Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Yosepher Ferdinand Komba (10 total)

MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika majibu ya msingi ya Waziri amesema ugonjwa unaotokana na minazi haujapatiwa ufumbuzi. Katika Mkoa wa Tanga, tuna Chuo cha MATI Mlingano, Chuo cha Utafiti. Je, Serikali ina mpango gani wa kukifufua kile chuo ili wakulima wa mazao mengine kama korosho, mkonge, michungwa waweze kupata uhakika wa mazao yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, tunafahamu umuhimu wa Chuo na Kituo cha Utafiti cha Mlingano. Mimi mwenyewe katika ziara yangu ya Mkoa wa Tanga nilipata fursa ya kutembelea pale, kuangalia changamoto zilizopo na tayari Wizara iko kwenye mkakati wa kutatua changamoto mbalimbali ambazo tuligundua katika kituo hicho ili iweze kuwasaidia wakulima wa Mkoa wa Tanga na maeneo mengine ya Tanzania katika kuboresha kilimo.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mradi wa dharura ambao anaouongelea Mheshimiwa Waziri hatua za awali zilianza tangu 2015, mradi ambao unatoka Pongwe kuleta maji Muheza. Hata hivyo, nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni lini mradi huu utakamilika ili uweze kupunguza adha ya maji kwa wananchi wa Muheza Mjini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ameongelea Mto Mnyodo. Kuna madhara makubwa yametokana na mvua zinazoendelea kunyesha, vyanzo vingi vya maji vimeharibika, lakini Waziri amejibu hapa kwamba wanategemea upatikanaji wa fedha ndipo watarekebisha vyanzo hivi vya maji. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie, kwa sababu hili ni suala la dharura la uharibu wa vyanzo vya maji, ni lini hiyo fedha itapatikana ili kutengeneza vyanzo hivi ili wananchi waendelee kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Komba tukubaliane tu, si kwa nia mbaya lakini ni kweli kwamba Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Muheza amekuja ofisini mara tatu na nilimuagiza aje pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji ya Tanga, tukafanya utaratibu, sasa hivi tuko kwenye utaratibu wa manunuzi. Ni kweli kwamba mradi unaanza utekelezaji mwezi Juni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini utakamilika, baada ya kukamilika kwa taratibu za manunuzi na kumpata mkandarasi, ndani yake sasa baada ya kusaini mikataba ndipo tutajua ni lini sasa mradi utakamilika; lakini shughuli imeshafanyika na mradi unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 2.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la uharibifu, mvua imenyesha sana Tanga na taarifa ninayo, Kamati ya Ulinzi na Usalama na nimeshaipata ile nyaraka ya uharibifu uliotokea kwenye maeneo mengi. Kwa hiyo, sasa hivi taarifa hiyo, kwanza itapelekwa kwa Mheshimiwa Jenista kwenye ile Kamati ya Maafa, lakini wakati huo hu na sisi tutachukua hiyo nakala, baada ya kupata taarifa ya Mheshimiwa Jenista na sisi tutafanyia kazi ili tuhakikishe tumekarabati miradi hiyo kwa haraka ili wananchi wapate huduma ya maji. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi hilo tunalifanyika kazi. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake haya mazuri, majibu yenye kutia moyo, majibu ambayo yanaonyesha dhamira ya kweli ya Serikali katika kuondokana na dhana hii ya upungufu mkubwa wa chakula, hasa katika mikoa kame, mikoa ya katikati.
Mheshimiwa Spika, majibu yake haya yameonyesha kwamba wanakopesha vyama vya akiba na mikopo kama SACCOS. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anasemaje juu ya wananchi wa Jimbo langu ambao wengi wao hawajajiunga na SACCOS, wataweza kupatiwa mikopo hii ya matrekta?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali imeanza kuonesha nia na wanawekeza katika kuunganisha matrekta hapa nchini, ikiwemo pale TAMCO Kibaha.
Je, katika kuwahi msimu huu wa kilimo anaweza akatutengea matrekta hata matano tu ambayo tuko tayari kuyalipia kwa awamu ya kwanza katika Jimbo la Manyoni Magharibi, Halmashauri ya Itigi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba katika majibu yangu ya msingi nikianzia na lile swali lake la pili nimejibu kwamba wananchi wanaweza wakajiunga katika vikundi ili waweze kukopeshwa kupitia katika Mfuko wa SACCOS. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile nikija katika swali lake la kwanza, ameuliza kama wananchi wanaweza wakakopeshwa mmojammoja. Na mimi naomba nimwambie kabisa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi kwamba Wizara ya Kilimo imefanya utaratibu kupitia Mfuko wake wa Taifa wa Pembejeo na Kilimo, kwamba tunaruhusu mkulima yeyote mmojammoja kuweza kukopa jinsi anavyotaka.
Mheshimiwa Spika, kubwa la msingi aweze kwenda kwenye halmashauri zetu kule atakutana na maafisa wa kilimo na mkurugenzi, atajaza fomu atapeleka katika mfuko wetu wa pembejeo akiwa na proforma invoice yake na sisi kupitia mfuko huo tuko tayari hata kutoa mifuko kwa wakulima na mikopo kwa wakulima wadogo wadogo. Ahsante. (Makofi)
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Muheza kuna mradi wa maji kutoka kwenye Kata ya Pongwe kuja Muheza Mjini, mradi ambao umeanza tangu mwaka 2016, lakini wananchi wa Muheza wamekuwa na wasiwasi juu ya ukamilishwaji wa mradi ule.
Mheshimiwa Waziri anaweza kutuambia ni lini wananchi wa Muheza tutapata maji kutokana na mradi ule ili kupunguza adha ya maji katika Wilaya ya Muheza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa
Naibu Spika, mradi wa Muheza ni kweli tumesaini mkataba mwaka jana na kazi inaendelea vizuri na juzi tumelipa fedha, tunatoa bomba la maji kutoka tenki la Pongwe kupeleka katika Mji wa Muheza. Sasa hivi mkataba bado unaendelea siyo kwamba mkataba umekamilika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba ule mradi ukisha kamilika maji yatapatikana Muheza.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, tatizo la ongezeko la bandari bubu katika Mkoa wa Tanga ni kutokana na uwezo mdogo wa Bandari ya Mkoa wa Tanga. Je, Waziri anatuambia nini kuhusu kuboresha Bandari ya Tanga kwa maana ya kina na miundombinu ili ongezeko hili la bandari bubu liweze kupungua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna mradi ambao sasa hivi unaendelea, unatarajiwa kukamilika karibuni wa kuongeza kina katika lile eneo ambalo sasa hivi tunalitumia. Vilevile unafahamu kwamba tuna nia pia ya kuanzisha bandari kubwa zaidi ya Mwambani na kama sehemu ya mradi ule mkubwa wa kuhakikisha mizigo ya kutoka Uganda inapita katika reli ile ya kutoka Tanga – Musoma na Bandari ya Mwambani. Mipango hii ya Serikali ni thabiti na tumeanza kuitekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hilo la kuongeza kina ni karibuni tu mwezi ujao kazi hiyo itakuwa imekamilika.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi wa umwagiliaji katika Kata ya Misozwe, Jimbo la Muheza ambao umekamilika zaidi ya miaka kumi, lakini mradi ule mpaka sasa hivi haujaanza kwa sababu wananchi wa eneo lile ambalo lina mradi hawajalipwa fidia. Je, ni lini watalipwa fidia ili waweze kupisha mradi uanze?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kuwa na nia ya utekeleza wa miradi mikubwa kwa ajili ya manufaa kwa wananchi, lakini zipo athari kwenye utekelezaji wa miradi kupita maeneo ya watu. Nataka niwahakikishie wananchi hawa, sisi kama Wizara ya Maji na Umwagiliaji tutahakikisha kwamba wale wananchi wanaostahili kulipwa wanalipwa fidia. Ila tutamlipa mwananchi anayestahili kulipwa na yule asiyestahili hatalipwa. Ahsante sana.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza Waziri wakati anajibu, nafahamu Wilaya ya Muheza ni moja kati ya wilaya ambayo iliyofutiwa hati mashamba zaidi ya sita toka wawekezaji ambao mengi yao yalikuwa mashamba ya mikonge. Kutokana na hilo kumekuwa na tatizo kubwa sana la migogoro, sasa naomba niulize kuhusu kwanza watumishi, Serikali imejiandaaje hasa kwa mwaka huu inatuambia nini wananchi wa Muheza kwenye suala la watumishi, tutawaongezea watumishi wangapi ukizingatia tatizo la watumishi linatuathiri sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Rais alipokuwa anaenda kuzindua bomba la mafuta kule Tanga alipopita Muheza aliahidi na aliwaambia wananchi watagawiwa maeneo bure walime na kuyaendeleza, lakini wananchi wa Muheza hawakuamini hivyo, wamekuwa wanalipishwa gharama za upimaji na wamekubali. Hata hivyo, kuna migogoro mikubwa sanasana, wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza wanaohusika na ardhi wamekuwa wanauza maeneo ya wananchi kwa watu tofauti ambao siyo wakazi wa Muheza. Nataka nipate kauli ya Serikali, je, wapo tayari kutuma timu maalum iende Muheza ikasimamie masuala ya ugawaji wamashamba na viwanja hasa katika maeneo haya sita ambayo yamefutiwa hati?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri katika swali lake la msingi, lakini naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yosepher kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la watumishi nadhani hata kipindi kilichopita Bunge lililopita tulilizungumzia kwamba baada ya watumishi sasa kuelekezwa kwenye Wizara ya Ardhi, tayari tulikuwa tunafanya utaratibu wa kupata ikama yao na kujua wanataaluma tulionao ni kiasi gani ili waweze kusambazwa katika Halmashauri kulingana na uhitaji na kazi hiyo inafanywa na Ofisi ya Rais, TAMISEMIkwa sababu suala la uhamisho litasimamiwa na Wizara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika suala zima la ugawaji wa mashamba na wakati tumeenda kwenye ziara ya Kamati ya Ardhi suala hilo tulilikuta, lakini tayari Ofisi ya Halmashauri pale Muheza walikuwa wameshaanza kugawa hekari tatu tatu kwa wananchi katika yale mashamba yaliyorejeshwa na suala la kulipishwa katika suala la upimaji ni makubaliano ya Halmashauri yenyewe ambayo walikaa wakakubaliana na kiasi cha wao kuchangia na ndicho hicho kilichofanyika. Kwa hiyo suala linalofanyika linafanyika kutegemeana na mamlaka zenyewe za upangaji na matumizi bora ya ardhi. Kwahiyo hilo ni suala ambalo lipo chini ya halmashauri na Serikali inalisimamia kulingana na makubaliano ambayo yanakuwa yamefikiwa, hakuna migogoro ambayo itaendelea kwa sababu kila kitu kinasimamiwa.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Waziri ameeleza sababu ya kufungwa kwa eneo hili la madini, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, ni utaratibu gani ambao wameuandaa baada ya manyanyaso makubwa kwa wananchi, baada ya unyanyasaji mkubwa kunyang’anywa mali kuumizwa, ambao ulitokea kwenye eneo hili la madini. Wao kama Wizara wamechukua hatua gani kwa wananchi wa eneo lile, ambao walipata manyanyaso makubwa baada ya kugundua madini kwenye eneo hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri atuambie huyo mwekezaji mkubwa au mwekezaji mzawa, wao kama Wizara wameshamtafuta au wameshampata au wameshatangaza au ni lini atapatikana ili aanze uchimbaji ili wananchi wanaozunguka eneo lile waweze kunufaika nalo? Ahsante.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Yosepher kama ifuatavyo; kwanza hili la manyanyaso kama lipo na lilifanyika na watu walinyang’anywa mali zao ni muhimu tu tukatumia vyombo vyetu tulivyonavyo vya usalama kupitia Jeshi la Polisi malalamiko haya yaweze kuwasilishwa ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili je, tumetafuta muwekezaji naomba tu nimpe taarifa kwamba watanzania wengi sana ambao wameomba kuchimba kwenye maeneo hayo na nieleze tu kwamba Mheshimiwa Adadi tulienda pale SAkale tukafanya mkutano kwa wananchi na kwa watu ambao walionesha nia ya kuwekeza tumewapa taratibu za kufuata kwa sababu kwa kweli kuchimba pale ni kwenye mto ni lazima tuzingatie sheria ili tusije tukaharibu chanzo cha maji, kwa hiyo wako wengi tumewapa taratibu za kufuata ili waweze kuchimba kwa mujibu wa sheria.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ni dhahiri Mheshimiwa Waziri anafahamu wakazi hawa wananchi hawa wa maeneo ya Kata ya Genge, Kata ya Tanganyika, Kata ya Tingeni na Kata ya Bwembwera wamekuwepo katika maeneo haya zaidi ya miaka 50.

Naomba nifahamu kwa kuwa Serikali ilikuwa inaendelea kupeleka huduma na Serikali imesajili mpaka baadhi ya vijiji ambavyo vina maeneo yaliyopitiwa na reli ambayo sasa hivi imeekewa ‘X’. Je, Serikali iko tayari kuwalipa fidia wananchi wale kwa kuwa wao ndio walibariki wananchi kuendelea kuishi pale zaidi ya miaka 50? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Wilaya ya Muheza kunaendelea urasimishaji wa makazi na katika maeneo na nyumba za watu ambao wana ‘X’ wamewekewa ‘X’ wanaambiwa na wao walipe kwa ajili ya urasimishaji. Nilitaka kufahamu Mheshimiwa Waziri yuko tayari kusitisha zoezi hili ili mpaka wananchi wale wenye nyumba za ‘X’ wapatiwe ufumbuzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kwamba wananchi wanastahili kupewa ile huduma muhimu ambazo Serikali inapaswa kuwapa wananchi inastahili wazipate kwamba hakuna sababu ya kuwaadhibu wananchi kutokana na makosa labda ambayo yalitokana na watendaji. Kwa hiyo kupata huduma wananchi ni haki yao, lakini niseme tu kwamba kuhusu fidia, zoezi la kulipa fidia linafanyika kwa mujibu wa sheria, tutaangalia Sheria ya Ardhi, Sheria ya Ardhi ya Vijiji ndio inatumika kulipa fidia kwa wananchi, kwa maana hiyo Mheshimiwa Mbunge ukubaliane na mimi kwamba fidia inalipwa kutokana na sheria na taratibu ambazo zipo, kwa wale wanastahili kulipwa fidia Serikali inaendelea kufanya hivyo kwa sababu ni haki yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu urasimishaji wa maeneo ambao zoezi linaendelea niseme tu kwamba sio vyema kurasimisha maeneo ambayo sio halali na mimi nafahamu wataalam waliopo kwenye maeneo haya watarasimisha maeneo tu ambayo ni halali kurasimisha na niseme tu kwamba Serikali itawachukulia hatua watumishi ambao watarasimisha maeneo ambayo hayastahili kurasmishwa kwa sababu ni kuvunja sheria, kwa maana hiyo wale watu waliowekewa ‘X’ kwa maana ya kupisha niwasihi tu wapishe maeneo haya kwa sababu ni maeneo ya reli na sio vyema kuendelea kuendeleza maeneo haya, kwa sababu tutaendelea kupata hasara bila sababu.

Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Mbunge tusaidiane tu kwamba wananchi wa maeneo haya ya Muheza uwashauri kwa maeneo ambayo unaona kabisa kiuhalali yako maeneo ya reli wapishe maeneo haya na kama kuna tatizo lilijitokeza kutokana na utendaji basi Serikali itachukua hatua kutokana na namna ya hali ilivyokuwa. Ahsante.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa. Nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, nilipenda kutoa nyongeza tu kwenye swali la pili la Mheshimiwa Yosepher.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba lengo na dhamira ya Serikali ni kuwawezesha Wananchi. Sasa unapokuta kwamba yuko kwenye eneo ambalo halitakiwi lifanyiwe urasimishaji maana yake ameingia kwenye eneo ambalo haliko kwenye mpango. Sasa na unaposema kwamba kuzuia watu wengine mpaka ufumbuzi upatikane, wale watu tayari wako ndani ya maeneo ambayo hayaruhusiwi kujengwa kwa sababu ni kwa kazi nyingine ambayo imewekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niombe tu Halmashauri zetu wawe makini katika kuangalia namna ambavyo vipimo vya barabara na reli ambavyo vimekaa kiasi kwamba watu wasiingie kwenye yale maeneo. Na sasa hivi Wizara imeanza kuweka mpango wa upimaji katika maeneo yanayopitiwa na reli. Kwa hiyo, ni vizuri wakazingatia yale masharti ambayo tunayatoa ili baadae wasije wakajikuta wameingia kwenye eneo ambalo haliruhusiwi. Ahsante.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama ambavyo aliyejibu swali amekiri kwamba Shule hii ina changamoto nyingi. Shule hii imeanza mwaka 1995 lakini iko ndani la eneo la shamba ambalo lilikuwa la Mkonge la Mjesani Estate, na mpaka sasa tunavyoongea shule hii haina hatimiliki ya lile eneo, kwa hiyo walimu na watendaji pale wamekuwa wanaishi kwenye shule ile kama vile wamepanga. Kwa hiyo nilitaka nifahamu, Wizara ina mkakati gani wa kuhakikisha shule hii inapata hatimiki ya eneo ili iweze kufahamu mipaka ya eneo lake kama Shule?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kama ambavyo amesema Mheshimiwa Waziri. kuhusu suala la maj. Pale kuna Mto Zigi ambao ndio wanaoutumia wanafunzi kuchota maji kwa ajili ya matumizi pale shuleni, na kumeshatokea ajali zaidi ya mbili ya wanafunzi pale kutaka kuuawa na mamba, ule mto una mamba. Je, Serikali kama mdau mkuu kwenye hili suala la elimu wako tayari kushirikiana na halmashauri na wadau wengine kuhakikisha milioni 7.6 inapatikana kwa wakati ili kupeleka maji kwenye shule ile?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yosepher Komba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunahitaji maeneo yote ya Umma yapimwe na yapate hatimiliki ili kuwa na uhalali wa eneo hilo lakini pia kupunguza migogoro ambayo inatokana na wananchi kuvamia maeneo hayo ya umma ikiwemo Mashule kama alivyotaja. Naomba nimuelekeze Mkurugenzi wa Halmashauri hii ya Mkinga atume wataalam wapimaji wakapime eneo hilo ili waweze kupata hati na kuondoa migogoro ambayo inaweza kuwepo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anazungumzia habari ya maji. Tumesema kwamba tathmini imeshafanyika, zinatakiwa shilingi milioni 7.6, na Serikali ipo tayari kushirikiana na halmashauri, na pia Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na sisi. Sote kwa pamoja tuhakikishe kwamba tumepata maji katika eneo hili na watoto wetu waweze kupata huduma nzuri na masomo yaendelee.