Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Lucy Simon Magereli (12 total)

MHE. ISSA A. MANGUNGU (K.n.y MHE. LUCY SIMON MAGERELI) aliuliza:-
Machimbo ya Madini ya ujenzi yaliyoko Kigamboni yanatoa malighafi muhimu sana inayosaidia ujenzi katika jiji la Dar es Salaam; machimbo haya yanatoa ajira kwa zaidi ya wakazi 6,000 na ndiyo machimbo yenye mwamba laini kwa Mkoa wa Dar es Salaam ukilinganishwa na madini yanayotoka Goba:-
(a) Je Serikali haioni kuwa utaratibu wa kuratibu zoezi la kufunga machimbo haya utakosesha ajira kwa watu zaidi ya 6,000?
(b) Je, kwa kufunga machimbo hayo, Serikali haioni kuwa inawanyima fursa wananchi wa Dar es Salaam na Pwani kupata madini ya bei nzuri na kuwapunguzia gharama za ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini hapa nchini hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Sheria hiyo imeweka utaratibu Maalum wa uchimbaji wa madini ikiwemo kuacha umbali wa mita 200 kutoka makazi ya watu yaani bufferzone.
Umbali huo umekadiriwa kitaalam kuzuia madhara yanayoweza kutokea kutokana na shughuli za uchimbaji hasa maeneo ya makazi. Kwa sababu hizo sasa, Wizara ya Nishati na Madini inafanya mipango wa kutathmini namna bora ya kuendelea uchimbaji madini ya ujenzi katika mkoa wa Dar es Salaam hasa bila kuathiri mazingira, afya pamoja na maeneo ya wakazi kama nilivyoeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaona umuhimu sasa wa kupanua fursa na kuwezesha wananchi wengi kushiriki katika shughuli za uchimbaji wa madini haya. Hata hivyo Serikali inachukua fursa hii kutoa wito kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote kwa wachimbaji wote ili kuzingatia sheria zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na kuongeza pato la Taifa.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE (K.n.y. MHE. LUCY S. MAGERELI) aliuliza:-
Matatizo ya migogoro ya ardhi na mipango miji ni suala nyeti sana linalohitaji kutazamwa sana katika zama hizi; na hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aligawa ramani za maeneo ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam lakini zoezi hilo halikufanikiwa kutokana na kukosa mkakati ulioambatana na matumizi ya ramani hizo:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ramani hizo zinapatikana kwa nchi nzima ili kusaidia kuongoza matumizi ya ardhi katika miji mingi nchini?
(b) Waziri Mkuu aliyepita, Mheshimiwa Mizengo Pinda alisema, Serikali ingeuza Government Bond ili kupata fedha za kugharamia mradi huu. Je, agizo hilo limefikia hatua gani katika utekelezaji?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na. 418 la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) yote kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007, kifungu cha 21(1) kinaeleza kwamba mipango yote iliyoidhinishwa na Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji kwa maana ya Mipango Miji ya jumla (Master plan) na ile ya kina (michoro ya mipango miji) itahifadhiwa na mamlaka husika ya upangaji kwa maana ya Halmashauri ya Jiji, Manispaa, Miji na Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli matatizo ya migogoro ya ardhi na mipango miji ni suala nyeti sana linalohitaji kupatiwa mtazamo wa kipekee. Ni kweli hivi karibuni niligawa ramani za maeneo ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam na zoezi hilo lilifanyika kwa lengo la kuwawezesha viongozi wa ngazi za mitaa kushiriki kikamilifu katika udhibiti wa ujenzi holela na uvamizi wa maeneo ya umma, maeneo ya wazi na yale yaliyohifadhiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu ina jukumu la kuhakikisha kuwa michoro yote ya mipango miji iliyoidhinishwa na Wizara inatumiwa kwenye Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa na nakala zake kupelekwa katika Halmashauri husika na mamlaka hizo zina jukumu la kuweka michoro hiyo hadharani ili umma uweze kuona na kulinda maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Serikali kuuza bond ili kupata fedha za kugharamia mradi huu, suala hili halijatekelezwa, badala yake kila Halmashauri inaelekezwa kutumia vyanzo vyake vya ndani vya mapato kwa kushirikiana na sekta binafsi. Hii ni kutokana na Sheria ya Mipango Miji inayotoa fursa kwa wamiliki binafsi wa ardhi kuandaa mipango ya matumizi kwa mujibu wa sheria.
MHE. LUCY S. MAGERELI aliluliza:-
Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano kumekuwa na mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa shughuli za Bunge kwa kupunguza muda. Bunge sasa hukaa kwa siku 10 hadi 12 tu jambo ambalo linasababisha muda wa kuchangia na Mawaziri kujibu hoja kuendelea kupunguzwa hadi kufika dakika tano tu kitu ambacho kimepunguza kabisa ufanisi wa chombo hiki muhimu chenye majukumu muhimu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuliwezesha Bunge
kufanya shughuli zake kwa ufanisi kwa kuliongezea bajeti?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Serikali kuliwezesha Bunge kufanya shughuli zake kwa ufanisi ni kwa kutoa fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali kwenda kwenye Mfuko wa Bunge Fungu namba 42 kwa kuzingatia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge, taarifa ya utekelezaji ya Mfuko wa Bunge na hali ya upatikanaji wa fedha. Kifungu cha 45(b) cha Sheria ya Bajeti kinatuelekeza tufanye hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msingi huo, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Mfuko wa Bunge uliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 99 na hadi Februari, 2017 jumla ya shilingi bilioni 62.6 sawa na asilimia 68 ya bajeti ya mfuko huo zilitolewa. Serikali inaahidi kutoa fedha zote zilizobaki kwenye bajeti ya fungu hili yaani shilingi bilioni 8.3 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi bilioni 6.7 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kabla ya tarehe 30 Juni, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka ujao wa fedha, Serikali imeongeza bajeti ya Mfuko wa Bunge kutoka shilingi bilioni 99 mwaka 2016/2017 mpaka shilingi bilioni 121 mwaka ujao wa fedha.
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-
Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI ya Februari, 2017 fedha za wafadhili zinaendelea kupungua na baadhi yake kuwa na masharti yasiyoendana na mila na desturi za Kitanzania.
Je, Serikali imejipangaje kuendeleza huduma zilizokuwa zikitolewa na wafadhili, hususan dawa za kurefusha maisha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie kwamba Wadau wa Maendeleo wameendelea kutoa msaada wa dawa za kurefusha maisha (Antiretroviral Drugs - ARVs) mbali na kwamba Serikali imeendelea kupinga maadili mbalimbali yasiyoendana na mila na desturi za Kitanzania kwa kutoa miongozo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha tunajipanga vyema na upatikanaji, hususan wa dawa za kurefusha maisha (ARVs), Serikali kwa sasa imeanzisha Mfuko Maalum wa UKIMWI unaojulikana kama AIDS Trust Fund (ATF). Mfuko huu utachangiwa na Serikali, mashirika, sekta binafsi pamoja na wahisani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kuu la mfuko huu ni kuchangia upatikanaji wa dawa za kurefusha maisha hapa nchini.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. LUCY S. MAGERELI) aliuliza:-
Askari wa JWTZ wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi kwa kutesa raia na saa nyingine Jeshi la Polisi. Matukio haya yamekuwa yakifanyika maeneo ya starehe, kwenye foleni za magari, mitaani na katika magari ya usafiri wa umma. Hivi karibuni Mkoani Tanga, kijana mmoja kondakta wa daladala alimzuia mtoto wa mwanajeshi kupanda daladala yake bila nauli, alikamatwa na kuteswa na wanajeshi ndani ya Kambi, kitu kilichopelekea kifo chake.
(a) Je, sheria ipi inawapa wanajeshi haki ya kutesa raia?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani kukomesha hali hii?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna sheria yoyote inayowapa haki wanajeshi kutesa raia au kuvunja sheria.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya wanajeshi kushambulia raia au raia kushambulia wanajeshi mara nyingi yamekuwa yakijitokeza katika mazingira yanayohusisha kutofautiana kauli, ulevi, wivu wa kimapenzi na hata ujambazi. Hivyo katika kushughulikia hali hii, mara nyingi kesi hufunguliwa kwenye mahakama za kiraia na hukumu kutolewa kwa mujibu wa sheria zilizopo hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria inashauriwa wanaokubwa na kadhia hii wapeleke mashtaka kwa mujibu wa taratibu zilizopo ili sheria ifuate mkondo wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taratibu zilizopo za Jeshi letu la Ulinzi, afisa au askari anapopatijkana na hatia katika mahakama za kiraia na kuhukumiwa adhabu ya vifungo au nyinginezo, pia hupoteza sifa za kuendelea kulitumikia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Aidha, maafisa na askari mara kwa mara wamekuwa wakiaswa kuishi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-
Matatizo ya migogoro ya ardhi na Mipango Miji ni suala nyeti sana linalohitaji kutazamwa sana katika zama hizi; na hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aligawa ramani za maeneo ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam lakini zoezi hilo halikufanikiwa kutokana na kukosa mkakati ulioambatana na matumizi ya ramani hizo:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ramani hizo zinapatikana kwa nchi nzima ili kusaidia kuongoza matumizi ya ardhi katika miji mingi nchini?
(b) Waziri Mkuu aliyepita Mheshimiwa Mizengo Pinda alisema Serikali ingeuza Government Bond ili kupata fedha za kugharamia mradi huo; Je, agizo hili limefikia hatua gani katika utekelezaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Na. 8 ya Mipango Miji ya Mwaka 2007 katika Kifungu cha 21(1) inazipa Halmashauri mamlaka ya kupanga na kuhakikisha ramani za Mipango Miji ya jumla (master plan) na ile ya kina (michoro ya mipango miji) iliyoidhinishwa na Wizara yenye dhamana na ardhi zinahifadhiwa na kusambazwa kwa wadau. Halmashauri zinaendelea kutekeleza jukumu hili kwa kutoa elimu na tafsiri sahihi ya michoro ya Mipango Miji kwa wananchi ili kuhakikisha kunakuwa na usimamizi shirikishi kwa lengo la kudhibiti uendelezaji holela.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali kuuza bond ili kupata fedha za kugharamia mradi huu, suala hili halijatekelezwa badala yake kila Halmashauri imeelekezwa kutumia vyanzo vyake vya mapato ya ndani kwa kushirikiana na sekta binafsi. Utaratibu huu unatokana na Sheria ya Mipango Miji inayotoa fursa kwa wamiliki binafsi wa ardhi kuandaa mipango ya matumizi kwa mujibu wa sheria.
MHE. MWITA M. WAITARA (K.n.y. MHE. LUCY S. MAGERELI) aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Kimbiji na Mpera chini ya Kampuni ya Serengeti Limited ulianza Machi, 2013 na Desemba 2016 ulitarajiwa kukamilisha visima 20 ambavyo vitawahudumia wananchi wa Kigamboni na Mkuranga. Waziri wa Maji na Umwagiliaji Oktoba, 2016 akitembelea mradi huo na kuagiza ukamilike kwa wakati uliopangwa vinginevyo kampuni ingelipa gharama za ucheleweshaji lakini hadi leo mradi huo haujakamilika:-
(a) Je, Serikali imeshawajibisha kampuni hiyo kwa kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo?
(b) Je, ni lini mradi huo utakamilika ili kuondoa adha kwa wananchi wa Kigamboni ambao wengi wao wanatumia maji ya visima vifupi ambavyo sio salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako kabla sijamjibu ndugu yangu, naomba nitoe shukrani za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusikia kilio cha Waheshimiwa Wabunge kuhusu suala zima la utekelezaji wa miradi vijijini na ameagiza Wahandisi wote waje katika Wizara ya Maji. Nataka niwaambie Wahandisi wa Maji wanyooke na asiyekubali kunyooka basi tupo tayari kumnyoosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mradi wa Uchimbaji wa Visima vya Maji vya Kimbiji na Mpera umechelewa kutekelezwa. Serikali imechukua hatua za kimkataba dhidi ya kampuni husika ikiwa ni pamoja na kukata malipo kwa ucheleweshaji wa kazi (liquidated damage). Mradi wa visima vya Kimbiji na Mpera ilikuwa ukamilike Mei, 2018 sasa unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, maji ya visima hivyo yataanza kutumika baada ya kukamilika kwa awamu ya pili ambayo itahusu ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji ambao utaanza kutekelezwa katika bajeti ya mwaka 2018/2019. Kwa sasa ili kuondoa adha ya wananchi wa Kigamboni wakati wanasubiri kukamilika kwa mradi mkubwa wa Kimbiji na Mpera, Serikali imeanza kutekeleza miradi mbalimbali minne ya uboreshaji wa huduma ya maji kwa mpango wa muda mfupi kwa wakazi wa Kigamboni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo ni pamoja na:-
• Ujenzi wa mtandao wa mabomba ya kusambaza maji kutoka Ruvu Chini kupitia bomba linalovuka bahari eneo la Kurasini kwenda Kigamboni ili kusambaza maeneo ya Tipper, Chuo cha Mwalimu Nyerere na Kigamboni Ferry kuelekea Mjimwema;
• Mradi wa kuendeleza kisima cha Gezaulole ambacho maji yake yatasambazwa Gezaulole na maeneo ya jirani kuelekea Mjimwema;
• Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji kutoka visima vya Vijibweni kuelekea maeneo ya ofisi mpya ya Manispaa ya Kigamboni; na
• Kuendeleza kisima kirefu cha mita 600 cha Kisarawe II ili kufikisha maji Kibada na maeneo ya viwanda (light industry zone) la Kimbiji. (Makofi)
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-

Tangazo la Serikali Namba 257 kifungu cha 6 kinaelekeza faini za makosa ya barabarani kulipwa kwa Askari aliyeandika faini au kwa OCD au Ofisi ya Mhasibu aliyeko karibu. GN hiyo imetoa nafasi ya kulipa ndani ya siku saba (7) na iwapo faini haitalipwa ndani ya siku saba (7) mkosaji atafikishwa Mahakamani ndani ya siku 10:-

(a) Kwa nini Askari wa Usalama Barabarani huamua kushikilia magari ya wanaokamatwa wakati huohuo, wakati sheria inasema walipe ndani ya siku saba (7)?

(b) Katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna mashine za kielektroniki (POS) za kulipia faini na ANPR ambayo husaidia kufuatilia ambao wanakwepa kulipa faini walizoandikiwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza upatikanaji wa POS na ANPR ili kuepusha mifarakano na usumbufu unaojitokeza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba kifungu cha 6 cha Tangazo la Serikali Namba 257 alichokinukuu kilishafanyiwa marejeo mwaka 2015 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali mnamo tarehe 30/01/2015 na kuwa Kanuni namba 30/2015 ya Sheria ya Usalama Barabarani ambayo imelenga kutengeneza mfumo wa ulipaji wa tozo za papo kwa papo kwa njia ya kielektroniki. Kanuni hii pia inasomwa pamoja na Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 iliyorejewa mwaka 2002, kifungu cha 95.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukamataji wa magari na kisha kuyashikilia upo kisheria, kifungu cha 87, kifungu kidogo cha (a), (b) (c) na (d) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 iliyorejewa mwaka 2002, magari haya hushikiliwa kulingana na uzito wa kosa alilofanya dereva mfano makosa hatarishi kama ubovu wa gari ambapo gari linatakiwa likafanyiwe ukaguzi na Mkaguzi wa Magari, makosa ambayo dereva au mmiliki anatakiwa apelekwe Mahakamani na kadhalika.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa ulipaji tozo za papo kwa papo kwa njia ya mtandao ulianza kutekelezwa kwa majaribio katika Mikoa mitatu ya Kipolisi ya Ilala, Kinondoni na Temeke ambapo jumla ya mashine za kielektroniki (POS) 360 na kamera za kufuatilia magari yanayodaiwa faini (ANPR) 3 zilizotumika na kuonyesha ufanisi na mafanikio makubwa. Kuanzia Apili, 2018, mfumo huu ulianza kutumika nchini kote ambapo mashine hizi za kielekroniki (POS) zipatazo 3,000 zilipelekwa mikoa yote nchini na mashine za ufuatiliaji wa magari (ANPR) zipatazo 400 zinatarajia kusambazwa mikoa yote nchini kuondoa usumbufu usio wa lazima.
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-

Wilaya ya Kigamboni inakabiliwa na tatizo la msongo mdogo wa umeme na matukio ya kukatika umeme ya mara kwa mara hata mara tatu kwa siku:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukomesha tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na tatizo la umeme kupungua nguvu (low voltage) katika maeneo ya Manispaa ya Mji wa Kigamboni kutokana na uchakavu wa mifumo ya umeme pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya umeme kutokana na kasi ya ujenzi wa nyumba za makazi na viwanda. Serikali kupitia TANESCO inaendelea na kazi ya kuboresha hali ya umeme (voltage improvement) kwa kuongeza njia za umeme na transformer katika maeneo ya Kigamboni yakiwemo Vijibweni, Kibugumo, Kibada, Uvumba, Kisota, Maweni na Kwa Thoma.

Katika kushughulikia tatizo hili, Serikali kupitia TANESCO mwaka 2017 ilifanya matengenezo kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Kupooza Umeme Kigamboni kwa kukiongezea uwezo wake kutoka MVA 5 iliyokuwa inahudumia wateja 3000 kufikia MVA 15 yenye uwezo wa kuhudumia wateja 12,000. gharama ya mradi ni shilingi 1,500,000,000/=.

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha ujenzi wa Kituo Kipya cha Kupooza Umeme cha Kurasini cha 132/33KV kitakachopeleka umeme wa uhakika katika maeneo ya Kigamboni. Ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka 2018 na utakamilika mapema mwezi Aprili, 2019 na hivyo kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme Kigamboni.

Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine Serikali kupitia TANESCO inaendelea na kazi ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 132 kutoka Kurasini hadi Dege na ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme cha MVA 120 katika eneo la Dege Kigamboni. Mradi huu ulianza kutekelezwa kuanzia mwezi Januari, 2018 kwa gharama ya shilingi bilioni 16 na utakamilika ifikapo Septemba, 2019. Kukamilika kwa mradi huu kutaimarisha na kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Mbagala na Kigamboni na hivyo kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la kukatika umeme kwa Wilaya za Kigamboni na Temeke. Ahsante.
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-

Sera ya cost sharing ilianzishwa ili kuisaidia Serikali kibajeti katika maeneo ya afya na elimu, hadi leo ni bayana kuwa sera hii imeshindwa na hatimaye Serikali kurejea tena katika kugharamia Elimu ya Msingi na Sekondari:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Elimu ya Tanzania ambayo imeporomoka sana katika shule za Umma inakuwa yenye ubora unaotarajiwa?

(b) Je, Serikali inafanya nini kuhusu madai ya stahiki ya walimu ambazo hazijalipwa kwa muda mrefu sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, kama lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya Tanzania inaendelea kuimarika siku hadi siku katika Shule za Umma na binafsi. Ili kuhakikisha kuwa ubora wa elimu unaendelea kuimarika zaidi, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Mfano, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019, zaidi ya shilingi bilioni 56.5 zimetumika katika uboreshaji wa miundombinu katika shule 588. Kati ya hizo Shule za Msingi ni 303 na Sekondari ni 288 yakiwemo madarasa 1,190, mabweni 222 na vyoo 2,141.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imesambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia vikiwemo vifaa vya maabara na kemikali na vifaa vya kielimu kwa ajili wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule za Msingi na Sekondari. Pia katika kipindi cha mwaka 2017 hadi Aprili, 2019, Serikali imeajiri jumla ya Walimu 17, 884.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imeendelea kuimarisha Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule ambapo imenunua na kusambaza magari 45 ya Udhibiti Ubora wa Shule na pikipiki 2, 897 kwa ajili ya Maafisa Elimu Kata. Pia katika mwaka 2019/2020 Serikali inatarajia kujenga Ofisi 100 za wadhibiti ubora wa shule na kuongeza idadi ya watumishi ili kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madai ya stahiki za walimu, Serikali imeendelea kulipa madai hayo yahusuyo mishahara na likizo ambapo kwa kipindi cha Juni hadi Oktoba, 2018 Serikali ililipa zaidi ya shilingi bilioni 16 kwa madai ya malimbikizo ya mishahara. Aidha, hadi kufikia Desemba, 2018 Serikali pia ilipeleka jumla ya shilingi bilioni 5.07 kwenye Halmashauri 184 kwa ajili ya malipo ya likizo za walimu.
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-

Mwaka 2018 Serikali ilipitisha Sheria ya Udhibiti ya Taasisi Ndogo za Fedha SACCOS, VICOBA, Vikundi vya kuchangishana na kukopeshana, vyote vipate usajili na kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania:-

(a) Je, zoezi hili limeshatekelezwa kwa asilimia ngapi na ni taasisi ngapi zimesajiliwa?

(b) Je, Serikali haioni kuwa zoezi hili ni over – regul ation na kuwanyima fursa ambayo imekuwa ikiwasaidia wakopaji na wakopeshaji wadogo kusaidiana katika jamii zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako Tukufu lilitunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha Mwaka 2018. Baada ya Sheria hiyo kutungwa Serikali ilianza mchakato wa kuandaa Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha. Kanuni hizo zinalenga madaraja manne ya watoa huduma yaliyoanishwa kwenye Sheria. Aidha, mchakato huu ulihusisha ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za walengwa ili kuweza kutengeneza kanuni zinazozingatia hali halisi ya biashara zao pamoja na matakwa ya sheria. Mchakato wa kuandaa Kanuni umekamilika na hivyo kutangazwa kwenye gazeti la Serikali Na. 575 tarehe 2 August Mwaka 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa mujibu wa sheria hii, walengwa wamepewa makataa yaani grace period ya mwaka mmoja baada ya kununi kutolewa ili waweze kujiandaa kulingana na matakwa ya kanuni hizo. Kanuni zitaanza kutumika rasmi baada ya muda wa makataa kupita ikiwemo zoezi la usajili. Hivyo basi, hadi sasa hakuna taasisi yoyote iliyosajiliwa kupitia Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kutungwa kwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha siyo kunyima jamii fursa ya kusaidiana kwa njia ya kukopesha na kukopeshana, bali ililenga kutatua changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2000. Changamoto hizo ni pamoja na kiwango kikubwa cha riba na ukosefu wa utaratibu wa kuwalinda walaji na wadau wa sekta ndogo ya fedha kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio ya Serikali yetu kuwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, itaimarisha usimamizi na udhibiti wa sekta ya huduma ndogo za fedha na hivyo kuakisi matarajio na mahitaji ya wadau, kasi ya ukuaji na mchango wake katika sekta nzima ya fedha na uchumi wa taifa letu kwa ujumla.
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-

Ujenzi wa chujio la maji katika Bwawa la Manchira, ambalo ni chanzo pekee cha maji katika Mji wa Mugumu, Wilayani Serengeti umechukua muda mrefu sana na kusababisha wananchi kukosa amani na kupata maji yasiyokuwa na ubora kwa matumizi ya binadamu:-

(a) Je, Serikali ina kauli gani juu ya ujenzi wa chujio hilo na lini litakamilika?

(b) Je, ni lini Serikali itakamilisha mfumo wa usambazaji maji toka Bwawa la Manchira ili kuwafikishia wananchi wote wa Mji wa Mugumu na maeneo ya jirani huduma ya maji?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli ujenzi wa chujio katika Bwawa la Manchira umechukua muda mrefu, sababu kuu ikiwa ni upungufu uliojitokeza katika usanifu wa chujio na udhaifu katika uwezo wa kifedha wa mkandarasi aliyekuwa anatekeleza mradi huo. Kutokana na mwenendo usioridhisha wa utekelezaji, Wizara na kuzingatia ushauri wa kitaalam mnamo tarehe 8/1/2020 iliamua kuvunja mkataba wa ujenzi wa chujio hilo.

Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) na Mugumu (MUGUWASA), zimeelekezwa kutathimini na kupitia gharama zinazohitajika ili kukamilisha ujenzi wa chujio hilo kwa kutumia wataalam wa ndani (Force Account). Wizara itatoa fedha zitakazohitajika kukamilisha ujenzi wa chujio hilo linalohudumia Mji wa Mugumu.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wote wa Mji wa Mugumu na maeneo ya jirani, Serikali kupitia fedha za mkopo kutoka India, itakarabati na kupanua mtandao katika Mji wa Mugumu. Usanifu wa awali umefanyika ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa matenki mawili ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa mita 5,000 na 500, ulazaji wa bomba zenye vipenyo mbalimbali zenye urefu wa kilomita 200 na kutoka urefu wa sasa wa kilomita 42 na ukarabati mkubwa wa bomba za sasa na uboreshaji wa chujio.