Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Felister Aloyce Bura (15 total)

MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Eneo la Msalato lenye kilometa tisa katika ujenzi wa barabara ya Dodoma – Kondoa – Babati kwa kiwango cha lami bado halijakamilika.
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa kipande hicho kilichobaki cha Dodoma – Manyara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kipande cha barabara chenye urefu wa kilometa 8.65 cha eneo la Msalato ni sehemu ya barabara ya Dodoma – Kondoa hadi Babati yenye urefu wa kilometa 251. Barabara hii inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na imegawanyika katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni barabara ya kutoka Dodoma mpaka Mayamaya yenye urefu wa kilometa 43.65; sehemu ya pili, ni barabara ya kutoka Mayamaya mpaka Mela yenye urefu wa kilometa 99.35 na sehemu ya tatu, ni barabara ya kutoka Mela mpaka Bonga yenye urefu wa kilometa 88.8. Aidha, barabara ya kutoka Bonga hadi Babati yenye urefu wa kilometa 19.6 ilishajengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa sehemu ya Dodoma hadi Mayamaya yenye urefu wa kilometa 43.65 unaendelea. Utekelezaji umefikia asilimia 80 ambapo jumla ya kilometa 35 zimeshawekwa lami na zimebakia kilometa 8.65 katika eneo la Msalato.
Mheshimiwa Spika, ujenzi ulikuwa umesimama kwa muda kutokana na Mkandarasi kutokulipwa kwa wakati. Kwa sasa Serikali inaendelea kulipa madai ya Wakandarasi akiwemo Mkandarasi anayejenga barabara hii ya Dodoma hadi Mayamaya.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea malipo, Mkandarasi anayejenga barabara hii sasa yuko kwenye maandalizi ya kuanza ujenzi na kazi inatarajia kukamilika mwezi Desemba, 2016.
Kituo cha afya cha Chamwino Ikulu kinahudumia zaidi ya Kata 20 za Wilaya ya Chamwino na wanawake na watoto wa kata hizo wanategemea sana huduma za kituo hicho, lakini hakina vifaa tiba muhimu kama vile ultra sound:-
Je, ni lini Serikali itanunua ultra sound kwa ajili ya kituo hicho?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kituo cha afya cha Chamwino hakina ultra sound kwa ajili ya huduma za mama na wajawazito na watoto. Kifaa hicho kinagharimu shilingi milioni 72.0 ambazo hazijawekwa kwenye bajeti ya Halmashauri kutokana na ukomo wa bajeti. Hata hivyo Halmashauri imewasilisha maombi ya mkopo wa shilingi milioni 72 katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili kupata fedha zitakazowezesha kifaa hicho kununuliwa, katika Bajeti ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, wagonjwa wanao hitaji huduma hiyo kwa sasa, wanapewa Rufaa kwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ambapo huduma hiyo inapatikana.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Benki ya wanawake nchini ilianzishwa kwa nia ya kuwasaidia wanawake kupata mikopo kwa haraka na kwa riba nafuu.
Je, ni wanawake wangapi wameshanufaika na mikopo ya benki hiyo kwa Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) ilianzishwa mwaka 2009 katika misingi ya kujiendesha kibiashara ikiwa na jukumu mahsusi la kuwapatia wanawake mikopo yenye masharti nafuu na kwa haraka. Kimsingi benki hii inatoa huduma zake kwa wananchi wote bila ubaguzi na ndiyo maana tunasema hii ni benki pekee kwa wote. Benki ya Wanawake kwa Mkoa wa Dodoma ilianza kutoa huduma zake Disemba, 2012 ikiwa na vituo vinne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Septemba, 2016 benki kwa Mkoa wa Dodoma ilikuwa jumla ya vituo 18. Walionufaika na mikopo katika Benki ya Wanawake katika Mkoa wa Dodoma ni watu 19,740 kwa kipindi cha kuanzia Disemba, 2012 hadi Septemba, 2016; mikopo hii ina thamani ya shilingi 6,231,891,236. Kati ya hao wanawake waliopata mikopo hiyo ni 16,676 yenye thamani ya shilingi 5,063,765,641 sawa na asilimia 81 ya mikopo yote na wanaume wakiwa 3,064 ambao wamepata mikopo yenye thamani ya shilingi 1,168,125,595 sawa na asilimia 19.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Serikali imeanzisha Benki ya Kilimo kwa lengo la kusaidia wakulima wakubwa na wadogo kupata mikopo ya pembejeo kwa haraka:-
Je, ni lini Benki hiyo itaanza kutoa huduma kwa wakulima wadogo wadogo wa Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilianza rasmi shughuli zake mwishoni mwa mwaka 2015. Hadi kufikia Desemba 2016, Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilikuwa imeshatoa mikopo ya jumla ya Sh. 6,489,521,120/= kwa miradi 20 ya kilimo katika Mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga. Sambamba na utoaji wa mikopo, benki inatoa mafunzo kwa wakulima na hadi sasa imeshafanya mafunzo kwa vikundi 336 vya wakulima wadogo wadogo vyenye jumla ya wanachama 44,400 katika Mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Dodoma, Benki imepata nafasi kwa ajili ya kufungua ofisi katika jengo jipya la PSPF ambapo inasubiri kukabidhiwa ofisi hiyo Julai, 2017, baada ya mkandarasi kukamilisha ujenzi. Aidha, benki imeshaanza kutafuta miradi ya kilimo ya wakulima wadogo wadogo yenye sifa za kukopesheka iliyopo katika Mkoa wa Dodoma na mikoa mingine ya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufanikisha azma hii, benki imemwandikia barua Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma kumwomba aipatie miradi mizuri ya kilimo ambayo mkoa unapendekeza Benki iifikirie katika zoezi la kutoa mikopo. Pamoja na hayo, benki inaandaa utaratibu wa mafunzo yatakayotolewa kwa wakulima wadogo wadogo nchi nzima ikianzia na Mkoa wa Dodoma. Ni matumaini ya benki kuwa mikopo kwa wakulima wadogo wadogo na wakati kwenye Mkoa wa Dodoma itaanza kutolewa mwishoni mwa mwaka 2017.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 aliyekuwa mgombea Urais kupitia tiketi ya CCM Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliwaahidi wananchi wa Kongwa na Mpwapwa kujenga barabara ya Mbande – Kongwa - Mpwapwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mbande – Kongwa – Mpwapwa yenye urefu wa kilometa 49.19 ilifanyiwa usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami na usanifu ulikamilika mwaka 2013. Baada ya kukamilika kwa usanifu Serikali imeanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu ambapo mwezi Julai, 2017 sehemu ya barabara yenye urefu wa kilometa 11.7 kutoka Mbande kuelekea Kongwa ilianza kujengwa. Hadi mwishoni wa mwezi Oktoba, 2017 kiasi cha kilometa tano za sehemu ya barabara ya Mbande - Kongwa zimekamilika kujenga hadi tabaka la juu (basic course). Mkandarasi anaendelea na kazi ya ujenzi kwa kiwango cha lami.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Mkandarasi anayejenga Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino anaidai Serikali shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kukamilisha jengo la Halmashauri.
Je, ni lini Serikali itamlipa mkandarasi huyo kiasi hicho cha fedha ili ujenzi huo uweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Dodoma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, madai ya Mkandarasi aliyejenga Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, mpaka sasa ni shilingi milioni 758.2 yakiwemo madai yaliyohakikiwa ya shilingi milioni 368.0 na madai ambayo hayajahakikiwa ya shilingi milioni 390.2 ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri hiyo imepokea shilingi milioni 700 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi. Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/ 2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zinapaswa zitumike kulipa deni ambalo Mkandarasi anadai kabla ya kuendelea na kazi nyingine. Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka ili kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo la Halmashauri unakamilika.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha mradi wa maji wa maporomoko ya Ntomoko Wilayani Kondoa?
NAIBU WA WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Ntomoko ulilenga kutoa huduma katika vijiji 18 vya Wilaya ya Kondoa na Chemba lakini kutokana na uwezo mdogo wa chanzo kumesababisha kutokidhi mahitaji ya huduma ya maji katika vijiji hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo mwezi Novemba 2017 Wiraza kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI iliunda timu ya pamoja ya Wataalam kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu wa kina wa mradi huo pamoja na kutafuta chanzo kingine mbadala ili kuongeza wingi wa maji utakaokidhi mahitaji ya wananchi katika vijiji hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mapitio ya usanifu wa kina timu hiyo ilibaini kuwa chanzo cha Ntomoko hakina tena uwezo wa kuhudumia vijiji hivyo. Ili kukidhi mahitaji ya maji kwa vijiji hivyo, Serikali imepanga kukarabati miundombinu iliyoko pamoja na kujenga bwawa lenye mita za ujazo milioni 2.8 kwenye eneo la Kisangali katika kijiji cha Mwisanga litakalotoa huduma kwa vijiji vyote 18. Usanifu wa bwawa hilo pamoja na bomba kuu kutoka kwenye chanzo hadi makutano ya kijiji cha Lusangi umeshafanyika. Ujenzi huo unatarajiwa kuanza katika bajeti ya mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto zilizojitokea awali juu ya ukarabati wa miundombinu ya mradi huo, Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DUWASA) kutekeleza ukarabati wa mradi huo badala ya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Hepatitis ni ugonjwa hatari usiofahamika vizuri kwa wananchi walio wengi:-
(a) Je, dalili za ugonjwa huo ni nini;
(b) Je, ugonjwa huo una chanjo.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maambukizi ya Homa ya Ini husababishwa na virusi ambavyo vinapoingia mwilini mwa binadamu hushambulia ini pekee na hivyo kulifanya kushindwa kufanya kazi vizuri. Katika hatua za mwisho mwathirika wa ugonjwa huu anaweza kupata saratani ya ini. Virusi vya homa ya ini vipo katika makundi matano, yaani (A), (B), (C), (D) na (E).
Mheshimiwa Naibu Spika, dalili za homa ya ini ni pamoja na ngozi na macho kuwa na rangi ya njano, kukojoa mkojo wenye rangi nyeusi, joto la mwili kupanda, kuwa na mafua, kichwa kuuma, kukosa nguvu, kupata kichefuchefu, kutapika, tumbo kuuma upande wa juu kulia na kupungua uzito.
Mheshimiwa Spika, maambukizi ya homa ya ini yanategemeana na kundi la Virusi. Kundi la B, C na D huambukizwa kwa niia ya kuongezewa damu yenye virusi vya ugonjwa huo, kujamiiana, utumiaji usio salama wa sindano na vitu vingine vyenye ncha kali, utumiaji wa dawa za kulevya kwa kujidunga sindano yenye virusi vya ugonjwa huo, majimaji ya mgonjwa kumpata mtu mwingine ambaye ana kidonda, pia mama anaweza kumwambukiza mtoto wake wakati wa kujifungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, aina ya homa ya aina ya ini inayosababishwa na virusi vya kundi (B) Hepatitis B (HBV) ndiyo inayoongoza kwa maambukizi nchini. Aina ya Kirusi cha A na E huambukizwa kwa njia ya kinyesi na kutokuwa na majisafi na salama (faecal oral) ambazo hufanana kwa kiasi kikubwa na uambukizwaji wa magonjwa ya kuhara.
Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa Hepatitis B unaweza kukingwa kwa kutumia chanjo na chanjo hii hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ya virusi hivyo na hutoa kinga kwa kipindi chote cha maisha yake. Hapa nchini chanjo hii inapatikana kwa watu wazima na watoto wachanga. Kwa watoto wachanga, chanjo hii ipo katika mchanganyiko wa chanjo ya pentavalent ambayo watoto wachanga hupatiwa, katika mwaka 2017, asilimia 98 ya watoto walipata chanjo hii. Kwa wenye maambukizi ya virusi aina (C), kwa sasa hakuna chanjo. (Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Wananchi wa Kanda ya Kati ni wakulima wazuri wa zao la alizeti:-
Je, Serikali haioni ni muda muafaka sasa wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko kuanzisha Mfuko mahsusi wa uendelezaji wa zao la alizeti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na jitihada mahsusi za kuendeleza zao la alizeti ambazo ni pamoja na kuwa na Mfuko wa kuendeleza zao hilo. Kutokana na umuhimu huo, Serikali kwa kushirikiana na wadau, imeandaa Mkakati wa Kuendeleza zao la Alizeti nchini (Sunflower Development Strategy 2016 – 2020) ambapo unalenga kuongeza uzalishaji na tija; kuboresha ubora wa mbegu za alizeti; kuimarisha tasnia ya alizeti kwa kuboresha uratibu miongoni mwa wadau; kuchochea ukuaji wa tasnia ya alizeti kwa kuweka sera wezeshi; na kuhakikisha uwepo wa masoko ya uhakika kwa mazao ya alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ilianzishwa ili kufanya biashara na pia kushirikiana na wadau wengine katika kuendeleza mazao mchanganyiko. Hivyo, Bodi hiyo haiwezi kuanzisha Mfuko wa kuendeleza zao la alizeti peke yake bali kwa kushirikiana na wadau wengine wa zao la alizeti. Aidha, pale itakapokubalika, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko itakuwa ni miongoni mwa wadau muhimu wa kuanzisha Mfuko huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitatu (3) mfululizo wadau wa alizeti wamekuwa wakikutana kujadili changamoto mbalimbali ya zao hilo na kuzitafutia ufumbuzi. Katika kurasimisha jitihada hizo na kuwa na Jukwaa la Wadau, Wizara iliitisha kikao cha wadau kwa ajili ya kujadili namna bora ya kuendeleza zao la alizeti hususan katika upatikanaji wa mbegu bora, huduma za ugani na teknolojia bora za usindikaji wa alizeti. Aidha, katika ushirikishwaji huo wa wadau, suala la Mfuko wa Kuendeleza zao la Alizeti litajadiliwa kwa kina na kama inaonekana ni muda muafaka wa kuanzisha Mfuko huo, wadau watakubaliana kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uanzishwaji wa mifuko zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wizara tayari zipo jitihada za kuimarisha utafiti wa mazao ya mbegu za mafuta ambapo kwa zao la alizeti Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI imejipanga kuendeleza kusafisha mbegu za awali aina ya “Record” kwa ajili ya kuzalisha madaraja ya msingi na hatimaye daraja la kuthibitishwa. Kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa mbegu bora za alizeti kupitia Wakala wa Mbegu wa Taifa (Agricultural Seed Agency-ASA) na kuhamasisha makampuni binafsi ya kuzalisha mbegu bora za alizeti.
Aidha, katika jitihada hizo, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko inashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Muungano wa Wazalishaji wa Zao la Alizeti Tanzania (Tanzania Sunflower Processors Association – TASUPA) na Mfuko wa Kuendeleza Masoko ya Mazao ya Kilimo (Agricultural Market Development Trust-AMDT) katika kuhakikisha wakulima wa alizeti wanapata mbegu bora na huduma za kilimo bora cha alizeti.
MHE. FELISTER A. BURA aliuza:-

Kituo cha Polisi Chipanga kilijengwa kwa nguvu za wananchi takribani miaka 18 iliyopita:-

Je, ni lini kituo hicho kitafunguliwa na kutoa huduma kwa wananchi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Polisi Chipanga kilichopo Wilaya ya Bahi Mkoa wa Dodoma kilijengwa muda mrefu kwa nguvu za wananchi wa eneo hilo, lakini baadaye jengo hilo lilipangiwa matumizi mengine ya makazi ya Walimu hadi ilipofika mwezi Februari, 2017. Baada ya jengo hili kutumika kama makazi kwa muda mrefu, maeneo mengi yanahitaji marekebisho ili kuweza kukidhi mahitaji ya kutumika kama Kituo cha Polisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini ya maeneo yanayohitajika kufanyiwa ukarabati ni milango, madirisha kuvuja na nyufa katika paa, vyoo, vyumba viwili vya ofisi, chumba cha mahabusu na chumba cha kuweka silaha kwani kwa sasa kilivyo hakiwezi kutumika na kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi maeneo mbalimbali nchini wana mwamko wa kujenga Vituo vya Polisi ambayo kwa namna moja au nyingine Serikali imekuwa ikivimalizia na kwa kuwa mahitaji ya kufanya ukarabati wa vituo nchini ni makubwa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali kupitia Jeshi la Polisi, itaendelea kufanya juhudi mbalimbali ili kuweza kukimalizia kituo hicho na kianze kutoa huduma kwa wananchi wa Chipanga.
MHE. FELSTER A. BURA aliuliza:-

Mkoa wa Dodoma una upungufu wa Walimu 527wa Sayansi:-

Je, ni lini Serikali italeta Walimu wa kutosha wa sayansi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa Mkoa wa Dodoma una shule 221 za sekondari zikiwa na wanafunzi 72,254. Mahitaji ya Walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati ni Walimu 1,641 na Walimu waliopo ni 916, hivyo pungufu ni Walimu 527 sawa na asilimia 32 ya mahitaji halisi.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kuajiri Walimu wa masomo hayo kwa awamu na kwa sasa kibali cha kuajiri Walimu 4,549 kimetolewa ambapo kati ya hao Walimu 1,374 ni wa masomo ya Sayansi na Hisabati. Taratibu za kuajiri Walimu hao zinakamilishwa ili kuwapanga Walimu hao katika Halmashauri zenye upungufu ikiwepo Halmashauri za Mkoa wa Dodoma. Ahsante.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-

Kutokana na Serikali kuhamia Dodoma, mahitaji ya maji safi na salama yamekuwa makubwa na kwa sasa mgao wa maji kwa wakazi wa Dodoma umeshaanza:-

Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuhakikisha wakazi wa Dodoma wanapata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, chanzo kikubwa cha uzalishaji maji kwa matumizi ya wakazi wa Jiji la Dodoma ni visima virefu vilivyochimbwa katika Bonde la Makutopora eneo la Mzakwe. Kuna jumla ya visima vya uzalishaji maji 24 na visima vitano vya kuchunguza mwenendo wa maji ardhini (observation boreholes) vimechimbwa katika bonde hilo. Uwezo wa visima vilivyopo Mzakwe kwa sasa pamoja na uwezo wa usafirishaji wa maji ni mita za ujazo 61,500 kwa siku.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha huduma ya maji inakuwa ya uhakika, Serikali kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Jijini Dodoma, imeongeza chanzo kingine cha maji eneo la Ihumwa chenye uwezo wa kuzalisha maji mita za ujazo 2,773 kwa siku. Chanzo hiki kina visima nane na kinahudumia Mji wa Serikali uliopo Mtumba pamoja na Kijiji cha Ihumwa.

Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuboresha huduma ya maji, kwa mpango wa muda mfupi Serikali inaendelea na utafiti wa maji chini ya ardhi na uchimbaji wa visima virefu katika Mitaa ya Ntyuka, Michese na Nala na uendeshaji wa visima nane katika Mji wa Chamwino. Mpango wa muda wa kati wa ujenzi wa Bwawa la Maji la Farkwa litakalotumika kama chanzo cha nyongeza cha majisafi katika Jiji la Dodoma.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-

Ranchi za Taifa ni rasilimali muhimu na fursa kubwa katika kuchangia Pato la Taifa na Uchumi wa nchi yetu:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza thamani ya mazao ya mifugo iliyopo kwenye ranchi zetu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni ya ranchi za Taifa (NARCO) imeandaa Mpango Mkakati wa Kibiashara wa miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 – 2021 – 2022 kwa lengo la kuendeleza na kueneza ufugaji bora hususan ufugaji wa ng’ombe bora wa nyama (boran) kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi kwa kutumia mbinu za kisasa. Maeneo ya kipaumbele katika mpango mkakati huo ni pamoja na kuiwezesha NARCO kuingia ubia na makampuni mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, NARCO imeingia ubia na kampuni ya NICAI ya Misri kwa ajili ya kujenga machinjio ya kisasa na kiwanda cha kuchakata mazao mbalimbali ya mifugo. Aidha, NARCO imeomba fedha kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa la Kilimo na Chakula (IFAD) kiasi cha shilingi bilioni 20 ambapo andiko la mradi (concept note) kwa ajili ya kuendeleza ranchi nane za NARCO limepitishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuongeza idadi ya mifugo ikiwemo ng’ombe wazazi kufikia 20,000 katika kipindi cha miaka mitano ili kuwa na uzalishaji endelevu wa kibiashara. Kuanzisha utaratibu wa kukodisha vitalu ambapo wafugaji wanaomilikishwa vitalu lazima kupatiwa mafunzo ya ufugaji wa kisasa ikiwemo unenepeshaji wa mifugo ili kuongeza uhakika wa upatikanaji wa malighafi za viwandani kama vile nyama, maziwa na ngozi. Ranchi za NARCO zote zitajenga madarasa maalum kwa ajili ya mafunzo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na juhusi za kufanya maboresho makubwa ya NARCO ili kuongeza uwezo wa mtaji, ufanisi na tija hasa kufikia lengo la kuchakata mazao ya mifugo yetu nchini na kufikia masoko ya ndani na ya kikanda.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-

Mkoa wa Dodoma una mahitaji ya walimu 11,676 kwa uwiano wa 1:40 kwa shule za msingi. Kwa sasa walimu waliopo ni 7,382 na hivyo kuwa na upungufu wa walimu 4,410 sawa na asilimia 38.

Je, ni lini Serikali itaajiri mwalimu wa kutosha Mkoani Dodoma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA W. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI,naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Bura, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiajiri na kuwapanga walimu kwenye Halmashauri kwa awamu. Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019 Serikali imeajiri walimu 14,422 ambapo 10,695 ni walimu wa shule za msingi na 3,727 ni walimu wa shule za sekondari. Mkoa wa Dodoma umepatiwa walimu 699 wa shule za msingi kati ya walimu 10,695 walioajiriwa wa shule za msingi. Serikali itaendelea kuajiri walimu kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-

Serikali ilipata ufadhili wa kujengewa uwanja wa michezo Mkoani Dodoma kutoka Serikali ya Morocco.

Je, ni lini uwanja huu wa Michezo utaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mfalme Mohamed VI alipofanya ziara yake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Oktoba, 2016 alitoa ahadi ya kufadhili miradi mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa msikiti mkubwa na ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo nchini. Baadhi ya ahadi kama ujenzi wa msikiti zimeshakamilika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa uwanja wa michezo wa kisasa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua uwanja huo ujengwe katika Jiji la Dodoma eneo la Nane Nane. Maandalizi yote ya msingi ikiwa ni pamoja na kutenga eneo lenye jumla ya ekari 328.6, kupima eneo lote la mradi, kufanya tathmini ya mazingira na kijamii (Environmental and So cial Impact Assessment), topographical survey, geotechnical survey na kuandaa mchoro wa awali wa uwanja tarajiwa yamefanywa.

Mheshimiwa Spika, kimsingi maandalizi ya awali ambayo yalipaswa kufanywa na Serikali ya Tanzania yamekamilika kwa kiasi kilichokusudiwa. Aidha, mawasiliano baina ya Serikali mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Morocco kuhusu kukamilisha mradi huu yanaendelea.