Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Oliver Daniel Semuguruka (73 total)

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya kiafya yanayoikabili Wilaya ya Busokelo yanafanana na Wilaya ya Karagwe, haina Hospitali ya Wilaya, inayo Hospitali Teule ya Nyakahanga inayotoa huduma za tiba kwa Wilaya mbili, Karagwe na Kyerwa. Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya ili kuboresha huduma za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Karagwe hawana hospitali, lakini naomba niwapongeze kwamba wanafanya juhudi kubwa na ndiyo maana pale tumempeleka kijana mmoja anaitwa Dkt. Sobo, daktari mzuri sana wa upasuaji kama DMO. Ni kweli changamoto hizi, ninapata taarifa kutoka kule kila siku kwamba hakuna Hospitali ya Wilaya. Maeneo haya ni miongoni mwa maeneo tuyoyawekea kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tunajua kwamba kule mnatengeneza kikosi kazi cha kuweza kuhudumia maeneo yale, naomba katika bajeti ya mwaka unaokuja sasa wekeni kipaumbele chenu ili tuhakikishe sasa Karagwe badala ya kutumia hospitali ya DDH, tutumie Hospitali zetu za Wilaya kwa kuhakikisha kwamba tunaweka nguvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba, ikiwezekana kama kuna kituo cha afya ambacho mnatumia pale kipewe nguvu ili baadaye kipandishwe kuwa hata Hospitali ya Wilaya kwa kuanzia linaweza likawa jambo jema. Lakini naomba nikwambie kwamba, Serikali itaunga mkono juhudi zote za wana-Karagwe na watu wa Mkoa wa Kagera.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lililoulizwa Na. 278, linafanana na barabara ya Mzani – Nyakahula – Mrusagamba – Mrugalama iliyopo Wilaya ya Ngara, Kagera. Pia kuna barabara ya Karagwe kupitia pori la Kimisi, Tubenako Ngara ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi zitajengwa. Je, ni lini Serikali itakamilisha barabara hizo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu awali, dhamira yetu ni kutekeleza ahadi zote ambazo viongozi wetu walizitoa katika nyakati mbalimbali, kuanzia awamu ya nne na awamu ya tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Oliva kwamba barabara hizo alizoziongelea, maadam zilitolewa ahadi, nasi tutazichukua ili tuweze kuzishughulikia kwa namna ambavyo uwezo wa kifedha utakavyokuwa unatujaalia.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa sababu kubwa ya ukosefu wa elimu kwa wakulima ni uchache wa Maafisa Ugani. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Maafisa Ugani kwa kila kijiji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa wakulima wa kahawa hupeleka kahawa zao nchi jirani kufuata bei nzuri. Je, Serikali ina mpango gani kuongeza bei ya kahawa ili wananchi hawa wasipeleke nchi jirani?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyojibu katika swali la msingi kwamba tuna upungufu wa Maafisa Ugani 6,022, hii ni idadi kubwa. Vilevile kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba Serikali inasomesha Maafisa Ugani hawa zaidi sasa katika vyuo vyetu ili kukabiliana na huu uhaba ambao upo na vibali vya kuwaajiri vinaendelea kutolewa. Kwa hivyo, hivyo hivyo tunakwenda kukabiliana na huo upungufu na nina uhakika baada ya miaka michache ijayo kama nia ilivyo ya Serikali na Mheshimiwa Mbunge, kila kijiji kitakuwa na Maafisa Ugani wanaotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kahawa kuruhusiwa kuuzwa nje ya nchi, nikijibu swali lililotangulia nimesema kwamba kahawa hatutakubali iende nje kwa sababu tunavyo viwanda vya kuhudumiwa hapa hapa nchini. Hii kahawa bei yake itakuwa nzuri tukiondokana na msururu wa kodi hizo ndogo ndogo zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la kahawa leo tunapozungumza hapa lina kodi 26, ni kodi nyingi sana na ndiyo maana tunafanya sasa uchambuzi ndani ya Serikali ili kuona hizo kodi ambazo kwa kweli zinastahili kuondolewa, ziondolewe ili kuwapa wakulima unafuu. Kwa sababu kodi zikitozwa wanunuzi hawalipi wao, zinahamishiwa kwa muuzaji wa kahawa ambaye ni mkulima. Kwa hivyo, tukizipunguza hata kwa wanunuzi na watu wengine, mwisho wa siku atakayenufaika ni mkulima kwa sababu kodi hizo zitakuwa zimepungua na bei ya kahawa zitakuwa zimepanda.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa zana ya D by D inaonekana bado haieleweki hata kwa sisi Wabunge; je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ikiwemo sisi Wabunge na Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hii dhana imekuwa ni dhana ngeni, japo imeanza muda mrefu; lakini hata ukifanya rejea, wakati mijadala yetu katika bajeti mbalimbali za sekta unaona kwamba hata Waheshimiwa Wabunge, ile concept nzima ya D by D bado haijakaa vizuri. Leo hii tulivyokuwa tukijadili katika Wizara ya Elimu, tulivyokuwa tukijadili katika Wizara ya Afya, ukiangalia michango ya Wajumbe wengi sana dhana ya D by D haijakaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndiyo maana hata katika kikao chetu tulivyokuwa tukifanya na Wizara ya Afya, Wataalam na sisi Viongozi Wakuu tulivyokuwa tukibadilishana mawazo tukasema ni vyema sasa dhana hii kwanza ikiwezekana iingie hata kwa watu walioajiriwa wa Serikali, wajue falsafa halisi ya dhana ya D by D. Maana yake katika Mpango huu imetupa changamoto pana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tutaangalia jinsi gani tutafanya ili mradi hata Wabunge na Waheshimiwa Madiwani wote kwa pamoja na Watumishi wote wa Serikali wajue nini concept ya D by D? Nini maana ya dhana ya kurudisha madaraka kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hoja yake ni ya msingi, nadhani tutaifanyia kazi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba uelewa siyo mzuri sana kwenye dhana hii ya ugatuaji wa madaraka, nami napendekeza tu kwa sababu dhana hii ina maudhui makubwa sana katika msingi wa utawala wa nchi yetu. Inapokuwa haieleweki, inasababisha hata mijadala wakati mwingine kutoka nje ya context na pengine siyo kawaida kuonekana pengine mjadala huo anayetoa kwenye context ni mtu ambaye ana nafasi kubwa na kwamba jambo hili lipo kikatiba sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napendekeza na pengine naomba kwa kupitia swali hili tuone utaratibu kwa sisi Serikali na Bunge; namna ya kufanya kwanza semina hata kwa Wabunge wote kabisa kwenye jambo hili. Mfanye semina na ikibidi kile Chuo chetu cha Uongozi ndiyo kije kituwezeshe katika jambo hili na kama tuna Wataalam ndani ya Serikali tunaweza tukatoa Watalaam, lakini kama kuna wataalam ndani ya Bunge, tutoe. Kwa sababu jambo hili kwa mimi ambaye ni mwanataaluma wa eneo hilo, napata nalo shida sana. Kusema ukweli context imepotea kabisa kwa sababu watu wanatafuta hata kwa upungufu fulani wanafikiri solution ni ku-centralize tena badala ya ku-decentralize. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani tuone namna bora ya kuweza kufanya semina kubwa nzuri ya watu kupata uelewa juu ya jambo hili.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Tatizo la barabara ya Kidatu na Ifakara linafanana na barabara ya junction ya kuelekea Rusumo almaarufu kama zero-zero kupitia barabara ya Nyakahula - Rusahunga mpaka Nyakanazi. Hiyo barabara imekuwa ikifanyiwa ukarabati mara kwa mara lakini bado inaharibika kwa muda mfupi sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya matengenezo makubwa katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hiyo anayoongelea hivi sasa tunavyoongea ina mkandarasi anayefanya matengenezo. Ni kweli hoja anayoongelea kwamba, kunakuwa na matengenezo ya mara kwa mara na hii inatokana na matumizi makubwa sana ya malori makubwa yanayopita katika barabara hiyo na naamini matengenezo ya sasa yamezingatia ukubwa wa matumizi ya barabara hiyo na hivyo matengenezo yake sasa yatakuwa ya muda mrefu tofauti na huko nyuma.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Jeshi la Polisi lina uhaba wa vitendea kazi vya kisasa kuweza kudhibiti matukio ya uhalifu; je, Serikali ina mpango gani kutoa vifaa vya kisasa zaidi kwa askari wetu waliopo katika maeneo ya mipakani?
Swali langu la pili; ili askari aweze kufanya kazi zake na kudhibiti matukio ya uhalifu kwa ufanisi ni muhimu akawa na mazingira rafiki kuanzia nyumbani.
Je, ni lini Serikali itatekeleza kwa vitendo ahadi ya kujenga makazi ya hadhi ya askari wa Jeshi la Polisi katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa na concern ya hali ya usalama katika mpaka wa Kagera, lakini naomba tu nimthibitishie kwamba, si Jeshi la Polisi ama Serikali kupitia Jeshi la Polisi kwa kutambua umuhimu na unyeti wa maeneo ya nchi yetu yaliyoko mipakani ikiwemo Kagera huwa kwa kawaida inatoa kipaumbele katika ugawaji wa vifaa katika maeneo hayo hususan vitendea kazi ikiwemo silaha, magari na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni kwamba, kwa Mkoa wa Kagera pekee tunahakikisha kwamba tunawapatia Askari wetu walioko mipakani silaha za kutosha lakini silaha nzito ili kuweza kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu ambao mara nyingi wamekuwa wakisababisha ukosefu wa amani katika mikoa yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hakuna hata Kituo kimoja cha Polisi katika mipaka ya nchi yetu ambacho hakina gari mpaka sasa hivi tunavyozungumza. Kwa hiyo, ni kuonesha kwamba tunatoa nguvu kubwa sana na kipaumbele katika maeneo ambayo yapo mpakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili ni kweli kuna matatizo ya makazi, sio tu Kagera lakini katika mikoa mbalimbali nchi nzima na ndiyo maana tumekuwa tukizungumza hapa kuna mipango ya Serikali ya ujenzi nyumba 4,136 ambayo mpaka sasa hivi tunasubiri approval kutoka Hazina ili mradi ule uanze kutekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kagera, kuna ujenzi wa nyumba 12 ambazo tunaendelea nazo hatua kwa hatua kadri ya pesa zitakazopatikana tumalize katika eneo la Buyekera ambalo litasaidia kupunguza makali ya matatizo ya makazi kwa askari wetu.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana
kwa kuniona. Matatizo yaliyopo ya usikivu wa simu Jimbo la Nanyumbu ni sawa
na yaliyopo Wilaya ya Ngara katika Kata ya Mganza, Nyakisasa, Keza, Kabanga
na Rusumo, ambayo yanaingiliana na nchi jirani za Rwanda na Burundi. Je,
Serikali ina mpango gani wa kuboresha usikivu wa simu katika Kata hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa
Naibu Spika, nimemsikia na vilevile nilimsikia Mbunge wa Jimbo ameeleza kwa
muda mrefu sana matatizo ya Jimbo hilo. Namwona pale nimhakikishie na
nimhakikishie Mheshimiwa Semuguruka kwamba, upacha wao ni lazima uzae matunda katika miaka hii mitano na tutafuatilia maeneo hayo ili hatimaye
mawasiliano yapatikane ya uhakika.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa sasa MSD ina Bohari Kikanda. Je, Serikali ina mpango gani wa kufungua Bohari ya MSD kila Mkoa ili kurahisisha usambazaji wa madawa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Serikali imejiandaaje kudhibiti upotevu, wizi wa dawa kwa watumishi wasio waaminifu katika zahanati na vituo vya afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza kuhusu Serikali kujenga bohari za dawa kila mkoa; kwamba tuna mpango gani; kwa sasa hatujawa na mpango wa kufanya hivyo kwa sababu tunaamini utaratibu wa kuwa na bohari kwenye kila kanda bado haujakwama. Ni kwamba tunahitaji kufanya maboresho kidogo tu ili tuweze kuongeza tija na ufanisi kwenye kuhakikisha vituo vya umma vinapata dawa kadri ambavyo vinahitaji na kwa haraka kadri ambavyo inawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mfumo wetu wa sasa hivi wa Supply Chain Management, tunaamini bado haujakwama na ndiyo maana tumeendelea kuuboresha. Tulikuwa na changamoto kidogo za kifedha, ambazo kama ambavyo sisi Wabunge ni mashahidi na naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa azma yake thabiti ya kuongeza upatikanaji wa dawa kwa kutuongezea bajeti kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, changamoto ya kifedha tuliyokuwanayo ambayo ilikuwa inashusha tija na ufanisi, sasa inaelekea kuondoka na mfumo wa upatikanaji wa dawa umeimarika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu udhibiti, naomba nitumie Bunge lako Tukufu kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote, Madiwani wote na Viongozi wote kuanzia Viongozi wa Mikoa na Wilaya washiriki kikamilifu katika kusimamia udhibiti wa mfumo wa upatikanaji wa dawa kwenye vituo vyetu kwa sababu, jambo hili haliwezi kuwa ni la sisi tu tuliopo Fungu 52, kwa maana ya Wizara ya Afya pekee. Kwa sababu, mfumo wetu wa udhibiti upo, kwamba kwenye kila zahanati, kila Kituo cha Afya na kwenye kila hospitali, kuna Kamati ya Udhibiti wa Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi ambapo ndani yake kuna viongozi wa kuchaguliwa na kuna watendaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba, mfumo huu hausimamiwi ipasavyo. Kama ungefanya kazi ipasavyo, kwa hakika, tungeweza kudhibiti wizi na ubadhirifu wa madawa ambao umekuwa ukitokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, kama kuna mtu ana taarifa yoyote ile ya mahali ambapo kuna wizi ama upotevu wa dawa ambao umejitokeza, atupe taarifa na sisi tutachukua hatua haraka.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona niulize swali ndogo la nyongeza. Matatizo ya usikivu wa simu yaliyopo Mpanda vijijini ni sawa na yaliyopo Wilaya ya Ngara kata Muganza, Nyakisasa Keza, Kabanga na Rusumo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha usikivu wa simu katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Serikali ina nia ya dhati kabisa yakufikisha mawasiliano kila sehemu na hasa, eneo hili analoliongelea ni maeneo ya mpakani na maeneo ya mpakani tuna utaratibu maalum wa kuhakikisha kwamba mawasiliano yanafika haraka katika maeneo hayo. Kwa hiyo Serikali itahakikisha inafikisha mawasiliano mara fedha zitakapozipata.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Tatizo la maji lililoko Mkoa wa Pwani linafanana kabisa na tatizo la maji lililopo Jimbo la Ngara ambapo tunapata maji kwa wiki mara moja au mara mbili. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hili la maji katika Wilaya ya Ngara?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Wizara yangu inatafuta mkandarasi mshauri ambaye ataanza kufanya design ya kutumia maji ya Mto Rubuvu kupeleka Ngara kwa sababu yale maji ni mengi kwa hiyo yatasambaa maeneo mengi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikwambie tu kwamba Serikali, Wizara yangu haijalala tayari inaangalia maeneo yote na kutumia vyanzo vilivyopo kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata maji safi na salama.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona niulize swali dogo la nyongeza. Matatizo yaliyopo Iramba Mashariki yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo Wilaya ya Ngara. Vijiji vingi vya Wilaya ya Ngara, hasa Tarafa ya Lulenge, havina umeme. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane nawe kuwapongeza Wabunge Viti Maalum na Wabunge wote ambao kwa kweli Bunge zima hili leo ni ushuhuda kwamba, limekuwa likifuatilia miradi ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Oliver kwa swali lake zuri ameuliza kwamba, Vijiji vya Wilaya ya Ngara ni lini vitapatiwa nishati ya umeme. Nataka nimjibu kwamba, kama ambavyo tumekuwa tukitoa taarifa ndani ya Bunge lako na si taarifa tu kwamba labda ni porojo ni kweli, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli inatekeleza huu mradi kabambe wa kupeleka umeme katika vijiji vilivyosalia 7,873.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe pia ni shahidi. Jana wakati tunahitimisha taarifa ya Kamati yetu ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Waziri wangu wa Nishati alitoa taarifa kuwashwa kwa umeme katika vijiji 24 katika utaratibu huu wa REA awamu ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wilaya ya Ngara Mkandarasi yupo anafanya kazi. Ameanza zile kazi za awali za upembuzi na kadhalika lakini kwa sasa Wakandarasi wote nchi nzima wana-mobilise vifaa na wengine wako site wanaendelea na kazi mbalimbali. Nataka nilitibitishie Bunge, ile awamu ya kwanza ambavyo ni vijiji 3,559 tumesema mpaka Juni, 2019 viwe vimekamilika halafu tunaanza safari nyingine ya kumalizia vijiji vingine. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina masawali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Kabanga Nickel una mda mrefu sana, kama nilivyouliza kwenye swali langu la msingi, tangu mwaka 1970 na wachimbaji walianza tangu mwaka 1973. Wananchi wa Ngara tulikuwa tukiona ndege za wazungu zikija na kuondoka wakidai kwamba wanapeleka sample na hawarudi tena, isije ikawa kama makinikia. Je, huu mgodi wa Kabanga Nickel utaanza lini rasmi ili wananchi wa Ngara na Serikali kwa ujumla tuweze kunufaika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Sheria na mauziano ya Makampuni inataka mnunuzi na muuzaji kulipa kodi ya Serikali. Mgodi wa Kabanga Nickel umekwisha kubadilisha wamiliki zaidi ya wanne. Je, Serikali Kuu na Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Ngara imenufaika vipi na huo umiliki wa kubadilisha wamiliki kila mara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Semguruka kwa jinsi anavyofuatilia maslahi ya wananchi wa Mkoa wa Kagera pamoja na wananchi wa Ngara kwa ujumla wake. Nampongeza pia anavyoshirikiana na Waheshimiwa Wabunge wengine majirani wa Biharamulo, Ngara na wengine, hongera sana Mheshimiwa Semuguruka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na swali la kwanza. Ni kweli kabisa huu mradi umeanza tangu mwaka 2009, kwa kweli si miaka ya 1970 iliyopita. Hata hivyo niseme tu kwamba kazi inayofanyika sasa hivi ni kukamilisha upembuzi yakinifu, na natarajia kufungua mgodi mara tu baada ya bei ya nickel kuimarika. Hata hivyo tumempa muda wa mwaka asipofanya hivyo eneo hilo tutalichukua tutawamilikisha wawekezaji wengine wenye nia na uwezo wa kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, manufaa yatakayopatikana mgodi huo ukifunguliwa ni pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wengi wa Bugarama na Kanyenyi, kadhalika watalipa mafao ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na uhamishaji, Sheria za Kodi zinamtaka mmiliki yeyote akihamisha au kuuza hisa au leseni yake anatakiwa kulipa capital gain ya asilimia 10 na kwa upande wa Sheria ya Madini kifungu cha 9(1) cha mwaka 2010 kinataka mmiliki akianza kuhamisha analipa dola 3,000. Kwa hiyo, atakapofika hatua hiyo Mheshimiwa Semuguruka haya mafao ya Serikali yataingia. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Nina swali dogo la nyongeza. Kwa nini Serikali isiwezeshe lishe kwa kaya duni ambazo zinatumia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hatuna mpango wa kuwezesha chakula kwenye kaya duni au kaya yoyote ile. Tunaamini wagonjwa na watu wengine wanapaswa kuhudumiwa na familia zao. Hata hivyo, tunatoa dawa ama kemikali ambazo zina nutritive effect, zina effect ya kuongeza lishe kwenye miili ya wagonjwa wanaotumia dawa hizi. Kwa hiyo, tunawapo multivitamins na dawa nyingine inatosheleza kwa kweli kuhimili mikikimikiki ya ART.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona niulize swali dogo la nyongeza. Tatizo la maji lililoko Kibamba linafanana kabisa na tatizo la maji lililoko Wilaya ya Ngara hasa Kata ya Mbuba, ambayo ina shule za sekondari mbili wanafunzi wanatembea kilomita mbili kwenda kufuata maji mabondeni na husababisha wanafunzi kukatisha masomo yao kwa kupata mimba na ukizingatia tamko la jana la Mheshimiwa Rais. Je, Serikali ina mpanga gani wa kumaliza tatizo hili, hasa katika Kata hii ili kunusuru ndoto za wadogo zetu, au watoto wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba katika hizo shule mbili kiko kisima pale Ngara Mjini ambacho pampu yake ilikuwa imeharibika, tayari Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hilo amefanya juhudi, mashine imepatikana. Wizara ya Maji na umwagiliaji tunampelekea fedha ili akaongeze mashine nyingine na kumpa fedha kwa ajili ya kutandika mabomba kutoka kwenye hicho chanzo ili shule zote mbili hizo ziweze kupata maji, tuondoe usumbufu wa watu kutembea mwendo mrefu na kupata hayo madhara ambayo unayazungumza.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niulize swali dogo la nyongeza. Swali lililoulizwa namba 167 linafanana kabisa na Wilaya ya Ngara. Wilaya ya Ngara haina jengo la Mahakama, inatumia jengo la DC.
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya Ngara? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ngara imepangiwa kujengewa Mahakama ya Wilaya katika mwaka wa 2019/2020 na pia Mahakama ya Mwanzo Lulenge mwaka 2019/2020. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri; ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na taarifa za viwanda tunazozisoma na kuzisikiliza kila siku, kwa jibu ni kuwa Kagera bado tuko nyuma katika viwanda. Sasa nini mpango wa Wizara yako kushirikiana na mimi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kagera kuhamasisha ujenzi wa viwanda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wananchi wa Kagera wajasiriamali wadogo wadogo ili waweze kupata mikopo ya riba nafuu ili waweze kufungua viwanda?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada za uhamasishaji zinaendelea, shughuli zinazofanywa na Wizara ya Mifugo za kuondoa uvuvi haramu zinalenga kuona kwamba katika ziwa letu tunapata samaki wa kutosha ili viwanda vya samaki viweze kujengwa. Lakini yako makampuni ambayo tumeshawasiliana nayo, kiwanda cha kutengeneza maziwa kitajengwa Kagera. Pia kampuni moja kutoka Uganda ya Uvan inataka kujenga kiwanda cha vanilla. Suala la uhamasishaji ni endelevu.
Nipende kukuahidi wewe na Wabunge wenzangu na wananchi katika Mikoa ambayo nataka kufanya kazi nayo ya uhamasishaji ni pamoja na Kagera, Kigoma, Mara, Katavi na Ruvuma. Katika miezi minne ijayo tutafanya kampeni kubwa…
…ya mazao ya shamba ambayo tunataka kuyaimiza yaweze kuzalisha bidhaa za viwandani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuwawezesha wananchi akina mama na akina dada kifedha…

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba tunao mfuko wa NADef. Jambo la muhimu si pesa, jambo la muhimu ni kwenda kupata idea na kupata mawazo SIDO. Mkishapata mawazo kupitia SIDO mtanufaika na mfuko wa NADef lakini iko mifuko mingine ambayo iko chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nitakapozindua kitabu cha mwongozo wa kujenga viwanda kwa local government katika bajeti yangu siku ya Alhamisi kitabu hicho kitagawiwa mtaweza kujua pesa zinapatikana wapi.( Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Ujenzi wa Kituo cha Polisi Keza, Wilaya ya Ngara, kilichojengwa kwa nguvu za wananchi, kitakamilika lini maana kina zaidi ya miaka saba kimeezekwa bado finishing. Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Keza nacho ni miongoni mwa vituo ambavyo havijakamilika. Bahati njema ni kwamba mwaka huu wa fedha katika Mkoa wa Kagera tumetenga takribani bilioni 1.56 kwa ajili ya kumaliza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo haijakamilika, ikiwemo nyumba pamoja na vituo vya Polisi. Hiyo inaonesha azma ya Serikali ya kuweza kukabiliana na changamoto ya kumaliza vituo hivi ambavyo havijakamilika pamoja na nyumba za Askari nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ipo na pale ambapo hali ya kifedha itakaa vizuri basi tutakamilisha kituo hicho pamoja na vituo vingine ambavyo kama alivyosema mwanzo kwamba viko sehemu mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Oliver Semuguruka amesema, ni kweli tuna vituo vingi ambavyo vimeshafikia hatua hiyo, niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wamechangia kwa kiwango kikubwa sana. Kwa sababu ni wengi tu siwezi kuwataja wote, lakini natambua Mheshimiwa Maige, Mheshimiwa Ritta Kabati, Mheshimiwa Oran Njeza na wengine wengi ambao mmechangia ujenzi wa vituo hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo kilichoulizwa, Mheshimiwa Ulega hapa ndiye aliyekianzisha, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wameongelea sana masuala haya ya vituo ambavyo vimeshafikia hatua ya kukamilishwa pamoja na nyumba za vijana wetu ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi, kwa sababu bado tuko hapa na bajeti tumeshapitisha, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wanipenyezee maeneo ambayo yana vituo hivyo ili tunavyomaliza Bunge twende tukae ngazi ya Wizara tuweze kuweka vipaumbele ili tusiharibu nguvu kazi za wananchi ambazo zimeshafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Joseph Selasini ameliongelea sana jambo hili, leteni hivyo vituo ili tutakapokwenda kukaa kwenye ofisi tuweze kuona kile tulichonacho na kuweza kumalizia vile ambavyo vimeshafikia hatua za kumaliziwa. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Swali namba 19 lililoulizwa linafanana kabisa na changamoto iliyopo Jimbo la Ngara. Hivi juzi tulishuhudia gari zikiungua border ya Rusumo na ikapelekea kifo cha dereva, hakukuwa na gari la zimamoto. Je, ni lini Serikali itatuletea gari la zimamoto Wilaya ya Ngara?
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Oliver kutokana na kuumwa kwake na maendeleo ya vyombo ama taasisi zetu zilizopo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mkoa wa Kagera ikiwemo Jeshi la Zimamoto. Kuhusiana na Wilaya ya Ngara, ukiachilia mbali mikakati ambayo nimeizungumzia nikijibu swali la msingi la Mheshimiwa Aisharose Matembe ambalo linagusa Wilaya zote nchini, mikakati ni ile ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuna pia tuna mipango mingine mbalimbali ambayo tunaendelea nayo, ambayo tunaamini kabisa ikikaa sawa basi changamoto hii ya upungufu wa magari ya zimamoto itapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mpango wa kuweza kupata mkopo kupitia nchi za Belgium na Australia ambayo itatuwezesha kupata vitendea kazi ikiwa ni pamoja na magari mapya kabisa. Michakato ya kupata mikopo hiyo nayo inakwenda vizuri na iko katika hatua nzuri pale ambapo itakapokuwa imekamilika naamini kabisa tukichanganya na mikakati niliyozungumza katika swali la msingi basi matatizo ya magari ya zimamoto na vitendea kazi nchini ikiwemo Ngara yatakuwa yamepungua kwa kiasi kikubwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Tatizo lililopo Mtwara linafanana kabisa na tatizo lililopo Mkoa wa Kagera. Umeme ukatika mara kwa mara hasa Bukoba Mjini, Bukoba Vijijini, Muleba, Missenyi na Karagwe. Je, ni lini tatizo hili la kukatika umeme litakwisha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Oliver naye ameuliza ni lini Mkoa wa Kagera suala la kukatika kwa umeme litapungua kama siyo kumalizika kabisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli tunatambua Mkoa wa Kagera ambao kwanza wanapata umeme kutokea Uganda, tunanunua kama megawati 10 kutoka Uganda ambazo tunazisambaza katika maeneo yale, lakini Serikali pia kwa kuliona hilo, ndiyo maana sasa imejitahidi kuunganisha Wilaya za Ngara na Biharamulo kwenye Gridi ya Taifa. Mkakati huo unaendelea na pia tuna mpango wa kujenga transmission line ili umeme ambao utazalishwa katika maeneo ya Rusumo ambao tumeingiza megawati 80 tuweze kusambaza katika maeneo ya Mkoa wa Kagera na kuweza kutatua tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Mbunge na ninampongeza kwa ufuatiaji wake na Wabunge wote wa Viti Maalum ambao wanafuatilia sekta ya nishati, nawashukuru sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kuchelewa kwa kesi hizi ni vidhibiti kutopelekwa maabara kwa Mkemia Mkuu haraka ili kuthibitisha. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa marekebisho ya sheria yaliyofanyika mwaka 2017, hivi sasa Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Kifungu cha 4(n) ambacho kimeongezewa baada ya marekebisho kimeweka utaratibu wa kwamba hivi sasa kwa kuzingatia kwamba kuna mashauri mengi ambayo yanasimama kwa kusubiri vidhibiti kutoka katika Ofisi ya Mkemia Mkuu, sasa kupitia sheria hii imeanzishwa laboratory katika Ofisi ya Kamishna Jenerali ili kuhakikisha kwamba mamlaka pia nayo iwe na wajibu huo wa kuchunguza na kutoa taarifa ili kujaribu kusaidia expedite kesi hizi zisichukue muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwondolee hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ilichukua hatua kwa marekebisho hayo ya sheria na hivi sasa ukiacha Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Jeshi la Polisi lakini... kazi hiyo pia.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Changamoto iliyopo Njombe inafanana kabisa na changamoto iliyopo uwanja wa ndege wa Bukoba kwamba ni mfupi na kupelekea ndege kutua kwa shida au kuruka kwa shida mfano kama Bombadier. Je, ni lini Serikali itaongeza urefu wa uwanja huo?
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS JOHN KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie uwanja wa ndege wa Bukoba, yako maboresho muhimu yamefanyika na huduma inaendelea vizuri na ndege zinashuka vizuri na miruko imeongezeka. Pia ule mpango wa kuuboresha uwanja huu tunaendelea na hatua ya kutathmini maeneo ambayo tutahamisha wananchi, Mheshimiwa Mbunge anafahamu ili sasa ule urefu wa sehemu ya kurukia na kutoa ndege iweze kuongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba zile hatua za kufanya maboresho ya viwanja mbalimbali nchini ziko kwenye mpango na Waheshimiwa Wabunge wanafahamu, mara kadhaa tumezungumza namna ya viwanja, hata leo nimerejea kuzungumza viwanja vingi ambavyo tunaendelea kujenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuimarisha ili kuhakikisha kwamba tuna viwanja wa ndege ambavyo vitamudu kutoa huduma katika maeneo ya Mikoa yote. Tutaendelea kutoa maeneo mengine ambayo ni maalumu kama ilivyoonekana kwamba uwanja wa ndege wa Mafia, kama nilivyozungumza jana, tunaupeleka katika hatua uwe na hadhi ya kimkoa ili huduma ziongezeke.

Mheshimiwa Naibu Spika, viko viwanja vingine ambavyo tunaendelea kuvipanua. Kwa mfano, tunaendela kupanua uwanja wa ndege wa Kigoma, Tabora, Shinyanga na Bariadi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge waamini tumejipanga kuhakikisha kwamba pamoja na Serikali kuendelea kuliboresha shirika letu kwa kununua ndege, italeta maana pale ambapo Serikali inanunua ndege na ndege zinaenda kuwahudumia Watanzania kwa ujumla. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, wananchi wamesubiria fidia kwa muda mrefu sana na kabla ya ujenzi wa lami, fidia huwa inatangulia. Sasa Serikali inawaambiaje wananchi wangu wanaoishi kwenye hii barabara kuanzia Nyakahanga, Nyaishozi, Nyakasindi hadi Benako Ngara?

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Bugene kupitia Nkwenda – Kaisho - Mlongo ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa Karagwe, Kyerwa na Misenyi. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii muhimu kwa uchumi wa Wilaya hizi na Taifa kwa ujumla.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) : Mheshimiwa Naibu Spika, ni utaratibu wa Serikali kulipa fidia kwanza kabla ya kuanza ujenzi. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wa maeneo haya ambapo mradi utapita watalipwa fidia zao kabla ujenzi haujaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia mambo mbalimbali ya maendeleo katika eneo lake lakini pia niwapongeze wananchi kwa kupisha mradi; kwa maana hiyo kwamba kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa ajili ya maendeleo yetu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, amezungumza juu ya barabara hii ambayo inakwenda Mrushaka – Mlongo kilometa 125. Mimi nimetembelea eneo hili, ni eneo muhimu sana sasa kuunganishwa kwa sababu ni sera ya Serikali kuunganisha nchi yetu na nchi za jirani. Barabara hii Mheshimiwa Mbunge anaitaja inatuunganisha sisi Tanzania na Uganda. Kwa hiyo, tunayo mipango ya kuijenga kwa kiwango cha lami lakini namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, asiwahishe shughuli na ikiwezekana tunaweza kuteta ili ajue mpango wa Serikali juu ya kuijenga barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tunaendelea kuihudumia hii barabara na maeneo ambayo ni korofi. Kwa mfano, ile milima, maeneo ya Rwabunuka kuna mipangilio ya milima ambayo ni mikali sana. Tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza kushughulikia maeneo korofi wakati tunajiandaa kuiboresha hii barabara katika kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa maeneo haya wavute subira, tumejipanga vizuri na tunafahamu maeneo haya ni muhimu sana kwa uchumi. Tutashughulikia barabara hii muhimu.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Tatizo la fidia lililopo Babati linafanana kabisa na tatizo la fidia lililopo katika mradi wa umeme wa Rusumo Wilaya ya Ngara. Je, ni lini wananchi wa Kata ya Mlukulazo na Mtobee watalipwa fidia kwa maeneo yao yaliyoathiriwa na mradi wa Rusumo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oliver la masuala ya fidia katika mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Rusumo la megawati 80 pamoja na njia yake ya Msongo wa KV 220 kutoka Rusumo - Nyakanazi. Kwanza Mheshimiwa Mbunge Oliver nimpongeze kwa kufuatilia suala hili la malipo ya fidia; lakini kwa kuwa mradi umeanza na fidia ililipwa pengine wapo wananchi ambao wana malalamiko au bado hawajalipwa, naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge, baada ya hapa tu nitalifuatilia kuona wakazi wa Kata ya Mlukulazo na Kata nyingine ambayo ametaja kwamba wanalipwa stahiki zao kwa sababu mradi ule unaendelea mpaka sasa ambao una manufaa makubwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niulize swali dogo la nyongeza. Matatizo ya usikivu wa simu yaliyopo Same Magharibi ni sawa na matatizo yaliyopo katika Wilaya ya Ngara, Kata za Keza, Mganza, Mrusagamba, Mgoma, Kabanga na Rusumo, ambapo yanaingiliana na nchi jirani za Rwanda na Burundi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha usikivu wa mawasiliano katika kata hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia maendeleo katika eneo lake. Niseme tu maeneo ya mipakani yanazo changamoto za kuingiliana kwa mawasiliano. Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote jambo hili tumeshalitambua na tuna mkakati wa kuwasiliana na wenzetu nchi za jirani kwa sababu upo utaratibu ambao tunajiwekea kwamba ile minara iwekwe umbali fulani ili ipunguze changamoto hii ya kuingiliana kwenye mawasiliano. Pia, tunaendelea kusimika minara katika maeneo haya ya mipakani ili kuhakikisha wananchi wetu wa maeneo hayo hawapati changamoto hii ya kuingiliana kwa mawasiliano.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kuniona niulize swali dogo na nyongeza. Kumekuwa na taarifa za kupotosha juu ya michango mashuleni hasa baada ya elimu bure:-

Je, ni nini maelezo ya Serikali kuhusu suala hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, kwa kufuatilia suala la elimu na hasa hususan watoto wa kike, kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengi hasa wanawake wanafanya kusemea wanawake wenzao ili na wenyewe baadaye wawe wana mambo mazuri huko mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, nimefanya ziara mbalimbali kwenye Halmashauri nyingi tangu nimepata nafasi hii ya kuaminiwa na Mheshimiwa Rais, lakini ni kweli kwamba kumekuwa na watu wanapotosha. Wengine wanapotosha kwa kutojua, lakini wengine wanapotosha kwa makusudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango mashuleni haijazuiliwa. Kilichofanyika, umewekwa utaratibu. Huko nyuma ilikuwa kuna michango mingi mashuleni na inaratibiwa na Walimu. Ilikuwa wanaunda timu yao, kiasi kwamba badala ya kuwa na jukumu kubwa la kufundisha na kusimamia elimu, ikawa wengi wanagombana na wanafunzi na wazazi ili michango iende pale shuleni. Baada ya Serikali kuliona hilo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imetoa waraka wa mwaka 2015 ambao umeanza kutumika mwaka 2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba waraka huu Waheshimiwa Wabunge waupate kwa kuwa unapatikana, wausome. Waraka huu unaelekeza namna michango inavyoweza kuratibiwa katika shule zetu na umetaja kila mtu na kazi yake. Kama ni ngazi ya kijiji, kama ni ngazi ya mtaa, kama ni Kamati ya Shule au Bodi ya Shule, kama ni Waheshimiwa Madiwani kwa maana ya WDC, kama ni Waheshimiwa Wabunge na Halmashauri ngazi ya mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango kama ni kwenye shule kwa mfano, kuna upungufu wa Walimu na tunajua kwamba tuna upungufu wa Walimu hasa masomo ya sayansi kwa sekondari na msingi. Wazazi wenyewe kwa utashi, wakaamua kuona kuna ulazima wa kupata mwalimu hata wa kujitolea kwa michango kidogo. Kikao cha wazazi kinaitishwa, kinasimamiwa ama na Mkurugenzi au na Mkuu wa Wilaya ili wazazi ambao hawana uzwezo wasilazimishwe. Pia baada ya kukubaliana, watoto ambao wazazi wao au walezi hawatakuwa na uwezo kuchanga, ni marufuku kuwazuia kutoenda shuleni kusoma ili wakatafute michango hiyo, wachange wale wenye uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo utaratibu uliotolewa na walaka unaeleza, Waheshimiwa Wabunge wausome, wale ambao wanapotosha wananchi kwamba michango hairuhusiwi. Haiwezekani kuna watu wanakaa kwenye kijiji fulani, kwenye kata fulani, wana uwezo kwa mfano kuchimba kisima cha maji katika shule, hawawezi kuzuiliwa. Cha muhimu, ni lazima tujue nani anachanga na fedha inasimamiwa na nani? Walimu wabaki na jukumu la kufundisha na watu wengine tusaidie miundombinu hii. Kazi ya kuifanya elimu iwe bora Tanzania, ni kazi ya Serikali, kazi ya Wabunge na kazi ya wadau mbalimbali wote ambao wanapenda maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGULUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kivuko hiki cha Kyanyabasa wanafunga kazi saa 12.00 jioni ambapo inaleta adha kubwa kwa wananchi. Kwa mfano, imetokea umeuguliwa usiku, inakulazimu kuzunguka Kishogo – Nyakibimbili – Ibwela – Katelero kuja kwenye Hospitali ya Wilaya inayojengwa Kanazi eneo la Bujunangoma:-

Je, ni lini Serikali itatuondolea adha hiyo ya kufunga kivuko mapema? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Tatizo lililopo katika kivuko cha Kyanyabasa ni sawa na kivuko kilichopo Kata ya Kashalu maarufu kwa jina Kansinda kinachounganisha Wilaya ya Bukoba na Misenyi:-

Sasa ni lini Serikali itaweka kivuko cha Uhakikika kuliko kuvuka na mitumbwi ambapo inahatarisha maisha ya wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayofanya, kwa sababu mara nyingi kwa kweli amekuwa akitusumbua kwa nia ya kuhakikisha wananchi wa eneo hili la Kagera wanapata huduma nzuri. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nakupongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maswali yake mawili, niseme, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, ni kwamba tumedhamiria kufanya maboresho makubwa ya kivuko hiki. Nimesema kwamba pia tutaweka taa pale. Tukiweka taa za usalama pale na tutahakikisha kwamba tunatoa huduma vizuri usiku na mchana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe hofu Mheshmiwa Oliver kwamba tumejipanga kuona tunatoa huduma usiku na mchana. Hata hivyo kwa sasa eneo lile tunavusha kwa kutumia dakika tano tu, tunafanya mivuko pale mara 35 hadi 40 ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri. Kwa hiyo tuendelee kuwasiliana tu na pale ambapo kuna dharura, kwa mfano tuna wagonjwa au misiba na hata wakati wa sherehe kama harusi, tuwasiliane. Tuko tayari kuwahudumia usiku na mchana wakati harakati za kufanya maboresho makubwa yanaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu eneo eneo alilotaja la Kata ya kasharu umeita mwenyewe Kasinda, nielekeze tu wenzetu upande wa TAMESA waende wakaangalie kwa makini eneo hili tuone namna nzuri ya kuleta huduma hii ili tuwaokoe wananchi na hatari ambayo inaweza ikasababishwa na kuvuka kwa kutumia mitumbwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge, suala hili nitalisimamia ili tuone kwamba tunafanyaje wananchi hawa nao waendelee kunufaika na huduma nzuri ya vivuko kuliko kutumia mitumbwi?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuulizwa swali dogo la nyongeza. Wilaya ya Ngara hatuna gari la Zimamoto na yameshatokea majanga mara nyingi na ya kusababisha vifo; na ni barabara inayopitisha magari makubwa yanayobeba mafuta yakielekea nchi za jirani Rwanda, Burundi na Kongo:-

Je, ni lini Serikali itatuletea gari la Zimamoto Wilaya na Ngara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza niendelee kumpongeza Mheshimiwa Oliver kwa jinsi ambavyo amekuwa akipambana kuhakisiha kwamba changamoto mbalimbali zinazohusu vyombo vya usalama katika Mkoa wa Kagera zinapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja yake ya kupeleka gari la zimamoto katika Wilaya ya Ngara, nimhakikishie kwamba pale ambapo mikakati ambayo nimeizungumza kwenye jibu la msingi itakapokuwa imekaa tayari, basi moja katika maeneo ambayo tunayazingatia ni Wilaya ya Ngara.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupatikana Mkandarasi wa Mradi wa Lwakajunju katika Jimbo la Karagwe lakini bado wananchi wa Karagwe hawajajua ni lini mkandarasi huyo atakwenda kuanza. Je, ni lini utekelezaji wa Mkandarasi wa maji wa Lwakajunju utaanza ili kuwatua ndoo wakina mama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa jasiri, mpambanaji kwa wanawake wenzake kwa Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninachotaka kusema sisi kama Wizara ya Maji na kupitia Mheshimiwa Rais tunamshukuru sana tumepata fedha zaidi ya dola milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa miradi katika miji 28 lakini tunashukuru jitihada kubwa ambazo zimefanyw ana Waziri wetu kwa maana ya Mheshimiwa Mbarawa kuhakikisha Mhandisi Mshauri amepatikana kwa haraka na ameshapita katika miji yote sasa hivi tunakamilisha document kwa maana ya kupata kibali ili kumpata mkandarasi na ujenzi wa mradi ule uweze kuanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na kaka yangu Bashungwa siis Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo katika kuhakikisha mkandarasi anapatikana kwa wakati na utekelezaji wa mradi wa maji kwa maana ya kumtua mwanamama ndoo kichwani unaanza mara moja. Ahsante sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Changamoto iliyopo Temeke na Mwananyamala inafanana kabisa na changamoto iliyopo Jimbo la Ngara, Hospitali ya Nyamiaga haina mashine ya kufulia nguo. Je, ni lini Serikali itatuletea mashine ya kufulia nguo ili kutatua changamoto hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Oliver Semguruka, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera kwa kazi kubwa ambayo naye anaifanya katika kufuatilia masuala mbalimbali ya afya katika Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo Serikali tunayafanya lakini vilevile kuna mambo ambayo hivi vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya nayo inapaswa kuvifanya. Wanafanya makusanyo ya fedha na sisi Serikali tunawapelekea bajeti, ni wajibu wa Mganga Mkuu Mfawidhi wa hospitali ile na Mganga Mkuu wa Wilaya kuweka ununuzi wa mashine za kufulia ndani ya mipango yao. Gharama za mashine za kufulia sio gharama kubwa, ni vitu ambavyo Hospitali hii ya Nyamiaga wanaweza wakafanya kwa kupitia bajeti zake za ndani. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Swali lililoulizwa namba 256 linafanana kabisa na changamoto iliyopo Wilaya ya Ngara katika mradi wa Muhweza, ni miongoni mwa vijiji 10, lakini mradi huu umechukua muda mrefu sana bila kukamilika. Je, ni lini mradi huu utakamilika ili kuwatua ndoo kina mama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, dada yangu Mheshimiwa Oliver amekuwa mpambanaji mahili katika kuhakikisha kuwapigania wananchi wa Kagera ili waweze kupata huduma hii muhimu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini, kutokana na swali lake nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge, nimelipokea na nilifuatilie kwa haraka na tuweze kuongeza nguzu zetu ili mradi huo uweze kukamilika na wananchi waweze kupata huduma hii muhimu.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

(i) Je, Serikali itapeleka lini fedha ilizoahidi kwa ajili ya kujenga mabweni na maktaba pale Bugene Sekondari ambao ni A-level peke yake ya Serikali kwenye wilaya ya watu laki tatu na tisini?

(ii) Je, Mheshimiwa Waziri upo tayari kuambatana na mimi pamoja na Mbunge wa Jimbo Mheshimiwa Bashungwa ili ukajionee mlundikano wa wanafunzi Bugene Sekondari kwa sababu ya upungufu wa mabweni?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza naomba nianze kujibu swali la pili kwa kwanza nipo tayari tutaambatana pamoja hakika tutaenda kufanya kazi nzuri tu kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifupi niseme nimpongeze sana Mheshimiwa Oliver, kwa sababu yeye na Mbunge Mheshimiwa Innocent wamekuwa wakipambana sana kuhakikisha Halmashauri ya Karagwe inafanya vizuri. Eneo hili ndio maana hata ile shule ya kwanza tuliyoipatia shilingi 190 ni kwa ajili ya maombi yao waliyoyaleta ofisi kuhakikisha tunasaidia wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na upande wa Bugene sekondari tunajua ni wazi kweli idadi ya wanafunzi ni wengi, naomba nikuhakikishie Serikali itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunaongeza fedha pale kwa ajili miundombinu ile iweze kuimarika vizuri tuweze kupokea watoto ambao tunatarajia si muda mrefu tutawatangaza. Kwa hiyo, hii ni commitment ya Serikali tutafanya kila liwezekanalo tutaongeza fedha kuimarisha miundombinu ya pale.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona niweze kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kabla ya kuuliza swali naomba kutoa pole nyingi kwa Wananchi wa Mkoa wa Kagera kwa mafuriko kwa ajili ya mvua nyingi zinazoendelea kunyesha. Mimi Mbunge wao na Serikali tuko pamoja, nawapa pole sana Ndugu zangu wa Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Spika, sasa swali la nyongeza, changamoto iliyopo Rungwe inafanana kabisa na changamoto iliyopo Wilaya ya Ngara katika Kata ya Mlusagamba, Kata ya Bukiriro na Mganza. Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge Oliver na kumpongeza, hii ni mara yake ya tatu anasimama ndani ya Bunge hili kuulizia masuala ya nishati katika Jimbo la Ngara. Hizo kata alizozitaja ikiwemo Msagamba, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwa miradi ya REA inayoendelea kata hizi zimeingia kwenye REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili, ambao unaanza tarehe 01Julai, 2019, tuko katika hatua za kuandaa makabrasha ya zabuni. Kwa hiyo, nimtoe hofu tu kwamba, na Wananchi wakazi wa Ngara kwamba, Serikali yetu ya Awamu ya Tano imedhamiria ifikapo 2020/21 maeneo yote, vijiji vyote vikiwemo vijiji vya Wilaya ya Ngara viwe vimewaka umeme. Kwa hiyo, nimtoe tu wasi Mheshimiwa Mbunge aendelee kushirikiana na sisi katika kufuatilia hayo maeneo yake, asante sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Watendaji wa Vijiji na Mitaa ni muhimu sana katika uchaguzi huu, lakini kuna vijiji vingi havina watendaji. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kujaza nafasi hizi kabla ya uchaguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu unasimamiwa na watendaji wa ngazi za chini wale Watendaji wa Vijiji na Mitaa, Watendaji wa Kata na mpaka ngazi ya Halmashauri na ni kweli kwamba kuna baadhi ya maeneo ambayo hayana watendaji hawa, lakini nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, uko utaratibu wa Kiserikali bahati nzuri hawa ni watumishi wa Serikali. Tunaendelea kuchukua hatua kuajiri na kuziba mapengo. Ikitokea uchaguzi unafika eneo fulani au kijiji hakuna Mtendaji, wale watumishi wa Serikali wakiwepo watumishi wa afya, walimu wanapewa jukumu watasimamia kwa sababu wote wanaitwa, wanapewa semina na mafunzo na wanaapishwa kiapo cha utii, halafu wanafanyakazi za Kiserikali na wakimaliza kazi hii wanarudi kwenye majukumu yao ya kawaida. Ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona, Shule ya Sekondari ya Mumiterama iliyopo Wilaya ya Ngara imeanzishwa mwaka huu na haijawahi kupatiwa fedha yoyote kwa ajili kuendesha.

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka pesa katika shule hiyo, kwa sababu ina changamoto nyingi, maji usafiri na makazi ya watumishi?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuruku, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipokee ombi lake, kwa sababu shule inapokuwa inaanzishwa kwanza kuna mambo ya kuzingatia, tunaangalia vigezo mbalimbali, Ofisi ya Rais TAMISEMI, pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Sasa kama shule imesajiliwa imeanza kweli haijawahi kupelekewa fedha naomba Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi cha maswali na majibu tuwasiliane tuone ni kwa nini haijapata na kama kuna ukweli wowote tuweze kuchukua hatua, ahsante. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Rwakajunju ulioko Karagwe, nimeshauliza sana maswali katika Bunge la Kumi na Moja na mara zote huwa najibiwa kwamba mradi huo utatekeleza hivi karibuni lakini hadi sasa bado haujatekelezwa. Nini majibu ya Serikali kuhusu mradi huu ili kuwatua ndoo akina mama wa Karagwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi huu utatekelezwa kwa awamu katika mwaka wa fedha wa 2021/2022.
MHE. OLIVER D. SEMGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Changamoto ya barabara iliyoko Tunduru Kusini inafanana kabisa na changamoto iliyoko wilaya ya Ngara ya barabara ya Murugalama - Lulenge - Mizani yenye urefu wa kilomita 85. Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu swali la nyongeza la kwanza, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii barabara aliyoitaja ambayo inapita eneo la Mgalama - Lulenge nina hakika zitajadiliwa katika kipindi hiki cha bajeti, kwa hiyo, awe na subira.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali lililoulizwa namba 211 linafanana kabisa na wakulima wa Mkoa wa Kagera wanaolima kahawa. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wanunuzi wanaotaka kununua Kahawa kwenye vyama vya msingi. Je, inaruhusiwa? Nilikuwa napenda tamko kutoka kwa Serikali. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, vile vile jambo hili limekuwa likifuatiliwa kwa karibu na Mheshimiwa Innocent Bilakwate na Mheshimiwa Innocent Bashungwa. Naomba nisitoe kauli na hii kauli vyama vya ushirika wa Mkoa wa Kagera kwa maana ya KDCU na KCU. Niseme tu kwamba wanunuzi binafsi, soko la kununua kahawa, soko la kununua mazao yaliyoko kwenye vyama vya ushirika ni masoko huria. Wanunuzi wanaruhusiwa kwenda kuingia mikataba na vyama vya msingi.

Mheshimiwa Spika, na nitumie kauli hii kuwaagiza KDCU na KCU wasimzuie mnunuzi yeyote anayetaka kununua kahawa moja kwa moja kwenye chama cha msingi na wala wasiwatishe viongozi wa vyama vya msingi kuwazuia kuingia mikataba na wanunuzi. Mnunuzi aseme bei anayonunulia na kiwango anachonunulia na wawaruhusu kushindania katika AMCOS level na wasiwachaji tozo zinazohusiana na union kama mnunuzi anaenda kununua kwenye chama cha msingi. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Wilaya ya Ngara ina changamoto ya uhaba wa askari na Wilaya hii inapakana na nchi jirani za Rwanda na Burundi. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka askari wakutosha ili wananchi waweze kulindwa na mali zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, tuna mpango gani sasa wa kupeleka askari ama ulinzi katika maeneo ambayo ameyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, narejea tena kusema kwamba wajibu na jukumu la Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kupitia Jeshi la Polisi ni kuhakikisha kwamba maeneo yote yanapata huduma ya ulinzi na usalama ili wananchi waishi kwa amani. Ikiwa pana watu wageni, ndani ya Tanzania hii lakini wajibu wetu ni kupeleka. Nimtoe hofu, asiwe na wasiwasi, maeneo hayo kwa kuwa amehisi kwamba yana upungufu wa ulinzi, tunayachukua na tunapeleka ulinzi ili wananchi na wao waweze kuishi kwa amani na wapate huduma za ulinzi na usalama. Nakushukuru.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize Serikali ni lini kupitia Wizara ya Maji itapeleka maji kutoka Ziwa Victoria katika Mji wa Bihalamuro kama alivyoahidi Hayati Rais Magufuli mwaka jana akiwa anaomba kura kwa ajili ya kuwatua ndoo wakina mama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver, Mbunge wa Viti Maalum, Kagera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maji kutoka Ziwa Victoria yanatarajiwa pia kunufaisha wakazi wa Jimbo la Biharamulo na hii binafsi nilishaenda kufanya ziara maeneo ya Biharamulo na mipango mikakati inakwenda ukingoni sasa ili tuweze kuona mwaka ujao wa fedha kadri ambavyo fedha itakuwa ikipatikana, Biharamulo nao wawe wanufaika namba moja.

Mheshimiwa Spika, nipende kumpongeza Mheshimiwa Oliver amekuwa mfuatiliaji mzuri na sisi hatutakuwa kikwazo, tutahakikisha wote ambao mnafuatilia kwa kina hii kazi ya usambazaji maji na kuleta maji kutoka Maziwa yetu Makuu ikiwa ni mpango mkakati wa Wizara kutumia Maziwa Makuu inakwenda kutimia. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize Serikali ni lini kupitia Wizara ya Maji itapeleka maji kutoka Ziwa Victoria katika Mji wa Bihalamuro kama alivyoahidi Hayati Rais Magufuli mwaka jana akiwa anaomba kura kwa ajili ya kuwatua ndoo wakina mama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver, Mbunge wa Viti Maalum, Kagera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maji kutoka Ziwa Victoria yanatarajiwa pia kunufaisha wakazi wa Jimbo la Biharamulo na hii binafsi nilishaenda kufanya ziara maeneo ya Biharamulo na mipango mikakati inakwenda ukingoni sasa ili tuweze kuona mwaka ujao wa fedha kadri ambavyo fedha itakuwa ikipatikana, Biharamulo nao wawe wanufaika namba moja.

Mheshimiwa Spika, nipende kumpongeza Mheshimiwa Oliver amekuwa mfuatiliaji mzuri na sisi hatutakuwa kikwazo, tutahakikisha wote ambao mnafuatilia kwa kina hii kazi ya usambazaji maji na kuleta maji kutoka Maziwa yetu Makuu ikiwa ni mpango mkakati wa Wizara kutumia Maziwa Makuu inakwenda kutimia. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Barabara ya Bugene, Karagwe kupitia pori la Kimisi hadi Ngara Mheshimiwa Hayati Magufuli akiwa Karagwe mwaka huu mwezi wa Januari alitangaza ianzwe kuwekwa lami naomba kujua utekelezaji wake umefikia wapi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo ni kweli barabara hii iliahidiwa na ilikuwa ni agizo la Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli barabara hii imetengewa fedha katika bajeti iliyopitishwa kwa hiyo itakuwa ni kati ya barabara ambazo zitaanza kutekelezwa kujengwa kwa kiwango cha lami mara bajeti itakavyoanza kutumika ahsante. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninalo swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba commitment ya Serikali, ni lini itajenga hizi kilometa 128.5 za barabara hii kupitia Pori la Kimisi hadi Benaco Ngara kwa kiwango cha lami? Kwa sababu nilishauliza mara nyingi sana ndani ya Bunge hili, najibiwa upembuzi yakinifu, upembuzi yakinifu, sasa naomba commitment ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY
K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, Kagera kwamba siyo tena tunaongelea upembuzi yakinifu ama usanifu wa kina. Naomba nimhakikishie kwamba tupo kwenye hatua za manunuzi. Mkandarasi wa barabara hii ameshapatikana na tupo kwenye majadiliano namna ya kuanza hii barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi kwamba jinsi anavyofuatilia tutaanza na kilometa 60 kuanzia Bugene kuelekea Kasulo, yaani Benaco. Kwa hiyo, siyo tena habari ya kubabaisha, ni habari ya ukweli kwa sababu tayari tupo kwenye hatua za manunuzi. Kwa hiyo, awe na uhakika kwamba kazi anayofanya kufuatilia, sisi tunafanya na fedha hii tayari imeshatengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi huo. Ahsante. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, Mji wa Bukoba uko katika mkoa unaopakana na nchi jirani zaidi ya tatu. Je, ni lini Serikali itajenga soko kuu Bukoba Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mji wa Bukoba ni miongoni mwa miji ambayo iko kwenye mpango mkakati ambao utakwenda kujenga masoko, barabara, vituo vya mabasi vya kisasa. Nimpongeze sana Mheshimiwa Oliver Semuguruka, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Stephen Byabato, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, amekuwa mfuatiliaji wa mara kwa mara na Serikali iko kwenye hatua za mwisho za kuanza utekelezaji wa mradi huo. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba, soko hilo, lakini pamoja na maeneo hayo mengine yatafayiwa kazi baada ya mradi huo kuanza. Nakushukuru sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu masuri ya Serikali, ninalo swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itaiwezesha hospitali zote za kanda kutoa huduma ya tiba ya kansa kwa asilimia 100?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo anahangaika na matatizo ya wananchi na akinamama wa Kagera, lakini jinsi ambavyo anashirikiana na Wabunge wa majimbo kwa kuwafuata kwenye viti vyao na kuwauliza mambo ambayo wanaweza wakafuatilia kwa pamoja. Hili linaonesha ni kwa nini umeaminika miaka iliyopita na sasa unaendelea kuaminika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda niseme tu kwamba Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, amenunua kifaa chenye thamani ya shilingi bilioni 18 ambacho ni kifaa pekee kwa Afrika Mashariki kwa sasa na viko vitano tu kwa Afrika ambacho kina uwezo wa kusaidia kupima kansa na kiko Ocean Road na kinazalisha mionzi ambayo ilikuwa tunaenda kuchukua Afrika Kusini. Kwa maana hiyo sasa mionzi iliyokuwa inachukuliwa Afrika Kusini hata nchi za Afrika Mashariki sasa watakuwa wanachukua hapa Ocean Road.

Mheshimiwa Spika, lakini hiyo haijatosha kwa Kanda ya Ziwa; kwa Kanda ya Ziwa tayari Serikali imepeleka shilingi bilioni 7.4 kwa ajili ya kuboresha miundombinu pale na kununua vifaa ili kuweza kutoa huduma pale kwa asilimia 100, KCMC imeshapelekwa shilingi bilioni sita kwa ajili hiyo na kwa upande wa Kanda ya Mbeya sasa hivi tukio kwenye hatua, inatakiwa ufanyike ujenzi kujenga kituo kimoja ambacho kinashughulikia kansa kwa eneo lote. Tayari michoro imeshachorwa na sasa tathmini inafanyika ili kujua sasa ni shilingi ngapi itumike hiyo kazi ianze mapema. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA, Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Kuna mpango gani wa kuboresha miundombinu ya Hifadhi za Ibanda na Rumanyika zilizopo Wilaya ya Kyerwa ili kuvutia watalii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna hifadhi nyingi ambazo tumeshazitangaza ikiwemo ya Ibanda, Rumanyika, pia Kyerwa. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tuna zindua Phase II ya programu ya Royal Tour. Kwa hiyo, maeneo haya pia tutaweza kuyaingiza ili yaweze kuwa ni ya kimkakati katika kuhakikisha kwamba vivutio hivi tunavitangaza vizuri. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Serikali ilitueleza kwamba kuna viwanda vya kuanzia 3,500,000 na katika Mkoa wetu wa Kagera kina mama wamekuwa wakikopeshwa mikopo isiyo na tija.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwakopesha hivyo viwanda badala ya pesa ili kutengeneza ajira nyingi mkoani kwetu Kagera? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Kagera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifatilia sana kuhusiana na wafanyabiashara wakina mama wajasiriamali katika Mkoa wa Kagera. Nimshukuru sana kwa kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Oliver. Lakini kuhusiana na mitaji hii ni kweli wajasiriamali wadogo hasa akina mama tunataka kupitia Shirika letu la Viwanda Vidogo kuwakopesha viwanda au teknolojia rahisi za kufanyia biashara zao badala ya kuwapa fedha ambazo wakati mwingine zinaweza kutumika katika malengo yasiyokusudiwa.

Kwa hiyo, moja ya mikakati ni hiyo kuwapa viwanda ili iwasaidie kuzalisha bidhaa ndogondogo pia waweze kukidhi mahitaji ambayo wameomba katika mikopo hii. Nakushukuru sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Je Serikali haioni umuhimu wa kuwaelimisha watumiaji wa bandari ikiwemo ya Kemondo na Mwanza juu ya Sheria za Tozo zinazo zinazotungwa kuliko kukutana nazo barabani? (Makofi)

Swali langu la pili je, ni aina gani za tozo? Napenda kujua hilo, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kutoza tozo ama kutunga Sheria za Tozo kwanza unaanzishwa na Mamlaka ya Bandari yenyewe TPA na hatimaye unapelekwa kwa mdhibiti ambaye ndiye TASAC na TASAC ana wajibu wa kuitisha wadau wote wa sekta hiyo ama maeneo ambako hiyo tozo itakuwa inagusa katika tozo.

Sasa ninamuelekeza ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini pamoja na TASAC watoe elimu, waende katika hizi bandari za Kemondo pamoja na bandari zingine nchini kwenda kutoa elimu kwa jamii ili waeleze ni aina gani ya tozo wakienda bandarini watakutana nazo na kwa kiwango gani.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili anataka Mheshimiwa Mbunge afahamu aina ya tozo ambazo bandari inatoza; tuna tozo ya aina nyingi, lakini zimegawanyika katika makundi mbalimbali; kuna tozo za lazima ambazo tunaita ni ports statutory charges, lakini kuna tozo tunazoziita wharfage, wharfage ni aina ya tozo ambayo ukitumia miundombinu ya bandari unatozwa, lakini kuna tozo za show handling hizi ni tozo ambazo meli inapokuja mpaka kwenye gati la bandari inapokuwa inashusha mzigo ama kupakia mzigo pia unatoza na kuna tozo za ziada, ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Wilaya ya Ngara ina vyanzo vikuu vya maji ambavyo ni Mto Ruvugu na Mto Kagera. Pamoja na uwepo wa vyanzo hivi tatizo la maji katika Wilaya ya Ngara limekuwa ni kubwa mno.

Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kujenga mradi mkubwa unaotosheleza wananchi wa Wilaya Ngara? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, kutoa Mkoa wa Kagera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Ngara ni moja ya wilaya ambayo tumeipa jicho la kipekee kabisa kuona kwamba tunaenda kutatua changamoto za maji. Niseme tayari tuna miradi ambayo ipo kwenye utekelezaji, lakini tuna miradi ambayo tutaendelea nayo hivyo tatizo la maji linakwenda kukoma.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kuna Soko la Kimataifa lililoanza kujengwa katika Kitongoji cha Nzaza Kata ya Kabanga Wilayani Ngara 2014 na ujenzi huo ukasimama ghafla: Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi huo wa soko hilo kwa manufaa makubwa ya wananchi wa Ngara na wakulima kwa ujumla? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mbunge Viti Maalumu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, soko lilopo pale Kabanga katika Wilaya ya Ngara ni kati ya masoko sita ambayo Wizara imepanga kuyamalizia katika mwaka huu wa fedha. Hivyo soko hili lipo katika mpango na litatekelezwa.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.

Ili kuweka taarifa sahihi kwa wananchi wangu wa Bukoba Mjini. Je, Serikali kupitia TARURA ina maana kuwa barabara hizi zimehamishiwa TARURA badala ya TANROADS nilitaka kujua hilo maana hizi barabara ni za TANROADS siyo za TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kumekuwepo na malalamiko mengi ya fidia kwenye miradi ya aina hii. Je, Serikali inatoa ahadi gani kwa wananchi wangu wa Bukoba Mjini endapo wakipitiwa katika hii barabara watapata fidia kwa uharaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba anasema barabara hii huenda imehamishwa kutoka TANROADS kwenda TARURA, nimwambie tu kwamba hapana ni kwa sababu Serikali hii ni moja na inafanya kazi kwa pamoja nasi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA na TANROADS tunafanya kazi kwa umoja. Kwa hiyo, kikubwa katika swali lake la msingi alilouliza hapa juu ya kuhakikisha usanifu unakamilika na ujenzi wa barabara unaanza vitafanyika kama ambavyo ameainisha hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuhusu fidia anataka tu mara baada ya usanifu ni wananchi wale walipwe fidia kwa wakati, Serikali italipa fidia kulingana na tathmini ambayo itafanywa katika maeneo hayo. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa sana kwenye mitandao ya simu, hasa Vodacom, ukiwa unaongea ina-stuck au inakoroma huku inaendelea ku-charge. Ningependa kujua nini tatizo katika mitandao hiyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya kwa Mkoa wa Kagera, vilevile suala hili Mheshimiwa Waziri tayari ameshaunda timu ya kuzunguka nchi nzima kujiridhisha na huduma za mawasiliano nchini. Ni kweli kabisa kumekuwa na changamoto kama hizo, lakini tunaamini timu hii itakapokamilisha kazi yake basi tutachukua hatua stahiki ili wanchi wapate mawasiliano ya uhakika. Ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Mradi wa umeme wa Rusumo uliopo Wilaya ya Ngara ulitarajia kukamilika Desemba mwaka jana 2021 lakini mradi huo mpaka sasa haujakamilika.

Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi huo ili kutatua tatizo la umeme Wilaya ya Ngara na Kagera kwa ujumla? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli mradi wa umeme wa Rusumo unaotarajiwa kuzalisha megawatts 87 unatekelezwa na ubia wa nchi tatu ambazo ni Tanzania, Ruanda na Burundi. Ni kweli ulitarajiwa ukamilike Desemba mwaka jana lakini kwa sababu ya changamoto za ugonjwa wa UVIKO-19 ambao wenzetu uliwakabili zaidi yetu, mradi huo umechelewa lakini maelekezo ya Serikali hizi tatu ni kwamba ifikapo Novemba mwaka huu mradi huu uweze kukamilika ili wale wananchi ambao Mheshimiwa Oliver anawafuatilia wa Jimbo la Ngara lakini na wa Mkoa wa Kagera kwa ujumla na Tanzania kwa ujumla waweze kunufaika na upatikanaji wa umeme unaotoka kwenye mradi huu wa Rusumo. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Changamoto kubwa inayokabili wananchi wa Ngara ya mawasiliano ya simu ni kuingiliana na nchi jirani za Rwanda na Burundi.

Ninataka kujua, ni nini mkakati wa Serikali ili kutatua changamoto hiyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka Mbunge wa Viti Maalum Kagera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kabisa kwamba ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge huyu ameendelea kuwa msumbufu kweli kweli kwa ajili ya kuhakikisha maeneo hayo yanatafutiwa ufumbuzi. Lakini vilevile natambua pia usumbufu ambao nimeendelea kuupata kutoka Mbunge wa Jimbo la Ngara Mheshimiwa Ndaisaba kwa sababu haya maeneo tuliyatembelea na tukagundua kabisa kuna changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizopo; ya kwanza, si kwamba hatuna minara, kuna maeneo ambayo tuna minara lakini nguvu yake haikuwa inatosha. Hivyo tulitoa maelekezo kwa watoa huduma kuhakikisha kwamba minara yao inakuwa na nguvu ili huu mwingiliano usitokee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna maeneo mengine ambayo hatukuwa na minara ndiyo maana mwaka jana sasa kupitia mradi wa special zone na borders, yaani mipakani na maeneo maalum, tulihakikisha kwamba kuna baadhi ya maeneo ambayo tunaenda kujenga minara yakiwemo maeneo ya Ngara ambapo kuna miradi tisa ambayo inaenda kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Je, ni lini eneo la Nyangoye katika Barabara ya Uganda – Bukoba Mjini litarekebishwa, ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais, ili kuondoa ajali zinazotokea mara kwa mara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Kagera, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, lilikuwa agizo la Makamu wa Rais na sasa hivi kinachoendelea ni kufanya usanifu wa namna ya kuijenga barabara hiyo. Ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Je, ni lini uwanja wa ndege wa Bukoba Mjini utawekewa taa na mnara wa kuongoza ndege ili kuongeza usalama wa watumiaji wa uwanja huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kiwanja cha ndege cha Bukoba kwenye mwaka wa fedha ujao na kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais tumetenga takribani bilioni 2.9 kwa ajili ya ujenzi wa control tower pamoja na taa za kuongozea ndege katika kiwanja hiki, ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Mradi wa Maji Kyerwa, Nyaruzumbula mpaka Kamuli ni lini utaanza?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyoeleza Tarehe 10 mwezi Mei, tunawasilisha bajeti yetu, nataka nimhakikishie kama Mheshimiwa Rais alivyosema mambo ni moto, mambo ni fire tutakwenda vizuri katika kuhakikisha jambo hili linaenda vizuri. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Soko Kuu la Bukoba Mjini ni chakavu na dogo kwa matumizi ya sasa, je, lini Mradi wa TACTIC utaanza ili soko hilo lijengwe?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba Manispaa ya Bukoba iko katika awamu ya pili ya utekelezaji wa Mradi wa TACTIC (Tier II). Kwa hiyo nimwondoe hofu, kama ambavyo Mbunge wa Jimbo, Mheshimiwa Stephen Byabato analifuatilia na jambo hili linakwenda kutekelezeka. Ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mradi wa Maji Kyerwa Nyaruzumbula mpaka Kamuli utaanza lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu tayari tuna mkandarasi wakati wowote mradi utaanza kufanyiwa kazi. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona, je, ni lini Mradi wa TACTIC utaanza ili soko na stendi vijengwe Bukoba Mjini? Hili swali nimeshaliuliza zaidi ya mara tatu ndani ya Bunge hili, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimtoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeanza utekelezaji wa Mradi wa TACTIC kwa awamu ya kwanza lakini awamu ya pili pia tathmini zinaendelea na awamu ya tatu itakwenda kutekelezwa. Kwa hiyo, Halmashauri ya Bukoba pia ipo katika moja ya awamu hizi na mradi huu utatekelezwa, ahsante. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itakuja na mkakati wa uzalishaji miche kwa kutumia teknolojia ya chupa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti yetu ya mwaka 2023/2024 zimetengwa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuwajengea uwezo TARI – Maruku ili waweze kuanza teknolojia mpya ya uzalishaji wa miche safi kupitia tissue culture ambayo itasaidia sana katika kutatua changamoto hii ya ugonjwa wa mnyauko.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa muda mrefu imekuwa na mpango wa kujenga Mahakama ya Mwanzo Kata ya Izigo, Wilaya ya Muleba, ningependa kujua utekelezaji wa ujenzi wa Mahakama hiyo umefikia wapi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na naomba nijibu swali la Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wetu wa Kagera katika Wilaya ya Muleba Kata hii ya Izigo, Tarafa ya Izigo iko kwenye mpango wa mwaka huu, tunakwenda kujenga mwaka huu Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu Jimbo la Ngara, Kata ya Murukulazo kwa sababu mawasiliano yanasuasua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa eneo hilo lina changamoto kwa sababu liko mpakani kule na linapata huduma kutoka maeneo ya ndani ambapo minara yake haina nguvu sana. Tulishatuma wataalam wetu katika maeneo haya kwa sababu yapo katika miji ambayo ni ya kimkakati na Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba, maeneo yote ya kimkakati tunahakikisha tunaimarisha huduma ya mawasiliano. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge tunalifanyia kazi. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona.

Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa barabara ya Katoma hadi Bukoli kwa kiwango cha lami ndani ya Wilaya ya Misenyi, Mkoani Kagera?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Semuguruka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Katoma kwenda Bukoli ipo inaendelea kujengwa lakini kwa awamu. Mwaka huu wa fedha imetengewa pia fedha ambapo tunategemea kwamba tutajenga zaidi ya kile tulichokuwa tunakijenga ili kuikamilisha barabara yote kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Je, ni lini Serikali itajenga Skimu ya Umwagiliaji Muhuruzi - Nyakahura Wilaya ya Biharamulo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwenye kitabu chetu cha bajeti, kiambatisho Namba 11 Ukurasa wa 206 tumeitaja Skimu ya Muhuruzi katika Wilaya ya Biharamulo kama sehemu ambazo zitajengwa katika mwaka huu wa fedha unaoanza Julai. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kazi inafanyika katika mwaka wa fedha ujao.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini barabara nne zitajengwa eneo la Nyangole, Bukoba Mjini ili kutimiza ahadi ya Makamu wa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nne eneo la Nyangole, ambayo iko Bukoba Mjini ilikuwa ni ombi la Mheshimiwa Mbunge wa Bukoba Mjini, Mheshimiwa Byabato, wakati Makamu wa Rais amefanya ziara katika Mji wa Bukoba. Ninamshukuru kwanza Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mbunge, kwa kuendelea kufuatilia utekelezaji wa ahadi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Oliver pamoja na Mheshimiwa wa Bukoba Mjini na wananchi wa Bukoba Mjini agizo hilo tayari tumeshaanza utekelezaji. Katika hii barabara tutafanya kazi tatu, moja itakuwa ni kuondoa, kupunguza zile kona, kupunguza mteremko, lakini pia kujenga barabara ya njia mbili zinazoshuka na njia mbili zinazopanda, tutaanza na kilometa nne, lakini mpango ni kujenga kilometa tano kutoka hapo Nyangoya hadi Bukoba bandarini. Ahsante. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Mpango wa kutekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Kata za Magata, Muleba, Buleza, Chikuku na Kagoma utaanza lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Kagera, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maeneo haya aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge Oliver, kwanza tulishakaana naye ofisini na tulishamwelekeza. Mheshimiwa Mbunge nakupongeza kwa ufuatiliaji, hizi kata ulizozitaja kama tulivyokubaliana ni lazima mwaka ujao wa fedha tuhakikishe na zenyewe zinakwenda kupata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi kilichopo Kata ya Keza Wilayani Ngara kilijengwa kwa nguvu za wananchi, lakini mpaka sasa hakijamalizika; je, ni lini Serikali itamalizia kituo hicho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wananchi wa Ngara wamejitahidi kujenga kituo hicho na tunampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ngara na ahadi yetu ni kwamba katika mwaka ujao vituo vya kumalizia kwa mujibu wa bajeti yetu ni 13, vituo vingine vitaendelea kupangwa kwa kipaumbele katika bajeti zinazofuata katika miaka ijayo huko mbele. (Makofi)

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali la nyongeza. Changamoto iliyopo Kiembe Samaki inafanana kabisa na changamoto iliyoko Wilaya ya Ngara kituo cha Polisi cha Rurenge kimchakaa kabisa mpaka kinavuja. Je, ni lini Serikali itakifanyia ukarabati kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimwa Oliver kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inatambua uchakavu wa Kituo cha Polisi Rurenge tena ambacho kiko karibu na mpaka. Kama nilivyoeleza katika majibu niliyomjibu hivi karibuni ni mpango wa Serikali kuvikarabati vituo vyote kikiwemo hiki cha Rurenge na hivi vituo vya mpakani Mheshimiwa Mbunge tutavipa msisitizo maalum, nashukuru.

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Nkenge – Misenyi tunaishukuru Serikali kutujengea vituo vya afya vya Kanyigo, Kakunyu na Kabyaile. Je, ni lini Serikali itatupelekea watumishi wa afya katika vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Semuguruka amekuwa akifuatilia sana suala la watumishi katika vituo hivyo na nimhakikishie kwamba Serikali kama ilivyoanza kuajiri sasa tutahakikisha tunaendelea kuajiri, lakini pia kupeleka watumishi katika vituo hivyo. (Makofi)

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Kwa vile Serikali ilishaahidi kutoa bilioni moja kuanzia Julai na tunaamini itakuja; je, sasa Manispaa ya Bukoba Mjini ianze kutangaza tender kama TARURA wanavyofanya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili kwa kuwa stendi ya Bukoba Mjini imewekwa katika miradi ya TACTIC, naomba kujua utekelezaji wa mradi huu utaanza lini katika Manispaa ya Bukoba?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Semuguruka kwa namna ambavyo anashirikiana kwa karibu sana na Mheshimiwa Mbunge Stephen Byabato, Mbunge wa Bukoba Mjini kuhakikisha miradi inakwenda vizuri, lakini nimuhakikishie kwamba suala la ahadi ya Serikali ya bilioni moja ni ahadi ya Serikali na tutahakikisha fedha hiyo inakwenda mwaka wa fedha ujao tunaoanza Julai ili kazi zianze. Lakini ni vema tusubiri fedha ziingie ndipo tuanze kutangaza zabuni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili kuhusiana mradi wa TACTIC unaoanza awamu ya pili mwaka wa fedha baada ya 2022/2023. Ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana ninalo swali moja la nyongeza. Kwanza, niishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri ya kutia moyo. Kwa kuwa umekiri kuwepo kwa maporomoko hayo ambayo ni kivutio lakini yamepotea baada ya uchepushaji kwenye mradi wa umeme Rusumo. Je, huoni sasa ipo haja kupitia Wizara yako na Wizara ya Nishati mshirikiane kurejesha maporomoko hayo yawe kama awali ili yaendelee kuwa kivutio katika Wilaya yetu ya Ngara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Semguruka kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kwa kushirikiana na kampuni ya umeme ambayo itapewa jukumu la kuendesha mradi ule wa umeme pale Rusumo tayari wanamkakati wa kupanda miti katika eneo lote lile la ukanda wa mradi ule, ni imani yetu kwamba baada ya kufanyika upandaji wa miti ule hali ya upatikanaji wa maji katika eneo lile itaimarika na hivyo uwezekano mkubwa wa kivutio hiki kuendelea kutumika.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona; ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye vitongoji zaidi ya asilimia 70 katika Wilaya ya Kyerwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali tumeanza mpango wa kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote vilivyobakia 36,000. Kwa kuanza, tumeanza kwa miradiya ujazilizi ambayo tumeshaweka wakandarasi na vilevile tunategemea kuendelea kutafuta wakandarasi kwa Mradi wa Vitongoji 15 kwenye kila jimbo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, vitongoji katika Jimbo la Kyerwa na vyenyewe vitafikiwa, ahsante. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nina swali moja la nyongeza.

Je, wakati huo ambao taratibu za kujenga kingo zinaendelea, Serikali haioni haja ya kutoa fedha angalau Shilingi milioni 100 kwa ajili ya kusafisha Mto Kanoni ili kupunguza athari zake hususan Kata nne ambazo zinaathirika zaidi; Kata ya Bilele, Bakoba, Hamugembe na Nshambya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Oliver Semuguruka kwa kadri anavyowakilisha wananchi wa Mkoa wa Kagera, lakini pia, anavyowasemea ipasavyo wananchi wa Mkoa huo. Vile vile nampongeza sana Mheshimiwa Stephen Byabato, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini anavyowasemea na kuwawakilisha ipasavyo wananchi wa Bukoba na anavyoshirikiana na Waheshimiwa Wabunge wa Viti Maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitambue kwamba wapo Waheshimiwa Madiwani, Mstahiki Meya na Mkurugenzi wa Bukoba Manispaa. Nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi kuhakikisha wakati tunasubiri mradi huu wa ujenzi wa kingo kwa maana ya mradi wa TACTIC, watenge fedha kwa kadri inavyowezekana kuendelea kuboresha kingo na kina za Mto Kanoni ili kuzuia madhara hayo wakati bajeti hiyo inakuja kutekelezwa, ahsante. (Makofi)