Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jumaa Hamidu Aweso (6 total)

MHE. JUMAA H. AWESO aliuliza:-
Ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani - Saadani yenye kilometa 178 kwa kiwango cha lami ni ahadi ya muda mrefu ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Rais wa Awamu ya Tano:-
Je, ni lini sasa ujenzi huo utaanza hasa ikizingatiwa kuwa ahadi hiyo ni ya muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara wa Tanga - Pangani - Bagamoyo yenye urefu wa kilometa 178 ni sehemu ya Mradi wa Kikanda wa barabara ya Malindi – Mombasa - Lunga Lunga/Tanga - Bagamoyo. Mradi huu wa Kikanda unaratibiwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani – Bagamoyo kwa kiwango cha lami ilianza Januari, 2011 na kukamilika Novemba, 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Benki ya Maendeleo ya Afrika tayari imeonesha nia ya kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii. Taratibu za kumpata mkandarasi zitaanza baada ya kupatikana kwa fedha za ujenzi.
MHE. JUMAA H. AWESO aliuliza:-
Jimbo la Pangani linakabiliwa na tatizo sugu la maji hususan katika Kata za Mkalamo, Masaika, Mikunguni, Mkaja, Mwera na Bushiri.
Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hili ambalo limesababisha kuzorotesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa kata hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Nchini tangu mwaka 2006/2007. Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani imekamilisha miradi ya ujenzi wa miradi mitano katika vijiji sita vya Madanga, Jaira, Bweni, Kwakibuyu, Mzambarauni na Kigurusimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 kiasi cha fedha shilingi milioni 531.1 zimetengwa kutekeleza miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani ambapo kiasi cha shilingi milioni 55 zimeshapelekwa. Aidha, Serikali ilitekeleza miradi ya maji katika vijiji vya Mkalamo, Kata ya Mkalamo, Stahabu, Mtango, Mikinguni, Mikocheni na Sange Kata ya Mkwaja, Mwera katika Kata ya Mwera, Kipumbwi Kata ya Kipumbwi na Msaraza Kata ya Bushiri na Masaika Kata ya Masaika kupitia Awamu ya Pili ya
Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inayotarajiwa kuanza Julai 2016. Aidha, fedha zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ni shilingi milioni 668.2.
MHE. JUMA H. AWESO aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Pangani ina uhitaji wa X-Ray ili kutoa huduma hiyo kwa wananchi ambao hutembea mwendo mrefu kufuata huduma hiyo Tanga Mjini:-
Je, ni lini Serikali itapeleka X-Ray katika Hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani imeomba mkopo wa kiasi cha shilingi milioni 70 kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa ajili ya ununuzi wa X-Ray mpya katika Mwaka wa Fedha 2016/2017. X-Ray iliyopo ni chakavu kiasi cha kuhitaji matengenezo kila baada ya miezi mitatu kupitia wakala wake wa Philips. Kwa sasa wagonjwa wanapata huduma ya X-Ray kupitia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri imefanya mawasiliano na NHIF kwa ajili ya kupata mkopo huo na mazungumzo yanaendelea. Aidha, Halmashauri zinashauriwa kuweka kipaumbele katika kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa X-Ray kutokana na umuhimu wake kwa afya za wananchi.
MHE. JUMAA H. AWESO Aliuliza:-
Zao la nazi ni kitega uchumi na chanzo cha mapato kwa wananchi wa Halmashauri ya Pangani lakini zao hili linashambuliwa sana na ugonjwa wa mnyauko ambao umeliathiri zao hilo kwa kiwango kikubwa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kufanya tafiti kuhusu ugonjwa huo ili kupata dawa inayofaa ili kuwawezesha wakulima waweze kuendeleza kilimo hicho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa kunyong’onyea wa minazi (Lethal Dieback Disease) umekuwa ukifanyiwa utafiti kwa zaidi ya miaka 25 na Kituo cha Utafiti Mikocheni. Katika kipindi hicho aina mbalimbali za minazi ya kigeni mifupi na asili mirefu ilichunguzwa ili kuweza kupata minazi yenye ukinzani dhidi ya ugonjwa huo. Aina zote zilionekana kushambuliwa na ugonjwa kwa viwango tofauti. Minazi mirefu kutoka Mkoa wa Tanga na Lindi na aina mbili za minazi mifupi ilionekana kustahimili zaidi kuliko aina zingine ikiwemo aina ya East African Tall (EAT).
Mheshimiwa Spika, aina hizo za minazi inayovumilia ugonjwa huo imepandwa katika shamba la mbegu huko Chambezi na Bagamoyo na mbegu zinauzwa kwa bei nafuu ya shilingi 2,000 kwa wakulima wanaohitaji. Pia Kituo cha Utafiti Mikocheni kinaendelea na uchunguzi wa kubaini wadudu wanaoeneza ugonjwa huu. Aidha, kituo kinaendeleza ushirikiano na taasisi nyingine za Kitaifa na Kimataifa zinazotafiti ugonjwa huu katika kutafuta suluhisho la kudumu la tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, tiba ya ugonjwa huu haijapatikana hadi sasa, hivyo, wataalam wanaelekeza kuzuia ugonjwa huu kwa njia mbalimbali ikiwemo kupanda mbegu zitokanazo na minazi iliyoonekana kuwa na ustahimilivu wa ugonjwa; kukata na kuteketeza makuti ya minazi iliyoathirika mara dalili za ugonjwa zinapoonekana; kutopanda miche ya minazi iliyooteshwa katika sehemu zenye ugonjwa; kutoruhusu kusafirisha miche ya minazi kutoka sehemu zenye ugonjwa kwenda sehemu zisizo na ugonjwa; kuangalia matumizi mbadala ya minazi mipevu inayokufa kama kutengeneza samani na bidhaa nyingine zenye thamani; na wakulima kuchanganya mazao kwenye mashamba yao ya minazi ili kupata mazao mengine kutoka katika mashamba hayo endapo minazi yao itakufa kwa wingi kutokana na ugonjwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inashauri Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Wilaya nyingine zilizoathiriwa na ugonjwa huu kuwa na mipango ya kuendeleza zao hili kupitia mipango yao ya maendeleo kwa kuvisaidia vikundi vya wakulima katika Wilaya zao ziweze kupata mbegu zinazostahimili ugonjwa huu na pia kuanzisha vitalu vya miche bora ya minazi.
MHE. JUMAA H. AWESO aliuliza:-
Ujenzi wa barabara ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na hata ajira na mawasiliano. Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani –Saadani hadi Bagamoyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Tanga – Pangani – Saadani - Bagamoyo yenye urefu wa kilometa 246 unajumuisha madaraja makubwa ya Pangani na Wami Chini, barabara za mchepuo katika Jiji la Tanga na Mji wa Pangani pamoja na barabara zinazoingia kwenye hoteli za kitalii za ufukwe wa Bahari ya Hindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni sehemu ya Mradi wa Kikanda wa Barabara ya Malindi – Mombasa – Lungalunga – Tanga – Pangani - Saadani haadi Bagamoyo na unaratibiwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ilikamilika mwezi Juni, 2015 chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank). Aidha, kutokana na gharama za mradi huu kuwa kubwa, taratibu za kupata fedha kutoka African Development Bank na washirika wa maendeleo wengine zimechukua muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi milioni 4,435 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Tanga – Pangani – Saadani - Bagamoyo wakati taratibu za kupata fedha zaidi kutoka African Development Bank na washirika wa maendeleo zinaendelea.
MHE. JUMAA H. AWESO aliuliza:-
Licha ya Wilaya ya Pangani kubarikiwa kuwa na Bahari ya Hindi lakini wavuvi wa Pangani hawajanufaika ipasavyo na bahari hiyo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wavuvi wa Pangani mitaji na vitendea kazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya uvuvi nchini kwa kutekeleza mikakati yenye lengo la kuendeleza uvuvi nchini wakiwemo wavuvi wa Wilaya ya Pangani ili waweze kupata ajira, lishe, kipato na kuchangia katika pato la Taifa. Miongoni mwa mikakati hiyo, ni pamoja na kuondoa kodi katika zana za malighafi za uvuvi zikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu (twines) na vifungashio. Kodi hizo zimeondolewa kupitia Sheria ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 2014. Vilevile kupitia East Africa Publication on Common External Tariff, injini za uvuvi na malighafi zinazotumika kutengeneza zana mbalimbali za uvuvi na viambata vyake zimepewa punguzo la kodi ili kuwezesha wavuvi kumudu bei za vifaa hivyo. Pia Serikali inatoa ruzuku kwenye zana za uvuvi ambapo mvuvi anatakiwa kuchangia asilimia 60 na Serikali asilimia 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Pangani ni eneo la kimkakati katika masuala ya uvuvi na hasa uvuvi wa dagaa katika vijiji vya Kipumbwi na Pangani Mashariki na uvuvi wa pweza katika kijiji cha Ushongo. Serikali imewawezesha wavuvi wa Pangani kwa kuwapatia mafunzo ya kuongeza thamani na uvuvi endelevu wa pweza. Katika mwaka 2017/2018 kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa soko la samaki ambapo fedha imeshapelekwa katika akaunti ya Kata ya Pangani Mashariki ili ujenzi uanze mara moja. Kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo kutawanufaisha wavuvi wa Pangani na hivyo kupata mtaji na vitendea kazi katika shughuli za uvuvi. Natoa wito kwa Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Madiwani wa Pangani kufuatilia na kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha hizi ili lengo la Serikali la kuwawezesha wavuvi wa Pangani liweze kutimia. Vilevile Mheshimiwa Mbunge aendelee kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani na wananchi kupiga vita vitendo vya uvuvi haramu wa kutumia mabomu na hivyo kuhatarisha uendelevu wa rasilimali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa Usimamizi wa Uvuvi na Maendeleo Shirikishi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) imeendelea kutoa mafunzo ya uvuvi endelevu kwa wavuvi ambapo katika Halmashauri ya Pangani, BMUs tatu za Pangani Mashariki, Pangani Magharibi na Boza zimenufaika na mafunzo hayo. Katika mwaka 2017/2018 Serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa BMUs zilizobaki za Bweni, Ushongo Sahabu, Kipumbwi, Sange, Mikocheni, Mkwaja na Buyuni ambazo ziko ng’ambo ya Mto Pangani. Pia, Halmashauri ya Pangani imetoa uwakala kwa BMUs nne kati ya 11 za Wilaya ya Pangani kukusanya mapato ya uvuvi ambapo asilimia 10 ya mapato hayo wanapewa BMUs. Fedha hiyo ikitumika vizuri inaweza kuwapatia wavuvi wa Pangani mitaji na vitendea kazi.