Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Hussein Mohamed Bashe (94 total)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-

Je, kwa nini Serikali inahamasisha kilimo cha pamba kwa wananchi huku ikiwa haina uwezo wa kupeleka dawa za kuulia wadudu na zinapopatikana huwa ni chache?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza si sahihi kusema kuwa Serikali inahamasisha kilimo cha pamba ikiwa haina uwezo wa kupeleka sumu za kuulia wadudu na hata zinapopatikana huwa ni chache. Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha mazao yote ikiwemo zao la pamba ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kama sehemu ya utekelezaji wa hamasa za kilimo cha pamba, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 eneo la ekari 1,488,406 lililimwa na kuzalisha kiasi cha tani 132,961. Chupa milioni 4.6 za viuadudu zenye thamani ya shilingi bilioni 16.8 na vinyunyizi 15,300 vyenye thamani ya shillingi milioni 462 vilinunuliwa na kusambazwa mwaka huo. Aidha, katika msimu wa 2018/2019 eneo la ekari 1,865,000 lililimwa na kuzalisha kiasi cha tani 222,725 ambapo chupa milioni 6 za viuadudu vyenye thamani ya shilingi bilioni 29 na vinyunyizi 23,000 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.8 vilinunuliwa. Vilevile, katika msimu wa 2019/2020 eneo la ekari 1,786,890 lililimwa na kuzalisha kiasi cha tani 350,473 ambapo chupa milioni 8.2 zenye thamani ya shilingi bilioni 41 na vinyunyizi 20,000 vyenye thamani ya shillingi bilioni 1.6 vilinunuliwa.

Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2017/2018 jumla ya ekapaki 965,300 na vinyunyizi 3,302 vilisambazwa katika Mkoa wa Geita. Aidha, jumla ya ekapaki 736,345 na vinyunyizi 3,020 vilisambazwa katika mkoa huo katika msimu wa 2018/2019. Kwa msimu wa 2019/2020, Mkoa wa Geita umekwisha kusambaziwa kiasi cha ekapaki 8,748 na usambazaji bado unaendelea.

Mheshimiwa Spika, uchache wa viuadudu vya zao la pamba umechangiwa na baadhi ya wakulima kutumia viuadudu katika kupulizia mazao mengine kama vile mahindi na viazi vitamu ili kudhibiti viwavijeshi. Vilevile, kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya viongozi wa vijiji katika baadhi ya maeneo ukiwemo Mkoa wa Geita ambapo viuadudu havikupelekwa kwa wakulima na badala yake kuuzwa katika maduka ya pembejeo kinyume na taratibu za usambazaji wa viuadudu vya zao la pamba. Watu zaidi ya 12 walikamatwa na kati yao 9 walifunguliwa mashtaka ambapo watu nane (8) walihukumiwa kifungo cha miezi sita jela kila mmoja. Serikali itaendelea kufuatilia upatikanaji wa viuadudu vya zao la pamba na kuhakikisha vinawafikia wakulima kwa wakati.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-

Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuwasaidia Wakulima nchini hususan wakulima wa tumbaku ili zao hili la biashara liweze kuwasaidia wakulima na Taifa kwa ujumla kwa kuingiza fedha za kigeni:-

(a) Je, Serikali inawahakikishiaje wakulima wa tumbaku katika Mkoa wa Tabora ikiwemo Wilaya ya Urambo kwamba mbolea itakuwepo mwezi Agosti wanapoanza kilimo cha tumbaku kulingana na makisio yao;

(b) Je, wanunuzi wangapi wamepatikana hadi sasa ili wakulima walime tumbaku nyingi kwa bei ya ushindani ili kumnufaisha Mkulima na Taifa kwa ujumla.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwa ridha yako naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na kwa kila jambo. Jambo la pili nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani aliyoionesha kwangu na imani aliyowaonesha wananchi wa Jimbo la Nzega. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Jimbo la Urambo lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, makisio ya mahitaji ya mbolea kwa Mkoa wa Tabora ni jumla ya tani 9,000 sawa na asilimia 42 ya mahitaji ya mbolea ya zao la tumbaku nchini ya tani 21,582. Kati ya kiasi hicho tani 205 za NPK ni kwa ajili ya vitalu na tani 8,887 NPK kwa ajili ya mashambani. Aidha, mahitaji ya Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ni jumla ya tani 2,468 ambapo tani 50.73 ni NPK kwa ajili ya vitalu, tani 1,741 ni NPK kwa ajili ya mashambani na tani 676 mbolea aina ya CAN kwa ajili ya shambani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia tarehe 15 Agosti, 2019 upatikanaji wa mbolea katika Halmashauri ya Urambo kwa ajili ya vitalu ni mifuko 1,014 sawa na upatikanaji wa asilimia 100 na usambazaji unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 10. Vilevile mbolea mashambani, zabuni na mikataba yote imekamilika kwa sharti kuwa mzabuni awe amekamilisha usambazaji wa mbolea hizo juma la kwanza la mwezi Oktoba, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanunuzi wakubwa wa tumbaku hapa nchini ni kampuni za Alliance One Premium Active Japan Tanzania International leaf, Tanzania Leaf Tobacco Company Limited pamoja na kampuni ndogo ya wazalendo inayoitwa Grand Tobacco Limited. Aidha, Serikali inaendelea kufanya majadiliano ya mwisho na kampuni ya British American Tobacco ili kampuni hiyo ianze kununua Tumbaku kwa wakulima katika msimu wa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imeshafanya mazungumzo na nchi ya China ili iweze kununua Tumbaku kutoka Tanzania ambapo tayari nchi hiyo imeainisha aina ya mbegu za Tumbaku ambazo wanataka zizalishwe nchini ili kukidhi ladha ya Tumbaku wanayohitaji. Mbegu hizo kimsingi hazizalishwi nchini kwa sasa taratibu za kitaalamu na za kisheria zinaendelea ili aina hizo ziweze kuzalishwa nchini na kufungua fursa ya soko la China. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Kutokana na ufinyu wa ardhi na ongezeko la watu kwenye visiwa vya Ukerewe, pamoja na ardhi kutokuwa na rutuba, kumesababisha Kilimo kisicho na tija:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya utafiti wa kisayansi ili kuwashauri wananchi wa Ukerewe aina ya mazao yanayopaswa kulimwa na jinsi ya kutumia eneo dogo la ardhi kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN MOHAMED BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ni kufanya utafiti wa tabaka na afya ya udongo katika kanda zote saba za kiikolojia za kilimo nchini, ikiwemo kanda ya Mwanza. Utafiti huo wa kisayansi unalenga kubaini aina za virutubisho na tabia za udongo katika maeneo mbalimbali pamoja na kubaini mimea na mazao yanayostawi kwenye udongo husika ili kuweza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kiasi, aina na matumizi sahihi ya mbolea za viwandani na asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Ukerewe ambayo wananchi wengi hulima mihogo, mpunga, mtama, mahindi, viazi vitamu na machungwa, utafiti wa awali unaonyesha kwamba, udongo wake una mboji kiasi kidogo cha asilimia 1.3 ukilinganisha na kiwango cha asilimia 2.5 ambacho ndicho kiwango cha mboji katika udongo wenye rutuba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile utafiti umeonyesha kwamba kiwango cha tindikali kwa maana ya pH ni 5.4 ukilinganisha na pH ya 6.6, kiwango ambacho kinafaa kwa mimea ya kufyonza virutubisho kutoka kwenye udongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa kiasi hicho cha tindikali katika maeneo hayo kunaashiria kwamba kuna upungufu wa virutibisho vya nitrogen, phosphorus, potassium, sulphur, calcium na magnesium. Aidha, kulingana na matokeo hayo, inashauriwa kutumia mbolea zenye virutubisho vya nitrogen, potassium, phosphorus, sulphur, calcium na magnesium, ambazo ni pamoja na Minjingu, mazao ya ramila, samadi na CAN, UREA na DAP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sampuli za udogo zimechukuliwa katika kanda na mkoa mbalimbali nchini ukiwemo Mkoa wa Mwanza unaojumuisha Wilaya ya Ukerewe kwa lengo la kubaini viwango vya virutubisho vilivyopo katika sampuli hizo ambapo kwa sasa tathmini ya kina inaendelea kufanyika katika maabara ya TARI, Selian.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kukamilika kwa tathmini hiyo kutasaidia kushauri wakulima kuweka viwango vya mbolea vinavyohitajika kulingana na virutubisho stahiki kwa mazao husika na aina ya mazao na yanayopaswa kulimwa katika maeneo husika.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-

Wilaya ya Malinyi tangu mwaka 2014 mpaka sasa inakabiliwa na mlipuko wa panya wanaoshambulia mbegu za mazao ya Mpunga na Mahindi katika kipindi cha upandaji:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kusambaza sumu maalum ya kuua panya hao?

(b) Kwa kuwa upatikanaji wa sumu ya panya una changamoto nyingi: Je, Serikali ina mkakati gani mbadala katika kukabiliana na panya hao waharibifu wa mazao shambani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kumjibu Mheshimiwa Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, visumbufu vya mazao wakiwemo panya husababisha upotevu wa mazao nchini. Milipuko ya panya imekuwa ikitokea katika Mikoa ya Tanga, Lindi, Mtwara, Mbeya, Songwe, Iringa, Pwani, Shinyanga, Arusha, Kilimanjaro na Morogoro ikiwemo Wilaya ya Malinyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wana wajibu wa kupambana na panya katika mashamba yao wakati wote kwa kutumia mbinu husishi wakiwa wachache. Aidha, inapotokea panya kuongezeka na kufikia zaidi ya 700 kwa ekari, Serikali huratibu ugawaji wa sumu kali kwa wakulima ambayo ina uwezo wa kudhibiti panya kuanzia dakika 45 hivyo kuzuia ufukuaji wa mbegu.

Serikali kwa kutambua athari za sumu kali kwa binadamu na viumbe wengine, wakati wa mlipuko hutumia wataalam wake kutoka Kituo cha Kudhibiti baa la Panya cha Morogoro kusimamia uchanganyaji wa sumu hiyo na chambo na kuwagawia wakulima ili kuhakikisha kuwa wakulima wanapata huduma hiyo kwa wakati. Wizara ya Kilimo inanunua sumu kabla ya msimu wa kilimo kuanza na kwa kushirikiana na TAMISEMI inahamasisha wananchi kuchangia chambo kwa ajili ya kuchanganya kwenye sumu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati mingine ni pamoja na kutoa elimu ya udhibiti wa panya kwa Maafisa Ugani na wakulima, kuhamasisha wakulima kufanya usafi wa mashamba, kutumia mitego ya ndoo ya kuchimba ardhini, kuvuna kwa wakati, kutokulundika mazao shambani na kutumia sumu tulivu aina ya tambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sumu hii ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Wizara ili kupunguza matumizi ya sumu kali ambayo hutumika wakati panya wakiwa wachache. Aidha, nashauri Halmashauri ambazo hupata milipuko ya panya mara kwa mara kutenga bajeti kwa ajili ya kushirikiana na Wizara kufanya udhibiti endelevu wa panya mashambani.
MHE. AJALI R. AKBAR aliuliza:-

Je, Serikali imejiandaa vipi katika kuwapatia wakulima wa Korosho pembejeo za uhakika na kwa wakati?
MHE. AJALI R. AKBAR aliuliza:-
Je, Serikali imejiandaa vipi katika kuwapatia wakulima wa Korosho pembejeo za uhakika na kwa wakati?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Akbar Ajali, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka wa fedha 2012/2013 Serikali kupitia Bodi ya Korosho ilianzisha utaratibu wa ununuzi wa pamoja wa pembejeo za zao la korosho (bulk purchase) kwa lengo la kuhakikisha wakulima wa korosho wanapata pembejeo bora za uhakika na kwa wakati. Aidha, utaratibu huo unatoa unafuu wa bei kwa wakulima, udhibiti wa ubora na upatikanaji wa pembejeo hizo kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya viuatilifu vya zao la korosho katika msimu wa mwaka 2019/2020 ni tani 30,000 za sulphur ya unga na lita 500,000 za viuatilifu vya maji. Kiasi cha viuatilifu kilichopo nchini tangu mwanzoni mwa msimu wa 2019/2020 ni tani 19,000 za sulphur ya unga na lita 270,000 za viuatilifu vya maji. Kiasi hicho kipo katika Bodi ya Korosho Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, TANECU wanazo tani 4,000 za sulphur ya unga, wafanyabiashara binafsi wanazo tani 7,000 za sulphur ya unga na viuatilifu vya maji lita 700,000. Kwa hiyo, jumla ya viuatilifu vilivyopo nchini ni sulphur ya unga tani 30,000 sawa na asilimia 100 ya mahitaji ya viuatilfu vya maji na lita 970,000 sawa na asilimia 194 ya mahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati, Serikali kupitia Bodi ya Korosho inahamasisha Kampuni binafsi kusambaza na kuuza pembejeo hizo kwa bei elekezi ambazo viuatilifu vya maji lita moja ni shilingi 14,500/= kwa viuatilifu aina ya Movil 5, shilingi 27,000/= kwa viuatilifu aina ya Badimenol na shilingi 28,500/= kwa kiuatilifu aina ya Duduba 450 na bei elekezi kwa sulphur ya unga kilo 25 ni shilingi 32,000/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Korosho imeweka utaratibu wa kuwakopesha wakulima pembejeo hizo kupitia vyama vya msingi vya Ushirika (AMCOS) ili kurahisisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati. Aidha, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu (TPRA) inaendelea kukagua ubora wa viutailifu katika maduka na maghala ya wafanyabiashara kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanapata viuatilifu vyenye ubora.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha Sheria ya Vyama vya Ushirika ili kuondoa upungufu uliopo, hususan kwenye upande wa Uanachama na kuipa Serikali nguvu za Kisheria juu ya Vyama vya Ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Msuha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ingawa sote tunaelewa kuwa ushirika ni dhana ya hiari, lakini Serikali ni msimamizi mkuu wa vyama vya ushirika pale ambapo viongozi wake au vyama vyenyewe havitekelezi malengo yaliyokusudiwa na ushirika. Serikali inakiri vyama vinakabiliwa na changamoto za kiutendaji, usimamizi, viongozi kutokuwa waadilifu na upungufu wa kimfumo wa uendeshaji wa baadhi ya Vyama vya Ushirika hapa nchini. Hata hivyo, vipo baadhi ya Vyama vya Ushirika ambavyo vinafanya vizuri, mfano, Chama cha Ushirika cha Chai kilichopo Wilaya ya Mafinga kinachoitwa Chamkonge na Chama cha Ushirika cha Kahama (KACU).

Mheshimiwa Naibu Spika, ushirika ndicho chombo cha kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi kwa kuwaunganisha wakulima ili kuwa na nguvu ya pamoja katika kutoa huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo na kutafuta masoko ya mazao. Aidha, Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2015 – 2020 Ibara ya 22(g) na 86(a) inaelekeza kuifanyia mapitio Sera ya Vyama vya Ushirika na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Ushirika na upatikanaji wa takwimu zitakazosaidia kuandaa mipango na kuleta mageuzi katika sekta ya ushirika na kuimarisha uchumi wa taifa na kuviimarisha vyama vya ushirika kuwa na uwezo wa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ya ndani na nje kwa kuweka mfumo madhubuti wa ukusanyaji, uchambuzi na uenezaji wa taarifa za masoko na kutoa elimu juu ya uongezaji thamani na biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo ipo katika hatua za mwisho kuleta Bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Maendeleo ya Ushirika yatakayoendana na mahitaji ya sasa ambayo yatahusisha mabadiliko ya mfumo na muundo wa uongozi ili kuendana na mahitaji ya teknolojia na kuleta ushindani wa kibiashara.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO (K.n.y. MHE. JOSEPH K. MHAGAMA) aliuliza:-

Miongoni mwa mambo yanayokwamisha ukuaji wa sekta ya kilimo nchini ni pamoja na kukosekana kwa maduka ya pembejeo za kutosha maeneo ya vijijini ambako ndiko walipo wakulima wengi. Miongoni mwa sababu za kukosekana maduka hayo ni gharama kubwa ya kufuzu (certifications) kama vile TOSC 1 – Sh. 100,000; TPRI – Sh.320,000; TFDA - Sh.100,000; leseni na kadhalika na hivyo kufanya gharama kuwa zaidi ya Sh.600,000:-

Je, ni kwa nini Serikali isiondoe gharama hizi ili kutoa hamasa kwa wajasiriamali kupata mafunzo, kufuzu na kuwekeza maduka ya pembejeo ili kusogeza huduma kwa wakulima wadogo na kuharakisha kasi ya ukuaji wa kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo katika hatua za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa kutatua changamoto zinazokabili sekta ya kilimo zikiwemo za biashara ya pembejeo kama zilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara (Blue print). Aidha, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa, pembejeo zenye ubora zinapatikana kwa wakulima kwa urahisi na kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutoa hamasa kwa wajasiriamali wanaohitaji kufungua maduka ya pembejeo vijijini, mwaka 2017/2018, Serikali ilifanya mapitio na kufuta jumla ya tozo tano katika biashara ya mbegu ambazo ni Sh.100,000 ya Cheti cha Usajili na Utambuzi wa Muuzaji; Sh.50,000 Cheti kwa ajili ya aina ya mbegu; Sh.5,000 Cheti cha Majaribio ya Mbegu; Sh.2,500 ada ya nakala ya cheti na Sh. 5,000 ada kwa ajili ya Cheti cha Majaribio.

Mheshimiwa Naibu Spika, viuatilifu ni sumu ambayo huweza kuhatarisha maisha ya binadamu, mifugo na mazingira kama havitatumiwa kwa usahihi. Hivyo muuzaji lazima awe na taaluma maalum ya viuatilifu kwa mujibu wa Sheria Na. 13 ya mwaka 1997 ya Udhibiti wa Visumbufu vya Mimea kama ilivyo kwa maduka ya dawa za binadamu. Aidha, mfanyabiashara anapotaka kufungua duka la viuatilifu hupatiwa mafunzo maalum ya siku sita kwa gharama ya Sh.320,000 kwa mujibu wa Kanuni Na.31, kifungu cha 3 cha Kanuni za Huduma za Afya ya Mimea, hivyo, gharama za mafunzo ya viuatilifu haziwezi kukwepeka.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, ni vigezo vipi vinatumika kumpata Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kumjibu Mheshimiwa Leah Komanya swali lake, kama ifuatavyo:-

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika anapaswa kuwa na sifa kuu mbili ambazo ni kuwa mwanachama wa Chama cha Ushirika; na awe na sifa ya kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushirika. Aidha, sifa nyingine ni sawa na zile za utaratibu wa uteuzi wa Wajumbe wa Bodi ya Ushirika ambazo zimeelezwa katika Kanuni za Maadili, kifungu 134(3) na Jedwali la Pili la Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, pamoja na maelezo hayo, Wizara imebaini upo upungufu katika sheria kuhusu taratibu na sifa za kumpata Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika. Wizara inakamilisha mabadiliko ya Sheria ya Ushirika ili pamoja na mambo mengine kuiboresha na kupata viongozi bora. Mabadiliko hayo yatazingatia kuweka mfumo wa kupata viongozi wenye uaminifu na uadilifu, uwezo wa usimamizi, kiwango cha elimu na teknolojia. Aidha, sheria iliyopo ilikidhi mahitaji na mazingira ya wakati huo ambayo inafanyiwa maboresho ili kuendana na mazingira ya sasa. Mwanachama wa Chama cha Ushirika hatapaswa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika endapo atakuwa na mgongano wa maslahi na Chama cha Ushirika katika kufanya shughuli za biashara zinazofanywa na Chama cha Ushirika husika.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA (K.n.y. MHE. DUNSTAN L. KITANDULA) aliuliza:-

Kata za Kigongoi, Mhinduro na Bosha Wilayani Mkinga zinalima kwa wingi viungo vya chakula kama vile hiliki, mdalasini, pilipili manga na karafuu:-

Je, Serikali ipo tayari kuwawezesha Wakulima hao kupata mbegu bora ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwekeza katika mazao mbalimbali ya kilimo yakiwemo mazao ya viungo ambayo mahitaji yake yanaendelea kuongezeka ndani na nje ya nchi. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeanza kufanya utafiti wa kupata mbegu bora za mazao ya viungo na mazao mengine ya bustani aina ya horticulture ili kuongeza uzalishaji na tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inapitia Sera ya Kilimo ya Mwaka 2013 ambapo sekta ndogo ya mazao ya bustani ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayozingatiwa. Vilevile, kutokana na umuhimu wa mazao hayo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itafanya kikao cha wadau wa mazao hayo tarehe 8 Novemba, 2019 ili kuandaa Mkakati wa Miaka Mitano wa Kuendeleza Mazao ya Bustani. Mkakati huo unalenga kuongeza uzalishaji, ubora wa mazao na kuimarisha mifumo ya masoko ya mazao hayo. Aidha, mkakati huo utakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa unaolenga Taifa letu kufikia uchumi wa kati mwaka 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua hizo, Serikali inaendelea kutoa elimu ya kilimo bora cha mazao ya viungo na mazao mengine; uhifadhi, usindikaji na masoko kwa kushirikiana na Sekta Binafsi kikiwemo Chama cha Wadau wa Mazao ya Viungo Tanzania (Tanzania Spices Association – TASPA), Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) na vyama vingine vya wakulima.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-

Wananchi wa Tarafa ya Amani wamelima zao la pilipili manga kwa wingi, hivi karibuni bei ya zao hilo imeanguka sana kutoka 12,000/= hadi 4,000/= jambo linalowaumiza sana wakulima:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutuma wataalam kubaini ni kwa nini zao hilo limeshuka thamani?

(b) Je Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima hao ili waweze kulima kilimo cha kisasa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la pilipili manga ni miongoni mwa mazao ya bustani yanayoendelea kupewa umuhimu wa kuzalishwa hapa nchini kutokana na mahitaji yake kama kiungo na dawa za binadamu. Kutokana na umuhimu huo, mwezi Machi, 2019, Serikali ilituma wataalam kufanya tathmini ya hali ya uzalishaji wa mazao ya viungo ikiwemo pilipili manga kwenye Halmashauri za Wilaya ya Muheza na Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ilibaini kwamba bei ya pilipili manga imeshuka kutoka shilingi 13,000/= kwa kilo mwaka 2017 hadi shilingi 4,500/= kwa kilo katika mwaka 2019 kutokana na ongezeko la uzalishaji kwa zao hili nchini pamoja na nchi wazalishaji wakubwa ambao ni Vietnam, Indonesia, Sri Lanka, Brazili na India. Aidha, uzalishaji wa ndani uliongezeka kutoka tani 7,800 mwaka 2014/2015 mpaka tani 12,300 mwaka 2017/2018. Aidha, uzalishaji duniani kwa mwaka 2017 ulifikia tani 725,000 ikilinganishwa na mahitaji yanayokadiriwa kuwa tani 400,000 kwa mwaka. Hali hii ilisababisha kuyumba kwa soko la pilipili manga, kushuka kwa bei na kipato cha wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Wadau wa Mazao ya Viungo imepanga kutoa elimu kwa vikundi na Vyama vya Wakulima katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Muheza kuhusu kilimo bora cha mazao ya viungo likiwemo zao la pilipili manga, uhifadhi na kuzingatia viwango vya ubora ili kukidhi mahitaji ya masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeanza hatua za kupitia upya Mkakati wa Kuendeleza Mazao ya Viungo na Mkakati wa Kuendeleza Mazao ya Bustani ili kuendana na mahitaji ya sasa. Katika kutekeleza azma hiyo, tarehe 8 Novemba, 2019 Wizara ya Kilimo itafanya kikao cha cha Wadau wa mazao ya bustani ili kuandaa Dira ya Uendelezaji wa Mazao hayo.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-

Licha ya juhudi kubwa za Serikali kumsaidia Mkulima wa zao la Tumbaku, bado zipo changamoto anazokabiliana nazo ikiwemo kutopata makisio na pembejeo kwa wakati, masoko ya uhakika na wanunuzi wengi wa Tumbaku ili kuleta ushindani wa bei:-

(a) Je, Serikali ina mikakati gani ya kuondoa changamoto hizo ili Mkulima ajiendeleze kiuchumi?

(b) Je, Serikali inashirikianaje na Wakulima wa Urambo ili wawe na Kiwanda cha Tumbaku Urambo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukuwa hatua mbalimbali ili kuondoa changamoto kwenye tasnia ya tumbaku zinazohusiana na baadhi ya wakulima kutopata makisio ya uzalishaji, upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na Masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msimu wa kilimo wa 2019/2020 makisio ya uzalishaji wa tumbaku ya jumla ni kilo milioni 42 yalitolewa mwezi Julai na Kampuni tatu ambazo ni Alliance One, Japan Tobacco International Leaf Services na Premium Active Tanzania Limited. Kutolewa mapema kwa makisio hayo kumewezesha Vyama vya Ushirika vya Wakulima wa Tumbaku kuagiza mbolea kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya mbolea kwa zao la tumbaku nchini ni tani 14,951 za mbolea ya NPK na tani 3,000 za mbolea ya kukuzia. Mbolea yote imeshapokelewa nchini na usambazaji unaendelea kwenye Vyama vya Msingi. Kwa Wilaya ya Urambo hadi kufikia tarehe 31 Oktoba jumla ya tani 1,774 zimesambazwa kati ya mahitaji ya tani 2,160 ya mbolea sawa na asilimia 82.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha tumbaku inayozalishwa hapa nchini inapata soko la uhakika, Serikali inaendelea na mazungumzo ili kufungua soko la tumbaku katika nchi wanachama wa COMESA (Algeria, Misri na Sudan), ambao niwateja wakuu wa tumbaku ya Moshi inayozalishwa nchini. Serikali ilituma ujumbe wa wataalam watano kwenda nchi ya China kujifunza namna bora ya uzalishaji wa tumbaku inayohitajika kwa soko la China.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufutia mafunzo hayo, aina tano za mbegu za tumbaku zimeingizwa nchini kwa ajili ya kufanyiwa majaribio katika maeneo ya uzalishaji wa tumbaku nchini. Tayari majaribio kwenye jumla ya eneo la ekari 10 yanaendelea nchini chini ya usimamimizi wa Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku (TORITA) na Bodi ya Tumbaku. Aidha, Serikali imefanya mazungumzo na Kampuni ya British American Tobacco Ltd ambayo imeonesha nia ya kununua jumla ya kilo milioni nane ya Tumbaku inayozalishwa hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kwamba wawekezaji wa tumbaku waliopo nchini wanaendelea kuongeza uwekezaji, mwezi Septemba, Wizara ya Kilimo ilikutana na Kampuni za wanunuzi wa tumbaku kwa lengo la kujadili na kupata ufumbuzi wa changamoto zilizopo. Kutokana na kikao hicho, ilikubalika kuondoa kesi zilizofunguliwa na Tume ya Ushindani na kufanya makubaliano ya kirafiki nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, matatizo yanayohusiana na sula la kodi ya VAT, mchakato wa kuweza kupitia VAT returns kwa taasisi hizo nne unaendelea; na pale ambapo madai yao ya halali yataonekana, basi Serikali itawalipa kufuatana na utaratibuwa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Urambo imetoa ekari 20 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kusindika tumbaku. Taratibu za umilikishwaji wa ardhi kisheria kwa ajili ya kiwanda zinakamilishwa. Aidha, Serikali itashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya TADB na Chama Kikuu cha Ushirika cha Urambo ili kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinaanzishwa.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italeta Muswada wa kudurusu Sheria ya Tumbaku ya mwaka 2004 Bungeni?
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, zao la tumbaku hapa nchini husimamiwa na Sheria ya Tumbaku Na. 24 ya Mwaka 2001 Sura ya 202 ya Sheria za Tanzania pamoja na Kanuni na Sheria ya Tumbaku ya Mwaka 2012 (Tangazo la Serikali Na. 392 la Mwaka 2012). Kabla ya Sheria Mwaka 2001 zao la tumbaku lilikuwa likisimamiwa na Sheria ya Bodi ya Tumbaku ya Mwaka 1984 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 1997 ambazo zilifutwa kwa Sheria ya Tumbaku Mwaka 2001.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya urasimishaji uanzishaji wa Bodi za mazao, Sheria ya sekta ya Tumbaku ilifanyiwa marekebisho na Bunge Mwaka 2009 kupitia Sheria Na. 20 ya Marekebisho ya Sheria. Pamoja na mambo mengine Sheria ya Tumbaku iliweka tafsiri ya maneno mbalimbali ikiwemo usimamizi, ugharamiaji wa majukumu ya pamoja, muendelezo wa zao kuwa miongoni mwa majukumu ya pamoja, ugharamiaji wa majukumu ya pamoja, mkutano wa wadau wa wakulima, kilimo cha mkataba, majukumu ya udhibiti na tafsiri yake.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya marekebisho ya Sheria za Kanuni za Tumbaku yanaenda sambamba na marekebisho ya Sheria za Bodi za Mazao ambapo Serikali inakusudia kuanzisha Mamlaka ya Mazao ya Kimkakati (Tanzania Strategic Crop Authority- TASCA) ikiwemo zao la Tumbaku. Aidha, Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Bodi za Mazao kwa ajili ya kuanzisha mamlaka hiyo unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni katika Mkutano wa Kumi na Nane, mwezi Januari, 2020.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-

Serikali ya Awamu ya Kwanza ilikuwa na mazao ya kimkakati ya biashara kama Kahawa, Pamba, 9 Pareto na Katani ili kuwa chachu ya kukuza Viwanda:-

Je, Serikali ya Awamu ya Tano ina mkakati gani mahsusi wa kuanzisha uzalishaji wa mazao na kaulimbiu ya Tanzania ya Viwanda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano ni mwendelezo wa Serikali za Awamu ya Kwanza, Pili, Tatu na Nne, ambapo Sekta ya Kilimo ya kama ilivyokuwa katika awamu zilizopita, imeendelea kuwa uti wa mgongo kwa uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, kutoka Serikali za awamu zilizopita hadi sasa vipaumbele vya mazao vimekuwa vikibadilika kulingana na mahitaji na watu na wakati. Aidha, mazao ya kibiashara yameendelea kuwa kipaumbele kwa Serikali za awamu zote. Hata hivyo, fursa za mazao mengine kulingana na mahitaji ya watu zimeendelea kupewa kipaumbele katika kupanga mipango na mikakati ya Sekta ya Kilimo katika Serikali ya Awamu ya Tano. Ongezeko la watu limesababisha mazao ya chakula na mazao ya bustani (horticulture) kuendelea kuwa sehemu muhimu ya mazao ya kibiashara.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuendeleza mipango ya Serikali za Awamu zilizopita, sera mpya ya kilimo ya mwaka 2019 inatarajia kutoa vipaumbele vya Sekta ya Kilimo katika maeneo makuu manne ambayo ni mazao ya mkakati ambayo ni Pamba, Katani, Chai, Korosho na Kahawa, kwa ajili ya malighafi za viwanda. Mazao ya horticulture yenye thamani kubwa (high value commodities), uzalishaji wa mbegu ili kuifanya Tanzania kuwa muuzaji wa mbegu nje (major seed exporter) na mazao ya chakula ambapo lengo ni kuzalisha kibiashara.

Mheshimiwa Spika, aidha, takwimu zinaonesha kuwa kufikia mwaka 2050 mahitaji ya chakula duniani yataongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 ya sasa na hivyo Tanzania inatarajia kutumia fursa ya kijiografia kuzalisha zaidi mazao ya chakula kwa ajili ya biashara.

Mheshimiwa Spika, pamoja na utekelezaji wa mipango hiyo, utekelezaji wa programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo ASDP-II unatarajiwa kuwa chachu ya kukuza Sekta ya Kilimo hasa kwa kuzingatia maeneo manne ya vipaumbele ya programu hiyo ambayo ni usimamizi endelevu wa matumizi ya ardhi na maji, kuongeza tija na faida katika kilimo, upatikanaji wa masoko na kuongeza thamani na kuiwezesha sekta katika uratibu, ufuatiliaji na utathmini. Mkakati ni pamoja na mkakati wa shirikishi na sekta nyingine, hususan sekta za kibiashara na viwanda kwa kuwa sekta hizo haziwezi kukuwa endepo sekta hii ya kilimo hususan agro-processing haitatimiza wajibu wake ipasavyo.
MHE. AMINA N. MAKILAGI Aliuliza:-

Vyama vya Ushirika ndio mkombozi wa wakulima na wafugaji.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha vyama hivyo vinaimarika na kuleta tija kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirika ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020 kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 22 kifungu (f), (g) na (h) kuwa ushirika ndiyo suluhu pekee inayoweza kumkwamua mkulima mdogo kupitia kuungana na kutengeneza chombo imara cha kuwatetea.

Aidha, Wizara inatambua mapungufu yaliyomo sasa katika mfumo wa vyama vya ushirika wa mazao mbalimbali ikiwemo pamba, kahawa, miwa, ufuta ambapo baadhi ya viongozi ambao sio waaminifu wamekuwa wakifanya vitendo visivyofaa ikiwemo ubadhirifu wa rasilimali za ushirika, hali iliyopelekea ushirika kutoaminika miongoni mwa wanachama walio wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Tume imeendelea kuimarisha misingi ya utawala bora na uwajibikaji katika Vyama vya Ushirika kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara mara mbili kwa mwaka na kaguzi za mwisho wa mwaka, kusimamia chaguzi za viongozi na mikutano mikuu ya vyama vya ushirika na kufuatilia utekelezaji wa hoja zinazotokana na matokeo ya ukaguzi na uchunguzi. Aidha, Wizara inafanya tathmini kupitia mfumo mzima wa ushirika kwa kuangalia muundo wake, uendeshaji, usimamizi wa rasilimali zake na fedha za wanachama ili kuleta tija na kufanya uwe wa kibiashara zaidi kuliko udalali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati mingine ni pamoja na kuhamasisha wadau mbalimbali hususan vijana, wanawake na vikundi vyenye mwelekeo wa ushirika kujiunga au kuanzisha vyama vya ushirika ili kuongeza idadi ya wanachama, kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo yaani SACCOS kwenye vyama vya ushirika vya kilimo na masoko yaani AMCOS ili kuwajengea wakulima tabia ya kuweka akiba na kupata mikopo yenye masharti nafuu. Aidha, Wizara kwa sasa inahuisha Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002, kuandaa mkakati wa utekelezaji pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 na Sheria ya Ukaguzi ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 1985 ili kuongeza ufanisi katika ushirika. (Makofi)
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA Aliuliza:-

Kutokana na kuwepo kwa magonjwa sugu yanayoathiri mazao ya ndizi, mihogo, minazi na matunda kama michungwa, miembe na kadhalika kumesababisha wakulima kutozalisha kwa kiwango kinachostahili lakini pia mazao haya kukosa masoko ya uhakika nje ya nchi.

Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha magonjwa haya yanapatiwa suluhisho la haraka ili kilimo kiwe na tija na kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sayaka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli magonjwa sugu ya mazao yanaathiri uzalishaji, tija na ubora wa mazao hivyo kusababisha hasara kwa mkulima. Katika kushughulikia changamoto hiyo, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na usugu wa visumbufu hivyo. Mikakati hiyo ni pamoja na kuimarisha tafiti, kuzalisha na kusambaza kwa wakulima mbegu zenye ukinzani dhidi ya magonjwa mbalimbali. Kwa mfano, mbegu za muhogo aina ya Kiroba, Kizimbani, Kipusa, Chereko, Mkuranga 1 na Mkombozi zinahimili ugonjwa wa Batobato na mchirizi kahawia, miche bora ya migomba aina ya FHIA 17, FHI 23, Nshakara na Nyoya zinahimili ugonjwa wa unyanjano wa zao la migomba. Aidha, mikakati mingine ni kuimarisha huduma za ukaguzi wa mimea na bidhaa za mazao yanayoingizwa nchini ili kuzuia uingizwaji wa visumbufu vamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utafiti wa ndani, kikanda na kimataifa ili kupata mbegu kinzani na viuatilifu katika mazao mbalimbali ikiwemo migomba (Resistant and Tolerant Cultivars). Utafiti wa ugonjwa mnyauko bakteria katika zao la migomba unaendelea katika taasisi za utafiti wa kilimo za Maruku, Uyole, Tengeru pamoja na nchi ya Uganda. Aidha, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kushirikiana na Shirika la Belgium Technical Cooperation (BTC) zimetafiti kuzalisha na kusambaza miche bora ya migomba 6,000,000 katika wilaya za Mkoa wa Kagera na Wilaya za Kasulu na Kankonko Mkoani Kigoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima na maafisa ugani wanaendelea kupatiwa mafunzo ya mbinu za udhibiti wa vusumbufu vya mimea kwenye mazao hayo ili kuongeza uzalishaji na tija. Serikali inawahimiza wakulima kutumia mbegu zenye ukinzani dhidi ya magonjwa.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-

Nchi yetu kwa muda sasa imekumbwa na uhaba mkubwa wa mbegu hasa za mahindi na maharage ambayo ni mazao ya chakula, kwa taarifa zilizopo Wizara ya Kilimo 2018 nchi yetu inazalisha mbegu hizo kwa asilimia zisizozidi 35 tu:-

(a) Je, kuna mkakati gani wa kutatua tatizo hilo ili angalau nchi itosheleze kwa asilimia 70?

(b) Je, ni kwa nini shamba la mbegu la Bugaga lililopo Wilaya ya Kasulu lisiwe kitovu cha kuzalisha mbegu za mahindi na maharage?

(c) Je, ni kwa nini Serikali haiwekezi katika uzalishaji wa mbegu hizo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko Mbunge wa Kasulu Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, upatikanaji na uzalishaji wa mbegu bora ikiwemo za mahindi ngano, maharage, mpunga, soya, alizeti, mtama, ufuta na mbegu za mazao ya bustani kwa msimu 2018/2019 ulifikia tani 49,000, kati ya hizo tani 38,000 sawa na asilimia 78 zilizalishwa nchini, tani 8,361 sawa na asilimia 17 ziliagizwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, mikakati ya Serikali ya kuongeza uzalishaji wa mbegu ni pamoja na kuwezesha Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kuongeza uzalishaji wa mbegu bora katika mashamba ya Mwele, Dabaga, Mbozi, Msimba, Bugaga na Arusha, kutumia Taasisi za Utafiti wa Kilimo kuzalisha mbegu mama, msingi na zilizodhibitiwa ubora na kukodisha maeneo kwa mashamba ya ASA kwa kampuni binafsi za mbegu ili kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za mazao mbalimbali ikiwemo mahindi na maharage.

Mheshimiwa Spika, aidha, mkakati mwingine ni kuongeza eneo la umwagiliaji katika mashamba ya mbegu ya Msimba, Arusha, Dabaga na mashamba ya vituo vya utafiti kutoka hekta 200 hadi 600, kushirikisha taasisi za umma kama Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuzalisha mbegu bora pamoja na vikundi vya wakulima wadogo kuzalisha mbegu za daraja la kuazimiwa ubora.

Mheshimiwa Spika, shamba la mbegu la Bugaga lililopo katika Wilaya ya Kasulu lina ukubwa wa hekta 200. Shamba hilo linamilikiwa na ASA na kwa sasa linatumika kuzalisha mbegu bora za mahindi, maharage na alizeti. Aidha, shamba hilo linatumika kuzalisha miche bora ya mchikichi, miche ya matunda ya machungwa na maembe. Pia Serikali imeanza kuchimba kisima cha maji katika shamba hilo ili kuwezesha uzalishaji wa mbegu kwa kipindi chote cha mwaka. ASA imejenga kitalu nyumba cha kukuzia miche ya michikichi pamoja na kuandaa bustani ya kukuzia miche hiyo ya michikichi na miche ya matunda.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuongeza uzalishaji wa mbegu ambapo Serikali katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 imetenga takribani shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya utafiti wa mbegu kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mbegu – TARI na uzalishaji wa mbegu kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo – ASA kwa ajili ya kuzalisha mbegu kwa njia ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji mara tatu hadi nne zaidi ya sasa.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuzisihi Halmashauri kutotumia maeneo yaliyotengwa kwa tafiti za kilimo kwa shughuli zingine ikiwemo kujenga stendi za mabasi. Aidha, Wizara ya Kilimo itaamua kuyaachia maeneo haya kwa shughuli zingine baada ya kujiridhisha kwamba maeneo haya hayana tija kwa shughuli za kilimo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI) Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapelekea wakulima pembejeo kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kurudi tena ndani ya Bunge. Pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani yake kwangu.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali huratibu mahitaji, upatikanaji, usambazaji, matumizi na kuhakiki wa ubora wa pembejeo za kilimo ili ziweze kufikishwa kwa wakulima kwa wakati zikiwa na ubora stahiki. Katika kutekeleza jukumu hilo, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati. Mikakati hiyo, ni pamoja na kupata mahitaji halisi ya pembejeo za kilimo kutoka kila Mkoa kabla ya msimu wa kilimo kuanza, kuwasiliana na makampuni ya pembejeo na kuyahimiza kusambaza pembejeo hizo mapema kulingana na mahitaji ya kila Mkoa kabla ya msimu wa kilimo.

Mheshimiwa Spika, wakulima kupitia Vyama vyao vya Ushirika wanahimizwa kuainisha na kuwasilisha mahitaji ya pembejeo mapema kwa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) ili waweze kununua mbolea wanazohitaji kwa wakati kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa pamoja ambao katika mwaka 2020, wakulima wa Mikoa kama Iringa, Mbeya waliingiza mbolea moja kwa moja kutoka kiwandani katika nchi za Morocco na China. Aidha, Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya uzalishaji na uagizaji na uthibiti wa mbegu bora na viuatilifu nchini ikiwemo kuhamasisha uzalishaji wa pembejeo hizo ndani ya nchi ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara wa pembejeo kujenga maghala makubwa kwa ajili ya kuhifadhi pembejeo hususan katika maeneo yenye mahitaji makubwa ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati wote. Utekelezaji wa mpango huu ulianza mwaka 2019 ambapo Wadau wa Maendeleo wakiwemo African Fertilizer and Agribusiness Partnership waliwezesha ujenzi wa jumla ya maghala 12 mwaka 2019 yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya tani za mbolea 50,000 katika Mikoa ya Kilimanjaro, Morogoro, Arusha, Iringa, Rukwa, Njombe na Songwe. Aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha pembejeo nchini ili kuongeza upatikanaji wake kwa wakati na bei nafuu kwa wakulima.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza:-

Mashamba yaliyochukuliwa na Vyama vya Ushirika Wilaya ya Hai yameshindwa kuendelezwa huku Wananchi hawana mashamba ya kulima:-

Je, kwa nini Serikali isiyarudishe mashamba hayo kwa Wananchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kumjibu Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Hai ina jumla ya mashamba 17 yanayomilikiwa kihalali na Vyama vya Ushirika. Mashamba hayo yana jumla ya ekari 10,139.5 kati ya hizo ekari 7,769 zimekodishwa kwa wawekezaji na ekari 580 zimepewa taasisi mbalimbali ili kuweza kuongeza mapato katika Vyama vya Ushirika husika na jumla ya ekari 1,789 zinatumika na wanachama wa Vyama vya Ushirika kwa shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Spika, kama kunatokea kusuasua kwa matumizi ya mali za Vyama vya Ushirika ikiwemo mashamba, ni jukumu la Serikali kusaidia Vyama hivyo kuendeleza mali hizo. Mathalani, Aprili, 2020, Tume ya Maendeleo ya Ushirika ilituma Timu ya Wataalam Wilayani Hai kufanya tathmini ya mashamba yote yanayomilikiwa na Vyama vya Ushirika ikiwa ni pamoja na uwekezaji unaofanyika na kutoa ushauri kwa vyama hivyo kuhusu uwekezaji husika.

Mheshimiwa Spika, baada ya tathmini iliyofanyika, mwezi Julai 2020, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika ilitoa Mwongozo kwa Vyama vya Ushirika vinavyomiliki mashamba kuyaendeleza na kufanya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo ili kuwanufaisha wanachama na kwa sasa mashamba yote yanatumika.

Mheshimiwa Spika, aidha, Tume ya Maendeleo ya Ushirika inaendelea kufanya urasimishaji wa mali zote ikiwa ni pamoja na mashamba yanayomilikiwa na Vyama vya Ushirika na kuweka mikakati endelevu ili mali hizo ziweze kutumika kwa manufaa ya wanachama wa ushirika na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Serikali haina mpango wa kuchukua mashamba yanayomilikiwa na Vyama vya Ushirika, bali itaendelea kusimamia na kushauri vyama kuendeleza mashamba hayo kwa kutekeleza mipango ya uwekezaji itakayonufaisha Wanachama wa Vyama vya Ushirika. Aidha, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wanachama au viongozi wa Vyama vya Ushirika watakaobainika kutumia mashamba hayo kwa maslahi binafsi.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI) Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapelekea wakulima pembejeo kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kurudi tena ndani ya Bunge. Pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani yake kwangu.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali huratibu mahitaji, upatikanaji, usambazaji, matumizi na kuhakiki wa ubora wa pembejeo za kilimo ili ziweze kufikishwa kwa wakulima kwa wakati zikiwa na ubora stahiki. Katika kutekeleza jukumu hilo, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati. Mikakati hiyo, ni pamoja na kupata mahitaji halisi ya pembejeo za kilimo kutoka kila Mkoa kabla ya msimu wa kilimo kuanza, kuwasiliana na makampuni ya pembejeo na kuyahimiza kusambaza pembejeo hizo mapema kulingana na mahitaji ya kila Mkoa kabla ya msimu wa kilimo.

Mheshimiwa Spika, wakulima kupitia Vyama vyao vya Ushirika wanahimizwa kuainisha na kuwasilisha mahitaji ya pembejeo mapema kwa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) ili waweze kununua mbolea wanazohitaji kwa wakati kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa pamoja ambao katika mwaka 2020, wakulima wa Mikoa kama Iringa, Mbeya waliingiza mbolea moja kwa moja kutoka kiwandani katika nchi za Morocco na China. Aidha, Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya uzalishaji na uagizaji na uthibiti wa mbegu bora na viuatilifu nchini ikiwemo kuhamasisha uzalishaji wa pembejeo hizo ndani ya nchi ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara wa pembejeo kujenga maghala makubwa kwa ajili ya kuhifadhi pembejeo hususan katika maeneo yenye mahitaji makubwa ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati wote. Utekelezaji wa mpango huu ulianza mwaka 2019 ambapo Wadau wa Maendeleo wakiwemo African Fertilizer and Agribusiness Partnership waliwezesha ujenzi wa jumla ya maghala 12 mwaka 2019 yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya tani za mbolea 50,000 katika Mikoa ya Kilimanjaro, Morogoro, Arusha, Iringa, Rukwa, Njombe na Songwe. Aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha pembejeo nchini ili kuongeza upatikanaji wake kwa wakati na bei nafuu kwa wakulima.
MHE. ORAN M. NJEZA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza uzalishaji wa zao la pareto ambalo mahitaji yake duniani ni makubwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya maua makavu ya pareto duniani ni wastani wa tani 11,000 na yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia mbili hadi kufikia tani 14,000 kwa mwaka ifikapo 2025. Ongezeko hilo linatokana na kuongezeka kwa matumizi ya viuatilifu na bidhaa za tiba kwa kuwa, pyrethrin ni halisi kwa maana ni organic.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa pareto duniani ni Australia, Tanzania, Rwanda na Papua Guinea ambapo Tanzania inazalisha wastani wa tani 2,400. Bei ya pareto inategemea kiwango cha sumu kinachopatikana kwenye pareto na kwa sasa mkulima anapata malipo ya awali ya Sh.2,500 kwa kilo na hadi mwisho wa kukamilika kwa mzunguko wa mauzo inafikia hadi Sh.4,000 kwa kilo kutegemea kiwango cha sumu inayopatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuendelea kuongezeka kwa mahitaji ya pareto duniani malengo ya awali ni kuongeza uzalishaji wake kutoka wastani wa tani 2,400 kwa mwaka hadi kufikia tani 3,200 ifikapo mwaka 2025. Aidha, kufikia malengo hayo Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuanzisha mashamba ya pamoja, kwa maana ya block farming, kwenye halmashauri zinazozalisha pareto ikiwemo Halmsahauri za Mbulu na Mufindi ambazo zimeonesha utayari wa kutenga maeneo ya mashamba ya pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mikakati mingine tumeanzisha mfumo wa uendelezaji wa zao wa kanda (zone) unaowashirikisha wawekezaji na wadau wote kwa mnyororo wa thamani. Ili kudhibiti ulanguzi wa pareto tumeelekeza halmashauri zote zinazolima pareto kuanzisha na kuimarisha vituo rasmi vya ununuzi wa pareto badala ya kuuza pareto majumbani na kwenye maeneo ya maficho. Vilevile katika kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri kulingana na ubora wa pareto, Serikali imeanzisha utaratibu wa kuweka mtaalam wa maabara wa Serikali kutoka TARI Uyole kwa ajili ya kuhakiki viwango vya sumu kiwandani badala ya kutegemea viwango vinavyotumiwa na wanunuzi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kukarabati miundombinu ya Skimu za umwagiliaji za Mnazi – Kwemkwazu na Mng’aro – Kitivo ambazo zimeharibiwa kabisa na mvua?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Jimbo la Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua athari zilizosababishwa na mvua zilizonyesha msimu 2019/2020 na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya umwagiliaji na baadhi ya mito kuhama ambapo takriban skimu 70 za umwagiliaji nchini ziliathirika zikiwemo skimu za Kwemkwazu – Mnazi na Kitivo - Mng’aro katika Jimbo la Mlalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha miundombinu ya umwagiliaji inarejea katika hali ya kawaida, Serikali imeanza kukarabati miundombinu hiyo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo eneo la Ruaha Mbuyuni, Mlenge na Magozi Iringa Vijijini. Aidha, Serikali itaendelea kukarabati miundombinu ya skimu nyingine kwa haraka zikiwemo skimu za Mnazi na Kitivo, Mng’aro katika Jimbo la Mlalo na zitapewa kipaumbele ili kuhakikisha zinakamilika na kurudi katika hali yake ya kawaida na hivyo kuwahudumia wakulima wa maeneo hayo.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST Aliuliza: -

Mfumo wa ununuzi wa kahawa kupitia Vyama vya Ushirika umekuwa mwiba kwa wananchi wa Kyerwa na Karagwe kupitia KDCU:-

(a) Je, kwa nini Serikali isiruhusu watu binafsi kununua kahawa moja kwa moja toka kwa mkulima?

(b) Je, ni lini wakulima wanaodai watalipwa fedha zao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Anatropia kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa ununuzi wa kahawa hapa nchini unawaruhusu wanunuzi binafsi kununua kahawa kutoka kwa wakulima kupitia Vyama vya Ushirika.

Kahawa inayoruhusiwa kwa wanunuzi binafsi ni ile ambayo tayari imepitia utayarishaji wa ngazi ya awali na ikiwa tayari kupelekwa kiwandani au kuuzwa kwenye soko la mnada au soko la moja kwa moja. Pia Vyama vya Ushirika vinaruhusiwa kuingia makubaliano na kampuni binafsi kupitia utaratibu wa kilimo cha mkataba, utaratibu wa wafanyabiashara kwenda moja kwa moja kwa wakulima, maarufu katika Mkoa wa Kagera butura, hauruhusiwi kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera hadi kufikia tarehe 20 Januari, 2021 katika msimu wa 21 jumla ya wanunuzi binafsi saba wamenunua kiasi cha kilo milioni 13 za kahawa maganda kupitia kwenye Vyama vya Ushirika. Kutokana na maboresho hayo ya kuruhusu wanunuzi binafsi na Vyama vya Ushirika wameweza kulipa bei ya Sh.1,200 kwa kilo ya kahawa ya maganda kwa msimu wa 21 ukilinganisha na kiasi cha Sh.1,100 kwa kilo katika msimu uliotangulia wa mwaka 2020. Aidha, Bodi ya Kahawa itatoa vibali mapema kwa wafanyabiashara binafsi ambao wako tayari kununua kahawa katika msimu wa mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya ya Karagwe (KDCU) katika msimu wa kahawa wa mwaka 2020/2021 kimekusanya kahawa maganda kilogramu milioni 40.5 zenye thamani ya shillingi bilioni 48 kutoka katika Vyama vya Msingi 123. Aidha, hadi kufikia tarehe 18 Januari, Chama Kikuu cha Ushirika (KDCU) kilishamaliza malipo yote ya wakulima wa Mkoa wa Kagera.
MHE. NDAISABA G. RUHORO Aliuliza:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza mazingira wezeshi ya kuongeza bei ya zao la kahawa ili wakulima wa zao hili waweze kunufaika kama ambavyo wakulima wa nchi jirani ya Uganda wanavyonufaika?

(b) Utaratibu wa ununuzi wa zao la kahawa unapitia Vyama vya Ushirika, hali inayoonekana kutovutia ushindani. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi ili kuvutia ushindani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ndaisaba, kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua tunazochukua kwa ajili ya kuongeza bei bora ya kahawa kwa wakulima wa Mkoa wa Kagera na Tanzania nzima; moja tumeanza utaratibu wa kuwapatia vifaa kwa ajili ya kuweza kuchakata kahawa yao na badala ya kuuza kahawa ghafi wauze kahawa ambayo imeshaanza kuchakatwa. Aidha, Serikali inafufua na kujenga upya na kuimarisha ushirika wa wakulima kupitia umoja wao waweze kuamua na kupata bei nzuri ya kahawa. Pia, Serikali imeanza kuruhusu mifumo ya direct export ambapo Vyama vya Ushirika na wakulima moja kwa moja wamekuwa wakiuza moja kwa moja kwa wateja. Hatua nyingine ambayo Wizara inachukua sasa hivi tumeanza mchakato wa kutafuta identification logo ambapo kahawa ya Tanzania kokote kule itakaponywewa duniani iweze kutambulika kwamba ni Tanzania produce.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ununuzi wa kahawa hatua ambazo tunachukua kama Wizara ni kwamba Serikali sasa hivi tumeruhusu ushindani wa moja kwa moja wa makampuni binafsi, lakini vile vile yakishindana na Vyama vya Ushirika. Aidha, katika kuhakikisha kama nchi kufikia malengo ambayo tumejiwekea ya mwaka 2025 yaliyoainishwa katika Ilani kufikia tani 300,000 Serikali inatekeleza mkakati wa kuongeza uzalishaji wa miche bora ya kahawa ambapo jumla ya miche bora milioni 55 inazalishwa na kusambazwa kwa wakulima. Aidha, mkakati uliopo ni kuzalisha miche bora milioni 20 ambayo itakuwa ni specific kwa ajili ya organic coffee.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA Aliuliza:-

Serikali imezuia kampuni binafsi kununua kokoa katika Wilaya za Kyela na Rungwe kwa msimu huu na Vyama vya Ushirika havina uwezo wa kununua kokoa hizo kwa wananchi:-

Je, ni lini Serikali itaruhusu tena kampuni binafsi kuendelea kununua kokoa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijazuia kampuni binafsi kununua kokoa kwa wakulima bali imezuia mfumo wa ununuzi wa ulanguzi maarufu kama “njemke” ambao umekua ukimlalia mkulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia mfumo wa Vyama vya Ushirika imekuwa ikikusanya na kuuza mazao hayo kupitia minada ya wazi katika kusaidia kutambua bei za mazao hayo (price discovery). Kwa kutumia utaratibu wa ushirika wakulima waliouza kokoa kwa mfumo wa stakadhi za ghalani bei ya kokoa ilipanda kutoka Sh.3,000 mpaka kufika kiasi cha Sh.5,000 katika msimu wa 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mfumo huo wakulima hupeleka kokoa katika Vyama vya Msingi na kupata asilimia 60 ya bei ya soko. Baada ya mnada kufanyika hupewa kiasi kilichobaki ili kufikia bei ya mnada kwa kuzingatia gharama za usafiri, uhifadhi, ushirika na ushuru. Bei hii iko juu ukilinganisha na bei ya ununuzi binafsi kabla ya ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia faida inayopatikana kupitia kuuza mazao katika ushirika, Serikali haitoruhusu makampuni binafsi kununua kokoa kwa wakulima kwa kununua kuyafuata shambani. Aidha, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaendelea kuimarisha na kujenga uwezo wa Vyama vya Msingi ili viweze kukusanya, kununua kokoa yote kwa wakulima na kuwasaidia wakulima kupata pembejeo sambamba na kuwa na nguvu ya pamoja katika kusimamia bei.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA Aliuliza:-

Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa zao la kokoa haujamnufaisha mkulima:-

Je, ni lini sasa mfumo huo utabadilishwa ili kukidhi lengo la ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Mlaghila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani ni utaratibu unaowezesha biashara kufanyika kwa kutumia bidhaa ambazo zinakuwa zimehifadhiwa katika ghala lililopewa leseni kwa mujibu wa sheria kifungu cha 5(a) cha sheria ya mwaka 2005 na marekebisho ya mwaka 2015.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mfumo huu, mmiliki wa bidhaa anapewa stakabadhi ambayo inathibitisha ubora, uzito, idadi ya vifungashio na umiliki mahsusi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani kwa zao la kokoa umesaidia kuimarisha bei ya zao la kokoa kutoka wastani wa Sh.3,000 kwa kilo katika msimu wa 2017 hadi kufikia Sh.5,011 katika msimu wa 2019/ 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani umesaidia kuimarisha na kuweza kugundua bei halisi na hivyo kumpa mkulima bei nzuri za zao hilo. Pia mfumo huu umeimarisha upatikanaji wa takwimu za uzalishaji na umesaidia ukusanyaji wa ushuru halali kwa Halmashauri za Kyela, Rungwe na Busokelo unaotokana na zao la kokoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika msimu wa 2018/2019 jumla ya tani 7,532 ziliuzwa ambapo jumla ya Sh.33,697,643,289.75 zilipatikana na kulipwa kwa wakulima na Sh.1,033,098,535.20 zilipatikana ikiwa ni ushuru kwa Halmashauri zote tatu. Katika msimu 2019/2020 jumla ya tani 9,483 ziliuzwa na wakulima kupata jumla ya Sh.45.721 na Halmashauri kujipatia jumla ya shilingi bilioni 1.367. Hadi kufikia tarehe 21 Januari 2021, jumla ya kokoa zilizouzwa ni tani 7,000 na kiasi cha shilingi bilioni 33 zimelipwa kwa wakulima na Halmashauri ya Rungwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kusimamia ubora wa kokoa kupitia Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani na hivyo ubora wa zao la kokoa umeongezeka kwa kuwa katika mfumo huu kokoa inaandaliwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na matakwa ya walaji.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA Aliuliza: -

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Tabora kuwa na soko la uhakika la zao la tumbaku?

(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuruhusu soko huria kwa zao hilo ili wakulima wanufaike?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo mfumo wa sasa wa uuzaji wa tumbaku nchini ni wa soko huria ambao unaruhusu kampuni yoyote yenye sifa kuingia mkataba na mkulima kabla ya uzalishaji wa tumbaku ambapo mkulima anakuwa na uhakika wa soko, ubora na bei ya kuuzia tumbaku yake. Wizara inaendelea kuboresha mfumo huo ili uwe mfumo wa uwazi na kuleta mfumo wa flow market competition.

Mheshimiwa Naibu Spika, soko la tumbaku linategemea mahitaji ya dunia. Katika soko la dunia ambapo mahitaji ya tumbaku katika soko la dunia yamekuwa yakishuka kwa wastani wa asilimia sita mpaka saba katikamsimu wa mwaka 2019/2020. Hali hiyo, imetokana na mambo mengine ikiwemo janga la Corona na na kampeni ya kidunia ya kupunguza matumizi ya bidhaa za tumbaku. Lakini msimamo wa Serikali ni kuendelea kulijenga soko la tumbaku nchini na kuongeza transparency katika soko hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hatua zingine ili kuongeza ushindani katika soko la tumbaku. Serikali imeruhusu kampuni nane za Kitanzania ambazo zimeshiriki katika msimu wa 2019/2020 na katika msimu huu wa 2020/2021 kampuni hizi zimetoa jumla ya mikataba yenye uzito wa jumla ya kilo milioni 17 kati ya hizo kilo milioni 9.7 zitatoka kwa wakulima wa Mkoa wa Tabora kutokana na jitihada hizo za kutafuta masoko. Sasa uzalishaji wa tumbaku katika Mkoa wa Tabora utaongezeka kutoka kilo milioni 16 katika msimu wa mwaka 2019/2020 hadi kufika kilo milioni 32 katika msimu wa mwaka 2020/2021.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutafuta soko la uhakika la mazao ya mahindi, maharage na mihogo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kutafutia wakulima masoko ya mazao ya kilimo ikiwemo Serikali yenyewe kununua mahindi na maharage kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, Bodi ya Mazao Mchanganyiko, kufanya makubaliano ya (Government to Government), masoko ya kikanda, pamoja na kuwatafutia wafanyabiashara ambao watanunua mazao ya wakulima moja kwa moja katika masoko ya nchi za nje vilevile kupitia Balozi zetu. Aidha, Serikali imeendelea kuondoa urasimu katika mifumo ya kutoa vibali vya kusafirisha na Serikali haijafunga mipaka ya kuuza mazao nje ya nchi. Kila mfanyabiashara ambaye atapata soko, Wizara ya Kilimo itaendelea kumsaidia kumpatia vibali vinavyostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha 2019/2020 Serikali iliuza jumla ya tani 111,846 za mahindi katika nchi za Afrika Mashariki na kati ya hizo Kenya walinunua jumla ya tani 69,000; Uganda tani 19,000; Zambia tani 900; Rwanda tani 13,000; Burundi tani 7,000 na DRC tani 1150. Aidha, sambamba hilo Serikali bado inandelea kutoa vibali vya kusafirisha mazao nje ya nchi bila ya masharti.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwezi Mei hadi Desemba Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula walinunua jumla ya tani 73,000 za mahindi kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima. Serikali inaendelea kujenga ghala kwa ajili ya kuongeza uwezo wa uhifadhi. Bodi ya Mazao Mchanganyiko imenunua jumla ya tani 24,000 za mahindi kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima. Aidha, Wizara imeomba kibali kutoka Hazina kwa ajili ya kuruhusu taasisi zake ziweze kuchukua fedha katika taasisi za benki na iweze kununua moja kwa moja mazao kutoka kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea kuhamasisha ununuzi wa mazao ya mihogo ambapo kampuni nne za nje ambazo ni Dar Canton, Jielong Holdings, TAEPZ na EPOCH Agricultural Development Company zimenunua jumla ya tani 300 za mihogo mikavu kutoka kwa wakulima. Wizara inaendelea kutoa elimu na kanuni za uzalishaji wa mihogo bora ili iweze kukidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa.
MHE. ASSA N. MAKANIKA Aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwekeza yenyewe katika zao la Mchikichi badala ya kuziachia Halmashauri ili kukabiliana na upungufu wa mafuta nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Makanika, Mbunge wa Jimbo Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2019/2020 hadi mwaka 2020/2021, Serikali imewekeza Jumla ya Sh.5,820,361,798 kwa ajili ya kuendeleza zao la mchikichi ambapo hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2021 jumla ya miche bora ya michikichi 2,244,935 imezalishwa na jumla ya miche 1,456,111 imesambazwa kwa wakulima katika Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Kigoma na miche 788,824 inatarajiwa kusambazwa kwa wakulima katika msimu wa 2020/2021. Aidha, katika mwaka 2021/2022, Serikali imetenga jumla ya Sh.3,158,200,000 kwa ajili ya kuzalisha na kusambaza mbegu na miche ya zao la michikichi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya mafuta ya kula yanakadiriwa kuwa tani 570,000 kwa mwaka. Hata hivyo, uzalishaji wa mafuta ya kula nchini unakadiriwa kufikiwa wastani wa tani 205,000 na kufanya upungufu wa wastani wa tani 365,000 kwa mwaka ambapo hupelekea kama nchi kutumia wastani wa kiasi cha shilingi bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo kwa mazao mengine, Serikali hwekeza katika utafiti, uzalishaji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo, huduma za ugani, udhibiti wa visumbufu vya mazao na utafutaji wa masoko. Aidha, katika utekelezaji wa mikakati hiyo Serikali imekuwa ikishirikiana wdau mbalimbali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa na sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama sehemu ya mkakati wa kujitosheleza kwa mafuta ya kula, mwaka 2018, Serikali iliamua kuanzisha Kituo Maalum cha Utafiti wa Zao la Michikichi cha TARI Kihinga, Mkoani Kigoma ili kuendeleza zao hili kwa ufanisi zaidi. TARI Kihinga ikishirikiana na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), halmashauri na sekta binafsi katika utafiti, uzalishaji wa miche bora ya michikichi na kuisambaza kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya umma na binafsi kuendeleza zao la mchikichi na mazao mengine ya mbegu za ili kuwezesha nchi kujitosheleza kwa mafuta ya kula. Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinashauriwa kuwekeza katika mazao ya kilimo kutokana na mapato yanayotokana na ushuru wa mazao (produce cess) likiwemo zao la michikichi.
MHE. AIDA J. KHENANI Aliuliza:-

Utaratibu unaotumika sasa kuwakopesha matrekta wakulima unawasababishia hasara kwa kuwa wanatozwa riba kubwa: -

Je, kwa nini Serikali isibadili utaratibu huo ili kuleta tija?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya pembejeo na zana za kilimo ikiwemo matrekta kwa wakulima hutolewa kupitia mifumo mbalimbali. Mojawapo ya mifumo hiyo ni kupitia Sekta Binafsi ambapo kampuni zinazofanya biashara ya pembejeo na zana za kilimo hutoa mikopo kwa wakulima mmoja mmoja ama kupitia vikundi. Aidha, mfumo mwingine ni kupitia Taasisi za Serikali kama Mfuko wa Taifa wa Pembejeo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ambazo hutoa mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa wakulima ukilinganisha na kampuni binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwepo kwa mifumo hiyo, baadhi ya wakulima hushindwa kupata mikopo ya pembejeo kutokana na riba kubwa na masharti mengine yanayotolewa na watoa huduma. Kutokana na changamoto hizo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeanza kuwatambua watoa huduma wote wanaotoa mikopo ya pembejeo za kilimo ikiwemo matrekta ili kujua aina ya huduma na mikopo inayotolewa kwa wakulima pamoja na riba wanazotoza. Hatua hiyo itasaidia kutambua changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi ikiwemo kupunguza riba, kuweka utaratibu unaomuwezesha mkulima kurejesha mkopo kulingana na mapato ya mkulima kwa msimu wa kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo zinaendelea kutoa mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa wakulima, ambapo zinatoza mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta kwa wastani wa riba ya asilimia 6 hadi 10 kulingana na aina ya mkopo. Lengo la jitihada hizo ni kuwawezesha wakulima kupata zana bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na tija. Katika mwaka 2020/2021 hadi Februari Mfuko wa Taifa wa Pembejeo umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 959,500,000. Kati ya mikopo hiyo, mikopo ya matrekta makubwa 16 yenye thamani ya shilingi 729,000,000.00 imetolewa. Aidha, Benki ya Maendeleo ya Kilimo imetoa mikopo ya matrekta makubwa 62 yenye thamani ya shilingi bilioni 5.6.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ili kuongeza matumizi ya zana bora za kilimo na kuongeza tija katika kilimo, Serikali imepanga kuhamasisha Sekta Binafsi kuanzisha vituo vya kutoa huduma za kukodisha zana za kilimo kwa lengo la kusogeza huduma za upatikanaji wa zana za kilimo kwa wakulima na kupunguza matumizi ya jembe la mkono kutoka asilimia 53 ya sasa hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima wa Jimbo la Singida Magharibi wanaoteswa na ndege aina ya selengwa kula mazao yao na kuwarudisha nyuma kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini vile vil ekumshukuru Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita kwa kuendelea kuniamini katika nafasi hii ya utumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi kwa niaba ya Waziri wa Kilimo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ndege aina ya selengwa ni moja ya aina ya kasuku wadogo waliopo nchini. Ndege hao wapo kwenye uhifadhi wa dunia kisheria kama ndege walio hatarini kutoweka toka mwaka 1985. Aidha, ndege hao wana tabia ya kuishi kwenye maeneo karibu na vyanzo vya maji na hula mbegu za nafaka zilizokomaa tofauti na ndege aina ya kwelea ambao hula nafaka zikiwa katika hatua ya maziwa. Ndege mmoja ana uweza wa kula kati ya gramu 45 – 60 kwa siku hivyo kundi lenye ndege wastani wa milioni moja linaweza kula kati ya tani 45 hadi 60 ya nafaka kwa siku moja. Kwa ulaji huu idadi ya ndege ya selengwa isipodhibitiwa inaweza kuleta madhara ya kiuchumi kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2004 idadi ya ndege hao imekua ikiongezeka na kuonekana katika maeneo ya mikoa ya Singida, Simiyu, Shinyanga na katika hifadhi za Taifa za Serengeti. Ili kudhibiti, Wizara ya Kilimo imeanza utaratibu wa kupata vibali ili tutumie mitego maalum kuanza kuwadhibiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia taarifa ya uwepo wa ndege aina ya selengwa katika Kata ya Minyuve, Mtunduru, Ihombwe na Makilawa za Jimbo la Singida Magharibi zilizotolewa taarifa na Mheshimiwa Mbunge mwezi Mei, 2020 Wizara ya Kilimo ilipeleka wataalam katika Mkoa wa Singida kwa ajili ya kutambua maeneo yenye mazalia ya ndege hao na kubaini kuwepo kwa mazalia ya ndege aina ya selengwa katika vijiji 12 ambapo yatakuwa yanafanyiwa tathmini kila mwaka kwa ajili ya kuchukua hatua za kuwadhibiti. Vijiji hivyo ni Pohama, Ngimu, Muhanga, Mguli, Mkola na Shahana katika Wilaya ya Singida, Ushora, Uruhu na Mlandala vilivyo katika Wilay aya Iramba na Iyumbu katika Wilaya ya Ikungi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbinu ya kuwadhibiti ndege aina ya selengwa ni tofauti na ile ya kudhibiti ndege aina ya kwelea kwelea wanaodhibitiwa kwa kutumia kiuatilifu kinachonyunyizwa kwa kutumia ndege. Kutokana na uwezo mkubwa wa ndege aina ya selengwa kusikia sauti ya ndege inayonyunyizia kiuatilifu na tabia yake ya kujificha, udhibiti kwa kutumia mitego umeonesha ufanisi zaidi. Hivyo, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Halmashauri pamoja na wakulima, Wizara itapeleka wataalam kuwadhibiti ndege hao katika kipindi cha mwezi Mei na Julai, 2021 kwa kuwa ndicho kipindi ambacho ndege wanatarajiwa kuwa wamejikusanya kwa makundi kutokana na kuvutiwa mazao yaliyokomaa na vyanzo vya maji vilivyotuama katika kipindi cha kiangazi.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya muda mrefu ya Mhe. Rais ya ujenzi wa Bwawa la umwagiliaji kwenye Bonde la Mto Mkomazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali Mheshimiwa Timetheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu ya Umwagiliaji ya Mkomazi ipo katika Kijiji cha Manga Mikocheni, Kata ya Mkomazi, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe. Skimu hiyo ina jumla ya hekta 5,000 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambapo kati ya hizo, hekta 200 zimeendelezwa kwa kujengewa miundombinu ambazo zilifadhiliwa kutokana na fedha za ndani za halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo kupitia Ofisi ya Tume ya Umwagiliaji ilifanya mapitio ya upembuzi yakinifu ya awali na kubaini hitaji la Sh.3,379,000,000 ili kuendeleza bonde hilo. Kati ya fedha hizo Sh.4,041,000,000 ni kwa ajili ya ujenzi wa bwawa na Sh.2,337,999,000 ni za ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji. Ujenzi wa Skimu ya Mkomazi pamoja na bwawa lake upo katika Mpango wa Umwagiliaji wa mwaka 2018 (National Irrigation Master Plan). Mkakati mpana wa Serikali ni kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji ili ifikapo mwaka 2025 tuwe na uwezo wa kumwagilia hekta milioni 1.2 ambapo Skimu ya Mkomazi ni mojawapo ya skimu zitakazotekelezwa katika mkakati huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji wenye lengo kufanya matengenezo ya miundombinu na kujenga miradi mpya. Pia Wizara imeelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuanzia sasa kujenga miradi kwa kutumia wataalam wa ndani kwa utaratibu wa force account kwa Mfumo wa Usanifu na Ujenzi (Design and Build).
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE Aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuliendeleza zao la zabibu Mkoani Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa zabibu kwa sasa ni wastani wa tani 16,000 kwa mwaka ukilinganisha na uwezo uliopo wa kuzalisha zabibu wastani tani 150,000 kwa mwaka. Mahitaji ya mchuzi wa zabibu kwa mwaka ni wastani wa lita milino 15 ambapo uzalishaji wa ndani wa nchi kwa mwaka tunazalisha wastani wa lita milioni 5 na jumla ya lita milioni 10 zinaagizwa kutoka nje zenye thamani ya dola milioni 6. Sasa Serikali imeliingiza zao la zabibu kuwa mingoni mwa mazao ya kimkakati ambayo yamepewa kipaumbele katika kuendelezwa n Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza zao la zabibu Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuhakikisha upatikananaji wa miche bora kupitia TARI na halmashauri za wilaya husika, kuimarisha huduma za ughani katika zao la zabibu, kuongeza upatikanaji wa soko kutoka wastani wa asilimia 65 hadi 85, kuongeza tija ya uzalishaji wa tani 6.25 kwa hekta hadi kufika tani 30 ifikapo mwaka 2025. Vilevile kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika tasnia ya zabibu, kufufua na kuanzisha mashamba makubwa ya zabibu na kutenga na kulinda ardhi kwa ajili ya kilimo cha zabibu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuijengea uwezo TARI kuendelea na utafiti na kuzalisha miche kwa kuongeza bajeti ya utafiti wa mazao ya kilimo ikiwemo zao la zabibu kutoka shilingi bilioni 7.3 mwaka 2021 hadi kufika bilioni 11.63 mwaka 2021/2022.

Aidha, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuwanunulia vitendea kazi Maafisa Ugani ambao hawana vyombo vya usafiri katika Mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeweka mkakati wa kufufua mashamba makubwa ya zabibu ambayo uzalishaji wake unasuasua. Katika kutekeleza adhima hiyo Serikali imefufua shamba la Chinangali II lenye ukubwa ekari 602 lilipo Wilaya ya Chamwino kwa kukarabati bwawa la maji na visima vilivyopo shambani.
MHE. YUSTINA A. RAHHI Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma za ugani Mkoani Manyara kutokana na upungufu wa wataalamu wa kilimo na mifugo katika ngazi ya Kata na Vijiji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kijiji na kata kuwa na afisa ugani mmoja. Hadi sasa mahitaji ya maafisa ugani kulingana na vijiji, mitaa na kata zilizopo ni 2,538; na maafisa ugani waliopo ni 6,704 sawa na asilimia 33 ya mahitaji ya uwiano wa afisa ugani mmoja kwa vijiji vitatu. Aidha, kwa taarifa za mwaka 2020 Mkoa wa Manyara kuna jumla ya maafisa ugani 188 sawa na asilimia 49 ya mahitaji ya maafisa ugani 386. Kwa hali hiyo Mkoa wa Manyara una maafisa ugani zaidi ya wastani wa nchi ulioko sasa.

Mheshimiwa Spika, pia Wizara katika kukabiliana na uhaba wa maafisa ugani tumeanzisha mfumo wa kieletroniki wa Mobile Kilimo uliounganishwa kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa na wizara. Mfumo huo unawezesha wakulima kutumia simu za mkononi kutuma ujumbe mfupi na kuomba ushauri wa kitaalamu na kujibiwa na afisa ugani aliyesajiliwa kwenye mfumo.

Mheshimiwa Spika, hadi kufika mwishoni mwa mwezi Agosti, 2021 maafisa ugani wote na kaya za kilimo zaidi ya milioni 4.5 wamejisajili kwenye mfumo kati ya kaya za kilimo milioni saba. Kutokana na mfumo huo wakulima wengi wamekuwa wakipata ushauri wa huduma za ugani kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI inaendelea kuajiri maafisa ugani kadri vibali vya ajira vinavyopatikana, na wagani hao wapelekwe kwenye maeneo yenye upungufu wa Maafisa Ugan ikiwemo Mkoa wa Manyara.
MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukifufua Kituo cha Utafiti na Uzalishaji Mbegu cha SKU – Suluti cha Shirika la Kilimo Uyole kilichopo Wilayani Namtumbo ambacho kwa sasa hakifanyi kazi na majengo yake yameharibika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Suluti chenye jumla ya hekta 378 ni miongoni mwa vituo vidogo vilivyo chini ya Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI – Uyole) vinavyofanya utafiti na uzalishaji wa mbegu kwa kufuata ikolojia. Kwa muda mrefu kituo hiki kimekuwa kikizalisha chini ya uwezo na hivyo kusababisha maeneo ya mashamba kutotumika kikamilifu na miundombinu mingine ikiwemo nyumba, maghala na baadhi ya mashine kuharibika kwa uchakavu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ikolojia ya Suluti, TARI, Serikali katika Mwaka wa Fedha wa 2021/2022 ina mpango wa kumaliza mgogoro wa ardhi katika eneo la hekta 100 zilizovamiwa, kupeleka kiasi cha fedha shilingi milioni 200 kwa ajili ya kulima mbegu za alizeti, mahindi na soya. Kati ya hizo, milioni 70 zitatumika katika kilimo cha alizeti, milioni 100 zitatumika katika kilimo cha mahindi na milioni 30 zitatumika kwa kilimo cha soya.

Mheshimiwa Spika, vilevile Wizara ina mpango wa kukarabati majengo na kuongeza watumishi kutoka watumishi wawili kwenye kituo hicho na kufikia watumishi wanne. Mpango wa Wizara katika msimu wa Fedha 2021/ 2022 ni kuiwezesha TARI kuongeza uzalishaji wa mbegu mama za mahindi na soya. Vilevile TARI inatarajia kulima hekta 200 za alizeti ambapo mbegu hizo zitawafikia wakulima ili kuzalisha alizeti na kupunguza uhaba wa mafuta ya kula nchini.
MHE. AHMED ALLY SALUM Aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa skimu ya Umwagiliaji iliyopo Kata ya Isholo, Wilayani Shinyanga utakamilika baada ya kusimama tangu mwaka 2014?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum Mbunge wa Jimbo la Solwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo chini ya Programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) kupitia Mpango wa Kuendeleza Kilimo Wilayani (DASIP) ambao ulianza mwaka 2006 na kumalizika Disemba, 2014 umejenga skimu mbalimbali za umwagiliaji ikiwemo mradi wa umwagiliaji Ishololo. Kazi zilizokuwa zimefanyika katika mradi wa Umwagiliaji Isholo ni ujenzi wa tuta la bwawa ambao ulifikia asilimia 26.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mradi huu kuwa miongoni mwa miradi ambayo haikukamilika chini ya mpango tajwa kufuatia fedha iliyotengwa kutotosha kumaliza kazi zote, katika mwaka 2016, baada ya Wizara kupitia upya Mpango Kabambe wa Umwagiliaji, mradi huu umepangwa katika vipaumbele na umebainisha njia nzuri ya kumalizia ujenzi wa skimu ya Ishololo.

Mheshimiwa spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kuendeleza ujenzi wa skimu hii katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP 2020-2025). Aidha, Tume inaendelea kutafuta fedha kutoka Vyanzo mbalimbali vya Fedha ili kukamilisha ujenzi wa mradi huo katika mwaka wa fedha 2021/2022 na hivyo kuwawezesha wakulima wa Ishololo kunufaika na skimu hiyo.
MHE. MARGARET S. SITTA Aliuliza: -

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwezesha kampuni za wazawa ili ziwalipe wakulima mara wanaponunua Tumbaku?

(b) Suala la kupata wanunuzi zaidi wa kununua tumbaku ni la muda mrefu; je kuna mafanikio yaliyopatikana?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mama Margaret Simwanza Sitta Mbunge wa Jimbo la Urambo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu biashara ya tumbaku imekuwa ikiendeshwa bila kampuni za kizawa kushiriki katika biashara ya Tumbaku na kampuni za nje pekee ndizo zilikua zinashiriki katika biashara ya tumbaku. Wakati wa ununuzi wa tumbaku kupitia kampuni za nje ununuzi wa tumbaku ulishuka hadi kufikia tani 42,000 za mkataba na baada ya kampuni za wazawa kuingia katika ununuzi wa uzalishaji umeongeza kufikia tani 68,571 za tumbaku kupitia kilimo cha mkataba. Katika masoko ya tumbaku ya msimu wa kilimo 2020/2021 jumla ya kampuni tisa zinanunua tumbaku ya wakulima zikiwemo kampuni saba za wazawa. Hata hivyo, Kampuni hizo zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya kupata mitaji ya kutosha hali inayosabisha kuchelewa kuwalipa baadhi ya wakulima.

Mheshimiwa Spika, katika kutatua changamoto hiyo, Mwezi Mei, 2021 Wizara ya Kilimo ilikutanisha kampuni za wazawa na taasisi za fedha kwa lengo la kukubaliana masharti nafuu yatakayowezesha kampuni hizo kupata mikopo kwa riba nafuu. Mafanikio ya majadiliano hayo yameanza kupatikana ambapo benki ya CRDB imeridhia kuzikopesha kampuni mbili za Mo Green International na Magefa Growers Limited. Aidha, Serikali inaendelea kushirikiana na kampuni za ununuzi wa tumbaku na taasisi za fedha katika kutatua changamoto ya fedha.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta soko la tumbaku katika nchi mbalimbali hasa nchi za Uarabuni, Afrika na Ulaya. Katika msimu 2020/2021 nchi yetu imefanikiwa kupata masoko mapya kwa kuuza tumbaku kwa majaribio katika nchi ya Romania, Poland na Uturuki. Aidha, sampuli za tumbaku zimetumwa nchini China na Korea Kusini kwa ajili ya masoko hayo. Juhudi za kuirejesha kampuni ya TLTC zinaendelea na mwishoni mwa mwezi Septemba 2021 Wizara itakutana uongozi wa kampuni hiyo.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu kama nchi kuendelea kulea makampuni ya wazawa ili yawe na uwezo wa kununua tumbaku kama makampuni ya kigeni yanavyounganisha na taasisi za fedha.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itahakikisha minada ya zao la Korosho na Ufuta inafanyika kwa wakati mmoja ili kuondoa mporomoko wa bei kwa baadhi ya maeneo yanayolingana kwa misimu sawa ya kuvuna mazao hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally, Mbunge wa Kibiti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatumia mifumo miwili katika minada. Mfumo wa kwanza ni mfumo wa TMX na wa pili ni mfumo wa kutumia sanduku ambao umekuwa ukitumika katika maeneo mengi kwa muda mrefu katika nchi yetu. Serikali itaendelea kutumia mifumo yote hiyo miwili ili kuhakikisha minada inafanyika kwa wakati mmoja kwenye maeneo yenye msimu wa mavuno unaofanana ikiwemo Mkoa wa Pwani ili kuongeza ushindani wa bei na uwazi katika mauzo ya Korosho, Ufuta na mazao mengine.

Mheshimiwa Spika, kuanzia msimu wa 2019/2020 Serikali kupitia Bodi ya Korosho, Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Soko la Bidhaa kwa kushirikiana na Vyama Vikuu vya Ushirika, imeanza kutekeleza mauzo ya Korosho na Ufuta katika minada ya kielektroniki sambamba na mfumo wa uwekaji zabuni kwa njia ya sanduku kwa zao la Korosho.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya mfumo wa kielektroniki yatasaidia kuendesha minada kwa wakati mmoja na kujenga mazingira bora ya ushindani na kuondoa changamoto iliyopo sasa ambapo baadhi ya wanunuzi hulazimika kwenda kwenye minada inayofanyika kwa nyakati tofauti. Ili kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri, Serikali inasimamia suala la ubora na uzalishaji wa tija ili kuhakikisha mazao ya Korosho, Ufuta na mazao mengine yanafikia viwango vya ubora vinavyohitajika sokoni, pamoja na kuimarisha uwazi katika uendeshaji wa minada kwa lengo la kuimarisha ushindani wa bei.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza hatua hizo, Serikali kupitia Bodi ya Korosho ya Tanzania na Soko la Bidhaa, zimeweka utaratibu wa kusajili wanunuzi wa Korosho na Ufuta mapema kabla ya msimu wa mazao kuanza, na kuhakikisha mazao yaliyokusanywa na wakulima kupitia Vyama vya Ushirika yanatangazwa kwa wanunuzi mapema ili kuvutia wanunuzi wengi watakaoshindana kwa bei kulingana na ubora wa mazao yao ili mkulima aweze kuuza mazao yake kwa bei itakayompatia faida.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -

(a) Je, ni lini miradi ya kilimo cha umwagiliaji ya Kyamyorwa na Buhangaza iliyopo Wilaya ya Muleba itakamilika na kuanza kutumika?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza Bonde la Mto Ngono kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini kwa Pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu ya Buhangaza na Skimu ya Kyamyorwa zilizoko Muleba Kusini zote mbili kwa ujumla zina eneo la ekari 700. Wizara ya Kilimo imeshafanya kuendeleza jumla ya ekari 215 na ili kuhakikisha kwamba miradi ya kilimo cha umwagiliaji inakamilika na kuanza kutumika ikiwemo miradi hiyo miwili, Wizara imeweka vipaumbele. Cha kwanza, ni kuhakikisha kwamba miradi yote ambayo ni kiporo iliyokwishajengwa ili kubaini kama kuna upungufu unaosababisha kushuka kwa ufanisi wa uzalishaji na kufanyia tathmini, kuhuisha usanifu uliofanyika awali kwa utaratibu wa kutumia wakandarasi na kuiweka kwenye mfumo wa usanifu na ujenzi kwa maana ya utaratibu wa force account. Kwa hiyo tathmini ya awali inafanyika ili kuweza kuangalia mahitaji halisi ya skimu hizo mbili kuweza kuzikamilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uendelezaji wa bonde la Mto Ngono, katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, Serikali ilifanya upembuzi yakinifu katika bonde hilo lililopo katika Wilaya za Misenyi na Bukoba Vijijini na kubaini eneo lenye hekta 11,700 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuendeleza bonde la Mto Ngono kwa kuanza na ujenzi wa Bwawa la Kalebe lenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo milioni 268 ambazo zitaweza kumwagilia eneo lote la hekta 11,700. Bwawa hilo litatumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, kuzalisha umeme, maji ya mifugo, ufugaji wa samaki na kuzuia mafuriko. Aidha, Andiko la Mradi limewasilishwa kwa wadau wa Maendeleo na majadiliano ya kupata fedha za utekelezaji wa mradi yanaendelea. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:-

Pamoja na Kyerwa kuwa na wakulima wengi wa kahawa bado soko linakuwa gumu.

Je, ni lini Serikali itafikiria kubadilisha mfumo wa ununuzi wa kahawa kwa wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa kahawa umeongezeka kutoka tani 47,000 kwa mwaka 2016/2017 mpaka tani 59,000 kwa mwaka 2019/2020. Aidha, katika msimu wa 2020/2021 lengo la uzalishaji ni tani 70,000 za kahawa safi, ambapo hadi kufikia Machi, 2021 uzalishaji umefikia tani 67,676 sawa na asilimia 96.7 ya lengo. Kati ya hizo, Mkoa wa Kagera pekee unazalisha tani 39,667 ambayo ni sawa na asilimia 58.8 ya uzalishaji wa nchi nzima na Wilaya ya Kyerwa inazalisha tani 19,000 kati ya 39,000 zinazozalishwa na Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2020/2021 mifumo ya masoko inayotumika ni soko la awali, mnada na soko la moja kwa moja. Katika mifumo yote, wakulima hukusanya kahawa yao kupitia vyama vya ushirika. Mifumo hiyo inalenga kuondoa biashara ya kahawa isiyo rasmi inayotumiwa na walanguzi maarufu kwa majina ya butura (Kagera), Njemke au kata kichwa kwenye mikoa mingine ikiwemo Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2020/2021 tani 67,676 zilizozalishwa tayari zimeuzwa kufikia Machi, 2021, tani 20,296 zenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 53.5 sawa na asilimia 30 za mauzo yote zimeuzwa kwa njia ya mnada. Kadhalika, kufikia Machi mwaka huu jumla ya tani 47,108 zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 79.2 sawa na asilimia 69.9 ya kahawa yote iliyouzwa zimeuzwa kwa njia ya minada.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa inaamini mifumo ya masoko inayotumika ni mizuri na itaendelea kuboreshwa kulingana na mahitaji yanavyojitokeza ili kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika na yanayotoa bei nzuri. Hatua zinazoendelea kuchukuliwa kwa sasa ni kuimarisha bei za kahawa kwa kuongeza ubora kuanzia shambani hadi sokoni, kuongeza tija ili wakulima waongeze kipato na kuimarisha vyama vya ushirika. Hatua nyingine ni kuendeleza viwanda vya ndani vya kuongeza thamani na kutafuta masoko mapya ikiwemo kuingia mikataba na nchi au wanunuzi wenye uhitaji mkubwa.
MHE. MARIAM D. MZUZURI aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha wakulima nchini kuwekeza katika kilimo cha mazao ya alizeti, michikichi na karanga ili kuokoa kiasi cha fedha zinazotumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Ditopile Mzuzuri, mkulima na mjasiriamali katika sekta ya kilimo kuwa Serikali inaona umuhimu wa kuwekeza kwenye mazao ya kuzalisha mafuta ambapo uwekezaji huo unatekelezwa chini ya mikakati ya kutatua changamoto katika sekta ya uzalishaji wa mafuta kwa kushirikisha Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu - Wizara ya Viwanda na Biashara. Mikakati hiyo inalenga kutatua changamoto ya uzalishaji wa mbegu za mafuta ili kujitosheleza kwa mahitaji ya ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2020/ 2021 Serikali imewekeza jumla ya shilingi 5,820,361,798 kwa ajili ya kuendeleza zao la chikichi ambapo kufikia tarehe 31 Januari jumla ya miche bora ya michikichi 2,244,935 imezalishwa na kusambazwa kwa wakulima. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga jumla ya shilingi 3,158,200,000 kwa ajili ya kuzalisha na kusambaza mbegu na miche ya zao la michikichi.

Mheshimiwa Spika, Katika kuhakikisha uzalishaji wa mbegu za alizeti unaongezeka katika mwaka wa fedha 2020/ 2021 Serikali imeiwezesha taasisi ya ASA jumla ya bilioni tatu kwa ajili ya kuzalisha mbegu za alizeti. Vilevile, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imepanga kuiwezesha ASA shilingi bilioni 10.6 ili kuzalisha tani 5,000 za mbegu ya alizeti kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mbegu za mafuta

Mheshimiwa Spika, katika kupunguza gharama za kilimo kwa mkulima Wizara imeanzisha miradi ya block farming katika mikoa ya uzalishaji mbegu za mafuta ikiwemo alizeti michikichi na pamba ambapo katika mwaka ujao wa fedha Serikali tutatoa kipaumbele kwa kilimo cha uzalishaji mbegu kwa mfumo wa block farming kwenye baadhi ya mikoa kwa ajili ya uzalishaji mbegu za alizeti, pamba na michikichi. Mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanakadiriwa kufika tani 570,000 kwa mwaka. Aidha, uzalishaji wa mafuta ya kula nchini unakadiriwa kufikiwa wastani wa tani 205,000 na kufanya upungufu wa wastani wa tani 365,000 kwa mwaka, ambapo husababisha nchi kutumia shilingi bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi kwa mwaka.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuliingiza zao la parachichi katika mazao ya kimkakati kutokana na zao hilo kuiingizia nchi fedha za kigeni?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, parachichi ni miongoni mwa mazao ya bustani ambayo yanapewa kipaumbele katika Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kutokana na umuhimu wake katika kuongeza kipato na lishe kwa wakulima na jamii kwa ujumla. Zao hilo ni miongoni mwa mazao yanayokua kwa kasi na limeonesha mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Spika, aidha, mauzo ya parachichi nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 3,279 mwaka 2015 hadi tani 9,000 mwaka 2018. Mauzo hayo yameliingizia Taifa kiasi cha Dola za Marekani milioni 8.5 kutokana na masoko ya nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza na Kenya.

Mheshimiwa Spika, zao la parachichi limeingizwa tayari kuwa miongoni mwa mazao ya kimkakati na wizara ipo katika hatua za awali za mapendekezo ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mazao ya Bustani (Hotculture Development Authority) ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia mazao ya bustani likiwemo zao la parachichi ili kuongeza tija na kukidhi mahitaji ya soko la ndani, kikanda na Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inaendelea kukamilisha mkakati wa kuendeleza tasnia ya mazao ya bustani ya mwaka 2021 – 2030 utakaotumika kama dira ya kuwekeza katika Sekta ya Horticulture itakayojumuisha zao la parachichi. Mkakati huo umehusisha wadau wote muhimu kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya horticulture.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha gharama za usafirishaji wa mazao ya horticulture ikiwemo parachichi zinapungua, Serikali ipo katika hatua za awali kuanzisha Kituo cha Huduma za Biashara ya Mazao ya Kilimo (Agricultural Logistics Hub) kwenye eneo la ekari 20 katika ukanda maalum wa uwekezaji (Export Processing Zone – EPZ) Kurasini, Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na sekta binafsi, TAHA kwa maana ya TPSF, TAHA na Wizara ya Viwanda na Biashara, kituo hicho kitakuwa ni kituo cha huduma ya pamoja (One Stop Centre) chenye wataalam na miundombinu ya mnyororo wa baridi (cold chain) wa kuhifadhi mazao kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa bei nafuu tofauti na hali ilivyo sasa ambapo baadhi ya mazao hulazimika kusafirishwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Nairobi ama Bandari ya Mombasa kwa kuwa na mindombinu thabiti.

Mheshimiwa Spika, kutekelezwa kwa mkakati wa kuendeleza mazao ya bustani na kuanzishwa kwa mamlaka ya kusimamia mazao hayo likiwemo zao la parachichi kutaongeza tija na mchango mkubwa katika pato la mkulima na Taifa.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kufufua zao la Kahawa nchini ambalo ni moja ya mazao ya kimkakati?

(b) Je, ni lini Makampuni binafsi yataruhusiwa kununua Kahawa kwa Wakulima moja kwa moja bila kupitia Vyama vya Ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inaendelea kutekeleza Mkakati wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya Zao la Kahawa wenye lengo la kuongeza tija na ubora wa kahawa nchini. Utekelezaji wa mkakati huo umewezesha kuongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 43,872 za kahawa za msimu wa mwaka 2017/2018 hadi tani 67,000 msimu wa 2020/2021. Aidha, wastani wa bei kwa wakulima wa kahawa kavu aina ya Arabika umeongezeka kutoka shilingi 3,500 kwa mwaka 2019/2020 hadi shilingi 4,000 kwa mwaka 2020/2021 na bei ya kahawa ya maganda ya Robusta imeongezeka kutoka wastani wa shilingi 1,100 kwa mwaka 2019 hadi shilingi 1,200 mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mkakati wa Wizara ni kuhakikisha kwamba tunaongeza tija; uwekezaji mkubwa katika Taasisi yetu ya Utafiti ya TaCRI; mfumo wa masoko; kuboresha mfumo wa ushirika, uzalishaji na ugawaji wa miche. Mpaka sasa Wizara imeshaanza mradi wa uzalishaji wa miche milioni 5.5 kwa ajili ya kuendelea kugawa bure kwa wakulima wa kahawa nchini. Vilevile Serikali imeipatia Taasisi ya TaCRI jumla ya shilingi milioni 300 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kuhusu mfumo wa wanunuzi wa kahawa kupitia Vyama vya Ushirika umelenga kuongeza ushindani katika soko la awali kulingana na ubora wa kahawa na pia kuwawezesha wakulima kuwa na nguvu ya pamoja ya kushauriana ili kupata bei nzuri na kunufaika na kilimo, hivyo kuondokana na walanguzi ambao wamekuwa wakiwalaghai baadhi ya wakulima. Hivyo, kampuni binafsi na wenye viwanda vya kahawa wanaruhusiwa kununua kahawa kutoka kwa wakulima kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi na Vyama Vikuu.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha uzalishaji wa zao la Vanila nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la vanila hulimwa kwa wingi katika Mikoa ya Kagera, Morogoro, Tanga, Mbeya, Arusha na Kilimanjaro ambapo uzalishaji umekuwa ukiongezeka kutoka tani 229 mwaka 2015 hadi kufikia tani 1,949 mwaka 2020. Katika kuhamasisha uzalishaji wa zao la hilo, Wizara ya kilimo imefanya tathmini ya kutambua wadau na masoko ya vanila ndani na nje ya nchi na kuzifahamu changamoto zinazokabili zao hilo ikiwemo upatikanaji wa mbegu bora. Wadau wakubwa wa vanila ni pamoja na Shirika la Msalaba Mwekundu Umoja wa Wazalishaji wa Viungo (Tanzania Spice Producer Association), Chama cha Wakulima wa Viungo vya Amani, Chama cha Maendeleo ya Wakulima (MAYAWA), Taasisi ya Kilimo Endelevu SAT, Ushirika wa Wazalishaji Viungo wa Mtamba lakini Kiwanda cha Natural Extract Limited kilichopo Mkoani Kilimanjaro na Chama cha Wazalishaji wa Vanila Mkoani Kilimanjaro.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali itaongeza upatikanaji wa miche bora ya vanila nchini kwa kuhamasisha wazalishaji wa ndani na kuandaa utaratibu wa kuingiza miche bora kutoka nje ya nchi. Pia Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhamasisha uendelezaji wa zao la vanila na mazao mengine ya viungo kwa kutoa mbinu bora za kilimo cha vanila ili kujadili maendeleo ya tasnia ya viungo. Hadi kufikia Machi, 2021 jumla ya wakulima 1,387 wa zao la vanila wamepatiwa mafunzo ya kanuni na mbinu bora za uzalishaji. Aidha, katika kuimarisha huduma za ugani kwa zao hilo, Maafisa Ugani 20 wamepatiwa mafunzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Utafiti cha TARI – Tengeru kinafanya utafiti wa mazao ya bustani likiwemo zao la vanila na viungo. Kituo hicho kimeanza ukusanyaji wa vinasaba vya mazao likiwemo zao la vanila kwa ajili ya kufanya utafiti wa aina bora za vanila ili kuboresha uzalishaji. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha International Trade Centre imeandaa mfumo maalum wa kutambulisha mazao ya viungo yanayozalishwa Tanzania katika masoko ya nje. Vilevile, Serikali itaendelea kusimamia mikakati yote inayolenga kuongeza uzalishaji tija na kuboresha mazigira ya biashara ya zao la vanila na mazao ya viungo.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mabwawa makubwa na Skimu za Umwagiliaji za Choma Chankola, Ziba na Simbo ambazo zimefanyiwa upembuzi yakinifu kwa zaidi ya miaka sita sasa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Choma Chankola lipo katika Kijiji cha Choma Chankola, Kata ya Choma, Wilaya ya Igunga. Usanifu wa bwawa hili umeonyesha kuwa lina uwezo wa kutunza maji mita za ujazo 6,825,757 na maji haya yaliyovunwa yanaweza kumwagilia hekta 400 za mpunga. Hata hivyo, bwawa la Choma pamoja na mabonde yote ya Ziba yanayofaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, yameingizwa kwenye Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa mwaka 2018 kwa ajili ya utekelezaji wake. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Bwawa la Simbo lililopo katika Kata ya Simbo, Wilaya ya Igunga usanifu wake umekamilika. Bwawa hili lina uwezo wa kutunza maji lita 15,228,000 na maji yaliyovunwa yanaweza kumwagilia hekta 1,000 za mpunga. Bwawa hili pia lipo katika Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa Mwaka 2018 kwa ajili ya utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, andiko la Programu ya Ujenzi wa Mabwawa katika Mikoa Kame ya Tanzania (Participatory Dams Development Programme in Semi-Arid Areas of Tanzania) limekamiliika ambapo mabwawa haya ni miongoni mwa mabwawa 88 yaliyopangwa kujengwa katika programu hiyo. Andiko limeshawasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya kutafutiwa fedha na utekelezaji wake.
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA aliuliza:-

Je, Serikali imejipanga vipi kutafuta Soko la uhakika la zao la mahindi kwa wakulima wa Mikoa ya Kusini hususan Mkoa wa Njombe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo inatekeleza mikakati mbalimbali ikishirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Viwanda na Biashara katika kuwatafutia wakulima masoko ya mazao ya kilimo ikiwemo kuwaunganisha wakulima wa mahindi na wasindikaji wa mahindi kwa ajili ya unga na chakula cha mifugo, kuondoa vikwazo na kupunguza gharama za biashara na kupunguza ukiritimba na kuanza kutoa vibali vya kuuza mazao nje bila ya kuwa- charge. Vilevile, Wizara ipo katika hatua za awali kuhakikisha kwamba inaanzisha Idara ya Masoko na sekta binafsi; Serikali kununua mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Mazao mchanganyiko na Serikali kufanya makubaliano ya kibiashara baina ya Tanzania na nchi zenye fursa ya masoko zikiwemo nchi za DRC, Kenya, Sudan ya Kusini, Rwanda, Burundi na kutumia njia mbadala kuhakikisha wasafirishaji wanapata huduma za usafirishaji ikiwemo vibali kiurahisi. Pia Mkoa wa Njombe kuunganishwa na wanunuzi ikiwemo Kampuni ya Silverland ambayo katika msimu wa 2020/2021 imenunua jumla ya wastani wa tani 40,000 za mahindi.

Mheshimiwa Spika, kupitia jitihada hizo, kipindi cha mwezi Julai 2020 hadi Desemba 2020 wakulima na wafanyabiashara wameuza tani 89,725 za mahindi nchini Kenya, Burundi na DRC. Bodi ya Mazao na Nafaka Mchanganyiko imenunua jumla ya tani 24,000 za mahindi kutoka kwa wakulima. Pia, kufikia mwezi Mei, 2020, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) amenunua jumla ya tani 73,000 za mahindi zenye thamani ya shilingi bilioni 48 kutoka kwa wakulima na vikundi mbalimbali kwenye kanda zote nane. Kati ya hizo, jumla ya tani 11,000 za mahindi zimenunuliwa kutoka Kanda ya Makambako inayojumuisha Mkoa wa Njombe ambao ulizalisha tani 332,000 za mahindi katika mwaka wa 2019/2020.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2021, Wizara inaangalia uwezekano wa kuwa na maghala katika nchi zenye masoko makubwa ya mazao ikiwemo nchi za DRC na South Sudan kwa lengo la kuhifadhi na kutangaza mazao ya kilimo na hivyo kuyauza kwa urahisi katika nchi hizo.
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji katika Mikoa ya Kigoma, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma na Morogoro ili kuongeza mazao ya kilimo yatakayosafirishwa kupitia SGR?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambart Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kutekeleza na kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji katika mikoa inayopitiwa na reli ya kisasa ya mwendokasi kuanzia Mkoa wa Pwani na kufanya kutathmini maeneo yote yenye sifa ya kufanya uzalishaji kwa kutumia njia ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 na 2020/2021 eneo linalomwagiliwa limeongezeka hadi kufikia hekta 695,045 na hivyo kufikia asilimia 58 ya lengo la kufikia hekta milioni 1.2 ifikapo 2025. Ongezeko hilo limetokana na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu za umwagiliaji za Kilangali Seed Farm (Kilosa) kupitia mradi wa ERPP na akimu 13 za SSIDP kupitia mradi wa SSIDP. Serikali inakamilisha ujenzi wa awali kwa skimu za umwagiliaji katika Mikoa ya Shinyanga, Tabora, Kigoma, Singida, Morogoro, Dodoma na Kagera. Aidha, Serikali itaendelea na ukamilishaji wa skimu hizo hili ziweze kutumiwa ipasavyo na wakulima.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inakamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa Mradi mkubwa wa Umwagiliaji katika Mkoa wa Kigoma wenye hekta 3,000 ambapo ujenzi wa mradi huo wa Luiche unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Aidha, miradi mingine ya umwagiliaji inayopitiwa na reli ya SGR itakayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2021 ni pamoja na Skimu za Ngomai (Kongwa), Idudumo (Tabora) na Msufini pamoja na Shamba la Mbegu la Msimba (Morogoro).
MHE. ALLY A. MLAGHILA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia Mto Songwe, Kiwira, Mbaka na Lufilyo ili kuongeza uzalishaji wa mpunga na kukuza uchumi wa nchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Mlaghila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji pamoja na fursa zilizopo katika Bonde la Mto Songwe pamoja na mabonde ya Mito Kiwira, Mbaka na Lufilyo, Serikali ilitekeleza miradi mbalimbali katika mabonde hayo. Katika Wilaya ya Kyela, kupitia Mpango wa Kilimo awamu ya kwanza (ASDP I), Serikali ilijenga Maghala mawili ya kuhifadhia mpunga katika skimu za Makwale na Ngana. Aidha, wakulima walipata mafunzo ya uendeshaji wa skimu, kilimo chenye tija na masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imekamilisha ujenzi wa Skimu ya Mbaka iliyogharimu Sh.358,877,336.48. Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na Uchimbaji wa mfereji mkuu mita 1,900; Ujenzi wa tuta la bwawa (formation of embarkment) urefu wa mita 450 na usakafiaji wa mfereji mkuu kwa zege mita 1,355.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina Mpango wa kuendeleza hekta 3,005 za umwagiliaji katika Bonde la Mto Songwe kwa ubia baina ya Serikali ya Tanzania na Malawi chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bonde la Mto Songwe. Aidha, Serikali itaendelea na juhudi za kutafuta fedha ili kuendelea na uendelezaji wa mabonde hayo pamoja na mabonde mengine nchini kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -

Ununuzi wa zao la pamba utaanza mwezi Mei au Julai: -

Je, Serikali inatarajia kuwalipa wakulima watakaouza pamba kwa utaratibu gani kabla ya kuanza kwa ununuzi wa zao hilo ifikapo Mwezi Mei – Julai, 2021?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu wakulima wa pamba wamekuwa wakilipwa fedha za mauzo ya pamba kwa utaratibu wa fedha taslimu kwa maana ya hard cash kupitia Vyama vya Ushirika. Hata hivyo, mfumo huo umekuwa ukisababisha changamoto kwa wakulima ikiwemo wizi na ubadhirifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya viongozi wa AMCOS kwa kutoroka na fedha za wakulima hasa katika msimu ambao ipo changamoto ya uuzaji wa ununuzi mfano msimu wa 2019/2020. Katika kutatua changamoto hizo, Serikali katika msimu wa 2020/2021, imeratibu kwa majaribio mfumo wa kulipa wakulima kupitia akaunti za benki na simu za mkononi (mobile money).

Mheshimiwa Spika, mfumo huo umeleta mafanikio ambapo baadhi ya benki ikiwemo CRDB, NMB, Azania na NBC zimewezesha wakulima kufungua akaunti za Benki bila malipo na baadhi ya akaunti za wakulima kufutiwa tozo ikiwemo tozo za withdraw. Aidha, pamoja na mafanikio hayo, kumekuwepo na changamoto katika matumizi ya mfumo huo kutokana na kukosekana kwa matawi ya benki katika baadhi ya maeneo yaliyo karibu na wakulima. Taarifa za Benki na majina ya wakulima kutofautiana na hivyo kuchangia kukwamisha malipo ya wakulima kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, katika kutafuta suluhu ya changamoto hizo msimu wa 2021/2022 fedha za wakulima zitalipwa katika kaunti za AMCOS, kwa maeneo ambayo hayana changamoto za ukosefu wa ukaribu wa matawi ya benki. Aidha, Serikali itaruhusu kutumia mifumo yote ya malipo ikiwemo mfumo wa malipo wa fedha taslim hususan pale ambapo mazingira hayaruhusu kufanya malipo kupitia benki na mitandao ya simu. Aidha, mfumo wa malipo ya fedha taslim utasimamiwa na AMCOS na mnunuzi ili kudhibiti ubadhilifu wowote unaoweza kujitokeza hususan pale ambapo malipo yanapokuwa zaidi ya shilingi 10,000.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-

(a) Je, ni nini kinasababisha Tanzania kutojitosheleza kwa mafuta ya kula?

(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha mikoa yenye ardhi ya kutosha ya kuzalisha zao la alizeti hususan Mkoa wa Mara inatambuliwa rasmi na kupewa mahitaji yote ya mbegu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniface Mwita Getere, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanakadiriwa kuwa wastani wa tani 570,000 kwa mwaka. Hata hivyo, uzalishaji wa mafuta ya kula nchini unakadiriwa kufika wastani wa tani 205,000 na kufanya upungufu wa wastani wa tani 365,000 kwa mwaka, ambapo husababisha nchi kutumia wastani wa Shilingi bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje kwa mwaka.

Aidha, uhaba wa mafuta ya kula nchini umetokana na uzalishaji mdogo wa mazao ya mbegu za mafuta yakiwemo alizeti, michikichi, pamba unachangiwa na matumizi hafifu ya teknolojia ikiwemo mbegu bora na usindikaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha mazao ya mafuta ikiwemo alizeti, michikichi na pamba katika mikoa yote yenye ardhi na hali ya hewa inayofaa kwa kilimo cha mazao hayo. Aidha, Serikali imeweka msukumo wa kuimarisha huduma za ugani nchini ambapo katika bajeti ya 2021/2022, Wizara imepanga kuwezesha Maafisa Ugani 680 wa Mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu pikipiki kwa ajili ya ufuatiliaji, kupatiwa mafunzo rejea na kuwezesha wagani hao kuanzisha mashamba ya mfano ya alizeti na pamba pamoja na kuanzisha mashamba ya (Block Farm) ambayo tunafanya pamoja na Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Lengo la uwezeshaji huo ni kuleta ufanisi katika kutoa huduma za ugani ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itawekeza jumla ya bilioni 10 kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za mazao yakiwemo ya mbegu za mafuta kwa kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji na kupanua mashamba ya mbegu ya Wakala wa Serikali (ASA), mbegu hizo zitasambaza kwa wakulima kwa Mikoa yote itakayozalisha mazao hayo ikiwemo Mkoa wa Mara kupitia ASA na wasambazaji binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuingia kwenye uzalishaji wa mbegu na ipo tayari kufanya majadiliano na makampuni au watu wenye nia ya kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbegu ili kuweka utaratibu wa kupunguza gharama za uzalishaji wa mbegu kwa tija.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la Kahawa limekuwa likilimwa kwa wingi katika Jimbo la Hai lakini zao hili kwa sasa limekosa tija.

Je, Serikali haioni kuwa ni wakati sahihi wa kufufua zao hilo katika Jimbo la Hai?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo, Mbunge wa Hai kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza kuchukua hatua za kufufua zao la Kahawa katika mkoa wa Kilimanjaro likiwemo Jimbo la Hai. Hatua hizo zinatokana na kushuka kwa uzalishaji kutoka tani 3,486 mwaka 2014/2015 hadi kufikia tani 1,428 mwaka 2020/2021 sawa na asilimia 59. Kushuka huko kumechangiwa na baadhi ya wakulima kuacha kuyahudumia mashamba kulikosababishwa na kuzorota uliokuwa muhimili wa uzalishaji wa kahawa Mkoani Kilimanjaro. Sababu nyingine iliyochangia ni mabadiliko ya tabia nchi yaliyopelekea ukame na kukosekana kwa maji ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kufufua zao la kahawa Mkoani Kilimanjaro likiwemo Jimbo la Hai kwa kufanya mambo yafuatayo:-

(i) Kukifufua na kukijenga upya Chama Kikuu cha Ushirika wa Kahawa Mkoa wa Kilimanjaro KNCU kwa kurejesha mali zilizouzwa kiholela na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha ubadhilifu wa mali za Ushirika;

(ii) Kuimarisha Taasisi ya Utafiti wa kahawa Tanzania (TaCRI) kwa kuipa rasilimali ili itekeleze majukumu yake kikamilifu ya utafiti wa zao la kahawa na uzalishaji wa miche bora ya Kahawa;

(iii) Kuhamasisha upandaji wa miche bora ya kahawa kwa kuwauzia wakulima kwa bei ndogo ya shilingi 100 ambapo jumla ya miche 1,203,300 imesambazwa kwa wakulima 3,270 na miche 810,000 imesambazwa katika Wilaya ya Hai;

(iv) Kumaliza migogoro ya kimkataba iliyopo kati ya Vyama vya Ushirika na Wawekezaji katika mashamba 17 ya kahawa; na

(v) Kufufua na kuimarisha viwanda 12 vya kati vya kuchakata kahawa CPU vinavyomilikiwa na wakulima wadogo, Viwanda vyote hivyo vipo katika Wilayani Hai.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hizi zinazochukuliwa na Serikali zitachochea ufufuaji wa zao la kahawa Mkoani Kilimanjaro ikiwemo Wilaya ya Hai na maeneo mengine nchini.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa Wakulima wa Kahawa ndani ya muda mfupi pale wanapomaliza kupima Kahawa zao kwenye AMCOS?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate Mbunge wa Kyerwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto za mfumo wa soko Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kurejesha ununuzi wa mazao matano ya kimkakati kupitia vyama vya ushirika ili kunufaisha wakulima, wanunuzi na wafanyabiashara na Serikali kwa ujumla. Uamuzi huu ulikuwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020 iliyoelezwa katika sura ya 2 Ibara ya 22 kuviimarisha na kuviwezesha vyama vya Ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mfumo wa soko la Kahawa Serikali hainunui kahawa bali imeweka mfumo wezeshi kwa wakulima kuuza mazao yao kupitia mfumo wa Ushirika ambapo wanunuzi binafsi wameruhusiwa kununua kahawa kupitia vyama vya Ushirika, kwa maana ya vyama vya msingi mwongozo wa bodi ya kahawa unaelekeza kuwa Wakulima walipwe ndani ya siku tatu pindi AMCOS inapofanya makubaliano ya Kampuni yenye leseni ya wanunuzi binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha vyama vya Ushirika vimeshauriwa kutafuta masoko mapema ili kuwezesha kupata fedha kutoka taasisi za TADB au wanunuzi wanaoingia nao mkataba ili kuwezesha kulipa wakulima pindi wanapoleta kahawa kwenye vyama vyao vya msingi.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaandaa wakulima wadogo wa miwa (outgrowers) wa Bagamoyo ili kuwa na uzalishaji mkubwa na wenye tija?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo kimejiwekea mipango inayotekelezwa kwa awamu. Awamu ya Kwanza, kiwanda kinatarajia kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika hekta 2,050 za mashamba yake. Hadi kufika mwezi Desemba, 2020 jumla ya hekta 1,700 zimelimwa, kati ya hizo hekta 750 zimewekewa mfumo wa umwagiliaji wa matone.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wadogo wa miwa (outgrowers scheme) watahusishwa katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ambayo inatarajia kuanza mwaka 2022/ 2023. Katika awamu hiyo, Serikali kwa kushirikiana na mwekezaji imetenga eneo lenye hekta 3,600 kwa ajili ya wakulima wa miwa (outgrowers) ambao watazalisha na kuuza miwa yao katika Kiwanda cha Miwa cha Bagamoyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwanda unategemewa kukamilika ifikapo Juni, 2022 kwa hiyo miwa ya wakulima itakomaa wakati kiwanda kimeanza kufanya kazi. Hivyo, wakulima hao watakuwa na uhakika wa soko la miwa watakayozalisha.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Asilimia 70 ya wakazi wa Mkoa wa Songwe wanategemea kilimo: -

Je, ni lini Serikali italeta pembejeo za kilimo kwa bei nafuu ambayo wakulima wengi wataweza kumudu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tumeanza kuboresha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo kwa maana ya mbegu, mbolea na viuwatilifu, kuratibu mahitaji ya pembejeo kutoka katika mikoa na kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya makampuni kupeleka na kuuza. Majukumu hayo yanatekelezwa kwa kutumia mfumo wa bulk purchase hasa katika eneo la mbolea.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwa mfumo huu wa ununuzi bei za ununuzi kwa maana ya Free on Board zimepungua. Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni gharama za usafiri na bima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza upatikanaji wa pembejeo kwa kuvutia wawekezaji wa kampuni binafsi hasa katika eneo la mbegu, mikataba maalum kwa ajili ya kupunguza gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati mingine ni kuanzisha mifumo ya ugharamiaji wa sekta ikiwemo uanzishwaji wa Mfuko wa Pembejeo (Credit Guarantee Scheme) pia kupunguza au kufuta baadhi ya tozo na ada. Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali imepitia na kufuta tozo 12 katika mbegu na tozo nne za mbolea ili kupunguza bei na gharama za pembejeo hizo.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:-

Je Serikali ina mpango gani wa kutumia mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora hususani za alizeti ambayo ndio zao la uti wa mgongo wa uchumi wa mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango wa zao la alizeti katika kuongeza upatikanaji wa mafuta ya kula hapa nchini ambapo asilimia 68 ya mafuta ya kula yanatokana na zao hilo ikilinganishwa na mazao mengine ya yanayochangia asilimia 31.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za mafuta nchini kwa kutenga fedha jumla ya shilingi bilioni 40 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya uzalishaji wa mbegu ya Wakala wa Mbegu wa Serikali ili kuzalishaji mbegu za alizeti na mazao mengine.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu hiyo kutawezesha kuongeza uzalishaji wa mbegu za alizeti kutoka tani 538 katika msimu wa 2019/2020 hadi kufikia tani 10,000 za mbegu bora za alizeti mwaka wa fedha 2019/2030 ambazo zitatosha kutumika katika eneo la hekta milioni 1.2 zinazoweza kuzalisha tani 500,000 za mafuta ya kula.

Mheshimiwa Spika, kwa kuthamini umuhimu wa zao la alizeti, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeendelea kugundua na kuzalisha aina mpya ya mbegu bora za alizeti zenye sifa ya kutoa mavuno na mafuta mengi na zenye ukinzani dhidi ya magonjwa kutoka aina 1 hadi 17 za zao la alizeti katika msimu wa 2019/2020.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itawalipa wananchi wanaodai miche ya mikorosho deni ambalo ni la muda mrefu tangu mwaka 2017?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela Mbunge wa jimbo la Lulindi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika msimu wa mwaka 2017/ 2018 Serikali kupitia Bodi ya Korosho iliingia mikataba na wazalisahji wa miche 678 ili kuzalisha miche 13,661,433 ya korosho yenye thamani ya shilingi 5,317,107,679. Aidha, jumla ya miche 12,298,000 sawa na asilimia 92 imesambazwa kwa wakulima katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani, Tanga, Singida, Tabora, Dodoma, Kilimanjaro, Morogoro, Njombe, Mbeya, Iringa na Songwe.

Mheshimiwa Spika, malipo kwa wazalishaji hao yamechelewa kutokana na zoezi la uhakiki kuchukua muda ili kujiridhisha kabla ya kufanya malipo hayo. Kutokana na uhakiki uliofanywa katika awamu ya kwanza na timu ya wataalamu kutoka Serikalini jumla wazalishaji miche 382 waliozalisha miche milioni tano yenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 wameshalipwa.

Aidha, kupitia uhakiki wa awamu ya pili uliofanyika mwezi Agosti hadi Oktoba 2020, ulibaini kuwa jumla ya miche milioni 5.8 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.660 ilihakikiwa na bado kulipwa. Aidha, Serikali inakamilisha utaratibu wa malipo kwa wazalishaji hao wa miche na watalipwa.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza:-

(a) Je, Serikali ina mpango wa kuwajengea miundombinu ya kisasa akina mama wa Tabora itakayoweza kukausha mboga kama uyoga, mchicha na majani ya maboga kwa njia ya kisasa zaidi ili kuongeza kipato?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha masoko ya ndani na nje ya nchi ilia kina mama wa Tabora wanaokausha mboga waweze kuuza mboga hizo kwa faida?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrew Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Tabora kama ifuatavyo kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa kilimo wakiwemo USAID-kupitia mradi wa Lishe, Shirika la Mpango wa Chakula Dunia (WFP) na JICA kupitia mradi wa TANSHEP imekuwa ikijenga uwezo wa wadau kuhusu matumizi ya teknolojia mbalimbali ikiwemo usindikaji wa mazao ya bustani. Serikali pia inahamasisha matumizi ya teknolojia ya ukaushaji wa mboga kwa kutumia nishati ya jua kwa kuwa teknolojia hiyo ni nafuu na rahisi kutumika ikilinganishwa na teknolojia nyingine.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na FAO inatarajia kutekeleza Mradi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 7.3 utakaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia ili kuwasaidia kina mama wa Mkoani Tabora na Katavi kuimarisha masoko na kusaidia katika teknolojia ya uhifadhi mazao.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na SIDO na miradi na TANSHEP katika sekta horticulture kuunganisha wakulima na masoko ili kuboresha masoko ya ndani na nje ya nchi. Serikali kwa kupitia SIDO imekuwa ikiwapatia akinamama mafunzo ya ukaushaji wa mazao ili yawe na ubora unaotakiwa. Mafunzo yanalenga kufikia viwango vya bidhaa vinavyotambuliwa katika viwango vya TBS. Aidha, wasindikaji hao watakuwa wakipelekwa kwenye maonesho ya aina mbalimbali kama vilevile nanenane ili kutangaza bidhaa zao. Serikali pamoja na Wizara ya Viwanda kupitia SIDO, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na Umoja wa Wajasiriamali Mkoa wa Tabora wanaendelea kuwatafutia majengo wakinamama ambayo yatatumika katika kusindika na kama display centres. Aidha, SIDO imeandaa mkakati wa kuwaingiza wasindikaji watakaokidhi vigezo katika portal ya SIDO.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA K.n.y. MHE. ENG.STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Bonde la Mto Ruhuhu lililopo Kata ya Lituhi linawanufaisha wananchi kwa kuweka miundombinu ya Kilimo na umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Jimbo la Nyasa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Bonde la Mto Ruhuhu linalojumuisha sehemu ya Wilaya Ludewa Mkoni Njombe na Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma linalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji. Upembuzi yakinifu wa awali kuhusu kilimo cha umwagiliaji katika bonde hili ulifanyika mwaka 2013/2014 na kubaini uwezekano wa kujenga bwawa kubwa; matumizi mbalimbali ikiwemo kilimo cha umwagiliaji kwa takribani hekta 4,000 na kufua umeme wa megawati 300. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania linaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Bwawa la Kikonge lililopo ndani ya Bonde la Mto Ruhuhu kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na uendelezaji wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji chini ya Bwawa la Kikonge.

Mheshimiwa Spika, mara baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu itakapokamilika na kutathimini gharama halisi, Serikali itatafuta fedha za ujenzi wa bwawa hili pamoja na fedha za ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji chini ya Bwawa la Kikonge ili kuongeza uzalishaji na tija ya mazao ya kilimo katika eneo hilo. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA K.n.y. MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha kilimo cha mkataba kwa njia ya outgrower scheme ili kupanua wigo wa upatikanaji wa soko kwa wakulima wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha mkataba kinawezesha wakulima kuwa na soko la uhakika na wanunuzi kununua kuwa na mazao yenye ubora kulingana na mahitaji. Aidha, kilimo cha mkataba kinachangia kutatua changamoto za upatikanaji wa pembejeo za kilimo na kuimarisha upatikanaji wa mitaji kutokana na makubaliano baina ya mkulima, taasisi za fedha na wanunuzi wa mazao husika kulingana na mahitaji ya soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 kilimo cha alizeti kitakuwa cha mkataba na mpaka sasa Wizara imewasiliana na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji ili kusimamia kilimo cha mkataba. Kilimo cha mkataba kimeleta matokeo mazuri katika zao la ngano katika Mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha.

Aidha, tayari Serikali imekutana na makampuni ya Pyxus Tanzania Agriculture Limited, Mount Meru, Mwenge Sunflowers na makampuni mengine yanayozalisha mazao ya alizeti kama Jackma CO. Ltd. yamefanya vizuri katika mikoa ya Manyara katika kilimo cha mkataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutumia kilimo cha mkataba Wizara kwa kushirikiana na Sekta binafsi inaendelea kuhamasisha wakulima kushiriki katika kilimo cha mkataba ambacho kimeonesha mwelekeo mpya katika kuhakikisha masoko ya uhakika, bei nzuri na viwango bora vya mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatekeleza haya kwa kuzingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 na maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa sekta ya kilimo ijitegemee.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Bonde la Ruvu linatumika kwa kilimo cha umwagiliaji ili kukabiliana na changamoto ya usalama wa chakula?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete Mbunge wa Jimbo la Chalinze kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Bonde la Ruvu ni moja kati ya mabonde yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambacho kinasaidia uhakika wa chakula na kukabiliana na changamoto ya usalama wa chakula. Serikali imeianisha takribani skimu 21 zenye eneo la ukubwa wa takribani hekta 85,075 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Ruvu katika Mikoa ya Morogoro na Pwani. Aidha, jumla ya hekta 1,284 zimeendelezwa kwa kuwekewa miundombinu ya umwagiliaji na wakulima wanatumia eneo hilo kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu zote zilizopo katika Bonde la Ruvu kama zilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Umwagiliaji wa mwaka 2018. Aidha, utekelezaji wa mpango huo umeshaanza katika skimu za Tulo (Morogoro DC), Msoga (Bagamoyo DC), Kwala (Kibaha DC) na Bagamoyo.
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, upi mpango wa Serikali katika kukwamua zao la zhai ambalo ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yenye changamoto nyingi nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Jimbo la Lupembe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa zao la chai kutokana na mchango wake katika Pato la Taifa, ajira kwa wadau wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa zao na kipato kwa wakulima wa chai. Katika kuongeza uzalishaji na tija ya zao la chai, Serikali inaendelea kuwekeza katika utafiti na uzalishaji wa miche bora ya chai ambapo hadi kufikia Mei, 2021, Taasisi ya Utafiti ya TRIT imefanikiwa kuzalisha aina mpya nane za miche za zao la chai zinazohimili ukame, ukinzani na magonjwa, zenye tija nzuri ya uzalishaji na ubora wa vionjo vya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Taasisi za TARI na TRIT kwa kushirikiana na Kampuni ya Mbolea ya Minjingu inaendelea na majaribio ya mbolea ya Minjingu kwenye mashamba ya chai. Hatua nyingine ni kutoa mafunzo ya vitendo kwa wakulima 2,000 wa chai kupitia mashamba darasa 97 katika Halmashauri za Wilaya za Njombe, Rungwe na Mufindi kwa lengo la kuongeza tija, ubora na ushindani wa chai ya Tanzania kwenye masoko ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Serikali imeendelea kuhamasisha wakulima wa chai kutumia umwagiliaji katika na baadhi ya wakulima chini ya makampuni ya Uniliver na DL wameanza kufanya majaribio ya matumizi ya mifumo ya umwangiliaji kwenye kukuza chai. Vilevile kupitia Mradi wa Agri-connect Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa ajili ya kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya chai, kahawa na bustani katika Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe na Katavi ambapo barabara zilizojengwa hadi kufikia Mei, 2021 zina urefu wa jumla ya kilometa 87.

Aidha, Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) inaendelea kuhamasisha Vyama vya Ushirika katika zao la chai kutumia mfumo wa uagizaji wa mbolea bulk ambapo mwezi Februari Chama cha Ushirika wa Mazao na Masoko Mkonge kilifanikiwa kuagiza tani 500 mbolea aina ya NPK kwa ajili ya zao la chai.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa masoko ya chai na ifikapo Desemba, 2021 tutakuwa na mnada wa chai nchini Tanzania kwa mara ya kwanza ambao utafanyika Jijini Dar es Salaam na kutoa fursa kwa wazalishaji wakubwa na wadogo kushiriki kwenye uuzaji wa chai ndani ya nchi badala ya kupeleka chai kwenye mnada wa Mombasa nchini Kenya.
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuendeleza mashamba ya Karatu –Bendhu pamoja na kuwalipa wafanyakazi wa mashamba hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Awack Tlemai, Mbunge wa Jimbo la Karatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu ina jumla ya mashamba 33 yanayomilikiwa na wawekezaji katika tasnia ya mazao ya biashara na chakula. Kati ya mashamba hayo 33 mojawapo ni Shamba la Bendhu lililopo Kata ya Oldeani lenye ukubwa wa hekta 472, Mwekezaji wa shamba hilo aliyemilikishwa kwa miaka 99 kuanzia 1948 hadi 2047, ameliendeleza kwa asilimia 49 kwa kilimo cha mazao ya ngano na kahawa. Aidha asilimia 45 ya shamba linalimwa na wafanyakazi kwa ajili ya kujikimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mashamba yote 33, Shamba la Bendhu ndiyo lenye mgogoro wa mirathi iliyotangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na.6 la tarehe 5 Februari, 2021 katika ukurasa wa 13. Kutokana na mgogoro huo uzalishaji wa mazao katika shamba hilo uliyumba na kusababisha malipo kwa wafanyakazi kutofanyika kwa wakati. Aidha, wafanyakazi wa shamba hilo walifungua kesi Na.8 ya mwaka 2015 katika Kamisheni ya Usuluhishi na Maamuzi (CMA) Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na majadiliano ya kesi hiyo, mwezi Desemba, 2020 yalifikiwa makubaliano kwamba wafanyakazi wataendelea kulipwa kadri ya mapato yatakavyokuwa yanapatikana kutokana na uzalishaji katika shamba hilo. Pia, utekelezaji wa makubaliano hayo unasimamiwa na Chama cha Wafanyakazi. Aidha, nia ya Serikali ni kuona utekelezaji wa makubaliano hayo unafanyika bila changamoto yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na shauri la mirathi kuwa mahakamani, Serikali inasubiri maamuzi ya Mahakama juu ya shauri hilo. Aidha, hakuna migogoro iliyopo katika mashamba mengine 32 ya Karatu. Hata hivyo mkakati wa Serikali ni kuendelea kufuatilia mashamba yote ya uwekezaji yaliyopo Wilayani Karatu na kwingineko nchini ili kuhakikisha mashamba hayo yanaendelezwa na kuzalisha kwa maslahi ya nchi. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Je, ni lini makubaliano ya kibiashara yatafanyika baina ya taasisi za Umma na makampuni binafsi yanayolima kahawa Mkoani Kilimanjaro ili kuzalisha miche bora yenye ukinzani dhidi ya magonjwa na kuigawa kwa wakulima bila malipo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa miche bora ya kahawa hufanyika kupitia wakulima binafsi, vikundi vya wakulima, Vyama vya Ushirika, Taasisi ya Utafiti ya TaCRI na mikataba baina ya TaCRI na kampuni binafsi au shirika.

Mheshimiwa Spika, kutokana na gharama kubwa ya uzalishaji wa miche hususani pale ambapo hakuna ufadhili maalum wa taasisi au shirika, kumekuwepo na utaratibu wa wakulima kuchangia gharama kidogo ili kuwa na uzalishaji endelevu na upatikanaji wa miche bora.

Mheshimiwa Spika, mathalani wakulima hutakiwa kuchangia kiasi cha shilingi 100 kwa kila mche sawa na asilimia 10 ya gharama halisi ya mche. Kati ya Julai, 2016 mpaka 2021 TaCRI imezalisha jumla ya miche 2,308,606 ambayo imeendelea kusambazwa Mkoani Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, TaCRI imekuwa ikiingia mikataba ya kuzalisha miche bora yenye ukinzani dhidi ya magonjwa na kuisambaza kwa wakulima kadri ya mahitaji. Mikataba hiyo ni pamoja na uzalishaji wa miche 100,000 uliofanyika kati ya mwaka 2018 na 2019 ambapo TaCRI ilishirikiana na Ushiri AMCOS ya Wilayani Rombo kuzalisha miche hiyo.

Mheshimiwa Spika, TaCRI kati ya mwaka 2016 na 2019 ilishirikiana na Taasisi za Hivos na Solidaridad kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa miche bora ya kahawa ambapo jumla ya miche 890,677 ilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima katika Wilaya za Same, Mwanga na Moshi.
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaunganisha Wakulima wa Mikoa ya Kusini hususan Mkoa wa Njombe na Wawekezaji wa nje na ndani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa kuwaunganisha wakulima na wawekezaji wa ndani na nje ili kuwa na mfumo endelevu unaowapa fursa ya wote kuwepo na kwa faida ya pande zote mbili. Katika kutekeleza mpango huo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekuwa inaratibu makubaliano kati ya wanunuzi/wasindikaji na wakulima kupitia kilimo cha Mkataba kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa teknolojia, pembejeo pamoja na masoko.

Mheshimiwa Spika, kupitia ushoroba wa maendeleo wa SAGCOT, Wizara imehamasisha wawakezaji Tanzania Agrofood Ltd & Olivado Ltd katika Mikoa ya Njombe na Iringa ambao wameunganishwa na wakulima wadogo na kuwezesha kuongezeka kwa mauzo wa mazao mbalimbali mfano parachichi. Mauzo yameongezeka kutoka tani 3,696 mwaka 2015 hadi tani 7,190 mwaka 2019.

Aidha, bei parachichi pia imeongezeka kutoka shilingi 1,200,000 kwa tani mwaka 2015 hadi shilingi 1,800,000 kwa tani mwaka 2020. Uwepo wa kampuni hizo zinazowahakikishia wakulima soko imekuwa ni chachu ya kuongezeka kwa uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia program ya Agri-connect inayotekelezwa kwa uratibu wa Wizara ya Kilimo moja ya nguzo zake ni kuunganisha wakulima na wewekezaji katika mnyororo wa thamani. Programu hiyo katika Mikoa ya Kusini ukiwemo Mkoa wa Njombe ambapo mazao ya kipaumbele ni mazao ya bustani, chai na kahawa. Programu hiyo inalenga kuwaunganisha wakulima na masoko ya ndani na ya nje.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo sugu la soko la zao la tumbaku nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, soko la tumbaku linategemea mahitaji katika soko la dunia. Mahitaji ya tumbaku na bidhaa zake yamekuwa yakishuka katika Soko la Dunia kwa wastani wa asilimia sita hadi saba kwa mwaka. Hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na kampeni ya kidunia ya kupunguza uzalishaji na matumizi ya tumbaku pamoja na bidhaa zake, pamoja kuanza matumizi ya sigara aina mpya inayotumia kilevi cha kutengeneza maabara (Laboratory nicotine) iitwayo e-cigarette.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku Tanzania inaendelea kutafuta masoko ya tumbaku kwa kuwashawishi wanunuzi waliopo kuongeza kiwango cha ununuzi kwa njia ya mkataba, kutafuta wanunuzi wapya na pia kutafuta masoko mengine mapya nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua hizo, wanunuzi wakubwa wameongeza ununuzi wa tumbaku kutoka kilo 39,000,000 katika msimu wa mwaka 2017/2018 hadi kilo 57,000,000 msimu wa mwaka 2021/2022, sawa na ongezeko la asilimia 46. Serikali imehamasisha wanunuzi wapya na kwa msimu wa 2021 kampuni nane za kizawa zilingia mkataba na wakulima kununua kilo 17,000,000. Katika hatua nyingine Serikali imeendelea kutafuta masoko mapya ambapo, Serikali inaendelea kutafuta soko la China na tayari walileta aina ya tumbaku wanayotaka na majaribio yamefanyika na sampuli ya tumbaku hiyo imepelekwa kwa hatua zaidi.

Mheshimiwa Spika, jitihada za kutafuta masoko zinaendelea katika nchi mbalimbali, Serikali inaamini kuwa baada ya muda mfupi tatizo la soko kwa wakulima wa tumbaku wa Tanzania linaenda kupungua.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaondoa kabisa utaratibu wa kununua mazao kwa mkopo ambao unaendelea kutumiwa na baadhi ya Taasisi jambo ambalo linasababisha manung’uniko kwa Wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomari Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ni Taasisi za Serikali pekee chini ya Wizara ya Kilimo ambazo imekuwa ikizitumia kuchochea soko la mazao ya wakulima hasa mazao ya nafaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia NFRA na CPB imetumia jumla ya bilioni 119 kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya nafaka ambayo yatauzwa katika masoko ya ndani na nje.

Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Oktoba, 2021 NFRA imetumia jumla ya bilioni 37 kununua jumla ya tani 75,000 za mahindi na CPB imetumia jumla ya bilioni 12 kwa ajili ya tani 27,000 za mahindi na ununuzi unaendelea. Aidha, ununuzi huo umefanyika katika Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Songwe, Rukwa, Katavi, Shinyanga, Arusha na Dodoma.

Mheshimiwa Spika, NFRA na CPB hazitumii utaratibu wa kukopa wakulima wa nafaka kwani, zimekuwa zikinunua nafaka kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima na kufanya malipo mara baada ya mapokezi ya nafaka katika vituo vya ununuzi. Katika msimu wa 2021/2022 taasisi hizi zinaendelea na ununuzi wa nafaka kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima kwa utaratibu wa malipo ya fedha taslimu na si kwa njia ya kuwakopa wakulima.
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha zao la chai nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la chai linaingizia Taifa fedha za kigeni zaidi ya dola milioni 60 kwa mwaka na kutoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya watu 50,000 viwandani na mashambani. Zao hili linalimwa katika Wilaya 12 na Mikoa sita ambayo ni Mbeya, Njombe, Iringa, Tanga, Kagera na Mara ambapo wakulima wadogo wa chai wapatao 32,000 hujishugulisha na kilimo cha zao hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaendelea na jitihada za kuendeleza zao la chai kwa lengo la kuongeza uzalishaji, tija na ubora kwa kutenga fedha za kwa ajili ya utafiti, upatikanaji wa miche bora ya chai, kuimarisha miundombinu, kutoa mafunzo na masoko. Kwa mwaka 2021/ 2022, Serikali imetenga fedha za maendeleo jumla ya shilingi 400,000,000 kwa ajili ya kuzalisha miche 1,000,000; kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo na kuendeleza mashamba mama manne yanayosimamiwa na Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai (TSHTDA) ya Korogwe na Lushoto.

Mhasimiwa Mwenyekiti, kupitia Mradi wa AGRICONECT jumla ya Euro milioni tano na laki tano zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza zao la chai katika mnyororo wa thamani katika kipindi cha miaka minne inayoishia 2023/2024 katika Wilaya za Rungwe Busokelo, Mufindi na Njombe. Mradi unaotekelezwa na Kampuni za IDH, TRITI na TSHTDA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha shilingi 290,722,500 zimetengwa kwa ajili ya kuzalisha miche 750,000, kutoa mafunzo kwa wakulima hususani kanuni bora za kilimo, kuimarisha Vyama vya Ushirika vipatavyo 34 na kuimarisha huduma za ugani. Miche itakayozalishwa imelenga kutumika kuziba mapengo kwa kuanzisha mashamba mapya. Aidha, ufadhili wa AGRICONEC na kwa kushirikiana na sekta binafsi, Wizara inaratibu uanzishwaji wa mnada wa chai katika kuhakikisha kuwa chai ya wakulima inapata bei nzuri na soko la uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnada huo wa chai nchini unatarajiwa kuanza rasmi mwishoni mwa mwaka huu. Wizara kwa kushirikiana na wadau inakamilisha mkakati wa chai utakaoishia mwaka 2030. Wenye lengo mahususi ya kuongeza tija, uzalishaji wa ubora wa chai, ufanisi katika kutoa huduma za ugani pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuvutia wawekezaji. Mkakati huu unalenga kuongeza uzalishaji wa chai kutoka tani 33,000 hadi kufikia tani 9,000 chai kavu, ifikapo mwaka 2030 na kuongeza matumizi ya teknolojia katika mnyororo wa thamani na kuimarisha mfumo wa masoko. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha Miradi ya Umwagiliaji ya Ilemba, Ng’ongo, Maleza, Mititi, Itela, Ilembo na Nkwilo katika Jimbo la Kwela?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mpango wa Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji Wilayani (DIDF), kwa mwaka 2008/2009 na mwaka 2009/2010 ilitenga jumla ya shilingi milioni 650,000,000/= kwa ajili ya kuendeleza skimu ya umwagiliaji ya Ng’ongo, yenye ukubwa wa hekta 650 ambazo ujenzi ulianza kutekelezwa mwaka 2012 na kukamilika mwaka 2013. Fedha hizi zilitumika kujenga banio na mfereji mkuu wenye urefu wa mita 1,725 pamoja na miundombinu yake.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kupitia (ASDP II) imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwenye skimu ya umwaguliaji ya Ilembe yenye ukubwa wa hekta 800. Aidha, kazi ya kupima mashamba imekamilika na usanifu wa kina upo hatua za mwisho katika skimu ya umwagiliaji ya Ilembe.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeanza kufanya tathmini ya kina katika miradi yote ya umwagiliaji katika Mikoa ya Rukwa na Katavi. Tathmini hiyo ni pamoja kuangalia kwa kina upungufu kwenye skimu hizo na kutambua maeneo mapya na pia kufanya usanifu wa kina na kutathmini gharama za ujenzi wa miundombinu hiyo ili kuanza kutenga fedha katika bajeti zijazo.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE aliuliza: -

Nchi yetu imekuwa na mipango mkakati wa kuzalisha mafuta ya kula kiasi cha kutosheleza soko la ndani.

(a) Je, ni kwa nini Serikali isiboreshe mpango ya kuzalisha mafuta ya mawese kimkakati kwa kuhamasisha kilimo cha zao hilo katika Mikoa ya Kagera, Tanga, Pwani, Katavi na Mbeya?

(b) Je, ni kwa nini Serikali isitumie mfumo wa kilimo kikubwa cha pamoja (block farming) ambapo Serikali hubeba gharama za awali na hatimaye sehemu ya gharama hukatwa kwenye mauzo ya Mkulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Charles John Mwaijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa ya Kagera, Tanga, Pwani, Katavi na Mbeya na Halmashauri za Mikoa hiyo inaendelea kuhamasisha uzalishaji wa zao la michikichi katika maeneo yanayofaa kuzalisha zao hilo.

Uhamasishaji huo ni pamoja na kuzitaka Halmashauri hizo kuanzisha vitalu vya kuzalisha miche bora ya michikichi aina ya Tenera, kutoa mafunzo kwa wakulima na wataalam kuhusu kilimo bora cha michikichi na kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata mafuta ya mawese jirani na maeneo ya uzalishaji ili kusafirisha mikungu ya michikichi kwenda viwandani.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uhamasishaji huo baadhi ya Halmashauri za Wilaya zimeanzisha vitalu vya kuzalisha miche bora ambapo Ngara (Kagera) imeanzisha kitalu cha miche 100,000; Mkuranga (Pwani) miche 20,000; Tanganyika (Katavi) miche 70,000 na Kyela (Mbeya) miche 26,600.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Halmashauri zenye maeneo makubwa yanayofaa kwa kilimo cha michikichi inaendelea kuhamasisha kilimo cha mashamba ya pamoja (Block farming) ili kuzalisha kwa tija na kurahisisha huduma kwa wakulima. Baadhi ya Halmashauri hizo ni Uvinza (Kigoma) ekari 5,000 na Uyui (Tabora) ekari 12,000. Uhamasishaji unaendelea kwa mikoa mingine yenye sifa hizo.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa utoaji wa mbegu bora za alizeti ili kuongeza uzalishaji wenye tija kwa Wakulima katika Wilaya ya Kishapu?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ni miongoni mwa Halmashauri zenye fursa ya uzalishaji wa zao la alizeti nchini. Kutokana na umuhimu wa nchi kujitosheleza kwa mafuta ya kula, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inatekeleza Kampeni ya Kitaifa yenye lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti kwa kuimarisha utafiti, kuongeza uzalishaji wa mbegu bora, kutoa elimu bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeongeza bajeti ya Taasisi yetu ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kutoka Shilingi bilioni 7.5 kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 11.6 kwa mwaka 2021/2022 na bajeti ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kutoka Shilingi bilioni 5.42 kutoka 2020/2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 10.8 kwa ajili ya utafiti na uzalishaji wa mbegu bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mikakati hiyo upatikanaji wa mbegu bora za alizeti umeongezeka kutoka tani 587 mwaka 2021 hadi tani 2,124 mwezi Januari, 2022. Kati ya hizo ASA imesambaza tani 1,600 kwa bei ya ruzuku ya Shilingi 3,500 kwa kilo, ambapo tani 48 za mbegu bora za alizeti zimesambazwa katika Mkoa wa Shinyanga na usambazaji wa mbegu unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na mahitaji. Aidha, katika msimu wa 2022/2023 Serikali inalenga kuzalisha na kusambaza tani 5,000 za mbegu bora za alizeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako tukufu, naomba kutoa wito kwa viongozi katika Mikoa na Halmashauri kuhakikisha kuwa mbegu zinazosambazwa kwa wakulima zinatumika kulingana na malengo yaliyokusudiwa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha bei ya mbolea inashuka hadi kufikia kiwango cha Wakulima kumudu kuinunua ili kuiepusha nchi yetu kukumbwa na janga la njaa?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye eneo (a), (b) na (c), kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakiri kwamba bei ya mbolea katika Soko la Dunia na hapa nchini imepanda kwa msimu wa mwaka 2021/2022 ikilinganishwa na msimu wa mwaka 2020/2021. Kupanda huko kwa bei hakutokani na Serikali au wafanyabiashara wa ndani kupandisha bei, bali kumetokana na kupanda kwenye Soko la Dunia na wakulima wote duniani wameathirika na upandaji huo uliotokana na athari za UVIKO. Mfano, hadi kufikia mwezi Januari, 2022 bei ya Urea ni Dola za Kimarekani 700 kwa tani ikilinganishwa na Dola za 350 kwa msimu wa 21, sawa na ongezeko la asilimia 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto za kupanda kwa bei za mbolea nchini, Serikali inachukua hatua za muda mfupi na muda mrefu. Hatua za muda mfupi zilizochukuliwa mpaka sasa ni pamoja na kununua mazao ya nafaka kwa bei ya juu kuliko bei ya soko ambapo mahindi yalinunuliwa kwa bei ya shilingi 500 badala ya 200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhakikisha kwamba bandari zetu zinatoa kipaumbele cha kushusha mbolea ili kupunguza tozo za bandarini, ununuzi wa mbolea kwa mfumo wa (BPS) katika baadhi ya mazao mfano Tumbaku. Matumizi ya reli kusafirisha mbolea katika maeneo ambapo reli inapita. Matumizi ya mbolea mbadala kama NPS na NPS-Zinc na kuruhusu ushindani kwenye uagizaji wa mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda mrefu zilizochukuliwa ni pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya mbolea. Kutokana na uhamasishaji huo, Kampuni ya Itracom Fertilizers kutoka Burundi inaendelea na ujenzi wa kiwanda cha mbolea Mkoani Dodoma chenye uwezo wa kuzalisha tani 600,000 za mbolea na tani 300,000 za chokaa kwa mwaka. Wawekezaji wengi zaidi wanaendelea kujitokeza kutoka nchi mbalimbali kama vile Misri na Saudi Arabia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekutana na uongozi wa kiwanda cha mbolea cha Minjingu kujadili namna kiwanda hicho kinavyotakiwa kuzalisha mbolea kulingana na mahitaji ya udongo na kuongeza uzalishaji wa mbolea kutoka tani 30,000 hadi kufika 100,000 kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inatambua umuhimu wa mbolea katika uzalishaji wa mazao ya chakula ili kuihakikishia nchi Usalama wa Chakula. Kutokana na tathmini iliyofanyika ambayo iliangalia changamoto hii pamoja na utabiri wa mvua, ulioonesha hatutapa mvua nyingi kwa miaka miwili iliyopita, bado maoteo ya uzalishaji yanaonesha nchi itaweza kujitosheleza katika chakula. Mpaka sasa maeneo mengi ya nchi yanaendelea kupata mvua nzuri. Matumizi ya mbolea yapo kwenye asilimia 50 ya kawaida ya mazao ya shambani. Kwa hali hiyo, Wizara ya Kilimo inapenda kuwahakikishia wananchi kwamba, nchi haitakumbwa na janga la njaa.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapunguza gharama za vibali vya kuanzisha biashara ya kuuza pembejeo za kilimo Vijijini ambapo TFRA, TOSCI na TPRI huchukua takribani shilingi 600,000 kabla mfanyabishara hajaingiza mtaji dukani?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Madaba, kama ifuatavyo: -

Mhashimiwa Mwenyekiti, watoa huduma wa pembejeo ikiwemo mbegu, viuatilifu na mbolea katika ngazi zote, wanatakiwa wawe na uelewa mpana wa huduma wanazozitoa. Gharama za kuanzisha biashara ya pembejeo hizo hutokana na mafunzo maalum yanayotolewa na taasisi husika kwa lengo la kujenga uwezo kwa Mawakala na Kampuni za pembejeo ili kutoa huduma stahiki kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu Na. 18 ya mwaka 2003 na marekebisho yake ya mwaka 2014 pamoja na Kanuni za mwaka 2007 na marekebisho ya mwaka 2017; hakuna tozo za kuanzisha biashara ya mbegu, isipokuwa kuna ada ya mafunzo ambayo ni shilingi 150,000 kwa kampuni na wazalishaji/ mawakala wasambazaji wa mbegu bora. Aidha, kwa wazalishaji wa mbegu za kuazima (Quality Declared Seed) hutozwa shilingi 50,000 kwa ajili ya mafunzo maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa viuatilifu na ukaguzi wa eneo la duka linalofunguliwa ni kiasi cha shilingi 172,500 na shilingi 350,000 hutozwa kwa ajli ya mafunzo. Malipo haya ni kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Mimea ya mwaka, 2020. Kwa upande wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania - TFRA hakuna tozo kwa mfanyabiashara anayetaka kuanzisha duka la kuuza mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kuboresha mazingira ya wazalishaji na wasambazaji wa pembejeo ilifuta tozo na ada mbalimbali kwa upande wa mbegu jumla ya tozo 12 zilizokuwa zikigharimu jumla ya shilingi 180,500 zilifutwa. Vilevile Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea ilifuta tozo nne zilizokuwa na shilingi 2,240,000. Hivyo, nitoe wito kwa wafanyabishara wenye nia ya kuanzisha maduka ya pembejeo kujitokeza na kuanzisha maduka hayo ili kusogeza huduma hiyo karibu na wakulima. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza: -

Je, ni kwa nini Mfuko wa Pembejeo ambao ulianzishwa kwa lengo la kuwasaidia wakulima wadogo waliopo Vijijini haupokei Hati za Kimila ambazo ndizo zilizopo Vijijini?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Mwenisongole Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka, 2005 hadi 2010, Mfuko wa Pembejeo uliwahi kupokea hati za kimila kama dhamana kwa majaribio, ambapo Wilaya ya Mbozi ndiyo iliyokuwa pilot study kwa ajili ya kupewa hati hizo. Baada ya kutoa mikopo hiyo, Mfuko wa Pembejeo ulikabiliwa na changamoto ya mikopo kutofanyiwa marejesho. Aidha, Mfuko wa Pembejeo ulipojaribu kuuza mashamba hayo ilishindikana kwa ajili ya kufidia mikopo, iliyotolewa; haukufanikiwa kutokana na mashamba hayo kuwa ya jamii au ya ukoo unaoishi pamoja na siyo la yule mwenye hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Wilaya ya Mbozi, Mfuko ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi 480,422,335 kwa wakulima 28. Kati ya fedha hizo shilingi 135,947,935 zilirejeshwa na shilingi 344,563,400 bado hazijarejeshwa mpaka sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto zilizojitokeza, Bodi ya Wadhamini mwaka, 2016 ilisitisha utoaji wa mikopo kwa kutumia hati hizi kama dhamana, mpaka hapo zitakapofanyiwa marekebisho kwenye Sheria ya Ardhi ya Vijiji (The Village Land Act) ili kuondoa changamoto hizo. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wakulima wa mazao ya viungo kama Iliki, mdalasini, pilipili manga na karafuu wa Kata ya Kigongoi, Mhindano na Bosho Wilayani Mkinga ili waweze kuongeza uzalishaji wa thamani ya mazao hayo?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mazao ya viungo yanayojumuisha Karafuu, Pilipilimanga, Pilipili Kali, Mdalasini, Hiliki, Tangawizi na jamii hiyo ya mazao ya viungo, hulimwa zaidi katika Mikoa ya Tanga, Morogoro, Mbeya, Kilimanjaro, Kigoma na Ruvuma. Aidha, katika Mkoa wa Tanga Wilaya ya Mkinga na katika Kijiji cha Kigongoi na vijiji vidogo jirani yake ndiyo wanazalisha mazao ya viungo zaidi ikiwemo Hiliki, Mdalasini na Pilipilimanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuendeleza mazao ya bustani yakiwemo mazao ya viungo, inatekeleza Mkakati wa Kuendeleza Mazao ya Bustani wa Mwaka 2021 - 2031 wenye lengo la kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia bora na kuimarisha usimamizi na uratibu. Aidha, mikakati mingine ni pamoja na kutoa mafunzo ya wataalam na wakulima kuhusu kanuni za uzalishaji wa mazao ya viungo, kuunganisha wakulima na wanunuzi wakubwa, na kuanzisha vitalu vya kisasa vya miche ya viungo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na chama cha wasindikaji wa viungo (TASPA) na wasindikaji wa mazao ya viungo wameanza kuwashirikisha wakulima wa viungo Wilaya ya Mkinga kwa kuanzisha vitalu vya kisasa vya viungo. Mfano, Kampuni ya Trianon Investment Ltd yenye Kiwanda cha Viungo Lusanga – Muheza tayari imeanza kununua mazao kwa wakulima wa viungo Mkinga na imedhamiria kugawa miche bora kutoka katika bustani bora ya kuzalisha miche iliopo kiwandani.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeanza kuhamasisha wakulima kuanzisha na kujiunga na Vyama vya Msingi vya Ushirika ili kukuza uwezo wao wa kifedha kupitia mikopo na kuwa na nguvu ya pamoja katika soko; na pia Serikali kuweza kuwapatia mafunzo ya uzalishaji bora na uongezaji thamani wa mazao yao. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza: -

Je, ni kwa nini Mfumo wa Stakabadhi Ghalani hautekelezwi kikamilifu kiasi cha kuwawezesha Wakulima kupata fedha wanapohitaji?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unawezesha wakulima kuuza mazao yao kwa bei ya ushindani, wanunuzi kupata mzigo wenye ubora pamoja na Halmashauri kupata takwimu halisi za mauzo na mapato. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba zao la kahawa, ufuta na korosho ni baadhi ya mazao ambayo huuzwa kupitia mfumo huo. Mfumo huo, umekuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo baadhi ya wanunuzi kuchelewesha malipo kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hiyo Serikali itaimarisha usimamizi wa mwongozo unaoainisha muda maalumu wa kuwalipa wakulima kwa kuchukua hatua za kisheria kwa wanaokiuka taratibu.
MHE. JUSTINE L. NYAMOGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga bwawa la maji katika Kata ya Nyanzwa kwa ajili ya skimu ya umwagiliaji?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justine Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa bwawa na Skimu ya Umwagiliaji Nyanzwa. Aidha, mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bwawa na Skimu ya Umwagiliaji Nyanzwa.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha matokeo ya tafiti za kilimo yanawafikia wakulima?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Tarime, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha matokeo ya tafiti za kilimo yanawafikia wakulima, Taasisi za Utafiti na Idara ya Ugani hutumia njia mbalimbali kufikisha taarifa za utafiti na matumizi ya teknolojia ambazo ni pamoja na kufungua mashamba darasa na mashamba mfano katika maeneo ya kilimo, kutengeneza na kusambaza majarida ya tafiti za kilimo, uwezeshaji wa shughuli za ugani, kuwepo kwa siku ya mkulima, warsha kwa wadau, ushirikishwaji wa wakulima kwenye tafiti na kukusanya takwimu za kiutafiti.

Mheshimiwa Spika, vilevile, safari za mafunzo, vituo mahiri na atamizi vya uhaulishi teknolojia katika viwanja vya Nanenane, maonesho ya kilimo na biashara, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii. Vilevile simu za kiganjani, maandiko ya kisayansi na machapisho.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Taasisi za Utafiti zimeshiriki katika maonesho ya Nanenane yaliyofanyika Kitaifa Jijini Mbeya katika Kiwanja cha John Mwakangale na Viwanja vingine vya Kikanda.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufikisha mbegu za Soya kwa Wakulima wa Jimbo la Newala Vijijini hasa katika Kata za Tarafa ya Chilangala?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijin,i kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2022/2023 Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Newala imetenga shilingi 6,000,000 za kuwezesha ununuzi wa kilo 3,000 za mbegu bora za soya. Mbegu hizo zitasambazwa kwa wakulima wa soya katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala ikiwemo Tarafa ya Chilangala.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeiwezesha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania kituo cha Utafiti (TARI) Naliendele kilo 2,260 za mbegu ya msingi ya soya itakayotumika kuzalisha tani 90 za mbegu iliyothibitishwa ubora ili kuimarisha upatikanaji wa mbegu katika Mikoa ya Kusini kwa msimu wa mwaka 2023/2024 na kulifanya zao hilo kuwa la tatu kwa wakulima wa kusini baada ya korosho, ufuta na sasa Soya.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa maksudi wa kuwavutia Wawekezaji katika Kilimo cha zao la Muhogo Wilayani Muheza?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mkakati wa kuendeleza tasnia ya muhogo wa miaka kumi kati yam waka 2020 mpaka mwaka 2030 unaolenga kuimarisha utafiti na uzalishaji wa mbegu bora za zao la muhogo, kuongeza uzalishaji wa muhogo kutoka wastani wa tani 8.2 hadi tani 24 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Serikali inaendelea na jitihada za kuwavutia wawekezaji ambapo mwaka 2018 kampuni ya CMTL-Tanzania Limited ilipatikana na kupewa eneo la ekari 10 katika Kata ya Mbaramo kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kuchakata muhogo. Serikali inafuatilia ili mwekezaji awekeze kulingana na malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la MEDA inasambaza jumla ya pingili 700,000 za mbegu za mihogo aina ya Mkuranga 1 na Kiroba katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kwa ajili ya kupandwa katika eneo la ekari 175.
MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, ni lini miradi ya umwagiliaji katika Vijiji vya Nyamterela na Katunguru pamoja na Vijiji vya Kwinda na Isole itakamilika Wilayani Sengerema?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao, Mbunge wa Sengerema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/ 2023, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Katunguru yenye hekta 600 iliyopo kijiji cha Nyamterela Wilayani Sengerema.

Vilevile Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Usole yenye hekta 1,000 iliyopo katika kijiji cha Kishinda.
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, Serikali inachukua hatua gani kudhibiti kuongezeka kwa bei ya mbolea nchini hasa Mkoani Ruvuma?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei za mbolea duniani imekuwa ikiongezeka kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na mahitaji hususan kwenye nchi zenye watumiaji wakubwa wa mbolea kama vile China na India. Ongezeko hilo kwa msimu wa 2021/2022 limechangiwa na athari za UVIKO- 19 na vita kati ya Nchi ya Urusi na Ukraine ambao ni wazalishaji wa malighafi zinazotumika katika utengenezaji wa mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka utaratibu wa kudhibiti upandishaji holela wa bei za mbolea kwa kuhusisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini, inafanya tathmini ya gharama halisi ya mbolea na kutoa bei elekezi. Mwezi Machi, 2022 Serikali kupitia TFRA imetoa bei elekezi za mbolea za DAP, UREA, CAN na SA katika Mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuondokana na utegemezi wa uagizaji wa mbolea nje ya nchi, Serikali inaendelela kuvutia uwekazaji wa viwanda vya mbolea hapa nchini. Baadhi ya wawekezaji waliojitokeza ni pamoja na kampuni Itracom inayojenga kiwanda cha mbolea Jijini Dodoma chenye uwezo wa kuzalisha tani 600,000 na Kiwanda cha Minjingu kuendelea na kuongeza uzalishaji kutoka uwezo wa tani 100,000 za sasa hadi kufikia tani 500,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako Tukufu Serikali inasisitiza viongozi wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa bei elekezi zinazotolewa zinazingatiwa katika vituo vyote vya mauzo ya mbolea. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti madalali wanaodalalia mazao ya wananchi yakiwa shambani kwa bei wanazozitaka?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe Mbunge wa Jimbo la Hai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mpango wa uanzishwaji wa vituo rasmi vya uuzaji na ununuzi wa mazao ya kilimo karibu na maeneo ya uzalishaji ili kumuwezesha mkulima kuuza mazao yake kwa bei ya soko na kuzuia uuzwaji wa mazao shambani. Vilevile Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa ghala za kuhifadhia mazao katika maeneo ya uzalishaji ili kuwezesha wakulima kuhifadhi na kuuza mazao yao.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje katika kuondoa changamoto ya ucheleweshwaji wa viuatilifu kwa wakulima wa zao la korosho?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa huko nyuma kumekuwa na ucheleweshwaji wa viuatilifu. Katika kuondoa changamoto ya ucheleweshwaji wa pembejeo unaosababishwa na mlolongo mrefu wa manunuzi kutoka kwa mzalishaji hadi kumfikia mkulima, Serikali inasimamia uagizaji wa pembejeo kwa kupitia Kamati ya Pamoja ya Pembejeo inayoundwa na Vyama vya Ushirika ambavyo kimsingi ni wakulima wenyewe. Kutokana na utaratibu huo, jukumu la Serikali ni kufuatilia mchakato huo ili manunuzi yafanyike kwa muda muafaka na pembejeo kuwafikia wakulima kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2022/2023 Vyama Vikuu vimeagiza sulphur ya unga tani 25,000, viuatilifu vya maji lita milioni 1.5 pamoja na mabomba ya kupuliza 35,000 kwa ajili ya msimu wa 2022/2023 na hadi kufikia Aprili moja jumla ya tani 1,600 na lita 730,724 tayari zimeshapokelewa na kiasi kilichobaki kinatarajiwa kupokelewa kufikia mwisho wa mwezi Mei.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, lini Miradi ya Umwagiliaji katika Vijiji vya Msange na Mnghamo – Singida Kaskazini itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Ighondo Ramadhani Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi wa Mughamo na kuanza ujenzi wa bwawa na miundombinu mingine ya umwagiliaji katika Skimu ya Msange.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kusaidia kuongezeka kwa bei ya zao la chai kwa wakulima nchini?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, bei ya zao la chai hutegemea mwenendo wa Soko la Dunia, soko la ndani na ubora wa chai sokoni. Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha uwepo wa mazingira bora yanayoleta ushindani ili kuchochea bei ya chai. Katika hatua ya awali, kwa mwaka 2023 bei ya chai imeongezeka kutoka shilingi 312 hadi shilingi 366 kwa kilo. Aidha, mikakati mingine ya kupandisha bei ni kuongeza uzalishaji wa miche bora ya chai, kuendelea kuhamasisha matumizi ya chai nchini, kuanzisha mnada wa chai, kutoa ruzuku ya mbolea na miche bora ya chai ili kuongeza tija na uzalishaji na kuandaa mwongozo wa ubora wa majani mabichi ya chai na kuanzisha kiwanda cha kusindika chai maalumu.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapa pembejeo wakulima wa mbogamboga nchini?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa 2022/2023, Serikali imeendelea kutekeleza mpango wa utoaji wa ruzuku za viuatilifu, mbegu na mbolea kwa mazao yote yanayozalishwa nchini. Kwa kipekee utekelezaji wa mpango wa ruzuku ya mbolea ni kwa mazao yote ya nafaka, mbogamboga, mikunde na mazao mengine yote yaliyozalishwa na wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wakulima ndio wananufaika na pembejeo za ruzuku, wanapaswa kujisajili kwa kuainisha mashamba na mazao anayozalisha na hivyo kuweza kununua pembejeo za ruzuku kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Serikali. Lengo la Serikali kutoa ruzuku za pembejeo kwa mazao yote, ni kupunguza gharama kwa wakulima, kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwanda.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kushusha bei ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo ili kuongeza uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kupunguza gharama za upatikanaji wa mbolea na pembejeo nyingine kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na tija kwa mazao ya kilimo. Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa ruzuku ya mbolea, mbegu bora kwa mazao ya alizeti, miche ya chikichi, parachichi, chai na kahawa pamoja na viuatilifu vya mazao ya korosho, pamba na viuatilifu kwa ajili ya kudhibiti milipuko ya visumbufu vya mimea ikiwemo viwavijeshi, inzi, panya, kweleakwelea na nzige.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Aprili, 2023 jumla ya tani 349,922 za mbolea zimenunuliwa na wakulima 799,937 kwa bei ya ruzuku. Vilevile, Serikali imetoa jumla ya lita 48,033 za viuatilifu vya kudhibiti viwavijeshi, ekapaki 1,823,688 za viuatilifu vya pamba, tani 15,015.03 na lita 2,684,470.5 za viuatilifu vya zao la korosho, tani 1,004 za mbegu bora za alizeti na miche bora 61,486,981 ya mazao mbalimbali kwa utaratibu wa ruzuku. Aidha, utaratibu wa utoaji wa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima utaendelea kufanyika kulingana na bajeti ya Serikali. (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -

Je, kwa kiasi gani Taifa linanufaika na vijana wanaopelekwa kwenye mafunzo ya kilimo Israel?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Israel zilikubaliana kushirikiana kwa kuanzisha programu ya kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaomaliza Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati vya Mafunzo ya Kilimo na Mifugo nchini Israel. Lengo la programu hiyo ni kuongeza ujuzi na maarifa juu ya teknolojia za kisasa.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2015 hadi sasa, jumla ya vijana 261 wa Kitanzania wamenufaika na mafunzo ya kilimo kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Israel (Ministry of Foreign Affairs Israel’s Agency for International Develeopment Cooperation) kupitia Agrostudies.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza kuwatumia vijana waliohitimu mafunzo kwa vitendo nchini Israel kupitia programu ya BBT na Block farm ambapo wanapata fursa ya kuwashirikisha na vijana wengine uzoefu wao kutoka nchini Israel. Hadi sasa jumla ya vijana 79 walioshiriki mafunzo nchini Israel ni miongoni mwa vijana 812 walio kwenye mafunzo ya kilimo biashara katika Vituo Atamizi. Baada ya kipindi cha mafunzo, watapata fursa ya kufanya kilimo biashara kupitia mashamba ya pamoja ya block farms chini ya BBT.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA K.n.y. MHE. AHMED A. SALUM aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Kata ya Ishololo wilayani Shinyanga utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K. n. y WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Jimbo la Solwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Ishololo wenye ukubwa wa hekta 600 ni mojawapo ya miradi ambayo ilikuwa ikitekelezwa kupitia mpango wa kuendeleza kilimo wilayani (District Agricultural Sector Investiment Projects). Kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB). Ufadhili wa mpango huu ulifikia kikomo tarehe 31/12/2013 kabla ya mradi huo kukamilika. Wakati mpango wa utekelezaji wa DASIP unafikia kikomo, Utekelezaji wa Mradi wa Ishololo ulikuwa umefikia aslimia 23.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya mapitio ya usanifu katika mradi wa Ishololo ili kupata gharama halisi za kukamilisha mradi huo. Ukarabati wa mradi huo utapangwa katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta mbegu mpya za migomba?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali kupitia Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha TARI – Tengeru imefanikiwa kutumia teknolojia ya chupa (Tissue Culture) katika kuzalisha mbegu bora aina ya TARIBAN 1, TARIBAN 2, TARIBAN 3, TARIBAN 4, FHIA 17 na FHIA 23 ambayo ina ukinzani dhidi ya magonjwa (Madoa meusi na Panama (banana wilt) ambayo yamekuwa yakiathiri tija na uzalishaji wa zao la migomba. Uzalishaji wa miche hiyo pia unafanyika kupitia vituo vya utafiti vya TARI – Uyole na TARI – Maruku.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2023 jumla ya miche 30,000 imezalishwa na kusambazwa kwa wakulima katika Mikoa ya Kilimanjaro miche 5,000, Kigoma miche 9,000 na Kagera miche 9,000. Uzalishaji na usambazaji wa miche hiyo unaendelea ili kuwafikia wakulima katika Mikoa ya Morogoro, Mbeya, Arusha na maeneo mengine yenye fursa ya uzalishaji wa zao la migomba ili kuwezesha wakulima kupanda mbegu bora za migomba na hivyo kuongeza tija na kipato cha mkulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa mwaka 2023/2024 Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania imepanga kushirikiana na maabara binafsi za Crop Bioscience na maua mazuri kuzalisha na kusambaza takribani miche 1,500,000 ya migomba aina ya Grand Nain ambayo itasambazwa kwa wakulima wakiwemo wakulima wa Mkoa wa Kilimanjaro.
MHE. CHARLES M. KAJEGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga skimu za umwagiliaji Kata za Kisorya, Igundu, Kwiramba, Namuhura, Butimba na Kasuguti - Mwibara?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Charles Muguta Kajege, Mbunge wa Mwibara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na zoezi la kubaini maeneo yote yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji nchini ili kuyapima na kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kupata sgharama halisi za kutekeleza miradi hii kabla ya kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Tume imejipanga kuyafikia maeneo mbalimbali yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji nchini ikiwemo maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji yaliyopo ndani ya Jimbo la Mwibara ili kuingiza kwenye mpango wa utekelezaji, nakushukuru.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:-

Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha bei ya Zao la Mkonge haitetereki?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha bei ya zao la mkonge haitetereki, Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Mkonge imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha soko la ndani kwa kuongeza matumizi ya ndani katika kutengeneza bidhaa zilizoongezwa thamani kama vile kamba, mazulia, magunia, mapambo na bidhaa za ufumaji na kupunguza matumizi ya bidhaa kutoka nje kama uagizaji wa kamba za plastiki, mazulia na vifungashio.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea kutenga bajeti kila mwaka kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kununua mashine mpya za kuchakata (makorona) ili kuhakikisha kuwa, ubora wa mkonge unaochakatwa unakidhi matakwa na viwango vya soko la ndani na soko la kimataifa na hivyo kuimarisha bei ya zao hilo, nakushukuru sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-

Je ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa skimu za umwagiliaji za Karema na Kabage Mkoani Katavi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge Jimbo la Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilitenga kiasi cha shilingi 84,910,676 kwa ajili ya ukarabati wa mfereji mkuu wa skimu ya umwagiliaji Karema ambapo Mkandarasi amefikia asilimia 80 ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga bajeti ya miradi hiyo ambapo mradi wa umwagiliaji Kabage upo katika hatua ya manunuzi na mradi wa umwagiliaji Karema upo katika hatua za mwisho za usanifu wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji. Ujenzi wa miundombinu katika skimu hizo utakamilika mwaka 2023/2024.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, Serikali inawasaidiaje wakulima wa parachichi Iringa ili waweze kulima kilimo chenye tija?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwawezesha wakulima wa parachichi Mkoani Iringa na kwa nchi nzima, Serikali inachukua hatua zifuatazo: -

(i) Kuzalisha miche milioni 20 kwa kushirikiana na sekta binafsi na kuziuza kwa njia ya ruzuku;

(ii) Kufanya utaratibu wa usajili wa wazalishaji wa miche;

(iii) Kuandaa mwongozo wa kusimamia soko la parachichi na kuandaa mfumo wa madaraja;

(iv) Serikali kujenga vituo vya kuhifadhia parachichi la kuchakata na kuhifadhi (common use facility) katika mikoa mitatu kwa maana ya Dar es Salaam, Kilimanjaro - Wilaya ya Hai na Iringa - Wilaya ya Mufindi, Kijiji cha Nyororo).
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaweka utaratibu wa mbolea kuwekwa kwenye vifungashio vya kilo tano, kumi, 15, 25 na 50?
WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa mahitaji ya mbolea kwa wakulima yanatofautiana hususan kwa wakulima wa mazao ya bustani na mazao mengine ya nafaka. Uhitaji wa mbolea ya mazao ya bustani ni wa kiasi kidogo ikilinganishwa na mazao mengine ikiwemo nafaka na mizizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukidhi mahitaji ya aina hiyo na matakwa ya Sheria na Kanuni ya 32(4) ya Kanuni za Mbolea za Mwaka 2011, Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) imeelekeza waingizaji, wazalishaji na wasambazaji wa mbolea nchini kuanza kufungasha mbolea katika ujazo unao tofautiana kuanzia kilo 5, 10, 25 na 50 ili kuwawezesha wakulima kupata mbolea kulingana na mahitaji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu wa 2023/2024,,Kampuni tatu zimeshaanza kufungasha mbolea, kampuni hizo ni (ETG Inputs Limited, Yara Tanzania Limited na Minjingu Mines and Fertilizers Limited) hata hivyo Serikali inaendelea kuhimiza Kampuni za Mbolea nchini kufungasha katika ujazo tofauti ili kukidhi mahitaji ya wakulima, kuongeza matumizi ya mbolea na kupunguza vitendo vya baadhi ya mawakala kufungua mifuko.