Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mashimba Mashauri Ndaki (27 total)

MHE. MASHIMBA M.NDAKI: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina swali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa wananchi walionufaika na fedha hizi za mikopo wanakatwa kupitia waajiri wao, lakini hawapati taarifa kwamba ni lini deni lao hilo litaisha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kutoa taarifa hizo kwa wanufaika hao wanaokatwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kuwashukuru na kuwapongeza sana hao ambao tayari wameshatambua wajibu wao wa kurudisha mikopo, kwani heshima ya mtu ni kukopa kwa staha, lakini pia dawa ya deni ni kulipa.
Mheshimiwa Spika, kwa misingi hiyo, napenda kusema kwamba katika mfumo wetu wa kulipa kupitia sheria zilizopo, tumegundua pia kulikuwa na upungufu wa aina mbalimbali ikiwemo na baadhi ya maeneo mengine, badala ya kukata kwa kutumia 8% ya mshahara, wamekuwa wakikata aidha kwa kusema ni shilingi nane au vinginevyo. Pia hizo taarifa zimekuwa hazipatikani siyo kwa wale ambao wanakatwa, lakini pia hata kwa bodi katika kuhakikisha kwamba watu wote wanalipa.
Mheshimiwa Spika, kwa misingi hiyo, tunashukuru kwa ushauri, lakini pia na sisi wenyewe tumekuwa tukifanyia kazi ili kuona kwamba wanufaika wanaolipa na sisi Serikali, wote tunakuwa na taarifa zinazostahili.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. MASHIMBA M.NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile pia usikivu wa Redio ya Taifa ni dhaifu sana kwenye Mkoa wa Simiyu na kwa vile hakuna mwakilishi Mkoa wa Simiyu anayewakilisha TBC wala Redio ya Taifa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwa na mwakilishi Mkoani na pia kuboresha usikivu huo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mikoa ambayo nilitembelea mwanzoni ni pamoja na Mkoa wa Simiyu na nilipofika ni kweli nilikuta tatizo la TBC kutokuwa na mwakilishi. Hii ilitokana na kwamba Mkoa huu ulikuwa ni sehemu ya Mkoa wa Shinyanga. Kwa hiyo, TBC ilikuwa na mwakilishi pale Shinyanga, ulipopatikana Mkoa mpya taratibu zilikuwa zinafanyika za kupata mwakilishi pale, bahati mbaya taratibu hizo zilikuwa zinakwenda taratibu. Nilipotoka pale tumeagiza na taratibu hizo zimekamilika na sasa Mkoa wa Simiyu utakuwa na mwakilishi wa TBC na hivyo kazi za TBC zitafanyika vizuri katika Mkoa wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado liko tatizo la usikivu kama ilivyo katika mikoa mingine ambayo inakabiliwana tatizo hilo na Mkoa wa Simiyu ni katika mikoa ya kipaumbele katika uboreshaji wa matangazo ya Shirika la Utangazaji la Taifa.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Hospitali ya Wilaya ya Maswa ina majengo mazuri na yamekamilika, mojawapo ni jengo la upasuaji, lakini hakuna vifaa kwa ajili ya kazi hiyo ya upasuaji na wataalam; na kwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alifika hapo akaahidi kwamba vifaa vitakuja na wataalam Madaktari wawili wataletwa kwenye Wilaya ya Maswa. Sasa Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, baba mwenye nyumba akisema maana yake hiyo hoja imekwisha. Kama Rais amekuja ameshatoa ahadi hiyo, ndiyo maana nimesema jukumu kubwa ni kwa jinsi gani tutafanya katika utekelezaji. Sasa katika hili, nini tunachotaka kufanya? Tunataka kuangalia jinsi gani tutatumia fursa zote kwamba hospitali hii iweze kupata huduma. Hata hivyo, naomba niwaambie ndugu Watanzania kwa ujumla kwamba, sasa hivi Wizara ya Afya tuna mradi mmoja mkubwa sana, ambao sisi Watanzania tunashirikiana na wenzetu wa Uholanzi, mradi wa shilingi bilioni zisizopungua 44.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu kazi yake kubwa itakuwa kuweka vifaa tiba katika hospitali zetu za kanda na hospitali za mikoa na kwa sababu Maswa kuna kipaumbele maalum, tutaangalia jinsi gani tutafanya eneo hili lipate vifaa tiba. Sambamba na kuweka kwamba wataalam waweze kupatikana ili mradi wananchi wapate huduma za upasuaji katika Hospitali ya Maswa.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa barabara hii inatumiwa na magari mengi yanayotoka Meatu, Kwimba, Maswa, Bariadi na hivyo kufanyiwa matengenezo mara kwa mara na kuigharimu Serikali. Serikali haioni kuna haja sasa ya kuanza kuitengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa vile madaraja matatu aliyoyataja Mheshimiwa Naibu Waziri yote yako Wilaya ya Kwimba. Kuna daraja moja ukitoka tu Kijiji cha Malampaka na kuingia Wilaya ya Kwimba halijajengwa, je, ni lini sasa hilo daraja nalo litakarabatiwa lipanuliwe ili kuweza kusaidia barabara hii iweze kudumu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea ushauri wake na TANROADS wataangalia kama kutakuwa na uwezekano wa kupanua lile daraja pamoja na kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Watakapotoa ushauri wa kitaalam Serikali itazingatia mahitaji hayo.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa vile bwawa hili lilikuwa likihudumia sio Kijiji cha Mwamihanza tu ni pamoja na Kijiji cha Isulilo, Kijiji cha Kidema na Kijiji cha Kulimi; na kwa vile Halmashauri na Wizara mpango wao uko mbali sana. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa dharura wa kuwapatia maji wananchi wa vijiji hivi, wakati tunasubiri mpango wa Halmashauri na Wizara?
Swali la pili, kwa vile pia Serikali ilishachimba mabwama mengi huko nyuma na sasa hivi mengi yao yamejaa mchanga, kama vile bwawa la Shishiu, bwawa la Jihu, bwawa la Sola, yamejaa mchanga na hivyo hayaingizi maji. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuyafufua mabwawa haya yaweze kujaa maji na kuyatunza ili wananchi wafaidike na huduma iliyokuwa ikitolewa kwenye mabwawa haya pamoja na mifugo yao.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, bwawa hili tutalitengea fedha mwaka wa fedha 2017/2018, ni kweli kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge ni mbali na hasa kwa kuzingatia kwamba bwawa hili linahudumia Vijiji zaidi ya vitano, katika Kata ya Kilimi, ambavyo ni Mwabayanda, Ilamata, Kulimi na Mwandu. Kwa hiyo, wananchi hawawezIe kusubiri mpaka mwaka wa fedha 2017/2018. Namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, bwawa hili tutahakikisha tunatafuta fedha hata kama ni za dharura ili tuweze kulikarabati na kwa sababu mpango wa Serikali baada ya miezi sita, mwezi wa Desemba kunakuwa na marudio ya bajeti, kufanya budget review, basi tutahakikisha Mheshimiwa Mbunge, tunampa kipaumbele ili kuweza kuweka fedha kuhakikisha kwamba bwawa hili tunalikarabati ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ameeleza kwamba kuna mabwawa mengi ambayo yamejengwa muda mrefu, lakini mabwawa haya yamejaa mchanga na kwamba Serikali ina mpango gani kukarabati haya mabwawa. Swali la Mheshimiwa Mbunge ni zuri, lakini swali hili pia limewahi kuulizwa na Mheshimiwa Andrew Chenge, kwamba katika maeneo yake kuna mabwawa ambayo yalijengwa zamani, yana magugu maji na yamejaa mchanga. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika haya mabwawa yaliyojengwa yana matatizo makuu mawili: Moja, yanajaa michanga na pili, yanakuwa na magugu maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji sasa hivi, tayari inajipanga na itaanza kufanya ukarabati kwa kuondoa magugu maji kwa kutumia njia mbili, njia moja ni njia ya kibailojia; tayari tumeshafanya mazoezi kupitia Ziwa Victoria, tuna wadudu wanaitwa mbawa kavu, ambao wakiwekwa kule wanakula yale magugu maji. Pia tutahakikisha kwamba tunaondoa mchanga kwenye haya mabwawa kwa kufanya utaratibu ambao unajulikana kama dredging, kuhakikisha kwamba tunapanua capacity, mabwawa yaendelee kupata maji.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nashukuru pia kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi tuna wataalam wengi katika sekta mbalimbali kama nilivyozitaja; na watalaam hao wapo hapa nchini na wengine wanafanya kazi za chini zaidi kuliko viwango vyao vya utaalamu na ujuzi. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kurejea Sheria hii ya Ajira kwa Wageni ili kwamba Watanzania hawa ambao wana ujuzi kwenye maeneo tofauti tofauti waweze kupewa au kuajiriwa nafasi hizi za juu kwenye NGOs na taasisi binafsi zilizoko hapa nchini? Swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwenye majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri anasema mgeni anapoombewa kibali anarithisha utaalam kwa Mtanzania. Je, Serikali ina utaratibu gani wa kufuatilia kama kweli hawa watu walioajiriwa wanarithisha huo utaalam kwa Watanzania kwa sababu tunaona wanapewa hizi kazi halafu anaendelea kufanya kazi hizo miaka miwili, anamaliza mkataba anaongezewa miaka mitatu mingine, anaendelea nenda rudi. Sasa Serikali ina utaratibu gani wa ufuatiliaji juu ya jambo hili, ili kuhakikisha kwamba Watanzania ambao wako chini ya huyu ambaye atarithisha baadaye…
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Wanapata hizi nafasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameuliza Serikali haioni umuhimu wa kurejea sheria hii na ihakikishe kwamba inatekelezwa, ili Watanzania waajiriwe katika nafasi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema pale awali, Sheria hii Namba Noja ya mwaka 2015 ndio sheria ambayo inatusaidia katika uratibu wa ajira kwa wageni. Kwa hiyo, kabla ya mgeni hajaomba nafasi yoyote katika nchi yetu hii utaratibu ni kwamba, lazima Kamishna wa Kazi ajiridhishe juu ya ujuzi ambao mgeni huyo anao na nafasi ambayo anaiomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tutaendelea kuisimamia sheria hii kuhakikisha kwa kwamba wale wageni wote wanaokuja na wenye ujuzi ambao unapatikana nchini, basi nafasi zao hizo wasipewe na badala yake Watanzania waweze kuchukua nafasi hizo. Hilo linafanyika na tumekuwa tukifanya kaguzi mbalimbali ambazo tumebaini baadhi ya wageni wengi ambao mwanzo walitoa taarifa za uwongo na baadaye baada ya kubaini kwamba, ni taarifa za uwongo tumefuta vibali vyao na nafasi zao wameendelea kupewa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili, alitaka kujua ni utaratibu gani ambao huwa tunautumia katika urithishaji wa ujuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria Namba Moja ya mwaka 2015, inaeleza wazi ya kwamba, mgeni yeyote ambaye anapata kibali cha kufanya kazi lazima kitengenezwe kitu kinaitwa succession plan ambayo inawasilishwa kwa Kamishna wa Kazi ya kuona ni namna gani mgeni huyu amekuwa ana Mtanzania ambaye anamu-understudy na anajifunza kupitia kwake. Kwa hiyo, ziko fomu maalum ambazo zinajazwa na kuwasilishwa kwa Kamishna wa Kazi kuthibitisha kwamba ni kweli kuna Mtanzania ambaye yuko chini na kweli ananufaika na ujuzi wa mgeni huyo.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imeshatenga eneo ambalo Shirika la Nyumba la Taifa wanatakiwa kujenga nyumba, sasa ni miaka miwili.
Je, Shirika la Nyumba bado lina mpango wa kujenga nyumba kwenye Mji wa Maswa au mpango huu umesitishwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, National Housing bado inayo dhamira ya dhati ya kujenga nyumba katika maeneo yetu kwa nchi mzima na hasa pale Halmashauri zenyewe zinapokuwa ziko tayari zimetenga maeneo kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa eneo na Maswa bahati nzuri nilifika na nafahamu eneo lilipo bado dhamira ya Shirika iko pale pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo
linatakiwa kufanyika kwa sababu mara nyingi pia tumekuwa tukilalamika kuwa bei ya nyumba kuwa kubwa, sasa Halmashauri ambazo zina maeneo kama Maswa wanatakiwa kuwa wamefanya maandalizi ya miundombinu katika maeneo yao, ikiwepo suala la barabara, suala la maji na suala la umeme ili watakapo kuja kujenga zile nyumba basi ziwe na gharama nafuu kama ambavyo inatarajiwa kuwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo napenda
kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya shirika bado ipo pale pale kujenga nyumba kwa kihakikisha Watanzania wanakuwa na makazi bora.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa, mikoa niliyoitaja inakumbwa na tatizo la upungufu wa chakula mara kwa mara; na kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema wanao huo mpango kabambe wa kuanzisha au wa kujenga mabwawa kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini. Je, Serikali inaonaje juu ya kuyapa kipaumbele maeneo ya Mikoa hii ya Shinyanga, Mwanza, Singida, Dodoma, Tabora ili kuweza kujenga mabwawa hayo ili wazalishe chakula wakati mvua zinapokuwa hafifu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa, pia katika Wilaya ya Maswa tuna mabwawa madogo madogo mengi, likiwemo bwawa la Seng’wa, Mwamihanza, Masela, Sola na mengine. Je, Serikali ina mpango gani wa kuyafufua mabwawa haya kwa kuwa, sasa yamejaa mchanga, ili yatumike kuwapatia wananchi wetu maji, lakini pia yatumike kwa kilimo cha mboga mboga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ametaja Mikoa ya Shinyanga, Tabora na mikoa mingine ambayo ina uhaba wa mvua na kwamba, je, Serikali ina mpango gani wa kuipa hii mikoa kipaumbele katika ujenzi wa mabwawa. Sasa ipo timu ya wataalam ambao wanapitia maeneo yote yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yao itatuelekeza sasa ni sehemu gani ambayo inaonekana kuwa na kipaumbele kwa ajili ya kuwekewa hayo mabwawa. Wakishakamilisha hiyo taarifa, mwaka huu wa fedha tulionao basi tafiti zitaelekea kwenye hayo mapendekezo ya maeneo ambayo yanahitaji kujengwa mabwawa na maeneo ambayo yana ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili limezungumzia kuhusu Maswa, wilaya yake na kwamba kuna mabwawa yaliyopo tayari, lakini yameshajaa mchanga. Sasa Serikali ina mpango gani. Tulishasema katika Bunge hili, tumeelekeza halmashauri kuhakikisha ama zinasanifu kujenga mabwawa kila wilaya, kila halmashauri au kufanya ukarabati wa mabwawa hayo yaliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale ambapo wanashindwa tumewaelekeza kwamba, wawasiliane na sisi, ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kwamba, tunafanya ukarabati au tunajenga mabwawa na hasa pale inapokuwa kwamba, mabwawa hayo yanahitajika kwa ajili ya maji safi na salama ya matumizi ya majumbani. Kwa hiyo, niendelee tena kusisitiza halmashauri zihakikishe kila mwaka zinatenga fedha kwa ajili ya miundombinu ya mabwawa madogo ya maji.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nishukuru pia kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini nataka kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Serikali pia ilitenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kufanya usanifu na ushauri kwa mradi huu wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwa miji hiyo mitatu. Mwaka huu pia wameweka kama shilingi bilioni mbili kama alivyosema. Je, Serikali inatuhakikishiaje sisi wananchi wa Maswa Magharibi, kwamba kazi hii sasa itafanyika mwaka huu na mradi uweze kuanza mwakani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa miradi mingi ya visima vifupi alivyovitaja Mheshimiwa Waziri inakauka wakati wakiangazi kikali, mwezi wa nane, wa tisa na wa kumi. Je, Serikali haioni sasa kutupatia maji kutoka vyanzo vya kudumu kama mabwawa makubwa pamoja na miradi kama hii ya kutoa maji Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Ndaki kwa sababu kwanza ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji, lakini pia amekuwa ni Mheshimiwa ambaye tunaongea naye sana, anakuja ofisini kufuatilia suala la maji katika jimbo lake na nilishawahi kutembelea katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la kwanza ni kwamba katika bajeti ya mwaka 2016/2017 tumetenga shilingi bilioni moja na mwaka huu haujaisha, hela hiyo ndio iliyotufanya tuanze kufanya usanifu wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda kupeleka Malampaka, na kuna kazi kubwa ambayo imeshafanyika, na ni matarajio yetu kwamba baada ya kukamilisha uzanifu tunaanza sasa kutangaza, na fedha hiyo tutaangalia utaratibu ili iweze kuanza kutumika katika mradi huu tukishapata wakandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya utaratibu, kama nilivyokwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeona tuwatumie KASHWASA. Wale KASHWASA wana utaalamu mkubwa wameshatekeleza mradi mkubwa, kwa hiyo kutakuwa na wepesi kidogo kwa kushirikiana na halmashauri yako tuhakikishe kwamba mradi huu unatekelezwa kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la visima vifupi, ni kweli kabisa maeneo mengi tumechimba visima vifupi lakini hivi vinapata maji kipindi cha mvua na muda kidogo wa miezi michache baada ya mvua. Kutokana na hilo basi sasa hivi tunafanya utaratibu, kama ulivyopendekeza mwenyewe, kuangalia sehemu inayofaa kuchimba mabwawa tunahakikisha kwa kushirikiana na halmashauri tunasanifu na tunachimba mabwawa yaweze kutunza maji kama ambavyo bwawa lile la Maswa linatunza maji na kulisha vijiji 11 pamoja na mji wa Maswa, lakini pia na kutumia vyanzo vya kudumu kama bomba la KASHWASA kama tunavyotaka kufanya sasa hivi ili kuachana na visima vifupi.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Serikali kuhusiana na barabara hizi, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kuna madaraja makubwa matatu kwenye barabara hizi ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amezitaja na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imekuwa ikileta bajeti yake ili iweze kuyajenga madaraja haya matatu lakini TAMISEMI wanapunguza bajeti hiyo kiasi kwamba Halmashauri imeshindwa kujenga haya madaraja matatu. Je, Serikali inasema nini juu ya madaraja haya kwa sababu yasipojengwa ni kikwazo kikubwa kwa usafiri kwa wananchi wa Wilaya ya Itilima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga daraja la Mwabasabi, ni ya mwaka juzi. Serikali inasema nini juu ya ujenzi wa daraja hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wakati mwingine bajeti zinakuja lakini kutokana na ukomo wa bajeti mapendekezo mengine ya Halmashauri yanakuwa yamekwama. Katika mchakato wa bajeti ya mwaka huu tulivyokuwa tukipitisha hapa, tuliona ni jinsi gani Ofisi ya Rais, TAMISEMI itahakikisha inaangalia vipaumbele katika maeneo korofi hasa kuondoa vikwazo na ndiyo maana tumepitisha bajeti ya shilingi bilioni 247.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajitahidi kuangalia katika mpango wetu wa kuondoa vikwazo maeneo mbalimbali pale ambapo kuna vikwazo vya msingi katika ujenzi wa madaraja tutatoa kipaumbele. Naomba niwasihi wataalam wetu kule site waanze kufanya designing na needs assessment katika maeneo mbalimbali ili kuonyesha ni gharama kiasi gani zinahitajika katika ujenzi wa madaraja haya ambayo yatahusika. Kwa hiyo, naomba niseme kwamba kama Serikali tunalichukua hili lakini katika mpango wetu wa kuondoa vikwazo tutatoa kipaumbele katika maeneo haya. Lakini suala la ahadi ya Mheshimiwa Rais, naomba niwahakikishie lengo kubwa la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kwamba ahadi hizi zote zinatekelezeka. Naomba nimhakikishie kwamba katika kipindi hiki cha utekelezaji wa Ilani 2015 - 2020 daraja hili ni miongoni mwa maeneo ambayo tunaenda kuyajenga, lengo kubwa ni ili ahadi ya Mheshimiwa Rais iweze kutekeleza katika maeneo hayo.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa shamba hlili la Shishiu hakuna mifugo inayokusanywa pale na kwakuwa pia katika masterplan ya Waizara ya Mifugo wana lengo la kuzalisha mbegu na malisho kwa ajili ya mifugo ili kuweza kuboresha ufugaji wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa kuwa lengo la Wilaya ya Maswa sio kubadilisha lakini ni kuitumia kwaajili ya kuzalisha mbegu na malisho. Je, Serikali haioni umuhimu wa kufikiria upya uamuzi wake huu ili kwamba eneo hili lipewe kwa Wilaya sio kumilikisha ili waweze kutumia kwa ajili ya kuzalisha mbegu na malisho kwa ajili ya mifugo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa pia maeneo kama haya yako mengi nchini Mheshimiwa Naibu Waziri ametaja vituo 28 pia ziko Ranchi nyingi ambazo wala hazitumiki ipasavyo; je, Serikali inaonaje ikifanya vituo hivi pamoja na Ranchi kama vituo vya kujenga uwezo wafugaji wetu ili kwamba waweze kuzalisha mbegu na malisho ambayo ni changamoto kubwa kwenye nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi kwa swali zuri kabisa la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa maeneo haya kama nilivyoeleza katika jibu la msingi bado unabaki palepale hasa ikizingatiwa ya kwamba tunakwenda katika kipindi cha Tanzania ya viwanda na eneo nyeti kabisa hili la viwanda vya uchakataji na mazao ya mifugo ndio hasa unaoangaliwa. Ninachoweza kumshauri Mheshimiwa Mashimba Ndaki yeye na wenzake katika Halmashauri ya Maswa wanaweza kuandaa mpango mkakati na wakauwasilisha katika Wizara kwa ajili ya kutazamwa kama itawezekana kuweza kuandaa hati ya maridhiano kwa maana ya memorandam of understanding kuweza kufanya haya anayoyasema ya kuboresha bila ya kubadilisha lile lengo la msingi la kutumika kwa maeneo haya kwa ajili ya mifugo na kuongeza thamani ya mifugo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili hili la Ranch, naomba nimwambie Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki na Waheshimiwa Wabunge wote, katika masterplan yetu ambayo inaendelea kuandaliwa ni kwamba maeneo haya tunawapa umuhimu mkubwa sana na shirika letu la Ranchi za Taifa hivi sasa tuna mpango mkubwa wa kulihuisha na lina mpango mzuri wa kuhakikisha kwamba Ranchi zetu zinakwenda kusaidia kuinua tasnia hii ya huduma za mifugo na hatimaye kuleta kipato kikubwa kwa nchi yetu. (Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naitwa Mashimba Mashauri Ndaki hivyo ukisema Mashauri Ndaki bado ni sawa. Niulize swali moja la nyongeza, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri.
Kwa kuwa, tuna chuo kizuri cha VETA pale Maswa Mjini na kwa kuwa pia, tuna Chuo cha Maendeleo ya Jamii Malampaka, wakati huu ambapo matayarisho ya kujenga Chuo cha VETA cha Mkoa yanaendelea, Je, Serikali ina mpango gani wa kuviboresha vyuo hivi viwili ili viweze kuanza kuchukua vijana wakati tunaendelea na mpango wa kujenga Chuo cha VETA mkoani?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwamba Serikali ina mpango gani wa kuviboresha vyuo vya ufundi vya Malampaka na Chuo cha Ufundi cha VETA niseme tu kwamba, Serikali itafanya mapitio ya uendeshaji wa mafunzo ya ufundi stadi nchini. Nimekuwa nikisikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge na maswali ambayo wamekuwa wakiuliza kuhusiana na suala la mafunzo ya ufundi stadi VETA ni kwamba, Wizara ya Elimu inaona kuna umuhimu wa kufanya tathmini ya mafunzo ya ufundi stadi yanatolewa katika vyuo vyote nchini kwa lengo la kuangalia upya aina ya mafunzo yanayotolewa, kuangalia teknolojia inayotumika, na niseme tu kwamba hili ni zoezi ambalo baada tu ya kufunga Bunge lako hiyo ndiyo kazi agenda namba moja ambayo tutafanya tathmini kwa nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikiwasikiliza sana Waheshimiwa Wabunge michango yao mizuri na maswali yao kuhusiana na VETA wamekuwa pia wanahoji kuhusiana na teknolojia, kwa mfano baadhi ya vyuo vya ufundi vinaendelea kutumia labda cherehani za miguu, wakati zimepitwa na wakati kwa hiyo hiyo ni tathmini ya ujumla ambayo itahusisha nchi nzima ikiwa nii pamoja na maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyauliza. Baada ya hapo hatua mahsusi zitachukuliwa katika kuhakikisha kwamba VETA zinatoa mafunzo ya kisasa, mafunzo ambayo yanaendana na mahitaji ya sasa hivi ya viwanda tunavyotarajia kuvianzisha.
MHE. NDAKI M. MASHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa mradi wa maji kutoka Busega, Bariadi, Itilima hata Maswa Mjini unaishia Maswa Mjini kwa maana ya Jimbo la Maswa Mashariki na kwa kuwa Wizara Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri nimewashauri kwa Jimbo la Maswa Magharibi tuunganishwe na mradi wa maji unaotoka Ngudu, Malya, kuja Malampaka. Je, Serikali ipo tayari sasa kuchukua ushauri wangu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme tunaupokea ushauri, tutaufanyia kazi, lakini maji yatatoka wapi? Itategemea na utafiti wa wataalam kuangalia sehemu ambayo itakuwa ni rahisi kuyafikisha maji. Kwa hiyo, niseme tu kwamba ushauri wake tunaupokea na lengo siyo kupeleka maji mijini tu, hapana. Kama nilivyosema katika jibu nililojibu muda mfupi uliopita ni kwamba tutakuwa tunaendelea kutenga fedha, kama maji yanatosheleza, yaendelee hata nje ya miji.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo Mradi wa Maji wa Haydom, Mradi wa Maji wa Chujio Wilaya ya Maswa na wenyewe umekuwa wa muda mrefu sana. Mkandarasi amepewa extension ya kwanza hakumaliza, akapewa ya pili, hakumaliza akapewa ya tatu hakumaliza.
Je, Serikali inaonaje kumwondoa huyu mkandarasi na kuweka Mkandarasi mwenye uwezo zaidi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Mkandarasi yule amechukua muda mrefu katika utekelezaji wa mradi, lakini mradi ule uliharibiwa tangu wakati wa usanifu wake. Walisanifu kujenga chujio sehemu ambayo siyo yenyewe, baadaye walivyoingia katika eneo la mradi ikabidi tena wakae kubadilisha, lakini hali m ulipofikia kwa sasa amebakisha sehemu ndogo sana, ameagiza vifaa kutoka nje ya nchi, hatuoni kwamba kwa sasa itakuwa ni busara kumsimamisha kwa sababu vile vifaa vikishafika ni kazi ya kufunga tu na mradi unaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na nishukuru hata bwawa ambalo litahudumia lile chujio sasa hivi mvua zimenyesha maji yamejaa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ninakuomba uwe na subira baada ya muda kidogo tu huo mradi utaanza kufanya kazi. (Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuwa na sheria ni zuri kwa upande mmoja, lakini kwa upande wa pili Halmashauri zetu zinakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi. Sasa Serikali inatoa tamko gani kuhusu kuziwezesha Halmashauri zetu hizi kuweza kukusanya pesa za kutosha ili ziweze kuwalipa watu hawa ambao ni muhimu sana kwenye maendeleo ya vijiji vyetu?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la ukusanyaji wa mapato la Halmashauri kuwa katika hali ngumu ya uchumi, kwanza ni commitment yetu wote Wabunge na Madiwani kuhakikisha kwamba Halmashauri zetu zikusanye vizuri. Kwa sababu, miongoni mwa kigezo kimojawapo cha existence ya Halmashauri lazima iweze kukusanya mapato ndiyo maana imepewa ridhaa kuwa Halmashauri kamili. Katika hili sasa ndiyo maana katika kipindi hiki kilichopita tumetoa maelekezo mbalimbali katika suala zima la ukusanyaji wa mapato, hasa kutumia mifumo ya electronic.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, katika maeneo mbalimbali tuna- success story kwamba leo hii kwa kutumia mifumo ya electronics tumepata mafanikio makubwa. Sasa maelekezo yangu nadhani twende katika compliance vizuri katika matumizi mazuri ya hii mifumo, kuna mahali pengine mifumo ipo, lakini haitumiki vizuri, watu wana-divert kutoka katika mifumo ya ukusanyaji wa mapato hivi, mifumo ile sasa inajukana ipo, lakini wengine hawapati manufaa katika hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwasihi sana Wakurugenzi wote katika Halmashauri zote twende kuhakikisha kwamba katika idara zetu za fedha tunazisimamia vizuri. Lengo kubwa ni kwamba, mapato yaliyopangwa kupitia Mabaraza ya Madiwani yaende kukusanya vizuri ili tukuze mapato katika Halmashauri zetu. (Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali ndogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la Mkuu wa Wilaya ya Maswa limeshajengwa lakini limebakia umaliziaji. Mheshimiwa Naibu Waziri alishafika hapo na kuliona sasa anaweza kutuhakikishiaje kwamba mwaka unaoanza wa fedha, fedha kidogo kwa ajili ya umaliziaji zimetengwa ili Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa aweze kuhamia kwenye jengo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge mwaka huu wa fedha unaokuja tutamaliza lile jengo la Mkuu wa Wilaya, tuna kila sababu kuhakikisha Wakuu wa Wilaya wetu majengo yao yote yanakamilika na tumejipanga katika hilo, Mheshimiwa Ndaki wala usihofu tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo ile kazi kubwa iliyobakia pale tuweze kuiimaliza ili Mkuu wetu wa Wilaya afanye kazi katika mazingira rafiki. (Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa, pesa hizi za Mfuko wa Barabara zinapelekwa kidogo kidogo, kwa mwezi au baada ya miezi kadhaa. Je, Serikali haioni kuna sababu sasa ya kupeleka fedha hizi kwa mkupuo ili Halmashauri iweze kupangilia vizuri ujenzi na ukarabati wa barabara zake kwa umakini zaidi kuliko hivi sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo ni zuri lakini kama mnavyofahamu tunakwenda kwa utaratibu wa cash budget, kadri tunavyopata, tunavyokusanya pesa hizi za barabara ndiyo tunazipeleka hivyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba aondoe hofu Serikali itajitahidi kwa kadri iwezekaavyo na kwa sababu tumejielekeza vizuri katika makusanyo ya mapato, nina imani katika Jimbo lake na najua kwamba katika Mji wake wa Mwasa ana ahadi ya ile barabara ya Mheshimiwa Rais ya kilometa tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu barabara hiyo tumeiingiza katika mpango wa bajeti barabara ile ya one point something billion itaingia pale. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie kwamba tutajitahidi kukusanya fedha na kuhakikisha kwamba commitment zote za Serikali tulizoziweka ziweze kutekelezeka katika Majimbo.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa, sababu mojawapo ya utendaji mbovu wa Mabaraza ya Ardhi ni kwa sababu hawana weledi na mafunzo ya kutosha; na kwa kuwa pia Halmashauri ndiyo yenye jukumu la kuwapa mafunzo Wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Halmashauri hizi hazina pesa, Serikali inaonaje kupiga marufuku Mabaraza ya Ardhi ambayo hayajapata mafunzo ya kutosha kufanya kazi yake mpaka hapo yanapokuwa yamepata mafunzo ya kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kupiga marufuku kwamba Mabaraza yasifanye kazi jambo hilo naomba niseme kwamba hatuwezi kupiga marufuku hapa, isipokuwa tunachotaka kufanya ni kwamba niwasihi hasa Wakurugenzi wa Halmashauri zetu zote 185 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pale inapobainika kwamba kuna Mabaraza ya Kata ambayo uelewa wao ni mdogo katika utaratibu tunaokwenda nao katika kuyaboresha kipindi hiki cha mpito, lazima wahakikishe wanatumia ile staffing yao iliyokuwa katika Halmashauri kuona watafanyaje kuhusu capacity building kwa watu hawa, lengo kubwa waweze kutoa haki stahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hoja ya msingi, kwa hiyo, hatuwezi kusitisha hivi sasa, lakini tutaendelea kuwasihi Wakurugenzi wetu wa Halmashauri zetu wafanye capacity building kwa kushirikiana na Wanasheria tuliokuwa nao, lengo kubwa likiwa, Mabaraza haya yaweze kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mwaka jana niliuliza swali kuhusiana na bwawa la Mwamihanza nikaambiwa Serikali inatafuta fedha; mwaka huu pia nimeuliza juu ya miradi hii ya umwagiliaji kwenye vijiji hivi vitatu majibu ya Serikali ni kwamba bado Serikali inatafuta fedha. Sasa nataka kuiuliza Serikali, pesa itapatikana lini? Kwa sababu kwenye Bwawa la Masela usanifu ulishafanyika na watu walishaondolewa kwenye eneo ambalo bwawa litachimbwa. Sasa Serikali inapata pesa lini ili kuanza ujenzi wa Bwawa la Masela?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inapata pesa kidogo sana, ndiyo maana miradi mingi ya umwagiliaji inakwama. Mradi wangu wa Bukangilija umekwama wa Mwatigi umekwama wa Kulimi umekwama sasa ni lini Serikali itatenga kiasi cha fedha cha kutosha ili kushughulikia miradi ya umwagiliaji hapa nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze kwanza Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyofanya kazi. Pili, amezungumzia kuhusu suala la uchache wa fedha na lini Serikali itatoa fedha. Pamoja na Serikali kutoa fedha lakini kupitia ziara tulizokuwa tumezifanya tumeona katika miradi mingi ya umwagiliaji kumekuwa na changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, tuna miradi ya zaidi ya 889 ambayo imejengwa lakini miundombinu yake haijakamilika, lakini la pili ipo miradi 54 ambayo imejengwa lakini haifanyi kazi kabisa. Kutokana na changamoto hiyo Waziri wangu akaona haja ya kupitia mpango kabambe wa mwaka 2002 wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili kuangalia namna gani tutaweza kutumia fedha ingawa kwa uchache lakini miradi iwe yenye tija. Nataka nimhakikishie kupitita mapitio haya tuliyoyafanya miradi ile ambao tumeiorodhesha na tumeibainisha ipo haja ya kutengeneza maaboreshe na ili hata kama miradi inatekelezawa lazima iwe miradi ambayo imekamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu miradi yake ambayo ameelekeza, katika miradi ambayo tumeanisha na yeye tutamuweka katika utekelezaji ili miradi iende kwa wananchi kama zamani. (Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Suala hili ni nyeti sana na sijui kwa muda tulionao kama unatosha kulizungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri anasema pamba itauzwa kwa kukusanywa na Vyama vya Ushirika vilivyoko kwenye maeneo yetu, makampuni wataenda wanunue pamba hapo. Tunajua wote ushirika kwenye nchi yetu hali yake ilivyokuwa na sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kuuliza swali, nisirefushe maneno, je, Serikali imejiandaa kwa namna gani kuhakikisha kwamba huu ushirika tunaouzungumza uko imara na kwamba utahakikisha mkulima hapotezi pamba yake na bei ya pamba inapanda kulingana na mahitaji?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ni kweli ushirika kwa miaka ya nyuma hapa umekuwa na tatizo sana hasa ushirika wa zao la pamba. Siyo siri kwamba wakulima wengi wa pamba walipoteza pesa zao kutokana na viongozi wa Ushirika ambao hawakuwa waaminifu na hivyo kupelekea Serikali wakati ule kuruhusu watu binafsi kuingia katika kununua pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Ndaki na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba tumefanya jitihada kubwa sana kwanza za kuhakikisha kwamba viongozi waliochaguliwa katika Vvyama vya Msingi vya Wakulima wa Pamba safari hii ni wale viongozi waadilifu ambao hawatachezea pesa za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimetoa rai kwa Viongozi wa Ushirika katika Vyama vya Msingi nchini kote kwamba yule anayetaka kuonja sumu kwa kuiba pesa ya wakulima wa pamba afanye hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na matatizo ya ushirika yaliyokuwapo, lakini lengo la Serikali ni kuhakisha kwamba ushirika utaimarika, wizi katika ushirika utakoma na wakulima wapate sauti ya pamoja kupitia ushirika. (Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Bunge lako limechaguliwa na wananchi na wananchi hao ndio wanachama wa Vyama vya Ushirika wa Mazao wa Kuweka na Kukopa, kwa nini Serikali inaona mashaka kuleta taarifa za COASCO hapa Bungeni ili zichambuliwe na kujadiliwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kama kikwazo ni Sheria ya Ushirika aliyoitaja Mheshimiwa Waziri, nataka kuuliza, ni lini sasa Serikali itaileta sheria hiyo hapa Bungeni ili ifanyiwe marekebisho na hivyo kutoa nafasi ya kujadili hesabu hizi za ushirika za wananchi wetu na ukizingatia Serikali sasa hivi inaweka nguvu nyingi kuufufua ushirika? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba nimjibu Mheshimiwa Ndaki Mashimba maswali yake mawili madogo ya nyongeza kwa pamoja na kwa ufupi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia sana masuala yote ya vyama vya ushirika na amekuwa ni mfuatiliaji mzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi, kama Serikali tuko katika kufanya mapinduzi ya vyama vya ushirika kwenye kuboresha, kufufua na kuimarisha. Kwa maana hiyo, sote tuelewe kabisa kwamba kila zao lina msimu wake katika kulima na kwa maana hiyo hata katika ukaguzi wa mahesabu unatofautiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo sisi kama Serikali hatupati kigugumizi jambo lake tumelipokea. Kama nilivyosema katika lile jibu langu la msingi, kwenye ile Sheria Na. 6 ya mwaka 2013, kifungu cha (4)(1)(b), tutalichukua jambo hili na tutalifanyia kazi ili tuweze kuleta Bungeni kwa ajili ya kurekebisha hiyo sheria ndogo ili mfumo mzima wa vyama vya ushirika na ile dhana nzima ya kuimarisha, kufufua na kuboresha vyama vya ushirika iweze kutiliwa mkazo. Nakushukuru.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi ndiye mwakilishi wa wananchi wa Kijiji cha Igwata na Jimbo la Maswa Magharibi. Msitu huu ulipanuliwa na wakati wanapanua hawakushirikisha wananchi, ukamega mashamba ya watu. Sasa nataka niulize maswali ya nyongeza. Moja; kwa nini Serikali isirejeshe mashamba haya yaliyomegwa kwa wananchi ili waendelee kuyatumia kwa shughuli zao za kilimo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sehemu ya mashamba au eneo lililomegwa kuna makazi ya watu, Serikali inasemaje juu ya watu hawa ambao wameweka makazi kwenye eneo ambalo limeongezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mashimba Ndaki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia sana malalamiko ya wananchi wake ambayo yalitokana na uwekaji wa alama. Sisi kwenye Wizara yetu kimsingi hatukuchukua mashamba mapya ila tuliweka alama, lakini naomba nimpongeze sana kwa namna alivyofuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi ambalo tunaendelea nalo sasa katika Wizara yetu ni kupitia upya malalamiko yote yanayoletwa na Waheshimiwa Wabunge pamoja na viongozi wa Serikali katika maeneo husika. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge kama uchukuaji wa eneo hili una malalamiko, Wizara yetu inapokea malalamiko hayo na tunatekeleza agizo la Mheshimiwa Rais la kuhakikisha kwamba, tunarejesha maeneo ambayo yana malalamiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili, iwapo kuna wakazi ambao wakati wa uwekaji wa mipaka hii walikumbwa na zoezi hili nitamtuma Afisa wetu wa TFS kwenda kuangalia. Iwapo itathibika kwamba, maeneo hayo wananchi bado wanayahitaji tuta-review mipaka ili kuweza kuwaachia waweze kukaa.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa muda niulize maswali mawili ya nyongeza. Nishukuru pia kwa majibu ya Mhshimiwa Waziri lakini nilikuwa na ushauri mmoja na swali moja. Ushauri kwa kuwa Serikali imeamua kutoa maji kutoka kwenye maziwa makuu kama Ziwa Victoria na maziwa mengine ili kuwapa wananchi wake maji ya kutosheleza ingekuwa vizuri sasa inapobuni miradi hii ikafikiria kuwapa maji watu wanaohusika, lakini pia ikafikiria mbele uhitaji wa maji jinsi ulivyo mkubwa kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano Mradi wa Maji wa Ngudu kama ungebuniwa vizuri ungeweza kabisa kutoa maji kwenye vijiji na kata nilizozitaja. Kwa hivyo inapobuni miradi ifikirie kupeleka mradi kwa watu wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali kwa kuwa pia nilishapeleka andiko kwaajili ya kupata maji ya Ziwa Victoria kutoka Wilaya Kishapu kwenda Kata ya Sengwa yenye vijiji vya Seng’wa, Mwanundi, Mandela, Mwabomba na Seng’wa yenyewe. Ni lini sasa wizara itaweka pesa kwenye mradi huu ili uweze kutekelezwa?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya ziada ya Mheshimiwa Ndaki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni ushauri tumeupokea ambapo na ni mipango ya Serikali kwamba tukianza kutengeneza miradi mikubwa lazima tuangalie maeneo ya mbali ili kuhakikisha wananchi wengi wanapata maji safi na salama na ndio maana sasa hivi miradi yote tunayojenga tunaochukua maji kutoka Ziwa Victoria tunatoa maoteo au tunapeleka maji mpaka kilometa 12 inapopita bomba kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kweli tumepokea andiko lake na andiko hilo lina gharama takribani shilingi bilioni kwa ajili ya kutoa maji kwenye bomba kuu la Kashuasa na kupeleka maji kwenye vijiji vya Manawa, Sengwa, Mwabomba, Mandale na Mwanundi ambao tunalipitia sasa hivi na mara baada ya kulipitia tutafanya utaratibu wa manunuzi ili tuhakikishe kwamba wananchi wa maeneo hayo wanapata maji safi na salama kutoka Bomba kuu la KASHUASA.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa sasa lugha ya alama inatumika kwenye chombo kimoja tu cha TBC lakini TV stations zingine hazina ikiwa ni pamoja na TV station ya hapa Bungeni. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba TV stations karibu zote zina wakalimani na watafsiri wa lugha ya alama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipongeze pia maswali ambayo yamejibiwa na Naibu Waziri lakini kama ambavyo swali limeulizwa kwamba sisi kama Serikali tuna mpango gani katika kuhakikisha kwamba vyombo vyote vinatoa huduma ya ukalimani kwa watu ambao wana tatizo la ulemavu, sisi kama Serikali ambao tumekuwa tukisimamia masuala mazima ya habari, kwa upande wa TBC ni wazi kwamba tumeboresha na sasa hivi tuna wakalimani zaidi ya wanne na vipengele vyote muhimu ikiwepo taarifa ya habari na vipindi maalum, wakalimani wa lugha za alama wamekuwa wakitoa hizo tafsiri. Ni takwa la kisheria kuwa na wakalimani na sisi kama Wizara ambayo tunasimamia masuala ya habari tumekuwa tukisisitiza kwamba vyombo vyote vya habari vikiwepo vyombo vya umma pamoja na binafsi vihakikishe kwamba vinakuwa na wakalimani wa lugha za alama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wamiliki wote wa vyombo vya habari kuhakikisha kwamba wanatekeleza takwa hilo la kisheria kwa kuwa na wakalimani wa lugha za alama. Nashukuru. (Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kata za Mwabayanda, Kulimi na Kata ya Mwangonoli zote hazina kabisa mawasiliano ya simu. Je, Serikali ina mpango gani kuzipatia kata hizi mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Ndaki Mbunge wa Maswa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kata hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja, tumeziingiza kwenye awamu ya kufanya tathmini. Tumeshafanya awamu ya kwanza, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya kutoka hapa hizi kata kwa ustadi kabisa tuzipitie ili tukaziingize katika utaratibu wa kuzifanyia tathmini na pale fedha zitakapopatikana tuhakikishe tunafikisha huduma ya mawasiliano katika kata hizi, ahsante sana.
MHE MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Njia Panda - Ikungu kwenda Malampaka kilometa 14 au 15 inajengwa kwa lami, leo ni mwaka wa sita lakini zimejengwa kilometa nne tu. Sasa naomba kujua ni lini Serikali itatenga kiasi cha pesa cha kutosha ili kuweza kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni muhimu kuunganisha Mkoa wa Simiyu na Kituo kikubwa cha SGR pale Malampaka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kuhusu swali lake la muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja ni kweli ndio barabara ambayo inaunganisha SGR, Mkoa wa Simiyu na hata watu ambao wanaweza kwenda na ndio kituo sahihi na hiyo barabara ndiyo inayounga. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itafanya kila kinachowezekana kuhakikisha kwamba ahadi iliyoitoa ya kujenga hizo kilometa 14 ambazo bado kilometa 10 tunaikamilisha ili kuhakikisha kwamba Kituo cha Malampaka kitakuwa ni muhimu sana kwa wananchi wa Maswa na Bariadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inafahamu na itahakikisha kwamba inaijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa kuna malalamiko kwamba hata kazi ndogo ndogo kama za usafi, kufyeka na ulinzi, mkandarasi anatoa wafanyakazi maeneo ya mbali badala ya maeneo ya Seke, Malampaka na Malya. Je, Serikali inamshauri nini mkandarasi huyu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa pia kuna malalamiko kwamba mkandarasi ambaye ndiyo mwajiri hapeleki au anapeleka michango kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kusuasua, je Serikali inasemaje juu ya malalmiko haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, amezungumzia kuhusiana na watu wengi kutoka nje ya eneo la mradi. Moja, nimetoa takwimu ya watu ambao wameajiriwa kutoka kwenye eneo hilo katika Mkoa wake wa Shinyanga.

Pili, nimkumbushe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu ni wa Kitaifa. Hata hivyo, Serikali itaendelea kumsimamiwa na kumsisitiza kwamba, anatafuta kwanza wafanyakazi kwenye eneo husika kabla hajepeleka kipaumbele kwenye maeneo mengine ya nje ya eneo husika.

Mheshimiwa Spika, hoja yake pili ni kuhusiana na michango ya NSSF, kwamba pengine mkandarasi anasuasua. Tunafahamu Sheria ya NSSF (The National Social Security Act) Revised ya 2018 Cap. 50, inamtaka mkandarasi au mwajiri kuhakikisha kwamba anapeleka makato hayo NSSF mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba kuna changamoto kubwa sana kwenye upande wa mkandarasi huyu kwa sasa. Tayari tumeshaanza vikao kupitia wenzetu Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa ajili ya kukaa naye na kuweka commitment, mara tu anapolipwa fedha aweze kupeleka michango hiyo kwenye Mifuko ya Hifadhi za Jamii. Pia, aweze kuwalipa na wazabuni mbalimbali wa ndani. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, naona umesimama.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, napenda tu kuongezea kwenye kile kipengele cha mkandarasi kutopeleka michango kwenye Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Mheshimiwa Spika, nakiri kweli kuna madai ambayo mkandarasi anadaiwa na Mfuko umekuwa ukifatilia madai hayo na kuna makubaliano ambayo NSSF imeweka na mkandarasi ambapo tunataka madeni haya yakamilike ndani ya mwaka mmoja.

Mheshimiwa Spika, nimesimama pia kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kuna utaratibu ambao umewekwa kati ya NSSF na mkandarasi kwa wale ambao wanatakiwa kulipwa mafao yao sasa, kuna utaratibu maalum wa fedha zao kupatikana ili wasiathirike na malipo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba, kama Wizara ambayo tunasimamia mifuko ya hifadhi ya jamii, tutahakikisha kwamba madeni haya tunayafatilia ili haki za wafanyakazi zisipotee. Ahsante sana.