Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Eng. Edwin Amandus Ngonyani (6 total)

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:-
Wilaya ya Namtumbo haina huduma stahiki za Hospitali ya Wilaya wala Vituo vya Afya licha ya kuwepo kwa Sera ya kila Wilaya iwe na Hospitali ya Wilaya na kila Kata iwe na Kituo cha Afya.
(a) Je, sera hiyo kwa Wilaya ya Namtumbo itatekelezwa lini?
(b) Makadirio yaliyofanywa na TBA kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo ni shilingi bilioni19. Je, Serikali ipo tayari kutenga na kutoa kiasi hicho katika bajeti ya mwaka 2018/2019?
(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa vitendea kazi na wataalam katika Vituo vya Afya vitano vilivyopo Namtumbo ili viweze kutoa huduma bora za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo ulianza rasmi mwaka 2010 na unatekelezwa kwa awamu tofauti ambapo mpaka sasa unaendelea. Aidha, kiasi cha shilingi milioni 600 kimeshatumika kwa ajIli ya kujenga majengo ya utawala, jengo la wagonjwa wa nje yaani OPD, chumba cha kujifungulia yaani labour room, kichomea taka (incinerator), msingi na jamvi kwa chumba cha akina mama wajawazito (maternity ward) pamoja na mfumo wa maji safi na taka (water and sewage system). Kwa mwaka 2017/2018, Halmashauri imepokea shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuendeleza na kumaliza jengo la wodi ya akina mama wajawazito.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo la upasuaji ili kuimarisha huduma za upasuaji katika hospitali hiyo.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Namtumbo ina jumla ya vituo vya afya saba ambapo vitano vinamilikiwa na Serikali na viwili vinamilikiwa na mashirika ya dini. Vituo vya Afya vya Serikali ni Namtumbo, Msindo, Mputa, Mkongo na Lusewa. Vituo vya Afya vya mashirika ya dini ni Namabengo na Hanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, huduma ya upasuaji wa dharura kwa akinamama wajawazito inafanyika katika Kituo cha Afya Hanga. Katika Kituo cha Afya Lusewa, jengo la upasuaji lipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji na vifaa vya upasuaji vipo katika mchakato wa kununuliwa lakini kuna tatizo la maji ambalo pia linashughulikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Namtumbo kimepokea jumla ya shilingi milioni 400 tarehe 21 Desemba, 2017 kwa ajili ya ujenzi, ukarabati wa majengo ya upasuaji, wodi ya wazazi, maabara na chumba cha kuhifadhia maiti ambayo kazi yake inaendelea katika hatua za ukamilishaji na inategemea kukamilika tarehe 30 Aprili,2018. Aidha, Serikali imeagiza vifaa vya chumba cha upasuaji kwa ajili ya kutoa huduma ya upasuaji kwa akina mama wajawazito (CeMOC) kwa Vituo vya Afya vya Msindo na Mputa ili kuondoa tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi.
MHE. DAIMU I. MPAKATE (K.n.y. MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI) aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Nne iliahidi kuanzisha Mkoa mpya wa Selous.
a) Je, ahadi hiyo itatekelezwa lini?
b) Je, Serikali haioni kuwa mpaka wa Kusini wenye urefu wa zaidi ya kilometa 600 na wenye mikoa miwili tu sio salama kiulinzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 15 Julai, 2013 Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa ziarani Wilayani Tunduru alikutana na wazee wa Tunduru walioomba mkoa mpya wa Selous. Katika majibu yake alielekeza taratibu zifuatwe kisheria, kwa maana hiyo, hakuahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelekezo hayo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma imeratibu vikao kadhaa vya kisheria kikiwemo Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Ruvuma cha tarehe 28 Novemba, 2017 kilichosisitiza ombi la kuundwa kwa mkoa mpya wa Selous wenye Wilaya nne za Tunduru, Tunduru Kusini, Namtumbo na Sasawala, Tarafa 10, Kata 53 na Vijiji 212 kwenye eneo lenye kilometa za mraba 38,988 na idadi ya watu 499,913 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetafakari kwa kina maombi hayo na kuyaona kuwa ni ya msingi. Hata hivyo, kutokana na changamoto ya kuimarisha kwanza miundombinu kama majengo ya Ofisi na nyumba za Watumishi na mahitaji mengine kama vifaa ya Ofisi, Watumishi wa kutosha na vyombo vya usafiri kwenye maeneo mapya ya utawala yaliyoanzishwa tangu mwaka 2010 na 2012, Serikali imesitisha uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala hadi maeneo mapya yaliyopo yaimarishwe kikamilifu.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ulinzi na usalama katika mpaka wa Kusini, ipo mikakati ya pamoja baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Msumbiji kuhakikisha kuwa mpaka huo upo salama. Nawaomba wananchi waendelee na shughuli zao bila wasiwasi wowote.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:-
Katika bajeti ya mwaka 2017/2018, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Namtumbo:-
(a) Je, gharama za ujenzi wa chuo hicho hadi kinakamilika ni kiasi gani?
(b) Je, ni lini ujenzi wa chuo hicho utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Edwin Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inategemea kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha VETA cha Wilaya ya Namtumbo kwa makadirio ya Sh.6,321,320,292.40.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya ujenzi ilianza mwezi Machi, 2017 na inakadiriwa kuchukua muda wa miezi
18. Hivyo, ujenzi wa chuo hicho unategemewa kukamilika ifikapo Septemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, itaendelea na ujenzi wa vyuo hivyo kwa ajili ya kuandaa Rasilimali Watu watakaotumika katika viwanda ili kufikia lengo la Serikali kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025. Aidha, vyuo hivi vitasaidia kuwapatia vijana wetu ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:-

Je, Wizara ya Kilimo inashirikianaje na Wizara nyingine zinazohusika na uwekezaji wa mambo ya nje kutafuta soko la tumbaku nchini Misri badala ya kulazimika kutumia nchi za Uganda na Kenya peke yake?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014/2015, uzalishaji wa tumbaku ya moshi (Dark Fire Cured Tobacco- DFC) ulisimama Mkoani Ruvuma kutokana na kukosa soko. Jitihada za Serikali zikawezesha kampuni ya Premium Active Tanzania Limited kuonesha nia ya kununua tumbaku hiyo ya DFC ambayo hapa nchini huzalishwa Namtumbo na Songea Vijijini, Mkoani Ruvuma. Kampuni hii ilieleza kuwa lipo soko kubwa la tumbaku aina ya DFC nchini Misri na Algeria, lakini tumbaku ya Tanzania inauzwa kwa bei ya juu kutokana na kodi inayotozwa ikilinganishwa na aina hiyo ya tumbaku kutoka nchi za Uganda na Kenya kwa kuwa nchi hizo Uganda, Kenya, Algeria na Misri ni wanachama wa Jumuiya ya COMESA na kwa hiyo kodi za kuingiza tumbaku, chai na bidhaa nchini Algeria na Misri kutoka Uganda na Kenya ni za chini ukilinganisha na Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hilo, Wizara ya Kilimo inashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuanzisha mazungumzo na Nchi Wanachama wa COMESA na nchi kama Misri na Algeria kupitia Balozi zetu ili kuandaa makubaliano maalum yaani bilateral agreement yatakayowezesha nchi yetu kupeleka tumbaku katika nchi hizo kwa kodi nafuu. Mazungumzo hayo yamefikia hatua nzuri na matarajio ni kufungua milango ya soko hilo na hivyo kuongeza kipato kwa wakulima na Taifa kwa ujumla. Aidha, makubaliano hayo yakikamilika Tanzania inaweza pia kuuza chai nchini Misri na Algeria kwa faida kuliko ilivyo hivi sasa au badala ya kuuza chai kupitia mnada wa Mombasa nchini Kenya.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:-

Wananchi wa Vijiji vinavyounda Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori waliopo Namtumbo miaka 14 iliyopita walikubaliana kuacha ardhi yao kwa shughuli za hifadhi na kwamba ardhi hiyo isitumike kwa makazi wala kilimo cha mazao ya kudumu isipokuwa mpunga pekee. Wananchi washiriki kutunza njia za asili za wanyama hususan tembo na walikubaliana kwamba mipaka ya ardhi husika ingepitiwa upya baada ya kupita miaka 10 kuanzia mwaka 1996 walipoingia makubaliano:-

(a) Je, kwa nini Serikali imekiuka makubaliano hayo na kuwakaribisha wafugaji kwenye maeneo ya wananchi yaliyokuwa yakitumika kwa kilimo cha mpunga?

(b) Je, ni lini Serikali italipa fidia wakulima ambao mashamba yao ya mpunga yameathiriwa na ng’ombe wanaochunga katika mashamba hayo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo zilizoanzishwa kwa kushirikisha wananchi wenyewe na kutangazwa katika Gazeti la Serikali. Aidha, Serikali haijabadili matumizi ya ardhi hiyo na kuwapatia wafugaji isipokuwa wapo baadhi ya wafugaji waliovamia maeneo hayo bila kufuata taratibu. Serikali inaendelea kuwabaini na kuwaondoa wafugaji ambao wamevamia maeneo yasiyoruhusiwa na kuwapeleka katika maeneo yaliyotengwa rasmi kwa shughuli za ufugaji.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, wapo baadhi ya wakulima waliovamia na kufanya shughuli za kilimo katika eneo la Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori kinyume na sheria. Hivyo, hakuna fidia itakayolipwa na Serikali kwa wakulima waliovamia na kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yasiyoruhusiwa. Viongozi wa Mkoa na Wilaya wanaelekezwa kusimamia na kuhakikisha yanatengwa maeneo rasmi kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo kuepuka uvamizi wa hifadhi.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:-

Mkoa wa Ruvuma umepata mnunuzi wa tumbaku ambaye amekubali kuwawezesha SONAMCU kufufua kiwanda cha kuchambua tumbaku na kugeuza green leaf kuwa dry leaf. Aidha, kutokana na changamoto za kodi na soko mnunuzi huyo hajaweza kutekeleza azma yake.

Je, Serikali inasaidiaje kutatua changamoto zinazomkabili mnunuzi huyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Edward Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Spika, kufuatia kuondoka kwa kampuni mbili za ununuzi wa tumbaku Mkoani Ruvuma msimu wa 2014/ 2015, wakulima walikosa soko la uhakika. Kutokana na hali hiyo Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Mheshimiwa Mbunge Ngonyani walifanya juhudi za kutatua changamoto hiyo.

Mheshimiwa Spika, jitihada hizo zilisaidia kupatikana kwa mnunuzi wa tumbaku ambaye ni Kampuni ya Premium Active Tanzania Limited ambayo ilianza kununua kilo 250,000 na sasa imeongeza hadi kilo 1,000,000. Serikali pia inapongeza nia ya kampuni hiyo ya kutaka kukiwezesha Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa huo cha SONAMCU kufufua kiwanda cha kuchakata tumbaku.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo Wizara ya Kilimo ipo tayari kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na mwekezaji huyo kutafuta ufumbuzi wa changamoto za mnunuzi huyo ili kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inatimiza azma hiyo njema kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na taifa kwa ujumla, ahsante.