Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jamal Kassim Ali (7 total)

MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:
(a) Kwa vile Naibu Waziri ameeleza kwamba kuna database maalum ambayo TRA wanayo na kule Zanzibar inatumika, je, huu mfumo una tatizo gani, kwa sababu mizigo yote ambayo inapitia Zanzibar kuja Bara asilimia 100 ya mizigo ile inatozwa kodi inapoingia Tanzania Bara, wakati sheria inayotumika ni hiyo moja, na mamlaka ambayo inasimamia kodi na Kamishna ni huyo huyo mmoja?
(b) Mheshimiwa Naibu Waziri, alieleza katika jibu lake kwamba endapo vitu vinatoka Zanzibar kuja Bara wanaagalia tozo la awali ambalo lilitozwa Zanzibar na kuangalia ile tofauti ambayo kwa mujibu wa database zao wanam-charge yule mtu. Sasa je, kwa mtu ambaye ana tv moja anapopita bandarini pale kutokea Zanzibar hana entry…
NAIBU SPIKA: Naomba uulize swali Mheshimiwa Jamal,
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Ahsante Mheshimiwa NAibu Spika, je, mtu ambaye kwa vitu ambavyo ni item moja moja kama tvna redio anapotoka Zanzibar kuja Bara wanatumia mfumo gani wa kukokotoa hiyo kodi?
NAIBU WAZIRI WA FEHDA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kodi inazotozwa kwa bidhaa zinazotika Zanzibar kuja huku kwetu, kwanza naomba nisahihishe, mfumo huu wa Import Export Commodity Database unaotumika Tanzania Bara kule Zanzibar hautumiki. Ndiyo maana inaonekana kule ambako hawatumii mfumo huu, bidhaa kule tathmini inapofanyika mara nyingi huonekana ipo chini ya thamani ya kiwango ambacho kinatakiwa kulipiwa kodi inapokuja Tanzania Bara.
Hivyo ndiyo maana bidhaa zinazotoka Zanzibar kuja huku zinatozwa tena kodi. Siyo kodi mara mbili lakini ni kuangalia utofauti wa kodi wa thamani, zilizothaminiwa kutoka Zanzibar na ambazo zimethaminiwa huku Tanzania Bara. Hivyo, tunaomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waweze kufanya haraka kujiunga na mfumo huu, ili kwa pamoja hili tatizo wanalopata wafanyabiashara wetu wasiweze kulipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bidhaa hiyo moja moja, mfumo ni huohuo mmoja, inapofika kama haikuzalishwa Zanzibar, inapofika Forodhani inatakiwa ichajiwe utofauti ule wa kodi ambao utaonekana ilichajiwa Zanzibar na huku Tanzania Bara. Ahsante.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nitakuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza.
Moja, kwa vile Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza kwamba kila mteja katika kila ngazi anabeba gharama zake. Je, Naibu Waziri atakubaliana nami kwamba bei ambayo inatozwa Shirika la Umeme la Zanzibar yaani ZECO, ambaye ni mteja wa jumla (bulk purchaser) kwa unity moja ya KVA ambayo ni shilingi 16,550/= ambayo ni bei kubwa kuliko wale wateja wa reja reja wa ngazi ya kati na ngazi ya chini kuwa hii bei siyo stahiki kutozwa ZECO. Je, lini Serikali itaitaka EWURA sasa kufanya maboresho ya bei hii na kuitoza ZECO bei stahiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Jamali kwa kutukumbusha kwamba gharama za umeme zinatakiwa zishuke. Nimhakikishie tu kwamba kuanzia mwezi wa Nne tulipofanya marekebisho ya bei watumiaji wakubwa kabisa wakiwemo ZECO tuliwapunguzia kwa asilimia 2.4, ilikuwa ni punguzo kubwa kweli kweli ukilinganisha na wateja wengine wadogo wadogo. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Jamal kwamba bei za gharama kama nilivyosema, zinategemea hasa mambo mawili:-
Jambo la kwanza ni vyanzo vya kuzalisha umeme. Vyanzo vinapokuwa vya bei nafuu na bei ya umeme inapungua. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Jamal kwamba ni kweli kabisa kwa unity moja kwa sasa kwa watumiaji wakubwa ni shilingi 16 na 55 unit, lakini zitaendelea kupungua kulingana na gharama ya uzalishaji wa umeme unavyoshuka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Jamal nakuhakikishia tutaendelea kulifanyia kazi na EWURA bado wanaendelea na mchakato wa ku-review bei kulingana na gharama za umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni lini sasa EWURA watafanya marekebisho hayo? Kwa sasa hivi tunazalisha umeme mwingi sana wa kutumia gesi na kwa kiasi kingine kikubwa kwa kutumia maji. Tumeeleza sana vyanzo vya gesi na jinsi ambavyo bei inaendelea kupungua. Kwa sasa hivi atupe muda tuendelee kuzalisha kwa vile ambavyo mmetupa bajeti, siyo muda mrefu, EWURA tena wataingia uwanjani kuanza ku-review bei. Kwa hiyo, Mheshimiwa Jamal nikuhakikishie kwamba bei itaendelea kuangaliwa wakati hadi wakati.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipatia fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa wafanyabishara wengi wetu ni wadogo na wa kati na wengi wao wanakabiliwa na changamoto kubwa ya mitaji. Je, Serikali ina mkakati gani ya kuhakikisha taarifa ya fursa hii inawafikia? Lakini pia katika mwaka uliopita trend ya mauzo ya hisa katika soko letu la hisa la Dar es Salaam linaonyesha kushuka, na share nyingi ambazo zilizokuwa traded pia price zake zimeshuka. Je, ni nini mkakati wa Serikali katika kutatua changamoto hii?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa maana ya mkakati, kikubwa ni elimu kwa umma. Kwa kweli soko hili watu wengi hawalielewi, na tumeendelea kusisitiza kwamba Capital Market and Securities Authority na DSE wenyewe waongeze jitihada katika kutoa elimu kwa umma. Lakini pia nitumie nafasi hii kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge kama nilivyosema katika jibu langu la msingi nao pia wachangie kutoa elimu, kwa kweli kuna fursa kubwa katika kuiongezea mitaji makampuni mbalimbali kwa wananchi wetu kununua hisa katika makampuni hayo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli trend inashuka lakini kilicho kikubwa kama nilivyosema ni kwa sababu ya uelewa mdogo na kwa hiyo, Serikali inafanya jitihada kupitia taasisi hizi kuongeza elimu kwa umma na fursa hizi zitaongezeka katika siku zijazo ndio matumaini ya Serikali.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, Mheshimiwa Waziri katika jibu lake la msingi amekiri kwamba moja ya mambo muhimu kabisa ya Watanzania hawa kwenda kuwekeza kwenye viwanda ni pamoja na kuwa na mitaji. Watanzania hawa wamefanya biashara kubwa sana na Serikali na wana madeni makubwa ambayo wanaidai Serikali.
Je, Serikali haioni ipo haja sasa madeni haya ambayo wamekuwa wakidaiwa kwa muda mrefu kuyalipa kwa haraka ili Watanzania hawa nao sasa wapate fursa ya kwenda kushiriki katika uchumi wa viwanda ambao Mheshimiwa Waziri ameeleza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, Serikali haioni ipo haja sasa ya kuja na sera maalum ambayo itatoa special incentive package kwa wawekezaji wazawa Watanzania ili nao waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda kutokana na kuwa nyuma kiteknolojia, kifedha na mambo mengine ambayo ukiwaweka na wenzetu wa mataifa mengine Watanzania hawa hawawezi ku-compete? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo wapo wafanyabiashara, wakandarasi ambao wamefanya kazi na Serikali na wanadai stahiki yao, Serikali itawalipa. Utaratibu wa Serikali unapitiwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha amekuwa akilisema mara kwa mara kwamba jambo kubwa ni kufanya uhakiki na kadri uhakiki unapofanyika hao watu wanalipwa na niwahakikishie kwamba Serikali itawalipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na vivutio, sasa hivi kuna vivutio, suala la muhimu kwa wafanyabiashara wa Tanzania au kwa Watanzania ambao wangependa kupewa vivutio maalum waone hivi vivutio vilivyopo watuambie ni wapi sio vizuri. Hatuwezi kubadilisha vivutio, kwanza anza utuambie hiki siyo kizuri hiki ndiyo kizuri ndiyo tutabadilisha.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ameonesha wazi kwamba transaction ambazo zinafanyika kupitia E-Commerce zinaongezeka na Mamlaka ya Mapato (TRA) hawana access ya moja kwa moja ya kuona hizi transaction ambazo zinafanyika kupitia E-Commerce;
Je, Serikali inasema nini sasa kuhusu kujijengea uwezo aidha wa ku-establish link baina ya mfumo huu wa EFDs na ule wa TCRA ambao baadhi ya transaction zinaweza kupatikana kwenye ule mfumo wa TCRA?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, suala la wataalam Mheshimiwa Waziri angefafanua zaidi anapokusudia Serikali imeamua kuongeza uwezo kwa wafanyakazi alimaanisha ni kwa namna gani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza, kwanza kabisa naomba niseme kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi siyo kwamba hatuna access na hatuzifikii hizo taarifa hapana! Taarifa hizo tuzazifikia kwa sababu hata transaction zinazofanyika kati ya TANESCO unanunua kupitia simu yako unaoneshwa kabisa kodi ipi inalipwa wapi na inalipwa kwenda wapi, hizo zote zinakuwa accessed na mfumo wetu wa EFDs kule Mamlaka ya Mapato. Kwa hiyo, tuna uwezo wa ku-access ila nimesema changamoto za kiteknolojia zinakuwa siku hadi siku na ndipo niliposema kwa swali lake part (b) kwamba tunaendelea kuwawezesha watendaji wetu kuwapa uwezo zaidi kulingana na mabadiliko ya mifumo ya kiteknolojia yanavyotokea siku hadi siku. (Makofi)
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Issa Mangungu na wananchi wa Mbagala nitakuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Serikali katika mwaka unaokuja 2017/2018 wamepanga kutoa ajira za walimu. Je, ni walimu kiasi gani ambao wamepangwa kwenda kuajiriwa katika Wilaya ya Temeke hususan katika jimbo la Mbagala, katika shule za sekondari za Kingugi, Mbande, Charambe, Toangoma na Mbagala Kuu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali katika mwaka huu imeajiri walimu wengi wapya, je, ni lini sasa Serikali itawapatia stahiki zao walimu hawa wapya na pia kuwapatia makazi ili kuwawesha kufanya kazi yao kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema pale awali kwamba tuna mpango wa kuajiri walimu, lakini katika hili sasa hivi tunafaya vile vile na tathmini ya idadi ya walimu ambao wametoka katika system ya kiserikali mara baada ya vyeti fake. Kwa hiyo, tutaleta taarifa rasmi hapa baadaye kwamba idadi ya walimu ambao wamekutana na vyeti fake ambapo hivi sasa kuna deficit ambayo itakuwepo, lakini na idadi ya walimu wapya. Kwa hiyo, tutaleta taarifa rasmi ya idadi ya walimu. Hata hivyo naomba nikuhakikishe Mheshimiwa Jamal kwamba kwa Mkoa wa Dar es salaam maeneo ya Temeke na mimi nafahamu sana Temeke ilivyogawanyika mpaka kwenda kule ndani maeneo ya Toangoma tutaangalia ni jinsi gani tutafanya ili maeneo hayo kama ambavyo umeainisha tuweze kuwapeleka walimu wa kutosha ili vijana wetu wanaokwenda kujiunga, waweze kupata elimu hiyo inayokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande wa pili wa swali lako nadhani Mheshimiwa Jamal, nimesahau kidogo kipengele cha pili.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpongeza Naibu Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya. Pamoja na majibu mazuri aliyotoa nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa vile Sera ya Serikali yetu ni kwenda kwenye uchumi wa viwanda na viwanda vingi vimekuwa na uhaba wa malighafi ambazo zinatokana na bidhaa za mazao na kupelekea viwanda vyetu kuagiza malighafi kutoka nchi za nje, je, Serikali ina mkakati gani kupitia benki hii sasa kuanza kukopesha wakulima wakubwa ambao wataongeza uzalishaji wa malighafi ambazo zitaenda kulisha viwanda vyetu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, benki hii imekabiliwa na uhaba wa mtaji, ilianzishwa kwa mtaji wa shilingi bilioni 60 lakini lengo lake lilikuwa kufikia mtaji wa shilingi bilioni 80. Je, nini commitment ya Serikali kuhakikisha kwamba mtaji wa benki hii utaongezeka ili kusaidia kuongeza idadi ya wakopeshaji lakini pia kuongeza single borrow limit kama ambavyo maelekezo ya BOT yameelekeza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Jamal, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nieleweke kwamba Benki yetu ya Kilimo ni benki ya kisera tofauti na zile benki zingine za kibiashara. Benki hii ya Kilimo ambayo ni ya kisera ilikuwa imeundwa kwa makusudi maalum kwa ajili ya kusaidia wakulima wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake hili kuhusu wakulima wakubwa, ni kweli hawa Niche Farmers kwa maana ya wakulima wakubwa sera na sheria yetu ni katika kuhakikisha kwamba na wenyewe wanafanya na wakulima wadogo kwa maana ya outgrowers ili kuweza kuongeza ule mnyororo wa thamani katika mazao yetu ya kilimo. Katika Benki yetu ya Kilimo ni kwamba wenyewe tunaposema ni benki ya kisera ni kwa sababu riba yao ni ndogo zaidi kutoka asilimia 8 hadi asilimia 12 kulingana na wakati ule ambao wao wenyewe wanaomba kama ni muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu ambao unafika miaka 15.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusu mkakati pamoja na mtaji, kama nilivyosema hii ni benki ya kisera kwa maana hiyo Serikali imewekeza asilimia 100 katika benki hii ili kuhakikisha kwamba inawakomboa wakulima. Mheshimiwa Spika, ahsante.