Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Stephen Julius Masele (4 total)

MHE. STANSLAUS H. NYONGO (K.n.y. MHE. STEPHEN J. MASELE) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itahakikisha vijiji vilivyo ndani ya kilomita tano kutoka bomba kuu la maji ya Mradi wa KASHWASA vinapatiwa maji vikiwemo vijiji vya Kolandonto, Ibadakuli na Kuzumbi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Julius Masele, Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetekeleza mradi wa maji safi kutoka Ziwa Viktoria kwenda Manispaa ya Shinyanga kupitia bomba kuu la KASHWASA. Katika kuhakikisha vijiji vilivyopo umbali wa kilometa 12 kandokando ya bomba kuu vinapatiwa maji, Serikali inaendelea kuunganisha maji kutoka bomba hilo hatua kwa hatua kulingana na upatikanaji wa fedha. Hadi sasa jumla ya vijiji 12 tayari vimeunganishwa kati ya vijiji 40 vilivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mradi wa kupeleka maji katika Mji wa Kishapu Mkoani Shinyanga. Kupitia mradi huo kijiji cha Kolandoto kinatarajiwa kupata huduma ya maji. Kwa sasa kazi ya ulazaji bomba kuu unaendelea na tayari kilometa 22 zimelazwa. Vijiji vya Ibadakuli na Kizumbi vinapata huduma ya maji safi kutoka Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira SHUWASA. Kwa sasa mtandao wa maji uliopo haujafika vijiji vyote ambapo Serikali inaendelea na mazungumzo na Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa ambao wameonesha nia ya kusaidia fedha za ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji katika maeneo hayo.
MHE. STEPHEN J. MASELE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itataifisha Kiwanda cha Nyama Shinyanga Mjini baada ya mwekezaji kushindwa kukiendesha?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Julius Masele, Mbunge wa Shinyanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuvirudisha viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo havifanyi kazi ili vifanye kazi, viongeze ajira na kuchangia Pato la Taifa. Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina tunafuatilia mikataba ya viwanda vyote vilivyobinafsishwa na kufanya tathmini ya kina ili kujiridhisha kabla ya kuvirejesha Serikalini. Tathmini hiyo inaendelea nchi nzima ikihusisha wataalam kutembelea mikoa yote ya Tanzania ili kujua hali halisi ya viwanda hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Nyama Shinyanga ni kati ya viwanda 55 vilivyofanyiwa tathmini kwa lengo la kukagua ufanisi na kuhakiki utekelezaji wa masharti kulingana na mikataba ya ununuzi kwa mujibu wa agizo la Mheshimiwa Rais wakati wa ufunguzi wa Bunge la Kumi na Moja. Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina wameshakutana na mwekezaji wa Kiwanda cha Triple S Beef Ltd na Msajili wa Hazina amemtaka mwekezaji wa kiwanda hicho kuwasilisha mpango mkakati na andiko la biashara wa kuendeleza kiwanda hicho. Nia ya Serikali ni kumpa fursa ya kwanza mwekezaji huyo ili aendeleze kiwanda kama ilivyokubalika kwenye mkataba wa kuuziana. Endapo atashindwa kutumia fursa hii ya mwisho aliyopewa kiwanda kitatwaliwa wala siyo kwamba kitabinafsishwa.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO (K.n.y. MHE. STEPHEN J. MASELE) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza ahadi ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na mitaa ili kutatua tatizo la ajira na mitaji kwa vijana na kina mama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali Mheshimiwa Stephen Julius Masele, Mbunge wa Shinyanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 13 Juni, 2016 wakati nikijibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kuhusu lini ahadi ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji itaanza kutekelezwa nilisema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 59.5 katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulitaarifu Bunge lako kuwa tayari waraka wa Baraza la Mawaziri utakaoongoza utoaji wa fedha hizo umeshaandaliwa na kujadiliwa katika Kamati ya Makatibu Wakuu (IMTC) hivi sasa waraka huo unasubiri kujadiliwa na Baraza la Mawaziri ili kuweka mfumo utakaoratibu utoaji wa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Hivyo namuomba Mheshimiwa Mbunge asubiri utekelezaji wake mara baada ya Baraza la Mawaziri kuujadili.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE (K.n.y. STEPHEN J. MASELE) aliuliza:-

Kumekuwepo na kero kubwa ya wananchi wanaotumia Bima ya Afya kunyimwa dawa katika zahanati na maduka ya dawa nchini kwa kisingizio cha malipo kutoka NHIF kuchelewa:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kimkakati wa kuhakikisha malipo yanafanyika kwa ufanisi ili kuboresha mfumo mzuri wa matumizi ya kadi za Bima hususani kwa wazee nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Stephen Julius Masele leo ni Siku ya Saratani Duniani na naomba kuwakumbusha Watanzania kwamba saratani ni tatizo kubwa ndani ya nchi yetu takribani watu 55,000 kwa mwaka wanapata ugonjwa huo wa saratani na ni 13,000 tu ambao wanafika katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya ikiwa ni takribani ni asilimia 25 na asilimia 70 wanafika wakiwa na hatua ya mwisho kabisa ya ugonjwa. Kwa hiyo, nilikuwa nataka kutumia fursa hii kuwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kupata huduma na upimaji na matibabu ya saratani ni bure.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Julius Masele, Mbunge wa Shinyanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya huingia mkataba na vituo vya kutolea huduma , mkataba ambao huanisha makubaliano juu ya utaratibu wa kutoa huduma bora kwa wanufaika wake na uwasilishaji wa madai ya gharama ya huduma za afya zinazotolewa kwa wanachama wake. Utaratibu huo huwataka watoa huduma kuwasilisha madai yao kwa wakati ndani ya siku 30 baada ya mwezi husika wa madai ili kuwezesha kuanza kwa mchakato wa madai hayo kulipwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, sheria inautaka mfuko kukamilisha malipo ya madai ya watoa huduma ndani ya siku 60 toka siku ambayo madai husika yamewasilishwa katika Ofisi za Mfuko zilizopo katika mikoa yote nchini. Kwa sasa mfuko unalipa madai kwa wastani wa siku 45. Hata hivyo baadhi ya madai yamekuwa yakichelewa kulipwa kutokana na ucheleweshaji wa kuwasilisha madai kwa baadhi ya watoa huduma. Watoa huduma kutozingatia miongozi ya tiba kama ilivyoainishwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kwa maana ya Standard Treatment Guidelines. Vitendo vya udanganyifu na baadhi ya watoa huduma kutozingatia makubaliano yaliyoainishwa katika mkataba wa huduma baina yao na mfuko.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia mfuko kwa sasa unaendelea kufanya maboresho ya huduma zake ikiwa ni pamoja na kufanya mambo yafuatayo:-

(i) Kutumia zaidi TEHAMA katika utayarishaji wa madai na kuwezesha watoa huduma kutayarisha madai kwa wakati;

(ii) Kuimarisha ofisi za mikoa na kugatua zaidi shughuli za mifuko hasa malipo kwa watoa huduma, viwango vya malipo mikoani vimeongezwa ili kuzipa ofisi za mikoa uwezo wa kulipa madai makubwa;

(iii) Kuendelea kutoa elimu kwa watoa huduma wote waliosajiliwa na mfuko ili kuwasilisha madai kwa wakati na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu;

(iv) Mfuko unaendelea kuwakumbusha watoa huduma kuzingatia miongozo ya tiba na maelekezo mengine yanayotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa lengo kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora za afya.