Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Elibariki Emmanuel Kingu (17 total)

MHE. ELIBARIKI E. KINGU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya kaka yangu Mheshimiwa Jafo, nilikuwa nataka nipate hakikisho kwa sababu hivi tunavyozungumza mimi na wananchi tumeanzisha ujenzi wa zahanati katika vijiji 19 kwa nguvu zetu.
Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atanihakikishia kwamba zahanati hizi za Nkunikana, Puma, Msambu, Unyangwe, Chungu, Kinyampembee, Mpetu, Mayaha, Misake, Maswea, Nsogandogo, Kipunda, German, Mahonda, Iyumbu, Mlandala, Kaugeri, Mduguyu, Mpugizi na Namnang’ana ambazo tumezianzisha kuzijenga ndani ya kipindi cha miaka miwili katika huu mgao, Mheshimiwa Naibu Waziri ananihakikishia kwamba na zenyewe zinakwenda kukamilishwa? Hizi ambazo tumezianzisha sisi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza kama nilivyosema pale awali, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Kingu kwa kazi kubwa anayofanya katika ile Wilaya yote ya Ikungi kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa bajeti wa mwaka huu tumetenga karibuni shilingi bilioni 251 katika Local Government Development Grants, lakini katika hizo karibu shilingi bilioni 68 kwa ajili ya kuboresha vituo vya afya na zahanati, yaani yale maboma yaliyojengwa. Katika hizo nilisema pale awali 1.4 billion ni kwa ajili ya Halmashauri ya Ikungi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tu Kamati ya Fedha itakapokaa pale, katika vipaumbele vya umaliziaji wa maboma, haya maeneo ambayo tumesema tutawaletea fedha, basi ni vyema katika ule mpango ni lazima tuhakikishe maboma haya yamekamilika kwa sababu Serikali ndiyo imeshafanya jambo lake hilo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Mheshimiwa Kingu alileta concern kubwa ya Halmashauri yake kuhusu changamoto ya afya. Ndiyo maana kama Serikali kwa ujumla, hivi sasa tunawapelekea fedha za kwanza, karibu shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya pale Ihanja ambapo tunajua pale kutakuwa na theater kubwa na maabara. Kwa hiyo, eneo lile litabadilika.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kutakuwa na fedha nyingine kwa ajili ya ununuzi wa vifaa. Kwa hiyo, Serikali iko tayari kuhakikisha kwamba wananchi wa Halmashauri yote ya Ikungi inapata huduma nzuri kama tunavyotarajia.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, nina nyongeza ndogo. Kwanza kabisa kwa kifupi sana na mimi nimpongeze sana dada yangu Juliana na nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuona vijana wanaweza kumsaidia. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa je, Serikali ipo tayari kuweza kuitumia Miji aidha Mji wa Dodoma au Singida kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Spika, inajulikana kabisa kwamba Singida sasa hivi tayari tuna kiwanja cha kisasa kabisa cha Namfua ambacho kimeshafanyiwa miundombinu ya kisasa na Singida tunaendelea tuna hoteli za kisasa ambazo zimejengwa na wazalendo.
Mheshimiwa Spika, Dodoma pia tunaona Serikali yetu imehamia hapa na Mheshimiwa Rais anakuja hapa, Waziri Mkuu tayari tunae hapa na Makamu wa Rais anakuja. Sasa kwa nini Serikali isiamue tu kwa makusudi kuchagua mikoa hii miwili kati ya Singida au Dodoma kufanyika mashindano ya AFCON 2019? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuweza kuwapongeza Wabunge wote wa Mkoa wa Singida kwa jitihada zao nzuri ambazo wamezifanya katika kurekebisha Uwanja wa Namfua. Nichukue nafasi hii kuomba Wabunge wote lakini vilevile mikoa yote ya Tanzania kuweza kuiga mfano huu mzuri ambao umeoneshwa na Wabunge wa Singida lakini vilevile wananchi wa Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikienda sasa kwenye swali lake la msingi ambapo amependekeza kwamba nini Uwanja wa Namfua, Singida usitumike katika mashindano haya. Niseme kwamba moja ya vigezo ambavyo huwa vinazingatiwa katika kuchagua haya maeneo. Jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba huo mji ambao unapendekezwa uweze kuwa na viwanja ambavyo vinakidhi ubora wa Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kigezo cha pili ni lazima kwamba mji huo uweze kuwa na hoteli ambazo zitaweza ku- accommodate wageni wote ambao watakuja katika mashindano hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme kwamba kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, Mheshimiwa Kingu kwamba sasa hivi kuna Kamati ambayo imeundwa na Mwenyekiti wa hiyo Kamati ni Waziri wangu Dkt. Mwakyembe.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme kwamba nimtoe hofu mimi kama Naibu Waziri nitamshauri Waziri wangu Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe sasa aangalie namna gani kwamba ile Kamati ambayo imeundwa ifike Singida ili kuweza kukagua ile miundombinu ya michezo ambayo ipo katika Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika swali la pili ametaka kujua kwamba kwa nini Dodoma isitumike katika mashindano haya. Kwanza napenda nichukue nafasi hii kuweza kumpongeza sana kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa sababu kwa jitihada zake yeye binafsi sasa hivi Dodoma tunajengewa uwanja mkubwa kabisa wa Kimataifa wa michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba hii inaonesha kabisa kwamba Rais wetu ni Rais ambaye ana ushawishi mkubwa sana kwa Mataifa ya nje lakini inadhihirisha kwamba Rais wetu ni mwanadiplomasia na ni Rais ambaye anapenda michezo ndio maana ameweza kumshawishi Mfalme wa Morocco kuja kutujengea kiwanja hapa katika Mkoa wa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba wazo lake ni zuri na niseme sisi kama Wizara tunachukua hilo wazo lakini kama ambavyo nimesema awali, kwamba uwanja huo unajengwa kwa msaada wa Mfalme wa Morroco. Kwa hiyo, sisi kama nchi hatuwezi kumpa deadline kwamba uwanja huo ukamilike ndani ya muda gani.
Mheshimiwa Spika, tunachokifanya na nimwombe kabisa Mheshimiwa Kingu kwamba endapo uwanja huo utakamilika kabla ya hayo mashindano kufanyika mwaka 2019, basi tutaangalia ni namna gani ambavyo uwanja huo unaweza kutumika katika mashindano hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Naomba na mimi niulize swali moja tu, ni lini Serikali ya Chama cha Mapinduzi itakwenda kutekeleza miradi ya visima 10 vilivyochimbwa Jimbo la Singida Magharibi katika vijiji vya Minyuge, Mpetu, Kaugeri, Mduguyu pamoja na Vijiji vya Mnang’ana, Munyu na Irisya ukizingatia Jimbo la Singida Magharibi ni miongoni mwa Majimbo ambayo yana changamoto kubwa sana ya maji? Naomba nipate jibu serious kutoka kwenye Serikali serious. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kingu kutoka Singida Magharibi, kama ifuatavyo:-

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Siyo daktari.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Nimekutunuku au siyo. Wanasema dalili nje huonekana asubuhi, daktari rudi shule ukapate hiyo profession. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni maeneo yote ambayo yalishafanyiwa usanifu tunakuja kuhakikisha kazi zinafanyika ndani ya wakati. Hivyo visima vyote vitachimbwa kadiri ambavyo vipo kwenye bajeti na maji tutahakikisha hayaishii kwenye kisima bali yanatembea kwenye bomba kuu na kuwafikia wananchi kwenye mabomba yao katika makazi lakini vilevile katika vituo vya kuchotea maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote yanakwenda kutekelezwa kwa kipindi hiki kilichobaki cha mwaka wa fedha na mwaka wa fedha 2021/2022. Isitoshe nitafika kuona eneo husika na kuleta chachu zaidi kwa watendaji wetu, japo tayari tuna watendaji wazuri katika Wizara na wanafanya kazi vizuri sana. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nilikuwa nina swali dogo moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tathmini inaonesha zaidi ya tani 200 za mazao aina ya alizeti zimeteketezwa na ndege hawa. Je, Mheshimiwa Waziri na Serikali wako tayari kupeleka mitego hii haraka kwenye Kata za Mwalu, katika Vijiji vya Mwalu, Minyuve, Mayaha, Ifyamahumbi, Kipunda, Maswea, Igombwe, Ihanja, Mahonda, Mtunduru, Songandogo pamoja na Gerumani ili kuweza kuwasaidia wakulima wetu kwa sababu, kwa kweli jambo hili liko very serious kwa wakulima wa alizeti katika Jimbo la Singida Magharibi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kingu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri Mheshimiwa Kingu amekuwa akifuatilia jambo hili kwa muda mrefu kwa ajili ya wananchi wake na yeye ndio aliyesababisha Wizara ya Kilimo mwaka jana mwezi Mei tukapeleka wataalamu kwa ajili ya kufanya tathmini na kuweza kutambua katika central corridor maeneo yenye maotea ya mazalia ya ndege hawa. Nataka tu nimwambie na nimpe commitment na kuwapa commitment wananchi wake na wananchi wa mkoa wa Singida kwamba Wizara kuanzia mwezi Mei itapeleka wataalamu na vitendea kazi kwa ajili ya kuanza kushughulika na wadudu hawa, ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana, sana, sana, ambayo kimsingi yatawatia moyo sana wapiga kura wangu pamoja na wananchi wa Jimbo la Singida Magharibi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Mradi wa Maji wa Kata ya Mtunduru umechukua muda mrefu sana katika kukamilika.

Nilikuwa nataka nijue; je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutoa agizo kwa Serikali ku-release fedha haraka ili mradi wa maji wa Mtunduru pamoja na vijiji vya Igombwe uweze kukamilika haraka?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza kama yangu Mheshimiwa Kingu. Kiukweli wewe ni Mbunge unayetosha mpaka chenji inabaki. Kubwa ambalo ninataka niseme, sisi Wizara ya Maji tunapokea fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji kupitia Mfuko wa Maji kila mwezi. Ndani ya mwezi huu tutatoa fedha kwa ajili ya mradi wako kuhakikisha tunaukamilisha. Ahsante sana (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru sana na kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza pia kukuona umekaa kwenye hicho kiti kwa kweli kimeku-fit sawasawa. Kama Mbunge kijana nakupongeza sana, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza ni kwamba imekuwa ni habari kwa kweli ya muda mrefu sana, wananchi wa Mkoa wa Singida tumeendelea kupata ahadi, ahadi, ahadi ambazo kwa kweli kimsingi ningependa sana kaka yangu na mtani wangu ninaye muheshimu sana watupe commitment kama Serikali; uwanja huu wa ndege wa Mkoa wa Singida. ambao kimsingi tuko jirani kabisa na Makao Makuu ya nchi lini Serikali inakwenda kuanza ujenzi wa uwanja huu kwa maslahi ya wananchi wa Mkoa wa Singida? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nipate commitment. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Immanuel Kingu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza katika ujenzi wa uwanja wa ndege au kama ilivyo kwenye barabara tayari uwanja huo umefanikiwa kupata hatua ya kwanza. Tumesema usanifu na upembuzi yakinifu umeshafanyika; maana yake tayari hapa tulipo tunajua angalau inahitajika gharama kiasi gani. Tunatafuta mapato ya ndani, lakini pia na washirika wetu wa maendeleo. Tukipata fedha hata kesho Mheshimiwa Kingu, uwanja huu utaanza kujengwa.

Naomba nikuhakikishie kwa niaba ya Serikali kwamba tuna nia ya dhati kwamba kila Makao Makuu ya Mkoa kuwe na uwanja wa ndege ili uweze kutoa huduma katika maeneo yale. Kila Mheshimiwa Mbunge angeweza kupenda baada ya Bunge kuahirishwa apande ndege itue nyumbani kwake kwenye mkoa wake, achangie mapato, lakini pia na wageni wengine wapate huduma kirahisi sana. Ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo zimekuwa zikitolewa na Serikali kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa maboma fedha nyingi zimeonekana zimeshindwa kuyakamilisha maboma yaani kiwango cha shilingi milioni 50 zinakwenda kwenye vijiji lakini maboma hayaishi.

Je, Serikali imefanya tathmini ya kina kujua kwamba level ya maboma iliyofikiwa kwa nguvu za wananchi inahitaji fedha kiasi gani ili kumaliza maboma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ninaomba kumuuliza Waziri ni lini sasa Serikali itapeleka watumishi katika zahanati ambazo zimetengewa fedha na kukamilika ili kuhakikisha wananchi wetu wote wanapata huduma katika zahanati husika katika maeneo husika? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Kingu kwa uchapakazi wake mzuri kwa kuwasemea wananchi wa Jimbo la Singida Magharibi na kwa kweli Serikali tutaendelea kumpa ushirikiano kuhakikisha wananchi wanapata miradi hiyo ya maendeleo kwa ustawi wa jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi ambazo zimepelekwa kwenye ukamilishaji wa maboma ya zahanati, kila boma ambalo limefikia hatua ya lenta linatengewa shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji na tathmini ilifanyika kwa sababu ramani zile zilitolewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na BOQ zake zilionesha jengo likijengwa mpaka hatua ya lenta likipewa shilingi milioni 50 jengo lile linakamilishwa bila changamoto yoyote na ndiyo maana katika maboma 555 yaliyopelekewa takribani shilingi 27,750,000,000 mwaka wa fedha uliopita zaidi ya asilimia 85 ya maboma yamekamilika, yameanza kusajiliwa kwa ajili ya kuanza kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tathmini ilifanyika, lakini kuna variation za kimazingira za hapa na pale ambazo nazo huwa tunazizingatia na kama inajitokeza variation kama hiyo basi tunaona namna nzuri ya kukamilisha ujenzi wa zahanati hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili ujenzi wa zahanati na vituo vya afya kwa ujumla wake unakwenda sambamba na mpango mkakati wa kuajiri watumishi ili zahanati na vituo vianze kutoa huduma na tayari Serikali tumefanya tathmini ifikapo Juni, 2022 tutakuwa na vituo 1,073 ambavyo vitakuwa vimekamlika na tumeshafanya tathmini ya mahitaji ya vifaa tiba, lakini pia na watumishi na kwa kadri ya bajeti yetu tutaendelea kupeleka watumishi ili vituo vile vianze kutoa huduma na kupunguza upungufu wa watumishi katika maeneo hayo, ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, barabara inayotoka Singida kwenda Sepuka kupita Ndago mpaka Kizaga yenye urefu wa kilomita 95 iliahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapunduzi toka mwaka 2015 na Rais Hayati Dkt John Joseph Pombe Magufuli alipokuja kwenye kampeni kwenye Jimbo langu aliahidi kujengwa kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami: -

Je, ni lini Serikali ya Chama cha Mapinduzi itakwenda kutekeleza ahadi hii ikiwa ni moja ya kumbukumbu ya kuenzi ahadi za Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kingu, Mbunge wa Singida kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja ya kutoka Sepuka hadi Ndago, kama alivyosema ni ahadi ya Kiongozi wa Kitaifa; na moja ya vipaumbele vya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatimiza ahadi zote za Mheshimiwa Rais. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii itajengwa. Namwaomba Mheshimiwa Mbunge mara baada ya hapa kwa sababu pengine ni kipindi cha bajeti, basi tunaweza tukaonana ili tuone namna ambavyo tunaweza tukaingiza kwenye bajeti zinazoendelea kupangwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali nyongeza kwamba kwa kuwa barabara hii ilitajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi wa mwaka 2015/2020 haikutekelezwa; ikatajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya 2020/2025 na mpaka sasa hivi tunavyozungumza bado hakuna mchakato wowote wa barabara hii.

Nini kauli ya Serikali kwa wananchi wa Jimbo la Singida Magharibi na wananchi wa Mkoa wa Singida na Iramba kwa ujumla juu ya barabara hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali na kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi na kama alivyosema imetamkwa kwenye Ilani, Serikali inasema inategemea kutangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami mwishoni mwa mwezi huu wa kumi na mbili kwa ajili ya kuanza kuijenga yote kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kujua ni lini Serikali itatekeleza ujenzi wa Barabara ya Singida- Sepuka-Ndago mpaka Kizaga yenye urefu wa kilomita 95 ambayo imeahidiwa kwenye Ilani zote za Uchaguzi 2015 -2020 na 2020 - 2025 lakini mpaka leo barabara hii haijaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kingu, Mbunge wa Singida, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoianisha ni kweli imeainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ni azma ya Serikali kuijenga hii barabara kwa kiwango cha lami kama ilivyoahidiwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mipango ipo na katika utekelezaji wa Ilani wa miaka hii mitano nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii itajengwa kadiri fedha itakavyopatikana. Ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nataka nijue sasa commitment ya Serikali kwa Kata zilizobaki, kwa maana katika majibu ya msingi inaonesha kwamba kuna Kata moja tu imejengewa majosho na Jimbo la Singida Magharibi ni moja ya Majimbo ambayo yana wafugaji wengi sana: -

Je, Serikali lini itakwenda kutekeleza ujenzi wa majosho katika Kata za Igelansoni, Makilawa, Mwaru, Igombwe pamoja na Minyuge?

Swali la pili: Je, Waziri yuko tayari kuongozana nami Mbunge akajionee namna wafugaji wanapata adha kulingana na changamoto ya magonjwa katika mifugo yao kutokana na kutokuwepo kwa majosho?
WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Elibariki Kingu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, natambua ya kwamba uhitaji wa majosho nchini ni mkubwa na kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tumeelekezwa kuweka josho kwenye kila Kijiji kilicho na mifugo. Kwa hiyo, kwenye mpango wetu wa Wizara, mwaka huu fedha tutakaouanza tumeweka pia mpango wa kuendelea kujenga majosho kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini. Sasa tutatoa kipaumbele kwenye maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Kingu; Gelansoni, Iyumbu, Igombwe na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juu ya suala la kuambatana naye ili twende kukutana na wafugaji wake. Niko tayari kufanya hivyo na pengine kama tutapata wakati, weekend mojawapo tunaweza kuambatana ili tukutane na hao wafugaji.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilikuwa naomba kuuliza swali: Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Mgungira – Magungumka – Ufana – Mwankalaja kwenda Kaugeri, Mlandara hadi Mwaru? Kwa maana barabara hii imejengwa madaraja kwa kipindi cha miaka 12, mpaka leo madaraja haya hayajakamilika kwa maana ya kujengewa tuta.

Je, ni lini Serikali itatoa fedha ili TANROADS waweze kukamilisha ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kingu, Mbunge wa Singida, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba tu Mheshimiwa Kingu tuweze kuonana. Kama barabara imejengwa kwa miaka 12 na haijakamilika, tuweze kuona changamoto ni nini? Nitakuomba Mheshimiwa Mbunge baada ya hapa tuweze kukaa tuone nini cha kufanya kuikamilisha hii barabara muhimu sana kwa Wana-Singida lakini pia wananchi wa Jimbo lako. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI E. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa fedha hizi asilimia kumi zinazotolewa kama mikopo zinatokana na tozo pamoja na kodi ambazo wananchi kwa ujumla wengi wanashiriki kuzitoa na zinazokusanywa katika halmashauri yetu;

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuwapitia vijana wote mikopo bila kuwabagua, kama vile Serikali vijana wengi waliojiajiri katika sekta za uzalishaji, ujasiriamali, kilimo na boda boda,?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wanaume, kwa maana ya akina baba nao pia wamekuwa wakijishughulisha na shughuli za uzalishaji. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuwapatia nao mikopo bila kuwabagua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Elibariki Kingu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba asilimia kumi inatokana na mapato ya ndani na inagusa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Na niseme dhahiri kwamba mikopo hii haina ubaguzi wowote kwa vijana, kwa wanawake, wala watu wenye ulemavu. Suala ambalo wanatakiwa kufanya kwa mujibu wa sheria na kanuni za asilimia kumi ni kuomba kupitia vikundi vyao vya ujasiriamali. Na vijana wote wanaomba kupitia vikundi na wakawa na sifa hizo hakuna anayebaguliwa, wote wanapewa mikopo hiyo katika mazingira ya halmashauri zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha kwamba tunawapa fursa vijana wote wanawake na watu wenye ulemavu ili waweze kujiendeleza katika shughuli za kiujasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la wanaume, utoaji wa mikopo hii ni kwa mujibu wa sheria, na sheria yetu ambayo tuliipitisha katika Bunge hili ilisema vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu. Vijana ni umri wa chini wa miaka 35, lakini hoja ya msingi ni kwamba wanaume walio wengi ukilinganisha na makundi haya tayari wanauwezo wa kuwa dhamana, kwa maana ya ardhi, majengo na biashara ambazo zinaweza kutumika kama collateral kwenye mikopo ukilinganisha na makundi haya. Ndiyo maana tuliweka kipaumbele kwa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kwa sababu hawana collaterals zinazowawezesha kupata mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kufanya tathmini kuona uwezekano wa kuingiza wanaume kwa kadri itakavyoona inafaa. Ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya kaka yangu Naibu Waziri Deo Ndejembi nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Shule ya Msingi ya Muhintiri inakabiliwa na changamoto hizo hizo ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri ametoa majibu kwa Shule ya Puma.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kwenda jimboni kujionea msongamano mkubwa wa wanafunzi katika shule hiyo na kuangalia namna ya kuweza kuwasaidia wanafunzi wa Shule Msingi ya Muhintiri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Kingu kuelekea katika shule hii ya Muhintiri ili kujionea msongamano huo na kuweza kuona ni hatua gani Serikali inaweza ikachukua kuweza kutoa msongamano huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya kuwahakikishia Wana-Singida Magharibi kwamba kabla ya mwezi ujao tutakuwa tumesainiwa mkataba wa ujenzi wa barabara ya lami, kilometa 76; tunaipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu; je, Serikali sasa iko tayari kuifanyia upembuzi yakinifu barabara ambayo inatoka Singida – Mtunduru – Ighombwe – Iyumbu mpaka Tabora ambayo itaunganisha na barabara inayokwenda Kwamtoro – Kiteto mpaka Tanga ili kuwarahisishia wananchi wa Singida mawasiliano ya Tanga, Singida na Tabora?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali iko tayari kuipandisha hadhi barabara ya Puma – Ihanja – Iseke – Mwintiri – Igelansoni mpaka Itigi ili kuwapunguzia adha wananchi kutokana na uharibifu mkubwa wa barabara hii unaotokana na hali za mvua zinapokuwa zikinyesha?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa karibu katika barabara hizi zote na hatimaye tunakwenda kusaini mkataba mwezi ujao (Juni).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la kwanza kuhusu upembuzi yakinifu katika hii barabara ya Singida – Mtunduru – Ighombwe – Ngungira mpaka Iyumbu yenye kilometa 113, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Singida Magharibi kwamba katika bajeti ya mwaka tutakaoanza 2023/2024 ambao mlipitisha bajeti siku ya Jumanne, tumetenga fedha takribani shilingi 165,041,665 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, na kwa maana hiyo barabara hii ipo katika mpango kama maandalizi ya kuja kuijenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kupandisha hadhi barabara ya Puma – Ihanja – Mwintiri – Iyumbu; barabara hii inahudumiwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA) na sisi Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tuko tayari kama itapandishwa hadhi kwa kufwata utaratibu ule ambao umewekwa, kwa maana ya kupitia kwenye vikao maalum, kupitia DCC, inakwenda kwenye Road Board ya Mkoa, na hatimaye Mwenyekiti wa Bodi anaandika barua kwa Mheshimiwa Waziri ili Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi atume timu kwenda kuikagua hii barabara na hatimaye tutoe hiyo ridhaa ya kupandishwa hadhi barabara hii, ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nina swali moja dogo la nyongeza.

Kwa kuwa, idadi kubwa ya mahabusu walioko kwenye magereza zetu wanaipa mzigo mkubwa sana Serikali yetu kuwahudumia. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuleta sheria ambayo itawezesha watuhumiwa wakapewa nafasi ya kujidhamini wenyewe ili kuipunguzia Serikali mzigo na kuwapunguzia adha wananchi wanaotekesaka kwenye magereza, kwa makosa mbalimbali ambayo kimsingi yanaweza kudhaminika?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la mtuhumiwa kujidhamini au kudhaminiwa ni kuhakikisha kwamba anarudi mahakamani kwa tarehe itakayotakiwa. Kwa hivi sasa Serikali imejikita katika mpango wa kuweka anwani za makazi pindi zoezi hili litakapokamilika tutakuwa na uwezo wa kujua kila mtu anaishi wapi, hivyo kutakuwa na uwezekano wa kujidhamini wenyewe. Kwa hiyo, kazi ambayo Mheshimiwa Nape anaifanya ikikamilika, pamoja na vitambulisho vya Taifa NIDA, itawawezesha Watanzania kujidhamini wenyewe, hivyo kupunguza msongamano wa mahabusu ambao watakuwa wako nje. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Nilikuwa nataka niulize swali la nyongeza. Ni lini Serikali itakwenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa mawasiliano kwa wananchi wa Kata ya Igombwe pamoja na Ihanja ambapo kuna minara inasuasua sana ikizingatiwa kwamba Kata ya Igombwe ndiyo Kata inayochangia kwa kiwango kikubwa pato la Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Elibariki Kingu, Mbunge kuhusiana na changamoto ya Kata ya Igombwe pamoja na Ihanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu minara tayari imejengwa, ipo. Changamoto ni kwamba Mheshimiwa Mbunge, amesema inasuasua. Tutawaelekeza TCRA kwa sababu kwa mujibu wa sheria, wao wana dhamana ya kuhakikisha kwamba watoa huduma wote wanazingatia quality of service. Kwa hiyo, tutahakikisha tunawatuma watalamu wetu wakajiridhishe, tatizo liko wapi? Kama mnara umezidiwa, basi tujue kwamba tunaongeza nguvu na kama mnara una changamoto ya kiufundi, basi wachukue hatua kuhakikisha kwamba wananchi wa Igombwe na Ihanja ambao ni wananchi wa Mheshimiwa Kingu na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wanapata huduma ya mawasiliano. (Makofi)