lakini Waziri wa Sheria Mheshimiwa Mwakyembe pia yupo. Naomba ninukuu Kifungu cha12 cha Sheria ya Baraza la Michezo, Kifungu hicho kinachohusu usajili wa vilabu kinasema;
“Msajili atakataa kusajili au kutoa msamaha wa usajili kwa chama cha michezo, ikiwa (a) Ikiwa ameridhika kwamba chama hicho ni tawi la au; kimeshirikishwa au; kina uhusiano na shirika au kikundi chochote chenye mwelekeo wa kisiasa isipokuwa chama au chombo chochote cha Chama cha Afro-Shiraz cha Zanzibar au chombo chochote cha chama hicho.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Afro-Shiraz ipo kwenye Sheria ya Baraza la Michezo, Chama cha Afro-Shiraz hakipo tena hata katika Katiba ya Zanzibar, hata katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini sheria hiyo tayari imeshafanyiwa marekebisho na bado Chama cha Afro-Shiraz kinaonekana baada ya miaka sijui mingapi kwa sababu ilikufa mwaka 1977.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata maswali mengi ya kujiuliza kwanza, kwa nini iwe Afro-Shiraz isiwe TANU. Kwa hiyo, inaonekana kwamba Waziri hata alipochaguliwa kuwa Waziri hata hii sheria hakuipitia. Inaonekana Serikali haipitii sheria na kuangalia sheria ambazo zinatakiwa kufanyiwa marekebisho. Jambo la msingi Serikali pitieni sheria ni aibu. Leo tunakuta Afro-Shiraz katika Sheria ya Michezo, ASP. Baada ya kuweka sawa hilo, tuendelee sasa na soka, mimi ni mdau mkubwa wa soka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana, Tanzania leo unasimama hapa unazungumza, ni ya mwisho katika viwango vya FIFA katika mpira wa miguu katika East Africa ni ya mwisho. Ya kwanza ni Uganda, ambayo inashika nafasi ya 72, ya pili ni Rwanda ambayo inashika nafasi ya 87, ya tatu ni Kenya inayoshika nafasi ya 116, ya nne ni Burundi inayoshika nafasi ya 122, lakini Tanzania inashika nafasi ya 129. Tumewazidi kila kitu hizo nchi nyingine. Hizo ni takwimu ambazo ukitaka kuzidadavua nenda kwenye website ya FIFA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana kwa sisi watu wa michezo kuona leo Taifa kama Tanzania ndiyo Taifa la mwisho kabisa katika soka kwa East Africa. Ukubwa wa nchi, uchumi wetu, tunapitwa na Kenya tu kwenye uchumi, kwenye population, kwenye eneo tuko juu. Maana yake ni kwamba hakuna mkazo katika michezo hasa soka mchezo ambao unapendwa na watu wengi Tanzania hasa ukifanya tafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Wazungu wanasema one swallow does not make a summer. Inashangaza sana leo Mheshimiwa Nape, alikuja kwa mbwembwe sana na kumtangaza kama Mbwana Samatta ndiyo shujaa wa Tanzania katika mpira wa Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni ya mwisho katika nchi zenye wachezaji wa wanaocheza Kimataifa. Tanzania ni ya mwisho, nataka nikupe takwimu. Tanzania ina wachezaji kumi tu nje ya nchi, Mheshimiwa Nape huwajui, nina hakika huwajui. Lakini Rwanda ina wachezaji 17 wanaocheza nje soka la kulipwa, Burundi wana wachezaji 25, Kenya wana wachezaji 32 wanaocheza nje na Uganda wana wachezaji 41. Watu wanajitahidi kadri siku zinavyokwenda kuwekeza katika mpira wa miguu, ndiko wanakotakiwa wawekeze kwa sababu mpira wa miguu, mfano chukua mchezaji mmoja tu, Victor Wanyama mchezaji wa Kenya anayecheza Southampton ya Uingereza analipwa kwa wiki pound 30,000 ni sawa na shilingi karibu milioni 300 kwa wiki moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnakwenda kuwekeza kwenye boda boda, hii ni Serikali gani isiyokuwa na mipango mizuri bwana eeh? Mnakwenda kuwekeza kwenye boda boda Rais anasema mshahara mwisho shilingi milioni 15, kwa mwezi Yaya Touré wa hapo Ghana anapata zaidi ya bilioni tatu kwa mwezi.
Jambo lingine ambalo ni muhimu sana ni suala la mapato ya michezo. FIFA wanakuwa na Financial Assistance Program (FAP) wanatoa dola 250,000 lakini wana Goal Project ambazo wanatoa dola 400,000. Tanzania Football Federation inapotoka nje kuwakilisha nchi inawakilisha kama Tanzania ambapo Zanzibar nao wanahitaji kupata hizo fedha. Hakuna takwimu zozote zinazoonesha kwamba Zanzibar wanapata hizo fedha, lakini kuna vyama tofauti vya michezo kama International Basket Ball Federation (FIBA) wanaleta fedha ndani, Zanzibar hatupati, tuna International Boxing Association wanaleta fedha hazipatikani, kuna Internationa Golf Federation zinakuja fedha kutoka nje hatupati, kuna Internationa Handball Federation hatupati fedha, kuna sports association chungu nzima za nje, Zanzibar hatujui mambo haya yanakwenda vipi, wala mambo yanakuwa vipi yaani tupo tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiisoma hii iko katika mambo ya Muungano, mambo ya nje ni mambo ya Muungano, kwa hivyo mnavyotoka International Zanzibar tupo. Zanzibar tukizungumza tayari unatoka nje tu ya nchi, tukiwa ndani fanyeni shughuli zenu za ndani lakini kwa nini mnapokwenda nje misaada ile ya kimichezo Zanzibar hatuioni au mnaipeleka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nape namalizia kwa kusema tunakwenda katika Olympic ya Rio de Janeiro 2016. Tanzania toka mwaka 1964 ina medali mbili tu za shaba, Kenya wana medali 86, wana medali 25 za dhahabu, kama haujaja na medali lazima ujiuzulu kwa sababu hatuwezi tena kuvumilia kuona kwamba Tanzania ndiyo imekuwa shamba la bibi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, siungi mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Kwanza nianze kwa kumpongeza Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa hotuba yake ambayo pamoja na mambo mengine neno Ngariba lilizua taharuki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na hoja yangu kwa kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nyuma huku kwenye Katiba katika orodha ya Mambo ya Muungano orodha ya kwanza, Kifungu Na. 15 kinachohusu mafuta na gesi, ambacho hivi karibuni mwaka 2015, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria tatu, Sheria ya Petroleum, Sheria ya Mafuta na Gesi ya Revenue na Sheria ya Ustawi wa Mafuta na Gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo linanisikitisha sana dhamira na lengo ya sheria hizi tatu ilikuwa ni kwamba, zinapitishwa sheria, baada ya kupitishwa sheria tunapitisha Katiba mpya, baada ya kupitishwa Katiba mpya, mafuta yanaondolewa katika Mambo ya Muungano. Jambo la kusikitisha ni kwamba, sheria zinaendelea kufanya kazi, kila mmoja kwa upande wake, lakini bado Katiba inatambua kwamba mafuta na gesi ni mambo ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni la ajabu sana, Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa mara ya kwanza kabisa na kwa ajabu kabisa, katika Sheria ya Oil and Gas Revenue Management Act ya mwaka 2015, Kifungu Na. 2 (2) kimetoa mamlaka kwa Baraza la Wawakilishi kutunga sheria, zinazohusiana na mambo ya revenue za mafuta na gesi. Jambo ambalo tunajiuliza Bunge la Jamhuri ya Muungano linapata wapi mamlaka ya kuitungia sheria, maana yake kuliagiza Baraza la Wawakilishi litunge sheria. Maana yake ni kwamba unafanya Baraza la Wawakilishi wanatunga sheria kwenye Mambo ya Muungano, jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 64 (3). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, chukua Katiba uangalie, kwa hivyo sasa jambo hili limetutia mashaka sana na Baraza la Wawakilishi tayari wameshatunga Sheria ya Oil and Gas ya mwaka 2016, sheria Na 6, Sheria ambayo inafanana kabisa copy and paste na sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hivyo, Legislature mbili zina sheria mbili za oil and gas. Jambo ambalo ukisoma Katiba Ibara ya 63 ile sheria ya Zanzibar inakuwa batili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyofahamu mimi na wanaojua sheria na watu wengine, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, linatunga sheria kutokana na Katiba ya Zanzibar, kwa hivyo, kuiamuru maana yake hata ungeiamuru kwa mfano, sheria ile madhali imepewa amri na sheria nyingine ile sheria itakuwa ndogo haiwezi kuwa sheria sawa na hii. Kwa hivyo, jambo hili linaleta utata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hata ukizitazama hizo sheria zenyewe lengo lilikuwa ni kuyaondoa mafuta katika Muungano, lakini sheria zile ukiziangalia zote zinasema sheria hizi zitatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, sasa unajiuliza ikiwa lengo kuyaondoa mafuta katika Muungano mbona hizi sheria bado ni za kimuungano,. Hilo ndilo jambo ambalo ni la kujiuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la kushangaza Katiba mpya ambayo ilikusudia kuja kuondoa hayo mambo ya mafuta na gesi katika Mambo ya Muungano haipo. Ukitizama Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020, nimeipitia ukurasa kwa ukurasa, hakuna mahali popote panapozungumzia kutakuwa na Katiba mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna mahali popote ambapo kaahidi kuleta Katiba, ukifuatilia maneno yake, maneno yake yalisema kabisa kwamba Katiba siyo ajenda yake, lakini jambo la mwisho hata ukitazama fedha zilizotengwa kwenye bajeti hakuna fedha kwa ajili ya Katiba mpya. Kwa maana hiyo, Katiba mpya haipo. Kwa hivyo, zile sheria kuendelea kufanya kazi pande tofauti ni makosa, ni kuvunja Katiba na ninyi watu mnaohusika na Muungano mpo, Mawaziri mpo, Mwanasheria Mkuu upo! Pia unatunga sheria za Muungano mambo ya mipaka baharini huweki, sasa mafuta ambayo yatagundulika baharini itakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupendekeza kwamba, kwa sababu pesa hamna za kuanzisha Katiba mpya, leteni Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tutumie kipengele Namba 98(1)(b) tuondoe mambo ya mafuta katika mambo ya Muungano. Itakuwa kazi rahisi sana, tutapiga kura tu third majority kwa kila upande kwa Muungano, tutaliondoa jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nilisemee ni suala zima linalohusu fedha za misaada, nakusudia kusema GBS pia na nizungumzie suala zima linalohusu Pay As You Earn na mambo mengine. Fedha hizi za Pay As You Earn zimekuwa ni tatizo kubwa sana, haziendi kwa wakati unaotakiwa Zanzibar, kwa hivyo Zanzibar inapata shida sana kwenye fedha hizi. Tunawaomba fedha hizi zifike kwa wakati unaotakiwa ili Zanzibar ipate kufanya shughuli zake.
Pili; fedha ambazo zinatoka katika Institution za Muungano ambazo zina-genarate fund, hizi fedha haziendi kabisa, tunaomba Serikali ya Muungano kwamba fedha hizi mzipeleke kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Wizara ya Fedha, miradi ambayo imeiva Zanzibar ni miradi ya International kama UN na mambo mengine na misaada mbalimbali inayotoka nje za nchi. Mnapopelekewa miradi ile iliyoiva Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha anachelewesha sijui kwa makusudi tuseme ama vipi, lakini ile miradi inakaa mpaka inafika wakati sasa hata gharama hiyo ya miradi yenyewe inakuwa imekwenda sana. Kwa hivyo tuiombe Serikali jambo hili pia nalo mlifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la fedha za Mfuko wa Jimbo; fedha za Mfuko wa Jimbo zinazokwenda Zanzibar hazijawahi kukaguliwa, nasema tena hapa kwamba hazijawahi kukaguliwa kwa miaka saba, hii ni kutoka na sheria. Ndiyo maana Jaji Warioba alipokuja na Tume yake akasema, tuna sababu ya kuwa na Serikali tatu, kwa sababu sheria haimruhusu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano kukagua fedha zile katika Hazina ya Zanzibar, kwa hivyo, fedha zile hazijakaguliwa na aje mtu anisute. Kwa hivyo, fedha za Serikali zinatoka kutoka Serikali Kuu ya Jamhuri ya Muungano, kwanza zinachelewa, zinakopwa na Serikali ya Mapinduzi, lakini hazikaguliwi, kwa hivyo sasa ifanywe kama ambavyo imefanywa kwa MIVARF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye MIVARF baada ya kukamilisha utaratibu wa mchakato wa tenda wa kufanya kazi pesa za MIVARF ambazo zinatolewa na Benki ya Afrika pamoja na IFAD zinakwenda moja kwa moja katika akaunti ya……..
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina ugomvi na Waziri lakini najua dhamira yake pia katika maslahi ya Taifa. Nataka niishauri Wizara pamoja na nchi kwa ujumla, nikumbushe kwamba mwaka 1997 Waziri Amani Karume wakati huo akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Waziri William Kusila kwa upande wa Tanzania Bara waliunda kamati ambayo ilikuwa ikiongozwa na Profesa Mahalu. Kamati ile pamoja na mambo mengine ilikuwa ikichunguza mambo ya Maritime Law. Kamati ile ilitoka na mapendekezo kwamba kuwe na chombo cha pamoja ambacho kitaweza kusimamia mambo ya marine kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kwa sababu kiujumla mambo ya marine siyo mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lile lilidharauliwa na wala halikufanyiwa kazi, kwa hiyo, mwaka 2001 SUMATRA wakatunga Sheria ya SUMATRA na wenzao Zanzibar wakawa wamenyamaza kimya. Lakini mwaka 2003 wakatunga ile sheria ya The Merchant Shipping Act. Sheria ya SUMATRA ikatoa mamlaka kwa Mamlaka ya SUMATRA kuweza kusajili meli. Mwaka 2006 Zanzibar walivyoona kwamba aah, hawa
wenzetu tayari wameshatunga sheria na mambo yanaendelea na wao wakatunga Sheria ya Maritime Transport Act ambayo ilifuatiwa na sheria baadae mwaka 2009 ya Zanzibar Maritime Authority (ZMA).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ushauri ule ulidharauliwa kilichotokea SUMATRA wakawa wanasaliji meli inapeperusha bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Zanzibar wakawa wanasajili meli zinapeperusha bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini katikati hapa hakuna chombo chochote ambacho kinawaongoza, kila mmoja anafanya vyake. Kama kuna chombo kilikuwa kinawaongoza nafikiri Mheshimiwa Waziri atuambie.

Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar wakasajili meli za Iran ambazo ziliwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa, meli zile zikaleta mzozo mkubwa. Kwa hiyo, baada ya kusajiliwa kwa meli zile wakafanya ujanja ujanja wenyewe kwa wenyewe wakalimaliza lile suala.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, baadaye Zanzibar wakasajili tena meli ambazo zilikamatwa na cocaine katika Bahari ya maji ya Uingereza ikiwa na tani tatu za cocaine. Kile chombo hakipo, baada ya kudharau ule ushauri haikupita muda sana, ikakamatwa meli ya Gold Star kule Italy ikiwa na tani 30 za bangi. Kwa hiyo, kile kitendo cha kukataa ule ushauri kwa sababu hili jambo siyo la kimuungano ukitoka katika foreign affairs linaingia jambo la Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Tanzania imekuwa ikiendelea kupata aibu na wanaofanya hivyo mimi nawajua na wanafanya kwa lengo gani. Viongozi waandamizi wa Zanzibar wanashiriki kikamilifu katika kuhakikisha kwamba wanajipatia fedha kwa njia ambazo hata Taifa kuligharimu haina tatizo.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa nazungumza na viongozi wa Zanzibar kuhusu hili jambo, wakaniambia kwamba baada ya matukio hayo kwanza wakaweka mfumo wa kielektroniki ambao sasa IMO wanakuwa wanaziona meli zikisajiliwa. Ule mfumo password waliyonayo SUMATRA, Zanzibar wakaitaka password SUMATRA hakuwapa. Nakubaliana nao wasiwape kabisa, kimsingi hapo sina tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar wanasema ukipitia sheria yao ile ya Maritime Transport Act, kifungu namba 8 wanadai kwamba 8(1) ukija (e) ukisoma huku kinasema kama ni Zanzibar wenye mamlaka ndiyo waliosajiliwa na International Maritime Organisation (IMO), SUMATRA wao hawajasajiliwa na IMO, kwa hiyo haki ya kupata password ni ya kwao.(Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshauri tu Mheshimiwa Waziri kwamba kwanza password wasipewe, pili; lazima tutengeneze chombo katikati hapa ambacho kitatusaidia kufanya mambo haya yasitokee tena. Kwa sababu kuna watu pale kazi yao wanatumia hii sehemu ya kusajilia meli kwa kujipatia kipato binafsi. (Makofi)

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikushauri kwamba ukae na timu yako mambo haya ni hatari kwa Taifa ili uweze kulitatua tatizo hili kiuangalifu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni bandari kuhusu suala la flow meter. Tatizo la flow meter lilikuwa ni kubwa sana katika nchi hii, mafuta yakiibiwa kulikuwa kuna vituo vya mafuta havina idadi. Bandari sasa na watu wengine wameanza wanataka pale flow meter iliyopo pale Kigamboni iondolewe ipelekwe TIPER, maana yake mahali ambako palikuwa pakiibiwa mafuta ndipo sasa wanataka flow meter iondolewe wapate kuiba mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ujajiuliza flow meter hii tumeifunga kwa dola za kimarekani milioni 16 mwaka mmoja uliopita, bandari wamepeleka watu sita training, wawili kutoka TRA, wawili kutoka Vipimo na wawili kutoka Bandari, wamepelekwa training kwa ajili ya operation ya flow meter, lakini watu hao hawapo wamehamishwa kwenye flow meter.

Mheshimiwa Naibu Spika, flow meter ile wanashusha mafuta machafu, flow meter inapiga alarm wanakwenda kuzima alarm, wanashusha mafuta machafu. Hawana dhamira njema, ukiwauliza wanakwambia pale flow meter ilipo itaharibika mara moja kwa sababu mafuta yanakuwa hayajatulia machafu, nani kawambia walete mafuta machafu! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanasema kwa sababu ya Kenya zile bomba ziko mbali na matenki yako mbali ndiyo flow meter ina uwezo wa kudumu siyo kweli. Kenya kwanza mabomba yote ni ya Serikali kutoka Mombasa mpaka Nairobi. Mabomba yanayopitisha mafuta ya Kenya tena yapo juu yanaonekana, ya Tanzania yako chini yamejificha yako chini kabisa, sasa watu wana uwezo mkubwa wa ku-bypass mafuta yale wakayachukua. Mheshimiwa Waziri hili usilikubali hawa wanataka kuiba mafuta kwa shinikizo la makampuni ya mafuta ili waweze kuiba mafuta. Kwa hiyo, suala hili Mheshimiwa Waziri lazima uwe mwangalifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu kwa nini watu mmewasomesha, Uingereza, South Africa, mmewasomesha Marekani kuhusu flow meter halafu mnakwenda kuchukua watu wengine mbali mnakuja kuwaweka sasa ambao hawajaenda training mahali popote. Wamepelekwa training miezi mitatu, kwa hiyo, lengo hasa ni kuiba mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri hili ukilikubali basi utaingia kama yule Waziri mmoja aliyeandika kwa maandishi kwamba suala la flow meter zisimamishwe ili wapime kwa kijiti wapime kwa kijiti, wanapima kwa kijiti halafu nchi hii bwana! (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, dhamira yako naijua vizuri sana.
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mimi nianze na ripoti ya ukaguzi wa fedha ambayo TFF wenyewe waliwataka TAC wafanye na waliwakabidhi tarehe 19 Januari, 2016 ripoti namba A/1/2015/2016. Ripoti hii ukifungua ukurasa wa 28 kuna fedha ambazo zimetumiwa na TFF kupitia Rais wake Jamal Malinzi ambazo haziko kwenye document na fedha hizo wamelipana wao wenyewe na pia wakakopeshana wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo amelipwa Michael Richard Wambura bila kuwa na ushahidi wowote ni shilingi milioni sitini na saba mia tano na senti hamsini na nne. Fedha ambazo imelipwa kampuni ya Panchline Tanzania Ltd. ambazo hazina ushahidi wowote na hizi kampuni ni kampuni zao wenyewe tunajua, ni shilingi milioni mia moja na arobaini na saba laki moja hamsini na nne mia mbili ishirini na tisa. Fedha nyingine ambazo zimelipwa zikiwa hazina ushahidi ni fedha ambazo wamelipwa Atriums Dar Hotel Ltd. ambazo zilikuwa ni USD 28,000 sawasawa na shilingi milioni hamsini na tisa, ukifanya grand total pesa zote ambazo hazina mahesabu yoyote na zinaliwa ni shilingi milioni mia mbili sabini na nne na kitu kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni ripoti, ukitaka ushahidi Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe nitakukabidhi, ripoti ya ukaguzi ambayo Wizara kwa vyovyote mnajua, Baraza la Michezo linajua lakini pia TAKUKURU wanajua lakini Serikali imekaa kimya haijasema chochote. Kwa hiyo, naomba Wizara kwa jambo hili ilichukue ilifanyie utaratibu na wakati wa ku-wind- up nitataka majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti nyingine ya ukaguzi ni hii ya fedha za wadhamini, tarehe siioni vizuri lakini imefanywa na ma-auditor wa Breweries. Ukiipitia ripoti hii TFF wametafuna fedha za wadhamini zaidi ya shilingi bilioni 5.5 na hii ripoti nitakupa. Tena hii ni ripoti ya ukaguzi, haya maneno hayatoki kwenye kichwa tu kwa sababu ya mapenzi ama vipi. Tumalize jambo la TFF twende mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina masikitiko sana, mimi ni mpenzi mkubwa wa soka, lakini sidhani kwa mtindo huu inaweza kukua wala sifikirii, wala sina mawazo hayo mimi nina mawazo mengine ambayo nitapendekeza baadaye. Kwanza nionesha namna gani soka haiwezi kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo wanakusanya TFF kwa ajili ya kukuza mpira wa miguu zinatoka FIFA ambazo ni fedha kidogo, ni dola 250,000 kwa mwaka. Fedha zinazopatikana Serikalini mnazijua hata kufika hazifiki lakini fedha zinazopatikana kutoka CAF ambazo sio nyingi ndiyo zinazotegewa lakini mpira hauwezi kuendeshwa na fedha hizo ni kidogo sana. Fedha nyingine ni za makusanyo za usajili wa kadi na fomu, wanasema players transfer fee, players contract registration fee, fedha kidogo sana hizo, league participation fee, fine as appeal maana yake hata ile fine ya timu ya Simba imo hapa, sponsorship deals na hizi ni mpaka zitokee na sales market right. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipendekeze na kwa mtindo huu tusifikirie kimaskini kama anavyofikiria Mheshimiwa Mwamoto kwamba twende zetu huko vijijini tukatafute wachezaji, hapana, tuiunganishe Wizara yako na Wizara ya Viwanda ili ile dhana ya Rais Magufuli kwamba tuwe na tuwe na uchumi wa viwanda iweze kufanya kazi. Tufanye kitu ambacho nchi nyingi wamefanya wamefanikiwa wanaita sports industries ambapo inakusanya michezo yote, hockey imo humo, mwendesha baiskeli yumo humo kila kitu kimo humo. Leo unataka kukuza michezo, unaletewa jezi kutoka China, unakwenda kununua mpira Pakistan, huo mpira unakuwaje? (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, nina masikitiko makubwa sana, tunafanya vibaya sana katika Olympic, vibaya tena vibaya sana. Mheshimiwa nikuulize kitu kimoja, kuna Wanyamwezi wengi sana, samahani Wanyamwezi, pamoja na Wasukuma basi tunashindwa hata kupata mtu wa kurusha tufe? Mheshimiwa Waziri unashindwa hata mtu wa kurusha mkuki, vifua vyote vile, nguvu zote? Mheshimiwa Waziri tukienda kwenye ngumi kila siku tunapigwa, basi nguvu zote tulizonazo tupigwe siye tu kila siku? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ni kwamba hatujaandaa watu wetu, hatujaandaa sekta ya michezo. Kwa hiyo, mimi nipendekeze tena tunapokuwa na hiyo sport industry tunakuwa na michezo mingi ndani, tusifikiri kimaskini, lazima tupate fund kubwa, tutumie PPP, tupate ma-expert, tuwashawishi watu, Serikali iingilie kati pamoja na sekta binafsi ili tuwekeze tuwe na Olympic Park, tuweze kukuza hiyo michezo vinginevyo tutakuja kusema Jamal Malinzi kapiga hela, tutasema maneno ambayo hayawezi kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo cha msingi tupate hiyo sport industry inaweza kutusaidia sana. Maana yake ni kwamba tutajenga viwanda ambapo mipira ya michezo yote tutaweza kuzalisha sisi wenyewe, tutaweza kuzalisha jezi sisi wenyewe, viatu tutaweza kutoa sisi wenyewe, ngozi za ng’ombe tunazo tunaweza kufanya kila kitu sisi wenyewe, hapo hiyo soka inayozungumziwa ndiyo inaweza kukua, tusifikiria kimaskini. Tukishakuwa na hiyo sport industry ndiyo tunaweza kufanya kitu, lakini ukisema leo tukatafute watu sijui Shinyanga, sijui wapi tuunde timu ya Taifa, sio rahisi kabisa. Kwa hiyo, mimi napendekeza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni muhimu sana, nirudi tena pale TFF. TFF ni Tanzania Footbal Fedaration maana yake ni kwamba Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tulitakiwa sisi tupate Makamu Mwenyekiti ama mbadilishe jina liwe jina lingine lakini mkisema ni chombo cha Tanzania halafu Zanzibar hawana ushiriki katika jambo hili inakuwa haliko sawa. Nafikiri tukae tuangalie upya namna gani tutawashirikisha Zanzibar katika hiyo TFF pamoja na kwamba Mheshimiwa Ally Saleh anasema siyo vizuri, lakini tutakaa pamoja tutalizungumza jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nizungumzie sanaa, sanaa imezidi imevuta mipaka sasa. Maana nyimbo sasa zinazoimbwa zilivyokuwa na matusi kama ninyi wenyewe Serikali hampo, sijui BASATA wanao-control wanafanya kazi gani? Michezo ya kuigiza (bongo movie) hizi, watu wanakaa wamevua mashati, wanabusiana, wanafanya mambo ya ajabu ajabu, huwezi kukaa na familia yako ukatizama, huwezi kukaa na mtu yeyote ukatizama na nyie mpo na nyie mnatizima, tatizo lenyewe na ninyi mnatizama. Hiyo ndiyo shida, utafikiri kama hatuna control. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, japo dakika zangu hazijaisha lakini baada ya kusema hayo niseme kwamba siungi mkono hoja mpaka Mheshimiwa Waziri atakapojibu hoja zangu, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza mimi nioneshe masikitiko yangu makubwa kwa Wizara ya Viwanda. Kimsingi niseme tu kwamba Kamati ya Bunge ambayo inasimamia viwanda na biashara ni Kamati ambayo inatakiwa imshauri Rais kuhusu mambo ya viwanda lakini kamati hiyo haijawahi kwenda hata gerezani kukagua viwanda wala haijawahi kwenda Kenya, China wala India; sasa sijui inamshauri vipi Mheshimiwa Waziri na viwanda vyake. Kwa hiyo, mimi nioneshe tu masikitiko yangu kwamba jambo hili si sahihi kwa kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hasa nilitaka kuzungumzia maeneo kama mawili ama matatu na hasa nataka kuongelea Tanzania and China Logistic Centre ya Kurasini. Mara ya kwanza mradi huu ulizungumzwa katika ile China-Africa Corporation mwaka 2009 kule Cairo. Mradi huu mwaka 2012 ulianza kuingia katika Bunge na kuwashawishi Wabunge. Katibu Mkuu wa Viwanda sasa Dkt. Meru alikuwa wakati huo mimi nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara alikuwa haondoki katika Kamati kama vile yeye ni Mjumbe wa Kamati na kuishawishi Kamati ikubali huu mradi wa Kurasini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulianza kutathmini ile thamani ya wale watu ambao wanatakiwa kulipwa fidia, uthamini ule. Uthamini wakati huo ukawa shilingi bilioni 60, tukashawishiwa kwamba lazima tufanye uthamini haraka haraka ili muda usije ukaongezeka huyu mwekezaji akakimbia. Hata hivyo tukakaa kwa miaka mitatu baadaye, tulipokuja kulipa shilingi bilioni 60 tukaambiwa fedha zimeongezeka shilingi bilioni 40 tena. Kwahivyo, tumelipa shilingi bilioni 101 badala ya shilingi bilioni 60; lakini baadae tukaambiwa mradi huo haupo, mradi huo umekwenda wapi ooh yule mbia kaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuna shilingi bilioni hizo zote zimelipwa wala huo mradi wenyewe haupo na tukashawishiwa kuambiwa kwamba mradi huu utaingiza ajira za moja kwa moja milioni 25 na ajira indirect zaitakuwa laki moja. Kwa hiyo, sisi tukaingia katika malumbano makubwa na Serikali kwenye jambo hili kutaka EPZA wapewe pesa ili huu mradi uweze kwenda. Mheshimiwa Mwijage mradi uko wapi? Mradi huna. Ukisoma huu mpango wa mwaka mmoja huoni hasa kipi ni kipi na Serikali ya China wakati ule ilisema kwamba itatoa shilingi bilioni 600 tukilipa shilingi bilioni 60, jambo ambalo mmetudanganya, hakuna kitu kinachoendelea baada ya miaka minne. (Makofi)

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwijage nataka ujibu hasa, usije ukatuambia maneno ya ajabu ajabu, uje ujibu hasa kwa nini mradi huo haupo na fidia imetolewa na fedha zimeongezeka na lini mradi huu utaanza na upo katika mpango wa mwaka mmoja, sidhani kama katika mpango huu tunaweza kuona jambo hilo, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumzia Mini Tiger Plan ambao mimi nina interest kwa sababu mradi ule ikiwa utasimama basi na Zanzibar itafunguka kiuchumi. Kwa hiyo, huu ni mradi kila siku nilikuwa ninauombea dua, ulikuja nao mwaka 2002. Ule mradi ukasema kwamba una awamu mbili; awamu ya kwanza ni kulipa fidia hekta 2500 lakini tufanye kwa ujumla, mpaka sasa kumelipwa shilingi bilioni 26.6; zinahitajika kulipwa shilingi bilioni 51.1 lakini mradi haupo na baadhi ya watu 1700 wamelipwa fidia na wengine hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kujua kwamba huu mradi upo? Ukitizama kitabu chenu cha Mpango wa Maendeleo ya mwaka mmoja utakuta kwamba hata huyo mwekezaji hayupo. Wakati ule tulikuwa tukiambiwa Oman na China wapo watakuja, na lakini Mheshimiwa Rais pia mwenyewe kasema kwamba hiyo sio priority yake. Pale palikuwa pana mradi wa bandari na viwanda lakini humu ndani mnasema kwamba mtajenga barabara katika eneo hilo la Bagamoyo, reli, umeme na maji. Ni reli gani itakayokwenda kule kwa mwaka mmoja? Jamani tuwe realistic katika mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, Mheshimiwa Mwijage utujibu, na huu mradi upo? Isije ikawa kama tulivyofanyiwa Kurasini, watu walikuwa wana deal yao wakalipwa fidia na baada ya kulipwa fidia mradi ukapotea na huku mnataka muwalipe watu fidia halafu mradi upotee kama ambavyo mmetufanyia huku.

Mheshimiwa Naibu Spika, milioni 400 CBE zimetafunwa na Mkurugenzi wa Fedha pamoja na Mkuu wa Chuo. Jambo hilo alilisema Mheshimiwa Waitara mwaka wa jana hapa, lakini hakuna ripoti yoyote. Badala ya kwenda kufanya ukaguzi Dar es Salaam ambapo ndiko zilikoliwa ninyi mkaenda mkafanya ukaguzi Dodoma na Mwanza, inawezekanaje? Fedha zimeliwa kwa wengine mnakwenda kufanya ukaguzi kwa wengine…

T A A R I F A . . .

MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeipokea taarifa hiyo kwa upendo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, twende sasa katika misamaha ya kodi. Nakubaliana na alichosema jana ndugu yangu Mheshimiwa Serukamba kuhusu misamaha ya kodi na kodi ambazo zinasumbua hasa upande wa Tanzania Investment Centre. Lakini ukija sasa kwenye maeneo ya uwekezaji SEZ misamaha ya kodi ambayo ipo haina haja ya kuongezwa tena, ni mingi sana. Naomba nisome baadhi ya misamaha ya kodi ambayo inawavutia wawekezaji katika eneo la uwekezaji la SEZ. Msamaha wa malipo ya kodi ya ushuru kwa mashine, vifaa, magari ya mizigo, vifaa vya ujenzi na bidhaa nyingine yoyote ya mtaji mkubwa itakayotumika kwa madhumuni ya maendeleo ya miundombinu ya uwekezaji katika maeneo maalum ya SEZ, huo ni msamaha wa kwanza. Lakini msamaha wa pili ni msamaha juu ya malipo ya kodi kwenye kampuni katika kipindi cha miaka kumi, msamaha wa tatu ni msamaha juu ya malipo ya kodi ya zuio la kodi, gawio na riba kwa miaka kumi, msamaha juu ya malipo ya kodi ya malipo kwa miaka kumi, msamaha wa ushuru wa forodha, kodi ya ongezeko la thamani na kodi nyingine; msamaha wa malipo ya ushuru wa stamp kwenye vyombo vyote vinavyofanya hivyo na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upendeleo ya uhamiaji hadi wa watu watano katika kipindi cha mwanzo cha uwekezaji na baadae wakizingatia masharti wataongezwa; msamaha wa malipo ya VAT. Kwa hiyo, kuna misamaha katika SEZ ambayo ni mingi sana EPZA, hakuna haja ya kuongeza misamaha kwenye eneo hilo. Tuangalie zaidi kwenye TIC tujue ni namna gani tunafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni kuhusu PVoC; tunazungumza ile Pre-shipment Verification of Conformity. Eneo hili ilipitishwa programu ya kuzuia bidhaa bandia kuingia ndani ya nchi, tukapitisha hiyo na TBS ikapitisha. Lakini jambo la ajabu toka mwaka 2012 bidhaa bandia zimezagaa katika Tanzania, TBS, FCC na FDA wapo. Sasa namna gani bidhaa zinazagaa? TBS aidha hawafanyi kazi yao vizuri kwa sababu kwanza kuna tatizo, tatizo lililopo ni kwamba TBS wanazuia sub-standard lakini hawana uwezo wa kuzuia fake kwa sababu substandard na fake ni vitu tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kikiwa chini ya kiwango na kitu fake vinatofautiana kabisa, kwamba ikiwa chini ya kiwango maana yake ni kwamba kile kitu sio halisia lakini halisia, unaweza kitu original kimetengenezwa na Kampuni ya Sony akakitengeneza mtu katika eneo vile vile kuliko kile lakini hicho kikawa ni fake na si sub-standard.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo bidhaa bandia Mheshimiwa Mwijage kila kona ya Tanzania inatusumbua. Mkiulizwa kila siku mnasema mnawafanyakazi kidogo na kuna vituo vingi, maana kuna vituo 38 au 48 lakini mnadhibiti vipi bidhaa fake? Hiyo ndio issue yetu tunataka. TBS wamekwenda mbali Tanzania mpaka tunaingiza mafuta machafu, TBS wanakwenda kukagua wanaruhusu mafuta machafu yanaingia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi leo nilikuwa na hayo lakini nimwambie tu Mheshimiwa Mwijage… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Ngwali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kuendeleza pale ambapo pameachwa na Mbunge wa Mkinga, Mheshimiwa Dunstan Kitandula juzi Jumamosi alipokuwa akichangia. Niseme tu kwamba Mheshimiwa Dunstan Kitandula alikuwa ni Makamu Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara katika msimu uliopita ikiongozwa na Mwenyekiti makini, Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hoja mbili tu na zote zitahusu mambo ya uvuvi. Nilipochukua kitabu hiki nilikuwa nikiangalia kwenye cover ya kwanza hapa nikaona hii eco culture, nilipoiona nikaona mambo mazuri, nikafungua ndani hakuna kitu kabisa, niseme ukweli. Unapozungumzia eco culture huwezi kuzungumzia kutengeneza bwawa fulani ambapo mabwawa yenyewe yametengenezwa na wananchi, lakini unazungumzia dhana pana sana ambayo ni lazima Serikali iwe imejipanga katika kuhakikisha kwamba hiyo eco culture (ufugaji wa samaki) ambao sasa hivi karibu nusu ya watu duniani wanakula samaki wa kufuga, inafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uwe na eco culture lazima uwe na fishing habours ambazo hutuna. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017, ametenga shilingi milioni 500 pesa za ndani kwa ajili ya utafiti pamoja na shilingi milioni 24 za nje kwa ajili ya utafiti. Hebu tukitoka Waziri nitampa clip, Kenya wametenga bilioni 6.6 kwenye eco culture sasa lazima uwe na hizo fishing ports ambazo zitakuwa na dry dock, kutakuwa kuna maji ya kutosha, kutakuwa na facilities zote, ndiyo unaweza kufanya jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia inatakiwa uwe na fisheries laboratory, hakuna lab zozote za kukagua hao samaki kama wana viwango au hawana. Inatakiwa kuwe na fish market, soko la nje na la ndani la kuuza samaki hao lakini pia ahamasishe walaji wa samaki kwa sababu kiwango cha kimataifa sasa hivi cha ulaji wa samaki, kila mtu anatakiwa ale kilo 20 kwa mwaka, Tanzania tunakula nusu yake, tunakula kilo nane kwa mwaka. Kwa hiyo, lazima fedha hizo zitengwe kwa ajili ya kuhamasisha watu wale samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia unatakiwa uwe na ile fish landing site. Sehemu ambayo utaweka hizi eco culture zako, ufugaji wa samaki ambayo imefanyiwa uchunguzi wa kutosha lakini na mazingira lazima yawe yameandaliwa, sijui kama Sekta ya Mazingira wana study yoyote waliyotoa juu ya suala hilo la ufugaji wa samaki. Vilevile unatakiwa uwe na viwanda vya kuchakata hao samaki, huna. Unatakiwa uwe na cold chain facilities pamoja na ice plant, huna. Sasa hao samaki jamani wana mipango gani, watuoneshe hiyo mipango ambayo kweli wanayo kwa ajili ya huo ufugaji wa samaki. Hamna mipango yoyote na haimo humu, humu wameandika tu, wamekaa na wataalam kaandikiwa Waziri, wame-copy sijui mahali gani, wameweka, hakuna kitu, hiki hapa kitabu hakuna chochote ndani yake, hiyo ilikuwa hoja yangu ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu kuu inahusu uvuvi katika Bahari Kuu. Uvuvi katika Bahari Kuu, hicho nacho ni kichekesho cha mwaka. Kwanza nataka kujua, wametoa leseni ngapi kwa mwaka huu na meli ngapi zilizokuja kuvua katika Bahari Kuu na meli ngapi zilizokamatwa lakini na mapato. Nataka kujua katika Bahari Kuu mwaka 2016/2017 wamepata kiasi gani? Nilikuwa nikizungumza na Zanzibar Makao Makuu juu ya suala la mapato wakaniambia na ni uhakika, vinginevyo itakuwa wamefanya tofauti hawakuwaambia wenzenu wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015/2016 fedha zilizopatikana katika uvuvi wa Bahari Kuu ilikuwa ni Dola za Kimarekani milioni 2.9 lakini mapato 2016/2017 yameshuka mpaka dola laki 6.9, mapato yameshuka. Watuambie kwa nini mapato yakashuka kwa kiwango hicho, ni kwa nini vinginevyo watakuwa wanafanya tofauti, Zanzibar hawajui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu tatizo lenyewe hizo pesa zinagawiwa katika mafungu matatu; 50 percent inakwenda kwenye mamlaka, asilimia 30 inakwenda kwa Jamhuri ya Muungano na asilimia 20 inakwenda Zanzibar. Sasa ukizigawa hizo pesa, dola 600,000 maana yake Mamlaka zinakwenda kama dola 300,000, ukija ukigawa 30 percent maana yake zinakwenda kama dola 100,000 na kidogo Jamhuri ya Muungano, Zanzibar zinakwenda dola 60,000. Sasa niulize, jamani ni kweli wako serious? Mapato ya Bahari Kuu nchi inapata dola 100,000, sawasawa na msimamizi wa ghala la unga la Bakhresa? Nchi inapata dola 100,000 mapato ya Bahari Kuu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu sasa walipoona hilo hawaliwezi, wakaja tena na jambo la ajabu, wakaja kubadilisha regulations. Wanasema wanataka kubadilisha regulations kwenye sehemu za kodi lakini tuzungumzie kuhusu bycatch, tuzungumze pia na mabaharia. Hizo regulations ambazo wamebadilisha, wanataka sasa kwamba wale wavuvi wanaovua Bahari Kuu, zile meli zikishapata samaki wale bycatch eti ichukue ije iwauzie katika nchi husika. Sasa mtu anavua katika Bahari Kuu mbali huko aje na meli mpaka ufukweni ambapo hiyo bandari yenyewe huna kwanza lakini na hiyo gharama ya mafuta na mambo mengine atazipata wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu uvuvi wa tuna ni uvuvi wa ndoano kwa hiyo haiwezekani. Halafu utajuaje kwamba wamepata bycatch wangapi, wala huna utafiti, wewe unaona meli ikiingia inakwenda kuvua utajuaje sasa, huwezi kujua. Kwanza nataka kujua ni meli ngapi zilizovua safari hii? Hizo meli zenyewe za kuvua hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda unakwenda mbio, nizungumzie suala zima la meli za uvuvi. Tanzania imesajili meli za nje ambazo zinapeperusha Bendera ya Tanzania 407, 407 ukizitia pale Dar es Salaam pote pale baharini zikipeperusha Bendera ya Tanzania huwezi kuona kitu. Katika hizo meli 407, Waziri hajui meli za uvuvi zilizosajiliwa ni ngapi au Waziri atuambie meli za uvuvi zilizosajiliwa ambazo zinazopeperusha Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo yenyewe haikusajili Jamhuri ya Muungano wala Zanzibar haikusajili imesajiliwa na Kampuni ya Feltex iliyopo Dubai, kwa hiyo hajui. Pia hajui ana mabaharia wangapi anasema sasa, katika hizo kanuni wanazobadilisha wataingiza mabaharia katika meli ambazo zitakuja kuvua, nani unampa leseni halafu unamwekea masharti, haiwezekani. Hata hizo kanuni mnazozibadilisha ni kiini macho tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watafanya vilevile kama lilivyokuwa zao la ngozi, zao hilo tuliweka 20 percent kodi kusafirisha nje, halafu tukaweka 40 percent kodi kusafirisha nje, lakini viwanda hakuna. Mwisho mwaka 2012 tukaweka kodi asilimia 90 ambayo ngozi ikawa inasafirishwa kwa njia ya magendo kwa sababu hata ukiiacha hapa inaoza. Sasa ndiyo hilo wanalofanya wao, wataweka kodi kubwa, wataweka sheria nyingi, mapato hayo wanayoyapata, hiyo 100,000 watakuwa hawapati, hilo ndilo tatizo lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema asilimia 90 kama ya ngozi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nianze na hoja yangu kwenye ukurasa wa 47 kitabu cha bajeti kwenye maneno madogo sana ambayo nataka kuzungumzia kuhusu Electronic Revenue Collection System; ambayo mfumo mpya ulianzishwa hivi karibuni, mfumo ambao kimsingi nakubaliana nao na nakubaliana nao kwa sababu kabla ya uanzishwaji wa mfumo huu makampuni ya simu yalikuwa yakikusanya fedha wenyewe baadae wakiwaita Serikali ndio wakiaanza kugawana mapato. Pamoja na kuwepo mfumo wa TTMS lakini mfumo wa TTMS ulikuwa haukusanyi kodi, hiyo ndio kasoro Mheshimiwa Zungu alipigia kelele sana ulikuwa haukusanyi kodi.

Kwa hiyo, sasa kilichoendelea nikwamba makampuni ya simu yalikuwa na uwezo mkubwa sana wakufanya ambavyo wanajua dhidi ya kodi ya Serikali. Na hasa napongeza hata kwa upande wa Zanzibar sasa kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiingiza vocha maana yake kodi ya Serikali pale pale inachukuliwa na kwa upande wa Zanzibar ukiingaza vocha kodi inachukuliwa pale pale inakwenda ZRB, kwa hivyo kiufupi nikukubaliana na Serikali kwenye jambo hili ni jambo zuri na linafaa kuungwa kuungwa mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nilikuwa nazungumzia suala la michezo ya bahati nasibu. Michezo ya bahati nasibu sasa hivi pamoja nakuleta negative impact katika jamii, lakini imekuwa ni sehemu ambayo kama Serikali watakaa pamoja kuifanyia kazi ni sehemu ambayo inapatikana kodi kubwa sana kwa Serikali. Kwa mfano, sheria iliyokuweko sasa inawapa Gaming Board kukusanya kodi, lakini kwa mchezo ambao ulivyoendelea lazima tubadilishe sheria, TRA kwa sababu wanamtandao mpana wao ndio waweze kukusanya kodi kila maeneo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na habari hii unaijua vizuri, nadhani katika bajeti ijayo kwa sababu nafikiri tumechelewa katika bajeti ijayo lazima tubadilishe sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ile GGR manaake ile Gambling Gross Gambling Revenue ambayo tunakusanya kwenye betting peke yake tuna- charge asilimia sita, asilimia sita ambayo kwa mujibu wa makadirio ya Gaming Board kwa mwaka huu kwa mwaka 2016/2017 basi tungeliweza kukusanya shilingi bilioni 24. Lakini kwa mujibu wa makadirio ya mwaka 2017/2018 tutaweza kukusanya shilingi bilioni 39 nukta kadhaa, lakini tukiongeza kutoka kwenye sport betting asilimia sita kwenda asilimia 20 pekeyake tutaweza kukusanya shilingi bilioni 37 kwa hivyo hilo ni eneo moja. Lakini katika casino pia tuna-charge sasa hivi katika pato ghafi la kamari tuna-charge asilimia 15, lakini tukiongeza tukifika asilima 20 manaa yake tutaweza kukusanya shilingi bilioni 20. Kwa hiyo hapo bado hatujaenda katika zile za slot machine; slot machine kwa sasa tunachaji shilingi 32,000 kwa slot machine moja.

Kwa hivyo lakini tukipeleka kwenye 60,000 tunaweza ku-charge shilingi bilioni 2.7 pia tunaweza kwenye upande wa competation yaani lottering Mheshimiwa Waziri wa Fedha tunapoteza fedha, lazima tubadilishe sheria. Sheria ile tubadilishe ili isiwe inamilikiwa na mtu mmoja, tuongeze watu ambao wataweza kuendesha lottery ya Taifa ili tuweze kukusanya shilingi bilioni 10 na inawezekana kabisa.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri mimi ningeomba katika bajeti ijayo jambo hili tukae jumla ya fedha ambazo tutazikusanya itafika shilingi bilioni 69 naa na kama TRA watakusanya vizuri basi tunaweza kufika hata shilingi bilioni 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu tuzungumzie suala la medical tourism, sports tourism na beach tourism. Medical tourism wenzetu wa Kenya wametenga kwa pesa za Tanzania shilingi bilioni 22. Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuonesha njia, tunayo ile Jakaya Kikwete Cardiac Institute tunapokea wageni mbalimbali ambao wanakuja pale sasa kupata matibabu. Lakini ina double impact ya kwanza tunapata fedha moja kwa moja kutoka kwa wageni. lakini wageni wale wakifika pia wanatumia fedha kwa ajili ya mawasiliano, wanasafiri, wanakula tunapata pesa nyingi kutoka kwao. Lakini kinachosikitisha mpaka sasa Serikali haikutenga fedha yoyote katika eneo hili jambo ambalo tukilinganisha na trains za standard gauge pamoja na ndege ambazo Serikali wanazinunua tukiweza kuimarisha sekta ya afya katika nchi yetu na mzunguko wa nchi zilizotuzunguka hiyo itaweza kutusaidia sana na itaisaidia Serikali kuongeza mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Mheshimiwa Waziri tunachokizungumza hapa ni kwamba hata sasa, hata hawa wataalamu ambao wanaendesha hiyo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete bado hatuna wa kutosha kutoka nchini kwetu tunaagiza watu mbalimbali wanakuja kufanya, hatujawekeza fedha kuwasomesha watu wetu katika eneo hilo. Kwa hivyo mimi niiombe Serikali kwamba katika jambo hili ijitahidi inavyopaswa lakini iweze kuwekeza fedha kwa mfano, Tanzania sasa hivi kwa mujibu wa takwimu za karibuni wanasafirisha Watanzania wanaokwenda India kutibiwa karibu watu 23,000. Ukitizama Kenya wanakwenda karibu watu 40,000; ukitizama Sudani watu 8,000; ukitizama Nigeria karibu watu 34,000 wanakwenda, sasa tungeifanya sisi tungepata fedha nyingi sana. ili Mheshimiwa Waziri nikushauri kwamba bajeti ijayo uhakikishe kwamba unatenga fedha katika eneo hili kwa ajili ya maslahi ya Tanzania na watu wetu na afya itaboreka nina uhakika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie tena suala la blue economy, Ethopia hawana hata bahari, bahari yao ndogo sana kule pembeni pembeni lakini wana meli commercial ship 18 Tanzania tumezungwa na bahari hatuna commercial ship hata moja. Mizigo yote yanapita baharini asiimia 95 hili ni eneo situ kwamba kila kitu kifanywe na Serikali lakini Serikali itakapoonyesha dhamira basi stakeholders watakuja kufanya hiyo shughuli si lazima mfanye ninyi, kwa hivyo eneo hilo nalo pia lina tatizo.

Mheshimiwa Waziri aqua culture yaani ufugaji wa samaki. Uganda wanatumia ziwa Victoria pekeyake aqua culture inachangia pato la Taifa asilimia 7.5 tuna maziwa tuna Victoria, Tanganyika, tuna Nyasa tuna na bahari yaani acro culture hatuchangii hata shilingi 100 katika Pato la Taifa haiwezekani, lazima Mheshimiwa Waziri tukubali maeneo mengine ya kuweka fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho Mheshimiwa Waziri ambalo niliseme ni kuhusu mambo ya madini; na mimi kwenye madini ni seme kidogo ili na mie niweke kumbukumbu sahihi. Usalama wa Taifa wako wapi? Mali zote hizo zilizoibiwa siku zote Usalama wa Taifa wako wapi? Na nini jukumu la usalama wa Taifa katika nchi? Ikiwa Usalama wa Taifa wameacha mambo yote haya yameharibika kiasi hiki, hata sisi pia siwanaweza kutuuza?

Kwa hiyo, nafikiri usalama wa Taifa wajitathimini wasitake kumbebesha mtu mwingine msalaba wakati wao wana access ya kujua mambo mengi yanayotendeka katika nchi. Kwa hiyo jukumu la usalama wa Taifa, Mheshimiwa Rais kimsingi tunakubaliana naye katika mambo ya kupambana na watu ambao wanafanya tofauti lakini hakikisha Kitengo/ Taasisi cha Usalama wa Taifa inarekebishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru asante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nianze kidogo na ufanyaji biashara baina ya Tanzania Bara na Zanzibar. Wakati anahitimisha Waziri wa Muungano na Mazingira, Mheshimiwa January Makamba alisema kwamba kutokana na kero za ufanyaji wa biashara kuwa nyingi, wanadhamira/wanakusudio kuiunganisha Zanzibar katika mfumo wa TANSIS ili kurasimisha kodi za pamoja baina ya Zanzibar na Tanzania Bara ili kuondoa hilo jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napingana sana na jambo hili kwa sababu unaporasimisha kodi za pamoja, Zanzibar watakuwa katika wakati mgumu sana, itawalazimu washushe kodi zao za ndani na mimi nistaajabu sana Serikali ya Muungano kwa nini watu wanachukua hizi baadhi ya kelele wanataka kuleta jambo ambalo litaongeza tatizo la mzozo wa Muungano kuliko ilivyo sasa. Kwa hiyo, niiombe tu Serikali kwa sababu dakika sina, hili jambo la kuiunganisha Zanzibar katika Mfumo wa TANSIS wasilifikirie kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Mheshimiwa Mwijage ni kwa nini Kenya, Tanzania na Zanzibar na nchi nyingine tu zimepiga marufuku kabisa utengenezaji na uingizaji wa mifuko ya plastiki katika nchi. Tuna viwanda 41 tu ambavyo vinatengeneza mifuko ya plastiki ambapo viwanda hivyo vinazalisha asilimia tano tu, asilimia 95 inakuwa imported kutoka nje. Sasa kuna tatizo gani? Nyuma ya mfuko wa plastiki kuna nani ambaye anashinikiza viwanda hivi viendelee na tuendelee kuharibu mazingira jambo ambalo litatusababishia madhara makubwa kama Taifa, nini nyuma yake kuna kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka niende katika suala zima la viwanda na umeme. Tumebishana na tumezungumza sana kuhusu umeme, wengine wanazungumzia kuhusu Stiegler’s Gorge lakini na wengine wanazungumzia kuhusu umeme wa gesi lakini energy mix ndiyo inayotumika duniani kote, hatuwezi kuwa na umeme wa kutegemea mfumo mmoja tu wa umeme. Lazima tuwe na umeme, huku upatikane na huku upatikane. Lengo letu sote tunajenga nyumba moja, lengo letu ni kupata umeme ambao utafika megawati 5,000 na zaidi. Hizo ndiyo dhamira ya Serikali na mimi nakubaliana nao kwenye energy mix kwenye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu Mheshimiwa Mwijage na Ofisi ya Waziri Mkuu, ninyi ndiyo mnaratibu mradi wa Bagamoyo ambao mkatutamanisha, mkatumbia eneo hili ni la SEZ tutapata kuweka, tutajenga bandari kubwa ambayo itakuwa meli za kizazi cha nne zitafunga. Wenzetu Kenya tayari meli zinafunga. Meli ya mita 300 karibuni tu ilifunga, sasa sisi meli meli kubwa ambayo MV Lienna ambayo ndiyo ina mita 420 tulidhani itakuja kufunga kabla Kenya haijafunga, lakini mpaka leo mradi huu unasuasua. Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inaratibu kwa sababu jambo hili linaratibiwa na watu wengi, inakuwa shida hamtuelezi, hakuna maelezo ya kutosha yanayoonesha kwamba jambo hili litamalizika kwa muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne kwa haraka haraka; Mheshimiwa Mwijage, Serikali iseme tu kama imeshindwa kuzuia bidhaa bandia zinazoingia nchini. Tumeanzisha mfumo wa PVOC ambao ni free shipment kule kuzuia lakini mpaka leo bidhaa fake zinaingia. Tumeanzisha hiyo halafu tukasema tutafanya Direct Inspection (DI) hapa bandarini lakini bado bidhaa fake zinaingia. Lakini polisi ambao unasema, nilikuwa nasoma kitabu chako mnataka kutumia mpaka Interpol kuzuia bidhaa fake. Polisi hao wenyewe ndiyo wanaoshiriki katika mambo hayo ya kuingiza hizo bidhaa feki, hiyo Interpol gani mnayotaka kutumia? Mheshimiwa Mwijage hilo rekebisheni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la tano Mheshimiwa Mwijage suala la gypsum. Gypsum paper zinaingia kwa asilimia 25, gypsum board zinaingia za asilimia 45. Sorry ni asilimia 25 kwa 25. Kwa hiyo, zikiingia 25, 25 ushindani ndani ya viwanda vya ndani haiwezekani kwa sababu tuna uwezo, tuna viwanda vinne vya gypsum kama sikosei, lakini vinazalisha gypsum board milioni 25 kwa mwaka. Demand ya Tanzania ni milioni 10 au 12, sasa tunalinda viwanda au tunabomoa viwanda? Kwa hiyo na hilo pia lirekebisheni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo la mwisho, sio la mwisho kama muda utakuwepo lakini kwa mfano teknolojia, tuna CAMARTEC, tuna TEGRO na kadhalika zinatumia teknolojia ya kizamani wakati mwendo wa teknolojia sasa hivi umebadilika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, anafanya vizuri, lakini Katibu Mkuu, mzee Iyombe, ni miongoni mwa watu mahiri ambao wanalazimu watambulike katika utumishi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na e-Government, Wakala wa Serikali Mtandao (eGA). Kabla ya kusema chochote napendekeza moja kwa moja kwamba Serikali ituletee Muswada wa sheria hapa Bungeni tuibadilishe eGA kuwa mamlaka. Nayasema hayo kwa sababu kama wakala hana uwezo wa ku-enforce, yeye kazi yake ni kushauri, hawezi kudhibiti wala hawezi kufanya kitu chochote ambacho hata mlaji anapokataa kufuata zile regulations na ile miongozo; kama wakala hana uwezo wa ku-enforce sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali ilete Muswada wa sheria hapa tubadilishe. Kwa sababu gani; kwa sababu katika dunia ya sasa ukitazama research iliyofanywa na cyberspace, inavyofika 2025, internet users watakuwa 4.7 billion, wanafunzi waliohitimu kwenye hisabati, sayansi, engineering, technology, watafika milioni kumi na sita kwa mwaka. Ongezeko hilo linahitaji uwepo wa chombo ambacho kitaweza kukabiliana na mabadiliko hayo (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eGA ikiendelea kubaki kuwa wakala haiwezi kabisa kukabiliana na mwendelezo huo mkubwa wa teknolojia. Kwa hiyo, niiombe Serikali ilete hapa Muswada na kama Serikali hawakujibu hili jambo tunaweza kupambana. Kadri teknolojia inavyoongezea ndivyo uhalifu unavyoongezeka. Idadi ya watu inavyoongezeka na uhalifu wa mtandao unaongezeka, hatujui sasa eGA wametengewa kiasi gani cha kuwawezesha kukabiliana na hali ya teknolojia inavyobadilika; hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya ambapo tunawazidi kwa idadi ya watu ambao wanakwenda kwenye milioni 50 sasa hivi watumiaji wa intaneti ni asilimia 85, wana about watu milioni ishirini na tisa. Uganda ingawa wana watu milioni arobaini lakini wanakwenda kwenye asilimia 42, Tanzania bado tumebaki kwenye asilimia 38, jambo ambalo linatufanya; kwanza eGA yenyewe ipo kwenye Serikali, haipo mahali popote, haipo nationwide. Kwa hiyo, hiyo ni sababu ya kwamba kama hatukuwekeza mapema, kama hatukuwekeza leo, tutajuta kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimalize hili nije kwenye Usalama wa Taifa; na hapa ndipo ambapo mara zote huwa nalisemea suala la Usalama wa Taifa. Usalama wa Taifa nafikiri hawana Kitengo cha Economic Intelligence Unit. Mheshimiwa Rais anasema katika mkutano na wafanyabiashara kwamba kuna kiwanda cha sukari hewa kilichokuwa kikiagiza sukari, Usalama wa Taifa hawajui. Baada ya kiwanda kuagiza na kuleta ndipo habari zinapatikana, kabla hawajaleta Usalama wa Taifa haukuiarifu Serikali kwamba jambo hili halipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaingia mikataba ambayo inaumiza nchi, why Usalama wa Taifa hauiambii Serikali? Au, je, kitengo hiki kwanza kipo na kama kipo kina uwezo gani? Je, teknolojia ipi ambayo inatumia? Mtuambie. Kama ni hivyo kimetengewa kiasi gani kwa ajili ya kuokoa uchumi wa nchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawapa mfano; kwenye tenda hizi za Serikali, mfano flow meter Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda kule kwenye flow meter bandarini, akasema kwamba hii flow meter itafanya kazi baada ya wiki mbili, flow meter haijafanya kazi hadi leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais akasema flow meter hii lazima ifanye kazi, flow meter haikufanya kazi. Tenda ya kwanza imepelekwa, mtu mmoja kapeleka kampuni sita, kampuni sita zikawa saba wakati wa submission akaondoa kampuni zote tano ikabakia moja; Serikali haijui. Wafanyabiashara wale wa mafuta wanachezea, tenda ikafutwa ikawekwa tenda nyingine, consultant akapewa bilioni mbili tenda ikaenda ikafutwa, Usalama wa Taifa sasa hivi wao ndio wameichukua tenda ili wafanye wao, haiwezekani. Haiwezekani hivyo, lazima tubadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Usalama wa Taifa, Mheshimiwa Waziri, nishauri kwamba hiki kitengo kisishughulike na haya mambo madogo madogo huyu kaandika nini yule kaandika nini, mambo madogo, wasimamie maslahi mapana ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize na Usalama wa Taifa nije kwenye hoja yangu ya tatu ambayo ni Shirika la Elimu Kibaha. Shirika hili liliingia mikataba mitatu na ndiyo maana nasema Usalama wa Taifa wana matatizo. Katika mkataba wa kwanza ulikuwa na hekta 310 ambazo Serikali imepangisha Shirika la Elimu Kibaha kwenye ile ardhi kwa miaka 66 kwa shilingi milioni 120. Sasa ardhi inapangishwa kwa miaka 66 kwa milioni 120, kweli jamani? Hizo pia zilipwe cash ili dola isije ikapanda kwa sababu iko in terms of dollars. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mkataba wa pili wa Kisarawe, kwa Mheshimiwa Waziri Jafo, pamoja na Kibamba, kuna hekta 110 umeingiwa pale na huyu Mkurugenzi kachukuliwa hatua kaondolewa tu; pamoja na yote haya aliyoyafanya lakini kachukuliwa kaondolewa kawekwa pembeni, hakuna hatua yoyote iliyofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Usalama wa Taifa sasa itabidi tusaidie sisi; pale Tanzania Internal Logistics Center, Kurasini, pale Serikali imelipa fidia hela nyingi, nasahau kichwani kidogo, lakini baada ya kuwekeza hayo makubaliano na China mwisho wamewekwa kiwanda cha misumari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imelipa bilioni sitini, niziache, lakini sasa logic yangu ni hii kwamba why unawekeza kiwanda cha misumari badala ya kuwekeza ile hub ambayo Mheshimiwa Mwijage alituambia Afrika Mashariki ndiyo itakuwa hub kubwa; kwa sababu Usalama wa Taifa hawajui kwamba hizo pesa zilizotolewa na Serikali bilioni mia moja kwamba zinafanya kazi anapewa nani. Zilikwenda kwenye mifuko ya watu na sasa kwa taarifa nilizonazo wamewekeza kiwanda misumari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niseme kuhusu hili ambalo tunalizungumza, juu ya vijana wetu wa Pemba waliochukuliwa. Tuiombe Serikali ya Muungano, sisi ni wenzenu, tukae pamoja tuone hili jambo, ni jambo dogo sana, hakuna sababu ya jambo kama hili tukapiga kelele kila wakati kuwaambia jamani hivi na hivi, hebu tukae pamoja tuone tunalitatuaje; kwanza ni kupatikana hawa watoto.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze hoja yangu na Kituo cha Uwekezaji cha TIC. Kituo cha Uwekezaji cha TIC kilianzishwa kwa malengo maalum ya kuisaidia nchi katika uwekezaji; kuratibu, kusimamia lakini kuishauri Serikali katika maeneo mbalimbali ili nchi hii katika uwekezaji iende mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha ni kwamba leo wawekezaji wamekuwa wapo katika taabu sana. Utamkuta Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, OSHA, Afisa wa TBS na Afisa wa TFDA, wote hao wana mamlaka ya kumkamata mwekezaji wakaita vyombo vya habari wakamwonesha hadharani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji yule ameleta pesa zake nchini, amewekeza, ameajiri Watanzania; hebu Serikali mtuambie, ninyi mnaona fahari gani? Mnaona sifa gani? Serikali inapata faida gani kumwonesha mwekezaji kama jambazi au mtu ambaye hana maana yoyote? Mtu huyu ameajiri watu chungu nzima na Serikali ipo na watu hawa wanaendelea kufanya mambo mabaya kama hivyo na wanaachiwa tu, hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba Serikali kwenye jambo hili mlikomeshe, likome kabisa, kwa sababu hali ya wawekezaji nchini; hebu niwaeleweshe kwamba wawekezaji ni jamii moja. Mnapomfanyia mmoja tu, dunia nzima inapata taarifa na wanaambiana. Ushindani wa kibiashara uliokuwepo sasa hivi katika nchi jirani, ninyi mnaujua. Kwa hiyo, siyo jambo jema, ni jambo la aibu kwa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni Kituo cha TIC. Kile kituo cha TIC cha huduma kwa pamoja (One Stop Center) kimewekwa pale kwa ajili ya kusaidia wawekezaji, lakini kile kituo Maafisa waliopelekwa katika eneo lile kwenye kile kituo, hawana mamlaka ya kumaliza hayo matatizo ya wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukitazama Sheria hii ya Tanzania Investment Act ya mwaka 1997 kifungu Na. 24 kinawapa mamlaka TIC kwa mradi uliosajiliwa pale, watano waruhusiwe waingie kufanya kazi katika hiyo kampuni. Wao wana hiyo sheria, lakini Sheria ya Kazi, The Non- Citizen Development Regulation Act, hii inasema sasa yule anaruhusiwa watu watano automatically, tena kwa mradi fulani, siyo kampuni. Sasa huyu Kamishna wa Kazi kumpatia hicho kibali sasa cha kufanya kazi inachukua miezi sita, miezi saba, jambo ambalo hizo sheria zina-contradict. Kwa nini ikiwa TIC sheria imeruhusu, halafu huyu mpaka sasa kuomba kwake anapata shida na mara nyingi zinakuwa rejection na TIC ndiyo wanaosimamia hiyo shughuli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye Kituo cha Uwekezaji, Sheria ya Immigration Act ya mwaka 1995, naye Kamishna wa Immigration lazima atoe kibali cha resident permit. Mwekezaji lazima awe na vibali viwili, lakini hao TIC wenyewe, ukienda kwenye kile kituo cha huduma kwa pamoja huwakuti wala hawana mamlaka. Hivyo nini maana ya kuwepo hicho kituo cha pamoja? Maana yake ni nini? Suala la vibali, tuseme ukweli, nanyi Serikali mnajua vibali vya kazi imekuwa tatizo, shida kubwa sana katika nchi hii. Kama wawekezaji ni wezi, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, Serikali inawachukulia wawekezaji, yaani mwekezaji anaonekana kama kaja katika nchi kuchukua mali za nchi. Mwekezaji siyo hivyo ilivyo jamani. Mheshimiwa Mavunde sasa hivi Kamishna wa Kazi amekuwa mungu mtu kabisa, imekuwa tatizo kubwa. Sawa, hilo tuliache, lakini katika uwekezaji tuna tatizo lingine ambalo lazima tulioneshe hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mabadiliko ya mara kwa mara ya vivutio vya uwekezaji. Wizara ya Fedha kama Wizara ya Fedha wanajua wanafanya nini kwa wawekezaji. Kwa mfano, ukipitia bajeti ya mwaka 2009/2010 Serikali ilifuta ile capital goods ikapelekea idadi ya miradi kushuka kutoka miradi 871 mwaka 2008 mpaka kufika miradi 500 mwaka 2010.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha katika bajeti ya mwaka 2012/2013 ilipunguza kiasi cha Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 100 hadi asilimia 90 na pia ikapunguza VAT kutoka asilimia 100 mpaka 45. Katika bajeti 2013/2014 Serikali ilipunguza kiasi cha msamaha wa Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 90 mpaka 75. Mambo hayo yote Wizara ya Fedha, vivutio vile vikiwa haviwekwi kwa mpangilio vikawa vya kudumu, mnawasumbua wawekezaji. Wawekezaji wanasumbuka sana. Mwekezaji anakuja kuwekeza leo katika nchi katika vivutio hivi, baada ya mwaka mmoja mnaondoa, hiyo siyo sahihi. Mnafanya vitu vya ajabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipendekeze kitu kimoja. Mheshimiwa Waziri alete sheria hapa Bungeni, ile TIC iwe mamlaka. Ikiwa authority, inaweza kutusaidia. Mnapoleta sheria, Maafisa wa TIC wakawa ni Maafisa wenye kuweza kuamua, ndiyo tutakapokuwa na maana, lakini ikiwa mtaendelea na utaratibu ambao upo sasa, hakuna chochote mtakachokifanya kikawa. Hakuna uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema ikiwa sheria hizi zitaendelea kuwa kama zilivyokaa kwa namna hii, kama hamjaleta sheria hapa Bungeni tukaibadilisha kuwa mamlaka kama ilivyokuwa Rwanda, Burundi na Kenya, haiwezekani. Maana yake hata tukifika hapa kuja kuzungumza haya maneno, inakuwa mambo yametufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufanyaji biashara na sijui msaada gani hasa Kituo cha Uwekezaji kinatoa kwa wawekezaji wa ndani. Serikali, kwa mfano Wizara ya Maji, inazuia watu wanaosafirisha mchanga kwa ajili ya kuuza wasifanye kazi usiku lakini kuingiza material mchana mjini, foleni yake unaijua. Mkandarasi anahitaji cubic meters 2,000 kwa siku, local investor ana uwezo kutokana na hali ya Dar es Salaam ilivyo na sehemu nyingine kupeleka cubic meters 100. Kuna nchi gani watu wanazuiwa kupeleka material usiku, kufanya kazi usiku jamani? Sisi tunaiga wapi ufanyaji wa biashara? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, lakini niombe Waziri wa Fedha hayupo lakini na Naibu wake anaendelea kufanya mazungumzo kwa hiyo hana concentration ya hiki ambacho nataka kuzungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwekezaji yeyote ili awekeze katika nchi lazima awe amepata mambo mawili; malighafi au soko. Mheshimiwa Rais ametembea Tanzania nzima kuhamaisha watu wajenge viwanda, Mheshimiwa Rais ana nia nzuri sana na mapinduzi ya viwanda, lakini tuna mifumo Tanzania ambayo Mheshimiwa Rais anahamasisha viwanda lakini hiyo mifumo inaua viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tuna mfumo wa stakabadhi ghalani, mfumo huu unaendeshwa kwa utaratibu wa auction kwa maana ya mnada, lakini ule mnada unaruhusu hata wanunuzi kutoka nje wanunue ile malighafi, kwa mfano korosho. Sasa unapokuwa na international mnada ule ukawachukua watu waliojenga viwanda, ukawahusisha na wanunuzi wa nje, watu waliojenga viwanda hawawezi kununua malighafi kwa sababu hawawezi kushindana bei na mnunuzi wa nje. Kwa hiyo viwanda vinajengwa lakini malighafi ile kwa mfano korosho inachukuliwa inakwenda nje. Sasa maana yake nini; maana yake viwanda vinakufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni lazima tutafute utaratibu, na nashauri tutafute utaratibu ambao tutakuwa tuna minada miwili ambapo mnada mmoja utawahusisha kupata malighafi viwanda vya ndani lakini mnada wa pili utahusisha viwanda vya nje na mambo mengine. Hilo jambo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kahawa, mwaka jana tu walijaribu kutaka ku-adapt mfumo wa stakabadhi ghalani, uliwagharimu sana. Viwanda vilijengwa, viwanda vipo vipya kabisa wakati wa ununuzi wa kahawa, kahawa ikanunuliwa na Vyama vya Ushirika, walipokwenda kutaka kununua kahawa wakaambiwa waende kwenye auction, walipokwenda kwenye mnada wanataka kuuziwa kahawa iliyokobolewa. Sasa nini maana ya kujenga hivi viwanda? Kwa hiyo tunaposema mapinduzi ya viwanda tuwe na utaratibu sasa wa kulinda hivi viwanda ili hizo malighafi zinazozalishwa Tanzania tuzipate.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, tunataka kukusanya kodi, kumetokea wajanja wachache wametengeneza programu inaitwa PVoC, PVoC ni programu ya kufanya ukaguzi wa bidhaa nje ya nchi, programu hii ilianza mwaka 2012 kama sikosei. Programu hii inamfanya TBS ambaye ndio Wakala wa Serikali katika ukaguzi huo imechukua mawakala, imeingia mkataba na mawakala, Bureau Veritas, CoC, wameingia na Intertek, wameingia na SGS. Hawa wanakagua bidhaa nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba bidhaa zile hazikaguliwi nje ya nchi. Mimi nimekwenda Japan, nimekwenda China, ukaguzi hakuna, lakini ili ukaguliwe lazima upate certificate ya TBS ya nchi husika. Sasa kinachofanyika, wao wakishapata ile certificate ndiyo wanakuandikia zile documents kwamba umekaguliwa lakini ukweli hawakaguliwi na unalipa dola 800. Sasa kwa nini tulipe dola 800 nje tusifanye direct inspection hapa Tanzania tukalipa dola 800 hapa? Wale mawakala wa kazi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nadhani kama huu unaweza kuwa ni mradi wa mtu. Kuna watu wana miradi yao na hakuna kontena ya biashara inayokuja Tanzania ambayo haina certificate ya CoC. Kwa hiyo hebu chukua containers elfu tatu kwa mwezi na kwa mwaka ni containers ngapi halafu hizo fedha zinalipwa nje ya nchi. kwa hiyo tunakosa mapato, Serikali inakosa mapato bila sababu na dhamira ya PVoC ilikuwa ni kuzuia bidhaa bandia zisiingie nchini, lakini bidhaa bandia zimeongezeka baada ya huo mfumo. Kwa hiyo hata hiyo dhamira haipo na fedha zinapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la nne, Mheshimiwa Waziri, amekuja ni vizuri; East African Comon Tariff wamefanya jambo jema sana; wamekwenda wameweka kodi kwa ajili ya kulinda viwanda vya ndani lakini kukuza biashara katika Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. Hata hivyo, wanapofanya hivyo wanasahau kitu kimoja; Zanzibar inategemea exportation asilimia 95, maana yake ni kwamba waki-copy kodi ambazo zimewekwa Afrika Mashariki maana yake Zanzibar hawawezi kuingiza bidhaa. Kwa hiyo ushauri ni nini; wanapofanya haya mambo Mheshimiwa Waziri wachukue walau Waziri wa Fedha wa Zanzibar wakae pamoja, otherwise Zanzibar ni lazima wafanye magendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tano, nimetazama katika vitabu vya Mheshimiwa Waziri vya miradi ya maendeleo, vya mipango sikuona kitu kimoja; tumejenga flyover ile pale TAZARA tumeondoa foleni pale tumepeleka foleni kule Vingunguti.

Mheshimiwa Spika, tutafungua Terminal Three kesho kutwa; tuna Terminal One, Terminal Two na Terminal Three; bora utoke South Afrika inaweza kuwa ukafika mapema kuliko kutoka pale mpaka Hyatt Regency Kilimanjaro. Sasa kwa nini Serikali isitoe Branch ya Standard Gauge ikapeleka moja kwa moja Airport ili tufanye usafiri wa kwenda Airport ukawa rahisi? Kwa sababu kwa sasa ikifunguliwa na hiyo Airport mpya maana yake traffic itakuwa ni kubwa sana. Kwa hivyo niiombe Serikali itafute utaratibu wowote unaona ambao unafaa lakini tuhakikishe safari za kutoka katikati ya mji kwenda Airport ni rahisi kiasi kwamba kila mmoja anaweza kwenda kwa wakati ambao anautaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho; sitaki niseme mengi; kwanza natambua uwepo wa Comrade Shamsi Vuai Nahonda Waziri Kiongozi wa zamani wa Zanzibar; lakini niseme kwamba tuna miradi ya maendeleo yanayohusu watu wa Zanzibar. Mheshimiwa Waziri Wizara ya Fedha imekuwa kikwazo sana kwa sababu hata wewe mwenyewe; Mheshimiwa Waziri wa Fedha sijui kwa nini hatupendi Wazanzibar. Kuna barua hii aliandikiwa kabisa na Saudia Fund for Development; hii ni original kabisa. Napenda Mheshimiwa; mpe aone ubaya wa Mheshimiwa Waziri Mpango.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiisoma utaona namna gani alivyokuwa hatupendi, ana roho mbaya kabisa. Mradi wa bilioni 26 BADEA walishasaini kwa miaka mitano nyuma, barua umeletewa hata kujibu hujajibu, basi si ujibu kwamba haiwezekani? Au kama haiwezekani basi tukopesheni ninyi Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mnajua kwamba Zanzibar hawawezi kukopa kwa sababu hawana sovereign guarantee, wanaokopa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa niaba ya Zanzibar, wewe unajua hilo. Kwa hiyo Mheshimiwa Mpango hebu tukuombe, hii barabara ni barabara muhimu sana kwa sababu Pemba kule tuna barabara moja tena imebomoka. Phase one mmefanya vizuri mmetutengenezea barabara tuwanashukuru, lakini tukubali hii barabara ya Wete Chake imalizike usitufanyie hivyo bwana. Mheshimiwa Mpango nitizame maana unaandika hunitizami kama vile kwamba hili jambo hulitaki kulichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, na nikuombe tu niende moja kwa moja kwenye hoja. Na hoja yangu itahusiana na maadili (LGBTQ).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Chombo hiki ni cha Kikatiba. Kimeanzishwa na kimetajwa katika Katiba, Ibara ya 131(1)(2).

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha kabisa ni kuona kwamba chombo hiki ambacho ndicho chenye haki ya kutupa taarifa za uhakika kimedharauliwa, hakifanyi kazi, kimekaa tu kinatoa taarifa ambazo zinamalizia huko. Kwa mujibu wa Katiba, naomba ninukuu, Ibara ya 131(3)(b) inasema;

(3) Kila mwaka wa fedha Tume itatayarisha na kuwasilisha kwa Waziri anayesimamia haki za binadamu taarifa kuhusu-

(a) shughuli za Tume katika mwaka uliotangulia;

(b) hali ya utekelezaji wa hifadhi ya haki za binadamu katika Jamhuri ya Muungano,

Na Waziri atawasilisha mbele ya Bunge kila taarifa iliyowasilishwa kwake na Tume mapema iwezekanavyo baada ya kuipokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu 2011 taarifa haijawasilishwa na sijui kama inafika kwa Waziri. Tume inatoa taarifa lakini taarifa ile inakaliwa, haiji. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba hali iliyokuwepo Tanzania kuhusu haki za binadamu ni mbaya kuliko tunavyofikiria lakini hatupati taarifa. Eti leo tunategemea taarifa kutoka kwa NGO tunategemea taarifa kutoka kwa mtu atuelezee habari ya human right katika nchi yetu? Haiwezekani. Sasa, kama hatuitaki Tume basi tuifute. Tume haina wafanyakazi, haina
bajeti, bajeti yake ndogo sana, haiwezi kufanya chochote, na tumeianzisha kikatiba kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kwanza ni kuvunja Katiba lakini pia kuvunja katiba ibara ya 18(2) kwa Tume kushindwa kutoa taarifa zinazoendelea kwa wananchi. Kwa wale wenye watoto nje ya nchi Amerika au Ulaya au Asia, kumlea mtoto nje ya nchi siku hizi ni bora na ni salama zaidi kuliko kumlea katika nchi yetu ya Tanzania. Hii ni kwa sababu watoto wa nje ya nchi wanaharibika, Ulaya na Amerika, sisi watoto tunawaharibu. Style ya maisha yetu ya kuishi, tutaishi na jamaa ndani ya nyumba huyu mjomba, kaka, shangazi, sijui nani, wale ndio wanaoharibu Watoto. Tume inaripoti kuhusu jambo hili na hizi ripoti hazitolewi kwa sababu wazee wenyewe wanaficha ripoti kwa sababu wanaona aibu, lakini hali ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu inashangaza, zamani ilikuwa kumtwaza mwanamke taabu sana, mpaka uandike barua, mwalimu aikamate, taabu sana. Siku hizi unapeleka simu unawekewa namba lakini zamani vitendo hivyo vilikuwa hakuna, leo vitendo hivyo vinatokea wapi? Na bado tume tumeitelekeza; hili sio jambo jema. Niombe Serikali kwamba, kwa hali ilivyo mbaya ni bora tuache taarifa ya CAG tusome taarifa ya Tume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili niseme kuhusu Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali. Tumeanzisha hiyo Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali lakini ipo chini ya Wizara. Tunashukuru Serikali imepeleka fedha kule kiwanda cha Dodoma, bilioni nane, vilevile tumepeleka kama bilioni sita kwa ajili ya kununua mashine. Sasa hawa watu lazima wawe wakala, lazima wajitegemee. Huwezi ukapeleka pesa ukaanzisha hiyo biashara halafu wakategemea OC kipuri kikiharibika wasubiri miezi mitatu wamemuandikia Katibu mkuu. Nafikiri tuuharakishe mchakato unaoendelea ili kumfanya huyu Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali awe wakala, na pia tumpe mapato na watumishi ambao wanaweza kufanya hiyo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana; wakati wa ziara ya Kamati tulivyokuwa tukienda kukagua miradi. Jengo la Msajiri wa Vyama vya Siasa ambaye anasajiri chama cha kisiasa kimoja kwa miaka mitano linajengwa kwa bilioni 20. Kwa hiyo jengo linajengwa kwa bilioni 20, kwani bilioni mbili haiwezi kujenga jengo? kwani bilioni tano hawezi? Jengo la TAKUKURU ni bilioni 24; tunaharibu fedha za Serikali badala ya kuziweka katika mambo ya maana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kile ambacho ni cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kinatumia bilioni nane tu, na mashine yake ni bilioni sita tu lakini ita-generate fund kwa bilioni 20 kwa mwaka. Lakini pia kama tutakiwezesha vizurini zaidi ya bilioni 40 hapo itafanya asilimia 55, lakini leo unachukua fedha unazipeleka kwa mtu anakaa na kiyoyozi anasajiri chama cha siasa, sijui anafanya nini, haiwezekani. Hatuwezi kutumia hivyo fedha za Serikali, fedha za Serikali lazima zitumiwe kwa utaratibu, kwa utaratibu huo hauelekei kama sisi ni nchi maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna majengo hapa yamejengwa kwa bilioni 100, tunayajua sasa haiwezekani. ingekuwa jengo hilo linajengwa ndani yake lina biashara hiyo sawa, lakini halifanyi biashara, jengo limekaa tu halafu nani ataliendesha? Halafu sie tupitishe bajeti hapa tukaliendeshe tena hilo jengo la bilioni 20 pamoja na maintenance yake, tupitishe hapa likafanye kazi? Haiwezekani hizo fedha sisi tuna haribu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.