Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe (17 total)

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza na nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa sababu kuu za ufaulu duni ni miundombinu mibovu ya ufundishaji na kujifunza. Je, Serikali imeweka mkakati gani kwa shule za Njombe?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa waathirika wakuu ni wasichana, kwa sababu wanapewa kazi nyingi na wazazi wao majumbani, je, Serikali ina mkakati gani kumsaidia mtoto huyu wa kike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la miundombinu mibovu, hili ni kama tulivyosema katika bajeti yetu ya mwaka huu wa fedha kwamba tumeelekeza katika maeneo mbalimbali ili angalau kuongeza speed kwenye hii changamoto tuliyo nayo hivi sasa ya wanafunzi wengi sana tuliowasajili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo vilevile kuwafanya walimu wafundishe katika mazingira rafiki. Ndiyo maana katika bajeti ya mwaka huu mkoa wa Njombe peke yake tumetenga kiwango cha fedha cha kutosha ili kuhakikisha maeneo mbalimbali yanaweza kufikiwa. Ndiyo maana tukifanya rejea ya bajeti yetu tuliyopitisha hapa hapa, siwezi kukupa takwimu halisi, lakini tumeugusa Mkoa wa Njombe kuangalia kipaumbele hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la miundombinu Mheshimiwa Mbunge nadhani na wewe ni mpiganaji mzuri katika eneo hilo. Ukiachia miundombinu, vilevile miongoni mwa mambo ambayo yanachangia sana ni suala zima la malezi. Wakati mwingine wazazi wanakuwa irresponsible, hawawajibiki vya kutosha kuhakikisha watoto wao wanawasimamia kwa karibu.
Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie wakati napita pita maeneo mbalimbali, kuna maeneo mengine utakuta madarasa yapo ya kutosha, hali kadhalika walimu wa kutosha lakini shule zile tulizozipitia hakuna hata mwanafunzi aliyepata division one au division two. Kwa bahati mbaya zaidi unaweza kukuta walimu wengi wa sayansi hakuna lakini wa arts wapo na bado huwezi ukaona “C” moja au “B” moja ya Kiswahili wala ya civics; ni kwamba concentration ya watoto imekuwa chini. Kwa hiyo, jukumu letu kubwa sambamba na kuongeza miundombinu tuna changamoto kubwa ya kuwahamasisha wazazi kusimamia suala zima la taaluma za watoto wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuwaokoa vijana wetu wa kike. Ni kweli suala la mimba kwa watoto wa kike limekuwa kubwa, ndiyo maana mchakato wetu sasa hivi ni tunajielekeza katika ujenzi wa shule za sekondari za bweni hasa kwa upande wa wanawake. Lengo letu ni kuhakikisha zile changamoto zinawapata watoto wanapokwenda shuleni ziweze kupungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Afya wiki iliyopita alisema kwamba wale mabaradhuli wanaohakikisha wanaharibu watoto wa watu, tuhakikishe wanachukuliwa hatua kali ili hawa watoto wa kike waweze kupata elimu yao kama ilivyokusudiwa.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli sijaridhika kabisa na majibu ya Naibu Waziri, Jeshi la Zimamoto linafanya kazi katika mazingira magumu sana. Mfano, Mkoa wangu wa Njombe hawana ofisi, wanatumia majengo ya Idara ya Maji, hawana magari; na tukiangalia Mkoa wa Njombe kijiografia umekaa vibaya sana na matukio ya moto ni mengi.
Nilikuwa nataka kujua time frame, ni lini Serikali itatoa vifaa au vitendea kazi kwa Jeshi la Zimamoto?
Swali langu la pili, kwa kuwa huduma ya Zimamoto iko zaidi mijini, lakini matatizo ya moto yako mengi sana vijijini. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha hata watu wa vijijini wanapata huduma hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi kwamba tuna matatizo ya ofisi pamoja na vitendea kazi nchi nzima kwa Jeshi la Zimamoto; na ukiangalia katika Wilaya zote takribani za nchi nzima kwa upande wa Tanzania Bara ni Wilaya 20 ambapo kuna Ofisi za Zimamoto mpaka sasa hivi pamoja na magari.
Hata hivyo, Serikali imefanya jitihada kubwa sana kuhakikisha kwamba tunatanua wigo ili huduma hizo ziweze kufika mpaka vijijini na ndiyo maana tuna mpango sasa hivi wa kuhakikisha kwamba tunapeleka huduma za Zimamoto katika Wilaya zote nchini hatua kwa hatua kwa kuanza kupeleka Maofisa ili waweze kutoa elimu na baadaye kadri vifaa vitakavyopatikana tutapeleka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na magari pamoja na vitendea kazi, katika bajeti ya mwaka huu tumetenga takriban shilingi bilioni 1.5 kununua magari mawili, tutaangalia ni maeneo gani ya kipaumbele tuweze kupeleka.
Naomba nichukue fursa hii kumwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutashauriana na Makao Makuu Idara ya Zimamoto tuone uharaka wa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna mpango mwingine, tunafanya mazungumzo sasa hivi na Austria pamoja na Belgium, Kampuni ya SOMAT ya Belgium ili kuweza kupata mkopo wa Euro bilioni tano pamoja na Euro milioni 1.9 ambazo zitasaidia kuweza kununua vifaa viweze kupunguza makali ya upungufu wa vifaa katika maeneo mbalimbali nchini mwetu.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-
Swali la kwanza, kwa kuwa tatizo la pembejeo
limekuwa la muda mrefu na ni sugu katika Mkoa wetu wa Njombe. Je, Serikali iko tayari sasa kuanzisha Kiwanda cha kutengenezea mbolea katika Mkoa wa Njombe?
Swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Njombe ni kati ya
Mikoa inayotoa viazi au inayolima viazi kwa wingi; Njombe peke yake inalima au inatoa viazi tani 900,000 kwa mwaka, lakini tatizo ni kwamba soko limeingiliwa na watu wa Kenya.
Je, Serikali iko tayari sasa kuwazuia watu wa Kenya wasilete viazi nchini Tanzania ili wakulima wetu wa viazi waweze kuwa na soko zuri?
NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Serikali kujenga Kiwanda cha Mbolea Njombe; Serikali ya Awamu ya Tano inahamasisha ujenzi wa uchumi wa viwanda, kwa hiyo, tuko tayari kushirikiana na Mbunge pamoja na wadau wengine wowote ambao wanataka kuanzisha Kiwanda cha Mbolea- Njombe. Vilevile ni lazima niseme kama nilivyosema, tunategemea bei ya pembejeo ishuke kuanzia mwaka unaokuja kwa sababu karibuni tutaanza utaratibu wa kuagiza mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement). Kuhusiana na suala la ushindani wa Wafanyabiashara kutoka Kenya; kimsingi tunabanwa na itifaki za Kikanda kuhusiana na biashara, kwa hiyo ni vigumu moja kwa moja kuwazuia wakulima wa Kenya isipokuwa tunachofanya ni kujenga mazingira ambayo wakulima wetu wanaweza wakazalisha kwa tija ili waweze kushindana na wafanyabiashara wengine kutoka Kenya.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nipende tu
kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba ushindani siyo mbaya na mara nyingi Wakenya wanapokuja kununua viazi kutoka kwetu ni kwa sababu kuna tofauti kati ya msimu wa viazi kuzalishwa Njombe na Kenya, kwa hiyo tusiogope
ushindani lakini tujizatiti zaidi tuweze kuzalisha kwa tija ili tuweze kushindana.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, katika Mkoa wa Njombe kuna matatizo makubwa sana ya mawasiliano hasa maeneo ya mwambao katika Wilaya ya Ludewa kama Rupingu, Ibumi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea minara watu wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyoshirikiana na Mbunge wa Jimbo la Ludewa katika kuhakikisha kwamba eneo la Mwambao linashughulikiwa kikamilifu. Kwa sababu swali hilo limeulizwa muda siyo mrefu na tumelijibu hapa likiulizwa na Mheshimiwa Deo Ngalawa na leo linaulizwa na Mheshimiwa Lucia Mlowe nawashukuruni sana kwa ushirikiano wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekuwa nikilijibu kupitia Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo kwamba eneo hilo tutahakikisha tunajenga minara katika kipindi hiki na itakapofika mwaka 2020 tatizo hilo tutakuwa tumelitatua. Siyo hilo tu na lile lingine la kutoboa barabara katika ukanda ule wa Ziwa, tutakuwa tumeshashughulikia hayo matatizo.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri amekuwa akiahidi kila siku juu ya bili kupanda kwa wananchi wetu. Hapa ninavyoongea nina bili ya maji ya shilingi 700,000 ambapo maji hayatoki lakini unaletewa bili.
Sasa naomba kujua, je, ni lini, tunaomba ututajie kabisa Mheshimiwa Waziri utatekeleza ahadi hii kwa wananchi wetu kwa sababu wanaumia sana? Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Bili hii ni ya miezi mitatu, lakini maji hayatoki kabisa. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshatoa maelekezo kwenye mamlaka zote kwamba haiwezekani mtu akalipa bili ya maji ambayo hajatumia. Kwenye mamlaka zote tumeweka bodi za kusimamia uendeshaji wa mamlaka zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba sana ndugu zangu, kama kuna mtu ambaye kapelekewa bili ambapo hakupata maji, basi mahali pa kupeleka ni pale kwenye bodi, maana hili ni suala mahususi ili liweze kushughulikiwa. Hatuwezi kuwa na jibu la moja kwa moja kwa sababu siyo wote wanaopata bili ya maji ambayo hawajatumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna special case, naomba uniletee. Pia Mheshimiwa Mbunge akiwa kwenye Jimbo lake apeleke kwenye mamlaka ile, hasa kwenye Bodi ya Wakurugenzi inayosimamia uendeshaji wa mamlaka hizi ili mtu alipie maji aliyotumia tu, kulingana na Sera yetu ya Maji ya mwaka 2002 na Sheria Namba 12 ya mwaka 2009, kwamba ni lazima wananchi tutachangia huduma ya maji. Sasa katika kuchangia ni pamoja na kulipa bili, lakini kama bili ina mzozo, basi tutalishughulikia jambo hili na kuweza kulimaliza.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza na nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali ilitembelea katika kiwanda hicho na kujionea migogoro katika kiwanda hicho na waliahidi kusaidia kutatua tatizo la migogoro hiyo haraka iwezekanavyo, je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
Swali la pili, kwa kuwa moja ya tatizo katika kiwanda kile ni kutokuwa na Bodi yenye uwiano kati ya mwekezaji na MUVYULU, je, Serikali itawasaidiaje wananchi wale kuhakikisha kunakuwa na uwiano wa bodi ili waweze kupata gawio na kuweza kuwaendeleza wale wakulima? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikiano, vile vyama vyenu vya MUVYULU vimekwenda mahakamani. Kwa sababu kesi iko mahakamani, suala lako (a) na (b) mimi mikono yangu inakuwa nje, siwezi kuliingilia. (Makofi)
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, wananchi wapatao 200 wa Makambako Kata ya Kivavi, Mtaa wa Mashujaa waliondolewa katika maeneo yao mwaka1997 bila kupewa fidia, kwa ajili ya kupisha ujenzi wa soko la kimataifa, wamefuatilia wananchi hawa lakini hadi leo hakuna majibu. Pia kuna wananchi wa Idofi waliondolewa maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa mizani hadi leo hawajapata fidia.
Je, Serikali inampanga gani wa kuwalipa wananchi hawa fidia zao?
Swali la pili, kwa kuwa kila Halmashauri kuna Maafisa Mipango Miji. Je, ni kwa nini wananchi wanajenga sehemu zisizo sahihi na Serikali inawaangalia tu mwisho wa siku wanaanza bomoa bomoa? Naomba kupata majibu (Makofi).
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na sehemu yake ya kwanza wananchi 200 wa Makambako na wale wa Kidozi kwamba walipisha miradi ya Serikali na mpaka leo hawajalipwa fidia. Naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mlowe kwamba mara pesa zitapopatikana watalipwa, kwa sababu Serikali inatambua kwamba ililitwaa lile eneo kwa ajili ya matumizi ya Serikali, kwa hiyo, asiwe na wasiwasi pesa ikipatikana watalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili anaongelea habari ya maafisa kwamba watu wanajenga ovyo na wanaangalia na hakuna hatua zinazochukuliwa baadae wanakuja kuwabomolea. Naomba nitoe rai tu kwa sababu pia ni sehemu ya Halmashauri na tunakaa katika vikao vyetu vya Halmashauri kwa maana ya Baraza la Madiwani, haya yanapotokea ni wajibu wetu pia kutoa maonyo kwa wale ambao wamepewa wajibu huo wa kufanya kazi lakini hawasimamii sawasawa. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge atakapokuwa amekaa katika Baraza lake la Madiwani wajaribu kuwakumbusha hasa wale watendaji ambao hawatimizi wajibu wao vizuri.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Kwa kuwa, katika Halmashauri ya Njombe Mji kuna tatizo kubwa la maji na Serikali imekuwa ikiahidi kuwasaidia wananchi kutatua tatizo hili la maji kupitia mradi wa Hagafilo lakini hakuna dalili yoyote.
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kutekeleza mradi huo ambao imekuwa ikiwahaidi wananchi siku zote? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Njombe ni miongoni wa Miji 17 itakayofaidika na mkopo kutoka Serikali ya India wa dola milioni 500, kwa hiyo nikukuakikishie pamoja na wananchi wa Njombe kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshajipanga tayari, mwaka wa fedha unaokuja tutasaini mikataba na kuekeleza mradi wa kuchukua maji kutoka mto Hagafilo na kuhakikisha kwamba Mji wa Njombe sasa unakuwa na maji.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona.
Kwa kuwa katika Mkoa wa Njombe na hasa katika Halmashauri ya Mji wa Njombe kumekuwa na tatizo kubwa sana la maji kwa muda mrefu, kuna mradi wa Hagafilo ambao wananchi wale waliahidiwa kwamba wataletewa mradi huo na kwamba fedha zingetoka huko India lakini hadi sasa hakuna chochote kinachoendelea. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ni kweli Mji wa Njombe unapata huduma ya maji kutoka kwenye Mto unaopita pale Njombe na hiyo huduma haitoshelezi, lakini ni kweli kwamba Mji wa Njombe ni kati ya Miji 16 ambayo itafaidika na mkopo kutoka Serikali ya India.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ni kwamba kinachoendelea ni kwamba Kamati ya Madeni Hazina imeshakaa na kuridhia mkopo huo wa dola milioni 500. Kwa sasa Serikali kupitia Hazina wanakamilisha taratibu za kusaini ile financial agreement, pia Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji sasa hivi inaandaa makandarasi watakaofanya usanifu wa haraka ili tuweze kuwaza tenda kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya huo mradi kukamilika nikuhakikishie Mheshimiwa Mlowe kwamba Mji wa Njombe sasa utakuwa na maji ya uhakika ambayo wananchi watapata maji safi na salama kwa wakati wote.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri bado kuna malalamiko makubwa juu ya dawa hizo zilizopitwa na wakati na bado watu wanapata dawa zilizopitwa na wakati. Hapa katika jibu lake amesema kuna watu wanaofuatilia, je, ni nani anaeyefanya monitoring ya Kamati hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna wagonjwa ambao mpaka sasa hivi wanapata matatizo kwa sababu vituo vyao ni mbali, wanatembea umbali mrefu na wengine wanakata tamaa wanaamua kuacha dawa. Je, Serikali ina mkakati gani kuongeza vituo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza nani anayefanya monitoring ya Kamati hiyo. Kwanza hii Kamati ya Dawa ni Kamati ambayo ipo kwenye kila kituo na Kamati hii inahusisha Watumishi kwa maana ya wataalam kwenye kituo husika lakini pia inahusisha wawakilishi wa wananchi ambao wanaingia kwenye Kamati hiyo ili kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma za afya kwenye kituo.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, hii ni Kamati shirikishi na ushirikishi wake unaifanya Kamati hii ipate uhalali wa macho ya wananchi kwa sababu wananchi moja kwa moja wamewakilishwa na kwa msingi huo wanajua wanachokipokea na wanashiriki aidha, kwa kusaini ama kwa kushuhudia mtu ambaye anasaini nyaraka hizo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama kuna upungufu wowote ule ambao unaweza kuwa umejitokeza, basi ushiriki wa wananchi kwenye eneo hilo utakuwa ni mdogo. Nitoe rai kwa Mheshimiwa Mbunge ashiriki yeye pamoja na Baraza la Madiwani kufanya ufuatiliaji wa kazi inayofanywa na Kamati ya Dawa ya kila Kituo na kwa kufanya hivyo tutakuwa tumetimiza wajibu wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jibu letu ni kwamba, wanaofanya Monitoring ni wenye mali, wenye mali ni wanaomiliki Kituo husika na wanaomiliki kituo husika, maana yake ni wananchi na wananchi wamehusishwa humo ndani na wawakilishi wa wananchi, ni wasimamizi wa vituo vyao vyote ndio maana wanaenda kufanya supportive supervision kila mwezi na kuna bajeti kwenye Halmashauri zote nchini ya kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu mkakati ya Serikali kuongeza vituo, kwanza kusema umbali ni mrefu sana hapana, kwa sababu toka Alma-Ata declaration hata kabla ya hapo toka Afya kwa wote miaka hiyo ya 70 Serikali imekuwa ikiongeza idadi ya Vituo siku hata siku na mwishoni tumekuja kuweka hili Azimio kwenye Ilani ya Uchaguzi kwamba tutajenga Kituo cha Afya kwenye kila Kata na Zahanati kwenye kila Kijiji ambalo sasa hivi tuko mbioni kutekeleza kwa kiasi fulani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, uwezo wetu wa kuwa na vituo ambavyo vipo karibu na wananchi umeongezeka sana toka miaka hiyo ambayo naisema ya Azimio la Afya kwa wote la miaka ya 1971 – 1972 na kwamba kuna umbali mrefu, hapana. Sema tumejiongezea malengo, sisi wenyewe tumeongeza target, targets za zamani zilikwishafikiwa na Serikali zilizopita, kwa hiyo tunachokifanya sasa hivi ni kuboresha huduma na kuongeza tena vituo vingi zaidi, lakini hakuna umbali mrefu.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kukanusha hilo ili kuweka sawa. Pia mkakati wetu ni huo ambao nimeusema wa kujenga Kituo cha Afya kwenye kila Kata na Zahanati kwenye kila Kijiji.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza, nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza; kwa kuwa kiwanda cha mbolea hakiwezi kujengwa Njombe kutokana na kutopatikana kwa malighafi; na kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Njombe wanalima mwaka mzima, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha mbolea inapatikana katika Mkoa wa Njombe kila wakati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Njombe mwaka jana wamelima kwa wingi mahindi ambayo yamekosa soko na hata mwaka huu bado wamelima mahindi kwa wingi yatakosa soko vile vile. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha inawatafutia soko la uhakika hawa wananchi wa Mkoa wa Njombe?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Serikali imekuwa ikifanya hivyo kuhakikisha kwamba mbolea inapatikana na si mara moja Waziri wa kilimo amekuwa akitoa taarifa juu ya upelekaji wa mbolea katika maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili kuhusu suala la masoko ya mahindi; kimsingi nizidi tu kuwakumbusha, ni kwamba Serikali imekuwa ikiendelea kutafuta masoko. Pamoja na kutafuta masoko tunazidi kusisitiza kuhakikisha kwamba mbali ya kuuza mahindi yakiwa ghafi ni vyema kuhakikisha kwamba mahindi hayo kwanza yanatengenezwa kama unga au chakula cha mifugo au kuhakikisha kwamba yameongezwa thamani badala ya kuyasafirisha mahindi ghafi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ambayo inapenda kusafirisha mali zake zikiwa ghafi kwa kweli si nchi ambayo itaweza kupiga hatua kubwa katika uchumi hususani katika malengo ya nchi, haya ya uchumi huu wa viwanda.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Niombe tu kuliarifu Bunge kwamba katika muda wa wiki moja ijayo tutafanya semina ya Bunge zima kuwaeleza mchakato mzima wa upatikanaji wa mbolea nchini. Tunatumaini kwamba katika semina hiyo Wabunge sasa tutakuwa tumekuwa na uelewa wa pamoja wa nini Serikali inafanya na kama zipo changamoto, basi hiyo itakuwa fursa nzuri ya kuzijadili ili tuweze kwenda kwa pamoja sawasawa.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu ya Waziri naomba niulize kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa watumishi wa Jeshi la Zimamoto wanafanya kazi katika mazingira magumu na mazingira hatarishi, lakini hawana vifaa vya kufanyia kazi. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha watumishi hawa anapata vitendea kazi nchi nzima?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Mkoa wa Njombe hadi sasa Jeshi la Zimamoto hawana Ofisi, je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inajenga Ofisi pale Njombe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna changamoto ya vifaa ama vitende kazi kwenye Jeshi la Zimamoto na tunafanya jitihada mbalimbali kukabiliana na changamoto hiyo. Moja katika jitihada ambazo tunafanya ni kutenga fedha kwenye bajeti yetu kila mwaka ili kuweza kununua vifaa zaidi ikiwemo magari na vitendea kazi vingine mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, vile vile tunajaribu kuimarisha mahusiano kati ya Jeshi la Zimamoto kupitia halmashauri pamoja na majiji mengine. Wakati huo huo tumekuwa tukibuni mikakati mbalimbali ikiwemo mikakati ya kuweza kuchukua program za mikopo ambazo sasa hivi tuna mchakato ambao unaendelea. Nisingependelea kuzungumza sasa hivi kwa sababu haujafikia katika hatua ya mwisho, lakini ni moja katika jitihada ambazo tunafanya kuhakikisha kwamba Jeshi la Zimamoto linapata vifaa.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la Njombe, ni changamoto ya Ofisi katika mikoa hii mipya. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalifahamu hilo na tunalichukulia kwa uzito na pale ambapo hali ya kifedha itaruhusu tutakabiliana na changamoto ya Ofisi katika Mkoa wa Njombe na mikoa mingine hususani mikoa mipya.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza, nina maswali mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Waziri amekiri kwamba kuna tatizo la upotevu wa maji kutokana na miundombinu mibovu. Hivi navyoongea bado kuna tatizo kubwa sana la uvujaji wa maji, mfano, Kisasa kuna mabomba hivi sasa yanaendelea kutiririsha maji lakini sioni juhudi inayoendelea hadi sasa hivi. Je, wana mkakati gani kuhakikisha tatizo hili linatatuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Jimbo la Njombe Kusini, Kata ya Ihungilo kuna mradi wa Utengule – Ngalanga ambao vifaa vilivyonunuliwa vilinunuliwa chini ya kiwango na hadi sasa hivi vifaa hivi, mabomba na viungio vyake vinaendelea kutitirisha maji na wananchi wanakosa huduma ya maji. Je, Waziri yuko tayari kwenda kutatua tatizo hili katika Kata hii ya Ihungilo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mlowe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, upotevu wa maji ni changamoto kubwa kwa sababu lina sehemu mbili, kwanza ni miundombinu yenyewe na pili ni wafanyakazi tunasema non commercial revenue water losses ambalo linatokana na baadhi ya wafanyakazi kushirikiana na wananchi katika kuiba maji. Tunapamba na mambo yote haya mawili na kuhakikisha kwamba tatizo la upotevu wa maji linamalizika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema sasa hivi kuna changamoto hizo lazima mtu akiona changamoto hiyo tuwasiliane na Mamlaka za Maji, tuwape taarifa ili waweze kwenda kumaliza tatizo hilo. Kila kwenye Mamlaka ya Maji tumeweka toll free number ambayo ni namba ya simu ambapo unaweza kupiga simu bure kueleza wapi kuna tatizo la upotevu wa maji na mara moja utakapofanya hivyo sisi tutachukua hatua za kuweza kupambana na upotevu huo wa maji. Hili la Kisasa kama alivyosema Mheshimiwa naamini wataalam wangu wamesikia na watakwenda kulishughulikia mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuhusu vifaa vilivyo chini ya kiwango. Ni kweli kabisa katika miradi mingi sana iliyojengwa vijijini, vifaa vingi vilivyopelekwa na wakandarasi viko chini ya kiwango na tumechukua hatua mbalimbali za kisheria na tutaendelea kuchukua. Naomba tu nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda pamoja tuhakikishe kwamba tatizo hili tunaliondoa ili wananchi wale waweze kupata maji safi na salama.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwenye jibu lake la msingi kwamba watumishi wanapaswa kulipwa mafao yao hata kama hawakuwa wanakatwa, lakini hilo halifanyiki. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba hawa watumishi wanapata mafao yao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa watumishi wastaafu wanapata pensheni yao ndogo sana, kuna watumishi wanapata Sh.50,000 kwa mwezi, kwa kweli kiasi hicho ni kidogo sana. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inaongeza kiasi hicho cha pensheni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba hili jambo analosema halifanyiki, siyo sahihi. Kwa sababu watumishi wote ambao waliajiriwa na walikuwa hawachangii kabla ya Mfuko wa Pensheni wa PSPF kuanzishwa walikuwa wakilipwa na Serikali Kuu kupitia Hazina. Kwa sasa kile kilichokuwa kinalipwa kupitia Hazina ndicho kimeunganishwa na malipo yao ya PSPF na wanalipwa pensheni yao yote kama ambavyo wanastahili kulipwa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, sina uhakika sana labda nikae na Mheshimiwa Mbunge ni wastaafu gani wanaolipwa pensheni ya Sh.50,000, kwa sababu Serikali iliongeza pensheni ambayo ni kiwango cha chini kutoka Sh.50,000 kwenda Sh.100,000 na Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii inalipa Sh.100,000 kwa watumishi wote kama kiwango cha chini. (Makofi)
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba kiwanja hicho kilijengwa kabla ya uhuru; na kwa kuwa kiwanja hicho kilijengwa kabla ya makazi ya watu hayajasogea maeneo yale na sasa hivi maeneo yale yamejaa makazi ya watu; na kwa kuwa Liganga na Mchuchuma ndiyo mradi ambao unakaribia sasa kuingia katika Mji wetu wa Njombe. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kukihamisha kiwanja hicho na kupeleka sehemu za Tanwati au Mgodeti, ama Ilembula? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS JOHN KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mlowe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali tunatambua umuhimu wa kujenga kiwanja hiki. Pia nafahamu Njombe ina fursa nyingi za kiuchumi, mojawapo Mheshimiwa Mbunge ametaja, tunafahamu pia uhitaji wa huduma hii ya usafiri, hususan wa ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu, suala la ujenzi wa uwanja huu pia mimi mwenyewe nimetembea Njombe, nimefanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa, lakini mara nyingi nimefanya mazungumzo na Mbunge wa Jimbo Mheshimiwa Mwalongo. Kwa hiyo, tulijaribu kuona namna bora ya kuweza kuendeleza uwanja huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mahitaji ya kuendeleza uwanja huu bado yapo, kwa sababu kwenye taarifa ile ya usanifu kama ingeonesha kutokuwa na mahitaji ya kuendeleza kiwanja hiki katika eneo hili, basi ningeshauri namna tofauti. Hata hivyo, jambo hili kama wana Njombe mtaona kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa mnaweza, mkalizungumze mlilete.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakutahadharisha tu kwamba kwa sababu kulikuwa kuna hatua ambayo imefikiwa na kuna gharama ambazo kama Serikali tumetumia kwamba kuhamisha uwanja huu kupeleka maeneo mengine kunaweza kupoteza fursa ambayo ilikuwa iko tayari imeshapatika kwa sababu inaweza ikatahitaji muda mrefu kufanya usanifu mpya na wananchi hawa wanahitaji huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri tu kwamba uwanja huu tuujenge na kama mtahitaji kuwa uwanja mkubwa, mzungumze katika level ya Mkoa halafu ushauri wenu muulete, sisi kama Serikali tutauzingatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba hadi sasa amefikia asilimia 25.2 barabara inayokwenda Njombe - Makete na asilimia 20 barabara ya Itone – Ludewa: Je, kama sasa hivi ni asilimia 25 na mwakani mwezi wa kwanza iwe imekamilika, ni muujiza gani utatendeka hapo kuikamilisha kwa miezi nane tu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Hali ya barabara za Njombe Mjini na Vijijini ni mbaya sana kwa kuwa mvua sasa hivi zinaendelea kunyesha. Kuna hali mbaya sana kwenye zile barabara na watu sasa hivi wamesimamisha shughuli, hawawezi tena kusafirisha bidhaa au mazao: Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inakarabati barabara hizi kwa haraka iwezekanavyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba tuko asilimia hizo 25.2 na asilimia 20 kwa eneo la Itone – Ludewa, lakini labda nilifahamishe tu Bunge lako kwamba Mkoa wa Njombe hali ya jiografia yake ni maalum sana, ni special. Udongo wa Njombe siyo mchezo, kwa hiyo, hata kufikia asilimia hizi ilitakiwa Mheshimiwa Mbunge aipongeze Serikali. Ndiyo unaona kwamba barabara hii ambayo tunaijenga Lusitu - Mawengu ni barabara chache sana tumeweza kujenga kwa kiwango cha zege.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kutokana hata na udongo wake tuliotumia kwa ujenzi, ulikuwa unatoka zaidi ya kilometa 200, kwa sababu udongo wa Njombe uko maalum kidogo. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango kazi ambao sisi kama Serikali tunausimamia, tutahakikisha kwamba kila wakati tunakwenda nao ili kama kutatokea zile natural calamity kama mvua kuwa nyingi, kama maporomoko katika maeneo haya, hata juzi tu barabara hii ilijifunga kwa sababu udongo wake unaporomoka sana. Kwa hiyo, nasi tunachukua hatua kila wakati ili kuhakikisha kwamba tunafanya marekebisho, ujenzi unaendelea, tukamilishe mradi huu kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ule mpango kazi yaani action plan tutaendelea kuisimamia ili kuona kama kutakuwa na matatizo makubwa ya hali ya hewa tuangalie alternative ya kufanya barabara hii ikamilike na barabara hii wananchi wa Njombe na Watanzania wanaitumia. Kwa hiyo, miujiza ni ile ya Mungu kwamba tunasimamia vizuri na mvua ziwe nzuri, tuombe Mungu pamoja ili tukamilishe barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu (b), amesema barabara za vijijini hali ni mbaya. Ni kweli kama nilivyosema, hali ya jiografia ni mbaya, lakini sisi tumejipanga vizuri ndiyo mana utaoa kwamba tunao mpango kama tukipata fedha tutaanza kutengeneza hii barabara ya kipande cha kutoka Kibena kwenda Lupembe kwenye mpango wa manunuzi tunaoendelea nao, kilometa 50, tuanze kupunguza na kuwafanya wananchi wa maeneo ya Njombe waweze kwenda Morogoro kupitia Madeke na Mlimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, yale maeneo ambayo yako korofi sana, tunaendelea kujenga barabara za zege kwa hiyo, zipo kilometa 126, ukitoka Lupembe pale ziko kilometa ambazo tunaendelea kuziunganisha na wananchi sasa wana-enjoy magari yanatoka Mlimba yanakuja Njombe. Kwa hiyo, ni hatua za Serikali kuwajali wananchi wa Njombe kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge, hata hii barabara tunayozungumza ya kutoka Mawengi – Lusitu, sehemu ya Itoni kwenda Lusitu na yenyewe tunaitazama kwa sababu ni muhimu tuwaunganishe vizuri. Pia tunatengeneza daraja kule Mto Ruhuhu ili wananchi hawa wa Njombe tuwaunganishe vizuri na wenzao wa Manda kule Ruvuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwa ufupi kwamba tumejipanga vizuri, Njombe iko so special lakini nasi kama Serikali tuko special kwa ajili ya Njombe ili wananchi wapate huduma vizuri.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la maji katika Mkoa wa Njombe bado ni kubwa sana. Maeneo mengi, vijiji vingi havina maji na hata Njombe Mjini bado tatizo la maji ni kubwa, je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuleta maji Njombe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Wizara tunatambua moja ya maeneo yenye changamoto ni eneo la Njombe, lakini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona haja kabisa ya kutupatia fedha zaidi ya dola milioni 500 kwa miji 28. Katika miji hiyo, mmojawapo katika Mji wa Njombe.

Nataka nimhakikishie tumekwishaandika mkataba haraka kwa maana ya wahandisi washauri wapo katika maeneo mbalimbali, itakapofika mwezi wa tisa wakandarasi wote watakuwepo site, nataka nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, itakapofika mwezi wa tisa wakandarasi watakuwa site katika utekelezaji wa mradi wa maji katika eneo la Njombe. Ahsante sana.