Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Upendo Furaha Peneza (11 total)

MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Wananchi wa Mtaa wa Katoma, Kata ya Kalawala Wilaya ya Geita wameathirika sana na shughuli za Mgodi wa geita Gold Mine (GGM) ambapo nyumba zimepata nyufa na kuanguka kutokana na mitetemo, milipuko ya mara kwa mara inayoletwa na kelele na vumbi linaloathiri afya za wananchi wa mtaa huo pamoja na vyanzo vya maji.
Je, ni lini wananchi hao wa Katoma watapewa fidia za mali zao ili waondoke katika eneo hilo jirani kupisha shughuli za Mgodi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kupata ufumbuzi wa malalamiko ya wananchi wa Mtaa wa Katoma, Wizara imeunda Timu ya Wataalam kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama athari zinazodaiwa na wananchi wa Katoma za kusababisha nyufa kwenye nyumba zao zinatokana na shughuli za ulipuaji wa baruti zinazofanywa na Mgodi wa GGM (Geita Gold Mine).
Mheshimiwa Spika, Timu hiyo itakamilisha kazi yake tarehe 25 Februari, mwaka huu na iwapo itabainika kuwa athari zinazolalamikiwa na wananchi wa Katoma zinatokana na shughuli za ulipuaji wa baruti kwenye mgodi huo, basi Serikali itahakikisha kuwa Mgodi wa GGM unalipa fidia stahiki kwa wananchi hao ili wahame na kupisha shughuli za uchimbaji madini kwenye eneo hilo.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha nia ya kutaka kuongeza mapato kwa ufuatiliaji na kuondokana na ukwepaji kodi bandarini, lakini kwa miaka mingi Serikali imekuwa ikikosa mapato kwa kutoa misamaha ya kodi kwa kampuni za uwekezaji katika sekta ya madini:-
Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuondokana na misamaha ya kodi inayotolewa kwa kampuni ya uwekezaji?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa vivutio vya aina mbalimbali kwa wawekezaji ili kuvutia uwekezaji nchini. Misamaha ya kodi ni moja ya vivutio vinavyotolewa kama moja ya njia ya kuwahamasisha wawekezaji ili wachague nchi yetu badala ya kwenda nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, misamaha hii hutolewa kwa mujibu wa sheria na mara nyingi kwa kipindi cha awali cha uwekezaji. Misamaha hii kama alivyoeleza Mheshimiwa ni pamoja na inayotolewa kwa makampuni ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta, gesi na madini na misamaha inayotolewa kupitia maamuzi ya Kamati ya Uwekezaji ya Taifa (NISC) na kwa kutumia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua upungufu uliopo katika kutumia kodi kama kivutio cha uwekezaji. Tatizo kubwa ni wale wanaotumia fursa hii kuhujumu mapato ya Serikali au pale misamaha inaposababisha kutokuwepo ushindani sawa kati ya kampuni moja na nyingine katika sekta ile ile. Hata hivyo, kama nilivyoeleza awali, uwekezaji utakaolazimu kushindania wawekezaji na nchi nyingine duniani au kuhamasisha uzalishaji nchini wenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi walio wengi na kivutio cha kodi kikawa ndicho kigezo muhimu cha kufanya uamuzi tunalazimika kutoa misamaha ya kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kufanya mabadiliko katika sheria ili kupunguza misamaha ya kodi inayotolewa kwa ridhaa, yaani misamaha inayotolewa kwa kampuni moja moja kwa mikataba na kwa kupitia kwa mamlaka ya Waziri wa Fedha na Mipango. Ili kuboresha kivutio cha misamaha kwa wawekezaji, kodi imekuwa ikipunguzwa katika bidhaa na shughuli za jumla zinazo-cut across.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada za kuondoa upungufu unaoendana na misamaha ya kodi, napenda nikiri kuwa pamoja na vivutio vingine muhimu kwa kuvutia wawekezaji, misamaha ya kodi itatumika pale inapobidi. Aidha, tofauti na zamani tutaperemba misamaha hiyo mara kwa mara ili kuipima tija yake.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupunguza misamaha ya kodi kufikia asilimia moja (1%) ya GDP?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, azma ya Serikali ya kupunguza misahama ya kodi kufikia asilimia moja ya pato la Taifa ni mkakati unaotekelezwa kwa awamu na kwa kuzingatia mazingira ya kiuchumi, kijamii na sheria zilizopo. Juhudi za kutekeleza azma ya kupunguza misamaha ya kodi zilianza kufanyika mwaka 2010/2011 baada ya kubaini kuwa, kwa wastani misamaha yetu ilikuwa imefikia takribani asilimia 3.2 ya pato la Taifa kwa mwaka, katika kipindi cha mwaka 2006/2007 hadi 2009/2010.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2009/2010 Serikali iliamua kupitia upya sheria zinazohusu misamaha ya kodi ili kuondoa misamaha ambayo haikuwa na tija katika Taifa letu. Katika mapitio hayo Serikali ilibaini kuwa takribani asilimia 60 hadi asilimia 64 ya misamaha yote ya kodi ilikuwa inatokana na kodi ya ongezeko la thamani – VAT. Baada ya kubaini hali hiyo, Serikali kupitia Bunge lako Tukufu ilifanya maboresho ya Sheria ya VAT, Sura ya 148 na kuondoa misamaha ambayo haikuwa na tija kwa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa, hususan za kurekebisha upeo wa misamaha inayotolewa chini ya Kituo cha Uwekezaji – TIC na Sekta ya Madini, zimesaidia kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia asilimia 1.9 ya pato la Taifa kwa mwaka wa fedha 2014/2015. Katika kipindi cha Julai, 2015 hadi Machi, 2016 kiasi cha kodi kilichosamehewa ni shilingi milioni 564,106.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwenendo huu ni matarajio yetu kuwa kiasi cha msamaha wa kodi katika Mwaka wa Fedha 2015/2016 kitakuwa ni shilingi milioni 752,141.9 sawa na asilimia 0.84 ya pato la Taifa. Kutungwa upya kwa Sheria ya VAT ni eneo moja ambalo limeleta ufanisi mkubwa katika kutimiza azma yetu ya kupunguza misamaha ya kodi, hadi kufikia asilimia moja ya pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, baadhi ya misamaha ya kodi haiepukiki katika mifumo ya kodi hapa nchini na popote duniani. Suala la msingi ni kuwa Serikali itahakikisha kuwa misamaha yote ya kodi inatolewa kwa mujibu wa Sheria za Kodi zilizopo.
Katika siku za usoni usimamizi wa misamaha utajengwa katika mifumo imara ya udhibiti inayozingatia matumizi ya teknolojia. Lengo la muda mrefu ni kuweka mfumo wa misamaha ya kodi unaokubalika Kimataifa, pia misamaha hiyo iwe ni ile inayochochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.
MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y MHE. UPENDO F. PENEZA) aliuliza:-
Kufuatia vifo vyenye utata vya kisiasa na vinavyohusisha vyombo vya dola, aliyekuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda alitoa ahadi katika Bunge la Kumi ya Serikali kuunda Mahakama ya Coroner (Coroner‟s Court) kwa ajili ya kuchunguza vifo mbalimbali vyenye utata:-
Je, Serikali iko katika hatua gani kutekeleza ahadi hiyo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na msingi wa swali hili kuwa na utata, napenda ieleweke wazi kuwa uchunguzi wa vifo vinavyotokea katika mazingira yenye utata ambayo sababu zake hazijulikani, hufanywa kwa uchunguzi maalum (inquest) na mchunguzi maalum anaitwa coroner kwenye Mahakama Maalum ya Uchunguzi (Coroner‟s Court). Utaratibu huu tumekuwa tukiutumia hata kabla uhuru chini ya Sheria ya Uchunguzi Maalum (Inquests Ordinance) Sura ya 24. Sheria hii ilifutwa na kutungwa upya kuwa Inquests Act No. 17 ya 1980 ili kuendana na mazingira mapya ya haki jinai nchini baada ya uhuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii mpya iliridhiwa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere tarehe 21 Mei, 1980, chini ya kifungu cha 5(1) Waziri wa masuala ya Sheria wa wakati huo alitangaza sifa za uteuzi za kuwa Coroner na chini ya kifungu cha 5(2) na (3), Jaji Kiongozi kwa kushauriana na Jaji Mkuu, aliwateua Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi kuwa Coroners au Makorona.
Aidha, kwa tangazo la Serikali Na. 252 la tarehe 16 Julai, 2004, Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi ziliteuliwa kuwa Mahakama za Coroner pale zinapoketi kwa uchunguzi wa vifo vyenye utata.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kusambaza maji katika Kata za Kasamwa, Shiloleli, Bulela, Nyarugusu, Bukeli na maeneo mengine ya Wilaya ya Geita na Mkoa wa Geita kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Geita kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 imepanga kutumia shilingi milioni 593.14 kwa ajili ya kuboresha huduma za maji katika Kata za Kasamwa, Shiloleli, Bulela, Nyarugusu na Bukolina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa miundombinu ya maji kwa kutumia chemchemi ya Mawemeru katika Kata ya Nyarugusu; uchimbaji wa visima virefu katika Kata ya Bulela na Shiloleli na kuboresha miundombinu ya maji iliyopo katika kata ya Kasamwa na Kanyara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa mzima wa Geita Serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 8.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji ambazo zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Fedha hizo zitatumika kujenga miradi ya maji 22 ili kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Tatizo la makazi duni kwa wananchi husababisha afya mbovu na hivyo kupunguza nguvu ya uzalishaji.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata makazi bora?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Hali Halisi ya Miji Tanzania iliyoandaliwa na Mtandao wa Miji nchini (Tanzania Cities’ Network - TACINE) ya mwaka 2014, wastani wa kiwango cha ujenzi holela katika miji saba ya Tanzania Bara na Manispaa ya Zanzibar ilibainika kuwa ni asilimia 67 ya maneno yaliyojengeka. Mengi ya maeneo haya hayana miundombinu na huduma za msingi kama vile maji safi na salama, barabara na mifereji ya maji ya mvua na udhibiti wa maji taka na taka ngumu. Hali hiyo husababisha mafuriko, milipuko ya magonjwa, mazalio ya mbu na inzi, na mandhari mbaya ya kuishi yanayopelekea afya duni na kupunguza nguvukazi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali imeandaa programu na mikakati mbalimbali kukabiliana na hali hiyo kama ifuatavyo:-
(i) Programu ya Kitaifa ya Kurasimisha Makazi Holela Nchini ambayo inalenga mwaka 2013 mpaka 2023 inayolenga kurasimisha makazi mijini na kutoa fursa kwa maeneo kupangwa, kupimwa na kumilikishwa na kisha kutoa huduma za msingi na miundombinu.
(ii) Programu ya Kitaifa ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Kila Kipande cha Ardhi ya mwaka 2015 mpaka 2025 inayolenga, pamoja na mambo mengine, kuzuia kudhibiti ujenzi holela ambao husababisha kuwepo kwa makazi duni; na
(iii) Kuandaa mipango Kabambe katika Miji (Master Plans) kwa miji 30 kwa kushirikisha Halmashauri za miji na Wilaya itakayosaidia kusimamia na kudhibiti uendelezaji miji. Hadi sasa Mipango Kabambe ya Arusha, Mwanza, Singida, Tabora, Mtwara, Kibaha, Musoma, Korogwe na Songea imeandaliwa na makampuni binafsi na ipo katika hatua za mwisho za maandalizi.
Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa mamlaka na Serikali za mitaa kutenga fedha za kutosha katika bajeti zao kila mwaka kwa ajili ya kuongeza kasi ya kupima, kupanga na kumilikisha ardhi katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi kupata makazi bora.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Je, Serikali inatumiaje fedha za Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi (Adaptation Fund) zinazotolewa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI (K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia nchi (Adaptation Fund AF) chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi zilizotolewa mwaka 2013 zinatumika kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo ya Jiji la Dar-es-Salaam. Gharama za mradi huu ni Dola za Marekani milioni tano na zinatekeleza kama ifuatavyo:-
(i) Kujenga ukuta wa bahari katika maeneo ya Barabara ya Obama (zamani Ocean Road wenye urefu wa mita 820) na Kigamboni (Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere wenye urefu wa mita 380)
(ii) Kujenga miundombinu ya mitaro ya maji ya mvua katika Mtaa wa Bungoni, Kata ya Buguruni, wenye urefu wa mita 1,003 na Mtaa wa Miburani, Kata ya Mtoni wenye urefu wa mita 800.
(iii) Kurudisha matumbawe katika ukanda wa Bahari ya Hindi, eneo la Sinda, Dar-es-Salaam lenye ukubwa wa mita za mraba 2000.
(iv) Kuendesha mafunzo kuhusu matumizi endelevu ya nishati na kusambaza majiko banifu kwa familia 3000 za Manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni.
(v) Kupanda mikoko katika eneo la takribani hekari 40 katika maeneo ya fukwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) hutolewa kupitia njia mbili, yaani Mawakala wa Kimataifa (Multination Implementing Entities – MIEs) na Taasisi za Kitaifa (National Entities – NIEs) ambazo zimesajiliwa (accredited) na mfuko huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unaotekelezwa katika Mkoa wa Dar-es-Salaam fedha zake zote zimetolewa kupitia katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Hifadhi ya Mazingira (UNEP) ambaye ni Wakala wa Kimataifa. Ili kuweza kupata fedha nyingine Serikali inakamilisha sasa mchakato ambapo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inatarajia kusajiliwa (accredited) baada ya kukamilisha masharti yanayohitajika kuwa Taasisi ya Kitaifa ya kuratibu fedha zinazotolewa na Mfuko huu.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y MHE. UPENDO F. PENEZA) aliuliza:-
Je, Serikali imeweka mikakati gani kuimarisha huduma za umeme, maji, afya na elimu katika maeneo ya vijijini ili kuongeza uzalishaji katika maeneo hayo na kuzuia wimbi la watu kukimbilia mijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza uzalishaji katika maeneo ya vijijini kwa kuimarisha huduma za umeme, maji, afya na elimu kwa lengo la kuzuia wimbi la watu kukimbilia mijini Serikali inatekeleza mikakati ifuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kuendelea kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari kwa kujenga na kukarabati madarasa, vyoo, maabara, mabweni, nyumba za walimu, mabwalo, maktaba kwa kuzingatia mahitaji ya shule husika. Pia kujenga shule mpya katika maeneo ambayo shule za msingi na sekondari ziko mbali. aidha, mkakati wa madawati kwa kila shule, mkakati wa kujenga maabara kwa shule za sekondari na ajira mpya kwa walimu wapya wa michepuo ya sayansi ni miongoni mwa mikakati mahususi ya kuboresha sekta ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, kuendelea kuboresha miundombinu kwenye sekta ya afya ambapo kwa mwaka huu wa fedha pekee Serikali inajenga na kukarabati vituo vya afya 183 kwa gharama ya shilingi bilioni 81 vitakavyokamilika ifikapo tarehe 30/4/2018; ambapo shilingi bilioni 35.7 zimetolewa kwa ajili ya vifaa tiba. Ili kuongeza upatikanaji wa dawa Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi shilingi bilioni 260 mwaka huu wa fedha 2017/2018 ambazo zimesaidia sana kuongeza upatikanaji wa dawa mijini na vijijini. Pia kipaumbele maalum kimewekwa kuhusu kuongeza watumishi wa afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya nishati vijiji 7,873 kati ya vijiji 12,545 vya Tanzania Bara vitapatiwa umeme kuanzia mwaka huu wa fedha 2017/2018 hadi 2021. Umeme utasambazwa hadi kwenye maeneo yote ya shule, zahanati, vituo vya zfya, hospitali, mitambo ya maji, viwanda vidogo vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa.
Aidha, huduma za maji zitaboreshwa zaidi kupitia utekelezaji wa awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Serikali pia itaendelea kuimarisha barabara vijijini ili kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji hasa wa mazao kwenda kwenye soko.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawapatia wachimbaji wadogo wadogo maeneo yaliyopimwa na kuwa na uwepo wa madini kama dhahabu, ikiwemo Moroko katika Mkoa wa Geita na maeneo mengine yenye madini nchini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 1996, Serikali kupitia Wizara ya Madini imekuwa ikitenga maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini. Tangu kipindi hicho hadi sasa, Wizara ya Madini imetenga jumla ya maeneo 46 katika sehemu mbalimbali nchini yenye ukubwa wa hekta 281,533.69. Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kadiri yatakavyokuwa yanapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Geita Wizara imetenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini na kutoa leseni kama ifuatavyo: Eneo la Nyarugusu leseni 41; eneo la Rwamgasa leseni 36; eneo la Isamilo/ Lwenge leseni 22 na eneo la Mgusu leseni 22. Kwa sasa eneo la Moroko alilolitaja Mheshimiwa Mbunge lipo ndani ya leseni ya utafiti yenye Na.8278 ya mwaka 2012 inayomilikiwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita. Maeneo mengine ya mkoa huo yataendelea kutengwa kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 16 cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na Marekebisho yake ya mwaka 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara kwa kutumia taasisi zake za GST pamoja na STAMICO itaendelea kufanya utafiti ili kubaini uwezo wa mashapo ya madini katika maeneo mbalimbali nchini na kuyatenga kwa ajili ya uchimbaji mdogo wa madini. Hii itawezesha wachimbaji wadogo wa madini kufanya kazi na kuchimba kwa uchimbaji wa tija. Ahsante.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI (K.n.y. MHE. UPENDO F. PENEZA) aliuliza:-

Je, katika mwaka 2016/2017 na 2017/2018 Serikali ilikusanya kiasi gani cha kodi ya 18% (VAT) kwa taulo za kike (sanitary pads) zote zilizotengenezwa nchini na zile zilizoingizwa nchini kabla ya kodi hiyo kuondolewa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/ 2017, Serikali ilikusanya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya kiasi cha shilingi bilioni 3.01 na shilingi bilioni 2.54 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kwenye bidhaa ya taulo za kike zilizoingizwa nchini pamoja na zile zilizozalishwa hapa nchini kabla ya kodi hii kuondolewa Juni, 2018.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-

Wananchi wa Mtaa wa Mgusu wanaoishi ndani ya mipaka ya Mgodi wa Geita Gold Mine wanaathirika sana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka zinazomwagwa katika maeneo karibu na wananchi.

Je, ni lini Serikali itatoa agizo kwa Geita Gold Mine kulipa wananchi fidia ili watoke katika eneo lililomilikishwa Mgodi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini naomba nijibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nijibu kama swali lilivyoulizwa na kama ni marekebisho hayo anayoyasema Mheshimiwa Mbunge basi tunaomba arudishe swali alete jingine jipya tutamjibu kwa lile eneo lakini hapa tumemjibu kadri lilivyoulizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mtaa wa Mgusu uko kilomita 4.5 kutoka eneo la uchimbaji la Nyamulilima Star and Comment la GGM ambapo kwa sasa uchimbaji unaendeshwa kwa niia ya chini kwa chini yaani Underground Mining Operations. Mawe ya Dhahabu yanayozalishwa katika eneo hilo hupelekwa kwenye eneo maalum la uchenjuaji yaani Processing plant ambalo lipo umbali wa kilomita 19 kutoka Mtaa wa Mgusu. Kwa umbali huo ni wazi kuwa ni vigumu kwa taka ngumu kufika katika Mtaa huo. Hata hivyo ukingo wa miamba isiyo na madini yaani Waste Rocks umewekwa ili kuzuia miamba hiyo kutoka nje ya eneo la uchimbaji.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, Kifungu cha 96(1) na 97(1)(a) na (b) vinaeleza kuwa, fidia inapaswa kulipwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi katika hatua ambapo muwekezaji anataka kuanza kuchimba madini baada ya kushauriana na Mamlaka ya Serikali za Mtaa husika na kujiridhisha juu ya madhara yanayoweza kusababishwa na uchimbaji huo.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mtaa wa Mgusu wengi wao wanajishughulisha na uchimbaji mdogo wa madini. Hata hivyo tathimini ya mazingira iliyofanywa na mgodi wa GGM haionyeshi uwepo wa madhara yanayohitaji kuhamishwa kwa wananchi wa Kitongoji hicho. Aidha, Wizara kupitia Ofisi ya Madini Mkoa wa Geita itaendelea kusimamia na kukagua eneo hilo.