Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Halima Abdallah Bulembo (34 total)

MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara haijataja asilimia ngapi itakwenda kwa vijana wa kike na wa kiume; naomba Wizara ichukue ushauri wangu kwamba zile fedha zitakapopelekwa halmashauri waweze kusema asilimia kumi itakuwa kwa vijana wa kike na wa kiume na hii itapunguza mkanganyiko katika halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze katika maswali yangu mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
(a) Je, kwa nini Serikali isianzishe dhamana kwa vijana kukopa (credit guarantee scheme for youth)?
(b) Je, Serikali inaona kuna umuhimu wa kujenga mfumo madhubuti wa hifadhi ya jamii ili kuwezesha vijana kuweka akiba yao ya uzeeni, kupata bima ya afya na hata kuweza kupata mikopo katika biashara zao?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, katika eneo la kwanza la mikopo kwa ajili ya vijana, upo mpango wa muda mrefu na wa muda mfupi. Kwa sasa Serikali imeendelea kutoa mikopo kwa vikundi mbalimbali vya vijana kupitia katika SACCOS za Halmashauri lakini mpango wa muda mrefu ni kuja kuanzisha benki maalum ya vijana ambayo ndiyo itakuwa sehemu pekee ya vijana wengi kupata mikopo. Kwa hiyo, mpango wa muda mrefu ni uanzishwaji wa benki lakini tumeanza na SACCOS kwa ajili ya kuwajengea tabia vijana ya kufahamu masuala ya fedha kwa maana ya ukopaji na nidhamu ya urudishaji fedha.
Mheshimiwa Spika, la pili la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwashirikisha vijana, tayari katika programu mbalimbali za Mifuko ya Hifadhi za Jamii wamekuwa na eneo hili la kuwashirikisha vijana kupitia shughuli mbalimbali. Mojawapo ni Shirika la NSSF ambao tayari wameanzisha programu ambayo inaitwa AA Plus kwa maana ya Akiba na Afya kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, ambapo wanafunzi watachangia Sh. 20,000 kwa mwezi na watapata matibabu bure kwa muda wote ambao watakuwepo vyuoni lakini atakapohitimu mafunzo yake ya chuoni ile fedha anaweza kurejeshewa au akiamua ibaki kama akiba basi anaendelea kuitumia ikiwa ni sehemu yake pia kumsaidia baadaye kupata mikopo akiwa mwanachama wa shirika.
MHE. HALIMA A.BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya madhara ya Madaktari feki wamekuwa wakisababishia wagonjwa hawa vilema vya maisha au kupoteza maisha kwa ujumla.
Je, kuna utaratibu wowote wa fidia kuwafidia watu hawa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, japo kuwa Mheshimiwa Halima Bulembo ni jirani yangu ungenitonya kwamba utaniuliza swali. Kwanza hakuna tukio lolote lile ambalo limewahi kuripotiwa ambapo Daktari feki amesababisha madhara kwa mgonjwa. Madaktari feki hawa mara nyingi kwa matukio ambayo tunayafahamu wamekuwa wakitoa huduma kisanii tu kwa malengo ya kutaka kukusanya pesa hususani zile wa rushwa kutoka kwa wateja. Lakini haijatokea wakafanya haswa kitendo cha kwenda kutoa tiba kwa mgonjwa, hususani labda kufanya operesheni ama kufanya procedure. Kama ingewahi kutokea hivyo pengine labda kungekuwa kuna sheria ambayo ingekuwa inatuongoza kwamba nini kiwe fidia kwa mteja yoyote yule ambaye atakuwa amesababishiwa madhara kutokana na Madaktari feki.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Nakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa fursa hii. Watafiti Joel Lugala na Jesse Mbwambo katika andiko lao la kitafiti linalosema au lililoandikwa street children and street life in urban Tanzania; the culture of surviving and its implication for children health la mwaka 2013; watafiti hawa katika hitimisho lao wanasema, Serikali ya Tanzania hailijui tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Na kwa majibu ya Serikali ni dhahiri tatizo hili halieleweki na hitimisho hili ni thabiti. Je Serikali itachukua hatua gani kulielewa tatizo hili kwani linazidi kukuwa siku hadi siku? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inatambua mfumo wa uchumi umebadilika hayo yanayosemwa kwamba watoto watalelewa na ndugu, au walezi hayapo kwa sasa. Watoto yatima wamekuwa wakinyanyaswa, wakidhulumiwa mali zao na ndugu wa wazazi; je, Serikali ipo tayari kubadili mtazamo wake kuhusu watoto wanaoishi katika mazingira magumu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum kwa swali lake zuri la nyongeza aliloliuliza, lakini pili akiwa Mbunge mdogo kuliko wote hapa Tanzania amekuwa siku zote mstari wa mbele kutetea haki za vijana na watoto. Ni Mbunge wa kutiliwa mfano na ninakupongeza na ninaomba uendelee kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujibu swali Lake…
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Nalijibu Mariam haraka za nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujibu swali lake napenda kusema na narudia tena kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kwamba mtazamo na msimamo wa Serikali uko wazi na hautotetereka. Kwamba sehemu ya kwanza na ya muhimu na ya lazima kwa malezi ya mtoto wa Kitanzania ni kwenye familia yake. Kama imetokea kwa sababu moja ama nyingine wazazi wamefariki ama hawana uwezo wa kutoa malezi yanayohitajika kwa mtoto, familia pana (extended family) inapaswa kuchukua jukumu hilo na kama haiwezekani jamii pana inapaswa kuchukua jukumu hilo. Yote haya yakishindikana, sasa inakuwa ni wajibu wa Serikali kuwachukua watoto hawa na kuwatunza kwenye makao maalum kwa ajili ya malezi ya watoto, huo ndio msimamo wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na msimamo huu haimaniishi kwamba Serikali hailielewi tatizo hili, tatizo hili tunalifahamu, Serikali imefanya tafiti mbalimbali, na pamoja na hiyo tafiti ya akina Joe Lugala na wenzake tunaifahamu, na tumeifanyia, kazi na haimaanishi kwamba tafiti hiyo basi ndio hiyo hiyo tu hakuna tafiti nyingine na kwamba inatoa mwongozo wa kila kitu hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tafiti nyingi zimefanyika na zote tunazichambua na tunazifanyia kazi. Naomba nimtoe shaka Mheshimiwa Halima Bulembo kwamba Serikali iko macho kuhusiana na suala hilila malezi ya watoto, na kwamba tutaendelea kusimamia msimamo wetu, kwamba kisaikollojia, kijamii, na kwa maana ya kutoa ulinzi stahiki na mapenzi yanayohitajika kwa watoto wa nchi hii Serikali itakuwa mstari wa mbele. Nitoe rai kwenu nyote Waheshimiwa Wabunge na watanzania wote kwa ujumla mnaonisikiliza tujitahidi kuwalea watoto na kuhamasisha jamii ziwalee watoto kwenye unit ya family.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana, lakini nataka kuongeza suala moja. Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, jukumu la kwanza la malezi ya mtoto liko chini ya wazazi la pili familia. Lakini kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto, kifungu cha 94 kinasema ni jukumu la Serikali za Mitaa kuhakikisha kinachukua hatua zote za kuhakikisha watoto wanaoishi katika mazingira magumu haki zao zinatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama kusisitiza Wabunge wote, ni Wajumbe wa baraza la Madiwani. Sisi Wabunge tumechukua hatua gani ya kuhakikisha watoto yatima katika wilaya zetu, katika halmashauri zetu wanapata haki ya elimu, wanapata haki ya elimu ya ufundi wanapata malazi, na wanapata chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili jambo si la Serikali kuu ni jambo letu sisi wote Wabunge, tunapokaa kwenye mabaraza ya madiwani tujiulize mmechukua mikakati gani ya kupambana na tatizo la watoto yatima na watoto wa mitaani. Niliona niiweke hivyo wazi, wakisubiri Wizara ya Afya wao wakae tu kama si kipaumbele chenu haliwezi kuwa kipaumbele cha Watanzania kama sisi Wabunge hatutatia mkazo suala la watoto yatima,
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna raia wa kigeni ambao wamekuwa wakitumia udhaifu wa mfumo wa hati za kusafiria na kuwawezesha kusafiri kinyume cha utaratibu na kuwawezesha kutenda makosa kwa kigezo cha Utanzania. Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba wanapatikana lakini hatujajua wala hatujawahi kusikia ni hatua gani ambazo zimekuwa zikichukuliwa. Je, Serikali imewachukulia hatua gani maofisa hawa wanaojihusisha na utoaji wa hati hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Maafisa Uhamiaji ambao wanajihusisha na ukiukwaji wa taratibu wamekuwa wakichukuliwa hatua mbalimbali. Miongoni mwa hatua hizo ni kuwafukuza kazi pamoja na kuwashtaki. Hata hivyo, naomba nichukue fursa hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba tupo katika hatua za mwisho za ukamilishwaji wa uanzishwaji wa Mahakama ya Kijeshi katika Idara ya Uhamiaji kama ilivyo katika majeshi mengine ikiwemo Polisi ili kuweza kuwa na utaratibu wa uchukuaji wa hatua hizo kwa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kabisa pale mchakato huo utakapokuwa umekamilika, basi tutaweza kufanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi. Kwa wale ambao tumekuwa tukiona mazingira tu yanaashiria utendaji mbovu au ukiukwaji wa sheria ikiwemo rushwa bila ya kupata ushahidi tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwahamisha katika vituo vyao vya kazi.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na swali zuri lililoulizwa juu ya ajira ya kilimo kwa vijana wa Mkoa wangu wa Kagera, Serikali katika bajeti ya mwaka 2016/2017, ilionesha nia na dhamira ya dhati ya kuinua ajira kwa vijana. Je, Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wake katika sera ya ajira ya vijana katika sekta ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba katika mpango wetu wa bajeti ya mwaka huu tuna mikakati mingi ya kuwasaidia vijana kupata ajira kwenye sekta ya kilimo. Kama nilivyokwishasema, tayari Wizara inashirikiana na vijana wengi ili kuhakikisha kwamba wanajihusisha katika shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari vijana wengi tumewasaidia kuingia kwenye Vyama vya Ushirika, lakini vilevile tayari vijana tunawaunganisha katika fursa za mikopo. Mfano mzuri, ni fursa iliyopo katika benki ya NMB ambayo tayari wametenga shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kilimo cha biashara na kwa wale vijana ambao wameunganika katika vikundi kama wale niliosema wanaosaidiwa na Mheshimiwa Ester Mmasi tayari tunaongea na NMB ili waweze kutoa mikopo kwa ajili ya vikundi hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile NMB wako tayari kutoa elimu ya kilimo kwa ajili ya vijana ambao watapata mkopo. Vilevile, katika kutekeleza kusudio letu la kuhakikisha vijana wanapata ajira kupitia kilimo, tumetenga hekari 220 katika bonde la Rufiji ili liweze kuwa shamba darasa ili vijana wengi waweze kuelewa namna zaidi ya kujihusisha na kilimo. Kwa hiyo, kama ninavyosema kuna mipango hiyo na Mheshimiwa Halima namfahamu ni mtu ambaye anawapigania sana vijana nae vilevile ili…
Ili aweze kupata maelezo zaidi, namkaribisha…
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba niulize swali moja dogo la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, changamoto kubwa katika kuanzisha Benki za Maendeleo ni mtaji. Hivi sasa nchini kwetu tumejiwekea utaratibu kwamba kila Halmashauri hutenga 5% kwa ajili ya vijana. Bajeti ya mwaka huu katika Serikali za Mitaa imekusanya takriban shilingi bilioni 600 ambapo katika ile 5% ya vijana ni sawasawa na shilingi bilioni 30. Iwapo fedha hizi zitatumiwa vizuri, tunaweza kuanzisha Benki ya Vijana zenye matawi katika kila Halmashauri na tukiweza katika hili, tutaweza kutatua suala zima la mikopo kwa vijana.
Je, Serikali haioni ni vyema sasa, Halmashauri zote nchini kuwa wanahisa wa Benki za Vijana na kutumia fedha hizi kama mtaji wa kuanzisha benki hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Spika, nataka tu nianze kwanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwafuatilia vijana wa nchi hii na amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba vijana wengi wanapata fursa ya mitaji na mikopo.
Mheshimwa Spika, katika swali lake la msingi, ni kweli kwamba umekuwepo utaratibu wa utengaji wa 5% za mapato ya ndani kwa kila Halmashauri ambao lengo lake kubwa ni fedha hizi kwenda kuwafikia vijana. Kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, lengo kubwa la uanzishwaji wa benki hii ni kutaka ije imilikiwe baadaye na vijana kupitia SACCOS za kila Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatua ya kwanza ambayo Serikali tuliianza ni kwamba mwaka 2014/2015 alitafutwa mtaalam kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na baadaye sasa Serikali tukaanza kuchukua hatua; mojawapo ni kuhakikisha kwamba kila Halmashauri nchi nzima inaanzisha SACCOS ya vijana ili baadaye SACCOS hizo za vijana ndiyo zije zimiliki hisa katika hii benki.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwondoe hofu tu Mheshimiwa Bulembo kwamba tukikamilisha uanzishwaji wa SACCOS katika Halmashauri, kazi itakayofuata sasa itakuwa ni namna ya kuutafuta huo mtaji na wazo alilolitoa ni wazo jema. Kama Serikali, tunalichukua, tutaona namna ya kuweza kulifanyia kazi.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, tatizo linalozikabili zahanati nyingi nchini siyo upungufu wa dawa tu, bali pia huduma kwa akinamama wajawazito, hususan katika wodi zao huduma ni mbaya, ni hafifu, vifaa stahiki hakuna: Je, ni lini Serikali itahakikisha inaboresha afya kwa akinamama wajawazito katika hospitali na zahanati zote za Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nitoe majibu ya uhakika kwamba, kwanza nimkumbushe Mheshimiwa Halima Bulembo kwamba kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika vipaumbele vitano kwenye Sekta ya Afya ambavyo vimeandikwa mle ni pamoja na kuboresha huduma za akinamama wajawazito na watoto.
Kwa maana hiyo, naye kama Mwana-CCM mwenzangu lazima anafahamu kwamba jitihada za kupunguza matatizo na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye huduma za akinamama wajawazito, zimekuwepo, zitaendelea kuwepo na ndiyo maana hata leo tutakapowasilisha bajeti yetu ataona tuna mikakati mahususi ambayo imejikita kwenye kuboresha huduma za uzazi kwa akinamama wajawazito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hili ni jambo ambalo Mheshimiwa Rais mwenyewe alilizungumza pia hapa Bungeni na sisi wakati anatukabidhi majukumu haya alituagiza tulisimamie kwa nguvu za kutosha. Kwa hiyo, ni jambo ambalo kwa hakika hatulifanyii mzaha hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba huduma za uzazi zitakuwa bora na yeye atajifungua salama kadiri Mungu atakavyomsaidia.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Je, Serikali haioni umuhimu wa kugeuza Kambi za JKT kuwa vyuo vya VETA ili pamoja na mafunzo ya Kijeshi, vijana pia hasa wale wa kujitolea waweze kupata mafunzo ya ufundi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa sasa, hususani kwa wale vijana wanaoingia kwa kujitolea yana awamu mbili, kuna mafunzo ya Kijeshi ya miezi sita ya kwanza na baada ya hapo kuna mafunzo ya Stadi za Kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Jeshi la Kujenga
Taifa linafanya utaratibu wa kupata usajili wa VETA ili waweze kutoa vyeti hivyo kwa wale wanaomaliza pale JKT. Kwa hiyo ni kwamba, Stadi za Kazi zinatolewa, zitaendelea kutolewa na usajili unatafutwa ili hatimaye vijana wanaomaliza pale siyo tu wawe wamemaliza JKT bali pia waweze kupata vyeti vya VETA. (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nchi nyingi duniani stesheni za reli ni vituo vya biashara tofauti kabisa na nchini kwetu Tanzania. Serikali inaweza kueleza ni kwa nini stesheni kubwa kama Morogoro, Dodoma, Tabora na Mwanza huduma huwa zimedumaa na hakuna huduma za biashara? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, TRL ipo tayali kushirikiana na sekta binafsi kuendesha stesheni za reli kwa kuziboresha ikiwemo kuweka hoteli, huduma za maduka na kadhalika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo kuuliza kitu ambacho Serikali nayo imekuwa ikijiuliza ni kwa nini wafanyabiashara hawachangamkii fursa za kufanya biashara katika maeneo ya stesheni za reli. Kwa sababu ametupa nguvu zaidi leo, suala hili tutaendelea kulisukuma, TRL waangalie uwezekano wa kuwahamasisha wafanyabiashara washirikiane nao kama wataona hili linafaa katika mazingira ambayo wanafanyia biashara hiyo ya reli.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. RCC ya Mkoa wa Kagera ilishatoa kibali kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Karagwe, lakini suala hilo linakwamishwa na Wizara ya TAMISEMI kwa sababu haitaki kutoa usajili ili hospitali hiyo itengewe bajeti na ujenzi uanze mara moja. Je, ni lini Wizara ya TAMISEMI itaamua kutoa usajili huo ili ujenzi uanze mara moja ili kuokoa akina mama na watoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la dada yangu Mheshimiwa Halima Bulembo na kwanza nimpe hongera sana kwa kazi kubwa aliyofanya katika sekta hii ya afya, hongera sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, bahati nzuri nimefika Karagwe, bahati nzuri pia anafahamu hata pale Karagwe kulikuwa hakuna DMO. Sisi TAMISEMI ndiyo tukamchukua kijana mmoja anaitwa Sobo tukampeleka pale, ni daktari mzuri sana wa upasuaji. Hata Karagwe pale tulikuwa hatuna centre ya Serikali ya kufanya upasuaji sasa hivi upasuaji pale Karagwe katika kituo cha afya umeanza.
Si hivyo tu, lilivyotokea tetemeko la ardhi, Serikali imefanya juhudi kubwa sana kuboresha kile kituo cha afya na hivi sasa tunapeleka takribani shilingi milioni 500 kufanya wananchi wa Karagwe wanapata huduma nzuri ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie kwamba katika ofisi yetu hakuna kibali kitakachokwama isipokuwa wakati mwingine ni changamoto ya bajeti. Tunachukua mawazo yote ya Wabunge wa Karagwe, tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo kutekeleza vipaumbele vyenu mlivyoweka katika mpango wa bajeti maana siyo suala la kibali, kibali sisi hamna tatizo isipokuwa ni pamoja na kuona ni jinsi gani tutenge bajeti kuhakikisha tunajenga hospitali ya wilaya.
Kwa hiyo, ni jukumu la Serikali, tutafanya kila liwezekanalo wananchi wa Karagwe kama tunavyofanya sasa tutaendelea kufanya hivyo ili mradi huduma ya afya ipatikane vizuri katika Wilaya ya Karagwe na Halmashauri yake kwa ujumla. (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri, migogoro ni moja ya sababu inayokwamisha jambo hilo, lakini migogoro hiyo haijazuia wananchi wetu kufanya biashara. Ni kwa nini Serikali isirahisishe movement ya wananchi wetu hasa hasa vijana wa Kitanzania kuchangamkoa fursa ya soko kubwa la Congo ikizingatiwa Congo ni land locked country? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyozungumza tuna utaratibu mzuri tu ambao unatumika na uko kwa mujibu wa sheria, wa wananchi ambao wanahitaji kufanya biashara, kwa Watanzania ambao wanahitaji kwenda Congo na wale wa Congo ambao wanahitaji kuja Tanzania. Utaratibu uliopo sasa hivi ni utaratibu wa kutumia viza ambazo zinaitwa business visa kwa nchi ya DRC. Lakini hoja ya msingi hapa ilikuwa ni jinsi ambavyo tunaweza kufanya ili kuwa na utaratibu ambao utakuwa ni mzuri zaidi. Ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba utaratibu wa viza uliopo sasa hivi si kikwazo kwa biashara kwa mtu yeyote ambaye anahitaji kufanya biashara katika nchi hizi mbili.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo kwa kutambua umuhimu wa kurahisisha zaidi tunatarajia kwamba amani itakapokuwa imetengemaa katika DRC mazungumzo yetu yatakamilika haraka ili tuweze kuwa na utaratibu mzuri zaidi.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera kuna vijiji ambavyo vimewekwa katika mpango wa Rea Awamu wa Pili, vijiji kama Songambele, Kitwe, Mulongo lakini havikupatiwa umeme. Vijiji hivi hivi pia vimewekwa katika Mpango wa REA Awamu ya Tatu. Je, Serikali itahakikisha katika Mpango huu wa REA Awamu ya Tatu, vijiji hivi havitakosa umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Kyerwa ambapo vimebakia 27 vitapelekewa umeme vijiji vyote na siyo tu vijiji ambavyo umetaja vya Mulongo pamoja na Songambele lakini viko vijiji na chuo vya ufundi pale Kyerwa na chenyewe tutakipelekewa umeme. Kwa hiyo vijiji vyote 27 vilivyobaki vitapelekewa umeme katika mradi wa REA Awamu ya Tatu.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya asilimia 56 mpaka 60 ya watanzania ni vijana lakini vijana wanashindwa kutimiza malengo yao ama ndoto zao kutokana na gharama kubwa ya upangaji wa nyumba za makazi hasa mijini kuwa kubwa na wamiliki kutaka kupewa kodi za mwaka au miezi sita.
Je, ni lini sasa Serikali itafuta utaratibu huu na sisi kama Bunge tutunge sheria itakayowalazimisha wamiliki wote kupokea kodi ya kila mwezi badala ya mwaka ama miezi sita kama ilivyo sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze kwa kuona kwamba ipo haja ya kuona kwamba wapangaji wa nyumba wanakuwa na sheria ambayo inasimamia katika suala zima la upangaji. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge kwamba Wizara tayari imekwishaliona hilo na tayari tupo kwenye mchakato wa kuanzisha mamlaka itakayosimamia masuala yote ya nyumba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sheria hiyo ambayo italetwa hapa Bungeni, tumeangalia suala zima la ukomo wa kutoa kodi za nyumba, hiyo ya miezi sita na mwaka mmoja haitakuwepo kwa sababu tumeona inaumiza watu wengi. Kwa hiyo, kodi itakuwa inalipwa kwa mwezi mmoja mmoja na wakati huo huo utatakiwa kuweka kama amana ya miezi mitatu kwa ajili ya shughuli ambazo zinaweza kuwa, kwa hiyo nimesikia na tunalifanyia kazi. (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa naibu Spika, mwaka jana tumeshuhudia Serikali yetu ikijaribu kupunguza tatizo la utumiaji wa madawa ya kulevya kwa kuwataja hadharani watumiaji na wauzaji jambo lililosaidia kupunguza lakini siyo kumaliza tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee. Nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia mwaka jana Serikali yetu ikijaribu kupunguza tatizo la utumiaji wa madawa ya kulevya kwa kuwataja hadharani watumiaji na wauzaji lakini jambo hili halikumaliza tatizo bali ilipunguza tu, suala hili bado lipo tena kwa wingi zaidi na wanaoathirika ni vijana wa Kitanzania ambao ni nguvu kazi ya nchi. Je, ni lini sasa Serikali itaona umuhimu wa kujenga rehab zitakazotambulika ili kumaliza janga hili? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda nichukue fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Halima Bulembo kwa namna ambavyo anawapigania vijana wa Taifa letu la Tanzania, lakini amekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya vijana. (Makofi)
Mheshimiwa naibu Spika, ni kweli tunafahamu kwamba moja kati ya njia ya kuwarudisha waathirika wa dawa za kulevya katika hali yao ya kawaida ni pamoja na kuwa na sober houses nyingi na rehabilitation centers ambazo zitawasaidia kuwarudisha kururdi katika hali yake ya kawaida. Ndiyo maana katika majibu yangu ya msingi nimesema, moja kati ya mkakati ambao tunao ni uanzishwaji wa tiba ambao inaitwa occupational therapy ambao lengo lake kubwa ni kumsaidia muathirika huyu wa dawa za kulevya kurudi katika hali yake ya kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utaratibu huo, waathirika wote wa dawa za kulevya ambao watapelekwa katika vituo vyetu mbalimbali watafundishwa stadi mbalimbali za kazi ili baadaye akirudi asirejee katika matumizi ya dawa za kulevya. Katika mpango wetu huo, Serikali tunaanza utoaji wa tiba hiyo katika kituo ambacho kinajengwa hapa Dodoma katika eneo la Itega. Hali kadhalika tunafanya kazi pia na taasisi na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kwamba tunawasaidia vijana wetu wa Kitanzania wasipate madhara zaidi ya matumizi ya dawa za kulevya.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 8 Septemba, 2016 niliuliza swali kama hili na nikatoa utafiti nikampa Naibu Waziri ambao ulionesha Serikali ya Tanzania haijui tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Baada ya kusikiliza majibu ya Serikali, nalazimika kusema kwamba bado Serikali haijalijua kwa undani suala la watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Je, ni lini sasa Serikali itaamua kufanya utafiti na kuja kutupa namba sahihi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema kwamba Serikali haijui takwimu sahihi na hapa katika majibu yangu ya swali la nyongeza ambalo lilikuwa limeulizwa na Mheshimiwa Maryam Msabaha nimetoa takwimu naomba nizirudie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mikoa sita ambayo tumefanya ukaguzi kwa maana ya Mkoa wa Mwanza, Dar es Salaam, Iringa, Mbeya, Dodoma na Arusha tumebaini watoto 7,748 kati yao 6,365 walikuwa wanashinda mitaani na kurudi majumbani na watoto wengine 1,383 hushinda na kulala mitaani.
Katika hawa watoto Mheshimiwa Halima Bulembo 952 tumeweza kuwarudisha na kuwaunganisha na familia zao. Kwa hiyo, naomba nimalizie kwa kusema kwamba Serikali inatambua tatizo hilo na imeshachukua hatua.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo yaliyoko Longido yanafanana kabisa na ya mkoani kwangu Mkoa wa Kagera Wilaya ya Bukoba Vijijini, Kata ya Maruku na Kanyangeleko ambapo kumekuwa na mradi mkubwa wa maji uliojengwa tangu miaka ya 60 mpaka 70 na mradi huu uliweza kufanya kazi kwa miaka 10 na uliwahudumia wananchi wengi. Mradi huu tayari una vyanzo, una matenki, kinachohitajika katika mradi huu ni ukarabati. Je ni lini mtaukarabati mradi huu ili uweze kuwahudumia wananchi wa Bukoba Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze anasoma historia, mama huyu anawapenda wananchi wa Kagera na kwa sababu ni mama anahusika na kuchota maji, kwa hiyo uchungu wake anaujua. Amesoma historia miaka ya 60 na 70 kwamba mradi huu ulijengwa na kuwahudumia wananchi kwa muda wa miaka 10, lakini sasa hivi ni kwamba umechakaa unataka ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa taarifa hii na nimwagize Mkurugenzi wa Maji wa Kagera aweze kuangalia na Mheshimiwa Rweikiza ameshaniambia kuhusu mradi huu na nimeshawaagiza Wakurugenzi wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, waende wakauangalie mradi huu kuona unahitaji nini ili tuweze kuufanyia ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba katika awamu ya pili ya maendeleo ya sekta ya maji, tunataka kuhakikisha kwamba miradi yote ya zamani inafanyiwa utafiti na tunaikarabati ili iendelee kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokuwa inatarajiwa.

WAZIRI OFISI YA RAIS TAMISEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji kwa majibu mazuri sana, yanayohusiana na masuala ya maji. Hata hivyo, nataka niongezee tu kwenye jibu hilo juu ya swali liloulizwa na Mheshimiwa Bulembo, ambaye amezungumzia juu ya miradi ya maji iliyojengwa miaka mingi na ilikuwa imefanya kazi kwa ufanisi, lakini leo hii ama imechakaa, ama miundombinu yake haitoshelezi idadi ya watu iliyoongezeka ama vijiji vilivyoongezeka na kwa hivyo inashindwa kumudu na watu wanapata shida ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, kwa ujumla wetu, sisi ndio wenye Majimbo na tunatoka kwenye maeneo haya, kama miradi hii haitabainishwa na kuorodheshwa kwenye mipango ya Halmashauri ya kila mwaka, siyo rahisi sana Serikali ikaweza kuitekeleza. Serikali inaamua mambo yake na kupanga na kuyatekeleza kupitia kwenye bajeti. Sasa kama haisomeki kwenye bajeti siyo rahisi kuiona na hata mimi ambaye kwa kushirikiana na Wizara ya Maji tunatekeleza miradi mbalimbali, kwa namna ambavyo tunaletewa na Halmashauri husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo la kwanza ni kuiweka kwenye mipango ya maendeleo au ya kwenye bajeti, ikisomeka hivyo inakuwa rahisi kuiona, lakini pia kuitengea fedha na kuikarabati miradi hii. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwenye bajeti inayokuja, miradi yote ile iliyochakaa muiweke kama kipaumbele cha miradi ya kukarabatiwa, siyo miradi mipya, miradi ya kukarabatiwa, ili Wizara ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Maji tuweze kukaa na kuona kama tuje na mpango gani, au program gani ili tuweze kuitekeleza miradi hii.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Tumekuwa tukiona mapori mengi ya hifadhi yakiingiliana na makazi ya watu katika jamii na mapori hayo yamekuwa yametengwa kwa muda mrefu sana.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kugawa mapori haya ya hifadhi yaliyotengwa kwa muda mrefu kwa wananchi, ili waweze kufanya shughuli za kijamii kama kilimo, na mifugo na hii itaweza kuwaondolea adha ya migogoro ya wafugaji na wakulima?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inayo taarifa na inatambua kwamba iko kiu kubwa ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi kwamba pengine wangechukua maeneo yale ili waweze kuyatumia katika shughuli zingine za kibinadamu, ikiwemo kilimo, ufugaji, pamoja na shughuli zingine. Lakini ni kweli pia sisi sote ni wananchi na nchi ni moja na kwamba sababu za kuifadhi maeneo hayo zilizingatia pia uhitaji wa mahitaji yetu ambayo ni ya kudumu ya muda mrefu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu utaratibu ule, wa kuweza kuyatwaa maeneo haya na kuyatumia kama Hifadhi, yalikuwa ni maamuzi yetu sisi sote pamoja, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, tulishirikisha Vijiji, Wilaya pamoja na Mikoa ili kuweza kukubaliana kwamba maeneo hayo yahifadhiwe kwa sababu ambazo zina maslahi mapana zaidi, si kwa Taifa tu, lakini pia hata kwa wananchi ambao ni wa nchi nzima na sio wale wanaoishi kwenye maeneo yale tu pale walipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, narejea tena kusema kwamba kwa sababu umepita muda mrefu tangu maeneo hayo yalipotwaliwa kuwa kama hifadhi, pengine mazingira yamebadilika, pengine kuna sababu ambazo zinaweza zikaonekana kwamba zina uzito zaidi hivi sasa, ndio maana nimesema Serikali inakwenda kulishughulikia suala hili kimkakati, itakuwa ni pamoja na kushirikisha wananchi upya, wote twende tukaangalie na tupime kwamba je, sasa tuseme nchi hii isiwe na hifadhi kabisa? Maeneo yote tutwae kwa ajili ya shughuli zingine za kibinadamu? Pengine hiyo itakuwa ni upande mmoja haiwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tukisema kwamba kinyume chake kwamba maeneo yale ya hifadhi yote yabaki kama yalivyo, pengine kuna maeneo tunatakiwa kufanya marekebisho kidogo. Sasa tukatae kwa sababu kuna Sheria, hata kama kuna ukweli kwamba kwa sasa hivi kuna sababu za msingi, pengine na yenyewe itakuwa si sahihi. Ndio maana tunasema kwamba sasa Serikali pamoja na wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo, na pengine wananchi kwa nchi nzima wakitoa maoni tutakwenda kufika mahali sasa tukubaliane kwamba maeneno yapi tunahifadhi, kwa sababu zipi ambazo zitakuwa ni kwa maslahi ya taifa. Niwakumbushe sio kwa maslahi tu ya Taifa, sisi kama nchi tumesaini pia mikataba ya kimataifa, kuhusu masuala ya uhifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, muda hautoshi ningeweza kusema zaidi lakini napenda kuishia hapa, tunakwenda kufanya zoezi hili kwa pamoja, kutatua kero hizi kwa namna ambayo itakuwa ni endelevu, na ya kudumu.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ilani ya Chama cha Mapinduzi moja ya ahadi kubwa iliyotolewa ilikuwa ni kujenga VETA katika kila Wilaya Tanzania nzima. Kwa kuwa Mkoa wa Kagera unaongoza kwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne lakini wanashindwa kujiendeleza kutokana na ukosefu wa vyuo hivyo. Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha vijana hawa wanajengewa vyuo hivyo angalau hata katika Wilaya tatu za Mkoa wao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa Mkoa wa Kagera ni kweli kuna uhitaji wa fursa hizo, lakini tayari kuna Chuo cha VETA pale Makao Makuu ya Mkoa. Vilevile kuna Chuo cha Wananchi Karagwe (KVTC) ambacho tunaendelea kukifanyia ukarabati na sasa hivi tayari tupo kwenye hatua za mwisho ili kiweze kuchukua wanafunzi wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Gera ambacho nacho kilikuwa katika hali mbaya sasa hivi kimeshafanyiwa ukarabati na tutaendelea kukiboresha ili kiweze kuchukua wanafunzi wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niseme kwamba, kwa Mkoa wa Kagera kuna fursa kubwa ambapo tuna chuo tunategemea kukijenga kule Muhengele ambacho kitakuwa kinatoa mafunzo ya ujuzi wa juu zaidi kidogo kulingana na mahitaji ya soko kwa kushirikiana na ndugu zetu wa China.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo wagonjwa wote wa akili wanaranda mitaani hata miongoni mwetu tunaweza kuwa wapo wagonjwa wa akili. Kwenye nchi za wenzetu wamefanya utafiti wa wagonjwa wa akili nchi kama Marekani, Uingereza na Australia, tafiti zao zinasema katika kila watu wanne kuna mgonjwa mmoja mwenye tatizo la akili. Je, ni lini sasa nchi yetu itamua kufanya utafiti kama huu ili kubaini tuna wagonjwa wangapi wa akili nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikubaliane na Mheshimiwa Halima Bulembo kwamba, siyo wagonjwa wote wa akili wanarandaranda mitaani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa tafsiri ya afya ya Shirika la Afya Duniani inasema kwamba being health is not just merely absence of disease is mental, physical and social well-being. Sasa siyo kwamba tu unapokuwa na mwili umeathirika ndiyo unaweza ukasema kwamba wewe umeathirika. Kwa hiyo, katika suala la afya ya akili, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba si kila mtu anayerandaranda mitaani ndiyo mwenye ugonjwa wa akili, hata sisi inawezekana kama nilivyokuwa nimesema, katika swali langu la msingi, tunakadiria kwamba asilimia moja ya Watanzania wana matatizo ya akili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya akili naomba niendelee kutoa maelezo tuna matatizo mengi sana ya akili. Kuna sonona ambayo ni depression, kuna schizophrenia, kuna mania, obsessive complusive disorder, kuna mlolongo mkubwa sana ambao ni mpana sana na ambao kwa kweli hatuwezi tukafanya utafiti wa moja kwa moja kuweza kubaini katika jamii, ila tunaweza tukalifanya kwa wale ambao wanafika katika vituo vyetu vya afya na wale ambao tunaweza kuwabaini katika jamii. (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, tuhuma hizi zimekuwa zikijirudia mwaka hadi mwaka na kwa muda mrefu. Nchi nyingi duniani huwatumia watu wake kwenda kufanya kazi nje ya nchi ili kuingiza remitance, fedha za kigeni. Mfano India ni nchi ambayo inaongoza dunia kwa remitance, inaingiza dola za Kimarekani bilioni 69. Je, ni kwa nini sasa Serikali yangu isione umuhimu wa kuingia makubaliano na nchi hizi zinazohitaji wafanyakazi, ili kukuza sekta hii, kuwalinda na kuiboresha zaidi? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE YA NCHI NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba nchi nyingi zimeingia mikataba na nchi ambazo zinaajri watu ambao wanatoka nje ya nchi nyingine na kwamba, wanapata remitance. Kama nilivyowaambia kwamba, sisi tumeweka makubaliano, yani kuna mikataba kati ya sisi pamoja na nchi hizi za kiarabu kwa hiyo, mikataba ipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu tuweke utaratibu wa kuzihusisha nchi nyingine, nadhani zaidi ya hizi nchi za kiarabu, tutafanya hivyo na tunaupokea ushauri.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Ninaomba nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa kipindi kirefu tumekuwa sasa tukipokea hayo malalamiko ya namna Watanzania na baadhi ya wafanyakazi kutoka nchi nyingine za Afrika wanavyopata shida kule wanakokwenda kufanya kazi nje ya nchi zao. Huduma hii ya kuwaunganisha Watanzania na watafuta wafanyakazi nje ya nchi ya Tanzania inasimamiwa na Sheria ya Wakala wa Huduma za Ajira Na. 9 ya mwaka 1999.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa katikati, mwaka huu mwezi wa pili kwenda wa tatu, nilisimamisha huduma hizo kwa nchi nzima ya Tanzania ili kufanya ukaguzi wa kutosha wa kujiridhisha kama wakala hawa wanafanya kazi zao kwa kufuata sheria. Wanafahamu Watanzania wanaoenda kufanya kazi huko nje wanaishije, wana matatizo gani na nini kifanyike ili kuwaokoa kwenye kadhia wanayoipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliunda timu imefanya utafiti na matokeo hayo wameshaniletea. Tumegundua kwamba ziko fursa nyingi za ajira kule nje ya nchi yetu ya Tanzania kama vile Saudi Arabia, Qatar na nchi nyingine. Lakini aina ya ujuzi unaotakiwa kule nje kama tutajipanga vizuri ndani ya Serikali na ninalihakikishia Bunge lako tutaanza kufanya hivyo, tuna uwezo wa kuwapeleka Watanzania wengi kwa mikataba rasmi na wakarudisha mapato ya kutosha kwenye nchi yetu na wakapata ajira nje ya nchi ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mdogo tu; kule Saudi Arabia wanahitaji wafanyakazi takribani 2,000 wa ujuzi wa kati na ujuzi wa juu kwenye fani kama za marubani, madaktari, walimu, madereva na za kazi za namna hizo ambazo zina ujuzi.
Ninalihakikishia Bunge lako baada ya ripoti hii sasa tutajipanga sawasawa na Watanzania watapata ajira zenye staha nje ya nchi na watarudisha mapato ndani ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kwa TANESCO hasa eneo la uzalishaji, lakini hasara ya Shirika la TANESCO imekuwa inaongezeka kwa kasi zaidi. Kati ya mwaka 2015 mpaka 2017 ambapo TANESCO wameongeza hasara ya shilingi bilioni 124 mpaka shilingi bilioni 346.
Swali langu, Serikali ina mkakati gani unaotekelezeka kuhakikisha inapunguza hasara hizi na hatimaye kupata faida? (Makofi)
Swali langu la pili, TANESCO itagawanywa lini ili kutofautisha uzalishaji na usambazaji wa umeme? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri katika swali hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba kwa muda mrefu Shirika letu limekuwa likijiendesha kwa hasara. Napenda kutoa taarifa tu katika Bunge lako kwamba hivi sasa Shirika la TANESCO limeanza kuongeza uzalishaji kuliko miaka iliyopita. Kipindi cha Julai mwaka 2017 hadi Machi mwaka huu, revenue ya TANESCO kwa wiki imeongezeka kutoka shilingi bilioni 29.1 mpaka shilingi bilioni 32.5. Kwa hiyo, ni maendelea mazuri ya Shirika letu katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu zilizochangia ni pamoja na kwanza kuzuia kuingiza vifaa kutoka nje, kitu kilichokuwa kinaligharimu shirika kwa kiwango kikubwa sana. Kitu cha pili ni kuwaunganisha wateja na LUKU kwa nchi nzima ambao ni mpango unaendelea na ni matumaini yetu Shirika litaendelea kuwaunganisha wateja na kupata mapato makubwa, na lingine ni kuondo kana na mafuta kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyojibu.
Mheshimiwa mwenyekiti, swali la pili kwamba ni lini Shirika litagawanywa? Mantiki kubwa ya Shirika hili ni kulionyesha kwamba linafanya kazi kwa manufaa. Suala la kuligawa ni suala ambalo ni endelevu, ni suala ambalo tunatakiwa kulitafakari kwa kina sana kwa sababu kufanya hivyo ni lazima pia tuangalie madhara yake. Mantiki kubwa vile vile ni kwamba lazima Shirika lijiendeshe kifaida na liweze kumudu majukumu yake na kazi hizo zinaendelea.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuku kwa kuniona. Kumekuwa na malalamiko mengi ya waathirika wa dawa za kulevya wanapokuwa rehab (rehabilitation) wanakaribia kupona wahusika wanawachoma tena dawa ya kulevya ili wasiweze kutoka na lengo limekuwa ili waendelee kujipatia fedha.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha rehab zao wenyewe ili kuweza kuwasaidia waathirka hawa dawa za kulevya?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia kubwa ya sober house zinamilikiwa na watu binafsi na hilo lililolalamikiwa na Mheshimiwa Mbunge hatujapata malalamiko rasmi. Hata hivyo niseme tu kwamba kwa kuzingati hizi sober house nyingi ziko chini ya watu binafsi tumeamua sasa kutengeneza miongozo ambayo itasaidia namna bora ya management ya hizi sober house ili inapotokea mazingira ya namna hiyo tuwe tuna sehemu ya kuweza kukabiliana nao, kwa sababu miongozo ile itakuwa inaeleza mtu ambaye ni muathirika wa madawa ya kulevya awe treated vipi. Mpango wa Serikali, katika swali lake, ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na sober house nyingi za Serikali ili kuondokana na changamo hii ambayo wananchi wengi wanaipata hasa kutokana na gharama kubwa ya kulipia katika hiyo sober house.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Tumepokea hii taarifa sasa mara kadhaa na hata wakati wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Waheshimiwa Wabunge wametuarifu kwamba uko mchezo mbaya unaoendelea kwenye sober house; badala kuwasaidia vijana wetu wapone na waondoke ndani ya sober house, lakini taarifa ambazo tumekuwa tukizipokea ni kwamba wamiliki wa sober house wanataka kuendelea kuwaweka vijana wetu pale kwa faida binafsi. Naomba sasa nitoe tena agizo kwa wamiliki wa sober house wote ambao wana mchezo huo ambao umekuwa ukisemekana wauache haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninatumia muda huu pia kuiagiza mamlaka sasa kuanza kufanya uchunguzi wa kina na atakaye bainika ana tabia hiyo aweze kuchukuliwa hatua haraka sana na hiyo itatusai kuwaokoa vijana wetu kutokuendea kutumia dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
MHE. HALIMA ABDALLAH BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Moja ya changamoto mbalimbali za maji ni ukosefu wa vyanzo vya maji, lakini sisi Mkoa wa Kagera Mwenyezi Mungu ametujaalia tuna vyanzo vingi vya maji. Ukiachilia mbali Ziwa Victoria tuna mito mingi ukiwemo Mto Kagera, lakini shida ya maji imekuwa ni kubwa zaidi na kuna wakati Wilaya ya Ngara kuna wanafunzi walilipotiwa kukosa masomo kwa sababu ya kutafuta maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo Serikali imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa ya maji nchini lakini Mkoa wa Kagera umekuwa ukiwekwa pembeni. Waziri atakubaliana na mimi sasa umefika muda Mkoa wa Kagera uwe una mradi mkubwa mmoja wa maji ili uweze kusambaza maji katika vijiji vyote vya Mkoa wa Kagera na huyo Mkandarasi Mshauri atakubali suala hili la kimkakati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu langu la pili, Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la AFD lilikubali kufadhili Mradi wa Maji Bukoba Mjini. Je, Serikali ipo tayari kuwaomba Serikali ya Ufaransa iendelee kufadhili Mkoa wa Kagera ili waweze kutatua tatizo la maji kuwasaidia wananchi hasa hasa akinamama na watoto wa Mkoa wa Kagera? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILAIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekati, napenda kumpongeza mdogo wangu Mheshimiwa Halima Bulembo; ni miongoni mwa Wabunge makini sana katika Bunge hili na amekuwa ni mtetezi mkubwa sana kwa akinamama na watoto katika suala zima la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie, jukumu la Wizara ya Maji ni kuhakikisha Wanakagera wanapata maji na si maji tu, ni kwa maana ya maji safi salama na yenye kuwatosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu kwa kuona hali ya changamoto ya maji kwa Mkoa wa Kagera tumetekeleza Mradi mkubwa sana katika Mji wa Kagera zaidi ya bilioni thelathini na mbili katika kuhakikisha wananchi wa Bukoba wanapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; tuna mradi mwingine katika miji 17, tunaenda kujenga mradi mkubwa sana katika Mji wa Kayanga kwa kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa katika kuhakikisha wananchi wa Kagera wanaenda kupata maji hayo. Kingine, katika Bajeti ya mwaka 2018/ 2019 tumetenga zaidi ya Sh.13,520,000,000/= katika kuhakikisha wananchi wa Kagera wanapata maji. Niwaombe sana wataalam wetu wa maji wa Mkoa wa Kagera wasilale na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Kagera wasimamie fedha hizi katika kuhakikisha zinaenda kutatua tatizo la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili nataka nimtie moyo Mheshimiwa Mbunge; ukisoma Mathayo-7 inasema ombeni nanyi mtapewa, bisheni hodi nanyi mtafunguliwa. Tumeshawafungulia wananchi wa Kagera, sisi tuko tayari kuendelea kuwatafuta wafadhili katika kuhakikisha tunaenda kutatua tatizo la maji Kagera. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kuna utaratibu wa kuunganisha wilaya kwa wilaya. Wilaya ya Bukoba Vijijini inapakana na Wilaya ya Misenyi kutoka katika Kijiji cha Msira kwenda katika Kijiji cha Bulembo, pale katikati kuna mto na watu wanaoishi pale wengi ni wakulima wa zao la kahawa. Je, ni lini Serikali itaamua kuunganisha vijiji hivi kwa kujenga barabara ili kuwarahisishia wakulima hawa wa zao la kahawa usafiri wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunafahamu umuhimu wa kuunganisha wilaya kwa wilaya kwa kiwango cha lami na nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mipango ipo kwa ajili ya kuunganisha Wilaya ya Bukoba Vijijini na Misenyi na taratibu mbalimbali za kiuhandisi zimeshaanza kuhakikisha kwamba kiwango hicho kinawekwa hivi karibuni pesa zitakapopatikana.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakurushukuru. Serikali itakubaliana na mimi kwamba sekta binafsi ina mchango mkubwa katika elimu. Mwaka jana wanafunzi takriban 19,000 waliokuwa wanaingia kidato cha tano walikosa nafasi katika shule za Serikali. Mheshimiwa Naibu Waziri, hamuoni imefika wakati sasa kuzipunguzia kodi shule binafsi ili hawa wanafunzi wanaokosa nafasi katika shule za Serikali waweze kumudu ada elekekezi katika shule binafsi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima Bulembo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba sekta binafsi ina nafasi nzuri sana katika kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu. Serikali itaendelea kushirikiana nao ili kuondoa changamoto zinazowakabili ili waweze kuwekeza kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeshaondoa tozo na kodi kubwa nne ambazo zilikuwa zinawaletea changamoto. Tupo tayari kujadiliana nayo ili kuangalia ni namna gani tunaweza kuboresha mazingira ili waweze kuwekeza kwa urahisi zaidi.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru. Ukiachilia mbali Mkoa wa Kagera uko karibu zaidi na Ziwa Victoria, lakini Mkoa wa Kagera una uhaba mkubwa wa maji. Ni lini sasa Wizara itaamua kubuni mradi mkubwa wa maji kama ule unaotoa maji Ziwa Victoria kwenda Tabora, ukizingatia Mkoa wa Kagera uko karibu zaidi na Ziwa Victoria? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua maji ni uhai nasi kama Wizara ya Maji jukumu letu ni kuhakikisha tunawapatia wananchi maji. Tumefanya jitihada mbalimbali wananchi ambao ni wakazi wanaoishi pembezoni na maziwa kuhakikisha wanapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mkurugenzi wa eneo husika aandae mradi ambao sisi kama Wizara tutaangalia namna ya ku-support kwa haraka wananchi wake waweze kupata maji kwa haraka safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 iliahidi kujenga VETA katika kila Wilaya. Je, ni lini sasa Serikali itaanzisha mkakati wa kujenga VETA katika kila Wilaya ili kuwasaidia vijana kupata ujuzi wa kuweza kujiajiri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeainisha kwamba Serikali itajenga VETA katika kila Wilaya. Serikali imeanza ujenzi wa VETA katika baadhi ya Wilaya na mpango upo wa kujenga VETA katika kila Wilaya na kila Mkoa, lakini tunajenga kadri fedha zinavyopatikana. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango upo pale pale. (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Maji kuhakikisha inawafikishia wananchi wote maji Tanzania, lakini kumekuwa na kero kubwa na mbaya zaidi kutoka Wizara ya Maji ya kubambikia wananchi bili.

Je, ni lini Wizara hii itaweka mkakati wa kutatua kero hii kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni haki ya mwananchi kupatiwa maji, lakini pamoja na haki hiyo ya kupatiwa maji, mwanachi naye ana wajibu wa kulipia bili za maji, lakini siyo kulipia tu, anatakiwa alipie bili za maji ambazo siyo bambikizi. Sisi kama viongozi wa Wizara tumeshawaita Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Maji na tukawapa agizo na kuwaandikia hadi mkataba, kwa maana ya kuhakikisha kwamba hili tatizo wanaliondoa kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba ambao tumekubaliana ni katika kuhakikisha Mamlaka zote tunatoka sasa katika mfumo wa zamani tuwe katika pre-paid meter. Nataka nitumie nafasi hii tena kuwaagiza kuanzisha suala zima la pre-paid meter katika kuhakikisha tunaondokana na malalamiko haya ili kuhakikisha kwamba wananchi wanalipia maji kadri wanavyotumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii, wote tunatambua jambo kubwa linalotuweka Watanzania pamoja ni kutokuwa na ubaguzi, lakini mikopo ya wanafunzi wa Chuo Kikuu imekuwa ikitolewa kwa ubaguzi. Mfano, mimi nimepata division one nasoma Feza, mwenzangu kapata division one anasoma Msalato, atakayepewa mkopo ni yule anayetoka Msalato kwa maana ya kwamba wa Feza ni wa kishua, wa Msalato ni maskini, huu ni ubaguzi wa hali juu, tunajua hustles zinazotumiwa na wazazi kuwapeleka watoto wao shule nzuri tu na si kwamba wana pesa nyingi sana. Je, Wizara itakubaliana na mimi umefika wakati sasa wa kubadilisha kigezo cha kupata mikopo na kigezo kikuu kiwe ni ufaulu wa mwanafunzi badala ya kwamba huyu ana mahitaji zaidi ya mwenzie? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Halima kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi vigezo vilivyowekwa ni hasa vinazingatia hali halisi ya uhitaji wa mwanafunzi kwamba mwanafunzi mwingine hana uwezo. Kwa hiyo kama hana uwezo ndiyo atakayesaidiwa kwanza.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi nina swali moja tu la nyongeza. Pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Shirika letu la Ndege la Taifa, kumekuwepo na malalamiko makubwa ya wananchi hususan kuhusu bei za tiketi. Ni kwa nini Serikali isione kuna umuhimu wa kupunguza gharama hizi za tiketi ili wananchi wengi waweze kumudu usafiri huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, itapelekea shirika kuongeza routes badala ya kuwa na route moja kwa siku wanaweza kuwa na route mbili mpaka tatu. Mfano Dodoma – Dar es Salaam kuna route moja...

MWENYEKITI: Ahsante sana, umeeleweka.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Halima Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei za safari za ndege za ATCL huwa zinapangwa kutokana na hali ya soko. Ni ukweli usiopingika kwamba ATCL wako kwenye ushindani na sisi Serikali tunaendelea kuwa-encourage na watu wengine waendelee kutumia usafiri wa anga kupeleka ndege zao maeneo mbalimbali. Sasa hivi wanashindana na watu kama Precision na mashirika mengine, kwa hiyo, hayo mashirika mengine kutokana na ushindani huo ndiyo bei inajipanga yenyewe, huwa inapangwa kutokana na market force.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri kabisa na pili nimefurahi kusikia Mheshimiwa Waziri ametambua kuwa Mkoa wa Kagera ndiyo mkoa pekee nchini unaopakana na nchi nyingi za Afrika Mashariki. Mkoa wa Kagera unapakana na nchi nne za Afrika Mashariki kati ya tano kwa maana ya Burundi, Rwanda, Uganda, Tanzania yenyewe ambayo Kagera imo na hata Kagera inaifikia Kenya kwa kupitia Ziwa Victoria.

Ni kwa nini sasa Serikali isione kuna umuhimu wa kuufanya Mkoa wa Kagera kuwa kituo kikubwa cha biashara Afrika Mashariki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa hivi sasa Mkoa wa Kagera ndiyo mkoa pekee unaolima na kuzalisha kahawa nyingi nchini na hata tafiti zimeonesha hivyo kwamba Mkoa wa Kagera unazalisha asilimia 65.6 mpaka sasa, lakini kumekuwepo na malalamiko mengi ya utoroshwaji wa kahawa kutoka Mkoa wa Kagera kwenda Uganda.

Ni lini sasa Serikali itajenga mnada wa kimataifa Mjini Bukoba ili kahawa zote za maeneo ya Maziwa Makuu ziuzwe Mjini Bukoba? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge jinsi anavyowapigania wakulima wa kahawa wa Mkoa wa Kagera, hii inaonesha namna gani alivyokuwa jirani na watu wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali kwa kutambua umuhimu wa Mkoa wa Kagera kwenye uchumi wa Taifa hili na hasa uzalishaji wa kahawa kama alivyosema, inazalisha zaidi ya asilimia 40 ya kahawa yote nchini, lakini ndiyo mkoa unaoongoza kwa kilimo cha kahawa aina ya Robusta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumeshapanga sisi kama Serikali kwamba kuanzia msimu wa mwaka huu tutakuwa na minada ya kanda kwenye kanda zote nne za uzalishaji wa kahawa hapa nchini; kwamba tutakuwa na mnada wa Kanda Kagera, Kilimanjaro, Nyanda za Juu na kule Ruvuma. Pia nimtoe wasiwasi kwa mujibu wa takwimu na hali halisi ilivyo, kahawa yote ya Mkoa wa Kagera asilimia zaidi ya 90 inauzwa katika soko la moja la moja (direct export) na mpaka sasa tunapoongea, wakulima hasa Chama Kikuu cha Ngara kimeshaanza kuleta makubaliano hayo, kahawa yote imeshauzwa imebaki tu asilimia 10 ambayo ndiyo itaenda kwenye mnada. Ahsante sana.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, wanafunzi wengi waliokuwa wanasoma shule binafsi wamekuwa wakinyimwa mikopo ya elimu ya juu kwa kigezo kuwa wazazi wao wana uwezo wa kuwalipia. Je, ni kwa nini sasa Serikali isifute kigezo hicho kwa sababu si wanafunzi wote wanaosoma binafsi wana uwezo, lakini wengine wamekuwa wakienda binafsi kwa kukosa nafasi katika shule za umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Halima Bulembo ni kati ya Wabunge wanaowakilisha vijana Bungeni na hakika na hili sidhani kama ni la mjadala, amejitahidi sana katika miaka hii muhimu kufanya kazi yake vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina hakika vijana wenyewe wanamfuatilia na hata anapouliza swali hili sasa la leo, ni katika jitihada hizo za kuwakilisha vijana katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sheria yetu inayotuongoza kwenye mikopo haibagui watoto wanaosoma kwenye shule binafsi. Sheria inataka tu tutumie vigezo vile vya kuangalia uwezo wa mtu kujilipia masomo ya chuo kikuu. Kwa hiyo, kinachofanyika ni kwamba, waombaji wote tunawafanyia kitu kinaitwa minutes testing, wanajaza fomu, tunangalia taarifa na kuangalia kama wanaweza wakajifadhili. Kwa hiyo, mtu anaweza akawa amesoma kwenye shule binafsi, lakini kumbe amefadhiliwa, tunachoomba, kama mtu amefadhiliwa, alete ushahidi, alete kiambatisho wakati anajaza fomu.

Mheshimiwa Spika, mwaka huu, kuna wanafunzi 500 ambao wamesoma shule binafsi, wengine wamesoma mpaka Feza School, lakini kwa sababu wameleta uthibitisho wa kwamba wamesomesha na wazazi wao hawana uwezo, tunawasomesha. Kwa hiyo, naomba niendelee kutoa rai na ufahamu kwamba, kusoma kwenye shule binafsi siyo kigezo cha kukosa mkopo! Tunaaangalia uwezo, inawezekana mtu amesoma lakini kafadhaliwa.

Mheshimiwa Spika, naomba vilevile ifahamike kwamba, tuna rasilimali kidogo na tuna wahitaji wengi, ndiyo maana, kama tukipata fursa ya kutoa mikopo, tutatoa kwanza kwa wale ambao hali zao ni mbaya zaidi, kabla hatujatoa kwa wengine kwa sababu tunataka tulete ulinganisho katika elimu. Tunafanya kitu kinachoitwa equity, kwa hiyo, hakuna upendeleo, ni sheria ambayo imetungwa na Bunge hili, ndiyo inatuelekeza.

Mheshimiwa Spika, na katika miaka hii tumefanikiwa kuendelea kuongeza wigo wa wanafunzi wengi kupata mikopo na ndiyo maana mwaka huu tumeweza kuongeza kutoka wanafunzi 41,000 wa mwaka wa kwanza, hadi kufikia wanafunzi 45,000. Nina hakika tutaendelea kuboresha taratibu hizo za kutoa mikopo na ikiwezekana huko mbele ya safari, kadri uwezo utakavyoruhusi, inawezekana hata kila mtu yeyote anayetaka mkopo akapata. Isipokuwa tunapenda kuendelea kusisitiza kwamba ule ni mkopo. Kwa hiyo, kama mzazi ana uwezo wa kumsomesha mwanaye, asitafute mikopo kwa sababu baadaye atawajibika kulipa.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa niishukuru Wizara kwa majibu yao mazuri lakini kiukweli mabadiliko hayajaanza kufundishwa vyuoni wala shuleni na TANESCO wamekuwa wakitumia nyaya za zamani. Kwa hiyo basi, kuna mkanganyiko mkubwa zaidi na ukizingatia sasa hivi tuko katika uchumi wa viwanda. Hivyo basi, naiomba Serikali yangu itafute namna sahihi ya kutatua mkanganyiko huu ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza katika kuchanganya nyaya za umeme. Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, pamoja na kupokea ushauri kwa sababu jambo hili ni la muhimu, naomba nitoe maelezo kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, kimsingi hizi rangi hazina athari kwa ujumla wake isipokuwa chimbuko la mabadiliko haya ya rangi ilikuwa ni kwa ajili ya kuweka mazingira wezeshi kwa upande wa wenzetu ambao tumekuwa tukichukua standard zao (Commonwealth) walipokuwa wameungana na hawa nchi za Ulaya. Kwa hiyo, unakuta watu wa AU walikuwa na standard zao na watu wa British walikuwa na standard zao ilibidi wawianishe na ndiyo zikatokea hizi rangi nyingine ambazo zimejitokeza.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa mazoea, watu wetu walikuwa wamezoea mtindo huu wa red yellow, blue. Sasa kinachofanyika ni kwamba kupitia TBS, kuanzia mwaka 2010 tulianza kufanya huo uwianisho na tayari tumeshafikia hatua nzuri. Vilevile ili kuondoa hizi changamoto ambazo zinaweza kusababisha madhara kutokana na watu kuchanganya hizo rangi japo pia tunasisitiza na sheria inasema kwamba mtu anayefanya wiring installation iwe kwenye high voltage au low voltage lazima awe na uwezo wa kutosha na awe amethibitishwa au kama akifanya mtu mwingine asiyethibitishwa lazima apeleke kwa aliyethibitishwa.

Kwa hiyo, tunategemea kwamba TBS itakuja na huo mwongozo maalum unaoelekeza hizi standards ili sasa ziweze kutumika kwa mkazo zaidi. Hata hivyo, suala la mpito hilo hata kwenye nchi nyingine lilifanyika.

Mheshimiwa Spika, pia nawaomba wakandarasi wanapokuwa wamefanya kazi inayochanganya mfumo wa zamani na mfumo wa sasa, waweke maelekezo pale kwenye main switch ili mtu yeyote anayefika aweze kujua kwamba mfumo huu umechanganywa.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri kabisa, lakini nina maswali mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mkoa wa Kagera siyo vijiji peke yake ambavyo havijapata umeme wa REA. Kumekuwa na Taasisi kubwa kama shule na Vituo vya Afya ambavyo bado havijapata umeme wa REA na kupelekea kushindwa kutoa huduma zinazotakiwa kwa wakati. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha taasisi hizi zinapata umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, wananchi wa Mkoa wa Kagera wamekuwa wakikumbwa na kadhia ya kulipishwa nguzo za umeme. Serikali au Wizara inazungumziaje kadhia hii inayowakuta wananchi wa Mkoa wa Kagera? Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Halima Bulembo anapofuatilia masuala ya umeme katika Mkoa wa Kagera. Nampongeza sana na kweli kazi kubwa imeonekana kutokana na jitihada zake hasa kwa kupitia vijana. Hongera sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika masuala yake mawili ya nyongeza. Swali la kwanza anataka kujua kuhusiana na upelekaji wa umeme katika taasisi za Umma. Naomba nitoe maelekezo kwa Halmashauri zetu na Waheshimiwa Madiwani wanaonisikiliza. Ni kweli Serikali imekuwa ikipeleka umeme katika maeneo yote hasa vijijini lakini baadhi ya taasisi zimekuwa hazilipiwi na wamiliki wa taasisi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana wamiliki wanaohusika walipie gharama ya 27,000 ili taasisi zote zipelekewe umeme. Maelekezo na mwelekeo wa Serikali ni kuhakikisha taasisi zote zinapelekewa umeme. Nakupongeza Mheshimiwa Halima Bulembo kwa sababu katika Mkoa wa Kagera hadi sasa taasisi 897 zimepelekewa umeme na hii ni jitihada kubwa. Naomba maeneo mengine ambayo hayajapelekewa umeme, wanaohusika waendelee kulipia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia taasisi tukiwa na maana ya shule, Vituo vya Afya, Zahanati, Misikiti, masoko na hata kama kungekuwa na maeneo madogo ya viwanda. Kwa hiyo, nitoe sana ombi kwa Waheshimiwa Wabunge kupitia kwa Madiwani na Wenyeviti wa Halmashauri tupeleke kwa kulipa shilingi 27,000/= katika Taasisi za Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili kuhusu kulipishwa nguzo; ni kweli zipo changamoto katika baadhi ya maeneo, yapo maeneo bado Wakandarasi na Mameneja wa TANESCO wanaendeleza kutoza nguzo wateja. Naomba nitoe tamko kali sana kupitia Bunge lako Tukufu kwamba ni marufuku kutoza nguzo kwa wateja wote; iwe Mkandarasi awe Meneja wa TANESCO, awe Injinia, awe Kibarua wake ni marufuku kulipiza mteja nguzo. Hii ni kwa sababu Serikali imegharamia kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)