Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Edwin Mgante Sannda (25 total)

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa matatizo yanayoikumba Mafinga yanafanana kabisa na yale yanayoikumba Hospitali ya Mji wa Kondoa kwa maana ya kwamba Kondoa inahudumia Halmashauri tatu za Kondoa Mjini, Kondoa Vijijini pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Chemba. Je, Serikali ina mpango gani na inafikiria nini katika kuongeza rasilimali fedha na rasilimali watu ili kukidhi mahitaji?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hospitali ya Kondoa demand yake imekuwa kubwa na kama nilivyosema awali ajenda yetu kubwa ni kuongeza rasilimali watu pale Kondoa. Concern ya kaka yangu Mheshimiwa Nkamia, Mbunge wa Chemba ni kujenga Hospitali ya Wilaya Chemba ili kupunguza population. Juzi juzi tulivyokuwa tunafungua Hospitali yetu ya Mkoa hapa, Mheshimiwa Nkamia alipeleka ombi maalum kwa Mfuko wa Bima ya Afya Taifa kuangalia uwezekano wa kujenga Hospitali ya Chemba ili kupunguza ile population.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika suala la rasilimali watu tutajitahidi kadri iwezekanavyo kwa huu mgao unaokuja tuangalie Hospitali ya Kondoa tunaisukuma vipi. Hali kadhalika katika suala la rasilimali fedha kama nilivyosema ukiachia hii bajeti ambayo tumeitenga ni lazima sasa twende tukasimamie makusanyo ya mapato kwa nguvu zote. Mifumo hii ya kielektroniki ikitumika vizuri katika sekta ya afya mafanikio yake ni makubwa sana na tutaondoa kero nyingi sana za wananchi katika kupata huduma za afya.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Kwa kuwa dhamira inaonekana ni dhahiri ni mchakato tu unaendelea, je, ni lini Serikali itatoa maagizo kamili kwa Wizara zake zote ili pale panapotakiwa ujenzi wowote mpya au uendelezaji wa majengo au miundombinu ya Ofisi zake ifanyike Dodoma badala ya kuendelea kufanyika Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, labda nianze kwa ufafanuzi kwamba tofauti na nchi nyingine, kwa mfano kama vile Rwanda ambapo Makao Makuu yalitamkwa kabisa kisheria, Tanzania hatukuwa na Sheria inayotamkwa kwamba Makao Makuu ni Dodoma. Kilichotokea ni kwamba Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu yenyewe ndio iliyoanzishwa kisheria.
Sasa sheria hii ndio itatoa kwamba itakuwa binding, itailazimisha Serikali kuhamisha Makao Makuu Dodoma; kwa maana hiyo basi kuharakisha mchakato wa uendelezaji wa Makao Makuu na baadaya kufanyika hivyo ina maana kila kitu kitakuwa kinafanyika Dodoma kwa mujibu wa sheria.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mazingira ya baadhi ya Halmashauri kuwa upya na changa kama ilivyo Halmashauri ya Mji wa Kondoa, vyanzo vya mapato ya ndani, huwa ni vidogo sana na hafifu; je, Serikali haioni umuhimu kupitia Wizara zake husika zenye dhamana kwa vijana na akina mama kuweka walau ruzuku fulani kufikia ukomo ili iweze kukidhi mahitaji ya vijana na akina mama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tumesema kwanza hii asilimia kumi siyo peke yake ndiyo inayowagusa vijana, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, kuna Mfuko wa Uwezeshaji wa Vijana, kwa hiyo, tunachokifanya na lengo mi kwamba vijana na kina mama weweze kupata fursa kutoka maeneo mbalimbali, ninajua Halmashauri nyingine ni changa kama ulivyosema Mheshimiwa kwenye Wilaya yako ya Kondoa, Serikali imejipanga ukiacha own souce ya ten percent, kuna Mfuko wa Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, hali kadhalika kwa mujibu wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, katika Ilani yake imezungumza kwamba kutakuwa na mgao wa shilingi milioni 50, lengo kubwa ni kwenda kusukuma nguvu zile za vijana na kina mama katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya shughuli za uchumi.
Kwa hiyo, nadhani kwamba mpango wa Serikali utaendelea kuboresha ili vijana na akina mama waweze kupata nguvu za kujenga uchumi katika nchi yao.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, kwa fursa. Wilaya ya Kondoa hususan pale Kata ya Kolo na nyinginezo, ipo michoro ya mapangoni ambayo ni vivutio vikubwa sana vya kihistoria kwa ajili ya utalii, lakini vimekuwa havitangazwi sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuvitangaza ili kizazi cha sasa na cha baadaye kitambue hii fursa na kuweza kuitumia ili hatimaye pia kipato kiongezeke?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, michoro ya kwenye mapango ya Kondoa ni mojawapo kati ya maeneo ya utalii wa kiutamaduni na utalii wa kihistoria ambao tayari unafahamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ambayo imebaki sasa hivi ni ya kuweza kuboresha matangazo kwa maana ya utangazaji wa utalii; na nimesema katika majibu yangu ya maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Kuchauka, kwamba tunachokifanya sasa hivi ni utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao unasisitiza juu ya diversification of tourist attractions, kwamba tunataka kuendelea kuboresha na kutanua wigo wa vivutio vya utalii ili tuondokane na vivutio vya utalii vinavyohusiana na wanyamapori peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, chini ya mpango huu, chini ya utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano, tunakwenda kutangaza zaidi vivutio ambavyo ni vipya; vimekuwepo lakini vimekuwa havitiliwi mkazo, lakini sasa tunakwenda kuvitilia mkazo kwa maana ya kwamba tutaboresha zaidi matangazo kwa ajili ya vivutio vya aina hiyo.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tunashukuru sana kwa kazi ya barabara inayoendelea kutoka Dodoma - Kondoa - Babati ingawa inakwenda kwa kasi ya kusuasua. Tatizo moja kubwa wakati wa ujenzi kuna alama na maelekezo mbalimbali yanayotakiwa yawepo wakati wa ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Barabara hii hizi alama zinapungua maeneo mengine hakuna kabisa, kwa hiyo, unakuta watu wanapotea kilomita kadhaa halafu ndiyo urudi tena. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi hawa waweke hizi alama ili kuondoa ajali na upotevu wa muda wa namna hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wote wa maeneo yote ya wakandarasi watatu wa kuanzia hapa Dodoma mpaka mwisho kabisa, wa CHICO, namuelekeza Regional Manager wa Dodoma asimamie kuhakikisha kwamba alama za barabarani zinazowaongoza wananchi wanaopita na magari yao ziwe zinawekwa na kusimamiwa muda wote zisiwe zinaondolewa ili wananchi wale wanaopita na magari yao wasipate shida ya kupoteapotea au kutumbukia kwenye mitaro. Namuelekeza atekeleze hilo na mimi mwenyewe nitafuatilia.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, kwa fursa. Wilaya ya Kondoa hususan pale Kata ya Kolo na nyinginezo, ipo michoro ya mapangoni ambayo ni vivutio vikubwa sana vya kihistoria kwa ajili ya utalii, lakini vimekuwa havitangazwi sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuvitangaza ili kizazi cha sasa na cha baadaye kitambue hii fursa na kuweza kuitumia ili hatimaye pia kipato kiongezeke?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, michoro ya kwenye mapango ya Kondoa ni mojawapo kati ya maeneo ya utalii wa kiutamaduni na utalii wa kihistoria ambao tayari unafahamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ambayo imebaki sasa hivi ni ya kuweza kuboresha matangazo kwa maana ya utangazaji wa utalii; na nimesema katika majibu yangu ya maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Kuchauka, kwamba tunachokifanya sasa hivi ni utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao unasisitiza juu ya diversification of tourist attractions, kwamba tunataka kuendelea kuboresha na kutanua wigo wa vivutio vya utalii ili tuondokane na vivutio vya utalii vinavyohusiana na wanyamapori peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, chini ya mpango huu, chini ya utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano, tunakwenda kutangaza zaidi vivutio ambavyo ni vipya; vimekuwepo lakini vimekuwa havitiliwi mkazo, lakini sasa tunakwenda kuvitilia mkazo kwa maana ya kwamba tutaboresha zaidi matangazo kwa ajili ya vivutio vya aina hiyo.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza; kama alivyoeleza Naibu Waziri mpaka sekondari elimu bure, lakini pia ukienda Chuo Kikuu kwa elimu ya juu tunayo mikopo ya wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kundi lililobaki ni kidato cha tano na cha sita. Kwa kuwa changamoto ya uwezo wa kugharamia elimu iko pia kwa wananchi hasa ambao nao wanakwenda kidato cha tano na cha sita ambapo imepelekea baadhi yetu nikiwemo mimi kuweka mpango mahsusi kwenye Majimbo yetu ya kuwalipia wanafunzi wanaofaulu kwenda kidato cha tano na cha sita; pamoja na changamoto ya uwezo wa Serikali; je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kulijumuisha kundi hili la kidato cha tano na cha sita kwenye Mpango wa Elimu Bure? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Swali la pili. Ili mpango wowote ufanikiwe, ni lazima kuwe na lengo na dhamira ya dhati ya kuhakikisha jambo hili linafanikiwa na kuwekewa mikakati. Kama tunavyozungumzia kwenye upande wa maji, tunasema mpaka 2020/2021 tuwe tumefikia asilimia 85 ya Watanzania wawe wanapata maji safi na salama; je, Serikali haioni umuhimu sasa kuweka muda mahususi kwa maana ya time frame na malengo lini tutaanza kutoa elimu bure kwa kidato cha tano na cha sita kama ilivyo kwenye maeneo mengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaingia kwenye maswali, naomba nikiri kwamba Mheshimiwa Sannda ni mmoja kati ya Wabunge wanaofuatilia sana masuala ya elimu. Pale Wizarani amezoeleka sana kiasi kwamba haulizwi tena kwamba anataka kuonana na nani? Kila siku utamkuta yupo mlangoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kama Serikali ina nia ya kuhakikisha kwamba hata kidato cha tano na sita nao wanapata mpango ule wa elimu bure, kwa sasa Serikali imeweka nguvu nyingi katika kukabiliana na changamoto ambazo zimejitokeza baada ya elimu bila malipo kuanza kutekelezwa, lakini baadae kadri fedha na uwezo utakapoimarika tutafikiria hata kwa elimu ya kidato cha tano na sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwamba kwa nini angalau tusiweke basi mpango wa muda mrefu; nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na kwamba haionekani kwenye mipango yetu kuhusu muda, lakini nia yetu kama Serikali ni kuhakikisha kwamba kadri uwezo unavyoongezeka kuendelea kutoa changamoto zinazowakabili wananchi kwenye Sekta ya Elimu na ikiwezekana huko mbele kadri uchumi wetu utakapoimarika kama nchi, hakuna shida hata mpaka Chuo Kikuu inaweza ikawa elimu bure kama ilivyo kwenye baadhi ya mataifa ya Ulaya.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika kuipunguzia mzigo Hospitali ya Halmashauri ya Mji, Kondoa ambayo inahudumia zaidi ya halmashauri tatu, zahanati za Kata mbili za Kolo pamoja na Kingale zimewekwa katika mpango wa kupandishwa hadhi na kuwa vituo vya afya. Je, ni lini sasa Serikali italeta hizo fedha kwa ajili ya kutekeleza hiyo awamu ya kuweka vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ME. JOSEPH G. KAKUNDA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Edwin Sannda, Mbunge Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Zahanati za Kolo na Kingale zikipandishwa hadhi zinaweza sana kupunguzia mzigo hospitali ya wilaya. Kama nilivyojibu swali la Mheshimiwa Dkt. Tulia, naomba awe karibu sana kimawasiliano, mwezi Agosti na Septemba ili tuone namna ya kuzipatia fedha zahanati hizi hatimaye ziweze kupandishwa hadhi na Wizara ya Afya ziwe vituo vya afya.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika jitihada za kuendelea kuinua ubora wa elimu suala la kuimarisha kitengo hiki cha udhibiti ubora ni suala ambalo kwa kweli halina mjadala. Hali ilivyo sasa hivi wale wenzetu pale ni kama wamevunjika moyo na wamekata tamaa kwa kukosa motisha.
Mheshimiwa Spika, je, ni lini sasa Serikali itawaweka hawa watumishi wa kitengo hiki kwenye viwango kama ilivyo maafisa elimu au walau waweze kupewa posho za madaraka kama zilivyo za Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Wataribu wa Elimu Kata? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua mbalimbali kujaribu kuboresha namna tunavyofanya udhibiti ubora. Kitu cha kwanza kikubwa ambacho kimefanyika ni kubadilisha mfumo wenyewe.
Mheshimiwa Spika, huko nyuma tulikuwa tunazungumzia kuhusu ukaguzi au tulikuwa tunawazungumzia wakaguzi wa shule, sasa hivi mfumo ule umebadilika tunasema ni udhibiti ubora. Mfumo ambao wanaohusika sio wale wadhibiti ubora tu lakini hata walimu wenyewe na wadau wengine kama wazazi kwa mfano kama kuna watu wanamiliki shule binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mfumo uliopo sasa ni mfumo ambao ni shirikishi; tunaamini mfumo huo utatusaidia kwa sababu kila mmoja wetu anahusika.
Mheshimiwa Spika, vilevile changamoto ambazo zipo kama nilivyosema kwenye jibu la msingi kwa mfano kama magari, vitendea kazi na idadi ya Wadhibiti Ubora wenyewe kama nilivyosema Serikali inaendelea kuboresha na kwa kuanzia nafikiri karibuni tutagawa hata magari kwa zaidi Halmashauri 40 kama sehemu hiyo ya jitihada zetu za kuhakikisha kwamba tunaondokana na upungufu wa vitendea kazi vilivyopo.
Mheshimiwa Spika, vilevile tuna mpango wa kujenga ofisi zaidi ya 50 kwenye Halmashauri zetu, lengo ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha huduma ya udhibiti ubora.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kusema kwamba kwa sasa hatutegemei tena tuwasikie Wadhibiti Ubora wakifanya kazi za kipolisi, ni lazima washirikishe wadau wote wakati wanafanya zoezi la udhibiti ubora.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kondoa Mjini tulichimba visima kumi, tumepata usambazaji wa visima vitano, lakini bila ya ukarabati wa miundombinu ya maji pale mjini, hizi gharama zilizotumika kusambaza visima vitano ni sawa na bure.
Je, ni lini Serikali itatuletea fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya maji mjini ambayo pia ni ahadi ya Waziri Mkuu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, nikushukuru lakini kikubwa nataka nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Sannda kwa jitihada anazozifanya, sisi kama Wizara ya Maji lazima tumuunge mkono. Kikubwa nimuombe Mhandisi wa Halmashauri ya Kondoa asilale, fedha tumeshapitishiwa na Bunge a-rise certificate na sisi tutamlipa kwa wakati mkandarasi atakayetekeleza mradi huo katika kuhakikisha tunaondoa tatizo la maji.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu ni Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, ni sera, sheria na kule kwenye halmashauri zetu lisipotekelezwa ni hoja ya ukaguzi lakini bado kuna changamoto za utekelezaji. Je, ni lini sasa Serikali itatoa waraka mkali kabisa ambao utaelekeza halmashauri zote zitekeleze na zisipotekeleza ziweze kuwajibishwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la rafiki yangu Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jambo hili tumelitolea maelezo hapa mara kadhaa na hata tukifanya rejea wakati nawasilisha bajeti yetu ya mwaka wa fedha 2018/2019 tulisema wazi kwamba katika ajenda hii ya mikopo ya akina mama na vijana sasa suala hili linakuwa si la hiari tena. Nimesema wazi mara kadhaa kwamba jamani fedha hizi hazifiki Hazina zinaishia katika halmashauri zetu. Jukumu letu kubwa sisi kuhakikisha tunasimamia katika Kamati za Fedha ili fedha hizi ziweze kufika kwa vijana na akina mama, hilo ndilo jambo la msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana katika Finance Bill ya mwaka huu tumeleta kifungu maalum kwa ajili ya enforcement ya jambo hilo. Ni imani yangu kwamba baada ya Sheria hiyo ya Fedha kufika hapa, Wakurugenzi wote, lakini niwatake Madiwani wote na Wabunge wote katika halmashauri zetu tuweze kuwa imara kuhakikisha utaratibu wa fedha hizi ambazo zinatengwa na katika bajeti ni lazima zitengwe, ziweze kuwafikia vijana na akina mama wetu. Kwa hiyo, hili ni jambo letu sisi sote na si jambo la mtu mmoja na kwa vile sheria inakuja nadhani hapa itakuwa hakuna suala la negotiation, tutakwenda kwa mujibu wa sheria itakavyotuongoza. (Makofi)
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wananchi wa Kondoa Mjini walikusanya nguvu sana wakajenga Kituo cha Polisi kidogo pale Mjini Stand. Kituo hiki sasa kina zaidi ya mwaka kimefungwa kutokana na upungufu na ukosefu wa askari. Je, ni lini sasa Serikali itatuletea askari kituo kile kifunguliwe na kifanye kazi iliyokusudiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Edwin Sannda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni kweli sababu hasa ni askari peke yake tunatarajia kuajiri askari 1,500 hivi karibuni, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupatia kibali cha kuajiri askari hao, tunaamini kwamba itasaidia kupunguza changamoto ya askari. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge, mimi na yeye tupange utaratibu hata weekend moja twende hapo tukaangalie ili kama changamoto tu ni hiyo na kwa sababu tunahamasisha wananchi washiriki ujenzi wa vituo haikubaliki hata siku moja kuona kituo kimekamilika halafu hakitumiki. Mimi nataka nimuahidi kwamba kama itakuwa ni changamoto tu ya askari mimi na yeye tutashirikiana kulikamilisha hilo na tutakizindua kituo hicho ili kiweze kufanya kazi.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi mvua za mwaka 2017 mwishoni na mwaka huu 2018 zimevuruga sana miundombinu katika Jimbo la Kondoa Mjini. Moja ya barabara iliyoharibika sana ni barabara ya Kingale ambapo mpaka daraja lenye mawasiliano makubwa sana kati ya Kingale na maeneo ya jirani lilivunjika. Daraja hilo limekuja kuangaliwa na watu wa TARURA Mkoa na watu wote wamelichunguza, mpaka sasa hivi bado halijafanyiwa kazi.
Je, ni lini sasa Serikali italeta mpango wa dharura wa kurudisha mawasiliano pale Kingale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba tumekuwa na mvua nyingi ambazo zimesababisha uharibifu mkubwa kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anasema katika swali lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika pesa ya dharura ambayo ilikuwa imetengwa kwa ajili ya matengenezo ya dharura, theluthi mbili ya pesa hiyo imetumika katika kurudishia miundombinu katika Mkoa wa Dar es Salaam, kwa sababu uharibifu uliotokea kwa Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa mkubwa sana. Hata hivi leo hii navyoongea almost pesa yote iliyokuwa imetengwa ya dharura imeisha kwa sababu mvua zimenyesha, miundombinu mingi ikawa imeharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikubaliane na Mheshimiwa Sannda na sababu sasa hivi na mvua nazo hata huko Kondoa hazinyeshi, kabla hatujaanza utekelezaji wa hiyo bajeti ambayo tulipitishiwa na Waheshimiwa na Wabunge, kama Serikali tutaona kuna haja ya kuchukua hatua zozote endapo maeneo hayo hayapitiki, tutafanya hivyo ili wananchi waendelee kupata huduma.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Hapa naweza nikasema ni pale ambapo Golikipa wa Simba anapigiwa shuti la penati na mshambuliaji wa Yanga halafu yeye anaenda kushoto goli linaingia kulia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, majibu yaliyotolewa na Serikali pamoja na shukrani zote, lakini kidogo yamekwenda tofauti na malengo ya swali lenyewe. Huu utaratibu wa Hospitali Tembezi tumekuwa tukiufanya hasa sisi wenyewe Wabunge tukishirikiana na Ofisi ya Mkoa. Tumefanya mara kadhaa, kama mara tatu na tunatarajia tena mwezi wa Septemba, 2018 tutapata nyingine kutoka Marekani.
Mheshimiwa Spika, nilichokuwa nikitarajia hapa ni ubunifu huu tulioanza nao kutokana na uchache wa huduma za kibingwa lakini pia na huduma nyingine za afya, kwenye ngazi ya Halmashauri na kwenye ngazi ya Wilaya tuupeleke kwenye vijiji, ndiyo maana niliainisha vijiji vingi ambavyo tunavizungumzia hapa.
Mheshimiwa Spika, kwa kawaida tumekuwa tunachukua gari la chanjo na mengineyo ya miradi kufikisha huduma za kliniki za watoto, chanjo, huduma za akinamama wale, lakini sasa zinafanyika nje kwenye uwazi, jambo ambalo halina staha sana, ndiyo maana tukawa tunahitaji Kliniki Tembezi. Huu ni ubunifu tuliofanya kwenye ngazi ya Wilaya, sasa tuufanye kwenye ngazi ya Vijiji. Je Serikali haioni umuhimu wa kuenzi na kuiga ubunifu huu kwenye ngazi ya vijiji? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuweza kujenga Zahanati kwenye kila Kijiji kama ilivyo sera yetu, gharama yake ni kubwa sana na haya maeneo yote niliyoainishwa unaweza ukazungumzia maeneo matano mpaka sita ambapo ukipata gari moja la namna hiyo la Kliniki Tembezi, linaweza likakusaidia kuweza kumaliza huduma ya kujenga Zahanati nne. Je, ni lini basi, na kwa kuwa tunafahamu uwezo wetu ni mdogo bora tufanye...
Eeh! Mheshimiwa Spika, ni lini basi, Serikali itaiga ubunifu huu na kutuletea Mobile Clinic Van kwa ajili ya maeneo yetu ya Kondoa? (Makofi
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu kwanza nimpongeze Mheshimiwa Sannda kwa jinsi ambavyo amekuwa akipigania wananchi wake kuhusiana na suala zima la afya. Wiki iliyopita alikuwa anaongelea juu ya suala la gari la wagonjwa, lakini leo anaongelea juu ya Mobile Clinic.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake alilenga gari linalotembea kwa ajili ya kutoa huduma. Sasa kwa namna ambavyo swali limekuja ndiyo maana anasema ni kama tumehamisha goli, lakini siyo nia ya Serikali kuhamisha magoli kwa sababu majibu yote tunayo.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza anauliza uwezekano wa kuiga hili jambo zuri ili kuvipunguzia vijiji vingi badala ya kufuata huduma maeneo ya mbali. Naomba tukubalianae na Mheshimiwa Sannda kwamba ni nia ya Serikali, pale ambapo uwezo unakuwa umeruhusu hatuna sababu ya kutowapelekea wananchi huduma jirani yao.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, anaomba tuige utaratibu mzuri ili kuwa na Mobile Clinic Van. Utakubaliana nasi kwamba wananchi wengi wamejitokeza, wametoa nguvu zao katika ujenzi wa Zahanati na Vituo vya Afya. Pamoja na wazo jema hili, lakini itakuwa siyo busara nguvu ile ambayo imetumiwa na wananchi tukai-dump halafu tukaanzisha jambo lingine. Kwa kadri nafasi itakaporuhusu na nguvu ya kibajeti ikiruhusu, wazo hili ni jema, naomba tulichukue kama Serikali kulifanyia kazi kwa siku za usoni. (Makofi)
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na pia nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu. Labda niseme tu kweli tunaishukuru Serikali kupata, nitumie lugha ya haka kagari, tumepata gari aina ya Suzuki Maruti ndogo sana ambayo kwa mazingira ya Jimbo la Kondoa lina uwezo wa kufanya shunting katika kata tatu za mjini tu, huku pembezoni litakuwa haliwezi kwenda kabisa kwa sababu njia haziruhusu. Je, ule umuhimu wa uhitaji wa huduma hii, Serikali haioni?.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; barabara kubwa imekamilika ya kutoka Dodoma kwenda Babati. Ongezeko la uhitaji wa huduma za dharura umekuwa mkubwa kweli, ajali ni nyingi kila uchao tunapata taarifa hizi, gari hili haliwezi kumudu. Je, ni lini sasa Serikali itatuletea gari la wagonjwa lenye kukidhi mahitaji ya hospitali ya Mji Kondoa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Sannda anaita ‘kagari’ lakini gari zile zimetengenezwa kwa ajili ya mazingira ya Kiafrika na ukitazama jiografia ya Kondoa ukilinganisha na maeneo mengine ambayo gari zile zimepelekwa, nimtoe wasiwasi, wanasema ‘ukubwa wa pua siyo wingi wa makamasi’. Ile gari itamudu kufanya kazi iliyokusudiwa na katika maeneo ambayo gari kama zile zimepelekwa hatujapata malalamiko yoyote. Ni vizuri, wanasema ‘asiyeshukuru kwa kidogo hata ukimpa kikubwa hawezi kushukuru’. Ni jitihada za Mheshimiwa Rais na tuna kila sababu ya kuziunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, anauliza ni lini sasa itapatikana gari nyingine. Naomba nimhakikishie kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba inapunguza adha ya usafiri hasa kwa wagonjwa wetu, pale ambapo uwezo utaruhusu zikapatikana gari zingine tutaanza kuzipeleka maeneo ambayo hawakupata magari kabisa. (Makofi)
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nachukua fursa hii kushukuru na kupongeza majibu mazuri ya Serikali. Pia niseme tu kwamba ushauri wa kuendelea kutumia Chuo cha Munguri kilichopo sasa tumeupokea na tunaendelea kuutumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, uwepo wa VETA utaongeza sana na kupanua wigo wa fursa za elimu ya ufundi ili kuendeleza azma yetu ya viwanda. Siyo hivyo tu, lakini pia kuongeza ajira kwa vijana. Swali; je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba maboresho haya mliyoyasema yanaingizwa kwenye Mpango na Bajeti ya VETA ili azma hii itekelezwe kwa haraka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naelekea huko mzee, swali la pili, azma ya kuwa na VETA ina maslahi mapana sana kwa wanachi, siyo tu kwa wananchi wa Jimbo la Kondoa Mjini, lakini kwa Kondoa nzima kama Wilaya. Pia uwepo wa Taasisi ya kitaifa kama hii yenye hadhi ya VETA na sasa Kondoa ni Halmashauri ya Mji, itaongeza tija kubwa sana kwenye kuchangamsha uchumi wa Kondoa. Swali je, Serikali inatupa commitment gani ya kuhakikisha inaharakisha mchakato huu mara tu baada ya kupokea hiyo barua kutoka Kondoa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kweli amekuwa akifuatilia kuhakikisha kwamba majengo yale yanatumiwa kwa ajili ya VETA. Naomba nimhakikishie kwamba kwa sababu Serikali ina azma na imedhamiria kujenga VETA kila Wilaya na kila mkoa, sisi tukikuta kwamba kuna majengo ambayo yamekuwa tayari tunakimbilia kwa sababu gharama ni ndogo kwa sababu tunataka tuweze kuwaletea wananchi maendeleo na kupata ile elimu ya ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie mbele yako kwamba pindi sisi tutakapopata barua ya kutuhurusu tutumie yale majengo tutaendelea na utaratibu wa kukarabati ili wananchi wa Kondoa waweze kupata ile huduma. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara yetu hatuwezi tukawa kikwazo cha yeye kufanikiwa lengo lake hilo kwa ajili ya wananchi wake. Kwa hiyo naomba nimshauri wakakae na halmashauri yake watupatie barua, wakinipa kesho mimi niko tayari hata mwenyewe kwenda kukagua eneo lile ili tuweze kuendelea na taratibu zinazofuata.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwenye Kata ya Kolo, Jimbo la Kondoa Mjini tulipata ufadhili mkubwa sana wa wenzetu wa MKAJI kwa ajili ya kukarabati Zahanati kwa lengo la afya ya mama na mtoto, na waliweka lengo kubwa sana mkazo mkubwa kwenye huduma ya maji, kimekarabatiwa kisima kirefu, kimemalizika sasa hivi takriban miezi mitatu. Kinachokwamisha ni supply ya umeme pale ili huduma hiyo iweze kuanza kutumika. Tumewaomba TANESCO Wilaya, TANESCO Mkoa mpaka sasa hivi bado tunasubiria. Je, ni lini sasa wenzetu wa TANESCO watatuletea ule umeme ili zoezi zima la wenzetu wa MKAJI lianze kuleta tija?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kwamba hili swali lake ni zuri linahitaji utekelezaji, nimwahidi Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi cha maswali na majibu na ratiba ya Bunge tukutane na pia nitafanya ziara maalum na wataalam wa TANESCO katika maeneo hayo ili kuhakikisha kisima hiki kinapata huduma hii ili dhamira iliyotarajiwa kwa ujenzi wa zahanati na ukarabati hiyo iweze kufikiwa, ili iweze kupata maji na huduma iweze kutolewa. Ahsante.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nipongeze majibu mazuri ya Serikali kutoka kwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu mazuri hayo, basi nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, ripoti hii ya utafiti wa awali sisi kama watu wa Ausia na kule Kondoa hatuna, kwa hiyo hata kuweza kujua kuna kiwango cha chokaa kiasi gani imekuwa ni mtihani na ukizingatia kwamba madini haya ni muhimu sana katika kazi za ujenzi, sasa tunataka kujua, ni hatua gani na wao kama Serikali watatusaidia ili twende kwenye utafiti wa kina tuweze kujua madini kiasi gani yapo kule tuendelee na hatua ya pili ya kupata mwekezaji na hatimaye kuanza kunufaika na uwepo wa madini hayo? Hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ili Mheshimiwa Naibu Waziri akajiridhishe na hali halisi iliyoko pale akifika site, je, anaonaje sasa mimi na yeye pamoja na wataalam wake wa Wizara tukaongozana tukaenda site tuweze kuharakisha mchakato huu wa wananchi wa Kondoa Mjini waweze kunufaika na madini haya ambayo yanaonekana yako kwa wingi.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edwin , Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru sana Mheshimiwa Sannda kwa kazi nzuri anayoifanya kwa wananchi wa Kondoa, wananchi wa Kondoa nadhani watamtazama tena hapo mwakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu ni kwamba, alichokisema na majibu yangu ya msingi nilivyosema ni sawa, Wizara yetu kupitia GST tunafanya tafiti za kina kupitia zile QDS yaani Quarter degree sheets, tunafanya kitu wanaita Geophysical Survey ambayo inatambua uwepo wa madini katika maeneo hayo na kwa kweli kwa nchi nzima tuna ramani inayoonyesha uwepo wa madini na kila sehemu ni madini gani yako katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utafiti wa kina ambayo ni geochemistry ambayo inafanywa mara nyingi na mwekezaji mwenyewe. Anakwenda anafanya utafiti wa kina kujua deposit iliyopo pale na kama deposit hiyo anaona yeye inaweza ikamlipa, ikawa economical, sasa hatua ya pili ya kuomba leseni ya uchimbaji, anakuja kuomba kwetu na tunampatia kwa ajili ya uchimbaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba utafiti wa kina umeshaonesha madini katika maeneo niliyoyataja na sasa hivi tunakaribisha wawekezaji wengi waje wawekeze kwa sababu utafiti wa kina unahitaji fedha nyingi.

Kwa hiyo sasa hivi tunaweka mahusiano mazuri na maeneo mbalimbali kwa mfano jana nimepokea ugeni kutoka China, wao wanataka kutusaidia kufanya tafiti za kina kuweza kutambua maeneo na deposit zilizopo katika maeneo mbalimbali ili kuweza kuwasaidia wachimbaji kuwapa taarifa za kijiolojia na waweze kwenda kuwekeza maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ameuliza kwamba niko tayari kwenda Kondoa na wataalam, mimi nimweleze tu ni kwamba niko tayari, tunaweza tukaenda Kondoa na niko tayari muda wote na wataalam wapo, lakini pale panapohitajika tutaweza kubeba timu ya wataalam kwenda nayo, lakini kwa kufika pale na kujionea niko tayari wakati wowote.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza, kwanza fursa za vyanzo vya mapato na uwezekano wa kuongeza mapato inatofautiana baina ya halmashauri na halmashauri. Hili suala la malalamiko lina kosa msingi linabaki kuwa dhana.

Sasa je, Serikali huwezi kulinganisha kati ya Kondoa au Geita au hata Dar es Salaam fursa za mapato zilizopo, na Madiwani ni sehemu ya wanaoweka nguvu ya kukusanya mapato na kuongeza mapato. Serikali haioni umuhimu wa kuwaruhusu walipe kadiri ya uwezo wa halmashauri zao ili pia iwe sehemu ya motisha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, lini sasa maana tulipata Waraka wa kutuambia tulipe 40,000 na hapa tunazungumzia posho za vikao peke yake, lini sasa maslahi mengine tunaendelea kuruhusu kadiri ambavyo inafanya kazi. Lini sasa tutapata Waraka wa kufafanua ili ule Waraka uliotolewa mwezi Januari uweze kupitwa maana Serikali inafanya kazi kwa maandishi?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Waheshimiwa Madiwani wanafanya kazi kubwa sana ya kusimamia mapato, kwa kukusanya lakini pia na ndiyo maana fedha nyingi hapa tunapeleka halmashauri Waheshimiwa Madini kupitia vikao vyao na Kamati mbalimbali ndiyo wanapaswa kusimamia na kwa kweli tunawashukuru sana wamekuwa wakifanya hivyo. Majibu yangu ni kwamba ni kweli Mheshimiwa Waziri wa Nchi wakati anamalizia hoja yetu hii ya bajeti ya TAMISEMI, aliahidi mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba jambo hili linafanyiwa kazi na naomba niwaahidi kwamba, Waheshimiwa Wabunge wote na Waheshimiwa Madiwani popote walipo wavute subira ndani ya wiki hii Mheshimiwa Waziri atatoa maelekezo na jambo hili litafikia mwisho ambapo tunaamini kwamba utakuwa ni mwisho mwema, ahsante.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nitumie fursa hii kushukuru majibu ya Serikali sambamba na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, namba moja, ni miaka tisa sasa toka tumeingiza zaidi ya milioni 143 kwenye mradi huu na hakuna ambacho kimeweza kuwa realized mpaka leo. Ukichukua faida ambazo tungezipata kwa mradi ule watu 12,000 kunufaika tungekuwa tu kwa mwaka tunapata zaidi ya bilioni 50; mpaka leo tunazungumzia miaka tisa tungekuwa tumetengeneza zaidi ya bilioni 500, ukiangalia hii opportunity cost peke yake acha multiplier effect kipindi cha uchumi wa viwanda na mazao ambayo yangetokana na matokeo yale ya pale kwenye mradi ule tungekuwa tumepiga hatua kubwa sana kwa wananchi wa Kondoa.

Je, ni lini sasa Serikali itafikia hatua ya kuweza kufanya hii tathmini ya kina na hatimaye kufanya hii tathmini ya kina na hatimaye kukamilisha mchakato mradi huu utekelezwe? la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ili Mheshimiwa Naibu Waziri uweze kujiridhisha na fursa iliyoko kule fursa kubwa sana.

Ni lini sasa mimi na wewe na pamoja na wataalam wako tutaongozana tuende pale Mongoroma tukaone nini kinaweza kikafanyika kwa haraka zaidi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kujua kwamba huu mradi umechukua muda mrefu zaidi ya miaka tisa na hela pale tumeshawekeza ni lini sasa kwamba tumeanza kuuharakisha huu mchakato.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kwanza kumhakikisha Mheshimiwa Mbunge pamoja na kwamba sijafika katika mradi huu, lakini viongozi wetu, Wahandisi wetu wa Kanda ya Umwagiliaji Kanda ya Dodoma tayari wako kwenye mchakato wa kuufanyia tathmini ya kina ili kubaini gharama halisi za sasa badala hizi za miaka kumi iliyopita ili kuingiza katika mpango kabambe wa umwagiliaji ambao tumeuhaulisha ile Sera ya mwaka 2013 kwa hii ambayo Sera Mpya ya mwaka 2018 mradi huu pia tunaenda kuutekeleza na tathmini itafanyika haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, pili kama nilivyojibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kafumu kwamba mradi mbadala au njia mbadala ya kutekeleza miradi hii mikubwa ni kutumia Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa sasa hivi kwa sababu tunaondoka kwenye kilimo kile cha kujikimu tuko kwenye kilimo cha kibiashara. Kwa hiyo, lazima sasa tuwekeze ndiyo maana tumewaletea benki hii yenye riba rafiki kwa wakulima ili kuenda kuendeleza miradi mikubwa kama hii kwa sababu ile ni benki ya kimkakati.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili niko tayari baada ya bajeti yetu inayoanza kesho tarehe 17 Mei na kumalizika tarehe 20 Mei tuonane tupange ikiwezekana tarehe 21 na 22 Mei mimi na wataalam wangu tuko tayari kufika Kondoa ili kuliangalia.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimwa Spika, nakushukuru. Labda tu kabla ya kuuliza maswali yangu ya nyongeza, nikuombe tu univumilie kidogo kwa sababu haya majibu ya Serikali sioni matumaini kabisa.

Mheshimiwa Spika, kwanza tunazungumzia uchumi wa viwanda na tegemeo kubwa lazima tuweze kuzalisha wanasayansi wa kutosha kabisa. Sasa mimi natoa mfano tu wa Mkoa wetu wa Dodoma tulikuwa kwenye vikao vya ALAT hata kwako Mheshimiwa Spika tuko chini ya 20% ya ukamilishaji wa maboma ya maabara. Sasa huu uchumi wa viwanda unakwenda kulishwa na watu kutoka wapi kama tunawapeleka watu wa masomo mengine na siyo wanasayansi?

Mheshimiwa Spika, unapozungumzia shilingi milioni 8 ambazo Halmashauri ya Mji Kondoa tumeidhinisha hizi ni zile fedha ambazo nimezitoa mimi kupitia Mfuko wa Jimbo mwaka jana na tulikwishazitoa. Boma moja la darasa linajengwa kwa shilingi 25 sisi tunazungumzia shilingi milioni nane. Hebu Serikali ione ni namna gani tunakuja na mkakati wa dharura sasa kama ambavyo tumefanya kwenye maboma ya madarasa na kwenye nyumba za walimu ili tuweze kukamilisha hizi maabara nchi nzima. Swali la kwanza hilo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, walau mimi nina maabara moja tu kati ya sekondari nane (8) ambayo imekamilika na yenyewe haina vifaa. Ni lini tutapata angalau hivyo vifaa vya maabara kwenye hata hiyo moja ambayo mpaka sasa imeshakamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba majibu ya Serikali tafadhali.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFlSI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ameuliza maswali mawili, moja anauliza mkakati wa Serikali wa kumalizia maabara ambazo wananchi wameweka nguvu zao lakini jambo la pili anataka kujua ni lini tutapeleka vifaa katika shule yake.

Mheshimiwa Spika, tulisambaza vifaa vya maabara kwenye shule na maabara mbalimbali. Nafikiri baada ya kutoka hapa mbele tuwasiliane tuone ni kwa nini maabara yako moja ambayo imekamilika haikupata vifaa ili tuweze kupeleka vifaa katika shule yako hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini nikupongeze sana kwa swali muhimu, ni kweli kwamba tunahitaji uchumi wa viwanda na tunahitaji zaidi wanafunzi wetu wasome masomo ya sayansi na huwezi kusoma sayansi kama hauna maabara zenye vifaa na wale wataalam wa maabara ili waweze kufanya mazoezi kwa vitendo. Tunampongeza Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine ambao kwa kupitia Mfuko wa Jimbo wamepeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha maabara. Najua wengine wamejenga madarasa, wengine wamenunua madawati na wengine wamejenga nyumba katika maeneo ya jirani ili walimu wetu waweze kupanga kwa bei nafuu sana.

Mheshimiwa Spika, nilichosema hapa ni kwamba Serikali ina mpango, kwenye bajeti hii Waheshimiwa Wabunge wote tumetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maabara. Tulishatoa taarifa kwenye Halmashauri walete taarifa ya maabara ambazo zimekamilika, vifaa vinanunuliwa na vinasambazwa katika maeneo yale. Tunaendelea kutoa wito tupate hizo taarifa ili tuendele kukamilisha zoezi hili.

Mheshimiwa Spika, umesema vizuri hapa kwamba hapa tunazungumzia maabara katika shule za sekondari na katika mpango wetu ule wa kupata fedha zile ambazo zina kizungumkuti huko na wenzetu wameshiriki, katika mpango ule nilisema juzi hapa tunajenga shule mpya za watoto wa kike maalumu 26, tunajenga madarasa na mabweni kwa maana ya mabwalo zaidi ya 300 na tunakamilisha maabara zaidi ya 400. Kwa hiyo, huenda hii fedha ingekuja kwa wakati na ndiyo ulikuwa mpango wa Serikali hii kazi ya kulalamikia maabara hata kama isingeisha ingepungua sana. Tutoe wito Waheshimiwa Wabunge kama nilivyosema juzi hii kazi Serikali ni yetu sote tulishirikiane fedha zikitafutwa tunapeleka fedha Halmashauri, tunapeleka fedha kutoka Mfuko Mkuu lakini pia tunatumia wadau mbalimbali ili tuweze kupata fedha tuweze kukamilisha miundombinu mbalimbali ya elimu.

Mheshimiwa Spika, tushirikiane katika jambo hili na kama ambavyo umeshazungumza katika Bunge hili. Pia sisi kama Wizara tunakwazwa sana na mambo haya kwa sababu tunaweka mipango na Wabunge wameleta maombi mbalimbali pale Wizarani, fedha zimeiva halafu kuna watu wanaweka kitumbua mchanga. Ahsante sana.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Hospitali ya Mji wa Kondoa inahudumia takriban Halmashauri sita. Tunazungumzia Kondoa Vijijini, Chemba, Kiteto, wakati mwingine mpaka Hanang’ na Babati. Bajeti tunayopata ni shilingi milioni 45 kati ya milioni 160 ambayo tunahitaji kutoka Basket Fund. Nimelizungumzia sana suala hili Bungeni hapa.

Je, ni lini sasa Serikali itakubaliana na uhalisia wa mahitaji hayo na kutuongezea bajeti yetu kukidhi mahitaji ya wananchi wa maeneo hayo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, tuna changamoto katika maeneo ya miji ukiachia ile Halmashauri ya Mji wa Kondoa lakini kwa dada yangu Mheshimiwa Esther Matiko pale Tarime na hali kadhalika kwa Mheshimiwa Chumi pale Mafinga. Ndiyo maana tumewaagiza wataalam wetu sasa hivi wanafanya analysis kuangalia changamoto kubwa ya idadi ya watu na mgawanyo wa fedha ili tuweze ku-regulate vizuri ili mradi maeneo hayo yaweze kupata huduma vizuri. Kwa hiyo, naomba tuwe na subira kidogo, wataalam wetu wanafanya kazi hiyo, naamini katika Mpango wa Bajeti yetu ya mwaka wa fedha 2020/2021 jambo hilo tutali-address vizuri kwa maslahi mapana ya wananchi wetu.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pale jimboni Kondoa tunazo shule mbili, Shule ya Iboni na Shule ya Ubembeni ambazo zinavitengo vya watoto wenye mahitaji maalum zote ziko kata moja ya Chemchem ambayo ni kata ya katikati kabisa katika jimbo zima. Hali ya mapato yetu ya ndani ya Halmashauri ni ndogo sana ambayo imetupelekea mpaka mimi mfuko wa jimbo kuweza kusaidia miundombinu stahiki kwa ajili ya wale watoto pamoja na choo, walimu pia hatuna.

Je, Waziri ni lini unaweza ukafanya utaratibu wa kutuupa uzito na kuja kufanya tathimini ya kina ili tuweze kuweka miundombinu stahiki na walimu wa kututosheleza ukizingatia watoto hao wenye mahitaji maalum wanaendelea kuongezeka siku hadi siku?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Sannda kwa jitihada zake kwa kutumia mfuko wa Jimbo ili kuhakikisha kwamba miundombinu wezeshwi inajengwa katika shule hizo, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba watoto wote wenye uhitaji maalum hawaachwi nyuma na suala zima la uhitaji wa walimu ambao wanatakiwa waajiriwe naomba nimuhakikishie kama sisi Serikali tutazingatia maombi yake.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Wananchi wa vijiji vya Chemchemi, Tampori, Iyoli kule Kata ya Kingale pamoja na Muluwa Kata ya Serya wamekuwa wakipata athari kubwa sana kutokana na wanyama waharibifu hawa tembo, almaarufu kule Zanzibar, Unguja ya Kusini kama ndovu.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru sana Serikali, wameanza kufanya malipo ya vifuta jasho na vifuta machozi kuanzia mwaka 2016 kwa baadhi ya vijiji, lakini athari hizi zimeanza 2012, taratibu zote zilifuatwa na pia madai yakawasilishwa Wizarani.

Sasa Je, kuna mpango gani wa kufanya malipo ya maeneo yaliyoachwa tangu mwaka 2012 kwa watu wote na kwa maeneo yote ambayo yalipata athari?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba athari za wanyama zimeendelea kuwepo na kwa sasa hivi zimeendelea kusumbua nchi nzima. Labda tu nitumie nafasi hii kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba kabla ya miezi michache iliyopita, ilikuwa ni jukumu la TAWA peke yake kupitia kikosi cha KDU kwenda ku-respond na matukio ya wanyama waharibifu yanapotokea, lakini Wizara imefanya marekebisho kama ilivyo kwenye maelekezo na hivi sasa popote ambapo tuna Hifadhi ya Taifa au tuna pori la akiba iwe ni TANAPA au TAWA au ni TFS katika eneo hilo, wanawajibika ku-respond na wanyama waharibifu wanapotokea kwenye maeneo ya vijiji. Kwa hiyo, maelekezo haya tumeshayatoa kwenye Taasisi zetu zote hizi.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tulianza kulipa mwaka 2016 na hii ilisababishwa na kutokuwepo kwa kumbukumbu za kutosha huko nyuma. Mwaka 2018 peke yake Wizara yangu imelipa shilingi bilioni 1.6 kama kifuta jasho na fidia. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tatizo la kutokulipa huko nyuma pamoja na kumbukumbu lilikuwa pia ni tatizo la fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, mwaka huu peke yake mpaka leo tuna madai ya wananchi yanayofikia takriban shilingi bilioni 3.2 lakini mfuko wetu hauwezi kuzidi shilingi bilioni 1.6. Kwa hiyo, pale ambapo kumbukumbu zitaonyesha kwamba kuna wananchi bado wanadai, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara yangu itafanya mpango wa kulipa.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Sisi kwetu pale Kondoa hospitali tunayo lakini hospitali ile inahudumia zaidi ya Halmashauri tatu za Chemba, Kondoa Vijijini, Babati na wakati mwingine mpaka Hanang. Kwa hiyo, mahitaji ya huduma yamekuwa ni makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tunaipongeza Serikali kwa kukamilisha ile barabara ya kutoka Dodoma - Babati. Kunapokuwa na maendeleo na changamoto zinaongezeka sana. Kukamilika kwa barabara ile kumeongeza sana mahitaji ya huduma ya hospitali ikiwemo huduma za dharura. Nimelia sana kuhusiana na suala la ambulance, tuna tatizo kubwa sana la ambulance. Ni lini sasa Serikali itaipatia Hospitali ya Mji wa Kondoa ambulance mpya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Edwin Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kwa niaba ya Serikali kupokea pongezi ambazo zimetolewa na Mheshimiwa Mbunge. Mheshimiwa Mbunge wakati anajenga hoja yake anaeleza jinsi ambavyo wananchi wengi wanalazimika kwenda kutibiwa kwenye Hospitali ya Kondoa Mji na hii tafsiri yake ni kwamba huduma inayotolewa pale ni nzuri ndiyo maana wananchi wanalazimika kutoka hata Chemba kwenda kupata huduma pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Serikali kuhakikisha kwamba inapunguza adha kwa wananchi kutembea umbali mrefu ndiyo maana hata Halmashauri ya Chemba inajengewa Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, hiyo influx ambayo imekuwepo itapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la msingi ambalo anataka kujua lini Serikali itapeleka ambulance ili kupunguza adha, amesema mara nyingi sana na Serikali ni sikivu, katika mgao ambao utapatikana kwa siku za usoni hakika Kondoa hatutaisahau.