Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zainabu Mussa Bakar (21 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea juu ya kuimarisha taasisi ya Utawala Bora. Kuhusu eneo hili la utawala bora Serikali ijipange vya kutosha kwani inaonekana kutosimamiwa kwa uadilifu ipasavyo bali Serikali inakwenda kwa hamasa za kisiasa zaidi kuliko kiuadilifu kwa kufuata misingi ya kidemokrasia. Demokrasia inamezwa kwa maslahi ya wachache na wengi kunyimwa haki zao. Wananchi wananyanyasika vibaya sana, hata vyombo vya dola vinaendeshwa kisiasa zaidi jambo ambalo si haki na halipendezi. Jambo hili linatufanya wananchi tukose imani na Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia rushwa na ufisadi unaendelea kwa kasi nchini. Hivyo TAKUKURU imarishwe kwa kupatiwa rasilimali watu na bajeti ya kutosha ili waweze kujikimu na kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mawasiliano ni jambo muhimu kwa binadamu hivyo ni lazima watu wajue taarifa mbalimbali za nchi yao. Hivyo, Serikali isiwanyime wananchi wake na walipa kodi walio wengi haki yao ya msingi ya kuliona Bunge lao na Wawakilishi wao wanavyowatetea. Hiyo ni haki yao ya msingi na ya Katiba wanataka wapate taarifa muhimu za bajeti zinazoendelea na taarifa za Majimbo yao walizozileta.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi hewa Serikalini. Hili ni tatizo, Serikali ijipange na ifuatilie ufisadi huu ipasavyo kwani linaumiza kodi za wananchi, watumishi kujipandikizia mishahara miwili miwili si jambo jema. Hivyo, Serikali ifanye kazi ya ziada kuondoa watumishi hewa na wachukuliwe hatua za kisheria wanaohusika na hayo.
Kwanza, Makatibu Tawala, Wakurugenzi, watendaji waliosababisha uwepo wa watumishi hewa wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo. Pili, Serikali iunganishe mifumo ya rasilimali watu inayojitegemea. Mifumo ifuatayo iunganishwe, vizazi na vifo, malipo Serikalini, namba ya Kitambulisho cha Taifa, mfumo wa malipo ya kodi na malipo ya pensheni. Tatu, Tume ya Utumishi wapewe watumishi na vitendea kazi vya kutosha ili wafanye kazi kwa ufanisi na kutimiza majukumu yao kwa umakini zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). TASAF ni jambo jema kwa wananchi kwa sababu inawasaidia sana. Ila pesa hizi ni nyingi sana; kwa kupewa wananchi pesa taslimu hakuwezi kuondoa umaskini na badala yake kwa kuanzishiwa miradi kunaweza kuondoa umaskini na kuweza kujikimu kimaisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba maoni yetu yazingatiwe ili kuendeleza Taifa letu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha maoni yangu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ya Viwanda haiko kama Serikali haitakuwa na malengo makini kwa Watanzania. Kwanza, Serikali ijikite kwa kutoa vipaumbele ni viwanda vipi kwanza waanze navyo. Serikali ijali wawekezaji wa ndani wanapowekeza kwenye viwanda na iondoe sheria kandamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuwe na miundombinu mizuri kama ya barabara bora zenye viwango, ambazo zitaruhusu bidhaa kusafirishwa kwa urahisi zaidi. Kuwe na uhakika wa umeme na siyo wa mafuta. Kwa upande wa biashara, wafanyabiashara wapunguziwe riba kwenye mabenki ili kwe na urahisi wa kufanya biashara na Watanzania wengi wawekeze kwenye biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wageni wakiwekeza kuwe na asilimia ya kuajiri Watanzania isiyopungua asilimia 90. Pia kuwe na masharti ya uwekezaji kuwa wanapowekeza, waboreshewe miundombinu katika eneo walilowekeza. Vilevile Serikali ifanye jitihada za makusudi za kupanua wigo na
fursa za kuanzisha masoko yenye masharti nafuu. Serikali ijifunze kutoka nchi nyingine vipi wamefanikiwa katika biashara na viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tuweze kuendeleza viwanda vidogo vidogo kama SIDO na vinginevyo ili wananchi wapate ajira na kuwe na soko la karibu na uhakika ili kuuza bidhaa zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wanahitaji Serikali iimarishe viwanda ambavyo kwa kuanzia vitaleta tija na kuendelea kama walivyoendelea nchi za jirani na za mbali na siyo kila siku hadithi. Wanatarajia kuona Tanzania ya viwanda vyenye neema mbalimbali na imeondokana na umasikini ulioenea. Pia Serikali itatue changamoto zilizopo katika sekta hii ili tufikie malengo tunayotarajia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZAINABU MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ni sekta muhimu sana kwani inaleta pato kubwa kwa Taifa letu. Hivyo ni sekta ya kuthaminiwa sana na siyo ya kudharauliwa kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaitaka Serikali ibadili utaratibu uliopo kwa utoaji wa leseni kwa wafanyabiashara wanaosafirisha watalii kwa kuondoa sharti la umiliki wa magari matano ndipo wapewe leseni ya kufanya biashara hiyo. Kiwango hiki kipunguzwe angalau yawe mawili au moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na vivutio vingi tulivyonavyo vya watalii ni lazima pia kuwe na matangazo ambayo pia yatawavutia watalii, vinapotangazwa vivutio ndiyo watalii watakuja. Hivyo ni lazima tuwe na mpango madhubuti na bajeti ya kutosha ya kufanya matangazo ya vivutio vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia jambo lingine ni miundombinu imara husaidia na ni kivutio pia cha watalii kwani unapokuwa na miundombinu mizuri kunawafanya watalii wafike eneo hilo kwa urahisi bila ya machovu na kuweza kufurahia safari aliyokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia viwanja vya ndege viimarishwe ili watalii waweze kufikia vivutio hivyo kwa wepesi zaidi. Jambo lingine ni malazi mazuri yenye mvuto na sehemu nzuri za kujenga hoteli hizo ambazo watalii zitawavutia. Ni vema Serikali kuzingatia pia maoni ya wananchi. Vilevile kuwa na kanuni zinazowabana watalii ambazo zingeleta madhara kwa wanajamii na kizazi chetu. Kwa mfano, kuwe na maadili ya kuzingatia kama vile uvaaji wa mavazi yasiwe yanakihirisha, yawe ya heshima. Kushirikisha watu au wananchi vilivyo kufuata silka na mila au tamaduni husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu watoto wetu ni wenye kuiga sana mambo, watoto wengine wameharibika na kuwa hawana maadili hasa sehemu nyingi za fukwe na zenye hoteli kubwa, maadili yameporomoka kwa kuona wanayofanya. Watoto wengi huacha shule ili tu wapate ajira ya kutembeza watalii maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Serikali iyaone haya na kuyafanyia kazi ipasavyo. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo ni uti wa mgongo, hii ina maana kuwa kilimo ni kila kitu na ni uhai wa Watanzania. Hivyo eneo hili linataka litiliwe maanani na kupewa kipaumbele kwani Watanzania walio wengi ni wakulima. Kwa kweli Watanzania wanahitaji yafuatayo katika kilimo ili kiwe kilimo bora na chenye tija:-
(i) Pembejeo na trekta ili wapate kilimo bora chenye tija;
(ii) Mbolea nzuri;
(iii) Wataalam au Mabwana Shamba ambao watawaelimisha kulima kilimo bora chenye kuleta tija;
(iv) Zana hizi zifike kwa wakati ili waendane na mipango ya kilimo;
(v) Pia wanahitaji miundombinu ya kuweza kulima kilimo cha umwagiliaji. Hili ni suala la kutilia maanani na kukipa kipaumbele kwa sababu Watanzania wengi ni wakulima hivyo wanatarajia Wizara hii iwawezeshe ili wawe na kilimo endelevu chenye manufaa;
(vi) Madawa ya kuondolea maradhi mimea na mazao;
(vii) Kupata masoko ya uhakika nchini; na
(viii) Kutatua migogoro iliyopo baina ya wakulima na wafugaji kwa kuwapatia ardhi ya kutosha kila mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa ufugaji, hii pia ni sekta muhimu sana na yenye kuleta tija. Hivyo wafugaji waelimishwe namna ya kushughulikia mifugo yao kuanzia kuwalisha, kuwatunza. Hivyo sekta hii inahitaji utaalam wa kuweza kushughulikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii inatupatia kitoweo cha nyama, hivyo mifugo hii inasaidia sana Watanzania. Naomba maeneo yafuatayo yaimarishwe:-
(i) Kupewa shamba la mifugo;
(ii) Madawa ya mifugo;
(iii) Viwanda vya kusindikia nyama na maziwa;
(iv) Kutengwa maeneo maalum ya malisho ya mifugo na kilimo;
(v) Kufanya utafiti wa kutosha ili tuwe na ufugaji wenye tija;
(vi) Vitendea kazi vya utafiti;
(vii) Serikali kuruhusu uzalishaji kwa Kiwanda cha Maziwa ambacho kitanunua maziwa kutoka kwa wafugaji;
(viii) Upanuzi wa mapori ya akiba; na
(ix) Kutoruhusu uingizaji wa nyama kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakapoimarisha maeneo haya ya ufugaji na kilimo, nchi yetu itachukua hata nafasi ya pili au ya kwanza kwa kilimo bora na ufugaji wa kisasa na kuleta pato zuri la Taifa letu na hata migogoro itaondoka kati ya wakulima na wafugaji na tutakuwa na kilimo cha biashara chenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya uvuvi ni muhimu sana na ni sekta ambayo tukiendeleza italeta tija kwa Taifa na pato zuri sana, ila sekta hii inasumbuliwa na changamoto zifuatazo:-
(a) Uvuvi haramu wa mabomu na nyavu ndogondogo. Mabomu haya huharibu mazalia ya samaki (matumbawe);
(b) Wavuvi kutopata vyombo imara vya kuvulia (zana za kisasa za kuvulia);
(c) Viwanda vya kusindikia na kuhifadhi samaki;
(d) Boti bora za kuvulia;
(e) Kudhalilishwa kwa wavuvi wadogo kwa kuchomewa moto nyavu zao;
(f) Kukosekana kwa elimu ya uvuvi. Watu wengi wanavua kwa mazoea tu;
(g) Jambo lingine la muhimu ni kuanzisha bandari ya uvuvi kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi; na
(h) Kukosekana kwa soko ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo tunaiomba Serikali itatue changamoto hizi katika sekta hii ili kukuza pato la Taifa. Tunamwomba Waziri achukue mawazo haya kwa ajili ya kuliokoa Taifa letu la Tanzania tuwe na kilimo, ufugaji na uvuvi bora wenye tija na Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia iangalie kwa jicho pevu sekta hii kwa kuilipia zile shilingi bilioni mbili kama Mahakama ilivyotoa amri kuhusu meli ya uvuvi maarufu kama “kesi ya samaki wa Magufuli” iliyokuwa ikiwakabili wavuvi raia wa China wamiliki wa meli ya uvuvi ya TAWARIQ.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila la kheri, Mungu ibariki Tanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZAINAB M. BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunitunuku zawadi ya kusimama hapa. Pili, naunga mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitaelezea suala la bajeti kushuka. Bajeti ya Wizara ya Elimu imeshuka sana wakati tunaiangalia Wizara hii kama ni Wizara mama na dira ya Wizara zote. Nasema hivyo kwa sababu Wizara hii ndiyo inayozalisha madaktari, mameneja, wahandisi na viongozi leo tunaipunguzia bajeti. Mwaka jana tulitenga 1.4 mara hii tumeshuka mpaka 1.3. Hivi kweli tupo tayari kuisaidia Wizara hii ambayo ndiyo kioo cha nchi hii ama tunaibeza tu? Kwa sababu mfumo wowote mzuri ndiyo utatufanya tupate matokeo mazuri na wanafunzi na viongozi bora lakini tukiendelea hivi tutaendelea kuwatumbua viongozi kutokana na kwamba hatujaweka ufanisi mzuri katika suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna vitendea kazi kutokana bajeti yetu tumeiweka katika upungufu huu. Tutaendelea kukosa madawati, maabara na vyumba vya kusomea wanafunzi kutokana na kushuka kwa bajeti ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu ndiyo tegemeo la nchi hii lakini leo tunawazalilisha au wako chini kabisa. Tunashindwa kuwaongezea mishahara ambayo itawakidhi kwa mahitaji yao ya kila siku. Mwalimu huyo huyo asomeshe mtoto wake na anahitaji pesa za matumizi mengine mwisho wa siku anakuwa na msongo wa mawazo na ndiyo maana anafanya mambo mengine ambayo hayaeleweki. Kwa hivyo, tunakuomba Mheshimiwa Prof. Ndalichako uwaangalie kwa jicho la huruma walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na suala la uhamisho. Uhamisho wa ualimu imekuwa ni kilio. Tunawatenga walimu na wenza wao kwa kipindi cha muda mrefu, waonane likizo hadi likizo, hiyo siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu yupo Kigoma mwenza wake anafanya kazi Dar es Salam, hatuoni kwamba tunawazalilisha na kwamba Serikali au Wizara hii inavuruga ndoa za walimu wetu? Kwa nini tusiwape uhamisho wakawa karibu na wenza wao? Hivi ni Serikali ya Mapinduzi ndiyo mkakati wake kuona ndoa za watu zinavurugika? Nataka unipe majibu kuhusu uhamisho wa walimu ambao wenza wao wako mbali kama watapewa uhamisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuja kwenye suala la kubadilishwa kubadilishwa kwa mitaala hili limekuwa ni suala la kawaida na kwamba hakufanywi tafiti za kina na wala walimu hawashirikishwi katika masuala haya ya kubadilisha mitaala, jambo ambalo linapelekea wanafunzi wetu kufeli sana. Kwa mfano mzuri nikija kule kwetu Zanzibar sidhani kama walimu wa Zanzibar wana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZAINABU MUSSA BAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, awali nimshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kuniwezesha kuwa na pumzi na kusimama hapa. Pili nikishukuru chama changu kwa kuniwezesha pia kuwa hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda na mimi nichangie katika Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. Elimu ni kila kitu katika Taifa hili la Tanzania na Taifa lolote duniani. Elimu ni suala nyeti na ni suala ambalo linaigusa Taifa. Hata katika dini zetu suala hili limetiliwa mkazo, nikirejea katika dini yangu ambayo mimi ni muumini, dini yangu ya kiislamu tumeamrishwa kutafuta elimu hata kama ni China na vilevile elimu ni faradhi kwa muislamu wa kike ama wa kiume, na hata katika dini zote nadhani suala hili limetiliwa mkazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama suala hili limetiliwa mkazo katika dini zote na katika tamaduni zote, ni muhimu pia na Walimu tuwape umuhimu huo huo. Imekuwa ni rahisi sana kwamba walimu hatuwatendei haki katika Taifa hili, Walimu wanapata matatizo mengi kusomesha watoto wetu, wanajitahidi kufundisha watoto wetu kihaki lillah! Leo hii ndiyo tunaodharau Walimu hao, leo hii hatuwasikilizi mahitaji yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mtu ambaye anakupa kitu muhimu; hivi mtu ambaye anakuthamini, wewe huwezi kumthamini, ni kwa nini? Hiyo siyo haki na hatuwatendei haki kama inavyopaswa. Walimu hao hao leo wanapodai madai yao Serikali inawawekea kitimoto. Aidha, wanapoandamana wataweza kufukuzwa kazi, ama kitimoto cha aina yoyote cha kuweza kuwadhalilisha hao Walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipowathamini Walimu wetu, hivi tutawathamini nani wengine?
MHE. ZAINABU MUSSA BAKARI: Kwa sababu Walimu hawa ni muhimu katika kila sekta. Wewe usingekuwa kiongozi kama hukupitia kwa Mwalimu, asingekuwa daktari kama hakupitia kwa Mwalimu, asingekuwa Rais kama hakupitia kwa Mwalimu. Sasa inakuwaje tunawakandamiza na kuwadhalilisha? Mwalimu huyu anasomesha miaka 50, lakini leo ukienda hana hata mahali pa kukaa. Hii ni haki? Ni kweli tunawatendea haki? Mwalimu huyu anasomesha miaka 50, hana uwezo hata wa kumiliki baiskeli. Lazima Taifa hili likae, litafakari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoamini ni kwamba Mwalimu ni mtu wa pili baada ya mzazi na anaweza kutoa radhi zikatufika. Naamini katika mwelekeo huo huo, ni kwamba mambo mengi hatuendelei kwa sababu tumewadharau Walimu. Tutapanga mikakati, mipango ya kila aina lakini hatutaendelea kwa namna hii na style hii tunavyowafanyia Walimu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee hapo hapo!
MHE. ZAINABU MUSSA BAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tuliambiwa walimu wanatarajiwa kuajiriwa mnamo mwezi wa Tano, sasa tunaingia mwezi wa Sita, Walimu hawajaajiriwa. Naiuliza Serikali, itawaajiri lini Walimu ambao wamekwisha kwenda kuchukua mafunzo? Walimu ambao wamejitolea, ambao wamesoma pengine hata mikopo wamekosa; angalau wafute jasho lao kwa kupata hiyo ajira, kwa sababu elimu yetu haikuandaliwa kwamba unapomaliza shule ujiajiri mwenyewe, hiyo haipo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala linguine, nizungumzie suala la elimu kwa upande wa Zanzibar. Suala la elimu kwa upande wa Zanzibar ni tete na ndiyo maana ikawa wanafunzi wa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita wanafeli sana. Hapo mwanzo nilidhani kwamba pengine elimu ya Form Four mpaka „A‟ level kwa kule Zanzibar labda ni elimu ya juu, kwa sababu suala ambalo linahusiana na Muungano ni suala la elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza, wanafunzi wa Form Four wanafanya mitihani inayotungwa Tanzania Bara na siyo Tanzania Zanzibar. Mitaala hiyo inacheleweshwa, ndiyo maana watoto wengi wanafeli. Wakati mwingine mwingine anaulizwa pengine habari za pamba, kule Zanzibar hajaiona, wala hajaijua, naomba kuwasilisha.
MHE. ZAINABU MUSSA BAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika suala la kubadilishwa kwa mitaala bila ya kufanya utafiti wa kina na wala kushirikishwa kwa Walimu ambao ni wadau wakubwa sana. Hili ni suala lililozoeleka kwa kipindi sasa, pia mtaala umejikita kuwakaririsha wanafunzi. Kwa mfano kwa upande Zanzibar sidhani kama Walimu wanashirikishwa ipasavyo. Hata hivyo, mitaala ikibadilishwa haipatikani kwa muda muafaka, tukizingatia wanafunzi wa Zanzibar wanafanya mitihani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa form four na form six.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri, Mheshimiwa Ndalichako atuambie hii ni Wizara ya Muungano ama vipi. Kama sio kuna makubaliano yoyote waliyofanya na Wizara ya Elimu ya Zanzibar ama Serikali, ni yapi? Mbona hatuoni ofisi za Wizara ya Elimu ya Muungano kama ilivyo kwa TRA na Wizara ya Mambo ya Ndani. Kama zipo, Unguja ipo wapi na Pemba wapi? Je, Waziri ameshawahi kutembelea mara ngapi? Kwa nini Walimu walipwe na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar badala ya kulipwa na Serikali ya Muungano na kuzingatia wanatumwa na Serikali ya Muungano na kwa utofauti mkubwa wa mshahara wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yote hayo si masuala ya Muungano kwa nini Zanzibar tusiachiwe kuwa na mitaala yetu na kutunga mitihani wenyewe? Naomba Mheshimiwa Waziri anijibu masuala haya ili kuondoa ukakasi uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu waongezwe mishahara na kupandishwa madaraja kwa wakati na kupewa stahiki zao kwa wakati. Hii itasaidia Walimu kufanya kazi kwa ufanisi, tukizingatia wanatuzalishia viongozi. Tusikubali wafanye kazi katika mazingira magumu na msongo wa mawazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa uhaba wa Walimu wa sayansi, hiki ni kilio cha nchi nzima, kwa mfano katika wilaya nzima utakuta Walimu wa sayansi wawili mpaka wanne, hii ni hatari kubwa. Waziri atuambie ana mkakati gani madhubuti wa kupata Walimu wa sayansi. Pia ina mkakati gani wa kuongeza wanafunzi wa kike kwenye masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupatiwa majibu na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni ufunguo wa maisha, pia elimu ni bahari na haina mwisho. Hivyo elimu ni muhimu sana katika maisha yote na ya kila mtu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la elimu kuna changamoto zake zikiwemo za taaluma yenyewe na wanaotoa taaluma hiyo. Nazo ni kama ifuatavyo:-
(1) Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa vitabu vya kufundishia. Hili ni tatizo mojawapo katika sekta hii na suala ambalo linakatisha tamaa kuwa tunataka wanafunzi wafaulu lakini hatuna vifaa vya kuwawezesha kufaulu.
(2) Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa maabara. Hili nalo ni tatizo kubwa katika Sekta ya Elimu. Hii inasababisha hata kutokuwa na Walimu wa sayansi, kwani mambo mengi tunasoma kwa theory kuliko practical, kwa mfano skuli au vyuo havina maabara z kutosha.
(3) Mheshimiwa Mwenyekiti, mitaala mibovu. Pia hili linachangia elimu kuzorota na hatutafika tunakotaka kufika katika elimu na hata katika Tanzania ya viwanda.
(4) Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mfumo wetu wa elimu ni mbovu. Wenzetu wamefanikiwa katika nchi zao kwa kuipa kipaumbele elimu, hali hiyo inatokana na kuijengea mfumo mzuri kwa kuwafundisha wanafunzi wao fani maalum wakiwa wadogo na wakubwa yaani primary hadi vyuo vikuu. Mfano, wanafunzi “x” wanasomea fani ya ufundi kulingana na kipawa chao na “y” wanasomea fani ya unesi kuanzia mwanzo wa masomo yake hadi mwisho. Leo hii katika Taifa letu tumeifanya elimu kama mzigo wa masomo mengi na kupelekea wengi kukatisha njiani au kusoma kwa kukariri zaidi ile nyanja kuliko kufahamu ili aweze kupata kufaulu tu. Hivyo, huwa tunapata wanafunzi ambao si wafanisi bali ni waigizaji tu, hivyo Serikali izingatie ushauri wetu kwa uzalendo wa Taifa letu.
(5) Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu hawana makazi bora; hivyo Serikali iwajengee Walimu makazi kama inavyofanya kwenye sekta nyingine, mfano, Sekta ya Ulinzi, Sekta ya Jeshi la Taifa na sekta nyingine.
(6) Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wapewe posho za kuwakidhi mahitaji yao kama usafiri na uhamisho kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna changamoto katika Sekta ya Elimu katika Taasisi ya Mikopo kama ifuatavyo:-
(1) Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwafikii walengwa, kama tunavyoelewa kanuni ya mikopo iliwekwa kwa wale wasiojiweza kupata elimu hususan maskini, lakini la kushangaza wanaofaidika zaidi ni watoto wa vigogo kama vile Mawaziri, Wabunge, Maafisa na wengine na kupewa mikopo kwa asilimia 100, lakini wale walengwa hupewa wachache tena kwa asilimia chache kwa mfano asilimia 40, 30, 20 na hata asilimia 10 na wengine kukosa na kushindwa kuendeleza masomo yao.
(2) Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mikopo haifiki kwa wakati na badala yake wanafunzi wanadhalilika kwa kujiuza, kuwa ombaomba kwani huwa wako mbali na familia na hata familia zao zinashindwa kuwasaidia kutokana na hali zao za ugumu wa maisha.
(3) Mheshimiwa Mwenyekiti, kutorejeshwa kwa mikopo hii; Serikali na Wizara ya Elimu hawajajipanga wala hakuna kanuni inayosimamia haya. Kwa mfano, wanafunzi wengi wanaona ni takrima ama hisani imepewa tu jina la mkopo na ndiyo maana toka waajiriwe hawajakatwa hata siku moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la elimu kwa upande wa Zanzibar, ni mgagaisho mtupu; hatutofautishi elimu ya juu ni ipi na elimu ya sekondari kwani wanafunzi wa O Level na A Level wanafanya mitihani kutoka Tanzania Bara wakati suala hili ni la Zanzibar. Je, Serikali ya Jamhuri ya Muungano inapora madaraka ya Serikali ya Zanzibar? Naomba majibu kwenye hili; kama ni suala la Muungano mbona haiwaajiri Walimu hawa kwa Jamhuri ya Muungano na wanaajiriwa na Serikali ya Zanzibar na hawalipwi sawa na Jamhuri ya Muungano wakati wanafanya kazi za Jamhuri ya Muungano isipokuwa kusimamia mitihani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni muhimu sana hasa ukizingatia ni Wizara ya Ulinzi wa nchi, mipaka yetu na kulijenga Taifa letu liwe bora na salama. Serikali ione umuhimu ya kutoa fedha zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuboresha mfumo wa mawasiliano salama Jeshini chini ya Fungu 57. Hii ni muhimu sana kwa utekelezaji wa mfumo wa mawasiliano ambao utasaidia katika kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali itoe fedha zote zilizoidhinishwa kwa ajili ya utunzaji wa zana, magari na mitambo katika mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaitaka Serikali kulipa madeni ya kimkataba kwa kutenga fedha zaidi kwenye miradi ya maendeleo Fungu 57. Tunaitaka Serikali kutoa nyongeza ya mishahara kwa wanajeshi wetu. Kwani hili ni hitaji la kisheria na kikanuni na pia ni kichocheo cha ari ya kufanya kazi kwa bidii zaidi. Serikali itoe kipaumbele kwa maslahi ya wanajeshi kwa kuwa ni kada ambayo imejitoa kwa gharama ya uhai wao katika kulinda mipaka ya nchi yetu dhidi ya adui yoyote kutoka nje na kuhakikisha kwamba lipo salama wakati wote. Kwa hiyo, si vizuri wanajeshi kuanza kulalamika kwa suala hili ambalo ni stahiki yao ya kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isifanye suala la kisiasa ama ubabaishaji katika kuwapandisha vyeo wanajeshi. Tunaitaka Serikali iwapandishe vyeo wanajeshi wote wanaostahiki kulingana na sheria, sio nusu wapandishwe na nusu hawapandishwi, huo si uadilifu. Kuna malalamiko kwamba wanajeshi 8,000 waliofuzu kupandishwa vyeo mwezi Desemba, 2018; lakini ni 4,000 tu waliopandishwa na ilhali sifa wanazo. Je, Serikali ituambie ni lini watawapandisha vyeo wanajeshi hao?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na kuniwezesha kutoa mchango wangu kwa njia ya maandishi. Hivyo, naanza kutoa mchango wangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wananchi haturidhishwi na mwenendo wa utolewaji wa fedha za bajeti zinazoidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa REA. Takwimu zinaonyesha kwamba, katika miaka mitatu ya fedha iliyopita 2013/2014 hadi Aprili, 2015/2016, wastani wa REA umekuwa kwa asilimia 60 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, wananchi hawaridhishwi na uwekezaji wa vinasaba katika mafuta. Ili hali, TRA wana vituo njiani vya ukaguaji wa mafuta ni kupoteza pesa za walipa kodi wa Tanzania, ni kuwanyanyasa walipa kodi na kutajirisha mtu binafsi anayetengeneza vinasaba. Hivyo, Waziri atueleze ni kwa nini wanaona tabu kuondosha vinasaba kwani havisaidii?
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, mgodi wa makaa ya mawe, Kiwira, utaanza uzalishaji utaongeza umeme na uzalishaji huu utaboresha sana upatikanaji wa umeme wa kufikia malengo tunayotarajia kuliko kutofanya. Aidha, kudharau au kujali maoni ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kupeleka fedha, zinazoidhinishwa kwa wakati na kupelekwa kama vile zilivyoidhinishwa badala ya kupeleka pungufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, Serikali itueleze kuhusu madini ya Tanzanite, inakuwaje yanauzwa India, Kenya na Afrika Kusini kwa wingi zaidi ya Tanzania na Tanzania, inachukua nafasi ya nne na India nafasi ya kwanza ilihali, madini hayo yanapatikana Tanzania peke yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, hii hatuoni kama ni uharamia unaofanywa na wawekezaji na hata wachimbaji wadogo kuuza holela madini haya? Serikali haina udhibiti wa kutosha kwani Serikali haioni umuhimu wa kufunga mgodi mpaka ijipange kuliko kumalizika kwa madini bila Tanzania kupata faida yoyote na badala yake kuambulia aibu na kukosa Pato la Taifa na kuwapa umaarufu nchi nyingine na Tanzania kuendelea kuwa maskini na kutajirisha nchi nyingine ilI hali madini yale yanatoka Tanzania pekee.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kwa kuwa, Serikali haina dhamira ya dhati ya kudhibiti madini yanayotoroshwa, ambayo ni ghafi kwani haitoi kauli yoyote. Hivyo, tunaomba, na tunaishauri Serikali, usimamizi wa migodi hii, uangaliwe na Taifa letu lipate pato la kutosha kuliko kunufaisha Mataifa mengine ambayo hayazalishi madini haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la gesi ni muhimu na litasaidia Tanzania kupata umeme mwingi na kusaidia viwanda kuimarika. Vile vile iuzwe, itumike majumbani katika shughuli mbalimbali kuliko kuendelea kununua kwa makampuni mengine ya kuuza wakati, Tanzania tunayo gesi ya kutosha. Pia, Serikali iandae mpango mkakati utakaoweza kusimamia vizuri gesi asilia pamoja na kutafuta masoko madhubuti na ya uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali iwekeze katika miundombinu na utalaam wa madini ya vito ili kuwezesha ukataji na uuzaji wa Tanzanite kufanyika hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Serikali isimamie kwa umakini wa hali ya juu ukamilishwaji wa miradi na vipaumbele vya uzalishaji vya umeme ili kutuwezesha kupata umeme wa kutosha hapa nchini ili tuwe na viwanda vya kutosha vyenye kukidhi mahitaji ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa Serikali ijipange kutekeleza haya kwa moyo wa dhati na sio kuwarubuni Watanzania. Tunapenda kuona Tanzania inaneemeka na rasilimali zake na kuipata Tanzania tuitakayo, iliyoimarika na kupiga hatua za maendeleo mbele zaidi na siyo kila siku tukawa watu wa kurudi nyuma tu na ku-enjoy mafanikio ya wengine tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia nawatakia kila la kheri Serikali na naiombea iwe na moyo wa dhati na kutekeleza yale tunayowaelekeza na kuyafanyia kazi kwa wepesi zaidi ili kuleta maendeleo ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha maoni ya wananchi wangu. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Walimu ni kiungo muhimu sana kwa walimu ila Serikali ipunguze msururu wa vitengo vinavyowasimamia walimu angalau viwe viwili au vitatu tu. Maoni yangu katika Muswada huu ni kama ifuatavyo:-

(i) Majukumu yanagongana kati ya Tume na Bodi, kwa nini zisiunganishwe ikawa chombo kimoja kuliko kuwa na utitiri wa vyombo vinavyowahudumia walimu ilhali majukumu yao yako sawa?

(ii) Leseni zisilipiwe ama kama ni lazima zilipwe basi ni kwa kuanza kujisajili tu na siyo kila baada ya kipindi fulani.

(iii) Hizi ada ni nyingi, kwa mfano, ada ya leseni na ada ya cheti cha usajili huku ni kuwakandamizi walimu kwa utiriri wa ada sasa imekuwa kama ni chanzo cha mapato.

(iv) Nidhamu ya mwalimu haiangaliwi kwa utaratibu wa tabia yake. Nidhamu utaijua pindi utakapomwajiri na sio kabla ya ajira.

(v) Vigezo viwe ni vile vyenye kuhusiana na taaluma ya ualimu.

(vi) Walimu wapewe stahiki zao zote ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na sio kulimbikiziwa madeni. Walimu wapolimbikiziwa stahiki zao watakuwa na misongo ya mawazo na hawatawajibika ipasavyo.

(vii) Napendekeza kuwe na chombo kimoja tu chenye kuwahudumia walimu ndipo maadili yatafuatwa na kuwa makini zaidi kuliko kuwa na vyombo vingi. Kwa kuwa na vyombo vingi kutasababisha maadili kuporomoka kwani kila mmoja ataongoza kwa misingi yake hivyo kutakuwa na mkanganyiko wa maadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kusema huu mpango haukidhi viwango ambavyo tulivitarajia, wala haukutosheleza matakwa ya Kitaifa na maendeleo tunayoyataka. Kwanza, haujatupa tathmini; tumefikia wapi? Tumekwama wapi? Tuanzie wapi baada ya kupitisha bajeti ndani ya mwaka huu? Huu ni mpango gani usioonesha dira na hali halisi ya mambo yalivyo katika kila sekta?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni mkanganyiko au mgongano wa wazi kati ya kanuni za Bunge na Sheria ya Bajeti kuhusu uwasilishwaji wa mpango na makisio ya bajeti katika mwaka wa fedha unaofuata. Kikawaida, pale panapotokea mgongano kati ya kanuni na sheria, basi, sheria ndiyo husimama, lakini Bunge letu, huipa kanuni kipaumbele. Tukizingatia Kifungu 21(2) cha Sheria ya Bajeti, mapendekezo haya ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa yalikuwa yawasilishwe katika Bunge la Januari – Februari. Hii ni kwa ajili ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha unaoendelea na makisio ya hali ya uchumi kwa miaka mitatu ya fedha inayofuatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea kutoa mchango kuhusu mapendekezo ya Mpango huu wa Maendeleo ya Taifa, tunashuhudia hali ya kiuchumi ikiyumba sana ndani ya nchi hii. Hii ni kutokana na sababu tofauti tofauti.
(i) Sekta ya Kilimo imeathirika hasa kutokana na mabenki kuzuia kutoa mikopo kwa wakulima kama ilivyokuwa hapo awali; Benki kujitokeza na kutoa mikopo kwa wakulima ili kuendeleza kilimo bora chenye tija;
(ii) Pia uchumi umedorora kupitia Sekta ya Utalii na kukaribia kufa. Hii ni kutokana na Serikali kuongeza kodi ya ongezeko la thamani, hivyo Serikali imesababisha kupungua kwa watalii kuja Tanzania na hivyo kukosa pato la Taifa;
(iii) Serikali kukamata bidhaa na mali za wafanyabiashara wakubwa, hali iliyosababisha wafanyabiashara kufunga biashara zao nchini kwa kuhofia mali zao kuchukuliwa na Serikali, jambo ambalo linazorotesha uchumi, hivyo Sheria ichukue hatua ya kuwawajibisha wahujumu uchumi wa nchi hii jambo ambalo linasababisha uchumi unakuwa tete;
(iv) Serikali imetengeneza watumishi hewa na kusitisha ajira kwa sababu ya kuwa inafanya uhakiki wa watumishi wake. Jambo hili limepelekea kuyumba kwa uchumi na pesa nyingine kulipwa watumishi kama sehemu ya usumbufu wakati kumewafanya wasomi wa taaluma mbalimbali kuishi kama ombaomba ndani ya nchi yao na kudhalilika kutokana na elimu waliyopata. Wananchi wamekuwa wakimbizi kwenye nchi yao hali inatisha. Serikali izingatie hali ya wananchi na raia wake. Serikali bora ni yenye kujali raia wake na kuweza kuwajibika;
(v) Sekta ya Afya ndiyo iko hoi na kuzorota zaidi. Tumeshuhudia kukosekana dawa, chanjo na vifaa tiba katika hospitali zetu nchini, huku maelfu ya wananchi wakipoteza maisha huku tukishuhudia Waziri wa Sekta hii na Makamu kulumbana, mmoja anasema ziko, Mkuu wake akisema hakuna dawa, chanjo na vifaa tiba na hali ni tete. Hivyo Serikali itafakari kauli hizi na kuwapatia wananchi wao huduma nzuri ya afya ili kunusuru janga hili nchini;
(vi) Sekta ya Elimu pia ni changamoto. Elimu imekuwa bure lakini ni bora ilivyokuwa ya kuchangia kwani Serikali ilikuwa haikujipanga kuhusiana na hilo. Wanafunzi wa Elimu ya Juu wanakosa mikopo hali inayowakatisha tamaa wanafunzi hawa kumaliza masomo yao. Walisomeshwa na wazee kwa hali na mali ili waje kuikwamua jamii na yeye binafsi kutokana na hali duni waliyokuwa nayo. Pia Serikali inashawishi watu wajiajiri wenyewe; hali inajulikana kwamba elimu yetu haifanyi mtu aweze kujiajiri. Hivyo, Serikali ijipange kuwa na mfumo wa elimu hii na ndiyo washawishi watu wajiajiri. Tunatakiwa kujiandaa hivyo, ndiyo tutoe hamasa;
(vii) Tulishuhudia na kuahidiwa viwanda, lakini mpaka sasa hakuna kiwanda hata kimoja, jambo ambalo halikutengenezewa plan nzuri, bali Serikali ilikurupuka bila kujiandaa vya kutosha na kusababisha hali ya uchumi kudorora;
(viii) Suala la Bandari; mizigo imepungua hali inayosababisha uchumi kuzorota na mapato kupungua. Kiukweli Serikali imefilisika japokuwa Serikali haikubali, lakini kuwepo viashiria hivyo ni wazi kuwa imeshindwa. Ila naishauri Serikali kuwa makini na kufanya tafiti mbalimbali ili kuinasua nchi hii ya Tanzania katika giza hili nene; na
(ix) Halikadhalika, tunaishauri Serikali irudishe mamlaka ya kuwa Halmashauri kuchukua kodi za nyumba na vyanzo vingine ili zitumike kwenye Halmashauri kuimarisha na kuanzisha miradi kuliko kupewa TRA hali ambayo inaonesha imeshindwa kutekeleza hilo kipindi cha kwanza na hiki cha pili mpaka sasa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo, mifugo na uvuvi ni sekta muhimu sana kwa uchumi na maendeleo ya nchi na Watanzania kiujumla. Sekta hizi zimeendelea kutoa mchango mkubwa ikiwemo kuwa chanzo cha kipato kwa asilimia 65 ya Watanzania, kuhakikisha usalama wa chakula, kuchangia Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 28 na mauzo ya nje kwa zaidi ya asilimia
24. Ingawa sekta hizi ni muhimu sana lakini zina changamoto nyingi sana ambazo zinaathiri ukuaji wake; changamoto hizo ni kama zifuatazo:-

(i) Utengaji na utoaji mdogo wa fedha za bajeti ya maendeleo.

(ii) Wataalam wa utafiti kuwa wachache ama kukosekana.

(iii) Miundombinu duni kwa mfano utoaji wa taarifa za tahadhari na upungufu wa viwanda vya bidhaa zake.

(iv) Athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa mfano kuongezeka kwa ukame, magonjwa ya mimea na mifugo, mvua zisizotabirika na mashamba kuingiliwa na maji ya chumvi na kuathiri mazao na vyanzo vya maji baridi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenendo wa bajeti ya Wizara hii kwa mwaka 2017/2018 si wakuridhisha japo kwamba sekta hizi hutoa mchango mkubwa sana kwa Taifa. Takwimu zinaonesha kwamaba wastani wa bajeti ya Wizara kwa sekta hizo ni asilimia 2.2 kwa kipindi hicho tu ya Bajeti ya Taifa ambacho ni kiwango kidogo sana ukilinganisha na lengo la kufikia asilimia 10 kama Serikali ilivyoridhia katika Azimo la Malabo kwa kipindi cha mikaka mitano ya mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu kwa Wizara hii ni kuwa haijapewa kipaumbele cha kuridhisha katika Bajeti ya Serikali japokuwa vimeendelea kutoa mchango mkubwa kwa Taifa ukizingatia kwamba tunakwenda kwa kasi ya Tanzania ya viwanda. Pia mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuathiri maendeleo ya sekta hizi na Taifa, jambo ambalo pia limesisitizwa na Waziri wa Fedha na Mipando kwenye Bunge mwezi Machi 2017; kwa hiyo napendekeza yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kuwe na utengenezaji wa bajeti halisi na utoaji wa fedha za kutosha na kwa wakati kwa kuwa wastani wa utoaji wa fedha kwa sekta hizi ni chini ya asilimia 60. Hivyo naishauri Serikali ifanye marejeo katika utaratibu wa utengaji wa fedha za bajeti ili kufuata uhalisia wa makusanyo yake japo kwa Mheshimiwa Rais ameonesha jitihada kubwa ya kupunguza rushwa na matumizi yasiyo ya lazima na tija kwa raia lakini utoaji wa fedha wa bajeti uwe wa kutosha na kwa wakati, kwa hiyo, Serikali inahitajika.

Mheshimiwa Mwenyeki, pia kuongeza jitihada na kuweka mikakati mahususi na kabambe ya upataji wa mapato ya nje ya vyanzo vya kodi. Taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa Bunge Machi mwaka huu inaonesha kuwa vyanzo vingine vya mapato kutofanya vizuri ukilinganisha na vyanzo vya kodi. Hii inajumuisha misaada ya wahisani, mapato ya Serikali za Mitaa na mauzo ya nje, pia uwekezaji mzuri wa misaada ya wahisani na mikopo tunayopata ili kupunguza na kuacha kabisa uteegemezi huo kwa kipindi kijacho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongeza utengaji wa bajeti ya maendeleo kutoka vyanzo vya ndani kwa mwaka 2016/ 2017. Vyanzo vya ndani vilichangia kwa asilimia 26 tu ya Bajeti ya Wizara ambapo mwaka 2017/2018 inategemewa kupanda mpaka kufikia asilimia 40 ya makusanyo ya mapato kwa vyanzo vya ndani kutokana na sekta husika kuboreshwa na kuwa za kisasa zaidi. Hii inajumuisha matumizi ya pembejeo na zana bora za kilimo, kuwekeza katika miundombinu bora ya kilimo, mifugo na uvuvi na kuboresha tafiti. Haya yakifanyika yatasaidia kufikia na kuvuka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli kwa Wizara ambayo bado yapo chini kwa mwaka 2016/2017 ambapo lengo lilikuwa ni kukusanya kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni nne kiwango ambacho ni kidogo sana ukilinganisha na uwezo wa sekta hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya tabianchi kupewa kipaumbele, yaani ni kuhuisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika bajeti ya Wizara na sekretalieti za mitaa. Ninatambua jitihada zilizofanywa na Wizara hii kuhuisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika mipango yao, hata hivyo bado hicho hakijafanyika vizuri katika bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukizingatia masuala ya kijinsia, yaani ni kuandaa na kutoa taarifa za kibajeti zenye mchanganyiko na mchanganuo wa kijinsia. Taarifa hizi za mchanganuo zitasaidia zaidi katika mipango na maamuzi katika sekta hizo ambazo zinachangiwa zaidi na wanawake. Hivyo basi mahitaji maalum yatatambuliwa na kuwekewa mikakati mizuri na imara ya utekelezaji. Vilevile kuboresha mkakati wa kuwasaidia wakulima wanawake wadogo wadogo. Hivyo Wizara na Serikali kiujumla inahitaji kupitia upya na kuboresha utekelezaji wa kuwasaidia wakulima wanawake na wakulima wadogo wadogo ili waje na mrengo wa kijinsia na hivyo kuwasaidia ikiwemo katika upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuajiri Maafiasa Ugani wa kutosha, hii itaongeza uwezo wa Serikali kutoa elimu ya ugavi kwa sekta hizo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi. Hivyo agizo la kusitisha ajira zikiwemo za maafisa ugani lisitishwe, Wizara iombe kibali mara moja cha kutoa ajira kwa mamlaka husika, na pia suala hili liwekwe katika bajeti za Halmashauri zote zenye uhitaji ili kufanikisha utekelezaji wake. Pia kuboresha uwezo wa maafisa waliopo ili kuendana na mabadiliko ya taaluma na teknolojia kwa kupewa mafunzo rasmi ya vyuoni, semina elekezi na pia ziara ya mafunzo kwa maeneo mengine ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ya viwanda haitakuwepo kama kilimo hakitapewa kipaumbele na kuzitumia sekta hizi vizuri na kuziboresha na kuziwekea bajeti ya kutosha na kufika kwa wakati kwa maslahi ya umma na Taifa hili kwa ujumla wake. Vilevile kuweza kuithamini kauli yetu ya kuwa kilimo ni uti wa mgongo na kilimo kwanza yenye Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ZAINAB MUSSA BAKARI: Mheshimiwa Naibu Spika, Maji ni Uhai. Maji ni kila kitu katika maisha ya kila siku ya binadamu; ndiyo maana ukaja msimamo kuwa maji ni uhai. Tukizungumzia uhai tunazungumzia maisha ya kuweza kuishi na kuleta afya njema ambayo yatatengeneza uwezo wa mwanadamu na viumbe vingine viweze kuishi na kuleta tija na mwisho kutimiza kiu yetu ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Serikali ione sasa umuhimu wa kuvuna maji. Yaani iandae mkakati wa makusudi wa kuvuna maji hususani wakati wa mvua na hata maji yanayoporomoka katika milima yetu. Ni jambo la ajabu wakati wa mvua kuwa na mafuriko na baadaye mifugo na binadamu ikaanza kufa kutokana na ukame. Kuwe na utaratibu wa kujenga mabwawa ya kuhifadhia maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuwe na mfumo wa kuvuna maji kwa kuhakikisha nyumba zote zinazojengwa ziwe na mfumo wa kuvuna maji wakati wa mvua, hii itasaidia sana kero hili kuondoka. Pia suala la kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini limejadiliwa, sana na leo hii niulize Wizara na Serikali, uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini utaanza lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji ni suala nyeti na hasa kwa sababu Rais wetu anatamani kuwatua kina mama na watoto kuwatua ndoo ya maji kichwani, hivyo kuna haja ya kutimiza azma ya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Hivyo Serikali ione sasa umuhimu wa kuokoa taifa hili kwa kuwanusuru kina mama na watoto vifo.

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia tisa ya vifo vya watoto vinatokana na kutumia maji yasiyo safi na salama. Kuna maradhi ya milipuko kama vile Typhod, Kipindupindu na kuharisha na kutapika. Ni wakati sasa wa kupunguza vifo hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iongeze bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Mfuko tulioongeza tujue matumizi yake yakoje. Pia tunaomba kuwe na tozo, kila lita moja ya mafuta itozwe 100 kwa kila lita ziende kwenye maji au Mfuko wa Maji. Hali kadhalika asilimia 70 ipelekwe kwenuye miradi ya maji vijijini na asilimia 30 miradi ya mijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sasa wakati wa kumtua mama ndoo kichwani umefika; nazungumza hivyo kwa msisitizo; ni wakati sasa kina mama na watoto kufanya kazi nyingine za kimaendeleo badala ya kufuata maji sehemu za mbali na kutumia saa moja kutafuta maji au wastani dakika 33 kufuata maji. Ni shida na ni kero sana kwa wananchi; wananchi wanakosa kushiriki mambo mengi ya kimaendeleo. Hata hivyo zile mita 400 za kupata maji si toshelezi, hivyo Serikali ikishirikiana na Wizara walione hili kuwa ni bughudha na kero kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ione umuhimu wa hili na kuongeza bajeti ya maji ili tupate muda wa kufanya kazi za maendeleo. Pia lazima tuwe na msisitizo katika Kilimo cha Umwagiliaji kwani Kilimo ni Uti wa Mgongo hivyo tutumie mito yetu vizuri kwa kuweka mfumo mzuri wa kuweza kumwagilia ili kilimo hcetu badala ya kungojea mvua tu tutumie vyanzo hivi ili kuweza kukuumarisha kilimo chetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali izingatie suala hili kwa upana na huruma ili iweze kumuokoa Mtanzania katika shida hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni Wizara yenye majukumu muhimu katika maendeleo ya nchi yetu. Sisi kama Wabunge tuna wajibu wa kuwakumbusha na kuwashauri. Majukumu ya Wizara hii ni kama ifuatavyo:-

(i) Kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na nje ya nchi pamoja na matumizi yake;

(ii) Kubuni na kusimamia utekelezaji wa sera za uchumi na kijamii kwa ujumla;

(iii) Kuandaa na kutekeleza bajeti ya Serikali;

(iv) Kufuatilia utekelezaji wa mipango ya kupunguza umaskini katika sekta mbalimbali;

(v) Kusimamia Deni la Taifa na upatikanaji wa rasilimali fedha;

(vi) Kusimamia Tume ya Pamoja ya Fedha;

(vii) Kulipa na kuandaa watumishi Serikalini;

(viii) Kudhibiti biashara haramu ya fedha pamoja na ufadhili wa ugaidi na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati sasa umefika kwa Serikali kulipa deni la ndani. Kwa kulipa madeni ya ndani itatufanya tuweze kuendelea katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo na kutimiza vizuri mikakati tuliyoiweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upatikanaji wa fedha kutoka Hazina limekuwa ni la kuchelewa sana. Kwa muda mrefu sana sasa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imekuwa ikichelewesha sana kupeleka fedha kwenye Wizara na Idara mbalimbali za Serikali kama zilivyoidhinishwa na kufanya shughuli za kimaendeleo kushindwa kufanyika na kushindwa kutimiza malengo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za Muungano ni changamoto ya muda mrefu. Iko wazi kabisa kwa kuwa kuna mamlaka tatu ambazo ziko dhahiri wala haziepukiki lakini imekuwa utamaduni fedha za Muungano kutumiwa na Tanganyika wakati Zanzibar ikikoseshwa fedha hizi ambazo ziko kisheria. Hivyo, tunaiomba Wizara ya Fedha kupitia Serikali kutatua kero hii ya muda mrefu na mamlaka hizi zipewe haki zake na zionekane ili kuepusha migongano isiyo ya lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya mazingira imetengewa fedha kidogo sana ukizingatia mazingira ni eneo muhimu kwa maisha ya viumbe vyote vyenye uhai. Kwa hiyo, nashauri sekta hii iongezewe fedha ili iendane na hali halisi ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti naishauri Serikali kupunguza utitiri wa kodi kwa wananchi na wafanyabiashara. Jambo hili linapelekea biashara nyingi kufungwa na Serikali kukosa mapato ya kuendesha nchi yetu. Pia Serikali ifike mahali ifahamu kwamba katika biashara ya kila Mtanzania Serikali ni shareholder kwa asilimia 30% hivyo iwawezeshe wafanyabiashara wafanye biashara ili kuendeleza biashara na kuleta pato kwa Tanzania badala ya kuwafukuza na kufunga biashara na Serikali kukosa mapato kwa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwe inatekeleza ahadi zake na utekelezaji uonekane. Hii imeonekana kwani mwaka jana Serikali iliahidi kugawa EFD machine kwa wafanyabiashara lakini mpaka leo haijagawa machine hizo. Hili linarudisha nyuma maendeleo ya umma. Pia napenda kujua ni utaratibu gani unatumika kugawa EFD machine na watu gani wanapaswa kutumia hizi EFD machine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ihakiki madeni ya watumishi na watoa huduma. Bado tunasisitiza Wizara ya Fedha na Mipango kuendelea kuhakiki na kulipa madeni mbalimbali ya ndani hasa watumishi, wakandarasi, wazabuni na watoa huduma wengine ambao baadhi yao walikopa benki kupata mtaji ili waweze kutoa huduma kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa dunia kwa kuweza kunifikisha katika hali ya uzima katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nawashukuru Viongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kufanya kazi kwa hali ambayo ni ngumu sana. Jambo la tatu, kabla sijaendelea kuchangia, naunga mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba hii ya Waziri Mpango ambayo ni hotuba ya Serikali, nimeshangaa kwamba hotuba nimesoma yote, lakini halijazungumziwa suala la ajira. Suala la ajira ni suala muhimu kwa kila Mtanzania. Tunaona watu wanamaliza Vyuo mamia kwa mamia, lakini mwisho wa siku wanaranda na vyeti vyao mifukoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Serikali hii inawapenda Watanzania ni bora wachukue suala hili walifanyie kazi vizuri sana. Kwa sababu suala la ajira ni muhimu kila mtu anapatia mahitaji yake. Nasema hivi kwa sababu wananchi wa Tanzania hawajapewa elimu ambayo
itawawezesha kujiajiri. Pindi watapewa elimu ya kujiajiri ndiyo hili suala ambalo pengine lingeweza kufanywa, kwa hivi lilivyofanywa katika bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka kulizungumzia ni suala la kilimo; Kilimo ni uti wa mgongo. Marais mbalimbali walikuja na kauli mbiu mbalimbali. Kuna wengine ambao walisema Kilimo kwanza, lakini naona katika bajeti hii haijapewa kipaumbele. Kilimo kimedharauliwa, ukiangalia kwamba kilimo chetu kinakuwa kwa asilimia 1.7, hii ni kwamba Serikali hii ya CCM haijakipa kilimo kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kilitarajia kifikie asilimia sita ya kukua lakini mpaka sasa hivi kilimo kimefikia asilimia 1.7. Hii ni ndoto kwamba tutategemea Serikali ya Viwanda, Serikali ya Viwanda itakuwa haipo kwa sababu kilimo hakijapewa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nakusudia kulizungumza ni kwamba Serikali hii katika bajeti yake Mheshimiwa Waziri Mpango, haijatuambia kwamba imetekeleza kupunguza umaskini kwa kiasi gani? Nimesoma bajeti hii lakini sijaona sehemu ambayo Serikali kama imejipanga na kama iko tayari kuwasaidia Watanzania kutuambia kwamba wamejipanga ni namna gani watapunguza umaskini Tanzania? Tunawaona akinamama na akinababa wanaangamia kutokana na kwamba umasikini umekithiri katika nchi hii ya Tanzania. Tukizungumzia umaskini ni kwamba, katika maeneo mengi wananchi wa Tanzania wako katika hali duni. Kwa hiyo, ni muhimu sana bajeti hii ilikuwa ielezee ni kiasi gani itapunguza umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la Motor Vehicle. Katika bajeti hii tukiangalia ukurasa wa 48, tumeambiwa kwamba watu ambao wana magari wamesamehewa ada ya kulipa Motor Vehicle. Kiukweli ni kwamba ada hii haikutolewa bali imepelekwa kwenye vyanzo vingine. Ni jambo ambalo linawaumiza Watanzania hususan watu ambao wanaishi vijijini. Tozo hii imewekwa katika mafuta ya taa Sh.40/=. Hii inamkandamiza mwanamke wa kijijini, inawakandamiza wananchi wote wa vijijini kwa sababu wao ni watu wa hali duni, kuwalipia watu wenye wanamaslahi makubwa, watu wa kati na wakubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukisema kwamba hatujamkandamiza Mtanzania ambaye yuko katika hali ya chini, hii itakuwa siyo kweli kwa sababu bajeti yetu imeonesha kwamba inawapendelea sana watu wa kati na matajiri kuliko watu wa chini. Kwa hiyo, naiomba Serikali, kama ikiwezekana, ada hii kama hawataki waiweke katika Motor Vehicle, basi waifute kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nitakalozungumzia ni kuhusu madini. Madini ni Rasilimali muhimu katika Tanzania hii. Ni jambo la kushangaza kwamba madini yetu yanaibiwa kila siku kwa sheria za ovyo ambazo zimetungwa na Serikali ya CCM. Leo hii wanakaa hadharani kutaka kujisafisha jambo ambalo haliwezekani. Ni bora kwanza waseme ukweli kwa sababu kulikuwa na Waheshimiwa Wabunge wengi wa Kambi Rasmi ya Upinzani wakilizungumzia suala hili, lakini mkiwaona sio lolote sio chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Tanzania imeshaibiwa matrilioni kwa matrilioni ndiyo leo tunaona kwamba mtu au Kiongozi anatoka hewani na kusema kwamba tunaibiwa. Tumeibiwa sana na tutaendelea kuibiwa kama hatutarekebisha mikataba yetu na sheria zetu. Nasema hivyo kwa sababu gani? Tuna madini pia ya Tanzanite ambayo Tanzania pekee ndiyo ambayo…

TAARIFA . . .

MHE. ZAINAB MUSSA BAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza taarifa hiyo siipokei, kwa sababu mimi sikumtaja kama ni Mheshimiwa Rais. Kama umejishuku itakuwa ndio huyo huyo. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuchangia katika maoni yangu ni kwamba Tanzania hii ni pekee ambayo inazalisha Tanzanite, lakini leo kama hatuibiwi, Tanzania ni nchi ya nne ambayo inauza Tanzanite. Hivi nchi nyingine madini haya wanapata wapi kama itakuwa hatuibiwi? La muhimu ni kukaa tukaweza kurekebisha sheria zetu, zikaletwa hapa ili tuondoe janga hili la kuibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzungumza, ni kwamba… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nashukuru kwa kupata nafasi nami nichangie katika hotuba hii ya Waziri Mkuu. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya nzuri baada ya kupata ajali. Nawashukuru Wabunge wote ambao walikuja hospitali na ambao walinifariji kwa namna moja au nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, namshukuru Mwenyekiti wangu kwa misukosuko aliyoipata, lakini ukiona giza linazidi ujue alfajiri inakaribia. Jambo la tatu, napenda niunge mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia katika mambo machache. Jambo la kwanza nitakalochangia ni mapato ya Serikali na sekta binafsi. Hii ni sekta muhimu sana kwa Taifa letu kwa sababu ni sekta ambayo inakusanya mapato ya Taifa. Sekta hii imekuwa ni kama adhabu kwa wananchi na sekta binafsi, kwa sababu katika sekta hii kuna milolongo mingi ya kodi. Kwa mfano, unapoanzisha biashara ama kampuni, kuna milolongo mingi ya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, utatakiwa kusajili biashara yako ama kampuni, inahitaji hela; pili, utatakiwa kodi ya mapato ya TRA, ni hela; kulipa kodi la zuio, ni hela; kulipa kodi ya ujuzi, ni hela; na hali kadhalika. Hivi kwa mlolongo huu wa kodi, sekta binafsi ndiyo maana zinafunga kampuni zao na wafanyabiashara wanafunga biashara zao. Kwa nini tusiweke kodi ambazo ni chache na kodi ambayo itakuwa ni rafiki kwa wananchi na sekta binafsi kuliko kuweka mlolongo huu ambao unasababisha biashara kufungwa na sekta binafsi kukimbia katika nchi yetu? Hatuoni kwamba hii ni hasara katika nchi yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoweka kodi ndogo ni kwamba wananchi wote watalipa kodi na Serikali itapata mapato ya kutosha, lakini tunapoweka utitiri huu wa kodi, inasababisha wale ambao tunasema wajiajiri washindwe kujiajiri; na wale ambao wataajiriwa na sekta binafsi, sekta binafsi zisiweze kuajiri kwa sababu hali ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongelee suala lingine la demokrasia nchini. Hali ya demokrasia nchini ni mbaya sana. Naomba tujitathmini. Serikali ya CCM ijitathmini, ni demokrasia gani ambayo inaonesha? Ni demokrasia gani ambayo wenzetu wanaotuangalia sisi tunawaonesha? Ni kwamba sasa hivi Serikali ya CCM inazuia vyama vya siasa kufanya kazi za siasa wakati Chama cha Siasa kazi yake ni kufanya siasa. Sasa unapoizuia unataka wafanye kazi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ina-base upande mmoja. Tunaona kwamba vyama vya Upinzani wanazuiwa kufanya mikutano, wanazuiwa kufanya kazi yao ya siasa. Tukiangalia Chama Tawala, kinafanya mikutano, kinafanya siasa, kinazunguka nchi nzima bila kubughudiwa, lakini leo vyama vya Upinzani ukitaka kufanya siasa, unaambiwa kuna intelijensia, sijui kuna namna gani, huo ni uoga. Hivyo ndivyo mnakufa kidogo kidogo kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kama hiki kikiendelea, mhakikishe 2020 hapa hamtashika dola, kwa sababu wananchi sio wajinga, wanaona yote mnayoyafanya.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Mlinga.

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka nimpe Taarifa mzungumzaji kuwa kufanya siasa siyo kufanya mikutano ya hadhara tu, kufanya siasa hata anayofanya Mheshimiwa Lipumba kuwaondoa wasaliti ndani ya CUF, hiyo ni siasa tosha. (Kicheko)

MWENYEKITI: Unasemaje na Taarifa hiyo Mheshimiwa?

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siwezi kupokea taarifa hiyo, kwa sababu ninavyojua chama cha siasa, ni kufanya siasa. Leo CCM wanafanya maandamano, lakini wakifanya Chama cha Upinzani inakuwa ni zogo, Polisi, ni kwamba ninyi mnajidai kutokana na kwamba mnalindwa na dola, lakini iko siku hiyo dola itavua jukumu la kuwalinda ninyi ambao mnawateka wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkiendelea hivyo, niwahakikishie 2020 mtalala kifo cha mende. (Makofi/ Kicheko)

MBUNGE FULANI: Waambie!

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niendelee kuchangia. Nataka nichangie katika maandalizi ya uchaguzi na Tume Huru. Tume Huru ni kilio cha siku nyingi katika nchi hii. Serikali ya CCM inajificha katika kivuli ambacho sijui nikiite kivuli gani kwa sababu hawataki kuleta Tume huru ya uchaguzi kwa sababu wanaona ikiletwa Tume huru ya uchaguzi ndiyo kifo chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia katika Tume hii hasa muundo, Maafisa wote wa Tume ni makada wa CCM, Wakurugenzi wote ni makada wa CCM walioshindwa uchaguzi. Hivi hapa kweli pafanyike uchaguzi upinzani, hata siku moja. Huko ni kujitekenya huku mkijichekesha wenyewe. (Makofi/Kicheko)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba Tume ya Uchaguzi ni huru sana na ndiyo maana huyu Mbunge anayezungumza ni Mbunge wa Viti Maalum baada ya Tume kutangaza Wabunge wa CHADEMA wengi wakapata Viti Maalum. Pia mimi nilitangazwa na Tume hii nikiwa CHADEMA na nimetangazwa tena nikiwa CCM, maana haipendelei kabisa. Hii Tume ni huru, waendelee kuchapa kazi, wanatenda haki na hiyo ndiyo taarifa. (Makofi/ Kicheko)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa…

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa hiyo kwa sababu alitoka huku akaenda huko, wakiweko huko wanakuwa kama wamerogwa fulani wanaropokwa ropokwa tu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama CCM inajiamini, ithubutu leo hii kuleta Tume Huru ya Uchaguzi. Kama CCM inajiamini, ithubutu leo hii kuleta Katiba mpya ya wananchi inayopendekezwa. Nawapa changamoto hiyo, mkiweza, nitajua mnajiamini, lakini mnashindwa kujiamini kutokana na kwamba mkileta Tume Huru ya Uchaguzi au Katiba ya wananchi inayopendekezwa kwa dola mtasahau.

KUHUSU UTARATIBU

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu…

MWENYEKITI: Kuhusu utaratibu kanuni ya ngapi?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI: Kanuni ya ngapi, nakuuliza?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia Kanuni ya 64(1) (a). Mheshimiwa Mbunge anayechangia hatatumia ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli. Mimi sijalogwa. Kwa hiyo, naomba athibitishe au afute hiyo kauli. Kikanuni, naomba athibitishe au afute hiyo kauli, mimi sijalogwa. Nathibitisha niko timamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba afute hiyo kauli au alithibitishie Bunge kwa mujibu wa kanuni hii.

MWENYEKITI: Endelea.

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niendelee kuchangia. Wakati watu wanadai Tume Huru ya Uchaguzi ziliundwa Tume zaidi ya tatu; iliundwa Tume ya Jaji Nyalali, Kamati ya Jaji Robert, baadaye ikaja Rasimu ya pili ya Katiba mpya na wananchi wote walitoa maoni yao kwamba wanataka Tume Huru ya Uchaguzi. Ni kwamba Tume iliyopo hapa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar siyo huru.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa Ulimwengu na vilivyomo ndani yake tukiwemo sisi wanadamu. Aidha, napenda tujue kwamba Allah ana sheria zake ambazo tunapaswa tuzitii na kuzifuata. Vilevile na sisi binadamu tumeandaa sheria zetu na kanuni ili kuzifuata na kuzitii ambazo ni sheria za nchi husika zinazotutaka kila raia kuzifuata na hakuna mtu aliye juu ya sheria. Kwa maana nyingine, ndiyo tukatengeneza Katiba ambayo ni Sheria Mama ya nchi yetu Tanzania. Ndiyo maana Bunge na Wabunge wako hapa kuilinda Katiba na hata Kiongozi wa nchi naye huapa kuilinda Katiba hii hii, kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Katiba na Sheria ndiyo Wizara nyeti na Wizara ambayo husimamia majukumu ya Katiba, Sheria, Kanuni na utaratibu zilizowekwa na vyombo halali vya maamuzi. Baada ya kutoa ufafanuzi huo, ama utangulizi huu napenda kutoa maoni yangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na upotoshaji na uvunjifu wa Sheria na Katiba yetu kwa wananchi na viongozi wa nchi na kuwa juu ya sheria, jambo ambalo siyo zuri na ni baya sana na litapelekea uchafuzi wa demokrasia na amani ya nchi, kwa sababu kuna ambao wako juu ya sheria na kuna ambao wako chini ya sheria; jambo ambalo ni baya sana na nalipinga kwa nguvu zote na naomba Bunge lako lipinge na Wizara husika itoe kauli na kupinga vikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi ambacho Taifa hili linapitia katika changamoto na ugumu mkubwa ni kipindi hiki. Kumekuwa na changamoto ya kutoheshimu utawala bora wa sheria; ni kipindi ambacho Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria mbalimbali za nchi na Kanuni zote hazifuatwi, badala yake kuvunjwa sheria kwa makusudi. Kwa hiyo, Wizara ya Katiba na Sheria ndiyo Wizara yenye jukumu la kuhakikisha kuwa nchi hii inaongozwa kwa kuzingatia Katiba ya nchi hii ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na msisitizo huu kuwekwa kwenye maneno ya utangulizi (Preamble) ya Katiba yetu, tangu mwishoni mwa mwaka 2014 mpaka leo, ninapotoa maoni yangu, nchi yetu imekuwa ikipitia katika kipindi kigumu cha janga la Kikatiba ambapo Serikali ya CCM haisimamii misingi ya Katiba ya mwaka 1977 wala haina mpango wowote madhubuti wa kurejesha mchakato wa Katiba pendekezwa ya Jaji Warioba ya mwaka 2014.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inathibitishwa na kauli ya Mheshimiwa Rais kuwa hajawahi kuahidi kuhusu Katiba Mpya na wala haikuwa sehemu ya ahadi zake za Kampeni kauli inayokinzana na Ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo katika ukurasa wake wa 206 – 207 kipengele cha 145(e) inasema “ Ili kuendeleza utawala bora, demokrasia na uwajikaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo 2015 – 2020, CCM itahakikisha kuwa Serikali inatekeleza yafuatayo: (e) Kukamilisha mchakato wa kutunga Katiba Mpya na kuanza kuitekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.” Mwisho wa kunukuu. Kwa hiyo leo hii Serikali ya Chama cha Mapinduzi inakana Ilani yake iliyoinadi kwenye uchaguzi na badala yake inaikanyaga Katiba kupitia viongozi wake. Huko ni kuvunja uaminifu na maadili ya Chama na Serikali yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na uvunjifu wa sheria na ukiukaji wa Katiba na Utawala Bora kwa mambo ambayo yanaendelea kujitokeza katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Kuna ushahidi wa kimazingira unayoonesha baadhi ya uteuzi kufanyika kwa fadhila baada ya wahusika kufanya vitendo vya kuwanyima haki watu wengine kwa lengo la kutekeleza matakwa ya utawala. Mfano, uteuzi wa Hakimu mmoja kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa Jaji wa Mahakama ya Tanzania, ni miongoni mwa teuzi ambazo zinaonesha ushahidi wa kimazingira kwamba ni fadhila kwake baada ya Hakimu huyo kufuta dhamana ya Kiongozi Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman A. Mbowe, pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini Mheshimiwa Esther Matiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uteuzi wa Jaji ulikuwa ni fadhila kwake baada ya kutekeleza hila au kile ambacho alielekezwa na mamlaka zilizomtuma ama kujipendekeza. Hali hii haikubaliki kwenye nchi ambayo inasimamia vizuri Demokrasia, Sheria, Kanuni na Utaratibu tuliojiwekea katika Katiba ambayo tuliahidi kuilinda na kuifuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, narudia kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria. Kwa hiyo, ni wakati wa kutenda haki na kusimamia Utawala Bora wa Sheria na kutimiza ahadi zetu tulizoweka mbele ya Mungu kwa kiapo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ni muhimu sana ukitoka Wizara ya Elimu. Hii ni Wizara yenye kushikilia maisha ya Watanzania. Bila kuimarisha Wizara hii, hakuna Serikali ya Viwanda wala Tanzania ya Viwanda kwani afya ni kila kitu. Watanzania wakiwa na afya bora ndiyo shughuli za kiuchumi zitakuwa na maendeleo, kwani mwenye kuleta maendeleo ni wananchi wenye afya bora na nguvu kazi ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nitoe maoni yangu katika Wizara hii. Kwanza ni upungufu wa rasilimali watu katika Wizara hii ya Afya. Sekta hii ina upungufu mkubwa wa rasilimali watu. Sekta hii ina upungufu wa watumishi kwa asilimia 49 katika mwaka wa fedha 2016/2017. Tunaomba Serikali itoe hitaji la watumishi wa sekta hii ya afya ili wananchi wapate matibabu kwa wakati na kwa ubora wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Mheshimiwa Waziri aone kilio cha Watanzania juu ya hitaji hili muhimu. Imekuwa na usumbufu kwa wananchi wanapohitaji matibabu wanachukua muda mrefu hospitalini, mtu anakwenda saa 12.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni ndiyo anapata matibabu kutokana na uhaba wa wahudumu. Mhudumu ana daktari mmoja, huyo anahitajika zaidi ya vitengo vitatu kwa wakati mmoja. Hii ni shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ituambie ni lini itatatua tatizo hili la upungufu wa watumishi katika sekta hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitazungumzia hali ya maambukizi ya VVU na UKIMWI nchini Tanzania. Hali hii inaendelea kukua kwa kasi zaidi kinyume na hali iliyotarajiwa. Dhana nzima ya 90 – 90 – 90 iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kuhusu HIV/AIDS mwaka 2013 kwamba ili kufikia mwaka 2020 kusiwepo na maambukizi ya UKIMWI Duniani. Kwa maana, kutambulika, waliotambulika wako kwenye matibabu ya ARV na wenye matumizi ya ARV, virusi vitakuwa vimefubaa na hakutakuwa na maambukizi mapya. Hii ndiyo azma ya 90 – 90 – 90.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Tanzania, hatujafikia hatua hii, ni hatari sana na ndiyo kwanza maambukizi yanazidi. Kwa mfano, vijana kati ya miaka 15 - 49 ndiyo rika hatari zaidi na wenye kuleta maambukizi zaidi. Hawa ni vijana ambao wako shuleni na vyuoni kwa asilimia 46. Je, Tanzania tumefikia wapi katika kufikia lengo la 90 – 90 – 90 na tukizingatia umebaki mwaka mmoja na nusu kufikia muda uliowekwa na Umoja wa Mataifa? Serikali itufahamishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali na Sekta hii itoe elimu kuhusu HIV/UKIMWI na isione haya kueleza vitu vinavyosababisha maambukizi, bila kificho. Kama Serikali haitaacha kupiga marufuku condom UKIMWI utaendelea kuwepo, kwani hivi ni vichochezi vya zinaa. Vitabu vya dini vinasema tusikaribie zinaa, zikishamiri maradhi yatazidi ama majanga na hili ni janga na siyo maradhi kwani kila maradhi huwa yana tiba ila UKIMWI hauna tiba. Ili UKIMWI uondoke, tuache zinaa tutake tusitake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii inatisha sana hasa tukizingatia maambukizi kwa vijana hawa wadogo. Hii ina maana nguvukazi ya Taifa hii inapungua na kufa pia kwa kasi sana na tusipochukua tahadhari tatizo hili ni zito na kubwa sana, huenda miaka ya mbele tutakosa kabisa vijana wenye afya bora wa kujenga Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia maambukizi mapya na kuweka sheria, kama ni kosa la jinai kufanya zinaa au vitendo hivi bila ya kuwa na ndoa. Kinyume na hayo tutatenga pesa ama fedha nyingi za kutibu na maambukizi yataongezeka na mwisho tutakosa nguvukazi za Taifa na hivyo Tanzania ya Viwanda itabaki kuwa ndoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda nikushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi. Pili naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza kwa hadithi moja ambayo inasema: “alamatu-l- munafiq thalatha; idha hadatha kadhaba, waidha’waada akhlafa, waidha’atumina khana; alama za mtu mnafiki ni tatu, akizungumza husema uongo, akiweka ahadi hatimizi na anapoaminiwa hufanya hiana. Hapo hapo kuna msemo kwamba ahadi ni deni na deni hilo utakwenda kulilipa mpaka mbele ya Allah (Subhanahu Wataala). (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeanza kwa maneno hayo kwa sababu zifuatazo; napenda kuzungumzia, kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano iliweka ahadi kujenga border post katika Bandari ya Wete mpaka sasa Bandari hiyo haina Border Post. Namtaka Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango akija aje atuambie, kuna kikwazo gani kilichosababisha kutojengwa kwa border post katika Bandari ya Wete? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitazungumzia tena juu ya masuala ya miradi mitatu ya Zanzibar. Huu ni Muungano na tulikubali wenyewe kuungana na kuna ahadi ambazo tuliwekeana kwamba tutatimiza kote kote bila upendeleo. Sasa, sijui katika hadithi hii kama Serikali ya Muungano itakuwa salama na itakwenda kujibu nini mbele ya haki?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mradi wa barabara ya Wete-Chakechake, hili ni suala ambalo lipo zamani.

Nashangaa, kipindi cha Waziri wa Fedha ambaye amepita, nadhani ni Marehemu, Mheshimiwa Mgimwa, alitia saini mkataba huu wa barabara ya Wete. Sijui kuna chokochoko gani na figisufigisu gani mpaka sasa hivi umekwamisha mradi huu usitekelezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hili kwa sababu, tunajifanya kwamba watu wa Tanzania Bara na watu wa Zanzibar ni ndugu wa damu. Ni damu gani ambayo inapenda kuangamiza wenziwe? Udugu huu wa makopa hatuutaki wala hatuutamani. Udugu wa kukutana kwenye madishi, huu siyo udugu. Udugu ni kufaana. Tujengeeni barabara hiyo ili mtimize ahadi zenu, siyo kila siku mnasema uongo. Mtu mwongo anajua mahali pake pa kwenda kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumza hili kwa uchungu sana. Barabara takribani kilomita 40 tu zinashindwa kujengwa. Ninyi huku Tanzania Bara mnajenga barabara hata kilomita 1,500 na kuendelea; hivi hamwoni huku ni kuwanyanyasa Wazanzibari? Wazanzibari wamewakosea nini? Wazanzibari mmewafanya, mme, aaah, sijui hata nitumie neno gani! Huku ni ninyi Serikali ya Muungano mnaingia katika alama za watu wanafiki ambazo ni tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuzungumzia suala la mradi wa airport ya Zanzibar. Dar es Salaam mnajenga airport, mmemaliza; terminals zinafika sijui four sijui ngapi? Kule Zanzibar, mnakuona sijui kama kichaka gani? Mpaka leo terminal three imeshindwa kumalizika kutokana na kwamba hamtaki kutia saini. Sijui roho hiyo mbaya mnaipata wapi? Sijui kwa nini mnataka Wazanzibar wasiukatae huu Muungano. Tukisema hivyo tunaambiwa ni wachochezi. (Makofi)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni suala ambalo halikubaliki.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia napenda kuzungumzia miradi mitatu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ni Mradi wa Barabara ya Wete hadi Chakechake, takribani kilomita 40; Bandari ya Mpiga Duro Malindi Zanzibar na Mradi wa Ujenzi wa Airport ya Pemba na hitimisho la Uwanja wa Ndege wa Unguja Terminal 3. Serikali ya Muungano ikishirikiana na Wizara ya Fedha wamekataa miradi hii isiendelee na Wazanzibar wasifaidike na miradi hii; uchumi wa Wazanzibar uendelee kudidimia. Nasema hivi kwa sababu Serikali ya Muungano imekataa kuweka saini kwenye miradi yote hii maana yake hawapendi kuona maendeleo katika upande wa pili wa Muungano yakitokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni unyanyasaji na ni hasadi ya hali ya juu kabisa. Serikali ya Muungano inashindwa kujenga kilomita 40 Zanzibar lakini Tanzania Bara wanajenga zaidi ya kilomita 1,500 za barabara; hii kama si hasadi ni nini? Kila siku tunaambiwa tu wachochezi tukizungumzia suala la Muungano, kwamba halina umuhimu wowote kwa maslahi ya Zanzibar. Leo hii limedhihirika kwa kukataa kuweka saini; halafu tunaambiwa ni ndugu zetu wa damu. Damu gani hii ya kudhulumiwa? Huu si ndio udugu wa makopa wa kukutania kwenye sufuria, ambao hauna faida yoyote ile? Bora ukatike, udugu huu hauna tija yoyote ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali ya Muungano iweke saini ili tujenge barabara, bandari ambayo inaweza kufunga gati kwa meli zisizozidi 5 ingawa ya Bagamoyo mlikata wenyewe ambayo ingeweza kufunga nanga meli takribani 35. Mliikataa wenyewe ila sisi tunahitaji hiyo bandari na viwanja vijengwe ili kuinua uchumi wa nchi yetu. Serikali hii ya Awamu ya Tano haijui kipaumbele chake. Iliingia madarakani kwa kujigamba, kujinata na mbwembwe tele kuwa ni Serikali ya viwanda mpaka, sasa hatuoni viwanda hivyo na vichocheo vya viwanda havipewi pesa za kutosha. Tukiangalia sekta ya kilimo imetupwa mbali wala haithaminiwi. Ni wazi kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Kilimo inachangia ajira kwa asilimia 70, Pato la Taifa kwa asilimia 28.2, lakini ukuaji wake ni mdogo sana na wa kusuasua, sawa na asilimia 5.2. Hali hii inapelekea kutofikia ndoto ya Tanzania ya Viwanda. Napenda kuishauri Serikali kuondoa kodi zifuatazo ili kufikia kwenye ndoto ya Tanzania ya Viwanda.

(a) Kodi kwenye uwekezaji wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

(b) Hali kadhalika kuondoa kodi kwenye viwanda vinavyotengeneza na kukarabati mashine, zana na pembejeo za kilimo, uvuvi na mifugo.

(c) Pia uwepo wa umeme wa uhakika.

(d) Kushirikisha sekta binafsi kwa kupitia mpango wa PPP.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri Mpango ayachukuwe haya na kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imewasusa watumishi wa umma ambao ni walipa kodi wa uhakika. Serikali hii imekuwa ikisuasua kuwapa watumishi nyongeza ya mshahara ya kila mwaka (annual increment) pamoja na madai yao mengi kama fedha zao za likizo, kupandishwa madaraja na malimbikizo ya mishahara; jambo ambalo ni la kisheria na kikanuni. Hata wanaopandishwa madaraja halafu unastahiki pindi wakipandishwa madaraja hulipwa mshahara uleule wa mwanzo; jambo ambalo si halali. Hata hivyo katika mwaka huu wa fedha nimeona takribani trilioni saba. Hizi ni za mishahara tu hizo nyingine sijaziona.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali ya Awamu ya Tano wataacha kuwakandamiza watumishi hawa? Huku ni kuwafanya maisha yao yaendelee kuwa magumu; na pia Serikali hii haina nia njema kwa watumishi hawa. Hali kadhalika kuna dalili ya kuwadhulumu mafao watumishi hawa ambao ni walipa kodi wa uhakika wa nchi hii. Tunaitaka Serikali iache mara moja tabia hii ya kuwadharau watumishi hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni kuhusu taulo za kike. Tunaitaka Serikali iache kigeugeu itoe hiyo kodi kama ilivyofanya awali ili watoto wetu wasitirike na kutowatoza kodi kutokana na maumbile yao na jinsi yao. Huu ni unyanyapaa na ubaguzi wa hali ya juu, kuwatoza kodi kila mwezi na wengine mwezi mara mbili kwa ajili ya maumbile yao. Jambo hili halikubaliki na hata dini zetu hazikubali. Naomba kuwasilisha na naunga mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani na yale yenye manufaa ya Waheshimiwa Wabunge wengine. Ahsante.