Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Luhaga Joelson Mpina (51 total)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Haya ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza ni suala lile la kwamba masuala ya gesijoto na tabianchi yanasimamiwa na Mkataba wa Kimataifa unaoitwa United Nation FrameWork Convetion on Climate Change. Katika mfumo wake kunakuwa na mtu au sehemu inaitwa focal point ambapo ndipo mambo yote yanapopitia.
Ni kwa nini hakuna sauti ya Zanzibar katika hiyo focal point ya Tanzania, hakuna mwakilishi wa Zanzibar ama alternatively au kutoka Zanzibar ili kuhakikisha maslahi ya Zanzibar yanalindwa katika suala hilo? La kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kumekuwa na taarifa na hali ndiyo ilivyo kwamba Zanzibar kama visiwa vingine vidogo vingi vinaweza kukabiliwa na tatizo hili la ongezeko la gesi na mabadiliko ya tabianchi na kwa hivyo hata uwepo wake upo hatarini. Je, Serikali ina mpango gani wa kudumu na wa muda mrefu katika kuhakikisha kwamba Zanzibar inatoka katika loop kubwa zaidi ya kuilinda ili iendelee kuwepo katika uso wa dunia. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza anasema kwamba ushirikishwaji wa Zanzibar hasa katika suala zima la climate change pamoja na ongezeko la gesijoto kwamba Zanzibar inashirikishwa namna gani. Tumekuwa tukishirikiana na Zanzibar kwa karibu na ndiyo maana hili suala la mazingira limewekwa Ofisi ya Makamu wa Rais ili kuweza kufanya ushirikiano mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Mkutano wa Paris tunaouzungumza ulihudhuriwa na watu kumi na saba, watano walitoka Zanzibar na Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikifanya kazi bega kwa bega na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kitengo cha Mazingira, ambapo tumekuwa tukishirikana kwa kila hali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi juzi hapa kuna suala lilitokea la kudidimia kwa ardhi, kuna sehemu kumedidimia kule Zanzibar, Ofisi yangu hapa ya Mazingira pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Kitengo cha Mazingira wameshiriki kufanya utafiti kuona tatizo hili linasababishwa na nini. Kwa hiyo, kwa ujumla tumekuwa tukishirikiana vizuri sana na Zanzibar hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo limezungumzwa hapa na Mheshimiwa la kuhusu Zanzibar kama kisiwa, kama tunavyojua ni kweli kabisa kwamba, sasa hivi ni dunia nzima ipo kwenye hali ngumu ya mabadiliko ya tabia ya nchi. Joto la dunia limeongezeka kutoka kwenye standard ya kawaida na kufikia nyuzi joto zero point nane tano. Dunia nzima tunahangaika sasa hivi kuhakiksha kwamba hizi nyuzi joto haziongezeki kufikia kuzidi nyuzi joto moja point tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kina cha bahari kimeongezeka kwa sentimita kumi na tisa. Kwa hiyo, hili ni tishio kubwa ambalo lazima tuchukue hatua za dhati za kuhakikisha kwamba tunakabiliana na matatizo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye Mpango wa Maendeleo (framework) ambayo tumeanza nayo sasa hivi, Kitaifa tunajipanga kuhakikisha kwamba Tanzania kama Tanzania inatenga fedha za kutosha kukabiliana na suala la mabadiliko ya tabianchi. Vilevile wahisani wetu, tunaendelea kuhakikisha kwamba wanashiriki katika kuhakikisha kwamba Tanzania inapata fedha za kutosha kuhusu suala zima la mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchini Ufaransa kwenye Mkutano wa Paris, Tanzania imepata fedha dola laki tatu kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabianchi. Vile vile tumepata fedha dola laki nne kwa ajili ya kuripoti mpango wa ripoti ya tatu kwa ajili ya kukabiliana na matatizo ya tabianchi. Pia tumepata fedha dola za marekani mia tatu hamsini na mbili, kwa ajili ya kuandaa tathmini ya kwanza ya kupunguza gesijoto nchini. Kwa hiyo, mikakati hii yote tunayoifanya na hatua ambazo tunazozifanya kupitia mpango wa maendeleo na bajeti yetu, zote hizi zitalenga katika kupunguza athari ya mabadiliko ya tabianchi.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niongeze machache katika kuyakamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Mkutano wa Paris, kila nchi ilitakiwa kutengeneza program inaitwa intended national determined contributions, yaani kila nchi itengeneze mpango wa namna ya kutekeleza makubaliano ya Paris. Katika kutengeneza mpango ule tumeshirikana na wenzetu wa Zanzibar kwa kutambua changamoto mahususi ya kwamba Zanzibar ni kisiwa, uchumi wake unategemea utalii, utalii unategemea fukwe na fukwe zinaathiriwa sana na kupanda kwa kina cha bahari. Kwa hiyo, tumefanya hivyo na tutaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba Zanzibar inabaki kama ilivyo katika uzuri wake na ubora wake ili isiathiriwe na changamoto hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu focal point tumeomba kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais ndio iwe focal point ya Taifa letu katika utekelezaji wa mkataba ule. Ile Ofisi ya focal point itajumuisha Wazanzibar, tutahakikisha hilo linatokea kwa sababu changamoto zetu hizi ni changamoto za pamoja. (Makofi)
MHE. SUZAN A. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni wazi kwamba Tanzania imeathirika sana na mabadiliko ya tabianchi, lakini vilevile sababu kubwa pamoja na kwamba kuna sababu za nje, lakini kuna sababu za ndani ambayo kubwa ni ukataji hovyo wa miti, lakini Serikali kwa muda mrefu imekuwa na kaulimbiu ya kusema kwamba kata mti panda miti.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nilikuwa nasikiliza au naangalia vyombo vya habari hapa Dodoma ambapo ni kati kati ya nchi na Makao Makuu, Mkuu wa Mkoa alikuwa anapanda miti na ikatolewa taarifa kwamba katika miti milioni mbili na laki tatu iliyopandwa ni miti mia tisa tu imeota, sawa na asilimia 0.039. Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba wanafuatilia ili miti inapopandwa iweze kuota ili kuondoa tatizo la mabadiliko ya tabianchi?
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ukataji miti na suala la kupanda miti isiote. Sasa hivi tunaandaa mkakati wa pamoja, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, pamoja na Maliasili na Utalii na wadau wengine kuhusu mkakati wa Taifa hili katika kuhakikisha kwamba tunapanda miti ya kutosha nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, tunawashirikisha kwa karibu sana wataalam wetu wa Chuo cha SUA ili kuweza kujua ni miti gani au ya aina gani inaweza kuzalishwa katika mazingira ya mkoa gani ikastawi kwa uzuri zaidi.Katika kufanya hivyo tayari report ya kwanza tumekwishaipata na tutahakikisha kwamba tunawashauri mikoa mbalimbali namna ya upandaji miti kulingana na mazingira waliyonayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nichukue wito huu kuwahamasisha Watanzania wote, tumeshaagiza kila Halmashauri kupanda miti 1,500,000 kila Wilaya kwa mwaka. Zoezi hili lifanyike na tutahakikisha kwamba wataalam wetu wanawasaidia katika kuhakikisha kwamba mbegu zinapatikana, zinazokubalika kulingana na mazingira hayo na wananchi wapande miti yenye faida na wao miti ya matunda na miti ya mbao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema pia hata suala ambalo lilizungumzwa jana na Mheshimiwa hapa kwamba, unapanda miti lakini mwisho wa siku viwanda vyetu vya juice vinakosa matunda ambayo yanastahili kwa ajili ya juice hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huu tunafanya utafiti pia wa kutosha kuona kwamba, miti inayopandwa, inatuletea na inatupatia matunda ambayo yatakuwa ni chanzo cha raw material kwa ajili ya viwanda vyetu vinavyojengwa hapa nchini. (Makofi)
MHE. ALI HAFIDH TAHIR: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya majibu ambayo hayakuniridhisha ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nilikuwa niseme maneno machache yafuatayo; Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kwamba kwa sasa wananchi wa Kichaka Punda, anazungumzia kwa sasa, ahadi ambayo imewekwa na Mheshimiwa Rais aliyepita ilikuwa ni tarehe 25 Januari, 2008 na hakuna kilichofanywa, yeye anazungumzia, leo kwa sasa. Ahadi haijatekelezwa.
(a) Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, anahakikisha kwamba Kituo cha Afya anachokuzungumzia anafahamu kwamba ni kibovu tangu tarehe 25 Januari, 2008 na hakuna marekebisho yeyote yaliyofanywa?
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, suala la umeme kwenda Skuli ambapo Mheshimiwa Rais alimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mheshimiwa Abdallah Mwinyi na Naibu Waziri, Mheshimiwa Machano Othman, kwamba umeme huo mpaka sasa haujafika na unachokizungumzia sasa hivi ni nadharia. Utakuwa tayari mimi na wewe baada ya kikao hiki tufuatane ili ukahakikishe kwa vitendo kwamba hayo yote uliyoyazungumza siyo kweli?
NAIBU WAZIRI (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir kwa jinsi ambavyo anafuatilia mahusiano ya Kimuungano na jinsi ambavyo ni Mwanamuungano wa kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati najibu swali langu la msingi sikusema kwamba hiki Kituo cha Afya kimeshajengwa, nilisema kwamba Ofisi yangu itafuatilia kwa karibu kuhakikisha kwamba hii ahadi ya Mheshimiwa Rais, iliyotolewa inatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusema kwamba kwa sababu sasa hivi ni kweli anazungumza jambo la tarehe 25 Januari, 2008 ambapo Mheshimiwa Rais aliahidi. Lakini tukubaliane tu kwamba leo ndiyo nalijibu swali hili na sasa tunaingia kwenye bajeti, tuhakikishe kwamba katika bajeti kwa maandalizi tunayoanza nayo sasa, hii ahadi ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nakubaliana naye kabisa kwamba niko tayari, baada ya hili Bunge kwisha nitafanya ziara Zanzibar, pamoja na mambo mengine, nitaenda kuona hii ahadi ya Mheshimiwa Rais, pamoja na umeme. Kwa sababu sisi baada kuwasiliana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ndiyo ilituletea taarifa kwamba tayari umeme umeshapelekwa eneo hilo la kijiji ambacho Mheshimiwa Tahir anakizungumza hapa. Kwa hiyo, kwa mantiki hiyo basi, kama siyo kweli, basi katika ziara hiyo yatabainika hayo na hatua za kuhakikisha kwamba ni lazima ahadi ya Mheshimiwa Rais iwe imetekelezwa tutahakikisha kwamba imetekelezwa.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Athari za mabadilko ya tabia nchi ni donda ndugu kwa Mji wa Pangani. Kwa kuwa Mji wa Pangani ni mji mkongwe ambao umejengwa pembezoni mwa Bahari ya Hindi na Mto Pangani, je, ni lini Serikali itajenga ukuta wa Mto Pangani kwa sababu ni ahadi ya muda mrefu na fedha zake tayari zipo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepania na penye nia pana njia. Tutaujenga ukuta huo na fedha tumekwishapata. Tunatarajia Aprili, 2016, tutaanza ujenzi wa ukuta Pangani ili kuwahakikishia wananchi wa Pangani kwamba maisha yanaendelea. Pamoja na matatizo makubwa ya mabadiliko ya tabia nchi lakini vilevile maisha lazima yaendelee. Tutatumia fedha za wahisani kutekeleza jukumu hili lakini pia tutaendelea kutenga fedha zetu za ndani katika bajeti kuhakikisha wananchi wetu wanaishi salama pamoja na athari hizo kubwa za mabadiliko ya tabia nchi ambazo zinajitokeza hapa nchini.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hivi karibuni tumeshuhudia kwa ukatili kabisa na pasipo kuzingatia haki za binadamu kwa kisingizio cha kutunza mazingira, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imebomolea wananchi ambao wanaishi kwenye mabonde na pembezoni mwa mito. Hata hivyo, tuna taarifa vilevile kwamba miaka minne iliyopita, wananchi hao walitakiwa wahamishwe kutoka mabondeni kupelekwa Mabwepande.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taarifa vile vile kwamba mgawanyo wa viwanja vya Mabwepande ulifanyika kinyume na utaratibu. Je, Serikali iko tayari kumuagiza Mkaguzi Mkuu wa Serikali afanye uhakiki wa viwanja vya Mabwepande ili tujue nani alipata nini na kama kuna tatizo lolote hatua muafaka zichukuliwe ili wananchi waliotarajiwa kupata viwanja hivyo waweze kupata haki yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Zoezi la bomoabomoa lililofanyika Dar es Salaam - Msimbazi, sheria na taratibu zote zilifuatwa. Nataka kusisitiza tu hapa kwamba hakuna tatizo lolote katika zoezi hilo. Kumtumia Mkaguzi wetu wa Hesabu za Serikali kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anaomba kama kuna mambo ya kutaka kujiridhisha sisi tuko tayari afanye hiyo kazi lakini sheria zote zilizingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, sasa hivi dunia imefikia kwenye wakati mgumu sana katika suala hili la mabadiliko ya tabia nchi. Ni lazima sisi viongozi wote tujipange na tuwe mstari wa mbele kuwaambia wananchi wetu waondoke mabondeni. Kwa sababu mafuriko sasa ni suala ambalo litaendelea kuwa permanent kulingana na madhara ambayo yapo sasa hivi yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi. Kwa hiyo, ni lazima sisi viongozi wote tuwe firm kuwaambia wananchi wetu bila kumumunya maneno, waondoke wote mabondeni kwa sababu ni kwa ajili ya afya na maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi tupo tayari Mkaguzi afanye kazi hiyo kwa sababu jambo hili lilifanyika kwa mujibu wa Sheria yetu ya Mazingira kwa maana ya kifungu cha 57(1) ambapo wananchi hawapaswi kuishi ndani ya mita 60 kutoka kwenye mabonde, mito au bahari. (Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la tabia nchi linakabili maeneo mengine. Mji wa Mikindani ni mji ambao uko chini ya usawa wa bahari na kwa miaka mingi maji yakijaa baharini huwa yanaingia mpaka katikati ya mji lakini yalikuwa hayaleti madhara kwa sababu kulikuwa na kingo ambazo zimejengwa ili kuzuia maji yasilete athari kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kingo hizo zimeharibika kwa kiasi kikubwa na kufanya maji yanapojaa baharini kwenda kule kwenye mji mpaka katika makazi ya watu. Je, Serikali ina mpango gani wa kurejesha tena zile kingo ambazo ziliwekwa hasa kipindi hiki ambacho maji katika usawa wa bahari yamekuwa yakiongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi?
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua tatizo kubwa la kuongezeka kwa kina cha bahari. Siku zilizopita nilieleza kwamba sasa kina cha bahari kimeongezeka kwa sentimeta 19. Serikali yetu inachukua hatua za kuhakikisha kwamba tunakabiliana na tatizo hili. Moja, ni pamoja na kuzikarabati zile kuta na tayari tuna miradi inayoendelea. Mwezi wa nne mwaka huu, tutaanza rasmi kuzikarabati zile kuta za bahari ili kuhakikisha kwamba tunadhibiti ule mmomonyoko ambao umefanyika kwenye kuta hizo na kuziwezesha kuwa bora zaidi ili kutokuendelea kumomonyoa kingo za bahari yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niseme kwamba hata kwenye mkutano huu wa juzi wa Paris, Serikali yetu ilipata dola za Marekani 1,052,000. Fedha zote hizi kazi yake kubwa ni kwanza kutupatia uwezo mkubwa wa kupata fedha zaidi kutoka kwenye vyanzo vya fedha vya mabadiliko ya tabia nchi kama Adaptation Fund, Least Developed Countries Fund, Green Climate Fund na maeneo mengine kama UNEP na tumejipanga vizuri tutakapopata fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mengine pia fedha hizi tutazitumia kufanya tathmini ya kina katika maeneo ambayo yameathirika sana na suala zima la mabadiliko ya tabia nchi ili tuweze kuchukua hatua mahsusi ya kutatua tatizo hili. Tutatumia fedha za wahisani lakini vilevile tutatenga fedha zetu za ndani ili kukabiliana na tatizo hili la mabadiliko ya tabia nchi ambalo sasa linatishia dunia, linatishia nchi yetu.
MHE. ALI HASSAN OMARY KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ambayo hata na mimi sasa nimeelewa nini tatizo na chanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zimewekwa hatua za kuchukuliwa kama ambazo tumeziona pale, namuomba Waziri ambaye anahusika na masuala haya ya mazingira na utafiti, japo siku moja twende tukaone ile hali tuweze kuangalia nini kifanyike ili tuweze kupata ufumbuzi zaidi ya hapa ambapo tumeona. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Ali Hassan King kwa jinsi alivyo na mapenzi mema hasa katika suala zima la mabadiliko ya tabia nchi. Ninachopenda kumhakikishia tu hapa kwamba niko tayari na tutafuatana na Mheshimiwa Mbunge tutatembelea maeneo haya yote ambayo yamedidimia na tutaungana na wataalam wengine kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Nataka nimwambie tu kwamba bila kupoteza muda siku ya Jumanne na Jumatano nitakuwa Zanzibar kwa ajili ya kazi hii na tutafuatana naye.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika ahsante. Kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Waziri amelijibu vizuri swali hili na vilevile linatoa siha kwa Watanzania, nina maswali mawili ya nyongeza (a) Mawaziri Wadogo katika miaka 1964 mpaka 1970 station yao ya kazi ilikuwa Zanzibar ili wapate kuelewa, Mawaziri wanabakia Bara, Mawaziri Wadogo ambao walikuwa na Wizara zao za Muungano huwa wanabakia Zanzibar. Je, Mheshimiwa Waziri suala hili analionaje kwa upande wa Wizara za Muungano?
(b) Kwa kuwa Mawaziri wa Muungano wana haki kuwepo Zanzibar mara kwa mara kutembelea katika taasisi zao za kazi, kwa nini wasijipangie kila baada ya miezi mitatu wabakie Zanzibar angalau kwa wiki moja kuona maendeleo ya Zanzibar na kuweza kupata ukweli wa utendaji wa kazi uliokuwepo pale? Asante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kuhusu Mawaziri Wadogo hasa wenye zile Wizara ambazo zinahusu Muungano kubaki Zanzibar, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi ni Mawaziri ambao ni wasaidizi wa Mawaziri wetu ambao tuko katika hizi Wizara za Muungano, ninachotaka nimhakikishie tu ni kwamba siyo tu kubaki Zanzibar, tutafanya kazi ya kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Waziri katika maeneo yote yanayohusu Muungano.
Mheshimiwa Spika, ninachotaka kumhakikishia kwa dhati kabisa ni kwamba Mawaziri hawa na mimi mwenyewe nikiwepo, na ofisi yangu ambayo iko Ofisi ya Makamu wa Rais pale Tunguu Zanzibar, nimepanga ratiba ya kuwepo ofisini pale mara kwa mara, shida zote na majukumu yote yanayonihusu mimi kwa maana ya wananchi wa Zanzibar watanipata kwa urahisi sana.
Mheshimiwa Spika, vilevile kwa sababu ofisi hii ndiyo ambayo inaratibu mambo ya Muungano, Wizara zote zinazohusu Muungano tumeshatoa maelekezo ya Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhakikisha kwamba katika maeneo yao wanatenga muda mwingi wa kuwepo Zanzibar ili wananchi wa Zanzibar wasipate shida ya kupata huduma.
Mheshimiwa Spika, hivyo ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi Naibu Mawaziri hatutapungua Zanzibar na wala hatutapungua upande mwingine, tupo mahali popote kwa ajili ya kushughulikia matatizo yote ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Waziri wangu wa Muungano kuwepo kule mara kwa mara ni hivyo hivyo kwamba tumeshakubaliana ofisini mimi na Waziri wangu na mpaka sasa hivi anaenda mara kwa mara tu Zanzibar. Mheshimiwa Mbunge ametutaka at least kwa miezi mitatu tuwe kule, lakini sisi karibu kila mwezi tunaenda Zanzibar na tutaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Zanzibar hawaoni gap lolote linalohusu mambo ya Muungano.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza.
Je ni lini sasa Serikali itaanza kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara yanayotokana na hii mifuko ya plastiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, tunaanza leo kutoa elimu ya uzingatiaji wa matumizi ya mifuko ya plastiki, wananchi waweze kuzingatia hilo, Sheria na kanuni hii yetu ya 2015 kwamba matumizi ya plastiki ambayo yanayoruhusiwa ni yale tu yenye makroni 50. Kwa hiyo, ni jukumu la Bunge hili na Wabunge wote, wadau wote na wazalishaji na wenye viwanda kuchukua jukumu na kuhakikisha kwamba plastiki zinazozalishwa ni zile tu zenye makroni 50 ambazo ndizo zimeruhusiwa na Kanuni, zaidi ya hapo hairusiwi na haikubaliki na watu watakaoenda kinyume watachukuliwa hatua kali za kisheria, tutachukua hatua kali kwenye viwanda ambavyo vitazalisha zaidi ya kiwango hiki kilichoruhusiwa ikiwa ni pamoja na kufunga kabisa viwanda hivyo. Hatutaruhusu matumizi hayo kwa namna yoyote yatumike nchini. Kwa hiyo, ni jukumu la Bunge hili, ni jukumu la wananchi wote, kuelewa kwamba plastiki iliyoruhusiwa ni ile yenye makroni 50 peke yake.
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, fedha zilizotolewa na wahisani ni zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa kipindi cha miaka mitano; je, ni fedha kiasi gani zilizopelekwa Zanzibar na kwa miradi ipi kwa lengo la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi? (Makofi)
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, kuna harufu kubwa ya ufisadi na matumizi mabaya ya fedha hizi za wahisani, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kuliambia Bunge hili Tukufu ni hatua gani hadi sasa zimechukuliwa na Serikali katika kukabiliana na ufisadi huo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Ngwali kwa swali lake zuri na jinsi ambavyo amebobea katika mambo ya mazingira na ndiyo maana swali lake hapa limekuwa refu sana. Kwanza katika hizo fedha shilingi bilioni 224 ambazo nimezitaja, tumepeleka Zanzibar zaidi ya sh. 17,234,056,000.80. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi ambazo tumezipeleka Zanzibar ni 7.7% ya fedha zote ambazo zilipokelewa na wafadhili, ambazo ni zaidi ya kiwango kilichowekwa cha General Budget Support cha asilimia 4.5. Kwa miradi ipi? Tumepeleka kwa miradi mingi Zanzibar.
Moja, ni mradi ule wa Kilimani ambapo tunajenga makingio, lakini na Kisiwa Panza, pia pamoja na miradi mingine ya upandaji mikoko kwenye maeneo hayo kwa maana ya Kilimani pamoja na Kisiwa Panza. Tunapanda mikoko pamoja na kujenga kuta na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ameuliza kwamba Ofisi hii imechukua hatua gani kwa ufisadi uliozungumzwa, hasa katika hotuba ya Kambi ya Upinzani wakati ule akiwasilisha hapa. Tuliahidi siku hiyo hapa Bungeni kwamba tutafuatilia tujue ukweli wa tuhuma hizi ukoje.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie kwamba tarehe 12 tulishamwagiza Chief Internal Auditor wa Ofisi yetu kufanya mapitio ya matumizi ya fedha za kuhimili mabadiliko ya tabianchi zilizotolewa kutoka muda ule wa mwaka 2010 mpaka mwaka 2015 ili kujua uhalali wa matumizi yake. Kazi hiyo imeanza na itamalizika baada ya siku 30 tu. Kwa hiyo, Bunge hili litapata taarifa nini kilichojiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama taarifa ile itakuwa imekwenda vizuri, maana yake hakuna ubadhirifu wowote, tuwapongeze watumishi wetu kwa kazi nzuri waliyoifanya, lakini kama tutagundua kwamba kuna ufisadi wa aina yoyote, nilihakikishie Bunge hili kwamba hakuna atakayepona wala atakayechomoka, tutachukua hatua kali stahili.
MHE. ESTHER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa suala zima la mazingira na changamoto zake lililoukumba Mkoa wa Mara linafanana kabisa na tatizo lililotokea hivi majuzi la mafuriko, kwa Mkoa wa Kilimanjaro na kuathiri sana maeneo ya ukanda wa chini, yaani Vijiji vya Vunjo, Kahe, pamoja na Chemchem: Je, Serikali ina mpango gani, katika suala zima la uhifadhi wa mazingira kwa Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu swali lililoulizwa kuhusu suala zima hili la mafuriko ambalo linalikumba Taifa letu. Tukubaliane katika principle za kimazingira, ambapo sisi wote humu ndani ni wadau, kwamba kila mtu anatakiwa achukue jukumu hili la tunapambana katika zoezi zima la kuhakikisha kwamba mazingira yetu yako salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua uharibifu wa mazingira uliofanyika Mkoa wa Kilimanjaro. Tunajua hali ya mazingira nchini sasa hivi ilivyo, kwa hiyo, zoezi hili na mafuriko haya na maeneo yote aliyoyataja na tumekuwa tukitolea taarifa kwamba mafuriko haya hayawezi kuwa ya mara moja. Tatizo hili litakuwa ni permanent sasa, kutokana na uharibifu wa mazingira tulionao hapa nchini. Tuchukue jukumu wote kwa pamoja, tumeagiza, sasa hivi tumekuja na mpango mkakati wa upandaji miti. Tunajua kabisa tukipanda miti, tutazuia kwa kiwango kikubwa mafuriko ya maji ambayo yanatokea, kwa maana kwamba ni kinga, lakini vile vile katika kurekebisha hali ya hewa kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba Waheshimiwa Wabunge mliunge mkono zoezi ambalo linasimamiwa na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais la upandaji miti, la kuhakikisha kwamba kila Wilaya inapanda miti isiyopungua 1,500,000 kwa mwaka. Nilivyotembelea Mkoa wa Kilimanjaro, nilikuta wana mkakati wa kupanda miti milioni tano kwa mwaka. Tufanyeni hili zoezi, lakini tushirikiane sana, wale watu wanaoharibu mazingira, miti inakatwa mno, hatuwezi kupona katika ukataji miti wa namna ile. Kila mwaka inafyekwa hekta laki nne, kila mwaka zinakatwa. Kwa hiyo, watu wote walioiandama misitu yetu na kuikata kiasi hicho tushirikiane kuhakikisha kwamba uharibifu huu unakomeshwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Vilevile jitihada nyingine za Serikali za kuleta nishati mbadala mnazisikia.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina swali la nyongeza au ni ushauri kwa Wizara husika. Mafuriko mengi yanayotokea sasa hivi ni kwamba miundombinu au zile njia za maji zimejaa michanga, pamoja na mabwawa yale ambayo ni reserves za mafuriko nazo zimeharibika. Sasa naishauri Serikali, Wizara husika hiyo ya mazingira, pamoja na Wizara ya Maji wawe na mkakati maalum wa kudhibiti zile njia za maji wachimbe zile drainage pattern za mito au/na mabwawa ili ku-conserve au ku-protect mafuriko yasitokee. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunapokea ushauri wake mzuri na ambao tunaendelea kuufanyia kazi siku hadi siku, lakini nitoe wito kwa Wabunge wote, kushiriki siku ya usafi. Inapofika tarehe ya usafi, Waheshimiwa Wabunge wote na viongozi wote lazima tuwe kielelezo kwa wananchi kushiriki usafi huu. Tutashiriki kuzibua hiyo mitaro, kufagia na tutashiriki kuhakikisha kwamba kila eneo linakuwa safi na salama.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kibamba na Ubungo katika ujumla wake ni Mji unaokua kwa kasi sana na ongezeko kubwa la watu linalohatarisha usalama wa mali na raia kitu ambacho Kituo cha Kibamba kinapochelewa kujengwa kinahatarisha usalama wa eneo hili. Serikali haioni umuhimu wa kulichukulia hili jambo katika udharura wake ili kituo kijengwe kwa haraka?
Pili, kwa kuwa tatizo la maslahi ya askari wa Kibamba na maeneo mengine hayatofautiani na yale ya Mbinga, Nyasa, Songea Vijijini, Namtumbo Tunduru na Madaba; haoni kuna ulazima sasa kwa Serikali kuboresha maslahi ya watumishi katika maeneo niliyoyataja ikihusisha fedha maalum kwa ajili ya operation za ulinzi na usalama pamoja na kuboresha makazi yao hususan maeneo ya kulala ili kusitiri utu wao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (K.n.y. NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI): Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kuhusu Serikali haioni udharura wa kujenga? Kama nilivyosema ni kwamba Serikali inatambua sana umuhimu wa kuboresha hicho Kituo cha Polisi cha Kibamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwamba, tayari tumewaongezea gari la pili kwa kuzingatia umuhimu huo huo na nikasema kwamba wakati wowote ule, Serikali inatafuta fedha sasa hivi kwa ajili ya kuanza kujenga vituo vya polisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukijibu hapa mara kwa mara kwamba sasa hivi tuna mpango kabambe wa kujenga nyumba za watumishi 4,136, ambazo zitaenda sambamba na ujenzi wa vituo vya polisi. Kwa hiyo, namuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tayari imeshachukuwa udharura wa suala hili na tutahakikisha kwamba tunajenga haraka sana iwezekanavyo ili kuweza kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo hayo ambayo yametajwa na Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge na concern ya Wabunge wengi sana ni kusikia maslahi ya Polisi wetu, Askari wetu; Serikali imekuwa ikifanya jitihada nyingi sana za kuhakikisha kwamba maslahi ya polisi yameimarishwa. La kwanza, askari ambao hawana nyumba tumekuwa tukiwapatia allowances za pango za nyumba ili waweze kulipia gharama hizo ambazo ni asilimia 15 ya mishahara yao kwa ajili ya kulipia pango.
Mheshimiwa Naibu Spika la pili, tumekuwa tukiwalipia kwa mfano, utalaam maalum, professional allowances. Mtu ana utalaam maalum; ni askari, lakini dereva. Tunamlipa vilevile posho ya asilimia 15 ya mshahara wake, lakini vilevile kwa mfano, unakuwa Polisi umeajiriwa leo, lakini wewe labda ni Doctor of Medicine, tayari umeshakuwa daktari, lakini umeajiriwa polisi na una cheo cha chini, unapewa mshahara sawa na wa daktari kama kawaida bila kujali cheo chako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, kuna hardship allowance kwa wale ambao wanafanya kazi ngumu mnawajua ninyi, FFU, ambao kila mwezi nao tunawapa allowances ya shilingi 100,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Bima ya Afya, askari anapomaliza tu mafunzo yake anakatiwa Bima ya Afya asilimia 100 na Serikali. Pia kuna suala lingine ambalo tumekuwa tukiwadhamini; wanapotaka mikopo kwenye taasisi za fedha pamoja na SACCOS, yote haya yamekuwa yakifanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili la mwisho ambapo Serikali imeboresha maslahi ya Polisi kuyapandisha kuyatoa kwa maana ya ration allowance ilikuwa shilingi 180,000 sasa ni shilingi 300,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wanaweza kuona jinsi Serikali ambavyo inazidi kuboresha maslahi ya askari wetu ili wajisikie kwamba wanafanya kazi nzuri ya ulinzi wa Taifa lao.
Sasa ameuliza, mambo mengine ya kupata fedha kwa ajili ya ulinzi…

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba niulize swali dogo tu la nyongeza kwa maslahi ya Polisi wa Njombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi limekuwa likijishughulisha sana na kusaidia polisi, lakini hali ya polisi katika Mkoa wa Njombe ni mbaya sana. Mkoa huu umeanza mwaka 2012 na mpaka leo hawana nyumba hapa moja.
Je, Mheshimiwa Waziri atanihakikishia kwamba katika nyumba hizo 4,136 zipo zitakazo jengwa katika Mkoa wa Njombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (K.n.y. NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uanzishwaji wa mikoa mipya ikiwemo Njombe, Geita, Simiyu na Mkoa mpya wa Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba, Wizara yangu itahakikisha kwamba katika huu mpango kabambe tunaouzungumza mikoa mipya itapewa kipaumbele na nimhakikishie kwamba Njombe, makazi ya askari wetu pamoja na vituo vyetu vitaimarishwa.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri lakini naomba niweze kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa amekiri kwamba wananchi wako tayari kupanda miti na kuna tatizo la vitalu vya miti, je, Serikali itaweka lini bajeti na utaalam ili kusudi vitalu vya miti viweze kuoteshwa katika kila Wilaya hapa nchini ili wananchi waweze kupanda miti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, miti mingi ambayo imekuwa inapandwa asili yake inatoka nje ya nchi siyo miti ya asili, je, ni lini sasa Serikali itaweka mkazo ili kusudi miti ambayo itaoteshwa kwenye vitalu ili wananchi waipande iwe ni miti ya asili ambayo ni rafiki wa mazingira na rafiki wa maji? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, suala la vitalu na Serikali kutenga bajeti, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya swali la msingi ni kwamba tayari tumeanza kutenga bajeti. Kwa mwaka huu kwa kuanzia tumetenga shilingi bilioni mbili na tunataka katika miaka ijayo ya fedha tuwe na wastani wa kutenga zaidi ya shilingi bilioni 20 kila mwaka ili kuweza kupanda miti inayostahili Kitaifa.
Vilevile tumesema kwamba Halmashauri zote zina jukumu pia la kutenga fedha kwa ajili ya shughuli hii na hivyo sasa katika mpango wa upandaji miti tuliouandaa wa mwaka 2016-2020 unabainisha haya na kwamba Halmashauri zote zitawajibika kuhakikisha tunakuwa na vitalu katika ngazi ya kata mpaka vijiji na kwenye taasisi kama shule ili wananchi waweze kupata miche na mbegu kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili amesema kwamba miti mingi inayopandwa ni ya kutoka nje, suala hapa siyo miti kutoka nje bali tunapanda miti yenye faida na wananchi tunawasisitiza wapande miti yenye faida. Kwa hiyo, wataalam wetu wanaohusika na misitu pamoja na hawa wa mazingira wamefanya upembuzi wa kujua kila eneo linafaa kupandwa miti ya aina gani, linafaa kupelekewa miti ya aina gani ambayo inaweza kustawi lakini vilevile yenye faida kwa wananchi kwa mfano, miti ya matunda, mbao, dawa kikubwa tumewaelekeza wataalam wetu wapeleke miti yenye faida.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na mikakati na Sheria na Sera za Kitaifa za Mazingira ya Mwaka 1997, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Mkakati wa Hatua za Kuhifadhi Mazingira 2008, pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012. Swali langu la nyongeza dogo, Serikali ina mpango gani maalum kwa Mkoa huu wa Simiyu kwa sababu hizi sheria na mikakati yote inaonekana ni ya Kitaifa zaidi? Ninachotaka ni kupata commitment ya Serikali maalum kwa Mkoa huu wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mkoa wa Simiyu kweli unategemea kupata maji kutokana na huu mradi wa Simiyu Resilient Development Programme wa kutoka Ziwa Victoria, lakini katika Mkoa huu Maswa itapata maji katika mradi huu katika phase ya pili. Vilevile jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri linasema kwamba utekelezaji wa kupata maji maeneo haya kutoka Ziwa Victoria unatekelezwa na Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba commitment ya Wizara ya Maji, ni lini itafufua mabwawa ya Wilaya ya Maswa kwa sababu itachelewa kupata maji. Kuna mabwawa mengi zaidi ya mabwawa 35 na yamefanyiwa upembuzi yakinifu yanahitaji shilingi bilioni 1.2 tu kufufuliwa ili watu waweze kupata maji na waweze kuotesha na kumwagilia miti yao. Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Mradi huu pia unapita kwenye jimbo lake la uchaguzi na vilevile unapita kwenye jimbo langu la uchaguzi. Napenda kuwahakikishia wananchi kwamba, mpango maalum ambao Mheshimiwa ameuzungumza hapa, ambao nataka kumwambia mpango maalum wa kunusuru Mkoa wa Simiyu ndiyo huu sasa wa mradi mkubwa kabisa wa Kitaifa ambao utagharimu Euro milioni 313. Serikali tunatarajia kuanza ujenzi huu ifikapo mwanzoni mwa mwaka 2017, tunatarajia tuwe tumeanza ujenzi wa mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia kwamba mradi huu umo ndani ya Ilani ya uchaguzi, lakini commitment ya Serikali na Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba lazima utekelezwe katika kipindi hicho. Mipango mingine ya Serikali inaenda yote kwa pamoja, tulizungumza hapa katika mpango wetu kwamba tumeanzisha Mfuko wa Mazingira sasa ambao tuna uhakika kwamba tutapata fursa nzuri ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi lakini tutapata fursa tena nyingine nzuri sana ya kuhakikisha kwamba tunapambana na uharibifu wa mazingira na kwamba tutaziimarisha taasisi zinazohusika katika usimamizi wa mazingira ili ziweze kusimamia mazingira vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo Mheshimiwa ameuliza hapa, ni kwamba, kuna mabwawa ya maji katika Wilaya ya Maswa ambayo kwamba hayako kwenye hali nzuri na kwa kweli yanahitaji kufufuliwa. Katika hatua hii ninachoweza kusema kwamba wataalam wa ofisi yangu ya mazingira pamoja na wa Wizara ya Maji watakwenda kufanya tathmini na kuona namna bora ya kufufua mabwawa haya ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Wilaya ya Maswa Mashariki la Mheshimiwa Nyongo wanapata maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na ya uchumi.

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongeze majibu ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri kuhusu commitment ya Serikali kwa Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya kuendeleza yale mabwawa ambayo tumeainisha mabwawa 35.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirejea bajeti yetu tumeweka bilioni sita, fedha za ndani kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, yapo mabwawa ambayo tumeyaainisha katika Mkoa wa Simiyu ambayo yatashughulikiwa na bajeti hii katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Swali la kwanza, kufuatia majibu ambayo yametolewa na Serikali na kukubaliana na ukweli kwamba kweli kingo za Ziwa Victoria zinalika na maji kusogea. Kutokana na majibu ya Serikali itakubaliana nami kwamba mita 60 za mwaka juzi siyo mita 60 za mwaka jana na mita 60 za mwaka jana siyo mita 60 za mwaka huu kiasi kwamba inaondoa hata usahihi wa majibu au ushauri uliotolewa wa kuwazuia wananchi wasifanye maendeleo ndani ya mita 60 kufuatana na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004. Kutokana na ukweli huo, Serikali inatoa maelekezo gani kwa experience hii ya Ziwa Victoria ambalo linaendelea kusogea na kuondoa usahihi wa application ya sheria hiyo ya mita 60 kama ambavyo Serikali imeshauri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 57(1) na kufuatia ukweli wa kijiografia wa Bukoba town na Mkoa wa Kagera kwa ujumla ambao kimsingi una milima, mabonde na mtiririko wa mito mingi na kwamba wananchi hawawezi kuwa na mahali pa kuweka makazi yao, Serikali inatoa maelekezo gani kwa experience hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza anazungumzia usahihi wa ziwa kusogelea wananchi na kwamba inaleta shida katika kutambua zile mita 60. Nilisema katika jibu langu la msingi kwamba tutaenda kufanya utafiti ili tuweze kuona hali halisi yenyewe ikoje. Kama maji haya yamesogea, yamesogeaje kwenda kwenye makazi ya watu ili tuweze kujua. Tutakapofanya hiyo tathmini ndiyo itakayotupa majibu kwamba ni ziwa lenyewe limewasogelea wananchi au wananchi wenyewe wamejenga ndani ya mita 60 au wamejenga ndani ya mwambao wa ziwa ambao hauruhusiwi. Kwa hiyo, tathmini ndiyo ambayo itatupa majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopata majibu haya ya tathmini huwa kuna njia nne za kufanya:-
(a) Unaweza usichukue hatua yaani not doing anything katika ulichokiona.
(b) Unaweza ku-accommodate tatizo kwamba wananchi waishi kulingana na hali ya mazingira ilivyo kwa maana ya kwamba sasa wao wenyewe wazuie uharibifu wa mazingira, wakubali hali ya mazingira ilivyo, wajenge nyumba na miundombinu ambayo inaendana na hali halisi.
(c) Unaweza kupeleka njia za kuwazuia (protection) kama ambazo alipendekeza mwenyewe Mheshimiwa Lwakatare kwamba unaweza ukajenga ukuta, unaweza ukapanda miti, unaweza ukafanya mbinu nyingine za kuzuia maji yale yasiendelee kuwasogelea wananchi.
(d)Unaweza uka-retreat ambapo sasa unawataka wananchi wao wenyewe wahame na wasipotaka kuhama unawahamisha kwa lazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapofanya tathmini tutakuja na jibu la usahihi wa ziwa hilo na hali ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mahali pa kuweka makazi na lenyewe vilevile linategemea tathmini tutakayoifanya ndipo hapo tutakapopata mwanya mzuri wa kuwashauri wananchi wa Bukoba nini cha kufanya. Ahsante.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa Sheria ya Mazingira namba 20 ya mwaka 2004, Kifungu cha 182 na 183 (1) (2) na (3) na kifungu cha 36(1) na (2) tunatambua uwepo wa Maafisa Usafi na Mazingira katika Halmashauri zetu nyingi na kwa kuwa wahitumu hao wanamaliza elimu yao ya vyuo vikuu kwa vyuo vyetu hapa kwa wingi sana toka mwaka 1987, je, ni lini Serikali sasa itatangaza ajira ya wataalam hao ili kukidhi mahitaji ya mkakati aliyotaja Waziri? Swali la kwanza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa maeneo mengi ya Nchi yetu mazingira yake yameharibika sana na kupelekea kuwepo ukame mkubwa na kusababisha njaa au uhaba wa chakula na hasa katika Jimbo langu la Bunda na Wilaya nzima ya Bunda. Je, Waziri yuko tayari kuitisha kongamano la kimazingira la kushirikisha Wabunge ili kujua hali halisi ya mazingira katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS-MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la Maafisa Mazingira; kama nilivyozungumza wakati nikijibu swali la msingi kwamba Maafisa Mazingira hawa tayari katika Halmashauri zetu wapo. Aidha, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge katika zile Halmashauri ambazo hawajaweza kuajiri watu hawa basi pale nafasi zitakapoanza kutolewa, Serikali itakapoanza kuajiri tena waajiriwe hawa wa Serikali zile Halmashauri zote zihakikishe kwamba zina Maafisa Mazingira katika Halmashauri husika kama maelekezo ambavyo yamekwishakutolewa. Lakini vilevile na Wizara zote ambazo hazina sekta hii ya mazingira wahakikishe kwamba wana hao maafisa katika sekta hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusiana na ukame ambao umepelekea uhaba wa chakula na Mheshimiwa Mbunge kupendekeza kwamba liwepo kongamano. Ninaloweza kusema kwamba wananchi wote na Wabunge wote ni lazima tukubali kwamba sasa tupo katika mabadiliko makubwa na tuko kwenye athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi ambapo sasa inatupasa sisi sote kuhusiana na kilimo, kilimo chetu sasa hivi ambacho kimekuwa na mvua ya kusuasua kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanaelezwa namna ya kutumia taarifa sahihi za wataalam wetu, tafiti zinazofanywa kulingana na mabadiliko ya tabianchi waweze kujua mbegu bora zinazohitajika kwa sasa hivi ili kupambana na huu uhimilivu wa tatizo la tabianchi, mbegu bora hizo zinazozungumzwa katika mazao hayo, lakini vilevile na mazao ambayo yanahimili ukame huo kulingana na mvua ambazo zinanyesha kwa kiwango cha chini sana sasa. Ipo mikoa iliyokuwa inapata mvua ambazo zinanyesha kwa kiasi kikubwa sana lakini leo hii mvua hizo zimekuwa za kusuasua, kwa hiyo, wananchi lazima wafundishwe hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makongamano na taarifa mbalimbali za kuwahujisha wananchi; Hizo tutaendelea kuzitoa kwa wananchi ili waweze kuwa na tahadhari na hali hii ya sasa hivi ya mabadiliko ya tabianchi na suala la makongamano hilo litazungumzika kulingana na kwamba tumeshaamua kwamba shughuli yoyote ambayo tutaifanya tuhakikishe tunazidhibiti matumizi ya hovyo ya Serikali na hivyo tutahakikisha kwamba elimu hii tunaifikisha bila gharama kubwa sana.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna asiyetambua kwamba mabadiliko ya tabianchi ni janga la kitaifa na kimataifa. Kwa kutambua hilo binafsi kama Mbunge wa Jimbo la Ngara kwa kushirikiana na wataalam wangu katika Halmashauri yangu ya Ngara tumejipanga kuanzisha programu ya kuwa na vikosi kazi vya kupambana na moto kama kisababishi kikuu cha uharibifu wa mazingira. Programu hiyo ambayo tutaiita Community Fire Brigade kuanzia kwenye ngazi ya vijiji na kata.
Sasa swali, Serikali kupitia Wizara ya Muungano na Mazingira wako tayari ku-support programu hii kwa kutoa fedha kwa sababu lengo ni kuanzisha vitalu, kupanda miti katika maeneo ambayo yameathirika na moto lakini pia
kuanzisha miradi ambayo ni rafiki wa mazingira kwa maana ufugaji wa nyuki kwa malengo matatu, moja, kulinda mazingira; lakini pili, kuinua kipato cha wananchi na tatu, kutoa ajira.
MWENYEKITI: Naomba swali kwa ufupi Mheshimiwa.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Tayari nimeshauliza swali…Serikali ipo tayari…
MWENYEKITI: Basi naomba ukae upate majibu!
MHE. ALEX R. GASHAZA: Haya!
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS-MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuanzisha mkakati huo katika Jimbo lake na Wabunge wengine waige mfano wa Wabunge kama mtazamo alionao Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kabisa kwamba ofisi yangu haina tatizo lolote, tunaomba huo mkakati wake atuandikie ili tuweze kuona jinsi ya kuuingiza katika mipango ya Serikali tuweze ku-support mpango huo ili kuweze kuhakikisha kwamba mazingira yanalindwa kwa gharama zote kuhakikisha kwamba mazingira yako salama lakini tunapambana nahii hali ya mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kweli inahitaji wadau mbalimbali wote wa Tanzania wote kwa ujumla kuunga mkono jitihada hizi.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, katika majibu yake Mheshimiwa Waziri amesema ili kupambana na suala la mmomonyoko wa ardhi katika kingo za bahari Serikali imechukua au itachukua hatua ya kujenga kuta katika kingo za bahari pamoja na kupanda miti ya mikoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmomonyoko wa ardhi katika kingo za bahari sasa hivi unakuwa kwa kiasi cha mita mbili kwa mwaka. Kiasi ambacho ni kikubwa sana. Je, Serikali inauwezo gani wa kujenga kuta katika ukanda wote wa bahari ili kuzuia mmomonyoko huu na hiyo elimu ya upandaji hiyo mikoko inatolewa kwa kiasi gani ambayo tunaweza tukakabiliana na kasi hii ya ukuaji wa mmomonyoko katika ardhi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS-MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli ipo kasi kubwa ya kuongezeka kwa kina cha bahari kumesababisha bahari kwenda kwenye makazi ya watu, kumesababisha mmomonyoko mkubwa sana wa fukwe zetu, lakini imesababisha pia hasara kubwa kwa sababu kuna baadhi ya majengo ya biashara na makazi yako kwenye hatari kubwa ya kumezwa na bahari na miundombinu mingine ya kiuchumi mikubwa kama visima vya gesi ambavyo na vyenyewe viko kwenye hatari vilevile ya kumezwa na bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachofanya kama Wizara ya Mazingira katika pande mbili zote tunayo Idara ya Mazingira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, lakini tuna Idara ya Mazingira pia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Serikali hizi zote kwa pamoja zinaendelea kufanya kazi ya kufanya tathmini ya kuweza kubaini hizi athari kila mahali sasa baada ya kubaini zile athari ambazo zinasababishwa na haya mabadiliko ya tabianchi tunaangalia kwamba ipi tuipe kipaumbele leo ili kuweza kuzuia athari ambazo zinaweza kujitokeza kwa muda mfupi kama sasa hivi tutakubaliana Wabunge wote kwamba hapa na mlitupitishia kwenye bajeti na sasa hivi kuta hizo zimeshaanza kujengwa, ukuta wa Pangani, ukuta wa Ocean Road, ukuta wa Kilimani na ukuta wa Kisiwa Panza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, visiwa hivi vyote ndivyo vilikuwa vipaumbele vyetu kwasababu maeneo haya yalikuwa yamepata athari kubwa na hivyo sasa naona Mbunge wa Pangani hapa ana hofu ni kwamba mkandarasi yuko site sasa hivi amekwisha ku-report sasa hivi ameanzia na Ocean Road na ndiyo huyo huyo ambaye atajenga ukuta wa Pangani ndiyo huyo huyo atayejenga ukuta wa Kilimani pamoja na Kisiwa Panza na anauwezo wa kutosha kufanya kazi hizo kwa muda tuliompa.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri yalitolewa na Naibu Waziri, lakini
ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Ulansoni, Nyalelembo Mkalama ambayo yanazalisha sana chakula, yameathirika sana na mmomonyoko wa ardhi. Je, Serikali ipo tayari kupeleka wataalamu kutoka Wizarani na kutoa ushauri namna ya kudhibiti hali hayo kupitia program maalum ya upandaji miti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa tupo katika mkakati wa upandaji miti kama ilivyoelezwa na Wilaya
ya Mkalama imeathiriwa na ukame, kutokana na kutokuwa na miti na mvua kutokunyesha, maeneo kama ya
Mwangeza, Ibada na Mpambala yatapata uhaba mkubwa wa chakula.
Je, Serikali iko tayari kuwasaidia wananchi hao ambao baadhi yao leo wamefika Bungeni kuweza kufuatilia
suala hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti,
kuhusu swali lake la kwanza la nyongeza ambalo anaomba kupeleka wataalamu katika maeneo hayo, namhakikishia kwamba kama Mheshimiwa alivyoomba, tutapeleka wataalam waliobobea katika mazingira, wataalam waliobobea katika masuala ya misitu kwa maana ya waliopo ofisi yetu na wengine walioko Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la kusema kuwasaidia kuhusu suala zima ambalo linajitokeza sasa hivi
la mmomonyoko mkubwa wa udongo, lakini ukame kutokana na miti imekatwa na uharibifu wa mazingira, hilo
kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi, kama kuna ombi mahususi, basi atuletee tutalishughulikia.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira ni suala mtambuka na watu wote wanahitajika kulinda mazingira.
Juzi au jana nafikiri, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii alitoa taarifa kwamba ni marufuku kuanzia Julai kusafirisha mkaa kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine, lakini tukumbuke kwamba miti ni nishati ambayo inatumika na watu wote, hasa mijini na vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni je, si muda muafaka sasa kwa Serikali kutoa ruzuku au tuseme kusubsidize gesi asilia kusudi watu wengi waweze kutumia gesi badala ya kutumia nishati ya mkaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti,
naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Mollel, ambaye kwa kweli ndiye alikuwa Katibu Mkuu wa Ofisi hii ya Makamu wa Rais katika miaka ya nyuma iliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba sasa ni muda muafaka kwa Serikali kutoa ruzuku, ndivyo
tunavyofanya na ndiyo maana mnaona mambo mengi ambayo tunayafanya sasa hivi ni kuhakikisha kwamba gesi
hii asilia pamoja na gesi imported zinakuwa na bei ambayo wananchi wanaweza ku-afford pamoja na jitihada
nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoweza kusema tu kwamba, ni muda muafaka sasa wa Serikali
kuendelea. Kwa hiyo, tutaendelea hivyo. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuhakikisha
tunafanya bidii kadiri inavyowezekana. Kwanza kuhakikisha kwamba, gesi asilia inasambaa nchini, lakini vilevile
kuhakikisha kwamba, imported gas inauzwa kwa bei nafuu ili wananchi wengi waweze kuitumia, waweze kuachana na nishati ambayo inapelekea uharibifu mkubwa wa mazingira kwa maana ya ukataji wa miti hovyo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Hivi sasa Serikali inatumia gharama kubwa sana katika kuanzisha mabwawa mapya kupitia maji ya mvua; lakini rasilimali hizi za asili nyingi zimeelekea kutoweka, kwa hiyo, nilidhani Serikali pia itakuwa na mkakati.
Mheshimiwa Spika, hivyo nina maswali madogo mawili, la kwanza, fedha zilizotajwa katika Bajeti ya Mwaka 2016/2017 hazikuweza kupatikana hadi sasa na hivi sasa tunaingia Bajeti ya Mwaka 2017/2018, lakini hali inayotishia ziwa hili inaonesha hivi punde litakauka; je, Serikali itatoa lini fedha milioni mia moja kupitia Mradi wa DADP’s ambayo imekusudiwa kwa nia njema katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amewajibu Watanzania pamoja na mimi na wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutuma timu ya wataalam kupitia maziwa yote ya asili katika nchi yetu ili iweze kutoa ushauri wa kitaalam na kuchukua hatua za kunusuru maziwa hayo kwa haraka na wataalam hao watakwenda lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba baada tu ya kupata swali lake hili nilifanya ziara katika Mkoa wa Manyara na kati ya maziwa ambayo nilikwenda kuyaona ni Ziwa Babati, tukiwa na Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini Mheshimiwa Pauline Gekul pamoja na Mheshimiwa Jitu Soni, na bahati mbaya siku ile Mheshimiwa alipata ajali, pole sana, lakini Mwenyezi Mungu alitusaidia.
Mheshimiwa Spika, basi niseme kifupi kwamba, bajeti haijakwisha, Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali la kwanza kwamba fedha hazijapatikana, milioni 100 lakini leo tuko Aprili na bajeti yetu inakwisha Juni. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba sisi tunafanya kila linalowezekana kama Serikali kuhakikisha fedha hizo zimefika ili zifanye kazi iliyokusudiwa; na zile nyingine zilizopangwa kwa ajili ya kazi nyingine inayofuata.
Mheshimiwa Spika, la pili, timu ya wataalam itakwenda lini; hili namhakikishia kwa sababu hili sasa nimeahidi kwa niaba ya Serikali, kwamba tutafanya tathmini katika maziwa yetu. Tunaelewa changamoto ambayo sasa vyanzo vya maji vimekabiliwa, mito mingi inakauka, maziwa yetu mengi yanakauka, mabwawa yetu mengi yanakauka.
Kwa hiyo, sisi kama wenye dhamana hii ya kusimamia mazingira, kwa dhati kabisa tumeamua na katika bajeti ya mwaka huu wa fedha inayokuja mtaona jinsi ambavyo tutaanza kushughulikia vyanzo vya maji, kurudisha uhai wa
vyanzo vya maji ili viweze kuleta tija.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuahidi kwamba niliyowaahidi kwenye maziwa ambayo nimeyataja kwanza wataalam watakwenda tena waliobobea kutoka kwenye sekta zote ambao wako competent na wataweza kutushauri kama Serikali ili tuweze kuja na mpango sasa madhubuti wa kuhakikisha kwamba maziwa yetu yanaendelea kubaki.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika nakushukuru, nina maswali madogo mawili ya nyongeza
kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ameliambia Bunge na kuwaambia Watanzania kwamba kuna kero 11 ambazo zimeshapatiwa ufumbuzi, naomba Mheshimiwa Waziri ututajie kero zote 11
ambazo tayari zimeshapatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, la pili; Mheshimiwa Waziri, Benki Kuu ni chombo cha Muungano na kilianzishwa mwaka 1966
baada ya kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki yaani East African Currency Board. Tangu kipindi hicho gawio la upande wa pili yaani ya Zanzibar imeonekana kwamba gawiwo (shares) hilo la upande wa pili hazitolewi kama ambavyo tulivyoweka shares zetu.
Mheshimiwa Spika, ni tatizo gani la msingi lililopelekea shares zetu za upande wa Zanzibar, kulingana na fedha ambazo tuliziweka, kwamba fedha hizi hazitolewi kama tulivyopangiwa au inavyotakikana kupatiwa sisi kutoka Zanzibar? Kama ni hivyo, sababu hizo ni kwa nini basi isionekane kwamba kuna haja ya haraka kuweza kupatiwa
ufumbuzi na fedha hizo kutolewa upande wa Zanzibar, naomba majibu ya haraka.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali ambalo limeulizwa na Mheshimiwa Mbunge la kwanza kama ulivyonielekeza ambapo ameomba kujua hizo
kero 11 ni zipi ambazo zimeshapatiwa ufumbuzi naomba kuzisema kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kero za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi ni:-
(1) Utekelezaji wa sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
(2) utekelezaji wa Merchant Shipping Act katika Jamhuri ya Muungano na uwezo wa Zanzibar kujiunga yaani
International Maritime Organization (IMO).
(3) Uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa bahari kuu.
(4) Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
(5) Uwezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukopa ndani na nje ya nchi.
(6) Wafanyabiashara wa Zanzibar kulalamika kutozwa kodi mara mbili.
(7) Mfuko wa maendeleo ya Jimbo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
(8) Ongezeko la gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO.
(9) Ushiriki wa Zanzibar na Taasisi za Kimataifa
(10) Ajira ya Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano.
(11) Utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia. Ahsante.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mheshimiwa Aweso.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mabadiliko ya tabianchi athari zake zimeonekana wazi wazi katika Mji wa Pangani. Serikali pamoja na jitihada kubwa wanazozifanya kukarabati ukuta wa Pangani, lakini bahari imekula kwa kiasi kikubwa kwa eneo la Pangadeco; je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya haraka kuhakikisha kwamba inaanza ujenzi wa ukuta kwa eneo la Pangadeco?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itafanya tathmini katika eneo lililobaki la Pangani ambalo kwa jina maarufu Pangadeco katika mwaka ujao wa fedha wa 2017/2018. Serikali itafanya tathmini ya eneo hilo na kutafuta namna bora tutakayoitumia, aidha kujenga ukuta au njia nyingine.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu yako mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kusema kwamba kuna sheria ya mita 60 kutofanya huduma yoyote kutoka kwenye chanzo cha maji, lakini bado vyanzo vya maji vinaendelea kuathirika katika maeneo ya wazi na mpaka ndani ya mbuga zetu ambayo ni maeneo yanayolindwa na kuhifadhiwa na Serikali.
Je, Serikali sasa ina mpango gani mahsusi wa kufanya utafiti wa miti ambayo inazalisha maji, iwe imepandwa kuzunguka vyanzo vya maji? Ni mkakati upi hasa mahsusi wa kudhibiti hivi vyanzo vya maji visiathirike? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mita 60 na vyanzo vya maji kuendelea kuharibiwa na utafiti ambao unafanyika, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulipokuwa tunaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Upandaji Miti wa mwaka 2016 hadi mwaka 2021, tulizingatia hayo na mpaka sasa hivi tumeshabaini aina ya miti inayofaa kupandwa katika vyanzo vya maji na utaratibu huu tutausambaza kwa wataalam wote. Kwa kushirikiana na TFS na wataalam wa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, tumeshaandaa tayari aina ya miti ambayo inafaa kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vyetu vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jithada unaziona, juzi hapa Mheshimiwa Makamu wa Rais amezindua mpango mkubwa wa kuokoa hali ya uharibifu wa mazingira ambayo inaendelea katika Mto Mkuu Ruaha. Katika kufanya hivyo, hatuishii hapo, tutaendelea kufanya tathmini katika vyanzo vyetu vya maji vyote ili tuje na solution ya uhakika na tuweze kutenga fedha zinazokidhi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mazingira haya tunayalinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile suala la mazingira ni gumu sana, ulinzi wake ni mgumu. Inatakiwa kila mwananchi, sisi wenyewe Wabunge tuhakikishe kwamba tunasaidia kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba mazingira yetu yanalindwa.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa uharibifu wa mazingira umekuwa ni tatizo sugu sana hususan katika Jimbo langu la Kilindi katika Kata za Negero, Mkindi, Kilindi Asilia pamoja na Msanja kutokana na shughuli za kibinadamu; je, Waziri yuko tayari kwa kushirikiana na Wataalamu wetu wa Chuo Kikuu cha SUA, kwa mfano, tuna Watalamu wazuri, akina Profesa Dhahabu na Mariondo kwa ajili ya kupeleka timu kule kuweza kufanya tathmini kubwa? (Makofi)
Swali la pili, suala hili la mazingira limekuwa ni sugu sana; je, Serikali iko tayari sasa kwa kushirikiana na Halmashauri kuhakikisha kwamba inapeleaka wataalamu wa kutosha wa mazingira kulinda maeneo yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshindwa kujizuia kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri, Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua. Nampongeza kwa swali lake zuri sana leo la mazingira hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yake ya nyongeza naomba niyajibu kama ifuatavyo:-
Moja, kwanza ofisi yangu inashirikiana vizuri sana na wataalam wa mambo ya mazingira hasa katika mambo ya hewa ya ukaa ambao wako pale SUA. Nimhakikishie kwamba ofisi yangu haina kipingamizi chochote cha kuja kufanya tathmini ya maeneo yaliyoathirika katika Kata alizozitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaunda hiyo timu, itakuja na hao wataalam na nimhakikishie kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais ina watalaam waliobobea katika mambo ya mazingira vizuri sana, kwa hiyo, hakuna kitu ambacho kitaharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwamba wasiwasi wake kuhusu wataalam wa mazingira ambao anahisi kwamba Halmashauri nyingi hazina wataalam na sekta nyingine, nimhakikishie tu kwamba hivi karibuni Waziri wangu anakamilisha orodha ya wataalam ambao tutawateua ambao ni Wakaguzi wa Mazingira (Environmental Inspectors) zaidi ya 400 hapa nchini na watasambazwa kwenye sekta mbalimbali. Hivyo basi, tatizo hili na kiu kubwa ya kuwahitaji wataalam hawa watakuwepo katika sekta kama Mheshimiwa Mbunge ambavyo ameomba.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Tatizo la Ranchi ya Mbarali linafanana kabisa na tatizo la Ranchi ya Mkata iliyoko Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro ambapo Ranchi ile hivi sasa imegeuka kuwa pori na Serikali imeshindwa kuiendeleza. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kubinafsisha Ranchi ile, mashamba yatolewe kwa wakulima na wafugaji ili kupunguza migogoro ya muda mrefu?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi na naomba nijibu swali la nyongeza ambalo ameuliza Mheshimiwa Devota Minja na kama ambavyo Naibu wangu amejibu vizuri sana maswali hapa Bungeni, tunataka Wabunge watuelewe. Kwanza Serikali haijashindwa kusimamia ranchi hizi, tunachokifanya kama Naibu Waziri alivyozungumza tunafanya tathmini sasa tupitie ranchi zetu zote tujue shughuli zinazofanyika.
Mheshimiwa Spika, tunajua upungufu uliopita kwamba zipo ekari sasa hivi, unakuta ekari moja imekodiwa mtu analipa Sh.500/= kwa mwaka. Kuna ekari zimekodiwa mtu analipa Sh.1,000/= kwa mwaka; kuna mahala ambapo uwekezaji hauendani na eneo lilivyo. Kwa hiyo tunafanya tathimini ili tuje na mpango mkubwa kwa sababu gani ranchi hizi shabaha ya kuanzishwa kwake haijaondoka toka tulivyoanzisha na ndio maana tunataka kupitia ranchi hizi tufanye mageuzi makubwa ya kuwa na viwanda vikubwa nchini kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wenye viwanda nchini wanapata mahali pa kutunzia mifugo yao kabla hawajachinja.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tunataka tuwa- transform wafugaji wetu, hatuwezi kuruhusu huu ufugaji wa mtu anafuga mifugo leo, anamchunga ng’ombe mpaka anakufa mwenyewe. Lazima tuwabadilishe wafugaji wetu tuwe na maeneo ambayo tutazalisha mitamba ya kutosha, tutazalisha ndama wa kutosha, tutazalisha mifugo ambayo inaweza ikagawiwa kwa wafugaji ili wafugaji wetu waweze kupata neema ya ufugaji huu.
Mheshimiwa Spika, kupitia ranchi hizi tunategemea kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi katika Taifa hili na kwa wafugaji Tanzania. Kwa hiyo, tuungeni mkono tutakapoleta mabadiliko yetu na Wabunge muache hili la kila mmoja kuhitaji ligawiwe kwa wananchi; tunataka ranchi hizi zitumike kwa faida ya Taifa na kwa mapana zaidi (Makofi).
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kamati ya Mheshimiwa Chenge iliyokuwa inapendekeza kodi mbalimbali mpya ilitoa mapendekezo ya kutumia uvuvi wa bahari kwa ajili ya kuongeza mapato na mara zote ni kwamba Serikali inasema boti za kisasa ambazo zinaweza zikadhibiti wavuvi wa kina kirefu hazipatikani.
Je, Serikali haioni kwamba kwa kutopatikana kwa boti hizo Serikali inakosa mapato makubwa sana kutokana na wavuvi haramu wa nchi mbalimbali duniani wanaokuja kuvua katika bahari yetu? Ni lini sasa boti hizo zitapatikana? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Selasini anaulizia juu ya uboreshaji wa sekta ya uvuvi na akihusisha na Kamati ya Chenge One ambapo mimi nilikuwa mjumbe wa Kamati hiyo tukiwa na Mheshimiwa Selasini. Nimwambie tu Mheshimiwa Selasini kwamba sasa kwa sababu mapendekezo yale tuliyapendekeza ili Waziri wa Uvuvi akayafanyie kazi na mimi ndiye Waziri wa Wizara hiyo sasa hivi aniachie ili tukamilishe mapendekezo hayo ambayo tulipendekeza kwa Waziri wa Uvuvi ambaye leo ni mimi. (Makofi)
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninaswali moja la nyongeza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba ina hakikisha wavuvi hawa wanapata sokola uhakika baada ya kuhamasisha uzalishaji kwa kuhakikisha kwamba kuna jengwa kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki katika ukanda wa Lake Tanganyika na hasa ukizingatia kwamba kuna specie ya kipekee katika Ziwa Tanganyika ya samaki anayeitwa migebuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali ina mkakati gani kuhakikisha viwanda vinajengwa katika ukanda ule? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI:Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa uvuvi katika Ziwa Victoria tumejenga mwalo wa kisasa pale Kibirizi ambapo mwalo ule tumeuwekea vifaa vyote muhimu ambavyo samaki akivuliwa anaweza kutunzwa hata kwa zaidi ya wiki mbili. Yote haya ni kuwafanya wavuvi wanapovua samaki kabla hawajafika sokoni wasiharibike yaani waweze kupata soko kabla hawajaharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais tumejenga pale mradi mkubwa sana wa ziadi ya takriban shilingi bilioni mbili zimetumika kwa ajili ya kutengeneza mwalo ule.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili la pili linalokuja ni la kujenga viwanda sasa kwa sababu tayari tumeshapata mwalo mzuri ambapo samaki wanapokelewa na kutunzwa. Kinachofuata sasa ni maandalizi ya kujenga kiwanda ili tuweze kuchakata samaki katika ukanda ule na tutafanya hivyo. (Makofi)
MHE. ZAINAB M. VULLU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya wavuvi wa Uvinza haina tofauti sana na hali ya wavuvi wa Ukanda wa Pwani ya Mkoa wa Pwani. Naomba nizungumzie hasa Kisiwa cha Mafia ambapo wanawake wengi wanajitahidi kulima kilimo cha mwani si kwa wao tu kwa mtazamo wa nje kwamba kinawapatia mapato lakini pia kilimo cha mwani kinasaidia kukuza samaki kuzaliana, kutunza mayai na hata kuhifadhi mazingira bora ya bahari. Kilimo hicho kinalimwa kwa shida sana,
Je, ni lini Serikali itahakikisha inawapatia nyenzo kama viatu, kamba na vifaa vingine vya kulimia mwani ili wananchi hao waweze kulima vizuri? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya vizuri sana Zanzibar katika kilimo cha mwani hasa kwa kuwatumia wataalam wetu hawa wa COSTECH pamoja na IMS. Tutapeleka wataalam wetu hawa katika eneo hili analolizungumza Mheshimiwa Mbunge ili waweze kwenda kuwafundisha wakulima wetu wanaolima zao la mwani ambalo tunalipendekeza sana sasa hivi kwa wakulima na kulipigania lifanyike kwa ajili ya kuongeza thamani za zao hilo na kujipatia kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo eneo hilo ambalo wakulima wanalima kwa shida tunatahakikisha kwamba tunaelekeza nguvu huko kuhakikisha wafugaji wale tunawapa mafunzo, tunawaonesha soko na vilevile tunawaunganisha kimtaji ili kuhakikisha kwamba zao hilo wanalilima vizuri zaidi kwa sababu lina soko la uhakika duniani. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kuwa uaharibifu wa mazingira ni janga kuu nchini.
• Je, Wizara inasema nini katika kutoa motisha kwa wale wenye maeneo yaliyotunzwa na kuhifadhiwa vizuri miti?
• Je, idara ya hali ya hewa imejipangaje katika kuhabarisha umma sambamba na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaenda kwa kasi hapa nchini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza anasema ni motisha gani ambayo inatolewa kwa watu ambao wanajitolea katika kupanda miti na kufanya shughuli za biashara hii ya miti kama Wizara na kama taasisi za Serikali. Motisha tunazotoa tunatoa katika taasisi mbalimbali kwa mfano Wakala wa Misitu. Wakala wa Misitu amekuwa akitoa motisha wa kusaidia vikundi vinavyozalisha miti na vinavyopanda miti katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyowahi kuzungumza hapa kwamba kwa sasa hivi tumefanikiwa Wakala wa Misitu sasa yuko kila wilaya na katika kazi moja ambayo tumewaekeza ya kufanya ni kuhakikisha kwamba wanapokuwepo pale wanatengeneza miche kati ya laki moja mpaka laki tano na wanagawia wananchi. Pili, wanasaidia vikundi vinavyozalisha miti na tatu wanawasaidia wananchi wanaotaka miti ya aina mbalimbali pamoja na kuwapa mafunzo au aina ya miti inayofaa kulingana na eneo fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhusu hali ya hewa sisi sote hapa ni mashahidi. Taasisi hii inayoshugulika na suala la utoaji wa hali ya hewa wamekuwa wakitujulisha kila wakati juu hali ya mvua kwa kila wakati na kila kipindi kwahiyo kati ya taasisi ambayo inafanya vuziri sana na mimi nachukua nafasi hii kuipongeza sana kwa sababu imekuwa ikitupa taarifa kila wakati, mwenendo wa wa mvua zilivyo, upungufu wa mvua ulivyo na jinsi ya wananchi wanavyotakiwa kuchukua hatua kulingana na hali inavyojitokeza. (Makofi)
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante leo ni karibu siku tatu BBC inatangaza kuhusu Ziwa Tanganyika kuathiriwa na kukata miti, na kutoweka samaki. Je, Serikali ina mpango gani kuzuia na kusaidia kuzungumza na nchi ya DRC Kongo, Burundi na Zambia ili kujenga kibanio katika mto Luguga ili maji yasiishe katika Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tutakachofanya tutafanya tadhimini ili tuone hasa ambacho kinasababisha upungufu wa samaki pamoja na uharibifu wa mazingira unaofanyaika katika Ziwa Tanganyika ili tuweze kujua hasa hatua stahiki tunazotakiwa kuchukua ili kuweza kurejesha hali hii, na katika kufanya hivyo ushauri alioutoa Mheshimiwa Keissy tutauzingatia baada ya kuwa tumefanya uhakiki na kubaini yawezekana zipo factors nyingine ambazo hazifahamiki kwa sasa. Kwa hiyo, zitafahamika tu pale ambapo tutafanya tadhimini na kujiridhisha.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru vyanzo vya maji vinaendelea kuathirika, na kupotea siku hadi siku nchini.
Je, Serikali imeanzisha vitalu vya miti inayotunza maji ili kuipanda na kuitunza kwenye vyanzo vya maji ili vyanzo vyetu vizidi kukua na kutoathirika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na Halmashauri pamoja na taasisi zingine kukosekana kwa wataalam wanaotuelekeza aina ya miti ya kupanda na wapi. Ndiyo tukasema TFS lazima iwepo kila sehemu, kwa sasa hivi huyu wakala wa misitu ndiye anayetoa ushauri wa miti aina gani inafaa kupandwa eneo gani, eneo la vyanzo vya maji linafaa kupandwa miti ya aina gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge huduma hizi zote mtazipata sasa kila Wilaya kwa kila Ofisi ya Wakala ya Misitu ambaye anatoa maelekezo haya.
Lakini Wakala hawa watai-guide vizuri sana halmashauri kuhakikisha kwamba inavipitia vile vyanzo vyote vya maji na kuenda kupanda miti inayofaa katika kulinda vyanzo vya maji.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kigamboni, Kata ya Kimbiji, tuna Kiwada cha Saruji cha Nyati. Nimesikia majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kuna Environmental Impact Assessment ambayo hufanyika lakini tuna changamoto kubwa sana ya vumbi linalotimka kutoka kiwandani katika kata ile. Bahati mbaya kabisa kile kiwanda kiko katikati ya makazi ya watu. Sasa hivi minazi yetu Kimbiji haizai, miembe haizai, michungwa haizai, mazao ya mahindi tukilima kuvuna tunashindwa kwenda kulima kwa sababu panakuwa na vumbi kali sana ndani ya mazao ambayo tunayalima.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba utusaidie kwenye hili, ni kweli Environmental Impact Assessment ilifanyika, na je ilitoa majibu sahihi? Mbona tunapata adha hii kubwa namna hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Nyati, nilipokea malalamiko ya kiwanda hiki na baada ya kuletwa, yalikuwa malalamiko mengi sana dhidi ya uchafuzi wa mazingira ya kiwanda hiki. Kwanza, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Environmental Impact Assessment ilifanyika katika kiwanda hicho na kiwanda kikajengwa, japokuwa katika utekelezaji wake zilijitokeza changamoto.
Mheshimiwa Spika, nilipokwenda kwenye ziara hiyo kulikuwa na changamoto ya hilo suala la vumbi, lakini suala la vumbi NEMC walikwenda kushughulika pamoja na kiwanda na kuhakikisha kwamba changamoto hiyo imetatuliwa. Kulikuwa na changamoto ya kulipa fidia wananchi waliokuwa wanaishi karibu sana na kiwanda, wananchi hao wote wamekwisha kulipwa fidia mpaka sasa hivi tunavyozungumza.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na tatizo la yale makaa ya mawe kwamba yalikuwa yako nje na yalikuwa mvua zikinyesha yanatiririka mpaka kwenye vyanzo vya maji na kuchafua vyanzo hivyo. Tatizo hilo lilishughulikiwa na sasa makaa hayo hayaendi tena kwenye vyanzo vya maji. Kama bado kuna tatizo hilo analolizungumza sasa hivi Mheshimiwa Mbunge, tutakwenda kujiridhisha kuona kama kiwanda hicho bado kina tatizo hilo na kuchukua hatua stahiki.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri machachari na kijana, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mifugo kuongezeka kwa wingi Ulanga limeanza tangu miaka ya 90 na tumepiga kelele lakini Serikali kwenye ujenzi wa majosho wako nyuma lakini kwenye kupiga chapa kwa sababu inawaingizia mapato wamekuwa wako mbele. Naomba commitment ya Serikali iseme kuwa mwaka huu 2018/2019 tutajenga majosho. Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwa kuwa kumekuwa na tatizo la masoko ya mifugo, masoko yaliyoko ni minada ya kienyeji ambapo wafugaji wanauza mifugo kwa bei nafuu. Je, lini Serikali itaweka utaratibu maalum wa masoko ili wafugaji wauze mifugo yao kwa bei ya faida? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga kwamba tutajenga josho katika jimbo lake mwaka huu ujao wa fedha pamoja na kisima, siyo josho tu ni pamoja na kisima cha kunyweshea mifugo maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunajua kuna tatizo la uanzishaji wa masoko ambapo watu wengine wanaanzisha masoko bila utaratibu na wengine wanakosa mwongozo. Kwa hiyo, hili tunalisimamia vizuri na katika mwaka huu wa fedha tutayamaliza yote haya. Tutahakikisha kwamba miongozo ipo ya kutosha kuhakikisha kwamba masoko mahali popote yanapoanzishwa yanazingatia miundombinu mahsusi inayotakiwa na eneo mahali linapohitajika.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Ulanga na Malinyi ni walewale. Suala hili la miundombinu la mifugo tumelipigia kelele muda mrefu na tumeielekeza na kuishauri Serikali watumie Mfuko wa Maendeleo ya Mifugo (Livestock Development Fund) ambayo inakusanywa kutokana na minada waweke percentage ili kuwa na uhakika wa kuhudumia miundombinu hiyo pamoja na malambo na majosho. Ni lini Serikali watatekeleza maagizo haya ambayo mara nyingi tumetoa hapa Bungeni?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni muda mfupi sana sasa hivi Waziri wa Mifugo na Mvuvi atawasilisha hotuba yake, masuala yote yamesheheni humo ataona mipango yetu madhubuti kabisa ambapo sasa mifugo nchi hii haiwezi kufa tena kwa kukosa malisho na maji. (Makofi)
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi. Kilwa ni miongoni mwa eneo ambalo mifugo inakuja kwa wingi na Serikali haijaandaa kabisa miundombinu. Serikali ina mpango gani kutujengea malambo Kilwa ile mifugo iliyopo pale iweze kupata afya inayostahili? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaanza na kisima kimoja mwaka huu ujao wa fedha kwa Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri anafanya kazi vizuri, lakini nimfahamishe Mheshimiwa Waziri eneo hili la uvuvi na ununuaji wa meli za uvuvi na ujengaji wa Bandari ya uvuvi ni suala very important lazima tulifanyie kazi kwa kina. Sasa swali la kwanza, Shirika la TAFICO ni lini litakamilika ili hizi meli ziweze kununuliwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kila siku tunasema tuna wataalam ambao wanafanya upembuzi yakinifu, lakini nimwambie Mheshimiwa Waziri hebu atueleze ni lini hawa wataalam watakamilisha huu upembuzi wao yakinifu ili hii bandari ya uvuvi iweze kujengwa kwa maslahi ya Watanzania. Ahsante.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza hapa kwamba tumeshampata mshauri elekezi na tayari ataingia mkataba mwezi huu huu na kulipwa malipo ya awali na atafanya kazi ndani ya miezi nane. Baada ya miezi nane tayari tutakuwa tumeingia hatua sasa ya ujenzi wenyewe. Kwa hiyo, atuvumile katika hiyo hatua, Mshauri Elekezi ameshapatikana na tayari zoezi litaanza. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Kwa mujibu wa Kanuni za Uvuvi, ukienda kifungu cha 45(3)(b), naomba nisome, kinasema:-
“No person shall: (b) fish, land or possess, process or trade in Nile tilapia or fish locally known as “Sato” the total length of which is below 25 centimetres.”
Mheshimiwa Spika, ukisoma Kanuni hii, ni kama inafikiria source ya Sato ni moja tu, Nile Tilapia lakini sasa Tanzania tuna-encourage watu kufanya aquaculture, maana yake sources za sato ziko nyingi, lakini tuna maziwa na mito na Kanuni hii imetumika kusababisha usumbufu mkubwa sana kwa watumiaji wa sato nchi nzima. Ni lini Serikali au ni kwa nini Serikali isisitishe sasa kukamata watu kwa kutumia Kanuni hii ambayo yenyewe tu inajichanganya na ina makosa mpaka itakapofanyiwa marekebisho? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nishukuru sana kwa swali hili la nyongeza la Mheshimiwa Kanyasu, lakini nimpongeze sana Naibu wangu kwa majibu mazuri sana aliyoyatoa hapo awali.
Mheshimiwa Spika, kama alivyoisoma Kanuni yetu na kama Naibu Waziri alivyoeleza, mwezi huu wa Saba, Wizara yangu itakuwa imemaliza zoezi la kufanya mapitio ya Kanuni ya Uvuvi pamoja na Sheria yenyewe ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003. Vilevile kwa nyongeza ni kwamba operesheni hizi zinazoendelea na wananchi wetu ambao wanajishirikisha na ufugaji wa samaki, kila wanapofikia kuvuna samaki wao wanawasiliana na ofisi yangu ambayo inakuwa inazo taarifa za uhakika juu ya uvunaji wa samaki hao ili kusije kukatokea usumbufu wa aina yoyote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kipindi ambacho Kanuni inarekebishwa, utaratibu umewekwa na Wizara kwa maana ya kwamba mawasiliano yako proper ya namna ya uvunaji kwa sasa wakati tunatengeneza Kanuni ambayo itakuwa ime-favour uvunaji wa samaki katika Ziwa Viktoria lakini wakati huohuo na wale wafugaji wetu wa samaki ambao wanafuga samaki kwenye maji.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Zoezi la uvuvi haramu limetekelezwa sivyo ndivyo katika maeneo mengi sana na wavuvi wengi sana wamepata hasara kubwa sana kutokana na zoezi hili. Zoezi hili limefanywa na wafanyakazi ambao kwa kweli hawakuzingatia maadili na hata kanuni za kazi zao. Ilifikia mahali Mheshimiwa Waziri akasema kwamba yeye hana wapiga kura wavuvi hao wenye wapiga kura wavuvi mtajijua wenyewe. Nataka kujua kauli ya Serikali, wavuvi ambao wameingizwa hasara kubwa sana watalipwa fidia kiasi gani na lini fidia hiyo italipwa?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, suala la uvuvi haramu tumeeleza mara kwa mara hapa Bungeni na jinsi ambavyo linaendeshwa. Waheshimiwa Wabunge tumewaomba mara kwa mara kwamba kama kuna mtu ambaye ameonewa katika eneo lolote lile tuletewe ili sisi tuweze kuchukua hatua. Leo ni miezi sita Wizara yangu inasisitiza suala la watu walioonewa kuwasilisha malalamiko yao ili waliohusika waweze kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo Wizara yangu haiwezi kujua ni kitongoji, kijiji na kata gani, ni lini, Mkaguzi nani na alifanya makosa yapi kwa sababu hatua za ukamataji zipo. Sasa ikiendelea kuzungumzwa hivi kila siku kwamba watu wameonewa, halafu ushahidi hupewi, Waziri huwezi kuwa kwenye nafasi ya kuchukua hatua.
Mheshimiwa Spika, hili Bunge ndiyo linalotunga sheria, kwa nini Waziri alaumiwe na kuandamwa kwa kuchukua hatua za watu ambao wamevunja sheria? Nataka niseme kwamba wananchi na watu wote wataendelea kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria tulizonazo leo na kwa mujibu wa Katiba tuliyonayo sasa, watakaguliwa mahali popote na wakibainika watachukuliwa hatua. Watu wote wanaojihusisha na uvuvi haramu bila kujali vyeo vyao, wataendelea kuchukuliwa hatua mahali popote walipo kwa mujibu wa sheria tulizonazo.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inasisitiza kama kuna mtu yeyote ambaye ana ushahidi dhidi ya manyanyaso au uonevu wa aina yoyote umefanywa na Afisa wangu siku hiyo hiyo hatua zitachukuliwa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimwia Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri. Kwa sababu makatazo yaliyokuwa yamefanyika Ziwa Tanzanyika yamemefanyika pia Ziwa Victoria hasa kwa kuzuia matumizi ya taa za solar kwenye shughuli ya uvuvi wa dagaa. Kwa sababu juzi Mheshimiwa Waziri niliona anatoa tamko kule Ferry, ni nini sasa kauli thabiti kwa wavuvi wa Ziwa Victoria ili waendee kutumia taa za solar mpaka pale utaratibu utakapo kamili?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimwa Mabula kwa swali lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba baada ya kutafakari sana malalamiko ya wavuvi wetu katika maziwa mbalimbali juu ya leseni nyingi, matumizi ya jenereta pamoja na matumizi ya taa za solar; na kwa mamlaka niliyonayo nikaamua kwamba sasa matumizi ya solar na jenereta yaruhusiwe na wananchi wasikamatwe kwa kutokuwa na leseni hivi sasa wakati tunatatua tatizo hili la kuwa na leseni nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachotaka kuwambia wavuvi wote na Mheshimiwa Mbunge ni kwamba nimeruhusu rasmi matumizi ya taa za solar na jenereta mpaka tarehe 1 Julai. Hata hivyo Serikali haikusudii kuzuia wananchi kutumia solar isipokuwa ni kuwa-guide kwamba ni solar zenye watts kiasi gani ambazo zitahitajika kutumika, hapo ndio tutatoa hizo guidelines tarehe 1 Julai.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, nimeletewa ujumbe hapa. Siyo utaratibu, utusaidie kuzungumza lile katazo lako, wale waliokuwa wamenyang’anywa majenereta na taa zao za solar watarejeshewa ama utaratibu utakuwaje?

Majibu Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwamba nimeruhusu matumizi hayo ya generator, taa za solar na wananchi wote ambao wameshikiwa zana hizo, warudishiwe bila masharti yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nilikuwa nataka kusisitiza katika hili jambo la kwamba suala la ulinzi wa rasilimali zetu hizi ni suala ambalo linahitaji kuungwa mkono na wananchi wote. Rasilimali hizi tulizonazo hapa nchini asilimia 37 ni maji, lakini mazao yetu ya uvuvi mengi yameharibiwa sana na suala la uvuvi haramu. Kwa hiyo, wananchi wote wanawajibika kuziangalia hizi sheria na kuziheshimu. Kwa sababu hata huyo Mama Ntilie anajua samaki wasioruhusiwa. Tukitengeneza mtandao huu wa huyu mama mdogo anaweza kuingia kwenye soko na samaki wasioruhusiwa, tutatengeneza mtandao ambao utawezesha kuwepo kwa soko hili.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, nawaomba sana, katika kipindi hiki kigumu cha
kubadilisha watu kuwaondoa kwenye uvuvi haramu, mtuvumilie. Kwa sababu hata huyo mama mjane tunayemhurumia leo, kesho hatapata samaki wa kuuza. Hata mama mjane, mtoto yatima, watoto hawaendi shule; hawataenda shule kabisa kwa sababu samaki hawatakuwepo majini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika kipindi hiki ambacho tunafanya transformation hizi kubwa, nakuomba sana na bunge lako Tukufu mtuvumilie kwa nia nje kwa sababu hatua hizi zote tunazochukua ni kwa ajili ya
Taifa letu na hatima ya uchumi wa nchi hii.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa. Kufuatia operesheni ya kijeshi iliyoendelea pale Mafia na kupelekea madhila na hasara kubwa sana kwa wavuvi ambao walinyang’anywa zana zao halali za kuvulia, wengine mashine zao za boti zimezuiwa; wengine compressors zao, wangine magenereta yao yamezuiwa na hifadhi ya bahari. Mheshimiwa Waziri alitoa taarifa hapa kwamba vitu vyote hivi viachiwe. Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana atakuwa tayari kufuatana nami twende Mafia, Jibondo, Tumbuju na Kilimnoni akaonane na wavuvi ili awaelezee kiuhalisia zoezi hili lilivyokwenda?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Dau, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari kwenda na nimeshamkubalia Mheshimiwa Mbunge, tukimaliza tu Bunge hapa kuanzia Jumapili, nitakuwa ukanda huo kutembelea maeneo hayo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kukiweka sawa ni kwamba saa nyingine tunapozungumzia wananchi wetu, wanaweza kuwa wako sahihi kulingana na malalamiko yao, lakini wanaweza kuwa wahalifu. Sasa ni vizuri pia tukawa makini na hilo kwa sababu kama ni wahalifu halafu wanazungmziwa kupata unafuu hapa Bungeni, nadhani itakuwa ni utaratibu ambao haukubaliliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka niseme, mimi niko tayari. Waheshimiwa Wabunge, hakuna hata sababu kwa mfano mhalifu mmoja wa kumzungumzia hapa Bungeni. Sisi tuko hapa kama ofisi, kama kuna mtu yoyote ameonewa mahali popote, lete tushughulikie, hakuna hata sababu ya kuhangaika kuuliza swali hapa. Kwa sababu wengine ni wahalifu. Sasa Bunge likigeuka kuwa linazungumzia wahalifu kila siku, litakuwa linapoteza muda wake mwingi. Saa nyingine wengine wanataka huruma ya Mheshimiwa Waziri, sasa huwezi kuipata huruma kwa kuvunja sheria halafu unataka utetewe na Bunge.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kumekuwepo na operesheni inayofanywa na Wizara ya Mifugo katika mipaka yetu ya Tanzania hasa eneo la Namanga na ambapo wafugaji wetu wamekuwa wakipata matatizo makubwa ya kunyang’anywa mifugo na wakati huo huo sheria hairuhusu mifugo kutaifishwa lakini ipigwe faini; na operesheni hii haishirikishi wananchi wanaohusika wala viongozi wa maeneo husika na imesababisha madhara makubwa sana kwa wafuaji wetu. Nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba wafugaji wanaoenda kutafuta masoko nje ya nchi kwa sababu hakuna viwanda huku ndani, hawapati madhara na madhila wanayopata katika mipaka yetu ya Tanzania, hasa Namanga?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Laizer, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wetu wanapofanya shughuli zao za biashara wanashauriwa kuzingatia sheria za nchi zilizowekwa ili wasiweze kupata usumbufu wowote ambao unaweza kujitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Mbunge anazungumzia kama mifugo imekamatwa halafu ikakosa mwenyewe, sheria inawaelekeza wale waliokamata mifugo kuitafisha na baadaye kuipiga mnada hadi pale yule mwenyewe atakapokuwa amepatikana. Nimhakikishie kwamba operesheni hizi haziendi hivyo. Kwa hiyo, wananchi wanachotakiwa ni kutoa ushirikiano tu wa kuhakikisha kwamba wanafuata sheria na taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado sasa hivi soko la nje ni kubwa kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge mwenyewe kwamba tuna tatizo la viwanda hapa nchini, lakini Waheshimiwa Wabunge kwa sababu baadaye taarifa ya Kamati itawasilishwa, niwahakikishie kwamba mipango tuliyoipanga ni mizuri, viwanda vyetu vingi vitakamilika hivi karibuni na suala la wananchi wetu kuhangaika kutafuta masoko nje litakuwa limekoma kwa sababu karibia kila kona tutakuwa na viwanda vikubwa vyenye uwezo wa kuzalisha na tutakuwa na uwezo mkubwa wa kuuza mpaka nje ya nchi.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilikuwa nataka nipate ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. Wanatumia kigezo gani katika kupanga ushuru wa dagaa hasa dagaa zinazotokea bahari ya Hindi? Wafanyabiashara walikuwa wanalipwa kwa gunia la kilo 100 shilingi 10,000/=, lakini sasa hivi kilo moja wanalipisha dola moja. Kwa hiyo, gunia hilo sasa hivi limefika mpaka shilingi 250,000/=. Wafanyabiashara wameshindwa kufanya biashara hiyo. Serikali inasema nini kuhusiana na jambo hilo kwa sababu linaathiri biashara katika mpaka wa Tunduma? Ahsante.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Mwakajoka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake. Vigezo vya kupanga ushuru wa dagaa au wa bidhaa au wa mazao yoyote ya uvuvi, hutegemeana na thamani ya zao lenyewe linalohusika. Kwa hiyo, hiyo ndiyo hasa zana yake, thamani yake ili Taifa liweze kunufaika na mazao yake hasa yanapotokea kuuzwa nje. Kwa hiyo, kama kuna shida yoyote ambayo katika kubadilisha tozo aidha, zimeweza kuleta mkwamo mkubwa wa biashara, sisi tutatathmini, tutaangalia. Mheshimiwa Mbunge, kama hilo limeleta shida, tutaangalia kwa sababu sasa hivi tunaingilia tunaanza kuzitazama tozo zetu upya kama unavyojua tunaingia kwenye bajeti, kama kuna mahali itaonekena tozo hizi zimewekwa kubwa sana kuliko biashara ilivyo, tutazipunguza na hilo halina matatizo yoyote.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nina swalo dogo la nyongeza, Jimbo la Mchinga, Jimbo la Mtama, eneo la Sudi, Jimbo la Lindi Mjini, hupitiwa na Bahari ya Hindi na vijana hutegemea uvuvi ili kujiongezea uchumi wao na vitendea kazi kwa kweli ni duni sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia vijana hawa boti ili waweze kuinua uchumi wao? Ahsante.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Salma Kikwete ameiandikia Wizara kuiomba kusaidia vijana hawa, lakini na hapa Bungeni amesimama kuuliza swali la nyongeza. Nilienda kwenye maeneo hayo kwa vijana hao ambao wanafanya shughuli zao vizuri sana za uvuvi. Ninachotaka kusema kwa ufupi tu, najua mahitaji ya boti ni makubwa, lakini kwa kuanzia tutampa boti moja kwa ajili ya vijana hao.
MHE.DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwakunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Wavuvi katika Ziwa Victoria, moja ya mambo yanayowakwaza sana ni masoko ya uhakika ya mazao ya samaki. Sasa katika Jimbo la Buchosa tulikuwa na soko mojaambalo lilihudumia karibu wavuviwote wa Jimbo hilo na Wizara ililifunga kwa maelezo kwamba halikuwa linasimamiwa vizuri, lakini tuna uhakika, suala la usimamizi wa soko hilo ni jukumu la Serikali na kwa hiyo, ilipaswa yenyewe ndiyo iweke usimamizi mzuri ili wananchi waweze kuuza mazao yao. Sasa swali langu, ni lini tu Waziri atakwenda kufungua soko hili ili wananchi wasiendelee kuhangaika? Ahsantesana.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nitakwenda mwezi huu, soko hilo tutalifungua.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Makete tumekwenda pale na Waziri kutembelea kile kituo tukaona kwamba idadi ya ng‟ombe wanaotakiwa kuwepo pale ni 4,000 lakini sasa hivi wako ng‟ombe 750 tu. Ni Lini Serikali itapeleka ng‟ombe wa kuzaliana Kitulo? Ahsante.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru sana kwa majibu yaliyokuwa yakiendelea Mheshimiwa Naibu Waziri na swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na Kituo cha Kitulo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namuunga mkono kabisa kwamba Kituo chetu cha Kitulo ndiyo Kituo pekee cha uzalishaji wa Ng‟ombe wa maziwa bora hapa nchini kwetu, na ni kweli kabisa kwamba idadi ya Mifugo imepungua kwenye lile shamba letu; na kama yeye mwenyewe alivyosema hivi karibuni nilikuwa kwenye ziara katika eneo hilo.

Nataka tu nimhakikishie kwamba tunakamilisha mipango ya kuhakikisha kwamba shamba letu hilo tunaliboresha upya kuanzia uoteshaji wa nyasi katika shamba lenyewe pamoja na miundombinu mingine iliyochakaa. Vilevile kuhakikisha kwamba ng‟ombe wanarejeshwa mle, kwa maana ya kuongeza idadi ya ng‟ombe, ili iendane na ukubwa wa eneo na mahitaji ya wananchi ambao kwa sasa wanahitaji mitamba mingi sana kila sehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tukuhakikishie kwamba ujio wangu ule ndiyo ilikuwa mipango ya kuanza kununua ng‟ombe wengine na kujaza kwenye hilo shamba lakini na kuhakikisha kwamba mahitaji ya wananchi wa Tanzania wanaohitaji mitamba bora kutoka Kitulo wanaipata mitamba hiyo.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini niwashukuru pia kwamba sasa wataanza kuchimba kisima kirefu kwa ajili ya wafugaji wa Ruvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi hii ya Serikali ni ya mwaka 2012/2013 na mwaka 2015 wataalamu walikuja Kata ya Ruvu na kubainisha maeneo ya majosho na malambo pamoja na visima virefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa imeshakuwa ni muda mrefu na wafugaji wale wa Kata ya Ruvu wanahangaika sana kuhamisha mifugo huku na kule. Je, Serikali haioni kwamba kwa sasa na hasa kwenye bajeti hii inayokuja ya mwaka 2020/2021 wakatenga fedha za kutosha ili waweze kukamilisha ahadi yao ambayo ilishakubalika mwaka 2012/2013 ili wananchi hao wa Ruvu waweze kupata hii huduma ya malambo na majosho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutembelea Wilaya ya Same na kuona maeneo ambayo yanahitaji miundombinu ya mifugo kusudi wafugaji wale waweze kupata miundombinu hiyo na mifugo iweze kupata huduma hiyo kama inavyotakiwa?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa David Mathayo ambaye ni Waziri Mstaafu wa Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi, na kwamba nijibu maswali yake mawili kama alivyouliza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niko tayari kufanya ziara jimboni kwake mara tu baada ya Bunge hili kumalizika na kwenda kukutana na wafugaji wa maeneo hayo na kukagua miundombinu yao na kutafuta namna ya kuiboresha ili waweze kupata sehemu nzuri ya kunyweshea mifugo yao lakini pamoja na kuogeshea mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nakubaliana na yeye kwamba katika bajeti hii inayoanza tutaingiza mradi wa lambo katika jimbo lake; ambao umekuwa wa muda mrefu sana kama alivyoeleza mwenyewe, tangu yeye mwenyewe akiwa Waziri na mpaka leo hii ahadi hiyo haijatekelezwa. Sasa safari hii tutaitekeleza kwa kuweka bajeti kwenye mpango wetu wa Serikali ambao tutauanza hivi karibuni.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Matatizo ya wavuvi wa Ukerewe yanafanana sana na matatizo ya wavuvi wa Kisiwa cha Mafia. Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana mezani kwake kuna barua kutoka kwangu na kwa wavuvi wangu tukiomba ruzuku ya msaada wa zile mashine.

Je, ni lini majibu yake yatatoka?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake hili la nyongeza akiulizia suala la zile mashine za ruzuku, tukitoka hapa Bungeni aje pale ofisini kwa ajili ya utaratibu wa kupata zile mashine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala hili la vijana na wavuvi wetu kuhakikisha wanaheshimika katika mabenki na mahali popote pale, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa Uvuvi Database ambapo ndiyo kilikuwa kipengele kikubwa sana kilichokuwa kinawafanya wavuvi wetu wasiaminike kwenye mabenki kwa sababu ya shughuli zao za kuhamahama na kila mtu mwenye benki anakuwa na mashaka juu ya fedha zake atakapozipeleka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipoanzisha Uvuvi Database sasa hivi benki yotote ile ikitaka kumkopesha mvuvi ambaye yupo Buchosa, Ukerewe, Mafia na maeneo mengine watamuona mpaka na kazi zake anazozifanya. Hii inaenda kuongeza imani kubwa kwa wavuvi wa nchi yetu na ile dharau iliyozoeleka ya kwamba wavuvi hawakopesheki sasa itakuwa mwisho. (Makofi)