Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Martin Alexander Mtonda Msuha (20 total)

MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na pia nashukuru kwa pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni lini sasa hii kazi ya upembuzi yakinifu itakamilika ili ujenzi uanze?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, wananchi wa Mbinga pamoja na Nyasa wanafurahi na wanaishukuru Serikali kwa kupata mradi wa ujenzi wa barabara wa Mbinga – Mbamba Bay chini ya mradi wa Mtwara Corridor. Je, Serikali haioni haja sasa kwa kutumia fursa hii kuunganisha kipande cha barabara inayotoka Unyoni mpaka Kijiji cha Mango Wilayani Nyasa kupitia Mapera, Maguu na Kipapa? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martin Mtonda Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Martin Mtondo Msuha pamoja na Mheshimiwa Stella Manyanya kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha Wilaya yao ya Mbinga inakuwa na miundombinu ya uhakika ili mazao wanayoyalima hasa kahawa inalifikia soko kwa urahisi na kwa bei nafuu. Mimi niwapongeze sana na nawahakikishieni kwamba nikiwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Mheshimiwa Waziri wangu tutahakikisha dhamira yenu inakamilika katika kipindi hiki cha miaka mitano kwa kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, kwanza naomba tuikamilishe na suala la tunaikamilisha lini kwa maana ya kutoa tarehe sio rahisi sana kwa sababu kwa sasa tupo katika hatua ya kumpata huyo mkandarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mtuamini kwamba tuna nia ya dhati, kazi hiyo tutaifanya na tutaisimamia na itakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili, naomba niwajulishe Waheshimiwa Wabunge wote wa Wilaya ya Mbinga kuanzia Mheshimiwa Mtondo Msuha, Mheshimiwa Stella Manyanya na Mheshimiwa Sixtus Mapunda kwamba mwaka huu tunaanza kuijenga ile barabara ya kutoka Mbinga - Mbamba Bay.
Naomba mtupe fursa tuikamilishe barabara hii. Mtakumbuka ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kutembea kwa taxi kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay na kutoka Bukoba hadi Mtwara itakuwa imekamilika kikamilifu kabisa. Baada ya hapo, nawahakikishia nguvu zetu zote tutakuwa tunaelekeza katika barabara hizo zingine ikiwa ni pamoja na hii barabara ya kutoka Unyoni hadi Mango kupitia vijiji ambavyo Mheshimiwa Mtondo Msuha amevitaja.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante! Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa umbali wa kutoka Songea na Mamba Bay - Nyasa bado ni mrefu, Serikali haioni haja ya kufunga mitambo angalau kwenye milima ya Mbuji ili kuongeza usikivu katika tarafa hizo zilizotajwa?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upembuzi uliyofanyika, huu mtambo utakaofungwa Mbamba Bay utakuja kukutana na mtambo uliofungwa hapa Matogolo na kwa pamoja usikivu utaongezeka badala ya kufunga kwenye Kata ya Mbuji kama anavyosema. Ni upembuzi wa Kitaalam umefanyika na hili likifanyika tutaongeza usikivu katika eneo lake na kwa sababu ni matokeo ya utafiti tunaamini hili likifanyika basi hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge anayaombea hapa yatakuwa yamefanyika na usikivu utaongezeka.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kuuliza maswali mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazingira ya Jimbo la Mlimba yanafanana kabisa na mazingira ya Jimbo Mbinga Vijijini, je, Serikali itapeleka maji lini katika Miji ya Maguu, Matiri na wa Rwanda ambao una taasisi nyingi sana zikiwemo sekondari za form five na six?
Mheshimiwa Naibu Spia, swali la pili, katika Jimbo la Mbinga kuna miradi miwili ya maji iliyokuwa ikiendelea katika Kata ya Mkako lakini pia mradi mwingine katika Kata ya Ukata kupitia Kijiji cha Litoho. Ni lini Serikali itakamilisha miradi hii ya Mkako pamoja na Ukata ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maji salama na safi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itahakikisha inapeleka maji katika maeneo ya Mbinga Vijijini, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tayari tumeanza Programu ya Pili ya Utekelezaji wa Maendeleo ya Sekta ya Maji Nchini. Kama nilivyokwishatoa majibu kwamba wafadhili wametuahidi dola za Kimarekani bilioni 3.3 ambazo zitatumika kutekeleza miradi ya maji hapa nchini, hii ikiwa ni pamoja na miradi ya Mbinga Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu wa fedha Mbinga Vijijini tumewatengea fedha. Niagize na naomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane tutengeneze mpango mzuri wa matumizi ya fedha hizi tulizozitoa katika hii bajeti ya mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai ili kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo ya Mbinga Vijijini wote wanapata maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili umesema kwamba kuna miradi miwili ambayo bado haijakamilika. Tumeshaelekeza kwamba miradi ile ambayo haikukamilika katika Programu ya Kwanza ya Utekelezaji wa Sekta ya Maji ndiyo tunaanza kuikamilisha kabla hatujaanza miradi mipya. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane na Halmashauri yake kuhakikisha kwamba kwanza tunakamilisha miradi hii kabla hatujaanza kuingia kwenye miradi mipya.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nami pia niungane na Serikali kwanza kuwapongeza wananchi wa Kata za Mkumbi, Kata za Kipololo na Ukata ambao walikubali kupisha mradi huu kwa ustawi wa uchumi wa Wilaya yetu. Hata hivyo nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa upana wa barabara hii, barabara hii inaanzia Mbinga Mjini inapita Litowo lakini pia inaunganisha na Wilaya ya Nyasa. Mfadhili amekubali kujenga kutoka Longa hadi Litoho; kuna kipande cha kilomita 15 kutoka Mbinga Mjini haji Kijiji cha Longa. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kutumia nguvu zetu za ndani ili kukamilisha kipande hiki cha kutoka Mbinga Mjini hadi Longa chenye umbali wa kilomita 15?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, barabara yetu inayotoka Mbinga Mjini kwenda Hospitali ya Litembo kupitia Kijiji cha Tanga – Uyangayanga - Kindimba - Mundeki ni muhimu sana kwa vile Hospitali hii inatumika kama Hospitali yetu ya Rufaa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuijenga barabara hii inayoelekea Hospitali ya Rufaa ya Litembo ili kurahisisha huduma za afya katika eneo hilo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nami nawapongeza sana wananchi hawa kwa sababu barabara hii ina Euro karibu milioni nne ambayo ukipiga mahesabu inaenda karibu shilingi bilioni kumi na eneo lile nadhani Mheshimiwa Mbunge anafahamu, kwanza kuna changamoto kubwa sana ya milima; lakini tumepata ufadhili mkubwa, kwa hiyo, hata zao la kahawa sasa watu watakuwa na fursa ya kuweza kusafirisha vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lake ni kwamba hiki kipande cha katikati cha kutoka Mbinga Mjini mpaka Longa ambacho kina kilomita 15 ni jinsi gani tutafanya sasa kipande hiki kiweze kuunganishwa? Mheshimiwa Mbunge, tumelisikia hili, lakini naomba michakato hii sasa ianze katika bajeti kuonyesha kwamba kuna uhitaji kutoka Halmashauri husika, nasi tutaangalia kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua kwamba barabara hii, hiki kipande cha kilomita 15 bajeti yake itakuwa ni kubwa, lakini nadhani kwanza muanze kuangalia jinsi ya kufanya kwamba Halmashauri ionyeshe kipaumbele katika eneo hilo. Katika mchakato wa bajeti, Serikali itaangalia namna ya kufanya ili eneo hilo sasa liweze kupewa kipaumbele, angalau kipande cha lami kiweze kuunganishwa na mwisho Nyasa na Mbinga iweze kuunganika vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kusema kutoka Mbinga Mjini mpaka Kihesa ambako kuna Hospitali, wananchi wanapata huduma pale, vilevile naomba nirejee katika jibu langu la kwanza kwamba tuweke kipaumbele na Serikali haitasita kuona kwamba kwa sababu ni maeneo ambayo wananchi wanapata huduma hasa ya afya, nasema kipaumbele hiki lazima tukifanyie kazi.
Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi ile anayoendelea kuifanya na Madiwani wake, waweke katika mpango, Serikali itaujadili kwa kina na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI hatutasita kushirikiana na Halmashauri ya Mbinga kuhakikisha maeneo haya yanapata huduma kama maeneo mengine.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Spika, asante pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, mpango wa REA III una-cover mwaka 2016 mpaka 2019/2020. Serikali ina mpango gani kushirikisha Waheshimiwa Wabunge katika kupanga maeneo ya kupeleka umeme katika miaka hiyo husika kuzingatia kwa bajeti ya kila mwaka?
Mheshimiwa Spika, swali la pili Mkoa wa Ruvuma haujaunganishwa bado na umeme wa Gridi ya Taifa. Ni lini sasa mradi wa umeme wa Gridi ya Taifa kutoka Makambako kwenda Songea utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, nishukuru kabisa Mheshimiwa Mbunge ametukumbusha kwamba tuwaambie Waheshimiwa Wabunge. Kwanza kabisa niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, mradi wa REA Awamu ya Tatu unaoanza sasa tunatumia utaratibu ufuatao:-
Mheshimiwa Spika, wakandarasi watakapokuwa wanaingia site kuanzia Disemba mwaka huu, hatua ya kwanza itakuwa ni kukutana na kukubaliana na Waheshimiwa Wabunge kabla hawajaanza kazi kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nitoe tu angalizo lingine, kwamba tumeweka utaratibu sasa mahali ambako kuna Ofisi zetu za TANESCO tumeandaa kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa kuweka vituo rasmi ili wananchi wasiende kwenye Ofisi za TANESCO ila wafanyakazi wa TANESCO wakae kwenye vituo ambavyo Serikali za Mitaa zitakuwa zimetambua.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wabunge pamoja na Diwani watashirikishwa sana kabla ya utekelezaji wa mradi huu kuanza.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mradi wa Makambako – Songea, mradi wa Makambako – Songea una sehemu tatu za utekelezaji. Sehemu ya kwanza ni ujenzi wa distribution line ambao inachukua urefu wa kilomita 900 kwa maeneo yote ya Mbinga, Songea na maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, mradi huu ulianza mwaka juzi na unakamilika mwakani mwezi Julai. Sehemu ya pili ni kujenga transmission line ambayo imeanza mwaka jana na hivyo itakamilika mwezi Septemba, 2018. Hatua ya tatu ni kujenga substations tatu, moja ikiwa Makambako, nyingine Songea na nyingine eneo la Madaba, kwa ujumla wake kazi zote zitakamilika mwezi Mei, 2018.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa vile madeni haya yamechukua muda mrefu; je Serikali iko tayari kufikiria kulipa pamoja na riba kwa Mawakala hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kumekuwepo
na tatizo la pembejeo ambazo hazina ubora; je, Serikali ina mpango gani kuimarisha ukaguzi wa maduka ya pembejeo za kilimo ili kuhakikisha wananchi hawa wanapata pembejeo zenye ubora stahiki? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na madeni ulipwaji wake kucheleweshwa na hivyo kustahili kulipwa riba; nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ucheleweshwaji wa ulipwaji umetokana vilevile na kasoro ambazo hata Mawakala wenyewe wanahusika katika kasoro hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba suala la pembejeo limekuwa ni moja kati ya maeneo ambayo kuna wizi mkubwa sana wa fedha za umma. Kwa hiyo, ukiona kwamba kuna ucheleweshaji kidogo ni kwa sababu tunataka tufanye malipo sahihi, hatutakubali tena fedha za umma ziibiwe na wajanja wachache kwa kisingizio kwamba huduma imetolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, pamoja na kwamba tunathamini mchango mkubwa sana wa Mawakala wa Pembejeo katika kuendeleza Sekta yetu ya Kilimo, lakini niwaeleze tu kwamba hili ni eneo ambalo Serikali imepoteza fedha nyingi sana. Katika ukaguzi wa awali ambao tumefanya kama Wizara katika mikoa nane ambayo imepata ruzuku kubwa, walikuwa wanadai shilingi bilioni 36. Kati ya hizo ni shilingi bilioni nane tu ambazo zimeonekana zinaweza kulipwa bila utata. Kwa hiyo, unaweza kuona ni kwa kiasi gani tumekuwa tukipoteza fedha nyingi kwa kukimbilia kulipa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, naombeni wale mnaotoka maeneo ambayo pembejeo ya ruzuku imepelekwa, mtufahamishe upungufu unatokea kule. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Keissy kwa sababu yeye amekuja mbele na kutueleza kuhusu udanganyifu uliofanywa na Mawakala katika Jimbo lake. Vilevile juzi Mheshimiwa Flatei Massay, naye kaeleza upungufu uliotokea Wilayani kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kulipa madeni yale ambayo ni sahihi, lakini kwa bahati mbaya sana kuna Mawakala ambao hawana makosa lakini wanapata matatizo kwa sababu ya makosa ya Mawakala ambao sio waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile lazima niseme udanganyifu huu haukufanyika na Mawakala peke yao, hata Maafisa wa Serikali wamekuwa ni sehemu ya mfumo mbovu ambao umekuwa ukiibia fedha Serikali. Kimsingi tu, katika Serikali ya Awamu ya Tano hili hatutaki litokee na ndiyo maana tumebadilisha mfumo na kwa sasa hatuna tena mfumo wa vocha.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya maji na umwagiliaji nchini imetekelezwa chini ya kiwango ukiwemo mradi wa maji unaotekelezwa katika Kata ya Mkako, Wilayani Mbinga. Mradi huu wa Mkako ulikuwa ukabidhiwe katika Mbio za Mwenge zilizofanyika wiki iliyopita, wananchi waliukataa kwa sababu hautoi maji kabisa. Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam Wilayani Mbinga kukagua Mradi wa Mkako pamoja na miradi mingine ya Kigonsera, Litoho na ya kijiji cha Kiongo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, amesema kwamba miradi mingi ya maji imejengwa chini ya kiwango. Sawa inawezekana ni hilo, lakini sisi taarifa tuliyonayo ni kwamba miradi mingi ilibuniwa lakini baada ya kujengwa vile vyanzo vya maji vimekosa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inawezekana ni kwa ajili ya kukosa maji au ilikuwa vimejengwa vibaya, hilo linahitaji utafiti ili tuweze kulidhihirisha na tuweze kulitolea majibu katika Bunge hili.
Hata hivyo, kama kweli mradi umejengwa chini ya kiwango, basi Halmashauri husika inatakiwa ilione hili, iweke wataalam walifanyie uchunguzi kuona tatizo lilikuwa liko wapi. Wakiona kuna tatizo sheria stahiki zitachukuliwa ili tuweze kuhakikisha kwamba mradi huo tunauboresha wananchi wapate maji safi na salama.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Wilayani Mbinga yako mawe mawili makubwa ya ajabu ambayo yanafahamika kwa jina la Mawe ya Mbuji; mawe haya yanasadikika kuwa ni jiwe la kike na la kiume; lakini pia katika mawe hayo viko viumbe hai vyenye kimo kifupi sana vinavyofanana na binadamu, viumbe hivi huwa vinajitokeza hasa msimu wa michezo ya utamaduni. Je, ni lini Serikali itafanya utafiti ili kubaini ni viumbe vya aina gani hivyo ambavyo vinaishi katika mawe hayo na hatimaye kutangaza eneo hilo kama eneo la utalii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye maswali ya nyongeza yaliyotangulia, nimesema nchi hii ni tajiri sana ya vivutio vya utalii, jambo ambalo hatujalikamilisha bado na tunaendelea kulifanya ni kuwa na orodha ya vivutio hivyo vilivyohakikiwa kwa sababu siyo kila kitu ambacho mtu mmoja anaweza kukiona kwamba kinatosheleza kuwa kivutio cha utalii, kinakuwa hivyo; ni mpaka wataalam wanaohusika waseme kwamba sasa hiki kinakidhi viwango vya Kimataifa vya kuwa kivutio cha utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii, tayari imeshawasiliana na Halmashari zote nchini ili kuweza kuviorodhesha vivutio hivyo, vifike Wizarani, tuvifanyie uchambuzi halafu tuweze kuviweka katika makundi (grading) halafu tuweze kuweka mkakati wa pamoja wa namna gani ya kutangaza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema jukumu la kutangaza lisiwe jukumu la Serikali peke yake; kama mnavyofahamu na mnavyoona, dunia ya sasa ni kama kijiji; na kila mmoja akitumia wajibu wake wa kutumia mifumo ya mawasiliano ya kisasa, tunaweza kutangaza nchi yetu kwa namna ambayo ni ya mafanikio zaidi.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninalo swali moja la nyongeza.
Lipo tatizo kubwa na la muonekano na upatikanaji
wa TBC1 kwenye maeneo mengi ya Wilaya ya Mbinga lakini pia ukanda mzima wa Ziwa Nyasa hususani kule kwenye tarafa ya Mhagati, Tarafa ya Mkumbi lakini pia Tarafa ya Namswea. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha upatikanaji wa TBC1 katika maeneo tajwa hapo juu ukizingatia hicho ndicho kituo pekee kutoa matangazo bila kulipia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama tutakumbuka katika bajeti ya mwaka huu zilitengwa shilingi bilioni tatu zaidi kama fedha za maendeleo kwa TBC na hizi ni pamoja na kuboresha television ya TBC1 pamoja na usikivu wa redio. Kwa hiyo, mpaka sasa katika maeneo aliyoyataja ya Mhagati, Namsweha na maeneo mengine, TBC bado inafanya tathmini kuona mgawanyo huo wa fedha uelekee wapi kwa upande kwa radi na uelekee wapi kwa upande wa television. Naomba kuwasilisha na ahsante.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, jambo mojawapo linaloyumbisha uzalishaji wa kahawa hususan Mbinga, ni kutokuwa na bei ya uhakika mwaka hadi mwaka. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha mfuko wa kuimarisha bei ya mazao hususan kahawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuambatana na mimi baada ya mkutano huu, ili akajionee mwenyewe ni jinsi gani utekelezaji na uzambazaji wa miche mipya ya kahawa unavyofanyika na Kituo cha TaCRI - Ugano, kama ilivyojibiwa kwenye swali la msingi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa jimbo hilo kwa ajinsi ambavyo anafuatilia kwa ukaribu sana katika zao zima hili la kahawa katika Jimbo lake. Lakini nikija katika swali lake la (a) ni kwamba, sisi kama Wizara kupitia Bodi ya Kahawa tunatoa bei elekezi kwa wakulima wale wadogowadogo wote kwa maana ya kwamba, farm gate market kwamba wawe wanapata bei elekezi kupitia njia ya mtandao wa simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile tumegundua kwamba, njia hii ya mtandao wa simu iko more effective ukilinganisha na ile minada mingine, lakini hii tunaifanya kila wiki. Lingine naomba nitoe rai hata kwa wakulima wale wadogowadogo wote katika mashamba kwamba, wanapaswa wazingatie sana ubora wa zao hili la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine vilevile kule Moshi ambako tunafanya mnada, huu mnada kule Moshi hatuwezi tukafanya kwa bei elekezi kwa sababu, mnada wa kule unategemea sana soko la dunia na kwa maana hiyo, soko la dunia inategemea na wakati wa ile market price iliyoko wakati huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho naomba nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kuongozananae kwenda kujithibitishia zao la kahawa. Ahsante.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Wilayani Mbinga yako mawe mawili makubwa ya ajabu ambayo yanafahamika kwa jina la Mawe ya Mbuji; mawe haya yanasadikika kuwa ni jiwe la kike na la kiume; lakini pia katika mawe hayo viko viumbe hai vyenye kimo kifupi sana vinavyofanana na binadamu, viumbe hivi huwa vinajitokeza hasa msimu wa michezo ya utamaduni. Je, ni lini Serikali itafanya utafiti ili kubaini ni viumbe vya aina gani hivyo ambavyo vinaishi katika mawe hayo na hatimaye kutangaza eneo hilo kama eneo la utalii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye maswali ya nyongeza yaliyotangulia, nimesema nchi hii ni tajiri sana ya vivutio vya utalii, jambo ambalo hatujalikamilisha bado na tunaendelea kulifanya ni kuwa na orodha ya vivutio hivyo vilivyohakikiwa kwa sababu siyo kila kitu ambacho mtu mmoja anaweza kukiona kwamba kinatosheleza kuwa kivutio cha utalii, kinakuwa hivyo; ni mpaka wataalam wanaohusika waseme kwamba sasa hiki kinakidhi viwango vya Kimataifa vya kuwa kivutio cha utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii, tayari imeshawasiliana na Halmashari zote nchini ili kuweza kuviorodhesha vivutio hivyo, vifike Wizarani, tuvifanyie uchambuzi halafu tuweze kuviweka katika makundi (grading) halafu tuweze kuweka mkakati wa pamoja wa namna gani ya kutangaza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema jukumu la kutangaza lisiwe jukumu la Serikali peke yake; kama mnavyofahamu na mnavyoona, dunia ya sasa ni kama kijiji; na kila mmoja akitumia wajibu wake wa kutumia mifumo ya mawasiliano ya kisasa, tunaweza kutangaza nchi yetu kwa namna ambayo ni ya mafanikio zaidi.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa mujibu wa majibu ya Serikali niliyonayo mezani jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri halijakamilika bado part ‘B’. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri itabidi nikutane na Mheshimiwa Msuha ili tuone ni kwa nini anafikiri swali langu au swali lake halijajibiwa vizuri. Kwa sababu sisi tulivyoliangalia tumejiridhisha kwamba alichotaka tumekijibu kwa sababu kimsingi aliuliza maswali mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kwa nini Mfilisi bado anashikilia mali za chama hicho na tumejibu kwamba mfilisi hashikilii. Akauliza swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kulipa deni la wakulima ambalo la shilingi milioni 424, hili nalo tumesema Serikali inaendelea kuangalia utaratibu wa kulipa. Kimsingi Serikali imeji-commit kwamba itaendelea kulipa. Sasa kama anaona bado halijajibiwa, nafikiri hakuna tatizo niko tayari kukutana naye, tujadiliane kwamba kwa nini anahisi bado halijajibiwa.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, nitakuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wataalam wakati wa kuweka mipaka katika baadhi ya maeneo wamekuwa wakishirikisha upande mmoja badala ya kushirikisha pande zote mbili na hivyo kusababisha migogoro ya mipaka katika maeneo hayo hususani mipaka ya vijiji vyetu. Je, nini kauli ya Serikali ili kuondoka na tatizo hilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kule Jimboni kwetu Mbinga Vijijini kuna migogoro ya mipaka kati ya Vijiji vya Kilagano, Lugagala na Liganga ambavyo vipo Jimbo la Peramiho, Songea Vijijini. Upande mwingine mgogoro huo unasisha Kijiji cha Litumbandyosi, Mabuni pamoja na Luhugara kwa upande wa Jimbo la Mbinga Vijijini. Je, lini Serikali itashuka ili kwenda kutatua mgogoro huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza kwamba wataalam wamekuwa hawashirikishi pande zote zinazohusika kwenye maeneo ya utawala, hilo ni tatizo na tumeshawapa maelekezo kwa sababu ya migogoro ambayo imesababishwa na kadhia hiyo. Hapa nchini tunayo jumla ya migogoro 366 ambayo imeibuliwa na Kamati ile ya Pamoja ya Wizara mbalimbali ambayo sasa hivi inashughulikiwa. Sasa hivi tumeshawaelekeza wataalam wetu wale wanaoratibu, wakienda kwenye eneo lolote watakapoanza upimaji upya lazima washirikishe pande zote mbili au pande zote zinazohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kuhusu migogoro inayoendelea chini ya uratibu wa Wizara ya Ardhi kitaifa, migogoro yote nchini imeanza kushughulikiwa tangu mwezi Aprili, 2018 na tunaimani mpaka mwisho wa mwaka huu migogoro yote itakuwa imeshughulikiwa ile ya kijiji kwa kijiji, kata kwa kata, wilaya kwa wilaya, mkoa kwa mkoa, maeneo ya wananchi na maliasili na maeneo mengine yote ambayo yana migogoro tuna imani kwamba mpaka mwisho mwa mwaka huu yatakuwa yametatuliwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARTIN A. M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri yenye kutia moyo wananchi wa Mbinga na Nyasa nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga kwa kiwango cha lami barabara inayotoka Mbinga kwenda Litembo hospitali kupitia Kijiji cha Muyangayanga, Kindimba na Mahenge, je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali kupitia swali namba 438 lilojibiwa hapa Bungeni tarehe 27 Juni, 2016 ilisema kwamba taratibu za kumpata mwandisi mshauri kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa barabara inatoka Kitai hadi Lituhi ulikwishakamilika, je, barabara hii ya kutoka Kitai hadi Lituhi itajengwa lini kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali tunaendelea kuratibu ahadi za viongozi ili kuhakikisha kwamba ahadi hizi zinatekelezwa. Yako maeneo ambayo kwa kiasi kikubwa ahadi zimeshatekelezwa na yako maeneo ambayo pia tunaanza kufanya utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge na kwa vile amekuwa mfuatiliaji mzuri labda saa nyingine tuonane kwa sababu ninalo kabrasha ambalo linaonesha hatua mbalimbali ya hizi barabara ambazo zimeahidiwa na viongozi ili tuweze kuona lakini aweze kuwa na uhakika na hatimaye awaeleze wananchi wa eneo la Mbinga Vijijini juu ya hatua ambayo tumeshaifikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kwamba amewahi kujibiwa hapo awali kwa ujenzi wa barabara hii ya Kitahi – Lituhi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ziko barabara nyingi ambazo usanifu wake umekamilika, Serikali inajipanga kutafuta fedha ili kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo barabara hii ya Kitahi - Lituhi nimeipita kwa sababu najua pia tunajenga daraja kubwa katika Mto Luhuhu, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mbinga ni kwamba kwanza barabara hii tumeiboresha sana kuhakikisha inapitika na kwa umuhimu wa ujenzi wa hili daraja kubwa tunapitisha material mbalimbali katika eneo hili kuliko kuzunguka kupitia kule Madaba. Kwa hiyo, tunaendelea kuiangalia kwa makini barabara hii lakini wakati huo tunatafuta fedha ili kiweza kujenga barabara katika kiwango cha lami.
MHE.MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Gereza la Kitai lililopo Wilayani Mbinga ni moja ya magereza kongwe nchini. Gereza hili linakabiliwa na ukachavu wa miundombinu yake ikiwemo uchakavu wa lango kuu la kuingilia gerezani, bwalo la kulia chakula la wafungwa, lakini pia uzio wa kuzunguka gereza hilo umechakaa na unahatarisha usalama wa Maafisa Magereza wanaolinda wafungwa hao. Je, ni lini Serikali itakwenda kukarabati miundombinu katika gereza hilo la Kitai?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu la swali hili halitatofautiana sana na jibu ambalo nimejibu katika swali la msingi la Mheshimiwa Shangazi. Kitakachokuwa tofauti ni kwa sababu lilikuwa ni swali la msingi. Inawezekana pengine bahati ile ambayo Mheshimiwa Shangazi ameipata isiende sambamba na gereza la Kitai kwa maana ya kupata ile mashine, lakini ni kutokana na uchache wa hizo mashine zenyewe na changamoto tulizokuwa nazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba tushirikiane kutumia dhana ile ile ambayo nimeizungumza katika jibu langu la msingi; kwamba tunaweza haya matatizo madogo madogo ya kukarabati magereza yetu tukayafanya kwa kutumia rasilimali za maeneo husika bila kutengemea bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya Serikali imetengwa lakini changamoto ni nyingi. Hivyo, kwa mambo madogo madogo kama haya tunaweza tukakaa tukashirikiana na Mheshimiwa Mbunge tukakae, baadaye tuandae utaratibu ikiwezekana hata mimi niende kwenye ziara kwenye jimbo lake ili nikapeleke uzoefu ambao nimeupata katika maeneo mengine uliosaidia kufanya marekebisho na ukarabati wa magereza ya maeneo mbalimbali nchini.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pia nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nitakuwa na swali moja tu la nyongeza. Kata ya Litumbandyosi iliyopo Wilayani Mbinga inakabiliwa na uhaba mkubwa wa upatikanaji wa maji safi na maji salama. Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi ya visima virefu katika Kijiji cha Kingoli, Luhagara, Mabuni na Litumbandyosi? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri. Vile vile nilishukuru sana Bunge lako Tukufu limetuidhinishia bajeti na katika bajeti tuliyoidhinishiwa Mbinga tumeitengea Sh.1,773,000,000 katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Nimwombe Mhandisi wa Maji wa Mbinga asilale atumie zile fedha katika kuhakikisha anatatua tatizo la maji kikiwemo Kijiji cha Kingole. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, hata hivyo ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni kwa kiasi gani Serikali imesambaza tafiti hizo za gharama za uzalishaji kwa wakulima wa kahawa ili kuwawezesha kufahamu msimu hadi msimu kama wanauza kwa faida ama hasara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wakulima wengi wamekuwa wakilalamika juu ya bei duni ya mazao yao mwaka hadi mwaka; je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya tafiti za gharama za uzalishaji kwenye mazao mengine ya kipaumbele kama pamba, tumbaku, chai, korosho yakiwemo mahindi ili kuwawezesha wakulima hao kufahamu gharama zao za uzalishaji na hivyo kufahamu kama wanauza kwa hasara au kwa faida mwaka hadi mwaka? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Msuha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua matokeo ya tafiti hizi zimewafikia namna gani wakulima wa Tanzania; nataka nimueleze Mheshimiwa Mbunge, matokeo yote ya tafiti hizi tumeyifikisha kwa wakulima kwa njia mbalimbali; kwa njia ya mawasiliano ya television, radio na magazeti na vipeperushi vingine, lakini pia kwa kushiriki Taasisi zetu za TACRI na zingine zinazofanya utafiti wa kahawa na mazao mengine kwenye Maonyesho kama Nane Nane na maonyesho mengine ili wakulima na watu wengine wapate elimu ile pale. Pia zaidi, tuna mpango ambao ni endelevu ulioanza tangu SDP I wa kujenga kila kata vituo vya elimu kwa wakulima ili kutoa elimu kwa wakulima muda wote.


Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, anataka kujua kwamba, je, tafiti hizi za kujua gharama ya mazao mengine hasa mazao yale ya kimkakati na mazao ya mahindi ikoje. Kwanza nataka nimpe uelewa vizuri Mheshimiwa Mbunge na nimpongeze kwa kazi kubwa anayoifanya. Zao la mahindi ni moja ya zao la kimkakati. Labda Waheshimiwa wengi hapa wanashindwa kutambua kwamba kipaumbele cha kwanza cha Taifa ni mazao yale zamani tulikuwa tunaita mazao ya chakula. Kwa sasa hivi hatujaweka hiyo demarcation kwamba kuna mazao ya chakula na mazao yote ya biashara. Sasa hivi mazao yote ni ya biashara ila kipaumbele tumeyapa haya mazao nane ya mwanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujua tumefanya tafiti ngapi; tumefanya kila zao na kila mwaka kupitia ikutano yetu yote ya wadau. Kwa mfano, nimpe kwenye zao la korosho, kilo moja ya kuzalisha korosho ni Sh.1,350 na kwenye kilo moja ya kuzalisha mahindi, heka moja inatumia Sh.740,000. Kwa hiyo, kila mwaka tunafanya na kupeleka elimu hii kwa wakulima.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu ya Serikali lakini pia
nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa kupeleka mnada wa kahawa Wilayani Mbinga kuanzia msimu ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kumetokea changamoto kadhaa katika mfumo huu mpya ikiwemo kuchelewesha malipo kwa wakulima, wakulima kulipwa bei tofauti lakini pia kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya watendaji wa AMCOS. Je, Serikali imejipangaje kutatua kero hizi kwenye msimu ujao wa kahawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwepo mabadiliko ya bei msimu kwa msimu, je, Serikali inajipangaje ama ina mpango gani wa kuanzisha Mfuko wa Kuimarisha Bei ya Kahawa (Price Stabilization Fund) ili kuondokana na tatizo hili la mabadiliko ya mara kwa mara ya bei ya kahawa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martin Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua changamoto zilizojitokeza katika msimu uliopita hasa ya kuchelewesha malipo kwa wakulima pamoja na wakulima kulipwa bei tofauti na bei ambayo ilitangazwa na Serikali ama iliyouzwa mnadani. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Msuha kwa ufuatiliaji wa wakulima wa kahawa nchi nzima kupitia wakulima hawa wa Mbinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kujibu swali lake napenda kusema kwamba madai yake ni ya kweli, mimi mwenyewe nilifika katika Mkoa wa Ruvuma na tuliongea na wakulima walithibitisha hilo. Kilichotokea mwaka jana kama unavyokumbuka, ndiyo ulikuwa mwaka wa kwanza kutumia mfumo huu wakulima wenyewe kwenda kuuza kahawa yao Moshi kupitia vyama vyao vya ushirika. Kwa hiyo, kahawa ile walivyokoboa na kuipeleka mnadani ilichelewa sana kuuzika kutokana na anguko kubwa la bei katika soko la dunia na katika soko la mnada hapa nchini. Kwa sababu walienda kuuza wenyewe, ilikuwa hamna namna nyingine lazima wasubiri mpaka kahawa iuzwe ndipo walipwe. Hata hivyo, kadiri watakavyoendelea kuuza kwenye mnada ndivyo hivyo wakulima wataweza kulipwa pesa zao kwa kuzingatia na mauzo kwenye mnada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili amesema kwamba tumejipangaje. Mwaka huu tumejipanga kupeleka minada hiyo katika kanda zao lakini pili ni kuruhusu wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika kama wakipata soko la moja kwa moja kuuza nje ya nchi tutatoa vibali hivyo ili wauze moja kwa moja. Kwa taarifa tu ni kwamba mpaka sasa tumeshapata wanunuzi ambao wapo tayari kuingia mkataba na Serikali kwa ajili ya kuuza kahawa hiyo kupitia mnada wa moja kwa moja (direct export market) kwa ajili ya kahawa hiyo na tayari mahitaji ya wanunuzi wale ni makubwa kuliko uzalishaji uliopo nchini.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya serikali; hata hivi nitakuwa na swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya changamoto kubwa ambayo inavikabili vyama cha ushirikia kwa maana AMCOS wilayani Mbinga ni nikukosa mitaji kwa ajili ya undeshaji washughuli zake, jambo ambalo linasabisha kukopa kutoka kwenye benki za biashara kwa riba kubwa.

Je, serikali ina mpango gani wa kufungua tawi la Benki ya Kilimo Wilayani Mbinga ili kuziwezesha AMCOS hizo kukopa kwa riba naafuu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Msuha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba vyama vingi vya ushirika ama watanzania wengi walioko sekta ya kilimo walioko vijijini wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mitaji na hasa pale ambapo wamekuwa wakikopa katika benki za biashara. Serikali iliaangiza Tanzania Agriculture Development Bank kuingia akubaliano na benki za bishara kama NMB na CRDB; na benki zote hizi sasa hivi zina mahusiano ya moja kwa moja na Benki ya Kilimo. Umetengenezwa utaratibu ambapo mwananchi ama taasisi yoyote ambayo inajihusisha na kilimo iliyoko wilayani inaweza kwenda katika dawati lililopo katika NMB ama CRDB ambalo linaiwakisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni benki ambayo kimkakati hawezi kwenda kufungua matawi nchi nzima katika kila wilaya kwa sababu ya namna ambavyo imeundwa. Ni benki ya kimkakati ambayo ni ya uwekezaji wa muda mrefu katika sekta ya kilimo na haifanyi commercial activities. Kwa hiyo ningemshauri Mheshimiwa Mbunge awahamasishe vyama vyake vya msingi vya ushirika viende katika Benki za NMB ama CRDB zilizopo katika wilaya zetu ambazo zitayari zina madawati ya mahusiano ya kibiashara na Benki ya Maendeleo ya Kilimo, na huko watapata huduma wanazohitaji za muda mrefu.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Niipongeze Serikali kwa majibu mazuri katika swali hilo. Pia kwa dhati kabisa nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa kupeleka Mnada wa Kahawa Wilayani Mbinga kuanzia msimu huu wa mwaka 2019. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni kweli Serikali imepeleka zao la korosho katika Kata za Rwanda na Litumbandyosi. Changamoto ya wakulima hao ni upatikanaji wa miche bora na kwa bei nafuu. Je, Serikali iko tayari kuendelea kutoa miche ya mikorosho bora kwa bei nafuu au bure kwa wananchi wa Kata ya Rwanda na Litumbandyosi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika jibu la msingi, Serikali imekiri kuwa ilitoa mafunzo ya uzalishaji wa miche bora ya mikorosho katika vikundi sita vya Jembe Halimtupi Mtu, Chapakazi, Twiga, Juhudi, Kiboko na Korosho ni Mali lakini vikundi hivi bado vinaidai Bodi ya Korosho. Je, ni lini madeni ya vikundi hivyo yatalipwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tupo tayari kupeleka miche ya mikorosho kwa bei nafuu kwa wakulima wa Wilaya ya Mbinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kama tunavyofahamu deni likivuka mwaka madeni yote haya ya Serikali yanahamia Hazina. Sasa hivi Serikali tuko kwenye hatua za mwisho za kumalizia uhakiki na vikundi vyote ambavyo uhakiki umemalizika vimeshaanza kulipwa na hivi alivyovitaja vitaanza kulipwa baada ya uhakiki kukamilika.