Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu (34 total)

DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Kwa kuwa, Mkoa wa Tabora ni kati ya Mikoa ambayo tunalima pamba sana hususan Wilaya ya Igunga, na kwa kuwa miaka ya nyuma tulikuwa na kiwanda hicho cha nyuzi lakini pia tulikuwa na kiwanda cha kuchambua pamba kule Manonga ginnery katika Jimbo la Manonga.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua hicho kiwanda ili kiweze kulisha kiwanda cha nyuzi cha Tabora?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mwizikulu, Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Uwekezaji na Mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwa Mheshimiwa Mchungaji Manjelwa, ili Manoga ginnery ifanye kazi na Viwanda vya Tabora ni lazima ule mkakati mzima wa kuanzia pamba mpaka nguo upitiwe wote. Kama nilivyoeleza ni pamoja na kuzuia nguo zinazokuja katika ushindani usio sawa. Tukiweza kutekeleza hayo wakulima wakaridhika, hivi viwanda vitafufuka vyenyewe, lakini wale waliokuwa wamepewa na Mheshimiwa Mkapa na awamu zilizopita, wakashindwa kutumia fursa hiyo tutawanyang‟anya viwanda hivyo, tutawapa Watanzania wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii ninyi ndiyo wawakilishi wangu, nendeni mkawaambie wananchi anayeona upenyo wowote kwamba mtu anazembea aniletee kielelezo na mimi nitatumia mamlaka niliyonayo kwa kufuata Sheria, tumpe yeye na yeye ajasilie.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo katika swali la msingi, Wilaya ya Igunga nayo ina zahanati kama Jogohya, Mbutu, Mwazizi na Kalangale ambazo hazijakamilishwa. Je, Serikali nayo itaelekeza jicho lake huko kwenye Wilaya ya Igunga pia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Dalaly Peter Kafumu kwamba eneo lako pale, mpaka Jimbo la Manonga kwa Mheshimiwa Gulamali kuwa ni miongoni mwa eneo ambayo nimepanga kuyatembelea. Kwa sababu licha ya suala zima la umaliziaji wa zile zahanati, lakini pia kuna vituo vya afya ambavyo vimejengwa ambavyo hata upatikanaji wa vifaa vyake inaonekana kuna uchakachuaji umefanyika. Na ndio maana nimepanga ziara maalum kwa Wilaya yako ya Igunga licha ya kuangalia namna ya kumaliza zile structure, lakini pia kuangalia juu ya habari niliyoipata ya ubadhirifu uliofanyika katika baadhi ya maeneo. Kwa hiyo lazima nifike site kuja kupambana na hayo yaliyotokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, na naomba nikuhakikishie kwamba wale wote ambao inaonekana wamefanya ubadhirifu katika majengo ya afya tutawachukulia hatua. Uwe na amani ya kutosha, Serikali iko kwa ajili ya kupambana na mambo ya maendeleo katika nchi yetu.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu ambayo hayatoshelezi.
Kwa kuwa mimi nimezaliwa na kukulia katika mbuga hii, ni mashahidi kwamba mbuga hii ilitelekezwa, kwa hiyo, wananchi wengi wakulima na wafugaji walihamia katika mbuga hii. Matokeo yake wanyama na hao ndege anaosema wametoweka; kama wamebaki ni sehemu ndogo sana; na kwa kuwa eneo hili mwaka 2014 lilisababisha mauji ya wakulima watano kutokana na mgogoro wa wakulima: kwa nini Serikali isikubali ombi hili? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa hivi nchi inakabiliwa na migogoro ya wafugaji na wakulima, sisi sote ni mashahidi; na kwa kuwa mwaka 2011 Serikali hii ilifanya tathmini ya mbuga zile ambazo zimepoteza sifa na Wembere ilikuwa ni mojawapo; kwa nini Serikali isilitazame upya jambo hili na kuitenga mbuga hii ili wananchi wanaoishi kwenye eneo hilo waweze kulima na kufuga bila kugombana; lakini pia wanaweza kubakiza eneo dogo kwa ajili ya hawa ndege hawa anaowasema? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la Wembere hivi sasa ninavyozungumza, limegawanywa katika vitalu vinne; Kitalu kinachoitwa Wembere Open Area Central One, kitalu kinachoitwa Wembere Central Area Two, Wembere Game Controlled Area upande wa Kusini, lakini pia upande wa Kaskazini kuna Wembere Open Area, vyote hivi vikiwa ni vitalu vinavyopaswa kuendesha shughuli za uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, mojawapo ya kitalu, kwa mfano, hiki cha upande wa Kaskazini, Wembere Open Area hakijawahi hata kupata mwekezaji kwenye shughuli hizo za uwindaji. Lakini vipo vitalu ambavyo vinafanyakazi, kwa mfano kile cha Open Area Central One, kinatumika na ndiyo hicho ambacho nimesema ni mojawapo ya vitalu vinavyoiingizia fedha Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tunazungumzia mazingira halisi ambayo Mheshimiwa Mbunge anatoka, wakati huo huo tunachokizungumzia ni suala la utaalam vilevile, basi nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba arejee azma ya Serikali tuliyoitangaza hapo awali, kwamba sasa tunataka kufanya zoezi Shirikishi; yeye pamoja na wananchi kwenye eneo linalohusika kwenye maeneo hayo ya Wembere pamoja na timu ya wataalam ambayo tayari tumeshasema baada ya Bunge hili tunakwenda kwenye maeneo hayo kuhakiki, twende tukaoneshane.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuchanganye utaalam na maoni ya wananchi ili tuweze kufikia muafaka sasa kujua kama kuna eneo ambalo ni sehemu ya eneo hili ambalo litaonekana halifai kuendelezwa tena kwa shughuli hii ambayo sasa hivi inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, basi itakuwa hivyo. Kwa sasa hivi tutaendana na sheria kama ilivyo mpaka hapo mabadiliko yatakapofanyika baada ya zoezi lile la Serikali.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu utafutaji wa madini katika eneo la Kalambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, sasa hivi kule mitaani kuna malalamiko kwamba utafutaji umepungua sana, wawekezaji hawaji kwa sababu ambazo hazielezeki. Kwa nini Serikali sasa isichukue hatua madhubuti ili kuhakikisha kwamba utafutaji unakua na tuweze kupata migodi mingine siku za usoni? Ahsante sana.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, msemaji ni geologist nilikuwa nadhani anajua jiolojia na madini duniani yanakwendaje. Hayo yaliyoko mitaani sio ya kitaalam kwamba utafiti umepungua. Ni kwamba kila baada ya miaka fulani madini yanatafutwa yanawekwa store yanakuwa mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya vita ya kwanza, Wajerumani na Wafaransa walileta vijana wao kutafuta madini Afrika. Kufika mwaka wa sitini, madini yakawa ni mengi sana duniani ndiyo maana utafutaji ulizorota hata sekta yetu ya madini miaka ya 70, 80 ikazorota. Miaka ya 90, madini yakapungua dunia, utafutaji ukawa wa nguvu sana na Afrika ilichukuwa asilimia 30 ya bajeti ya utafutaji wa madini duniani kote.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimuambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hata China ambayo ndiyo mchimbaji na mtumiaji mkubwa wa chuma duniani vilevile amepunguza kutumia chuma na ndiyo maana unaona hata Zambia uchumi wao umeyumba kwa sababu walikuwa wanategemea sana shaba iliyokuwa inapelekwa China. Kwa hiyo, hili sio jambo la Tanzania ni kwamba dunia ina madini mengi, utumiaji wa chuma,shaba umepungua sio kwa Tanzania tu lakini utafutaji utakuja tena, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, teknolojia ya dunia inabadilika huwezi ukang‟ang‟ania kila siku dhahabu, chuma au shaba. Sasa hivi madini yanayotafutwa kwa wingi sana duniani ni haya nilivyosema yanayotumika kwenye simu zetu, rare earth elements. Madini hayo hayajapungua duniani yanatumika kwenye simu, televisheni, kwa hiyo, yanatafutwa kwa nguvu sana.
Kingine ambacho kinatafutwa madini ya kutengeneza mabetri kwa sababu hesabu inaonyesha kwamba itakapofika karibu mwaka 2040, asilimia kubwa ya magari mengi duniani yatakuwa ni yanayotumia umeme. Kwa hiyo, madini kama graphite na mengine ndio yanatafutwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo kwamba utafutaji umepungua bali ni madini gani utafutaji wake umepungua. Sababu ni teknolojia ya dunia inabadilika na sisi Tanzania tunajielekeza kwenye madini ambayo ni adimu na ambayo yanatakiwa duniani. Ahsante.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa matatizo ya maji vijijini, Serikali imekuwa ikifanya miradi mingi kama ilivyo katika Jimbo la Kilwa Kaskazini. Mradi wa maji wa Kata ya Itunduru - Igunga, ulitekelezwa, miundombinu ikakamilika, lakini maji hayakupatikana, miundombinu imebaki white elephant. Nauliza ni lini Serikali itatafuta chanzo cha maji ili miundombinu hii iweze kutumika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kuna miradi ambayo ilikuwa ni ya kujenga miundombinu na kutafuta chanzo cha maji. Lakini kwa bahati mbaya vyanzo vya maji vile havikupata maji, kwa sasa tunaendelea, lile eneo ambalo halikupata maji tunatafuta eneo jingine karibu, ili tuweze kupata maji, wananchi waendelee kupata maji. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwenye hii Programu ya Pili yale maeneo ambayo tulitafuta maji tukakosa, lazima sasa tutafute maji tupate tukamilishe huo mpango ambao tulikuwa tumepanga. Kwa hiyo, hilo eneo lako pia, tutahakikisha kwamba tunatafuta chanzo kingine ili uweze kupata maji.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kule Wilaya ya Igunga Jimbo la Igunga kulikuwa na Kata za Kiningila, Sakamaliwa na Kinungu, zilikuwa zimewekwa kwenye Mpango wa Mawasiliano kwa Wote, lakini pia Jimbo la Manonga Kata ya Goweko na Kata ya Mwanshiku. Ni lini sasa mradi huu utatekelezwa kwa maana yake tulitegemea mwaka 2015 na mwaka 2014 yafanyike? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mila zetu, ukiulizwa swali na bosi wako huruhusiwi kujibu kwenye hadhara. Namuomba Mheshimiwa Dalaly Peter Kafumu tukutane ofisini ili tuweze kuwatendea haki wananchi wa Jimbo hili la Igunga pamoja na Jimbo jirani ambalo ameliulizia. Nakuomba sana tuonane ofisini ili tuweze kukutana na wataalam halafu tuliweke sawa, tuone ni namna gani ya kufanya.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yasiyotosheleza sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Swali la kwanza; kwa kuwa kutunza dhahabu kwenye hazina ya nchi yoyote ni kuashiria utajiri wa nchi hiyo; kwa mfano, nchi ya Marekani ina dhahabu zaidi ya tani 8,100 kwenye hazina yake, lakini nchi ya Ujerumani 3,300 na nchi ya Italia ina tani 2,450. Kwa nini Tanzania tunachelea chelea kutunza dhahabu wakati sisi sasa hivi ni wazalishaji wa dhahabu duniani?
Swali la pili, kwa kuwa Tanzania ni nchi inayozalisha dhahabu kama Ghana, ina tani nane kwenye ghala yake, lakini Afrika ya Kusini ina tani 125. Na kwa kuwa kwa kipindi cha muda mrefu dhahabu imekuwa ikipanda thamani. Miaka ya 1900 dhahabu ilikuwa zaidi ya dola 200, miaka ya 2000 ilikuwa zaidi ya 500; sasa hivi ni zaidi ya dola 1000. Kwa nini Serikali inachelea kwamba dhahabu inatelemka bei. Kwa nini sasa Serikali isifanye utafiti ikaangalia nchi zingine zinafanyaje na ikatunza dhahabu kwenye hazina yake kwa ajili ya kupandisha uchumi wa nchi yetu? Ahsante sana.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza, sababu kubwa ya msingi ya Benki Kuu ya nchi yoyote kuweka akiba yake katika dola ni kujiwekea akiba (reserves), hiyo ndiyo sababu ya msingi ya Mataifa yote. Hata katika historia wakati wa vita, dhahabu ilichukuliwa kama mkivamia nchi moja kitu cha kwanza mnachokimbilia kuchukua kwa wale mliowashinda mnachukua ile dhahahu kwa sababu ina hesabika ndiyo inabeba thamani ya vitu. Kwa hiyo, sana siyo kuonesha kiwango cha utajiri katika nchi kama sababu ya msingi ya kuweka akiba yako katika dola. Vilevile tunachelea kuweka akiba yetu katika dola kwa sababu ya msingi….
Mheshimiwa Spika, tunachelea kuweka akiba yetu katika dhahabu kwa sababu ya tabia ya bei ya dhahabu katika miaka ya karibuni kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyoeleza.
Mheshimiwa Spika, hata huko Ghana ambako ni kweli wana akiba ya dhahabu ya tani 8.4 ambayo siyo sehemu kubwa sana ya akiba yao ya reserves na wamekuwa na akiba hiyo toka mwaka 2000, kiasi hicho hakijabadilika. Hali kadhalika Afrika ya Kusini toka mwaka 2016 wamebakiwa na tani 123.8 tu na kiasi hicho kimeteremka na kufikia tani 183.1, lakini ni wasiwasi huo wa mwenendo wa bei ya dhahabu katika soko la dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi Serikali inafanya uchambuzi kuona uwezekano kama tunaweza tukaweka sehemu yetu ya akiba katika Tanzanite badala ya dhahabu lakini hii ni kazi ambayo inaendelea.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake ambayo hayatoshelezi kwa
sababu niliwahi kuuliza swali hili lakini nimepata majibu yale yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la msingi, ni kwa nini tuendelee
kutumia dola katika kununua, siyo uhuru wa soko. Sasa swali la kwanza, kwa nini
Tanzania isitumie utaratibu wa nchi zingine kama Zambia, South Africa, Ghana,
Dubai na Ulaya? Wote tumesafiri tumeona ukifika tu kwenye nchi hizo
unaachana na matumizi ya dola lazima ubadilishe na ukalipe kwa hela yao.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa nini au ni lini Serikali sasa
itakagua haya maduka ya fedha ambayo kwa kweli kuna taarifa za ki-intelijensia
zinasema wanatumika kutorosha fedha zetu? Wakaguliwe, mapato yao
yajulikane na ijulikane pia ni jinsi gani wanazitumia hizi fedha na kuziweka kwenye
soko letu la Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la
kwanza, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi Sheria yetu ya Benki Kuu ya
mwaka 2006, Sehemu ya Tatu, kipengele cha 26 kimeweka wazi kabisa kwamba
fedha halali kutumika ndani ya nchi yetu ni shilingi ya Kitanzania. Pia Sheria ya
Usimamizi wa Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 inaruhusu mtu yeyote kupokea na
nimeeleza kwa nini Serikali yetu imepitisha sheria zote mbili, dhamira ikiwa ni
kukuza uchumi wetu na kuwa na fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie tu Dokta Kafumu
kwamba nchi nyingine hufuata utaratibu kutokana na mazingira ya nchi yao.
Kwa nchi yetu hatujaona athari kubwa ya kuruhusu wageni wetu kutumia fedha
hizi ndani ya uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni lini Serikali itakagua, naomba
nimwambie kwamba, Serikali yetu inakagua siku hadi siku. Kama nilivyosema
katika jibu langu la msingi Serikali yetu haijalala, Benki Kuu kwa kushirikiana na
Mamlaka ya Mapato zinakagua siku hadi siku na sasa miamala yote ya maduka
haya ya kubadilishia fedha yanakuwa monitored na Benki Kuu kupitia TRA. Pia
tunaendelea kuimarisha mifumo yetu ili kuhakikisha fedha na uchumi wetu uko
salama kabisa.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba niulize swali kwamba mwaka 2013 Mji Mdogo wa Igunga ulianzishwa na tumekuwa na tatizo hili ambalo wanalisema wote kwamba umeanzishwa lakini haufanyi kazi. Namshukuru Waziri ameeleza kwenye swali namba 142 kwamba ni Halmashauri inatakiwa isimamie, lakini sisi tumejaribu kuishauri Halmashauri isimamie jambo hilo na nimeweza kufika ofisini kwake mara moja na akaahidi kwamba angeweza kuandika Waraka wa kumwambia Mkurugenzi au kuiambia Halmashauri ifanye jambo hilo na halijafanyika.
Namuomba Mheshimiwa Waziri hebu utusaidie kwa sababu DED sasa hivi hataki kabisa kuisikiliza hiyo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Igunga na hawana bajeti, hawana gari, wana mtendaji tu. Tunaomba Mheshimiwa Waziri utusaidie kama ikiwezekana njoo Igunga ili mamlaka hii iweze kuanza. Ahsante sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia swali la Mheshimiwa Mbunge na tutawasiliana tuone namna bora ya kulifanya jambo hili kwa sababu ni kweli tumekwishazungumza na ni kweli nilikwishatoa maagizo lakini halitekelezeki. Kama nilivyosema, mamlaka hizi zinapoanzishwa zinalelewa na Halmashauri Mama. Kwa hiyo, kama hakuna mipango madhubuti inayopanga mchakato wa namna ya kutafuta rasilimali fedha na rasilimali watu basi tatizo linakuwa kubwa zaidi. Kwa hiyo, tutajaribu kuliona namna lilivyo na halina tofauti sana na scenario za Miji mingine Midogo iliyoanzishwa ili tuone namna bora ya kuweza kulifanya.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali ya nyongeza kwamba barabara ya kutoka Igurubi mpaka Igunga kwenda Loya tuliiombea na tulishapeleka maombi kwamba ipandishwe hadhi. Leo mwaka wa tano kuna shida gani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi ya kupandisha hadhi barabara tunayoyashughulikia sasa ni ya muda mrefu ya kuanzia mwaka 2011/2012 mpaka sasa. Kwa hiyo, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara yako nayo tutakuja kutoa majibu ipi imekubalika kupandishwa hadhi, ipi imekubalika kukasimiwa na ipi tutapendekeza ibakie kwenye Halmashauri, muda sio mrefu maadamu Waziri wangu tayari ameshaanza kulifanyia kazi kwa kasi inayotakiwa kwa sasa...
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa nchi yetu ina maeneo mengi ya masalia ya Wafalme pamoja na majengo; kwa mfano, Mtemi Shomali Mwanansali wa Igurubi, kuna majengo ya Mtemi Humbi Ziyota Mwanantinginya pale Ziba. Kwa nini Serikali sasa isiyatambue maeneo haya yote yenye majengo na masalia ya Watemi nchini kote na kuyatangaza? Najua wenzetu kutoka Ulaya watakuja kuyaangalia. Ahsante sana.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo yalikuwa makazi au hata ni makazi hata sasa ya viongozi wetu wa kimila; Watemi, Mamwinyi na wengineo, kweli ni maeneo ambayo licha ya kwamba ni ya kihistoria, yana vivutio kwa sababu kimsingi yana record ambayo inaweza kutupa hata mafundisho kwa ajili ya siku za usoni. Kama ambavyo tunajua historia na faida zake, kwamba unaangalia tulikotoka, hapa tuliko na huko mbele tuendako, inaweza kuwa ni mchango mkubwa sana kwa upande wa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza tukajiuliza, hivi ni kwa kiasi gani sisi wenyewe kwanza tunatembelea maeneo hayo? Ni kwa kiasi gani sisi wenyewe tunayapenda maeneo hayo na tunayatunza kabla hatujafikiria hata kuyatangaza kwa ajili ya watalii kutoka nje? Sasa wito nilioutoa kabla na napenda kuurudia tena hapa, tuanze sisi wenyewe kwanza kwenye Halmashauri zetu kuanza kuthamini maeneo hayo, kuyaweka vizuri katika ubora wake, halafu baada ya pale, kuwasiliana na Wizara ya Maliasili na Utalii na kuweza kuona namna gani tunaweza kuviboresha na kuvitangaza vivutio hivyo ndani na nje.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa muda sasa nchi za SADC ili kukuza fursa za uwekezaji na soko la pamoja zimeendesha mradi wa ku-harmonise au kuwianisha sera na sheria za nchi hizi ili kuweza kuvuna rasilimali hizi, lakini pia soko liwe la pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali ya Tanzania imeshirikije kwenye mradi huu mpaka sasa? Tumefikia wapi? Maana bila ku-harmonise sheria zetu, soko hili haliwezi kuwa la pamoja na wala hatuwezi kuvuna rasilimali hizi vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Nje, huwa tuna-co-ordinate na kuhamasisha Wizara za Kisekta ili zihakikishe kwamba sera au sheria ambazo zinatofautiana na sheria au sera zilizowekwa na jumuiya, ziwe zimekuwa harmonized na zoezi hili ni endelevu kwa sababu inategemea na matukio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa data zilizokamilika nitampa Mheshimiwa Mbunge ili aweze kuelewa tulipofikia.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake ambayo yametoa matumaini kwamba watafanyia research udongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi, Jimbo la Igunga ni Jimbo ambalo udongo wake hauwezi kujengwa kwa kukwangua barabara lazima uweke tuta kwahiyo hela zinazotengwa kwa Halmashauri hizi hazitoshi kabisa kujenga hizi barabara.
Swali la kwanza, je, kwa nini Serikali isilete upendeleo kwenye Jimbo hili la Igunga ikasaidia kujenga barabara za vijijini?
Swa li la pili, kwa azma ya Serikali ya kuunganisha Mikoa Tanzania, kwanini Serikali isijenge kwa kiwango cha lami barabara inayotoka Kolandoto kupitia Igurubi kwenda Igunga, Mbutu na kwenda mpaka Loya kwenye Jimbo la Igalula na mpaka Tura kwenye barabara ya lami itokayo Tabora kwenda Dodoma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo swali lake la msingi linaeleleza jinsi ambavyo eneo lile linahitaji kutazamwa kwa umakini kwani udongo ule ni tofauti na maeneo mengine.
Kwanza naomba nikubaliane naye kwamba siyo kama suala la upendeleo lakini ni vizuri tutakatazama kulingana na hali ya barabara zile na naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, essence ya kuanzia TARURA, Waheshimiwa Wabunge wengi tumekuwa ni mashahidi hapa tumekuwa tukiomba barabara zetu zipandishwe hadhi zichukuliwe na TANROADS kwasababu tukiamini TANROADS inafanya kazi vizuri zaidi. Naamini kwa kuanzishwa kwa chombo hiki cha TARURA hakika barabara zetu zitatengenezwa katika kiwango ambacho kitakuwa bora zaidi. Naamini na barabara hii ya Mheshimiwa Kafumu nayo kwa kupitia TARURA na kwa sababu inahitaji kiasi kingi che fedha, fedha ambayo itatengwa na Serikali itakuwa nyingi ili kuweza kukidhi hali ya barabara hiyo.
Kuhusiana na swali lake la pili la kuunganisha barabara kutoka Kolandoto mpaka Tura ambayo kimsingi jiografia yake inaonyesha ni kwamba itakuwa ni kiungo kikubwa sana mpaka kufika Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kama Serikali tulichukue, tulifanyie kazi halafu tuone namna itakayokuwa bora katika kulitekeleza.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa nchi yetu ina maeneo mengi ya masalia ya Wafalme pamoja na majengo; kwa mfano, Mtemi Shomali Mwanansali wa Igurubi, kuna majengo ya Mtemi Humbi Ziyota Mwanantinginya pale Ziba. Kwa nini Serikali sasa isiyatambue maeneo haya yote yenye majengo na masalia ya Watemi nchini kote na kuyatangaza? Najua wenzetu kutoka Ulaya watakuja kuyaangalia. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo yalikuwa makazi au hata ni makazi hata sasa ya viongozi wetu wa kimila; Watemi, Mamwinyi na wengineo, kweli ni maeneo ambayo licha ya kwamba ni ya kihistoria, yana vivutio kwa sababu kimsingi yana record ambayo inaweza kutupa hata mafundisho kwa ajili ya siku za usoni. Kama ambavyo tunajua historia na faida zake, kwamba unaangalia tulikotoka, hapa tuliko na huko mbele tuendako, inaweza kuwa ni mchango mkubwa sana kwa upande wa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza tukajiuliza, hivi ni kwa kiasi gani sisi wenyewe kwanza tunatembelea maeneo hayo? Ni kwa kiasi gani sisi wenyewe tunayapenda maeneo hayo na tunayatunza kabla hatujafikiria hata kuyatangaza kwa ajili ya watalii kutoka nje? Sasa wito nilioutoa kabla na napenda kuurudia tena hapa, tuanze sisi wenyewe kwanza kwenye Halmashauri zetu kuanza kuthamini maeneo hayo, kuyaweka vizuri katika ubora wake, halafu baada ya pale, kuwasiliana na Wizara ya Maliasili na Utalii na kuweza kuona namna gani tunaweza kuviboresha na kuvitangaza vivutio hivyo ndani na nje.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna dhuluma sana miongoni mwa wananchi wetu, ni lini sasa Serikali itachukua hatua kwa sababu kuna matukio mengi sana ambayo siwezi kuyaorodhesha hapa, yako kule kwenye Jimbo la Igunga ambapo wananchi wengi sana wamedhulumiwa. Ni lini sasa Serikali itachukua hatua hizo badala ya kutoa onyo tu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kwenye Kijiji cha Lugubu, kijiji kiliamua kutenga eneo moja kuwa eneo la hifadhi, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya watendaji waliwaruhusu wananchi wawili waingie kwenye hilo eneo na kukazuka mgogoro mkubwa sana wa ardhi ambao Mahakama ya Ardhi na Mahakama ya Mwanzo wameshindwa kuurekebisha huo mgogoro. Je, ni lini sasa Serikali itatusaidia jambo hili ili tuweze kutenga eneo katika Kijiji hicho cha Lugubu? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba lini tutaanza kuchukua hatua naomba nikuhakikishie kwanza naomba ikiwezekana atupe orodha sasa hivi, kama kuna watu wa aina hiyo basi tuanze kuelekeza mara moja jinsi gani watu ambao wanakwamisha haki za watu ambao wanadhulumu kwa makusudi na wao wamepewa dhamana tuweze kuwachukulia hatua. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba nimsihi kama ana orodha sasa hivi naomba aikabidhi kwangu tuweze kuifanyia kazi haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine katika Kijiji cha Lugugu ambalo amezungumza kwamba kuna eneo la kijiji limetengwa lakini kuna watu wawili wamekabidhiwa eneo hilo, eneo ni mali ya kijiji, kwa kweli inatia huzuni. Katika hili naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutalifanyia kazi. Naomba nimwelekeze Mkuu wetu wa Wilaya ya Igunga aweze kufanyia uchunguzi wa haraka katika eneo hilo kipi kinachojili ili mradi mwisho wa siku haki ya wananchi iweze kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo hilo halitavumilika hata mara moja na kwa vile nimekubaliana na Wabunge wa Mkoa wa Tabora kwamba nitakwenda Mkoa wa Tabora lakini nitakuwa na interest ya kufika eneo hilo kwenda kujua ni ubadhirifu gani unaofanyika ambao unanyima haki za watu, lengo kubwa tuhakikishe wananchi wanapata huduma inayotakiwa. (Makofi)
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuwa Wilaya ya Ugunga na Jimbo la Igunga kwa ujumla lina uhitaji mkubwa sana wa mabwawa kama ilivyo Lupa; na kwa kuwa mabwawa ya Mwanzugi na Igogo sasa yamefikia uhai wake, yalijengwa miaka ya 1970, hayana nafasi tena ya kuendelea.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutujengea mabwawa mengine mawili kwa ajili ya umwagiliaji kama yalivyokuwa haya mabwawa mawili? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa hoja ya Mheshimiwa Mbunge kwamba mabwawa mengi uhai wake umeisha kwa sababu ya mabwawa hayo kujaa udongo badala ya kujaa maji. Kwa bahati nzuri Jumamosi iliyopita, nilikwenda kutembelea Chamwino, nimeenda kutembelea Bwawa la Chalinze nalo nikakuta lina shida hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimeunda kikundi cha wataalam ili tujaribu kutafuta teknolojia ambayo inaweza ikayaondoa matope kwenye bwawa bila kutumia gharama kubwa. Tukishafaulu hilo Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie, tutatumia teknolojia hiyo ili kuhakikisha mabwawa yote nchini tunaondoa udongo badala ya kuanza kuchimba mengine. Sawa, mengine tutachimba, lakini haya yaliyopo ni lazima tuyahifadhi.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Igunga kwenda Mwanzugi hadi Itumba ilikuwa na mkandarasi wa TARURA aliyewekwa na TARURA anaijenga, lakini uharibifu ulikuwa mdogo sana. Sasa hivi kutokana na mvua kama ulivyosema barabara hiyo imeharibika sana, naiomba Serikali itakuwa tayari kweli kuongezea bajeti kwa ajili ya kuijenga hiyo barabara ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Igunga? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu kwa ujumla ni kweli hali ya mvua zimekuwa excessive kwa maana ya kwamba kuna maeneo mengi yameharibika. Tunazo taarifa kule Koga hapapitiki, lakini tunazo taarifa kule Solwa hapapitiki na maeneo mbalimbali. Kama nilivyosema wakati nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine kwamba tumejipanga kuhakikisha kwamba maeneo yanapitika.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dalaly Kafumu sana muda mwingi tumezungumza juu ya barabara hii na kwa kweli swali lako nazungumza juu ya kuongeza bajeti. Tumejipanga kuitazama hii barabara, najua pia una hamu ya kwenda kuunganika na wenzetu kule upande wa Nyahua. Kwa hiyo, tunaitazama kwa umakini na tutakapopata fursa tutaendelea kuongeza bajeti ili hatimaye hii barabara iweze kutengenezwa vizuri na ipitike muda wote na pia ni huduma kwa wananchi wetu wa Igunga na maeneo ambayo yanazunguka Igunga. (Makofi)
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jimbo la Igunga kama lilivyo Jimbo la Ulyankulu, tuna kata kadhaa ambazo bado hazina mawasiliano. Kata hizo ni pamoja na Kiningila, Isakamaliwa, Mwamashiga, Mtunguru na Kata ya Mwashiku Jimbo la Manonga. Ni lini basi Serikali itasaidia ili wananchi hawa waweze kupata mawasiliano? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Dalaly kwa sababu mara nyingi sana tumekuwa tukikutana ofisini kwa ajili ya kuongelea kata zake hizo alizozitaja ambazo ni kweli hazina mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru vilevile kwamba ameshatuandikia hata kwa maandishi na hii taarifa yake tayari iko kwa watu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ambao tumekubaliana kwamba mwezi saba mpaka wa tisa tutakuwa na ziara nchi nzima kuhakikisha tunaweka mawasiliano ya eneo hilo. Namhakikishia tu Mheshimiwa Dkt. Kafumu kwamba nitakapokuwa nakwenda maeneo ya Igunga nitamtaarifu ili tuwe wote kutembelea maeneo haya. Ahsante.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naishukuru sana Serikali kwa kuendelea kujenga barabara za lami kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais. Naomba sasa nimwulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga imekuwa ikisuasua kwa miaka minne sasa kuilea hii Mamlaka ya Miji Mdogo; na kwa kuwa Mkurugenzi mara kadhaa amesikika akisema kwamba hii Mamlaka ya Mji Mdogo inaweza kufutwa wakati wowote, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuwaita Mkurugenzi, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mtendaji wa Mamlaka hiyo ili waje hapa wapate maelekezo maalum ili waweze kuilea vizuri kama sheria inavyosema?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa idadi ya wakazi wa Mji wa Igunga sasa imezidi, wako zaidi ya 50,000 kiwango ambacho kinaruhusu kuanzishwa kwa mamlaka kamili; na kwa kuwa makusanyo ya mapato kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Igunga pale mjini sasa hivi yanaweza kuzidi shilingi bilioni 2, kiasi ambacho kinaweza kuiendesha mamlaka kamili. Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuanzisha Mamlaka Kamili ya Mji wa Igunga?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt. Dalaly Kafumu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala zima la kumwita Mkurugenzi pamoja na Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hata kabla ya kuwaita, katika maeneo ambayo tulitakiwa kutembelea, nami mwenyewe binafsi nilitakiwa kutembelea ni pamoja na Igunga. Naomba nimhakikishie, kuna mambo mengine ambayo tutajadiliana tukiwa site, naamini naye Mheshimiwa Mbunge akiwepo, ili kwa ujumla wake tulitazame suala hili tuone namna nzuri ya kuhakikisha kwamba Halmashauri inaendelea kuwa na nguvu yake lakini na Mji Mdogo nao uendelee, kwa sababu lengo ni kuhakikisha kwamba Igunga inaendelea kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili ambalo ameuliza kwamba kwa kiasi ambacho pesa inakusanywa na Mji wa Igunga, ifike mahali ambapo sasa iweze kujitegemea kwa kuwa na mamlaka kamili, ni jambo jema. Hata hivyo, nayo ina tafsiri yale tofauti. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba Halmashauri ya Igunga inakuwepo pamoja na vyanzo vyake kwa ujumla. Sasa kuna uwezekano mkubwa ambapo ukisema Halmashauri ya Mji ijitenge, maana yake Halmashauri nayo inategemea vyanzo kutokana na mji, ikiunganisha na vile ambavyo ni vya nje ya mji ndiyo maana Halmashauri ya Igunga inakuwepo. Kwa hiyo, ni vizuri suala hili kwa picha kubwa zaidi ili tuone namna nzuri kutoiua Halmashauri ya Igunga lakini wakati huo huo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Igunga nayo ifanye kazi kama ilivyokusudiwa na wananchi.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.
Wilaya ya Igunga ina Kata 35 na ina Vituo vya Polisi saba, Kituo cha Igunga, Nanga, Ziba, Simbo, Sungwizi na Choma na Igurubi lakini ina magari mawili tu ya polisi. Nauliza ni lini Serikali itasaidia Wilaya ya Igunga ikapata magari mengi ili kuhudumia wananchi wetu?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kafumu kwa kulileta swali ambalo linaungwa mkono na jiografia ya Wilaya ya Igunga na naitambua Wilaya ya Igunga na natambua umuhimu wa swali alilouliza Mheshimiwa Kafumu, niseme tu tutaweka uzito pale tutakapokuwa tunagawa vitendea kazi kulingana na upatikanaji wake.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, nakushuru. Swali la kwanza, kwa kuwa barabara hii ya Buhekela-Miswaki-Loya mpaka Iyumbu na ile barabara ya Igunga-Itumba-Simbo ni barabara ambazo zinapita kwenye Mbuga ya Wembele mahali ambapo ni lazima ujenge tuta kubwa ili barabara iwezekane siyo kuchonga, kwa hiyo, kuna madaraja mengi yanahitajika kujengwa.
Mheshimiwa Spika, Sh.225,000,000 za barabara ya Iyumbu na zile Sh.297,000,000 za barabara ya Itumba hazitoshi kabisa kuzijenga barabara hizi. Waziri anatoa commitment gani kuhusu kuongeza bajeti ili kujenga hii barabara kwa kiwango ambacho zitaweza kupitika wakati wowote?
Swali la pili, kwa kuwa ile barabara ya Igunga-Itumba- Loya kipande cha Itumba - Loya hakina fedha, kwa sababu inaenda Simbo kwanza. Ni lini basi Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kile kipande cha Itumba-Loya? Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli swali hili amekuwa akiuliza sana kuhusu kipande hicho cha Mbuga ya Wembele ambayo inahitaji special consideration na ni ukweli usiopingika kwamba inahitaji bajeti kubwa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama Serikali tunalitambua hili, lakini kinachogomba ni suala la bajeti, pale hali itakavyokuwa imeimarika hatutasahau kwa sababu eneo lile linahitaji pesa nyingi. Naamini katika bajeti zijazo, kabla hatujafika 2020 tutakuwa tumeshaikamilisha. (Makofi)
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza; kwa kuwa Vituo vya Utafiti wa Kilimo kama Uyole kama alivyoeleza Mheshimiwa kwenye jibu lake vina umuhimu wa pekee katika kuendeleza mazao yote. Ni lini basi Serikali itafikiria kuja katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako sisi maeneo sio tatizo, wakajenga kituo cha kushughulikia zao la pamba kama ilivyo Uyole na Naliendele kwenye zao la korosho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Igunga sisi tuna kituo kidogo cha Mbegu na ardhi yao ni nzuri lakini kama Serikali tunajipanga kuhakikisha kwamba tunapanua suala zima la vituo vyetu vya utafiti na hata ukizingatia kwamba sasa hivi tumehakikisha kwamba tuna Taasisi yetu ya TARI ambayo itakuwa inajitegemea kwa masuala yote ya utafiti kwa ajili ya kuboresha na kuweza kuandika maandiko mbalimbali ili waweze kupata pesa nyingi zaidi kutoka kwa wahisani mbalimbali katika kuhakikisha suala zima la utafiti linatendewa ubora na haki inayostahili. Ahsante.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pia namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake. Hata hivyo, niseme tu kwamba swali langu la msingi ni nini kimesababisha kupungua kwa shughuli za utafutaji wa madini, mafuta na gesi kwenye nchi yetu halijajibiwa na hilo ndilo swali langu la kwanza la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la nyongeza ni kwamba, mwaka jana tulitunga sheria nzuri za kulinda rasilimali za uziduaji, yaani madini, gesi na mafuta ambazo ni “The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act, 2017”; The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms) Act, 2017; na ile Sheria ya Madini ilirekebishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu; sheria hizi ni nzuri sana, lakini zimesababisha changamoto kadhaa ambazo zimefanya kupungua kwa shughuli za uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kuwekwa kwa asilimia 25 ya retention kwa wachimbaji wadogo wanapotaka kuuza madini. Kodi hiyo inawafanya wachimbaji wadogo washindwe kufanya biashara ya wazi. Je, ni lini Serikali itachukua hatua kurekebisha changamoto hizi ili kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Madini na Mafuta? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya msingi nimejaribu kuelezea ni jinsi gani wawekezaji wanavyozidi kuongezeka kuomba leseni za kufanya tafiti pamoja na leseni za uchimbaji mkubwa na uchimbaji wa kati, vile vile wakiwepo wachimbaji wadogo. Ongezeko hili limezidi na hii inaonesha dhahiri kwamba bado wawekezaji wanazidi kuja kutaka kuwekeza kwenye nchi yetu. Hii ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya sheria ambayo tuliyopitisha katika Bunge lako Tukufu mwaka jana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile mabadiliko yale ya sheria yalikuwa ni kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi yetu. Hata hivyo, tunaendelea kuboresha na kuna kanuni ambazo tumezitoa mwaka huu wa 2018 ambazo kwa kweli wawekezaji wengi walisubiri kuangalia zile kanuni zinakwendaje. Baada ya kuzitoa zile kanuni wengi wamezipitia, wameziona na wengi wameona kwamba wana uwezo wa ku-comply, yaani wana uwezo wa kuendana na zile kanuni na sheria kadri tulivyoweza kuibadilisha. Kwa hiyo wawekezaji wanaendelea kuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunaendelea kuwawezesha GST waweze kufanya tafiti za kina, waweze kufanya tafiti hadi kufanya zile resource estimation, kwa maana ya kuangalia resources tulizonazo ili baadaye tuwe na uwezo wa kuifanya GST iweze kuuza leseni kwa njia ya mnada. Ili wawekezaji wanapokuja wawe wanakuja kwa nia ya kuchimba tu, ili tuwaondoe katika ile nia ya kutaka kuja kukwekeza kwa maana ya utafutaji wa madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule utafutaji wengine unawafanya wasite kuja. Hata ukiangalia dunia nzima siyo Tanzania tu uwekezaji katika kutafuta madini umepungua kidogo. Kwa hiyo sisi kama Serikali inabidi tujiongeze kuangalia namna ya kufanya resource estimation, kuangalia kwa kina ili mwekezaji anapokuja aje kuwekeza kwa maana ya kuchimba tu si kutafuta. (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumuuliza swali moja Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa, moja ya mbinu za kuhamasisha wawekezaji ni kushauriana nao na hasa sekta binafsi; na kwa kuwa nafahamu Serikali ilianza mashauriano ya kila mwezi na wawekezaji, naomba kufahamu kitu gani hasa kimejadiliwa na mwelekeo wa Serikali ni nini kwenye jambo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali sasa imekuja na mpango wa kuhakikisha kwamba tunakaa na sekta binafsi kujadiliana changamoto zilizopo, mpaka sasa tunavyozungumza vimeshafanyika vikao vitatu ambapo viwili vilifanyika Dar es Salaam na kimoja Dodoma. Kikao hicho sasa ndiyo kimetengeza hasa hii Blue Print kutokana na changamoto ambazo walizisema sekta binafsi ambazo zinawakwaza kwenye ufanyaji wa biashara, Serikali ikaichukua na ndiyo maana tumetengeneza hiyo document kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira wezeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama Serikali tunafahamu kwamba ni muhimu sana kuitunza na kuilea sekta binafsi kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pia naishukuru Serikali kwa kutuletea fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya afya viwili. Pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi inaelekeza kwamba tujenge zahanati kila kijiji na Wilaya ya Igunga na Jimbo la Igunga mahsusi kuna vijiji ambavyo zahanati zimejengwa zikakamilika zaidi ya vijiji 10 kikiwepo Kijiji cha Kagongwa, Mgongolo, Makomelo, Chagana, Imalanguzu, Mwamakona na vijiji vingine. Ni lini Serikali itakwenda kukamilisha yale yaliyobaki pia kuleta watumishi ili zahanati hizo ziweze kuanza kufanya kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Wilaya ya Igunga pamoja na Jimbo la Igunga na nchi nzima kwa ujumla wananchi walijenga maboma mengi sana ya zahanati ili kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini mpaka sasa hivi maboma hayo yapo tu na tumeomba sana tangu mwaka juzi Serikali itusaidie maboma haya yakamilike ili zahanati zianze kutumika kwa wananchi wetu katika vijiji vyetu. Je, ni lini Serikali itakamilisha maboma hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mheshimiwa Dkt. Kafumu ameshatoa taarifa hii katika Ofisi ya Rais - TAMISEMI na ukilinganisha Igunga na maeneo mengine pia kuna maboma na zahanati nyingi ambazo zimekwishafanyiwa kazi. Tumeshaomba kibali kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi (Utumishi) ili tupate kibali cha kupata watumishi na wataalamu wa tiba katika maeneo haya ili waweze kutoa huduma. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvumilia, tukipata kibali hicho na kadri fedha zitakavyopatikana basi tutaajiri na kuhakikisha kwamba vituo vyote vinafanya kazi kama ambavyo nguvu za wananchi zimetumika katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kweli kwa taarifa tuliyonayo maboma ambayo yamekamilishwa nchini ni mengi kama ambavyo Jimbo la Igunga na Tabora kwa ujumla wamefanya. Hili nalo tunaomba tuahidi kwamba huu ni mwaka wa fedha, tumetenga fedha kwa bajeti ya mwaka 2019/2020 ili tumalizie maboma haya. Tunaomba wananchi waendelee kuisaidia Serikali kujenga maboma, tujitahidi kukamilisha ili huduma iweze kupatikana. Ahsante.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba niishukuru Serikali sana kwa kazi nzuri inayofanya ya kufanya utafiti wa awali ili kuchora ramani za kijiolojia. Hata hivyo, napenda niikumbushe Serikali kwamba iliahidi kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwafanyia utafiti wa kina maana yake minor exploration kwa kupitia STAMICO. Ni lini basi Serikali itafanya kwa sababu wachimbaji wadogo hawana huo mtaji wa kufanya huo utafiti wa kina kwa ajili ya uchimbaji wakiwemo hao wachimbaji na wanaotafuta madini ya chokaa kule Kondoa. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, Serikali ilitoa ahadi kuwasaidia wachimbaji wadogo kufanya tafiti mbalimbali na hasa tafiti za kina, kuweza kujua kuna kiasi gani cha madini katika maeneo mbalimbali na madini tofauti mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza tu STAMICO tayari imekwishanunua mtambo wa ku-drill yaani drilling machine kwa ajili ya kuweza kufanya tafiti za kina. Mtambo huo kwa kweli tayari upo na tumekwishaanza kufanya tafiti mbalimbali maeneo mbalimbali na niwaase tu wale wachimbaji wadogo ambao wanahitaji huduma hiyo wanaweza sasa hivi wakaleta mahitaji yao au maombi yao katika Shirika letu la Taifa, yaani STAMICO kwa ajili ya kufanyiwa hizo exploration.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tutaendelea kununua mashine mbalimbali ambapo tunaweza sasa tukaendelea kufanya tafiti za kina na kuweza kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa sababu tunatambua uchimbaji wao wa kubahatisha ambao unawatia hasara, wengine wanapoteza fedha nyingi kwa sababu ya kwenda kubahatisha. Uchimbaji wa kubahatisha unasababisha umaskini mkubwa. Ahsante sana.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Moja ya tatizo kubwa la wakulima wa pamba ni bei ndogo kwa sababu inasimamiwa na soko la dunia. Mwaka 2015/2016 na hata 2017, Serikali iliahidi kuanzisha Mfuko wa Kurekebisaha Bei ya Pamba. Nataka kuiuliza Serikali inasema nini juu ya ahadi hiyo ili wakulima wa pamba sehemu zinazolimwa pamba waweze kupata bei nzuri wakati wote?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kafumu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge angependa kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha tunasaidia kuinua bei ya pamba nchini. Kama mnavyojua suala la uinuaji wa bei ya pamba unatokana na factor mbalimbali ikiwemo factor ya tija na chini ya SDP II, Serikali tuna mpango mzuri wa kuhakikisha tunawasaidia wakulima wa pamba na mazao mengine nchini kuongeza tija sambamba na ku-plan mapema masuala ya masoko kwa wakulima wetu.

Kwa hiyo, kwa combination ya factor hizo mbili, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Kafumu kwamba tutaweza kuleta uchochezi wa kuinua bei ya pamba pamoja na mazao mengine nchini. Nimuombe baada ya hapa tukae tuangalie hata hili suala la Mfuko wa kuinua zao hili inaweza ikawa ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuinua zao hili.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante, bonde la Mto Manonga kama lilivyo bonde la mto Mkomazi kuna Skimu ya Umwagiliaji ya Igurubi, ambayo ilijengwa miaka ya 1980 lakini sasa hivi ilibebwa na maji wakati wa msimu wa mvua uliopita. Naiomba Serikali basi kama inaweza kwenda kuifufua hiyo skimu ili wananchi wa eneo hilo waendelee na kilimo cha mpunga, lakini pia skimu zingine ambazo za namna hiyo zilizoachwa kama kule Kibaha Vijijini na sehemu zingine ziangaliwe zote ili ziweze kufufuliwa, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru, kwanza ombi lake la kwenda kufanya ukarabati mkubwa kwenye skimu hii ya Igurubi kwanza tunalipokea, lakini nichukue nafasi hii kuwaeleza Wabunge wote skimu ziko nyingi sana katika Taifa hili, tuna eneo zaidi la hekta milioni 29 zinafaa kwa umwagiliaji na mpaka sasa miaka 58 tumeendeleza hekta 4,75,000 tu. Kwa hiyo, tukitumia au tukitegemea skimu hizi zote kuendeleza kwa kupata pesa za kibajeti tutachelewa sana, sisi kama Serikali na ndiyo maana tulianzisha benki ya mkakati ya Maendeleo Benki ya Kilimo kwa ajili ya kuendeleza miradi mikubwa hii.

Kwa hiyo sasa hivi Benki ya Maendeleo ya Kilimo itapita kila Halmashauri ambayo iliyokuwa na eneo hili la umwagiliaji kwa ajili ya skimu zingine tuziendeleze kwenye kilimo cha kibiashara kwa ajili ya kupata mikopo yenye riba nafuu ili badala ya kusubiri hela za kibajeti ili tuweze kuendeleze skimu hizi kwa muda mfupi Tanzania nzima.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Wilaya ya Igunga kwa kupindi cha miaka mitano sasa shughuli zake za uchumi zimeongezeka sana, watu wanalima, watu wanafuga na kuna fedha nyingi mzunguko ni mkubwa, lakini tatizo ni kwamba tuna benki moja tu Benki ya NMB. Benki ya CRDB walikuja wakafanya evaluation wakaona economic viability pale ni nzuri na wakaja wakatembea, lakini mpaka sasa hivi hawajaanzisha benki. Naomba Serikali, ni wakati sasa kama wanaweza kutusaidia kuiambia Benki ya CRDB wafungue tawi pale Igunga. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Peter Dalaly Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimepokea taarifa yake ya kwamba Benki ya CRDB ilifika na kufanya economic analysis na commercial viability ya Wilaya yetu ya Igunga, na mimi nimepokea maombi yake, nitawasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa CRDB kuhusu kujua utafiti huo umefika wapi na nini maamuzi yao, kama inaonekana kuna commercial viability nina uhakika mkubwa kwa sababu CRDB ni moja ya benki inayowafikia wananchi, watafika Igunga.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mwaka 2002, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, kanuni ililitangaza eneo lile kuwa eneo maalum lakini pia iliamua kujengwe ukuta na mwisho tanzanite itangazwe kuwa nyara. Naishukuru sana Serikali kwa kutekeleza hasa ujenzi wa ukuta, Serikali inayoongozwa na jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, wanafanya vizuri sana kuiendeleza sekta hii ya madini.

Mheshimiwa Spika, naomba basi niulize swali dogo la nyongeza; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekubali ushauri wangu, ni lini basi ushauri huu atautekeleza? Ahsante sana.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, mjiolojia mbobezi hapa nchini wa madini; nataka tu nimtoe wasiwasi kwamba jambo hili ndani ya Serikali tumeanza kulijadili kwa muda mrefu na katika hatua mbalimbali tulizowahi kufikia ni pamoja na mashauriano ya kuona namna gani ili tuweze kuyafanya madini haya ya tanzanite kuwa nyara ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie kwamba tunalichukua kwa uzito wake, lakini ilikuwa lazima tuanze kwa hatua ya kwanza ya udhibiti, na hatua ya kwanza ya udhibiti ilikuwa kujenga ukuta na kuweka mifumo ya usimamizi wa madini ya tanzanite.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo unakumbuka, katika madini ambayo yalikuwa hayajawahi kusimamiwa vizuri hapa nchini ni madini ya tanzanite yaliyopelekea kiasi cha madini ya tanzanite ambayo tulikuwa tunayaona kwenye mfumo rasmi wa Kiserikali ilikuwa ni asilimia tan tu ya madini yaayochimbwa.

Mheshimiwa Spika, sasa nafurahi kusema kwamba hatua ya mwanzo ya kuweka mifumo imeshakamilika, hatua ya pili ilikuwa kujenga masoko ili tuwe na uhakika wa mahali pa kuyauza, hatua ya tatu ni kuweka mitambo au viwanda kwa ajili ya kukata madini ili uongezaji wa thamani uweze kufanyika ndani ya ukuta.

Sasa hatua ya mwisho ni hiyo sasa ya kutangaza haya madini kuwa nyara ya Serikali, hili na lenyewe Serikali inalitafakari, baada ya muda wakati wa mashauriano Mheshimiwa Dkt. Kafumu na yeye tutazingatia kuchukua ushauri wake.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Bajeti ya mwaka jana nilipata fedha kwa ajili ya kujenga barabara ya kutoka Igunga kwenda Itumba na barabara ya kutoka Mbutu kwenda Kininginila lakini niliuliza swali Bunge lililopita kwamba kwa nini barabara hizi hazijajengwa na Waziri aliniahidi kwamba wataanza kujenga mara moja lakini hadi sasa barabara hizi hazijaanza kujengwa. Nini kinachojiri huku?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Kafumu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Kafumu, nafahamu kwamba tumeongea mara nyingi juu ya mtandao wa barabara katika Jimbo lake la Igunga na kwa kweli eneo lake hili ni bonde, kuna mabonde makubwa sana. Nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Kafumu kwamba tumejipanga na nimwombe tu baada ya Bunge hili tukutane ili angalau tuweze kupitia kwa upana kabisa juu ya barabara zake na kuona namna ambavyo tumejipanga kuzishughulikia. Ipo mipango mizuri tu, namwomba sana tuonane ili aweze kupata ufahamu wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba niulize swali, barabara ya kutoka Igunga - Itumba - Loya madaraja yake pamoja na barabara yenyewe imeharibika sana na ilipata fedha kwenye bajeti iliyopita lakini mchakato wa kumpata mkandarasi umechukua muda mrefu sana. Nimeongea na TARURA hata Makao Makuu bado sasa ni miezi sita. Je, ni lini barabara hii itakarabatiwa kwa sababu fedha ipo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la kaka yangu Mheshimiwa Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuseme kwamba kulikuwa na changamoto kwako na Nzega kule kwa Mheshimiwa Bashe, tumepeleka hela kwa pamoja daraja kule kwa Mheshimiwa Bashe limekamilika lakini kwako Mheshimiwa Dalaly bado kuna changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kueleza maneno mafupi, nimuagize Mtendaji Mkuu wa TARURA, Bwana Victor Seif ahakikishe kwamba ndani ya mwezi mmoja nipate matokeo nini kinafanyika eneo hilo kwa sababu fedha zipo hatuna sababu ya kuchelewa. Kwa hiyo Mheshimiwa Kafumu haya ni maelekezo yangu ndani ya mwezi mmoja nipate status ya ujenzi huo na ndiyo maana namuagiza Mtendaji wangu Mkuu wa TARURA afuatilie eneo hilo.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, napenda nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake nina maswali mawili ya nyongeza;

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye swali la msingi Kata za Isakamaliwa Mbutu, Igunga, Nguvumoja, Lugubu, Itumba na Igoweko kwenye Wilaya ya Igunga zimo ndani ya Mbuga ya Wembere na mimi nilizaliwa na kukulia humo na kuna migogoro mikubwa sana ya wafungaji wakulima pamoja na mbuga hiyo.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni kwa nini ile Kamati ya Mawaziri iliyokuwa imeagizwa na Mheshimiwa Rais kupitia maeneo ya namna hii ili kutafuta suluhisho haikufika Igunga?

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni lini Serikali itapima eneo hili kupunguza maeneo ambayo yamekosa sifa kuwapa wananchi, lakini maeneo ambayo yanahitaji kuhifadhi kama alivyoeleza umuhimu wake yaendelee kutumika?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia kwa umakini sana utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais kuhusu maeneo yote yenye migogoro na ambayo wananchi tayari wamekwishaanza kuyatumia lakini yamepoteza hadhi ya kuifadhi. Kwa ujumla wake pamoja na Wabunge wengine taarifa hii kama nilivyojibu kwenye Swali la Mheshimiwa Mipata iko mezani kwa Mheshimiwa Rais na tunasubiri maelekezo.

Mheshimiwa Spika, kwa kujibu swali lake la kwanza Kamati ilipewa mwezi mmoja kuwa imekamilisha taarifa ya nchi nzima na kwa kweli haikuweza kuzunguka nchi nzima kufikia maeneo yote, lakini kwa kutumia mfumo wa Serikali ambayo ipo kila sehemu kupitia Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, Kamati ilipokea maeneo yote yenye malalamiko ya nchi nzima. Kwa hiyo, ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba eneo hili pamoja na Kamati kutokufika katika eneo hilo, limo ndani ya mjadala ambao tuliuendesha katika Kamati ya Mawaziri Nane na majibu yatakapotoka itakuwa pamoja na eneo hili.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni lini Serikali itaondoa maeneo ambayo yamepoteza hadhi ya uhifadhi. Yapo maeneo mengi nchi nzima yenye hali kama hii na ndiyo ambayo sasa hivi yamevamiwa na wananchi na tumeelekezwa na Serikali kuangalia kama yamepoteza hadhi tupendekeze kuyaachia ili wananchi waweze kuyatumia, pamoja na swali lake la kwanza tunasubii maelekezo ya Kamati ambayo Mheshimiwa Rais aliiunda.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Kafumu ambaye katika nyakati tofauti tofauti amewaleta wazee kutoka katika Kata zilizoathirika nami binafsi nimeonana nao na kuwapa ahadi kwamba maombi yao yamefika mahala muafaka na tutayashughulikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili kuongezea kwenye majibu mazuri aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba katika mchakato wa kuchora ramani upya ya Pori Tengefu la Wembere ili kulipandisha hadhi sehemu yake kuwa Pori la Akiba tutazingatia maombi ya wananchi wa Kata ambazo zimetajwa, eneo la pori la akiba litakalobaki litakuwa dogo zaidi kuliko hili la square kilometa zaidi 8,000 lililopo sasa. Lengo hasa ni kubakisha walau eneo dogo ambalo litakuwa intact na ambalo tutalilinda ipasavyo kwa ajili ya faida za kiuhifadhi na hiyo connectivity kati ya hifadhi zilizopo kusini na hifadhi ambazo ziko upande wa Kaskazini, maombi ya wananchi yatazingatiwa na kwa hivyo eneo ambalo wanaweza kulitumia kwa kufuga kwa kilimo na kwa makazi litabaki kwa wananchi na wataishi kwa uhalali kuliko ilivyo sasa wananyanyasika.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana Serikali kwa kutuletea maji kutoka Ziwa Victoria na kuhakikisha kwamba Kata tano za Nanga, Bukoko, Mwamashiga, Igunga, Mbutu na Itundulu zitapata maji, lakini nipende kuiuliza Serikali, ni lini sasa Serikali itafikisha maji ya Ziwa Victoria kwenye kata zingine zilizobaki?

Swali la pili, shida ya maji kwenye kata ambazo mabwawa au miundombinu yake iliharibika ni kubwa sana na wananchi wanateseka. Naomna kufahamu, Serikali ina- commitment gani juu ya kukarabati miundombinu hii kwa sababu majibu ya Naibu Waziri yanaonekana ni ya jumla. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana, lakini kikubwa sisi kama Serikali kutokana na changamoto hii ya maji, tumeona haja ya kutumia zaidi ya bilioni 600 katika kuhakikisha tutatatuoa tatizo la maji katika Wilaya ya Igunga, Nzega pamoja na Tabora. Lakini ametaka mkakati ni lini tunakwenda kukamilisha? Mradi ule unatakiwa ukamilike mwaka 2020, Mheshimiwa Waziri ametoa agizo pindi itakapofika mwezi huu wa tisa mradi uwe umekamilika na wananchi waweze kupata huduma ya maji na sisi tutalisimamia hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu swali lake la pili, kuhusu suala la fedha za ukarabati. Katika Bunge lako Tukufu, tarehe sita mwezi huu, tuliidhinishiwa zaidi ya bilioni 610 katika kuhakikisha tunatekeleza miradi ya maji, lakini katika Jimbo la Igunga tumetenga zaidi ya bilioni moja. Nimuombe sana na watalamu wetu wa Igunga waone haja sasa hizi fedha ziwe kipaumbele katika kuhakikisha zinatumika katika kukarabati miundombinu hiyo na wananchi waweze kupata huduma muhimu ya maji.