Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Upendo Furaha Peneza (16 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mungu kwa kunipatia fursa hii ya kuweza kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya nchi yetu tuna changamoto kubwa ya mimba za utotoni zinazopelekea watoto wa kike kuacha shule. Suala hili ni vyema Serikali ikachukua hatua kwa kuhakikisha elimu ya afya ya uzazi inatolewa mashuleni ili watoto waweze kutambua mabadiliko ya miili yao na kuwawezesha watoto kufanya maamuzi sahihi. Serikali ihakikishe kuwa clubs za wasichana zinaundwa mashuleni na kila shule iwe na matron au mwalimu wa kike atakayewajibika kusimamia clubs hizo na utoaji wa elimu ya afya ya uzazi (sexual reproductive health).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la utoro mashuleni ambapo watoto wa kike wengi wanakuwa watoro kutokana na suala la menstruation period ambapo mtoto wa kike anaingia kwenye siku zake kwa siku tatu hadi nne ambapo kwa mwaka hufanya siku 48. Kama mtoto hatapata sanitary pads, atashindwa kwenda darasani na hivyo kuathiri ufaulu wake darasani au kupelekea watoto wa kike kuacha shule kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itoe ruzuku ya sanitary pads kwa watoto wa shule ambapo watoto watapata sanitary pads (taulo za kujihifadhi) kwa bei rafiki ya shilingi 500 kwa pakiti badala ya shilingi 3000 hadi 4000 ya bei ya sanitary pads kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iongeze pesa za mkopo wa wasichana vyuoni ambapo waongezewe shilingi 40,000 kwa semister au shilingi 80,000. Ongezeko hili litasaidia wasichana kumudu mahitaji yao ya pads. Pendekezo la shilingi 40,000 na shilingi 80,000 linatokana na bei ya sanitary pads kwa sasa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii kuweza kuchangia Wizara hii muhimu ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, naomba tu uniruhusu nisome kidogo baadhi ya vipaumbele katika sekta ya mifugo ambapo kuna kuimarisha usimamizi wa ardhi kwa kutenga maeneo ya malisho, kuimarisha upatikanaji wa maji na malisho ya mifugo, kuimarisha tiba na udhibiti wa magonjwa ya mifugo na kufanya sensa ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2015/2016 baada ya kuteuliwa kuwa Mbunge, nilipangwa katika Kamati ambayo ilikuwa ni kubwa kidogo kwa maana Kamati ya Kilimo, Mifugo pamoja na Uvuvi zikiwa pamoja. Vipaumbele ambavyo vinasemwa leo ni vipaumbele ambavyo vimekuwepo tangu mwaka wa kwanza kabisa mimi nimekuwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndani ya Bunge kipindi Wizara hii ipo pamoja bado haijatenganisha kulikuwa kumetokea ushindani wa aina fulani baina ya Wabunge kwa maana Wabunge wa Kilimo na Wabunge waliotoka katika maeneo ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ametusaidia, amezitenganisha Wizara hizi. Hata baada ya kututenganisha tatizo limebaki kama lilivyokuwa tangu mwanzo nilipoingia katika Bunge hili. Mwaka wa kwanza kabisa 2016/2017 Serikali haikutenga pesa yoyote kwenda katika upande wa mifugo. Mwaka 2017/2018 Serikali imetenga shilingi bilioni sita kwa maana ya shilingi bilioni nne upande mifugo na shilingi bilioni mbili upande wa uvuvi. Pesa ambazo hazijapelekwa mpaka leo hii tunajadili bajeti nyingine. Leo Serikali inatenga tena bajeti ya shilingi bilioni 12 kwa maana ya bajeti hii na nina wasiwasi kwamba pesa hizi vilevile zinaweza sizipelekwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kipaumbele cha kwanza kwamba kuimarisha usimamizi wa ardhi kwa kutenga maeneo ya malisho, tunashawishika Wabunge kuwaambia wananchi kwamba Serikali ni sehemu mojawapo ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Serikali ni washirika moja kwa moja kuhakikisha kwamba wakulima na wafugaji hawawezi kupatana na mapigano yaendelee. Kwa sababu kama tunatenga pesa na Bunge linapitisha ili kazi iweze kufanywa na Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, kutenga maeneo ya malisho kwa ajili ya wafugaji na hilo halifanyiki, maana yake ni kwamba wanaoshiriki kuwaua wakulima, wanaoshiriki kuwaua wafugaji na Serikali imo miongoni mwao lakini wao ni background players katika mauaji hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ifike wakati sasa kwa sababu Serikali yenyewe inashiriki kwa nyuma katika mauaji haya, basi ione umuhimu wa kuona kwamba ni lazima pesa hizi ziwe zinatengwa ili kazi ambayo imepangwa kufanywa iweze kufanywa. Tunaongea kifua mbele kwamba Wizara imekusanya maduhuli shilingi bilioni 21 kutoka kwenye mifugo, lakini tukiangalia kwamba wamewasaida nini hao wafugaji mpaka kwa hizo tozo wanazozitoa, hakuna lolote ambalo linafanyika kuweza kuwasaidia wafugaji.

Mheshimiwa Spika, kwa tozo ambazo zipo kwa maana ya leseni za biashara, tozo za kusafirisha ng’ombe, tozo za kulipia kila ng’ombe wanapokuwa wakihama katika eneo moja kwenda lingine ni vizuri sasa hizo kodi zikapunguzwa, kwa sababu kama mtu humsaidii katika kuhakikisha ya kwamba anakuwa na mazingira bora ya kuweza kuwatunza wale ng’ombe wake, ni muhimu sasa Serikali walau ikapunguza maumivu kwa hawa wafugaji ili kuhakikisha kwamba wanaweza walau wakaendelea bila ya tozo hizi za manyanyaso.

Mheshimiwa Spika, katika kilimo Serikali ilipunguza tozo na sasa Serikali iangalie pia namna ya kuweza kupunguza tozo ambazo zinawakabili wafugaji ili na wao kwa kile walichonacho basi washiriki katika kusaidia mifugo yao na wao wenyewe badala ya kuendelea kuilipa Serikali.

Mheshimiwa Spika, nitaongelea pia kidogo suala ambalo ameliongelea Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Kamala. Suala hili pia ni tangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba akiwa Waziri wa Wizara hii yote kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, ndani ya Kamati Serikali ilitoa ahadi ya kwamba inafanya mchakato wa kuhakikisha kwamba ranchi zote ambazo ziligaiwa kwa watu zamani, ambazo hazifanyi kazi ziweze kurejeshwa na watu wengine wapatiwe ili maeneo ya kufugia ng’ombe ziweze kupatikana. Suala hili sasa ni miaka mitatu halijatimia Wizara ni hii tumeendelea kuongea mpaka mwisho hakuna linalofanyika, kwa sababu tu Serikali inashindwa kutoa hela. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ifike mahali sasa hawa wananchi ambao Rais anawaita anawapenda ni maskini, hebu tuwepende kwa vitendo kwa hela kupatikana ili kuboresha mazingira ya wananchi waweze kuwa vizuri. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii nami kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 3(1) inasema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayofuata mfumo wa vyama vingi. Maana yake ni kwamba vyama vyote ambavyo viko Tanzania vyote vinasajiliwa kulingana na Katiba na sheria ambazo ziko ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo tungetegemea kwamba sheria ambazo zinaruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara iweze kuheshimiwa ili wananchi wakapate fursa ya kusikiliza vyama hivi vya siasa lakini pia vile vile kutimiza wajibu ambao upo kutokana na Sheria ya Vyama vya Siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha kusikitisha ni kwamba Jeshi letu la Polisi na mtakubaliana na mimi kwamba Vyama vya Upinzani havina uadui wowote na Jeshi la Polisi na ndiyo maana pamoja na kwamba katika bajeti hii upinzani hatujawa na hotuba mbadala kwa sababu ya changamoto zilizopo, lakini kwa miaka mingi ambayo imekuwa ikipita upande wa upinzani umekuwa ukitoa maoni namna gani ya kuboresha maisha ya askari wetu. Tumekuwa tukifanya hivyo kwa sababu tunatambua kazi kubwa waliyonayo ndani ya jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo maoni kutoheshimiwa, leo Jeshi la Polisi limekuwa ni sehemu ya kukandamiza demokrasia ndani ya nchi hii. Jeshi la Polisi limekuwa pale mtu anaposimama na kuikemea Serikali, mtu anaposimama na kuonesha kwamba hapa Serikali imekosea, mtu huyo anabadilika na kuwa adui, ataitwa mchochezi, ataitwa majina ya kila namna ili mradi tu kuhakikisha kwamba uongozi au Awamu hii haisemwi, haikoselewi badala yake ni kusifiwa tu kwa mema tu wanayoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna hiyo hatutaweza kwenda na kama Jeshi la Polisi sasa hivi kwa kazi ambayo inaifanya, mfano, kama dada mmoja ametangaza maandamano ya tarehe 26, viongozi wangu wa Geita, Katibu wangu, wamekamatwa kana kwamba ni sehemu ya Mange Kimambi. Uwoga ambao unatengenezwa ni kana kwamba wananchi wa Kitanzania hawaruhusiwi kusema na kuikosoa Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa tutakubali kwenda kwa kile tu ambacho kinasemwa na Rais, kwenda kwa kile tu ambacho Serikali inasema, basi hatutafika na tunaendelea kurudi nyuma. Jeshi letu la Polisi leo kwa kazi yote ambayo wameifanya na nitasema tu kwamba kipindi cha nyuma tukiwa na IGP Said Mwema alianzisha mpango wa kutengeneza jamii iwe na urafiki na polisi wetu. Mpango ambao sasa hivi unaendelea kurudi nyuma hatua nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakandamiza demokrasia Polisi wale wa ngazi za chini wanajengeka ubabe wa hatari. Raia wamekufa mikononi mwa polisi, kijana wa Mbeya ameuawa mikononi mwa polisi, ndugu yake Heche ambaye amezikwa jana ameuawa mikononi mwa polisi kwa kuchomwa kisu. Hatuwezi kuwa na Taifa ambalo watu ambao tunategemea watulinde na mali zetu ndiyo wanaotuangamiza na kutufanya tufe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanaanza kwa sababu ya ubabe ambao umeanza wa kushughulikia viongozi, watu ambao wanatoa mawazo mbadala, sasa yanaenda mpaka kwa raia ambao kwa namna moja ama nyingine inawezekana wana ukosefu katika maeneo yao, ubabe wa hatari unafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haina sababu ya Jeshi la Polisi kujitengenezea uadui kwa sababu hawana nyumba za kutosha, wanaishi na sisi kwenye jamii, ni ndugu zetu, ni waume zetu, ni shemeji zetu. Tungependa tuishi nao kwa amani, hakuna haja ya kuua watoto wetu akina Akwilina halafu leo jalada hilo linafungwa kana kwamba polisi wameshindwa kufanya uchunguzi hata baina yao wao wenyewe kumtambua ni nani halisi aliyepiga risasi na kumuua Akwilina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishia kumfariji mama kwa sababu anatoka familia ya kimaskini na hakuna la maana lolote linalofanyika. Kesho, keshokutwa, Watanzania ambao wameumizwa na Jeshi la Polisi kutochukua hatua yao, watatumia nguvu kuwashughulikia watu, watawaua polisi jambo ambalo halitakuwa jema. Sasa ni vyema tukachukua hatua hiyo mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi hiyo ambayo si halali ya kukandamiza demokrasia nchi hii ambayo polisi wamekuwa wakiifanya, kule Geita kuna mauaji ya akinamama ambayo yanafanyika. Sasa hivi mama akienda shambani kule Nyangh’wale anatekwa, anavunjwa shingo, wanauawa. Wanatafutwa akinamama wajawazito na akinamama tu wengine katika maeneo ya shamba, suala ambalo limejenga hofu kubwa sana. Sasa ningeomba hii nguvu kubwa ambayo inatumika kudhibiti maandamano ya magari yote hayo tunayaona barabarani, polisi na vifaa vyao hebu vitumike basi viende Nyangh’wale, hawa akinamama wafanye shughuli zao kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili nitamuomba kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba anijibu kama mtu anayetegemea kuwa Rais ndani ya nchi hii siku moja.

Alitutangazia kwamba alikuwa na nia na alishiriki kwenye kura za maoni ndani ya chama chake, kwa hiyo, sidhani kama hiyo nia imekufa mapema hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi kwamba Wabunge wa Viti Maalum wapo humu Bungeni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibara 66 na Ibara ya 78 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazungumza uwepo wa Wabunge wa Viti Maalum ambao majina yao yanapendekezwa na vyama vyao na baadaye wanapatikana na kuunda ile asilimia isiyopungua 30 ya watu ambao wako ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pamoja na Wabunge wengine wa Viti Maalum ambao tuko huku ndani tumekuwa tukizuiwa kufanya mikutano yetu ya hadhara. Namwomba Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Wabunge wa Viti Maalum tunaambiwa tufanye kazi, sisi sio Wabunge wa vyumbani, tufanye kazi chumbani tuongee na akinamama na hili linaleta mtazamo mbaya hata katika jamii, ndiyo maana Wabunge wa Viti Maalum wengi wamekuwa wakidhalilishwa kwa sababu watu hawajui kazi wanazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaache wanawake wafanye kazi, wafanye mikutano, wawawakilishe wananchi ili wananchi waone kama kweli hawa ni Wabunge ambao wapo kwa ajili ya kuwawakilisha. Badala yake tunaonekana kama tuko tu kumaliza mishahara ya Serikali, “unalipwa milionio 12, unalipwa milioni 12” sasa sawa! Kazi yangu haithamiwi, siruhusiwi kufanya kazi, sasa kwa nini nakuwa Mbunge? Kwa sababu kama unalipwa ujira basi ufanye kazi inayopaswa kufanyika na tunahitaji kuwakilisha wananchi wote. Watu wafanye mikutano katika maeneo yao. Kwa hiyo, naomba sasa sheria za nchi yetu ziheshimike, watu wawasikilize wananchi, huwezi ukaja humu ndani ukamwakilisha mwananchi ambaye hujamsikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wa Viti Maalum wafanye mikutano katika maeneo yao, kama ni katika mikoa na kuweza kuwawakilisha wananchi. Badala yake tutasema kwamba Serikali ya Awamu hii ya Tano ipo kukandamiza wanawake, Serikali ya Awamu hii ya Tano ipo kuzuia maendeleo ya wanawake, badala yake tutasema kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano inataka kutengeneza mazingira magumu ya wanawake kuwa Wabunge kwa sababu katika siasa tunasema it’s all about visibility, nani kakuona hata katika Viti Maalum, badala yake sasa kama tunawafunga watu, ngono zitatumika, rushwa ya hela itatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutawatisha jamii kutafuta nafasi za kugombea. Tuwaache wanawake waonekane na hata kuzuia mikutano ya hadhara, inaathiri hata vijana wengine wasionekane kwa sababu kwa vijana kama mimi tumekuja humu ndani ya Bunge kwa sababu ya kazi ambazo tumefanya, tumefanya mikutano, jamii imetuona ikatuamini. Kwa hiyo, si tu kwa hivi wanavyovunja sheria za nchi, lakini pia wanaathiri ndoto za akinamama, wanaathiri ndoto za vijana ambao wangependa siku moja kuwa viongozi ndani ya nchi, kuwa viongozi wema ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nategemea kwamba, katika majibu ambayo kaka yangu atanipatia asinijibu kwa kutoa sababu kama zile alizojibu kipindi kile Katiba na Sheria. Tuweke mstari wa mbele kama tunataka kuendelea na kama unategemea au siku moja unataka kuwa kiongozi wetu, basi show the art kwa majibu unayo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenisaidia na nimeweza kupata nafasi ya kuwa mwakilishi ndani ya Mkoa wa Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile naomba nichukue muda huu pia kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini kwa sababu katika kikao kilichopita niliuliza maswali kutokana na madhara mbalimbali yanayowapata wananchi wa Geita Mjini kutokana shughuli za mgodi na aliwajibika kama alivyoahidi ndani ya Bunge lako Tukufu kufika na kuongea na wananchi, kutembelea sehemu za waathirika.
Mheshimiwa Spika, nina imani hatua tuliyofikia hatimaye hawa wananchi yawezekana wakaondolewa katika eneo husika, lakini pia ataweza kuwasaidia vijana wengi waliojiunga na ushirika na wataweza kupewa maeneo ya kuchimba dhahabu katika maeneo ya Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika huu Mpango, tunazungumzia sana maeneo ya viwanda na katika kuangalia eneo kubwa la viwanda, katika Mpango wanaonesha ni jinsi gani ambavyo Serikali imejipanga na kuwekeza katika maeneo ya viwanda. Wameongelea maeneo ya EPZ na SEZ, wameongelea pia maeneo ya industrial park. Vile vile ukisoma ule Mpango wa mwaka mmoja ulikuwa unazungumzia ni namna gani hizi EPZ na SEZ hazijaweza kuchangia vya kutosha katika pato letu la Taifa.
Mheshimiwa Spika, tukiongelea masuala ya viwanda, tunaongelea mambo ya EPZ, lakini tunawapa watu maeneo makubwa ya kuwekeza, hawa watu pia tunawapatia misamaha ya kodi. Kwa hiyo, tunawapa maeneo ya kuwekeza lakini bado kama Serikali tunapoteza kodi. Kwa hiyo, ni vizuri pia Serikali ikaliangalia hili suala kwamba tunasema kuweka viwanda lakini kitu cha kwanza tuboreshe vitu vya msingi ambavyo ndivyo vinavyohitajika ili kuweza kupunguza kutoa misamaha ya kodi.
Katika hotuba ya Kambi ya Upinzani, imeweza kuonesha ni jinsi gani katika upande wa nishati ongezeko lilijitokeza katika Mpango uliopita ni kidogo, lakini pia katika miundombinu kwa maana ya barabara na vile vile hata katika kilimo ukuaji bado ni mdogo. Hata hizi EPZ zenyewe, bado wanaagiza hata raw materials wanazozitumia katika viwanda vyao. Kwa hiyo, ni lazima tuangalie kama Serikali kuweza kuwezesha kwanza nishati, tuwezeshe miundombinu na ndipo tukimbilie kwenye viwanda ili tuweze kuondokana na misamaha ya kodi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, naomba pia nizungumzie upande wa mapato ndani ya Serikali. Serikali imeonesha kwamba kuna upungufu na tunashindwa kutekeleza mambo mengi kutokana na kutokuwepo na mapato ndani ya Serikali yetu. Katika Sheria ya Local Government ya mwaka 1982 inaonesha kwamba Halmashauri zetu (local government), zitaweza kukusanya fedha ya asilimia 0.3 ya Service Levy katika maeneo hayo kutokana na shughuli za mgodi ama shughuli za uwekezaji wowote ule unaokuwa katika maeneo ya Halmashauri husika.
Mheshimiwa Spika, sheria hiyo pia imetoa kipengele ambacho Waziri ana uwezo wa kufuta kile kipengele cha 0.3 ya Gross Revenue na badala yake wanatoa kiwango ambacho wawekezaji hao wanalipa ndani ya Halmashauri husika. Kwa hiyo, tunapoteza fedha, tunapoteza mapato makubwa kutokana na sisi wenyewe kuzichezea sheria zetu na kutosimamia yale mambo ambayo tumeyapanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Service Levy hata hizo kidogo ambazo zimelipwa, tunashindwa kuona ni namna gani, kama Serikali kuu inaweza kusimamia kule chini ili angalau hii Service Levy inayotolewa 60% ya hiyo Service Levy iweze kutumika katika shughuli za maendeleo. Vile vile bado kama Serikali haiwajibiki kuhakikisha ya kwamba kiwango ambacho kinastahili kulipwa ili 0.3 ya Gross Revenue kuweza kui-determine, Serikali haiwajibiki kuwasaidia Halmashauri katika ku-determine hilo ili kuhakikisha kama Serikali na kama nchi tunapata mapato husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naomba nimpongeze kwa moyo wa dhati sana, kwa jitihada yake ya kusema ya kwamba watu walipe kodi. Binafsi kila nikienda sehemu, tunatafuta risiti tuweze kulipa kodi. Sasa kuna tofauti mbili kati ya Mwalimu Nyerere na Magufuli. Kuna tofauti moja tu, wote wanawapenda wananchi na tunawasikia na wanatamani kuona mabadiliko ndani ya wananchi, lakini Mwalimu Nyerere alianza kwake; kama ni kupunguza mshahara alianza kupunguza wa kwake akafuata wa wengine. (Makofi)
Kwa hiyo, namwomba pia Mheshimiwa Rais kwa kushirikiana na Serikali yake, mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haukatwi kodi ya aina yoyote ile. Kwa hiyo, nachukua pia fursa kuiomba Serikali iweze kuliangalia hili suala kwamba inawezekana kabisa kwamba labda fedha ambazo Mheshimiwa Rais anastahili kupata ni kidogo au hizo alizozitaja Shilingi milioni 9.5 ni kidogo, lakini siyo kukwepa kodi au kumwekea msamaha wa kodi kwa maana inaonesha kama ni upendeleo wa aina fulani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuwajibike kama Serikali, tuweke kodi kwenye mshahara wa Mheshimiwa Rais kwanza na kama ni kuboresha, iwe hatua inayofuata ili tupate ile leading by example, wananchi waweze kuwajibika kwenye kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna masuala ambayo yameongelewa katika Mpango, suala la monitoring and evaluation. Katika shughuli zetu za Kamati, mimi binafsi nimeona shida ambayo imejitokeza kule.
Kuna maeneo ambapo Wizara na katika Mpango inaonesha kwamba Waziri wa Fedha anasema, watashirikiana na Wizara nyingine kuhakikisha kwamba usimamizi huu au monitoring and evaluation inafanyika katika maeneo yote na Wizara zote. Hata hivyo, kuna shida ya hii decentralization by devolution. Binafsi naiona kama vile ina tatizo kwa sababu Wizara inashindwa kwenda kuwajibisha watu moja kwa moja kule chini. Kwa hiyo, naomba…
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA, SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA (MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE): Taarifa!
SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Waziri TAMISEMI....
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, hoja yangu ilikuwa ni kwenye mshahara wa Rais utozwe kodi, lakini pia vile vile kama Mheshimiwa Rais alituambia mshahara wake ni Shilingi milioni 9.5 sijui kama aliupunguza ama ilikuwaje, hilo mtatufafanulia ukoje, mimi binafsi siwezi kulisemea hilo. Hoja yangu ni kwamba mshahara wa Rais utozwe kodi, leading by example, yaani kuongoza kwa mfano. Ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee katika hoja zangu nyingine. Nilikuwa nimeishia kwenye upande wa decentralization by devolution, naomba pia hilo liweze kufanyiwa kazi. Huu mkanganyiko uliopo kati ya TAMISEMI na Wizara uweze kuondoka ili Wizara iweze kufuatilia mpaka kule chini tuweze kuona mambo yanaendaje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna upande huu wa maendeleo ya watu. Naomba nizungumzie kipengele cha makazi bora. Naomba niishauri pia Wizara kama inawezekana ipunguze kodi kwenye vifaa vya ujenzi ili wananchi wapate kujenga nyumba nzuri na badaye Serikali iende ikatoze kodi kwenye kodi za majengo. Tuwasaidie wananchi wetu waishi kwenye nyumba nzuri, wasipate magonjwa wasipate kuumwa na wadudu mbalimbali na waweze kufanya kazi vizuri kwa sababu watakuwa na afya njema.
Mheshimiwa Spika, kuna mahusiano makubwa sana kati ya makazi bora na afya za watu, pia katika upande wa elimu, upande wa wanawake, naomba pia Wizara iangalie kutenga fedha kwa ajili ya wanawake, tuweke suala la equity kwenye elimu.
Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali, imeweka msamaha wa kodi kwenye sanitary towels kwa upande wa wasichana, lakini sasa Serikali iweke fedha ya kusambaza pad mashuleni ili watoto waweze kusoma na wasikose muda wa darasani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ni kwenye upande wa good governance. Ili tuweze kuongoza vizuri kama Taifa, tunahitaji sana kuwa transparency, tunahitaji sana kuwa na accountability.
Mheshimiwa Spika, namwelewa Mheshimiwa wangu Rais John Pombe Magufuli ana nia njema sana, sana; lakini hiyo nia njema lazima iendane na transparency. Hatuwezi kuwa na Bunge ambalo linachuja taarifa! Yaani Bunge ambalo linafanya parental control ambayo inaenda kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuwa na Bunge ambalo hawataki wananchi waelewe Wawakilishi wao wanasema nini. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali mliopo hapa, mzingatie suala la transparency. Transparency ikiwepo, accountability itakuwepo na utumbuaji wa majipu hautahitaji Rais aende kila mahali, lakini wananchi wakiwa na taarifa husika, watawatumbua wao wenyewe katika maeneo yao, hata Wabunge wasiowajibika na wenyewe wataweza kushughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia hata Bunge lenyewe, tuchukue zamu zetu, tuwe wazi na tuweze kufanya kazi kwa uzuri na kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba tu niseme kwamba, kama Taifa na kama Wabunge, tunahitaji, vita ambayo tunakuwa tumeipigana na ambao wengine wameipigana kabla wengine hatujaingia Bungeni, inapaswa iendelee; lile suala la misamaha ya kodi na watu wanaosamehewa kodi kuweza kulipa. Kwa sababu tumechambua hata katika Sekta ya Afya, pesa nyingi haijapelekwa katika Sekta ya Afya, kwa hiyo, tunahitaji kuangalia kila pesa iliko ili tuweze kuhudumia watu wetu wasiweze kufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta hii ya Afya tuna Madaktari ambao wanatibu katika maeneo yetu, ambao wengi wamepata elimu kwa ngazi ya Diploma na hawa Madaktari wamekuwa wakisambazwa katika Vituo vya Afya lakini pia vile vile hata katika Hospitali za Wilaya katika maeneo mengi na wamekuwa wakifanya kazi na watu wasio na elimu ya Udaktari kama mimi, siyo rahisi sana kutambua kama ana degree ya Udaktari au hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo moja kwamba hawa watu pamoja na kutuhudumia vizuri na elimu ambayo wameipata kwa miaka mitatu, wakihitajika kwenda kusoma na kupata degree, inawalazimu tena kwenda kusoma kwa miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iliangalie hili. Mimi sio mtaalamu wa Udaktari, lakini waweze kuangalia ni namna gani wanaweza wakafupisha hii miaka ili angalau, kwa sababu kuna masomo wameshasoma katika kipindi cha Diploma basi wanavyosoma degree miaka iweze kupungua. Mfano ni katika elimu ya engineering hapa hapa Tanzania, wanafunzi waliomaliza Diploma katika vyuo vya Technical Schools kama Arusha Technical, wanapokwenda kusoma degree za engineering wanaanzia mwaka wa pili. Kwa hiyo, naiomba Wizara iweze kuliangalia hilo kama angalau tunaweza kuwasaidia hao Madakatari wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile hawa wanaosoma Diploma kwa jinsia ya kike, inawalazimu wanapomaliza elimu ya Diploma kwenda kufanya kazi kwa miaka mitatu ndipo waruhusiwe kwenda kusoma Degree kwa miaka mitano. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya alisema ndani ya Bunge hili Tukufu kwamba menopause inaanzia miaka 35.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukipiga mahesabu, kama binti atamaliza Diploma kwa miaka mitatu, akafanya kazi kwa muda wa miaka mitatu ndipo akasome hiyo degree ya miaka mitano, kwanza ndani ya hiyo miaka mitatu ya kufanya kazi kuna changamoto. Anaweza akaolewa na mambo mengine hapo katikati yakabadilika. Vile vile anaweza kufikia menopause hata hiyo elimu yenyewe ya Udaktari kwa maana ya MD hajaweza kuifikia. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iliangalie hilo na iweze kurekebisha ili watoto wetu wa kike angalau wapunguziwe muda wa kufanya kazi hapo katikati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile natambua juhudi za kuhakikisha kwamba tunaweka usawa wa kijinsia ndani ya Taifa letu. Kumekuwa na juhudi mbalimbali na harakati za wanawake mbalimbali na leo katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri Ummy aliweza kusema na kumshukuru mume wake kipenzi kwa maneno yake, kwa kumsaidia katika utekelezaji wa kazi. Pia nimemsikia Mheshimiwa Mama Mary Nagu, naye anamshukuru anasema mimi Nagu kanisaidia sana! Pia wanawake hapa ndani ya CHADEMA Mheshimiwa Mama Grace Tendega na mama zangu akina Mheshimiwa Susan Lyimo na wenyewe wanawashukuru waume zao kwa kuwasaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sasa Wizara iangalie umuhimu wa kuwashirikisha wanaume kuweza kuelewa uwezo wa wanawake katika kuwasaidia kuleta usawa wa kijinsia. Hatuwezi tukaifanya hii vita peke yetu, lakini tunahitaji kuwashirikisha wanaume. Kwa hiyo, naiomba Wizara iweze kutoa kama trainings kutoka kwa mashirika mbalimbali ili wanaume pia wapatiwe hii elimu wapate kuona nafasi ya mtoto wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo, naomba pia nimshukuru baba yangu mzazi ambaye kwa kupitia kwake, kwa kuona umuhimu wangu kwake, ana watoto watano, wa kiume mmoja na wa kike wanne na aliapa kwamba lazima atengeneze wanawake wanaoweza kujitegemea katika maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto kubwa zinazowakabili watoto wetu wa kike. Mheshimiwa Ummy katika Hotuba yake ameweza kutaja kwamba kuna vifo vya wanawake, bado vipo na hii hali inatisha, lakini tunaweza tukatambua kwamba baadhi ya watoto au watu wanaokufa kutokana na hivi vifo ni watu wanaobeba mimba kabla ya kufikia umri halisi wa kuweza kupata mimba. Kuna changamoto za kielimu pia ambazo zinawakabili watoto wetu, ndiyo maana wanashindwa kwenda shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, binti anaingia katika kipindi cha hedhi ambapo kama hana vifaa vya kujisitiri (Sanitary towels) anashindwa kwenda darasani sawasawa na mtoto wa kiume. Katika adult level msichana anaweza kwenda katika kipindi cha hedhi kwa siku nne, at maximum siku saba. Sasa binti akikosa darasani siku nne, somo kama ndiyo limeanza leo, baada ya siku nne maana yake hilo somo limekwisha. Kama ni siku saba, hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tutambue kwamba Serikali imeweka msamaha wa kodi kwenye sanitary towels, lakini bado sanitary towels zinapatikana kwa bei ya juu. Sanitary towels kwa bei ya chini kabisa Dar es Salaam ni sh. 1,500/=, lakini nyingine ni sh. 2,500/= mpaka bei ya juu zaidi. Sasa hapa suala linalokuja ni kwamba, Serikali itengeneze chombo maalum ambacho. Humu ndani tunapitisha misamaha ya kodi ili iwanufaishe wananchi, lakini mwisho wa siku inakuwa ni manufaa kwa wafanyabiashara na siyo wananchi tuliowalenga hapo mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali itengeneze chombo maalum cha kuangalia kila bidhaa tuliyoiwekea msamaha wa kodi kinasimamia na kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa bei iliyolengwa kwenye soko. Suala hilo pia linagusa mpaka maeneo ya dawa, kwamba dawa zimewekewa misamaha ya kodi, lakini ukienda madukani kwenye private pharmacies bei ni kubwa. Kwa hiyo, Serikali iliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala hilo hilo, tunasema kwamba Wizara hii ya jinsia iweke kipaumbele na kuhakikisha kwamba, sekta nyingine zote zinaangalia jinsia katika utekelezaji wa mambo yake. Katika kilimo, watu wote wanaofanya kilimo 80% ni wanawake. Usipowaangalia wanawake katika kilimo, maana yake ni kwamba kilimo lazima kife. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika elimu, ni vizuri sasa Wizara ya Afya kushirikiana na Wizara ya Elimu, ikatenga pesa, kama ni sh. 10,000/= kwa ajili ya Shule za Msingi kila mwanafunzi, basi kwa mtoto wa kike iwe ni sh. 12,000/= ama sh. 13,000/= ili ile sh. 3,000/= iweze kugharimia kwenda kulipia sanitary towels. Vile vile katika Vyuo Vikuu mkopo wa Chuo Kikuu uweze pia kugusa kuhakikisha kwamba wa msichana uwe juu zaidi ili kumsaidia asikose darasani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi sasa katika masuala yangu ya Mkoa wa Geita. Mkoa wa Geita tuna changamoto nyingi na tuna vijiji vingi ambavyo havina umeme. Naiomba Wizara ya Afya ishirikiane na Wizara ya TAMISEMI kuhakikisha kwamba, zahanati na vituo vya afya vinapatiwa umeme wa solar ama umeme kabisa kutoka gridi ya Taifa. Kwa sababu, mtu anaweza akajifungua usiku! Sasa mtu anazaaje gizani kwa kweli? Ni kitu kidogo ambacho kinakuwa kigumu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi tuna tatizo hilo hilo la CHF ambapo wananchi hawapati dawa. Vile vile CHF mtu akitoka Geita akienda Chato hapatiwi huduma; akitoka Geita akaenda sehemu nyingine, hapatiwi huduma. Hili nalo muweze kuliangalia ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza tukawasaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kuiomba Serikali kwamba, ikumbuke Hospitali ya Mkoa wa Geita ambayo mmeifanya sasa imekuwa ni Hospitali ya Rufaa, lakini haifanani hasa na kuwa na sifa hiyo ili iweze kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Geita. Pamoja na hilo, liangaliwe suala la kutafuta fast ferry kwa sababu, kutoka Geita kwenda Mwanza tuna maji pale katikati. Ukitegemea hizi ferry za kawaida, mgonjwa anaweza kufia ndani ya ferry. Kwa hiyo, ferry badala ya kwenda na mgonjwa inarudi na maiti. Kwa hiyo, tunaomba sasa tuweze kupatiwa pia fast ferry kwenye hilo ziwa kuhakikisha kwamba wagonjwa wanafikishwa on time katika hospitali zinazohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii, na naomba pia niweze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia tena fursa nyingine na kuweza kuzungumza ndani ya Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kusoma ripoti ya committee maalum iliyoundwa na Rais nimepata kutambua ya kwamba yawezekana kama nchi na katika vipindi vilivyopita na leo hii katika juhudi zinazofanywa na Rais wa sasa za kutafuta mapato mbalimbali lakini Serikali kwa vipindi vilivyopita ilishiriki kikamilifu kusababisha ukwepaji wa mapato ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema kauli hiyo ukiangalia katika mikataba ambayo iliingiwa na nchi hii, katika mkataba wa Bulyanhulu ambao uliingiwa mwaka 1994 kutokana na ripoti maalum ya committee ya Rais inaonesha ya kwamba suala la fuel levy ama mapato au misamaha ya kodi inayotokana na mafuta yanayotumiwa mgodini ilipitishwa kama government notice mwaka 1999. Lakini mgodi huu ulipata mkataba mwaka 1994 ambapo Bulyanhulu ni sehemu ya migodi ambayo inapokea misamaha ya kodi kwenye mafuta. Mwaka 2014 Bunge hili hili tukufu lilitunga sheria na kuilinda mikataba ile ambayo imepita kwamba watu hawa hawafai kuguswa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri kwa Serikali kwamba tusifike hatua tukasema tufunike kikombe tuendelee na mambo mengine, lakini kuna haja ya kupitia pale tulipotoka tuweze kuona kwamba kama kuna mapato mengine tunaweza tukayapata na tusifunike tu kwamba mikataba tulishaifanya basi, sehemu maalum ziangaliwe kuangaliwa ili kuweza kuongeza mapato ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna suala la service levy, mapato yanayolipwa na migodi ambayo ni asilimia 0.3 ya turn over ya migodi hiyo. Kwa miaka iliyopita Serikali iliweka fixed cost kitu ambacho ni tofauti kabisa na Sheria ya Serikali ya Mitaa ya mwaka 1982. Wakaweka fixed cost ya dola za Kimarekani 2,000 ambazo ndizo zinazofaa zilipwe katika Halmashauri zetu. Lakini mwaka 2014 yalifanyika mabadiliko na sasa service levy inalipwa kwa 0.3, ile ile ya turn over. Sasa naitaka Serikali iweze kusimamia na kuhakikisha kwamba inazisaidia Halmashauri hizi ili kuweza kutambua ni kiasi gani ambacho ni turn over wanayostahili kama Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Halmashuri zetu hazina uwezo mkubwa kwa hiyo Serikali iweze kulifanya hilo na kuweza kusaidia. Lakini vilevile tuna TMA na wao wahusike kuangalia, isiishie tu udhibiti kwa maana ya madini lakini waangalie katika eneo kubwa la kuangalia kiasi gani ambacho Halmashauri zetu zinastahili ili kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa Wizara zingine hasa ile inayohusiana na Mambo ya Serikali za Mitaa ni muhimu pia wakatambua ya kwamba dhahabu au madini yoyote yale hayatarudi tena kuwepo kwenye ardhi. Kwa hiyo, ni vyema basi tukaweza kuzishauri Halmashauri zetu, tukashiriki kikamilifu ili walau kiasi kinachotolewa kwa ajili ya service levy kitumike kwa ajili ya kuendeleza Halmashauri, kuweka mikakati au uwekezaji mkubwa ndani ya Halmashauri zetu lakini pia kuendeleza huduma za kimaendeleo badala ya hizo hela kutumika kwenye OC ili Serikali nayo ipange mambo mengine lakini pesa zitumike kwa shuguli za maendeleo zilizokusudiwa kwa ajili ya wananchi wa eneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Geita na katika maeneo ambayo yanapata shida kubwa sana kutokana na uwekezaji wa kampuni ya Geita Gold Mine, ni wananchi wa Geita. Wananchi hawa katika maeneo ya Katoma, Nyamalembo na Compound. Wananchi hawa wamekuwa wakiathirika na mitetemo, vumbi inayotoka migodini. Vilevile nyumba zao zimekuwa zikiathirika kwa nyufa. Mheshimiwa Naibu Waziri aliweza kuwatembelea wananchi hao na akagundua kasoro ambazo zipo na akaona matatizo ya kuchafuka kwa maji kwa maeneo ambayo wananchi wanaishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha kusikitisha, Mheshimiwa Naibu Waziri alitoa agizo kuwa mgodi kwanza kuziba mtaro ili maji yasiende kwenye visima vya maji, lakini pia kuhakikisha ya kwamba wananchi hawaendelei kunyanyasika katika eneo lao. Lakini nikutaarifu kwamba ni kitu cha kushangaza, mgodi huu una kiburi cha ajabu yaani hata agizo la Serikali hawakuweza kulitimiza na mpaka leo hii hicho hakijafanywa na badala yake Serikali inaangalia namna mbadala ya kuongea nao, badala ya kusaidia maisha ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna kesi mbalimbali ambazo zimejitokeza Geita, Mheshimiwa Waziri unafahamu kuna wananchi wa Maili Mpya katika eneo lile. Wananchi ambao walifukuzwa kwa kudhalilishwa, maeneo yao yakafukiwa, mgodi umechukua hilo eneo, lakini bado kuna wananchi wa Katoma ambao wengine hawakulipwa fidia hata kidogo, wamefukuzwa katika maeneo yao. Sasa haiwezekani kwamba tuna Serikali; kuna kipindi niliendelea kuitembelea nchi ya Norway katika mafunzo wakatuambia kwamba wafanyakazi walivyokuwa wananyanyaswa walifananisha manyanyaso yao na wafanyakazi wa Kiafrika wanaonyanyaswa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo tunanyanyaswa sisi ndani ya nchi yetu na wawekezaji hawa hawa bila kuzingatia haki za binadamu na uhuru wetu na afya zetu ndani ya Taifa letu. Kwa hiyo, ninaiomba sasa Serikali iweze kuangalia ni namna gani mtawasaidia wananchi wa Geita. Kutakuwa hakuna maana kwa wao kumpigia Rais Magufuli kura nyingi na kwa imani kubwa waliyonayo tena Rais kutoka nyumbani, halafu wakabaki na manyanyaso makubwa yanayofanywa na mgodi wa Geita Gold Mine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mtaa wa Nyakabale ni eneo ambalo liko ndani ya beacon ya mgodi. Eneo hilo wananchi wa Nyakabale kama unavyofahamu limefungiwa hata nyia yake. Wananchi hawawezi kutumia njia maalum waliokuwa wanatumia zamani kuelekea mjini, badala yake mgodi umeweka mabasi asubuhi na jioni, mgodi ume-limit movement ya wananchi katika eneo husika. Pia limechimbwa shimo la takataka ndani ya eneo lao ambapo sumu za mgodi zinamwagwa ndani ya Nyakabale katika Kata ya Mgusu. Hii inaathiri afya za wananchi wa Geita, zinaathiri afya za wananchi wa Nyakabale. Ninaomba Serikali mfuatilie hilo ili hali iweze kukomeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ni suala la wachimbaji wadogowadogo. Katika kipindi kilichopita Serikali iliwahamisha wananchi wa Samina na kusema kwamba inawapatia eneo lingine la uchimbaji. Kwa masikitiko makubwa sana Serikali ilitoa eneo ambalo halijapimwa na ilitoa pia sehemu ambayo utafutaji wa madini kwenda chini uko mbali sana. Sasa Serikali yetu hii naiomba inavyotoa maeneo ya madini yaliyo karibu kwa wawekezaji wawafikirie wazawa Watanzania ili waweze kufanya shughuli za uzalishaji.
ushirikishwaji katika maeneo ya uchimbaji wadogo wadogo. Kwa sababu wanawake wanapiga mawe, wanawake wanafanya shughuli za kwenye makarasha, wanawake wanafanya shughuli mbalimbali katika maeneo ya migodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia Wizara iweze kuliangalia hilo katika hizo ruzuku wanawake wa Geita pia ziweze kuwafikia na ziweze kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia wananchi wa Nyarubuso, ni wananchi wanao athirika kutokana na shughuli za ellusion ama uchenjuaji wa dhahabu. Serikali naomba itoe elimu nzuri kwa wananchi wa Geita, kwamba pamoja na uchenjuaji huo lakini waweze kufanya shughuli ya makusudi ya kwamba uchenjuaji usiathiri vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ninaiomba Serikali itoe kauli humu ndani, Ilitoa ahadi kwa wananchi wa Geita kuwapatia magwangala ama mabaki ya dhahabu, lakini tunafahamu Serikali haijafanya uchunguzi kujua ni kiasi gani watapata dhahabu katika magwangala hayo. Ninaomba Serikali itoe kauli ili mchanga huo basi wananchi kwa sababu wamekosa maeneo ya kuchimbia, sasa wanatafuta mabaki ya mchanga wa dhahabu kutoka katika kampuni ya Geita Gold Mine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itoe kauli ili kauli iliyotangazwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu tuweze kuelewa ina faida ama haina faida na lini itatekelezwa kwa wananchi wa Geita ili walao kama hamjawapatia maeneo walau wapatieni huo mchanga ili waweze kujifanyia shughuli zao za maendeleo, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii na namshukuru Mungu ambaye meniwezesha kufika katika Bunge hili la Bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajielekeza moja kwa moja kwenye mambo ya msingi ya kuchangia napenda niongelee suala moja. Hapa kuna miongozo kadhaa iliombwa na uliitolea ufafanuzi lakini utaratibu ambao umesema ufuatwe wa watu kwenda kwenye hizo taasisi za
ajira nadhani ni vizuri tukatambua kwamba hili suala sana sana linaelekea kwenye mambo ya human trafficking ambapo watu hawa wanasafirishwa kwa njia ambazo sio nzuri. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaangalia ni namna gani inawalinda watoto wetu kutokana na hiyo biashara haramu ili pia wasiweze kupatwa na matatizo. Kwa hiyo, suala hili naomba liangaliwe katika muktadha wa human trafficking.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni la mama yangu hapa Mama Mollel ambapo Baba yangu ninayemheshimu amelizungumzia lakini niseme tu mama alijiunga na CHADEMA katikati ya uchaguzi. Kwa hiyo, si vizuri kuwadhalilisha viongozi wetu ambao tunawaheshimu katika Bunge letu hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa najielekeza katika suala ambalo lipo mbele yetu hapa. Tunafahamu kwamba nchi yetu na viongozi wetu ambao wako hapa wameweza kutueleza kiundani kuhusu masuala ya utawala bora. Hata hivyo, katika masuala ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji
ni vitu vya msingi sana vya kuweza kuzingatiwa ili kuweza kuupata huo utawala bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha nyuma wananchi kwa kiasi kikubwa sana wameshiriki kikamilifu kushirikiana na Wabunge kwa ajili ya kuiwajibisha Serikali. Naongea hivi kwa maana moja kwamba kipindi cha nyuma tulikuwa na Bunge live ambapo wananchi wamekuwa
wakifuatilia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge wakiweza kusikiliza vipindi vinavyoendelea ndani ya Bunge ambapo imewasaidia wao kwanza kuelewa hata sheria zinazopitishwa ndani ya Bunge, kuelewa bajeti ambayo inawagusa moja kwa moja lakini pia kuna mambo mengine ambayo yameweza kuwagusa wananchi moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge hili upande wa Chama cha Mapinduzi waliunga mkono sana suala la Bunge live kuondolewa, lakini kuna watu ambao ni wanawake ambao ndiyo waathirika wakubwa kwa kuliondola hili suala la Bunge live. Jana tumesikiliza jinsi ambavyo idadi ya wanawake imepungua katika Baraza la Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na nafasi mbalimbali za Kiserikali. Kwa hiyo, sisi kama wanawake tuna nafasi ya kwenda kugombea katika majimbo na katika jamii zetu zilizojaa mfumo dume, Bunge live limeweza kubadilisha
umma na kuona kwamba wanawake wanaweza. Pia kuna mambo ya msingi mengi ambayo wanawake tumeweza kuyainua ndani ya Bunge hili, kuna masuala ya ndoa za utotoni uelewa watu umeweza kubadilika, kuna masuala mbalimbali yanayowagusa mabinti zetu kule nyumbani
wananchi wameweza kubadilika taratibu kutokana na kwamba wanasikiliza Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile kuna ripoti ya TWAWEZA ya mwaka 2012 inayoonesha kwamba masuala ya ukeketaji yamepungua kwa asilimia 21 na inatokana na mchango wa Bunge. Kwa hiyo, wananchi waliokuwa wakifuatilia Bunge wameweza kubadilika na kuona kwamba kuna haja ya kuweza kupunguza masuala ya ukeketaji na hii inatokana na mchango wa Bunge ndani ya Bunge hili letu
Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba yawezekana ni maagizo tunasingizia kupunguza matumizi ya Serikali kwa masuala ambayo yanaathiri masuala ya kijamii na kijinsia. Kwa hiyo, kama wanawake sasa kuna haja kubwa ya kusimama na kudai hili suala la Bunge live kwa sababu linatuathiri. Hata kama hamuwezi kuteuliwa kwenye Baraza la Mawaziri basi tukapata nafasi za uwakilishi kule chini na nina imani wanawake kwa pamoja hebu tufanye mambo ya msingi kwa ajili ya maisha yetu na watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine ambalo napenda kuzungumzia katika masuala ya Serikali za Mtaa na niseme tu namshukuru Naibu Waziri Mheshimiwa Jafo kwa kuweza kufika Geita na kwa kujibu swali langu ambalo lilikuwa ni kuhusu masuala ya maji na bwawa. Napenda tu pia uje utuambie ni lini sasa hiyo Tume ambayo ulisema itaundwa itaenda kuchunguza ubadhirifu ambao umefanywa katika
eneo hilo hapo Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna suala lingine Waheshimiwa Mawaziri wa TAMISEMI ambalo napenda kulitolea ushauri na pia imeshalitolea ushauri ndani ya Halmashauri yangu ambayo ninatoka. Geita ni kati ya Halmashauri nyingi ambazo zinapokea service levy ya 0.3% kutoka Mgodi wa Geita Gold Mine kutoka kwenye gross revenue, pesa hizi zinavyotumika nyingi zinatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya kuendesha shughuli mbalimbali za Halmashauri. Niiombe Serikali, tumetoa mwongozo hatujatunga sheria kuhusu utaratibu wa 5% kwa wanawake na 5% kwa ajili ya wanaume. Hebu tuweke utaratibu sasa kwamba walau 70% ya pesa zote zinazotokana na service levy ziweze kwenda kwenye shughuli za maendeleo na 30% ziingizwe katika matumizi ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili litatusaidia, hapa tunasema kwamba wananchi bado wana wajibu wa kuchangia huduma mbalimbali za kihuduma katika maeneo yetu, lakini kuna hela ambazo zinatoka katika maeneo ya mgodi, kwa hiyo naiomba sasa Serikali iweze kutoa
mwongozo huo ili pesa hiyo iweze kusaidia shule za maana zipatikane. Kwa sababu hizo hela hazina mwendelezo miaka si mingi pesa hizo zitakata kwani mgodi utamaliza shughuli zake. Kwa hiyo, ni afadhali sasa hizo pesa ziwe zimeshaingizwa kwenye shughuli za maendeleo za wananchi ili hata miaka ijayo watoto wetu watuone tuna maana, tulizitumia hizi hela kwa ajili ya faida yao, wamekuta huduma nzuri za afya na shule kutokana na kutumia hizi pesa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwamba tuna tatizo kubwa sana nchi hii. Mheshimiwa Rais alipokuwa anaingia madarakani alikataza mambo ya semina elekezi suala ambalo limezungumzwa pia katika hotuba ya Kambi ya Upinzani kwamba mafunzo elekezi ni suala nyeti sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwetu kule tuna shida, Mkuu wa Wilaya anawafukuza Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wakati sheria iko wazi, Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa anaondolewa na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi Mheshimiwa Rais yeye mwenyewe alikiri akasema kwamba yeye huu urais amepata tu, simu alipiga ikaitika. Kwa hiyo, kwa lugha nyingine yeye mwenyewe alikuwa anastahili elekezi fulani, namheshimu sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaangalia suala la watumishi wetu Serikalini tumekuwa na watu tunaowalipa mara mbili mbili. Hapa tunajifunza kwamba scheme of service inasema mtu anakuwa promoted baada ya miaka mitatu kutokana na ripoti ya utendaji wake mzuri, lakini suala
hilo halifanyiki ni kwa sababu Serikali hamna pesa, fedha nyingi mnalipa Wakurugenzi wawili, ma-DED wawili, ma-DAS wawili tutafika wapi kwa namna hiyo? Kwa hiyo, watumishi wa Serikali wanakosa morali kazi hazifanyika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wa Serikali wanavunjika moyo na zaidi ya hapo bado tunawatumbua kiholela bila kuheshimu hata nafasi wala mamlaka walizonazo. Hata ndugu zangu hapo Waheshimiwa Mawaziri nyie pia mnakumbwa na hilo, heshima ya kuthamini utendaji
wa mtu inakuwa haipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali iangalie hili suala kama hawa watu wanapangiwa maeneo wapangiwe wawe productive kuliko kukaa nyumbani. Serikali mnalipa watu mishahara ambao hawana kazi ya maana ambayo wanaifanya katika Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile haya masuala kwamba hatuna hela, Serikali ifanye mkakati itafute pesa watu tuwapandishe vyeo kutokana na ripoti na ufanyaji kazi wao mzuri ili tuweze kuwa na wafanya kazi wazuri ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi cha nyuma pamoja na kwamba Rais wa sasa alimbeza sana Rais aliyepita lakini alikuwa anatafuta viongozi au watu mpaka kutoka nchi za nje, watu wenye uelewa na wenye taalum fulani…
KUHUSU UTARATIBU...
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nadhani hata pamoja na kwamba tuna roho ya kuwatetea viongozi au mabosi wetu, lakini hebu tuwe wakweli, kama haya masuala hayakuandikwa hata kwenye vyombo vya habari mseme kwa sababu ni vitu ambavyo
vimeandikwa na vimesikika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi niseme tu na hata nilivyozungumzia masuala ya semina elekezi hata kwa Mheshimiwa Rais mwenyewe si kawaida. Mheshimiwa Rais kweli, kuna kuteua Wabunge hapa si imeleta shida mpaka imebidi mtu tena mwenye ulemavu atolewe ni masuala ya shida hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni kijana, naomba niseme kwamba naipenda nchi yetu hii, lakini pia namheshimu sana Mheshimiwa Rais, ni jirani yangu, ni baba yangu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Peneza jambo moja tu, kwa sababu nimesema ili tusianze kwenda mbele na nyuma, Rais wa sasa kuhusu kumbeza Rais aliyepita. Naomba hilo uliweke sawa ili tuweze kusonga maana hiyo sentensi ndiyo yenye kuleta taabu hapa.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, labda sijui kama ni neno kubeza niseme basi alikuwa akizungumzia upungufu kwenye utawala wake na yeye hawezi kuyafanya kama yeye alivyofanywa, labda niseme kwa mfumo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nimalizie kwa kusema neno moja kwamba naipenda nchi hii, lakini nathamini pia viongozi. Pia niseme kwamba tunahitaji…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa fursa hii ya kuweza kuchangia kwa maandishi. Natumia fursa hii ya kufanya wajibu wangu wa Kibunge kwa kuishauri Serikali katika bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa jana katika michango yangu Bungeni kwa Wizara hii nilitoa ushauri kwa Serikali kwamba Serikali iliangalie suala la hedhi na upatikanaji wa sanitary pads. Natumia fursa hii kuikumbusha Serikali haja ya kulishughulikia suala la hedhi ili kusaidia kupunguza mimba za utotoni na school drop-outs kwa watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iunde chombo ndani ya TFDA kitakachofanya kazi ya kusimamia bei ya bidhaa ambazo zimeondolewa VAT kama vile dawa na sanitary pads ili lengo la kuondoa VAT liweze kutimia kwa kuwasaidia wananchi kupata bidhaa hizo kwa bei rafiki tofauti na ilivyo sasa ambapo wafanyabiashara hujipatia faida kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa sanitary pads kunamfanya mtoto wa kike kukosa siku nne mpaka saba suala ambalo linajenga utoro shuleni. Watoto wakike hukosa ujasiri kwenda darasani kwa kuwa hawana vifaa bora vya kujihifadhia kipindi cha hedhi. Utoro huo wa siku nne hadi saba humfanya mtoto wa kike kupoteza muendelezo wa kimasomo na hivyo mtoto wa kike anakuwa katika hatari ya kufanya vibaya katika masomo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utoro pia unachangia katika ongezeko la school drop-outs, yaani kuacha shule kwa watoto wa kike ambapo baadaye huleteleza (husababisha) mimba za utotoni. Ni vyema Serikali ikalitazama suala hili kama suala muhimu na kuweza kulifanyia kazi ili kuwaokoa watoto wetu. Serikali ikisaidia kupatikana kwa sanitary pads kwa bei rafiki au bure itasaidia kuongeza kiasi cha ufaulu cha watoto wa kike kwa kuwa utoro utakoma na upatikanaji wa sanitary pads utapunguza idadi ya watoto wa kike wanaoacha shule na hivyo kupunguza mimba za utotoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu iratibu suala la upatikanaji wa pesa ili kugharamia sanitary towels. Serikali iongeze pesa kwenye capitation funds ili watoto wa kike wapate sanitary pads/ towels mashuleni. Katika kusimamia hilo, Serikali ihakikishe anapatikana mwalimu wa kike (matron) atakayeshirikiana na Mwalimu Mkuu wa Shule katika kusimamia pesa za capitation ambazo zitakuwa zimepangwa kwa ajili ya upatikanaji wa sanitary pads. Matron atawajibika kuunda girls club mashuleni ili kujua namna ya kutumia na kupata sanitary pads lakini pia girls clubs hizi zitasaidia kutoa elimu ya afya ya uzazi. Wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu wapatiwe ongezeko kwenye mkopo ili waweze kugharamia sanitary pads.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeandaa hoja binafsi ingawa kutokana na ufinyu wa nafasi sijaweza kuiwasilisha; pamoja na kwamba imewasilishwa kwa Mheshimiwa Spika na Katibu wa Bunge. Hoja hiyo niliijenga katika kuliomba Bunge liazimie kuitaka Serikali katika kubadilisha kifungu cha dawa kuwa katika fungu la matumizi ya kawaida ya Wizara. Kwa sasa kifungu cha dawa kiko kwenye fungu la bajeti ya maendeleo ya Wizara ambapo pesa hizo hazipatikani au kutolewa kwa kila mwezi na hivyo kuathiri upatikanaji wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fungu la bajeti ya maendeleo la Wizara katika magonjwa kama UKIMWI na TB hutegemea wahisani ambao huchelewa kutoa pesa hivyo huathiri upatikanaji wa dawa. Ni vyema sasa Serikali ikaweka pesa za dawa na vifaa tiba katika fungu la matumizi ya kawaida na ifuate vipaumbele kama ifuatavyo; kwanza, mshahara; pili, dawa za binadamu na vifaa tiba na tatu matumizi mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia dawa za binadamu kuwa na pesa za uhakika ambazo ni pesa za ndani na hivyo kuondoa tatizo la upatikanaji wa dawa. Kwa kusema pesa za dawa za binadamu na vifaa tiba namaanisha dawa pamoja na vifaa tiba wezeshi kama vile pamba, sindano, gloves na si vifaa kama x-ray machines ambazo zibaki kwenye fungu la maendeleo ya bajeti, ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nachukua fursa hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunisaidia na kuweza kuchangia katika bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kwanza ambacho napenda kuanza nacho ni kitu ambacho kimeongelewa na Wabunge na Watanzania wengi, ni suala la makinikia pamoja na ripoti ambazo zimetokana na Tume ambazo ziliundwa na Mheshimiwa Rais. Siku zilizopita tumepata pia kusikia kwamba President wa Barrick amekuja kwa ajili ya kuweza kufanya mazungumzo, ingawa kauli tunazozipata, kauli iliyotoka mdomoni mwa Rais na kauli iliyotoka katika Kampuni yenyewe ya Barrick ni maneno ambayo kidogo yanakinzana ambapo tunashindwa kuelewa ni kitu gani hasa ambacho kimeongelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu ambacho napenda tujiulize, ni kwamba tunaenda kufanya negotiations kwa kitu gani, tunaenda kufanya mazungumzo kwa ajili ya nini, tunaenda kufanya mazungumzo kwa ajili ya makinikia ama tunakwenda kufanya mazungumzo ili kuweza kuangalia vitu vyote ambavyo tumepoteza kutokana na mikataba hii? Kama tunakwenda kufanya mazungumzo ili kuangalia ni jinsi gani ambavyo Tanzania tumeweza kupoteza kutokana na sisi wenyewe kama Serikali, sisi wenyewe kama nchi, sisi wenyewe kama viongozi ambao wamekuwepo kwa kuingia mikataba mibaya ambayo imetuletea wizi namna hii, migodi yote iweze kuhusishwa katika mazungumzo haya. Kama tunataka tuangalie suala zima la mikataba, kama tunataka kuangalia suala zima la sheria, ni lazima tuangalie kwa migodi yote, hatuwezi kwenda kwenye mazungumzo na mtu mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye hili suala zima la makinikia, napenda kutoa tahadhari kidogo, kumekuwa na taarifa ambazo zinakinzana, lakini ningetaka kuiamini Serikali kwa Tume na ripoti ambayo imeitoa. Naomba pia tuangalie na tuweze ku-verify information ambazo tumezitoa na Serikali iende kwenye hatua ya mbele zaidi kufanya uhakiki ili kama tunaenda kwenye negotiations, kama tunaenda kwenye mazungumzo twende kama watu wasomi, twende na timu imara, twende na watu ambao wanaweza kusimamia kitu ambacho kipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kutokana na muhtasari wa ripoti iliyotolewa inazungumzia kwamba makinikia haya yameanza kusafirishwa toka mwaka 1998 lakini ukisoma katika ripoti ya Lawrence Masha na ripoti ya Jaji Bomani inaonesha kwamba production ya mgodi huu imeanza mwaka 2001. Kwa hiyo, hebu tukaangalie mambo yetu vizuri, twende tusidharaulike, kama tunapeleka Maprofesa kweli ionekane tuna information ambazo ni sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia suala hili halijatuletea athari au kuibiwa tu kama tunavyosema au Serikali kupoteza mapato lakini suala hili la migodi na mikataba ambayo Serikali imeingia imeleta mpaka wananchi wetu kupoteza maisha. Wananchi wetu wamepoteza maisha huku migodi hii ikilindwa na askari polisi wetu. Vyombo vyetu vya usalama vimepiga risasi watoto wetu wa Kitanzania kulinda uwekezaji wa Wazungu. Ndiyo maana tumepata vifo vya wananchi wengi vilivyotokea kule Tarime lakini na athari kubwa sana ambazo ziko katika Mkoa wangu wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya bado hayajaisha, ni miaka imepita tangu wananchi wa Tarime wamekufa lakini bado athari na shida zinaendelea. Ukisoma katika ripoti ya Jaji Bomani inataja maeneo mawili ndani ya Geita, eneo la Nyakabale ambalo wananchi wanaishi ndani ya leseni ya mgodi. Wananchi ambao barabara yao ya mwanzo imefungwa, hawawezi kupita barabara yao ya mwanzo kwa sababu ya mgodi. Wananchi wanateseka, wanahatari ya kubakwa kutokana na hii njia ambayo imetengenezwa na mgodi. Wananchi hawana huduma hata ya umeme wala maji katika eneo lao kwa sababu ni eneo lenye leseni ya mgodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wananchi wa Katoma wametajwa kwenye ripoti ya Bomani kwamba wananchi wa Katoma na Kompaundi hawa ni watu wanaoathirika na mitetemo ya mgodi, nyumba zao zinapasuka. Waziri Kalemani alikuja Geita kuongea na hawa watu wa migodi ili kuhakikisha ya kwamba haya yote yanamalizika.

TAARIFA.......

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu akae chini, kwa sababu kama yangekuwa yamefanyika hayo, tusingekuwa na kikao na Kalemani juzi hapo Geita. Akae chini hajui kinachoendelea Geita, haishi Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kitu ambacho nasema ni kwamba ninaumia kwa sababu haki za watu zinaendelea kuvunjwa. Tunaongelea kodi kupotea lakini haki za binadamu zinavunjwa katika maeneo haya yanayozunguka maeneo ya migodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitoe suggestions, tuna kitu ambacho kinaitwa service levy, 0.3 percent ya gross revenue ya hii migodi, mimi natoa wazo kwa Serikali na kwa Waziri Mpango, Serikali ilete sheria humu ndani, tutengeneze Development Fund. Pesa hizi zote zinazokusanywa zitaingizwa kwenye hiyo Development Fund ili kuhakikisha zinaenda kufanya shughuli za maendeleo katika maeneo husika ili wananchi hata baada ya shughuli za mgodi kuondoka waone kwamba kodi zilizopatikana zilijenga miundombinu kwa ajili ya watu wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichangie katika suala la kuweka mfumo wa bajeti unaozingatia usawa wa kijinsia. Nilipokuwa mgeni kabisa ndani ya Bunge hili nilichangia kuhusu suala la sanitary pads, nikasema Serikali iweke pesa ili kuhakikisha watoto wetu mashuleni wanapata sanitary pads. Ni kitu ambacho hakijafanyiwa kazi na Wizara ya Afya wala hakijafanyiwa kazi na Wizara ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunaona kwamba kama ni shughuli za maendeleo, watoto wa kike na wanawake wana haki sawa ya kushiriki katika uchumi wa Taifa lao. Kutokana na utofauti uliopo, wanawake na wasichana wanashindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli hizi. Kwa hiyo, niombe Serikali ipange pesa kwa kuzingatia kwamba kina mama wanaweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwawekee hela za kutosha kwenye dawa na hapa nilipendekeza kwamba pesa ya dawa ihamishwe kutoka kwenye development budget zipelekwe kwenye recurrent expenditure. Hela za dawa peke yake, vifaa tiba vibaki kwenye development budget ili kuhakikisha kwamba hela za dawa na maji ya uchungu zinapatikana ili akina mama wetu waweze kupata tiba na kuepusha vifo wakati wanajifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye masuala ya kilimo, akina mama ambao wana uwezo wa kumiliki ardhi mpaka leo hii ni asilimia nane tu, wengine wanatumia ardhi ambazo ni za waume zao na ardhi za ukoo. Kama Serikali katika bajeti yake, inaweka mifumo gani ya kuhakikisha kwamba akina mama wanaweza kutengewa pesa kuwainua ili na wao waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo za maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho naomba nipendekeze kwenye suala la property tax ambalo limeshazungumziwa na wengi. Mimi natoka katika Halmashauri ya Mji wa Geita hapo ndipo ninapoishi na wananchi wale…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kwanza kuipongeza Kamati hii ya Huduma na Maendeleo yaa Jamii kwa kuweka pendekezo la Serikali kutoa taulo za kujihifadhi watoto wa kike wakati wa hedhi na Serikali kutoa pads hizo bure mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wenzangu wanafahamu na jamii pia inafahamu, kwamba niliandika hoja binafsi na kuiwakilisha ndani ya Bunge, kwa maana ya kwa Katibu wa Bunge ambayo kwa bahati mbaya haijapata nafasi kwa sababu Ofisi ya Katibu imenijibu kwamba hoja ya kugawa pads bure mashuleni inavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 99(2) ya Ibara hiyo ya Katiba. Hayo ni majibu kutoka Ofisi ya Katibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, bado naipongeza Kamati kwamba wametoa mapendekezo ambayo mimi nimeambiwa navunja Katiba, kwamba sasa Serikali igharamie pads bure mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa hoja yangu ni moja, tuna watoto wa kike wengi mashuleni ambao wanashindwa kukaa vizuri darasani, wanashindwa kuwa na ujasiri wa kujifunza kwa sababu wana hatari ya kujichafua wakiwa katika kipindi cha hedhi.

Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu, amewahi kuliambia Bunge hili kwamba watoto wetu wanatumia vitambaa, wanatumia majani, wanatumia mchanga mpaka wanatumia mavi ya ng’ombe. Hiyo ilikuwa ni kauli ambayo kipindi anatoa kauli hiyo, alikuwa akijibu swali la Mheshimiwa ambaye sasa ni Naibu Waziri wa kupitia Watu wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shida hiyo inayowakuta watoto wetu, bado kuna haja kubwa ya Serikali kuona umuhimu ya kuwapa watoto wetu pads bure mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho ningependa kusema kwamba katika takwimu za Serikali, zilizotolewa na TAMISEMI kwamba wasichana wengi ndio wanaacha shule kuliko..

T A A R I F A . . .

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukaelewa mambo tunayoyajadili, tuache umbea kwenye mambo ya maana yanayogusa maisha ya watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya watoto wanaoacha shule katika kidato cha kwanza, kati ya wanafunzi 9,881 walioacha shule wasichana ni 9,337; kitado cha pili, ni 13,559 wasichana walioacha shule ni 12,617.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu hizi kuanzia form one mpaka form four ni udhibitisho tosha kwamba watoto wetu wanaacha shule kwa sababu ya kukosa vifaa muhimu kama vifaa vya hedhi. Serikali kupitia takwimu za TAMISEMI, imesema wazi kwamba sababu kubwa inayowafanya watoto wa kike kuacha shule ni utoro. Utoro wakiwa kwenye hedhi, siku tano za hedhi wanashindwa kuhudhuria darasani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ifike wakati sasa Bunge ione umuhimu wa kuweza kuwapatia watoto wetu pads bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya mahesabu, kwa bei ya chini kabisa, kama Serikali ingeweza kununua pad ya kila mtoto kwa shilingi 2,500, kwa watoto wa shule wote ambao ni 1,870,889, wanafunzi wa shule ya msingi kuanzia nusu ya darasa la tano, darasa la sita na darasa la saba, Serikali ingegharimia shilingi 46,762,000,000 ndizo ambao Serikali ingegharimia kuwanunulia watoto wetu pads. Kwa sababu ni Serikali, ingeweza kupata pads kwa bei chini kidogo, kwa hiyo, kama Serikali ingenunua pad kwa shilingi 1,500, basi Serikali ingetumia shilingi bilioni 28 tu kuwanunulia watoto wetu pads bure mashuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ikichagua kwamba tutumie re-usable pads suala ambalo mimi mwenyewe siliungi mkono sana kwa sababu vijiji ni asilimia 39 tu ya maji ndiyo yanayopatikana vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ingetumia shilingi 14,963,000,000 kugharimia watoto kama wangeweza kutumia re-usable pads.

T A A R I F A . . .

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, Bunge litakumbuka kwamba nilivyokuwa Mbunge mgeni kabisa kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017 ndiyo hoja iliyolifanya Bunge hili lote mkapiga makofi kwa kuunga mkono hoja hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Maria Kangoye ni Mbunge ambaye amewahi kuchangia hoja hii ya watoto kupata sanitary bure mashuleni. Mbunge ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Walemavu, ni binti ambaye amewahi kuuliza swali ndani ya Bunge hili na ndipo akapata majibu ya kuhusu sanitary pads. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge tulilomaliza Novemba, niliuliza swali na Mheshimiwa Jafo akanijibu kwamba Serikali inajaribu kuweka mikakati ya namna ya kulifanyia ili suala...

T A A R I F A . . .

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Hansard ipo, unaweza ukanipatia muda nikatafuta majibu ya Mheshimiwa Waziri nikakuletea hapa mbele. Nitakushukuru sana kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukiangalia katika takwimu leo na ninatambua michango ya mpaka Waheshimiwa Wabunge wanaume ambao wameweza kuzungumzia hii pads, hata Wabunge wanaume ambao wameunga kampeni ambazo tumezifanya mtaani. Ni ukweli kwamba kadri ya mtoto wa kike anavyopanda kimasomo, akitoka darasa la kwanza kwenda darasa la pili, kwenda darasa la tatu, kwenda darasa la nne, kwenda darasa la tano, ndivyo anavyoongeza uwezekano wa yeye kujipatia kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika takwimu zilizopo, ni kwamba kadiri mtoto anavyosoma, anavyofika Sekondari na kwenda mbele, anaongeza asilimia 15 mpaka 25 ya uwezo wa yeye kuweza kujiingezea kipato. Kwa hiyo, ninaomba watoto wa kike, Serikali tuache kuangalia Upendo unatoka kwa nani, tuangalie suala la msingi linalogusa watoto wetu wa Kitanzania. Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ukiangalia katika ripoti ya Kamati, Kamati katika vitu ambavyo vimependekezwa, katika ripoti yake ukurasa wa 22 kwamba maeneo ambayo wachimbaji wadogo wadogo wamekuwa wakipata shida na wao kutorosha madini kupeleka nje ya nchi. Kamati imetaja matatizo ni kodi ambazo ziliwekwa na kodi hizi ni kodi ya ya ongezeko la thamani (VAT 18%), kodi ya zuio (ithholding tax 5%), tozo ya ushuru (service levy 0.3%), tozo ya ukaguzi kwa maana ya (inspection free ya 1%) na mrabaha wa madini katika maeneo mbalimbali ambao wachimbaji hao wadogo wanatozwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakubaliana nami kwamba, pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais Magufuli alifanya kikao na wachimbaji wadogo na kukubaliana kwamba Serikali itafanya utaratibu wa kuondoa kodi hizi zinazowakabili wachimbaji wadogo, lakini ndani ya Bunge hili kuanzia mwaka 2017, tulipokuwa tukijadili Finance Bill ndani ya Bunge hili tatizo la withholding tax lilijadiliwa ndani ya Bunge hili na Mheshimiwa Mbunge wa Kahama pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa Nzega ambao na wenyewe ni Wabunge wa Chama cha Mapinduzi na kuonyesha kwamba hili ni tatizo na Serikali isikubali kupitisha kodi hizi ambazo zinaenda kuwakaba hawa wachimbaji wadogo wadogo. Hata hivyo, hatukuweza kusikiliza, leo miaka miwili baada ya kupitisha hiyo Finance Bill, tunarudi tunakaa na wachimbaji wadogo ili kuweza kuzifuata kodi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utakubaliana nami kwamba nchi hii sasa tumekuwa na matatizo mengi, kwa sababu hatusikilizi ushauri au hatuongei na wadau kabla ya kufanya maamuzi. Tulipokuwa tunaanza Bunge hili tulipata shida kwa Serikali kuweka kodi katika huduma za bandari. Serikali imepoteza fedha nyingi sana kwa watu kuhama kusafirisha mizigo kupitia bandari yetu, Bunge hili hili lilipitisha vilevile kwa Serikali kung’ang’ania wakati Wabunge wanashauri, Bunge likapitisha tena kwa maana ya watalii kutozwa VAT katika huduma ambazo wanazozitoa. Kila mwaka, mwaka unapita, ndipo tunapokuja kufanya mabadiliko, huku watu na kodi zimeshapotea.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Upendo Peneza, kuna taarifa. Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani.

T A A R I F A

MHE. UPENDO PENDEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la bandari mwaka mmoja baadaye tukafanya marekebisho, suala la Utalii mwaka mmoja baadaye tukafanya marekebisho, mapato tumeshapoteza na leo kwenye suala la wachimbaji wadogo miaka miwili baadaye. Watu wa Geita ni kati ya watu ambao wamewekwa ndani kwa sababu utoroshaji wa madini. Ni kwa sababu wakipiga mahesabu, wakifanya shughuli zao za uchimbaji mpaka wakauze, faida hawaioni. Kwa hiyo, naongea kwa sababu sehemu ya wananchi waliopo Geita ndio waliokamatwa kutokana na kadhia hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala ambalo nchi inabidi ifanye ni suala la kuzingatia ushauri kwa muda, ni suala la muda, kwa sababu katika utawala hakuna kujaribu, ndio maana nadhani hata Urais mwenye sifa anayegombea miaka 40, la sivyo wangeruhusu vijana wenye miaka 18 au 25, hata Tume ya Jaji Warioba walikataa kwa sababu tunategemea watu wanaotuongoza ni watu wenye experience, ni watu ambao wapo tayari kusikiliza ushauri wa watu, watu walioko tayari kuangalia impact kabla ya kufanya maamuzi ambayo tunaendelea kuyafanya ndani ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Geita watu wengine wanaopata leseni ni watu wanaopata leseni za uchenjuaji ambayo kwa Kiingereza wanasema processing and smelting, ni watu ambao wanachukua mchanga ambao umeshafanyiwa kazi na mtu mwingine, anauchukua anauozesha kwenye sumu aina cyanide na mercury kwa ajili ya kupata dhahabu tena. Watu hawa wanaofanya shughuli za uchenjuaji wana tozo nyingi sana zinazowakabili. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia na ningependa zaidi kujikita katika suala la mrundikano wa mahabusu ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu ambazo zipo ndani ya nchi yetu, kwa hali ya magereza ni kwamba katika watu wote ambao wapo magereza/mahabusu ni asilimia 53.3. Pamoja na hayo pia tuna sheria ndani ya nchi hii ambazo ni kandamizi na zenyewe pia zinachangia kuongeza idadi ya mahabusu hao ndani ya magereza yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano ni Sheria ya Money Laundering na hizi za Uhujumu Uchumi ambazo zimewekwa na hazimpatii mtuhumiwa dhamana anapokuwa amekwishashtakiwa. Sasa suala linalokuja ni kwamba, sheria hii sasa inatumika kuweza kuwaonea na kukandamiza watu na inawezekana hata baadaye ikatumika hata kuwaumiza watu kisiasa kwa sababu namna bora ya kuwaondoa watu katika maeneo ya nchi yao na kuwa huru ni kumpa mtu kesi ya money laundering. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mfano wa kesi ambazo zinaendelea, kesi inaendelea kwa miaka minne, miaka mitano hakuna usikilizwaji wa msingi unaoendelea hata upelelezi wenyewe haujakamilika. Sasa umempeleka mtu mahakamani kwa sababu gani kama upelelezi haujakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba tunahitaji kuwa na utashi wa kisiasa kati ya Ofisi ya DPP, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mahakama zetu ili hatimaye kuweza kuondoa hili tatizo. Kwa hilo, naiomba Serikali sasa iweze kuleta mabadiliko ndani ya Bunge hili, tuweze kubadilisha sheria hizo za Money Laundering ili tuache kuwaonea Watanzania, tuache kuwaonea watu ambao wanafanya kazi zao ndani ya nchi hii, kama mtu ana kesi, basi tutafute namna bora ya lawama hizi zisiweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna bora ambayo nadhani inaweza ikasaidia ni pamoja na kuwa na muda maalum wa kesi hizi kufanyika, hakuna muda ambao umewekwa kisheria. Tuwe na mfano, kama sheria zile za uchaguzi ambazo zina muda maalum kwamba kesi hii iishe ndani ya muda Fulani. Kwa hiyo kama kesi humpi mtu dhamana, angalau basi uweke kwamba itakwisha ndani ya miaka miwili au mitatu, huyo mtu awe ameshaondoka na tatizo hilo liishe, kama mtu anafungwa ama kama mtu huyo anaachiwa huru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niweze kuchangia katika suala linalotuhusu sisi Wabunge wa Viti Maalum. Wabunge wa Viti Maalum tupo ndani ya Bunge kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 66. Hata hivyo, kuna kitu kibaya ambacho kinaendelea ndani ya nchi hii, kilianza ndani ya Bunge hili Tukufu lakini na viongozi wengi wanaokaa ndani ya Meza wamekuwa ni watu ambao wanakemea tabia hiyo ya kipuuzi, naomba niite hivyo, lakini sasa tabia hiyo inaendelea huko nje ambapo Mheshimiwa Humphrey Polepole, Katibu Mwenezi wa CCM, amesimama na kusema Wabunge wa Viti Maalum wa CHADEMA wanapatikana mpaka wapitiwe na Mwenyekiti wao. Sasa ifike mahali tutambue kwamba huo ni udhalilishaji ambao hauruhusiwi hata na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Polepole amekuwa anafanya kazi kwenye asasi za Kiserikali kwa muda mrefu, sasa kama hatambui haki hizo za kimsingi ambazo zinatolewa hata na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni aibu kwa Chama cha Mapinduzi kuwa na Mwenezi anayedhalilisha wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo naiomba…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo…

MWENYEKITI: Ehe, hebu subiri, taarifa Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba amesema Katibu Mwenezi wa Chama, Humphrey Polepole ametamka kwamba Wabunge wa Viti Maalum wa CHADEMA wanapitiwa na Mwenyekiti wao. Sasa neno kupitiwa hatujaelewa labda atoe ufafanuzi.

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho naomba niseme ni kwamba ifike mahali nafasi za watu na vyeo walivyonavyo viheshimiwe. Ni aibu kwa kiongozi wa nchi hii kusimama na kusema kwamba mafanikio ya mwanamke ya kisiasa yanatokana na shughuli za kingono. Tunawajengea watoto wetu fikra mbaya ndani ya vichwa vyao kwamba hakuna tena jitihada, jibu pekee ni waende wakalalane na watu huko watapata nafasi. Sasa hatuwezi tukaruhusu kuwa na viongozi wa namna hiyo. Kitu ninachokiomba sasa ifike mahali tuiombe Wizara na Serikali utaratibu halisi wa upatikanaji wa Viti Maalum ujulikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, huu uchungu unaokuja sasa unajengeka na matusi ya namna hii…

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. UPENDO F. PENEZA: …ifahamike kwamba sasa tunahitaji mabadiliko ya Katiba kwa ajili tu…

MBUNGE FULANI: Taarifa ya ufafanuzi.

MWENYEKITI: Sitaki taarifa sasa.

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba tunahitaji pia mabadiliko ya Katiba ya nchi hii kwa ajili pia ya heshima ya mwanamke. Sasa ifike wakati Katiba iandike kwamba wanawake wakagombee, hata kama ni viti vya wanawake.

Mfano nchini Uganda, kuna viti vya wanawake lakini wanapigiwa kura na wananchi, inayotoa hata nafasi ya accountability, wananchi kuweza kumwajibisha Mbunge ambaye analipwa kwa kodi zao na Mfuko wa Jimbo wanapewa lakini… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii ya kuweza kuchangia. Nachukua fursa hii kutoa shukrani zangu za pekee kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kauli aliyoitoa kwamba uchaguzi mwaka huu utakuwa ni wa huru na haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuzungumza hilo, naomba pia nikumbushe kwamba Mheshimiwa Rais huyo aliyetoa kauli hiyo ndio Mheshimiwa Rais pia liyesema kwamba atamshangaa Mkurugenzi ambaye amemchagua yeye atakayetangaza mtu wa Upinzani kwamba ameshinda kwenye eneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya kauli hizi; hiyo ya kwanza kuhusu Wakurugenzi aliitamka zamani kidogo na hii ametamka siku za hivi karibuni. Nategemea kwamba inawezekana kuna badiliko kidogo Mungu ametusaidia. Kama hivyo ndivyo, basi tunamwomba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tufanye mabadiliko kwenye Sheria ya Tume ya Uchaguzi ili kuwaondoa Wakurugenzi hawa ambazo alishawaambia kauli ya kwanza, maana yake itakuwa ni mchanganyiko kidogo. Ulishamwambia mara ya kwana asitangaze, halafu sasa hivi ukimwambia ni huru na haki inaweza isieleweke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri tukabadilisha sheria hizi tuweze kuwaondoa na hatimaye tupate wasimamizi wa uchaguzi ambao watu wa Upinzani na wa Chama Tawala watakuwa huru na itaweza kutusaidia kutoka pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili pia linawaathiri wananchi, kwa sababu kama Mbunge wa CCM ana uhakika kwamba kwa vyovyote vile atatangazwa, kuna maana gani hata kurudi kwa wananchi kufanya kazi? Kikubwa zaidi utakuwa unaenda kwenye Chama chako kujitahidi kutengeneza mambo vizuri, basi. Kwamba nikishashinda kwenye kura za maoni, imetosha huku kwingine nitaibiwa halafu mambo yataenda. Hakuna maana kupinga ufisadi kama unahimiza wizi wa kura. Kwa hiyo, ninaomba sana kwamba hilo liweze kuzingatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna suala zima la suala la Daftari la Wapiga Kura. Daftari hili limeanza kuandikisha na muda umeenda kidogo. Katika maeneo mengi ambayo uandikishaji umefanyika, imekuwa ni zoezi ambalo siyo rafiki, limekuwa ni zoezi ambalo Serikali haitumii muda kuhimiza wananchi kwenda kujiandikisha na taarifa kutoka kwa wakati. Pia vingine ni kwamba daftari limekuwa likigongana na uandikishaji wakati wa Serikali za Mitaa. Daftari limekuwa likigongana pamoja na uandikishaji wa NIDA. Kwa hiyo, unakuta wananchi wamekuwa wakipata mgongano katika kujiandikisha kwenye daftari hilo la wapiga kura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachohitaji sasa, sheria inasema kwamba uandikishwaji ufanyike mara mbili kabla ya Uchaguzi Mkuu. Hii imefanyika mara moja na leo ni mwezi wa pili sasa. Tunajiangalia: Je, nchi nzima na ukubwa wake tutafanikiwa kuweza kuandikisha kwa ukubwa huo ambao tunahitaji ili kutimiza matakwa ya kisheria ya kuandikisha mara mbili kabla ya kufika kwenye Uchaguzi Mkuu ili wananchi wote wapate fursa ya kuweza kujiandikisha na kuweza kupigia kura viongozi wao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho lazima tuone ni Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ni uchaguzi ambao umefanya dhuluma kubwa sana. Tuna Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ambao hawahitajiki. Hata hivyo, hili suala limetoa funzo tena kubwa sana. Mkurugenzi anafanya wizi; hapokei fomu za watu, anachafua fomu za Wagombea katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, somo ambalo limepatikana ni kwamba tunapoenda kwenye uchaguzi Mkuu, pamoja na kutafuta hela za kampeni, sasa tunamdhibiti vipi Mkurugenzi? Suala sasa ni kwamba tunamdhibiti vipi Mkurugenzi? Fomu zipokelewe, zibandikwe kama inavyohitajika na uchaguzi uweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hali inavyoenda ni fujo kubwa itakayotokea ndani ya nchi hii, ni mauaji makubwa ambayo yatatokea nchi hii, watu hawatakubali haki yao iendelee kunyang‟anywa mwaka hadi mwaka. Kwa sababu hiyo basi, Mheshimiwa Mbowe ametumia busara sana, ni Mwenyekiti wangu wa Chama, namheshimu na pia Mungu amembariki hekima ya ajabu sana. Alipokuwa kwenye Mkutano wa Uhuru Mwanza tarehe 9 Desemba alisema kwamba ifike mahali nchi tufikie maridhiano, tuzungumze, tuondoe changamoto tulizonazo ili kuepusha maafa makubwa ambayo yanaweza kutokea ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana ameweka msisitizo kwamba anamaanisha ombi la maridhiano. Jana ametoa press conference ambayo imeandika barua na vitu gani ambavyo tunahitaji kubadilisha. Sasa mara nyingi katika nchi nyingine maridhiano yanafanyika baada ya watu kuuana, baada ya watu kukatana mapanga ndiyo watu wanakaa kwenye meza kuzungumza kwamba kila mtu ameshaonesha ubabe wake, sasa watu wanazidi kufa, sasa tukae chini tuzungumze mambo yaende. Sasa yeye ametumia busara kwamba tuzungumze kwanza kabla maafa hayajatokea. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa busara hiyo basi, ninaomba Mheshimiwa Rais atumie busara aliyonayo tukae chini tuzungumze, tubadilishe yanayowezekana, twende mbele…

MBUNGE FULANI: Kaa chini kelele wewe!

MWENYEKITI: Mheshimiwa Upendo malizia.

MHE. UPENDO F. PENEZA: …na tufanye uchaguzi wa haki ili hii amani tunayohitaji ndani ya nchi hii iweze kudumu.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kitendo cha uzalendo zaidi ya kuitakia nchi yako amani na maridhiano na kuomba maridhiano ni kitendo cha uzalendo mkubwa sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Upendo muda wako umeisha.

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi/Vigelegele)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. UPENDO F. PENEZA: Ahsante Mheshimiwa Spika, na nina mshukuru mungu kwa kunipatia fursa hii kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Nishati. Kama ambavyo umekwisha sikia wachangiaji wengine waliotangulia ni kwamba Bunge lako Tukufu ama Wabunge ambao wako ndani ya Bunge hili wana-concerns zao katika vitu viwili. Kuna concern ya kwanza kwa maana ya gharama, na kuna concern ya pili kwa maana ya mambo ya kimazingira yanayozunguka mradi huu wa Stiegler’s Gorge.

Mheshimiwa Spika, lakini katika suala zima la gharama leo tumeambiwa na Serikali na tumekuwa tumeambiwa tangu bajeti iliyopita kwamba mradi huu utagharimu trilioni 6.5. Lakini ukiangalia katika namna ambavyo Serikali imekuwa ikitoa hela mpaka sasa, ni dhahiri kwamba mradi huu hauwezi kuisha kwa miaka mitatu kama ambavyo Serikali inatuambia na kama haitaweza kuisha kwa muda wa miaka mitatu, maana yake ni kwamba tutalipa hela zaidi, tutalipa hela zaidi na hatimaye inawezekana tukafika hata kwenye gharama tunazoambiwa za trilioni 22.9.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti iliyopita Serikali ilitenga bilioni 700 lakini mpaka tuna.. kwa maana mpaka mwezi Desemba ulikuwa umetoa mia mbili sabini na kitu baadaye wamemalizia hizo bilioni 688 ambazo na bado hawajamalizia kwa maana ya kumlipa mkandarasi wa anayejenga huo mradi wa Stiegler’s Gorge. Na sasa hivi tumetoa trilioni 1.4 maana yake ni kwamba kama Serikali inakusudia kwamba tumalize huu mradi kwa miaka mitatu, ni kwamba ingekuwa inatoa zaidi ya trilioni 2 kila mwaka, ili kuhakikisha kwamba mradi huu unaweza kuisha kwa hiyo miaka mitatu ambayo imetengwa.

Mheshimiwa Spika, lakini zaidi ya yote ni kwamba leo tunazungumza gharama ya trilioni 6.5 kwa kujenga mradi mmoja. Mradi ambao ukiangalia kimazingira, watu wanaonesha concern kubwa na hata kama ukiuangalia mradi huu wenyewe je tukimaliza kujenga maji yatajaa kwa kutumia miaka mingapi ndani ya dam ili kuhakikisha kwamba huo umeme unaweza kupatikana.

Mheshimiwa Spika, tumeambiwa kwamba itatumia takriban miaka 10 ili dam hiyo iweze kujaa maji na hatimaye kuzalisha umeme, kwahiyo mpaka kupata umeme huo wa megawatt 2100, itatumia takriban miaka 27. Sasa kwa namna hiyo maana yake ni kwamba tunatumia hela nyingi kujenga kitu ambacho hatutapata matokeo ya haraka kama ambavyo tunategemea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, leo tunawaaminisha watanzania kwa kiasi kikubwa sana kwamba huu mradi ukiisha tutapata megawatt 2100 kitu ambacho si kweli. Lakini hata ukiangalia miradi ambayo imekwishaendelea ambayo inatumia maji kuna miradi ya Kihansi na hapo Mtera mpaka leo hii hakuna hata asilimia 40 ya uzalishaji unaoendelea katika maeneo hayo. Kwa hiyo, kama mifano tuliyonayo leo haitoi picha halisi mnatuambia vipi, kwa huo mradi ambao mnasema kwamba baada ya miaka mitatu utafika huko. Maana yake ni kwamba inawezekana tunataka tutengeneze historia kwamba awamu hii ilijenga huo mradi tukatelekeza vingine na ni uharibifu wa hela kama hatuwezi tukapata matokeo ya haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia vile vile tumeongelea suala zima la gesi na kuna pia vyanzo vingine ambavyo watu wamesema mix energy lakini katika hilo suala ukiangalia katika bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri ameiwakilisha hapa tuna miradi ya jua, tuna miradi ya upepo, tuna miradi ya maji hata katika maeneo mengine yote hii hiyo hela ya trilioni 6.5 kama ingegawiwa kwenye hiyo miradi midogo midogo tungepata zaidi ya hizo megawatt 2100 tena kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na zaidi ya hapo ni kwamba kama mradi wa umeme ungetengenezwa katika eneo moja usambazaji ungefanyika na hizo megawatt kuingizwa katika megawatt kuingizwa katika grid ya Taifa hata usafirishaji wa umeme kwenda kwa umbali mrefu kusingekuwa na upotevu wa umeme kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, tungeweza kuzalisha umeme wananchi wakapata umeme katika maeneo mbalimbali kwa kutumia hizo hizo trilioni 6.5 lakini kwa kuangalia au kuvipa vipaumbele miradi ambayo Serikali yenyewe imeweka kuna miradi ya maji, kuna miradi ya umeme, kuna miradi ya upepo ambayo Serikali sasa inaitupa pembeni na ukiangalia katika bajeti nzima ya maendeleo Serikali imetenga trilioni 2.1, trilioni 1.4 yote inatumika kwenye mradi wa Stiegler’s tunabakiza bilioni 68 tu itumike katika miradi mingine na kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali kitu ambacho hakitupi picha halisi ya Serikali kutaka kuifanya Tanzania hii, Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia ninaomba nizungumzie kuhusu suala la gesi. Naomba nizungumzie suala la gesi Tanzania ni katika nchi ambayo imekubali kufanya uvunaji wake wa gesi katika njia ya production sharing. Kwamba Kampuni ya TPDC inaingia pamoja na hawa wawekezaji na kuna mgawanyo kwa maana ya pesa ya ku-invest lakini pia kuna kugawana baadaye baada ya kuivuna hiyo gesi yenyewe. Lakini pamoja na matatizo yote ambayo TPDC wanayo ukosefu wa hela ya kuwawezesha wao kufanya utafiti na vitu mbalimbali lakini bado wanaweza kupata mgao wa gesi kupitia hii production sharing agreement.

Mheshimiwa Spika, sasa tulipitisha hapa sheria ndani ya Bunge mwaka 2017 sheria ambazo zimefanya wawekezaji ambao wako katika upande wa gesi kukimbia na leo hii hatuna uzalishaji mkubwa katika upande wa gesi, gesi ni kama vile imelala sasa. Lakini katika Bunge lililopita, Bunge hili lilikaa na tukapitia upya vipengele ambavyo vilikuwa vinawakandamiza wale wachimbaji wadogo wadogo na tukasahihisha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natumia muda huu kukuomba kwamba kamati inayohusika na mambo ya madini na nishati, iweze kukaa pamoja na Serikali pamoja na hawa wawekezaji kujadili ni changamoto gani ambazo zipo katika hizo sheria na hatimaye tutoke na njia moja ya kuweza kusahihisha mapungufu yaliyopo ili tupate njia ya kwamba tupate gesi, huku na miradi mingine inaendelea ili kuhakikisha tunapata hiyo mix energy production katika nchi hii kama ambavyo imekuwa ikisemwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haitaleta maana kama nchi imetumia takriban trilioni 3 kujenga bomba leo hii halina faida kwa nchi ni asilimia 6 tu haileti faida wala haileti value for money, kwa hiyo ni bora tukaboresha hizi sheria tukawekeza tukapata gesi na uzalishaji wa umeme pamoja na matumizi mbalimbali ya gesi yakaweza kuendelea ndani ya nchi hii.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni kwenye upande wa REA, kamati imetuonesha changamoto ambazo zipo katika mradi wa REA kwamba kuna ucheleweshwaji wa Serikali kutoa hela, kwa hiyo mnachelewesha katika huduma hizi za umeme wa REA kufanya kazi na huduma mbalimbali katika maeneo hayo, na hatimaye inazalisha ongezeko la pesa kwa maana ya hii mikataba wale contractors wanadai hela nyingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, lakini zaidi ya hapo pia hata wale contractors wenyewe wale waliofanya hizo kazi, na wenyewe pia wapo wanaochelewesha kazi hizo ni vizuri sasa Serikali ikaunda kitengo maalum cha monitoring and evaluation kwa ajili ya kazi hii tu ya umeme wa REA kuhakikisha ya kwamba wanaweza kuwasukuma wale contractors waliowapa kazi lakini na wenyewe pia waweze kutoa hela kwa wakati na kuwapa mikataba kwa wakati kuhakikisha kwamba miradi hii inaweze ikafanya kazi.

Mheshimiwa Spika, na kwenye hilo kwangu kwa upande wa Geita Serikali ilituahidi kutupa umeme kwa kupitia njia ya REA katika maeneo ambayo yanaitwa ni mitaa lakini kihalisia ni kama vile vijiji sasa tunaiomba Serikali iweze kutukumbuka katika Kata za Ihanamilo, Kata za Shiloleli, Kata za Bungw’ang’oko na maeneo mengine yote kuhakikisha kwamba umeme unaweza ukapatikana na ripoti ya kamati imeonesha kwamba Geita iko chini ya asilimia 40 na sisi tunahitaji umeme katika maeneo hayo kwa hiyo, tunaomba walau tuweze kupata umeme kupitia njia hii ya REA. Ahsante sana nashukuru. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami pia napenda nichukue fursa hii nichangie katika Muswada huu wa Upatikanaji wa Taarifa. Napenda nianzie katika section 6(1)(f) ambacho kinazungumzia infringe commercial interest.
Napenda kuishauri Serikali kwamba hapa hatujapata maelezo kamili ya kujua hizi commercial interest ni zipi kwa maana ya kwamba kuna taarifa ambazo zinaweza zikawa zinahitajika hasa katika maeneo ya mikataba ambayo nchi inakuwa imeingia na wawekezaji. Sasa kama tukisema na hizi pia ziko katika kile kipengele cha taarifa ambazo haziwezi zikapatikana, maana yake ni kwamba haya ni mambo pia yanayowagusa wananchi moja kwa moja na ni sehemu pia ya public interest.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia pia sehemu hiyo ya sub section 6(6) ambayo inazungumzia any person who discloses exempt information withheld by the public authority in controversion of this Act commit an offence and shall, on conviction, be liable to imprisonment for a term not less than 15 years.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kipengele hiki nilikuwa napendekeza ya kwamba maeneo haya mengine ya juu ambapo ukianzia kwenye sub-section (2) ambayo inazungumzia maeneo ya National Security, nilikuwa napendekeza kwamba hii adhabu au hiki kipengele kizungumzie yale mambo ambayo yako chini tu ya mambo ya National Security, lakini mambo ambayo yako juu, ambayo siyo mambo ya National Security, hayo basi tuyaache kwa sababu taarifa nyingine inaweza ikatoka chini ya hicho kipengele cha public interest.
Mheshimiwa mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia katika kipengele kingine cha (a), (b), (c), (d) na mengineyo, unaona kwamba kuna taarifa ambazo zinaweza zikatoka ambazo zinaweza zisiguse moja kwa moja usalama wa Taifa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba hiyo adhabu ibaki kwa yale maeneo tu ambayo yanazungumzia mambo ya National Security.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna kipengele cha 16 ambacho kinazungumzia; “The information holder may be defer the provision of access to information until the happening of a particular event including the taking of some action required by law or some administrative action or until the expiration of a specified time, what is reasonable to do so in the public interest or having regard to normal and proper administration practices.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuangalia hiki kifungu katika hii section ya 16, kitu ambacho kinaonekana hapa ni kwamba kwa hiki kifungu maana yake ni kwamba taarifa zozote zile hazitaweza kupatikana kwa sababu taasisi husika inaweza ikaamua kunyima zile taarifa kwa kisingizio cha public interest, lakini hii public interest tunai-define kwa muktadha upi ili angalau tuhakikishe wananchi hawawezi wakanyimwa taarifa?
Mhesimiwa Mwenyekiti, tukiiacha kama hivi na tukaipitisha, sheria hii na hii section ya 16 tukaiacha kama ilivyo, maana yake ni kwamba tunasema kwamba sheria tumeandika kama sheria ambayo inaruhusu mambo ya transparency, lakini kimsingi ni kwamba tunavunja. Tunatambua ya kwamba mambo ya uwazi na uwajibikaji ni sehemu ya msingi katika demokrasia na ni mambo muhimu pia katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika hiki kipengele cha 16, kama hatutaweza kukifanyia kazi, maana yake ni kwamba tutakuwa tumetimiza matakwa ya Kimataifa ya kututaka Tanzania pia tupitishe sheria hii ambayo inahusiana na mambo ya utoaji wa taarifa, lakini kama nchi hatutaweza kutekeleza haki ya Kikatiba ya wananchi katika kuhakikisha kwamba wanapata sheria. Kwa hiyo, naomba tu nitoe ushauri kwa Serikali ili kuweza kuona namna gani hiki kitu kinaweza kikaangaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni vyema tukafahamu ndani ya hili Bunge kwamba vyama vya siasa au upinzani kwa ujumla wake tusiuchukulie tu kwamba ni chama mbadala ambacho kiko tayari kusubiria nafasi ya kuweza kutawala, lakini tuchukulie kwamba ni sehemu pia ya kuwa wawajibishaji ndani ya nchi hii. Kwa hiyo, kama tunataka uwajibishwaji uweze kuwepo ndani ya nchi hii, lazima pia masuala ya uwazi yaweze kuwepo. Tunavyopitisha hii sheria tuangalie hicho kipengele, lakini pia tuangalie masuala mengine ambayo kama Serikali yamekuwa yakifungwa katika hilo suala zima la uwajibishwaji na upatikanaji wa taarifa, hasa kwa kuzingatia kwamba tulivyokuwa tunaanza hili Bunge, Serikali ilitangaza kuondoa Bunge la moja kwa moja la wananchi kutizama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba tumeifunga haki hiyo, leo tunapitisha hii sheria ambayo hatujui kiukweli kama hiki kipengele cha 16 kitabaki kama wananchi wataweza kupata hata hizi taarifa ambazo zimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapopata taarifa maana yake ni kwamba uweze kuwajibisha ofisi husika, maana yake ni kwamba uweze kupata majibu kutoka Serikalini. Nina imani kwamba vyama vya upinzani vina wajibu huo na hivyo Sheria ya Vyama vya Siasa naomba pia Serikali, viongozi walioko hapa, Mawaziri, waweze kumshauri Mheshimiwa Rais vyema kwamba ni bora kutii sheria za nchi zilizopo kwa sababu zimetungwa na Bunge hili. Kama tunaona ya kwamba sheria hazifai, basi ni vizuri pia Serikali ikaleta marekebisho ya hizo Sheria za Vyama vya Siasa ili tuweze kuziangalia na kuzibadilisha na kuweza kuondoa watu kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mlinga ametoa ushauri, tunamchukulia ni mtu wa masihara, lakini kuna vitu alivyoviongea vya msingi. Kwa hiyo, tuombe pia Serikali iweze kumshauri Mheshimiwa Rais kuweza kuitii Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo iliyomchagua, ndiyo iliyomweka madarakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mwalimu Nyerere mwenyewe aliweza kutamka katika hotuba yake akiwahutubia wananchi wa Tanzania kwamba Watanzania wasiruhusu kwa gharama yoyote ile mtu atakayeongoza kutoka kichwani mwake, lakini tuweze kuheshimu viongozi walioapa kwa Katiba na walio tayari kuilinda Katiba na wananchi wote tuweze kuwataka viongozi wetu kuweza kusimamia Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo siyo maneno yangu, ni maneno ya mtangulizi wetu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ambaye anaheshimika na kila mmoja wetu. Ahsanteni sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.8) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kabla sijaendelea na mchango wangu ningependa kuleta ombi katika meza yako ambalo pia litawakilishwa kwa Mheshimiwa Spika, kwamba tunakuwa kwenye Kamati zetu lakini kwa bahati mbaya kamati pekee ambayo inachukua rekodi ya mambo ambayo yamezungumzwa kwenye Kamati ni Kamati ya Bajeti peke yake. Kamati nyingine hakuna rekodi ya kazi ambazo zimefanyika kwenye Kamati na ni rahisi hata humu ndani kuingia na hata Serikali kutokukubaliana na vitu kwenda tofauti kwa sababu hatuna maandishi kimsingi ambayo yanatunza rekodi pamoja na michango ya Wabunge kupitia ndani ya Kamati zao. Nasema tu hivyo ili tulinde na tuweze kusaidia zaidi wananchi kwamba Kamati ilifanya nini na Serikali imeleta nini ili kuweza kutoa mwongozo katika majadiliano mbalimbali ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuomba kwamba Mheshimiwa AG yuko hapo na amesikiliza watu ambao tunatoka Kanda ya Ziwa jinsi gani ambavyo sheria hii ambayo inawagusa wavuvi, ni namna gani ambavyo siyo rafiki kwa wavuvi ambao ni watu wa chini, ni watu wadogo katika maeneo yetu. Sheria hii pia siyo hata rafiki kwa halmashauri zetu ambazo tunatoka kwa maana halisi ya kimapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo basi, unaona kabisa kuna ukinzani mkubwa katika sheria ambayo imeundwa. Unaniambia kwamba Waziri anayehusika na Uvuvi akasimamishe kazi watu ambao watu wako TAMISEMI, watu wasiomhusu, watu ambao hakuwaajiri, watu ambao hawasimamii, watu ambao hawana namna nyingine tu kukutana nao unamsimamisha mtu halafu unatoa taarifa kwa Waziri wa TAMISEMI ili amfanye nini sasa! Ampime aonekane vipi au baadaye akimrudisha kazini inakuwaje! Kwa hiyo, kimsingi bado kuna nafasi AG labda anaweza akaona namna kwamba anaweza akaamua hiyo aka- withdraw bado hatujachelewa kabla hatujafika mwisho kabisa kwa maana ya hii sheria kupitishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee katika upande wa mabadiliko yaliyokuja katika tasnia ya wataalam wetu wanasheria. Kama ambavyo mnafahamu kwamba tuna vyama mbalimbali, tuna Vyama vya Madaktari, tuna Vyama vya Wauguzi, tuna vyama mbalimbali ndani ya nchi yetu. Lakini mkazo mkubwa sana na Serikali inauleta katika Chama cha Wanasheria na imekuwa ni kazi sasa ya Serikali nadhani kwa sasa ni kama miaka mitatu au minne iliyopita tangu Mheshimiwa Tundu Lissu alivyogombea, imekuwa ni kama ni chombo ambacho kinaangaliwa na Serikali kwa jicho lingine. Kama ni chombo ambacho kinaikosoa Serikali, kama ni chombo ambacho kinaweza kikaleta sura tofauti wanapokuwa waki-deal na Serikali. Kabla hatujafikiria kubadilisha uwakilishi wa wanasheria katika kupiga kura na kuchagua viongozi wao tuwaangalie katika majukumu ambayo chama hiki kimepewa kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majukumu ambayo kimepewa kisheria yanasema chama hiki kina wajibu wa kisheria wa kulinda na kusaidia jamii katika masuala ya kisheria. Kwa hiyo, si kosa Mwenyekiti wa TLS akizungumzia uvunjwaji wa haki za binadamu ndani ya nchi hii. Si kosa Mwenyekiti wa TLS akizungumza kwamba Tanzania tuna uchaguzi ambao siyo huru, si kosa Mwenyekiti au kiongozi wa TLS akizungumza kuhusu mauaji au shida mbalimbali ndani ya nchi hii, si kosa. Si kosa kwa sababu ni wajibu anaopewa yeye ndani ya sheria ambayo imeweka TLS katika nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kusema kwamba sasa viongozi watakuwa wanachaguliwa ni watu ambao wametoka kwenye chapters, tukiangalia hizi chapters wanachaguana vipi, chapter ni kitu gani, hii kanda ni kitu gani, inaundwa na watu gani ambao hasa ndio wanaokuja kuwa hao viongozi ambao wanaenda kuwachagua viongozi kule juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikiangalia mfano Geita wale wanasheria iwe ni kumi, kumi na tano wataungana na sehemu nyingine, wanasheria wengi wako Dar es Salaam. Hiyo kanda tunaziundaje na uwakilishi wa maana tunaupata namna gani vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanaosema hata CCM na CHADEMA watu hatuji kote, lakini tunasahau kwamba hivi ni vyama vikubwa. Tunaanzia ngazi ya matawi, wanachama wanachagua, tunaenda ngazi ya kata viongozi wanachagua, tunaenda mpaka ngazi ya Taifa. Hizi ni chaguzi za kanda ambazo hazitakuwa na grassroot levels, hazina grassroot levels unazifananishaje na chama cha siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nashawishika kusema kwamba, umefika wakati nchi hii haipendi mambo mazuri, umefika wakati nchi hii tunaharibu vitu vizuri ambavyo vipo, hatutaki sauti tofauti, hatutaki sauti ya kuwatetea wananchi, ndiyo maana tunataka kuharibu mpaka uongozi unaotengeneza hiyo TLS. Kwa hiyo, hebu tuwe watu wa tofauti kidogo tuangalie na kwenye Kamati ya AG walitusomea kwamba wanabadilisha TLS kwa sababu ya mambo ya kimaadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni watu wazima, mimi nina zaidi ya miaka 18, humu Bungeni tunajuana vizuri, hivi utasema Upendo nisiwe mbunge kwa sababu ya suala la kimaadili! Haiingii akilini tusije Dodoma kwa sababu ya masuala ya kimaadili, haiingii akilini, kwa sababu ya gharama hawa ni watu wanaokutana kwa fedha zao, wanalipa na michango wenyewe, mnasema kuna gharama. Tena kibaya zaidi ni kwamba tukiwachagua kwenye chapters itabidi wale viongozi sasa walipiwe nauli ili waende wakakae kama ni watu 300, watu 500 then wachague uongozi ambao unahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana kwamba tufanye utaratibu ambao… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Upendo kwa mchango wako na ushauri wako.