Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Martin Alexander Mtonda Msuha (16 total)

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, kwa maandalizi mazuri ya Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa letu, kwa kipindi tajwa hapo juu. Mpango huu ni muhimu sana kwani ndiyo dira ya mwelekeo wa Taifa kwa miaka mitano ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huu, naomba sasa nichukue nafasi hii kuchangia kisekta kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Kilimo; naipongeza Serikali kwa juhudi ambazo imezifanya hadi saa katika kuboresha kilimo nchini. Hata hivyo, katika Mpango huu wa Maendeleo siajona mkakati wa kuendelea kuyaboresha mazao makuu ya biashara kwa maana ya zao la kahawa, tumbaku, korosho na pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa kahawa hususani wanazo kero nyingi sana ambazo zinawakatisha tamaa katika kuliendeleza zao hilo. Kero hizo ni pamoja na:-
(i) Bei kubwa ya pembejeo na utaratibu usiofaa wa kugawa mbolea kwa mtindo wa vocha ambazo zinakwenda kwa package ya mbegu, mbolea ya kupandia na kukuzia. Mkulima wa kawaha hahitaji mbegu wala mbolea ya kupandia. Vocha zinazotolewa hazitoshelezi badala yake imekuwa ni lawama kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu ni kuwa, Serikali ifuate mfumo wa kupeleka mbolea kwa mtindo wa vocha na itengeneze mfumo mwingine na kwamba mbolea hizo zipelekwe mapema kabla ya msimu.
(ii) Mfumo wa soko la kahawa hususani Mbinga ni mbovu sana. Walanguzi wa soko huria hudiriki hata kununua kahawa kwa wakulima ikiwa shambani kabla haijakomaa na kuvunwa. Wanaingia mikataba ya kuwaumiza sana wakulima. Endapo mavuno ya msimu huo hayatoshi kulipa deni basi walanguzi hao hunyang‟anya mashamba ya wakulima.
(iii) Kutokana na kuwa na soko huria wakulima wamekuwa wakilipwa bei tofauti tofauti ndani ya wilaya moja. Hii inakatisha tamaa sana kiasi kwamba wakulima wameanza kususia utunzaji wa mashamba hayo ya kahawa na ndiyo maana zao hilo limeporomoka kwenye orodha ya mazao makuu ya biashara nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu ni kuwa Serikali ichukue hatua za makusudi kupiga marufuku ununuzi wa kahawa mbichi ikiwa shambani. Mfumo huu kule Mbinga unajulikana kama “MAGOMA”. Lakini pia serikali ichukue hatua za makusudi kuimarisha Chama Kikuu cha Ushirika cha Mbinga kiitwacho MBIFACU na kuhakikisha mali ya chama kikuu cha zamani zinarejeshwa kwa chama hiki kipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Elimu; wananchi wa Wilaya ya Mbinga kwa ujumla wake wanaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa Sera ya Elimu Bure. Hata hivyo, kuna changamoto zifuatazo ambazo zinahitaji utatuzi wa haraka sana:-
(i) Utatuzi wa uhaba wa Walimu. Zipo shule zenye wanafunzi zaidi ya 300 darasa la I hadi IV na kuna Mwalimu mmoja tu.
(ii) Vyumba vya madarasa havitoshi kabisa. Zipo shule ambazo wanafuzi wanasoma zaidi ya darasa moja kwa chumba kimoja cha darasa kwa wakati mmoja kwa kugeuziana migongo.
(iii) Suala la vyoo vya kisasa ni tatizo kubwa sana katika shule zetu za msingi.
(iv) Nyumba za Walimu nazo ziangaliwe. Watumishi hao wanaishi katika mazingira magumu sana tena sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Nishati na Madini. Tunashukuru Serikali kwa kutekeleza Mradi wa Umeme Vijijini kupitia mpango wake wa REA. Hata hivyo, bado kuna vijiji vingi sana katika Wilaya ya Mbinga havikupata umeme kwenye REA II. Naomba Serikali sasa ipeleke umeme kwenye vijiji vilivyobaki ambavyo ni zaidi ya 150 kwenye mpango wa mwaka ujao.
Kwenye maeneo yanayotarajiwa kuzalisha umeme sijaona machimbo ya makaa ya mawe katika Kijiji cha Ntunduwalo, Kata ya Ruanda, Wilayani Mbinga yakitajwa kwenye mipango yote miwili wa mwaka mmoja wala ya miaka mitano. Eneo hili yupo mwekezaji anayechimba makaa ya mawe, naiomba Serikali imwangalie mwekezaji huyu na machimbo haya kwa namna ya pekee ili wananchi weweze kunufaika na uwekezaji wake. Kwa ujumla mwekezaji huyu na machimbo haya kwa namna ya pekee ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji wake. Kwa ujumla mwekezaji huyu hana mwelekeo wa kuzalisha umeme hivi karibuni. Mgodi huu uangalie upya kwani pia umekuwa kero kwa wananchi wa kata hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni ya ujumla; kwa kuwa kwa miaka kadhaa ya nyuma Serikali haikuwa na uwezo wa kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wakati sasa umefika, ningeishauri Serikali iangalie upya namna ya upangaji wa vipaumbele vya Kitaifa.
Vipaumbele hivyo vingepangwa kisekta badala ya kimiradi kama inavyofanyika kwa sasa. Mfano, miaka mitatu ya kwanza fedha zote za maendeleo zingepelekwa Elimu; miaka mitatu inayofuata fedha zote za maendeleo zipelekwe kwenye Afya na kadhalika. Uwekezaji katika miradi ungeweza kuonekana kwa macho na kwa tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi niungane na wenzangu kwanza kutoa pongezi kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya. Pia nichukue fursa hii kuwapongeza Mawaziri wote na hususan Waziri wa Kilimo na Naibu wake kwa uwasilishwaji mzuri wa bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi uliofanyika leo asubuhi. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, lakini pia kwa vile ni mara yangu ya kwanza na mimi kuchangia, nichukue fursa hii kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Mbinga Vijijini kwa kuniamini na kunituma niwe mwakilishi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na mchango kwenye eneo moja tu la kilimo kwa sababu tunavyoongelea Jimbo la Mbinga Vijijini asilimia mia moja wote ni wakulima na nitagusa mazao makubwa mawili. Zao la kwanza ni mahindi ambalo upande mmoja wa jimbo langu wanatumia kama zao la biashara, lakini pia zao la chakula. Kwa kiwango kikubwa pia Jimbo la Mbinga Vijijini tunalima kahawa ambayo ina changamoto nyingi ambazo tumeshazisikia siku nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mahindi, wakulima wa Jimbo la Mbinga Vijijini wana shida upande wa upatikanaji wa pembejeo kwani zinakwenda kwa kuchelewa na zikifika zinakuwa na bei ya juu ukifananisha na pengine na wauzaji wa rejareja. Kwa hiyo, naomba Waziri aangalie namna ya kuboresha upande huu na pengine ule mfumo wa voucher ni wa malalamiko sana, hauwafikii wakulima wote. Kaya nyingi zinakuwa hazipati huduma hiyo ya pembejeo kupitia mfumo wa voucher. Kwa hiyo, nashauri Waziri mhusika aangalie namna ya kuboresha mfumo wa usambazaji mbolea ili wakulima waweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni soko. Soko la mahindi limekuwa halina uhakika, uzalishaji ni mkubwa lakini uwezo wa Serikali kununua mahindi hayo ni mdogo sana. Kwa hiyo, mahindi mengi yanabaki kwa wakulima na wakati mwingine yanaharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ile bei elekezi ambayo inatolewa na Serikali, kwa sababu ya mfumo wa ununuzi wa hili zao la mahindi unapitia kwa mawakala unakuta mkulima hafikiwi na ile bei elekezi ya Serikali. Utakuta mkulima pengine ananunuliwa mahindi yake kwa shilingi 380 au chini ya hapo. Kwa hiyo, ile bei elekezi ambayo Serikali inakuwa imetoa inanufaisha watu wa kati. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie ni namna gani zile bei elekezi ziweze kumnufaisha mkulima moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tuna uhaba wa wataalam wa ugani. Vijiji vyetu vingi, kata zetu nyingi hazina wataalam wa ugani na hao wataalam bahati mbaya sasa hivi wanaunganisha kazi zote mbili, za mifugo pamoja na kilimo. Kwa hiyo, mara nyingi unakuta kazi wanayofanya ni upande wa mifugo kwenye kilimo wamesahau kabisa kusaidia wakulima.
Mheshimwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali iangalie mambo mawili kuhusiana na eneo hilo. La kwanza, kwenda kuziba hayo mapengo lakini la pili ikiwezekana kutenganisha kazi za hawa maafisa ugani, anaye-deal na kilimo abaki kwenye kilimo na wa mifugo abaki kwenye mifugo ili wakulima hao waweze kupata huduma kwa kiwango ambacho kinastahili.
Mheshimwa Mwenyekiti, nirudi upande wa kahawa. Uchumi wa wananchi wa Jimbo la Mbinga Vijijini unategemea zao la kahawa. Wakulima wa jimbo hili wamekuwa wakilima zao hili kwa mazoea kwamba tangu enzi za mababu wamekuwa wakilima kahawa lakini kwa kukosekana pia huduma za ugani, uzalishaji unashuka. Wakulima hawapati huduma za kuelekezwa ni namna gani wanaweza kuzalisha kwa tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni mzigo sana kwa wakulima hawa wa kahawa wa Jimbo la Mbinga Vijijini ni utitiri wa tozo, kuna tozo zipatazo 36 kwenye zao la kahawa. Mwisho wa siku unakuta mkulima bei anayopata inakuwa haimpi motisha kwa sababu ya hizi tozo. Nimuombe Mheshimwa Waziri anayehusika aangalie tozo hizi. Kuna tozo moja ya ugonjwa wa vidung‟ata. Ugonjwa huu ulikuwa ni wa mlipuko, lakini baadaye ulikuja kudhibitiwa. Hata baada ya ugonjwa huu kudhibitiwa wakulima wale wameendelea kukatwa tozo hii mpaka leo. Kwa kweli tozo hii ni kero sana kwa wakulima wa kahawa Wilayani Mbinga. Naomba Waziri mhusika atakapokuwa anapitia tozo mbalimbali kwenye zao la kahawa Mbinga, hii naomba iwe tozo la kwanza kuliangalia namna ya kuliondoa kwa sababu ni kero ya kwanza kwa wakulima wa Mbinga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la ushirika. Vyama vingi vya ushirika vya msingi Wilayani Mbinga havikopesheki kwa sababu ya mzigo wa madeni. Kwa vile vyama vya ushirika haviwezi tena kuhudumia hao wakulima, wanunuzi wa soko huria wanachukua nafasi hii kuwanyonya wakulima. Wananunua kama mawakala wakati mwingine wanauza wenyewe nje wakati fulani wanakiuzia chama kikuu cha ushirika. Hawa wanunuzi inafika mahali wanatengeneza umoja, wanafanya cartel kwa hiyo, wanavyokwenda wanakwenda na bei zao elekezi, mwaka huu tuanzie hapa na kwa sababu wakulima wanakuwa na shida unakuta wanalazimika kuuza kahawa yao kwa hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mfumo wa soko wa uuzaji kahawa kule Mbinga hauko rafiki kwa sababu utakuta kipindi hiki ambacho sio cha msimu hawa wafanyabiashara wa kati wanakwenda kufanya mikataba ya kununua kahawa ikiwa shambani. Inapokuja kipindi cha mavuno, mkulima anavuna, anatoa kahawa kama vile anatoa bure lakini kama haifikii deni wanunuzi hawa wanafika mahali pa kunyang‟anya mashamba ya wakulima. Wakati mwingine wakulima hawa wanabaki kuwa wakimbizi kwenye Wilaya yao. Nashauri Waziri mwenye dhamana na Wizara hii aangalie namna ya kurekebisha hali hii na pengine sasa ule ununuzi wa kwenda kununua zao la kahawa likiwa shambani upigwe marufuku. (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, jambo lingine ni kwamba Chama Kikuu cha Ushirika cha Mbinga kilipata matatizo ya kiuchumi miaka ya 1994 mpaka kikaja kikafa baadaye kikaanzishwa chama kingine kikuu cha Ushirika MBIFACU. Hicho chama ambacho kilikufa mwaka 94 kiliacha madeni makubwa kwa wakulima kiasi cha shilingi milioni 424. Wakulima hao walikuwa wanakidai hicho chama cha Ushirika ambacho kilikufa, Serikali iliagiza ukafanyike uhakiki wa madeni haya. Bahati nzuri Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alitoa taarifa yake mwaka 2013 baada ya kufanya uhakiki wa madeni ya wakulima waliokuwa wanakidai chama hicho madeni yapatayo shilingi milioni 424. Taarifa hiyo imebainisha ni vyama gani vinahusika, lakini pia imebainisha ni wakulima gani mmoja mmoja anahusika kukidai chama hicho. Sasa niiombe Serikali, iangalie namna ya kuwalipa hawa wakulima deni lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika kuanzisha Chama Kikuu cha Ushirika cha MBIFACU kuna mali nyingi sana ya Chama Kikuu cha Ushirika kilichokufa ambazo zinashikiliwa na mrajisi. Mali hizo ni majengo lakini yalikuweko magari…
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mhshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua nafasi hii kuungana na wenzangu kuwapongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Naibu wake kwa hotuba nzuri iliyosheheni mipango mizuri juu ya utekelezaji wa shughuli za Wizara hiyo kwa mwaka tajwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya ujenzi; kutokana na mvua nyingi zilizonyesha msimu uliopita, barabara nyingi za Jimbo la Mbinga Vijijini zimeharibika vibaya sana kiasi cha kuathiri shughuli za usafirishaji na uchukuzi ndani ya jimbo. Njia nyingi zilifunga mawasiliano kama barabara zifuatazo; Mbinga - Mkumbi - Lugari, Mbinga - Linda - Litowo, Linda - Muhongozi, Kigonsera - Matiri - Kilindi, Lipumba - Kihangimahuka, Muhongozi - Paradiso. Nimuombe sasa Mheshimiwa Waziri aweze kutoa waraka au agizo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa, aweze kuchukua hatua za haraka ili matengenezo ya barabara hizo yaweze kufanyika mara moja ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja kama lile la Mapera, Mto Lukanzauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iangalie uwezekano wa kuingiza kwenye mpango wake wa mwaka ujao kipande cha barabara ya kutoka Mbinga Mjini hadi Longa kwa kiwango cha lami ili kuunganisha na mradi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Longa hadi Litowo unaojengwa kwa ufadhili wa European Union kwani itakuwa ni kituko kuacha kipande hicho kuendelea kuwa cha vumbi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchukuzi; katika sekta hii naiomba Serikali iangalie yafuatayo; ununuzi wa meli mpya katika Ziwa Nyasa na upanuzi wa Bandari ya Mbamba Bay.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano; napenda kuipongeza Serikali kwa dhati kwa hatua iliyofikiwa katika sekta ya mawasiliano hususani mtandao wa simu za mkononi. Hata hivyo, naomba waombwe tena Kampuni ya Halotel ili iweze kufikisha mawasiliano ya simu za mkononi kwenye maeneo yafuatayo; Kingoli, Kata ya Litumbandyosi, Mihango Kata ya Kigonsera, Lukiti - Linda, Litembo - Litembo, Mahilo - Kitura, Kindimba Chini - Muungano, Sara - Muhongozi, Kilindi - Matiri, Barabara - Matiri, Kikuli - Mikalanga, Makonga - Miukalanga, Matuta - Kipapa, Mbuta - Kamabarage, Mhimbazi - Amani Makolo, Lipumba - Kihangimahuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na kuunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niwapongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa hotuba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Wizara/Serikali kuangalia uwezekano wa kuziongezea fedha programu za NACP/NBTS/NTLP kwa kuwa ufadhili wa PEPFAR/CDC umepungua sana. Serikali iangalie uwezekano wa kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ofisi ijulikanayo kama mradi wa NACP/NTLP Joint Office Project iliyopo nyuma ya ofisi za WHO. Mradi huu ulisimama miaka mingi iliyopita kufuatia Global Fund kuacha kutoa fedha kwa ajili ya jengo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Wilaya ya Mbinga tunaomba kuboreshewa huduma za upasuaji. Vilevile kwa kadri hali itakavyowezekana tunaomba hospitali hii ipatiwe chumba cha kuhifadhi maiti (mortuary).

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara iangalie uwezekano wa kukipandisha Kituo cha Afya cha Mapera ili kiweze kuhudumia kama Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga baada ya kuipandisha hadhi ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa kugawa vifaa tiba kwa kila Halmashauri. Ushauri wangu ni kwamba vifaa hivyo vigawiwe kupitia Mbunge kama ilivyofanyika kwenye mgao wa madawati ya chenji ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wa Wizara hii. Naomba kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina nia ya kupanua eneo la Hifadhi ya Taifa ya Selous hadi Wilaya ya Mbinga katika Kata za Litumbandyosi na Ruanda. Fukuto la migogoro ya mipaka katika eneo hili limekwishaanza kujitokeza. Hivyo naishauri Wizara ichukue hatua za haraka kwenda kuweka vizuri mipaka katika kata hizo za Litumbandyosi na Ruanda ili kuepusha migogoro hiyo inayofukuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa katika upanuzi wa hifadhi kwa niaba ya wananchi wa kata hizo naomba mipaka ikarekebishwe ili yale maeneo yanayolimwa waweze kuachiwa waendelee na shughuli zao za kiuchumi

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke wazi fursa zilizopo katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Misitu (Tanzania Forest Fund) ili wananchi wapate kunufaika nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mbinga katika kijiji cha Mbuji, Kata ya Mbuji yapo mawe makubwa mawili ambayo inasadikika kuwa mawe hayo ni Bibi na Bwana, kwa maana kwamba kuna jiwe la kiume na jiwe la kike. Katika mawe hayo unafanyika utalii ambao si rasmi na miaka ya hivi karibuni kuna mzungu alidondoka kwenye jiwe mojawapo hadi kupoteza maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mawe hayo kuna viumbe hai wanaoishi ambao wanafanana na binadamu isipokuwa wao ni wafupi sana. Viumbe hao wanafahamika kama “VIBUTA” kwa lugha ya Kimatengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ikafanye utafiti katika mawe hayo ili kubaini viumbe hivyo na kubaini fursa nyingine za kitalii. Inasadikika kuwa viumbe hao wanapatikana pia katika nchi ya Australia. Naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia taarifa zilizoko mezani kwako. Mimi nitachangia upande wa taarifa ya Hesabu za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge la Bajeti la 2016/2017 asilimia 40 zinapelekwa kwenye kutekekeleza miradi ya maendeleo, lakini miradi hiyo mingi inatekelezwa katika ngazi za Halmashauri. Pia katika mabadiliko ya sheria za fedha yaliyofanyika mwaka huu yamepandisha kiwango cha kuiwezesha Halmashauri kusaini mikataba kutoka kwenye shilingi milioni 50 mpaka shilingi bilioni moja. Hii ina maana kwamba Halmashauri hizi zinapewa uhuru zaidi wa kufanya maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa upande mwingine tunazo oversight committees, tunayo Ofisi ya CAG na tunazo hizi Kamati. Kwa bahati mbaya sana tunakwenda contrary kwa maana kwamba hizo oversight committees zimenyimwa uwezo wa kifedha kwenda kufanya ukaguzi wa miradi. Kwa hiyo, tunachotegemea kuona baada ya mwaka huu wa fedha ni kwamba pengine miradi hii haijatekelezeka kwa kiasi ambacho kinaridhisha kwa sababu ya hizo oversight committees kunyimwa uwezo wa kifedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya maeneo ambayo Halmashauri zote zilionekana kuwa na matatizo makubwa ni kwenye usimamizi wa mikataba na miradi ya maendeleo. Kati ya Halmashauri zote 66 ambazo tulizihoji mbele ya Kamati, zaidi ya asilimia 75 zilionekana kuwa na upungufu katika usimamizi wa mikataba. Mikataba mingi haikuweza kufikia mwisho kwa maana kwamba mingi ilivunjwa njiani na hivyo kuzisababishia Halmashauri kuingia gharama zaidi.
Kutokana na kuvunjika kwa mikataba hiyo ilisababisha pia miradi mingi kutokamilika kwa wakati na chini ya kiwango ambacho kilikusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya sana miradi ambayo iliathirika zaidi ni ya maji. Maeneo mengi miradi mingi ya maji ambayo ilikamilika pia haikuweza kutoa maji, lakini mingine pia imekwama kwa kipindi cha muda mrefu. Kwa mfano, mradi wa maji Wilayani Tunduru wa Nalasi na Nandembo ilionekana kuwa imekamilika lakini haitoi maji na mkandarasi ameshasaini. Huu ni udhaifu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo lakini pia mikataba husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ipo miradi mingine kama mradi wa ujenzi wa madarasa katika Kata ya Namswea Ndongosi. Shule ya sekondari ilishakamilika siku nyingi, lakini haikuweza kutumika kwa sababu fedha hazijatolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya kukamilisha hii shule ili iweze kutoa huduma ambayo imekusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo liliathirika sana kwenye hizi Halmashauri zetu ni matumizi nje ya bajeti. Halmashauri nyingi zimeonekana zimetumia fedha nyingi sana nje ya bajeti ambayo imepitishwa lakini Halmashauri hizi zilikuwa zinatumia kivuli cha maagizo kutoka kwa viongozi wa juu. Tulipowahoji kwamba hao viongozi waliwaambia wavunje Sheria za Matumizi ya Fedha za Umma wakasema hapana. Hiyo nayo ilipelekea kuathiri miradi mingi sana ya maendeleo kwa sababu fedha zote ambazo zilionekana kama ziko idle zilichukuliwa na kupelekwa kwa mfano kwenye ujenzi wa maabara kwenye shule zetu za sekondari. Bahati mbaya zaidi hizi maabara nyingi pia hazijakamilika japokuwa fedha nyingi sana zilichukuliwa kutoka maeneo mengine kwenda kutekeleza mradi huu wa ujenzi wa maabara.
Kwa hiyo, Kamati ilikuwa inashauri TAMISEMI wafanye juhudi pengine kwenda kutathmini ni kiasi gani fedha zilichukuliwa kutoka maeneo mengine zikatekeleza mradi wa maabara, lakini kuna tija kiasi gani imepatikana upande huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya miradi ambayo tulifanikiwa pia kuipitia ni mradi wa uuzwaji wa Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA). UDA ni shirika la umma ambalo lilikuwa chini ya Hazina. Shirika hili lilikuwa na jumla ya mtaji wa hisa milioni 15 lakini Serikali iliamua ku-issue hisa milioni 7.1 na ikabakiza hisa milioni 7.8 ambazo hazikuwa allotted. Kati ya zile hisa ambazo Serikali ili-issue, zile milioni 7.1 iliamua kutoa hisa zake asilimia 51 kuipa Jiji la Dar es Salaam, lakini baadaye Jiji la Dar es Salaam waliamua kuuza hisa zao zile asilimia 51 kwa Kampuni moja binafsi ambayo inaitwa Simon Group.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baadaye pia Bodi ya UDA iliamua nayo kufanya mchakato wa kuuza zile unissued and unallotted shares za milioni 7.8. Hisa za Jiji zililipwa na Simon Group na fedha hizo zikawekwa kwenye akaunti ya Amana Benki Kuu na fedha hizo bado zipo kwenye Akaunti hiyo, Jiji halijaweza kuzitumia. Fedha ambazo zilipatikana kutokana na uuzaji wa hisa hizo ni kiasi cha shilingi bilioni 5.875. Baadaye Serikali iliona kwamba uuzwaji wa zile hisa ambazo hazikuwa issued na kuwa allotted za milioni 7.8 ilikuwa ni kinyume na sheria na taratibu. Kwa hiyo, Serikali iliamua kuzuia mauzo hayo na Simon Group aliamua ku-surrender hisa hizo kwa hiyo zikabaki chini ya Msajili wa Hazina mpaka hivi tunavyoongea. Pia zile fedha ambazo zilipatikana kutokana na uuzwaji wa zile hisa za Jiji zile bilioni 5.8 hazijaweza kutumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kusubiri baadhi ya nyaraka kutoka kwa Msajili wa Hazina ili jambo hili liweze kufika mwisho, Kamati ilikuwa inapendekeza mambo mawili; la kwanza, Halmashauri za Manispaa za Dar es Salaam ziweze kushirikishwa katika umiliki wa UDA ili ziweze kuwa wabia wa uendeshaji wa kampuni hiyo kwani ndiyo kampuni ambayo inategemewa kusafirisha abiria ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuwauzia baadhi ya hiza zile ambazo hazikuwa allotted za milioni 7.8.
Lakini pia tulikuwa tunapendekeza kwa vile hizi fedha shilingi bilioni 5.8 ambazo zimebaki BOT bila kutumika, Serikali ingetengeneza utaratibu wa kuangalia ni namna gani fedha hizo zinaweza zikaruhusiwa zitumike kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ndani ya Manispaa zinazounda Jiji la Dar es Salaam badala ya kuzibakiza ziwe idle katika Akaunti ya Amana Benki Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo liligusa karibu Halmashauri nyingi ni upotevu wa nyaraka za matumizi. Utakuta mkaguzi anakagua unakuta nyaraka za thamani kubwa tu hazionekani lakini baada ya wakaguzi kuwa wamemaliza kazi yao wametoka Afisa Masuuli anakuja na majibu kwamba nyaraka hizo sasa zimeshapatikana na ziko tayari kwa ukaguzi.
Kamati inauliza kama kweli nyaraka hizo zilikuwa ni halisi kwa nini zisipatikane wakati zoezi la ukaguzi linafanyika na siyo baada ya zoezi kumalizika na pengine baada ya miezi mingi sana ndiyo nyaraka hizo ziweze kupatikana? Hilo limeonekana ni eneo ambalo lina udhaifu mkubwa katika utunzaji wa hizi nyaraka kinyume na taratibu na sheria za fedha zinavyohitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine lililoonekana kuwa na matatizo makubwa hasa kwenye Halmashauri mpya ni ufanyaji kazi wa Mfumo wa Uandaaji wa Taarifa za Fedha unaoutwa EPICOR. Halmashauri nyingi mpya hazijaunganisha kwenye mtandao huu kwa hiyo taarifa zao nyingi aidha wanatengeneza nje ya mfumo au wanasafiri kwenda kutengenezea kwenye Halmashauri ya jirani. Pia ilionekana kwamba taarifa nyingi haziwezi kutolewa na mfumo huu. Kwa hiyo, Serikali iangalie ni namna gani ya kuboresha mfumo huu ili uweze kukidhi mahitaji ya utengenezaji wa taarifa za fedha katika Halmashauri hizi husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ilionekana wahasibu wengi hawaufahamu vizuri mfumo huu. Wahasibu walio wengi hulazimika kutengeneza baadhi ya taarifa kwenye mfumo huu lakini taarifa nyingine kutengeneza nje ya mfumo na hivyo kukosa uwiano wa taarifa zinazotoka katika hiyo mifumo miwili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliona maeneo mengi yenye changamoto lakini kwa vile kuna wachangiaji wengi, naomba niunge mkono hoja na niwaachie wenzangu wagusie maeneo mengine. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupatiwa nafasi ya kuweza kuchangia hoja iliyopo mezani ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Nichukue fursa hii kuungana na Waheshimiwa wenzangu wote waliotangulia kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa wanayoifanya, ni kazi ambazo zinaonekana, sitahitaji kurudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niipongeze Serikali kwa kutupatia mradi wa barabara ya kutoka Longa hadi Kipololo, pia awamu nyingine Kipololo hadi Litowo kwa kiwango cha lami kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya (European Union).

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii inazo changamoto nyingi sana, barabara hii haiendi kwa speed ambazo zilioneshwa kwenye mikataba na makubaliano. Kipande cha kwanza cha kutoka Longa hadi Bagamoyo, ambayo iko kata ya Kipololo mkataba wake ulitakiwa ukamilike tarehe 30 Septemba, 2016 bahati mbaya hadi ninavyosema hakuna hata futi moja iliyoweza kutiwa lami mpaka sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kipande cha pili cha kutoka hapo kijiji cha Bagamoyo kwenda Litowo baada ya kufanya mabadiliko ya mkataba walitakiwa Wakandarasi wamalize kazi ile tarehe 31 Januari, 2017, bahati mbaya hadi nasimama hapa leo hii, barabara hii katika vipande vyote viliwili haijaweza kuwekewa hata nukta moja ya lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa barabara hii sijaiona kwenye kitabu cha mawasilisho ya Mheshimiwa Waziri, sasa sijajua iko mpango wa nje ya hii programu iliyoletwa ya 2017/2018 kwa mwendelezo au vinginevyo nitaomba tupate ufafanuzi baadaye ili iturahisishe pia ufuatiliaji wa ujenzi wa barabara hii.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu walitangulia pia kuchangia asubuhi Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi lakini pia kupitia swali la nyongeza Mheshimiwa Mpakate juu ya barabara inayotoka Kitahi kwenda Lituhi kupitia kwenye Mgodi wa Makaa Ngaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi si tu wa Mbinga lakini pia uchumi wa Taifa letu kwa ujumla. Barabara hii ya Kitahi - Lituhi ni barabara kubwa sana ikizingatia na upanuzi unaoendelea kufanyika kule kwenye makaa ya mawe Ngaka. Jambo linalofanyika sasa hivi kwa sababu madaraja ya ile barabara kutoka Kitahi kwenda Ngaka, kata ya Ruanda ni membamba wametengeneza bandari kavu karibu na Kitahi. Kwa hiyo, utakuta pana msururu mkubwa sana wa malori yanayotakiwa sasa kwenda kuchukua mzigo unaotoka machimboni na kuletwa kwenye bandari kavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuiombe Serikali iangalie, mwaka jana nilikuwa na swali juu ya barabara hii, niliambiwa kuwa upembuzi yakinifu ulikwisha fanyika. Bado kwenye kitabu cha mawasilisho ya Mheshimiwa Waziri barabara hii sioni kama inapewa kipaumbele cha kujengwa kwa lami. Kwa hiyo, ombi langu ni kwamba barabara hii ni ya kitega uchumi na bahati nzuri lazima niwe muwazi kwamba Mkuu wa Mkoa jana alinipigia simu baada ya kupata taarifa kwamba barabara hii haijatengewa fedha kuweza kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa ziarani Mkoani Ruvuma, mwezi Januari 2017; tukiwa kwenye makaa ya mawe ilionekana kwamba katika mkataba wa mwekezaji TANCOAL component mojawapo ya mkataba wake ni kujenga barabara hii kwa kipande cha kutoka Kitahi mpaka pale machimboni Ngaka. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali ifanye mapitio ya mkataba huu kama ilikuwa ni makubaliano ya yule mwekezaji atujengee barabara kwa kiwango cha lami, basi kazi hii aweze kufuatiliwa na atimize wajibu wake.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na barabara hizi ambazo nimezitaja pia tulikuwa na ombi, ile barabara ambayo ilikuwa inatoka Kitai kupitia Ruanda kwenye makaa ya mawe Lituhi kipaumbele sasa kisogezwe mpaka Ndumbi ambako tunajenga bandari mpya kando ya Ziwa Nyasa kwa Mheshimiwa Stella Manyanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo pia barabara ya kimkakati pia kiulinzi pia ambayo inatoka Lituhi mpaka Mbamba bay. Barabara hii ni muhimu sana siyo tu kwa uchumi ni kwa watu wa Nyasa na Mbinga pia ile barabara ndiyo ulinzi wa Ziwa Nyasa ukizingatia tunapakana na Malawi ambao hatuwaamini sana mpaka sasa hivi.(Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo barabara zingine muhimu ambazo tungeomba pia Wizara ingalie namna gani ya kuzipeleka kwenye ujenzi wa kiwango cha lami. Tunayo hospitali moja ambayo tunaitumia kama hospitali ya Rufaa ya Litembo, ili kufika kwenye ile hospitali tunazo barabara mbili, hii inayotoka Mbinga inapita Myangayanga kwenda Litembo tunayo inayotoka Nyoni - Mbuji kwenda Litembo. Barabara hii bahati mbaya sana kipindi cha masika haipitiki. Wiki iliyopita tu Diwani alinipigia simu kwa sababu ya barabara hii ile hospitali imeshindwa kubeba supplies kutoka Mbinga Mjini kupeleka kule Litembo ili watu waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikiri nilimpigia simu Meneja wa TANROADS na alikuwa ameshamtuma mhandisi kwenda kukagua maeneo ambayo ni korofi ili watu waendelee kupata huduma, niiombe Wizara walau barabara mojawapo kati ya hizi mbili ifikiriwe kwenye kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo barabara nyingine iliongelewa pia hapo awali ipo chini ya Mtwara corridor, barabara ya kipande cha Mbinga kwenda Mbamba bay. Barabara hii kwa majibu ya mwaka jana upembuzi yakinifu umekwishafanyika lakini pia uzinduzi wa barabara hii ulifanyika Katavi mwezi wa tatu mwaka jana kwa barabara inatoka Sikonge - Mpanda na hii ya Mbinga Mbamba bay. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mawasilisho ya kitabu cha Wizara ukurasa 28, item namba 50 inaongelea hii ya Katavi, ukienda kwenye ukurasa 244 inapoongelea sasa barabara ya Mbinga - Mbamba bay msimamo wa wizara unatofautiana. Kwenye kipande cha Mbinga - Mbamba bay kitabu kinaeleza kwamba upembuzi yakinifu zimeshafanyika zinatafutwa fedha kwa ajili ya ujenzi. Kwa kipande kile cha kutoka Sikonge - Mpanda unasema kwamba fedha zilikwishapatikana kupitia African Development Bank. Ninachofahamu miradi hii inatekelezwa kwa pamoja kwa nini huku kuwe na status tofauti na huku status tofauti? Mara ya mwisho wakati nafuatilia kwa Meneja wa TANROADS Songea walichoniambia mwezi wa kwanza mwaka huu walikuwa wanarekebisha design ya barabara ya Mbinga - Mbamba bay na hapakuwa na suala la fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wakati tutakapokuja kufanya Windup utuambie status ya upatikanaji wa fedha hizi, kwa sababu wananchi walishapisha maeneo ili ujenzi wa barabara hii uweze kufanyika mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo barabara zingine ambazo ni za ngazi ya Mkoa ambazo TANROADS hawakuwahi kupita tangu zipandishwe hadhi …...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wako umekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuungana na Waheshimiwa Wabunge walioipongeza Wizara kwa kazi nzuri inayoendelea kutekelezwa kupitia miradi mbalimbali ya maji. Kama Mjumbe wa Kamati ya LAAC nilifanikiwa kutembelea miradi kadhaa ya maji na umwagiliaji katika Mikoa, Wilaya za Lindi Manispaa, Nachingwea, Singida Manispaa pamoja na Tabora Manispaa. Kwa ujumla wake kati ya miradi yote tuliyotembelea haikutekelezwa kwa kiwango cha kuridhisha kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara kuunda team maalum kufanya tathmini ya miradi yote ya maji na umwagiliaji iliyotekelezwa kuanzia mwaka 2012/2013. Hili ni muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni wakati wa Mbio za Mwenge Wilayani Mbinga kulikuwa pia na uzinduzi wa mradi wa maji katika Kata ya Mkako Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga. Mradi huu ulikataliwa na wananchi kwa sababu umetekelezwa chini ya kiwango kwani mabomba yameunganishwa kwa moto badala ya connectors. Naomba Wizara ipeleke wataalam wake ili kubaini ubadhirifu huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaleta malalamiko haya rasmi kwa maandishi ofisini kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa hatua zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara ikamilishe visima vinne katika program ya visima 10 katika kila Jimbo. Visima hivyo vinne vipo katika Kata ya Litumbandyosi. Ushauri wa ujumla ni kwamba yapo maeneo ambayo kama wananchi watashirikishwa kikamilifu kwenye miradi ya maji, itapunguza sana gharama za miradi husika. Mfano, Wilayani kwetu Mbinga kuna vyanzo vingi vya maji vya gravity. Wananchi wapo tayari kujitolea kufanya kazi kama uchimbaji mitaro na kazi nyingine za kutumia nguvu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ituletee wataalam Wilayani Mbinga ili kutengeneza miradi shirikishi ya maji katika miji, Kata ya Maguu, Ruanda, Matiri, Nyoni, Litembo, Mikalanga, Ilela, Kambarage, Mkumbi, pamoja na Kindimba Juu. Hii inaweza kuwa model kwa maeneo mengine katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango huu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ninayo mambo machache nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na watendaji wake wote katika Wizara kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hili la upimaji wa ardhi, upangaji na urasimishaji wa makazi, wananchi wengi walikuwa wanalisubiri kwa muda mrefu sana uliopita. Kule kwetu Wilayani Mbinga zoezi hili limepokelewa kwa mikono miwili kiasi kwamba ukiangalia kwenye makadirio ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wametoka kwenye shilingi bilioni tatu mpaka shilingi bilioni tisa, lakini makusanyo yao mengi yanatoka kwenye upimaji wa mashamba, muitikio ni mkubwa kiasi kwamba tunategemea pia kuboresha uchumi wetu wa Mbinga kupitia mpango huu wa upimaji ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kumpongeza Mkurugenzi wangu Gombo Samandito Gombo yeye ni mtaalamu pia wa Mipango Miji na ndiyo maana zoezi hili linakwenda vizuri kule Mbinga. Ziko changamoto, changamoto ya kwanza ni elimu, mapokeo ya zoezi lenyewe wananchi wengi walidhani wakipimiwa mashamba yao Serikali inakwenda kunyang’anya mashamba hayo, inakwenda kumiliki mashamba hayo. Changamoto ya pili ni ada za ardhi za mwaka, changamoto ya tatu ni namna ya kugharamia upimaji mpaka watu wakapata hati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa mara nyingine Mkurugenzi wangu alifanya hesabu, Mbinga tunapima kipande cha heka moja kwa shilingi 100,000 lakini bado kuna changamoto namna ya kwenda, mtu ana mashamba ya heka kumi ishirini, tumeshirikisha sekta binafsi wale ni wafanyabiashara wamepata tender, wangependa wapime kiasi kikubwa ili wapate zaidi. Kwa hiyo, unakuta wale wakulima wamelimbikiziwa madeni katika eneo hili la upimaji. Nitoe shilingi milioni tatu kwa mkupuo hapana, tunaongeza umaskini kwa upande mmoja kwa hiyo iratibiwe namna ya kutengeneza malipo ya gharama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika zoezi hili yako maeneo ambayo watu waliona kama wanaonewa, kwa maana kwamba mapokeo yalikuwa watu wavunjiwe nyumba baadhi ya maeneo, kwa hiyo likaleta shida. Pale Mbinga Mjini maeneo ya Tangi la Maji kulitokea na Mkanganyiko huo mlijenga holela kwa hiyo inabidi tuwavunjie kabla ya mipango miji kuwafikia, ikawa shida, mtu huyu amekaa hapa miaka yake hamsini unamvunjia leo nyumba anakwenda wapi? Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri hili litolee maelekezo vizuri. Kama mnaamua kurasimisha makazi ya watu basi elimu ishuke wale Watendaji kule chini waielewe ili, zoezi lenyewe litekelezwe namna gani, vinginevyo kuna kauonevu ndani yake na pengine utekelezaji wake sasa unasuasua kwa sababu hiyo watu wanasita kwa sababu wanahisi sasa hapa nitavunjiwa, hapa nitahamishwa. Mheshimiwa Waziri kwa upande wa Mbinga mimi nilikuwa nataka kusema hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko changamoto kwa upande wa upangiliaji, upimaji na urasimishaji wa miji, mimi ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msingwa kule Dar es salaam Kata ya Msigani. Tunalo zoezi hili, tunayo kampuni binafsi ambayo imepitia kwenu Wizarani, imepitia Halmashauri, tumeshafanya mikutano kadhaa, mapokeo ni mazuri sana na nitumie pia fursa hii kukualika Mheshimiwa Waziri baada ya kumaliza mikutano hii nitakualika kwenye mtaa wangu tukazindue mpango wa upangiliaji miji kule Kata ya Msigani, tutaleta barua rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapokeo ni mazuri, changamoto iliyoko kubwa ni gharama hizi za upimaji, bei elekezi ni kweli Serikali imetoa lakini gharama za umilikishaji ni tatizo, Wizara hamjaziweka wazi, kuna tozo pale zipatazo tisa mpaka uje upate hati mjini, ndiyo maana hati nyingi hazijatolewa kwa sababu ya hizi gharama za umilikishaji. Ziko gharama pale zinahesabika, ziko tisa. Iko gharama ya kuchukua form, premium, ada ya hati miliki, lakini iko ada ya uandaaji wa hatimiliki, hati ya usajili na tunayo ada ya uandikishaji. Sasa tulifanya ukokotoaji pale kwenye Mtaa wangu wa Msingani Dar es Salaam kwenye kiwanja cha square metre 600 kinagharimu shilingi 873,000 ada ya umilikishwaji, acha ile ya upimaji kwa kampuni binafsi.

Kwa hiyo naomba Wizara muangalie upande huu, huo utatukwamisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ninayo mambo machache nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na watendaji wake wote katika Wizara kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hili la upimaji wa ardhi, upangaji na urasimishaji wa makazi, wananchi wengi walikuwa wanalisubiri kwa muda mrefu sana uliopita. Kule kwetu Wilayani Mbinga zoezi hili limepokelewa kwa mikono miwili kiasi kwamba ukiangalia kwenye makadirio ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wametoka kwenye shilingi bilioni tatu mpaka shilingi bilioni tisa, lakini makusanyo yao mengi yanatoka kwenye upimaji wa mashamba, muitikio ni mkubwa kiasi kwamba tunategemea pia kuboresha uchumi wetu wa Mbinga kupitia mpango huu wa upimaji ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kumpongeza Mkurugenzi wangu Gombo Samandito Gombo yeye ni mtaalamu pia wa Mipango Miji na ndiyo maana zoezi hili linakwenda vizuri kule Mbinga. Ziko changamoto, changamoto ya kwanza ni elimu, mapokeo ya zoezi lenyewe wananchi wengi walidhani wakipimiwa mashamba yao Serikali inakwenda kunyang’anya mashamba hayo, inakwenda kumiliki mashamba hayo. Changamoto ya pili ni ada za ardhi za mwaka, changamoto ya tatu ni namna ya kugharamia upimaji mpaka watu wakapata hati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa mara nyingine Mkurugenzi wangu alifanya hesabu, Mbinga tunapima kipande cha heka moja kwa shilingi 100,000 lakini bado kuna changamoto namna ya kwenda, mtu ana mashamba ya heka kumi ishirini, tumeshirikisha sekta binafsi wale ni wafanyabiashara wamepata tender, wangependa wapime kiasi kikubwa ili wapate zaidi. Kwa hiyo, unakuta wale wakulima wamelimbikiziwa madeni katika eneo hili la upimaji. Nitoe shilingi milioni tatu kwa mkupuo hapana, tunaongeza umaskini kwa upande mmoja kwa hiyo iratibiwe namna ya kutengeneza malipo ya gharama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika zoezi hili yako maeneo ambayo watu waliona kama wanaonewa, kwa maana kwamba mapokeo yalikuwa watu wavunjiwe nyumba baadhi ya maeneo, kwa hiyo likaleta shida. Pale Mbinga Mjini maeneo ya Tangi la Maji kulitokea na Mkanganyiko huo mlijenga holela kwa hiyo inabidi tuwavunjie kabla ya mipango miji kuwafikia, ikawa shida, mtu huyu amekaa hapa miaka yake hamsini unamvunjia leo nyumba anakwenda wapi? Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri hili litolee maelekezo vizuri. Kama mnaamua kurasimisha makazi ya watu basi elimu ishuke wale Watendaji kule chini waielewe ili, zoezi lenyewe litekelezwe namna gani, vinginevyo kuna kauonevu ndani yake na pengine utekelezaji wake sasa unasuasua kwa sababu hiyo watu wanasita kwa sababu wanahisi sasa hapa nitavunjiwa, hapa nitahamishwa. Mheshimiwa Waziri kwa upande wa Mbinga mimi nilikuwa nataka kusema hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko changamoto kwa upande wa upangiliaji, upimaji na urasimishaji wa miji, mimi ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msingwa kule Dar es salaam Kata ya Msigani. Tunalo zoezi hili, tunayo kampuni binafsi ambayo imepitia kwenu Wizarani, imepitia Halmashauri, tumeshafanya mikutano kadhaa, mapokeo ni mazuri sana na nitumie pia fursa hii kukualika Mheshimiwa Waziri baada ya kumaliza mikutano hii nitakualika kwenye mtaa wangu tukazindue mpango wa upangiliaji miji kule Kata ya Msigani, tutaleta barua rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapokeo ni mazuri, changamoto iliyoko kubwa ni gharama hizi za upimaji, bei elekezi ni kweli Serikali imetoa lakini gharama za umilikishaji ni tatizo, Wizara hamjaziweka wazi, kuna tozo pale zipatazo tisa mpaka uje upate hati mjini, ndiyo maana hati nyingi hazijatolewa kwa sababu ya hizi gharama za umilikishaji. Ziko gharama pale zinahesabika, ziko tisa. Iko gharama ya kuchukua form, premium, ada ya hati miliki, lakini iko ada ya uandaaji wa hatimiliki, hati ya usajili na tunayo ada ya uandikishaji. Sasa tulifanya ukokotoaji pale kwenye Mtaa wangu wa Msingani Dar es Salaam…

MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwenye kiwanja cha square metre 600 kinagharimu shilingi 873,000 ada ya umilikishwaji, acha ile ya upimaji kwa kampuni binafsi.

Kwa hiyo naomba Wizara muangalie upande huu, huo utatukwamisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuwapongeza Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya katika kuhudumia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie katika maeneo yafuatayo:-

Kwanza ni uhaba wa vituo vya kutolea huduma za afya; Halmashauri ya Mbinga ina jumla ya kata 29, tarafa tano na vijiji 121, lakini kuna zahanati 42 tu na vituo vya afya viwili hivyo kufanya upungufu wa zahanati 79 na uhaba wa vituo vya afya 27. Pamoja na upungufu huo wa vituo vya afya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga haikuletewa fedha za upanuzi/ujenzi wa vituo vya afya kama ilivyofanyika kwenye Halmashauri zingine. Hivyo basi niiombe Wizara iweze kutuletea fedha za upanuzi wa vituo vya afya vifuatavyo; Kituo cha Afya Mapera, Kituo cha Afya Kindimba Chini na Kituo cha Afya Matiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uhaba wa watumishi; kwa idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya tulizonazo Mbinga DC tuna mahitaji ya watumishi 324 wa kada mbalimbali za afya lakini waliopo ni 112 tu hivyo kufanya upungufu wa watumishi 212. Serikali ifikirie kwa haraka walau kutupatia watumishi 22 wanaohitajika ili vituo/zahanati mpya nne zilizokamilika hivi karibuni ziweze kufunguliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jengo la NACP/NTLP Joint Office; Programme za NACP/NTLP walikuwa na mradi wa ujenzi wa ofisi ya pamoja iliyopo Luthuli nyuma ya Ofisi za WHO. Jengo hilo lilikuwa linajengwa kwa ufadhili wa Global Fund. Tangu mwaka 2013 Global Fund waliacha kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo hivyo jengo hilo la ghorofa tatu limekwama na limeanza kuchakaa. Niiombe Wizara iangalie uwezekano wa kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Hospitali ya Mloganzila, niipongeze Serikali kwa ujenzi wa hospitali hiyo. Niiombe Serikali kuipa jicho la pekee hospitali hiyo kwa maana ya kupeleka watumishi wa kutosha. Wananchi wamekwishaanza kutoa malalamiko kuwa ukipelekwa Mloganzila basi unapelekwa pahali ambapo hapana usalama na uhakika wa tiba, vifo ni vingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri kwa kazi wanazofanya. Wizara hii ina changamoto nyingi sana. Hata hivyo, nawapongeza Majeshi yetu yote ya Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto. Kufuatia bajeti ya Wizara hii naomba kuwasilisha changamoto za Gereza Kuu la Kitai kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni uchakavu wa nyumba za watumishi. Hakuna uhaba wa nyumba za watumishi katika Gereza hilo, isipokuwa eneo la Gereza hilo lina tatizo la mchwa. Nyumba nyingi mapaa yake yameliwa na mchwa, hivyo zinavuja na hivyo zinaweza kuanguka wakati wowote na kuhatarisha maisha ya watumishi na familia za wanaoishi katika nyumba hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna uchakavu wa jiko pamoja na mesi ya chakula. Paa nalo limeliwa na mchwa, mesi haina sakafu, wafungwa wanapikia nje kwani jiko limevunjika kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa mlango wa Gereza; lango kuu la Gereza hilo ni chakavu sana kiasi kwamba inawapa ugumu sana wa ulinzi wa wafungwa. Lango hilo linahitaji ukarabati mkubwa sana. Uchakavu wa uzio (fence) iliyopo ni ya miti ambayo siyo imara, hivyo fence au uzio huo unahitaji kuangaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie kuhusu tatizo la maji safi na salama. Gereza lilifanikiwa kuchimba kisima. Kinachohitajika ni jenereta ama umeme jua ili kusukuma maji hayo kwa matumizi ya Gereza hilo. Tunaomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati ili afanye hima kupeleka umeme katika Gereza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni upungufu wa sare za Askari na wafungwa. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri alingalie hili, kwani wafungwa wamekosa uniform kiasi cha ku-repair sare hizo kwa mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu ukosefu wa gari kwa ajili ya kazi za utawala. Gereza hili halina kabisa gari, jambo ambalo linaleta ugumu sana katika kutekeleza majukumu ya kiutawala. Naomba hili lipewe kipaumbele kwa namna yoyote ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, naomba Vituo vyetu vya Polisi vya Mbinga Wilayani; Kituo cha Polisi, Maguu na Kituo cha Litembo, vitengewe fedha kwa ajili ya ukarabati pamoja na kupatiwa vyombo vya usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Spika, naungana na wachangiaji waliotangulia kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya. Nilipongeze pia Jeshi letu la Polisi kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya kutulinda usalama wa raia na mali zetu. Hivi karibuni kumezuka madhehebu mengi sana hususan ya imani ya Kikristo (Pentekoste). Madhehebu hayo mara nyingi hawana ratiba ya kuendesha ibada zao na mara nyingi huendeshwa kwenye makazi ya watu na mara nyingi wanapiga miziki kwa sauti ya juu usiku kucha.

Mheshimiwa Spika, jambo hilo ni kero kwa wakazi wa maeneo mengi. Hivyo naishauri Serikali kuwatengea maeneo maalum madhehebu hayo ya kuendeshea shughuli zao za ibada.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote na mimi nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya ya kutuletea maendeleo. Tumeona kwa macho miradi mikubwa inayotekelezwa. Lakini pia nichukue nafasi hii kukupongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa utendaji wako uliotukuka na kwa hotuba nzuri ya bajeti ya ofisi yako. Baada ya pongezi hizo sasa nianze kuchangia kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la afya. Napenda kuchukua fursa hii kuishukuru Serikali kwa kutuletea fedha kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Afya Mapera. Wananchi wa Tarafa ya Hagati wamenituma salamu zao za pongezi kwa Serikali ya awamu ya tano.

Hata hivyo tunaomba walau tungepata tena shilingi milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Matiri ambayo ina wakazi wengi. Ombi letu lingine ni kuhusu gari ya dharura ya wagonjwa kwa maana ya ambulance. Ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kuhusu TARURA, tumeshuhudia mvua nyingi sana katika msimu huu. Mvua hizi zimeharibu miundombinu ya barabara kwa kiwango kikubwa sana. Ushauri wangu ni kuwa Serikali ifanye upembuzi wa kina kila Wilaya ili kubani ukubwa wa tatizo. Baada ya zoezi hilo katika bajeti hii litengwe fungu maalumu kwa ajili ya kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa na mvua hizo.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa pili katika eneo hili ni kuwa bajeti ya TARURA ipande kufikia walau asilimia 70.

Kuhusu Mfuko wa Wanawake, Vijana na Walemavu, ushauri wangu katika eneo hili ni kwamba Serikali ione umuhimu wa kuweka ukomo wa kipindi cha kuchangia inside indefinitely. Kwani zipo Halmashauri zenye makusanyo makubwa sana ya ndani. Hivyo kama michango hiyo haitawekewa ukomo wa miaka ya kuchangia basi fedha hizo zitakuwa ni nyingi na pengine kupelekea matumizi mabaya.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kupata nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mezani ya bajeti ya TAMISEMI pamoja na ya Utumishi na Utawala Bora. Nami niungane na wenzangu waliotangulia kuchangia kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wa TAMISEMI pamoja na Naibu Mawaziri wake, pia, Waziri wa Utumishi na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na suala la uhaba wa watumishi katika sekta ya afya. Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, ina jumla ya zahanati 42, ina vituo vya afya viwili ambavyo vinahitaji watumishi wa kada mbalimbali wapatao 324. Waliopo hadi sasa hivi wanaohudumia katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ni 112 tu na kufanya upungufu wa watumishi 212. Kwa hiyo, niiombe Wizara iangalie ni namna gani ya kutupatia watumishi ili kuboresha utoaji wa huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Halmashauri yangu ya Wilaya ya Mbinga walikamilisha ujenzi wa vituo vinne kwa maana ya zahanati za kutolea huduma za afya na hivyo kufanya kuongeza uhaba wa watumishi katika Halmashauri yetu. Zoezi hili lilimlazimisha Mkurugenzi wa Halmashauri yetu ya Mbinga Vijijini kuwatoa watumishi ambao walikuwa wanahudumia kwenye vituo vya afya vinavyomilikiwa na Kanisa Katoliki ili waende kuhudumia hospitali hizi ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili lilileta mvutano mkubwa sana na kuharibu mahusiano kati ya Jimbo letu la Mbinga, pamoja na uongozi wa Halmashauri. Tunaiomba Wizara ili kurudisha uhusiano huu angalau ituletee watumishi 22 ili zahanati hizi Nne ziweze kufunguliwa na kurudisha mahusiano ambayo yanaelekea kuharibika kati ya Jimbo letu Kuu la Mbinga pamoja na uongozi wa Halmashauri kutokana na mvutano wa hawa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili lilishapelekwa ofisini kwa Katibu Mkuu wa Utumishi na nina imani atalifanyia kazi haraka iwezekanavyo ili zahanati hizi nne ziweze kufunguliwa na kutoa huduma zilizokusudiwa. Sambamba na upungufu huo wa watumishi wa Wizara ya Afya tunao upungufu wa watumishi wapatao 755 katika sekta ya elimu kwa ujumla wake. Kwa hiyo, tunaiomba pia, Wizara iangalie ni namna gani inaweza kutuletea watumishi katika sekta ya elimu kwa maana ya sekondari na msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wenzangu wamekuwa wakishukuru sana hapa kwamba, wamepatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa vituo vya afya, lakini Mbinga Vijijini hatujaletewa chochote mpaka sasa hivi. Nina imani Waziri amepitiwa tu au amejisahau, naomba aangalie ni kwa jinsi gani ambavyo hata Mbinga Vijijini atatukumbuka ili na tuweze kuletewa fedha kwa ajili ya ujenzi, aidha upanuzi wa vituo vya afya katika Wilaya yetu ya Mbinga. Hususan tunaomba fedha kwa ajili ya upanuzi wa vituo vya afya vifuatavyo: Kituo cha Afya Matiri, Kituo cha Afya Mapera na Kituo cha Afya Kindimbachini, angalau nasi tuwe na vituo vitatu vya afya katika Halmashauri yenye Kata ishirini na tisa (29). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru pia Serikali kwa kuniletea fedha kwa ajili ya ukarabati wa sekondari kongwe ya Kigotera, ujenzi wa madarasa manne, ofisi mbili za walimu na vyoo 10 katika Shule ya Msingi Maguu. Niishukuru Serikali kwa kuniletea vyumba nane vya madarasa na vyoo 20 katika mtaa wangu ninaotoka wa Msingwa, Kata ya Msigani, Wilaya ya Ubungo ambako mimi ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa. Naishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo tunayo maombi maalum. Tunazo sekondari zetu tano ambazo ziko kwenye mpango wa kupandishwa hadhi kutoka kwenye sekondari za kawaida kwenda kwenye A – Level. Kwa hiyo, tunaomba Wizara ituangalie namna gani inaweza kutu- support katika kuzipandisha hadhi sekondari zifuatazo: Sekondari ya Hagati, Sekondari ya Mkumbi, Sekondari ya Mahilo, Sekondari ya Langiro na Sekondari ya Kiamili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitamalizia na suala la TARURA. Tunaipongeza Serikali kwa kuunda TARURA, ni imani yetu kubwa sana chombo hiki cha TARURA kinaenda kutatua matatizo yote ambayo tulikuwa tunakumbana nayo hasa Wabunge wa Majimbo ya Vijijini. Barabara zetu zilikuwa hazihudumiwi kwa kiwango ambacho ni cha kuridhisha kutokana na usimamizi ambao ulikuwa si mzuri kutoka kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyochangia Wabunge wenzangu, tumeona TARURA ina-cover kilometa laki moja na kidogo, bajeti yake bado ni finyu. Kwa hiyo,
naiomba Serikali ione uwezekano wa kutenga huu Mfuko wa Barabara, Road Fund asilimia 50 kwa 50 ili kuiwezesha TARURA iweze kufanya kazi zake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana Meneja wa TARURA Mbinga. Nilipokuwa ziara mwezi wa 11 aliweza kunipa Mhandisi wake nikazunguka naye Jimbo zima ili kubainisha changamoto zilizoko kwenye upande wa usafiri. Pia, tulibaini kwamba, kuna barabara ambazo zinahitaji matengenezo ya haraka, nyingine zinahitaji kuwekezwa kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali kupitia Halmashauri yangu ya Wilaya ya Mbinga kwa maana ya TARURA, waangalie barabara itokayo Mapera kwenda Mikalanga, inaishia Ilela, barabara hii haijapitishwa grader tangu uhuru. Pia, waangalie njia ambayo inahudumia watu wengi na eneo ambalo linazalisha pia njia pacha kutoka Ngima hadi Ukiro pamoja na madaraja yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee sana niiombe Wizara kupitia TARURA Ubungo iiangalie Barabara inayotoka kwa Musuguri mpaka kwa Unju ambayo inaunganisha Ilala, pia barabara inayounganisha Maramba Mawili kuunganisha barabara inayotoka Mbezi kwenda Kinyerezi. Barabara hii inahudumia watu wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la ushauri. Barabara zetu zimepewa code number ambapo barabara hizi baada ya kupewa code number zinaingizwa kwenye mfumo wao wa dromas, nashauri kwamba TARURA waangalie uwezekano wa kuzi-grade hizi barabara kupewa namba kutokana na maeneo yetu ya utawala, kwa maana kwamba wafuate kama ni Kata, ifuate mtaa au kitongoji, ili wasimamiaji tuweze kufuatilia kwa rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukipewa network ya barabara kwa mfano ya Jimbo langu la Mbinga unaikuta barabara namba moja inatoka kwenye Kata nyingine, namba mbili inatoka kwenye Kata ambayo ni ya mbali sana.

Inatufanya ufuatiliaji wa hizi barabara kuwa mgumu. Kwa hiyo, nashauri TARURA wapange hizi codification kutokana na maeneo yetu ya utawala iwe rahisi kufuatilia kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara moja kule Mbinga ambayo ilikuwa inajengwa kwa ufadhili wa EU, barabara hii ilikwama kutokana na changamoto walizopata za udongo. Barabara hii inatoka Longa inakwenda mpaka Litoho. Niliambiwa kwamba, barabara hii imechukuliwa na TARURA. Niiombe sasa Serikali itenge fedha za kutosha, ili barabara hii imalizike kipande cha kutoka Longa hadi Kipololo ambapo ndipo changamoto kubwa ilijitokeza, lakini pia, niiombe Serikali iunganishe kipande cha kutoka Mbinga Mjini hadi Longa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja zilizoko mezani. Nitachangia Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. Na mimi nianze kuchukua fursa kwa kumpongeza sana Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ya kuzifikia Halmashauri zote 185 kwa maana ya ukaguzi na Taarifa yake ndiyo msingi kwa kazi za Kamati yetu ya LAAC. Nitakuwa na maeneo makubwa mawili tu ya kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni mfuko wa wanawake, vijana na walemavu. Eneo la pili ni la uhaba mkubwa wa watumishi katika Mamlaka za Halmashauri zetu nchini. Katika eneo ambalo limekuwa likijionesha kama lina udhaifu mkubwa kwenye halmashauri zetu ni madeni ya mfuko wa wanawake, vijana na walemavu. Halmashauri zetu zilikuwa hazipeleki michango hiyo kwa wakati kwa miaka kadhaa iliyopita lakini niipongeze Serikali ilisikia mapendekezo ya Kamati kwa kutengeneza sheria ambayo sasa imeifanya halmashauri zetu kuchangia kwa lazima katika mfuko huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na sheria hii, madeni ya nyuma yalikuwa ni mzigo mkubwa kwa halmashauri zetu lakini pia Kamati iliona ifike na mapendekezo ya kufuta madeni ambayo yalikuwepo kabla ya kutungwa kwa sheria hii mwaka 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue tena fursa nyingine kuipongeza Serikali kwa kufuta madeni hayo ambayo yalikuwa ni makubwa sana kwa halmashauri zetu. Mwaka 2019, Serikali ilikuja na regulations za jinsi ya kutoa mikopo kwenye vikundi vya akina mama, vijana na walemavu. Moja ya kifungu katika Kanuni hizi inaihitaji vikundi kurejesha baada ya miezi mitatu. Baada ya kuwa wamepata mkopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekutana na changamoto kwenye baadhi ya vikundi ambavyo vimepata mkopo na kushindwa kurejesha baada ya miezi mitatu kwa maana ya kutokana na asili ya biashara ambayo wanakwenda kuifanya. Kanuni hii imezichukulia vikundi vyote kana kwamba vinakwenda kufanya biashara inayofanana. Kwamba watakwenda kupeleka bidhaa sokoni ambazo ziko tayari lakini kumbe kuna vikundi vingine vinakwenda kuwekeza kwenye biashara ambayo inahitaji kuanza kuzalisha baada ya muda mrefu kidogo, pengine miezi sita au mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, nilikutana na kikundi kimoja ambao wao wanakwenda kuwekeza kwenye ulimaji wa matunda na mbogamboga kwa kutumia kitalu nyumba mpaka kupita miezi mitatu ambayo sheria inahitaji waanze kurejesha walkuwa bado wapo kwenye ujenzi wa kitalunyumba na wanahitaji kwa mujibu wa Kanuni hii ya 10 waanze kurejesha mkopo huo. Kwa hiyo, tunaishauri Serikali wakiangalie kifungu hiki, waweze kuvitenga vile vikundi katika ma-group. Vile vikundi ambavyo vinakwenda kufanya biashara straight away viwe na muda wake na vile ambavyo vina uwekezaji wa m uda mrefu viangaliwe ni kipindi gani vianze kurejesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine sheria hii inahitaji halmashauri ziendelee kuchangia kipindi chote indefinitely na lengo ni kutengeneza mfuko ambao utakuwa ni revolving. Ziko halmashauri zetu zingine zina makusanyo makubwa sana ya ndani, kuzifanya zichangie asilimia 10 kwenye mfuko huu kunatengeneza fedha nyingi sana ambazi zitakuwa zinaweza zikalea matumizi mabaya baadaye. Kwa hiyo, tulikuwa tunashauri Serikali iangalie namna ya kujenga mfuko huu. Iweke labda miaka mitano halmashauri zichangie hizo asilimia 10 kufikia labda miaka mitano, halmashari hizi ambazo zina mapato makubwa zinakuwa zimeshatengenza mfuko mkubwa ambao unaweza kujiendesha. Baada ya hapo hizo asilimia 10 zielekezwe kwenye matumizi mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nilihitaji kuchangia ambalo pia limejionesha kwa kiasi kikubwa kwenye vitabu vya Halmashauri zetu ni uhaba mkubwa sana wa watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Wakati fulani tunajiuliza kama halmashauri hizi zinaweza kuendeshwa kwa uhaba huo mkubwa wa watumishi, kwa mfano kule kwenye halmashauri yangu ya Wilaya ya Mbinga tuna uhaba wa walimu wa shule ya msingi wapatao 971 lakini watumishi Sekta ya Afya ni zaidi ya 400, huo ni uhaba. Wakati fulani tunajiuliza ni lini Serikali iliamua kufanya utafiti wa kiwango cha huduma ambazo zinatolewa kwa uhaba huo wa watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda wakati fulani Serikali ijiulize kama Serikali za Mitaa zinaweza kujiendesha kukiwa na uhaba huu mkubwa wa watumishi, hizo ikama zilitengenezwa kwa uhalisia wa mahitaji ya hizo Halmashauri zetu? Labda hiyo inaweza ikatuletea ufafanuzi kwamba hayo ma-gap ya watumishi ni halisia au ni hesabu tu ambazo zilitengenezwa bila kuzingatia uhalisia.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhaba huo unasababisha nafasi nyingi pia za Wakuu wa Idara kukaimiwa. Katika Taarifa za CAG zilizopita zinaonekana kwamba kuna madeni makubwa ya watumishi waliokuwa wanakaimu kwenye nafasi mbalimbali, unaweza kukurta mtumishi anadai mpaka milioni 50. Halmashauri moja inadaiwa milioni 400, 500 kutokana na posho za kukaimu nafasi mbalimbali za Ukuu wa Idara. Kwa hiyo, tunaishauri Serikali ifanye upekuzi mapema ili kuondokana na madeni ambayo si ya lazima wakati mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine hili la uhaba wa watumishi kwa mfano kule kwenye Halmashauri yetu ya Mbinga umefanya majengo mengi ambayo yamekamilika ya zahanati yasiweze kufunguliwa kwa wakati ni kutokana na uhaba wa watumishi wa Idara ya Afya kwa mfano zahanati ya Lukiti ambayo imepewa jina la Martin Mtonda Msuha haijafunguliwa kwa sababu ya uhaba wa watumishi. Zahanati ya kijiji cha Longa, zahanati ya Matuta na Kijiji na Ruanda. Zahanati hizi zote zimekamilika lakini hakuna watumishi wa kwenda kuanza kutoa huduma katika maeneo hayo. Kwa hiyo, nguvu za Serikali na za wananchi zimebaki hazitumiki ipasavyo kwa sababu ya kutosa watumishi wanaohitajika wa Idara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho kwa sababu muda bado ninao, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuona kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani umekuwa ni changamoto kwa Halmashauri zetu na hivyo basi kutokana na hamashauri zetu kutokukusanya mapato ya kutosheleza matumizi yao imesababisha halmashauri nyingi kubadilisha matumizi. Halmashauri nyingi zimekuwa zikikopa kutoka kwenye akaunti ya amana ili kukidhi mahitaji yake ya ndani. Jambo hili limesababishwa na kutoweza kukusanya mapato yao ya ndani kikamilifu. Niipongeze Serikali imeliona hili, juzi hapa wamegawa mashine za kukusanyia mapato zipatazo 7,229 ambazo zimesambazwa nchi nzima kwenye Halmashauri yetu. Ni imani yetu sasa mashine hizi zitasimamiwa vizuri na TAMISEMI kwa maana ya kwamba zile controls walizoweka ili wale watumishi wasiwe wanachezea tena zile mashine kuziweka offline wakati wakiwa wanaendelea na makusanyo itafanyika hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini uhaba huu wa fedha za ndani umesababisha pia madeni makubwa sana kwa madiwani wetu. Madiwani wetu hawajalipwa posho kwa muda miezi mingi karibu Halmashauri nyingi nchini. Kwa hiyo, naishauri pia Serikali iangalie namna ya kufanya uchambuzi wa madeni ambayo madiwani wetu wanadai tunavyoeleka kukamilisha miaka mitano ya kipindi chetu cha utawala.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa lakini pia Kamati ya PAC. Ahsante sana. (Makofi)