Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Twahir Awesu Mohammed (2 total)

MHE. TWAHIR AWESU MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Naibu Waziri, naomba nimuulize maswali madogo mawili. Je, Serikali iko tayari kwa sasa kupokea majina ya wananchi walionyanyaswa na kupigwa chini ya mikono ya Jeshi la Polisi?
Swali la pili; je, Serikali imewahi kuwatia hatiani Askari Polisi waliotajwa kuwanyanyasa raia kulingana na ukubwa wa makosa?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara tuko tayari kupokea majina ya aina hiyo na tuna kitengo rasmi ambacho kinashughulikia malalamiko ya wananchi na mara wanapopokea wakijiridhisha huwa wanachukua hatua.
Kuhusu swali la pili kama Serikali ama Wizara iliwahi kuchukua hatua kwa watu ambao wamelalamikiwa kunyanyasa wananchi. Wanachukua mara kwa mara na jana tu tulisema zaidi ya Askari 154 tayari waliwahi kuchukuliwa hatua hizo na hivi tunavyoongea Waheshimiwa Wabunge hata leo kwenye magazeti mmesikia kuna Askari wamefukuzwa kazi jana tu kwa kuwanyanyasa wanafunzi kinyume na taratibu za sheria za utendaji wa kazi.
MHE. TWAHIR AWESU MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, imekuwa ni kawaida sasa katika nchi yetu watu kutekwa, kupigwa, kuumizwa na hata kuuliwa. Kumekuwa na dhana kwamba Jeshi la Polisi linafahamu fika tendo hili, lakini wamelinyamazia. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anataka kuwaambia nini Watanzania ili isije ikafika hatua wakajichukulia sheria mikononi mwao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kumekuwa na katazo la kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Siku ya tarehe 8 Aprili, 2018, CCM mikoa miwili ya Pemba waliandamana chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi wakiwa wamebeba mabango wakiimba nyimbo za kuhatarisha amani, za uchochezi. Mheshimiwa Naibu Waziri nataka aniambie, hili katazo linahusu Vyama vya Siasa vya Upinzani pekee au ni kwa vyama vyote vya siasa? (Makofi).. Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sikubaliani na maoni ya Mheshimiwa Mbunge maana maoni yoyote yanahitaji yathibitishwe, yahalalishwe, yalinganishwe. Kwa takwimu ambazo ninazo zinaonesha hali ya uhalifu nchini inaendelea kupungua. Sasa anaponiambia kwamba sasa hivi kuna ongezeko la mambo ya uhalifu, akataja mengi tu, ninachoweza kusema ni kwamba tuna Jeshi la Polisi kwa sababu ya hulka ya baadhi ya binadamu kufanya au kufikiria kufanya uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi zote majeshi ya polisi au vyombo vya dola vipo kuzuia hizo hali, kwa hiyo hatuwezi kusema kwamba kuna Taifa duniani ambalo litakuwa halina element yoyote ya uhalifu. Ninachoweza kumhakikishia ni kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi yake nzuri na ndiyo maana hali ya uhalifu imepungua nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na wananchi, kwamba wachukue sheria mkononi, naomba tu nimsisitize Mheshimiwa Mbunge kwa wananchi wake na wananchi wengine ambao wananisikiliza hapa kwamba tunaendelea kusisitiza kwamba wausijaribu kuchukua sheria mkononi. Mamlaka za dola zipo kwa ajili yao na pale ambapo wanaona kwamba kuna tatizo lolote la uhalifu basi wawasilishe malalamiko yao katika vyombo husika na sheria itachukua mkondo wake. Kitendo cha kuchukua mkononi hakihalalishi aliyechukua sheria mkononi asichukuliwe hatua na yeye za kisheria pindi atakapokuwa amevunja sheria, hata kama atakuwa ametendewa kosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ametoa mfano wa tarehe fulani ambayo CCM waliandamana, bahati mbaya sina taarifa hizo, lakini ninachoweza kusema ni kwamba suala la kuandamana, suala la kufanya mikutano na kadhalika linapotokezea ni lazima Jeshi la Polisi litoe ulinzi ili shughuli ile kama ni maandamano au mkutano, kama umeruhusiwa lakini kwa mujibu wa sheria na taratibu zimefuatwa, lazima Jeshi la Polisi liwepo kutoa ulinzi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi tunachoweza kusema ni kwamba kipindi hiki ambapo Serikali yetu ya Awamu ya Tano ina shughuli nyingi za mafanikio makubwa kiuchumi na ninyi mnaona, ni mashahidi, kwamba Taifa letu linaendelea kupiga hatua kwa kasi kabisa na uchumi wetu unainuka na kero nyingi zimetatuliwa, Jeshi la Polisi lina jukumu la kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama. Hatuwezi kuendekeza kutoa ulinzi kwa maandamano, mikutano, hatuna askari wa kutosha kuweza kufanya shughuli hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunasema kwamba kwa taasisi yoyote au chombo chochote ambacho kitahitaji kufanya maandamano na mikutano isiyokuwa na tija, Jeshi la Polisi halina muda huo, lina muda wa kulinda maisha ya wananchi na usalama wao katika kipindi hiki ambapo Serikali yetu inapiga hatua kubwa ya maendeleo. Kwa hiyo, hii si kwa chama chochote, si kwa mtu yeyote haibagui mtu, ni sheria msumeno inakata pande zote mbili. (Makofi)