Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni (55 total)

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, utalii ili uweze kuendelea vizuri na uweze kuboresha Pato la Taifa ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi wanaoishi kando kando ya Hifadhi hizi za Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mgogoro sasa hivi wa wafugaji zaidi ya ng‟ombe 5000 kwa vijiji vya Kijereshi na Nyamikoma katika Jimbo la Busega ambao wamekamatwa kwa sababu ya askari wa Game Reserves kuwasukumizia kwenye hifadhi ili waweze kutoza fedha hawa wafugaji. Hii mifugo ina zaidi ya siku tatu imefungiwa kwenye pori. Hivi kweli kama tunataka ushirikishaji mzuri na uhifadhi wa maliasili zetu.
Je, Serikali inachukua hatua gani sasa kuruhusu hiyo mifugo, kwa sababu ng‟ombe hawana tatizo, ili waweze kuachiwa…

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba ninaomba tamko la Waziri wa Maliasili kuhusiana na mifugo hii ambayo imeingizwa kwenye hifadhi kinyume cha utaratibu na kwa nini imeendelea kufungiwa kule isiachiwe? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa…

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Nakushukuru kwa kunipa nafasi kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wanavijiji wanaopakana na Mbuga ya Serengeti katika eneo la Busega na vijiji hivyo ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja, wameingiza ng‟ombe zaidi ya 6000 katika eneo lao na ng‟ombe hao wamekamatwa na Askari. Jana usiku nimetoa maagizo kwamba ng‟ombe hao waachiwe na wanavijiji wachukue ng‟ombe zao bila kuchelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kusisitiza kwa wafanyakazi wa mbuga ya Serengeti kuwaachia ng‟ombe hao mara moja. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, tunatambua kwamba Serikali ina mzigo mkubwa sana kuhusiana na masuala ya madai ya walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuuliza kwamba kuna zaidi ya 3,000 ambao wamestaafu mwaka 2014 na mwaka 2015, mpaka sasa hivi hawajalipwa mafao yao. Je, ni lini Serikali angalau mafao ya watu ambao wameshastaafu tayari wanahitaji walipwe warudi majumbani kwao watalipwa pesa hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna Walimu wamestaafu, nami naomba nikiri kwamba hata katika Ofisi yangu kuna baadhi ya walimu walifika pale moja kwa moja kuleta madai yao. Kwa mfano, kuna mwalimu mmoja alikuwa akifundisha pale Bahi. Walimu wengi waliokuwa na changamoto, walikuwa katika Mfuko wa PSPF.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali imetoa maelekezo katika Mfuko wa PSPF kwamba haraka iwezekanavyo walimu wote waliokuwa wanadai, wahakikishe stahili zao zimelipwa, kwa sababu Serikali imefanya mchakato mkubwa sana kuiwezesha PSPF katika madeni iliyokuwa inadai kwamba iweze kupata mafungu ya kutosha ilimradi PSPF iendelee kulipa madeni na Serikali imetimiza hilo.
Sasa naomba nitoe agizo kwamba Mamlaka zinazohusika katika hii mifuko zihakikishe kwamba Walimu wote ambao waliokuwa wanadai waweze kupata stahili yao. Siyo jambo jema kutokuwalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano, mwalimu mmoja kutoka pale Morogoro alizimia kabisa kwa kudondoka kwasababu hakupata mafao yake. Ndiyo maana tumetoa maelekezo mazito na ni imani yangu kwamba Mfuko wa PSPF kwa sababu umeshaanza kupata mafungu yale yaliyokuwa yanadai Serikalini, iwalipe walimu wetu ilimradi waendelee kuishi maisha mazuri.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza, napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake na kama alivyosema kwamba nafuatilia, ni kweli nimefuatilia hii fedha imeshafika huko Busega na imeshafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri kasema kwamba, makusanyo yanazidi kuimarika na kwa kuwa, Busega ni moja ya Wilaya ambazo ni mpya na miundombinu bado ina matatizo hususan barabara. Barabara ya Mwamanyiri kwenda Badugu, Barabara ya Kisamba – Nyaruhande – Nyangiri na Barabara ya Mkula – Kijereshi – Lamadi. Je, kwa kuwa, makusanyo yanaimarika; Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa barabara hizi sasa zinaboreshwa ili ziende sambamba na bajeti jinsi inavyoimarika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, Mikoa Mipya ikiwemo Simiyu, Katavi, Geita, Njombe na Mkoa mpya wa Songwe, ina matatizo sana ya miundombinu na kwa kuwa, bajeti ambazo zimekuwa zikitengwa za Mikoa mama ni kubwa kuliko bajeti za mikoa mipya. Je, Serikali haioni kuna haja sasa kwa mikoa mipya hii na wilaya nyingine mpya zipewe kipaumbele cha kibajeti ili zipate mafungu ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri kwamba, hivi sasa kwa dhamira tuliyonayo kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano, nafurahi sana kufanya kazi katika Wizara hii. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, lazima tuimarishe barabara zote, hizi ambazo amezisema Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni na nyingine zote za wilaya zote na halmashauri zote Tanzania nzima. Tuna dhamira hiyo na naamini tutafikia malengo haya kwa namna tulivyodhamiria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la Mikoa mipya, naomba nichukue nafasi hii kuielekeza Bodi ya Barabara Nchini pamoja na TANROAD kuangalia kwa makini sana wanavyoweka migawo ya fedha za matengenezo. Wazingatie mahitaji mahsusi yaliyoko katika mikoa hii ambayo Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni, Mbunge wa Busega, ameitaja pamoja na mikoa mingine ambayo nayo ina mazingira mahsusi kwa maana ya mazingira magumu ya usafiri.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, katika ziara yake Mkoani Simiyu Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo, kuna mgogoro mkubwa wa hifadhi na wananchi wa Wilaya za Busega, Wilaya ya Bariadi, Wilaya ya Itilima na Wilaya ya Meatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Waziri Mkuu alitoa maelekezo na maagizo kwamba, Mawaziri wanne wakutane mara moja, leo ni miezi mitatu imepita hakuna kinachoendelea.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri lini sasa mtatii agizo la Waziri Mkuu la kukutana na kutatua migogoro hii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali kupitia Waziri Mkuu akiwa Mkoani Simiyu alitoa maelekezo. Maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa Simiyu yamekwishaanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tunayo taarifa iliyoandaliwa ya undani wa orodha ya migogoro yote inayohusika katika vijitabu ambavyo tayari vimeshagawiwa kwa Waheshimiwa Wabunge wote, nia ya Serikali imekwishaelezwa mara kadhaa hapa kwamba umefika wakati sasa baada ya kukusanya taarifa za awali tunakwenda kukusanya Wizara zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mmoja anafahamu, Waheshimiwa Wabunge wanafahamu na wananchi wote kwa ujumla wanafahamu kwamba sasa tuna vikao muhimu vya bajeti ambavyo vinakamilika mwisho wa mwezi wa sita, mara tu baada vikao vya bajeti tunakwenda kutekeleza ahadi hiyo ya Serikali ya kwenda kupitia upya migogoro yote hiyo kwa kushirikisha Wizara zote zinazohusika, lakini baada ya kukamilisha jukumu hili lililoko mbele yetu la Bajeti ya Taifa.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na kazi nzuri aliyofanya katika Jimbo la Rorya, naomba tu nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ahadi ya Serikali kupitia REA III itakamilisha mradi kabambe wa kuweka umeme katika Jimbo la Rorya kuanzia tarehe 1 Julai, 2016. Je, Waziri anawahakikishiaje wananchi wa Rorya kwamba katika REA III, vijiji vyote vilivyobakia kupata umeme vitapata umeme huo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa vile Mpango wa REA III uko mpaka Jimbo la Busega na kuna Kituo cha Afya cha Lukungu pale Lamadi hakina umeme na kimeshapatiwa tayari vifaa kutoka Shirika la AMREF. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kunihakikishia kwamba kupitia REA III Kituo hiki cha Afya cha Lukungu na chenyewe kitapata umeme huo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chegeni aliyeuliza kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa REA II tunatarajia itakamilisha kazi zake mwisho wa Juni, 2016. Nichukue nafasi hii, siyo kwa Jimbo la Rorya tu lakini na kwa Wabunge wengine, nimhakikishie Mbunge wa Rorya kwamba vijiji vyote ambavyo vilikuwa katika REA Awamu ya II ambavyo havitakamilishwa, pamoja na kwamba tunataka vikamilishwe, vitaingizwa katika REA Awamu ya III. Ni mpago wa Serikali kwamba vijiji vyote hapa nchini ambavyo havijapata umeme katika REA Awamu ya II vitapatiwa umeme katika REA Awamu ya III inayoanza Julai, 2016. Nirekebishe kidogo swali la Mheshimiwa, amesema tarehe 1 Julai siyo kukamilisha, tarehe 1 Julai sasa ndiyo tunaanza REA Awamu ya III itakayoendelea kwa miaka mitatu, minne hadi mitano, ile Awamu ya II ndiyo itakamilika Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na Jimbo la Busega kupatiwa umeme wa uhakika REA Awamu ya III, ni kweli viko vijiji vya Mheshimiwa Mbunge wa Busega, Mheshimiwa Dkt. Chegeni ambavyo vilikuwa viunganishwe umeme kwenye REA Awamu ya II lakini havijapata umeme ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Lukungu katika Mji wa Lamadi. Tunatambua eneo la Lamadi ni eneo la kibiashara kwenye Jimbo la Mheshimiwa wa Busega, eneo hilo litapatiwa umeme pamoja na vituo vingine na Kituo cha Afya cha Lukungu kitapatiwa umeme kwenye REA Awamu ya III.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimwia Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kwanza nimpongeze amekuwa anatoa majibu marefu na mazuri.
Kwa kuwa viwanda vya pamba au vinu vya pamba katika Wilaya ya Busega vingi havifanyi kazi kwa mfano, kule Ngasamo na Nasa; na kwa sababu Waziri amesema kwamba, ana mkakati wa kuvifufua viwanda hivi, Je, kupitia sera hii mpya ya viwanda kwa Serikali ya Awamu ya Tano, viwanda hivi vitakuwa ni sehemu ya mkakati huo?
WAZIRI WAVIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 02 Mei nimezindua mkakati unaitwa C to C (cotton cloth); ukiusoma ule mkakati unaanzia kwa mzalishaji wa pamba, azalishe kwa tija. Pamba ikiwepo ginnery zitafufuka, ginnery zilikufa kwa sababu pamba haikuwepo, kwa hiyo ni mchakato mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kama alivyosema hapa Mheshimiwa Ndassa. Ijumaa nitakuwa na wadau wenyewe wa pamba Mwanza ambapo Wakuu wa Mikoa wote watashiriki na Bodi ya Mazao itashiriki, tutayajadili yote hayo. Nipeni information zote zinazotakiwa kwa siku ya leo kesho naanza safari nitakuwa Mwanza yote hayo nitayafanya tu, ningependa viwanda vyote vifanye kazi ikiwemo kile cha Mzee Gulamali cha Manonga.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na matatizo yaliyozungumzwa ya watu wa Kijiji cha Kitunda ambayo kwa karibu sana yanafanana na watu wa Jimbo la Busega, ambako kule Busega tuna Ziwa Victoria, hawa wana Bahari. Sasa hivi usafiri wa majini ni tatizo na Waziri mwenye dhamana wakati ule alitembelea Kijiji cha Nyamikoma katika Wilaya ya Busega na akaahidi ujenzi wa gati, lakini mpaka sasa hivi sijajua Serikali inamefikia wapi? Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akawahakikishia wananchi wa Busega kwamba, lile gati la Nyamikoma litajengwa ili kusaidia usafiri kwa wananchi wa Jimbo la Busega na Majimbo mengine jirani kama Mwibara, Bunda na Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tuna maeneo mengi ambayo yameainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni anafahamu kwamba, katika aliyoyaeleza yamo. Nimhakikishie kile kilichoko katika Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi, ni wajibu wetu na ni lazima tukitekeleze katika kipindi hiki cha miaka mitano ambacho tumeahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni tulitafakari kwa undani kuchunguza katika kila kituo ambacho amekiorodhesha tuone. Hatimaye tumpe majibu kipi tunaanza lini na kipi kitafuata lini na hatimaye apate ratiba kamili ya utekelezaji wa ahadi hiyo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa kweli nimsifu sana kwa kazi kubwa anayofanya ya kufuatilia maslahi ya watu wako wa Jimbo la Busega. Ahsante sana.
MHE. DKT. RAPHAEL M.CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kwa kuwa Mkoa wa Simiyu ni moja ya mikoa mipya, tuna tatizo kubwa sana la kutokuwa na Hospitali ya Rufaa. Kwa vile Mheshimiwa Nyongo alikuwa ameomba kwamba, Hospitali ya Maswa ipewe hadhi hiyo ya kuwa hospitali ya rufaa, lakini Mkoa wa Simiyu tuliamua kwamba Bariadi ndiyo inafaa kuwa Hospitali ya Rufaa. Sasa kwa kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo, ni lini ujenzi huu wa kukamilisha Hospitali ya Rufaa kwa Mkoa wa Simiyu na mikoa mingine mipya ikiwemo Mikoa ya Songwe, Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Geita pamoja na Simiyu yenyewe, lini hii mikoa mipya itasaidiwa kupata hospitali za rufaa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa katika Wilaya mpya vilevile ndani ya mikoa hii mipya ikiwemo na Wilaya ya Usega, tuna tatizo la kutokuwa na Hospitali za Wilaya na sisi katika Wilaya ya Busega tumeiteua Hospitali ya Mkula kwa mkataba wa miaka miwili kuwa hospitali teule ili iweze kutoa huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Busega waweze kupata huduma za Kiwilaya. Lini mchakato huu wa Serikali utakamilika? Tumeshapeleka maombi Wizarani sasa ni muda mrefu lakini hatujapata majibu. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kukiri wazi kwamba, kwa mtazamo wake wa Hospitali ya Bariadi ambayo Serikali mwaka huu tunajielekeza kupeleka 1.4 billion kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa. Hapa maana yake, ule ujenzi uendelee na ni mtazamo mzuri, hata wao kule wanaona kwamba inastahili iwe Hospitali ya Kanda. Kwa hiyo, kikubwa zaidi tutaendelea kuipa nguvu hiyo Hospitali ya Bariadi, lengo kubwa ni kuwa hospitali inaweza kuhudumia ukanda wote ule. Pia suala zima la ujenzi wa Hospitali ya Mkoa, huu ni mpango mkakati wa Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa sababu tunajua tuna mikoa mipya ambayo, tumeianzisha kama alivyosema kuna Songwe na mikoa mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nini kinachohitajika kufanyika? Ni kwamba katika mwaka wa fedha, kwa sababu huu ndiyo mwaka wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano, imani yangu ni kwamba katika mwaka wa fedha unaokuja niwaombe sasa Waheshimiwa Wabunge, kwa umoja wetu na katika vikao vyetu vile vya kisheria, vikao vyetu vya Madiwani, hali kadhalika vikao vyetu vya RCC, jambo hili liwe kipaumbele ili mradi mwisho wa siku na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutakuwa tunakusanya mikakati yote ya mikoa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za mikoa. Hata hivyo, katika hili hatutosita kwa sababu lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba, kila mkoa unakuwa na hospitali yake ya mkoa na baadaye tunakuwa na hospitali za Kanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo katika swali la pili kwamba Busega hamna hospitali ya Wilaya, ni kweli na kwamba wanatumia hospitali ya Mkula kama ni hospitali teule, lakini bahati mbaya kibali bado hakijapatikana. Hivyo, tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Afya, lengo kubwa ni kupata kibali, lakini hata hivyo mpango mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba kila wilaya inapata hospitali ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekwenda mbali zaidi, kwa sababu sehemu zingine coverage ya Wilaya ndani yake kuna Halmashauri kadhaa. Sasa tunasema kwamba, ikiwezekana kila Halmashauri iwe na hospitali yake, kwa hiyo huo ndio mpango wa Serikali. Imani yangu kubwa ni kwamba, tutaungana na mpango huu wote kwa pamoja kusukuma juhudi za ukusanyaji wa kodi ili tupate fedha za kutosha, mwisho wa siku maamuzi yetu ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya na Mikoa yaweze kufikiwa. Hivyo, Mheshimiwa Chegeni endelea na spidi hiyo hiyo, nadhani kila kitu kitakuwa sawasawa.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda tu kuongezea majibu ya nyongeza kuhusu swali la pili la kibali cha Hospitali ya Mkula, kuwa district designated hospital, kwa ajili ya Wilaya ya Busega. Tayari Mheshimiwa Raphael Chegeni, Mbunge wa Jimbo hilo amewasilisha jambo hili Wizarani kwetu na amenikabidhi barua zake mimi mwenyewe hapa Bungeni juzi tu, hata siku tatu hazijapita, ili niweze kufuatilia suala hili. Namwahidi kwamba nitawakabidhi wataalam suala hili, ili waweze kufika maeneo ya pale Mkula, bahati nzuri napafahamu vizuri, wakafanye ukaguzi, wajiridhishe kama inakidhi vigezo na hatimaye Wizara ya Afya iweze kuipa kibali cha kuwa Hospitali Teule ya Wilaya.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini inafahamika kabisa kwamba vyama hivyo vya wafanyakazi vinakuwa vinachukua matakwa na mahitaji ya wafanyakazi wenyewe. Na kwa kuwa Serikali imekuwa ikiwasaidia sana waweze kuingia katika vyama hivi na Serikali hapa imetoa agizo kwamba itawachukulia hatua waajiri ambao wanawazuia kujiunga na vyama hivi.
Je, Serikali inatoa tamko gani kwa sababu baadhi ya wafanyakazi wanakuwa wamefanya kazi lakini wanakuwa na madai yao mbalimbali ambayo hawajalipwa na Serikali. Kwa mfano, Chama cha Walimu Tanzania kina madai mengi sana Serikalini lakini madai hayo bado hayajalipwa. Je, kupitia bajeti hii, Serikali itatoa tamko la kuwalipa walimu madai yao na malimbikizo yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tamko Serikali itasema nini, naomba nirudie katika majibu yangu ya msingi ya kwamba Serikali kupitia Sheria Namba 6 ya mwaka 2004 imeendelea kutoa msisitizo kuwataka waajiri wote kuruhusu wafanyakazi wajiunge katika vyama vya wafanyakazi. Na jambo hili ni la kisheria na Kikatiba, na vilevile sisi Tanzania tumekubaliana na ile ILO Convention Namba 87 ambayo inazungumza kuhusu uhuru wa wafanyakazi kujiunga katika vyama vyao.
Kwa hiyo, nichukue tu fursa hii pia kuwataka waajiri kwa kutoa tamko tena ya kwamba wahakikishe kwamba wanawaruhusu wafanyakazi wao wote kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwa sababu hii ni haki yao ya kimsingi ya kushirikiana kama ambavyo imesemwa kwenye sheria na kwenye Ibara 20 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongezea katika majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri,katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Ni kwamba, katika suala zima la madai ya walimu, tumezungumza kwamba sasa hivi Ofisi ya Rais - TAMISEMI inafanya uhakiki wa madai yote. Lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba walimu wote ambao wanadai, na si walimu peke yake bali katika kada mbalimbali, katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha unaokuja basi madai yote tuweze kuya-address; kila mtu afanye kazi kwa morale katika mazingira yake ya kazi.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa waathirika wengi wa ulemavu, kama alivyosema Mheshimiwa Amina Mollel, katika migodi hii wanapata matatizo mengi sana wanapojikuta kwamba wanapoteza viungo vyao au wanapata ulemavu wakiwa kazini; na kwa kuwa waajiri wengi na hasa migodi hii wamekuwa hawalipi fidia wafanyakazi hawa wanaopata matatizo, na Sheria Namba 20 ambayo inaanza kutumika kuanzia mwezi ujao Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba ndiyo itaanza kushughulikia masuala haya.
Je, kwa wale waajiri ambao wamekaidi kwa muda mrefu, Serikali inatoa tamko gani ili kusudi wafanyakazi hawa ambao wameumia wakiwa kazini waweze kupata fidia zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la msingi Mheshimiwa Mbunge anauliza Serikali inachukua hatua gani au inatoa tamko gani kwa waajiri wote ambao wanakaidi kuwafidia wafanyakazi ambao wameathirika kutokana na magonjwa yanayotokana na kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, Sheria Namba Nane ya mwaka 2008 ambayo imeunda Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi kupitia kifungu cha tano cha sheria hiyo itaanza kufanya kazi tarehe 1 Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa na maudhui ya Sheria hii ni kuhakikisha kwamba wafanyakazi wote wale ambao wamepata occupation diseases wanatibiwa kupitia mfuko huu; na wale ambao watakuwa wamepata ulemavu uliosababishwa na shughuli za kazi na wenyewe wanaweza kufidiwa au kupata mataibabu kutokana na aina ya ugonjwa walioupata kutokana na ripoti ya madaktari Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Serikali sasa inafanyaje? Katika mazingira haya kumtaka mwajiri atimize wajibu wake uko utaratibu ambao uko kwa mujibu wa sheria ambao umewekwa ya kwamba waajiri wote watatakiwa kwanza kuwasilisha michango yao kwa mujibu wa sheria ambapo Sekta Binafsi watatakiwa kuchangia asilimia moja ya wage bill ya kila mwezi, na katika sekta ya umma vilevile asilimia 0.5. sasa kwa wale ambao watakaidi kuchangia maana yake ni kwamba kwanza sheria inasema watatozwa fine ya riba ya asilimia 10 ya kile ambacho wamekichelewesha, lakini pili watapelekwa pia mahakamani na wakithibitika kwamba wameshindwa kuwasilisha michango hiyo adhabu ni kuanzia shilingi milioni 50 au pia kifungo kisichopungua miaka mitano mpaka kumi cha mkuu wa taasisi hiyo.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Napenda kuuliza swali moja.
Katika hii Mikoa na Wilaya mpya, nyingi zina matatizo ya kutokuwa na shule za kidato cha tano na sita. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzisaidia hizi Wilaya mpya ikiwepo Busega, ambayo mpaka leo hii hatuna shule ya A-Level? Mheshimiwa Waziri anaweza kunipa mkakati gani wa Serikali kusaidia hizi Wilaya na Mikoa mipya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba yapo baadhi ya maeneo makubwa hadi Wilaya nzima ambako hakuna shule ya kidato cha tano na sita, lakini nilisema hapa kwamba sekta ya elimu imekuwa decentralized na kwa hiyo maana ya decentralization ni kwamba mipango yote inapangwa kuanzia kule chini na ikiletwa kwetu ni kwa ajili ya kuona tu kwamba tunaipokea na kukubaliana na wadau kama ambavyo tunavyosema kwamba Halmashauri ndizo zinazomiliki shule hizi na kwa kufanya hivyo tunaamini kwamba ndiyo sera ile ya D by D inapokuwa imetekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninamsihi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama wao wataanzisha jambo hili wakalikamilisha, wakileta kwetu hatuna pingamizi kama watakuwa wameziteua shule watakazodhani zinaweza zikawa ni rahisi kuzifanya ziwe high school.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali madogo mawili. Kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kinaongoza kwa kuwa na utaratibu unaoeleweka na wa kidemokrasia ndani ya chama chake tofauti na baadhi ya vyama ambavyo vimekuwa havina uongozi wa demokrasia iliyoshamiri. Je, Serikali kupitia kwa Msajili wa Vyama anaweka utaratibu gani ili kuhakikisha demokrasia ndani ya vyama inatekelezwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa nchi yetu iko kwenye vyama vingi na baadhi ya wanasiasa wanagomea mijadala ndani ya Bunge kitu ambacho ni kuwanyima haki wananchi ambao wamewachagua ili waje kuwawakilisha ndani ya Bunge. Je, Bunge hili linazidi kuchukua hatua gani dhidi ya kitendo hiki cha kutowatendea haki wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza limeulizwa, Serikali kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa inahakikisha vipi demokrasia inakuwepo katika vyama vya siasa. Vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa sheria ambayo imevianzisha lakini vilevile vyama hivi vinasimamiwa na Msajili wa Vyama ambaye kazi yake kubwa ni kuratibu shughuli zote za vyama na amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba vyama vyote vinatii sheria ambayo imeviunda lakini na Katiba ya nchi ambayo inaelekeza masuala mbalimbali ya kiuongozi katika vyama hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa nafasi ya Msajili wa Vyama vya Siasa yeye siku zote ndiye amekuwa mlezi wa vyama hivi na popote pale ambapo kumekuwa kuna shida ya masuala ya kidemokrasia ndani ya vyama amekuwa akichukua hatua stahiki kwa maana ya kukutana na wadau na kuweka mambo sawasawa katika vyama hivi. Kwa hiyo, tunaendelea kuamini kwamba kwa nafasi ya Msajili ataendelea kuvilea vyama hivi na kuhakikisha demokrasia inakuwepo katika vyama vya siasa kama ambavyo vimeanzishwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili limeulizwa kwamba kama Serikali tunachukua hatua gani sasa kwa namna ambavyo hali inaendelea hapa Bungeni ambapo baadhi ya wenzetu wanatoka nje na hivyo wananchi kukosa uwakilishi kupitia uongozi wao humu ndani. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari jambo hili lilishatolewa ufafanuzi mara nyingi sana na wewe Naibu Spika ulishatoa maelekezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisirudie maneno mazuri ambayo umekwishayatoa, lakini msimamo unafahamika kwamba wote tumeingia humu ndani kwa ajili ya kutetea na kuwasilisha maslahi ya watu wetu. Kwa hiyo, ndugu zangu Watanzania wenzetu huko nje wanaona ambao wamebaki kutetea maslahi yao na ambao wametoka.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda niipongeze Serikali kupitia Mradi huu wa REA I, II na III. Kwa kuwa kuna Kata ya Badugu yenye vijiji vya Mwaniga, Manala, Badugu yenyewe na Busani mpaka leo wanaona nguzo za umeme zimepita tu, lakini hawajapewa transfoma. Je, Mheshimiwa Waziri ananihakikishia kwamba vijiji hivi vitapata umeme sasa kuanzia Julai?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vijiji vya Nyakaboja vilivyoko kwenye njia kuu ya kwenda Musoma, Vijiji vya Mngasa, Kalago na Lukungu ambako kuna kituo cha afya mpaka leo hakuna umeme. Je, Mheshimiwa Waziri vilevile atanihakikisha kwamba vijijni hivi ambavyo vinatoa na huduma za Hospitali ya Lukungu pamoja na Hoteli ya Serenity na Speke Bay ambazo zinaingiza mapato kwa nchi hii, vitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Kata ya Badugu kupatiwa umeme, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji vyote vya Kata ya Badugu, kama anavyojua Mheshimiwa mwenyewe ni kwamba maeneo yote ya Nyamikoma, Nyakaboja, Nyakungula pamoja na yale yote ambayo yanaunganishwa Kata ya Badugu yatapatiwa umeme kwenye awamu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, vijiji vya Kata ya Badugu ambavyo vimebaki ambavyo vinajumuisha maeneo ya Nyamanara, Nyamikoma, Nyazikungura pamoja na maeneo mengine ya Lamadi yatapatiwa umeme kwenye transfoma itakayofungwa kuanzia Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu umeme kwa vijiji ambavyo vinaungainisha hospitali ya Lukungu pamoja na hoteli ya Serenity iliyopo Lamadi, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Chegeni kwamba vijiji vyote vilivyobaki ambavyo ni vijiji 16 vitapatiwa umeme. Awamu ya kwanza ya REA kwenye Jimbo la Busega tulipeleka vijiji 22 na katika Awamu ya II ya REA kwenye Jimbo hilo hilo la Busega tumepeleka vijiji 18 na Awamu ya III ya REA kwenye Jimbo hilo hilo tunapeleka vijiji 19 vyote vilivyobaki. Vijiji hivyo ni pamoja na Ng‟wanangi, Ng‟wanale, Vijiji vya Lamadi vilivyobaki vyote vitawaka umeme kwenye Jimbo la Busega.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana. Napenda nishukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa muuliza swali ametoka Bungeni humu na ameliacha swali hili, mimi naomba niulize kama ifuatavyo:- (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa wananchi wa Luchelele wamekuwa kwa muda mrefu sana wakiahidiwa kuhusu suala la fidia; na pale Luchelele kulikuwa na mpango mpaka kujenga kiwanja cha golf ambacho mpaka leo hii imekuwa ni hadithi; na hii mara kwa mara tunaambiwa kuna fidia italipwa, imechukua muda mrefu. Sasa Serikali imefikia wapi kwa suala la fidia ili kweli wananchi wa Luchelele walipwe fidia yao na Serikali iendelee na mpango wake wa Luchelele kama ilivyopangilia?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Wilaya ya Nyamagana inapanuka kuelekea sehemu za Luchelele na kwa kuwa mipango mingi kule inafanyika. Je, Serikali kupitia Wizara yako, ina mkakati gani kuhakikisha kwamba ile Luchelele na St. Augustine yote inaendelezwa kwa mpango na masharti ya Mpango Mji wa Jiji la Mwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu yangu ya awali nilisema kwamba wananchi hawa watalipwa fidia na taarifa zilizopo kama nilivyosema ni kwamba kuna mkopo kutoka CRDB. Status ya mkopo huo ni nini na tumefikia wapi mpaka sasa? Ni kwamba walipoleta ile request, katika ile shilingi bilioni sita, CRDB walikuwa wameweka commitment yao kuwakopesha shilingi bilioni 5.5. Kwa hiyo, ilivyokuja ile request TAMISEMI, ikaonekana kwamba deni linalodaiwa ni tofauti na mkopo watakaoweza kupata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ikatakiwa clarification, ni jinsi gani pesa nyingine itaweza kupatikana hapo? Wakaandikiwa tena barua, Mkurugenzi wa Nyamagana ambayo ni barua ya tarehe 5 Mei, 2016 kumwambia kwamba alete mchanganuo huo sasa, ile tofauti ya shilingi bilioni 2.5 ambayo inatakiwa ku-top up na ile ambayo inatoka CRDB, kuona italipwa vipi na utaratibu wake utakuwaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakaleta hiyo feedback tena katika Ofisi ya TAMISEMI lakini hawakuambatanisha ule muhtasari wa vikao vilivyokubaliana hilo. Kwa hiyo, ofisi yetu imepeleka hiyo barua tena. Lengo ni kuleta zile attachments za makubaliano ya kikao ili mradi ofisi ya Rais, TAMISEMI iendelee na process ya kuhakikisha jambo hili linakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili kuhusu mikakati ya kuendeleza Wilaya ya Nyamagana; kama nilivyosema watu wa Nyamagana mpango wao mkubwa ni kuhakikisha maeneo hayo yanapimwa. Tunajua wazi kwamba Jiji la Mwanza ni kubwa sana, ndiyo maana katika suala zima la uendelezaji wake, tunaelekeza hizi Halmashauri na Manispaa zetu ziweze kuweka utaratibu mzuri wa mipango miji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana watu wa Jiji la Mwanza, kwa sasabu kwa utashi wao mzuri na mawasiliano mazuri wamesababisha Jiji la Mwanza libadilike. Kwa kushirikiana na LAPF wametengeneza center nzuri sana ya kibiashara. Ni imani yangu kubwa sana kwamba mpango ule walioufanya LAPF na mikakati yao ya upimaji katika eneo la Nyamagana kuelekea maeneo haya ya Luchelele itaendelea. Lengo kubwa ni kulibadilisha Jiji la Mwanza liendelee kuwa bora, katika suala zima la kuendeleza Kanda ya Ziwa ya nchi yetu.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nilitaka kuongezea tu katika majibu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la uendelezaji wa Mji wa Mwanza kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameuliza, Jiji la Mwanza pamoja na Majiji mengine kama 14 yako kwenye utaratibu wa kupanga Miji yao kwa maana ya kuwa na master plan; na Jiji la Mwanza ni mojawapo na master plan yake inaandaliwa na wameshirikishwa vizuri. Kwa hiyo, hata hawa ambao wako Luchelele wamekuwa considered katika ile master plan ambayo iko katika process ambayo inaandaliwa. Baada ya muda mfupi nadhani kwenye mwezi Juni hii itakuwa imekamilika na watakuwa katika utaratibu mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika suala la fidia siyo Luchelele peke yake, ni maeneo mengi labda kwa kutumia fursa hii pia niseme Wizara imejipanga katika kuhakikisha tunawakumbusha wale wote ambao Mashirika na Taasisi mbalimbali ambazo zinadaiwa wakimewo wenzetu wa Airport Dar es Salaam na maeneo mengine na hata yale yaliyochukuliwa na Jeshi. Tunawaandikia ili kuwakumbusha zile fidia waweze kuzilipa kwa sababu zimekuwa za muda mrefu na kadri zinavyokaa ndivyo jinsi gharama ya Serikali inavyokuwa kubwa hasa katika kupitia katika Mashirika yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutalizingatia na tutaendelea kulifuatilia na watu wa Mwanza, Luchelele na maeneo mengine watafidiwa.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, napenda tu kuuliza swali dogo kwa Mheshimiwa Waziri.
Kwa kuwa Bodi ya Pamba muda mwingi iko Dar es Salaam na Makao Makuu yako Dar es Salaam, na kwa kuwa Mkoa wa Simiyu ndio Mkoa unaoongoza kulima pamba hapa nchini. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wakulima ambao wamekuwa wakipata mbegu hizi na dawa ambazo haziwasaidii na wala hawapewi fidia. Ni lini Bodi hii itahamia karibu na Mikoa ambayo inazalisha pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ameshatoa agizo la Bodi ya Pamba kuhamia Mwanza na kwa taarifa tulizonazo ni kwamba wanatakiwa wawe wamehama kabla ya tarehe 10 mwezi huu.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili. Swali la kwanza, kwa kuwa hizi zana haramu, yaani nyavu pamoja na zana nyingine zinatengenezwa na viwanda vilivyoko hapa nchini na zinaagizwa kuingia hapa nchini na wafanyabiashara: Je, Serikali inachukua hatua gani kwa hao watu ambao wanaleta zana haramu hapa nchini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wavuvi haramu hasa ni watu ambao wanajitafutia riziki zao, wengi wamenyang’anywa zana zao na kuchomwa moto ili kuitikia agizo la kisheria la nchi: Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia hao wananchi ambao maisha yao yote yanategemea uvuvi lakini kwa sasa hawawezi kufanya kwa sababu wanakiuka sheria? Wanasaidiwaje kupata mikopo angalau waweze kuendesha maisha yao, lakini pili kufundishwa namna endelevu ya kufanya uvuvi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijaishia tu katika kukamata makokoro na zana nyingine haramu zinazotumika katika uvuvi, lakini vile vile kuhakikisha kwamba, pale yanapotengenezwa na yanapotokea, vilevile wanaohusika wanakamatwa.
Waheshimiwa Wabunge, kama mtakumbuka, ni karibuni tu meli iliyoingia katika bandari ya Dar es Salam ilishikwa ikiwa imebeba zana mbalimbali za uvuvi zikiwepo zana za kutengeneza makokoro na nyavu ndogo ambazo inaaminiwa zingeweza kutengeneza mpaka nyavu 20,000. Huo ni mfano tu wa kuonesha kwamba siyo tu tunakamata wavuvi, lakini vile vile hata viwanda na hata katika kuingiza vile vile tunadhibiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ifahamike tu kwamba, ugumu unaotokea ni kwamba zana za uvuvi au vifaa vinavyotumikia kutengeneza zana za uvuvi vile vile zinatumika kutengeneza vitu vingine ambavyo ni halali. Kwa mfano nyavu, siyo kwamba unakuta hasa kwamba ile bidhaa inayotoka kiwandani ni haramu; inaweza ikawa inatumika kwa ajili ya vitu vingine ambavyo vinaruhusiwa kisheria. Kwa hiyo, kidogo inaleta shida, lakini pale tunapobaini moja kwa moja kwamba ni kifaa au ni zana ambayo inaenda kutumika kufanya uvuvi haramu au kutengeneza zana za uvuvi haramu, tunachukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni kuhusu msaada gani Serikali inatoa kwa wavuvi wadogo? Nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Wizara hii, imeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba wavuvi wadogo wanaweza kupata mikopo kupitia katika Benki yetu ya Kilimo, lakini vile vile kuna mikopo ambayo inapatikana kwa ajili ya pembejeo kupitia Mfuko wa Pembejeo. Tayari Benki ya Uwekezaji ambayo nayo ina fursa kwa ajili ya mikopo na Wizara pia inakopesha vikundi mbalimbali vya wavuvi. Kwa hiyo, kuna fursa mbalimbali kwa vikundi na wavuvi ambao watahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha fursa zilizopo kwa ajili ya kutoa mikopo, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri mbalimbali imeendelea kutoa elimu kuhusu uvuvi endelevu na uvuvi bora kwa kupitia vikundi mbalimbali vya Beach Management Unit na tayari katika maeneo mengi ya nchi yetu, elimu hii imetolewa, lakini kama nilivyosema tunatoa elimu kupitia vyombo vya habari kama television na tunaamini imesaidia sana kupunguza tatizo la uvuvi haramu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu, uvuvi haramu ni kama uhalifu mwingine. Hata watu wakiwa na elimu namna gani, bado mara nyingi kuna tabia ya wahalifu kuendelea kuwepo, lakini Serikali itaendelea na jitihada za kupambana na uvuvi haramu.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna wilaya nyingi mpya ambazo zina matatizo sana ya hata kutokuwa na Hospitali za Wilaya. Na kwa kuwa majibu yake anasema kwamba kuna fedha ambazo zimetengwa, je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kunihakikishia kwamba katika Wilaya ya Busega kituo cha Nasa hizo fedha zitapatikana lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Dkt. Chegeni unafahamu na wewe kule kwako umenikaribisha, nakushukuru sana. Hicho kituo cha afya ulichokisema
miongoni mwa maeneo ambayo yana changamoto, na akina mama wanapata shida kubwa sana kupata huduma za upasuaji. Nilikueleza wazi kwamba katika kipindi cha huu
mwaka tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba tunajenga jengo la upasuaji kama nilivyosema katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuwa na imani,
kwamba Serikali kwa kupitia Wizara ya afya tuna mkakati mpana sana kuhakikisha kwamba tunapelekea huduma katika maeneo hayo na Mungu akijaalia kabla ya mwezi wa sita tunaweza tukaenda kuweka jiwe la msingi sawa sawa
na kituo cha afya cha Malya kule kwa ndugu yangu Ndassa.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya
Mheshimiwa Waziri, Halmashauri nyingi zina mapato kidogo na kwa vile baadhi ya vyanzo vya mapato Serikali Kuu
imevichukua, kwa hiyo, ina maana kwamba baadhi ya Halmashauri hazitaweza kulipa Wenyeviti kwa mujibu wa
majibu ya Mheshimiwa Waziri alivyosema hapa. (Makofi)
Je, Serikali ina mpango gani mbadala kuhakikisha kwamba Wenyeviti wote, regardless wanatoka kwenye
Halmashauri ipi na wenyewe waweze kupata malipo kama haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna wakati mwingine marejesho yanakuwa siyo rafiki sana, ndiyo maana katika utaratibu wa sasa inawezekana Wabunge wengine watauliza kwamba property tax imechukuliwa imeenda Serikali Kuu, tunafanyaje na haijaridi? Hili hata Waziri wa Fedha baadaye akija ku-table bajeti yake hapa katika mjadala mpana baadaye, itaonekana ni jinsi gani tutafanya. Lengo letu ni kuziwezesha Halmashauri zetu cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu changamoto hii hata Waheshimiwa Wabunge wengine wanaweza
wakasimama baadaye wakasema hata Madiwani wengine wamekopeshwa kwenye mabenki, wanataka kupelekewa mahakamani, ndiyo maana nasema katika mchakato huu mpana, mara baada ya kurekebisha sheria, kwa sababu sheria ile itakuja hapa mtaona kwamba Waziri mwenye dhamana atakuwa anapata fursa ya kuhakikisha Halmashauri zinaenda vizuri, kwa sababu zimewekwa kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 145 na utelekezaji wake Ibara ya 146.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waziri mwenye dhamana amepewa mamlaka hiyo kwa utaratibu wa sheria
za nchi Sura namba 287 na 288 ile ya vijijini na ile ya miji. Kwa hiyo, katika kurekebisha Sheria ya Fedha, itamsaidia sana Waziri mwenye dhamana kufanya maamuzi hayo mwisho wasiku kwa kuangalia jiografia ya Halmashauri hizi ambapo zenyewe zinatofautiana katika nguvu ya kimapato.
Halmashauri ya Ilala huwezi ukafananisha na Halmashauri ya Kakonko kwa mwalimu wangu pale, hizi zinatofautiana. Kwa hiyo, Waziri mwenye dhamana atakuwa anapata nafasi nzuri kuiangalia nchi kwa upana wake na kuangalia hizi Halmashauri, Madiwani na Wenyeviti ili kazi iende vizuri.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuweza kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri
ya Mawaziri na Naibu Waziri, kwa Wilaya ambazo ni mpya na Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumzia suala la Busega kwamba alikuta pale matatizo ya watumishi, je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia Wilaya hizi mpya ambazo zimeanzishwa zenye uhaba wa ikama ya watumishi? Vilevile pili baadhi ya watumishi walio wengi hawajalipwa mafao yao. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu pale awali ni kwamba tutajitahidi Halmashauri hizi mpya ambazo zimeanzishwa na bahati nzuri Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi) amezungumza wazi kwamba tuna hizi ajira mpya ambazo zinakuja lengo kubwa ni kuziba mapengo yote yaliyokuwepo katika maeneo yetu. Ofisi yetu imeshaanza kufanya tathmini ya kujua ni watumishi wangapi wanahitajika katika Halmashauri gani ili kuziba haya mapengo yaliyopo. Kwa hiyo, mtani wangu Mheshimiwa Dkt. Chegeni ondoa hofu zoezi hili litaweza kujibu matatizo ya watumishi katika Jimbo na Halmashauri yako ya Busega.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, suala la zao la pamba na usindikaji wake au kuongeza thamani ni suala la msingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Busega kuna vinu ambavyo ni vya viwanda vya Pamba kama cha Ngasamo na Sir Ginnery. Maeneo yote haya yamekuwa na viwanda ambavyo vimesimama, havifanyi kazi na hivyo kupelekea wananchi wengi na wakulima wa pamba kushindwa kuuza pamba yao kwa bei yenye kuongeza thamani. Je, Mheshimiwa Waziri ana mkakati gani? Pamoja na suala la Manonga na kwingineko ambako kuna viwanda ambavyo havifanyi kazi vizuri, kama Serikali kuna namna gani ya kuweza kuboresha viwanda hivi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, chanda chema huvikwa pete. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wanaotoka kwenye eneo la pamba, nenda kwenye mkakati wa pamba mpaka mavazi, ukurasa wa 91 majibu yote yako pale. Tutaweza kufaidika na pamba kama zamani, soko litakapokuwa linaweza kuvuta (the demand pull) na mojawapo ya mambo ya kufanya ni kuongeza ufanisi katika zao la pamba. Mwaka 2016 kwa kutumia ways and measures baada ya ku-control watu wasichafue pamba, nyie ni mashuhuda bei imepanda kidogo, tutaendelea na nikuahidi Mheshimiwa Mbunge tukitoka hapa nitakupa huo ukurasa namba 91 nilikuja nao nilijua itajitokea uone mambo mazuri. The productivity, pamba ina tatizo kwa sababu hakuna tija katika uzalishaji.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Lamadi ni mji ambao kijiografia unapanuka kwa kasi sana; na kwa kuwa Lamadi hiyo hiyo imeshakidhi vigezo ambavyo Mheshimiwa Waziri amevizungumza hapa, Wizara ya Ardhi imeshapima viwanja pale, miundombinu ya maji ipo, barabara zipo na Mheshimiwa Rais alipokuja alivutiwa sana na mji ule na akasema kwamba angependa uwe mji wa kibiashara, ufanye biashara kwa saa 24 kwa siku.
Je, Serikali haioni kwamba kama kuna kitu kinaitwa
hati ya dharura basi itumike kuufanya Mji wa Lamadi Mji mdogo ili kusudi iweze kuchochea maendeleo kwa wananchi badala ya kuendelea kuuacha hivi hivi ambapo baadaye unaweza ukaleta matatizo makubwa zaidi?
Swali la pili, kwa kuwa ukiangalia katika barabara inayotoka Mwanza kwenda Musoma, mji pekee ambao unakua zaidi ni Lamadi, Serikali haioni kwamba kuendela kuuachia kutangaza Halmashauri ya Mji Mdogo wa Lamadi itazidi kuleta matatizo makubwa zaidi kwa wananchi na kusababisha mpangilio ambao baadaye itakuwa ni tatizo kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Dkt. Chegeni mjukuu wa Mzee Mchengerwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, alivyosema kupeleka hati
ya dharura kwamba Mji wa Lamadi utangazwe kwa hati ya dharura, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Chegeni tulifika pale kwako Lamadi na mimi najua expansion ya mji ule unavyokua kwa kasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi ni kwamba kilio hiki tumekisikia na bahati nzuri Mheshimiwa Rais ameshaweka commitment pale alipokuwa site na bahati mbaya tulivyoangalia kuna baadhi ya changamoto ndogo ndogo ambazo zipo kuufanya mji ule tuutangaze rasmi. Naomba niseme kwamba jambo hili tunalichukua kwa pamoja, baadaye tujadiliane miongoni mwa zile changamoto zilizokuwepo tuziweke sawa ili mradi tuweze kufikia katika mpango ambao unastahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo lingine kuhusu kuutangaza rasmi, Mheshimiwa Chegeni naomba tutakapokaa baadaye vizuri na bahati nzuri na Mheshimiwa Waziri wangu wa Nchi hapa yupo na amekusikia naye jambo hilo analiangalia kwa karibu zaidi tutafanya utaratibu wa kuona jinsi gani tufanye ili commitment ya Mheshimiwa Rais ameiweka pale basi mwisho wa siku waone kwamba kulikuwa na Dkt. Chegeni amepigania Mji wa Lamadi umeweza kupatikana na kuufanya mji wa kibiashara uweze kuendana na hadhi kwa kadri tutakavyoweza kuutangaza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kilio chako tumekisikia, tutaakaa pamoja, tutajadiliana pamoja nini tufanye sasa cha haraka kwa mustakabali wa Mji wa Lamadi ambao unakua kwa kasi. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi, nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya makampuni haya kwa muda mrefu sana yamekuwa yakifanya udanganyifu na hasa katika miamala ya simu pamoja na muda wa maongezi kwa wateja na kwa kuwa Serikali tayari imeshaanza kudhibiti suala hili. Je, Serikali haioni kwamba ni busara na ni vyema kuendelea kudhibiti makampuni yote haya ya simu yaweze kulipa kipato sahihi na kutokuwanyonya wananchi katika suala la miamala ya simu pamoja na muda wa maongezi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana naye na ndivyo tunavyotaka kufanya na tunavyoEndelea kufanya kwa kutumia huu mtambo wa TTMS na makampuni yote hatutaacha hata moja tutayaingiza katika mfumo huu na kuhakikisha mapato yao yote yanayopatikana tunayafahamu na tunapata haki yetu.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu, hoja ya swali la Mheshimiwa Kishimba ni kwamba kumekuwa na utaratibu wa kumtahini mwanafunzi kwa mtihani wa mwisho na wakati mwingine unakuta mwanafunzi pengine zile siku za mwisho anakuwa na matatizo ambayo yanamfanya ashindwe kufaulu vizuri.
Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuangalia maendeleo ya mwanafunzi huyu ili kusudi maendeleo yake yawe ni sehemu ya mtihani wake wa mwisho ili kuondoa mchanganyiko huu?
Swali la pili, kwa vile kumekuwa na wizi wa mitihani mara kwa mara na hii inachangiwa kwa sababu wanafunzi wanajiandaa kwenda kushinda mtihani badala ya kujua namna ya kujibu mtihani.
Je, Serikali inatafuta mbinu gani mbadala za kuwasaidia vijana badala ya kukariri kufanya mtihani, wafanye mtihani kwa kuelewa namna ya kushinda mtihani?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kutumia matokeo endelevu yaani mwanafunzi amekuwa akipimwa katika muda wake anaokuwa darasani, vilevile hata wale wanaofanya shughuli za vitendo, kwa mfano wale wanaosoma masomo ya ufundi wamekuwa wakienda kwenye mazoezi wanafuatiliwa na pia shughuli za vitendo zimekuwa zikichangia asilimia 30 niliyosema katika mitihani ya mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mtihani wa mwisho ni kweli ndiyo unakuwa na nafasi kubwa zaidi kwa ajili ya hiyo asilimia 70; endapo mwanafunzi amepata tatizo siku ya mwisho ya mtihani, taarifa huwa zinatolewa na kuweza kuangalia kwamba alikuwa kwenye mazingira gani. Wakati mwingine mwanafunzi anashauriwa asifanye mtihani kama hali yake kwa mfano itakuwa ni ya ugonjwa ili aweze kurudia na kufanya mtihani wakati mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wizi kwa kiwango kikubwa Serikali imeweza kudhibiti tatizo hilo, nanyi mtakuwa mashahidi katika kipindi hiki, hasa toka tumeingia halijawahi kutokea tatizo la wizi wa mitihani. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ningependa kuweka msisitizo kwenye suala la wizi wa mitihani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kulihakikishia Bunge lako kwamba Serikali imedhibiti suala la wizi wa mitihani na kinachotokea ni udanganyifu katika mitihani, ambapo baadhi ya Walimu ama huwa baada ya kufungua zile karatasi za mitihani wanaenda pembeni wanawaandalia wanafunzi majibu na kuyapeleka katika chumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Serikali imekuwa pia makini katika kuhakikisha kwamba inaangalia kwa karibu usimamizi wa mitihani na wote ambao wanakuwa wanajihusisha na udanganyifu katika mitihani hatua zimekuwa zikichukuliwa na zitaendelea kuwa zinachukuliwa.(Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa viuatilifu hivi kwa kweli imekuwa ni hasara kubwa sana kwa wakulima, na kwa kuwa wakulima wa Jimbo la Bariadi na Jimbo la Busega katika msimu huu wamelima sana zao la mahindi lakini limeshambuliwa na funza, kitu ambacho kimesababisha watapata uhaba wa chakula, je, Serikali inachukua hatua gani za makusudi ili watu hao wanaoingiza viatilifu ambavyo havifai na viko chini ya viwango wanadhibitiwa na wanapewa adhabu kali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye maelezo yangu ya awali; kama Mheshimiwa Mbunge anawafahamu watu au makampuni ambao wameingiza viuatilifu ambavyo haviko katika ubora unaotakiwa kisheria tutawachukulia hatua. Hata leo hii hii akinipa list yao tutaanza kufanyia kazi na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwafungia na kuwaondolea leseni ya kuagiza na kuuza viuatilifu lakini vile vile kuwapeleka Mahakamani kwa sababu ni kinyume cha Sheria kuuza dawa na viuatilifu ambavyo havina ubora.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza, lakini sambamba na hiyo nakushukuru sana kwa kuweza kunipa pongezi kwa swali langu la ki-CPA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri, lakini kodi hii inasema ni road licence na yeye anasema ni kodi ya usajili wa gari ya mwaka kwa hiyo ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, je, haoni kwamba kodi hii kwanza inakusanywa kimakosa kwa sababu jina leke liko tofauti na lilivyo na pili haoni kwamba ingekuwa bora zaidi tungeikusanya kwa kutumia matumizi ya gari barabarani ili kuongeza kama mapato yake?? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna baadhi ya watu sasa wanasumbuliwa barabarani, kwa kudaiwa madeni ya gari ambayo pengine ina muda mrefu haifanyi kazi ipo nyumbani na wanadaiwa kwamba lazima alipe kodi hiyo. Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuna haja ya kutoa tamkoili watu wasisumbuliwe barabarani na traffic, polisi, pamoja na TRA juu ya suala hili la kulipa kodi hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kiutaalamu kodi hii au ada hii haitwi road licence, kama Sheria inavyosomeka pamoja na kanuni zake, zinasomeka The Road Traffic Motor Vehicles Registration, kwa hiyo hii ni motor vehicle ni ownership kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi. Sio kwamba inalipiwa kwa matumizi yake barabarani, kwa hiyo, sheria inasema hivi, lakini kwa lugha zetu za mtaani tunaiita hivyo. Lakini kimsingi hii ni ownership na sio sheria ya kutumia ni ada ya kutumia gari barabarani, hapana.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, ada hii ya leseni ya gari ya mwaka hutozwa kwa kila gari kulingana na ukubwa wa engine ya gari na kwa sasa kwa jinsi ilivyo sheria hii haitoi fursa ya kusamehe ada hii ambayo haikulipwa huko nyuma.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba ipo katika kanuni zetu sehemu ya nane kifungu cha 32 mpaka 34 inamuelekeza owner wa vyombo vya moto jinsi ya kufanya utaratibu upi afuate kama chombo chake hakitumii tena, haki-own tena ili aweze kwenda kwa registrar ambaye ni Katibu Mkuu Hazina ili aweze sasa chombo chake kuwa deregister na hataweza kudaiwa tena ada hiyo.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hii ni sheria lakini kama Serikali tumesikia kilio cha Wabunge wengi pamoja na wananchi tunalifanyia kazi, tunaifanyia kazi sheria pamoja na kanuni zake kuona jambo hili linafika mwisho ambao ni mzuri kwa Serikali yetu pamoja na wananchi wetu.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri katoa majibu mazuri sana, lakini mimi nina concern moja kubwa kwamba hawa tembo madhara yao ni makubwa sana katika Wilaya ya Busega ambayo inapakana na Wilaya za Bunda na Serengeti. Maelezo ya Mheshimiwa Waziri katika majibu yake amesema kwamba hawa tembo wanazidi kudhibitiwa, lakini mwishoni amesema kwamba tembo wameongezeka zaidi, sasa sijaelewa kwamba sasa kwa vile wameongezeka zaidi madhara yatakuwa makubwa kwa wananchi. Serikali sasa kupitia Wizara yake ina mkakati gani kuwaokoa wananchi ambao wanasumbuliwa na tembo kwa kusababishiwa hasara kubwa zaidi?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma nchi yetu ilikuwa na tembo wengi sana, wanafika 110,000, hivi sasa hatua tuliyofikia hapa wanyama hawa walipunguzwa sana na ujangili wakafika chini ya 10,000. Sasa hivi ndiyo idadi hiyo inaanza kukua na tunaanza kuwaona. Katika eneo lile la Serengeti na eneo la Maswa tunafanya utafiti kuangalia kama tunaweza kujenga uzio wa kuwatenganisha watu, mashamba yao na hifadhi. Tunafanya mazungumzo na wawekezaji wakubwa hapa nchini kwetu na mazungumzo yanaelekea vizuri. Sikupenda nifike mahali ninasema jambo hili, lakini Serikali inalichukulia jambo hili kwa uzito mkubwa sana na ndiyo maana tunafanya utafiti wa uwezekano wa kujenga uzio wa kilometa 140 tuone kwamba italeta afueni kiasi gani katika kuwadhibiti wanyama hawa.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yamejikita katika kuelezea uhalisia wa mifuko hii na changamoto zilizopo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwanza, kwa vile inaonekana wazi kwamba watumishi wengi na hasa wanachama wa mifuko hii wanapokuwa wameachishwa kazi au wametorokwa na waajiri wao wanahangaika sana kuweza kujikimu katika maisha yao na hiyo sio hiari yao isipokuwa wameachishwa kazi au wametorokwa na waajiri. Sasa Serikali haioni kwamba kuna haja hawa watu ambao wanapata dhahama hii, wasaidiwe kuchukua mafao yao ili wajikimu katika maisha yao wakati wakitafuta kazi zingine za kuweza kujipatia kipato?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kabisa kwamba mifuko hii ina changamoto nyingi sana, ikiwa ni pamoja na gharama za uendeshaji ambayo inakula mifuko ya wanachama hawa, lakini pili kutokana na kwamba mifuko hii imekuwa mingi mno na utitiri ambao mafao yao hata hayana tija kwa wanachama wenyewe.
Je, ni lini sasa Serikali, kufuatia kauli ya Mheshimiwa Rais siku ya sherehe ya Mei Mosi Moshi katika Mkoa wa Kilimanjaro alipotaka Serikali ilete hoja hapa Bungeni, Muswada wa kuweza kuigawa mifuko hii kutoka utiriri huu na kubakiwa na angalau mifuko miwili tu ambayo itakuwa na sekta ya umma au na sekta binafsi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba ni lini Serikali itatii maagizo ya Mheshimiwa Rais kwa kuleta Muswada hapa Bungeni ili tuweze kurekebisha suala la mifuko hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza naomba tu nirudie majibu yangu ya msingi ya kwamba katika kuliangalia suala hili la fao la kujitoa kama lilivyokuwa linaitwa, sisi kama Serikali na kupitia maazimio ya Bunge hili mwaka 2012 ambayo ilisema Serikali iangalie utaratibu mzuri wa kushughulika na suala hili la fao la kujitoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kama nilivyosema tayari tumekwishaanza maandalizi ya kuja na utaratibu mwingine mbadala ambao utamfanya mfanyakazi wa Kitanzania yule ambaye ataachishwa kazi na hajafikisha umri huo wa miaka 60 wa kuchukua mafao yake, tuone namna ya kuweza kuliweka sawa na kumsaidia asipate shida katika muda huu wote wakati bado anasubiria kupata ajira nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo kwa sababu jambo hili linakuja Bungeni, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira. Muda sio mrefu tutawasilisha mapendekezo yetu hayo na ninyi kama Wabunge mtapata nafasi za kuweza kuchangia na kutushauri vema sisi kama Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lke la pili; ni lini tutatii maagizo ya Mheshimiwa Rais ya kuunganisha mifuko hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba sisi baada ya tamko la Mheshimiwa Rais kazi hiyo imefanyika mara moja na katika majibu yangu ya msingi nimesema tayari tumeshakutana na wadau, tumezungumza namna bora ya kuunganisha mifuko hii na muda sio mrefu tutatoa pia taarifa sehemi ambayo tumefikia na tutawapa pia the way forward ya namna ambavyo mifuko hii itakuwa. Hivyo Mheshimiwa Mbunge vuta subira tu, hii yote iko katika mipango na agizo la Mheshimiwa Rais tumelitii na tumelitekeleza. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Maswali Namba 75 na swali Na 76 yanafanana lakini Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake ambayo ni mazuri sana amesema kwamba palipo na wananchi na kama wamehamasika na wameshajitolea kuanza kazi za ujenzi wa vyuo kama hivi, Serikali iko tayari kuweza kuwapa mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge lililopita, Serikali iliwakubalia wananchi wa Wilaya ya Busega kutenga eneo kwa ajili ya kuanzisha Chuo cha Ufundi Stadi (VETA). Je, wazo hili la Serikali bado liko palepale au limebadilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema mwenyewe, kama tayari kuna ahadi thabiti ya Serikali kuhusiana na chuo chake cha VETA Busega, leo hii haiwezi ikabadilika. Kwa hiyo, tuendelee na majadiliano tokea tulipoacha kutoka kwa wenzetu ili tuone namna bora ya kutekeleza ahadi hiyo. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na napenda nipongeze majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu haya yamejikita kuelezea taarifa ambayo siyo sahihi, kwa sababu migogoro mingi imekuwa ikichochewa na uhamishaji wa mipaka na ndiyo malalamiko ya wananchi katika maeneo husika, kwa vile Serikali imekuwa ikihaidi muda mrefu kwamba kuwe na mpango shirikishi kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii, TAMISEMI na Wizara ya Ardhi ili kuainisha mipaka vizuri zaidi, kitu ambacho kitaondoa migogoro na migongano iliyopo.
Je, ni lini sasa Serikali kupitia majibu haya, kwa sababu suala hili siyo mara ya kwanza au ya pili kuuliza hapa Bungeni, ni lini Serikali itakaa na wananchi wa maeneo husika ili kutatua mgogoro wa namna hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Mheshimiwa Naibu Waziri aliyekuwepo wakati ule Engineer Ramo Makani alitembelea maeneo husika yaliyotajwa kwa maana kwamba pori la Akiba la Kijereshi kwa wananchi wa kijiji cha Kijereshi, Mwakiloba, Lukungu na Mwamalole na akajione mwenyewe kwamba wananchi wana haki kwa kile wanachokizungumza, vilevile alikwenda Pori la Akiba la Sayanka akajionea mipaka imehamishwa wananchi wamekuwa miaka yote wanalima kabla ya mipaka kuwekwa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari sasa kuja ujionee uhalisia huu na uondokane na taarifa potofu ambazo zinazotolewa na wataalam wako? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kujibu naomba niitumie nafasi hii kumpongeza sana kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya kwa kweli akina Masunga na Hasunga nadhani ni machachari sana, hongera sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijibu maswali yake. Kuhusu matatizo na migogoro mbalimbali ambayo ipo katika maeneo mengi, ni kweli kabisa tumebaini kwamba kuna migogoro mingi ambayo aidha, imesababishwa na kutokushirikisha vizuri wananchi ama kutokana na sababu mbalimbali ama kuongezeka kwa idadi ya watu katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua mbalimbali katika maeneo mengi, kwanza tuliunda Kamati ya Kitaifa shirikishi ambayo ilishirikisha Wizara mbalimbali ambayo sasa imebainisha maeneo mbalimbali yenye migogoro na hivi sasa ipo katika hatua ya mwisho ya kubainisha na kutoa ushauri ili tuweze kufanya uamuzi ni maeneo yapi Serikali iweze kuyaachia kwa wananchi na maeneo yapi yabaki chini ya hifadhi. Baada ya taarifa hiyo kukamilika hivi karibuni nadhani kwamba taarifa hii itatolewa Bungeni na Wabunge wote watapata nafasi ya kuweza kujua.
Kuhusu kukaa na wananchi wa Jimbo la Mheshimiwa Chegeni mimi naomba nimuambie tu kwamba Serikali tuko tayari kukaa na wananchi ili kuweza kupitia mipaka hatua hadi hatua, mimi nimuahidi baada ya Bunge hili tutakaa naye tutapanga kwamba ni lini twende tukawatembelee ili na nijiridhishe kabisa kwamba madai anayoyasema na wananchi wanayoyasema kweli yanahusu hiyo mipaka na kama mipaka imesogezwa basi tuweze kuchukua hatua stahiki katika maeneo haya aliyoyataja. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na kwa Serikali yetu kwa mpango mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu kwa kweli ni mradi ambao una tija kubwa sana kwa wananchi wa maeneo husika katika Wilaya ya Busega, Wilaya ya Itilima, Bariadi, Maswa na Meatu. Kwa kuwa mradi huu utakapopita vijiji ambavyo vipo umbali wa kilomita 12, kushoto na kulia mwa bomba kuu, vitapata huduma ya maji: Je, Serikali ina mpango gani kwa vijiji ambavyo vipo nje ya mradi huu kupatiwa maji ili waweze kunufaika na mradi wa namna hii? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Ziwa Victoria lina maji mengi sana na mikoa mingi ina matatizo ya maji, kwa nini Serikali isiwe na mpango mwingine kabambe; baada ya Mkoa wa Simiyu kupata maji, basi Mkoa wa Singida na wenyewe upate maji na mpaka Dodoma nao waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa kunipa pongezi; lakini pili, vijiji vinavyotarajiwa kunufaika na mradi huu ambavyo vipo umbali wa kilomita 12 kutoka katikati ya bomba ni vijiji 223.
Swali lake namba moja ameuliza, vijiji ambavyo vipo nje ya zile kilomita 12; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya mradi kukamilika huwa tuna utaratibu wa kuendelea kutoa fedha kwenye mamlaka zilizo karibu na hilo bomba ili ziweze kuendeleza kupeleka maji kwenye maeneo ambayo hayakupitiwa na huo mradi. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya hivyo kama ambavyo tumeshaendelea kufanya kwenye mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Shinyanga.
Swali la pili, Ziwa Victoria lina maji mengi; ni kweli lina maji mengi. Kuna utaratibu gani wa kupeleka maji kwenye maeneo ambayo hayajapata maji ikiwemo pamoja na Mkoa wa Singida?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tayari tuna mradi tumepata Dola milioni 265 na mwaka wa fedha unaokuja tunasaini mkataba kwa ajili ya kupeleka maji ya Ziwa Viktoria, Nzega, Mkoa wa Tabora hadi Igunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumesema kwamba sasa hivi tutaanza kufanya utafiti, upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kupeleka maji pia katika Mkoa wa Singida ambao ni mkoa kame na hauna maji ya kutosheleza kule chini. Kwa hiyo, tunaendelea kufanya tafiti ili kuhakikisha kwamba maji yanawafikia wananchi wote.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Swali langu narudia pale pale kwamba kama alivyouliza Mheshimiwa Rweikiza ni kwamba ni lini Serikali itafikiria kuanzisha Mfuko huu wa Maji ili kuweza kuondoa kero kubwa kwa wananchi kuhusu matatizo ya maji kama ambavyo tumeweza kuondoa kero ya umeme sasa katika sehemu nyingi vijijini. Je, ni lini tutaanzisha huu Mfuko wa Maji? Nadhani ndiyo hoja ya msingi zaidi hapa.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna mambo mawili; Mfuko ulishaanzishwa. Mfuko tayari tunao na Mwaka huu wa Fedha tulionao Mfuko una jumla ya shilingi bilioni 158. Suala la pili sasa tunataka kuanzisha Wakala kwa ajili ya kutumia huo Mfuko ili tuwe na wakala utakaohakikisha kwamba tunapata huduma ya maji vijijini kwa haraka. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Suala la tembo pamoja na uharibifu wake ni suala zito sana. Linaongelewa hapa kwa juu juu lakini madhara yake ni makubwa sana kwa wananchi na hasa wanaozunguka maeneo hayo. Je, unaposema mapitio ya kanuni, ni lini sasa yatakuwa tayari? Swali hilo tu kwa sababu wananchi wana shida kubwa sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba sasa hivi tuko kwenye hatua ya mwisho ya kupitia hizi kanuni upya ili angalau kuweza kuvipitia hivi viwango vyote ambavyo vimekamilika. Kwa hiyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mwaka huu hautakwisha hizi kanuni zitakuwa zimeshakamilika.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Shule hii iliyotajwa na Mheshimiwa Gimbi na ninapenda nimshukuru kwa swali lake, lengo lake ni kwamba kuipandisha kuwa high school, lakini kwa mpangilio wa Wilaya ya Busega tumeipanga kuwa ni Chuo cha VETA. Je, ni lini Serikali kupitia Wizara ya Elimu itatusaidia kuwa na shule ya VETA katika majengo haya Sogesca?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ipo tayari kwa kila fursa inayojitokeza, kwa hiyo tutaenda kuangalia kuona kama inafaa, basi tutafanya hivyo.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa swali la msingi linazungumzia kuhusu kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto na kwa kuwa takwimu zinaonesha kwamba kila watoto sita wanaozaliwa watoto wanne sio wa baba mhusika. Je, Serikali inaonaje kuhusu udhalilishaji wa akinababa kwa kubambikiziwa watoto ambao siyo wa kwao ki-genetic? (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke kumbukumbu sahihi ili hii dhana ili isizidi kuenea. Si kweli kwamba watoto sita katika watoto wetu tuliokuwa nao wote si wa baba ama wazazi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke vizuri jambo hili. Takwimu ile ilikuwa inatokana na wale waliopeleka vipimo vyao kwa ajili ya vinasaba kutambua uhalali wa mzazi. (Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila mpangilio)

Naomba Waheshimiwa Wabunge mnisikilize, nataka tuelewane vizuri. Ni sawasawa unaenda katika wodi ya TB unataka kujua maambukizi ya wagonjwa wa TB katika wodi ya TB. Wale wote waliopeleka sample maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni wale ambao tayari wana wasiwasi kuhusiana na uzazi wa wale watoto na ndiyo maana hicho kiwango kilichopatikana kikawa hicho, lakini siyo kwamba kwa ujumla wetu Tanzania nzima watoto wengi hususan kwa akina baba siyo watoto wao, siyo kweli!
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiweke hiyo taarifa wazi ili sasa Wabunge na especially wanaume tusianze kukimbia majukumu yetu ya msingi. Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Kwanza nafurahi kukuona ukiwa mzima wa afya na tunakupongeza sana kwamba Bunge hili lilikuwa limeku-miss, sasa tunafurahi kukuona kwenye kiti chako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na makofi hayo na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, muuliza swali Mheshimiwa Mkundi amezungumzia suala la Ukerewe. Ukerewe inaunganishwa na barabara inayotoka Nyanguge kupita Busega mpaka pale Ndabaga. Barabara kuu ni mbovu kabisa, hata daraja la Mto Simiyu pale Magu halikidhi mahitaji ya usafirishaji katika mikoa hiyo. Je, Serikali inatoa commitment gani ya kuweza kukarabati barabara hii kutoka Nyanguge - Magu - Busega mpaka pale Ndabaga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze na kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa sababu barabara hii tumekuwa tukizungumza kwa maana ya kuifanyia maboresho.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba kabla commitment haijatolewa, lakini niseme tuko committed kwa sababu ule usanifu umefanyika na kwa maana hiyo, hata katika bajeti inayokuja, Mheshimiwa Mbunge tumetenga fedha kwa ajili ya kuboresha eneo hili.
Mheshimiwa Spika, niahidi tu kwamba baada ya Bunge nitatembelea eneo hili. Sijapata fursa ya kutembelea maeneo haya ili Mheshimiwa Mbunge tuweze kushauriana vizuri, na mimi nijionee mwenyewe namna gani tunaweza kusukuma kwa haraka ili barabara hii iweze kupitika.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza napenda nipongeze majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na kazi inayofanywa na Wizara hii ya Nishati katika kuwapatia umeme Watanzania. Hata hivyo, nina maswali madogo mawili:
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; pamoja na jitihada hizi kuna vijiji 10 vimesahaulika, Vijiji hivi ni kama Mwamigongwa, Rwangwe, Ilumya, Igabulilo, Mwamalole, Mwabayanda, tayari tulishaongea na Wizara kwamba kuna vijiji ambavyo katika mzunguko huu vimerudiwa kutajwa majina tena, tukasema wafanye substitution; Je, Wizara inalifanyaje suala hili ili kusudi vijiji hivi ambavyo vimerudiwa visirudiwe tena na ambavyo havina umeme viweze kupatiwa umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa umeme unasambazwa na moja ya agizo ni kwamba Taasisi za Serikali ziweze kupata umeme huu ikiwemo zahanati, shule na kadhalika na kuna baadhi ya maeneo ambayo umeme hu unasambazwa kwa mitaa michache. Je, nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba umeme unasambazwa kulingana na mahitaji ya watumiaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa. Kwanza nimpongeze sana kwa kazi nzuri ya kufuatilia miradi ya nishati katika Jimbo lake, lakini la pili amevitaja vijiji kumi ambavyo kwa maelezo yake vimesahaulika na ameunganisha hapo na vijiji ambavyo vimetajwa kwenye REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza ambapo inaonekana vina miundombinu ya umeme.
Mheshimiwa Spika, msimamo wetu wa Wizara ni kwamba vijiji vyote vyenye miundombinu ya umeme ambavyo vipo kwenye Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza vifanyiwe marekebisho na vijiji ambavyo havina miundombinu ya umeme. Kwa kuwa, amevitaja vijiji vyake kumi na kwa kuwa ameshafanya mawasiliano na Wizara na REA kwamba nia ya mradi huu wa Awamu ya Tatu ni kupeleka umeme kwenye maeneo ambayo hakuna miundombinu. Kwa hiyo, nataka niwaelekeze REA kwamba wafanye substitution kwa sababu ni jambo la kawaida na tumekuwa tukifanya katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ametaka tamko la Serikali juu ya maeneo ya Taasisi za Umma, ni kweli tumetoa tamko, tulitazama upungufu wa REA awamu zilizopita kwamba Taasisi nyingi za umma ikiwemo miradi ya maji, ikiwemo zahanati, vituo vya afya zilirukwa. Kwa hiyo, mradi wa REA Awamu ya Tatu tuliona tusirejee changamoto za REA awamu zilizopita.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naendelea kusisitiza agizo la Wizara na Serikali kwamba maeneo ya Taasisi za Umma yapatiwe vipaumbele katika kupeleka miundombinu ya umeme. Naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hili la Busega na maeneo yote kwamba hilo ndiyo tamko la Serikali ya Awamu ya Tano. Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa lengo la Serikali ni kumuwezesha mkulima huyu wa pamba ili aweze kupata thamani ya pamba yake na kwa kuwa pamba hii imekuwa na gharama kubwa sana kwa mkulima kutokana na bidhaa ya pamba inayoingizwa kutoka nje. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka zuio la makusudi ili pamba inayozalishwa hapa nchini itumike kuzalisha bidhaa za pamba hapa nchini?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezekano huo upo kama mazingira ya matumizi ya pamba hapa ndani yatakuwa mazuri yanayoweza kutumia pamba yote inayozalishwa hapa nchini. Kwa sasa hivi uwezo wa kutumia pamba yote tunayozalisha hapa nchini ni mdogo na kwa hiyo wafanyabiashara wanalazimika kupeleka hii pamba nje ya nchi, ndiyo maana sasa hivi tunafanya jitihada kubwa kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda kuhakikisha kwamba viwanda vya kutengeneza nguo, viwanda vya kutengeneza bidhaa za pamba vinajengwa hapa nchini ili soko la ndani liwe kubwa kuliko soko la nje kwa bidhaa zinazotokana na pamba.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, katika majibu yake amekiri tatizo la tembo linazidi kuongezeka na wananchi wengi sana wanapata madhara makubwa na wanaathirika sana na tatizo hili. Wananchi wa vijiji husika wakiwemo vya Matongo, Mwauchumu, Longalombogo na maeneo mbalimbali hapa nchini wameathirika sana. Nataka tu kujua Serikali sasa inachukua hatua gani za kimkakati, tuache hizi hadithi za kwamba tutafanya, tuko mbioni, ni lini tatizo hizi sasa tutalipatia ufumbuzi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Kikosi dhidi ya Ujangili kimeshajenga kituo pale Lukungu na kituo hiki maana yake ni kusaidia kufukuza wanyama waharibifu wakiwemo viboko. Je, ni lini kituo hiki cha Lukungu kitaanza kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Chegeni. Kwanza kabla sijajibu, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia na hii ni mara ya tatu kuliuliza hili swali, hii inaonesha kwamba hili swali ni muhimu sana katika eneo la Jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema kwenye jibu la msingi kwamba katika maeneo yote haya ambayo kuna matatizo sasa hivi tutachukua hatua za dhati kuanzia tarehe 1 Julai, 2018 wakati bajeti mpya itakapoanza kutekelezwa. Tumejipanga sawasawa kuhakikisha kwamba haya yote tutayatatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu hiki Kituo cha Kupambana na Ujangili (KDU) kwanza kama alivyosema mwenyewe tayari majengo yameshakamilika, tunachosubiri hivi sasa ni kuhakikisha kwamba rasilimali watu pamoja na vifaa vya kutendeakazi vinakamilika ili kusudi kile kituo kianze kufanya kazi katika mwaka wa fedha unaokuja.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Zoezi la uvuvi haramu limetekelezwa sivyo ndivyo katika maeneo mengi sana na wavuvi wengi sana wamepata hasara kubwa sana kutokana na zoezi hili. Zoezi hili limefanywa na wafanyakazi ambao kwa kweli hawakuzingatia maadili na hata kanuni za kazi zao. Ilifikia mahali Mheshimiwa Waziri akasema kwamba yeye hana wapiga kura wavuvi hao wenye wapiga kura wavuvi mtajijua wenyewe. Nataka kujua kauli ya Serikali, wavuvi ambao wameingizwa hasara kubwa sana watalipwa fidia kiasi gani na lini fidia hiyo italipwa?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, suala la uvuvi haramu tumeeleza mara kwa mara hapa Bungeni na jinsi ambavyo linaendeshwa. Waheshimiwa Wabunge tumewaomba mara kwa mara kwamba kama kuna mtu ambaye ameonewa katika eneo lolote lile tuletewe ili sisi tuweze kuchukua hatua. Leo ni miezi sita Wizara yangu inasisitiza suala la watu walioonewa kuwasilisha malalamiko yao ili waliohusika waweze kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo Wizara yangu haiwezi kujua ni kitongoji, kijiji na kata gani, ni lini, Mkaguzi nani na alifanya makosa yapi kwa sababu hatua za ukamataji zipo. Sasa ikiendelea kuzungumzwa hivi kila siku kwamba watu wameonewa, halafu ushahidi hupewi, Waziri huwezi kuwa kwenye nafasi ya kuchukua hatua.
Mheshimiwa Spika, hili Bunge ndiyo linalotunga sheria, kwa nini Waziri alaumiwe na kuandamwa kwa kuchukua hatua za watu ambao wamevunja sheria? Nataka niseme kwamba wananchi na watu wote wataendelea kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria tulizonazo leo na kwa mujibu wa Katiba tuliyonayo sasa, watakaguliwa mahali popote na wakibainika watachukuliwa hatua. Watu wote wanaojihusisha na uvuvi haramu bila kujali vyeo vyao, wataendelea kuchukuliwa hatua mahali popote walipo kwa mujibu wa sheria tulizonazo.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inasisitiza kama kuna mtu yeyote ambaye ana ushahidi dhidi ya manyanyaso au uonevu wa aina yoyote umefanywa na Afisa wangu siku hiyo hiyo hatua zitachukuliwa.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyiongeza.
Mheshimiwa Spika, ajira kubwa sana ipo kwenye sekta ya kilimo na uvuvi na Tanzania tumejaliwa kuwa na rasilimali hii ya ziwa pamoja na bahari lakini majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naona amajielekeza kidogo kutokujibu swali la msingi la Mheshimiwa Massaburi, ambaye yeye alitaka kujua pamoja na mafunzo yanayoendelea au mazungumzo yanayoendelea na EU nini mkakati wa Serikali kuongeza udahili wa hao wanafunzi? Maana yake 1,100 ni namba ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Wilaya ya Busega ni wadau wakubwa sana wa Ziwa Viktoria na zoezi la uvuvi haramu limeathiri sana vijana na hawana ajira. Nini mkakati wa Serikari wa kuwasaidia vijana hawa ambao sasa hawana ajira waweze kupata ajira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni juu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza udahili. Kama nilivyojibu katika swali letu la msingi tumehakikisha tunaimarisha vyuo vyetu vilivyo chini ya Wakala huu wa Uvuvi kwa maana ya FETA vile vya Gabimori na kule Mwanza, Mtwara na Kigoma. Kwa hivyo, kazi kubwa tuliyonayo katika mwaka huu wa fedha ni pamoja na kwenda na mpango wetu wa kushirikiana na wenzetu wa European Union ili mradi tuweze kuongeza uwezo wa kitaasisi ambao utapelekea kuendelea kuongeza idadi ya wanafunzi katika vyuo vyetu lakini kuwa na uwezo wa kitaaluma na kiteknolojia pia. Kwa hivyo, Mheshimiwa Mbunge ahakikishe tu kwamba wanafunzi au vijana waliopo katika Jimbo lake wawe tayari na wao kuweza kuingia katika vyuo hivi hasa kwa yeye palepale Mwanza Nyegezi ambapo watapata elimu hii na kule Rorya vilevile.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni mkakati gani tuliona kama Serikali, baada ya kuendesha Opesheni Uvuvi Haramu na vijana wengi kuwa wamekosa ajira tunawasaidiaje ili waweze kurudi katika ajira yao. Mkakati wetu Mkuu ambao umeelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 25 mpaka ya 27 ni kuhakikisha kwamba tunawaunganisha vijana hawa katika vikundi vya ushirika na kazi hii tumeshaianza.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati njema sana tunashirikiana vyema na Shirika letu la Umma la Hifadhi ya Jamii ya NSSF, tunao mpango unaoitwa Wavuvi Scheme. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Chegeni kwamba niko tayari kwenda kutoa elimu hii na wataalam wangu pale Busega ili vijana wa pale Busega wajiunge katika ushirika, kisha waweze kupata faida ya kuweza kupata mikopo na faida zingine zinazotokana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa vile sasa kuna mgogoro mwingine umeanza kuzuka kati ya wananchi na wanyama waharibifu kama tembo na viboko. Je, Serikali inasaidiaje wananchi ambao wanaishi kando kando ya hifadhi hizi pamoja na ziwa kuepukana na mgogoro huu ambapo sasa tembo wanajeruhi watu na kuharibu mali za watu pamoja na kuuwa watu lakini viboko wanafanya uharibifu mkubwa sana wa mazao ya wananchi. Serikali ina mpango gani sasa kuwasaidia wananchi hawa kuondokana na mgogoro huu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kumekuwa na changamoto ya wanyama wakali na waharibifu katika maeneo mengi nchini lakini Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba inawaelimisha wananchi ipasavyo kuhakikisha kwamba wanakabiliana na hao wanyamapori pamoja na kuweka maafisa katika kila wilaya kuhakikisha kwamba wanashirikiana na wananchi na wale wa vijiji kuhakikisha kwamba wanawadhibiti hao wanyama wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa kutumia Kikosi chetu cha Kupambana na Ujangili (KDU) na katika maeneo yale ambayo imeoneka kwamba wanyama wale wamezidi tumekuwa tukichukua hatua za kufungua kituo katika hilo eneo ili kuhakikisha askari wetu wanakuwepo hapo kwa muda mrefu na ili kuwadhibiti hao wanyama wakali na waharibifu. Kwa hiyo, naomba tu tuendelee kushirikiana tuhakikishe kwamba tunapambana na hao wanyama wakali na waharibifu.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekuwa kwa kweli na jitihada kubwa sana ya kushughulikia suala la maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini; na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri anajua kabisa kwamba rambo la Rutubiga ambalo lilichimbwa kupitia DASP ikatumia milioni zaidi ya 300 na halikufanya kazi mpaka leo hii.
Je, Mheshimiwa Waziri pamoja na rambo la Rutubiga, rambo la Rwangwe Shigara, Kijereshi na Nyaruhande?
Je, una mkakati gani wa kuhakikisha kwamba malambo haya yanafanya kazi na kuwapatia wananchi maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikwambie nimefanya utafiti wa kutosha na nimejiridhisha, Bwawa la Rutubiga lilipasuka wakati wanajenga lile tuta kwa sababu ya ukosefu wa maji kiangazi walifanya kitu kinaitwa dry compaction kwa jina la kitaalam walishindilia udongo bila kuuwekea maji. Ndiyo maana maji yalivyofika ikawa ni rahisi kupasuka, lakini wao wakasingizia kwamba kuna ndege alitoboa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sasa Mheshimiwa Mbunge tumejianda vizuri kabisa, tunatafuta teknolojia kwanza ya kuhakikisha kwamba mabwawa yote yaliyojaa mchanga, mchanga ule unatoka bila kutumia gharama kubwa. Lakini pia tutahakikisha tunajenga mabwawa mengi kwa kadri jinsi ambavyo itawezekana na kulingana na uwezo wa fedha.
Kwa hiyo, hata hayo uliyoyataja Mheshimiwa Mbunge na kwenye eneo lako kuna mabwawa mengi sana yaliyojengwa tutahakikisha tunayajenga.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami napenda tu kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa halmashauri nyingi kwa sasa hivi ziko taabani, kwa maana kwamba kimapato nyingi zinasuasua; na kwa kuwa Serikali imeendelea kuchukua baadhi ya vyanzo vingi vya halmashauri na hivyo kufanya halmashauri hizi kushindwa kufanya kazi na kutekeleza majukumu yake kama ilivyotakiwa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaamini kwamba kwa mwenendo huu unazidi kuuwa ile dhana ya kugatua madaraka ya D-by-D?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Chegeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza jukumu la msingi kubwa la Serikali ni kusimamia maendeleo ya wananchi wake wote kwa usawa. Kuna baadhi ya halmashauri unaweza ukakuta katika maeneo yao kuna vyanzo ambavyo vinaweza vikawa vinawapatia mapato ambayo kimsingi yakikusanywa kwa asilimia 80 hadi asilimia 100 yanaweza yakatoa mchango mkubwa sana katika pato la Taifa ili kuweza kuligawanya na halmashauri nyingine ambazo zina matatizo ziweze kupata japo kidogo. Kwa hiyo, huo ndiyo msingi wa baadhi ya kodi kuweza kuchukuliwa kukusanywa na TRA ili kusudi ule mgawanyo wa mapato kitaifa uweze kuwa mzuri zaidi kwa halmashauri zote au kwa maeneo yote, hilo ndio jambo la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na changamoto ambazo zipo katika halmashauri jambo la kwanza ambalo tumewashauri na Kamati ya Bunge imetoa ushauri ndani ya Bunge hili ni kwamba, kila halmashauri wakae chini katika vikao vyao vya mabaraza watathmini vyanzo vya mapato walivyonavyo kwa sababu halmashauri nyingi tu vipo vyanzo vya mapato ambavyo hawavikusanyi. Kwa hiyo, watathmini vyanzo vya mapato walivyonavyo na wanavyokusanya walete Mheshimiwa Waziri aweze kuwapitishia ili kusudi waweze kuongeza wigo wa mapato. Ahsante sana.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa swali zima limejikita kwenye mambo ya pembejeo; na kwa kuwa wakulima wengi sana wa mazao kama ya pamba, muhogo, chai na hata korosho, wamekumbwa na tatizo la wadudu waharibifu. Kwa mfano, wakulima wa pamba na wakulima wa mahindi wanasumbuliwa na yule fall armyworm wakulima wa muhogo wanasumbuliwa na cassava mealybug.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua ni nini mkakati wa Serikali kumwondolea adha mkulima ambaye anajitahidi kulima sana lakini anasumbuliwa na hawa wadudu au viwavijeshi ambao ni waharibifu zaidi? Nataka tamko la Serikali.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. American fall army worm wameonekana kwa mara ya kwanza nchini mwaka jana. Jitihada ya Serikali iliyofanyika ya kwanza ilikuwa ni kuhakikisha elimu inawafikia wakulima wote namna ya kukabiliana na hawa wadudu. Kwa hivyo, tulichokifanya ni kueneza hii elimu lakini na kufanya utafiti wa haraka kubaini ni aina gani ya dawa inayoweza kuuwa hawa wadudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa hiyo tumekwishaitangaza ili mwananchi akiona mazao yake yanashambuliwa atumie dawa hiyo kuuwa hawa wadudu. Tunafanya hivyohivyo na kwa visumbufu vingine vya mimea.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Je, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba Vyama vya Ushirika vimeshakufa muda mrefu na kwamba sasa wakulima wanalazimishwa wauze pamba kupitia Vyama vya Ushirika. Je, nini tamko la Serikali kuwasaidia wakulima wa pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama nilivyosema ni kwamba tumeamua kufanya total transformation kwenye Vyama vya Ushirika ili tuweze kuimarisha na kuboresha. Kwa maana hiyo, Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba wakulima wote kupitia Vyama vya Ushirika tutakuwa tunahakikisha wanapouza mazao yao wanalipwa pesa zao pale pale bila kungoja kupitia kule Benki. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, kwa kuwa msingi wa swali ni kuhamishwa kwa mipaka ambayo imesababisha mpaka na wanyama wamechanganyikiwa, matokeo yake wanyama sasa wanavamia makazi ya wananchi na hasa wanyama waharibifu kama tembo na viboko: Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba maeneo kama ya Vijereshi, Longalombogo na maeneo mengine ambayo yanaathiriwa na tembo kuongezeka kuja katika makazi ya wananchi yatadhibitiwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kimsingi sisi tunapokwenda kuweka mipaka tunafuata GN. Kwa sababu wananchi katika maeneo mengi walikuwa wanatambua mipaka yao kwa alama za asili, ndiyo wamekuwa wakifikiri kwamba tunaingia kwenye maeneo ya vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetambua maeneo mengi yenye migogoro na Wizara yetu sasa baada ya kumaliza zoezi la kuweka vigingi, inapitia upya kuangalia ni kwa namna gani migogoro hii itaisha? Kwa hiyo, tutafika Kijereshi na Longalombogo ili kwenda kuangalia ni kwa kiwango gani tunaweza tukatengeneza mipaka ili kuhakikisha kwamba wanyama hawa hawaleti tena madhara kwa wananchi.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba na mimi awaelekeze TARURA ili washughulikie barabara ya kutoka Shigara kwenda Ruangwe. Kijiji cha Ruangwe ni Kisiwa katika Wilaya ya Busega. Naomba maelekezo ya Waziri yaende kwa TARURA vilevile.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niwaelekeze TARURA katika Wilaya ya Busega, watembelee maeneo yaliyotajwa na Mheshimiwa Mbunge Chegeni na wapate majibu ya kero hiyo ambayo ameitaja hapa Bungeni. Ahsante.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii ya Uwekezaji kwa majibu mazuri na ya kina. Pamoja na majibu haya nina maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza; kwa kuwa Watanzania wana hamu kubwa sana ya kuingia kwenye uchumi wa viwanda kama ambavyo kauli ya Mheshimiwa Rais ambayo siku zote amekuwa akiisema na kwa kuwa Wizara hii iko chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nini kauli ya Serikali ya kuleta mabadiliko ya haraka na ghafla yaani radical change yatakayowezesha kutekeleza mapendekezo ya Blueprint ambayo amezungumza hapa na mikakati mingine ya kuharakisha uwekezaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wako baadhi ya wawekezaji wa ndani na nje ambao wamekuwa wakizunguka ofisi baada ya ofisi nyingine wakitafuta vibali mbalimbali vya uwekezaji, kitu ambacho kimekuwa kikichafua sana nchi hii kwa sababu wanaposhindwa kupata vibali hivi kwa muda wanahama kwenda nchi zingine na hii inakuwa haileti dalili njema kwa nchi yetu. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kipindi hiki cha Bunge la Bajeti awaite wawekezaji wote ambao wana kero mbalimbali, akutane nao pamoja na Mawaziri wengine wote ili kuhakikisha kwamba matatizo yao yanatatuliwa mara moja? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chegeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kuhusiana na tunatoa kauli gani ya kuleta mabadiliko ya haraka au kama alivyoeleza mwenyewe radical change, nipende kusema kwamba ni kweli ili tuhakikishe kwamba tunapata faida ya uwekezaji na biashara nchini, ni lazima mabadiliko ya kina yaweze kufanyika. Tayari kama nilivyoeleza kwenye majibu ya msingi Serikali imeanza kuchukua hatua kupitia maboresho mbalimbali na kama alivyoeleza mwenyewe mpango mzuri wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, tumeandaa pia mpango jumuishi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango kazi huu wa kuboresha mazingira ya biashara. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango huu utatekelezwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mpango kazi huo jumuishi tumeeleza kabisa ni masuala gani ambayo yanatakiwa kufayiwa kazi na Wizara ipi pamoja na taasisi zipi za kisekta na tutaendelea kuwafuatilia pia kwa mujibu wa road map ya utekelezaji wa mpango huo kwa namna tulivyojipangia. Pia tutaleta mpango huo kazi tutakapokuwa tayari ili na Waheshimiwa Wabunge waweze kuuona na kuweza kufuatilia na kuweza kujua ni hatua gani tumefikia katika utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili kama nitakuwa tayari kufanya kikao katika kipindi hiki cha Bunge kuwaita wawekezaji wote wenye kero mbalimbali. Kwanza nipende kusema ni ushauri mzuri, lakini la pili tayari tumeanza, nimejigawia vipaumbele, moja tumeanza na mikoa mbalimbali na tunaendelea kufanya hivyo kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa.

Pili, kwa kushirikiana na Mawaziri mbalimbali wa kisekta tutaendelea kufanya vikao mbalimbali vya kisekta kwa wawekezaji na wafanyabiashara ili kuhakikisha kwamba tunatatua kero zao mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Mbunge ni shuhuda tulipoenda Rungwe kupitia kampuni ile ya Rungwe Avocado pamoja na bwana Robert Clowes ambaye tulienda kuangalia na kutatua mgogoro ule kwenye sekta ile ya kilimo cha maparachichi.

Nimshukuru sana kwa ushirikiano ambao aliutoa kipindi hicho na naamini mgogoro ule sasa utafika sehemu nzuri na utaweza kumalizika. Pia nimhakikishie na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote na naomba pia ushirikiano wao wa dhati, endapo kuna mgogoro maalum kwa mwekezaji ambaye anamfahamu au katika Jimbo lake analoliongoza au mkoa wake, basi wasisite kunipa taarifa kwa sababu nimeteuliwa kwa kazi hiyo maalum na niko tayari kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, pamoja na mikoa, pamoja na sekta mbalimbali, ili kuweza kuhakikisha kwamba taswira yetu kama nchi katika uwekezaji tunaendelea kuikuza, wiki ijayo kuanzia tarehe 17 nitakuwa na kikao na wawekezaji wote wa kichina na tutaendelea kufanya hivyo na wawekezaji wa Uturuki, wa Marekani, Uingereza na nchi zingine kwa mujibu wa viwango vile vya nchi 10 zinazoongoza katika kuvutia mitaji nchini kwetu, lakini tutahakikisha pia na nchi zingine tutazingatia. Kwa hiyo nimshukuru Mheshimiwa Mbunge, lakini nitaomba ushirikiano wa Waheshimiwa Wabunge wa dhati. Ahsante.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri sambamba na matatizo ya Lushoto, Wilaya ya Busega haikupata mgao wa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma. Je Mheshimiwa Naibu Waziri, unaweza ukatoa maelekezo katika mgao huu na Wilaya ya Busega tupate mgao huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge wa Busega swali lake la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natambua kazi nzuri ambayo anaifanya katika Jimbo lake la Busega kuwasemea wananchi wake lakini sina hakika kwa sababu fedha zile zilisambazwa kwenye wilaya zote kwa maana ya Halmashauri inawezekana kwenye Jimbo hilo kuna bahati mbaya. Naomba tuwasiliane baada ya kipindi cha maswali na majibu tuone njia bora ya kumaliza shida hiyo. Ni nia ya Serikali kila Jimbo lipate mgao wa kupunguza shida ya maboma na kuchangia nguvu za wananchi ili wasilalamike.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda tu kumkumbusha kwamba Mheshimiwa Rais aliahidi barabara ya kutoka Dutwa Jimboni kwa Mheshimiwa Mwenyekiti kuja Ngasamo kuja mpaka Nyashimo iwekwe kwa kiwango cha lami na maandalizi yameshaanza kidogo kidogo. Nataka tu nipate comfort ya Serikali, ni lini sasa utekelezaji halisi wa barabara hii utaanza kwa ajili ya kuweka lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chegeni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Chegeni nafahamu barabara hii tumeizungumza sana, ni barabara muhimu na hatua kama alivyosema mwenyewe kwamba ziko hatua kwenye ujenzi wa barabara hii tumeshazifikia. Kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Chegeni kwamba tunaendelea kuhakikisha kwamba kila tukipata fedha barabara hii tunaijenga ili tuweze kuikamilisha barabara hii muhimu. Kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Chegeni na wananchi wa maeneo yote ya Dutwa na Simiyu kwa ujumla kwamba tunawaunganisha vizuri katika maeneo yao.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara na pamoja na jitihada nzuri za Serikali ya Awamu ya Tano ya kufufua viwanda, tayari kuna mpango ambao Serikali kupitia Mifuko ya Jamii inataka kufufua viwanda vya Ngasamo, na Nasa. Viwanda hivi viko katika Wilaya ya Busega na ni viwanda ambavyo vinatoa huduma nzuri sana kwa wakulima wa pamba. Nilitaka kujua tu ni lini Serikali sasa maana wanasema wanategemea, ni lini tutarajie kwamba kiwanda kama cha Ngasamo na kiwanda Nasa vitaanza kufanya kazi kuwahudumia wakulima wa pamba katika Wilaya ya Busega. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, sijui kama nitakuwa na majibu mazuri zaidi sana ya yale ambayo amesema Mheshimiwa Waziri wangu. Kimsingi niseme tu zao la pamba ni kati ya mazao ya kimkakati na ni zao ambalo linategemewa sana ikizingatiwa kwamba pale ambapo kunakuwa na uchakataji wa pamba katika hatua yoyote ile iwe ni kwenye pamba mwanzoni au kwenye utengenezaji wa nguo, ajira zinazotokea hapo ni nyingi sana. Kwa mfano kwenye kiwanda kama cha A to Z nilichokitembelea juzi unakuta kwamba ni watu zaidi ya 8,000 wameajiriwa pale kwa hiyo Serikali inaona umuhimu wa kuhakikisha kwamba viwanda hivi vinafanya kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hatua tulizonazo pamoja na ambazo amezieleza vizuri sana Mheshimiwa Waziri, tumekuwa tukikutana na wataalam wa aina mbalimbali lakini pia wataalam wetu kama TILDO wamekuwa wakienda kushirikiana katika kufuatilia wadau ambao tunaweza tukashirikiana nao. Hivi juzi tu tulikuwa na wataalam kutoka Korea na tunafikiria kwamba katika maeneo yote ambayo yanalima pamba, hizo ginneries pamoja na viwanda vya pamba katika kipindi hiki tunachoendelea nacho tuweze kuhakikisha kwamba angalau tunapata kiwanda kimoja kikubwa. Ahsante.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji naomba nijikite kwenye suala la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela kuhusiana na suala la pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli mnyororo wa thamani katika suala la pamba cotton to cloth unapaswa kufanyiwa mkakati mahsusi kwa kumwezesha mkulima aweze kupata thamani ya kile anachokifanya, lakini swali langu ni kwamba wakulima wa pamba ambao mwaka hadi mwaka wamekuwa wakifanya kazi ya kulima pamba wanakuwa wanapata hasara; kwa mfano leo hii wakulima wa Mkoa wa Simiyu na hasa Wilaya ya Busega wameuza pamba toka mwezi wa Tano mpaka leo hawajalipwa fedha yao? Sasa Mheshimiwa Waziri haoni kwamba hii ni ku-discourage wakulima wasiweze kufanya kilimo kizuri zaidi na nini tamko la Serikali juu ya hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Chegeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba baadhi ya wakulima wa pamba hawajalipwa fedha zao, pamba mwaka huu mpaka sasa hivi jumla ya bilioni mia nne kumi na saba zimeshalipwa kwa wakulima wa nchi nzima. Wakulima ambao hawajalipwa wanadai bilioni hamsini kufikia sasa hivi na sababu ya msingi ni nini? Ni kwa sababu lazima tufahamu kwamba pamba asilimia zaidi ya 80 inakwenda nje ya nchi, wanunuzi wetu wanakabiliwa na mtikisiko wa bei ambao umewakabili katika soko la dunia na sisi kama nchi tulitoa maelekezo ya bei ya kununulia kama Serikali. Haya yalikuwa maamuzi ya Serikali kwa ajili ya kumlinda mkulima asipate hasara, lakini Serikali imefanya intervention kuongea na financial institutions zote na kuweza kuwasaidia namna gani ya kupunguza interests kwa wanunuzi ili waweze kwenda sokoni kununua bei ya pamba kwa Sh.1,200.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, siku ya tarehe 14 tutakutana na Kamati ya wanunuzi wote makampuni yote yanayonunua ili kuangalia flow ya fedha inavyokwenda, lakini pamba yote iliyokuwa kwa wakulima imeshakusanywa, sasa hivi kilichobaki mkononi mwao ni tani 5,000 tu, ambayo tunaamini mpaka mwisho wa mwezi huu itakuwa imekwishaondoka mikononi mwa wakulima na msimu unapoanza tarehe 15 tunaamini wakulima wote pamba yao itakuwa imeondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili la intervention ya bei Serikali tunajitahidi kupunguza gharama kuanzia msimu huu unaokuja na hatutoingilia kupanga bei, bei itakuwa determined na soko na sisi jukumu letu kama Serikali itakuwa kuhakikisha mkulima hatopata hasara. Tutatafuta njia zingine za kumlinda mkulima kuliko kumwathiri mnunuzi. Hii ndiyo hatua ambayo tunachukua kama Serikali. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri katika dhana nzima ya uchumi kukua ukioanisha na maisha ya wananchi, kinadharia kwa kweli alivyosema ni sahihi kabisa na napenda nipongeze kwa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imekuwa ikifanya kazi sasa kurekebisha na kurahisisha maisha ya wananchi yaweze kuwa na unafuu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza; uhalisia wa maisha sasa hivi kwa wananchi ni ghali zaidi na hali ya maisha ya wananchi bado ni ngumu. Je, Serikali inaweka mkakati gani pamoja na kuonesha kwamba hata mkulima wa pamba ambaye anauza pamba yake anakopwa halipwi na bado anategemea ahudumie baadhi ya gharama zake mwenyewe, je, ni lini Serikali sasa itaachana na mtindo huu kwa kutoa guarantee kwa wakulima wa mazao yote ili waweze kuwa wanapewa bei ambazo zinawakomboa katika shughuli zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; sasa hivi bei ya vyakula inazidi kupanda na ukiangalia wananchi wengi wanaathirika na kupanda kwa bei ya vyakula. Gunia la mahindi sasa ni karibu Sh.100,000, je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza gharama hizi za maisha kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Chegeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, dhana ya kupanda bei, kushuka bei ni relative. Ni Bunge hilihili mwaka jana wakati bei ya mahindi kwa mkulima ilikuwa Sh.150, ni Wabunge hawahawa walilalamika na kusema kwamba kwa nini tunafunga mipaka. Sisi kama Serikali kupunguza gharama za bei sokoni hatua tunazochukua; moja ni kupunguza gharama za uzalishaji, mbili kuruhusu soko ku-compete, competition ndiyo itakayopunguza bei ya mazao sokoni. Pale ambapo mkulima anapata hasara hakuna mtu anayekwenda kum- subsidize. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kama Serikali hatua ya kwanza hatutaingilia bei kushusha, nini tunafanya; tunayo National Food Reserve Agency na nitumie Bunge hili kuwaambia Waheshimiwa Wabunge na Wakuu wa Mikoa; pale ambapo wanaona kwamba kuna upungufu wa mazao ya chakula sokoni wawasiliane na National Food Reserve Agency ambayo ita-supply chakula katika maeneo hayo ili kupunguza presha, lakini hatutaingilia kupunguza bei ya mazao kwa sababu wakulima wa nchi hii kwa muda mrefu wamepata hasara kwa kuwafanyia control mazao yao. Huu ni msimamo wa Serikali na ieleweke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, njia ya pili, tunahamasisha Watanzania, ardhi ya Tanzania ni potential kwa kilimo, watu wafanye jitihada kuongeza uzalishaji. Supply ikiwa kubwa, demand ikiwa ndogo mazao yatashuka bei, lakini hatutafanya intervention yoyote kwenda kupunguza bei. Njia pekee tunayofanya kama Serikali ni kutumia National Food Reserve Agency kwa ajili ya ku-supply mazao ya chakula sokoni na kupitia NFRA bei itapungua, lakini kusema bei ya chakula iko juu ni relative; ni saa ngapi bei ya chakula iko chini, ni saa ngapi bei ya chakula iko juu. Kitu cha muhimu ni kufanya jitihada kama nchi kuongeza purchasing power ya watu wetu na wakulima wetu waweze kufaidika. (Makofi)

SPIKA: Lile la pamba?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Spika, tatizo la pamba lililojitokeza mwaka huu ni special case. Ni kama ilivyojitokeza kwenye korosho mwaka jana; Serikali ilifanya intervention. Intervention tulizozifanya mwaka jana, mwaka huu hatukuzitumia, tumeruhusu soko, minada inaendelea, wakulima wanapata pesa yao on time na competition iko wazi.

Mheshimiwa Spika, tatizo la pamba lilijitokeza katika msimu uliopita niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, halitajitokeza msimu ujao, tutaruhusu soko, hatutafanya kutangaza control ya price, Serikali itakachokifanya kwa wakulima wa pamba wasipate hasara ni ku-control gharama za input kuanzia viuatilifu, mbegu na mambo mengine, lakini siku ya mwisho sokoni tutaruhusu bei ili wafanyabiashara waende wakutane na wakulima sokoni waweze kununua bidhaa ile na mtu apate pesa yake kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, hii ilikuwa ni special case kwa sababu bei ya pamba duniani imeanguka na sababu ya kuanguka ni kwa sababu ya mtikisiko na mgogoro uliopo kati ya China na Marekani, matokeo yake pamba imekosa bei. Serikali ikaamua kutangaza bei ya Sh.1,200 na ili wafanyabiashara wasipate hasara tukaamua kufanya mazungumzo na financial institution kuwapa incentive ili waweze kwenda kununua kwa bei ya Sh.1,200.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa wakulima wa pamba mpaka kufikia siku ya Ijumaa wamelipwa bilioni 437, ambacho hakijalipwa ni bilioni 43 tu ndizo ambazo hazijalipwa na sisi tunafanya jitihada kuhakikisha by the end of this month wakulima wa pamba waweze kulipwa fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatua ya pili ili wasipate shida kwa sababu msimu unaanza tarehe 15, nitumie nafasi hii kuwaambia wasambazaji wa mbegu wote wawasambazie wakulima bila kuwauzia halafu tuta-recover gharama ya mbegu msimu utakaokuja. Sasa hivi wakulima waende shambani kwa sababu malipo yalichelewa, lakini wapo ambao hawajalipwa, kwa hiyo wapewe mbegu.

Mheshimiwa Spika, namwelewa Mheshimiwa Dkt. Chegeni, moja ya wilaya ambazo zimeathirika sana ni Wilaya ya Mheshimiwa Dkt. Chegeni, lakini tatizo hili halitajiruudia msimu ujao. Nashukuru.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri yanatia matumaini mazuri. Napenda kufahamu mradi wa maji wa kutoka Bukabile katika Wilaya ya Busega kwenda katika Wilaya za Bariadi Itilima, Meatu na Maswa ni lini mradi huu utaanza kutelezwa, licha kwamba fedha zilishapatikana na mpaka sasa hivi tuliambiwa mwezi wa tisa tutasaini mkataba lakini mpaka sasa hivi hatujasaini mkataba wowote. Nataka kujua ni lini mradi huu sasa utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji napenda kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi kubwa sana. Lakini pia napenda nimfahamishe kwamba mkataba tumekwisha kusaini mradi ule na nikuombe Mheshimiwa Mbunge kutokana na kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Waziri ambayo ameitupia jicho katika Mkoa ule wa Simiyu ni kuombe tuweze kukutana tuweze kupeana update lini tutaweza kuutekeleza ili wananchi wako waweze kupata huduma ya maji. Ahsante sana.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba tu kupata ufafanuzi wa Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na majibu yake mazuri. Tatizo la barabara la Dutwa – Imalamate – Ngasamo kwenda mpaka Nyashimo lilikuwa kwenye ahadi ya Mheshimiwa Rais na huu ni mwaka wa nne kwamba iwe kwa kiwango cha lami.

Nilitaka tu kujua, ni lini sasa barabara hii itawekewa lami kulingana na ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amefuatilia sana hii barabara, kwa hiyo hata nikikutana naye nje huwa namwita Mzee wa Nyashimo kwa maana ya umuhimu wa barabara hii. Nafahamu pia Mheshimiwa Chenge anaizungumza sana barabara hii, lakini nafahamu pia kwamba iko ahadi ya Mheshimiwa Rais. Niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Chegeni kwamba ahadi zote za viongozi tunaendelea kuzitekeleza, kadri tunavyopata fedha tutatekeleza ahadi za viongozi.

Kwa hiyo, ahadi ni deni na usiwe na wasiwasi na mimi naifuatilia sana barabara hii kwa umuhimu wake ili tuweze sasa kwenda kwenye kujenga katika kiwango cha lami, tukipata fedha tutakwenda kujenga barabara hii.