Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mattar Ali Salum (14 total)

MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-

Kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) huandaa vijana kwa mafunzo mbalimbali kwa ajili ya kusubiri ajira katika vikosi vya ulinzi vya Muungano:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kutoa ajira kwa upande wa Tanzania Zanzibar?
(b) Je, ni asilimia ngapi ya vijana wanaoajiriwa kutoka upande wa Zanzibar?

(c) Je, kwa nini utoaji wa ajira katika Wizara hii kwa upande wa Zanzibar usijielekeze katika kwenye kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumu (JKU)?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salim Mbunge wa Shaurimoyo lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lina utaratibu wa kuandikisha Askari wapya kupitia Makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa. Jeshi la Kujenga Taifa hutoa nafasi katika Mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani. Kwa upande wa Tanzania Zanzibar nafasi hizo hutolewa kupitia Wizara inayoshughulikia Vikosi Maalum vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Vijana hao husailiwa kwa utaratibu uliowekwa na wanaofaulu hupelekwa katika Makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa kufanya mafunzo sawia na vijana wa kutoka Bara.

(b) Mheshimiwa Spika, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania halina utaratibu wa kuandikisha vijana kwa kufuata asilimia, bali ni vijana wanaokuwa na sifa zinazohitajika kuandikishwa bila kujali wanatoka upande gani wa Muungano.

(c) Mheshimiwa Spika, uandikishaji askari katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania haujielekezi moja kwa moja kupitia Jeshi la Kujenga Uchumi kwa sababu Kambi za JKU hazina utaratibu wa kuwaweka vijana wao makambini kama inavyofanyika katika Kambi za Jeshi la Kujenga Taifa. Vijana hao huripoti asubuhi na kurejea majumbani kwao ifikapo jioni, hivyo kusababisha kwa kutokuwepo kwa muendelezo mzuri wa mafunzo na malezi ya vijana wakiwa kambini. Kwa mantiki hiyo vijana hao hawapati mafunzo yaliyokamilika ikilinganishwa na vijana wenzao wanaopata mafunzo katika Kambi za Jeshi la Kujenga Taifa.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Mkokotoni kilichoko Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Kituo cha Polisi Mkokotoni bado haujakamilika. Hadi sasa kazi ya ujenzi wa kituo hicho imefikia asilimia 80 ikihusisha ujenzi wa jengo lenyewe, kupauwa na kupigia plasta kuta zote. Kazi kubwa iliyobaki ni kufunga milango, madirisha, kuweka sakafu, kupiga rangi na kununua furniture. Serikali inakusudia kumalizia ujenzi wa kituo hicho ndani ya mwaka wa fedha 2016/2017 kulingana na upatikanaji wa fedha za bajeti.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Makazi ya askari yamekuwa ya zamani pia mengine yamekuwa mabovu sana, mfano nyumba za Ziwani Zanzibar, Wete, Pemba na Chakechake Pemba hazikaliki kabisa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifanyia marekebisho nyumba hizo?
(b) Je, ni gharama gani Serikali itatumia kwa marekebisho ya nyumba hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo lenye sehemu (a), na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nyumba nyingi za makazi ya askari hazijafanyiwa ukarabati zikiwemo za Ziwani Zanzibar, Wete na Chakechake. Serikali ina mpango wa kuzifanyia marekebisho nyumba zote za polisi Unguja na Pemba kwa kadri uwezo wa fedha utakavyoongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama halisi za ukarabati wa nyumba zote za polisi Unguja na Pemba ni bilioni 1.5.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Wafanyabiashara wanaotoa bidhaa kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara hutozwa kodi Zanzibar na wanapofika Tanzania Bara hutozwa kodi tena; vilevile, wafanyabiashara wanaotoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar, hutozwa kodi tena Zanzibar. Hali hii husababisha wafanyabiashara kushindwa kuendelea na biashara kwani wanatozwa kodi mara mbili:-
(a) Je, Serikali inatambua uwepo wa utaratibu wa kutozwa kodi mara mbili kwa wafanyabiashara?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi na wa kudumu kutatua suala la wafanyabiashara kutozwa kodi mara mbili?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa utaratibu wa kutozwa kodi mara mbili kwa wafanyabiashara wanoingiza bidhaa za nje Tanzania Bara kupitia Zanzibar kwa sababu Tanzania Bara inatumia mfumo ujulikanao kama Import Export Commodity Database, ambao hautumiki kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, Import Export Commodity Database ni mfumo unaoweka kumbukumbu ya bei ya bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbukumbu ya bei za bidhaa mbalimbali zilizopo kwenye mfumo wa Import Export Commodity Database hutumiwa kama msingi wakati wa kufanya tathmini ya kodi ya bidhaa zinazoingizwa nchini pale thamani ya bidhaa husika inapoonekana kuwa hailingani na hali halisi. Hivyo basi, tofauti ya kodi inayotokana na kutotumika kwa mfumo wa Import Export Commodity Database kuthamini kiwango cha kodi kwa upande wa Zanzibar hukusanywa Tanzania Bara ili kuweka mazingira sawa ya ushindani kibiashara kwa bidhaa zote zinazoingia Tanzania Bara.
Mpango wa muda mfupi, muda mrefu na wa kudumu wa kutatua changamoto ya wafanyabiashara kutozwa kodi mara mbili, ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuridhia matumizi ya mifumo ya uthaminishaji wa kodi inayotumika ndani ya Idara ya Forodha ili kuondoa tofauti zilizopo za ukadiriaji wa kodi kati ya sehemu mbili za nchi yetu.
MHE. MATTAR ALI SALUM Aliuliza:-
Kuna malalamiko makubwa kwa upande wa Zanzibar kuhusu idadi ndogo ya wanafunzi wanaopata Mkopo wa Elimu ya Juu jambo ambalo linapunguza idadi ya wataalamu kwa upande wa Zanzibar, hivyo kuingia katika soko la ajira katika Afrika ya Mashariki na Kati na kuijenga nchi yetu kwa ujumla.
(a) Je, Serikali haioni kuwa Bodi ya Mfuko wa Elimu ya Juu inatakiwa kutenga asilimia maalum kwa wanafunzi kutoka Tanzania Zanzibar?
(b) Je, bajeti iliyotengwa kwa mwaka huo wa 2015/2016 ni kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Matta Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, lenye Sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu huzingatia matakwa ya sheria, kanuni, vigezo na miongozo itolewayo mara kwa mara na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Vigezo muhimu vinavyozingatiwa ni pamoja na kwamba muombaji awe ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, awe mhitaji, mlemavu au yatima. Aidha, muombaji anatakiwa kuwa amedahiliwa katika taasisi ya elimu ya juu na awe anachukua programu za vipaumbele vya taifa ambavyo ni ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa gesi na mafuta, sayansi za afya na uhandisi wa kilimo na maji.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2015/2016 kiasi cha shilingi 480,599,067,500 kilitumika kwa ajili ya kugharamia mikopo pamoja na ruzuku kwa ajili ya wanafunzi 124,358.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Tatizo la makazi kwa wanajeshi wetu ni kubwa kiasi kwamba maaskari wetu kupata usumbufu na kuathiri utendaji kazi wao.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba za makazi kwa wanajeshi wa upande wa Unguja?
(b) Je, ni nyumba ngapi Serikali imepanga kujenga Zanzibar?
(c) Je, ni lini ujenzi wa nyumba kwa upande wa Zanzibar utaanza?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inao mpango wa kuboresha makazi ya wanajeshi kwa kujenga nyumba za familia idadi ya 10,000. Kwa awamu ya kwanza ujenzi wa nyumba za familia za askari idadi 6,064 umefikia hatua ya mwisho kukamilika. Aidha, katika awamu hii hakuna ujenzi unaofanyika Unguja.
(b) Mheshimiwa Spika, katika awamu ya kwanza kwa upande wa Zanzibar, nyumba zimejengwa katika Kisiwa cha Pemba. Nyumba zilizojengwa ni ghorofa 40 zenye uwezo wa kuchukua familia idadi 320. Hatua inayofuata ni kukamilisha miundombinu ya umeme na maji ili nyumba hizo zianze kutumika.
(c) Mheshimiwa Spika, mchakato wa kuanza ujenzi wa nyumba za askari awamu ya pili unaotarajiwa kukamilisha ujenzi wa nyumba 10,000 unaendelea. Mgawanyo wa nyumba hizo utazingatia hitajio katika Kambi za Jeshi kwa ujumla ikihusisha Kambi za Unguja. Ujenzi huu utaanza mara mchakato utakapokamilika.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Jeshi la Polisi lina kazi kubwa ya kulinda usalama wa raia na mali zao, lakini cha kusikitisha ni kwamba askari wanaishi kwenye nyumba duni sana jambo ambalo linashusha hata hadhi zao hasa kwa upande wa Tanzania Zanzibar.
(i) Je, ni lini askari wetu watatengenezewa nyumba bora nao wajisikie kuwa Serikali yao inawajali?
(ii) Katika Makao Makuu ya Polisi pale Ziwani kuna majengo yaliyoachwa na wakoloni, je, kwa nini yasifanyiwe ukarabati mkubwa ili yaweze kutumiwa na askari wetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Jeshi la Polisi linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa nyumba za kuishi askari. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali ina mpango wa kujenga nyumba 350 za kuishi Askari Polisi Zanzibar. Katika idadi hiyo, nyumba 150 zitajengwa Pemba na nyumba 200 zitajengwa Unguja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kujenga nyumba mpya na siyo kukarabati nyumba za zamani zilizoachwa na wakoloni. (Makofi)
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Wananchi wengi hapa nchini hasa wanawake hutumia vipodozi ambavyo havina viwango vinavyofaa kwa matumizi ya binadamu. Pamoja na jitihada za Serikali kuzuia bidhaa hizo lakini bado vinaingizwa nchini na kutumika.
(a) Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kuzuia uingizwaji na utumiaji wa vipodozi hivi?
(b) Je, Serikali inaweza kutumia fedha kiasi gani kuzuia bidhaa hiyo kuingia nchini?
(c) Je, adhabu gani inatolewa kwa yeyote atakayekamatwa akiingiza nchini vipodozi visivyofaa kwa matumizi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, lenye sehemu (a) (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, TFDA imekuwa ikichukua hatua zifuatazo kudhibiti uingizwaji na utumiaji wa vipodozi. Vipodozi vyote hutakiwa kusajiliwa kabla ya kibali cha kuingiza nchi kutolewa. Mpaka sasa TFDA imesajili jumla ya vipodozi 3,179 ambavyo ndivyo vinavyorushusiwa kuingizwa na kutumika nchini. TFDA imefungua Ofisi saba za Kanda katika Mikoa ya Arusha kwa maana ya Kanda ya Kaskazini, Dar es Salaam - Kanda ya Mashariki, Dodoma - Kanda ya Kati, Mbeya - Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mtwara - Kanda ya Kusini, Mwanza - Kanda ya Ziwa na Tabora - Kanda ya Magharibi kwa lengo la kuimarisha ukaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 maeneo 3,648 yalikaguliwa ambapo kati ya hayo maeneo 120 yalikutwa na vipodozi ambavyo havina viwango vinavyofaa kwa matumizi kwa binadamu na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria. Vilevile jumla ya tani
407.82 za vipodozi vilivyopigwa marufuku vyenye thamani ya shilingi za Kitanzania bilioni 1.36 ziliteketezwa na TFDA na kesi 52 zilifunguliwa Mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sanjari na hilo, wakaguzi wa TFDA wamewekwa katika vituo vya forodha kwenye mipaka ya Namanga, Holili, Horohoro, Tunduma, Sirari, Kasumulu, Mutukula, Rusumo, Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere na vituo vingine vya forodha vilivyoko katika Mkoa wa Da es Salaam kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa bidhaa ikiwa ni pamoja na vipodozi vinavyoingizwa nchini.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017 TFDA ilitenga na kutumia jumla ya shilingi milioni 154.8 kwa ajili ya operation maalum ya ukaguzi wa bidhaa ikiwa ni pamoja na vipodozi. Aidha, katika mwaka 2017/2018, mamlaka imetenga fedha jumla ya shilingi milioni 132.16 ambazo zimekuwa zikitumika katika operation za kubaini na kukamata vipodozi haramu.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 91(b) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura ya 129 kinatoa adhabu isiyopungua miezi mitatu au kulipa faini isiyopungua shilingi 500,000 au adhabu zote mbili kwa pamoja kwa yeyote atakayekamatwa akiingiza vipodozi visivyofaa kwa matumizi ya binadamu. Sambamba na adhabu hii, vilevile mtuhumiwa anapaswa kugharamia uteketezaji wa vipodozi vyote vilivyokamatwa na wakaguzi.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Usafiri wa kutumia bandari ni usafiri muhimu sana na ni wa lazima kwa watu wanaotoka Tanzania Bara kwenda Unguja na Pemba; na zipo kampuni zinazotoa huduma ya usafirishaji lakini hazitoshelezi katika kutoa huduma hiyo muhimu.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kununua meli ili kukidhi mahitaji ya usafirishaji wa watu wetu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba usafiri wa kutumia bandari ni usafiri muhimu sana na hutumiwa na watu wengi wanaoishi maeneo ya mwambao wa Bahari ya Hindi hususan wanaotoka Tanzania Bara kwenda Unguja na Pemba. Ni kweli pia kampuni zinazotoa huduma ya usafirishaji katika maeneo hayo hazitoshelezi katika kutoa huduma hiyo muhimu kulingana na uhitaji wa abiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa mahitaji ya huduma za usafiri wa majini katika maeneo hayo kwetu ni fursa kwa sekta binafsi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kulitambua hilo Serikali imekuwa ikijenga mazingira wezeshi na kuihamasisha sekta binafsi kutoa huduma za usafiri kwa kutumia meli za kisasa kati ya wasafiri wanaotoka Tanzania Bara au kwingineko kwenda visiwa vya Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla juhudi za Serikali zimekuwa zikilenga katika kuhakikisha kuwa wakazi wa maeneo ya mwambao na visiwa vya Unguja na Pemba wanapata huduma za usafiri kwa njia ya maji zilizo salama na hivyo kuwaepusha kutumia vyombo vya usafiri huo visivyokidhi matakwa katika kubeba abiria na mizigo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uhamasishaji huo, kwa sasa kampuni ya meli ya Azam ilianza kutoa huduma ya usafiri baina ya Tanga, Unguja na Pemba kuanzia tarehe 29 Januari, 2017 kwa kutumia meli ya kisasa iitwayo Azam Sealink 2. Meli hii inatoa huduma kutokea Tanga kuelekea visiwa vya Unguja na Pemba mara moja kwa wiki. Aidha, kampuni hiyo iko tayari kuongeza safari baina ya Tanga, Unguja na Pemba kwa wiki mara itakapobainika kuwa abiria wanaosafiri katika maeneo hayo wameogezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaipongeza Kampuni ya Meli ya Azam kwa kuitikia wito wa kuanzisha huduma ya usafiri kwa njia ya maji baina ya Tanga, Unguja na Pemba na kuwataka wananchi kuepuka kutumia vyombo vya usafiri wa maji visivyokidhi matakwa katika kubeba abiria na mizigo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kutumia nafasi hii kuendelea kutoa wito kwa wawekezaji wengine kama ilivyo kwa Kampuni ya Meli ya Azam kuwekeza katika vyombo vya kisasa vya usafiri kwa njia ya maji ili kutoa huduma ya usafiri katika maeneo ya mwambao ya Tanzania ikiwamo na Visiwa vya Unguja na Pemba. (Makofi)
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Uvuvi wa Bahari Kuu unaingiza kipato kikubwa sana na unaweza ukachangia katika bajeti ya nchi yetu:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kununua meli za uvuvi?
(b) Je, Serikali imefikia wapi katika ujenzi wa Bandari ya Uvuvi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 - 2020 inaelekeza Serikali umuhimu wa nchi kuvuna rasilimali za uvuvi zilizopo katika ukanda wa Bahari Kuu kwa kuwa na meli za Kitanzania. Lengo la kununua meli hizo ni kuwa na meli za Kitaifa kuwezesha uvunaji wa rasilimali za uvuvi katika ukanda wa Bahari Kuu kwa lengo la kupata chakula na lishe, kuongeza Pato la Taifa na kutoa ajira kwa Watanzania watakaofanya kazi katika meli hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanikisha azma hiyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza utaratibu wa kufufua lililokuwa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) hatua itakayowezesha meli zitakazonunuliwa kuwa chini ya usimamizi wa TAFICO. Makadirio ya kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ni jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 45 ikiwemo maandalizi ya ununuzi wa meli za uvuvi. Aidha, Wizara inahamasisha Mifuko ya Kijamii, Taasisi, Mashirika ya Umma na Watanzania kuwekeza katika uvuvi wa Bahari Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara tayari imempata mtaalam mwelekezi atayefanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ambapo kukamilika kwa kazi hii kutawezesha kujua gharama halisi za ujenzi na aina na ukubwa wa bandari itakayojengwa. (Makofi)
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Polisi wanapowakamata watuhumiwa baadhi wanawaweka ndani kwa saa 24 na wengine zaidi ya saa 24.
• Je, ni makosa yapi mtuhumiwa anaweza kuwekwa ndani zaidi ya masaa 24?
• Je, ni makosa yapi ambayo mtuhumiwa anaweza kuwekwa ndani chini ya saa 24?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, kifungu cha 148(5)(a) mpaka (e) kinaeleza makosa mabayo mtuhimiwa anaweza kuwekwa kizuizini zaidi ya saa 24. Makosa hayo ni kama vile uhaini, mauaji, ujambazi wa kutumia silaha, kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, ugaidi, usafirishaji wa fedha haramu, mtuhumiwa aliyewahi kuhukumiwa kifungo kinachozidi miaka mitatu ama aliwahi kuruka dhamana na mengineyo.
Mheshimiwa Spika, makosa ambayo mtuhumiwa anaweza kuwekwa ndani chini ya saa 24 ni makosa yote isipokuwa yaliyoainishwa katika kifungu cha 148(5)(a) mpaka (f).
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-

Jeshi la Polisi lipo kwa mujibu wa sheria na hupaswa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi. Jeshi la Polisi linapowakamata baadhi ya watu huamuru wawekwe ndani zaidi ya saa 24 na kusababisha usumbufu mkubwa:-

Je, ni kesi zipi mtuhumiwa anapaswa kuwekwa ndani chini ya saa 24.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, makosa yote isipokuwa yaliyoainishwa katika kifungu 148(5)(a)-(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 yana dhamana. Watuhumiwa wake hawapaswi kukaa mahabusu zaidi ya saa 24. Aidha, watuhumiwa ambao wanakaa ndani zaidi ya saa 24 ilhali makosa yao yana dhamana hutokana na sababu kwamba watuhumiwa hao wameshindwa kutimiza masharti na vigezo vya kupata dhamana kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa la Jinai Kifungu cha 65 na 66, Sura ya 20 kama ambavyo imefanyiwa mapitio mwaka 2002.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-

Miongoni mwa kero za Muungano ni wananchi wa Zanzibar waletapo magari yao Tanzania Bara kutoruhusiwa kutembea mpaka yabadilishwe namba, wakati magari yanayotoka Bara yafikapo Zanzibar yanaruhusiwa kutembea kwa muda wote bila ya bughudha yoyote:-

(a) Je, Serikali inalifahamu suala hili?

(b) Kama ndiyo, je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kutatua suala hili ili Watanzania waendelee kufaidi matunda ya Muungano?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafahamu kwamba magari yaliyosajiliwa Zanzibar hayaruhusiwi kutembea Tanzania Bara bila kibali maalumu kwa sababu sheria zinazotumika kusajili vyombo vya moto, kati ya pande mbili za Muungano siyo sheria za Muungano. Kwa upande wa Tanzania Bara, usajili wa vyombo vya moto unasimamiwa na Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 pamoja na Kanuni zake na kwa upande wa Zanzibar usajili wa vyombo vya moto unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Usafiri wa Barabara Na.7 ya mwaka 2003. Aidha, majukumu ya usajili wa vyombo vya moto kwa upande wa Zanzibar husimamiwa na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Tanzania Bara husimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondokana na utaratibu wa sasa wa wananchi wa Zanzibar kuomba kibali maalum ili kutembelea magari yao Tanzania Bara, Serikali za pande mbili zipo katika majadiliano ili kuhuisha sheria na mifumo ya ukukotoaji kodi ya magari na hivyo kuwawezesha wananchi kutembelea magari yao pande zote za Muungano bila usumbufu. Aidha, mchakato wa kuhuisha sheria na mifumo ya ukokotoaji kodi utafuata taratibu zote zilizowekwa na Bunge lako Tukufu pamoja na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-

Kampuni ya Azam Marine ambayo inafanya biashara ya kusafirisha abiria kwa kutumia boti kupitia baharini, huuza tiketi kwa abiria kwa ajili ya safari lakini abiria anapochelewa safari tiketi hiyo huwa haitumiki na hivyo kusababisha hasara kwa abiria pamoja na usumbufu;-

(a) Je, Serikali inalijua hilo?

(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mattar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ina taarifa ya jambo hili kwa kuwa limekuwa likijitokeza mara kwa mara. Ufuatiliaji uliofanywa na Wizara yangu kupitia TASAC umebaini kuwa Kampuni iliyotajwa ina utaratibu wa namna abiria anavyoweza kuahirisha safari na namna nauli itakavyorejeshwa. Aidha, Kampuni hiyo imekuwa kuahirisha safari na namna nauli itakavyorejeshwa. Aidha, Kampuni imekuwa ikiruhusu abiria kutoa taarifa na kubadili muda wa safari bila gharama ya ziada ikiwa msafiri atatoa taarifa kabla ya chombo kuondoka. Utaratibu huu unatoa fursa kwa kampuni kuuza nafasi iliyoachwa wazi kwa wasafiri wengine ili kuepuka hasara.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa vyombo vya kampuni hii vimesajiliwa katika daftari la usajili linalosimamiwa na Mamlaka ya Bandari Zanzibar (ZMA), Wizara yangu kupitia TASAC itaendelea kufanya ufuatiliaji kwa kushirikiana na Wizara husika Zanzibar kupitia ZMA ili kusimamia utekelezaji wa utaratibu huu wa Kampuni ili uwasaidie abiria wanapoahirisha safari na kutoa taarifa kwa wakati.