Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mohamed Juma Khatib (2 total)

MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB aliuliza:-
Kumezuka wimbi kubwa sana lenye kutisha la ajali za bodaboda nchini kiasi cha kufanya hospitali zetu kupungukiwa na uwezo wa kuwahudumia waathirika wote wa ajali hizo.
(a) Je, Serikali inaweza kulieleza Taifa sababu za kutokea kwa wingi kwa ajali hizo?
(b) Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na utitiri wa ajali hizo bila kuathiri ajira hiyo ya bodaboda?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Mohammed Juma Khatib, Mbunge wa Chonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pikipiki za matairi mawili (Bodaboda) na za matatu (Bajaj) zilianza kutumika kubeba abiria mwaka 2008 Tanzania Bara na mwaka 2009 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliridhia vyombo hivyo vitumike kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria. Sababu kubwa za kutokea kwa ajali zinazohusisha bodaboda na bajaj ni uzembe wa baadhi ya waendesha pikipiki na bajaji kutokufuata Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimekuwa nikijibu hapa Bungeni, Serikali inatambua biashara hiyo inayofanywa na pikipiki za kubeba abiria na inathamini mchango huo katika kutoa ajira katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na ajali nyingi zinazosababishwa na bodaboda, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikichukua hatua dhidi ya waendesha pikipiki ambao hawazingatii Sheria ya Usalama Barabarani na kanuni zake pamoja na masharti ya leseni za usafirishaji. Aidha, Jeshi la Polisi limekuwa likitoa mafunzo kwa waendesha bodaboda juu ya matumizi bora ya barabara.
MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB aliuliza:-

Je, ni katika mazingira gani Askari Polisi anapaswa au hulazimika kumtesa Mtuhumiwa wa makosa mbalimbali wakati akiwa mikononi mwake au kwenye Kituo cha Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohammed Juma Khatibu, Mbunge wa Chonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, kifungu cha 11 kinaelekeza namna ya ukamataji. Aidha, kifungu hiki mahsusi cha ukamataji, hakimruhusu askari kumpiga au kumtesa mtuhumiwa wa makosa mbalimbali wakati akiwa mikononi mwa Polisi au kwenye Kituo cha Polisi.

Mheshimiwa Spika, Kanuni za Kudumu za Utendaji wa Jeshi Polisi la (PGO) zinakataza na kuelekeza utendaji mzuri wa Askari Polisi, ambapo askari yeyote atakapobainika kufanya vitendo vya kumpiga au kumtesa mtuhumiwa huchukuliwa hatua za kunidhamu ikiwepo kufukuzwa kazi na au kufikishwa Mahakamani.