Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ezekiel Magolyo Maige (14 total)

MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Mvua ya theluji ilionyesha terehe 3 Machi, 2015 ilisababisha maafa makubwa ambapo familia zilikosa makazi na Mheshimiwa Rais wakati huo aliwaahidi wahanga wa maafa hayo kuwa Serikali itasaidia kujenga nyumba 343:-
(a) Je, ni nyumba ngapi hadi sasa zimejengwa katika kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais?
(b) Je, ni kiasi gani cha pesa kinahitajika kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hiyo?
(c) Je, ni kiasi gani cha fedha na misaada ya kibinadamu ya aina nyingine iliyotolewa na Serikali katika kukabiliana na janga hilo?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolya Maige, Mbunge wa Msalala, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa nyumba mbili za mfano kwa lengo la kujua gharama halisi za ujenzi wa nyumba zilizoahidiwa na Serikali.
(b) Mheshimiwa Spika, jumla ya Sh.2,500,000,000 zinahitajika kugharamia ujenzi wa nyumba hizo. Gharama hizi zimepatikana baada ya kukamilika kwa tathmini ya gharama za ujenzi wa nyumba moja moja.
(c) Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na maafa haya Serikali ilitoa huduma za dharura za malazi, makazi ya muda na matibabu. Misaada mingine iliyotolewa na Serikali ni pamoja na mahindi tani 100.4, Sh.45,290,045 kwa ajili ya ununuzi wa maharage, mafuta ya kupikia na usafirishaji wa mahindi. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Mfuko wa Maafa ilitoa Sh.10,000,000 kwa ajili ya mahitaji mbalimbali.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA (K.n.y. MHE. EZEKIEL M. MAIGE) aliuliza:-
Kilio kikubwa cha wananchi waishio jirani na Mgodi wa Bulyankulu ni kunufaika na mgodi huo:-
(a) Je, ni kiasi gani cha pesa Mgodi wa Bulyankulu ulitumia katika miradi ya ujirani mwema?
(b) Je, kwa nini mgodi huo hautekelezi miradi yake kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ambako kuna wataalam na gharama za utekelezaji miradi ni ndogo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2015 Mgodi wa Bulyankulu kwa kutumia “Maendeleo Fund” ulitumia takribani dola za Marekani milioni 1.98, sawa na takribani shilingi bilioni 4.4 kwa ajili ya miradi ya ujirani mwema iliyotolewa na Kampuni hiyo ya Bulyankulu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni za Migodi huwa na utaratibu wa kutekeleza shughuli zake kwa kuajiri wafanyakazi kulingana na mahitaji yao na kwa kuzingatia sheria za nchi. Pamoja na hayo, kampuni hizo huruhusiwa kuajiri wakandarasi wafanyakazi katika taaluma za ujuzi ambao haupo nchini. Hadi sasa kampuni imeajiri wafanyakazi hapa nchini wapatao 1,168, kati yao wafanyakazi 517 wanatoka katika maeneo yanayozunguka mgodi huo. Aidha, miradi husika hutekelezwa kwa kushindanisha wakandarasi na wataalamu kutoka sehemu mbalimbali nchini wakiwemo kutoka Halmashauri husika na hasa ya Msalala.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tutachukua hali hii kama ombi rasmi la Mheshimiwa Mbunge wa Msalala ili kulitafakari na kulifanyia kazi na kukaa na wakandarasi pamoja na mgodi unaomiliki shughuli za Mgodi wa Bulyankulu.
MHE. SUBIRA K. MGALU (K.n.y. MHE. EZEKIEL M. MAIGE) aliuliza:-
Moja kati ya vikwazo vya utekelezaji wa Ilani ya CCM ni kutotolewa kwa fedha kwa ukamilifu na kwa wakati:-
(a) Je, ni kiasi gani cha fedha kilikasimiwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa mwaka wa fedha 2015/2016?
(b) Je, Serikali imetoa kiasi gani cha fedha za Miradi ya Maendeleo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Msalala hadi kufikia Desemba, 2015?
(c) Je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha fedha za maendeleo zinapatikana kwa wakati na kupelekwa kwenye miradi husika?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Masalala, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016, kiasi cha shilingi bilioni 4.1 kilitengwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Desemba, 2015 Serikali imeshatoa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala. Aidha, wahisani wametoa jumla ya shilingi bilioni 1.6 nje ya fedha zilizoidhinishwa katika bajeti ya Halmashauri hiyo kwa ajili ya miradi ya TASAF, SEDP na AGPHAI na kufanya fedha zote zilizopokelewa hadi Desemba, 2015 kufikia bilioni 3.1.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za miradi ya maendeleo zinapelekwa katika Halmashauri zote kulingana na makusanyo yanayofanyika. Mkakati uliowekwa na Serikali ni kuimarisha makusanyo ya mapato ya Serikali na kudhibiti upotevu wa mapato katika vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha fedha zinapelekwa kama zilivyopangwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA (K.n.y. MHE. EZEKIEL M. MAIGE) aliuliza:-
Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi matukio ya majanga na maafa kama mvua za mawe pamoja na matetemeko ya ardhi yameanza kutokea mara kwa mara na mara zote Serikali imekuwa haina maandalizi ya kifedha na vifaa vya kusaidia wahanga kwa muda mfupi na muda mrefu na badala yake imekuwa ikitegemea zaidi wasamaria wema wa Mataifa mengine:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali imekuwa haisaidii kifedha na vifaa zaidi ya kuhamasisha wasamaria wema wasaidie na wenyewe kubaki na jukumu la kupeleka wataalam kama Madaktari na kuratibu misaada pekee?
(b) Je, ni kwa nini Serikali isianzishe Mfuko wa Maafa Kitaifa ambao utakuwa unachangiwa wakati wote kwa njia endelevu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali inatambua kuwa ni wajibu wake kusaidia wananchi pindi wanapokumbwa na maafa yanayoharibu mfumo wa maisha ya kila siku. Katika kutekeleza wajibu huo Serikali imekuwa ikitoa misaada ya aina mbalimbali kwa waathirika wa maafa ikiwemo vyakula, malazi, vifaa vya kibinadamu na huduma za afya.
Vilevile Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kununua mahitaji ya dharura ya kibinadamu pamoja na kurejesha miundombinu iliyoharibika. Aidha, katika jitihada za kuhakikisha kuwa misaada inawafikia wananchi kwa haraka Serikali tayari ina maghala ya maafa yenye vifaa mbalimbali vya kukabiliana na maafa katika Kanda sita nchini.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema ifahamike kuwa suala la kukabiliana na maafa ni mtambuka na haliwezi kuachwa mikononi mwa Serikali peke yake kwani wakati mwingine maafa yanakuwa ni makubwa sana hivyo kuhitaji juhudi za pamoja baina ya Serikali, wadau wa maendeleo na wananchi katika kuyakabili na kurejesha hali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo Serikali ilileta Muswada wa Sheria ya Maafa uliopitishwa na Bunge lako Tukufu na kuwa Sheria Namba 7 ya mwaka 2015 ambayo pamoja na mambo mengine inaelekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Maafa na pia, Kifungu 31 kinaainisha vyanzo vya mapato vya Mfuko huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa wadau wa maendeleo pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na Serikali katika harakati zake za kujiandaa, kukabili na kurejesha hali, ili kuhakikisha jamii yetu inakuwa salama zaidi dhidi ya majanga mbalimbali.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Mwaka 2014/2015 Serikali iliahidi kuongeza usambazaji maji katika vijiji 100 vilivyoko umbali wa kilometa 12 kutoka bomba kuu la Ziwa Victoria hadi Kahama na Shinyanga. Serikali ilitenga na Bunge kupitisha shilingi bilioni nne ili kutekeleza mradi huo.
(a) Je, ni vijiji vingapi vimeshapatiwa maji kati ya hivyo vijiji 100 hadi sasa?
(b) Je, Serikali inafikisha lini maji ya Ziwa Victoria katika vijiji vya Mwakuzuka, Mwaningi, Kabondo, Ntundu, Busangi, Buchambaga, Nyamigege, Gula, Izuga, Buluma, Matinje na Bubungu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kuunganisha vijiji vilivyopo umbali wa kilometa 12 kutoka bomba kuu la Ziwa Victoria hadi Kahama na Shinyanga unatekelezwa chini ya programu ya maendeleo ya sekta ya maji. Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji vijiji 40 viliainishwa, kati ya hivyo vijiji 32 vimefanyiwa usanifu. Hadi sasa jumla ya vijiji 13 uunganishaji umekamilika na vijiji hivyo ni Nyashimbi, Magobeko, Kakulu na Butegwa, hilo ni Jimbo la Msalala. Ng’homango, Kadoto, Jimondoli, Mwajiji, Ichongo, Lyabusalu na Bukamba hili ni Jimbo la Shinyanga Mjini na Runere na Gatuli hii ni Kwimba; na vijiji viwili vilivyopo Shinyanga Vijijini ambavyo ni Mwakatola na Mwasekagi uunganishaji unaendelea. Hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 1.96 zimetumika kwa ajili ya kuunganisha maji kwa vijiji hivyo kutoka bomba kuu la Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Mwakuzuka, Kabondo, Ntundu, Busangi, Nyamigenge na Gula vipo katika mpango wa awamu ya kwanza na usanifu wake umekamilika na ujenzi unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, Serikali itaendelea kuunganisha vijiji vilivyobaki vikiwemo vijiji vya Mwaningi, Buchamba, Izuga, Buluma, Matinje na Bubungu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Msalala kwa kusaidiana na Mbunge wao wameanza ujenzi wa Vituo vya Afya Bugarama, Mega, Ngaya na Isaka na miradi hiyo ipo katika hatua nzuri.
(a) Je, Serikali imejipangaje kusaidia miradi hiyo ya ujenzi wa Vituo vya Afya?
(b) Je, Serikali imejipangaje kukamilisha maboma zaidi ya 28 ya zahanati kwenye vijiji mbalimbli Jimboni Msalala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa kujibu maswali, naomba uniruhusu nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya na nguvu kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pili, naomba nimshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Uongozi wote wa Bunge kwa malezi na maelekezo ambayo nimepata, bila kusahau Kamati ya Bajeti, chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Hawa Ghasia kwa malezi na ushirikiano ambao nimekuwa nikiupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kwangu kwa kuniteua kuhudumu katika nafasi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI. Uteuzi uliopokelewa kwa mikono miwili kwa wananchi wa Kalambo na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Msalala kwa jitihada anazofanya katika kuwahamasisha wananchi wake kuibua na kuanzisha miradi mingi ya ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya katika Jimbo lake la Msalala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ina jumla ya vituo vya afya vitatu ambavyo ni Lunguya, Chela pamoja na Bugarama vilivyosajiliwa kwa mujibu wa sheria. Kati ya vituo hivyo, ni vituo viwili ambavyo ni Kituo cha Afya cha Lunguya na Chela ndivyo vinavyotoa huduma za upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito.
Aidha, ujenzi wa vituo vingine vitatu ambavyo ni Isaka, Ngaya na Mega upo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi ambapo lengo la Serikali ni kuwa ifikapo mwaka 2020 vituo hivi viwe vimekamilisha miundombinu muhimu inayohitajika kustahili kuwa vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ina jumla ya maboma 31. Miongoni mwa maboma hayo, matatu ni vituo vya afya tarajiwa ambavyo ni Isaka, Mega na Ngaya. Aidha, kwa sasa Vituo vya Mega na Ngaya maboma yamepauliwa katika jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambapo Boma la Kituo cha Afya cha Isaka lipo kwenye hatua za lenta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali iliweza kukamilisha ujenzi wa zahanati mpya nne kwa gharama ya kiasi cha shilingi milioni 277 na saba ambazo zote zipo katika kata ambazo zilikuwa hazina huduma za afya kabisa. Zahanati hizo zipo katika Vijiji vya Nyaminje, Mbizi, Mwanase na Mwakata ambapo kukamilika kwake kumepunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika mpango wa kitaifa wa kuboresha vituo vya afya kwa ajili ya kutoa huduma za dharura kwa upasuaji wa akina mama, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imepatiwa kiasi cha shilingi milioni 400 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kujenga wodi ya wanawake, nyumba ya watumishi, jiko, jengo la kuhifadhia maiti na ukarabati wa miundombinu ya nyumba za watumishi iliyochakaa katika Kituo cha Afya cha Chela. Kituo cha Afya cha Chela tayari kina jengo la upasuaji, wodi ya wazazi, maabara, kichomea taka, shimo la kutupia kondo la nyuma na mfumo wa maji safi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga kiasi cha shilingi 336,742,394 za ruzuku ya maendeleo( CDG) kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati katika vijiji saba vya Nyamigege, Gula, Ikinda, Kalole, Jomu, Buchambaga na Ndala, kati ya hayo maboma 31.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Mwaka 2014/2015 Serikali iliahidi kuongeza usambazaji maji katika vijiji 100 vilivyoko umbali wa kilometa 12 kutoka bomba kuu la Ziwa Victoria hadi Kahama na Shinyanga na Serikali ilishatenga shilingi bilioni nne ili kutekeleza mradi huo.
(a) Je, vijiji vingapi vimeshapatiwa maji kati ya hivyo 100 hadi sasa?
(b) Je, Serikali itafikisha lini maji ya Ziwa Victoria katika Vijiji vya Mwakazuka, Mwaningi, Kabondo, Ntundu, Busangi, Buchambaga, Nyamigege, Gula, Izuga, Buluma, Matinje na Bubungu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Maige, Mbunge wa Msalala lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatekeleza mradi wa maji wa vijiji 100 vilivyopo kandokando ya bomba kuu kutoka Ziwa Victoria hadi Kahama, Shinyanga. Utekelezaji wa mradi huo unafanywa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika awamu ya kwanza jumla ya vijiji 40 vilivyopo katika Halmshauri za Msalala, Misungwi, Kwimba na Shinyanga vimetambuliwa na ujenzi wa miradi ya maji ambapo katika vijiji 33 umekamilika na baadhi ya vijiji vingine vinaendelea na ujenzi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vilivyotajwa juu ni miongoni mwa vijiji 100 vilivyotambuliwa. Tayari halmashauri ya Msalala imekamilisha usanifu wa kina kwenye vijiji vya Ntundu, Busangi, Nyamigege, Gula, Ntobo, Masabi na Chela. Aidha, vijiji vya Mwakazuka, Kabondo na Izuga zabuni zake zimeshatangazwa na KASHWASA na tayari mkandarasi amepatikana. Vijiji vya Mwaningi, Buchambaga, Buluma, Matinje na Bubungu vipo katika hatua za awali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga na kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vinavyoendelea na vilivyobaki kulingana na bajeti ilivyotengwa.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Ilani ya CCM 2015 - 2020 imeelekeza kwamba Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara inayounganisha Mji wa Kahama (Manzese) hadi Geita kupitia Mgodi wa Bulyanhulu na upembuzi yakinifu ulishakamilika na Mheshimiwa Rais katika ziara yake aliahidi ujenzi huo kuanza mwaka 2017/2018.
(a) Je, ni kiasi gani cha fedha kinahitajika ili kutekeleza mradi huo?
(b) Je, Serikali imejiandaaje kuanza ujenzi huo mwaka 2017?
(c) Kwa kuwa mara zote miradi ya Serikali huchelewa kutokana na ukosefu wa fedha, je, Serikali imewashirikisha wawekezaji wa Migodi ya Buzwagi, Bulyanhulu na Geita ili washiriki katika ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kahama hadi Geita yenye urefu wa kilometa 139 imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na Wizara imefanya mazungumzo ya awali na wawekezaji wa mgodi wa Bulyanhulu, Kampuni ya Acacia Mining, ili kuona uwezekano wa kushirikiana katika ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami baada ya Kampuni hiyo kuonesha nia ya kushirikiana na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambazo ni hatua za awali za maandalizi ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hizi zimekamilika, sasa ujenzi ndiyo hatua inayofuata. Aidha, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga shilingi 12,403,000,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami, barabara ya Kahama - Geita.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Wananchi wa Msalala hususan wakazi wa Bulyanhulu wamefanyiwa dhuluma nyingi sana na Mgodi wa ACACIA, Bulyanhulu ikiwemo kuondolewa kwenye maeneo yao bila fidia mwaka 1996 na kwa wale wanaopata kazi mgodini kufukuzwa kazi bila kufuata utaratibu, kupata madhara makubwa ya kiafya na hata kusababishiwa vifo; na Serikali ya Awamu ya Tano imesimama kidete kutetea wananchi na kuwaepushia dhuluma hizi.
Je, ni hatua gani imefikiwa katika mazungumzo kati ya ACACIA na Serikali kuhusu ulipaji fidia kutokana na dhuluma hizo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa madini, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Bulyanhulu unamilikiwa na Kampuni ya ACACIA na unaendelea shughuli zake za uchimbaji madini tangu mwaka 2000. Kabla ya kuanzishwa kwa mgodi huo fidia stahiki kwa ardhi ya wananchi iliyotwaliwa ililipwa. Kwa sasa mgodi hauna madai yoyote ya wananchi wa Bulyanhulu yatokanayo na fidia ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007 wafanyakazi wapatao 1,331 wa Mgodi wa Bulyanhulu walifanya mgomo kinyume cha sheria hivyo wakaachishwa kazi. Hata hivyo wafanyakazi 643 walirudishwa kazini. Tarehe 6 Novemba, 2007 wafanyakazi 658 waliogoma kurudi kazini walifungua kesi mahakamani na kuomba kufanyiwa uchunguzi wa kiafya ili kubaini hali za afya zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uchunguzi huo wafanyakazi 78 walionekana kuwa na matatizo ya kiafya. Kwa sasa kampuni ya ACACIA inajadiliana na Serikali kupitia OSHA na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuhusiana na madai yao ya matibabu na fidia kulingana na sheria za nchi. Ili kupunguza magonjwa yanayohusiana na kazi za migodini Wizara inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa kuzingatia usalama, afya mahali pa kazi, pamoja na utunzaji wa mazingira.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Wakati akihutubia mkutano wa kampeni Kharumwa Mheshimiwa Rais aliwaahidi wananchi wa Nyang’hwale kwamba barabara ya Kahama – Busangi – Kharumwa – Buyagu – Busisi itajengwa kwa kiwango cha lami; na Ilani ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 imesema barabara ya Kahama - Bulige – Solwa – Mwanangwa itafanyiwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami.
Je, kuna maandalizi gani yanayoendelea ya kutekeleza ahadi hiyo ya Rais na ile ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba kwanza nianze kwa kuwatakia ndugu zangu waislam wote nchini mfungo mwema katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kahama – Busangi – Kharumwa – Buyagu hadi Busisi yenye urefu kilometa 156.68 ni barabara ya mkoa inayounganisha mikoa mitatu ya Shinyanga, Geita na Mwanza. Aidha, barabara ya Kahama - Bulige – Solwa – Mwanangwa yenye urefu wa kilometa 150 ni barabara ya mkoa inayounganisha mikoa ya Shinyanga na Mwanza. Barabara hizi ni miongoni mwa barabara ambazo Serikali imepanga kuzijenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu kuwa Wizara yangu itaendelea kutekeleza ahadi za viongozi wakuu kwa awamu kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, barabara ya Kahama – Busangi – Kharumwa – Buyagu – Busisi itatekelezwa kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara ya Kahama – Bulige – Solwa – Mwanangwa (kilometa 150) ni kweli ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. Napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kuwa tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii umekamilika, kama ilani inavyoelekeza. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha za kugharamia ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Jeshi la Polisi kupitia IGP Ernest Mangu ambaye alifanya ziara Wilayani Kahama mapema mwezi Agosti, 2016 alitangaza kuanzisha Mkoa mpya wa Kipolisi wa Kahama na Wilaya za Kipolisi za Msalala, Ushetu na Kahama; na wilaya hizo mpya za kipolisi zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa askari na vitendea kazi vyao hasa vyombo vya usafiri:-
i. Je, ni watumishi wangapi wamepangwa Wilaya mpya ya Kipolisi ya Msalala?
ii. Je, Serikali iko tayari kusaidia vyombo vya usafiri hasa magari na pikipiki Wilaya ya Kipolisi ya Msalala?
iii. Je, Serikali imejipangaje kujenga ofisi za polisi wilaya na nyumba za makazi kwa askari katika Wilaya za Msalala, Ushetu na Kahama Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uhitaji wa huduma ya kipolisi katika maeneo ya Ushetu, Msalala na Kahama. Aidha, maombi ya Msalala kuwa Wilaya ya Kipolisi yameshakamilika na maombi ya Kahama kuwa Mkoa wa Kipolisi yanaendelea kuzingatiwa. Kwa sasa Wilaya ya Msalala ina jumla ya maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali 57.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nia ya Serikali kuona kuwa vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi vinapatikana ili kurahisisha utoaji wa huduma za polisi kwa wananchi. Wilaya mpya ya Msalala imepatiwa mgao wa gari moja jipya na taratibu za usajili zitakavyokamilika gari hilo litapelekwa Msalala kwa ajili ya kuhudumia wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Msalala, Ushetu na kahama Mjini ni miongoni mwa wilaya 65 nchini ambazo hazina majengo ya vituo vya polisi vyenye hadhi ya wilaya. Hata hivyo, halmashauri ya wilaya imeshatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo na makazi ya askari na ujenzi utaanza mara pale fedha zitakapokuwa zimepatikana.
MHE. SELEMANI J. ZEDI (K.n.y. MHE. EZEKIEL M. MAIGE) aliuliza:-

Wananchi wa Msalala wengi wao ni wachimbaji wadogo, lakini hawana maeneo ya kufanyia kazi, maeneo mengi ya kufanyia kazi yana leseni za wachimbaji wakubwa na hawazifanyii kazi:-

(a) Je, kuna leseni ngapi za utafiti wa madini zilizotolewa kwa maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala?

(b) Je, ni maeneo gani Serikali inadhamiria kuyatoa kwa wachimbaji wadogo wa Msalala?

(c) Je, kwa kuanzia, Serikali inaweza kuwaruhusu wananchi wafanye uchimbaji mdogo kwenye maeneo ya reef 2, Kijiji cha Kakola namba Tisa, Kata ya Bulyanhulu, Bushimangila na Msabi Kata ya Mega na Lwabakanga na Nyangalata Kata za Lunguya na Bulyanhulu?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ya Hamashauri ya Wilaya ya Msalala kuna jumla ya leseni hai 78 za utafutaji madini na leseni za uchimbaji mdogo 53 zilizokwishatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Msalala, Serikali imetenga eneo la Nyangalata lililopo katika Kata ya Lunguya lenye ukubwa wa kilometa za mraba 10.74 kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Hata hivyo, Serikali imedhamiria kutenga maeneo mengi zaidi katika Halmashauri ya Msalala, maeneo hayo ni Kata ya Segese maeneo mawili yenye ukubwa wa kilometa za mraba 19.67 na 9.84; Kata ya Mega lenye ukubwa wa kilometa za mraba 4.93; na Kata ya Kalole lenye ukubwa wa hekta 360.13.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haiwezi kuruhusu wachimbaji wadogo kufanya shughuli za uchimbaji katika maeneo ya Reef 2, Lwabakanga na Namba Tisa katika Kijiji cha Kakola, Kata Bulyanhulu kwa kuwa yamo ndani ya leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini (special mining license) Na. 44/99 inayomilikiwa na Kampuni ya Bulyanhulu Gold Mine. Aidha, maeneo ya Bushimangila na Masabi yaliyopo katika Kata ya Mega yamo ndani ya maeneo yaliyoombewa leseni ya uchimbaji mdogo (primary mining license). Hivyo, natoa wito kwa wananchi wa Halmashauri ya Msalala kuchangamkia fursa katika maeneo yaliyotengwa na kupewa leseni ya uchimbaji mdogo ya Nyangalata.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-

Serikali ya Tanzania ni mdau mkubwa wa Mradi wa Bomba la Mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga na Serikali pamoja na wawekezaji katika mradi huu walishateua eneo la kujenga kiwanda cha kuunganisha na ku-coat mabomba katika Mji Mdogo wa Isaka.

Je, ni hatua gani imefikiwa katika ujenzi wa kiwanda hicho?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania) linalojulikana kama bomba la Afrika Mashariki (East Africa Crude Oil Pipe – EACOP Project) umeainisha maeneo ya ardhi kwa ajili ya kazi za awali. Maeneo hayo yanazingatia vipaumbele vya mradi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kiwanda cha upigaji rangi mabomba uliopo kati ya Kijiji cha Sojo, Kata Igusule, Wilaya ya Nzega, Mkoa wa Tabora karibu na eneo la reli inayoenda Isaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwanda hicho muhimu katika mradi wa bomba utaanza mara tu baada ya kukamilika kwa zoezi la kuthaminisha na kutoa ardhi husika na kukabidhiwa mkandarsi wa ujenzi. Kwa sasa, taratibu za utoaji ardhi ziko katika hatua za mwisho na zinatarajia kukamilika mapema mwezi Julai, 2019. Mkandarasi anatazamia kukabidhiwa eneo la mradi na kupeleka vifaa mwezi Septemba 2019. Aidha, mpango wa usimamizi wa mazingira na jamii umekamilika na kuidhinishwa na Baraza la taifa la usimamizi wa mazingira NEMC.
MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y. MHE. EZEKIEL M. MAIGE) aliuliza:-

Wananchi wa Msalala kwa juhudi zao wamejenga mabweni katika Shule za Sekondari za Bulige, Busangi, Baloha, Mwalimu Nyerere, Lunguya, Ntobo na Isaka.


(a) Je, Serikali ipo tayari kuunga mkono juhudi hizo za wananchi kwa kuyatambua mabweni hayo na kuzipatia shule hizo ruzuku za uendeshaji wa mabweni kwa ajili ya umeme, maji, chakula na ulinzi?

(b) Je, Serikali ipo tayari kuongeza miundombinu kama mabwalo ya chakula na nyumba za matron katika Shule hizo?

(c) Je, ni lini Serikali itasaidia wasichana wa Msalala katika Kata nyingine kama Mwanase, Mwalugulu, Jana, Bugerema na Bulyanhulu kwa kuwajengea Mabweni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa Serikali kugharamia shule za bweni na shule za kutwa ni tofauti. Shule zilizotajwa na Mheshimiwa Mbunge ni za kutwa ambazo hupelekewa fedha za fidia ya ada na fedha uendeshaji. Ili shule hizo ziweze kupelekewa fedha kwa ajili ya chakula, ni lazima ziwe zimesajiliwa kama shule za bweni za Kitaifa. Shule za Kitaifa zina sifa ya kuchukua wanafunzi kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara na hushindanishwa kutokana na ufaulu wao.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongeza miundombinu ya mabweni na mabwalo ya chakula kwenye shule hizo, kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni kuongeza mabweni na mabwalo kwenye shule za bweni na kuongeza madarasa, maabara na matundu ya vyoo kwenye shule za kutwa. Katika mwaka fedha 2018/2019, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imepatiwa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya madarasa nane katika shule nne za sekondari. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2019/ 2020 kupitia program ya EP4R, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 58.2 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za sekondari nchini.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Serikali ni kuboresha miundombinu katika shule zote za Serikali. Nazielekeza Halmashauri ziendelee kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kujenga hosteli kwenye shule zilizoko katika maeneo yao ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kujifunzia kwa watoto wa kike nchini. Ahsante.