Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Lucy Fidelis Owenya (4 total)

MHE. LUCY F. OWENYA aliuliza:-
Barabara ya Old Moshi - Kiboriloni - Kikarara - Tsuduni - Kidia yenye urefu wa kilometa10.8 ni muhimu kwa uchumi wa wakazi wa Kata ya Old Moshi Mashariki na Taifa kwa ujumla hasa ikizingatiwa kuwa ni njia mojawapo ya kupanda Mlima Kilimanjaro.
Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kuzingatia ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Fidelis Owenya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Old Moshi hadi Kidia yenye urefu wa kilometa 10.8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Old Moshi - Kiboriloni - Kikarara - Tsuduni hadi Kidia ni barabara ya Wilaya inayohudumiwa na Halmashauri ya Moshi. Hata hivyo, ujenzi kwa kiwango cha lami utatekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kwa sasa kazi ya usanifu wa kina wa barabara hii upo katika hatua za mwisho kwa kuwa Mhandisi Mshauri tayari alishawasilisha rasimu ya usanifu ambayo tayari imepitiwa na TANROADS. Kwa sasa Mhandisi Mshauri anafanyia marekebisho ya rasimu ya usanifu ili kuzingatia maoni yaliyotolewa na TANROADS. Hatua itakayofuata baada ya kukamilika kwa marekebisho hayo ni kutangaza zabuni ili kumpata mkandarasi atakayetekeleza kazi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga jumla ya Shilingi milioni 2,583 ili kuanza ujenzi. Aidha, matengenezo mbalimbali ya barabara hii yanafanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi.
MHE. LUCY F. OWENYA aliuliza:-
Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imekuwa na tatizo la kukatika umeme mara kwa mara.
(a) Je, ni sababu zipi zinazosababisha hali hiyo?
(b) Je, ni lini tatizo hili litakwisha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Fidelis Owenya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa inayofaidika na utekelezaji hali ya utekelezaji wa miradi ya TEDAP. Mradi huu unafadhiliwa na Benki ya Dunia na unalenga kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme nchini. Kazi za mradi huu kwa Mkoa wa Kilimanjaro
zinajumuisha kuongeza uwezo wa vituo viwili vya kupoza umeme vya Trade School kutoka MVA 5 hadi MVA 15. Pia kuboresha miundombinu hiyo katika maeneo ya Boma Mbuzi kutoka MVA 10 hadi MVA 15. Hali kadhalika kubadilisha waya katika njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 kutoka milimita 100 hadi milimita 150. Vilevile kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme muhimu na bora.
Mheshimiwa Spika, mradi huu ulianza kutekelezwa mwezi Januari, 2014 na umekamilika kwa asilimia 95 ambapo sasa kilometa 50.95 kati ya kilometa 54.63 zimeshajengwa na waya zimeshaunganishwa.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha utekelezaji wa mradi huu kumekuwa na ulazima wa kuzia umeme katika baadhi ya maeneo ili kupisha marekebisho maalum na kwa usalama zaidi. Zoezi hili limekuwa likifanyika kwa kutoa taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari. Tatizo la
kukatikakatika kwa umeme katika maeneo ya Halmashauri ya Mji wa Moshi litaisha mara baada ya shughuli za Mradi huu kukamilika mwezi Mei, 2017.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE (K.n.y. MHE. LUCY F. OWENYA) aliuliza:-
Je, Moshi wa bangi una madhara gani kwa binadamu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Fidelis Owenya Mbunge wa Viti Maalum, kwa niaba ya Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali hili naomba niungane na wewe kumpa pole Mheshimiwa Lucy Owenya na watu wote walioguswa na msiba huu wa baba yake mzazi.
Mheshimiwa Spika, bangi ni mmea ambao huota sehemu nyingi duniani. Mara nyingi watu huvuta bangi kama sigara. Kemikali inayoleta ulevi na madhara mwilini kwa mtumiaji wa bangi inaitwa tetrahydrocannabinol (THC) ambayo hutoka kwenye moshi wa bangi inayochomwa au kuvutwa, hivyo moshi ambao unatokana na kemikali hiyo humletea mtu mwingine madhara sawasawa na ya mvutaji. Madhara hayo ni pamoja na akili kushindwa kuzingatia mambo kwa wepesi wake, huweza pia kuathiri vichocheo vya kike na vya kiume, kufanya mishipa ya kusafirishia damu kutokuwa na mnyumbuko halisi yaani kusababisha hardening of arteries na kuchanganyikiwa.
Mheshimiwa Spika, madhara ya kuvuta bangi hadharani ni makubwa hususani kwa vijana kwani madhara yake kwa mtu asiyevuta ni sawa na kwa ambaye anavuta. Ukweli wa madhara haya hudhihirika pale unapochukua sampuli ya damu na mkojo kwa mtu ambaye havuti bangi kwani utaikuta kemikali hii, hivyo kuonyesha uwezekano wa madhara ya moshi kwa mtu ambaye hatumii (passive cannabis smoker). Serikali inaendelea kutoa ushauri kwa vijana kuacha tabia ya uvutaji bangi na kushauri pia kwa wale ambao hawajaanza kuvuta kutojihusisha kabisa na uvutaji.
Mheshimiwa Spika, tunawashauri wale ambao wanavuta kutembelea vituo vya kutolea huduma kote nchini ili waweze kusaidiwa namna ya kuacha matumizi ya bangi.(Makofi)
MHE. MARWA R. CHACHA (K.n.y. MHE. LUCY F. OWENYA) aliuliza:-
Mradi wa Maji Vijijini katika Kata ya Old Moshi Magharibi katika Kijiji cha Mande haujatekelezwa kuanzia mwaka 2008; Je, ni sababu zipi zilizosababisha mradi huo kutokamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Fidelis Owenya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP I) Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ilipanga kutekeleza miradi ya maji katika vijiji 12. Kati ya vijiji hivyo ujenzi wa miradi umekamilika katika vijiji sita vya Korini Juu, Korini Kati, Korini Kusini, Kilima Juu, Kilima Kati na Golo na utekelezaji wa miradi iliyobaki unaendelea kufanyika katika awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II).
Mheshimiwa Naibu Spika, usanifu wa mradi wa maji wa Tela Mande ulikamilika mwaka 2013. Mkandarasi aliyeteuliwa hakuweza kuanza kazi na ulichelewa kutekelezwa kutokana na ufinyu wa bajeti. Halmashauri ya Wilaya ya Moshi iliutangaza mradi huu katika mwaka wa fedha 2017/2018 na kwa sasa mradi huo upo kwenye hatua ya tathmini (evaluation) ili kumpata mkandarasi wa ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, uUtekelezaji wa mradi huu unategemea kuanza mwezi Mei, 2018. Mradi huu utakapokamilika utahudumia wakazi 5,141 kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 kwa Vijiji vya Tela na Mande.