Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Susanne Peter Maselle (10 total)

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. SUSANNE P. MASELLE) aliuliza:-
Mwaka 2007 Serikali ilipima viwanja vya Luchelele Wilayani Nyamagana, Mwanza na iliendelea na mpango huo ambapo mwaka 2012 ilifanya tathmini na uhakiki kwa ajili ya kulipa fidia lakini hadi leo wananchi hao hawajawahi kulipwa fidia zao.
Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wananchi hao wa Luchelele kuhusu hatma yao hasa ikizingatiwa kuwa Waziri wa Ardhi alitoa ahadi mwaka 2015 kuwa atalitatua tatizo hili ndani ya mwezi mmoja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susanne Peter Maselle, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Luchelele lilipimwa mwaka 2008 likiwa na ukubwa wa hekta 873.38 ambapo viwanja vilivyopimwa ni 3,583. Katika zoezi hilo wapo wananchi waliokuwa ni wamiliki wa asili wa eneo hilo wapatao 683 ambao kwa makubaliano maalum yaliyofanyika tarehe 27/01/2013 chini ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, wamemilikishwa viwanja badala ya fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanaodai fidia katika eneo la Luchelele ni wale ambao walikutwa katika maeneo yao lakini baada ya upimaji, maeneo hayo ni kwa ajili ya Taasisi au barabara na idadi yao ni 671. Wananachi hao wanadai fidia ya shilingi bilioni sita. Kauli ya Serikali ni kwamba wananchi hao watalipwa fidia na tayari Halmashauri imeomba mkopo kutoka Benki ya CRDB ambao wamekubali kutoa mkopo huo ili wananchi hao waweze kulipwa fidia
MHE. SUSANNE P. MASELLE aliuliza:-
(a) Je, Serikali imechukua juhudi gani za makusudi kudhibiti vitendo vya kubambikizia watu kesi vinavyofanywa na baadhi ya askari wasiokuwa na maadili?
(b) Je, Serikali itakuwa tayari kuanzisha kitengo cha siri ndani ya Jeshi la Polisi kitakachoshughulikia adha hii?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susanne Maselle, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni, miongozo pamoja na taratibu na wale wanaobainika kukiuka maadili ya Jeshi, huchukuliwa hatua kwa kuwashitaki kijeshi kwa mujibu wa PGO 103 na 104 kwa kuwapa adhabu mbalimbali ikiwepo kuwafukuza kazi anaobainika kukiuka maadili ya Jeshi ikiwemo kubambikia watu kesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imefanya jitihada za kuanzisha Kitengo cha Malalamiko katika ngazi ya Makao Makuu, Mikoa na hata Wizara ili kutoa mwanya kwa mtu yeyote anayeona kuwa ameonewa, kuwasilisha malalamiko yake na malalamiko hayo kushughulikiwa. Hata hivyo, raia wanayo haki ya kulalamika katika vyombo vingine vya kisheria wanapoona hawatendewi haki kwa mujibu wa sheria za nchi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi limeweka wazi utaratibu wa namna ya kuwashughulikia askari wasio waaminifu, hivyo halitakuwa tayari kuanzisha kitengo cha siri kwa kazi hiyo kwani utaratibu uliopo unashuhudia na umekuwa na mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, siku za usoni kama hivyo ilivyo kwa mikoa michache hapa nchini ambapo kazi ya polisi itabaki kuwa ni ya kupeleleza kesi na mwenye mamlaka ya kupeleka kesi mahakamani ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali. (Makofi)
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA (K.n.y. MHE. SUSANE P. MASELLE) aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali imewanyang’anya ajira vijana waliokuwa wamejiajiri kwenye Machimbo ya Ishokelahela na baadaye ikaamua kubadili umiliki wa leseni kwa siri?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susane Peter Maselle, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji wadogo waliokuwa wanachimba Ishokelahela hawakuwa na leseni ya uchimbaji bali walikuwa wanachimba katika eneo la utafiti la leseni ya Kampuni ya Carlton Kitongo Tanzania Limited.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mwaka 2014, Serikali ilifanya mazungumzo na kampuni hiyo na kuwapatia wachimbaji wadogo hao leseni mbili za uchimbaji zenye jumla ya hekta 20. Wananchi hao waliweza kuunda kampuni yao inaitwa Isinka Federation Miners Co-operative Limited.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 kikundi kiliamua kubadilisha leseni zake mbili za uchimbaji mdogo na kuzifanya kuwa leseni moja ya mgodi wa uchimbaji wa kati lakini chini ya Kampuni yao ya Isinka Federation Miners Co-operative Limited. Umiliki wa leseni hizo haujabadilishwa hadi leo upo chini ya umiliki wa wachimbaji hao wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Machi, 2017, mgodi ulikuwa umeshakusanya tani 35,000 za mbale (ore) kwa njia ya ubia wa Kampuni ya Busolwa Mining pamoja na wachimbaji hao na waliweza kutoa fursa za ajira 164 za moja kwa moja.
MHE. SUSANNE P. MASELE aliuliza:-
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, imekuja na mikakati yake mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakiki watumishi wa umma, zoezi ambalo halikuwekewa muda wa kuanza na kumaliza (time frame) hali hiyo imesababisha usumbufu mkubwa na hata kuharibu mfumo wa watumishi wa umma, ikiwemo namna ya kuajiri.
(a) Je, Serikali inatoa kauli gani kwa watumishi wa umma walioajiriwa na kusainishwa mikataba ya ajira ndani ya Serikali ambapo ghafla mwaka 2016 Rais alitoa kauli ya kusimamisha ajira kupisha ukaguzi wa watumishi hewa?
(b) Je, Serikali inatambua kuwa watu hao tayari walikuwa watumishi na mchakato wa kuwaingiza kwenye payroll ulishaanza, lakini ukasitishwa ghafla na sasa wako mtaani na hawajui hatma yao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susanne Peter Masele, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba watumishi wote ambao walisitishwa kuingizwa katika orodha ya malipo ya mishahara (payroll) mwezi Mei, 2016 waliokuwa wakipisha zoezi la uhakiki wa watumishi wamesharudishwa katika orodha ya malipo na sasa wanaendelea na kazi na wamekuwa wakilipwa mishahara yao kama kawaida.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) ya swali la Mheshimiwa Masele, watumishi hao wanatambuliwa kama watumishi wengine wa umma.
MHE. SUSANNE P. MASELE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo kipaumbele cha leseni na vibali vya kuchimba madini kwa kuonesha mfano kwa wachimbaji wadogo wa machimbo ya Dhahabu ya Ishokelahela, Misungwi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Susanne Masele naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama hapa, lakini vile vile nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa Imani kubwa aliyonipatia na akaona naweza kumsaidia kwenye Sekta hii ya Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Susanne Peter Masele Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji wa Madini wadogo wa Ishokelahela Wilayani Misungwi walivamia na kuanza shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Leseni kubwa ya utafutaji wa madini inayomilikiwa na Kampuni ya Carlton KitongoTanzania Limited yenye ukubwa wa kilomita za mraba 12.4 tokea mwezi Julai, 2017. Kabla ya hapa wachimbaji hao walikuwepo lakini kwa kiasi kidogo. Mpaka kufikia sasa leseni hiyo imevamiwa na wachimbaji wadogo zaidi ya 1000 ambao wanachimba madini hayo ya dhahabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leseni ya Carlton KitongoTanzania Limited ilitolewa tarehe 5 Agosti, 2014 na itamaliza muda wake wa awali tarehe 4 Agosti 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi kwa kushirikiana na kampuni ya Carlton Kitongo Tanzania Limited ambaye ni mmiliki wa leseni hiyo waliamua kutenga eneo kwa ajili ya kuwaachia wachimbaji wadogo ambalo likuwa linamilikiwa na kampuni hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makubaliano hayo yalihitimishwa rasmi mwezi Desemba mwaka 2017 kati ya mmiliki wa leseni na vikundi ambayo viliungana kuunda kikundi kimoja kwa jina la Basimbi and Buhunda Mining Group. Nakala ya makubaliano hayo ipo Ofisi ya Madini Mwanza na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Misungwi. Vikundi hivyo vilipatikana baada ya Wizara kupitia Ofisi yetu ya Madini Mkoani Mwanza kutoa elimu ya umuhimu ya kujiunga katika vikundi na kuendesha shughuli za uchimbaji madini ili ziweze kuwa na tija zinazozingatia matakwa ya Sheria ya Madini na Kanuni zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuwapatia wachimbaji wadogo kipaumbele cha leseni na vibali vya kuchimba madini, leseni za wachimbaji madini katika eneo hilo zitatolewa kwa vikundi hivyo mara tu baada ya taratibu za kisheria za kushughulikia maombi hayo kukamilika.
MHE. SUSANNE P. MASELE aliuliza:-
Wananchi wakazi wa Kijiji cha Ishokelahela, Misungwi, Mwanza, wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kihalifu, kinyama na kikatili na Vyombo vya Dola kuwaondoa katika makazi yao na kuacha kuchimba dhahabu ili eneo hilo libaki kwa Mwekezaji anayetaka kuwaondoa kwa nguvu kinyume cha sheria:-
i. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu vitendo hivyo wanavyofanyiwa wananchi hao?
ii. Je, Serikali iko tayari kuunda timu kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mgogoro huo na kuchukua hatua stahiki ambazo zitamaliza kabisa mgogoro na kuwawajibisha wote ambao wamesababisha hali iliyopo sasa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susanne Maselle, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kijiji cha Ishokelahela ambao ni wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu wamekuwa na mvutano na Mwekezaji Isinka Federation 2014 Mining Cooperative and Society Limited anayefanya shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika eneo hilo kihalali. Mvutano huo umepelekea wananchi hao kutaka kuvamia eneo la Mwekezaji huyo bila kufuata sheria kitendo ambacho kinaweza kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi linao wajibu wa kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inaimarishwa katika eneo hilo kwa mujibu wa sheria, hivyo haliwezi kuruhusu wananchi kuchukua sheria mkononi na kuvamia eneo hilo ambalo linamilikiwa kihalali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba vyombo vya dola vimekuwa vikiwanyanyasa na kuwafanyia unyama wa kikatili wananchi katika makazi yao bali katika eneo husika Jeshi la Polisi limekuwa likiwazuia kuingia katika eneo ambalo sio mali yao kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala hili ni suala muhimu, hata hivyo, Serikali inaendelea kulifuatialia kwa karibu na kutafuta suluhisho la kudumu ili kuondoa migongano ambayo inaweza kuhatarisha amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nitumie fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge awahamasishe na kuwashauri wananchi wa Kijiji hicho ambao ni wachimbaji wadogo wadogo kuungana katika vikundi na kuomba leseni za uchimbaji ili wafanye shughuli zao kihalali.
MHE. SUSANNE P. MASELLE aliuliza:-
Mnamo tarehe 30 Januari, 2017, wavuvi wa maeneo ya Igombe na Ilemela Jijini Mwanza walikamatwa na kunyang’anywa nyavu, mitumbwi na mashine za mitumbwi yao na Maafisa wa Uvuvi wakidai wanatumia nyavu haramu ambazo ni “double” huku Serikali ikitaka watumie “single”:-
(i) Je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kutoa taarifa, elimu na muda kwa wavuvi pindi inapotaka wavuvi wafanye mabadiliko katika shughuli au zana zao za kazi?
(ii) Je, ni lini Serikali itatoa elimu kwa wavuvi wa Igombe na maeneo mengine ya Mwanza kuhusiana na uvuvi wa kutumia nyavu za single badala ya double ili wafanye kazi zao kwa uhuru bila bughudha ya kukamatwakamatwa?
(iii) Je, Serikali inataka wavuvi wavue samaki katika kina kipi cha maji na katika kina cha mita 50 na kuendelea watumie nyavu za mita ngapi kwenda chini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susane Peter Maselle, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutoa taarifa na elimu kwa wavuvi kuhusiana na usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi kupitia mikutano, vipindi vya redio na runinga. Pia, leseni za uvuvi huonyesha masharti yanayopaswa kufuatwa ili kuwa na uvuvi endelevu. Kimsingi elimu kwa wavuvi hutolewa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na wakati wanapopewa leseni na wakati wa kutoa huduma za ugani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutumia Maafisa Uvuvi wa Idara, Manispaa ya Ilemela na Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) imeendelea kutoa elimu kwa wavuvi wa Igombe na maeneo ya Mwanza juu ya katazo la matumizi ya nyavu za kuunga kwa maana ya double.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wanaweza kuvua katika tabaka lolote la maji kwa kutumia nyavu zinazoruhusiwa. Isipokuwa hawaruhusiwi kuvua katika maeneo ya mazalia ya samaki na maeneo tengefu. Aidha, katika kina cha mita 50, wavuvi wanapaswa kutumia nyavu zilizoruhusiwa zisizozidi macho au matundu 26 kwenda chini kwa upande wa Ziwa Victoria.
MHE. SUSAN P. MASSELE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo Kikuu cha Umma au Vyuo Vikuu vya Umma vyenye hadhi ya juu katika Mkoa wa Mwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NASERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA - K.n.y WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Peter Massele, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu katika kuandaa rasilimali watu itakayochangia katika kufikia azma ya Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Kwa sasa Serikali inatekeleza Mpango wa kuboresha Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zilizopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu mipya pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ili kuongeza nafasi za udahili na kuimarisha ubora wa elimu itolewayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa tuna idadi ya Vyuo Vikuu 11, Vyuo Vikuu vishiriki viwili na Taasisi za Elimu ya juu 32 zinazotoa Elimu ya juu nchini. Mkoa wa Mwanza una matawi ya Taasisi ya Elimu ya juu za Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT). Aidha, Mkoa una Tawi la Chuo kikuu Huria cha Tanzania (OUT) mbali na Vyuo Vikuu vya Mtakatifu Augustino na Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Bugando ambavyo vinamilikiwa na taasisi binafsi. Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu ni za Kitaifa ambapo hupokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaboresha mazingira vya Vyuo vilivyopo lakini kama itaona kuna umuhimu wa kuongeza Vyuo vingine itafanya hivyo katika maeneo yatakayoonekana yanafaa. Wito wangu kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo mengine ni kuendelea kutumia Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zilizopo katika Mkoa wa Mwanza. Ahsante.
MHE. SUSANNE P. MASELLE aliuliza:-

Bado kuna shida kubwa ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wetu hasa maeneo ya vijijini:-

Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kupunguza au kumaliza tatizo hilo kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya Misungwi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susanne Peter Maselle, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya maji kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya Misungwi, Serikali imekamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa thamani ya shilingi bilioni 12.85 kutoka katika chanzo cha maji cha Nyahiti ambapo wakazi wapato 64,280 wanatarajia kunufaika katika mradi huo hadi kufikia mwaka 2040.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mradi huo, Serikali inatekeleza mradi mkubwa kutoka bomba kuu la usafirishaji maji la KASHWASA utakaohudumia vijiji 14 vya Wilaya ya Misungwi kupitia miradi mitano. Mradi wa kwanza ni kufikisha huduma ya maji Mabale – Mbarika, mradi wa pili ni kufikisha huduma ya maji Igenge, mradi wa tatu ni kufikisha huduma ya maji Mbarika – Ngaya, Mradi wa nne ni kufikisha huduma ya maji Ngaya – Matale na mradi wa tano ni kufikisha huduma ya maji Matale – Misasi. Miradi hii ikikamilka itahudumia jumla ya watu 45,788.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeanza kutekeleza miradi katika vijiji vitano vya Kata ya Shilalo kupitia Programu ya Malipo kwa Matokeo, inayofadhiliwa na Benki ya Dunia. Miradi hiyo ikikamilika itahudumia watu wapatao 15,500. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO (K.n.y. MHE. SUSANNE P. MASELLE) aliuliza:-

Kutokana na umuhimu wa kimkakati katika nyanja mbalimbali za maendeleo kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi yetu kwa ujmla:-

Je, ni lini Jiji la Mwanza litakuwa na uwanja wa ndege unaoendana na hadhi na ukuaji wa kasi wa jiji hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege, Serikali iliingia mkataba wa ukarabati mkubwa wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza Oktoba, 2012 na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd (BCEG) wenye thamani ya shilingi 89,291,995,422. Mchanganuo wa fedha hizi ni kuwa Serikali ya Tanzania inachangia asilimia 82.5 na wabia wa maendeleo asilimia 17.5.

Mheshimiwa Spika, kazi kubwa zinazofanyika katika uboreshaji huu ni pamoja na kurefusha barabara ya kuruka na kutua ndege (runway) kutoka mita 3,300 kwa upana wa mita 45 hadi mita 3,800 kwa upana wa mita 45; kujenga majengo ya kuongozea ndege (control tower); kituo cha hali ya hewa; jengo la kupokea na kuhifadhi mizigo; kuboresha na kupanua maegesho ya ndege (aprons); kujenga barabara za viungio (taxways) na kituo cha umeme (power station).

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2019, ujenzi wa kazi hizi za mradi umefikia asilimia 87 na mkandarasi anaendelea vizuri na kazi ya ujenzi na anatarajia kumaliza kazi zote ifikapo Juni, 2019.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia ipo kwenye mazungumzo na wabia wa maendeleo ambapo wameonyesha nia ya kufadhili jengo kubwa na la kisasa la abiria litakaloendana na maboresho haya makubwa ya kiwanja pamoja na hadhi ya Jiji la Mwanza. Tunategemea kufikia Mwezi Oktoba, 2019, kazi za ujenzi wa jengo hili zitakuwa zimeanza.