Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ruth Hiyob Mollel (37 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia mada iliyoko mezani hapo na nimshukuru Mungu kuweza kuwepo mjengoni mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiiti, nimepitia review ya mwaka 2014/2015, vilevile ya mwaka huu wa sasa ambao tunauzungumzia. Kimsingi, tumekuwa na malengo mengi ambayo hayapimiki na nina maana gani ninaposema hayapimiki? Unakuta kwa mfano, mapitio ya mwaka jana tumesema tuta-train walimu 460, lakini hatuambiwi katika ule mwaka ni wangapi wamekuwa trained. Kwa hiyo, tunashindwa kujua sasa, hawa waliokuwa trained ni wangapi na mmeshindwa wapi kwa wale ambao hatukufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hata ukipitia huu Mpango wa sasa hivi ambao Mheshimiwa Waziri ameuleta, bado tatizo liko pale pale, anazungumzia kusomesha vijana wengi kwa mkupuo katika fani mbalimbali, lakini hasemi anafundisha vijana wangapi, wa fani zipi na kwa mchanganuo upi. Kwa hiyo, napendekeza kwamba katika Mpango utakaoletwa yale malengo yawe bayana, yaweze kupimika kusudi tuweze kuisimamia Serikali kwa jinsi ambavyo inatenda kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mpango umezungumzia suala la viwanda, tunataka Tanzania iwe nchi ya uchumi wa viwanda, lakini suala la rasilimali watu halijajitokeza bayana. Kwa sababu kama ni viwanda tutahitaji fani mbalimbali za kuweza kusukuma hili gurudumu la viwanda, lakini Serikali haijaleta mchanganuo wa fani zipi ambazo tutazihitaji kwa ajili ya huu uchumi wa viwanda.
Kwa hiyo, ni ushauri wangu Serikali ikachambue, ikaangalie kwa miaka kumi ijayo tunahitaji human capital gani, katika maeneo gani kusudi kila mwaka mpango wa mwaka unapoletwa hapa muweze kuainisha kwamba, mwaka huu Serikali itafanya hiki, mwaka wa kesho Serikali itafanya hiki, kusudi Bunge liweze kufuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Mpango huu ambao Mheshimiwa Waziri ameuwasilisha, kwa maoni yangu mimi kama Mbunge wa Chadema, vipaumbele ni vingi, wala havitatekelezeka. Kwa mfano, katika ukurasa wa 25, Ardhi na Makazi. Tumesema upimaji na utoaji hati miliki, naomba muangalie hivyo vipaumbele vya Ardhi, Nyumba na Makazi; hivi kwa mwaka huu hatuwezi kuvifanya, haviwezi kufanyika wala havipimiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tunataka Serikali ije na mchanganuo. Kwa mfano, anasema watapima majiji na vijiji na miji mikubwa. Sasa Serikali ituambie katika majiji, miji na vijiji ni vingapi? Ni mji mmoja, ni miji miwili, ni vijiji kumi kusudi itakapokuja taarifa ya utekelezaji tujue kama kazi hiyo imefanyika au haijafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia kuhusu rasilimali watu. Kama kweli tunataka kupata rasilimali watu ambayo itasaidia, Serikali katika kujenga uchumi huu, basi rasilimali watu hii iangaliwe tangu mwanzo. Waziri wa Elimu aangalie laboratories ngapi zinajengwa kwenye mashule, maana ndiko tunakochimbua wataalam ambao baadaye watakuja kusukuma huu uchumi wa kati ambao tunauzungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye suala la kilimo. Serikali imesema kilimo ni uti wa mgongo, ni kweli, lakini je, Serikali inafanya nini kweli kusimamia kilimo? Kwa sababu lazima tukubali, kilimo nchi hii bado ni subsistence farming. Kwa hiyo, wakulima wanatakiwa kuangaliwa kwa jicho la karibu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Serikali haijazungumzia kuhusu Extension Officers. Extension Officers wanahitajika wengi na ingependeza kama Serikali ingekuja kuangalia ratio ya Extension Officer na wakulima, kama tunavyofanya ratio ya madaktari na wagonjwa, nesi na wagonjwa, kwa hiyo na Extension Officers ifanywe hivyo hivyo, kusudi muweze kufanikiwa katika kuinua kilimo ambacho pia kinatoa ajira kwa watu wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa ushauri kwa Serikali; Wizara ya Kilimo, SUA na Vyuo vya Kilimo na mkulima wafanye kazi kwa pamoja (tripartite). Watu wa ugani wawezeshwe kwa vifaa, wawezeshwe kwa pikipiki, waweze kwenda kutembelea wakulima na wawe na mafaili kama ya wagonjwa hospitali. Nchi nyingine ndivyo wanavyofanya, unakuta Afisa Ugani anawajua wakulima wake kwa jina na ana file analokwenda kuangalia wakulima wake na kujua matatizo yao. Naishauri Serikali ichukue mapendekezo hayo ili iweze kwenda kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la viwanda tunavyo viwanda vingi na vingi vimekufaa. Serikali inahitajika kuangalia viwanda katika maeneo mbalimbali, kwa mfano, Tanga kuna matunda mengi sana, kiwepo kiwanda pale Tanga cha ku-process matunda. Mahali kama Shinyanga kuna nyama nyingi, ng‟ombe wengi sana, kuna pamba nyingi sana, viwepo viwanda vya ku-process vitu hivi ili itoe ajira na kukuza uchumi wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimshukuru Mungu kwanza kwa kuweza kusimama hapa na nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia kwenye hoja hii iliyopo hapa mezani.
Mheshimiwa Spika, naungana na Wabunge wote ambao wameshazungumza kuhusu afya, kwamba afya kwa kweli, ni msingi mkubwa sana wa uchumi. Taifa lenye afya ndiyo linaweza kujenga uchumi wa nchi hii. Kwa hiyo, nasema Mawaziri mna kazi kubwa sana ya kuona kwamba, Taifa hili linakuwa na afya njema.
Mheshimiwa Spika, ningependa kuzungumzia suala la mfumo wa afya. Mfumo wa afya umekaa vizuri kwa sababu tunaanza zahanati, tunakuja kituo cha afya, tunakuja mkoa na kadhalika. Mfumo umekaa vizuri sana kama tutautumia kwa ajili ya kuboresha afya ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, niseme kwamba, tukiangalia katika Hospitali ya Muhimbili kwa mfano, imejaa wagonjwa sana na huu mrundikano wa wagonjwa unatokana na kwamba hizi peripheral hospitals hazijawa na vifaa vya kutosha ambapo wagonjwa watatibiwa kule, kupunguza huu msongamano ulioko Muhimbili. Huu msongamano hautakwisha mpaka hizi peripheral hospitals Mwananyamala, Temeke, najua zimepanuliwa, lakini bado hazikidhi kuweza kupunguza msongamano ambao uko pale Muhimbili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri kwamba, Hospitali hizi za peripheral health centres, kuna hizi Hospitali za Rufaa ambazo zimeteuliwa za Mikoa zingepewa vifaa tiba vya kisasa kama CT Scan kusudi ianze kuchuja wagonjwa tangu pale mwanzo halafu Muhimbili waje wale ambao kwa kweli wanahitaji specialized treatment.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunapendekeza tuwe na CT Scan katika hizi referral hospitals, tuwe na CT Scans pia katika Hospitali za Mbeya najua pengine ipo, Bugando na KCMC kusudi hii influx kubwa inayokuja Muhimbili ipungue. Hata influx pia katika hizi Hospitali nyingine za Bugando, KCMC na Mbeya bado nao wanakuwa na wagonjwa wengi, lakini kama hizi referral hospitals za mkoa tulizoziteuwa zikifanya kazi, basi tutapunguza msongamano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nina mawazo kwamba hizi hospitali nyingine za Super Specialisation za Bugando, KCMC, Mbeya na Muhimbili na zenyewe zipewe vifaa tiba vya kisasa. Kwa mfano, tukiwa na vifaa tiba vya kisasa kabisa huu utaratibu wa kupeleka wagonjwa wengi nje utapungua.
Kwanza wagonjwa wengi watatibiwa hapa nchini na kwa yale maeneo ambayo hatuna uwezo nayo, kama kuna eneo ambalo hatuna specialization, tunaweza kuleta madaktari kutoka nje wakaja hapa kwa bei nafuu, wakatibu wagongwa wengi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kutibu wagonjwa wengi vile vile tunajenga uwezo wa wataalam wetu ndani ya nchi, kama tunavyofanya katika Kitengo cha Moyo, hii system ingeendelea pia kwenye maeneo ya magonjwa mengine ambayo tunapeleka wagonjwa nje.
Kwa hiyo, ni maoni yangu na maoni ya Kambi ya Upinzani kwamba, tuzi-strengthern tupunguze wagonjwa kupelekwa nje na wagonjwa wengi zaidi waweze kutibiwa ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri na kuna eneo ambalo hajaligusia sana, amezungumzia kuhusu watoto na changamoto za watoto, lakini kuna hawa watoto ambao wako katika mazingira magumu, ukipita mitaani Dar es Salaam utakuta watoto wengi wanaombaomba, wanatumiwa kuomba.
Mheshimiwa Spika, sasa ningependa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja aweze ku-share na sisi kuona ni hatua gani Wizara itachukua? Najua itahusisha labda na Wizara ya Elimu kwa sababu watoto wale wana haki ya kupata elimu, ni kwa jinsi gani mkakati utakaoletwa ili kuona jinsi gani hawa watoto wanasaidiwa kuondoka katika haya mazingira ambayo yanasababisha kukosa haki yao ya elimu na haki ya kutokunyanyaswa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna eneo moja pia ambalo wengine wameligusia, eneo la magonjwa ya akili. Nimeshakuwa na mgonjwa pale Muhimbili kwa kweli hali ya pale ile Faculty ya Psychiatric ni mbaya sana. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana uweze kwenda pale mahali. Pale wagonjwa wanafungiwa kama wako jela! Wanafungiwa, hawatoki na hawapati hata nafasi ya kupatiwa counseling kwa sababu yale maeneo hayawezekani.
Mheshimiwa Spika, najua kwamba kuna kazi ambayo tayari kile kitengo kimeshafanya, wameshafanya sketch ya kujenga kituo cha kisasa lakini hawana architectural drawings kwa sababu hawana fedha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, naomba uende pale uone na tutafute namna, hata kama kutafuta joint venture, kama inawezekana au donors whatever, lakini waweze kujenga kituo cha kisasa kwa sababu sasa hivi magonjwa ya akili yamezidi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, magonjwa ya akili yamezidi sana kwa sababu ya ulevi wa kupindukia, msongo wa mawazo, umaskini na madawa ya kulenya. Kwa hiyo, hawa wagonjwa wanaongezeka kwa wingi sana na kile kitengo hakiwezi kuhimili. Kwa hiyo, ni rai yangu kwako uende ukatembelee pale hali ni mbaya sana. Naomba uende pale uweze kuona hali halisi na uonane na hawa wataalam wa pale ambao tayari wana sketch na wameshakisia ni kiasi gani cha fedha kitahitajika kujenga kituo cha kisasa cha magonjwa ya akili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wengi wamezungumzia kuhusu suala la tiba ya wazee. Tunasema kwamba tiba ya wazee ni bure, lakini ukweli ni kwamba sio bure kiasi hicho. Bure ni kumwona Daktari tu lakini ikija kwenye suala zima la matibabu ambapo ndiyo msingi uliompeleka yule mzee hospitali kwa kweli inakuwa ni matatizo makubwa sana. Kwa hiyo, napendekeza kwamba tutafute namna ambayo tunaweza tukachangia zaidi hata kwenye NHIF ili zipatikane pesa ambazo tutawawezesha hawa wazee kupata hizi kadi za NHIF waende wakatibiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi pia ni mzee lakini advantage niliyonayo ni kwamba nina kadi ya NHIF lakini wapo ambao hawana advantage ya NHIF anakwenda pale hawezi kutibiwa. Huyu mtu ujana wake wote kaumalizia katika kujenga nchi hii, lakini wakati sasa ana uhitaji mkubwa hawezi kusaidiwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, kwa kweli hili jambo la wazee naomba mliangalie kwa jicho la huruma kabisa, tuone ni jinsi gani wazee wetu wanaweza kupata tiba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wamezungumzia kuhusu zahanati, vituo vya afya na hospitali za mikoa, kweli ziko chini ya TAMISEMI. Lazima tukubali kwamba pia anayesimamia na kutoa standards na kuona zahanati inatakiwa itibu nini, vituo vya afya vitibu nini, hospitali za mkoa ziwe na vifaa gani ni Wizara ya Afya. Kwa hiyo, napendekeza katika hospitali za mkoa, Wizara ya Afya iwe na wakaguzi ambao kazi yao itakuwa kwenda kutembelea hivi vituo vya afya na zahanati kuona kwamba zile tiba zinazotakiwa kutolewa pale zinatolewa.
Mheshimiwa Spika, udhibiti huu pia utasaidia kupunguza msongamano kwenye hospitali za wilaya na mkoa. Kwa hiyo, ni mawazo yangu kwamba tuwe na wakaguzi ambao watakuwa ni waajiriwa wa Wizara ya Afya ambao wataweza kwenda kusimamia afya kwa sababu usimamizi wa afya ni wa Wizara na hakuna mtu wa kumtupia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba ufanye hivyo kama fedha zitaruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante! Napenda ku-declare interest kwamba, nilishafanya kazi katika ofisi inayohusika na mazingira na najaribu kuangalia uhusiano wa uchimbaji wa madini na mazingira. (Makofi)
Natambua kwamba uchimbaji wa madini au madini yenyewe unajenga uchumi wa nchi yetu na una faida kubwa katika nchi yetu, hilo halina ubishi. Hata hivyo, ni ukweli pia kwamba uchimbaji madini unaharibu mazingira kama usipodhibitiwa na kusimamiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo migodi mikubwa na najua kwamba kabla hawajapata leseni lazima huwa inafanywa tathmini ya athari kwa mazingira ambayo tunaita Environment Impact Assessment (EIA) - tathmini ya athali kwa mazingira na baada ya hapo leseni zinatolewa, baada ya kutoa ile EIA inakuwa kwamba tunasahau kabisa kwamba kuna jambo sasa la kufuatilia kwa karibu ile migodi mikubwa inavyofanya shughuli zake na kuweza kuona jinsi gani wanavyoharibu mazingira kwa namna ya maji yenye sumu, namna ya afya ya wale wafanyakazi na mara nyingi tunakuwa reactive jambo limeshatokea ndiyo tunakwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba leseni zinapotolewa pamoja na kwamba EIA inafanywa na Wizara nyingine, lakini kunakuwa hakuna uhusiano wa karibu sana na sector Ministry. Mapendekezo yangu ni kwamba EIA inavyotolewa na certificate inapotolewa, hizi Wizara ziweze kuzungumza ili kusudi hata wakati wa kwenda kufanya ukaguzi tupate wale wadau wakubwa wote ambao wanahusika na migodi na wale wanaohusika na mambo ya mazingira pamoja na Wilaya zile zenye madini yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia Wabunge wengi wakichangia wanasema kwamba, watu wanapata leseni wanakwenda kwenye maeneo yao wao wenyewe wenye Wilaya zao hawana habari. Ina maana kwamba, Serikali inafanya kazi mkono mmoja haujui mfuko mwingine unafanya kitu gani! Kwa hiyo, tunahitaji tuwe na timu ambayo anayetoa leseni, anayefanya EIA na yule mwenye eneo lake ambalo migodi ipo wote wafahamu ni kitu gani kinachoendelea katika lile eneo kwa ajili ya kudhibiti na kuhakikisha mazingira yanakuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika speech ya Mheshimiwa Waziri kwamba kuna maeneo mwaka jana 2015/2016 walitenga heka 7,731 kwa ajili ya wachimbaji wadogo na mwaka 2016/2017 wametenga hekta 12, 000 ni jambo jema. Nashauri kwamba, wachimbaji wadogo nao pia wanaharibu mazingira sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepita Mererani, nilishapita wakati mwingine sehemu za kule kwenye diamond - Mwadui, wanachimba wanaacha mashimo, ile ardhi inakuwa tupu hakuna miti ni mashimo! Kwa hiyo, kuna umuhimu mkubwa sana kwa ajili ya kudhibiti na kuangalia kwamba mazingira yanarejeshwa katika hali yake ya asili. Najua wachimbaji wadogo wadogo wanakuwa na Environment Management Plans, lakini nani anawasimamia? Hakuna mtu anayewasimamia, wanachimba wanaacha!
Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza kwamba Wizara inayohusika ya Nishati na Madini, Wizara inayohusika na Mazingira na yale maeneo ambayo ile migodi inachimbwa, ile midogo midogo, watafute jinsi ya kuya-incentivised wale wachimbaji wadogo kusudi wahakikishe kwamba lile eneo lililochimbwa na kuharibiwa linarudishwa katika hali yake ya asili ya miti na majani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia pia katika taarifa ya Audit ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu alivyozungumzia kuhusu petroleum exploration na pia nimeona kwamba Ofisi ya Rais Mazingira wamefanya inspection tatu tu katika miradi karibu 71 na inaelekea kwamba hakuna uwezo mkubwa sana. Hili ni eneo pia ambalo ningependa Mheshimiwa Waziri alizungumzie ni jinsi gani inspections ya haya maeneo itaimarishwa ili kuhakikisha kwamba tunachunga mazingira yetu. Napendekeza pia hizi teams ziendelee kufanya kazi kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la umeme, najua kwamba mimi mwenyewe nilishavuta umeme nikaweka nguzo kama mbili, tatu na tunalipia gharama kubwa na naamini kuna wengi pia wanafanya hivyo na hizo nguzo baadaye ni za TANESCO pamoja na kwamba ni sisi ndiyo tumezilipia pamoja na LUKU tumezilipia.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda Mheshimiwa Waziri anapomalizia hoja yake atuambie ni kwa jinsi gani watu ambao wameweka hizo nguzo za umeme kwa gharama zao na hizo nguzo ni za TANESCO ni kwa namna gani wanaweza ku- compensate? Je, inawezekana ku- compensate kwa kupitia bill za umeme kwamba wewe umeweka nguzo tatu, bei ni kadhaa na kwamba labda bill ya umeme uwe unalipa kiasi fulani na ufidie kwa ile miti ya TANESCO ambayo umeweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitashukuru Mheshimiwa Waziri akitujibu hilo suala tuweze kujua ni jinsi gani TANESCO wanaweza kutu-compensate.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengi sana wamezungumzia suala la Nyamongo na mimi nasikitishwa kwamba, nilikuwemo suala la Nyamongo lilikuwepo, nimetoka sasa sijui karibu miaka mingapi suala la Nyamongo bado linaendelea. Mheshimiwa Waziri, hii Nyamongo ina shida gani, kwa nini hii issue haiishi? Maana yake imekuwa ya muda mrefu sana na miaka mingi, pengine labda kuna kitu Waheshimiwa Wabunge hatujui, labda kuna tatizo fulani, tunaomba Mheshimiwa Waziri anapomaliza hoja yake, atueleze kuna shida gani na hili suala la Nyamongo ambalo tumelizungumza miaka nenda miaka rudi!
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ambayo nimepewa kuweza kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niunge mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani ambayo ilitolewa kabla. Katika mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano ni Tanzania ya viwanda, nimepitia katika Mpango huo ambao umewasilishwa na nasikitika kusema kwamba, katika Mpango wote ambao umewasilishwa pamoja na umuhimu wa kukuza viwanda, sijaona ni kwa namna gani rasilimali watu imepangwa kusudi kusaidia kuendesha viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu mwaka jana katika ule Mpango kulikuwa na suala la kupeleka wanafunzi 159 wa petroleum and gas kwenda kusoma, lakini sioni katika mpango wa mwaka huu ni kwa jinsi gani tumefikia wapi na wale 159 kwamba wanatosha au tunahitaji ku-train watumishi wengine kwa ajili ya petroleum and gas.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mwaka jana Serikali iliahidi kwamba itajenga vyuo vinne vya ufundi katika mikoa mbalimbali lakini katika mpango wa mwaka huu Serikali haijaainisha kama bado tunaendelea na hivyo vyuo vinne vya ufundi, imekuja na mawazo mapya ya kutengeneza karakana, sijui miundombinu. Je, vile vyuo vinne ambavyo Serikali iliahidi itavijenga, imefikia wapi? Ingependeza zaidi kama tungeweza tukapata status ya yale ambayo yalisemwa mwaka jana tuweze kufuatilia kama kweli yanatekelezwa au la! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo ya elimu ya juu. Kama nilivyosema juzi, hii taasisi ya mikopo ilianzishwa ili kupanua udahili si kupanua udahili tu na kusaidia wanafunzi ambao ni wahitaji, lakini tumeona mwaka jana, kwa bajeti ya juzi hakuna pesa iliyotolewa ya kutosha na kwa mpango huu ambao umewasilishwa inasemekana kwamba udahili utaongezwa na tuta-train watu wengi, kama ikiwa mpaka sasa hivi bajeti inayotoka hata haikidhi wale wanafunzi waliokuwepo, je, ni kweli Serikali itakuwa na hiyo pesa ya kuingiza kwenye mzunguko mwaka kesho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ningependa Waziri anisaidie kujibu, kuna hii hoja ambayo imeshajitokeza kwamba kuna wanafunzi ambao wanaendelea wananyimwa mikopo, mimi nauliza busara ya kawaida tu inasema kwamba hawa wameshaingia kwenye mkataba na Loans Board na wamesaini mikataba ya jinsi ya kurudisha hiyo hela na leo Serikali inasitisha kuwapa mikopo hawa wanafunzi wanaoendelea, ni kwamba Serikali imekiuka utaratibu wake wenyewe wa kuwapa wanafunzi hawa mikopo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, busara ya kawaida ingekuwa kuendelea kuwapa hawa wanaoendelea, halafu mipango mipya au uhuishaji au utaratibu mpya ungeanza na hawa ambao ni wapya, ndiyo utaratibu tunaofuata. Ningependa kupata ufafanuzi kuhusu hawa wanafunzi wanaoendelea ambao walikuwa wanapewa mikopo na sasa inasitishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu, ni suala la Watumishi wa Umma. Naomba ku-declare kwanza interest kwamba nilikuwa Katibu Mkuu Utumishi. Nasikitishwa kwa jinsi ambavyo watumishi wamekuwa wanatumbuliwa left and right. Utakuta Mawaziri wanatumbua japokuwa tangu majuzi kidogo wametulia, Ma-RC wanatumbua, DC anatumua, DED anatumbua, wakati tunajua kabisa Mamlaka ya nidhamu ni watu gani ambao Rais amewakasimu. Hii inapelekea watumishi kukosa imani, kukosa amani na kukosa ubunifu na matokeo yake Utumishi wa Umma ambao ndiyo injini ya maendeleo utashindwa kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Makada wengi ambao hawakuwepo katika Utumishi wa Umma kabisa wamewekwa kwenye maeneo ya utendaji ambayo inakwenda ku-compromise uadilifu na uimara wa Utumishi wa Umma. Utumishi wa Umma duniani kote unaishi zaidi ya Wanasiasa. Wanasiasa malengo yao ni miaka mitano tu. Utumishi wa umma ambao ni legelege hautaweza kutekeleza huu Mpango ambao unaletwa. Kwa hiyo, hili jambo ni lazima liangaliwe kwa ukaribu sana ili kusudi Watumishi wa Umma wapate imani na waweze kufanya kazi zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Local Government Reforms, Serikali Kuu imekasimu madaraka kwa Local Government na kati ya maeneo ambayo ilikuwa imekasimu ni property tax au kodi ya majengo, tumeona Awamu hii ya Tano imeanza tena kurudisha collection ya property tax kwa TRA. TRA walishashindwa siku nyingi na ndiyo maana ilihamishiwa Local Government.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kigezo gani ambacho Serikali imetumia kuhamisha tena property tax kutoka Serikali za Mitaa kuja TRA wakati walikwishashindwa na tunajua kwamba Serikali Kuu imekasimu madaraka kwa Local Government. Inawezekanaje umpe mtu madaraka, umpe na rasilimali watu, lakini ukamnyima rasilimali fedha ya kuifanyia kazi, wakati Local Government ndiyo ina mashule, Local Government ndiyo ina hospitali, Local Government ndiyo ina barabara, watafanyaje hizi kazi ikiwa resources Serikali Kuu imewanyang’anya? Hili ni janga la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mikubwa ambayo imezungumziwa. Makaa ya mawe - Liganga, Mchuchuma, reli ya kati, general tyre, hizi story za siku nyingi tangu nikiwa Katibu Mkuu, nimestaafu miaka mitano sasa bado hadithi ni ile ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Bado hadithi ni ile ile. Tunataka Mheshimiwa Mpango aje atueleze ni namna gani hili jambo litatekelezwa. Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hoja ambayo ipo hapo mezani na na-declare kwamba mimi pia ni Mjumbe mmojawapo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa. Naona Mheshimiwa Suzan Kiwanga hajaja mimi nitaendelea tu na dakika zangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu kubwa ambalo nalikazia ni eneo la Utawala Bora ambalo Kamati imezungumza na kuainisha maeneo mbalimbali ambayo hayazingatii utawala bora katika Awamu hii ya Tano. Tukiangalia katika ile taarifa ya Kamati tumeona jinsi watu wanavyoswekwa jela kwa kutokuhudhuria tu vikao, ambayo ni kinyume za kanuni na taratibu za uendeshaji Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hata kule Singida, Daktari ameswekwa rumande, kwa sababu kuna mgonjwa alikufa. Mimi sitetei uzembe lakini kuna factors nyingi ambazo zinaweza kufanya mgonjwa kufariki dunia. Kwa vile huyu Daktari amewekwa rumande, nasikia ame-resign na sioni ni jinsi gani huyu Daktari angerudi tena akaweza kufanya kazi vizuri katika ile hospitali. Hata wale watumishi wengine ambao wanafanya kazi na yule Daktari watapoteza morali kabisa ya kufanya kazi. Sidhani kama wale wagonjwa watapata tiba stahiki na huduma stahiki kwa jinsi ambavyo mwenzao ametupwa rumande. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hao ndio wanyonge tunaowazungumzia, maana yake hakuna Mbunge atakwenda kutibiwa huko Singida tunakozungumza. Kwa hiyo ni muhimu Serikali ikazingatia kanuni na taratibu za kuchukulia watumishi hatua za kinidhamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona jinsi gani Mtwara kule, Walimu Wakuu wameteremshwa vyeo kwa sababu tu ya matokeo ya form four. Hiyo siyo sahihi, kwa sababu tunamtafuta mchawi. Mchawi ni Serikali yenyewe, haijawekeza kwenye elimu. Kama Mwalimu ana wanafunzi 100 darasani, hana vitendea kazi, marupurupu yake hayajalipwa, utamtegemeaje huyu Mwalimu afanye kazi kwa ufanisi? Kwa hiyo Serikali, ijikite katika kuangalia factors ambazo zinateremsha elimu yetu na inafanya wanafunzi wetu wasiweze kufaulu vizuri madarasani. Hivyo kwa kweli hiyo haipendezi hata kidogo, Serikali isitafute mchawi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nikaangalia pia hii Mihimili miwili ya Bunge na Mahakama. Nakumbuka juzi Spika alisema kwamba Bunge tuko huru kabisa, sikubaliani kama sisi Bunge tuko huru! Juzi hapa tumenyimwa Bunge live na sisi ni Bunge, hakuna mtu amesimama kulisemea mbali ya Wapinzani, halafu tunasema Bunge tuko huru, tuna uhuru gani? Tukitaka kusafiri nje, mpaka tupate kibali Ikulu, tuna uhuru gani? Wakati iko namna ya kudhibiti matumizi ya Serikali, unaifanya katika bajeti tool. Inasema Bunge ninyi kwa mwaka huu mtapata milioni kadhaa kwa ajili ya safari zenu, lakini siyo tuombe ruhusa kwa Executive. Ina maana Bunge limekuwa compromised na hakuna mtu anayelisemea. Kwa hiyo, sisi hapa ni Bunge butu, hatuna meno na huu ndiyo ukweli na lazima tuukubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia upande wa Mahakama, Mahakama tumenyimwa kufanya mikutano ya kisiasa na hiyo ni kinyume cha Katiba. Mahakama iko kimya, wala haijasema kitu. Jana Mheshimiwa Rais amesema kwamba wale Mawakili wanaowatetea watu ambao wamekosa wawekwe ndani, itakuwaje wawekwe ndani na juzi tumepitisha sheria ya Paralegals ya kutetea wanyonge. Sasa huyo Wakili unamweka ndani atamtetea nani?
watatetewa wale wenye pesa, kwa hiyo wale wanyonge watashindwa kutetewa. Hiyo haiendi sawa na lazima turudi katika misingi ya mihimili mitatu kila mmoja iwe inamwangalia mwenzake lakini kwa sasa hivi ilivyo Mahakama na Bunge tumekuwa compromised na huo ni ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja suala la decentralization kwa upande wa kimitaa. Ilipitishwa sera miaka kadhaa ya decentralization by devolution lakini kwa jinsi ambavyo Serikali inafanya sasa hivi, inapoka mamlaka ya Serikali za Mitaa. Tanzania ina kilomita za mraba karibu 945,000. Lazima Serikali za Mitaa iwe very strong na kwa mtindo huu, wamenyanganywa property tax na je, huu utawala bora tunaousema ni upi, wakati mkono wa Serikali wa Local Government unanyimwa pesa ambazo zingewasaidia kupeleka huduma kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili haliko sawa na ili neno la good governance tunalizungumza tu lakini kwa kweli hatulizingatii. Nashukuru sana Suzan Kiwanga amerudi sijui kama bado ana dakika. Ahsante.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ilikuwa ni hili la TASAF. TASAF tumekwenda kutembelea maeneo mbalimbali na wanafanya vizuri. Mimi naungana na wengine wote waliozungumza, napendekeza kwamba TASAF iendelee na TASAF sasa iwekewe mfumo mzuri kuweza kuwatambua. Kwa sababu inaelekea siyo kila mara Serikali ikishindwa kitu inafikiri kwamba itafanya kitu tofauti badala ya kuangalia imeshindwa wapi na kurekebisha. Kwa hiyo Serikali iangalie kwa nini huu mfumo haufanyi kazi vizuri na ni jinsi gani watu hewa wanaingizwa kuchukua hizo pesa za TASAF ifanyie kazi na siyo kumtafuta mchawi mwingine tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kunipa uhai na kuweza kuchangia hoja iliyoko mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro kati ya hifadhi na wananchi imekuwa sugu na ya muda mrefu. Nilipokuwa Mjumbe wa Bodi ya TANAPA ulitayarishwa mpango mkakati wa kutatua migogoro hiyo, watendaji wa TANAPA waliainisha maeneo yote yenye migogoro na wananchi, yaliwasilishwa kwenye Bodi ya Wadhamini na maamuzi yalifikiwa kama ifuatavyo:-

(a) Maeneo yenye migogoro na ambayo hayana madhara yoyote kwa hifadhi au ekolojia ya eneo la hifadhi waachiwe wananchi na mipaka irekebishwe.

(b) Maeneo yale yenye migogoro na uwepo wa human activities kuhatarisha bionuai na ekolojia ya hifadhi, wananchi washawishiwe kuachia maeneo hayo na Serikali iwape ardhi nyingine na kuwalipa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi haya hayakutekelezwa kwa sababu muda mfupi baadae aliyekuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Pinda aliunda Tume ya kuchunguza migogoro yote ya ardhi na kutoa mapendekezo, baadae tena Waziri wa Ardhi naye aliunda Tume kwa jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kwa Serikali kushindwa kutoa uamuzi kwa jambo nyeti linalogusa hisia za jamii. Serikali ichukue maamuzi magumu ya kutatua kero hii badala ya kujificha nyuma ya Tume na Kamati zinazoundwa kila mara ili tu isifanye maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro hii sasa na zaidi ya miaka kumi tangu nimeanza kuisikia, ni matumaini yangu kwamba kabla Awamu ya Tano haijamaliza muda wake wa miaka mitano itaacha alama ya kudumu ya kutatua kero hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nichukue pia nafasi hii kuwapa pole watu wa Arusha kwa ajili ya vifo vya Watoto wetu wa shule ya Lucky Vincent na Walimu pamoja na wafanyakazi Mungu awarehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya elimu ina changamoto nyingi sana na mengi yameshazungumzwa. Mimi nitajikita kwenye maeneo kama matatu tu.

Kwanza ni suala la lugha ya kufundishia. Kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala mkubwa sana kama tutumie kiswahili au tutumie kiingereza nafikiri baadae, kwa sababu tulishakubali kwamba kiswahili ndiyo lugha ya Taifa nafikiri huo ndiyo msimamo kwamba kiswahili ni lugha ya Taifa bila shaka na lugha ya kufundishia iwe kiswahili. Mpaka sasa hivi hatujachukua hatua. Tunakuwa na wanafunzi wanasoma kiswahili kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la saba, halafu unamtegemea mwanafunzi huyu aende form one akajifunze masomo kwa kiingereza! Kwa kweli huo ni mtihani mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa tumeamua kwamba kiswahili ndiyo tuwe nacho basi kazi ifanyike kubadilisha mitaala yote ya Sekondari mpaka Chuo Kikuu tujue tuna lugha moja kwa sababu ufanisi wa lugha inamjengea hata mtu confidence unakuwa na confidence kwamba unaweza ukaizungumza lugha yako vizuri na ukaeleweka na ndiyo maana kila mara tunasema Watanzania hatupati kazi Kenya ni kwa sababu ya confidence ya lugha. Tunafundisha watoto kiswahili na tunategemea wafanye mambo mengine kwa kiiingereza, kama tumeamua kiswahili basi tuende nacho moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya Serikali ya Awamu Tano ni Serikali ya Viwanda, nauliza hatujajua viwanda ni vipi kama ni textile, kama ni agri, kama ni nini sujui, lakini nilitegemea kwamba Wizara ya Elimu nayo itajipanga kuona kwamba sera ya viwanda ni hii na viwanda gani tunataka kuvianzisha basi Mheshimiwa Waziri aje atuambie katika kutekeleza hii sera ya viwanda ni skills zipi ambazo zinakuwa imparted kwa ajili ya baadae kutumika kama wataalam katika viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na hiyo ya viwanda, labs (maabara) ni muhimu sana na shule nyingi hazina maabara, tutakuaje sasa na Serikali ya viwanda wakati maabara zetu haziko sawa sawa? Nchi za wengine wanakuwa hata na mobile maabara, mobile kits za lab ambazo zinahamishika kutoka mahali pengine kwenda mahali pengine. Pengine hilo ni jambo muhimu pia la kuweza kujifunza kusudi tuwe na mobile lab kits ambazo tunaweza tukatembea nazo katika shule zetu na watoto waweze kafundishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi na kwenye kiswahili, kiswahili ni fursa pia Wizara imejipangaje ku-train wakalimani kwa sababu tayari African Union kiswahili kimekubalika, East Africa kiswahili kimekubalika, Wizara imejipangaje kutayarisha wakalimani wa kiswahili kwa sababu ni ajira pia kwa ajili ya Watanzania, vinginevyo tutakuta wakalimani watakuwa ni Wakenya wamejaa kule sisi wenyewe, wenye kiswahili chetu tutabaki nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge lako Tukufu lililopita, lilipitisha bill hapa kwamba wanafunzi wote wanaochukua loans wakatwe asilimia 15, wengine wameshalizungumzia na mimi nakazia hapo pamoja na hotuba ya Upinzani kwamba pamoja na kwamba hili Bunge lilipitisha 15 percent, lakini haikuwa inatarajiwa kwamba ingerudi nyuma kuhusisha wale wanafunzi wengine wote ambao walikuwa wamesaini mkataba wa asilimia nane.

Kwa hiyo, ni maoni ya Kambi kwamba siyo sahihi kwa sababu unakuwa ume-change position in the mid of the stream. Mimi nimesaini nitatoa eight percent, tumepitisha bill hapa 15 percent, hiyo isingemu-affect mtu ambae ameshasaini mkataba wa eight percent, ingehusisha wale ambao ni wapya... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mungu kunipa afya na nguvu kuwatumikia wananchi Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imejaliwa kuwa na maji mengi sana kutoka vyanzo mbalimbali kama maji juu ya ardhi, maji chini ya ardhi na maji ya mvua yanayosababisha mafuriko mara kwa mara. Hata hivyo, kila mara Tanzania imekuwa inakabiliwa na uhaba wa maji safi na salama katika maeneo mengi mjini na vijijini. Uhaba wa mvua unaosababisha ukame na kusababisha njaa na adha kubwa ya kiuchumi. Mfano, wanyama kufa na kukosekana kwa mazao, vilevile nchi imekuwa mhanga mkubwa wa mvua kubwa inayosababisha maafa ya mafuriko, uharibifu wa mazao na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka 53 ya uhuru pamoja na wataalam waliobobea katika taaluma ya maji na mipango, Serikali imeshindwaje ku-manage suala la maji ili kupunguza kero na umaskini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini Serikali haisimamii kwa Sheria ya Uvunaji wa Maji ya Mvua na Sheria ya Ujenzi irekebishwe kujumuisha miundombinu ya kuvuna maji kwenye majengo mbalimbali. Kwa nini mabwawa makubwa ya kukinga na kutunza maji kwenye maeneo ambayo kila mara kuna mafuriko na ya katumika kwa ajili ya kilimo, mazao na mboga mboga za muda mfupi ili kuinua uchumi wa wananchi na kupunguza umaskini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini maeneo yenye maji chini ya ardhi wananchi wasichimbiwe visima ili kuwanusuru na kero ya maji? Katika hotuba, maeneo yenye maji chini ya ardhi yameainishwa, lakini hakuna popote fedha imetengwa kwa ajili ya kuchimba visima vichache kwa vipaumbele?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai yangu kwamba Wizara ijipange kukusanya/kuvuna maji mengi yanayopotea na kwenda baharini. Nchi ya Israel ni mahali pazuri pa kujifunza, maji ni almasi, hakuna tone linalopotea. Hapa kwetu tuna maji mengi lakini tunafanya mzaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RUTH H. M0LLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mezani. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Waziri pamoja na Makamu wake, ninayo machache ya kushauri upimaji wa ardhi yote ya Tanzania ambayo ni 950,000 square kilometres, matumizi yake yajulikane na vile vile wamiliki halali wajulikane na kudhibiti wageni kumiliki ardhi nchini mwetu. Maeneo ya mlimani Usa Arusha kuna mashamba makubwa, mengine yana farasi kwa ajili ya burudani. Je, wenyewe hawa ni wamiliki halali? Je, matumizi yake ndiyo yaliyokubaliwa na Wizara au Kituo cha Uwekezaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itumie sekta binafsi katika upimaji na kupanga matumizi ya ardhi, kwa sababu wataalam Serikalini hawatoshi, vinginevyo itachukua miaka mingi sana zoezi hilo kukamilika. Serikali isitumie udhaifu wake kuumiza wananchi kwa mujibu wa sheria na kanuni. Kodi hulipwa kufuatana na eneo na matumizi ya ardhi, haiyumkiniki kusikia Tamko la Waziri kwamba, kodi italipwa kwa maeneo yote ambayo hayajapimwa. Je ni kosa la nani kwamba ardhi hiyo haijapimwa? Je, kodi hiyo italipwa kwa kigezo gani? Hakuna mtu wala taasisi iliyo juu ya sheria. Serikali yenyewe ndio imetunga Sheria ya Ardhi na lazima izingatie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba kuna improvement kwenye mchakato wa kupata hati miliki ya ardhi, bado juhudi zaidi inahitajika, bado kuna watumishi wanaojivuta. Napendekeza utoaji hati miliki zisizo na migogoro kwa wakati kiwe kigezo cha kupima utendaji wa watumishi wanaohusika na utoaji wa hati miliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali sasa ifanye maamuzi magumu ya kutatua kero ya migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi Serikali sasa iepuke kukwepa kufanya maamuzi ya kero hii kwa kuunda Tume na Kamati za kutoa mapendekezo miaka nenda, miaka rudi. Pamekuwepo na Kamati/Tume zaidi ya tatu na bado migogoro hii haijapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wanaopata nafasi ya kujiunga na masomo ya elimu ya juu wamekumbana na changamoto ya kupata mikopo, hasa wanafunzi wenye mahitaji. Ninatambua pia umuhimu wa kutoa fursa zaidi kwa wanafunzi wanaochukua masomo kusomea taaluma zenye upungufu, sayansi etc.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapendekeza Sera ya Elimu ya Juu na Kanuni zake zipitiwe upya, kwa sababu wanafunzi wanaofaulu kwa kiwango cha juu kidato cha sita ni wale waliosoma shule binafsi zenye mazingira mazuri ya kujifunzia, walimu, vitabu, maabara na kadhalika, matokeo yake, hao wenye uwezo ndio wanapata mikopo wakati si wahitaji. Karo za shule walizosoma ni ghali kuliko ya vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, lile lengo la kutoa mikopo kwa wahitaji na wanaotoka kwenye familia zenye uchumi mdogo/duni, halikufikiwa. Kwa wakati huu, utaratibu wa kutoa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ufanyiwe mapitio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyoko mezani. Na nichukue nafasi hii pia niwatakie kheri ndugu zetu Waislam, Ramadhan Karim kwa wote, Mungu awajalie mmalize mfungo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Fedha na Mipango ni moyo wa Serikali. Nasema moyo wa Serikali ni kama moyo wa binadamu unavyofanya kazi, kama usipofanya kazi vizuri kila kitu kinatetereka. Kwa hiyo, ninapenda kusisitiza unyeti wa Wizara hii ya Fedha na mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua katika mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kwamba, hii ni Serikali ya Viwanda. Katika kuangalia mpango wa miaka mitano, nikaangalia mpango ule wa mwaka mmoja, nikaangalia pia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, vimetajwa viwanda vingi sana ambavyo vinahitajika kufanyiwa kazi, vingine kufufuliwa, vingine kujengwa upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha hoja yake atuambie hii Tanzania yetu ya viwanda ni viwanda vya aina gani? Kwa sababu ni lazima tujue kama viwanda tunavyozungumzia ni agro-processing, kama ni textile industries, kama ni machinery, ili tuweze kuwa na lengo ambalo Serikali iweze kujipanga maana unapoainisha kabisa, kwamba, kama alivyofanya Mwalimu Nyerere yeye alikwenda kwenye Textile Industry, tukaona viwanda vingi vya nguo na resources zote zikapelekwa kwenye hayo maeneo kwa ajili ya kuleta ufanisi na ku-create ajira. Sasa ningependa Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha hoja yake atufungue macho kidogo, kujua hivi viwanda tunavyovizungumzia ni vipi ambavyo Serikali inajikita kuviamsha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona viwanda vingi, ni jambo jema, lakini kwa resources tulizonazo hatuwezi tukapeleka hapa kidogo, hapa kidogo, hapa kidogo. Ni lazima tuainishe maeneo madhubuti ambayo tunajua baada ya miaka mitano tunajua hii Serikali tutaipima kwa viwanda gani vilivyokamilika na vinavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo pia linaendana na kuelimisha Watanzania. Nchi nyingine za duniani ukienda Mauritius au Singapore au Malaysia unakuta mpaka tax driver anajua mwelekeo wa nchi yake. Je, Watanzania wote tunajua mwelekeo wa nchi yetu? Kama ni laa, basi kazi kubwa ifanyike ili kusudi kila mtu aweze kujua nini mwelekeo wa nchi yetu katika hii Sera ya Viwanda Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo itasaidia hata na wakulima kama ni agro-processing, wakulima watajipanga, kila mtu atajipanga na Serikali pia itajipanga kama ni kupeleka mbolea, kama ni kuhakikisha mashamba makubwa ya pamba, itajipanga vizuri na wataalam. Maana mwaka 2015 tulihitajika tuwe na Mechanical Engineering, Manufacturing Engineering, kama 17,000, lakini lengo halikufikiwa, kwa nini halikufikiwa? Ni kwa sababu bado hatujaainisha ni kitu gani tunataka kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mapato ya ndani. Hili jambo limezungumziwa na watu wengi kuhusu kodi ya majengo. Kodi ya majengo ina historia, Mheshimiwa Waziri anafahamu. Kwanza walikuwa wanakusanya TRA wakashindwa, jukumu hili likapelekwa kwa Halmashauri (TAMISEMI) wakafanya vizuri sana wakakusanya, sijui ni kitu gani sasa kimekuja hapa katikati kuona kwamba hili suala tena lirudishwe TRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa kidogo tu ya mkoani kwangu Dar es Salaam, Kinondoni na Ubungo walikuwa wamepanga kukusanya bilioni 10.5 Kinondoni ilikuwa wakusanye bilioni 7.5, Ubungo shilingi bilioni 3.0, wote ilikuwa wakusanye hizo pesa. Jukumu hili lilipoondolewa
wakaambiwa watapewa bilioni mbili, mpaka leo hawajapewa hata senti tano na hatujui kama hizi pesa zimekusanywa au hazijakusanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunakubaliana kwamba Serikali imeingia katika Sera ya D by D na unapotekeleza Sera ya D by D upeleke resources, upeleke na wataalam. Kitendo cha kunyang’anya property tax kwenye Halmashauri za Jiji na Manispaa ni sawa na kuwaambia wasifanye kazi, kwa sababu huduma zote za jamii zinapatikana kwenye Serikali za Mitaa ndiko kwenye afya, maji, barabara, ndiko kwenye kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inakuwaje kwa sababu Serikali Kuu imekasimu madaraka kwa Local Government, ni kama baba unasema mtoto wangu wewe nenda ukafanye A, B, C, D, chukua hela hizi, chukua resources hizi, sasa unainyang’anya tena halafu unategemea itafanya nini? Tunaomba Mheshimiwa Waziri ili akajitafakari, najua Sheria ilipita hapa lakini hiyo sheria ikatazamwe upya, kwa sababu mpaka sasa TRA wameshindwa kukusanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa Iringa tumekuta TRA Iringa wameshindwa kukusanya, wanawatumia tena hao hao watu wa Local Government kukusanya kuwatumia kama agency. Kama wao hawawezi kukusanya kwa nini wasiwaachie Local Government wazikusanye hizi pesa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja kwenye suala la fedha za miradi. Fedha za miradi tumekwenda kwenye Mikoa fedha za miradi hakuna, tumekuja hata kwenye Wizara, fedha za miradi hazipo hata kwenye Wizara katika taarifa zilizopita sasa hivi kwa mfano kilimo wanapata three percent, viwanda eighteen percent. Sasa ni kwanini Wizara isiende na realist budget. Kama bajeti ya kupeleka kwenye Wizara fulani ni bilioni mbili basi ipelekwe hiyo bilioni mbili na ipatikane, kuliko kusema unapeleka bilioni 100 kwa mfano kilimo halafu hakuna pesa inayokwenda. Hii ni unacceptable kwa kweli. Twende na uhalisia ile pesa iliyokusanya ndiyo hiyo igawanywe na hiyo iweze kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kidogo kwenye suala la Muundo wa Wizara. Najua Tume ya Mipango iko chini ya Wizara sasa hivi, Tume ya Mipango ndiyo think tank ya uchumi na mipango. Nikiangalia hata bajeti waliyopelekewa haitoshi, sasa katika hii dhana ya Tanzania ya viwanda ikiwa Tume ya Mipango ambayo ndiyo think tank ambayo inatakwa ikae na kufikiri, kupanga na kupangua haipati bajeti, tutafika huko tunakwenda? Sioni kama tutafika huko tunakokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kumalizia hoja yake atuambie mwelekeo wetu wa viwanda ni upi na ni viwanda gani ambavyo Serikali ina mpango wa kuhakikisha kwamba itakapofika 2020 vitakuwa vinafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami ili niweze kuchangia kwenye hoja iliyopo mezani. Pia nimshukuru Mungu kwa kunipa nafasi hii. Moja kwa moja naunga mkono hotuba ya Upinzani iliyowasilishwa kabla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa maendeleo huu utatekelezwa na Watumishi wa Umma, utatekelezwa na wananchi kwa ujumla. Ili Watumishi wa Umma waweze kutekeleza huu mpango wanahitaji kwanza kupata stahili zao zile wanazostahili, kama ni posho, kama ni mishahara, kama ni kupandishwa vyeo ili wawe na morali ya kuweza kufanya kazi kwa kujituma. Vilevile wanahitaji kupata refresher courses za kuwajengea uwezo wa kuweza kufanya kazi zao kwa utaalaam zaidi na hapa linakuja suala la mafunzo kwa ajili ya in service ambayo kwa muda mrefu yamesimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile watumishi wa umma wanahitaji kutiwa moyo wajue kwamba wanafanya kazi zao, wanaweza kufanya maamuzi bila kuogopa kutumbuliwa. Vinginevyo tutakuwa na utumishi wa umma wenye hofu ambao hauwezi kufanya kazi kwa kujituma na kwa ukamilifu kwa hofu ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile watumishi wa umma kama hawapati zile stahili zao kwa wakati tutarudi kule tulikokuwa zamani kwenda kufuga kuku – kukimbilia kufuga kuku, kukimbilia kuangalia ng’ombe kazi zinaachwa kufanyika ofisini. Kwa hiyo ni jambo muhimu sana kuangalia suala la Watumishi wa Umma ambao kwa kweli kwa muda sasa hawako vizuri na huo ndiyo ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengine ambao watatekeleza huu mpango ni wananchi wenyewe na wananchi wanahitaji amani, wanahitaji utulivu. Kuna hawa watu wasiojulikana ambao sasa hivi wamekuwa ni tishio kwetu. Ni lazima Serikali iingilie kati kuwahakikishia wananchi wake usalama wao. Nilikuwa Mkuranga juzi na katika kikao nilikuwa na wananchi tunafanya kikao, wanaogopa hata hizi bodaboda saa 11 hawawezi tena kwenda kwenye maeneo yao wanayoishi kwa sababu ya hofu. Kwa hiyo, tunahitaji Serikali itoe kauli ya kuwahakikishia wananchi usalama wao ili waweze kufanya kazi zao vizuri, kwa sababu bila kuwa na uhakika na usalama hata shughuli za kiuchumi hazitafanyika kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo Serikali za Mitaa na Local Government inayo historia. Tulipopata uhuru tulikuwa na Local Government ambayo ilikuwa na nguvu sana, lakini Serikali ya wakati huo ikaona kwamba pengine ni ku- centralize, tuka-centralize Serikali, tukaua Local Government lakini hatukufanikiwa. Serikali ikarudisha tena Local Government kwa sababu Tanzania ni nchi kubwa sana, ina kilometa za mraba 945,000 ni kubwa sana haiwezekani ikatawaliwa kutoka Serikali kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo sasa matokeo ambayo yamekuwa yanaendelea kutokea sasa hivi inaelekea kuziua Serikali za Mitaa na kuzipunguzia nguvu za kuendesha shughuli, wakati tunajua wazi kabisa kwamba Serikali za Mitaa ndiyo kwenye huduma za afya, ndiyo kwenye barabara, ndiyo kwenye elimu na maji. Kama Serikali za Mitaa hazitapewa uwezo wa kutosha, uwezo kwa maana ya rasilimali watu na uwezo kwa namna ya rasilimali fedha, huu mpango ambao tunauleta hauwezi kufanikiwa kwa sababu utekelezaji uko kwenye Serikali za Mitaa na ndiyo kwenye wananchi. Ina maana basi huu mpango hautafanikiwa na maendeleo tunayotaka kuleta Tanzania ya viwanda haitaweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivyo kwa sababu kwanza mwaka huu ilipangwa bajeti kama (approximately) ya bilioni 12, lakini iliyotoka ilikuwa ni bilioni moja tu na point ambayo ni about 11 percent. Sasa kwa mtindo huu, sijui kama kweli huko tunakokwenda Serikali hii itafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kwenye Local Government kama nilivyokwishasema awali na wengine pia wameshachangia, tumenyang’anya Local Government property tax, tumewanyang’anya ushuru wa mabango, ruzuku haiji kwa wakati sasa hiyo Local Government ambayo tunataka ifanye kazi itafanyaje kazi kama haipati resources?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba Local Government inafanya kazi kwa niaba ya Serikali kwa sababu Serikali kuu imekasimu madaraka kwa Local Government. Kwa hiyo kama Serikali ya Mitaa inafanya kazi, inafanya kazi kwa niaba ya Serikali, kama Serikali ya Mitaa ikishindwa ina maana Serikali Kuu na yenyewe imeshindwa. Kwa hiyo, kuna umuhimu wa kuimarisha Serikali za Mitaa ziweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja kwenye rasilimali watu tunahitaji kwa ajili ya huu mpango kufanikiwa. Katika mpango ule wa mwaka 2016/2017 - 2020/2026 wa mwaka jana ambao uliwasilishwa kulikuwa na taaluma ambazo ziliainishwa, kulikuwa na Wahandisi, watu wa construction, watu wa agriculture na yalitolewa malengo. Kwa mfano, katika agriculture na zingine lengo lilikuwa ikifika mwaka 2025 wataalam 145,000 wanategemewa kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika mpango wa sasa hivi kuna maeneo kwenye training kuna taaluma mbalimbali ambazo watu wanakwenda kusomeshwa. Swali langu ni kwamba tumeweka target hiyo ya 2025 na intervention 2015/2016 kwa mfano kwenye agriculture tulitegemea tuwe na wataalam 4,475, sasa napenda kujua, tukifananisha lengo lile la 2025 na tulivyoanza 2015/2016 kwa kuainisha kada zile ambazo zinatakiwa kufikiwa, je, tumekwenda vipi mpaka sasa hivi huu mwaka 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia Wabunge tuweze kufuatilia utendaji kazi wa Serikali katika kufikia yale malengo ambayo yameainishwa. Kwa hiyo, nitapenda sana kujua Serikali imefikia wapi katika kuainisha hayo malengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kila siku kilimo ni uti wa mgongo na sio uti wa mgongo tu, kilimo ndiyo kitatoa malighafi kwa ajili ya uchumi wa viwanda. Nimeangalia katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri, ameainisha tu activities ambazo zinatakiwa kufanywa kwa ajili ya kilimo lakini sijaona mahali popote ambapo ameainisha kwa mfano, watalaam wa kilimo hasa Maafisa Ugani ambao ndiyo wanaokwenda kuwasaidia wakulima katika uzalishaji, sijaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hata katika sikumbuki ukurasa wa hii ripoti ya sasa hivi ambapo imeainishwa taaluma mbalimbali nimeona watu wa VETA, sijui watu wa mambo ya hoteli, sijaona popote wameainishwa Maafisa Ugani ambao ni muhimu sana kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kuweza kulima vizuri na kwa kitaalam waweze kupata mazao ya kutosha. Kwa hiyo, ningependa kujua ni kwa namna gani Maafisa Ugani watapanga ili tuweze kupata Maafisa Ugani wa kuweza kwenda kusaidia wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishauri Serikali tuwe na Maafisa Ugani wa kutosha kama ambavyo tulivyo na Madaktari kwa ratio tunasema kila Daktari mmoja anatakiwa kutibu wagonjwa 10,000. Tuwe na ratio pia kwa ajili ya Maafisa Ugani kwa ajili ya wakulima kusudi Afisa Ugani aweze kuwafahamu wakulima wake kwa umakini na shida zao, wawezeshwe kwa kupewa hata pikipiki waweze kuwafikia wakulima, ndiyo tutaweza kuleta kweli mapinduzi ya kilimo katika nchi hii. Bila hivyo itakuwa ni kuzungumza hapa kila siku, tutaondoka, mambo yatabaki hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala la mikopo ya wanafunzi. Kama tunavyojua sasa hivi wanafunzi wengi hawajapata mikopo. Naishauri Serikali iangalie tena upya hii Sera na utekelezaji wa mikopo. Kwa nini nasema hivyo? Nasema hivyo kwa sababu, kwanza na-declare interest kwamba mimi ni mmojawapo walioanzisha Bodi ya Mikopo, sababu ilikuwa ni kuwasaidia wanafunzi wenye uhitaji….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii yakuchangia kwenye hoja iliyoko mezani. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala Bora na Serikali za Mitaa na naunga mkono hoja ambayo imewasiliswa hapo mezani na ninawapongeza wote ambao wamewasilisha hoja zao hapa mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita katika maeneo mawili. Katika lile zoezi la vyeti fake kuna watumishi kama 11,696 ambao walitolewa kazini na kati ya hao 3,301 wametoka Serikali za Mitaa. Kwa sababu hiyo sasa upungufu wa watumishi katika Serikali za Mitaa umeruka kuanzia asilimia 51 mpaka asilimia 54 ambayo ni karibu watumishi 57,700.

Sasa ningependa kujua Mheshimiwa Waziri wa Utumishi kuna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba serikali za mitaa zinapata watumishi ili kupunguza matatizo katika yale maeneo ya social services? Hilo la kwanza,

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, pia tungependa kujua nini hatima ya hawa watu ambao wamekutwa na vyeti fake? Najua kweli wamevunja sheria lakini wengine wamekutwa na haya maswahibu karibu wanastaafu na wameitumikia nchi hii kwa muda wote. Je, nini hatma yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili linahusu wale waliotolewa waliomaliza darasa la saba ambao alishindwa kuendelea mpaka form four, kwa utaratibu wa kawaida hawa watakuwa wamestaafishwa. Tungependa kujua, je, serikali ina mpango wa kuwalipa mafao yao kwa sababu wamestaafishwa? Naomba Mheshimiwa Waziri akija atueleze nini hatma ya watumishi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la mabasi ya mwendo kasi. Serikali imeanzisha huu mradi ambao ni mzuri ilianza vizuri, na lakini sasa hivi hali si nzuri. Si nzuri kwa sababu mabasi yanakuwa machache wakati wa peak hours watu wanasukumana kugombe ndani ya basi; na lengo la huu mradi lilikuwa ni kufanya usafiri uwe rahisi maana yake kama tunafuata kweli rappid transport kama ilivyo katik anchi za wenzentu basi hilo haliwezi kukaa muda mpaka lijae kama daladala. Inatakiwa watu wasafiri wakiingia hao hao walioingia wanaondoka linakuja basi lingine, linakuja basi lingine. Lakini mpaka sasa hivi huduma zimedorora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa kujua Serikali ina mkakati gani katika kuboresha huo usafiri wa mabasi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, inahusu karakana ya haya mabasi ya mwendo kasi. Inashangaza kwamba Serikali imewavunjia wananchi waliokuwa kwenye Mto Msimbazi, nyumba zao zikavunjwa. Hata hivyo ajabu ni Serikali yenyewe inajenga karakana ya mwendo kasi katika Mto Msimbazi. Mafuriko yalipokuja mwaka 2017/2018 lile eneo lilifurika, zile ofisi zilifurika maji mabasi yalikuwa kule ndani, vyombo vikaharibika mabasi yakaharibika na kuisabisha Serikali hasara kubwa. Je, Serikali itakuwa na mpango gani sasa kuona kwamba hatua zinachukulia ili kuepusha tena majanga mengine mvua nyingi zitakaponyesha katika lile eneo la Bonde la Msimbazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ten percent katika Halmashauri zetu. Halmashauri nyingine zimekuwa zinafanya vizuri. Lakini Halmashauri zingine zilikuwa hazitengi ile asilimia 10 inayotakwa kwa ajili ya wanawakena vijana maeneo mengine wamefanya vizuri, maeneo mengine hawajafanya vizuri. Tunapendekeza, kama ilivyosemwa katika taarifa yetu, kwamba ingekuja sheria ambayo italazimisha Halmashauri ziweze kutenga hiyo asilimia 10 ya vijana na wanawake ili wananchi waweze kujiweka katika makundi na kuchangia katika uchangia katika maendeleo yao.

T A A R I F A . . .

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne na nne jumlisha na mbili ni kumi, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dhana ya D by D. Serikali ya Awamu ya Tatu na ya Nne zimetumia mamilioni ya fedha za walipa kodi kugharamia maboresho ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Ugatuzi wa madaraka ni pamoja na kupeleka rasilimali watu wa kutosha na kupeleka rasilimali fedha za kutosha na kuziwezesha Serikali za Mitaa kukusanya kodi katika Halmashauri zao kwa ajili ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano imeua dhana nzima ya D by D kwa kunyang’anya Serikali za Mitaa vyanzo vikubwa vya mapato nazo ni kodi za majengo na kodi za mabango. Kunyang’anywa kwa vyanzo hivi ni kupunguza uwezo wa Serikali za Mitaa kuimarisha na kuboresha huduma za jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa Bunge kupitisha sheria ya kuondoa retention kutoka Taasisi za Umma kama TANAPA, Immigration, Polisi na kadhalika ni kupunguza uwezo wa Taasisi hizi kutimiza wajibu wao kwa kutumia vyanzo vya mapato. Uzoefu umeonesha fedha zikishaingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali hazirudishwi kabisa au zinarudishwa kidogo kwa taasisi husika. Matokeo yake ni huduma kuzorota.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iangalie upya uamuzi wake kwa sababu Serikali za Awamu ya Tatu na ya nne ziligundua kwamba ili taasisi zifanye vizuri waachiwe kutumia mapato yatokanayo na vyanzo vya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iimarishe jukumu lake la msingi la usimamizi na ufuatiliaji, jukumu ambalo bado Serikali haifanyi vizuri. Serikali inaposhindwa jukumu la usimamizi/ufuatiliaji na tathmini, inaibua solution nyepesi ya kuanzisha utaratibu/taasisi mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuitazama upya dhana ya D by D na kuimarisha Serikali za Mitaa kama ilivyokusudiwa.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia japokuwa sikuwa najua nachangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wasilisho la Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango nina mambo matatu ya kuchangia. Jambo la kwanza linahusu development budget ambayo kwa miaka yote tumekuwa tunapata development budget kidogo na tunakuwa na maoteo makubwa na ni kwa nini Mheshimiwa Mpango hatuwezi ku-budget maoteo realistic ambao haiwezi kuwa na tofauti kubwa, hilo ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu property tax. Nilipokuwa nachangia majuzi kwenye bajeti ya Wizara nililizungumzia hili la property tax na bado nalizungumzia kwa sababu kuchukua property tax ya Local Government tunaziua Local Government na dhana ya D by D inadhoofishwa kwa sababu maendeleo yote yako katika Local Gorvenment, ndiko kuliko na shughuli za jamii, elimu, maji, barabara na afya. Ikiwa property tax inachukuliwa basi hizi huduma za jamii zitakuwa hazipatikani kwa wakati na kukaa kusubiri return kutoka Serikalini inachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka jana Mheshimiwa Kamala alizungumza akasema kwamba D by D siyo lazima mtu akusanye mapato, lakini dhana ya D by D ni lazima upeleke resources za pesa ni lazima upeleke resources za watu kuiwezesha Local Government iweze kufanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo property tax ambayo imezungumzwa pia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia kuhusu zile nyumba ambazo hazijathaminiwa, ghorofa Sh.50,000/= nyumba zingine ambazo ni siyo za ghorofa ni Sh.10,000/=. Kwa kweli, kwenda kutoza Sh.10,000/= kwa nyumba za tope na majani ni sawasawa na kuwaongezea wananchi wetu umaskini. Kwa sababu wengine kwanza wako kwenye TASAF, sasa unampelekea pesa za TASAF, halafu unamtoza Sh.10,000/=, hiyo ataitoa wapi kama yeye hela yenyewe anaisuburi ya TASAF? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda wenzetu wa CCM wanatoka kwenye vijiji vina maendeleo sana lakini mimi nikiangalia kule kwangu Arusha kwa mfano, utakwenda kwenye vile vijumba vya majani unakuta huyu Mama watoto ni vumbi, ni nguo zilizochanika hizo shilingi 10,000 watazitoa wapi? Naona tutarudia kama wakati wa kikoloni ule wanapokuja watu wa kodi wazee wanaingia porini, hicho ndicho kitakachotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Menyekiti, napendekeza Mheshimiwa Mpango hiyo Sh.10,000/= ya kutoza nyumba za matope na nyumba za majani tafadhali sana iondolewe tuwapunguzie wananchi wetu umaskini. Napendekeza pia katika zile tozo za nyumba ya Sh.50,000/= kwa za ghorofa na zingine ambazo wanaishi wazee wastaafu au wazee wenye zaidi ya miaka 60 na kuendelea wasitozwe hiyo kodi ya Sh.50,000/= kwa ajili ya kurahisisha maisha yao, kama wanavyofanya watumishi wastaafu wa Serikali ambao hawalipi property tax katika nyumba wanazoishi. Kwa hiyo, wazee hawa wa miaka 60 na wenyewe kama ni nyumba ni ya ghorofa ni Sh.50,000/= haijathaminiwa kama anaishi humu ndani asitozwe hiyo kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi hii ya mafuta kwa kweli nasikitishwa kwa sababu tumetoa mzigo kutoka kwa upper class na middle class tumepeleka kwa watu wa chini. Kama kweli Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira ya kupunguza umaskini basi hiyo Sh.40/= ya mafuta itolewe kwenye mafuta ya taa. Kwa sababu hao tunaokwenda kuwadai Sh.40/= kwenye mafuta ya taa ni watu ambao kwa kweli maisha yao ni duni sana. Haiwezekani Shangazi yangu yuko kule yuko kwenye kile kijumba anatumia mafuta ya taa halafu tunamtoza Sh.40/= wakati huo mzigo ungetakiwa kubebwa na upper class na middle class.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza kama kweli tuna dhamira ya kweli ya kuwajali wanyonge hiyo Sh.40/= itolewe kwenye mafuta ya taa, wananchi wetu kule mikoani na vijijini waweze kutumia mafuta ya taa. Natofautiana na Mheshimiwa Mbunge aliyezungumza
akasema sijui utaleta gesi, hiyo gesi itakuja lini? Ni kama alivyozungumza Mbunge mwenzangu mmoja atakuwa kama yule First Lady wa Ufaransa, watu wanataka mkate yeye anasema wapeni keki. Kwa hiyo, ninayo hayo mapendekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Menyekiti, tukiangalia pia hata katika suala la mafuta japo wengine wanasema kwamba ooh! bei haiwezi kupanda lakini haiwezi ikaenda bure kuna mahali watu watalipa zaidi au kwa kusafirisha mizigo au kwa usafiri wa kawaida na wataendelea kulipa, nasisitiza ile Sh.40/= ya mafuta ya taa iweze kuondolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache naomba Mheshimiwa Mpango achukue mawazo yangu kama kweli Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira ya kuwaondolea wananchi umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es Salaam ina wakazi takribani milioni tano na Wizara ilikuwa na azma ya kuimarisha Hospitali za Temeke, Ilala na Mwananyamala ili kusogeza huduma za kibingwa kwa jamii na kupunguza msongamano kwenye Hospiatli ya Rufaa ya Muhimbili. Lengo hilo la kuimarisha hospitali kwenye Wilaya hizo halijafanikiwa na hivyo msongamano wa wagonjwa umeendelea kuwa kero. Naishauri Serikali kuimarisha hospitali hizo ili kusogeza huduma kwa jamii na kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi kubwa ya kupeleka wataalam wa fani mbalimbali kwenye vituo vya afya na dispensaries, bado upungufu ni mkubwa na umeongezeka zaidi baada ya kufukuza watumishi wenye vyeti fake, wengi wao wakiwa wataalam wa afya. Ni muhimu sasa kwa Serikali kupeleka wataalam wa kutosha ili kupunguza ratio ya wagonjwa kwa wataalam wa afya. Kama WHO standard ni daktari 1:10,000 lakini kwa Tanzania ni daktari 1:25,000, uwiano huu ni mkubwa sana na inafanya madaktari kulipua kazi bila ya kutumia muda wa kutosha kumsikiliza mgonjwa, kumpa ushauri nasaha na mwishowe tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali itekeleze mkakati maalum wa kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na kuhakikisha wanapunguza kazi kwenye maeneo mbalimbali. Serikali ianzishe mkakati wa kutoa motisha kwa watumishi wanaopangwa maeneo magumu yasiyokuwa na miundombinu rafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hoja iliyoko mezani. Uamuzi wa Serikali wa kuachia TBA kujenga majengo yote ya Serikali na Serikali za Mitaa ni uamuzi usiokuwa na tija. Haiwezekani TBA ifanye BOQ halafu ijenge yenyewe kitendo hiki ni kinyume kabisa na utawala bora na ni kinyume na sera ya Serikali ya PPP katika ujenzi wa majengo ya Serikali au Serikali za Mitaa. TBA ingefanya kazi yake ya manager wa miradi ya ujenzi kwa niaba ya Serikali kuhakikisha value formoney na ubora wa majengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, TBA imezidiwa na miradi, wanashindwa kukamilisha miradi kwa muda na hata ubora wake kama ilivyotokea kwa ujenzi wa mabweni ya Chuo Kikuu. Ninashauri Serikali hili jambo litazamwe upya au kuhusisha sekta binafsi, sekta binafsi ndiyo engine of growth na ndivyo inavyotengeneza ajira kwa wingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uchukuzi, Serikali ina mradi mkubwa wa reli ya standard gauge. Mradi huo utawaajiri wataalam waliobobea katika nyanja mbalimbali. Katika wasilisho la Waziri wa Fedha na Mipango katika eneo la rasilimali watu idadi ya wanafunzi watakaopelekwa katika mafunzo kwa ajili ya mradi huu haijafahamishwa kinaga ubaga.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali/Waziri mwenye dhamana ya uchukuzi awasiliane na Waziri wa Elimu ili kuhakikisha idadi inakuwa kubwa, ikionesha kwa namba ya wanafunzi watakaopelekwa vyuo vikuu pamoja na vyuo vya ufundi ili kutayarisha rasilimali watu ya kutosha kwa ajili ya reli ya standard gauge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, Njombe kuna uwanja wa ndege ambao haujaendelezwa na upo karibu na makazi ya wananchi. Nahitaji majibu ya Serikali juu ya mipaka halisi ya uwanja wa ndege Njombe Mjini na nini hatua ya wananchi wenye makazi karibu na eneo la uwanja wa Njombe?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuchangia hoja iliyoko mezani. Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania limejijengea heshima kubwa ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, kwa miaka hii ya karibuni tumeshuhudia wanasiasa hasa viongozi wakijihusisha kwenye mambo ya siasa, kwa mfano, Kamisheni ya Kijeshi kupokea Madiwani waliohama chama; na Wanajeshi kuwepo barabarani kuogopesha wananchi wasiandamane ilhali jukumu hilo ni la Polisi.

Mheshimiwa Spika, kuna usemi, “vyombo vya ulinzi na usalama wakilinda dola, wanakuwa adui wa wananchi”. Jeshi letu lilijengewa heshima kubwa ya kulinda mipaka yetu, hivyo liepuke kwa nguvu zote kuhusishwa na mambo ya siasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Jeshi liangaliwe upya kwa makini ili kuepuka vijana watakaotia doa Jeshi la Wananchi. Baada ya kumaliza mafunzo ya JKT, kabla ya kuajiriwa wafanyiwe psychometric test ili kubaini vijana wenye tabia na maadili ambayo hayakidhi maadili na nidhamu ya Jeshi. Kwa kutumia tool hiyo, Jeshi litafanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa vijana wenye tabia mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia hoja iliyoko hapa mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote waliosema kwamba kwa kweli elimu yetu inaendelea kushuka sana na elimu hii imeshuka kwa sababu kadhaa; na pia tumeshuhudia walimu wakuu wakifukuzwa kazi, walimu wakuu wakishushwa vyeo kwa sababu shule zao zimefanya vibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tunaita kwenye taaluma ya management services tunaita blame culture. Blame culture ni utamaduni ambao unatafuta mchawi. Jambo limeharibika unamtafuta mchawi wa kumbebesha huo mzigo kwamba yeye ndiyo amesababisha bila kuangalia ni sababu zipi zimefanya hizi shule zisiweze kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ziko nyingi, sababu moja ya kwanza ambayo naiona mimi kubwa sana ni mfumo ambao kila Waziri anayekuja anakuja na ajenda yake. Tulianza kuona shule zile za mchepuo agriculture na biashara zikaondolewa, akaja mwingine kaondoa michezo, kaja mwingine ka-introduce GPA, amekuja wa sasa amerudisha division, curricular zinabadilishwa kabla walimu hawajazifahamu vizuri, zimebadilishwa. Kwa hiyo kuna mambo mengi ambayo yanasababisha shule zetu zisiweze kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napendekeza kwamba sasa tuiombe Serikali iweke mfumo ambao utazuia Mawaziri wa Elimu kubadilisha mitaala, kubadilisha mifumo ya elimu bila ya kupata majadiliano na tukakubaliana elimu yetu iwe vipi na isiwe rahisi kwa Waziri tu anaamka asubuhi, anabadilisha mitaala au anabadilisha mfumo wa elimu, hilo ndiyo pendekezo langu la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuungana na marais wale wawili Mheshimiwa Mkapa na Mheshimiwa Kikwete waliosema tunahitaji mjadala mpana kuhusu elimu yetu kwa sababu kwa kweli elimu yetu haiko vizuri. Kwa hiyo, nashauri Serikali huo mjadala uweze kufanyika ili tuweze kuamua elimu yetu tunayoitaka ipi ambayo itatupeleka kwenye Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri pia Serikali juu ya mazingira ya kufundishia kwamba si mazuri, tukianzia na walimu. Walimu wote tunajua malimbikizo yao hawalipwi, hawapandishwi vyeo na hata mazingira ya kufundisha hayapo mazuri, msongamano wa wanafunzi madarasani, hizo ni changamoto kubwa ambazo zinaathiri elimu yetu hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, motisha ya walimu; tukiangalia statistics za BEST zinasema walimu 35 tu ndio ambao wana motisha, wakati walimu 63 hawana motisha ya kufanya kazi. Kwa hiyo, ili tuweze kupata elimu bora kwa kweli rasilimali watu ya walimu ingekuwa ndicho kitu cha kwanza kabisa kwa ajili ya kuwapa motisha waweze kupata moyo, waweze kufundisha, waweze kuwekwa kwenye mazingira mazuri na elimu yetu itaweza kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuangalia mnyororo wa elimu kwa ajili ya Tanzania ya Viwanda. Nimeangalia taarifa ya Mheshimiwa Waziri na bado sijaona kwa mfano katika admission au usajili wa wanafunzi hasa katika sayansi sijaona ni pool gani kubwa ambayo tumesema tutawasajili au tutaweka kwenye vyuo waweze kukidhi yale matakwa ya Tanzania ya Viwanda. Nimeona kwenye VETA tunaongeza wanafunzi 200,000 mpaka 250,000 na nikawa najiuliza, je, hawa 200,000 mpaka 250,000 ndio ambao tumewa-target kwa ajili ya Tanzania yetu ya viwanda? Maana ni muhimu kuinyambua na kujua ni skills zipi ambazo tutazihitaji kwa ajili ya shughuli zote za viwanda kwa Tanzania yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia pia katika taarifa ya Mheshimiwa Mpango ambaye alitaja baadhi ya madaktari sijui ma-engineer na nini, lakini tunahitaji kunyambua na kujua. Kwa mfano tungeweza kuona katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri ni pool gani kubwa ambayo tutakwenda kuisomesha kwa ajili ya Tanzania ya viwanda. Bado sijaona na ninapendekeza sana Mheshimiwa Waziri ajipange kusudi hata ile pool ya sayansi na teknolojia ikidhi yale mahitaji ya Tanzania yetu ya viwanda, kwa sababu bila hivyo tutajikuta tumekuwa na viwanda, tumekuwa sijui na Stieglers, tumekuwa na reli lakini hatuna pool kubwa ya wataalam…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kupata nafasi hii kuchangia hoja iliyopo mezani. Pamoja na kwamba kilimo ndicho kinachotoa ajira kubwa kwa Tanzania, bado bajeti inayotengwa kwa eneo hili ni ndogo sana. Hivyo ili kuleta mapinduzi ya kilimo mambo yafuatayo yazingatiwe:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itenge bajeti ya kutosha, Maafisa Ugani wapewe motisha kama pikipiki na watawanywe kwenye vijiji vyote, wakipewa malengo ambayo yatatumika kupima utendaji wao wa kazi. Uwepo mfumo unaoainisha kila Afisa Ugani anahudumia idadi gani ya wakulima wawe na majadala kwa kila mkulima na kufuatilia maendeleo yao, kama ilivyo kwa madaktari kwa uwiano wa daktari mmoja kwa wagonjwa10,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo uhusiano wa karibu kati ya Wizara ya Kilimo inayotoa sera na kusimamia kilimo, taasisi za mafunzo kama SUA na taasisi zingine za utafiti. Tafiti bora kwa mazao zifikishwe sasa kwa wakulima kwa mafunzo na mashamba darasa. Nchi zilizofanikiwa kwenye mapinduzi ya kijani, Serikali kupitia Wizara iligharamia mafunzo ya wakulima kwenye taasisi za utafiti ili kuhakikisha wakulima wanajifunza mbinu mpya za kilimo cha mazao mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mafunzo mashamba darasa huanzishwa kwenye vijiji ikisimamiwa na Maafisa Ugani, mashamba haya ndiyo hutumika kusambaza teknolojia ya uzalishaji kwa makundi mengi ya wakulima wadogo wadogo. Ni muhimu hii Wizara ya Kilimo ikapata msimamo wa Wizara ya Viwanda kujua ili viwanda gani vinavyozungumziwa ili Wizara ya Kilimo ijikite kwenye kilimo cha mazao ambayo yatahitajika kwenye viwanda vinavyoanzishwa. Uratibu wa Wizara zinazohusiana ni muhimu kuepuka mkanganyiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inapita katika kipindi kigumu sana kwa ongezeko la uhalifu hasa dhidi ya haki za binadamu. Yamekuwepo matukio mengi ya watu kutekwa, kupotezwa, kuuwawa na miili yao kuopolewa kutoka baharini na kwenye mito. Taharuki ni kubwa kwamba watu hawa wasiojulikana hawatambuliwi wala kukamatwa na vyombo vyetu vya usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya matukio makubwa ni kama la Mheshimiwa Lissu kumiminiwa risasi hadi leo hakuna hata mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa. Kibaya zaidi matukio haya yote yanayowapata wananchi hakuna hata siku moja mkuu wa nchi au Waziri wa Mambo ya Ndani amejitokeza na kuzungumza na wananchi kuhusu matatizo hayo na kuwapa a sense of comfort kuhusu usalama wao na mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda muafaka sasa kwa kiongozi wa juu kuzungumza na wananchi kuhusu usalama wa nchi. Ili haki ionekane kutendeka wananchi wapate taarifa mara kwa mara kuhusu kukamatwa kwa watu hao wasiojulikana wanaoharibu taswira ya Jeshi la Polisi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na mhimili wa Mahakama wawaachie wafungwa, mahabusu wanaotuhumiwa kwa makosa madogo madogo yanayodhaminika watumikie kifungo cha nje. Kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza msongamano mkubwa kwenye magereza na kupunguza gharama na kuepuka magonjwa ya maambukizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto liwezeshwe kwa kupatiwa rasilimali ya kutosha kama watumishi na zana za kazi ili kuwawezesha kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye Wizara, taasisi, majengo ya biashara na huduma kudhibiti majanga ya moto ambayo siku hizi yamekuwa yanatokea mara kwa mara. Kinga ni bora kuliko tiba, kuzuia majanga ya moto ni jambo muhimu sana kama hatua ya kulinda usalama wa wananchi na mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha maoni yangu kwa maandishi kuhusu hoja ya Waziri Mkuu. Awamu hii ya Tano, hali ya kisiasa si shwari sana kama tunavyoaminishwa. Utamaduni ulioanza kujengeka wa kubana Vyama vya Upinzani visishiriki siasa kwa uhuru kwa kusingizia taarifa za kiintelejinsia ilhali Chama Tawala wanaandama, wanaitisha mikutano ya ndani bila shida yoyote. Nia hii ovu ya double standard inachochea uvunjifu wa amani na kujenga chuki kubwa baina ya Chama Tawala na Vyama vya Upinzani, kinyume kabisa na maono na kazi kubwa aliyoifanya Baba wa Taifa kujenga mshikamano wa Kitaifa kwamba sisi wote ni ndugu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamata Wapinzani na raia na kuwajaza mahabusu kwa uonevu na kuwanyima dhamana ni hatari kwa amani na usalama wa nchi. Wizara husika ihakikishe kesi za mahabusu zinasikilizwa na haki kutendeka kwa kuachiwa kwa dhamana au kuhukumiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ushiriki wa sekta binafsi. Mimi nilikuwa Kiongozi aliyesimamia reforms Serikalini na katika reforms hizo ni dhana ya Public Private Partnership (PPP) kwa masikitiko makubwa nimeona jinsi dhana hii ya PPP ilivyoachwa kabisa. Miradi mingi ya ujenzi wa majengo ya Serikali wanapewa taasisi za Serikali, ni kama kutoa fedha kutoka mfuko wa kulia na kuhamisha mfuko wa kushoto kwenye suruali hiyo hiyo. Matokeo yake sekta binafsi imesinyaa, Serikali inasahau kwamba sekta binafsi inaposhamiri ndiyo inatoa ajira kwa wingi kuliko Serikali. Serikali isishangae kuona vijana wengi wasio na ajira, hii Serikali ya Awamu ya Tano ndiyo inayosababisha. Serikali ya Awamu ya Tano irejee kwenye Blueprint ya Awamu zingine na kuziendeleza, vinginevyo tutakuwa tunarudi nyuma kila Serikali mpya inapoingia madarakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kunipa fursa hii ili nitoe mchango wangu kwenye eneo hili la mazingira. Utunzaji wa mazingira ni muhimu sana kwa uhai wa binadamu. Utunzaji wa misitu, vyanzo vya maji, usafi wa mazingira ni sehemu ya uhai wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita zaidi kwenye utunzaji wa misitu kwa sababu ndiyo chanzo kikubwa kinachovuta mvua, hivyo kupata maji ya mvua kwa ajili ya kilimo na vilevile maji kwenye mito, maziwa kwa ajili ya ustawi wa jamii. Bado Serikali haijawekeza vya kutosha katika utunzaji wake. Tumeshuhudia misitu ambayo imetunzwa kwa muda mrefu ikikatwa kiholela. Tumeshuhudia makazi yakijengwa au shughuli za kibinadamu katika misitu mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wananchi wengi bado wanatumia nishati ya kuni na mkaa kwa matumizi ya nyumbani, ni kweli pia kwamba uchomaji mkaa umekuwa changamoto kubwa katika kuteketeza misitu na watumiaji wengi wa mkaa wanaishi mjini. Ni kwa nini sasa Serikali hii ya Awamu ya Tano isifanye maamuzi magumu kwa kutoa ruzuku kwenye mitungi ya gasi iliyojazana mjini ili kuwezesha watumiaji wengi waweze kununua mitungi hiyo kwa bei nafuu sana na kuachana na matumzi ya mkaa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna usambazaji wa gesi asilia kwa baadhi ya makazi na viwanda mbalimbali lakini zoezi hili ni la muda mrefu sana mpaka kuja kusambaa eneo kubwa la nchi. Utatuzi wa haraka wa kuinusuru misitu yetu na vyanzo vya maji ni matumizi ya mitungi ya gesi ya majumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kwamba Serikali itachukua hatua ili kunusuru mazingira na uhai wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mweyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ambazo ziko hapo mezani. Kwanza nichukue nafasi kuwapongeza Mawaziri wote wawili na Naibu Mawaziri wao na watendaji wote walioifanya hii kazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na tamko ambalo lilitolewa na Mheshimiwa Waziri wa Ofisi ya Rais, Utumishi kuhusu kurudishwa kwa wale watumishi waliomaliza darasa la saba ambao walikuwa wamefukuzwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe masikitiko yangu kwamba tangu awali hawa watumishi hawakutakiwa kufukuzwa kazi, kwasababu waliajiriwa kwa kigezo cha darasa la saba na mikataba yao ilikuwa ya darasa la saba. Kwa hiyo, hawakustahili kufukuzwa kazi na kwa kweli hiyo haikuwa sahihi na Serikali haikuwa sahihi. Sasa wamerudishwa kazini, tukumbuke wamekuwa nje ya utumishi wa umma karibu mwaka mzima, imesababisha familia hizi kupata matatizo ya kifedha, manyanyaso na kutokuwa na income. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua, pamoja na kwamba Serikali imesema walipe mishahara yao yote, lakini je, katika ule usumbufu ambao wameupata kwa muda mrefu karibu mwaka mzima, Serikali inasema nini kuhusu hilo la kuwafidia kwa sababu ya kupata shida kwa kukosa kazi wakati walistahili kuwepo kazini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala linalofuata ninalotaka kuchangia, ndiyo wote ambao walikuwa na vyeti vya darasa la saba wamerudishwa, lakini kuna wale madereva kwa mfano ambao walikuwa darasa la saba na hawakutolewa kazini, lakini kuna madereva ambao walikuwepo kabla ya Mei, 2004 lakini kwa sababu ya shinikizo la kupata vyeti, baadaye walikwenda wakapata vile vyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa tamko la Mheshimiwa Waziri ni kwamba wale wote ambao waliajiriwa kabla ya hiyo Mei, 2004 kile kigezo cha form four hakiwahusu. Kwa hiyo, wanatakiwa wote warudishwe. Napenda kujua, sasa hawa madereva kwa mfano, ambao walikuwepo kabla ya Mei, 2004 lakini baadae ikabidi watafute vyeti, kwa sababu wengine wakwenda kujaribu form four, wameshindwa, wakaenda kutafuta vyeti. Je, wanarudi pia? Naomba Mheshimiwa Waziri alitolee tamko kwa sababu sijaiona kama ameizungumzia katika tamko lake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusu hawa walioanza kazi baada ya Mei, 2004, ni kweli wameingia kwa vigezo ambavyo siyo sahihi, wamegushi vyeti ambayo kisheria siyo sawasawa, nasi hatuungi mkono, lakini pia ukitazama kwa upande mwingine, wamekuwa wanachangia kodi, NSSF, wengine ni PSPF, wengine ni Local Government Provided Fund (LGPF); je, Serikali inatoa kauli gani kuona kwamba hawa watumishi kweli pamoja na kwamba wame-forge vyeti ambayo sio sahihi, lakini pia wamekuwa wanakatwa kodi, wamekuwa wanachangia hifadhi ya jamii? Je, Serikali haioni ni sahihi basi kwa hawa watumishi angalau walipwe basi makato yao ya hifadhi ya jamii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipokuwa akijibu swali langu la nyongeza, alieleza kwamba kulikuwa na majadiliano kati ya Serikali na Vyama wa Wafanyakazi kuhusu jinsi gani ya kufanya ubinadamu kwa ajili ya ku-compensate hawa ambao wamefukuzwa kazi kwa makosa ya kughushi vyeti. Napenda kujua hayo majadiliano yamefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo pia watumishi ambao wametumia majina ya watu wengine kusoma, wengine wamepata udaktari, wengine wamemaliza u-nurse, wengine wamefanya ualimu; wamesoma hizo courses na wamehitimu, lakini kwa majina ya watu wengine. Napenda kusikia tamko la Mheshimiwa Waziri anasema nini juu ya watu hao? Kwa sababu tunao watu ambao wamesoma kwa maina ya watu wengine na ni watu wakubwa na wako kazini, kusiwepo na double standard. Lazima Serikali ionekane inatenda haki kwa watu wote bila ubaguzi wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja sasa kwenye suala la watumishi wa umma kutofungamana na itikadi za kisiasa. Hili jambo nilishalizungumzia siyo mara moja, wala mara mbili na ninaendelea kulizungumza. Labda ni-declare interest kwa sababu mimi mwenyewe nilikuwa mtumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa na watumishi ambao wanafungamana na itikadi, kuwa na watumishi ambao wakiwa katika utumishi wa umma wanajihusisha na mambo ya siasa kunadidimiza impartiality ya utumishi wa umma, inaua professionalism. Tunataka utumishi wa umma wafanye kazi zao kwa kuzingataia professions zao kwa ajili ya kuendeleza Taifa hili na kuleta maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari za watumishi wa umma kujiingiza katika siasa ni kukosa continuity katika utumishi wa umma. Kwa sababu utumishi wa umma ndiyo institutional memory ya nchi. Ikiwa tunakuwa na watumishi katika ngazi za juu ambao wanaletwa wakiwa kwenye Vyama vya Siasa inaharibu kabisa integrity ya utumishi wa umma. Tunaona mahali kama Japan, kila mara Mawaziri Wakuu wanaondoka, wanakuja, lakini utumishi wa umma unakuwa intact kwa sababu hauhusiani na chama chochote. Utumishi wa umma unatakiwa utekeleze sera za chama kilichoko madarakani with impartiality. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mtindo wa sasa hivi wa Awamu ya Tano ya kuingiza watu wenye mambo ya siasa kwenye utumishi wa umma, tunaua hiyo integrity na tuta-suffer kama nchi na itabidi kuja kufanya marekebisho makubwa sana. Kwa hiyo, ni maoni yetu kwamba Serikali sasa iangalie upya na turudi tulikotoka. Enzi zetu watumishi wa umma walikuwa hawaruhusiwi kujihusisha na siasa kabisa wanapokuwa watumishi wa umma. Wakitaka kujihusisha na siasa, watoke katika utumishi wa umma waende wakahangaike na siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la nyongeza za mishahara na kupandishwa vyeo. Watumishi wa umma ndio engine of growth ya nchi hii. Awamu hii ya Tano sioni kabisa kama Serikali iko serious na kuangalia rasilimali watu. Naona haiko serious kwa sababu tangu wameingia madarakani watumishi wa umma hawapati nyongeza zao za mshahara ambayo ni haki yao; hawapandishwi ngazi zao za mishahara, malimbikizo yao bado hayalipwi yakamalizika, kila siku ni hivyo hivyo na maneno mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila ya kuwa na Utumishi wa Umma wenye raha unaojiamini, kwa kweli hata hii dhana ya Tanzania ya Viwanda hatuwezi kuifikia. Kwa hiyo, naishauri Serikali, kwa kweli iweze kuangalia rasilimali watu, watumishi wapandishwe vyeo vyao, wapate increments zao ambazo wanastahili kwa sababu hizo increments za kila mwaka ndiyo zinawasaidia kupunguza makali ya inflation katika uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja kwenye suala la elimu. Sijaona kama kuna mnyororo mzuri. Tunazungumzia viwanda, ni jambo zuri; tunazungumzia standard gauge; tunazungumzia Stigler’s Gorge; lakini hatuzungumzii rasilimali watu ambayo itakuja kufanya hizo shughuli. Nikiangalia kwenye mnyororo wa elimu na nimesikia kwamba Serikali ina-train walimu wengi wa sayansi na teknolojia, ni jambo zuri. Kama Serikali ina-train walimu wa sayansi na teknolojia, ni mkakati gani basi unawekwa kuhakikisha kwamba maabara katika shule za sekondari zinakuwepo kusudi hawa Walimu wanapotoka kufundishwa sayansi na teknolojia, waende hata kwa vitendo kwenye laboratories katika vyuo vyetu. Kwa sababu malengo yote ya sayansi na teknolojia ndiyo ambayo inakuwa complement katika hiyo Tanzania ya viwanda. Huu mnyororo uendelee mpaka chuo kikuu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Nianze kwa kumpongeza Waziri wa TAMISEMI pamoja na Naibu wake. Mheshimiwa Waziri ninachoweza kusema kuhusu yeye ni kusema tu yeye ni mzalendo. Vile vile nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipa Wizara yake Katibu Mkuu mahiri, Mzee wetu Iyombe pamoja na wasaidizi wake ambao wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nianze kwa kuishukuru Serikali kwa niaba ya watu wa Siha kwa ajili ya shilingi bilioni 52 za barabara, shilingi bilioni mbili kwa ajili ya hospitali ya wilaya, shilingi milioni 700 kwa ajili ya Zahanati ya Umakiwaru, shilingi milioni 680 kwa ajili ya kumalizia miradi ambayo ilikuwa haijamaliziwa, shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya maji na shilingi milioni 931 kwa ajili ya daraja. Hiyo nimesema ili watu wajue kwamba watu wa Siha hawakukurupuka, walijua wanafanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watu wetu mwaka huu wameotesha kuanzia mwezi wa Nne na wengine sasa wanalima kwa juhudi sana kwa ajili ya kuzalisha. Kama watu wetu wanafanya hivyo ni muhimu sana Wizara husika kuanzia sasa kwa sababu tunataka tunyanyue uchumi wa watu wetu basi waanze kutafakari ni namna gani kilimo ambacho wanakifanya watu wetu sasa hivi kitakuwa na tija watakapofikia wakati wa mavuno. Kwa sababu imekuwa ni utaratibu wa kawaida kwamba inapofika wakati wa mavuno na mauzo mahindi yanafungwa na mipaka inafungwa ili wasiuze nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tutafakari namna mpya ya kufanya hilo kwa sababu kwa muda mrefu unaweza ukafikiri unadhibiti mfumuko wa bei kwa kuzuia mahindi yasiende nje, lakini kwa muda mwingine unaweza ukasababisha wananchi wakaacha kuzalisha mazao ya chakula wakaanza kuzalisha mazao mbadala. Matokeo yake hata ile bei ya mazao tuliyofikiri tunaidhibiti ikapanda na ikawa tu umefanya kazi ya muda mfupi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile soko la mbaazi. Nafikiri ni mapema sasa tuanze kushughulika na soko la mbaazi. Tumeambiwa kwamba nchi ya India ndiyo imekuwa ikinunua mazao yetu ya mbaazi, ni vizuri kwa sababu na sisi tunanunua dawa kutoka kwao tuanze kuzungumza sisi tunachukua dawa kwenu nyingi kwa ajili ya watu wetu na nyie mnachukuaje mbaazi yetu na tunaanza kujadili kuanzia hapo ili tuweze kufanya biashara yenye tija kwa ajili ya wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye Wilaya yangu ya Siha kuna ardhi kubwa sana, kuna ardhi ya NARCO zaidi ya heka 56,000 na ya TALIRI zaidi ya heka 14,000. TALIRI na NARCO wana ng’ombe kidogo sana na TALIRI wanafanya research ya mifugo bora lakini utaona NARCO wanataka kufuga mifugo waanze kuwa wachungaji. Nashauri TALIRI wafanye research ya mifugo na wazalishe mifugo mizuri sana, NARCO wafuge hiyo mifugo lakini wajenge kiwanda ndani ya NARCO na ile mifugo mizuri wapewe wafugaji wetu waweze kuzalisha mifugo na kiwanda ambacho kitakuwa pale Siha kiweze kutumika kwa ajili ya kuvuna hiyo mifugo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niende kwenye eneo la utawala bora. Nimesikia rafiki zangu wengi wamekuwa wakiongea na kukosoa kuhusu utawala bora, lakini utawala bora unaanzia kwenye nyumba yako. Namshukuru rafiki yangu Mheshimiwa Lusinde leo ameanza vizuri kwenye kuelezea eneo moja lakini nimesikia habari moja ikisema kwamba Mheshimiwa Lusinde hajasoma kitabu kizima. Naomba nitoe mifano ambayo haihitaji usome kitabu kizima ili uelewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge walioko hapa kuna Wabunge wanachangishwa zaidi ya Sh.500,000/= na wengine wanachangishwa zaidi ya Sh.1,500,000/= na ukipiga hesabu kwa mwezi mmoja ni zaidi ya Sh.73,000,000/= kwa mwaka mzima ni zaidi ya Sh.876,000,000/=. Nilisema juzi kidogo kelele nyingi zikapigwa lakini nikawa najiuliza Wabunge hawa leo wanakosa nafasi ya kufanya siasa kwenye Bunge hili kwa sababu imekosekana kuajiriwa tu wafanyakazi wanne lakini Wabunge hawa wamechumwa zaidi ya shilingi milioni 876. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua umuhimu wa wao kuhitaji watumishi hao…

TAARIFA . . .

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakubali kabisa sihitajiki kuingilia mipango ya chama chochote, lakini ukweli tu ni mmoja kwamba ni logic ya kawaida kama unapata milioni isiyozidi 460 kwa mwezi na unashindwa hata kuweka programu ya ndani ya nyumba yako vizuri…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizomea na wengine wakipiga makofi)

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu unamtaka Dokta Mollel apambane na wewe ili uweze kutimiza azma yako ya …

(Hapa baadhi ya Wabunge walizomea na wengine walipiga makofi)

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, unataka Dokta Mollel ashirikiane na wewe ili muweze kumiliki Benki Kuu, wazalendo kama sisi hatuwezi kuwakabidhi Benki Kuu kama milioni 400 hamuwezi kusimamia. (Makofi)

Mwenyekiti, lakini nimwambie dada yangu kwamba mimi namtetea kwa sababu Wabunge wa Majimbo wanachangishwa Sh.500,000/= na Viti Maalum wanachangishwa Sh.1,500,000/=

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme hapa tunazungumzia suala la utawala bora na watu wamekuwa wakitoka mapovu kwa ajili ya kujitahidi kuonesha kwamba Serikali iliyoko madarakani imeshindwa kujipanga na kuendesha mambo na wakijionesha kwamba wao ni Serikali inayotakiwa kuja kuwa Serikali mbadala kwa ajili ya nchi hii, lakini imeshindwa kusimamia milioni hizo nilizozitaja, basi kuna sababu kubwa ya kusema Watanzania wasiwaamini na hawana uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukafikiri shilingi bilioni mbili alizozitaja Mheshimiwa Lusinde hapa ni nyingi, ni nyingi kuliko zilizoko Serikalini kwa sababu ndiyo hela pekee walizokuwanazo. Kwa hiyo, hela 100% zimeenda mikono…

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuzungumzia suala la usalama. Vilevile limekuwa likizungumzwa suala la usalama kwenye Bunge hili, usalama sio suala la tu la vyombo vyetu vya usalama peke yake vilevile ni suala la watu wote na viongozi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kuna kikundi kidogo ambacho kimekuwa kiki-remote watu ambao wanapiga kelele hapa wasiojua wanachokifanya baada ya mirija yao kufungwa na wamekuwa wakitaka ku-propagate kwamba kuna usalama na wao wenyewe wakitumia…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizomea na wengine walipiga makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja iliyoko mezani na moja kwa moja ninaunga mkono maoni ya Kambi ya Upinzani ambayo yametolewa vizuri sana na Mheshimiwa Halima Mdee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana katika ule mpango ulioletwa nilizungumzia sana suala la rasilimali watu na katika ule mpango wa mwaka jana iliahidiwa kwamba shughuli zilizopangwa ni kusomesha wataalam katika fani adimu za mafuta na gesi, madaktari bingwa katika nyanja za moyo, figo, ubongo nje ya nchi na katika vyuo vya ndani vya Muhimbili na Benjamin Mkapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika taarifa ya utekelezaji hakuna mahali popote katika taarifa ya utekelezaji ambayo imetupa takwimu ya hao wataalam ambao tumewapeleka au nje ya nchi au katika vyuo tulivyovitaja na takwimu ni muhimu kwa sababu hiyo ndio itaweza kutuwezesha kupima kama tumefanikiwa au hatujafanikiwa na nikiangalia pia katika taarifa ya utekelezaji taaluma tu ambayo wapelekwa nje ya nchi ilikuwa ni wana hewa 17 ambao nafikiri ni civil avitation na injinia mmoja ndio ambayo imeoneshwa katika vitabu hiki cha utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa yako hii ya mwaka huu kuhusu suala la rasilimali watu umesema kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, umesema maeneo watakayopewa kipaumbele ni elimu na ujuzi hususani kusomesha kwa wingi wataalam kwenye fani na ujuzi adimu, afya na ustawi wa jamii, maji na usafi wa mazingira, vijana, ajira na wenye ulemavu, habari, utamaduni na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni suiting statement ambayo ningetegemea kwamba katika ule mpango ambao kile kitabu cha mpango mwaka huu tungenyambua to unbundle na kusema katika hizi nyanja za mkakati tutakuwa na wataalam wangapi kwa kila eneo, kwa mfano tuna mkakati huo wa ndege za Serikali, tuna hizi bombadier, tuna Dream linear ambazo zinakuja zingine, lakini sijaona popote Mheshimiwa Mpango ambapo umeainisha kwa sababu marubani wengi ni wa nje hata Mheshimiwa Ndassa pia amelizungumzia hili ni lazima tuone kinagaubaga wataalam wangapi tutawa-train. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye suala la ma- technician kwa Air Tanzania hatuna ma-technician kwa hizi ndege mpya wengi ni kutoka nje, je, Serikali ina mpango gani kuhakiksha kwamba tunakuwa na hawa ma- technician ambao watakuja kusimamia hizi ndege ili tupunguze gharama za kuwa na hawa ma-technician kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo muhimu sana tuna reli hii ya SGR tutakuwa na locomotives za za kisasa, kwenye katika taarifa iliyotolewa taarifa ni kwamba technical education tunajaribu kuongeza enrolment tunajaribu kukarabati, lakini hatujasema kwamba kweli tuna business plans ya SGR tutahitaji wataalam wangapi na tunaweka mkakati gani wa kuweza kupeleka watu hawa kuwasomesha na tupate namba, tujue ni wangapi kufuatana business plan kusudi hata hiyo reli inapokwisha tunakuwa tayari tuna wataalam kwa ajili ya hiyo reli, tuna wataalam kwa ajili ya kuendesha hizo locomotives ambazo tunategemea zitakuwa za kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mpaka sasa hivi katika suala la rasilimali watu sijaona mkakati wowote wa Serikali ambao umewekwa kushughulikia rasilimaliwatu, kwenye bajeti ya mwaka jana hakuna bajeti ambayo nimeona kinagaubaga ya kuonesha kwamba imetolewa bajeti kiasi gani kwa ajili ya mafunzo ya hawa wataalam wa mkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye suala la viwanda, viwanda primary source ni kama walivyozungumza wengi ni kilimo, lakini tukiangalia bajeti ya kilimo mwaka juzi ilkuwa ni 2%, mwaka juzi ile ilikuwa 11% bado hatujaona ni jinsi gani Serikali kwa kweli iko na ari (commitment) ya kuhakikisha kwamba agriculture inahimarishwa ili iweze kutoa input kwenye viwanda ambavyo tunataka kuvitayarisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ningetegemea kuona katika mpango numbers za Maafisa Ugani ambao watahitajika kwa ajili ya viwanda, nilitegemea kuona katika mpango tuweke ratio kwa mfano kama tunavyofanya kwa madaktari, daktari mmoja wagonjwa 8000 au 10000, tuseme ratio Afisa Ugani mmoja anategemewa ahudumie wakulima wangapi na waweze kupimwa na waweze kufuatiliwa. Kwenye hili eneo bado kazi inahitaji kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja pia kwenye suala la sekta binafsi, inasikitisha mimi nilikuwepo kwenye reforms tulipoanzisha mambo ya PPP, lakini Serikali ya Awamu ya Tano imerudi kabisa kwenye suala la ushirikishwaji wa sekta binafsi tumeona miradi mikubwa yote badala ya kufanya sekta binafsi inafanya Serikali yenyewe, tumeona miradi kwenye Halmashauri zetu inafanya Serikali yenyewe, matokeo yake sekta binafsi imedorola, sekta binafsi ndio mwajiri mkubwa kwa hiyo watoto wetu na vijana wetu wanakosa ajira kwa sababu sekta binafsi imedorola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye uwekezaji mazingira ya uwekezaji hata kufuatana na takwimu za dunia Tanzania ni nchi ya 163 kwenye mazingira mazuri ya uwekezaji Botswana wametushinda 86, Kenya 61. Ukija kwenye urahisi wa kufanya biashara Tanzania tuko 137, Kenya wako 80, Rwanda wako 41, tukija kwenye ada za usajili za wawekezaji kuanzisha biashara Tanzania ni dola za Marekani 250, Kenya 40, Rwanda ni 35; kwa takwimu hizi sekta binafsi haitaweza kufanikiwa kwa sababu watu watashindwa kuja kuwekeza na watakwenda kwenye nchi nyingine. Kwa hiyo, nashauri Mheshimiwa Mpango na wataalam wake waendelee kuona ni jinsi gani mazingira ya uwekezaji yataborehswa ili ku-attract wawekezaji wa ndani na nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nizungumzie sasa kidogo mimi kama Waziri kivuli wa utawala bora. Utawala bora ni kichocheo kikubwa sana cha kuleta wawekezaji na unapokuwa na viongozi ambao wanatoa kauli ambazo zinakimbiza wawekezaji, viongozi wanaotoa kauli ambazo zinakinzana hata na sera na matamko ya Serikali na bila kuchukuliwa hatua zozote hii yenyewe inatosha kuwakimbiza wawekezaji wasiweze kuja kuwekeza ndani ya nchi. Kiongozi yeyote hana maoni binafsi, kiongozi anapozungumza anazungumza kwa niaba ya Serikali ni lazima matamko yake yasikinzane na matamshi ya Serikali, matamko ya Serikali na sera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyoko mezani. Naomba ku-declare interest kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na naunga mkono moja kwa moja hoja iliyowasilishwa hapa mezani. Nitazungumzia maeneo matatu, nitazungumzia suala la Magereza, economic diplomacy na diaspora.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwenye Kamati kwamba Magereza yetu yana msongamano mkubwa sana na ilipofika Desemba, 2018 Gereza la Segerea lina wanaume 1,723, lakini wafungwa ni 158 tu wafungwa, kwa hiyo walioko rumande ni 1,565. Wanawake wako 313 na waliofungwa ni 66, kwa hiyo rumande wako 247. Kwa hiyo tuseme jumla pale Segerea kuna Mahabusu 1,812. Hii ni namba kubwa sana kwa watu ambao wako Mahabusu, upelelezi unaendelea haujakamilika, wako Mahabusu wanatumia pesa za walipakodi kula, wako Mahabusu badala ya kuweko uraiani wakifanya kazi na kuongeza juhudi za kusukuma gurudumu la maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna haja kubwa sana sasa Serikali ya Awamu ya Tano kuangalia mfumo wa kutoa haki, ukianzia na TAKUKURU, ukija na DPP mpaka na Polisi kuhakikisha kwamba upelelezi unafanyika kwa wakati kusudi hawa Mahabusu waweze kuhukumiwa watoke, kwa sababu wanapoendelea kukaa Mahabusu huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu na si sahihi na hata Mungu hapendi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napendekeza kwamba upelelezi ukamilike kwanza kabla ya kupeleka watu Mahakamani, wapelekwe upelelezi ukiwa umekamilika, kesi inasikilizwa, wanatoka na endapo kuna umuhimu wa kumweka mtu Mahabusu, tunayo best practice Zanzibar ambapo Zanzibar unakaa Mahabusu tu miezi tisa kama upelelezi haujakamilika unaachiwa huru. Kwa hiyo, hili jambo ni jambo la kufanyia kazi na namshauri sana Mheshimiwa Waziri, liweze kufanyiwa kazi…

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Kabisa ili haki iweze kutendeka….

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ruth Mollel kuna taarifa, Mheshimiwa Mchengerwa.

T A A R I F A

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siipokei hiyo taarifa, naomba aende Segerea, aende Keko akaangalie halafu aje na data hapa. Watu wanakaa mpaka miaka mine, miaka sita upelelezi unaendelea, hiyo siyo sahihi, hata mbele ya Mungu si sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hizi kesi zingine ambazo pia zinakalisha sana watu Magerezani, ni hizi kesi za utakatishaji fedha. Nashauri Serikali ya Awamu ya Tano iangalie tena hii sheria kwa sababu watu wabaya wanaweza kutumia huu mwanya kubambikizia watu kesi za utakatishaji pesa kwa makusudi, kusudi waweze kuendelea kukaa upelelezi unaendelea miaka na miaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo liweze kuangaliwa na kufanyiwa kazi, tukienda kwenye suala hili maana yake tunasema kwamba kama ikiwa watu wanakaa muda mrefu, kesi zao hazisikilizwi, upelelezi unaendelea, tunasema justice delayed is justice denied. Kwa hiyo mtu hajapewa nafasi ya kusikilizwa na saa nyingine anaachiwa hata kufidiwa hafidiwi, anakuwa amepoteza miaka yake jela, mahabusu, amepoteza watoto, amepoteza mke na kila kitu. Kwa hiyo hilo lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja pia kwenye suala la economic diplomacy. Kwa trend ya hivi karibuni hata kwa miaka mingi Ubalozi inakuwa kama ni zawadi au ni adhabu unasukumwa ukakae huko usionekane. Inabidi sasa kubadilisha huu utaratibu kusudi Ubalozi uwe ni shughuli ambayo mtu anakwenda kuifanya na waweze kupata elimu either trade au marketing au uwezeshaji kusudi wanapokwenda kule kwenye zile Balozi waende na utaalam ambao watakwenda kuutumia kutafuta miradi, fursa na mitaji kwa ajili ya kuiendeleza nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tumesikia Dokta mmoja anapelekwa Cuba, huyu ni mtaalam mzuri sana nafikiri wa anesthesia anajua economic diplomacy ni kitu gani? Atakwenda kufanya nini kule? Kwa hiyo, inabidi watu wapate elimu waweze kujua wanapokwenda kule siyo kugonganisha glass za wine, ni kutafuta fursa, fedha na mitaji kwa ajili ya nchi hii. (Makofi)

MHE. DKT. SUSAN A. KOLIMBA: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ruth Mollel, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Susan Kolimba.

T A A R I F A

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Utumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee. Pia katika kupeleka Mabalozi nje ya nchi kuwepo na vigezo vya kuweza kupima utendaji wao wa kazi na upimaji wao utakuwa ni kuweza kuleta mitaji, fursa za biashara na wale ambao wanashindwa warudishwe…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napendekeza katika ku-strengthen hii carrier ya diplomats katika mambo ya economic diplomacy hata mitaala ya Chuo Kikuu ya Political Science na International Relations iingizwe watu waweze kutoka kule wakijua kwamba sasa tunakwenda kuingia kwenye uchumi wa nchi na kuboresha maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani kulikuwa na Siku ya Mabalozi ambayo sidhani kama siku hizi ipo. Siku hii ilikuwa muhimu ambapo Mabalozi walikuwa wanakutana na kubadilishana uzoefu na kusaidia katika kutafuta mitaji kwa ajili ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala pia la Diaspora, tukubali kwamba tunao Watanzania wengi sana ambao wako nje ya nchi wanafanya kazi kule. Kulikuwa na ajenda ya kutengeneza kanzidata ya Diaspora, napenda Waziri atakapokuja kuzungumza hapa atuambie kwa mfano kule Diaspora tuna Watanzania wangapi. Kwa nini nasema hivyo?

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Taarifa.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu ni muhimu kwa ajili ya kuona ni jinsi gani ya kuwawezesha kuleta mitaji na pesa nyumbani ili kuongeza nguvu ya uchumi na kupunguza umasikini nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia katika nchi zingine, kwa mfano, kwa mujibu wa statistics za Benki ya Dunia, kwa mwaka Kenya wanaingiza 2 billion USD kwa mwaka kutoka Diaspora; Uganda wanaingiza 1.2 billion USD; Somalia wanaingiza 1.4 billion USD; Nigeria wanaingiza 21 billion USD, Tanzania tunaingiza ni milioni 456 USD. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia nami pia kwenye hii Wizara. Jambo kubwa ambalo napenda kulizungumzia ni kuhusu mikutano ambayo tunanyimwa kufanya, wakati kikatiba tunaruhusiwa kukusanyika na kukaa na kuzungumza mambo yetu kama vyama, lakini imekuwa ni vigumu kufanya hivyo kwa sababu tunazuiwa kufanya mikutano, hata mikutano ya ndani.

Mheshimiwa Spika, mimi ni Diwani wa Mkuranga, mwezi wa jana nilikuwa na kikao tume-book ukumbi kwa ajili ya kuwa na vikao vyetu vya chama kwa ajili ya kuchagua viongozi wa chama. Nimekwenda Mkuranga, polisi wamekwenda wamemtisha yule bwana mwenye hall pale Mkuranga, akakataa kutupa hall la kufanyia mkutano. Tukaondoka pale, tukaenda kwenye Ofisi za chama, tukakaa nje, lakini bado huwezi kuamini defender zimekuja zina-patrol, wana-patrol watu ambao tumekaa tunazungumza mambo yetu, hatuna silaha, hatuna kitu chochote, patrol inapita mpaka tumemaliza mkutano pale nje, tena nje ya Ofisi ya Chama, nikajiuliza yaani Tanzania tumefikia kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi tumekaa tunazungumza mambo yetu, hiyo petroli ya walipakodi inayozunguka na defender muda wote na maaskari wamejaa kwenye defender, ni sisi kweli wanatuchunga au wanatutisha. Nafikiri hapa tulipofikia si penyewe, tunataka tuirudie Tanzania yetu ambayo tulikuwa tunakaa, tunafanya mikutano yetu kama ni mikutano ya ndani ambayo imeruhusiwa, basi Mheshimiwa Waziri aje na kauli anapokuja kuhitimisha hoja yake atuambie kwanza ni sheria gani ambayo inatunyima sisi kuwa na vikao vyetu vya ndani, wakati chaguzi zinakuja ni lazima sisi kama chama tujipange kwa ajili ya kuingia kwenye chaguzi, tutajipangaje kama hata mikutano ya ndani wanatuzuia kuifanya. Naomba Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha hoja yake aweze kutuambia ni kanuni gani anayoitumia kutokuruhusu sisi kufanya vikao vyetu.

Mheshimiwa Spika, maandamano; maandamano ni namna moja ya wananchi kutoa…

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

SPIKA: Taarifa, pokea taarifa Mheshimiwa Ruth Mollel.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Ruth Mollel, kwanza mimi namheshimu sana na nafikiri kwamba yeye kwa fursa kubwa aliyoipata katika Jimbo langu la Mkuranga na namna ya kazi anayoshiriki kufanya pale, sikutegemea kama angeweza kuwa ni mmoja katika Wabunge wanalolishutumu Jeshi la Polisi. Nataka awe mkweli kwamba Mheshimiwa Ruth Mollel anafanya mikutano katika Kata ya Kitomondo amekutana na akinamama hadharani wala siyo mikutano ya ndani na anatoa vifaa na vitu mbalimbali. Amekwenda Kata ya Vikindu, amefanya mikutano, ametoa pesa misikitini, amefanyaje, hadharani wala siyo kwa kificho na Ofisi ya Chama cha CHADEMA Mkuranga haijawahi kuwepo. Sasa nadhani wakati Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani atakapo kuja kumjibu kwa kuwa anataka ayapate hayo anayoyaomba hapa, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, basi mpeni hiyo ladha ambayo anaitamani.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

SPIKA: Mheshimiwa Ruth Mollel taarifa hiyo.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, hiyo taarifa kwanza siipokei, kwanza kama Mbunge ni haki yangu kwenda kwenye huo Mkoa kuna kutoa msaada na vile vile kunizuia kufanya, hili jambo limetokea na ni lazima nitalisema kwamba walituzuia kufanya mkutano na defender zilikuwepo.

SPIKA: Kengele imelia kwa sababu ulikuwa umenani kidogo, nakuongezea dakika moja ili umalizie hicho cha mwisho.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nilikuwa nazungumzia suala la maandamano, kwamba watu wanapoandamana wanatoa hisia zao kwa sababu siyo kila mtu ana nafasi ya kumwona Rais, saa nyingine Rais haambiwi ukweli, lakini watu wanapoandamana kwa amani, wanatoa hisia zao kusudi Mheshimiwa Rais aweze kujua wananchi wake waliomteua na kumuweka madarakani wanamawazo gani na maeneo gani ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maandamano yaruhusiwe, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani atuambie ni kwa nini anazuia maandamano ya watu kutoa hisia zao. Wananchi wanahitaji kusimamiwa na kulindwa, waende waandamane kwa salama watoe hisia zao na hiyo ni namna mojawapo ya watu kutoa vitu ndani ya roho zao, ukiwafungia watu ndani yanakuwa matatizo makubwa sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya elimu kwa maandishi. Hospitali ya MUHAS Mloganzila ilianzishwa kwa madhumuni ya rufaa na pia, teaching hospital ilikuwa kujengwe hostel na nyumba za Madaktari na wataalam wengine, ili kuwezesha huduma kupatikana kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hii ya Mloganzila imeanza kutoa huduma, lakini Madaktari wanaotakiwa kutoa huduma wanasafiri kutoka makazi yao, wengine maeneo kama Mbagala kwa muda mrefu njiani mpaka Mloganzila. Watumishi hawa hawapewi msaada wowote kama petroli/ nauli kuwawezesha wafike kwenye kituo cha kazi. Matokeo yake ni kuwepo kwa upungufu mkubwa wa Madaktari na wataalam wengine wa afya. Ni muda muafaka sasa changamoto hiyo ya makazi ikapatiwa ufumbuzi na kwa muda huu wapatiwe nauli/mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Madaktari Bingwa waliofika miaka 65 wanapewa mikataba ya muda mfupi na wakati mwingine hata malipo yao yanasuasua na hawalipwi kwa wakati. Huu ni udhalilishaji wa wataalam wetu waliotumikia Taifa hili kwa muda mrefu. Wanafunzi wanaohitimu kwenye vyuo vikuu vya tiba, wengi wao hawana interest ya kufundisha, wengi wanakwenda kwenye public health na wengine nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha Madaktari Bingwa waliofikisha umri wa miaka 65 Wizara imeshindwa kuwatumia vizuri. Kwa nchi za wenzetu hawa ndio hazina kubwa ya Wahadhiri, wanafundisha mpaka uzeeni kabisa. Kwa sasa Madaktari Bingwa hawa wamehamia vyuo vya tiba binafsi/kanisa kama Bugando na KCMC, wengine wanakwenda nje ya nchi Botswana, Namibia, South Africa na kadhalika. Hivyo, muda si mrefu MUHAS itakuwa 3rd class teaching institution.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba, Wabunge wengi waliweka ukomo wa wataalam bingwa kuwa miaka 65, naishauri Serikali, ili kutumia hazina hii ya wataalam wapewe angalau mikataba ya miaka miwili-miwili na kulipwa gratuity kila wanapomaliza miaka yao miwili. Utakubaliana nami kwamba, umri wa kuishi umeongezeka, hivyo mtaalam bingwa wa miaka 65 bado ana nguvu kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii, nami niweze kuchangia katika itifaki hizi mbili. Moja, nitachangia ya solar energy na pia nitagusia kidogo kwenye hii ya PSMA ya FAO.

Mheshimiwa Spika, hii itifaki ya International Solar Alliances, tuliisaini mwaka 2015, tukiwa na ule Mkutano wa Climate Change, Paris, mwaka 2015 na sasa imeletwa turidhie. Tumeona kwamba baadhi ya nchi, kwa mfano India ambao pia waliridhia mkataba huu, wao wamefika mbali sana katika kutekeleza huu mkataba na kuanza kutumia energy hii ya solar ambayo ni muhimu sana; kwa sababu kwanza inafika vijijini, ambako energy nyingine ya umeme haifiki na vilevile ni energy ambayo ni safi kuliko tunavyoona kwenye energy nyingine ambazo zinaleta carbon monoxide katika mazingira.

Mheshimiwa Spika, sasa napendekeza kwamba, huu mkataba tumeusaini na ingekuwa ni vizuri vilevile kuhakikisha kwamba tunakuwa na mpango mkakati. Tumepitisha itifaki nyingi hapa na sijui Bunge lako Tukufu ni kwa jinsi gani linafuatilia hizi itifaki ambazo tunazipitisha hapa kuona kwamba zinatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, vilevile mradi huu utaongeza tija kwa wanavijiji na kuboresha maisha yao na kuwa na umeme wa kuwasaidia kuzalisha na kuongeza pato lao la nchi. Kwa hiyo, napendekeza kwamba, kuwepo na mpango mkakati na Waziri atueleze utakuwa vipi, ni kwa jinsi gani sasa, tuna solar energy na tuna REA? Tuone ni jinsi gani atajipanga, aweze kutekeleza hizi energy zote kwa pamoja; ya REA na Solar.

Mheshimiwa Spika, nitafurahi sana kama atakapokuja atatupa tu taarifa ni kwa jinsi gani hizi energy zote zitakwenda kwa pamoja? Kwa sababu tunajua REA nayo inakwenda vijijini na hii solar pia inakwenda vijijini; na solar ni rahisi zaidi kwa sababu haihitaji miundombinu mikubwa other than hizi solar panels na miundombinu mingine midogo midogo na jua tunalo kila siku. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri kwa mawazo yangu, itakuwa ni gharama nafuu zaidi kutekeleza hili la solar energy, sambamba na REA vilevile.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye suala ya ile itifaki nyingine ya kuzuia uvuvi haramu kwenye deep seas; ni vizuri tukaridhia huu mkataba, kwa sababu, kwanza kutakuwa na msaada, kwa sababu, bajeti yetu kama tunavyojua haikidhi mahitaji. Tutakuwa na bajeti ya msaada ambayo tutaitumia kwa ajili ya kujenga uwezo wa watu wetu na vilevile kulinda rasilimali yetu ambayo ni muhimu kama Wabunge wengine wengi walivyochangia. Siyo hivyo, kulinda rasilimali pia. Hata meli zinazokuja, zita-generate income ambayo itaingia katika mzunguko wa fedha.

Mheshimiwa Spika, tunajua jinsi ambavyo uvuvi haramu umekithiri. Kwa hiyo, kwa kuridhia huu mkataba, tutasaidia kulinda rasilimali zetu zisiweze kupotea na badala yake tuweze kupata fedha zika-generate revenue ambayo tutaweza kuendelea katika maisha yetu na kujenga uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, ninaipongeza Serikali kwa kuleta hizi itifaki hapa mbili tuziridhie na tuwe na monitoring system; hiyo ndiyo concern yangu kubwa. Tuna-monitor vipi sisi Bunge, kwamba hizi itifaki tunazopitisha hapa kila siku, zinafuatiliwa na zinafikia wapi? Maana yake, tunapimaje utekelezaji wa hizi itifaki? Ahsante. (Makofi)
Azimio la Kuridhia Itifaki ya Kinga na Maslahi ya Kidiplomasia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (The East Africa Community Protocol on Information and Communication Technology)
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi niweze kuchangia kidogo kwenye hii Protocol ya Afrika ya Mashariki. Maudhui yameshazungumzwa kwamba nini maudhui ya Itifaki hiyo, ninayo maeneo ambayo ningependa kupata ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutatua migogoro tumesema tutaridhiana na kuzungumza na kama ikishindikana tunakwenda Mahakama Kuu ya Afrika Mashariki nauliza Je, kama tuna migogoro hao Ma-judge wa hiyo Mahakama hawatakuwa na allegiances na Nchi Wanachama na hivyo kutoweza kutatua tatizo ambalo linatukabili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nafikiria hili ni jambo ambalo tunaweza kulifikiria na pengine kutafutia ufumbuzi mwingine. Vilevile kuna hili suala la wale waliokuwa wanafanya kazi East Africa ambalo limezungumzwa hapa ambao mpaka leo wanadai mafao yao, ningependa kupata kauli ya Serikali kwamba ina mpango gani kuhakikisha hao wanalipwa mafao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu inahusu pia Itifaki ambayo imeasainiwa na nchi wanachama wote isipokuwa Sudani ya Kusini, yenyewe haijasaini hii Itifaki mpaka leo, na bado wanapta benefits zote za East Africa wakati wao hawajasaini Itifaki hii, pamoja na kwamba wamesaini Vienna Convection, hata sisi pia tumesaini Vienna Convection lakini tumeridhia Itifaki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Serikali yetu au Jumuiya ya Afrika Mashariki ina Mkakati gani kuhakikisha kwamba na wenyewe hawa wanasaini hiyo Itifaki Mheshimiwa Waziri, nafikiri ni hayo matatu ambayo nimeyaona na ningepata kupata kauli ya Serikali ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ambayo imewekwa hapo mezani. Katika taarifa zote nilizosoma hakuna mahali katika Taarifa ya Utawala Bora na Utumishi ambayo imezungumzia group kubwa ambalo ni muhimu sana la watumishi wa Serikali, rasilimaliwatu. Kwa miaka mingi, minne sasa hawajawahi kuongezewa mshahara, na hili jambo nimeshalisema sijui mara ngapi katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati muafaka sasa Serikali ikaweka katika bajeti ijayo mishahara kwa ajili ya kuwaongezea watumishi ambao hali zao ni mbaya na wanahitaji kuboresha maisha yao na kuendesha familia zao. Itengwe bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya watumishi wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko pia suala la uhuru wa kutoa maoni. Awamu hii uhuru wa kutoa maoni umeminywa sana, ukitoa maoni yoyote ya kuikosoa Serikali, unatekwa au unapotezwa au unauawa au unafunguliwa kesi ya uchochezi. Wengine wamenyang‟anywa passports zao. Mfano mzuri ni yule Chief Executive wa TWAWEZA alinyang‟anywa passport, Mheshimiwa baba Askofu wa Kagera Niwemugizi, yeye pia alizungumza tu kuhusu Katiba mpya akanyang‟anywa passport yake na mpaka leo ninapozungumza hajarudishiwa passport yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora ni pamoja na kumwambia huyu Askofu kama passport yake hairudishwi kwa sababu gani na lini atarudishiwa passport yake maana ni kama sasa yupo kwenye house arrest. Hawezi kutoka nje ya nchi kwenda kwenye shughuli zake, hawezi kufanya chochote. Kwa hiyo ninaomba Serikali imueleze yule Bishop kama yeye si raia arudishwe kule alikotoka au arejeshewe pasi yake ya kusafiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye eneo lingine la utakatishaji fedha. hii dhana ya utakatishaji fedha imekuwa ni ngumu sana na imekuwa na uonevu mkubwa sana. Watu wanawekwa ndani kwa money laundering, wanakaa miaka, upelelezi unaendelea. Ni kwa nini TAKUKURU inapeleka hizi kesi kwa DPP ilhali haijamaliza upelelezi? Mimi naishauri Serikali, upelelezi ukamilike kabla ya kupeleka hizi kesi kwa DPP badala ya kuwanyima watu haki zao na kuwaweka rumande mwaka nenda mwaka rudi. Hii ni sawa na kuwa kama kifungo kwa saabu hakuna kitu chochote unachoweza kufanya ila ni kukaa ndani. Kwa hiyo upelelezi ukamilike ndipo watu wapelekwe Mahakamani, kesi zao ziende vizuri, kama ni kuhukumiwa wahukumiwe, kama hawana makosa warudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunao mfano mzuri Zanzibar, wenzetu ukienda kesi zote zinadhaminika, ukienda unawekwa ndani, ikifika miezi tisa upelelezi haujakamilika, unapata dhamana unatoka na kesi inaendelea. Kama una kosa unafungwa na kama huna kosa unaachiwa. Kwa hiyo tuna mfano mzuri ambao tunaweza kuiga kwa wenzetu wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninazungumzia suala la mahusiano. Suala la mahusiano ni kama hii issue iliyotokea Mambo ya Ndani; tunaona Waziri Lugola ametumbuliwa lakini ninajiuliza mimi kama Katibu Mkuu Mstaafu inawezekanaje Waziri atuhumiwe lakini Katibu Mkuu ambaye ndiye Afisa Masuhuli, yeye ndiye anasimamia mikataba, yeye ndiye anayesimamia kila kitu katika Wizara, inakuwaje? Ikanipa tafakari kubwa sana. Kwamba inawezekana Makatibu Wakuu na Mawaziri pengine hawapati semina ya kutosha kujua majukumu yao, majukumu ya Waziri ni yapi, majukumu ya Katibu Mkuu ni yapi; na inawezekana pia, naona Waziri wa Utumishi hayupo; kwamba je, Mawaziri wanapewa ile red book waweze kuzisoma na kuzielewa? Mimi sina hakika kama Mawaziri wote wamepewa ile red book, Mheshimiwa Jenista, wapewe red book wajue majukumu yao.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ruth Mollel subiri kuna taarifa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimpe Taarifa Mheshimiwa Ruth Mollel. Kwanza taratibu zote za utendaji kazi wa Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa Katiba, kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, zote zimefuatwa na kila instrument imeeleza kazi za Mheshimiwa Waziri na kila jambo ambalo Mheshimiwa Waziri anatakiwa kuwa nalo katika kutekeleza wajibu wake, vifaa, documents na zana zote za kiutendaji kila Waziri anazo, tuko full nondo hapa na kila mtu ana kila kitu!. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile tu naomba niendelee kumwambia dada Ruth, yeye aendelee kutushauri katika muundo wa utendaji kazi wetu na namna ya kufanya kazi lakini asiwe na mashaka. Rais wetu anatusimamia vizuri na sisi tunatekeleza wajibu wetu kama inavyotakiwa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ruth Mollel nafikiri umeelewa hayo ambayo ulikuwa unamuambia Mheshimiwa Jenista. Endelea Mheshimiwa Ruth.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama anavyosema Mheshimiwa Jenista ni sahihi basi liko tatizo; na kama liko tatizo litafutwe ni tatizo gani linalosababisha huu mtafaruku katika Wizara. Kwa sababu haiwezekani kuwe na mtafuruku kati ya Waziri na Katibu Mkuu kama hizo instrument zote zipo, basi iko shida na hiyo shida itafutwe ili itafutiwe dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala pia ambalo linahusu TAMISEMI na ul mradi wa DART. Ule mradi wa DART ofisi zile kila mara kunapokuwa na mafuriko maji yanajaa, na unajiuliza ingekuwa ni nyumba za watu binafsi sasahivi zingebomolewa na zikaondolewa; na hali hii inahatarisha usalama wa raia na pia usalama wa nchi yenyewe. Ni kwa nini sasa katika bajeti ijayo hizi ofisi za DART pale Jangwani zisiondolewe kwa sababu zipo katika mkondo wa maji na kila mara kumekuwa maji yanajaa mabasi yanasimama hayawezi kuyahudumia wananchi wakati wananchi wanahitaji huduma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho mimi nasema hivi kwamba Serikali iliyopo madarakani ni ya wananchi, ni wananchi ndio tumeiweka Serikali madarakani. Kwa hiyo Serikali inawajibika kwa wannachi, maana sisi ndio tumeiweka madarakani. Kwa hiyo tunapotoa maoni yetu. Tunapoikosoa Serikali, tunaisaidia Serikali iweze kwenda katika namna inayopaswa na kuboresha huduma na kutuhudumia inavyopaswa kwa kodi zetu ambazo zinakatwa kila mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni jambo muhimu sana, tujue kwamba hata Serikali inapofanya kazi vizuri inatimiza wajibu wake kwa wananchi na kwamba hawatupi msaada, sio msaada ni wajibu wa Serikali. na hiyo inatumika kwa kutumia kodi zetu sisi wenyewe. (Makofi)

MWENYEKITI: Malizia sentensi yako.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi/Vigelegele)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyoko mezani hapo.Naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani moja kwa moja, 100 percent. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni mtaalam wa rasilimali watu na kwa vile ni mtaalam wa rasilimali watu, interest yangu kubwa san imekua kwenye upande wa rasilimali watu.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyozungumza mara ya mwisho kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuhusu watumishi, ninaendelea kusisitiza kwamba katika awamu hii watumishi wamesahuliwa kabisa. Wamesahauliwa kwa sabbau katika maslahi yao, increment zao za mwaka hawapewi, vilevile hata ile nyongeza ya Mei mwaka juzi imepita, mwaka jana imepita na mwaka huu imepitra bila nyongeza yoyote ya mshahara wakati tunajua kwamba hali ya uchumi imekuwa ni ngumu, vitu vimepanda bei, kama nilivyosema na sasa nasema kwa mfano, kibaba cha unga cha kilo tano ulikuwa unanunua kwa shilingi 2,000 sasa unaunua kwa shilingi 6,000 na mshahara wa mtumishi umebaki pale pale.

Kwa hiyo, ninazidi kusisitiza kwamba watumishi wa umma kwanza ndiyo walipa kodi wazuri, kwa sababu wao wanalipa pay as you earn, wanapopokea mshahara wanalipa kodi ambayo hawawezi hata waka-forge, kwa hiyo, wanailipa kodi stahiki. Kwa mfano, mwaka huu tunategemea pay as you earn itakuwa 1.0 trillion tofauti na mwaka jana ambayo ilikuwa bilioni 998; kwa hiyo, tunaona jinsi ambavyo watumishi wa umma wanachangia kwa kiasi kikubwa katika mapato ya nchi yetu, lakini hatuoni ni kwa jinsi gani na wenyewe sasa wanasaidiwa kufanya maisha yao yawe rahisi kwa sababu wanachangia 67 percent ya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeangalia bajeti Mheshimiwa Waziri ametenga kama shilingi trilioni saba kwa ajili ya mishahara, kwa hiyo hii itakuwa ni mishahara hakuna hata nyongeza ya mishahara kwa ajili ya watumishi. Sasa mimi ninasikitika sana kwasababu watumishi ndiyo engine ya Serikali, leo watumishi wakiweka mgomo hapatatosha hapa, hakuna kitu kitaendelea, nchi yote itazizima, itasimama. Ni kwa nini Serikali ya Awamu ya Tano haioni umuhimu wa watumishi na kufanya maisha yao yawe rahisi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwa nini sasa kwenye hii pay as you earn Serikali ya awamu ya Tano ionyteshe huruma, ionyeshe interest ya watumishi kwa kuwapunguzia kodi ya pay as you earn? Naomba Mheshimiwa Mpango atakapokuja atuambie ni jinsi gani sasa waonyeshe good will kwa ajili ya watumishi ambao wanaitumikia nchi hii na kuindesha Serikali yenyewe kwa kuwapunguzia kodi ya pay as you earn.

Mheshimiwa Spika, nakuja tena kwenye suala la watumishi; watumishi wanaidai Serikali karibu shilingi bilioni 61 hii ni walimu pamoja na watumishi wengine. Wanadai nyongeza za mshahara, wanadai pesa za likizo, wengine perdiem, Serikali ikikudai itakukata mshahara, ukichelewa kulipa kodi ya ardhi utalipa interest, lakini inakuaje Serikali watumishi wanawadai pesa zote hizo watawapa interest kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli ni jambo la kusikitisha na mimi ninayo mapendekezo ambayo naishauri Serikali ili kuepuka hii adha ya malimbikizo kila siku ya madai ya watumishi miaka nenda miaka rudi, ni muhimu sasa katika pesa zile ambazo ni shilingi bilioni 666 ambazo zimetengwa kwaajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa basi Serikali ihakikishe hayo madeni yanalipwa, hilo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili; Serikali ifanye kazi ya ziada kuangalia ni mifumo ipi na taratibu zipi zinazofanya malimbikizo ya madeni na kuna namna ya kufanya. Namna ni kuangalia mfumo wenyewe unavyokwenda. Tunao wataalam wa kuchambua systems, tunaita process analysis. Tutafute watu wa process analysis watufanyie waone ni kitu gani kinachofanya haya madeni kila siku yanalimbikizwa katika Serikali na kufanya ulipaji unakuwa mgumu. Inakuwa ni rahisi kama nyongeza ya mshahara inachukua process mara moja unalipa pesa kidogo kuliko kuwa na malimbikizo kila mwaka inakuwa ni vigumu sana kulipa.

Kwa hiyo, nashauri watafutwe wataalam kama hatunao pale utumishi kwenye Ofisi ya Management Services tulete watu kutoka nje watusaidie kufanya uchambuzi wa huu mfumo ambao unaleta malimbikizo ya madeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna tatizo moja pia kubwa ambalo mimi naliona; tatizo kubwa ambalo Serikali inatakiwa kulifanyia kazi ni mfumo wa usimamizi na ukaguzi. Kila mara tunakuwa kama tunastushwa ni kwa sababu hatuna mfumo wa usimamizi na ukaguzi endelevu ambao utaweza kugundua matatizo haraka na kuyashughulikia haraka.

Mheshimiwa Spika, mimi pia napendekeza kwamba uwepo mfumo wa uwajibikaji, kwa watendaji, watendaji wanaohamisha watumishi wakijua hawana bajeti ya kuwalipa wawajibishwe, watumishi wanaoweka taarifa fake kwenye mtandao wawajibishwe na tutakapokuwa na huo mfumo wa kuwajibisha basi tutajenga mfumo ambao ni mwenye integrity, ambao unaweza kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ninakwenda kwenye suala la Ubalozi, Balozi zetu hali ya Balozi zetu ni mbaya sana nikiangalia Balozi ya Brussels ambayo jengo sasa karibu litakuwa condemned na inahitajika Euro 300,000 kuweza kulikarabati lile jengo liweze kukaa vizuri, basi katika pesa zile zilizotengwa priority ipewe lile jengo la Brussels ambalo linakutaka kuwa condemned.

Vilevile sisi kama Watanzania tunayo sifa duniani, lakini kama ikiwa tuna viwanja ambavyo tumepewa miaka nenda miaka rudi kujenga Balozi na hatujengi. Tuna kiwanja pale London kimeota magugu kinataka kuwa condemned kile kiwanja, ni kwa nini Serikali haiwezi kutumia mfumo wa mortgage financing kuweza kujenga Ubalozi wetu pale ukafanya hata biashara ukaweka na maduka na nini na ile pesa ambayo inalipwa kila mwaka. Kila mwaka zinalipwa bilioni 21 kwa ajili ya kulipa pango, kwa nini tusifanye mortgage financing na hizo pango zikatumika kulipia madeni ya benki. Mimi sijaelewa ni kwa nini, tuna kiwanja Oman miaka nenda miaka rudi. Tunaomba tutumie mortgage financing, ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia hoja iliyopo hapa mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyozungumza Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba kila mwananchi na kila mtu ana haki ya kupata taarifa. Hii ni haki ya msingi ambayo tumepewa na Mwenyezi Mungu na Serikali pia inatupa hiyo nafasi ya kupata taarifa wakati wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hii sheria ambayo ipo mezani na nina mawazo ambayo napenda kuleta mbele ya meza yako. Kwanza, namshukuru mwenzangu wa Kambi ya Upinzani kwa hotuba nzuri sana ambayo ameitoa na ninamuunga mkono kwa ile article 6 ambayo imeainisha information ambayo inakuwa exempt. Sasa najiuliza, kama hii information yote ni exempt, hiyo haki ya sisi kupata taarifa iko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukingalia hapo kipengele (e) ambayo inakataza private individual information, mimi nasema kwamba private information iko ndani ya kuta zako nne nyumbani, lakini inapokuja kwenye public, we have no private life in public. Kwa sababu kama kiongozi au kama mtu mwingine yeyote, unapotoka nje, wewe ni barua, ni mtu unayesomwa na jumuiya au na wananchi au na watu wa Jimbo lako. Kwa hiyo, hakuna private life kwenye public. Private life tunazo nyumbani kwetu wenyewe. Kwa hiyo, sioni kama hiki kifungu kinahitajika kuwepo hapa kwa sababu kinachochea kukosekana kwa maadili kati yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaangalia pia pale ambapo kuna informations ambazo hazitolewi mpaka baada ya miaka 30. Utakubaliana na mimi kwamba hata duniani kote, information zinakuwa categorized. Kuna information ambao unapata immediately, kuna information unaweza ukapata baada ya mwezi, kuna information miaka mitano, kuna information miaka 15 na kuna information miaka 30. Kwa hiyo, kama ni hivyo basi, tuainishe tujue information zipi zinapatikana immediately na information zipi ambazo haziwezi kupatikana mpaka baada ya miaka 30. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja pia kwenye suala la National Security. Nakubaliana kwamba National Security ni jambo muhimu, lakini kwa kweli ingependeza kama hii National Security tunge-interpret maana yake sijaiona. Nimeangalia kwenye interpretation haipo kwa sababu tunataka tujue kusudi isiwe ni kichaka cha kuzuia information zisitafutwe na kuibuliwa. Tukubaliane kwamba information inapoibuliwa ndiyo inaleta maendeleo, ndiyo inaongeza speed ya maendeleo katika Taifa lolote kwa sababu kama hakuna information na inatokea, watu wanashindwa kuibua hata ideas, wanashindwa kuibua vitu vya maendeleo. Kwa hiyo, National Security naomba ifanyiwe interpretation tujue what we mean by national security.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna issue nyingine ambazo tunajua ni security, kwa mfano, mambo ya vita, mambo ya intelligence ni national security. Kwa sababu tumeona hata juzi unaambiwa uchochezi ni national security. Uchochezi wenyewe hata haueleweki ni uchochezi gani. Kwa hiyo, tui-define hiyo national security. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye access of information, nimeangalia kwenye sheria inasema siku 30; siku 30 ni nyingi sana. Wakati mwingine unahitaji information immediately kwa sababu unaitumia; kwa sababu information delayed is no longer information na haifai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siku 30 ni nyingi sana, tunaomba itazamwe upya. Maana yake nikiangalia siku hizi tuna ICT, tuna IT unless kama bado tunaendelea na utaratibu wa kizamani ule wa kuweka ma-record na kuyafunga kwenye box. Siku hizi tuna mambo ya ICT, kwa hiyo, hakuna sababu yoyote ya mtu anataka information aipate mpaka baada ya siku 30; maana naona nyingine ukitaka tena zaidi siku 14. Tunataka information immeadiately, kama mtu anaitaka information aipate aweze kuitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taifa letu hili tunahitaji sheria ambayo ina-facilitate watu kutafuta taarifa na kuzifanyia kazi na kuleta maendeleo chanya katika Taifa letu. Kama tutaendelea na utaratibu wa kuzibwa midomo na kuzuiliwa kuzungumza, hatuwezi kufika popote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mchango wangu kwa ufupi sana. Ahsante.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa Mwaka 2017
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani. Moja kwa moja naunga mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo maeneo machache. Kwanza nilipenda nipate ufafanuzi, katika sheria kwenye clause ya 14 kuhusu kiasi cha precursor chemicals pale kwenye clause ya 3; inasema precursor chemicals or substance with drug related effect weighing more than 100 litres in liquid form or 100 kilograms in solid form, lakini kwingine inasema 100 kilograms below. Vilevile inapokuja kwenye cannabis na khats kuna mahali inasema, more than 50 kilograms, lakini ukienda kwenye 15A inasema below. Sasa ningependa kufahamu kama ni vitu viwili tofauti au ni mchanganyiko?

Mheshimiwa Naibu Spika, na kama tunazungumzia below mimi nitakuwa na mashaka sana kwamba vijana wengi sana watakwenda jela. Na nilifikiri kwamba hili suala la drugs lingejikita sana, kama walivyozungumza wenzangu, kwenye elimu na counciling kusudi vijana wajitambue waweze kuepukana n dawa za kulevya. Kwa hiyo, ningependa kupata ufafanuzi kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mimi naona adhabu kwa watu wanaokamatwa na cannabis na wanaokamatwa na mirungi ni kubwa sana ukiifananisha na cocaine. Mimi nilifikiri kwamba adhabu yake ingekuwa tofauti kidogo, kwa sababu cocaine athari yake ni kubwa zaidi kuliko cannabis na mirungi. Na tukiangalia kwa wenzetu Wakenya wao wamehalalisha, mimi sisemi tuhalalishe, wao wamehalalisha, lakini wao wanatumia mirungi tena kama raw material ya kutengeneza divai, wanatengeneza yoghurt, wanatengeneza na juice. Kwa hiyo, kuna umuhimu pia wa kutazama hivi vitu kwa mtazamo mpana zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, limekuja suala ambalo alilifanua Mheshimiwa Waziri. Nimefurahi kwamba hii council ya drugs au hii taasisi isiwe ndio soul ambayo watu wakitaka kuleta dawa, precursor substances na kuleta dawa ambazo mwishowe zinatengenezewa cocaine au dawa za kulevya, wao sio wapewe authority ya ku-import kwa sababu, kuna TFDA, tuna MSD. Kwa hiyo, nategemea kwamba, kutokana na maelezo ya Mheshimiwa Waziri inaelekea kwamba, labda hicho kipengele kitakuwa kimerekebishwa kwa sababu kitaleta mkanganyiko mkubwa sana na urasimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilitaka kulizungumzia ni kuhusu mabadiliko ya jina kutoka Government Chemist na kwenda Government Analyst. Kwa mtazamo wangu ninaposema Government Chemist yaani unaelewa kabisa unazungumzia mkemia na ninapozungumzia Mkemia Mkuu unajua kabisa Mkemia Mkuu ni nani, lakini tunaposema Government Analyst kwa kweli mimi naona hili neno analyst liko vague; policy analyst, economic analyst, research analyst, huyu analyst ni nani? Hilo suala moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ningependa kujua kama huyu Government Analyst jina hili linaoana na muundo wa watumishi wa wakemia kwa sababu, wakemia wana muundo wao. Unaanza mdogo, unapanda mkemia, mkemia senior mpaka unakuwa principal mpaka unakuwa Mkemia Mkuu. Ningependa kujua kuna uhusiano gani kati ya kuwa Government Analyst na kuwa mkemia kwa mujibu wa muundo wa utumishi wa wakemia?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshazungumzia kuhusu hiyo cannabis. Mimi nafikiri naomba niishie hapo na ningependa kupata ufafanuzi kuhusu hayo.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 5) wa Mwaka 2017
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Muswada uliopo hapo Mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, historia inaonesha kwamba ajira kwa watumishi wa umma zimekuwa hazitoki kwa muda mrefu na vile vile zoezi lile la kuondoa watumishi wengi katika utumishi wa umma limesababisha upungufu mkubwa wa vijana ambao wangeweza kukua katika utumishi wa umma waweze kuendeleza utumishi wa umma. Kwa hiyo, matokeo yake sasa tuliyokuwa nayo si katika fani tu ya madaktari na maprofesa lakini ni katika fani zote, kwamba tuna watu wengi wanastaafu lakini hatuna maafisa waandamizi hapo katikati ambao wanaweza kuchukua hizo nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii gap ambayo pia iliyowakumba madaktari na maprofesa inaongezewa pia na kwamba sasa hivi ajira hazitoki kwa muda muafaka, kuna madaktari wengi ambao wamemaliza shule MUHAS na kila mahali wako bado mtaani hawajapata kazi. Sasa ikiwa, sawa, kuongeza umri, hawa madaktari ambao wako mtaani ambao ndiyo baadaye tutakuwa na maprofesa na madaktari bingwa, Serikali inafanya jambo gani kwa ajili ya kuhakikisha hawa walioko sasa hivi mitaani wanaajiriwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, wote tumekuwa mashahidi katika kupitisha bajeti. Bajeti ya mafunzo ni kidogo sana, kwa hiyo matokeo yake tunakuwa hatuna wataalam (specialists) kwenye maeneo mbalimbali kwa sababu Serikali haitengi fedha za kutosha kwa ajili fedha ya mafunzo ya kujenga rasilimali watu. Kwa hiyo ni muhimu sasa Serikali kwanza ikatoa ajira kwa hao madaktari na wanachuo ambao wanafanya internship ili waweze kuongeza nguvu katika utumishi wa umma na vile vile pesa itengwe kwa ajili ya ajira ya watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wamezungumzia Ghana, Uganda, Kenya, Nigeria, Botswana wanakwenda mpaka miaka 70. Wanakwenda mpaka miaka 70 kwa sababu package wanayopata ni nzuri, ndiyo maana watu wako tayari kwenda mpaka miaka 70. Pia tumeona kwamba madaktari wetu wengi wako Botswana, mimi nina shemeji yangu yuko Botswana na he was one of the best neurosurgeons, yuko Botswana kwa sababu kule maslahi ni mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Serikali, pamoja na kuongeza hiyo miaka 60 mpaka 65, ambayo sidhani kama ni suluhu, Serikali iangalie ni kwa jinsi gani itaboresha maslahi ya madaktari, hao maprofesa ili wawe na moyo wa kubaki nchini. Maana kama unalipwa vizuri huwezi ukaondoka kwenda kwenye nchi nyingine, utabaki kwenye nchi yako kuweza kutoa contribution katika kuendeleza nchi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ni muhimu kwa Serikali sasa kuangalia package ya madaktari, package ya proffesionals kwa sababu wengi wasingependa kuendelea mpaka miaka 65, wengi wangependa kuchukua pesa zao waondoke kwa sababu ya maslahi duni. Kwa hiyo ni muhimu basi hii package yao ikaweza kuangaliwa upya ili iwape motisha ya kufanya kazi katika utumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile studies zimeonesha kwamba baada ya kustaafu life expectancy ni miaka 12 tu. Kwa hiyo kama wewe umeongezewa miaka ya kustaafu mpaka 65, package unayopewa mshahara wenyewe ni duni, life expectancy baada ya kustaafu miaka 65 miaka 12, hiyo hela sijui utaitumia kwa muda gani. Kwa hiyo ni vizuri miaka 60, 65 sawa lakini si suluhu, tuangalie kuongeza mishahara ya watumishi ili iwape motisha wabaki nchini na kuendelea kufanya kazi na kuchangia katika uchumi wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyopo Mezani na moja kwa moja naunga mkono maoni ya Kambi ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Kwanza kwa wale tuliokuwepo, tunakumbuka Serikali ilikuwa inafanya kila kitu; nakumbuka hata mpaka na kuuza nyama kwenye bucha Serikali ilikuwa inamiliki yale maduka ya nyama. Baadaye ilionekana kwamba Serikali haiwezi kufanya kila kitu. Tulipoingia Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne tukaja sasa na Sera ya PPP, maana hii ni ya siku nyingi ili kuiwezesha sekta binafsi ichangie katika maendeleo ya uchumi kwa sababu sekta binafsi ndiyo engine of growth, inaajiri watu wengi na inachangia sana mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka hii kama miwili, mitatu nimeona kama hii sera tunachosema ni tofauti na tunachofanya. Kwa mfano, wakati ule TBA kazi yake ilikuwa ni miradi mikubwa ya ujenzi. Kazi kubwa ya TBA ilikuwa ni ufuatiliaji, tathmini na usimamizi, lakini ghafla awamu hii TBA sasa ndiyo inajenga majengo makubwa ndani ya nchi na sekta binafsi tumeiweka kando. Sasa inakuwaje tena tunasahau kwamba sekta binafsi ndiyo engine of growth na ndiyo inaleta ajira na Serikali kazi yake kubwa ni usimamizi, ufuatiliaji na tathmini. Naona sasa Serikali imehama tena kwenye jukumu lake hilo inakwenda kwenye utekelezaji wa miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika miradi mikubwa kwenye Mpango wa Maendeleo kama ilivyozungumzwa kwenye maoni ya Kambi ya Upinzani, miradi mikubwa ya kibiashara katika Mpango wa Maendeleo ilikuwa itekelezwe kibiashara na iachiwe sekta binafsi, lakini ghafla Serikali yenyewe sasa imeichukua hiyo miradi mikubwa, inakopa na inafanya kila kitu wenyewe. Ukiangalia TBA kila kitu wanafanya wenyewe; wananunua vifaa, wanajenga na wanatathmini wenyewe, huo siyo utawala bora, inabidi turudi kwenye misingi ya utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ninavyoliona kwa Serikali ni usimamizi, tathmini na ufuatiliaji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake atueleze ni jinsi gani Serikali imejipanga katika kufanya kazi yake kubwa ya msingi ya usimamizi, tathmini na ufuatiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujui, mimi nasema tunajua tulipotoka; najua tumetoka kwenye uchumi wa kijamaa lakini mpaka sasa hivi sijui tunakwenda wapi? Sijui kwenye uchumi wa soko au hatupo kwenye uchumi wa soko. Tunaomba Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha atuambie tunakwenda wapi? Maana yake kwa jinsi navyoona Serikali inavyofanya kazi sasa ni kama tunarudi tena kule kule tulikotoka kwenye uchumi wa ujamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba inaiwezesha sekta binafsi kwa kuweka mazingira mazuri ili iweze kujiendesha na kuleta maendeleo. Tumeshuhudia jinsi ambavyo biashara nyingi zimefungwa kwa sababu wameshindwa kuendesha shughuli zao za biashara kutokana na mazingira ambayo siyo rafiki katika uwekezaji. Pamoja na miradi mikubwa tunayoizungumzia ya PPP lakini bado kuna wafanyabiashara ambao wanahitaji mazingira mazuri waweze kuendesha shughuli zao za biashara ili uchumi uweze kukua na tuendelee kupunguza umaskini katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuangalia suala la PPP, napenda Mheshimiwa Waziri akija kuhitimishia atuambie ni kwa jinsi gani ameangalia suala la rasilimali watu maana tumeona tumekuwa na mikataba mingi mibovu kwa sababu ya kukosa wataalam wenye utaalam wa kutosha uliobobea katika mambo ya mikataba na mikataba ya Kimataifa. Tumeshuhudia mikataba mingi mibovu ambayo imesainiwa na imetuingiza katika hasara kubwa kwa sababu tumevunja mikataba na sasa tunadaiwa left, right and center.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango wa Maendeleo na pia katika hotuba ya Elimu ya Juu hakuna mahali popote ambapo nimeweza kuona kulivyoanishwa hizi rasilimali watu tunazozizungumzia tunazohitaji kwenye mikataba. Ni vizuri kuwa na negotiating pool team ambayo imefunzwa vizuri, ipo very strong na ambayo itaweza kusimamia masuala ya mikataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye suala la fedha tunayo benki moja tu ya TIB. Tumeona benki nyingi, nyingine zimeshafungwa, Mheshimiwa Waziri wa Fedha anajua na benki nyingi wamepunguza wafanyakazi kwa sababu shughuli zao haziendi vizuri. Sasa ni jinsi gani Serikali itahakikisha kwamba tunakuwa na benki zaidi ili kuwawezesha watu binafsi kukopa, waingie ubia na Serikali kusudi waweze kuleta maendeleo katika nchi hii? Hayo mambo ni very serious na bila kuhakikisha sekta ya fedha ipo madhubuti, hata hili wazo la PPP tutalishindwa asubuhi kweupe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona pia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, amesema kwamba sasa wanategemea kwamba Serikali za Mitaa na taasisi binafsi ziweze kutengeneza proposals za kuhusisha sekta binafsi katika ubia. Napenda kumwuliza Mheshimiwa Waziri, hivi Local Government itapata wapi pesa ya kuandika proposal? Maana wamesema watenge kwenye bajeti yao, bajeti gani wakati property tax mmechukua, hela za mabango mmechukua na pesa nyingi zimechukuliwa kutoka Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za maendeleo wote tunajua hazipelekwi. Sasa Serikali za Mitaa itawezaje kujihusisha kweli kwenye PPP ikiwa vyanzo vyake vya mapato ni kidogo na inashindwa hata kusimamia huduma za jamii kwenye Wilaya na sekta mbalimbali? Mheshimiwa Waziri aje atueleze kuhusu hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea pia katika kuangalia hii PPP, maana katika PPP tuna Build Operate and Transfer, Build Operate and Own, Design Build and Operate na Joint Venture. Nadhani ni muhimu sana sasa kwa Serikali kuangalia mambo matatu ambayo nimeshazungumzia. Kwanza human resources, pili kuangalia financial base ya kuwezesha hivi vitu kufanya kazi na tatu kuhakikisha kwamba sheria na kanuni zinazingatiwa kwa ufasaha na kwa umakini ili kuwezesha private sector kuja ku-invest katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono maoni ya Kambi ya Upinzani.