Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mussa Ramadhani Sima (55 total)

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niulize swali dogo. Kwa kuwa Mkoa wa Singida tumejenga Hospitali ya Rufaa na mpaka sasa haijaanza kufanya kazi, je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha hospitali ile inaanza kazi kwa kupeleka vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli na katika ziara yangu hospitali hiyo ni miongoni mwa hospitali nilizozitembelea wakati wa ziara zangu mikoani na siku ile tulikuwa na Mheshimiwa Mbunge, miongoni mwa majengo makubwa sana yaliyojengwa ni lile pale Singida Mjini. Nilitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo kipindi kile na kwa Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha hospitali ile inafanya kazi. Ukiangalia inawezekana ikawa Hospitali ya Kanda kutokana na ukubwa wake kwa sababu kuna center kubwa ya akinamama kujifungulia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kusikitisha jana nilipata taarifa kwamba kuna watu wanataka kutoa vile vitanda kurudisha mjini, natoa agizo hakuna kuondoa kitanda au kitu chochote katika hospitali ile. Wiki ijayo nitakwenda Singida nataka niikute Hospitali ya Singida inafanya kazi. Sitaki kusikia hospitali ambayo uwekezaji wake ni mkubwa na wa mfano, watu wanatoa vitanda kupeleka sehemu zingine, tutawashugulikia watu wote wanaotaka kufanya ubadhirifu katika sekta ya afya.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona, naitwa Mwalimu Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika huu mpango wa Serikali wa kutoa elimu bure, napenda kufahamu Serikali ina mpango gani sasa kuboresha maslahi ya walimu kwa mpango utakaoitwa elimu bure na maslahi bora kwa walimu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua umuhimu wa ualimu, lakini vilevile tunatambua umuhimu wa watumishi wote wa umma. Lakini kwa kutambua umuhimu huo wa walimu kama Serikali, kwa miaka takribani nane tumeshapandisha takribani asilimia 160 ya mshahara wa walimu. Ukiangalia hivi sasa mwalimu wa chini kabisa anapata shilingi 419,000/=, na wa juu anapata shilingi 719,000/=. Tunatambua bado mazingira ya kuishi gharama ni kubwa na wanahitaji kuongezewa kipato na tutafanya hivyo kwa kadri hali ya uchumi itakavyokuwa ikiruhusu.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Singida mjini kwa asilimia kubwa ya wakazi wanajishungulisha na biashara za mazao hususani biashara ya vitunguu. Serikali ina mpango gani sasa wa kujenga Soko la Kimataifa la Vitunguu pale Misuna ambalo linawahusisha mpaka wenyeji wa nchi za Afrika Mashariki na Kati?
Swali la pili, kwa kuwa Serikali imeonyesha ina hisa nyingi kwenye Makampuni ya Umma, je Serikali ina mpango gani wa kuongeza hisa lakini pia hold share na kuongeza uzalishaji katika makampuni hayo? Ahsante.
HARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Sima kwa anavyoshughulikia masuala ya masoko na viwanda hapo Singida, hakuna asiyejua kwamba Singida ni wakulima wa vitunguu na wakulima maarufu sana wa zao la alizeti. Serikali inachofanya pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha kwamba sasa hivi inawasiliana na Halmashauri ya Singida ili kuona sasa zao la vitunguu linapewa kipaumbele na kuanzisha soko la kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa Singida pamoja na mambo mengine hadi sasa kwa kilimo cha vitunguu pamoja na alizeti nadhani ni Mkoa unaongoza kwa Tanzania kwa sasa ukifuatiwa na Mkoa wa Iringa. Hivyo Serikali inaona kuna umuhimu kweli wa kuanzisha soko la Kimataifa kama ambavyo tumeanzisha masoko mengine mipakani kwa ajili ya kuimarisha mazao ambayo yanalimwa hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mbunge ni kuhusiana na hisa za Serikali. Ni kweli kabisa Serikali ina miliki hisa katika makampuni mengi sana. Kwa sasa hivi kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi Serikali ina hisa katika makampuni 61 na katika makampuni yale asilimia kubwa ya hisa za Serikali ni chini ya 50. Kama mnavyotambua tuna asilimia kwa sasa hivi kwa mfano Tanzania Oxygen tuna asilimia 9.59, ukienda Kilombero Sugar tuna asilimia 25, ukienda Tanelec tuna asilimia 30. Lakini hata ukienda kwenye makampuni mengine kama migodi Mwadui tuna asilimia 25.
Mheshimiwa Naibu Spika, upo mkakati wa kuongeza za Serikali katika mipango ya kimkakati, mipango ya kimakakati kwa mfano mathalani kwa sasa hivi viwanda vyetu vya nguo kama Urafiki Serikali ina asilimia 49. Serikali inajaribu kuangalia uwezekano wa kuongeza hisa zake ili iweze kuwa na maamuzi ya uzalishaji katika viwanda vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiongeza suala lingine kuhusu uongezaji wa hisa katika kuweka asilimia za Serikali, katika mipango na miradi na viwanda vya kimkakati kama viwanda vya chuma cha Liganga, kama viwanda vya Kiwira, Serikali inaona kuwa na asilimia nyingi ili iweze kuwa na uwekezaji yenyewe kama ambavyo inaweza kufanya kwa maendeleo ya wananchi wake.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Naomba kuuliza swali la nyongeza, Serikali ina mkakati gani sasa kwa watumishi ambao wamestaafu kwa hiyari ama wengine wamebadilisha kazi kwa mfano kuwa Wabunge, ili kuendelea kuchangia Mfuko huu wa PSPF badala ya kuwaondoa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati uliopo kati ya Serikali na watumishi hawa, nadhani ni ndani ya mtumishi yeye mwenyewe kwamba kama anaona anaweza kuendelea kulipa anaweza kuongea na watumishi wa mfuko huu, Wakurugenzi wetu wote na wote wako tayari na wanapenda kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mussa Sima nikwambie mimi ni mmoja wa waliokuwa watumishi wa Serikali na sasa naendelea kuchangia malipo yangu baada ya mimi kwenda kuongea na Mkurugenzi wa Mfuko wa PSPF na sasa mimi naendelea kuchangia.
Kwa hiyo, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote, Waheshimiwa Watumishi wote na Watanzania kwa ujumla wanaoona wanaweza kuendelea kulipa basi waende wafike kwenye mifuko hii na wataweza kuendelea kulipa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza kabisa niwapongeze Waheshimiwa Naibu Mawaziri wote wawili kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama tu kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba sheria hizi za malipo ya pensheni na mifumo ya kuchangia katika mifuko ya pensheni zimehuishwa na sasa kila mtumishi wa umma ama mtumishi katika sekta binafsi anapohama kiajira kutoka ajira moja kwenda ajira nyingine ama anapotaka kuhamisha mafao kutoka mfuko mmoja kwenda katika mfuko mwingine kwa mujibu wa sheria sasahivi anaruhusiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni suala tu kila mtu kufikiria na kuona ni namna gani anataka kuendelea kuhuisha mafao yake na anaweza kuhusiaha katika mfuko wowote kwa kuhamisha kutoka mfuko mwingine kwenda mwingine kama anabadilisha ajira ama anaamua kufanya hivyo na sheria sasa hivi zinaturuhusu. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, niulize maswali madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa kila mwaka mwezi Julai kunakuwa na ongezeko la mshahara, kupanda vyeo ama madaraja kwa watumishi, lakini mpaka sasa Serikali haijafanya chochote.
Je, Serikali inatoa tamko gani kwa watumishi katika kuhakikisha kwamba hakutakuwa na mlundikano tena wa madai kwa kupandisha mishahara ya watumishi?
Pili, je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha madai haya hayatakuwepo tena? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimhakikishie tu kwamba tunaendelea kulipa madeni haya kwa kadri yanavyojitokeza na kwa kweli ukiangalia tangu mwaka 2013 tulipoanza kutumia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara, madai haya yamekuwa yakiendelea kupungua kwa nyakati mbalimbali.
Vilevile kwa upande wa madeni yanayotokana na kupandisha mishahara na kwa madeni yanayotokana na upandishwaji wa vyeo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tulishatoa maelekezo kwamba ni lazima madai haya yalipwe kupitia mfumo pindi watu hawa wanapopandishwa vyeo pamoja na madai haya yanapokuwa yamejitokeza ili kuhakikisha kwamba hatuleti milundikano ya madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunakikisha tunakuwa na mkakati endelevu, yapo madai mengine yanatokana na watumishi kuhama, tumeshaelekeza tuhakikishe kwamba mtumishi hahamishiwi kama hakuna fedha za uhamisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, madai mengine ambayo yamekuwa yakijitokeza kwa wingi ni masuala au madai ya posho ya kukaimu. Tumeshaelekeza pia na yenyewe, pindi barua ya kukaimishwa na marekebisho ya mshahara yanapotoka, basi mtumishi aingiziwe marekebisho hayo mapema na marekebisho ya mshahara yaweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukishuhudia baadhi ya waajiri wamekuwa hawatengi fedha kwa ajili ya matibabu, likizo na posho zao nyingine, matokeo yake imekuwa inasababisha sasa pindi mtu anapotakiwa kwenda likizo, inaleta madeni makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwaagiza waajiri wote, wanapokuwa wanapanga bajeti zao za kila mwaka, wahakikishe stahili za msingi na za kisheria na za kanuni za kudumu za Utumishi wa Umma zinatengwa ili kuhakikisha kwamba hawasababishi madeni, lakini vilevile kuhakikisha tunazingatia haki za msingi za watumishi hao. Nakushukuru.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba sasa niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali tayari imekiri kusambaza mabomba na kupeleka pampu, napenda kujua ni lini sasa utekelezaji wake unaanza kufanyika?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la maji ni kubwa katika Jimbo la Singida Mjini hususani kata za pembeni, Serikali inawaambia nini wananchi wa Jimbo la Singida Mjini kwa ajili ya kuhakikisha tatizo hili linaisha?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni lini mradi wa kusambaza maji katika Mji wa Singida utafanyika, tunahitaji shilingi milioni 730 na tayari tuna vyanzo viwili vya kupata hiyo fedha. Kwanza tumeshaomba fedha kutoka BADEA, lakini pili tumetoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Mamlaka wa Singida kuna fedha kidogo ambazo zipo, kwa hiyo wakati wowote mradi huu utaanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua ni lini tutakuwa na mkakati wa kuhakikisha kwamba Mji wa Singida unakuwa na maji ya kudumu. Kama nilivyojibu wakati wa bajeti kwamba tunaanza kujipanga ili tuweze kufanya usanifu wa kutoa maji Igunga kuyaleta Mji wa Singida ili kuhakikisha kwamba sasa tatizo la maji katika Mji wa Singida tunalimaliza. Tutamuagiza Mhandisi Mshauri, aanze kufanya kazi hiyo ili kuona ile pressure iliyoko Igunga inaweza ikafika Singida? Kama itakuwa inapungua basi wataalam watatushauri tufanyeje lakini Mji wa Singida ni mkame tutahakikisha kwamba tunawapa chanzo cha maji chenye uhakika.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize swali dogo la nyongeza. Wakati wa kampeni, Mheshimiwa Rais aliwaahidi wananchi wa Jimbo la Singida Mjini kwamba atajenga barabara kwa kiwango cha lami ya kuunganisha Kata zote za pembeni. Sasa, je, mchakato huu wa kujenga barabara utaanza lini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tumepewa ahadi zote ambazo viongozi wetu, Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, walizitoa sehemu mbalimbali za nchi, ahadi zote tunazo. Tulichowekea fedha ili tuweze kuanza kutekeleza katika mwaka huu wa kwanza tunaoanza ni zile barabara ambazo zilishaanza kufanyiwa kazi toka zamani na wakandarasi wako site.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tutakubaliana kwamba ni vyema tukamaliza kwanza ile kazi iliyoanza siku nyingi za nyuma ili wakandarasi wasiendelee kupata fedha bila kufanyia kazi kwa kutopewa fedha za ujenzi na hivyo wanaendelea kukaa pale bila kufanya kazi na tunalazimika kuwalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kipaumbele cha kwanza ni kukamilisha barabara ambazo zilianza. Nawahakikishieni Waheshimiwa Wabunge kwamba barabara zote ambazo Mheshimiwa Rais pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais waliziahidi na bahati nzuri tumeshazipata, tutahakikisha tunazipangia ratiba ya utekelezaji katika kipindi kitakachofuata.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru sana kwa kuniona, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Askari wetu wanafanya kazi kwenye mazingira magumu sana na wanafanaya kazi kwa muda mrefu bila kupanda vyeo mpaka kustaafu. Je, Serikali haioni haja sasa ya kutathmini upya vigezo vya kuwapandisha vyeo ili kuongeza ufanisi wa kazi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa kutumia weledi wake kama mtumishi wa umma na kutambua umuhimu wa motisha inayoambatana na upandaji wa vyeo kwa askari kama ilivyo kwa Mtumishi mwingine ili kuweza kuongeza ufanisi. Wazo lake ni zuri, tumelipokea na Mheshimiwa Rais alishaongelea kuhusu kuongeza motisha kwa watumishi wa umma wote hapa nchini mara baada ya kuwa ameshamaliza marekebisho na kutoa dira ya Serikali yake. Sisi wasaidizi wake tunatembea kwenye miguu yake, tunatembea kwenye maneno yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwahidi Mheshimiwa Mussa Sima taratibu hizo zitakapoanza kufanyika tutatoa kipaumbele kwa vijana wetu wazalendo wanaolitumikia Taifa kwa uzalendo na kwa moyo wao kwa ajili ya kuhakikisha raia wa Tanzania na mali zao wako salama.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Singida Mjini imejaaliwa kuwa na rasilimali ya vyanzo vya umeme kwa maana ya upepo na jua na yako makampuni tayari yamekwishajitokeza kwa ajili ya kuzalisha umeme huo. Sasa na sisi wananchi wa Jimbo la Singida Mjini tumejitokeza kwa maana ya kutoa maeneo yetu kwa ajili ya uzalishaji. Serikali sasa ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba umeme huo unazalishwa ili Singida Mjini iweze kupata viwanda vya kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Singida Mjini kunapita umeme wa kilovoti 40 kuelekea Shinyanga na Namanga na wananchi tayari wametoa maeneo yao kwa ajili ya kupisha mradi huo na wako ambao wameshalipwa fidia na wengine hawajalipwa fidia. Serikali inatoa tamko gani sasa kuhakikisha kwamba wananchi wote wanalipwa fidia kwa ajili ya kupisha umeme huo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, Serikali ina mpango mahususi wa kuendeleza wawekezaji binafsi katika umeme mbadala hasa katika maeneo ya Singida ambako kuna umeme wa upepo. Hata hivyo, mkakati wa Serikali wa kwanza, Serikali imetenga kupitia mradi wake wa REA shilingi milioni 42 kwa ajili ya kuendeleza wawekezaji binafsi watakaofanya katika uzalishaji wa umeme pamoja na mambo ya miradi ya maji. Kwa hiyo, wananchi wa Singida watapata pesa hizi kupitia mradi wa REA ambapo watawezeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mkakati mwingine badala ya kupitia mradi wake umeshafadhili sasa, nikizungumzia kwa nchi nzima miradi ya Lukonda kule Njombe pamoja na Ndoya kule Mbinga kama wajasiriamali wa Kitanzania ambao wanawezeshwa kupitia miradi ya Serikali, miradi ya REA. Kwa hiyo, miradi ya Serikali kupitia miradi ya REA kutoa mahususi kwa ajili ya kuendekeza wawekezaji. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Sima na kama kuna wawekezaji wengine kule Singida Mheshimiwa Sima basi walete wataalam wetu watashirikiana na watu wa REA ili waweze kushirikiana zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusiana na mkakati wa Serikali kulipa fidia kwenye Mradi wa backbone wa kilovoti 400. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Sima alivyoshirikiana na Serikali mpaka wananchi takriban 200 wakalipwa fidia awamu ya kwanza. Awamu ya pili nimhakikishie Mheshimiwa Sima, hivi sasa vijiji vyake 13 ambavyo vinaingia kwenye mradi ule vitalipwa fidia jumla ya shilingi milioni 722.7, malipo yataanza mwezi Februari mwaka huu na yatakamilika mwezi Machi na nimhakikishie kwamba vijiji vyake vya Misuna ambavyo vilipitiwa na umeme pamoja na Mtipa pamoja na Kisaki pia vitalipwa fidia kwa utaratibu huo.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
nishukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa Singida Mjini ni mji ambao unakua kwa kasi sana kwa sababu Serikali imehamia Dodoma, Serikali haioni haja
sasa ya kutenga fedha kwenye bajeti ya mwaka huu ili uweze kuwalipa fidia wananchi wa kwenye hilo eneo la Manga na Uhamaka ilitoe hilo eneo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa
Serikali imeanza ukarabati kwenye uwanja wa ndege wa sasa, je, Serikali itamaliza ukarabati huo lini ili na sisi tuweze kuutumia uwanja huo kwa kupanda ndege? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Sima na wananchi wa Mji wa Singida wawe na subira, tupate taarifa ya mwisho ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili hatua ya pili ifuate. Si rahisi tukaanza
kutenga fedha kwa mwaka huu na hasa vipaumbele ambavyo tulipitisha mwaka huu, mtakumbuka ambavyo tulipitisha katika mpango wa mwaka huu wa fedha, vinahitaji rasilimali fedha nyingi na hivyo hii kazi tutaifanya mara badaa
ya kazi hii ya upembuzi yakinifu kukamilika. Itakuwa sio rahisi kwa mwaka huu, mnafahamu kwamba bajeti ya mwaka huu tumeshaipitisha katika ngazi ya Kamati na hivi sasa tunaanza kuingiza katika hatua za Bunge Zima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu ukarabati;
nimhakikishie Mheshimiwa Sima kwamba kazi hii ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina itakapokamilika suala la ukarabati litafuata.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, namwomba Mheshimiwa Waziri awahakikishie wananchi wa Jimbo la Singida Mjini kwamba miradi hiyo aliyoitaja, miradi 33 iliyosajiliwa yenye kutoa ajira zaidi ya 4,000 itaanza lini?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Serikali imehamia Dodoma na yako Mashirika ndani ya Wizara, Ofisi za Kanda zipo Dodoma: Je, Mheshimiwa Waziri, sasa upo tayari Mashirika hayo kwa mfano TFDA, TBS na mengine kuanzisha Ofisi za Kanda Singida Mjini ili kuweka ufanisi wa kazi hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ile miradi 33 niliyoisema, nimesema kuanzia mwaka 1996 mpaka Aprili, 2017, miongoni mwa viwanda hivyo ni kiwanda cha mafuta cha Mount Meru, kimeshaanza kazi. Viwanda hivyo vimeshaanza kazi; na mojawapo ya viwanda hivyo ni Kiwanda cha Maziwa anachokijasiria Mheshimiwa Kingu. Tumeshaanza kazi. Tanzania sasa tunajenga viwanda. Sasa labda anieleze wapi anataka mimi nisukume kwa nguvu kusudi mambo ya nchi yetu yaendelee vizuri na yeye yamnyookee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuanzisha kanda za TBS na TIRDO, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna tija kuwa Dodoma ukaanzisha Branch Singida, kwa sababu unaweza kuondoka asubuhi ukafanya kazi Singida, ukarudi hapa, ukarudi tena, ukarudi tena. Kwa hiyo, itabaki Dodoma na itakuwa rahisi hata Mheshimiwa Waziri kwenda na Mheshimiwa, rafiki yake wakaweza kuhamasisha shughuli za viwanda.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa hatua hiyo. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; tangu mwaka 2016 mpaka sasa hakuna ongezeko lolote la mshahara kwa watumishi. Serikali inatoa tamko gani kwa watumishi hawa ambao wamekuwa na moyo mkubwa sana wa kujitolea?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tangu mwaka 2016 mpaka sasa hakuna kupandishwa daraja kwa mtumishi yeyote hususan Mwalimu. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kulipa malimbikizo ya mshahara kwa Mtumishi ambaye alistahili kupanda mwaka 2016 mpaka sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya rejea ya takriban siku mbili, Mheshimiwa Waziri anayehusika na mambo ya Utumishi (Waziri wa Utumishi na Menejimenti ya Utumishi wa Umma) alitoa maelekezo hapa kwamba katika hoja yetu ya Bajeti Kuu ilivyokuwa inapita watu walikuwa wanasema kwamba kwa nini sasa fungu hili la mshahara halipo?
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba Mheshimiwa Rais alizungumza wazi alipokuwa katika viwanja vya Mkoa wa Kilimanjaro katika siku ya Mei Mosi. Jambo hili limezingatiwa katika bajeti yetu hii tunayokwenda nayo hivi sasa. Ndiyo maana hata juzi Waziri wa Utumishi wa Umma alikuwa anatoa maelekezo kwamba kuna nyongeza ya fedha hapa ambayo itaenda ku-address jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la kupanda madaraja, hali kadhalika eneo hilo madaraja yalisimamishwa kutokana na zoezi maalum la uhakiki hasa wa vyeti feki na watumishi hewa. Vile vile naomba nifanye rejea ya Waziri wetu wa Utumishi wa Umma alipozungumza wazi kwamba suala la kupanda madaraja sasa limewekewa utaratibu mzuri, kila mtu atapanda kwa stahiki yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie kwamba kila mtu atapata stahili yake kwa kadri inavyotakiwa na hili Mheshimiwa Waziri amelizungumza wazi kwa sababu yeye ndiyo anahusika na Utumishi kwamba kila mtu atapata stahiki yake na jambo hili sasa hivi linakamilika na kila mtu atapanda daraja kama ilivyokusudiwa. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Waziri kwa majibu mazuri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa mwaka jana tuliomba fedha kwa ajili ya ukarabati Hospitali yetu ya Rufaa takribani shilingi bilioni 1.7 na tumekwishapata shilingi bilioni moja, je, fedha iliyobaki itakuja lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, nimuombe Mheshimiwa Waziri aseme kama atakuwa tayari kuambatana nami kwenda kuangalia hali ya Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa na Kituo cha Afya cha Sokoine. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika mpango wa bajeti ilitengwa karibuni shilingi bilioni 1.7 na ndiyo maana kwa mujibu wa Serikali kwa sababu mipango yake ni kuhakikisha miradi hii inatekelezeka tayari tumeshapeleka shilingi bilioni moja. Nishukuru sana wakati naongea na Sekretarieti ya Mkoa mwezi mmoja uliopita walikuwa katika michakato ya kuona ni jinsi gani fedha zile ziweze kutumika vizuri zaidi kuhakikisha kwamba jengo lile linakamilika. Hata hivyo, ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba hospitali hii inakamilika. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajitahidi kadri iwezekanavyo fedha zipatikane, mpango ule wa ujenzi wa Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili kwamba ikiwezekana tuweze kuongozana, nimwambie Mheshimiwa Mbunge tujipange ikiwezekana hata kesho mchana, tutoke hapa mara moja tukafanye kazi turudi tuendelee na kazi za Bunge kwa sababu ni lazima tuhakikishe kwamba tunawafikia wananchi kuweza kuwahudumia kwa karibu zaidi.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Serikali lakini bado kuna changamoto kubwa kwa akina mama wajawazito wanapokwenda hospitali za umma kwa ajili ya kupata vipimo na matibabu mengine, vifaa havipatikani. Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inafanya kazi nzuri sana ya zoezi la ukusanyaji damu salama na imetoa mwongozo mzuri kwa Halmashauri zetu kutenga bajeti kwa ajili ya kukusanya damu salama, lakini bado ziko Halmashauri zimeshindwa kutenga bajeti hiyo. Je, Serikali pia inatoa tamko gani kwenye Halmashauri hizi zilizoshindwa kufanya kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali langu la nyongeza na mwenyewe amekiri jitihada kubwa ambazo zinafanywa na Serikali ili kuhakikisha kwamba vifaa tiba vinapatikana na kuondoa adha na hasa kwa akinamama kama ambavyo na yeye mwenyewe amekuwa mdau mkubwa kuhakikisha kwamba akinamama hawapati adha hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee naomba niendelee kupongeza Halmashauri yake ambayo Mheshimiwa Mbunge amekuwa akihakikisha kwamba vifaa tiba vinanunuliwa. Nizitake Halmashauri zingine wahakikishe kwamba vifaa tiba vinatengewa pesa na vinanunuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na Halmashauri yake kwa sababu katika hizi pesa ambazo zimelipwa milioni 41 niliyotaja ni pamoja na kitanda cha upasuaji kimeshalipiwa, mashine ya kutolea dawa ya usingizi, jokofu la kuhifadhia damu kama ambavyo amesema Halmashauri zingine hazifanyi, wao wanafanya vizuri sana; mashine ya kufulia moja, vitanda vya kujifungulia vinne, mfumo wa hewa ya oxygen, vitanda vya kubebea wagonjwa. Kwa hiyo, kwa ujumla nizitake Halmashauri zingine zote nchini waige mfano mzuri ambao wenzetu wanafanya ambako Mheshimiwa Mbunge amesemea.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa fedha hizi zimeleta mgogoro sana zinapowekwa kwenye akaunti ya pamoja, je, Serikali haioni haja sasa kuzielekeza Halmashauri kuanzisha akaunti maalum kwa ajili ya hii asilimia 10 peke yake? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba tumechukua maoni ya Mheshimiwa Sima ambayo naamini ni maoni ya Waheshimiwa Wabunge wote na tutalifanyia kazi.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Kwa kuwa Tanzania ina wachezaji wachache sana wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi na kwa kuwa vijana wetu wa Serengeti Boys Under 17 walionesha kiwango kikubwa sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwekeza kwa vijana hawa ili tuwe na wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba timu yetu ya Taifa ya Serengeti imefanya vizuri sana katika historia ya nchi yetu na naomba nimhakikishie Mheshimiwa Sima kwamba juhudi za Serikali sasa hivi ziko katika maeneo mawili. Moja ni kuhakikisha timu hii tunaendelea kuilea kwa sababu hawa ndiyo wawakilishi wetu katika michuano yetu ya olympiki mwaka 2020, kwa hiyo hatuwezi kuwaacha tunaendelea kuwalea kwa karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nimhakikishie kwamba tuko kwenye mazungumzo na wadau mbalimbali, tumepata watu wengi nje ambao sasa hivi tunashirikiana kwa karibu kama Sport Pesa na timu ya Everton FC ambayo iko Premier League ya Uingereza ambao tuna mahusiano mazuri, tumeanza kuongelea kuhusu uwezekano wa kuweza kuchukua baadhi ya vijana wetu. Hayo ni mazungumzo bado hatujapata guarantee nisije nikasikia kesho magazeti yakesema sasa wanakwenda huko, tuko kwenye mazungumzo na tutaendelea kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nikuhakikishie Mheshimiwa Sima katika kipindi changu cha uongozi wa Wizara hii sitaruhusu kijana yeyote kwenye timu ya Serengeti achukuliwe na timu ambayo ina historia ya uchovu uchovu kiweledi hata kipesa na mimi mwenyewe nitasimamia katika kuangalia mikataba yao. Niwahakikishie tunawaangalia vijana wetu na wataendelea kutusaidia katika kuinua jina letu kwenye ulimwengu wa soka. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa hatua hiyo. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; tangu mwaka 2016 mpaka sasa hakuna ongezeko lolote la mshahara kwa watumishi. Serikali inatoa tamko gani kwa watumishi hawa ambao wamekuwa na moyo mkubwa sana wa kujitolea?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tangu mwaka 2016 mpaka sasa hakuna kupandishwa daraja kwa mtumishi yeyote hususan Mwalimu. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kulipa malimbikizo ya mshahara kwa Mtumishi ambaye alistahili kupanda mwaka 2016 mpaka sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya rejea ya takriban siku mbili, Mheshimiwa Waziri anayehusika na mambo ya Utumishi (Waziri wa Utumishi na Menejimenti ya Utumishi wa Umma) alitoa maelekezo hapa kwamba katika hoja yetu ya Bajeti Kuu ilivyokuwa inapita watu walikuwa wanasema kwamba kwa nini sasa fungu hili la mshahara halipo?
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba Mheshimiwa Rais alizungumza wazi alipokuwa katika viwanja vya Mkoa wa Kilimanjaro katika siku ya Mei Mosi. Jambo hili limezingatiwa katika bajeti yetu hii tunayokwenda nayo hivi sasa. Ndiyo maana hata juzi Waziri wa Utumishi wa Umma alikuwa anatoa maelekezo kwamba kuna nyongeza ya fedha hapa ambayo itaenda ku-address jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la kupanda madaraja, hali kadhalika eneo hilo madaraja yalisimamishwa kutokana na zoezi maalum la uhakiki hasa wa vyeti feki na watumishi hewa. Vile vile naomba nifanye rejea ya Waziri wetu wa Utumishi wa Umma alipozungumza wazi kwamba suala la kupanda madaraja sasa limewekewa utaratibu mzuri, kila mtu atapanda kwa stahiki yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie kwamba kila mtu atapata stahili yake kwa kadri inavyotakiwa na hili Mheshimiwa Waziri amelizungumza wazi kwa sababu yeye ndiyo anahusika na Utumishi kwamba kila mtu atapata stahiki yake na jambo hili sasa hivi linakamilika na kila mtu atapanda daraja kama ilivyokusudiwa. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na niipongeze Serikali kuwa wazi kwenye swali hili. Pia ni-declare interest, mimi ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka, Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Na. 12 ya mwaka 1967 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 1971 na Kanuni za Usajili wa Vyama vya Michezo, Namba 442 ya mwaka 1999, kifungu cha 7(2)(c)(ii), inatambua mamlaka ya Waziri na Waziri ndiyo mwenye maamuzi ya mwisho ya vyama vya michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini viko baadhi ya vyama katiba zao hazitambui mamlaka ya Waziri na vyenyewe ndiyo vyenye mamlaka ya mwisho ikiwemo TFF. Mheshimiwa Waziri, nikuombe sana, ikikupendeza kama utakuwa tayari kulinda, kuheshimu na kusimamia sheria hii iliyotungwa na Bunge na kuhakikisha vyama hivi kwenye katiba zao zinatambua role ama wajibu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, Serikali imekiri wazi katika ruzuku ambayo inatolewa TFF ni zaidi ya bilioni 10 na ile dola milioni tatu tunazungumzia karibu bilioni saba, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, kama utakuwa tayari uiombe TFF ilete mpango kazi kwenye mikoa yetu ili tuweze kujua fedha hizi zinatumikaje. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Sima kwa sababu amekuwa ni mwanamichezo mahiri na vilevile ni mdau mkubwa sana wa michezo katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na kujibu swali lake la kwanza ambalo ametaka kujua kama kuna vyama vya mpira ambavyo havitambui mamlaka ya Waziri. Mimi niseme kwamba tunatambua kabisa kwamba TFF pamoja na viongozi wake wote wanapaswa, wanalazimika na hivyo wanatambua mamlaka ya Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani? Ukisoma Katiba ya TFF, Ibara ya 1(2) inasema kwamba TFF ni chombo cha mpira ambacho kimesajiliwa chini ya Sheria ya Baraza la Michezo ya mwaka 1967 kama ambavyo umesema na marekebisho yake ya mwaka 1971. Kwa maana hiyo sasa, kimsingi kwa sababu Baraza la Michezo ambalo ndiyo ambalo linasajili TFF liko chini ya Wizara ya Habari, kwa maana lipo chini ya Waziri husika mwenye dhamana ya michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa sababu TFF iko chini ya Baraza la Michezo, kwa hiyo, kimsingi ni kwamba TFF inapaswa kutambua mamlaka ambayo Waziri kwa maana ya Serikali inayo. Naamini kabisa kwamba TFF inatambua mamlaka ya Waziri kwa sababu ni takwa la kikanuni na kikatiba na wanapaswa kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikija kwenye swali lako la pili ambapo unataka kujua hizi fedha za FIFA Forward ambazo zimetolewa, unaiomba Serikali iweze kuishauri TFF iweze kutoa mchanganuo wa fedha hizo mapema. Mheshimiwa Sima natambua kabisa kwamba wewe ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu katika Mkoa wa Singida na kwa jinsi mimi ninavyotambua ni kwamba humu ndani tuna Wabunge wengi ambao ni viongozi wa vyama vya mipira. Kwa hiyo, najua kabisa kwamba ninyi kama Wenyeviti pamoja na Makatibu ndiyo mhimili mkubwa kabisa wa TFF lakini kimsingi ninyi ndio washauri wakubwa wa TFF. Kwa hiyo, kwa sababu TFF ina taratibu zake, ina mikutano yake ambayo huwa mnakaa na kila mwaka huwa mnakutana, mna mkutano wa robo mwaka, nusu mwaka pamoja na wa mwaka, naamini mtakapokutana ninyi mna nafasi kubwa kabisa ya kuweza kuishauri TFF ili kuweza kuandaa huo mchanganuo wa fedha.
Niseme kabisa sisi kama Serikali tumelipokea wazo lako na tunakubaliana kabisa na wazo lako kwa sababu tunajua kwa namna moja au nyingine litasaidia kuweka uwazi wa mapato na matumizi na kuondoa sintofahamu ambazo zilikuwepo siku za nyuma. Ahsante. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri. Kwa kuwa hawa Makatibu Wasaidizi wa Tume wote hawajawahi kuteuliwa na hawatambuliki kisheria.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwateuwa hawa ili waweze kufanya kazi yao ipasavyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa mashauri mengi ya walimu yamekaa kwa muda mrefu kwa sababu ya ukosefu wa fedha na fedha nyingi haziendi, na leo Serikali imekiri imetenga shilingi bilioni 4.6; Mheshimiwa Waziri anawahakikishiaje viongozi hawa kwamba fedha hizi zitaenda kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama nilivyosema katika swali la kwanza kuhusu uteuzi. Uteuzi huwa ni hatua ya mwisho ya mchakato, na mchakato wenyewe huanza na upekuzi, kumpekua yule mtu unayempendekeza kwenye nafasi fulani. Kwa hiyo mchakato huo uko katika hatua za mwisho.
Napenda kulithibitishia Bunge hili na Mheshimiwa Mbunge kwamba mchakato huo wa upekuzi ambao Idara ambazo zinazofanya upekuzi anazifahamu Mheshimiwa Mbunge zitakapokamilisha upekuzi huo, Makatibu Wasaidizi wote katika Wilaya watateuliwa kwa mujibu wa mapendekezo ya huo upekuzi utakapokamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili naomba nimhakikishie kwamba wakati wa mazungumzo yetu wakati wa bajeti tumehakikishiwa na Waziri wa Fedha kwamba kwa mwaka ujao wa fedha, fedha hizi zitatoka kwa wakati. Ahsante sana.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ligi yetu ya Tanzania imekuwa ikitumia gharama kubwa sana hata kwenye usajili wa zaidi ya shilingi bilioni moja kwenye timu kadhaa, lakini wanaenda kupokea shilingi milioni 86 na wamecheza kwa mwaka mzima.
Je, Serikali ina mkakati gani kuifanya ligi hii ya Tanzania kuwa ina ushindani? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kama nimemwelewa vizuri Mheshimiwa Sima kuhusu usajili na ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimweleze Mheshimiwa Sima kwamba sisi kama Wizara bado hatujaona tatizo la usajili na ushindani katika ligi, lakini kama ni matumizi ya pesa, kwa kweli soka la leo ni la pesa. Usipokuwa na pesa, huwezi kabisa ukaendesha mchezo wowote wa mpira. Ndiyo maana unaweza kuona maendeleo mazuri ya timu kama Singida United, nao naomba niwapongeze kwa kazi nzuri ambayo wameifanya Kenya na tuwaombee kama ambavyo tunawaombea Simba waweze kufanya vizuri wawe washindi wa tatu katika mashindano ya Kenya.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naomba niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa changamoto kubwa inajitokeza kutokana na uhaba wa hawa Maafisa Utamaduni kwenye halmashauri zetu. Sasa Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Maafisa Utamaduni ili kuweza kukidhi haja ya Sanaa. Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba, hapo nyuma kulikuwa kuna changamoto kubwa sana ya Maafisa Utamaduni kwenye halmashauri zetu, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, halmashauri nyingi zilishaandika barua ya kuomba vibali kutoka Utumishi vya kuweza kuajiri Maafisa Utamaduni. Mpaka sasa hivi karibu halmashauri nyingi zina Maafisa Utamaduni.
Mheshimiwa Spika, kama haitoshi sisi kama Wizara, tunaendelea na mchakato wa kuonesha kwamba tunaajiri Maafisa Utamaduni wapya, hususani katika Mikoa na Halmashauri ambazo ni mpya. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tatizo hilo kwa kiasi kikubwa sana limeshashughulikiwa na Wizara yetu ya Habari, nadhani hata Waheshimiwa Wabunge mtakuwa mashahidi.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Singida Mjini tumeanza programu ya kupandisha hadhi shule zetu za sekondari kuwa kidato cha tano na sita ikiwemo Shule ya Sekondari ya Mungumaji. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutusaidia kukamilisha programu hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nikirejea majibu yangu ya awali ambayo nimeyatoa, kwanza yeye kama mwalimu namsifu kwa juhudi zake za kuendeleza sekta ya elimu katika jimbo lake lakini vilevile kutoa mawazo mazuri kwa ajili ya nchi nzima. Napenda kusisitiza kwamba maagizo ambayo tumeyatoa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ambao wanasimamiwa na Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ni kwamba kipaumbele lazima waendelee kukiweka katika shule zote ambazo wameziteua kwa ajili ya kuzipandisha hadhi kuwa za kidato cha tano na sita kwa maana hizo zitakuwa ni shule za nchi. Waweke kipaumbele kuhakikisha kwamba miundombinu inayohitajika yote kwa mujibu wa vigezo vilivyotolewa na Wizara ya Elimu inakamilika mapema iwezekanavyo ili kusudi shule hizo ziweze kutusaidia kupokea watoto wengi zaidi au vijana wengi zaidi wa kidato cha tano na sita.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kabisa kwenye ligi ya Uingereza ilijulikana kama Backlays English Premier League na siyo Backlays Premier League, pia hata Kagame Cup haikujulikana kama Kagame Cup inajulikana kama CECAFA Kagame Cup. Serikali haioni haja sasa kwamba umefika wakati wa kuitangaza Tanzania kwenye michezo na league yetu ikaitwa Tanzania Vodacom Premier League? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Kampuni ya Azam wameanzisha mashindano makubwa sana yanaitwa Azam Sports Federation Cup, nichukue fursa hii kuwapongeza sana, je, Serikali haioni haja sasa ya kushawishi na makampuni mengine yaweze kuanzisha mashindano ili ku-promote soko la Tanzania? (Makofi
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwalimu Mussa Sima kwa kifupi sana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pendekezo la kuweka jina la Tanzania kabla ya jina la mdhamini lina mashiko, tutalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kampuni nyingine kuiga mfano wa Azam, nami naunga mkono suala hilo. Natoa wito kwa makampuni mengine yajaribu kuiga mfano wa Azam ili tuweze kukusa soka katika nchi yetu.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa Serikali inatoa elimu bila malipo kuanzia chekechea mpaka kidato cha nne, wanafunzi wachache ambao hawajabahatika kwenda kidato cha tano wanaenda vyuo vya ufundi. Vyuo vya ufundi, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema wanalipia ada ya Sh.60,000/= na Sh.120,000/= kwa wale wa boarding. Je, Serikali haioni haja sasa kuondoa ada pia kwenye vyuo vya ufundi ili kuwawezesha watoto wengi kuweza kupata ujuzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sima, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya mwanzo kwamba Serikali inatoa ruzuku ya kutosha. Kwa hiyo, hili alilolileta Mheshimiwa Sima ni pendekezo, tunaomba twende tukalifanyie kazi tuweze kuangalia namna gani aidha kwa kupunguza au kwa kuondoa wakati huo huo tukiangalia wigo wa bajeti ya Serikali unavyokuwa.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Pamoja na uwepo wa viwanda hivyo 14 alivyovitaja, lakini bado Serikali inaagiza dawa na vifaa tiba kwa asilimia 80 kutoka nje. Je, tatizo ni ubora wa dawa zinazotolewa nchini ama ushindani wa kibiashara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali imesema ifikapo mwaka 2025 itafikia asilimia 60, napenda kujua tu, sasa hivi tuko asilimia ngapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, Tanzania bado hatujajitosheleza katika uzalishaji wa dawa kwa maana ya kuwa na viwanda vichache ambavyo vinazalisha dawa na vifaa tiba kwa ajili ya matumizi hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala siyo ubora, ni uwezo wetu ambao bado haujakidhi mahitaji ya ndani. Suala la ushindani ni suala lingine kwa sababu ushindani upo hata katika bidhaa ambazo tumejitosheleza, lakini specifically kwenye hili bado uwezo wetu wa kuzalisha ndani ni mdogo, ndiyo maana tumelenga kuhamasisha kupitia vivutio mbalimbali ili tuwe na wawekezaji wengi zaidi wanaowekeza katika viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kiasi ambacho kinaagizwa sasa, ni kweli hatujafikia uwezo wa kutengeneza asilimia zote za dawa kwa maana ya asilimia 100, bado tunaagiza zaidi ya asilimia 80 kutoka nje. Kwa hiyo, bado lengo letu kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, ni kufikia asilimia ya uzalishaji ifikapo mwaka 2025.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa nchi nyingi sana kama alivyoeleza zimeamua kwa dhati kuwa na mtaala wa Kiswahili na ukizingatia pia tunao vijana wengi wabobezi kwenye eneo hili la Kiswahili. Serikali inaweka mkakati gani kuhakikisha vijana hawa wanapata ajira kwenye maeneo hayo ili tusije kuzidiwa na nchi zingine za Jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kumekuwa na ongezeko kubwa sana la misamiati ambayo inatokana na matukio mbalimbali na misamiati hii inaweza kuathiri lugha yetu ya Kiswahili. Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na ongezeko la misamiati hii? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge amehitaji kufahamu Serikali inajipanga vipi kuwasaidia vijana wetu wapate ajira kupitia lugha hii ya Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, katika majibu yangu ya awali nilieleza kwamba Serikali ilishaanza mazungumza na Balozi zetu kupitia Wizara ya Mambo ya Nje kuhakikisha kwamba hawa wataalam ambao wamezamishwa, wameeleweshwa lugha ya Kiswahili na namna gani wafundishe wageni waweze kushirikiana katika Balozi zetu na madawati hayo yaanzishwe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia BAKITA tunalifahamu jambo hili na nimesema kwamba tuna wataalam zaidi ya 1318 ambao wapo tayari na tumekuwa tukiwasaidia na wamekuwa wakiwasiliana na BAKITA kwa karibu waweze kupata ajira hizo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili Mheshimiwa Mbunge alitaka kufahamu ni kwa kiasi gani Serikali inaangalia misamiati inapokuwa imezalishwa ni kwa kiasi gani tunafuatilia kama kuna mabadiliko ya mazingira. Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba Serikali kupitia BAKITA tumekuwa makini sana. Panapotokea mabadiliko yoyote ya kimazingira, ya kieneo au mazingira ya matukio yoyote BAKITA wamekuwa wakitafuta misamiati mbalimbali na kuhakikisha kwamba tunasanifisha misamiati hiyo lakini pia tunachapisha.

Mheshimiwa Spika, mfano, hivi karibuni nchi yetu imekumbwa na ugonjwa wa Covid lakini BAKITA tumejidhatiti na tumeshasanifisha covid – 19 inaitwaje kwa Kiswahili ambayo inaitwa UVIKO – 19. Nitoe rai kwa Watanzania kwasababu tunapenda lugha yetu tuhakikishe tunatumia lugha hii ya Kiswahili badala ya kusema covid – 19 tunaweza tukasema UVIKO – 19. Naomba kuwasilisha.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mradi huu wa TACTIC, Singida mjini pale unatarajiwa kujenga soko la kisasa la vitunguu, soko la Kimataifa. Pia, wananchi wa Singida Mjini wanataka kujua ni lini mradi huu utakamilika? Kwa sababu feasibility study imekwishafanyika. Sasa ni lini, ili waweze kuendelea na soko lao la Kimataifa?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kama nilivyojibu katika maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana na ndivyo ambavyo nitamjibu Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Mussa Sima, kwamba nafahamu kwamba kulikuwa na awamu ya kwanza ya majadiliano, sasa hivi tuko katika majadiliano awamu ya mwisho. Ndiyo maana katika sehemu ya huo mradi tumewatuma wataalam kuhakikisha wanaainisha maeneo yale muhimu yanayojengwa na mradi huu ni component ya mambo mengi ndiyo maana kuna masoko, barabara, kuna madampo ndani ya huu mradi wa TACTIC. Huu mradi utakapokamilika maana yake utasaidia mambo mengi ikiwemo mpaka kujenga stendi za kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba awe na subira kwa sababu tuko hatua za mwisho na hii kazi itafanyika. Ondoa wasiwasi. Chini ya Awamu ya Sita, barabara hizi zitajengwa, mradi huu utafika na wananchi wa Singida Mjini na maeneo yote ambayo yameainishwa katika huu mradi watafaidika na mradi huu. Ahsante.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana; kwa kuwa Serikali imeendelea na ukarabati wa Hospitali ya Rufaa ya Mandewa, nataka kujua tu ni nili itakamilisha ukarabati huo ili kuondoa adha inayojitokeza katika suala la kupata huduma ya afya katika Mkoa wa Singida? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tulishakwisha kusema hapa kwa bajeti ya mwaka 2021/2022 zimetengwa zaidi ya shilingi bilioni 57 kwa ajili ya kufanya ukarabati na ujenzi katika hospitali mbalimbali za rufaa hapa nchini hospitali aliyoitaja Mheshimiwa hapa ni mojawapo ya hospitali ambayo ipo kwenye mpango huo.

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Taifa letu la Tanzania linatambulika kabisa kwamba kilimo ni uti wa mgogo, na tangu uhuru tunatambulika kwamba taifa hili ni taifa la wakulima na wafanyakazi. Serikali imesema somo hili linafundishwa kwenye somo la maarifa ya jamii na stadi za kazi. Kimsingi ni mada wala si somo la kilimo ni mada zinafundishwa huko.

Mheshimiwa Spika, swali langu, swali langu, ni lini sasa...

SPIKA: Anayeuliza maswali haya ni mwalimu jamani enhee Endelea Mheshimiwa.

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, swali langu, ni lini sasa Serikali itaweka kipaumbele kuhakikisha kwamba somo hili la kilimo linafundishwa na linakuwa la lazima, kwa maana compulsory dhidi ya masomo mengine kama general study, develop and study ambayo kimsingi tija yake ni ndogo ukilinganisha na tija hii ya somo la kilimo? Serikali inasema ukienda sekondari unachagua maana yake ni option, sasa una opt nini ilhali kwenye msingi hujatengeneza somo?

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali, ikubaliane na mawazo haya kuhakikisha kwamba inalianzisha somo hili la kilimo kuanzia ngazi ya msingi mpaka chuo kikuu?

Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, Serikali imeanza mchakato wa mabadiliko ya mtaala wa elimu, na nichukue fursa hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Samia Suluhu alipoamua kwa dhati na kusema kuna haja kufanya mabadiliko ya mtaala wa elimu. Sasa swali langu hapa, ni lini Serikali itatuletea mchakato huu hapa Bungeni ili sisi tukachakata na kuhakakisha kwamba tunakuwa mstari wa mbele kuhakikisha elimu yetu hii tunaiwekea msingi ulio bora ili watoto wetu waweze kujiajiri na kuajiriwa kupitia na ujuzi huo? Ahsante sana.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, Ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kujibu muhimu kabisa la mwalimu mwenzangu, Mwalimu Sima. Kwa kweli maswali aliyouliza ni ya msingi. Tunatambua kwamba asilimia kubwa ya wananchi wetu ni wakulima. Kwa sasa hivi, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri wangu, somo la kilimo liko kwenye sekondari kama options na kwa upande wa shule za msingi tunafanya stadi za kazi; na tunafanya mapitio ya mitaala.

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu umetuwekea semina, lakini kabla hujatutangazie ile briefing mimi nilikuwa nimepanga tarehe 6 Novemba, 2021 nifanye semina, ingawa nilikuwa sikupanga kwa Bunge lote lakini nilikuwa nimepanga nifanye na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, niwapitishe mpaka sasa hivi Serikali imefikia wapi kwenye mapitio ya mitaala, wadau wanasema kitu gani na uchaguzi wa Wizara ni nini kutokana na maoni ya wadau na mwelekeo wa Serikali kutokana na maoni ya wadau ni nini, ili sasa Waheshimiwa Wabunge wapate nafasi ya kuweza kuweka maoni yao wakati tayari maoni ya wananchi wao tumeshayaweka Pamoja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, labda niahidi tu kwamba hili nitalifanyia kazi kiutawala kuangalia kwamba tarehe 6 ambayo nilikuwa nafikiria kuwa na semina na Waheshimiwa Wabunge tayari Mheshimiwa Wangu Spika kiongozi wetu umeishaichukua hiyo tarehe kwa hiyo tutaangalia utaratibu. Ahsante sana.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Singida Mjini hatuna Hospitali ya Wilaya na ipo ahadi ya Serikali ya kukabidhi majengo ya Hospitali ya Mkoa wa Singida kwa Hospitali ya Wilaya. Sasa nataka kujua ni lini ahadi hii itatekelezwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge, swali lake, kama lifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza alivyo na taarifa na tulivyotembelea mimi na yeye kwenye hospitali yake ya mkoa juzi, tumeona majengo ambayo yanajengwa hospitali mpya ya Mkoa wa Singida. Siyo muda mrefu mpaka mwezi Julai majengo yale yanakwenda kukamilika na hospitali ya mkoa itaondolewa kwenye eneo iliyokuwepo halafu na kuwaachia wilaya hiyo iendelee kutumia hospitali iliyoko pale. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, nadhani kwa majibu haya ya Serikali inanishawishi sasa kuja na Hoja Binafsi Bungeni ili tuwasaidie walimu, tuisaidie pia Serikali na vyama vya wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekiri kabisa kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini kwamba vyama sasa na wanachama wanapanga ada yao ambayo watalipa wanachama.

Sasa nataka kujua; Serikali inapata wapi uhalali wa kukusanya ada za wanachama na kuwapa vyama hali ya kuwa wanajua wako baadhi ya watumishi, hasa walimu wanakatwa bila ridhaa yao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kada ya ualimu ndiyo kada pekee sasa hivi ina vyama vitatu vinavyotetea haki za walimu. Kuna Chama cha Walimu ambacho kinatoza ada asilimia mbili; kuna Chama cha CHAKAMWATA ambacho kinatoza ada asilimia moja; lakini kuna Chama kingine cha KUWAHATA, chenyewe kimeweka fixed amount ya shilingi 5,000.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali haioni haja ya kuleta mwongozo ambao uta-regulate mwenendo wa vyama hivi ili sisi walimu tusiwe soko holela la watu kuja kujitafutia ujira kwenye nanihii yetu hii? Naomba majibu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Sima, amekuwa mtetezi mzuri wa maslahi ya walimu, na yeye mwenyewe amewahi kuwa kiongozi katika vyama hivi vya walimu na kwa hiyo, nimpongeze yeye pamoja na walimu wenzake; Mwalimu Kassim Majaliwa Majaliwa, Mwalimu Jenista Mhagama, Profesa Ndalichako na walimu wengine wengi pamoja na Mwalimu Spika ambaye leo tunaye hapa, Mheshimiwa Dkt. Tulia mwenyewe; nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye jibu, hapa ni kweli kwamba suala hili linasimamiwa kwa mujibu wa sheria na ni Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004. Sheria hii inatoa miongozo wa namna gani ambavyo vyama vya wafanyakazi vinaweza vikasimamia maslahi yake. Na ni takwa la Mkataba wa Kimataifa wa ILO (International Labour Organisation) Sheria Na. 3 katika mkataba huo katika kifungu cha tatu inaeleza kwamba vyama hivi viwe huru na vijiendeshe na kujitaribu vyenyewe, na Serikali anaendelea kuwa regulator tu.

Mheshimiwa Spika, sasa kwenye eneo la vyama kama alivyosema katika zile asilimia, vikao vikuu kwa mujibu wa katiba ndivyo vinakaa na kufanya maamuzi. Lakini hata hivyo, kwenye Chama hiki cha CHAKAMWATA tayari kimekwisha kusimamishwa na msimamizi wa masuala ya vyama vya wafanyakazi na kesi inaendelea, iko mahakamani.

Mheshimiwa Spika, pili, kwenye suala la Chama cha KUWAHATA ambacho wanachaji shilingi 5,000, wanaochajiwa ni wale tu ambao ni wanachama, kama siyo mwanachama hana haki ya kukatwa fedha hizo. Kwa hiyo tutafanya ufuatiliaji na tutashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuweza kuhakikisha haki za walimu zinalindwa kwa sababu walimu ndio nguzo kuu ambayo inatutengenezea Taifa letu, tunapata wataalam kutokana na walimu na walimu hawa ni wadau wa muhimu kwa Serikali hii ya Mama Samia Suluhu Hassan, na hatutawaacha, tutaendelea kutetea haki zao. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa kuwa Serikali iliweka mpango wa kujenga viwanja katika mikoa kumi na moja, ukiwemo Mkoa wa Singida. Sasa nataka kujua ni lini ujenzi huu wa Uwanja wa Ndege Mkoa wa Singida utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli mpango upo wa kujenga Uwanja wa Singida na kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza kufanya feasibility study ya Uwanja wa Singida. Ahsante.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mpango wa Serikali wa kujenga barabara ya bypass kuanzia Kata ya Kisaki - Unyamikumbi - Unyambwa mpaka Mtipa na feasibility study imeshafanyika; nataka kujua tu commitment ya Serikali ni lini ujenzi huu utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema usanifu umeishakamilika, sasa hivi Serikali inatafuta fedha ili tuweze kuanza kujenga kipande hicho cha bypass, ahsante.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Singida Mjini ni Mji ambao unakuwa kwa kasi sana na maeneo mengi hayana vituo vya Polisi hali inayopelekea askari wetu kusafiri kwa umbali mrefu. Je, Serikali haioni haja sasa umefika wakati wa kuwaongezea walau fedha ya mafuta ili waweze kufanya kazi yao vizuri ya usalama wa raia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mussa Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba Makao Makuu ya Mikoa yetu mingi kwa kweli yanapanuka sana na kuhitaji huduma za kipolisi kwa maana ya kuwa na magari, kuelekea kwenye maeneo hayo kuwahudumia wananchi. Niseme kama itakavyokuja kusomwa bajeti yetu hapa mwaka huu Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ameongeza fedha kwenye majeshi yetu ikiwemo Jeshi la Polisi ili kuimarisha shughuli za kiulinzi ikiwemo doria na mambo kama hayo. Kwa hiyo Wilaya ya Singida na Manispaa ya Singida ni moja ya Wilaya zitakazonufaika na ongezeko hilo la Bajeti. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nataka kujua, ni lini Serikali italeta fedha katika Kituo cha Afya cha Kisaki ambacho kimejengwa kwa nguvu za wananchi na Kituo cha afya cha Mwaja ambacho kilipokea shilingi milioni 250 za mwanzo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mussa Sima, Mbunge wa Singida, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawapongeza sana wananchi katika hicho kituo hicho cha afya ambao wamechangia nguvu zao na wanasubiri kuungwa mkono na Serikali. Niwahakikishie Serikali inatambua sana nguvu za wananchi na tutatafuta fedha, ikipatikana twende tukaunge mkono nguvu za wananchi kuhakikisha vituo vya afya vinakamilika. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali lakini tangu 2017 mpaka sasa ni miaka mitano hakuna kinachoendelea. Swali la kwanza, nataka commitment ya Serikali lini ujenzi wa uwanja huo ama ukarabati utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nataka kujua mkakati wa Serikali ambao utahakikisha ujenzi huu unafanyika kwa wakati? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika jibu la msingi, ujenzi huu utaanza pale ambapo Serikali itakuwa imepata fedha na kuupangia uwanja huu kuanza ujenzi. Kwa hiyo, commitment ya Serikali ni kwamba tayari tumeshaanza hatua za awali kwa maana ya kufanya usanifu na kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, tunaendelea kutafuta fedha pamoja na Washirika wa Maendeleo ili fedha ikipatikana tuanze kuujenga huu uwanja wa Singida.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami niungane na Dada yangu Jesca Kishoa jambo hili limekuwa la muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri kama atakuwa tayari yeye pamoja na hao wawekezaji GEO Wind na wengine tukutane kwa pamoja kabla Bunge hili halijaisha ili kuweza kujadili mstakabali wa mradi huu wa umeme wa upepo pale Singida Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sima la nyongeza kwamba Wizara tuko tayari kufanya jambo hilo kwa maslahi ya wananchi wa Singida na Watanzania kwa ujumla.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana; kwa kuwa Singida Mjini hatuna Hospitali ya Wilaya na kwakuwa Wizara ya Afya ilikuwa tayari kutukabidhi Hospitali ya Mkoa kwa maana ya yale majengo ya Mkoa ili tuanzishe Hospitali ya Wilaya. Sasa nataka kujua ni lini mtatukabidhi hayo majengo ya Mkoa tuweze kuanzisha Hospitali ya Wilaya? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ni kweli anaposema Mheshimiwa Mbunge Hospitali ya Mkoa iko sasa hivi kwenye eneo ambalo Hospitali ya Wilaya ndiyo inatakiwa iwepo na sasa kuna majengo mengine ambayo yanaendelea kujengwa kwenye eneo lingine. Lakini Mheshimiwa Mbunge ni kweli tuna majengo yanamaliziwa siyo muda mrefu ili Hospitali ya Mkoa iweze kuhama lakini nikuhakikishie tuna shida hiyo kule Geita, pale kwako tutahama polepole kwa sababu ukiama ghafla haraka haraka unaweza ukavuruga shughuli za tiba kwenye eneo lako, ili tusikuharibie siasa yako kabla ya mwaka 2025 tunamalizia majengo, tutahama polepole, lakini tutahakikisha kwamba hatutavuruga shughuli zako, cha msingi wape ushirikiano lile lile eneo na mshirikiane kwa pamoja kuweza kutoa huduma. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, ninaipongeza sana Serikali kwa majibu mazuri haya ambayo yanaleta matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Singida Mjini. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa, uwepo wa hospitali ya Wilaya unaenda sambamba na ujenzi wa vituo vya afya. Wananchi wa Kata ya Kisaki wamejenga kituo chao cha afya na Serikali ilileta Shilingi Milioni 50 na kituo hakijakamilika.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha kituo hicho cha afya?

Swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri utakuwa tayari kuambatana nami kwa ajili ya kwenda kutembelea maeneo yote hayo ambayo tumeyataja hapo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima kwa namna ambavyo anawatendea haki wananchi wa Jimbo la Singida Mjini, nimhakikishie kwamba katika zahanati ile ambayo tayari Serikali ilipeleka shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji katika Kata ya Kisaki, natoa maelekezo ambayo tayari Ofisi ya Rais TAMISEMI tulikwishayatoa kwamba zahanati zote ambazo zilipokea shilingi milioni 50 kama hazijakamilika ni lazima Halmashauri kupitia mapato yao ya ndani watenge fedha na kukamilisha. Kwa hivyo, natoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida kuhakikisha zahanati hiyo inakamilishwa.

Mheshimiwa Spika, pili, niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge tutakubaliana baada ya kikao hiki tupange ili twende kufanya ziara katika Jimbo lake. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu hayo ya Serikali lakini bado kuna changamoto kubwa sana ya wazee kupata huduma ya afya kwenye vituo vyetu vya afya, hususan hospitali zetu za rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niiombe Serikali kuna changamoto kubwa sana, umefika wakati wa kutoa tamko rasmi kabisa kwamba wazee hawa watibiwe bure na ikionekana kuna changamoto yoyote kwenye hiyo hospitali hatua zichukuliwe mapema.

Je, Serikali inatoa tamko gani sasa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge ameielezea vizuri na tunapokea ushauri wake, Waziri wa Afya kwa kushirikiana na Waziri wa TAMISEMI, watatoa maelekezo mahususi kwa maandishi kwa ajili ya hilo kutekelezwa kama inavyotakiwa. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Suala la uvujaji wa mitihani ni ukosefu wa maadili wa kuanzia anayeandaa, mratibu na anayesimamia. Sasa nataka kujua mkakati wa Serikali ambao unaenda kusaidia suala hili la ukosefu wa maadili ni upi? ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Sima kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya swali la msingi kwamba uvujaji wa mitihani kwa mara ya mwisho ulitokea mwaka 2008. Na kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili ni suala la kimaadili na sisi kama Serikali wajibu wetu ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kutoa elimu kuanzia kwa wale ambao wanaotunga mitihani vilevile wale wanaofunga, wanaosafirisha mpaka wale ambao wanakwenda kusimamia zoezi hili la ufanyikaji wa mitihani.

Kwa hiyo tunafahamu ni suala la kimaadili na tumekuwa tukitoa mavunzo ya athari za uvujaji wa mitihani kwa namna moja au nyingine, lakini nimwondoe wasiwasi kwa kiasi kikubwa na kama tukichukua takwimu kwa mara ya mwisho tukizungumza hilo suala la udanganyifu tu mwaka 2011 udanganyifu ulifanyika kwa wanafunzi 9, 736.

Mheshimiwa Spika, lakini mwaka 2021 ni wanafunzi 393 tu ndio ambao walifanya udanganyifu kwenye mitihani. Kwa hiyo tunaendelea kudhibiti na tunaamini baada ya muda si mrefu tunaweza tukapata achievement kubwa kuhakikisha kwamba hakuna mtu ambaye atajihusisha na udanganyifu wa mitihani.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa mradi wa bypass unaanzia Kata ya Kisaki - Nyamikumbi - Unyambwa mpaka Utipa umeshafanyiwa upembuzi yakinifu: Ni lini ujenzi huu utaanza?
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ilishafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Bypass ya Singida. Kitakachofanyika sasa ni kufanya mapitio upya na kupata gharama ya sasa ya ujenzi. Kwa hiyo, barabara hii baada ya fedha kupatikana tutaanza kuijenga ili kupunguza msongamano katika Mji wa Singida, ahsante. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; kwa kuwa uko mradi wa TACTIC wa kujenga soko la kisasa pale Ipembe lakini na soko la vitunguu. Nataka kujua ni lini mradi huu utatekelezwa ili wananchi waweze kupata huduma stahiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sima kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa TATCTIC una awamu tatu. Awamu ya kwanza tayari iko hatua ya kutafuta wakandarasi, awamu ya pili iko hatua ya usanifu wa mwisho na awamu ya tatu itafanyiwa usanifu. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba kabla ya mwaka 2025 Serikali imeweka commitment kuhakikisha kwamba miradi yote ya TACTIC itakuwa imekamilika kwa sehemu na mingi iko kwenye utekelezaji hatua za mwisho, ahsante.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka kujua tu ni lini Serikali italeta fedha kwa ajili ya kukamilisha Kituo cha Afya cha Kisaki? Pia ikikupendeza Mheshimiwa Waziri wakati unaenda Tabora upitie Singida uzungumze na wananchi wa Singida pale Kisaki. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Sima tutapokuwa tunaelekea Tabora basi tutahakikisha tunapita Manispaa ya Singida ili kuona kituo hiki cha Kisaki na tutafanya maamuzi tukiwa pale kadri ya bajeti itakavyoruhusu.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kujenga vyuo vingi vya VETA na ili kuweza kueta hamasa kwa wanafunzi na wazazi kujiunga kwenye vyuo hivi, Serikali ina mpango gani ama mkakati gani wa kutoa mikopo kwa wanafunzi hawa wanaojiunga na Vyuo vya VETA ama vyuo vya kati? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Sima, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba, tunatoa mikopo katika elimu ya juu na elimu hii ya kati. Tumetengeneza mkakati huo, lakini kwa mkakati wa muda mfupi tumezungumza na wadau ikiwemo benki na taasisi nyingine za kifedha. Wenzetu wa NMB tayari katika mwaka huu wametoa zaidi ya bilioni 200 kwa ajili ya mikopo katika kada ya hii ya kati ikiwemo na wanafunzi wa vyuo vya VETA na sisi kama Serikali tunatengeneza mkakati. Baada ya mapitio ya mitaala tutajua kitu gani cha kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naipongeza sana Serikali kwa majibu mazuri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa ziko fedha za uchangiaji wa elimu zinazotolewa na Serikali kupitia kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Wakuu wa Vyuo kwenda kwa Wadhibiti Ubora, fedha hizi zimekuwa na usumbufu mkubwa sana, lakini zimekuwa kero kubwa sana kwa Wakuu wa Shule pamoja na Wadhibiti Ubora. Serikali haioni haja sasa kwamba umefika wakati wa kubadilisha miongozo yake na sheria ili fedha hizi zitoke moja kwa moja Hazina na kwenda kwa Wadhibiti Ubora? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Wadhibiti Ubora wanafanya kazi yao vizuri sana; Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuwajengea uwezo ili kuongeza ufanisi wa kazi katika majukumu yao? Ahsante sana (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu ya swali la msingi, Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali kuhakikisha kwamba Wadhibiti Ubora wanakuwa kwenye mazingira salama ya kufanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyosema kwamba tunakwenda kubadilisha muundo wa kada hii ya Wadhibiti Ubora na sasa tunakwenda kuondoa ile Udhibiti Ubora ngazi ya kanda na kupeleka katika ngazi ya mikoa na katika kufanya hivyo tunasogeza huduma karibu zaidi ya wananchi na vilevile tunaimarisha utendaji kazi kwa ufanisi mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanya haya yote, tutahakikisha vilevile katika eneo hili la uchangiaji tunaenda kulifanyia kazi ili liweze kushuka moja kwa moja kwenda Ofisi za Wadhibiti Ubora badala ya kwenda kwa Walimu Wakuu au kwenda shuleni kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili la utendaji kazi, tumekuwa na utaratibu wa kuhakikisha kwamba Wadhibiti Ubora wanapata mafunzo ya mara kwa mara ili kuwajengea umahiri na kuwawezesha kufanya shughuli zao za kila siku kwa ufanisi, nakushukuru.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninataka kujua tu, kwanza ni lini vijiji hivyo vitafanyiwa tathmini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; pale Singida Mjini, Kata ya Unyamikumbi ndiyo kata pekee ambayo mawasiliano yanasumbua sana: -

Je, ni lini Serikali itatuletea mnara kwa ajili ya kutatua tatizo la mawasiliano katika kata ile?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima kwa niaba ya Mheshimiwa Katani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tathmini tayari imeshaanza kufanyika na awamu ya kwanza tumekamilisha vijiji 2,116. Kwa hiyo naamini kwamba katika awamu ijayo vijiji na kata za Litehu, Ngonja na Mkwiti zitaingizwa katika utekelezaji huo, na baada ya hapo, fedha zitakapopatikana tutafikisha huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, kipengele cha pili kuhusu Kata ya Singida Mjini pale, tutatuma wataalam wetu wakaangalie tatizo ni lipi hasa. Kama ni kuongeza nguvu tutafanya hivyo, na kama itahitaji kupeleka mnara tutafanya hivyo. Ahsante sana.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kulitokea changamoto katika shule yetu ya sekondari ya Utemini ambapo ilipelekea sasa kuwahamisha wanafunzi wale wote kuwapeleka kwenye shule zingine Utemini sekondari Mheshimiwa Waziri. Miundombinu haikuwa rafiki katika ufundishaji na Serikali ikawa imeahidi kuleta fedha za kujenga shule ya Utemini sekondari, nataka kujua tu ni lini fedha hiyo itakuja kuhakikisha shule hiyo inajengwa? ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sima, Serikali kwa sasa imetenga shilingi bilioni 63 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari katika kila Halmashauri hapa nchini. Muda si mrefu Waheshimiwa Wabunge wataona katika Halmashauri zao shilingi milioni 570 ndiyo minimum ambayo itapelekwa kwa sababu tumeangalia na uwiano wa maeneo na gharama za ujenzi, lakini minimum inakwenda shilingi milioni 570 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule za sekondari mpya ikiwemo hizi za katika Manispaa ya Singida.

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa kuwa barabara ya kuingia Singida Mjini, almaarufu kama barabara ya Kibaoni, imekuwa finyu: Ni lini Serikali itaitanua barabara hiyo na kuwa njia nne?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kinachofanyika ni study ya miji yote ambayo inaendelea kukua na Singida ikiwa mojawapo. Kwa hiyo, tunaendelea kufanya study kwenye miji mbalimbali ambayo tunaona kunahitajika kupanuliwa kwa barabara hasa zinazoingia kwenye miji. Hii ni pamoja na miji kama hii ya Dodoma, Singida ambayo tunaona kadiri kunapokucha magari yanaongezeka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea na usanifu wa hizo barabara ili tuone kama zinahitajika njia nne, ama njia sita, ahsante. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa wafanyakazi ni mali ya Serikali na Serikali ina wajibu kwa wafanyakazi hawa.

Je, haioni sasa umefika wakati mfanyakazi halazimishwi kujiunga kwenye chama bila hiari yake? Nadhani ni muhimu sana kutoa tamko hili Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Sima. Kama ambavyo nimejibu, amesema wafanyakazi ni mali ya Serikali. Nami niseme, tunawapongeza sana wafanyakazi wa Tanzania kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii kuliletea maendeleo Taifa letu, lakini tutaendelea kufanya mashauriano na kutoa ushirikiano na vyama hivi vya wafanyakazi ili waendelee kuwa na imani na vyama vyao na kuendelea kuliletea maendeleo. Ni mafanikio makubwa yamepatikana kupitia vyama hivi vya wafanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaona hata Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amepandisha madaraja, ameongeza fedha, anaendelea kupigania maslahi ya wafanyakazi. Kwa hiyo, niwatoe shaka wafanyakazi, tuko pamoja na tutaendelea kuwaratibu vizuri kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, ahsante. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nataka kujua tu, ni lini Serikali italeta vifaa tiba katika vituo vyetu vya afya na hospitali ya wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nitakaa na Mheshimiwa Sima kuweza kupitia katika fedha iliyokuwa imetengwa ya ununuzi wa vifaatiba kwa mwaka wa fedha 2022/2023, kuona Halmashauri ya Manispaa ya Singida imetengewa kiasi gani na kama ilikuwa haijatengewa tutaangalia katika mwaka wa fedha huu tunaoenda kuanza kuutekeleza wa 2023/2024 ili tuweze kuona namna gani fedha hiyo inaenda kwa haraka kupata vifaa tiba hivyo.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Mimi nataka kujua tu, Serikali imeweka mkakati gani wa kuondokana na hili daraja sifuri? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mussa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyozungumza katika swali lililopita, suala la ufuatiliaji au suala la elimu ni lazima pande zote ziweze kushiriki, kwa maana ya mwanafunzi mwenyewe, ni lazima atengeneze mkakati wa namna gani anaweza kujifunza na kuhakikisha kwamba anafaulu kwenye masomo yake. Pia kuna sehemu ya walimu na vilevile kuna sehemu ya wazazi. Kwa hiyo, sisi kama Serikali jukumu letu kubwa ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na miundombinu wezeshi ya kumwezesha mwanafunzi kuweza kusoma na kupata elimu yake sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile lazima tupeleke walimu wa kutosha kuhakikisha kwamba masomo yote yanafundishwa kwa vipindi vyote kwa wakati, kwa maana ya kutekeleza mtaala wetu kwa wakati na sehemu inayobaki ni ya mwanafunzi yeye mwenyewe kujitahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi kama Serikali mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kutengeneza facilities za kuwezesha wanafunzi wetu kufanya masomo yao vizuri, ahsante sana.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba mitihani hii imevuja na inasimamiwa na Wizara ya Afya. Nataka kujua wajibu wa NACTE katika kusimamia mitihani hii ni nini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Sima kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, wajibu wa NACTE kwenye uratibu wa zoezi zima la mafunzo katika vyuo vyetu vyetu vya kati ni pamoja na mitihani hii. Lakini kwa upande wa mitihani ile ya muhula wa kwanza, mara nyingi sana inafanyika na kusimamiwa na kuratibiwa na Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimezungumza kwenye majibu yangu ya msingi kwamba tunakwenda kuanzisha chombo maalum kitakachokuwa kinaratibu masuala haya ya mitihani katika Wizara ya Afya kwa ujumla wake ambayo itashirikiana sasa na NACTE kwa ukaribu. Kwa hiyo, matatizo haya tunakwenda kuyamaliza na kuyaondoa kabisa. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Singida Mjini tumekarabati na kujenga shule ya Sekondari ya Mungumaji na kila kitu kiko tayari na tumeomba ili kuweze kupandishwa hadhi kuwa Kidato cha Tano na Sita lakini mpaka sasa kibali hicho hakijatoka.

Je, ni lini Serikali itatoa kibali cha kuhakikisha sasa tunaanza shule ya Kidato cha Tano na Sita pale Mungumaji Sekondari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mussa Sima, Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Sima na Manispaa ya Singida Mjini kwa kufikia hatua hiyo kukamilisha vigezo vinavyohitajika na nimhakikishie Ofisi ya Rais TAMISEMI, tumelichukua hili na baada ya hapa nitafuatilia nione wapi tumekwama ili shule zianze huduma mapema. Ahsante.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa kuwa imefanyika sensa hapa hivi karibuni na ziko kata zimeonekana ni kubwa zaidi zinahitaji mgawanyo pamoja na tarafa ikiwemo Kata ya Mandewa na Kata ya Minga. Nataka kujua mkakati wa Serikali ni nini kifanyike sasa ili kuweza kuzigawa kata hizo na kusogeza huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Mussa Sima, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tunafahamu kwamba kuna kata kubwa, kuna tarafa kubwa na Serikali inatambua inatambua umuhimu wa kugawa maeneo hayo kusogeza huduma za kijamii, lakini utaratibu ni uleule tuanze kwenye Vikao vya Kisheria katika ngazi zetu za Vijiji, Kata, Wilaya, Mkoa kisha kuwasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kufanya tathimini ya vigezo hivyo na kuona uwezekano wa kupata maeneo hayo, ahsante. (Makofi)