Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Zubeda Hassan Sakuru (13 total)

MHE. HALIMA A. BULEMBO (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la matukio ya kihalifu nchini yanayohusishwa pia na upatikanaji wa hati za kusafiria zaidi ya moja zinazotolewa hapa Tanzania kwa baadhi ya wahalifu kiholela:-
Je, Serikali inachukua hatua gani katika udhibiti wa utoaji hati za kusafiria kiholela?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji hutoa Pasipoti na Hati za Kusafiria kwa raia yeyote wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Pasipoti na Hati za Kusafiria Na. 2 ya mwaka 2002 ili mradi amekidhi matakwa ya sheria hiyo. Pasipoti na Hati za Kusafiria hazitolewi kiholela kwa wahalifu kama Mheshimiwa Mbunge alivyouliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kutolewa Pasipoti au Hati ya Kusafiria, Idara ya Uhamiaji hufanya uchunguzi wa kujiridhisha kama mwombaji ni raia wa Tanzania na kama hana makosa kihalifu. Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji huchukua hatua zifuatazo ili kudhibiti utoaji holela wa Pasipoti pamoja na Hati za Kusafiria:-
(i) Kuwasiliana na idara mbalimbali ili kujiridhisha nyaraka zilizoambatishwa kwenye ombi la Pasipoti au Hati za Kusafiria mfano RITA;
(ii) Kuchukua hatua za kisheria na za kinidhamu kwa watumishi wanaobainika kujihusisha katika utoaji wa Pasipoti au Hati za Kusafiria kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu;
(iii) Kuweka masharti katika utoaji wa Hati za Kusafiria kwa mwombaji aliyeibiwa au kupoteza Hati za Kusafiria;
(iv) Kuwachukulia hatua za kisheria waombaji wa Pasipoti wanaotumia njia za udanganyifu;
(v) Kutuma taarifa za Pasipoti zilizopotea au kuibiwa kwenye Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) ili kuwakamata wahusika;
(vi) Kuimarisha mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu na takwimu za Watanzania walioomba na kupewa Pasipoti Makao Makuu ya Uhamiaji; na
(vii) Kuweka mfumo wa kielektroniki wa utoaji Pasipoti ili kuweza kutambua watu kwa usahihi na kuondokana na tatizo la kughushiwa kwa Pasipoti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Idara ya Uhamiaji pia hufuta Pasipoti za watu ambao wamepatikana na hatia za makosa ya biashara ya madawa ya kulevya, utakatishaji fedha, usafirishaji haramu wa binadamu, vitendo vya kigaidi au hata shughuli yeyote haramu kwa mujibu wa Sheria ya Pasipoti na Hati ya Kusafiria Na. 20 ya mwaka 2002.
MHE. PAULINE P. GEKUL (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Kuwepo na matukio ya vifo visivyokuwa vya lazima kunatokana na kutokuwepo kwa motisha kwa madaktari na wauguzi kwa kulipwa viwango duni vya mishahara na kutolipwa posho zao kwa wakati.
Je, Serikali inakabiliana vipi na changamoto ya maslahi kwa watumishi wa sekta hii muhimu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na madaktari, matabibu pamoja na wauguzi nchini ambapo Serikali imeendelea na jitihada zake za kuboresha mishahara ya watumishi wake mwaka hadi mwaka ikiwemo ya wataalam wa sekta ya afya kwa kuzingatia uwezo wa Serikali wa kulipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utafiti wa tathmini ya kazi na punde tathmini hiyo itakapokamilika, Serikali itapanga mishahara na motisha upya kwa watumishi wote wa umma wakiwemo wa sekta ya afya.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni shilingi 390,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kutokana na ukweli huu kati ya mwaka 2010/2011 hadi mwaka 2016/2017 vianzia mishahara kwa kada za wauguzi vimeongezwa kutoka shilingi 614,000 hadi kufikia shilingi 980,000 kwa mwezi kwa wahitimu wa shahada na shilingi 425,000 hadi shilingi 680,000 kwa wahitimu wa stashahada. Aidha, shilingi 260,000 hadi shilingi 432,000 zimekuwa zikilipwa kama kianzio cha mshahara kwa wahitimu wa astashahada.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vianzia mishahara kwa kada za madaktari na maafisa tabibu katika kipindi hicho vimeongezwa kutoka shilingi 886,800 hadi shilingi 1,480,000 kwa wahitimu wa shahada na shilingi 425,000 hadi shilingi 680,000 kwa wahitimu wa stashahada na mwisho shilingi 260,000 hadi shilingi 432,000 kwa wahitimu wa astashahada.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2016/2017, vianzia mshahara hivi ni vikubwa zaidi ikilinganishwa na vile vya watumishi wa Serikali Kuu na walimu kwa kuzingatia ngazi ya elimu zao kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Serikali Kuu kwa watumishi wenye astashahada wameanzia na shilingi 309,000; kwa walimu wameanzia na shilingi 419,000, kwa wauguzi wameanzia na shilingi 432,000; na kwa matabibu na madaktari wameanzia na shilingi 432,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa stashahada, Serikali Kuu kianzia mshahara kimeanza na shilingi 525,000, kwa upande wa walimu wenye stashahada ni shilingi 530,000, wauguzi shilingi 680,000/= na tabibu na madaktari shilingi 680,000. Kwa upande wa shahada, Serikali Kuu wameanzia na shilingi 710,000, walimu shilingi 716,000, wauguzi shilingi 980,000 na kwa upande wa matabibu na madaktari wenye shahada shilingi 1,480,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa wataalam wa afya na watumishi wote kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia viapo na maadili ya kazi zao. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi kwa kadri uwezo wake wa kulipa utakavyoimarika.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Kukua kwa soko huria katika utoaji wa huduma za anga nchini kumevutia na hivyo kuimarisha Sekta ya Usafirishaji wa abiria na mizigo. Baadhi ya Mashirika ya Ndege yamekuwa yakitoza nauli kubwa na hivyo kuongeza mzigo kwa watumiaji:-
Je, Serikali inatoa kauli gani dhidi ya ongezeko la nauli lisiloendana na uhalisia inayotozwa na baadhi ya Mashirika ya Ndege?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na sekta nyingine, nauli za ndege hutozwa kutegemeana na nguvu ya soko katika njia husika. Mpango uliopo ni kuongeza ushindani katika njia husika ili kupunguza nauli. Wizara yangu kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga imeendelea kutoa leseni kwa watoa huduma za usafiri wa anga ili kuleta ushindani kwa kutoa huduma zilizo bora na kutoza nauli ambazo abiria wanazimudu. Aidha, mamlaka huingilia kati kisheria kuweka kiwango kikomo pale tu inapoonekana kuna ukiritimba na wananchi wanaumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunakubaliana kuwa nauli kwa baadhi ya njia zilikuwa juu kutokana na kuwa na mtoa huduma mmoja. Baada ya Kampuni ya Ndege ATCL kuanza kutoa huduma katika njia hizo, nauli za ndege zimeshuka kutokana na ushindani. Kwa mujibu wa Ibara ya 25 ya Sheria ya Usafiri wa Anga (Civil Aviation Act, Revised Edition of 2006), Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) itaendelea kufuatilia kuchukua hatua pale inapobainika kuwa hakuna ushindani wa kutosha na wananchi wanatozwa nauli kubwa.
MHE. DEVOTHA M. MINJA (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Magereza mengi nchini hayapo katika viwango na ubora unaotakiwa na hivyo kuvunja haki za wafungwa.
Je, Serikali ina mkakati gani katika kufanya matengenezo na kulinda haki za wafungwa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Magereza limekuwa likitekeleza na kusimamia haki za wafungwa magerezani kwa kuzingatia Sheria ya Magereza Na. 34 ya mwaka 1967 (The Prisons Act. No. 34 of 1967 CAP. 58 R.E 2002) pamoja na sheria nyingine na Kanuni za Uendeshaji wa Magereza za mwaka 1968 (The Prisons (Prison Management) Regulations of 1968) G.N.19 of 23/01/1968 na marekebisho yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, haki za wafungwa zinazotekelezwa na kusimamiwa magerezani kwa mujibu wa Sheria ya Magereza na Kanuni zake nilizozitaja au msingi mwingine, chimbuko lake ni Mkataba wa Kimataifa unaohusu Taratibu na Haki za Wafungwa na Mahabusu. Haki hizo zimeainishwa wazi sehemu ya VII na IX ya Sheria ya Magereza na Kanuni za Uendeshaji wa Magereza kama ifuatavyo:-
(i) Haki ya kutenganishwa ambapo wafungwa hutenganishwa kutokana na umri wao, jinsia, aina ya kosa, afya na tabia.
(ii) Haki ya kupatiwa chakula na mahitaji mengine. Mfungwa hupewa chakula kama ilivyoainishwa na Kanuni za Uendeshaji wa Magereza niliyoitaja.
(iii) Haki ya kuwa na uhuru wa kupata mawasiliano na kutembelewa na ndugu na jamaa zake. Mawasiliano haya ni pamoja na kupokea na kuandika barua, kusoma magazeti na kusikiliza taarifa mbalimbali kutoka katika vyombo vya habari.
(iv) Huduma za afya. Huduma hizi hutolewa kwa mfungwa pindi anapoumwa wakati wote awapo gerezani.
(v) Haki ya kupatiwa malazi safi na ya kutosha ambapo mfungwa mmoja anahitaji eneo la mita za mraba 2.8.
(vi) Haki ya kukata rufaa pale anapoona hakutendewa haki katika hukumu iliyotolewa na Mahakama dhidi yake.
(vii) Haki ya kucheza michezo. Mfungwa anayo haki ya kushiriki na kucheza michezo ya aina mbalimbali na hii inafanyika magerezani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, zipo changamoto kwa Jeshi la Magereza zinazojitokeza katika kutekeleza baadhi ya haki hizo kutokana na msongamano wa wafungwa katika baadhi ya magereza na kutokana na hali halisi katika baadhi ya maeneo hayo niliyoyataja.(Makofi)
MHE. ZUBEDA H. SAKURU aliuliza:- Hivi sasa kumekuwa na wimbi la matukio ya ukamataji wa Wahamiaji haramu kwa wingi hapa nchini. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya ongezeko la matukio hayo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji imekuwa ikiendelea na mapambano dhidi ya wahamiaji haramu na kuwachukulia hatua za kisheria ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama. Katika kupambana na wahamiaji haramu Idara ya Uhamiaji huchukua hatua zifuatazo:-
(i) Kuendesha doria za misako ya mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini kwa kushirikiani na vyombo vya Ulinzi na Usalama ambapo katika mwaka 2016/2017 jumla ya watuhumiwa 9.581 na wahamiaji haramu walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali kisheria.
(ii) Serikali inaendelea kuimarisha vitendea kazi kama vile magari na kupanua wigo wa watumishi ili kuweza kudhibiti mipaka mingi iliyopo na kutoa elimu kwa umma juu ya madhara ya kuhifadhi wahamiaji haramu na kupambana na mitandao wa wasafirishaji haramu wa binadamu.
Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali ni kuendelea kuimarisha ulinzi wa mipaka na Serikali inaagiza wageni wote wanaoingia nchini wafuate sheria za nchi na wale ambao hawatafuata sheria hizo watachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na wale wanaojihusisha na usafirishaji na wale wanaowaficha wahamiaji haramu kuacha tabia hizo kwa sababu Serikali itachukua hatua kali punde itakapojiridhisha kwamba kuna watu wamefanya vitendo hivyo.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Baadhi ya Shule na Vyuo nchini vinaendelea kudahili wanafunzi pamoja na kutokidhi matakwa ya sheria mbalimbali.
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani kudhibiti vyuo na shule zinazoendelea kudahili wanafunzi huku zikiwa na mapungufu?
(b) Je, mpaka sasa ni vyuo vingapi na shule ngapi zilizofutiwa usajili kwa kutokukidhi matakwa ya kisheria.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina taratibu za kudhibiti ubora wa elimu na mafunzo yanayotolewa shuleni na vyuoni kupitia Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule katika maana ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. Baraza la Taifa la Elimu la Ufundi (NACTE) kwa vyuo na taasisi zinazotoa elimu ya kati na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa taasisi zinazotoa elimu ya juu. Shule na vyuo vinavyobainika kukiuka taratibu za utoaji elimu na mafunzo huchukuliwa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusitisha udahili wa wanafunzi, kusitisha programu zitolewazo, kupunguza idadi ya wanafuzni waliozidi na kufuta usajili wa taasisi husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018 Serikali imefuta usajili kwa shule saba za awali na msingi na shule moja ya sekondari. Vilevile vituo 16 vilivyokuwa vimedahili wanafunzi wa elimu ya awali na msingi kabla ya kusajiliwa viliagizwa kuwatawanya wanafunzi hao kwa kuwapeleka katika shule zilizosajiliwa na kufunga vituo hivyo. Katika mwaka 2016/2017 Serikali kupitia NACTE ilifanya uhakiki katika vyuo na taasisi 103 za elimu ya ufundi ambapo vyuo na taasisi 31 zilibainika kuwa na mapungufu na hivyo kufutiwa usajili.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha katika mwaka 2017/ 2018 uhakiki mwingine ulifanyika katika vituo, vyuo na taasisi 454 za elimu ya ufundi ambapo jumla ya vyuo na taasisi 59 za elimu ya ufundi zilibainika kuwa na mapungufu na hivyo walitakiwa kurekebisha mapungufu ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia tarehe Mosi Februari, 2018. Chuo kitakachoshindwa kurekebisha mapungufu yaliyobainishwa ndani ya kipindi kilichopangwa kitafutiwa usajili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa vyuo vikuu Serikali kupitia TCU ilifanya uhakiki wa vyuo vyote vya elimu ya juu nchini kati ya mwezi Oktoba, 2016 na Januari, 2017 ili kuhakiki ubora wa elimu inayotolewa vyuoni. Taarifa ya uhakiki ilionyesha mapungufu katika baadhi ya vyuo, kufuatia taarifa hiyo TCU kwa mwaka wa masomo 2017/2018 ilisitisha udahili wa wanafunzi wa Programu za Afya na Uhandisi kwenye vyuo vitano. Vilevile TCU ilisitisha udahili katika programu zote kwa mwaka wa kwanza kwa vyuo 14, aidha, katika mwaka huo wa masomo TCU imedhibiti na kuzuia vyuo vikuu kudahili wanafunzi katika programu ambazo hazijapata ithibati zipatazo 75 katika vyuo vikuu 22.
MHE. JOSEPH L. HAULE (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya muda mrefu katika kuimarisha ushiriki wenye tija kwa Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako naomba uniruhusu nitumie nafasi hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri kuipongeza timu yetu ya vijana ya Serengeti Boys kwa kuweza kufuzu kuingia mashindano ya nusu fainali katika mashindano ya CECAFA ambayo yanafanyika nchini Burundi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na timu zetu za michezo kuonesha kuwa matokeo yasiyoridhisha katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa, dalili za Tanzania kurejesha sifa yake ya zamani ya umahiri katika michezo zimeanza kuonekana baada ya mwanariadha wetu nyota Alphonce Simbu kushika nafasi ya tano katika mashindano ya mbio ndefu za Olympic Brazil mwaka 2016. Simbu na wanariadha wengine wa Tanzania waliendeleza rekodi hiyo ya ushindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Januari 2017, Simbu alinyakua medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Kimataifa ya mbio ndefu ya Mumbai – India; Aprili 2017 Cecilia Ginou Kapanga aliipatia Tanzania medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Beijing International Marathon nchini China; lakini vilevile tarehe 23 Aprili, 2017 Magdalena Chrispin Shauri alishika nafasi ya tano kati ya wanariadha 25,000 kwenye mashindano ya Hamburg Marathon nchini Ujerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Aprili, 2017 Emmanuel Ginouka Gisamoda alikuwa mshindi wa kwanza na kuipatia Tanzania medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Shanghai International Half Marathon. Lakini vilevile mwezi Aprili, 2017 Simbu alishika nafasi ya tatu kwenye mashindano makubwa ya London Marathon.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tumeona mafanikio yaliyojitokeza kwenye mchezo wa mpira wa miguu ambapo timu ya Taifa vijana Serengeti Boys ilifuzu kucheza fainali za michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 nchini Gabon na kufuta historia hasi tuliyokuwa nayo ya timu zetu kushindwa kufika ngazi hiyo kwa miaka yote 37.
Mheshimiwa Mwenyekiti, somo kubwa tunalojifunza ni umuhimu wa mazoezi toka umri mdogo hivyo mkakati wa Serikali wa muda mrefu ni kama ifuatavyo:-
(i) Kuimarisha michezo shuleni ili kuibua na kulea vipaji vinavyojitokeza. Hivyo basi, shule 56 za sekondari zilizoteuliwa mwaka 2013 na mwaka 2014 na Serikali kila mkoa kuwa shule za michezo hazina budi kuimarishwa kwa vifaa, ufundishaji na miundombinu ili ziweze kutekeleza wajibu wake.
(ii) Katika kuimarisha uongozi katika vyama vya mashirikisho ya michezo mbalimbali nchini kwa kuvisimamia kwa karibu ili vizingatie katiba na sheria za michezo.
(iii) Kuimarisha mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA ambayo ndiyo kisima kikubwa cha kuwapata wanamichezo wa michezo yote nchini. Ahsante. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Sherehe za Mwenge wa Uhuru zimeendelea kutumia fedha nyingi za walipa kodi huku Watanzania wengi wakiwa na maisha duni. Je, Serikali haioni umuhimu wa kurudisha Mwenge wa Uhuru katika Makumbusho ya Taifa na kuzifuta
sherehe hizo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenge wa Uhuru ni chombo kilichoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961 ikiwa ni tunu na ishara ya kuwepo kwa Taifa huru la Tanganyika. Dhana na falsafa ya Mwenge wa uhuru inatokana na maono ya mbali kupitia kwenye maneno yaliyosemwa tarehe 9 Desemba, 1961 nanukuu:-
“Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima mahali palipojaa dharau”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni umuhimu wa kuweka Mwenge wa Uhuru katika makumbusho ya Taifa na kuzifuta sherehe zake kwa sababu zifuatazo:-
a) Mbio za Mwenge wa Uhuru huwakumbusha Watanzania falsafa nzito ya Mwenge wa Uhuru inayotoa taswira ya Taifa ambalo Waasisi wetu walitaka kulijenga Taifa lenye amani, linalojitegemea na lenye kuheshimu misingi ya utu na usawa wa binadamu. (Makofi)
b) Mwenge wa Uhuru kupitia mbio zake umekuwa ni chombo cha kuchochea maendeleo ya wananchi, kwa mfano, kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, miradi ya maendeleo 6,921 yenye thamani ya shilingi trilioni 2.5 ilizinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi. (Makofi)
c) Kila mwaka, Mbio za Mwenge huambatana na ujumbe maalum unaohamasisha masuala muhimu ya Kitaifa kwa wananchi nchi nzima. Kwa mfano, kwa mwaka jana 2017 ujumbe ulikuwa “Shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu”. Mwaka huu wa 2018 ujumbe ni “Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu”. Aidha, kila mwaka wananchi hukumbushwa kuendelea na mapambano dhidi ya UKIMWI, malaria, rushwa na dawa za kulevya. (Makofi)
d) Mwenge wa Uhuru unaimarisha Muungano wetu, Mwenge wa Uhuru huzunguka nchi nzima Tanzania Bara na Zanzibar. Wanaokimbiza Mwenge wa Uhuru wanatoka sehemu mbili za Muungano. Kwa kufanya hivyo, Mwenge wa Uhuru unazidi kutuunganisha kama watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba Mwenge wa Uhuru unatumia fedha nyingi za walipa kodi. Kwa mfano, kwa mwaka 2017, Serikali ilitenga shilingi milioni 463 kugharamia shughuli za Mwenge wa Uhuru ukilinganisha na kiasi cha miradi 1,582 iliyozinduliwa yenye thamani ya shilingi trilioni 1.1 ni dhahiri kuwa hoja ya gharama kuwa kubwa siyo ya msingi. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kukabiliana na vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwa maana ya miezi tisa ya ujauzito au wenye uzito pungufu chini ya kilogramu 2.5 huwa katika hatari zaidi ya kupoteza maisha kuliko wengine kutokana na kushindwa kupumua, kupoteza joto, kupata uambukizo wa bakteria kwa haraka, kushuka kwa sukari mwilini (hypoglycemia) kutokana na kushindwa kunyonya, ugonjwa wa manjano kwa watoto wachanga na kadhalika. Tatizo la uzito pungufu unachangia asilimia 25 ya vifo vya watoto wachanga hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hizo za kiafya zinazotokana na kuzaliwa kabla ya wakati, Wizara imeendelea kuboresha huduma za watoto hao kwa kutekeleza afua mbalimbali kama vile moja, kuwapatia wajawazito dawa ya sindano ya dexamethasone injection kusaidia mapafu ya watoto kukomaa kwa haraka iwapo dalili za mama zinaonesha anaweza kujifungua kabla ya wakati ili kumsaidia mtoto anapozaliwa kuweza kupumua vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili; huduma ya kumsaidia mtoto kupumua (helping baby to breath) kwa wale wenye shida ya kupumua mara tu baada ya kuzaliwa. Huduma hii imefundishwa kwa wafanyakazi wa vituo vyote vya kutolea huduma hapa nchini na kila kituo ambacho kuna huduma za kujifungua kuna vifaa vya kumsaidia mtoto kupumua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu; kuanzishwa kwa huduma ya mama kangaroo (kangaroo mother care) ambayo humsaidia mtoto kutunza joto na ya nne; kununua vifaa vya kuhudumia watoto njiti ambayo wana matatizo ya kiafya kama vile oxygen concentrator, mashine ya kutibu manjano, mashine za kufuatilia hali ya mgonjwa kwa maana ya pulse oximeter na mashine za kuongeza joto.
MHE. JOSEPH L. HAULE (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-

Hospitali na Vituo vya Afya vinatakiwa kukidhi viwango vya utoaji huduma kwa wagonjwa; lakini hospitali na Vituo vya Afya vingi havina viwango vya utoaji huduma.

Je, Serikali ina mkakati gani mahsusi wa kuhakikisha Vituo vya Afya na hospitali vinakidhi viwango vya utoaji huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwenye Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye maeneo mbalimbali ya vituo vya kutolea huduma za afya ili kukidhi viwango vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha viwango vya utoaji huduma za afya nchini, katika mwaka wa fedha 2017/ 2018 na 2018/2019, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 285.17 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 67, ujenzi na ukarabati wa Hospitali za Wilaya tisa (9), Vituo vya Afya 304 na Zahanati 39. Vilevile, Serikali imejenga na kukarabati nyumba za watumishi wa afya nchini 301. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga shilingi bilioni 23.9 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri mpya 27 na ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya 52.


Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019, Serikali imeajiri jumla ya watumishi 8,444 wa kada mbalimbali za afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya afya, kuajiri wataalamu, kununua dawa, vitendanishi na vifaa tiba ili kuhakikisha vituo vya kutolea huduma vinakidhi viwango vinavyohitajika.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha Wakunga wa Jadi ili kupunguza vifo vya Mama na Mtoto hasa maeneo ya Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania iliridhia Mkataba wa Uzazi Salama mwaka 1994 katika mkutano uliofanyika nchini Misri. Mkataba huo unaelekeza kwamba kila mama anayejifungua atahudumiwa na mtaalamu mwenye ujuzi kwa kutilia maanani kwamba matatizo yatokanayo na uzazi hayatabiriki na yakitokea uhitaji kutatuliwa na wataalamu wenye ujuzi katika kuokoa maisha ya mama na mtoto mchanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inawatambua wakunga wa jadi kama watu muhimu katika jamii. Hivyo, Wizara kwa kutambua umaarufu wao katika jamii, inawatumia kufanya uhamasishaji wa wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya na ikibidi kuwasindikiza.
MHE. DEVOTHA M. MINJA (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-

Ongezeko la gharama za nishati nchini hasa umeme na gesi vimesababisha kuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya kuni na mkaa.

Je, ni lini Serikali itarasimisha biashara ya mkaa ili kupunguza makali ya maisha hasa kwa Watanzania wenye kipato duni?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, biashara ya kuni na mkaa inafanyika kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Misitu pamoja na Tangazo la Serikali Na. 324 la tarehe 14 Agosti, 2016 na Mwongozo wa Uvunaji wa Mazao ya Misitu wa mwaka 2007 uliofanyiwa marekebisho mwaka 2015. Hivyo biashara hii ni rasmi na haina kizuizi chochote kwa mwananchi yeyote, kinachotakiwa ni kufuata sheria na taratibu za kufanya biashara ambazo zimefafanuliwa vyema katika mwongozo wa uvunaji ambao unamtaka kila mvunaji wa miti kwa ajili ya nishati ya kuni na mkaa kuzifuata, kitu ambacho baadhi ya wafanyabiashara na wachoma mkaa hawatimizi.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya taratibu hizi ni pamoja na:-

(i) Kutambua na kutenga maeneo ya misitu kwa ajili ya kutengeneza mkaa.

(ii) Kila anayehusika na shughuli za biashara ya mkaa anatakiwa kusajiliwa na Meneja wa Misitu wa Wilaya na anatakiwa kuwa na leseni.

(iii) Maombi ya usajili na leseni yanapaswa kupelekwa kwa Afisa Misitu wa Wilaya na kujadiliwa na Kamati ya Kusimamia Uvunaji wa Wilaya; na

(iv) Kila mfanyabiashara wa mkaa anapaswa kulipia mrahaba kama ilivyoainishwa katika Jedwali Na. 14 la Sheria ya Misitu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uhaba mkubwa wa nishati ya miti, Serikali inawahamasisha Watanzania na wadau wote kuanzisha mashamba ya miti kwa ajili ya matumizi ya nishati.

Hata hivyo, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge kuisaidia Sekta ya Misitu kwa kuhamasisha matumizi ya umeme, gesi, uzalishaji wa nishati mbadala ili kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ambayo inaongeza uharibifu wa misitu.
MHE. ZUBEDA H. SAKURU aliuliza:-

Kumekuwa na vyama vingi vinavyotambuliwa kama vyama vya wasanii na wanamichezo nchini.

(a) Je, kuna jumla ya vyama vingapi halali vya wasanii na wanamichezo ambavyo vinatambuliwa kwa mujibu wa sheria?

(b) Serikali imechukua hatua gani dhidi ya vyama visivyo na usajili vya Sanaa na Michezo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru Viti Maalum lenye sehemu A na B kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Disemba mwaka 2019 vipo vyama 69 ambavyo vinatambuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Na. 23 ya mwaka 1984, ikisomwa pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2019. Kwa upande wa michezo vipo jumla ya vyama 11 kwa ngazi ya kata vyama 28 vya Wilaya, Vyama 193 vya Kimkoa na Vyama 74 vya Kitaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya BASATA namba 23 ya mwaka 1984; ikisomwa pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2019 na BMT ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kujihusisha na shughuli za Sanaa na Michezo pasipo na usajili na vibali halali vya Serikali. Vyama vya Michezo visivyosajiliwa haviruhusiwi kushiriki kwenye michezo yoyote rasmi inayofanyika kwenye ngazi za Wilaya, Mkoa au Taifa.