Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Yussuf Salim Hussein (48 total)

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Katika paragraph ya pili ya majibu yake ndiyo nitajenga maswali yangu ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 9 Desemba, 2016, nilikuwa nasafiri kutoka Dubai kurudi Tanzania nikakutana na binti wa Kitanzania anaitwa Zuhura Yussuf Manda, mkazi wa Tegeta Kibaoni, Dar es Salaam. Binti alipelekwa kufanya kazi na agent wa Kitanzania anayeitwa Amne, akafanya kazi Oman kwa miezi mitatu kwa Anna na badala yake Anna akampa dada yake ambaye anaishi Dubai anaitwa Zahra akafanya kazi kwa muda wa miezi mitatu. Huyu Zahra hawakuridhiana kwa hiyo ikabidi binti atoroke akutane na Mzungu ambaye alimchukua akampeleka kwenye Ubalozi wa Tanzania.
SPIKA: Sasa swali.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, hapo ndiyo swali langu linakuja. Alikaa katika Ubalozi wa Tanzania kwa kipindi cha miezi sita bila ya kupatiwa passport yake ambayo aliizuia mwajiri wake, bila ya kupatiwa vifaa vyake ambavyo alivizuia mwajiri wake hadi alipokuja Mtanzania mwingine kwa wiki moja ndiyo akatengenezewa safari ya kurudi Tanzania. Swali linakuja, je, ni utaratibu gani ambao Serikali imeweka sasa kwa wale ambao wameshafikishwa kwenye Balozi zetu kuweza kuwarudisha Tanzania kwa muda mfupi ili kuipunguzia Serikali gharama za kimaisha kwa kubeba mzigo wa watu wale ambao wako pale katika Balozi zetu? Hilo swali la kwanza.
SPIKA: Aaaah kaka! Kama kila mtu atachukua muda mrefu kiasi hiki kwa kweli kwa muda wa saa moja maswali hayawezi kwisha.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru, nilikuwa najenga hoja ili Waziri…
SPIKA: Tafadhali jielekeze moja kwa moja kwenye swali.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Ahsante! Nilikuwa najenga hoja ili Mheshimiwa Waziri akijibu ajibu vizuri…
SPIKA: Hapana usijenge hoja, nenda kwenye swali moja kwa moja. Kanuni zinataka uulize swali moja kwa moja.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, hawa ma-agent ambao wanaopeleka watu kufanya kazi nje ya nchi linapotokea tatizo kama hili wao wanawajibika vipi kurudisha gharama kwa Serikali kwa wale watu wao ambao hawakuwatendea vilivyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Spika, katika jibu letu la msingi tumesema Serikali imeweka utaratibu rasmi ambao utawasaidia Watanzania wanapofanya kazi nje ya nchi na kupata matatizo waweze kusaidiwa kwa haraka. Kwa hiyo, katika jibu langu la kwanza kwa swali la kwanza la nyongeza ili kupunguza gharama kwa Serikali, naomba kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu niendelee kuwaarifu na kuwaomba Watanzania wote wanapokwenda nje ya nchi watumie utaratibu ulio rasmi ambao utawasaidia wao kuwa salama na kupunguza gharama kwa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, linasema hawa ma-agent ambao wanawapeleka nje Watanzania halafu kunatokea matatizo wanaweza kutozwa kiasi gani kulipia gharama za fidia kwa waathirika? Majibu ni yale yale kama hukupitia kwenye utaratibu wa Serikali, Serikali itakuwa ni ngumu sana kufuatilia hizo haki zako. Ukipitia kwenye utaratibu wa Serikali, Serikali kupitia sheria tulizonazo tutasimamia na tutaweza kuchukua hatua kwa hao ma-agent ambao wanafanya mambo hayo kinyume cha sheria.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ambayo anajitetea na kijificha katika msitu wa njugu. Ni-declare interest mimi ni mtaalam wa misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilichouliza ninataka kujua Serikali ina mkakati gani mahsusi wa kuongeza idadi ya wanafunzi katika chuo kile ili kukabiliana na paragraph ya mwanzo ya majibu yako. Ieleweke kwamba tunaposema wataalam wa misitu (foresters) hasa ni wale certificate na diploma kwa sababu wale ndiyo field officers na kukosekana kwa wale ndiyo sasa hivi deforestation imeongezeka na afforestation imepungua.
Mheshimiwa Spika, nataka kujua mkakati upi wa Serikali wa kuongeza idadi ya wanafunzi wa certificate na diploma katika chuo kile ili kukabiliana na hali hii tuliyonayo katika nchi yetu ya uharibifu wa misitu na mazingira? (Makofi)
Swali la pili, mheshimiwa Waziri, Chuo cha Misitu cha Olmotonyi katika miaka ya 1980 kilikuwa na hadhi ya Kimataifa, sijui leo; na kilikuwa kinapokea wanafunzi kutoka nje ya nchi. Je, Serikali inasema nini katika kukiboresha chuo hiki kikaendelea kupokea wanafunzi kutoka nje ikawa ni moja kati ya source of income za Serikali hii, kuipatia fedha za kigeni? Nashukuru!
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Yussuf kwa maswali yake mazuri.
Mheshimiwa Spika, kwanza ni uwezo wa chuo kuongeza wanafunzi na katika jibu la msingi hapa, tumepanua chuo ili kiweze kuwa na hall ya mhadhara mmoja ambao unaweza sasa kubeba wanafunzi 200 kwa wakati mmoja. Tumepanua na nafasi nyingine na hasa kuboresha maktaba ili iwe bora zaidi na iweze kuwa na rasilimali za vifaa vya kujifunzia bora zaidi. Kwa kufanya hivyo tunaweza kuongeza wanafunzi wengi zaidi na kufanya chuo kitoe mafunzo mazuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba huko nyuma, Chuo cha Olmotonyi kilikuwa kinachukua wanafunzi kutoka nje ya nchi, lakini katika ngazi hii ya cheti na ngazi ya diploma, hii ni ngazi ya msingi sana kama elimu ya msingi kwenye mafunzo haya ya misitu.
Mheshimiwa Spika, katika mafunzo haya ya misitu nchi nyingi ambazo zilikuwa zinaleta wanafunzi kwetu zimejijengea uwezo wake wa kutoa mafunzo ya msingi. Siku hizi wanafunzi wa Kimataifa wanakuja kusoma kwenye chuo chetu cha misitu kilichopo kwenye Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine ambacho ndicho chuo bora zaidi kwenye fani ya misitu kuliko vyuo vyote Barani Afrika.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri. Pamoja na Tanzania kwamba tuna maeneo mengi mazuri kwa ajili ya kilimo cha miwa na viwanda tulivyonavyo vya sukari na pamoja na mbwembwe nyingi za Serikali ya Awamu ya Tano iliyonazo kukuza uchumi, lakini bado bei ya sukari katika nchi yetu ni kubwa sana na uwezo wa wananchi wetu ni mdogo. Je, ni lini Serikali itaangalia sasa uwezekano wa kupunguza bei ya sukari ili ifikie angalau pale tulipokuwa na tatizo la sukari wananchi wetu waweze kumudu kununua sukari?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikanushe Serikali ya Awamu ya Tano siyo ya kibabaishaji tunafanya kazi na kama alivyosema Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa tathmini ya mwezi Januari viwanda vyetu vya ndani vimeshazalisha asilimia 86 ya uhitaji wa sukari ndani ya nchi yetu, kwa hiyo, ninauhakika kwa demand na supply nguvu hii tayari tukishaweza kuzalisha asilimia mia moja bei ya sukari itashuka. Tukumbuke tu Waheshimiwa Wabunge nchi hii ni huru na inafuata soko huria, hatuwezi kuingilia hilo na turuhusu sasa Viwanda vyetu viweze kuzalisha asilimia mia moja na bei ya sukari itashuka na wananchi wetu watafurahia Serikali yetu ya Awamu ya Tano utendaji wake.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa
kunipa nafasi. Jimbo la Same Mashariki ni Jimbo ambalo lina ardhi nzuri kwa
kilimo cha tangawizi: Je, Mheshimiwa Waziri kwa nini huoni sababu wataalam
wake kushirikiana na wataalam wa TANAPA kuwapa elimu wananchi wa eneo
hili wakalima kilimo cha tangawizi ambacho hakidhuriwi na mifugo,
tukaondokana na mzozo wa wakulima na wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni
kweli kabisa kama alivyosema kwamba eneo la Same kutokana na hali ya hewa na aina ya udongo inafaa sana kwa zao la tangawizi, tayari Wakulima wa Same
ni wakulima mahiri wa zao la tangawizi, na tayari Serikali kwa kushirikiana kwa
karibu sana na aliyekuwa Mbunge wa Same Mheshimiwa Anne Kilango
Malecela, ambaye tunashukuru amerudi kwenye Bunge hili walishajenga
kiwanda kwa ajili ya kuchakata tangawizi kama njia ya kuwaongezea wakulima
faida zaidi.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, katika majibu yake Mheshimiwa Waziri amesema ili kupambana na suala la mmomonyoko wa ardhi katika kingo za bahari Serikali imechukua au itachukua hatua ya kujenga kuta katika kingo za bahari pamoja na kupanda miti ya mikoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmomonyoko wa ardhi katika kingo za bahari sasa hivi unakuwa kwa kiasi cha mita mbili kwa mwaka. Kiasi ambacho ni kikubwa sana. Je, Serikali inauwezo gani wa kujenga kuta katika ukanda wote wa bahari ili kuzuia mmomonyoko huu na hiyo elimu ya upandaji hiyo mikoko inatolewa kwa kiasi gani ambayo tunaweza tukakabiliana na kasi hii ya ukuaji wa mmomonyoko katika ardhi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS-MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli ipo kasi kubwa ya kuongezeka kwa kina cha bahari kumesababisha bahari kwenda kwenye makazi ya watu, kumesababisha mmomonyoko mkubwa sana wa fukwe zetu, lakini imesababisha pia hasara kubwa kwa sababu kuna baadhi ya majengo ya biashara na makazi yako kwenye hatari kubwa ya kumezwa na bahari na miundombinu mingine ya kiuchumi mikubwa kama visima vya gesi ambavyo na vyenyewe viko kwenye hatari vilevile ya kumezwa na bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachofanya kama Wizara ya Mazingira katika pande mbili zote tunayo Idara ya Mazingira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, lakini tuna Idara ya Mazingira pia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Serikali hizi zote kwa pamoja zinaendelea kufanya kazi ya kufanya tathmini ya kuweza kubaini hizi athari kila mahali sasa baada ya kubaini zile athari ambazo zinasababishwa na haya mabadiliko ya tabianchi tunaangalia kwamba ipi tuipe kipaumbele leo ili kuweza kuzuia athari ambazo zinaweza kujitokeza kwa muda mfupi kama sasa hivi tutakubaliana Wabunge wote kwamba hapa na mlitupitishia kwenye bajeti na sasa hivi kuta hizo zimeshaanza kujengwa, ukuta wa Pangani, ukuta wa Ocean Road, ukuta wa Kilimani na ukuta wa Kisiwa Panza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, visiwa hivi vyote ndivyo vilikuwa vipaumbele vyetu kwasababu maeneo haya yalikuwa yamepata athari kubwa na hivyo sasa naona Mbunge wa Pangani hapa ana hofu ni kwamba mkandarasi yuko site sasa hivi amekwisha ku-report sasa hivi ameanzia na Ocean Road na ndiyo huyo huyo ambaye atajenga ukuta wa Pangani ndiyo huyo huyo atayejenga ukuta wa Kilimani pamoja na Kisiwa Panza na anauwezo wa kutosha kufanya kazi hizo kwa muda tuliompa.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la fedha kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa sasa ni donda ndugu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mabadiliko ya Sheria ya VAT ya mwaka 2014 kama sikosei imepitishwa kwamba bidhaa zinazotoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar hazitozwi ushuru hapa Tanzania Bara na wanatakiwa watoze ushuru kule Zanzibar ambako ZRB wanatoza ushuru wa asilimia 18. Lakini bado TRA Zanzibar wanawatoza wafanyabiashara hawa trade levy ya asilimia tano kusema kwamba bidhaa ile ile mfanyabishara wa Zanzibar anatakiwa ailipie asilimia 23 ya kodi, je, huku si kumuonea mfanyabiashara huyu wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo ameanza yeye mwenyewe kusema Sheria ya VAT tuliipitisha hapa na tunaitekeleza kisheria. Hilo analolisema la wafanyabiashara kwamba wanaonewa nimuombe Mheshimiwa Mbunge kama na yeye ana uthibitisho wa hilo analolisema aweze kutupatia ili tuweze kufanyia kazi. Lakini kitu ambacho kipo tunajua kodi zote zinatozwa kulingana na sheria zilizopitishwa na Bunge lako
tukufu.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu yako mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kusema kwamba kuna sheria ya mita 60 kutofanya huduma yoyote kutoka kwenye chanzo cha maji, lakini bado vyanzo vya maji vinaendelea kuathirika katika maeneo ya wazi na mpaka ndani ya mbuga zetu ambayo ni maeneo yanayolindwa na kuhifadhiwa na Serikali.
Je, Serikali sasa ina mpango gani mahsusi wa kufanya utafiti wa miti ambayo inazalisha maji, iwe imepandwa kuzunguka vyanzo vya maji? Ni mkakati upi hasa mahsusi wa kudhibiti hivi vyanzo vya maji visiathirike? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mita 60 na vyanzo vya maji kuendelea kuharibiwa na utafiti ambao unafanyika, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulipokuwa tunaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Upandaji Miti wa mwaka 2016 hadi mwaka 2021, tulizingatia hayo na mpaka sasa hivi tumeshabaini aina ya miti inayofaa kupandwa katika vyanzo vya maji na utaratibu huu tutausambaza kwa wataalam wote. Kwa kushirikiana na TFS na wataalam wa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, tumeshaandaa tayari aina ya miti ambayo inafaa kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vyetu vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jithada unaziona, juzi hapa Mheshimiwa Makamu wa Rais amezindua mpango mkubwa wa kuokoa hali ya uharibifu wa mazingira ambayo inaendelea katika Mto Mkuu Ruaha. Katika kufanya hivyo, hatuishii hapo, tutaendelea kufanya tathmini katika vyanzo vyetu vya maji vyote ili tuje na solution ya uhakika na tuweze kutenga fedha zinazokidhi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mazingira haya tunayalinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile suala la mazingira ni gumu sana, ulinzi wake ni mgumu. Inatakiwa kila mwananchi, sisi wenyewe Wabunge tuhakikishe kwamba tunasaidia kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba mazingira yetu yanalindwa.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza. Ni dhahiri kwamba Watanzania wengi wanapoteza maisha katika bahari au katika maziwa zinapotokea ajali na ni ukweli uliowazi kwamba hatuna wataalam wa uokozi wa kutosha kama divers ndani ya nchi yetu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kikosi kazi chenye wataalam kama divers na wakiwa na zana za kisasa za uokoaji ili kuepusha ajali zinazotokea na kuokoa maisha ya watu wetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tuna kikosi maalum kwa ajili ya uokoaji kama kumetokea ajali, kikosi hicho kinashirikisha pamoja na Jeshi la Wananchi, Marine Police, SUMATRA na wadau wengine mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kawaida ajali ikitokea baharini chombo kinatakiwa kipeleke signal maalum ambayo tunaita distressing signals, signal hiyo ikipelekwa meli zote zilizopo zinakwenda kusaidia kuokoa kwa sababu ukisubiri wewe mpaka wataalam watoke Dar es Salaam na meli imetokea pengine kilometa 200 ulipo itakuwa ni too late. Kwa ufupi tu tuna vikosi maalum ambavyo ikitokea tu vikosi hivyo vinakwenda na vinafanya kazi hiyo. Kwanza Polisi, Jeshi la Wanamaji na Zanzibar kuna KMKM na wataalam wengine wapo ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia wale wanaopata ajali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kama Serikali kuwaimarisha hawa kiutaalam ili waweze kufanya kazi na teknolojia za kisasa za uokoaji.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu marefu ya Mheshimiwa Waziri, lakini naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza. Nchi yetu imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii na ni dhahiri majibu ya Mheshimiwa Waziri inaonesha nchi yetu inaona utalii ni mbuga na wanyama tu; na ni dhahiri kwamba ukanda wa bahari unawekwa katika majibu kuonekana tu kama nao upo. Ni dhahiri pia kwamba nchi yetu sasa hivi ina eneo kubwa la bahari kuanzia Tanga mpaka Mtwara lakini utalii wa baharini kama diving, fishing na snorkeling unakua kwa kasi na una fedha nyingi sana. Je, Serikali ina mpango gani madhubuti sasa wa kukuza utalii wa baharini katika nyanja hizo za fishing, diving na snorkeling? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuna matatizo makubwa ya upatikanaji wa umeme na maji katika maeneo ya uwekezaji na hili wawekezaji wanalalamika sana hata huko ambako unasema kwamba TANAPA wanafanya kazi pamoja na Ngorongoro. Wawekezaji wanalalamika kwamba kuna urasimu mkubwa wa kupata vibali vya uchimbaji wa visima au kupeleka umeme kwa ajili ya kutumia katika hoteli zao. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kweli kabisa wa kuondoa urasimu na gharama kubwa kwa wawekezaji katika kupata huduma hizi muhimu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kama amesikia vizuri kwenye jibu langu la msingi nilipokuwa nazungumzia diversification of tourism products (utanuaji wa wigo wa vivutio vya utalii), kwa bahati mbaya kwenye swali la msingi alisikia Ngorongoro na Hifadhi za Taifa za TANAPA akasema ni wanyamapori tu peke yake, lakini ukweli ni kwamba pale Ngorongoro tuna kivutio kikubwa sana ambacho kina sifa kubwa duniani na sasa hivi ni mwelekeo wa watalii wengi sana kuja kuona chimbuko la binadamu duniani ambayo si wanyamapori, hilo ni suala tu la kihistoria.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu suala lake la kukuza utalii katika maeneo mengine, ametaja mfano mmoja tu wa eneo la fukwe za bahari. Huo ni mpango wa Serikali na tayari tumekwishafanya kazi ya awali ya kufanya tathmini ukanda mzima wa bahari kutoka Tanga mpaka Mtwara jumla ya kilometa 1,000 na tumebaini maeneo kadhaa ambayo yana umiliki wa aina mbalimbali, maeneo mengine yanamilikiwa na watu binafsi na watu kama hao. Kwa hiyo Serikali iko kwenye mpango wa kuweza kuangalia namna bora zaidi ya kuweza kuelekeza uwekezaji kwenye maeneo hayo ili tuweze kuweka vivutio hivyo vya diving, fishing, snorkeling na aina nyingine ya utalii wa bahari na utalii wa fukwe.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la upatikanaji wa umeme na maji. Kwa ufupi kabisa, Serikali inayo taarifa juu ya changamoto hizo kwenye eneo hilo na tunachokifanya sasa hivi ni kushirikisha Serikali kwa ujumla wake; Wizara inayohusika na mambo ya umeme na ile inayohusika na maji, lakini pia kushirikisha wadau wa sekta binafsi wanaokwenda kuwekeza kwenye maeneo haya ya hifadhi ili tuweze kuona namna bora zaidi ya kurahisisha kuondoa urasimu, lakini pia kuwapunguzia walaji bei ya huduma hizi.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri katika swali la msingi (b); katika bajeti ya mwaka 2014/2015 Serikali ilisema ilizalisha vifaranga milioni 20 na kuwapa wafugaji wa samaki ili kuweza kuzalisha samaki. Sasa katika bajeti ya mwaka 2015/2016 na 2016/2017 ingawa haijaja, sijasikia Serikali ikisema tena kwamba wamepeleka vifaranga vingapi vya samaki kwa ajili ya wakulima. Je, mpango ule uli-fail ndio ikawa haikuja tena au ulifanikiwa? Kama ulifanikiwa ni kwa kiasi gani?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo wa nchi yetu wa kuzalisha vifaranga vya samaki umeongezeka sana hasa baada ya sekta binafsi kuingia katika biashara hii ya uzalishaji wa vifaranga vya samaki. Sasa hivi Morogoro, Dar es Salaam, Mkuranga na Mwanza kuna uwezo mkubwa tu wa watu binafsi kuzalisha vifaranga vya samaki hadi kufikia vifaranga milioni karibu 36. Kwa hiyo, tunaendelea tu kuhimiza na kutoa elimu kwa watu wenye nia ya kujiingiza katika biashara hii ya uzalishaji wa vifaranga waendelee kufanya hivyo ili kukidhi mahitaji makubwa ambayo yanazidi kuongezeka hapa nchini.(Makofi)
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mheshimiwa Waziri, mimi kama mtaalam wa misitu, naomba hili swali lijibiwe tena, halikujibiwa, la kwanza hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na majibu haya ambayo wataalam wa Mheshimiwa Waziri wamejaribu kuzunguka, unaposema FITI ni Chuo Cha Misitu, Chuo cha Nyuki kwa nini umekiacha? FITI ni consumers siyo misitu. Tukisema foresters ni yule ambaye unampa mbegu anakupa product ama ya timber ama ya log, huyo ndiyo mwanamisitu, sio unayempa ubao akafanya processing. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo, hivi kweli Watanzania tunajiangalia kwamba misitu ina umuhimu kwa maisha yetu na vizazi vyetu na viumbe vingine vilivyomo katika ardhi? Hekta 5,000 kuhudumiwa na mtu mmoja, tuko serious kweli? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, unaposema katika kipindi cha miaka 10…
Mheshimiwa Naibu Spika, sawa. Swali la pili, unaposema una wanataaluma 3,500 katika kipindi cha miaka 10, ni wastani wa 350 kwa mwaka. Hebu tupe mchanganuo kwa sababu katika vyuo vyote darasa halizidi watu 40 na ni madarasa mawili tena ya certificate, wanaochukua degree hawazidi watu 50 kwa siku. Kwa hiyo, mnatoaje watu 350 kwa mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza, pamoja na maelezo mengi ya utangulizi aliyotoa, nililoweza kulinukuu kama swali mahsusi ni kwamba, inawezekanaje hekta 5,000 zikahudumiwa na mtaalam mmoja wa misitu. Dunia inaendeshwa kwa sayansi na teknolojia, wataalam na miongozo mbalimbali. Mawazo na maoni ya mtu mmoja-mmoja yanaheshimiwa lakini yanatakiwa yakae ndani ya utalaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nasoma jibu langu nimenukuu kwamba takwimu hizi au viwango hivi vimewekwa kimataifa na vimewekwa na Shirika la Chakula Duniani la FAO. Sasa inawezekana Mheshimiwa Mbunge ana maoni mazuri zaidi kuliko yale ya Shirika la Kimataifa la Dunia, basi nafikiri maoni yake hayo afuate channels zinazofaa ili kuweza kwenda kuboresha hali hiyo kwa namna ambavyo ataona inafaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, nalo pia ni la takwimu. Anasema inampa mashaka kidogo kuona kama kweli tuna wataalam hao 3,500 kwa kuwa, kwa mujibu wa taarifa alizonazo yeye watalaam wanaozalishwa kwa mwaka kwa vyuo vyote ni 350, sasa ni muda gani utakuwa umepita huo kuweza kupata idadi ya watalaam hawa 3,500. Kwa sababu, hili ni swali linalohusiana na takwimu, swali lake hilo ili niweze kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuweza kumwambia namna gani tumefikia hapo, basi anione kwa wakati muafaka, hata mchana huu nitaweza kumpa mchanganuo mzuri. (Makofi)
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Watanzania wengi ni wakulima, wafugaji na wavuvi. Kwa mantiki hiyo, kisu na panga ni kitendea kazi muhimu na adhimu kwa kukamilisha kazi zao. Kama ni misuse, hata tai inaweza kutoa maisha ya mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini tafsiri sahihi ya neno silaha? Naomba majibu.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri ya silaha tunaitafsiri kufuatana na mazingira inapotumika. Kama mtu amebeba fimbo na anachunga, tunaelewa kwamba mazingira ya anakochunga anastahili kuwa na fimbo hiyo. Leo hii kama mtu anaingia Bungeni na amebeba kisu, ile inageuka kuwa silaha ambayo iko katika matumizi ambapo haitakiwi kuwa na huyo mtu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo, kama mtu anaenda kuangalia mpira (Ndondo Cup), hata kama kwenye utamaduni wake anatakiwa kuwa na mkuki, hatutarajii aende nao kwenye uwanja wa michezo, tunatarajia aende nao anakochunga ambako anaweza akakutana labda na wanyama wakali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, hata uholela tunaoungelea kama ambavyo silaha zote zina utaratibu wa maeneo ambapo zinatakiwa kuuzwa, tunatarajia pia hata kwenye matumizi ziwe katika mazingira yanapotakiwa kutumika. Hatuwezi tukaruhusu Watanzania kila mmoja akawa anatembea na silaha popote anapojisikia kuwa nayo kwa sababu udhibiti wake utakuwa ni hatari kwa namna ya kuweza kuhakikisha wale wasiopenda au wasio na silaha wanaweza wakapata athari popote pale ambapo mwenye silaha anaweza akaamua kuitumia. (Makofi)
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, sina wasiwasi na uimara, uwezo na weledi wa Jeshi letu katika kusimamia majukumu yake na ndiyo maana nje ya mipaka yetu sasa hivi tuko salama lakini ndani ya nchi yetu hali siyo salama na mifano miwili ya juzi ya Mbunge na Meja Jenerali inadhihirisha kwamba ndani ya nchi yetu tuna matatizo.
Je, ni kwa nini sasa Jeshi la Wananchi lisishiriki kikamilifu kukomesha matumizi ya silaha na mauaji ya raia wasio na hatia ndani ya nchi yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, navyoamini mimi au navyoelewa, silaha za kivita zinamilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na matumizi ya silaha ndani ya nchi yetu ni matumizi ya silaha za kijeshi ambazo zinatakiwa zimilikiwe na chombo hiki.
Je, kwa nini sasa Jeshi letu halioni ni wakati muafaka kutumia IO’s wake kuhakikisha kwamba inazikamata silaha zote za kivita ambazo zinatumika kwa matumizi mabaya ya kuua raia katika nchi yetu?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba kazi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni ulinzi wa mipaka lakini pale ambapo linahitajika au linaombwa kusaidia mamlaka nyingine iwe za kiraia au iwe Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama basi wanakuwa tayari kufanya hivyo. Tunavyozungumza ni kwamba mamlaka hizo ambazo ni Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vikihitaji msaada wa Jeshi, mara zote Jeshi linakuwa tayari kutoa msaada huo.
Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo sasa itaundwa task force itakayojumuisha Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama ili kuweza kulifanyia kazi tatizo hili la uvunjifu wa amani ndani ya nchi. Sina shaka kwamba kazi hiyo imeanza na nataka niwahakikishie wananchi wa Tanzania kwamba jukumu hili litafanywa vyema ili hali ya usalama ipatikane ndani ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la matumizi ya silaha za kivita; ni kweli kwamba silaha za kivita zinadhibitiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na kwamba ifanyike kazi maalum ya kuhakikisha kwamba silaha hizo zinapatikana, hiyo kazi inafanyika mara zote.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema bila shaka kwa kutumia task force hizi zilizoundwa kazi ya kuhakikisha kwamba raia au watu wengine wote ambao wanamiliki silaha za kijeshi au za kivita ambazo kikawaida au kitaratibu/ kisheria hawapaswi kuwa nazo zinapatikana na kurudishwa katika mamlaka zinazohusika. (Makofi)
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Waziri aliyoyajibu hata asiyoulizwa, maana yake kaulizwa ng’ombe wa maziwa tu kuku hatoi maziwa. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwanza kuna viwanda vingi vinavyozalisha maziwa hapa nchini, na kwa idadi ya maziwa ya pakiti tuliyonayo ndani ya nchi hii yanazidi mara tano au sita ya lita hizi alizozitaja. Je Mheshimiwa Waziri anataka kutuaminisha kwamba maziwa haya ya pakiti yanayozalishwa nchini ni zile tetesi kwamba ni unga unaotoka India unakuja kuzalisha maziwa hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili amesema wanategemea kuzalisha lita bilioni 3.8 ifikapo mwaka 2021/2022 ni kati ya miaka sita kuanzia leo. Mheshimiwa Waziri kuna miujiza gani ambayo mtaifanya kama Wizara muweze kuzalisha lita bilioni 1.7 katika kipindi hiki cha miaka sita? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba yako maziwa yanayozalishwa hapa nchini yanayotokana na unga wa maziwa na pia ni ukweli kwamba siyo maziwa yote yaliyo kwenye paketi ni yanatokana na huo unga wa maziwa. Wako wazalishaji wanaotumia unga wa maziwa kuzalisha maziwa ya paketi lakini pia wako wazalishaji wanaotumia maziwa ya paketi wanaotumia maziwa ya asili ya moja kwa moja. Viko viwanda vyetu wasindikaji wa maziwa huko Iringa na Tanga hawa hawatumii unga katika kuzalisha maziwa ya paketi ambayo yanauzwa hapa nchini. Lakini viwanda kama vya Bakhresa yeye anatumia unga katika kuzalisha baadhi ya maziwa anayotoa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili tutatumia muujiza gani kufikia hizo lita bilioni 3.8 muujiza ni ule tuliousema katika jibu letu la msingi kwamba combination ya hizo measures ya uzalishaji wa mbari safi, koo safi za mifugo uhimilishaji na uongezaji wa huduma katika mashamba yaliyopo na urasimishaji wa wavunaji wa maziwa katika vijiji vyetu huko, utatufikisha kwenye hili lengo letu la lita bilioni 3.8.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la mahitaji ya samaki limekuwa kubwa sana kwa sababu idadi ya Watanzania imekuwa na hata watoto wangu Wasukuma sasa wanajua utamu wa samaki wa baharini.
Mheshimiwa Waziri tatizo sio nyavu, sio ndoana wala sio nyuzi bali ni namna ya kuwafikia wale samaki, uvuvi wa kisasa unahitaji kuwa na gas cylinders na mask na vitu kama hivyo uzamie ufike kule, samaki sasa wanapatikana katika kina kikubwa cha maji. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wavuvi wetu na vifaa vya kisasa ambavyo vitawasaidia wavuvi wetu kuweza kuwafikia samaki huko waliko na sio nyavu, nyuzi na ndoana?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa swali la nyongeza la Mheshimiwa Salim alilouliza kwamba Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wavuvi hawa kuweza kupata fursa ya kwenda katika maeneo yenye samaki kwa urahisi. Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hatua za awali za kuhakikisha kwamba tunakwenda sambamba na ongezeko la mahitaji ya samaki, tumeingia mkataba na nchi ya Maldives ambapo hivi sasa tunakwenda katika kuboresha teknolojia yetu. Mvuvi anapotoka mwaloni au anapotoka pwani anapokwenda kuvua tayari patakuwa na vyombo vya satellite katika vituo rasmi kumwezesha kujua wapi samaki waliko kwa maana ya distance gani katika eneo la bahari au la ziwa. Teknolojia hii itamsaidia anapotoka pale kuwa na uhakika kwamba atakapokwenda pale atapata mazao hayo ya bahari na maziwa kwa urahisi na itamsaidia kutumia rasilimali kidogo ya mafuta na muda mchache lakini akiwa amepata mazao ya kutosha.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Naipongeza Serikali kwa kuweka mfumo huu wa EFDs kwa ajili ya kukusanya kodi ili kuhakikisha kwamba Serikali inapata mapato stahiki kulingana na biashara zinazofanyika ndani ya nchi yetu, huo ni upande mmoja wa shilingi katika kukusanya mapato.
Upande wa pili, je, ni lini Serikali sasa itaweka bei kwa kila bidhaa inayoingia nchini ili wafanyabiashara wetu wanaoingiza mali kutoka nje ya nchi ajue hasa kwamba nikiingiza gari aina fulani ya mwaka fulani inalipiwa kiasi fulani ili asikwepe kodi lakini na kumfanya mtu wa TRA kuwa na negotiation ya kodi ili Pato la Taifa liongezeke kwa mfanyabiashara wetu kujua hasa kwamba nikileta kitu hiki nakilipia ushuru huu? Kwa hiyo, yeye mwenyewe hakuna negotiation ili kuondoa mambo ya rushwa na mambo ya manung‟uniko kwa wafanyabiashara wetu. Ahsante. (Makofi)anajijua na
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, bei anazosema kwa ajili ya bidhaa zote zinazoingia nchini tunazo na ndiyo ambayo inakuwa ni base ya kuweza kufanya tax assessment kwa bidhaa zote zinazoingia. Kwa hiyo, tunazo bei hizo ambazo zinakuwa zimetumika kwa bidhaa hizo kwa muda wa miezi mitatu iliyopita, miezi sita, miezi sita ndani ya nchi yetu bidhaa hizo ziliingia kwa kiasi gani. Kwa hiyo hizo taarifa na database tunazo katika Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba tunazo hizo lakini pia Mamlaka ya Mapato huwasiliana na mamlaka za masoko mengine nje ya nchi yetu kuweza kujua bidhaa kama hizo zinauzwa kwa shilingi ngapi ili tunapofanya tax assessment kwa ajili ya wateja wetu, tuwe tunawatendea haki wateja wetu. Kwa hiyo, tunatumia njia zote hizo na database hiyo Mheshimiwa Mbunge ipo kabisa na tunaitumia.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ni dhahiri mbinu zote za ulinzi zinazotumika pamoja na ulinzi shirikishi bado hazijasaidia kutatua tatizo la uharibifu wa misitu na hususan misitu ya asili kwenye nchi yetu. Je, Serikali inafikiria nini sasa kuhusu mbinu mbadala ya kuhakikisha kwamba misitu yetu inahifadhiwa na kuendelezwa kwa ajili ya kizazi kijacho?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza siyo jambo jema sana kuthibitisha hapa kwamba jitihada zote zile za kisheria na zile za kupitia ushirikishaji wa wananchi zimeshindikana kuweza kuzuia tatizo hili la uharibifu wa mazingira. Napenda kuungana na Mheshimiwa Mbunge kuona kwamba jitihada hizo bado zipo na zinatakiwa kuendelea. Tunatakiwa tu kuboresha namna ambayo tumekuwa tukifanya hapo nyuma, maisha bado yanaendelea ili tuweze kuhakikisha kwamba uhifadhi wa mazingira unaendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaongeza idadi ya Wataalam ili waweze kusimamia vizuri zaidi, lakini pia tutaweza kusimamia misitu ili tuweze kupunguza uharibifu wa mazingira.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwa masikitiko makubwa niiombe Serikali inapokuwa haina majibu ya maswali tunayouliza basi wasitujibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili nilichangia bajeti 2015/2016 Naibu Waziri akiwa Olenasha yule pale akanijibu kwamba hivi ni vifaranga vya mfano milioni 21 ndio vimezalishwa kwa ajili ya kuwapelekea wakulima imo katika kitabu cha bajeti cha Wizara hii 2015/2016; leo Serikali inaniambia kutoka 2009/2010 mpaka 2017/2018 imezalisha vifaranga milioni 21 na kuvigawa. Tukisema Mheshimiwa Jenista anakuja juu ni uongo uliotukuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali haina majibu isitujibu kwa sababu tunafuatilia haya mambo.

Sasa mimi siwezi kukubali kama Serikali imezalisha ina mpango huu swali la kwanza ninalomuuliza Mheshimiwa hata siku hiyo katika mjadala wangu niliuliza hivi vifaranga miloni 21 kwa Tanzania kwa mwaka vinatosha hata mboga ya siku moja kwa Watanzania maana hata shemeji zangu wamasahi wanakula samaki Je, Serikali iko serious kweli? Kwa hiyo Je, vinatosha hata hizo tani 50 mnazosema ikifika 21 zinatosha hata kwa mboga ya siku moja? Wako serious hawa kweli? Swali la kwanza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, katika bahari sasa kuna upungufu mkubwa wa samaki baharini na ongezeko la walaji wa samaki limeongezeka, je, kule baharini mna mpango gani wa kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania; Wizara yetu ina nia thabiti ya kuhakikisha kwamba ufugaji wa samaki na kusambaza vifaranga kwa watu ni jambo ambalo linapewa kipaumbele. Mheshimiwa Mbunge ana wasiwasi na takwimu tulizozitaja zinazohusu usambazwaji wa vifaranga milioni 21 nilivyovitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie kwamba katika vituo vyetu nilivyovitaja, Kingolwira pale Morogoro ninao uhakika wa kwamba vifaranga hivyo vinazalishwa na vipo kwa ajili ya wakulima wetu na wafugaji wetu. Kama ana taarifa tofauti na hiyo sisi Wizara yetu ipo tayari kupokea taarifa yake iliyo tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nimwambie kwamba katika kuhakikisha kwamba ufugaji wa samaki unapewa kipaumbele Serikali tumehakikisha katika msimu huu tunaokwenda nao wa fedha wa 2018/2019 tunaendelea na mazungumzo ya Wizara ya Fedha ili kuhakikisha tozo na kodi mbalimbali ambazo zinazuia ama kurejesha nyuma sekta hii ya ufugaji wa samaki zinaondolewa kusudi Watanzania walio wengi waweze kufuga samaki, waweze kupata kipato, waweze kupata lishe na tuache biashara ya kuagiza samaki kutoka nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge katika swali lake la pili ametaka takwimu ya kwamba je, hii tani 50 niliyoitaja ndiyo inayotosheleza? Ni kwamba hivi sasa katika nchi uwezo wetu wa kuzalisha samaki ni tani 350,000 kwa mwaka, ambapo tani zaidi la 250,000 zinatoka katika Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hitaji la samaki katika nchi ni tani 700,000 kwa hiyo tuna gap ya tani 350,000 na ndiyo maana ni muhimu sana katika aquaculture katika kipindi hiki kuliko kipindi kingine chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameniuliza tuna mipango gani na bahari yetu. Mpango tulionao hivi sasa katika uzalishaji wa samaki kwenye bahari tuna kitu tunaita cage farming. Cage farming ni uzalishaji wa samaki wa kufugwa katika bahari, katika mito na katika maziwa. Mkakati huo tumeuanza na unakwenda vizuri. Tumeshaweka cage za kutosha pale Bagamoyo, zaidi ya cage 40. Tunaendelea kuweka cage vilevile katika Ziwa Victoria na maziwa yetu mengine ili kuhakikisha kwamba ufugaji wa samaki na kuzifikia hizi tani 50,000 unapatikana. Nawahamasisha Waheshimiwa Wabunge wote ya kwamba ufugaji wa samaki unalipa, na wewe Mheshimiwa Salim ingia katika ufugaji wa samaki uweze kunusurika pia vile vile katika kuinua kipato chako. Ahsante.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Waswahili wanasema usipoziba ufa utajenga ukuta. Imekuwa ni tatizo linaloendelea na ni maneno kila siku yanazungumzwa kuhusiana na uharibifu wa vyanzo vya maji na hususani Chemchemi.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha inatoa elimu kwa wananchi wote wanaozunguka maeneo ya vyanzo vya maji ili kuhakikisha kwamba wao ndio walinzi lakini hao hao wawe ndiyo watunzanji wa mazingira wa maeneo yale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sera yetu hii ya Taifa ya Hifadhi ya Mazingira pamoja na Sheria ya Mazingira tayari Mheshimiwa Waziri alishatoa miongozo na maelekezo kwa Halmashauri zote 185 Tanzania watuletee orodha ya vyanzo vyote vya maji ikiwa ni pamoja na changamoto. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tuko katika harakati za kuhakikisha kwamba tunaweka mikakati ya utoaji wa elimu kwa wananchi ambao wako kwenye vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kutangazwa kwenye Magazeti ya Serikali. Ahsante sana.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Naibu Waziri ametusaidia. Hili tatizo liko kutoka mwaka 2006. Sheria zipo, kanuni zipo na Ilani ya Chama cha Mapinduzi imesema hivyo, lakini iaonekana ni hadithi na ni mazungumzo tu humu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutuambia ni vyanzo vingapi ambavyo tayari wamevifanyia demarcation na rehabilitation kama sampling areas ya kuhifadhi vyanzo vya maji, kama kweli wana nia ya kuhifadhi vyanzo vya maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge kwamba ni vyanzo vingapi. Hadi mwaka 2017 tayari tulishabaini vyanzo 18, tumeshaviwekea mipaka tayari. Mwaka huu wa Fedha tulionao tulibaini vyanzo sita, tunaendelea kuviwekea mipaka na tutaendelea kufanya hivyo. Mheshimiwa Mbunge usubiri hotuba yangu inaanza Jumatatu tarehe 7 Mei, kwa hiyo, taarifa kamili utaipata vizuri zaidi kupitia kwenye hotuba yangu. (Makofi)
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Suala la migogoro ya ardhi, misitu, maliasili na wananchi inazidi kuongezeka kila siku hapa nchini hali ambayo inaipatia Serikali hasara kubwa ya kuweka ulinzi katika maeneo hayo, halikadhalika wananchi wanaathirika sana kwa kuchomewa majumba yao na mali zao kuharibiwa kutokana na zoezi hilo. Sasa inaonekana hii dhana ya ushirikishi inayotumika hapa labda inatumika vibaya au hawajashirikishwa kwa dhati. Je, Mheshimiwa Waziri na Serikali yake wako tayari sasa kuja Zanzibar kujifunza mbinu walizotumia katika haya na wakafanikiwa?
NAIBU WAZIRI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba niseme kwamba tuko tayari kabisa kwenda kujifunza mbinu bora za kuhakikisha migogoro hii haipo. Kama walivyofanya Zanzibar basi na sisi tungependa tutumie mbinu hizo hizo kuhakikisha kwamba huku migogoro yote inamalizika.
MHE. YUSSUF SALIM. HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri katika nchi yetu kuna mazoea ya kwamba miradi hii ya hifadhi ya mazingira inafadhiliwa fedha nyingi kutoka kwa wafadhili lakini wanapoondoka tu miradi yenyewe inakufa kwa mfano HADO, HASHI, katika ile miaka ya mwishoni mwaka miaka ya 1980.
Je, Mheshimiwa Waziri unatuhakikishiaje fedha hizi zitakazokuja sasa kwa ajili kukabiliana na tatizo la tabianchi zitatumika vizuri na zitakuwa endelevu ili kukidhi kile kiwango cha kupotea kwa misitu ya hekta laki 350,000 kila mwaka katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na tumeanza utaratibu wa kuwashirikisha wananchi moja kwa moja katika miradi yote ambayo inakuja na miradi hii wananchi wenyewe wanatengeneza utaratibu wa kuweza kusimamia. Kwa hiyo, ni imani yetu kwa kupitia watalaam wetu na wananchi kuwashirikisha moja kwa moja na nimuombe Mheshimiwa Mbunge na yeye awe sehemu ya kuhakikisha kwamba hili suala linakuwa endelevu. Ahsante.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya nchi yetu ya Tanzania imekuwa kama ni laana kwa mwanafunzi kufeli darasa la saba au form four, lakini India, mainjinia leo wanaoendesha mitambo ya gas and petroleum ni wale waliofeli darasa la saba.
Je, Serikali yetu lini itaona umuhimu wa kuwaendeleza vijana waliofeli darasa la saba na form four ili na wao waje kuwa mainjinia katika viwanda vyetu na mitambo yetu Nchini?

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Serikali na nchi kwa ujumla inathamini kila rasilimali ya mwananchi iliyopo nchini na ndiyo maana kupitia vyuo vyetu vya VETA, kupitia FDC, kupitia mafunzo yasiyo rasmi imekuwa ikiendelea kutoa mafunzo ili kuhakikisha kwamba vijana hao wanaendelea kuajirika na kujiajiri wao wenyewe.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yake amesema kwamba wale wanaokiuka taratibu hizi sheria inawapa mamlaka ya kuwafungia ama kuwapiga faini, zote hizo ni force approach. Dunia ya leo ni dunia shirikishi, Wizara ina mpango gani wa kuwashirikisha na kuwaelimisha wenye viwanda na kushirikiana nao kuona tatizo hili linamalizwa kabisa badala ya kutumia nguvu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kwamba kabla ya mwekezaji kuanza kuwekeza hatua ya kwanza sisi huwa tunatoa elimu. Mpaka afikie hatua ya kupata certificate ya EIA, maana yake amekidhi vigezo vyote. Kinachofuata akikiuka utaratibu ambao tumeuweka ni lazima tumpige faini.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Aaah, ni mimi bwana.
Nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nakubaliana na Mheshimiwa Waziri kwamba gharama za kupanda Mlima Kenya haziwezi kulingana na Mlima Kilimanjaro kwa sababu ya unique tuliyonayo katika mlima wetu. Tumezungumza na tour guides ambao wanafanya hiyo kazi, wanasema hiyo siyo sababu; sababu ni kuongezeka kwa 18 percent ya VAT katika gharama ambayo inamgusa moja kwa moja mtalii.
Je, Serikali lini sasa itakaa kuona kwamba hili ni tatizo na kuonda 18 percent kwa wageni wanaokuja ili waje kwa wingi na tukusanye kwa wingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ni kweli kabisa kwamba Serikali ilianzisha VAT katika huduma mbalimbali za kitalii ambazo zinatolewa, ni karibu takribani miaka miwili sasa imepita toka kuanzishwa kwa VAT.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tuliagizwa tufanye utafiti mpana zaidi tuone kama kweli hii VAT imeleta athari. Sasa katika kipindi kifupi ni vigumu sana kuweza kujua kama VAT imeleta athari au haijaleta athari. Kwa hiyo, sasa hivi ambacho tunakifanya, tunataka tufanye study kubwa, lakini pia tuone ni maeneo gani ambayo tunaweza kuyatumia ambayo tunaweza kupanua wigo wa kupata mapato mengi zaidi badala ya kutegemea tu suala la VAT.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili tutalifanyia kazi na tunaomba tuendelee kupata maoni zaidi na mawazo namna ya kuboresha huduma zetu hizi za utalii.
MHE. YUSSUF HUSSEIN SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kidogo nimeguswa hapa. Huyu papa ni papa mmoja na hadhuru mwanadamu na mara nyingi kwa kule kwetu sisi huwa mwezi Desemba wanatoka Somalia wanakuja zao mpaka wanakuja kupiga kambi Minai – Zanzibar wanakuwa kwa wingi sana na huyu papa huwa anawafuata wale dolphins. Mara nyingi huwa anawafuata wale dolphins, swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, kipindi cha Desemba mpaka Februari wanakuja na kurudi ni kipindi ambacho tunaweza tukafanya utalii mkubwa sana katika eneo letu la kuanzia mpakani na Kenya Duga mpaka Zanzibar. Je, Wizara yako imejipangaje sasa kutumia fursa hii ambayo wale dolphins na huyu papa wanatangaza nchi yetu wenyewe, sisi tutumie tu hiyo fursa. Lini tutatumia hiyo fursa ya kujenga hoteli katika ukanda huo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba katika kipindi hiki hawa potwe wanakuwa wengi sana katika maeneo haya au wanakuja katika maeneo haya. Pia kuna vivutio vingi sana ambavyo vipo katika ukanda wa bahari yetu hasa katika fukwe zetu hizi za bahari ambazo tunaweza tukafanya na ndiyo maana Serikali sasa hivi iko mbioni katika kuhakikisha kwamba tunaanzisha mamlaka ya kusimamia fukwe zote za bahari kusudi tuweze kufaidika na huu utalii wa baharini ambao tulikuwa hatujautumia kwa muda mrefu sana. Kwa hiyo, naamini katika hizi jitihada, pale ambapo zitakuwa zimekamilika na sheria itakapokuwa imeletwa hapa Bungeni basi hizi jitihada zitakuwa zimekwenda sambamba na hilo wazo la Mheshimiwa Mbunge. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nasikitika kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri hajajibu hili swali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuathirika kwa kilimo ni matokeo ya athari za tabianchi. Tuambie Serikali ina mikakati gani ya kukabiliana na athari hizi? Maziwa yanakauka, mito inakauka, misitu inapotea. Mna mkakati gani mliouchukua au ndiyo mko kwenye mipango tu? Ndiyo jibu tunalolitaka kutoka kwako. Nakushukuru.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ambalo Mheshimiwa Mwantum Dau Haji alitaka kujua Serikali tuna mipango na mikakati gani; nimeeleza kwamba mkakati wa kwanza tulionao tuliuandaa mwaka 2007 ambao unahusu uhimilivu katika mabadiliko ya tabianchi kwenye suala la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimejibu hapa kwamba mwaka 2012 tuliandaa mpango mwingine wa mabadiliko ya tabianchi tofauti na ule wa mwanzo. Vilevile nimejibu hapa kwamba mpaka sasa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na kupitia wataalam tunaandaa na tunakaribia kumaliza kupata sasa mpango mkakati endelevu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwenye suala la kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo kwamba mikakati haipo, nimeieleza hapa. Pia nimeelezea hapa kwamba hata juzi Mheshimiwa Rais amezindua ASDP Awamu ya Pili ambamo ndani mwake pia kuna mikakati mingi sana imezungumziwa. Pia mikakati na mwongozo niliousema ambao tumepeleka kwenye Halmashauri ambapo Maafisa Mipango wanatakiwa kuweka kwenye bajeti zao, tumeelezea kuhusu utafiti wa mbegu ambayo inahimili kwenye ukame pamoja na kilimo cha umwagiliaji na umwagiliaji wa matone.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mikakati hii ipo, Mheshimiwa Yussuf mtani wangu wa kisiasa, naomba uelewe Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni Serikali makini, ni Serikali ambayo inaongoza kwa kuwa na mikakati, tena mikakati ambayo inatekelezeka. Ahsante sana.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nimuulize mtani wangu kama anavyotaka. Mwishoni mwa miaka ya 80 kulikuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira ambao ulipelekea mmomonyoko mkubwa wa ardhi katika Mikoa ya Dodoma na Shinyanga na kukawa na miradi ya uhifadhi wa mazingira ambayo ilikuwa inaitwa HADO kwa Dodoma na HASHI kwa Shinyanga. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kufufua miradi ile ambayo ilipelekea Mikoa husika kuwa na hali nzuri kama ilivyo Dodoma sasa? Serikali ina mpango gani wa kuhuisha miradi kama ile katika mikoa mingine ambayo imeathirika zaidi kwa uharibifu wa mazingira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la mtani wangu wa kisiasa Mheshimiwa Yussuf, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 19 wakati tunajibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji tulieleza mikakati mbalimbali ambayo tunayo katika kuhakikisha kwamba tunapambana na uharibifu wa mazingira katika masuala ya vyanzo vya maji lakini pia kwenye ardhi kama ambavyo Mheshimiwa Yussuf amezungumzia. Tulisema mkakati ule tumehusisha wasomi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na utakuwa tayari hivi karibuni, unaonesha namna gani ambavyo katika nchi yetu maeneo yalivyoathirika, si tu kwa Dodoma huku ambako tunasema kuna ukame lakini pia maeneo yale ya wafugaji ambapo ardhi imeharibika kwa kiasi kikubwa. Mkakati ule tunauita ni Mpango Maalum Endelevu wa Matumizi Bora ya Ardhi pale ndipo ambapo tutakwenda kutekeleza mambo hayo kwa sababu mikoa yote ambayo ina shida kubwa zaidi ya mmomonyoko wa udongo imeanza kubainishwa katika mkakati ule. Nakushukuru sana.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Suala la wakulima limekuwa ni tatizo kubwa, kilio hawana mbolea, hawana pembejeo, hawana mbegu kwa wakati, lakini hata hiki kituo cha kilimo ambacho kinawasaidia wakulima kupata unafuu katika kilimo chao kimekuwa nacho ni tatizo. Je, Mheshimiwa Waziri hebu atuambie hasa ni upi mkakati wa Serikali? Nami naipongeza Serikali kwa kuweka kituo hiki hapa Tabora, ni upi mkakati wa Serikali sasa? Wa kuwapunguzia watoto wangu hawa Wanyamwezi na Wasukuma ugumu wa kilimo cha kutumia zana duni?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la wanyamakazi kwa mfano kule Nyanda za Juu Kusini, kilimo la maksai kimeimarika sana. Ni kweli upande wa huku Mikoa ya Magharibi hakijaimarika, lakini kwenye jibu langu la msingi nilisema kabisa kwamba, Wizara ya Kilimo kupitia TARI, tumeanzisha TARI ili kuhakikisha kabisa kwamba tunaimarisha na kuboresha vituo vyetu vyote vile vya utafiti pamoja na vya zana za kilimo ambavyo vinasimamiwa na halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Mheshimiwa Yussuf mpango mkakati wa Serikali upo imara, hususan Serikali hii ya Awamu ya Tano na ndio maana tumesema tuwe na TARI kuboresha na kuimarisha vituo vyetu vyote vya utafiti na nimesisitiza waandike proposals wasitegemee tu kabisa pesa ya Serikali au fungu la Serikali, wajiongeze. Nakushukuru.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kuna malalamiko makubwa kutoka kwa utatu wa uwekezaji katika maeneo yote ya uwekezaji, kwa maana ya jamii, Serikali, pamoja na mwekezaji mwenyewe, kila mmoja akilalamikia kwamba hapati stahiki zake. Je, ni lini Serikali itakaa pamoja sasa kuuweka utatu huu, kwa maana ya Serikali, jamii na mwekezaji na kuweka mazingira sawia ambayo kila mmoja atampa haki yake kuwe hakuna malalamiko katika uwekezaji kabla ya mwekezaji hajapewa kibali cha kuwekeza?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais mwaka jana alivyoanzisha Wizara Maalum kwa ajili ya Madini, kwa sababu zamani ilikuwa ni Wizara ya Nishati na Madini, lakini mwaka jana mwezi wa Kumi Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alianzisha Wizara Maalum inayoshughulikia Madini baada ya kuona umuhimu wa kuanzishwa Wizara hii. Kwa kweli tangu Wizara imeanzishwa, sisi tumeanza pale, tumeanza kukaa na wawekezaji, wawekezaji wa kati, wawekezaji wadogo na wawekezaji wakubwa, kuangalia changamoto walizonazo, kuangalia namna bora ya kuweka mazingira ya uwekezaji ili kila mwekezaji aondoke katika kulalamika kutokana na vikwazo anavyovipata katika kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi kama Wizara tuna mikakati mizuri katika kuhakikisha kwamba wawekezaji wanaokuja wanawekeza vizuri na wanawekeza bila vikwazo. Sasa hivi kuna wengine wamelalamikia kuhusu kodi, nao tumewaambia walete malalamiko yao tuyaangalie. Kwa mfano wawekezaji wa chumvi, kulikuwa kuna kodi 16, katika Bajeti hii zimeondolewa kodi 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni moja au kiashiria kimoja cha kuona kwamba Wizara inafanya kazi ya kuwasikiliza wawekezaji na wachimbaji kwa nchi nzima na kuangalia namna bora ya kuwaondolea vikwazo ili waweze kuwekeza na waweze kuchimba kwa faida. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupana nafasi, Mheshimiwa Waziri amesema kama askari au afisa amefariki analipwa dola 70,000. Sasa ningependa kujua dola 70,000 hizi wanalipwa warithi wake cash au kuna mgao wa Serikali unakatwa kutoka hizi kama ambavyo wanakatwa wale askari wanaoenda katika misheni zile, sijui umenielewa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, fedha hizi hazikatwi, wanapewa dola 70,000 zote lakini sio mwisho, hii ni fidia kutoka Umoja wa Mataifa lakini askari yeyote anayepoteza maisha ana fidia vilevile kutoka hapa nyumbani. Kwa hiyo, kuna fedha zinazotolewa na Wizara kwa ajili ya kulipa fidia familia ya wale ambao wamepoteza maisha wakiwa kazini.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba kuna Maaskari Polisi waliopandishwa vyeo, alipandishwa kutoka private kuja Koplo ametumikia Koplo kwa miaka minne, mpaka ameenda Sajenti hajapata mshahara ule wa Koplo na wengine mpaka wanafikia kustaafu wanakosa stahiki zao analipwa kwa mshahara ule aliotokea nao. Je, Mheshimiwa Waziri Askari kama hawa atawa-consider vipi katika zoezi analoendelea nalo ili wapate haki zao kulingana na Utumishi wao walivyotumikia nchi hii?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kusema kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, kwamba mishahara inaendelea kurekebishwa kwa Maofisa, Wakaguzi pamoja na Askari. Hata hivyo, kama kuna suala ambalo linamhusu Askari ambaye amemsema kwamba alipanda cheo na nirekebishe kidogo, Jeshi la Polisi hatuna private, tuna constable kuanzia constable akaenda Koplo, Sajenti na hajarekebishiwa, namwomba Mheshimiwa Yussuf anipe jina la Askari huyo ambaye amemsema ili nifuatilie nijue kwa nini apande vyeo vyote hivyo pasipo kurekebishiwa mshahara wake. Ahsante.
MHE. YUSSUF S. HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba niulize swali dogo la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri. Hii mito ambayo inatoka baharini na kuingia nchi kavu inakuwa na kasi sana wakati yale maji yapoingia ama yanapotoka, kwa sababu tabia ya bahari, maji yanapojaa yanakuwa yana nguvu sana na yanapotoka vilevile yanakuwa na nguvu. Maana yake ni kwamba ongezeko la soil erosion linakuwa kubwa kuliko linavyotarajiwa. Ni upi sasa mkakati wa Kitaifa wa Serikali kwa sababu ardhi yetu inapungua kwa kasi? Msimbati itakuwa ni moja kati mfano mzuri wa kasi wa maji haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni upi mkakati hasa wa Kitaifa wa Serikali kudhibiti suala hili la erosion katika kingo za bahari zetu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ulishaanza na nitoe mifano, ukiangalia kingo za bahari pale Ocean Road tumejenga. Pia ukienda Pangani tumejenga na maeneo mengine tutaendelea kadri ambavyo tutakapokuwa tunapata fedha za kuhakikisha tunakabiliana na haya mabadiliko ya tabia nchi. (Makofi)
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo swali, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na faida ya watalii kuja kuona vipepeo, nimegundua watalii wengi wakishaona wanafanya identification na wanachukua sample za vipepeo na kuondoka nazo. Je, Serikali yetu imeshafanya utafiti wanaenda kufanyia nini hivyo vipepeo wanavyochukua ili kuhakikisha hatupotezi rasilimali ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yussuf, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba watalii wengi baada ya kuona vipepeo hutamani kuondoka nao na baada ya kuondoka nao kitu ambacho tumegundua ni kwamba nao wanakwenda kufanya biashara ileile ambayo sisi tunafanya ili watalii waje Tanzania. Kwa hiyo, ni kwa sababu hiyo Wizara ikaona hamna sababu tena ya kuendelea kuuza wanyama hai nje ya nchi.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada za Serikali kuona inainua kilimo hiki au zao hili la muhogo ambalo ni tegemeo kubwa hususan kwa watu wa Mikoa ya Kanda ya Mashariki, lakini zao la muhogo linakabiliwa na magojwa ya Cassava Mill Bags. Je, nini kauli ya Serikali kukabiliana na wadudu hawa ambao wanaathiri sana zao la muhogo ambalo linawarudisha nyuma wakulima wanaolima zao hili?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Alichokisema ni kweli kabisa na haya masuala ya magonjwa ya mazao siyo kwamba yapo kwenye kilimo cha muhogo peke yake, bali mazao mengi yamekuwa yakiathiriwa sana na wadudu. Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ameshatoa msisitizo na ametoa maagizo kwamba viuatilifu ambavyo ni feki visitumike kwenye mazao. Yeyote ambaye atakamatwa anauza au anampatia mkulima viuatilifu feki ambavyo havisaidii kupambana na magonjwa na wadudu atachukuliwa hatua kali na Serikali. Kwa hiyo, hiyo ni elimu mojawapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua za makusudi kabisa na kupitia vituo vya utafiti kikiwemo Kituo cha Utafiti cha Naliendele na kituo cha utafiti ambacho kipo chini ya Wizara ya Kilimo cha pale Dar es Salaam wamefanya utafiti mzuri wa mbegu ambayo inahimili magonjwa kama hayo. Kwa hiyo, msisitizo ni kutumia mbegu ambazo zinahimili matatizo hayo.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Wabunge hawa wanapouliza kuhusu kero za Muungano na vipi zinatatuliwa, ni kwamba tunaporudi kwa wapiga kura wetu tunazikuta. Kwa hiyo, inaonesha kwamba kero za Muungano zinatatuliwa kwenye meza, lakini kwenye vitendo hakuna. Kwa mfano, msafirishaji wa ng’ombe kutoka Zanzibar akija akichukua ng’ombe Bara kupeleka Zanzibar analipishwa ushuru sawasawa na anayesafirisha kupeleka Kenya kwa Sh.37,500 badala ya Sh.7,500. Sasa ni ipi faidi ya Wazanzibari kuwa ndani ya Muungano? Nakushukuru.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli haikutazamiwa kwamba Mheshimiwa Mbunge atauliza ni zipi faida za kuwepo Muungano, kwa sababu hata yeye kuwepo kwake hili ni Bunge la Jamhuri ya Muungano. Muungano huu kwa pale tulipofikia hata haihitajiki kueleza faida zake kwa sababu zinaonekana dhahiri. Ukweli upo kwamba, zipo changamoto katika shughuli za kila siku za maingiliano na mahusiano hiyo haikataliwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko changamoto kubwa za kisera ambazo ndiyo zinashughulikiwa katika vikao vya viongozi, lakini kuna yale mambo ya kila siku kwamba Afisa Forodha pale ameamua mwenyewe kwa anavyoona afanye jambo. Tunachosema sisi kwa wananchi wa pande zote mbili ni kwamba yanapojitokeza mambo kama haya, kama hili alilosema Mheshimiwa Mbunge, yaletwe kwetu haraka kwa sababu ni masuala ya kiutendaji ambayo yanashughulikiwa haraka. Yako mambo mengi ya namna hii ambayo yametatuliwa kwa taarifa tu kwamba, kuna jambo hili sisi tunadhani haliendi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi tunasema kwamba, changamoto hizi ndogondogo zisitumike kuupa jina baya Muungano, kwa sababu wakati mwingine ndipo makosa yanapofanyika, kwamba inatokea tatizo ambalo lipo tu, ni la kiutendaji, la kibinadamu, lakini linatumika kwamba Muungano wetu haufai kwa sababu kuna kitu hiki. Muungano huu ni mpana zaidi na ni mkubwa zaidi na una maana kubwa zaidi kuliko changamoto zinazojitokeza kila siku.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo lililoko Tabora Mjini kwa watoto wetu ni sawasawa na tatizo lililoko Pemba kwa wazazi wao, tatizo la mawasiliano. Mheshimiwa Waziri swali hili uliulizwa mwaka jana na Wabunge wawili na ukaahidi kuja Pemba na ukaja Pemba wewe mwenyewe ukaona tatizo lililopo, hususan kwa Mheshimiwa Maida na Mheshimiwa Bi. Mgeni lakini hadi leo tatizo liko vilevile halijatatuka hakuna mawasiliano katika maeneo hayo. Sasa nini impact ya safari yako kuja Pemba zaidi ya marashi ya karafuu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Yussuf, rafiki yangu sana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nilikwenda Pemba mwezi Januari kwa ajili ya kukagua hali ya mawasiliano ya Kisiwa cha Pemba na ni kweli nilikuta hali si nzuri sana. Nikuhakikishie tu Mheshimiwa Yussuf kwamba impact ya safari yangu pamoja na marashi ya Pemba vilevile ni kuhakikisha tunawaletea mawasiliano ili wananchi wa Pemba waweze kuwasiliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tuliyoikuta kule ni kwamba kuna hali ya kijiografia ya mabonde na milima, halafu ina minazi mingi sana. Kwa hiyo, badala ya kuweka mnara mmoja u-supply radius ya kilometa 15 kama kawaida ina supply radius isiyozidi kilometa 4, kwa hiyo, inahitaji minara mingi sana. Kama unavyojua mnara mmoja ni shilingi milioni 300 mpaka 600, kwa hiyo, ni lazima tuwe na uwekezaji wa kutosha. Nakuhakikishia kwamba tutaweka uwekezaji huo kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ili wananchi wa Pemba na hasa kwenye kihoteli kile cha chini ya bahari waweze kupata mawasiliano.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Napenda nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu, kumekuwa na malalamiko mengi ya wanawake kwamba hawapati nafasi za kutosha katika shule kuanzia sekondari, vyuo na vyuo vikuu. Sasa ni mkakati wa Serikali kwamba wanawake wakifikia hapo waanze kubinywa au wanawake wenyewe wamezoea kudekezwa tu?

MWENYEKITI: Hebu tusaidiane kidogo, unauliza vizuri lakini hilo neno kudekezwa linyooshe tu.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aseme kuna mkakati kwamba wanawake wanabinywa au sasa wao wenyewe wanataka wasaidiwe tu kwenda vyuoni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti nilichokuwa nazungumzia katika maswali yangu yaliyopita ndiyo inajionyesha dhahiri hapa kwamba ni suala la mila, desturi na fikra potofu dhidi ya uwezo wa watoto wa kike kuweza kuendelea na kufanya vizuri kama watoto wa kiume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waheshimiwa Wabunge kila mmoja katika nafasi yake ajielekeze kwenye ukweli kwamba mtoto wa kike ana uwezo sawa na mtoto wa kiume, kwa hiyo, tuwasaidie waweze kusonga mbele.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri mahiri katika Wizara hii ya Muungano, lakini pamoja na hayo nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; bandari hiyo ambayo inatakiwa ijengwe Zanzibar pale Mpigaduru ina thamani au itagharimu dola za Kimarekani milioni 430, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshapata mdhamini au mkopo kutoka Exam Bank wa dola milioni 200, ni miaka nane sasa tokea mradi huu upite, Serikali ya Muungano imeisaidiaje Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupata mikopo au msahada wa kumalizia hapo palipobaki ikajengwa gati hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu Serikali ya Muungano imeingia mkataba wa kujenga gati ya Bagamoyo na Oman ndiyo wafadhili wa gati hii, lakini mkataba ule unaizuia Oman kusaidia tena nchi yoyote ya Afrika Mashariki kwa mujibu wa kilometa zilizowekwa kujengwa gati kama ile.

Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba mkataba huu ndiyo ulioifanya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikose msaada kutoka Oman kwa ajili ya kujenga gati ile?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa katika mazungumzo na mazungumzo hayo yanaelekea ukingoni kuhusu kukamilisha kipande cha rasilimali zinazotakiwa kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Mpigaduru. Tunafahamu kwamba ni moja ya ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM na ni bandari muhimu sana kwa uchumi wa Zanzibar na wote tunajua hivyo na tunafahamu hali ya bandari ya Zanzibar, sasa hivi ilivyo na msongamano. Kwa hiyo tunazungumza na wenzetu kuhakikisha kwamba tunafanikiwa katika hilo.

Mheshimiwa Spika, la pili, mkakataba wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo bado haujaingiwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kampuni ya China kwa kushirikiana na Oman. Kwa hiyo yale masharti yaliyopo yanayozungumzwa hayatumiki sasa kwa sababu bado utekelezaji rasmi haujaanza. Hata hivyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wazanzibari wote kwamba Serikali haitaingia katika maamuzi ambayo yataathiri ustawi na uchumi wa Zanzibar.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa safari za ndani za ATCL hakuna mkoa wowote unaoishinda Pemba kwa biashara ya ndege. Mheshimiwa Waziri ulituita mbele ya wadau ukatuahidi kwamba ikifika Novemba/Desemba, 2018 ATCL itaanza safari za Pemba. Hadi leo mwezi Aprili, 2019 haijaanza safari kuelekea Pemba, nini kauli yako Mheshimiwa Naibu Waziri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mwaka jana tuliongea na baadhi ya Waheshimiwa kutoka Pemba kuhusu uwezekano wa ATCL kupeleka ndege yao Pemba. Mpaka sasa hivi hatupingi kwamba kuna abiria wa kutosha Pemba lakini ndege zenyewe siyo nyingi kiasi hicho. Naomba Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine wote waendelee kuvuta subira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Mheshimiwa Rais ametupatia ndege mbili za Serikali, tunaendelea kuzipaka rangi ili zianze kutumika kwa ajili ya abiria. Kwa hiyo, naamini hata Pemba tutawapelekea ndege moja na sehemu nyingine mbalimbali tutaendelea kupanua wigo wa kusafirisha watu kwa usafiri wa anga.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nimrejeshe Mheshimiwa Naibu Waziri katika swali la msingi la kanuni za ufugaji bora na kilimo cha kisasa. Sasa ni wapi Mheshimiwa Waziri anaweza akatuambia kwamba ni sampling area ambapo Serikali inafanya ufugaji bora na kilimo cha kisasa ambacho kitaondoa hiyo migogoro baina ya wafugaji na wakulima, sampling area katika nchi ni wapi ili wengine wakajifunze?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwanza kwa pongezi zako hizi za kunielekeza kuwa najibu vizuri sana isipokuwa nijibu kwa kifupi na nitafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Yussuf kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wapi katika nchi? Nataka nimhakikishie tunayo maeneo mengi sana katika nchi ambayo yana wafugaji wanaofuga kisasa katika mikoa mbalimbali. Kwa kuwa amenitaka nijibu kwa mfano sehemu moja tu ambayo Mtanzania au Watanzania wanafanya; ukienda katika Mkoa wa Morogoro utakutana pale na Mfugaji wa kisasa anaitwa Profesa Shemu mwenye ng’ombe zaidi ya 700, ng’ombe wa kisasa wanaozalisha maziwa, huyu ni mmoja wa mfano. Ukienda Wilayani Chato kwa Mheshimiwa…

MWENYEKITI: Inatosha, ahsante.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika ripoti ya hivi karibuni ya Kituo cha Haki za Binadamu na Sheria imeonesha kwamba kuna ongezeko kubwa la unyanyasaji wa wanaume unaofanywa na wanawake hasa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani Tanga na Visiwa vya Unguja na Pemba. Nilikuwa nataka kujua ni lini sasa Serikali itaanza kuzuia ongezeko hili ili kusimama na ile kauli ya Mwenyezi Mungu ya Arrijalu qawwamuna ala-Nnisai.

SPIKA: Hivi hawa wanaume wananyanyaswaje mbona Spika haelewi.

Maswali mengine nashindwa hata kuyaruhusu, labda Mheshimiwa Naibu Waziri unaelewa tafadhali, nasikia wanaume wa Dar es Salaam wanaonewa sana, majibu tafadhali.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Wanaonewaje?

SPIKA: Anataka ufafanuzi wanaonewaje, Mheshimiwa Yussuf.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, katika ile ripoti walisema wanaume wananyanyaswa na wake zao, wanafanyishwa kazi ndani, wanapigwa, wananyimwa haki zao na wengine mpaka wanafikia kulazwa hospitali kwa vipigo wanavyovipata kutoka kwa wanawake.

WABUNGE FULANI: Aaaaa.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, ni ripoti ambayo imetolewa na Kituo cha Haki za Binadamu na Sheria, si ripoti yangu.

SPIKA: Kumbe jambo kubwa hili, inasemekana hata Wanyamwezi wanapata shida hiyo hiyo.

Mheshimiwa Naibu Waziri, yanatakiwa majibu ya uhakika hapa.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yussuf, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunakiri kwamba yapo baadhi ya matukio ya ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa wanaume. Hata hivyo, kwa sasa hatuna takwimu za Mikoa ambayo ameitaja zinazoonesha matukio haya ni makubwa kiasi gani. Kwa hiyo, sisi kama Wizara tutaendelea kufuatilia ili kubaini suala hilo.

Mheshimiwa Spika, pia amegusia ripoti ambayo sisi hatujaiona, nitamwomba Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki cha Bunge basi aweze kutupatia taarifa hiyo ili na sisi tuweze kufuatilia. Niendelee kusisitiza tu kwamba matukio haya ya ukatili wa kijinsia ni makubwa zaidi dhidi ya wanawake na watoto kuliko wanaume.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, wananchi wengi wameathirika kwa kukosa fedha zao ambazo waliziweka katika benki hii na Benki Kuu inapotoa leseni au kibali kwa ajili ya kufungua benki, wao wanakuwa ndiyo dhamana.

Mheshimiwa Spika, na kuna methali inasema dhamana ndiyo mlipaji, lakini hata mahakamani unapomchukulia mtu dhamana, akikimbia wewe ndiyo unakamatwa unahusika na suala lile. Kwa nini Benki Kuu isiwalipe hawa watu fedha zao, halafu wao wakaendelea na huo, kwa sababu watanzania wanaathirika na hili.

Sasa maana ya ninyi kuwa dhamana ni nini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nimesema kwenye majibu yangu ya msingi, uendeshaji wa taasisi za kifedha yakiwemo mabenki imeelezwa wazi kwenye sheria ya mabenki na taasisi za kifedha ya mwaka 2006. Benki Kuu haiwezi kuwa dhamana na kuchukua jukumu la kulipa wateja wote ndiyo maana ikaanzishwa Bodi ya Amana, kama nilivyoeleza, ambayo ina dhamana kubwa ya kuwalipa wateja ambao wanamiliki amana chini ya 1,500,000.

Mheshimiwa Spika, na niseme kwamba, asema wateja wengi wamepoteza, kwa experience tuliyonayo ndani ya Taifa letu, iknapofungiwa benki yoyote au taasisi yoyote ya kifedha, zaidi ya asilimia 90 ya wateja wa benki au taasisi husika ya kifedha, huwa ni wale wenye amana ya 1,500,000 kurudi chini.

Kwa hiyo, hawa asilimia 10 iliyobaki, ndiyo nimesema kwamba, Serikali mbili zimeshakutana, mwezi Aprili, tarehe 5, 2019 na tayari tumeshakubaliana jinsi ya kuliendea jambo hili ili wateja wateja wote sasa waliobaki ambao ni zaidi, waliokuwa na amana ya zaidi ya 1,500,000, waweze kulipwa amana zao.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nashukuru pia majibu ya Waziri kwamba amekiri kwamba Serikali haina Chuo inachotoa haya mafunzo, mafunzo yanayotoa ni ya swimming na snockling mafunzo haya ni muhimu sana kwa maisha ya watu wetu nchi yetu imezungukwa na bahari na maziwa na watanzania wengi wanatumia bahari na maziwa na mito kwa ajili ya kutafuta riziki zao.

Je, Serikali sasa haioni ni muda muafaka wa kuanzisha chuo na kama hawana walimu kutafuta walimu kuja kufundisha ili kuepusha maafa kama haya yaliyotokea Kilindini Kenya mtu amezama kwa siku saba hajatolewa katika bahari?

Swali la pili nchi yetu kama nilivyosema imezungukwa na bahari na mito na watu wetu asilimia kubwa ndiyo wanatumia bahari na mito kwa ajili ya kutafuta riziki zao.

Je, Serikali haioni sasa kwamba ni muda muafaka kutafuta vijana wakawafundisha risk who divers kwa ajili ya uokoaji zinapotokea ajali za baharini? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi ni kweli kwamba kama nchi hatuna chuo maalum kinachofundisha diving peke yake lakini vyuo vyetu vyote vya uvuvi ukianzia Nyegezi, Mbegani, Kunduchi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa wanafunzi wote wanaosoma masomo ya uvuvi au masomo ya sayansi ya majini lazima wasome somo hilo kama sehemu ya masomo ya lazima ya kufaulu na katika jibu langu la msingi nimesema kutokana na uhaba wa wataalamu Serikali ilikwisha chukua hatua ya kupeleka wataalamu watatu nje ya nchi ili wataalam hao watakaporejea waweze sasa kulichukulia somo hilo kama somo muhimu kwa ajili ya kwanza shughuli ya utalii lakini pili kwa ajili ya uokoaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba umefika wakati ambapo suala hili tunalichukulia kwa uzito mkubwa na mara wataalam hawa watakaporejea watatoa mafunzo kwa vijana wetu na kwa watu wote wanaoshughulika na kuongoza watalii.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru katika hifadhi ya Ruaha tatizo sio barabara tu, hata Mto Ruaha mkuu ambao ndio kitovu cha hifadhi ya Ruaha, unatanuka na unakauka kwa baadhi ya vipindi hali ambayo inahatarisha maisha ya wanyama na inahatarisha hifadhi nzima yenyewe kutoweka kabisa. Sasa Serikali inachukua hatua gani kuona kwamba ule mto hautanuki na maji yanaendelea kutitirika katika kipindi cha mwaka mzima ili wanyama wetu waendelee kuhuika katika hifadhi ile?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli historia inaonyesha Mto Ruaha ulikuwa una flow maji yake kwa mwaka mzima na kwa miaka ya hivi karibuni umeendelea kuwa na tabia tofauti kwa maana unapoteza maji katika kipindi cha miezi miwili mpaka mitatu kwa mwaka. Lakini sababu zinafahamika ikiwemo pamoja na matatizo ya taabu ya nchi lakini pia matumizi makubwa yanayofanywa na wakulima walioko kwenye mabonde yaliyoko juu Mto Ruaha.

Mheshimiwa Spika, katika mradi wetu wa REGROW moja ya maeneo ambayo yanaenda kushughuliwa ni pamoja na elimu kubwa itakayotolewa kwa wakulima hao. Lakini miundombinu ambayo itatengezwa ili kuwafanya wanaotumia maji kwa ajili ya kilimo katika maeneo hayo iwe ni miundombinu ya kisasa ambayo itaruhusu flow ya maji kuendelea kuwepo, kuliko hivi sasa hivi wakulima wanazuia maji na kuyaweka kwenye mabwawa ya akiba kwa mwaka mzima hata kama maji hayo hawayatumii. Kwa hiyo, mpango huu kwa ajili mto huo tunao katika mradi wetu mkubwa.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawli ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, ametaja vituo vya Mafia, Dar es Salaam na Tanga ambavyo vinatoa mafunzo ya elimu hii; nilikuwa nataka kujua vinatoa mafunzo kwa kiwango gani? Wanatoka Ma-diving instructor, diver masters au wanafunzi wa kiwango gani wanaotoka katika vituo hivyo vya kufundishia?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; siyo tu kwamba ile mitetemo wanapolipua wale wavuvi inawatisha na inawasumbua wale Ma-divers wanapokuwa chini ya maji lakini pia eneo ambalo limepigwa lile bomu huwa linaathirika sana na kupoteza ule uhalisia wake kiasi kwamba mpaka rangi ya eneo lile huwa inabadilika. Je, Serikali ina mpango wowote wa kufanya utafiti kuona ule uoto wa asili unarudi pale yale Matumbawe yaliyoharibiwa kwa muda wa miaka mingapi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kimsingi kwa mujibu wa swali lake la kwanza, mpaka sasa hatuna vyuo ambavyo vinatoa vyeti maalum lakini tuna vituo ambavyo vinatoa mafunzo kwa ajili ya kusindikiza watalii wanaokuja kwa ajili ya uzamiaji. Katika vyuo vyetu vyote vya Mbegani na wapi hatuna certificate maalum kwa ajili ya divers au snorkel au nini ambayo inatolewa katika maeneo hayo. Wanapata uzoefu kutokana na wale ambao wamekuwa waki-practice kwa muda mrefu kwahiyo vituo hivyo ndiyo nimevitaja katika jibu langu la msingi.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili amesema kuna utafiti gani unafanyika kujua athari zinzaotokana na ulipuzi; ni kweli kwamba milipuko inapolipuka ndani ya maji uharibu kabisa maumbile ya Dunia ndani maji na hasa Matumbawe ambayo ndiyo kivutio kikubwa cha wazamiaji na maeneo yote baharini na kimsingi maeneo haya ambayo yamekuwa ukifanyika uzamiaji yamekuwa ni maeneo yanayolindwa na kwa mfano, ukienda kule Mafia kuna kikosi maalum ambacho kinalinda maeneo hayo na kina patrol maalum. Kwa hiyo, uzoefu wa maeneo hayo kushambuliwa na wazamiaji haupo, kwa hiyo nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika maeneo ambapo tunapeleka watalii kwa ajili ya shughuli hii ni maeneo ambayo yanalindwa na kusimamiwa vizuri na hakuna uwezekano wa matumizi ya mabomu.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba tena ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kuongezea kujibu swali la Mheshimiwa la Mheshimiwa Yussuf kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza vilevile Mvuvi mwenzangu Mheshimiwa Kanyasu kwa majibu yake yale ya awali. Lakini pia nieleze tu kuwa katika chuo Kikuu cha Dar es Saalam katika kozi ya Aquatic Science moja ya jambo la msingi kabisa kwenye kozi ile watu wanafundishwa kitu kinachoitwa swimming and snorkeling.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, swimming and snorkeling mtu anayekwenda kupata shahada ya swimming mathalani mimi mwenyewe hapa ni lazima unafundishwa namna ya kuweza kuogelea na kuweza kuingia kwenye maji kwa muda mrefu na ndipo upate degree yako. Lakini kama haitoshi alivyosema Mheshimiwa Kanyasu kuwa Ndegani wanao utaratibu ambao wanashirikiana hasa na Mamlaka ya Bahari Kuu ambapo wanafundishwa pale kwa muda mfupi nakupewa udhoefu. Wataalam wetu ambao wanakwenda kuwa observer’s watazamaji katika meli hawa pia wanafundishwa namna hata ya ku-dive.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili la Matumbawe ni conservation, Matumbawe yanachukua si pungufu ya miaka 50 hadi 100 yale ambayo yamevunjwa na mabomu, kwa hivyo kitu pekee ambacho sisi wataalam wa Sayansi ya Majini tunachokifanya ni kuhakikisha kuwa maeneo yaliyoharibiwa namna hiyo yanakwenda kuhifadhiwa tumefanya jitihada kubwa kwa kupitia mradi wetu mkubwa unaitwa sea offish ukanda wa Pwani ambapo kuanzia Tanga kule MOA mpaka Mtwara maeneo ya Mtwara mwishoni kule tumekuwa na huo mradi ambao tunadhibiti na kuyalinda maeneo yetu ya miamba na tumeonesha mafanikio makubwa sana katika Wilaya ya Kilwa, hivi sasa hata mazao yanayopatikana katika miamba ile kwa maana ya Matumbawe yameongezeka kwa kiasi kikubwa sana.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Adhabu ya kaburi aijuaye maiti. Sisi tunaosafiri na Azam ndiyo tunafahamu adha yake.

Mheshimiwa Spika, hata ukisafiri na ile charter ya abiria 11 mzigo wa kilo 15 - 20 hulipishwi lakini ndani ya boti ya Azam unalipishwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri achukue mfuko mmoja wa mchele tuliogawiwa asafiri nao aone kama hatalipishwa. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ifuatilie suala hili na itupatie ufumbuzi.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, suala la huduma ya safari za majini mara nyingi ni kati ya abiria na mwenye mali. Ukifugua nyuma ya tiketi ile kuna masharti ambayo yanaandikwa kwa uwazi na kwa lugha nyepesi kabisa. Ninawashauri sana Watanzania tuwe tunasoma masharti yale ili kama ukiona hayakidhi mahitaji yako basi usiende. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nyuma tiketi ya Azam kuna maelezo yanayoeleza mpaka kiwango cha mzigo unachotakiwa kwenda nacho ndani ya meli. Sasa anayepima ni yule mwenye meli kama imezidi anaruhusiwa kukukatalia kwa sababu ndiyo mkataba ulioingia wewe abiria na yule mwenye meli. Kwa hiyo, nawashauri Watanzania tuwe tunasoma vigezo na masharti vya kuingia kwenye huduma hizo.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya kitaalamu ambayo ameyatoa na mimi kwa uhaba wangu wa elimu naweza nikayagawanya au nikayafanyia summary majibu yake katika mambo matatu kwamba mikoko ina faida ya kiuchumi, kijamii na kimazingira. Ameshaeleza umuhimu wake, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, pamoja na hizo faida za kiuchumi na kijamii zilizopo, je, jamii inayozungukwa na miti hiyo inapewa elimu ya kutosha juu ya umuhimu, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ametaja faida za kimazingira kwamba kuhifadhi udongo, upepo, bionuai na kuhifadhi sumu. Je, ni kipi kipaumbele cha Serikali katika uhifadhi huo wa kimazingira ambacho wamekifanyia kazi hadi sasa? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipokee shukrani zake lakini pia nimpongeze amekuwa mdau mzuri sana wa mazingira tangu tumeanza na tunashirikiana pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kuhusu kutoa elimu, ni kweli na sisi tunaendelea kutoa elimu na hili ni jukumu letu kama Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) na ili tuweze kufanikiwa jambo lolote katika utekelezaji wake elimu tumeipa kipaumbele. Hata hivyo, kipaumbele kikubwa ni mazingira na kwenye majibu yangu ya msingi nimeeleza namna ambavyo mikoko inavyotusaidia katika kuhifadhi kingo za maeneo ya Pwani hasa tunapokuwa na miradi ya mabadiliko ya tabia nchi katika kujenga zile kuta kwenye kingo tunatumia fursa hiyo hiyo katika mradi huo huo kuhakikisha tunapanda miti ya mikoko kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kutunza mazingira. Kwa hiyo, kipaumbele chetu ni kuhifadhi mazingira. Ahsante.