Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Magdalena Hamis Sakaya (18 total)

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Malengo ya TASAF III ni kunusuru kaya maskini hapa nchini na kutengeneza miundombinu kutokana na mahitaji na uibuaji wa kaya maskini unaofanywa na wananchi kwenye mikutano ya hadhara:-
(a) Je, ni vigezo gani vinatumika kuondoa kaya zilizopendekezwa kwenye mradi na kubakiza kaya chache wakati malengo ya kaya zinazohitajika, wananchi wameshapewa tangu awali?
(b) Katika Wilaya ya Kaliua, vijiji vilivyoingia kwenye miradi ni 54 tu, wakati katika vijiji vyote kuna kaya maskini sana. Je, ni lini Serikali itapeleka Mpango wa TASAF III kwenye vijiji vilivyobakia kwenye Wilaya hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kujibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Magdalena Hamisi Sakaya, Mbunge wa Jimbo la Kaliua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utambuzi wa Kaya za walengwa unapitia mchakato wenye hatua zifuatazo:-
Hatua ya kwanza ni Mpango wa kunusuru kaya maskini kutambulishwa kijijini na wataalam wanaotoka katika Halmashauri husika kwa kusimamiwa na Uongozi wa kijiji na kisha kuweka vigezo vya kaya maskini.
Pili, wakusanya taarifa wanachaguliwa kutoka miongoni mwa vijana wanaoishi kijijini hapo na kupitia nyumba kwa nyumba ili kuorodhesha kaya ambazo zinakidhi vigezo vilivyoainishwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji.
Tatu, orodha ya kaya zilizoorodheshwa na timu ya wakusanya taarifa kusomwa mbele ya Mkutano wa Kijiji na baada ya hapo jamii hujadili majina yaliyoorodheshwa na kufikia muafaka. Kaya ambazo jamii inaona hazistahili, huondolewa kwenye orodha na Kaya ambazo hazikuwa zimeorodheshwa, huingizwa kwenye orodha.
Nne, kutokana na orodha hiyo ambayo imeandaliwa, kaya hizo hujaziwa dodoso maalum linaloandaliwa na TASAF Makao Makuu kwa lengo la kupata taarifa zaidi za kaya.
Tano, dodoso hilo lililojazwa huchambuliwa kupitia mfumo maalum wa kompyuta ili kupata kaya maskini sana ambazo zinakidhi vigezo kulingana na taratibu za mpango huo.
Mwisho, baadhi ya kaya ambazo hazifikii kiwango cha alama zinazotakiwa huondolewa katika orodha.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya kaya maskini zilizotambuliwa na kupitishwa kwenye Mkutano wa Kijiji mara nyingine zimejikuta zimetolewa wakati wa kuchambua taarifa kutokana na taarifa ambazo mwanakaya aliyedodoswa anakuwa amezitoa wakati wa kujaziwa dodoso.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Kaliua, vijiji 54 vilivyoingizwa kwenye mpango huu wa TASAF ni asilimia 70 ya vijiji vyote ndani ya Wilaya hiyo. Hii ni kwa mujibu wa taratibu za mpango ambapo kila Halmashauri iliyomo ndani ya mpango, siyo Kaliua pekee, imeingiza wastani wa asilimia 70 tu ya vijiji au mitaa iliyomo ndani ya Halmashauri. Asilimia 30 ya vijiji na mitaa iliyosalia katika Halmashauri zote imepangwa kufikiwa katika mwaka 2016.
Serikali ilitoa maagizo hayo ili kuweza kufikia Vijiji, Mitaa, Shehia zote zilizobakia; na kwa upande wa Vijiji, Mitaa na Shehia zilizoanza ndizo zilizokuwa na hali mbaya zaidi. Kabla ya kuanza utekelezaji, takwimu za umasikini zilichukuliwa katika Vijiji, Mitaa na Shehia zote na kuorodheshwa kuanzia ambazo ni masikini sana mpaka zenye unafuu.
MHE. JOHN P. KADUTU (K. n. y. MHE. MAGDALENA H. SAKAYA) aliuliza:-
Njia pekee ya kuinua uchumi wa Taifa linalotegemea kilimo kwa sehemu kubwa ni pamoja na kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo na mifugo;
(a) Serikali ina Mkakati gani wa kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo kwenye Mikoa yote ya kilimo na yenye mifugo mingi nchini;
(b) Wafanyabiashara wa mazao ya kilimo na mifugo wanafanya udanganyifu mkubwa wa kujaza magunia lumbesa, kutanua madebe, pia kupima mifugo kwa macho na kwa kupapasa hali inayowaumiza na kuwapa hasara kubwa wakulima. Je, kwa nini Serikali inashindwa kuweka matumizi ya mizani rasmi kwa mazao hapa nchini?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya Mbunge wa Kaliua lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, na Serikali ya India kupitia Mradi wa Supporting India Trade and Investment for Africa (SITA) imefanya juhudi kubwa kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya nguo na mavazi, ngozi, mafuta ya alizeti na mazao jamii ya kunde. Tayari mikakati ya jinsi ya kuendeleza sekta hizo yenye mipango kamili ya utekelezaji imekwisha andaliwa na utekelezaji wake utaanza mwaka 2016/2017. Aidha, Wizara inapanga kuanzisha makongano ya viwanda katika mikoa ili kuwezesha uzalishaji wa bidhaa. Wizara inahimiza kila Wilaya kuanzisha mitaa ya viwanda vitakavyotumia malighafi zinazopatikana katika maeneo hayo ili kuhamashisha uongezaji thamani katika mazao hivyo kuinua kipato cha wananchi na kukuza ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha mapitio ya Sheria ya Vipimo, Sura ya 340 ili iendeane na mazingira ya sasa. Lengo la Serikali ni kumlinda muuzaji kwa kuwadhibiti wanunuzi wanaotumia njia za udanganyifu. Wizara yangu itawasilisha mabadiliko hayo Bungeni mara taratibu zitakapokamilika. Pamoja na marekebisho ya sheria ya vipimo niliyoitaja hapa juu, wakala wa Vipimo imewasilisha mapendekezo Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ya kutungwa kwa sheria ndogo (By- Laws) katika Mamlaka za Serikali za Mitaaa zitakazowaongoza wakulima na wafanyabiashara kufungasha mazao yao kwa mujibu wa sheria ya vipimo na kanuni zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kurahisisha usimamizi wa matumizi ya vipimo rasmi katika ununuzi wa mazao, Mamlaka za Serikali za Mitaa zitaainisha vituo maalum (Buying centers) katika vitongoji nchi nzima na kwa mazao yote na hivyo hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kusafirisha mazao ambayo yamefungashwa kinyume na sheria ya vipimo. Aidha, Wakala wa Vipimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa itaanzisha vituo maalum vya ukaguzi bila kusababisha usumbufu kwa wafanyabiashara. Maafisa Ugani walioko vijijini watumike kusimamia matumizi ya vipimo rasmi katika vituo hivyo na kutoa taarifa zote muhimu kwa wakala wa vipimo.
MHE. MAGDAENA H. SAKAYA aliuliza:-
Serikali ilifanya ukaguzi maalum kwenye Vyama vya Ushirika vya Mkoa wa Tabora pamoja na Chama Kikuu cha Ushirika (WETCU) tangu mwaka 2014 na kubaini ubadhirifu mkubwa uliofanywa na viongozi kwa kushirikiana na benki mbalimbali.
(a) Je, ni kwa nini mpaka leo ripoti hiyo haijawekwa wazi na hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wote waliohusika na wizi huo?
(b) Vyama vingi viko kwenye hali mbaya na havikopesheki na hivyo kupelekea wakulima kukosa pembejeo za kilimo. Serikali ina mpango gani mahsusi wa kusaidia vyama hivyo vya ushirika kwa kuzingatia mchango wa zao la tumbaku kwenye uchumi wa Taifa hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena H. Sakaya, Mbunge wa Kaliua lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri mwenye dhamana ya ushirika alikabidhi taarifa ya ukaguzi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kupitia kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora mnamo tarehe 18 Septemba, 2014 kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya makosa ya jinai yaliyobainika. Mwezi April 2016, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika alituma maafisa Mkoani Tabora kufuatilia hatua zilizochukuliwa. Ilibainika kwamba uchunguzi umekamilika na watuhumiwa watachukuliwa hatua za kisheria. Hadi mwezi Juni, 2016 maombi ya kuwafungulia mashtaka watuhumiwa yalipelekwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai akiridhia wafunguliwe mashtaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeanzisha kitengo cha sheria kwa ajili ya kuchukua haraka dhidi ya makosa ya jinai katika vyama. Tume imemwandikia DPP kuomba kibali kwa mujibu wa kifungu cha 133 cha Sheria ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013 ili wanasheria wake wapewe mamlaka ya kuendesha mashtaka ya kesi zinazohusu Vyama vya Ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyama vya msingi ambavyo havikopesheki, Serikali inaendelea kuvihimiza Vyama Vikuu vya Ushirika kuangalia utaratibu wa kuvikopesha kwa utaratibu wa kuanzisha revolving fund badala ya kutegemea benki. Chama Kikuu cha Ushirika (WETCU) kilielekezwa kuhakikisha vyama vyake vya msingi 112 kati ya 217 ambavyo havikopesheki viwezeshwe kukopesheka. WETCU imeviwezesha vyama 68 kushiriki kuzalisha tumbaku msimu ujao kwa kutumia fedha za revolving fund. Fedha hizo zinatokana na sehemu ya mgao wake wa ushuru wa iliyokuwa Apex ya tumbaku na sehemu ya ushuru wake jumla shilingi milioni 800. Inatarajiwa kwamba kwa vile fedha hizi ni revolving zitaweza kutumika kuviwezesha vyama vilivyosalia viweze kukopesheka.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI (K.n.y MHE. MAGDALENA H. SAKAYA) aliuliza:-
Wananchi wa Kitongoji cha Twende Pamoja, Kijiji cha Igwisi, Wilaya ya Kaliua wamekuwa wakipata athari kubwa za kiafya kutokana na milipuko ya baruti inayofanywa na Kampuni ya CHIKO, kupasua mawe na kokoto kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Kaliua mpaka Kigoma:-
(a) Kwa nini Serikali isiwalipe Wananchi hao stahiki zao ili waondoke sehemu hiyo na waende kuishi maeneo mengine ambayo ni salama?
(b) Kijiji cha Igwisi kinanufaikaje na Machimbo haya ya Mawe ambayo yapo kwenye eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya CHICO inatekeleza mradi wa ujenzi wa barabara wa kilometa 56 kuanzia Kaliua hadi Kazilambwa. Kipande hiki ni sehemu ya barabara kuu inayounganisha wilaya ya Kaliua, Mkoa wa Tabora pamoja na Mkoa wa Kigoma. Ili kupata madini ya ujenzi wa barabara, Kampuni ya CHICO inachimba mawe na kokoto katika leseni ya uchimbaji mdogo PML namba 001290CWTZ iliyopo katika Kijiji cha Igwisi iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini tarehe 12 Aprili, 2013 kwa TANROADS Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya uchimbaji wa mawe na kokoto inahusisha ulipuaji wa baruti inayoweza kusababisha madhara katika maeneo ya jirani. Ili kuepusha madhara kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo, tathmini hufanyika na kwa sasa tathmini ya wananchi 71 imefanyika na kati ya hao, wananchi 34 ni kwa ajili ya mazao na wananchi 37 ni kwa ajili ya makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya CHICO iliwapa fidia waathirika 71 jumla ya shilingi milioni 473.9 chini ya usimamizi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia TANROADS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Igwisi kinanufaika na Mradi huu ambapo kwa sasa eneo lao linapitika kwa kipindi cha muda mrefu bila kuwa na matatizo yoyote. Sababu nyingine ambazo zinachangia ni pamoja na kunufaika na uchimbaji huo kwa wannchi kuweza kufanya biashara katika maeneo hayo, lakini pia kwa Halmashauri kulipa service levy. Hivi sasa TANROADS inakusudia kulipa shilingi milioni 23 inachodaiwa kwa kipindi cha Aprili hadi Desemba, 2014.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA Aliuliza:-
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ni hifadhi ya kipekee hapa nchini, Afrika na dunia kwa ujumla; hifadhi hii ina vivutio vya kipekee pamoja na kuwa na matumizi mseto (multiple land use) ambapo wanyama na mifugo inachungwa pamoja; kutokana na upekee huo hifadhi hii imetambuliwa
na kuwekwa kwenye maajabu saba ya dunia chini ya Shirika la Uhifadhi Dunia (UNESCO).
Je, Serikali ina mpango gani endelevu wa kuhakikisha hadhi ya hifadhi hii inabaki kwenye ubora wake kwa ajili ya vizazi vya leo na vijavyo na pia kwa uchumi wa Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa eneo la hifadhi la Ngorongoro ni muhimu na lina hadhi ya kipekee inayotokana na wingi na ubora wa vivutio vyake ambavyo vinatambulika Kitaifa na Kimataifa. Vivutio hivyo ni pamoja na matumizi mseto ya eneo, uwepo wa viumbe hai walioko hatarini
kutoweka duniani na umuhimu wa kihistoria uliothibitishwa na tafiti mbalimbali kuwa binadamu wa kwanza aliishi katika eneo hilo takriban miaka milioni 3.6 iliyopita. Aidha, kutokana na sifa hizo Shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO kupitia orodha yake ya maeneo ya urithi wa dunia (World Heritage Sites) imelipatia eneo hilo hadhi ya kimataifa, ambapo tangu mwaka 1979 limekuwa moja ya maeneo ya Urithi wa Dunia
kwa kigezi cha thamani ya maliasili iliyomo (The Integrity for natural value).
Mheshimiwa Spika, pamoja na sifa zilizotajwa hapo juu, kuanzia Februari, 2010 eneo hili limepewa hadhi nyingine kwa kigezo cha eneo la rasilimali mseto za maliasili, malikale na utamaduni yaani the mixed heritage value hivyo basi kwa kutambua upekee huo kwa Taifa, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa eneo hili linabaki katika viwango bora vya uhifadhi kwa kuchukua hatua zifuatazo:-
(a) Kudhibiti ongezeko la idadi ya watu na mifugo ndani ya eneo la hifadhi, zoezi ambalo litaanza rasmi tarehe 12 Aprili, 2017 na kukamilika mwezi Juni, 2017. Aidha, wadau mbalimbali watashirikishwa katika zoezi hili ikiwemo mamlaka za Mkoa na mamlaka ya Wilaya, Taasisi ya Taifa ya Takwimu, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa na TAMISEMI.
(b) Kuendelea kuimarisha ulinzi wa wanyamapori na maeneo yote muhimu kwa shughuli za utalii kama vile crater na kutoruhusu shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo.
(c) Kufanya mapitio ya sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Hifadhi na kuiboresha ili iendane na hali halisi ya sasa.
Zoezi hili liko katika hatua za awali na linatarajiwa kukamilika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018.
MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Wilaya ya Kaliua inakabiliwa na tatizo kubwa sana la maji hali inayosababisha wananchi wake wengi kuteseka kwa kukosa huduma hiyo muhimu na kutumia muda mwingi kutafuta maji umbali mrefu na hivyo kushindwa kufanya shughuli za maendeleo.
Je, mradi mkubwa wa kutoka Mto Malagarasi kwenda vijiji vya Kaliua mpaka Urambo utaanza lini na kukamilika lini?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua tatizo la maji katika vijiji vya Kaliua hadi Urambo, Serikali imeanza kutekeleza mradi wa kutoa maji Mto Malagarasi kwa kumuajiri mtaalam mshauri ambaye anaendelea na kazi ya usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni ya ujenzi. Kazi hiyo imepangwa kukamilika mwezi Oktoba, 2017.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya usanifu wa mradi huo. Aidha, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, na mara fedha zitakapopatikana, itajulikana ujenzi wa mradi huo utaanza lini na kukamilika lini.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Kwa kuwa lengo la Serikali kuruhusu vyombo vya usafiri wa pikipiki kubeba abiria na mizigo ni kusaidia kurahisisha usafiri na pia kutoa ajira kwa vijana hapa nchini lakini ajali zinazotokana na vyombo hivi kwa sasa ni nyingi kuliko vyombo vingine.
(a) Je, Serikali inaweza kueleza ni ajali ngapi za bodaboda zimetokea kwa miaka mitatu toka mwaka 2015
- 2017 na ni watu wangapi wamepoteza maisha kwenye ajali hizo na walemavu ni wangapi?
(b) Je, Serikali ina mikakati gani ya uhakika ya kuokoa maisha na nguvukazi ya Taifa inayopotea kwa usafiri huu?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-
(i) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitatu toka Januari, 2015 hadi Februari, 2017 jumla ya ajali 5,418 za bodaboda zilitokea na kusababisha vifo vya watu 1,945 na majeruhi 4,696.
(ii) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inayo mikakati ya kukokoa maisha na nguvu kazi ya Taifa inayopotea kutokana na ajali za bodaboda. Mikakati hiyo ni pamoja na:-
(a) Kupitishwa kwa Kanuni ya Leseni za Pikipiki na Bajaji iliyopita mwaka 2009;
(b) kutoa elimu ya Usalama Barabarani mashuleni na kupitia vipindi vya redio, televisheni pamoja na vipeperushi;
(c) Kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa waendesha bodaboda;
(d) Kuimarisha usimamizi wa Sheria za Barabarani;
(e) Kusisitiza madereva wa bodaboda kuepuka kuendesha kwa mwendo kasi;
(f) Kuchukua hatua kwa vitendo vyote vya ulevi na kuweka viakisi mwanga (reflectors) ili kuonekana kwa urahisi; na
(g) Kusisitiza matumizi ya kofia ngumu ili kupunguza madhara punde ajali zinapojitokeza.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka mradi wa TASAF awamu ya III katika vijiji ambavyo havijapata mradi katika Jimbo la Kaliua?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa dada yangu Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kunusuru kaya maskini ambao umo ndani ya TASAF awamu ya III unaendelea na utekelezaji wake katika halmashauri 159 pamoja na Unguja na Pemba. Mpango wa kunusuru kaya masikini una sehemu tatu ambazo ni uhaulishaji fedha kwa kutimiza masharti ya elimu na afya kwa watoto walioko shuleni na wale wanaotakiwa kuhudhuria kliniki pamoja na walengwa kufanya kazi za ajira ya muda. Sehemu nyingine ni kukuza uchumi wa kaya kwa kuweka akiba na kuanzisha miradi ya kuongeza kipato na uboreshaji wa miundombinu ya elimu na afya ili kuwawezesha walengwa kutimiza masharti ya elimu na afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kunusuru kaya maskini unatekelezwa katika halmashauri 159 za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa maana ya Unguja na Pemba lakini si katika vijiji, mitaa na shehia zote. Mpango ulipoanza utekelezaji mwaka 2013, rasilimali zilizokuwepo zilitosheleza kufikia asilimi 70 tu ya maeneo yote, ambayo ni sawa na vijiji, mitaa, shehia 9,989 na maeneo yaliyobaki yana vijiji, mitaa, shehia zaidi ya 5000. Kila halmashauri nchini imegusa kwa wastani wa asilimia 30 ya maeneo yake ambayo hayajafikiwa na mpango wa kunusuru kaya maskini na hili si kwa Jimbo la Kaliua pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba yapo maeneo yenye kaya zenye vigezo vya umaskini na uhitaji ambavyo bado havijafikiwa. Serikali ipo katika hatua za mwanzo za kuanza kuandaa sehemu ya pili ya TASAF awamu ya tatu ambayo itaendelea kwa miaka mingine mitano. Lengo la sehemu hii ya pili ni kuzifikia kaya zote maskini nchini na kuimarisha utekelezaji wa mpango na kuwasaidia wananchi kuwa na shughuli za kiuchumi na uzalishaji zaidi ili waweze kuondokana na umaskini.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani endelevu wa kudhibiti ongezeko la watu hapa nchini, iendane na uwezo wa Serikali kupeleka huduma muhimu na za msingi kwa watu wake na wananchi kwa ukamilifu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, kasi ya ongezeko la idadi ya watu hapa nchini ni asilimia 2.7 kwa mwaka. Wastani wa kiwango cha uzazi cha watoto ni watoto watano kwa kila mwanamke mwenye umri wa kuzaa, yaani tangu akiwa na umri wa miaka 15 hadi 49. Ongezeko la idadi ya watu duniani ni matokeo ya mambo makuu matatu kwa pamoja ambayo ni vizazi, vifo na uhamiaji wa Kimataifa. Kwa Tanzania, kasi ya ongezeko la idadi ya watu inatokana na vizazi au idadi kubwa ya watoto ambao akinamama wanajifungua katika uhai wa maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ambayo kwa sehemu kubwa inachangia akina mama wa Kitanzania kuzaa watoto wengi ni pamoja na ukosefu au kiwango kidogo cha elimu kwa wasichana na akinamama. Tafiti zinaonesha kuwa, akinamama ambao wana elimu ya sekondari na kuendelea huzaa watoto wachache zaidi ikilinganishwa na wanawake wasiokuwa na elimu au wenye elimu ya msingi. Wasichana au akinamama wenye elimu wanakuwa na uelewa mpana kuhusu matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango, madhara ya mimba za utotoni, madhara ya kuzaa watoto wengi pamoja na madhara hasi ya baadhi ya mila potofu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina Sera ya Idadi ya Watu iliyoridhiwa na Serikali mwaka 1992 na kufanyiwa maboresho mwaka 2006. Lengo la sera hiyo ni kupunguza kasi ya ongezeko la idadi ya watu ili kuhakikisha kuwa, idadi ya watu iliyopo inaendana na huduma za jamii zilizopo. Baadhi ya mambo yaliyobainishwa katika sera hiyo ni namna Serikali ilivyojipanga kutoa elimu ya msingi na sekondari, usawa kijinsia, umri wa kuolewa, matumizi ya njia za kisasa na wajibu wa kila mdau tukiwemo Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu bila malipo, katika shule za msingi na sekondari inaonesha dhahiri kuwa Serikali imedhamiria kutekeleza Sera ya Idadi ya Watu kupitia nyanja ya elimu. Utafiti wa Afya ya Mama na Mtoto wa mwaka 2015/2016 umeonesha kuwa endapo mtoto wa kike atakaa shuleni kwa kipindi kirefu, uwezekano wa kuzaa watoto wengi ni mdogo kwa vile elimu inamsaidia kujitambua na inampa uwezekano mkubwa wa kujishughulisha na shughuli nyingine za kiuchumi na matumizi bora ya uzazi wa mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na Watanzania wote kwa ujumla kuwa, suala la udhibiti wa ongezeko la idadi ya watu nchini ni suala mtambuka linalohitaji usimamizi wa wadau wote na kwa ushirikiano wa pamoja. (Makofi)
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Serikali imeunda timu ya wataalam kutoka Wizara nne kupitia nchi nzima kuangalia hadhi za hifadhi zetu (Mapori ya Akiba na Hifadhi za Msitu) ili kuja na mpango utakaondoa kabisa migogoro ya ardhi inayotokea kati ya Hifadhi na Wafugaji, Wakulima na Hifadhi na watumiaji wengine.
(i) Je, ni lini kazi hiyo itakamilika?
(ii) Je, mpaka sasa Timu hiyo imetembelea maeneo mangapi na ni mikoa gani?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali iliunda timu ya Kitaifa kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya ardhi hapa nchini. Timu hiyo ilijumuisha wataalam kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya Takwimu.
Mheshimiwa Spika, kazi ya timu hii ni pamoja na kutembelea mikoa yote yenye migogoro; Kupitia na kuchambua kwa kina taarifa na mapendekezo yaliyowahi kutolewa na Kamati, Tume au timu mbalimbali kuhusu utatuzi wa migogoro nchini; Kuainisha vyanzo vya migogoro iliyopo; Kutembelea baadhi ya maeneo yenye migogoro ya muda mrefu pamoja na kukutana na wadau mbalimbali katika maeneo hayo; na Kutoa ushauri na mapendekezo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi nchini.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa timu imefanikiwa kupitia taarifa mbalimbali za migogoro; kutembelea Wilaya 20, Halmashauri 24, Kata 40, Vijiji 74 na kufanya majadiliano na wadau 1,106 katika Mikoa ya Morogoro, Kagera, Geita, Tabora na Katavi. Taarifa ya Timu imekamilika na mapendekezo yamewasilishwa katika Wizara husika kwa utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, jumla ya migogoro 1,750 ilifanyiwa uchambuzi. Kati ya hiyo 564 ilihusu uvamizi wa maeneo ya hifadhi; 218 mwingiliano wa mipaka ya kiutawala; 366 uanzishwaji wa vijiji ndani ya maeneo ya hifadhi; 204 migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji; migogoro 206 ilihusu wananchi na wawekezaji kwenye maeneo ya ranchi, mashamba na migodi; na migogoro 115 inatokana na madai ya fidia. Vilevile kulikuwa na migogoro 77 ambayo inatokana na mchanganyiko wa vyanzo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara husika itaendelea kushirikiana na wadau wakiwemo wananchi kufanyia kazi mapendekezo ya timu ili kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi iliyopo na inayoendelea kujitokeza nchini. Ni matumaini yangu kwamba utatuzi wa migogoro kwa njia shirikishi utasaidia kuondoa migogoro iliyopo kati ya wananchi, maeneo yaliyohifadhiwa na wawekezaji.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Maeneo mengi ya Wilaya ya Kaliua hayana mawasiliano ya simu ya uhakika:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kupeleka mawasiliano ya simu katika Jimbo la Kaliua kwenye Vijiji vya Mpanda Mlohoka, Usimba, Mwamashimba, Usinga, Kakoko, Ibumba, Kombe, Shela, Mkuuyuni n.k.?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli maeneo mengi ya Wilaya ya Kaliua hayana mawasiliano ya simu ya uhakika na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imekwishaviainisha vijiji vya Mpanda Mlohoka, Kakoko, Usinga, Kombe, Shela na Ushimba kwa kuangalia mahitaji halisi ya kufikisha huduma ya mawasiliano ikiwemo idadi ya wakazi, ukubwa wa eneo pamoja na jiografia ya vijiji husika. Baada ya kuviainisha vijiji hivyo, Mfuko wa Mawasiliano umeingiza mahitaji ya vijiji husika katika orodha ya vijiji vinavyotarajiwa kupatiwa huduma ya mawasiliano katika zabuni itakayotangazwa mwezi Juni, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Vijiji vya Mwamashimba, Ibumba na Mkuyuni vitaingizwa katika miradi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha hususani kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Katika kuelekea uchumi wa viwanda Tanzania, Serikali imedhamiria kuwepo kwa viwanda vya kimkakati.
Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Kiwanda cha Kuchakata ao la Tumbaku kinajengwa katika Mkoa wa Tabora?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamisi Sakaya, Mbunge wa Kaliua kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina viwanda viwili vya kuchakata Tumbaku vilivyopo Mkoani Morogoro. Viwanda hivyo ni Tanzania Tobacco Processing Company Limited na Alliance One Tobacco Processing Limited. Viwanda hivyo vina uwezo uliosimikwa wa kusindika tani 120,000 za tumbaku kwa mwaka lakini vinatumia wastani wa asilimia 50 tu ya uwezo huo kwa sasa. Uwezo unaotumika ni mdogo kutokana na mahitaji ya tumbaku kuendelea kupungua katika masoko ya nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usindikaji wa tumbaku una uhusiano wa moja kwa moja na tumbaku inayolimwa ambayo kwa sasa ni wastani wa tani 60,000 kwa mwaka. Uzalishaji umepungua kutoka tani 126,000 mwaka 2010/2011 hadi tani 54,000 mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya tumbaku yamepungua kutokana na kampeni zinazoendelea duniani za kuzuia kutumia tumbaku na bidhaa zake kutokana na athari za afya na mazingira. Kwa upande mwingine, kampeni hizo zimeathiri uwekezaji katika viwanda vya tumbaku na ajira ikiwemo Mkoani Tabora, takribani wafanyakazi 7,000 wamepunguzwa kazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zao la tumbaku bado lina mcahngo mkubwa katika uchumi wa Taifa, Serikali inaendelea kuwahamasisha wawekezaji kutafuta teknolojia bora zaidi ya kuwekeza katika Mkoa wa Tabora.
MHE. JOHN P. KADUTU (K.n.y. MHE. MAGDALENA H. SAKAYA) aliuliza:-
Serikali ilianzisha Wakala wa Misitu (TFS) kwa lengo la kuhifadhi misitu, kulinda na kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali ya misitu:-
Je, ni kwa kiasi gani Maafisa wa Misitu walioko Mikoani, Wilayani wameweza kuokoa misitu inayozidi kuteketea hapa nchini?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS) inasimamia misitu ya hifadhi ya Serikali Kuu ipatayo 455 sawa na hekta15.48 milioni ambayo ni takriban asilimia 35 ya eneo lote la misitu nchini. Eneo hili hujumuisha misitu ya asili na ile ya kupandwa (Forest Plantations). Aidha, TAMISEMI wanasimamia hifadhi 161 sawa na hekta 3.36 milioni wakati serikali za vijiji zinasimamia hifadhi za misitu 1,200 sawa na hekta milioni 21.6. TFS ina kazi za kutafiti, kuhifadhi, kulinda na kusimamia matumizi endelevu ya misitu yote nchini. Kazi hizi zinatekelezwa na Maafisa Misitu wa TFS waliopo katika Kanda Saba na Wilaya 135 za Tanzania Bara wakishirikiana na Maafisa Misitu waliopo chini ya Halmashauri za Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Misitu walioko Mikoani na Wilayani wameweza kusimamia hifadhi za misitu hii na kuwezesha kurejea kwa uoto wa asili katika misitu 271 nchini. Kazi zilizotekelezwa na Maafisa hao ni pamoja na soroveya (Survey and Resurvey) ya misitu husika; kuimarisha mipaka ya misitu kwa kuwezesha takriban kilomita 13,100 za mipaka hii kusafishwa; Kuweka vingingi (beacons) 14,200 vyenye kuonyesha mipaka na hifadhi; Kupanda miti katika mipaka ya misitu na kuweka mabango (sign boards) 4,553 kwa ajili ya kutoa taarifa za uwepo wa misitu ya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Maafisa Misitu wameendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu hatari ya kuwasha moto katika misitu ya hifadhi, athari za kilimo cha kuhamahama, ufugaji ndani ya hifadhi, uchimbaji wa madini na utengenezaji wa mkaa usiozingatia weledi.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-

Mkandarasi aliyepewa tenda ya kujenga barabara ya lami kutoka Urambo kwenda Kaliua kilometa 28 ameonyesha udhaifu mkubwa katika kutekeleza kazi hiyo tangu awali:-

Je, kwa nini Serikali isisitishe mkataba wa mkandarasi huyo haraka kwa kumpata mkandarasi mwenye uwezo na uzoefu ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo muhimu kwa wakati na ubora?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mradi wa Ujenzi wa kwa kiwango cha lami wa barabara ya Urambo-Kaliua kilomita 28 ni moja kati ya miradi iliyotengwa mahsusi na Serikali kwa ajili ya wakandarasi wa ndani ili kuwajengea uwezo na kupata miradi mikubwa ya barabara. Mchakato wa kumpata mzabuni ulifanyika kwa malengo hayo.

Mheshimiwa Spika, aidha, muungano wa Wakandarasi watatu wazalendo, Salum Motor Transport Limited, Annam Road Works Company Limited na Jossam Company Limited walikidhi vigezo na hivyo kushinda zabuni hiyo. Utekelezaji wa mradi huu ambao unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 ulianza rasmi tarehe 30 Agosti, 2017 na muda wa utekelezaji ni miezi 26. Hadi sasa wakandarasi hawa wameendelea na kazi japo kwa kasi ndogo lakini kwa kiwango cha kuridhisha ambapo utekelezaji umefikia asilimia 35.

Mheshimiwa Spika, kasi ndogo ya utekelezaji ilichangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa ambapo mvua nyingi ziliathiri utekelezaji ambapo mkandarasi ameomba kuongezewa muda. Hatua nyingine zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuhakikisha kuwa Mhandishi Mshauri wa mradi anaendelea kuwafundisha wakandarasi hawa kuhusu usimamizi wa miradi ili lengo lililopangwa liweze kufikiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa kutokana na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Seikali, mradi huu utakamilika kwa ubora na viwango vilivyopangwa kimkataba. Hivyo, kusitisha mkataba kwa hatua iliyofikiwa haitakuwa na tija kwa Serikali kwani tuna imani kuwa kutokana na mafunzo wanayoyapata wakandarasi hawa wazawa watakamilisha mradi huu kwa viwango vinavyotakiwa.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-

Matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini yamekuwa na athari kubwa kwenye uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa miji yetu:-

Je, Serikali ina mikakati gani ya kuondoa matumizi ya plastiki hapa nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa matumizi ya mifuko ya plastiki yameongezeka hasa kutokana na mifuko hii kutolewa bure kwenye maduka, masoko, migahawa na maeneo mbalimbali. Aidha, kutokana na baadhi ya nchi jirani kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki na kuruhusu uzalishaji kwa ajili ya soko la nje ya nchi, kumekuwa na wimbi kubwa la uingizaji wa mifuko ya plastiki nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia hali hii na mwelekeo wa Jumuiya ya Kimataifa wa kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki, Serikali inadhamiria kusitisha uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastiki katika siku zijazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imeanza kuchukua hatua zifuatazo katika kuelekea kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki:-

(a) Kuhamasisha wajasiriamali, vikundi vya akinamama na vijana, sekta binafsi na viwanda kuwekeza katika uzalishaji wa mifuko mbadala ikiwemo vikapu vya asilia, mifuko ya karatasi na vitambaa;

(b) Ofisi imeendesha mikutano miwili ya wadau katika Mikoa ya Dar es Salaam tarehe 6 Novemba, 2018 na Mwanza tarehe 18 Novemba, 2018, kuelimisha umma kuhusu changamoto na athari za mifuko ya plastiki na kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa mifuko mbadala kutokana na dhamira ya Serikali kusitisha matumizi ya mifuko ya plastiki katika siku zijazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mikutano hii, wadau na wananchi waliishauri Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika uzalishaji wa mifuko mbadala.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda kuchukua fursa hii, kwa mara nyingine tena kuhimiza viwanda vinavyozalisha mifuko ya plastiki na wadau wengine kujitayarisha kwa kubadili teknolojia na kutathmini fursa zinazojitokeza katika kuzalisha mifuko mbadala hasa katika kipindi hiki cha mpito wakati taratibu za maamuzi ya Serikali zikikamilishwa.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza kwa ukamilifu Sera ya Afya ya kutoa huduma za afya bure kwa wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka mitano pamoja na wazee wenye umri zaidi ya miaka 60?

(b) Mwaka 2014 Serikali ilianza utaratibu wa kuwapatia wazee vitambulisho kwa ajili ya matibabu bure kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali. Je, ni Wilaya ngapi zimekamilisha zoezi hilo muhimu ili kuokoa maisha ya wazee yanayopotea kwa kukosa huduma za afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya jitihada katika kutoa huduma bora za afya na zenye kufikiwa na watu kwa kuandaa sera na miongozo na kusimamia utekelezaji wake. Katika kutoa huduma hizi, Serikali imekuwa ikiyapa kipaumbele makundi maalum kama vile wajawaziti, watoto chini ya miaka mitano, wazee wasio na uwezo na wenye ulemavu ambao kwa namna moja au nyingine hawawezi kujishughulisha na shughuli za kiuchumi na kujipatia kipato kwa kuanzisha sera za matibabu bila malipo kwa makundi hayo. Tangu kuanzishwa kwa sera hii Serikali imekuwa ikisimamia kwa ukaribu kuhakikisha inatekeleza ipasavyo na watoa huduma katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya Serikali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizi ambazo Serikali imekuwa ikizifanya katika kuwapatia makundi haya matibabu bure, bado kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa sera hii kutokana na kuongezeka kwa magonjwa na idadi ya watu walio katika makundi maalum. Hali hii inasababisha watoa huduma kuwa na idadi kubwa ya watu walio katika makundi maalum wakati rasilimali kwa ajili ya kuwahudumia ni ndogo.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hii, Serikali iko katika hatua ya maandalizi ya mkakati wa ugharamiaji wa huduma za afya ambao lengo lake ni kuibua vyanzo mbalimbali vya mapato kwa ajili ya kugharamia huduma za afya kwa maana ya health care sector financing. Moja ya vyanzo vilivyopendekezwa katika mkakati huo ni uanzishwaji wa Bima ya Afya moja (Single National Health Insurance) ambayo uchangiajikatika bima hiyo itakuwani ya lazima kwa wote walio na uwezo wa kuchangia. Kulingana na taifiti zilizofanywa, njia hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza rasilimali fedha katika sekta ya afya na kuweza kugharamia makundi maalum yatakayohitaji msaaha wa kulipia huduma za afya. Mkakati huu unatarajia kukamilika na kuanza kutekelezwa mapema mara baada ya taratibu za Serikali za kufanya maamuzi zitakapokamilika.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa maagizo kwa watoa huduma watenge madirisha maalum kwa ajili ya kuwahudumia wazee na Halmashauri ziwatambue na kuwapa kadi za wazee kwa ajili ya matibabu. Hata hivyo utekelezaji wa utaratibu huu umekuwa na changamoto ambapo takribani asilimia 40 tu za Halmashauri zote zimeweza kutekeleza agizo hilo. Natoa rai kwa Halmashauri zote nchini kutekeleza agizo la Serikali la kutoa vitambulisho kwa Wazee.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA Aliuliza:-

Kutokana na kuwepo kwa magonjwa sugu yanayoathiri mazao ya ndizi, mihogo, minazi na matunda kama michungwa, miembe na kadhalika kumesababisha wakulima kutozalisha kwa kiwango kinachostahili lakini pia mazao haya kukosa masoko ya uhakika nje ya nchi.

Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha magonjwa haya yanapatiwa suluhisho la haraka ili kilimo kiwe na tija na kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sayaka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli magonjwa sugu ya mazao yanaathiri uzalishaji, tija na ubora wa mazao hivyo kusababisha hasara kwa mkulima. Katika kushughulikia changamoto hiyo, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na usugu wa visumbufu hivyo. Mikakati hiyo ni pamoja na kuimarisha tafiti, kuzalisha na kusambaza kwa wakulima mbegu zenye ukinzani dhidi ya magonjwa mbalimbali. Kwa mfano, mbegu za muhogo aina ya Kiroba, Kizimbani, Kipusa, Chereko, Mkuranga 1 na Mkombozi zinahimili ugonjwa wa Batobato na mchirizi kahawia, miche bora ya migomba aina ya FHIA 17, FHI 23, Nshakara na Nyoya zinahimili ugonjwa wa unyanjano wa zao la migomba. Aidha, mikakati mingine ni kuimarisha huduma za ukaguzi wa mimea na bidhaa za mazao yanayoingizwa nchini ili kuzuia uingizwaji wa visumbufu vamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utafiti wa ndani, kikanda na kimataifa ili kupata mbegu kinzani na viuatilifu katika mazao mbalimbali ikiwemo migomba (Resistant and Tolerant Cultivars). Utafiti wa ugonjwa mnyauko bakteria katika zao la migomba unaendelea katika taasisi za utafiti wa kilimo za Maruku, Uyole, Tengeru pamoja na nchi ya Uganda. Aidha, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kushirikiana na Shirika la Belgium Technical Cooperation (BTC) zimetafiti kuzalisha na kusambaza miche bora ya migomba 6,000,000 katika wilaya za Mkoa wa Kagera na Wilaya za Kasulu na Kankonko Mkoani Kigoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima na maafisa ugani wanaendelea kupatiwa mafunzo ya mbinu za udhibiti wa vusumbufu vya mimea kwenye mazao hayo ili kuongeza uzalishaji na tija. Serikali inawahimiza wakulima kutumia mbegu zenye ukinzani dhidi ya magonjwa.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wadau wote wanaotumia rasilimali ya maji katika shughuli zao wanashiriki pia kikamilifu kuhifadhi vyanzo vya maji ikiwemo misitu, mabonde na ardhi?
WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Jimbo la Kaliua kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha vyanzo vya maji vinahifadhiwa, Wizara imeweka utaratibu mbalimbali ili kuhakikisha wadau wote wanaotumia rasilimali ya maji katika shughuli zao wanashiriki kikamilifu kuhifadhi vyanzo vya maji ikiwemo misitu, mabonde na ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu hizi ni pamoja na kuweka muundo wa kitaasisi wa usimamizi wa rasilimali za maji ambao unashirikisha watumia maji kupitia vyama vya watumia maji, utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya 2009 sambamba na sheria ya nyingine zinazohusika katika utunzaji wa vyanzo vya maji na kuandaa na kutekeleza mipango ya pamoja ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini.