Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ally Seif Ungando (28 total)

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya ndugu yangu Naibu Waziri.
Je, Serikali haioni kila sababu ya kupeleka visima vya maringi kwa kuanzia katika maeneo hayo ya Delta?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niweke rekodi sawa katika harakati za kutekeleza miradi mimi naomba nimsifu huyu Mbunge maana siku zote anakuja pale ofisini kwangu na amekuwa akifanya juhudi kubwa kwa Jimbo lake, wakati mwingine anatumia hata resource zake mwenyewe kwa ajili ya Jimbo lake. Lakini mahitaji yake ni jinsi gani tutafanya visima vya ringi viweze kujengwa, naomba niseme ngoja tulichukue hili.
Lakini kwa ukubwa wake zaidi lazima tuseme kwamba maeneo ya Delta yote yana shida kubwa sana, nikisema suala la Delta halikadhalika hata juzi nilikuwa najibu swali la ndugu yangu Mbunge wa Jimbo la kule Mwanza, ni kwamba maeneo haya yenye delta yana matatizo makubwa sana siyo maji peke yake hata huduma nyingine za afya na elimu.
Kwa hiyo, nikuombe ndugu yangu kwamba tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo ikiwezekana ni kwamba maeneo haya tuweze kuyapatia huduma ya maji ili wananchi wa Kibiti na wao wajisikie kama sawa na wananchi wengine.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza la nyongeza. Maeneo ya Kibiti, Ikwiriri, Bungu kumekuwa na tatizo la umeme kukatikakatika.
Je, lini Serikali itamaliza tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishakueleza kwenye jibu langu la msingi na maelezo mengine ya nyongeza. Ni kweli kuna maeneo mengi ambayo bado umeme unakatika katika na sababu za kukatika nimezieleza. Lakini niseme tu, taratibu za kukamilika kwa kukatikakatika pamoja na matatizo mengine ya umeme tutakapokamilisha kusambaza hizi nguvu kubwa za kilovolt 400 na kilovolt 220 ambapo kazi rasmi itakamilika 2018/2019, kwa hiyo kuanzia wakati huo, maeneo ya Kibiti, maeneo ya Ikwiriri na maeneo mengine ya kule chini, tatizo la kukatika katika kwa umeme litakwisha kabisa.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kibiti ni mojawapo ya Wilaya inayolima mihogo kwa wingi lakini ina tatizo la soko ambapo mihogo mingi hutegemewa kuuzwa kwenye Mwezi wa Ramadhani. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kupeleka kiwanda cha kuchakata mihogo katika Wilaya mpya ya Kibiti?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda cha mihogo, nakuomba Mheshimiwa Ungando uje unione nitakuelekeza kwa Meneja wa SIDO. Pia nitakwenda nawe bega kwa bega tuangalie fursa ya malighafi iliyopo na kiwanda cha namna gani kinaweza kuanzishwa katika mipango hii. Nitafanya kazi na wewe.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Waziri. Je, sasa ni lini wananchi hawa wa Delta watapata mawasiliano hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, ni lini Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuambatana nami bega kwa bega ili twende kuangalia maeneo hayo na kuwapatia ufumbuzi wa mawasiliano hayo? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ni lini? Katika mpango wetu wa awamu ya pili, mpango huu utaanza mwezi Oktoba mwaka huu ambapo takribani vijiji 1,800 vitapelekewa mawasiliano. Kati ya vijiji hivyo na vijiji vya Mheshimiwa Mbunge tumeviweka kwenye mpango huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni lini tutakwenda, hiyo tutazungumza mimi na yeye kwenda kuangalia maeneo hayo pia na miradi mingine ya uchukuzi na ujenzi. (Makofi)
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia Mto Rufiji kutoa maji ili wananchi wa Kibiti, Bungu, Ikwiriri, Kimanzichana na Mbagala wafaidike na mto huo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ungando, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutumia Mto Rufiji au vyanzo vingine; haya tunafanya maamuzi baada ya kufanya usanifu wa maeneo yale tunayotaka kupeleka yale maji. Kwa hiyo, tunalinganisha gharama kwa wakati ule. Uwezo wa Serikali; kwa mfano, ukichukua maji kwenye mto na ukapeleka vijiji vingi au kilometa 100, gharama yake ni kubwa. Kwa hiyo, lazima uangalie uwezo pia wa Serikali. Kwa hiyo, kama kuna uwezekano wa kupata vyanzo ambavyo ni nafuu kwa gharama, tunaanza navyo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango ya muda mrefu, tulishajibu hapa Bungeni kwamba tunafanya usanifu wa kuona uwezekano wa kuchukua maji ya Mto Rufiji na kuleta maeneo ya mpaka Mkuranga. Kwa hiyo, jambo hilo linafanyiwa kazi na Serikali. Muda utakapofika, basi tutawajulisha Waheshimiwa Wabunge kama hilo linawezekana kwa bajeti inayokuja au baada ya hapo.
Pwani. MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nianze kusema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Waziri huyu ni mchapakazi, kweli tarehe 5 Januari, ni Waziri wa kwanza aliyefika maeneo ya Delta na nilifanya naye kazi na nikaonesha kweli kauli ya hapa kazi inatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niulize maswali yangu mawili; moja, je, kutokana na barabara hii kwamba kwa sasa ina maeneo mawili ya daraja hayapitiki, je, Serikali haioni kwamba ina kila sababu ya kukarabati madaraja hayo? Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Barabara ya kutoka Muhoro kwenda Mbwela ina matatizo makubwa hasa kwenye Daraja la Mbuchi, je, Serikali itatusaidiaje katika hilo la Mbuchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kupokea shukrani zake ndugu yangu Mheshimiwa Ungando, naomba nikiri, kweli nilikuwepo kule na tulitembelea visiwa 40 vya Deltakatika Jimbo lile la Kibiti. Barabara ya kutoka hapa Bunju mpaka Nyamisati kule ndani kwa kweli ina changamoto kubwa sana naomba tulipokee jambo hili kwa sababu katika programu yetu ya uondoaji wa vikwazo tutajitahidi ofisi yetu tufanye kila liwezekanalo kwa sababu tukiwasaidia wananchi wa eneo lile tutakuwa hata tumewasaidia wananchi wa Mafia kwa sababu wanaposafiri kutoka Nyamisati kwenda Mafia lazima watumie barabara ile. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika suala zima la Daraja la Mbuchi, na kwa sababu tulipita kule na vilevile tunajua kuwa tuna harakati ofisi yetu kutengeneza Daraja la Mbwela, tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo kuhakikisha mambo haya yote ofisi yetu inayashughulikia na Mheshimiwa Ungando amini Serikali yako tutakupa ushirikiano kwa sababu jimbo lako ni miongoni mwa majimbo yenye changamoto kubwa.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kutokana
na vitendo vya uhalifu vinavyoendelea ambavyo vinasababisha Kibiti kushindwa kukusanya makusanyo yake ya ndani, je, Wizara itaiangaliaje kwa jicho la huruma ili kuhakikisha wanapata Mwenyekiti wao wa Mamlaka ya Mji Mdogo Kibiti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kutokana
na ukweli kwamba Kibiti ni Halmashauri mpya Mkurugenzi na DC hawana vifaa vya kutendea kazi kama magari. Je, Serikali inaliangaliaje hilo kwa jicho la huruma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nitoe pole kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Kibiti na Rufiji kwa tatizo kubwa linaloendelea pale kwa sababu mpaka hivi sasa tumepoteza Wenyeviti wengi sana na hali hiyo inaogopesha.
Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko na wananchi wa Kibiti na Rufiji na tutaangalia nini cha kufanya kwa sababu sasa hivi ukiitisha uchaguzi pale hata Wenyekiti wenyewe kujitokeza kugombea nafasi yenyewe wanaogopa.
Kwa hiyo, Serikali inafanya kazi ya kurudisha hali ya utulivu na amani ili hali ya usalama iweze kukaa vizuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge amini kwamba Serikali yako itashirikiana na wewe kama inavyofanya hivi sasa ndiyo maana timu ya Mkoa wa Pwani iko kule site kuhakikisha mambo yanakaa sawa. Kwa hiyo, hili jambo tumelichukua kwa moyo wa dhati kabisa na tutashirikiana kupata ufumbuzi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la changamoto
ya magari, ni kweli na Mheshimiwa Ungando nikushukuru sana, tulipotembelea vile visiwa 40 vya delta kule tulifanya kazi kubwa sana, tokea asubuhi mpaka tulivyomaliza saa mbili usiku, nimebaini changamoto hizo. Ndiyo maana kipindi kile nilivyorudi haraka tukafanya utaratibu kuwaletea gari moja pale la Road Fund. Hata hivyo, Serikali imeona hili tatizo kwa DC na Mkurugenzi tutajitahidi nini tufanye kwa pamjoa kuisaidia Halmashauri hii mpya ambayo ina changamoto kubwa sana katika suala zima la vitendea kazi.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na mauaji yanayoendelea Wilayani Kibiti bado tunahitaji umeme. Je, Serikali ina mpango gani kupeleka umeme katika vijiji vilivyobakia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze nilienda kwake na tulitembea sana mpaka kwenye Kijiji cha Jaribu Mpakani na tulipeleka umeme Jaribu Mpakani. Hata hivyo, Serikali imekusudia kuangaza umeme vijiji vyote nchi nzima. Napenda nitoe nafasi hiyo kwa sababu, Mheshimiwa Ungando tumeshirikiana sana, lakini niseme tu vijiji vyote vya Jimbo la Kibiti vitapelekewa umeme sasa kupitia Mradi wa REA; hadi kufikia mwaka 2021 vijiji vyake vyote vya Kibiti vitakuwa vimeshapata umeme. (Makofi)
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru. Kwanza awali ya yote niishukuru Serikali sasa hivi amani Kibiti inazidi kuimarika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu, wananchi wa Kibiti wametenga takribani ekari 15 kwa ajili ya ujenzi wa Polisi Kanda Maalum. Je, ni lini watajenga kituo hicho?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya na kwa kweli amekuwa bega kwa bega kuzileta hoja za wananchi wa Kibiti pamoja na ukanda ule. Nimhakikishie tu, kwa sababu kanda tayari ilishaanza tayari tumeshateua uongozi na uongozi uko kazini kwa hiyo hatua inayofuata ni ujenzi wa jambo hilo na tunalielewa, tunategemea tu kulitekeleza kufuatana na mtiririko wa fedha kwa tutakapokuwa tunapata. (Makofi)
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Halmashauri ya Kibiti ni Halmashauri moja ambayo imetoka Wilaya ya Kibiti na kituo chake kikubwa cha afya Kibiti lakini hivi sasa kimezidiwa kutoa huduma.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Hospitali
ya Wilaya ya Kibiti? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hoja anayoizungumza Mheshimiwa Ungando ni hoja ya kweli na kwa sababu nilikuwa naye katika vile visiwa 40 vya Delta kwa kutwa nzima na changamoto ya afya kule ni kubwa sana, ndiyo maana katika kipindi cha sasa tumepeleka fedha katika kituo cha afya kimoja ambacho mimi na Mheshimiwa Mbunge tulizunguka mpaka usiku pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la progamu ya uanzishaji wa Hospitali ya Wilaya ya Kibiti, naomba nikusihi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutashirikiana kwa pamoja kwa sababu lengo letu kubwa zile Wilaya zote zilizokosa hospitali sasa tuweze kuwa na progamu maalum kwa ajili ya kujenga hospitali. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ungando naomba nikupe faraja kwamba tutashirikiana kwa pamoja tuangalie way forward tunafanyaje tupate Hospitali ya Wilaya ya Kibiti kwa sababu population ya watu pale ni kubwa hasa ukiangalia barabara ya Kilwa lazima tuhakikishe kwamba tunafanya jambo hilo kwa haraka. (Makofi)
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza awali ya yote sina budi kushukuru kwamba hali ya ulinzi Kibiti inazidi kuimarika. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu, kipenzi chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Kibiti sasa kinazidiwa, je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha ili kuwa Hospitali ya Wilaya ya Kibiti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba hospitali inazidiwa na tafsiri yake nini ambacho kinatakiwa kufanyika? Ni kwamba tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba tunajenga vituo vya afya vingi ili Hospitali ya Wilaya hiyo iwe na sehemu ya kupumulia.
Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu Mheshimiwa Mbunge awahimize wananchi wake waonyeshe nia ya kuanza ujenzi na Serikali itapeleka mkono pale ambapo tayari wananchi washaanza ujenzi.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; Serikali ina mpango gani wa kuajiri watumishi wa sekta ya ardhi ikiwemo Kibiti ambako kuna watumishi wachache?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia vifaa vya upimaji katika Wilaya mpya ya Kibiti kwa sababu mapato yake ya ndani yamekuwa madogo sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchache wa watumishi wa ardhi, naomba nimsihi Mheshimiwa Mbunge na ninaamini kabisa ana nia njema na amekuwa akipigania wananchi wa jimbo lake; katika ikama ambayo itakuwa imewekwa na halmashauri yake ni vizuri wakaonesha uhitaji wake na halafu utaratibu wa kuwaajiri watumishi wa ardhi kama ambavyo ilikuwa kwa watumishi wengine ikafuatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, uwezo wa Halmashauri ni mdogo kwa hiyo wanaomba vifaa vya kupimia ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi ambayo ndiyo Wizara yenye dhamana kwa kujua iko haja kubwa ya kuhakikisha kwamba ardhi inapimwa katika maeneo yote na Wilaya zote, juzi juzi Serikali kwa kupitia Wizara ya Ardhi wameweka katika mpango wa kuhakikisha kwamba Wilaya zote zinanunuliwa vipima ardhi ili iweze kurahisisha suala hili. Naamini na wao watakuwa wanufaika.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba niulize swali la nyongeza. Kutokana na mvua zilizonyesha, barabara yetu ya kutoka Mbwela kwenda Muholo imeharibika zaidi. Je, Wizara yake ina mkakati gani wa kutukarabatia barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Ungando amehamisha goli lakini ngoja nimjibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anachosema Mheshimiwa Mbunge ni kweli, ile barabara kwanza ni korofi na Mheshimiwa Mbunge anakumbuka siku ile tulikuwa delta mpaka usiku saa mbili ndipo tulirudi kwa kuwa barabara iliharibika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tumepitisha fedha za barabara za vikwazo na barabara hiyo tumeiweka basi nimhakikishie Mheshimiwa Ungando kwamba kwa sababu bajeti tumeipitisha jana na yeye amepiga kura ya ndiyo, bajeti hii sasa itakapoanza kufanya kazi katika eneo lake lile tutalipa kipaumbele ili barabara ile tuirekebishe sambamba na ujenzi wa yale madaraja ambayo yanakwamisha sana kuwapitisha wananchi wa Kibiti.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza sina budi kushukuru vyombo vya ulinzi na usalama hasa Kibiti tunalala usingizi.
Swali langu la nyongeza Kituo cha afya kibiti hasa kinazidiwa kutoa huduma, je, Serikali ina mpango gani wa kuijengea Kibiti Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli huko uhitaji mkubwa sana na kituo cha afya kilichopo kimezidiwa, naomba nimuondoe mashaka Mheshimiwa Mbunge na nimuhakikishie miongoni mwa hospitali 67 zinazotarajiwa kujengwa ni pamoja na Wilaya yake, kwa hiyo, wakae mkao wa kula Serikali inatekeleza ili kuondoa shida kwa wananchi. (Makofi)
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyogeza. Kwanza sina budi kuwashukuru vyombo vyote vya ulinzi na usalama, Kibiti hali shwari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, wananchi wa maeneo ya Delta, Mbwela, Msala, Salale, Mapaloni, Kiongoloni wana shida kubwa ya maji ambayo sasa inapelekea hata ndoa kulegalega kwenye nyumba. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia maji safi na sala katika maeneo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Delta tayari tumelifanyia utafiti na tumechimba visima kiasi. Ukienda zaidi ya mita tano unapata maji ya chumvi, kwa hiyo, sasa tunajaribu kuangalia mfumo mzuri ambao utahakikisha kwamba wananchi wa Delta wanapata maji bila shida, lakini ukienda mita nne tayari tumechimba visima wanapata maji safi na salama.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Moja, kwa kuwa kila penye mafanikio hapakosi kuwa na changamoto, je, Waziri sasa yuko tayari kufuatana na mimi kwenda Kituo cha Afya Mbwera kwenda kubaini baadhi ya changamoto za huu ujenzi unaoendelea hivi sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwamba hali ya Kituo cha Afya Kibiti majengo yake kwa kweli uchakavu wake hauridhishi. Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha ya kufanya ukarabati Kituo hiki cha Afya Kibiti ili kiweze kutoa huduma yenye tija kwa wananchi wa Kibiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ungando Mwenyekiti wa Wandengereko (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko tayari kwa sababu wanasema seeing is believing kama ambavyo juzi nilipata fursa ya kwenda Dar es Salaam kutembelea Kituo cha Afya Buguruni na kule inakojengwa Hospitali ya Wilaya kwa Mheshimiwa Waitara, niko tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kukarabati kituo kingine cha afya ambacho Mheshimiwa Mbunge anaomba, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba tunakamilisha na kukarabati vituo vya afya vingi kadri iwezekanavyo ili kusogeza huduma ya afya na hasa afya ya mama na mtoto kwa kadri itakavyowezekana. Kwa hiyo, kadri bajeti inavyoruhusu naomba nimhakikishie Mbunge kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba ukarabati unafanyika.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Kibiti ina mifugo mingi ya ng’ombe. Je, Serikali ina mpango gani wa kuijengea machinjio ya kisasa, malambo na majosho ili kuondoa migogoro baina ya wakulima na wafugaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba Halmashauri ya Kibiti ina mifugo mingi sasa, ni ukweli mifugo mingi imehamia katika Mkoa wetu wa Pwani, Wilaya za Mkuranga, Kibiti, Rufiji, Kisarawe zimepata mifugo mingi sana mara baada ya Serikali kukubaliana kuhamishia mifugo kutoka katika Bonde la Ihefu na kuhamia katika Mikoa ya Kusini na sisi tumepata neema hiyo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Ungando, kwa namna ambavyo tumejipanga katika Wizara ya Mifugo, tunataka tuhakikishe mfugo hii iende kuwa ni fursa kubwa sana kwetu sisi watu wa Mkoa wa Pwani. Ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha wa 2018/2019 ambao bajeti yake tunakwenda kuisoma hapa karibuni ataona haya aliyoyauliza ikiwemo ya malambo na majosho, yatakwenda pale katika maeneo yetu ya Wilaya za Mkuranga, Rufiji na Kibiti, ni kwa sababu ya wingi wa mifugo tuliyokuwa nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tuna mifugo mingi sana na mkakati pia ni kuhakikisha tunapata eneo la uchinjaji na ku-process nyama. Hii ni kwa sababu pia tuna advantage kubwa ya kuwa karibu na soko la hiyo nyama yenyewe maana nyama kuitoa Kibiti, Rufiji, Mkuranga ama Kisarawe ni rahisi zaidi kuipeleka Dar es Salaam kuliko eneo lingine katika nchi.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Wananchi wa Mwaseni na Ngorongo walipewa ahadi ya ujenzi wa mabwawa katika maeneo hayo, je, ni lini Serikali sasa itajenga mabwawa hayo ili wananchi hawa wafaidike katika maeneo hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Kibiti imeshindwa kukusanya mapato yake ya ndani kutokana na matatizo yaliyotokea. Je, ni lini sasa Serikali itawajengea mabwawa wananchi hao ili waongeze kipato chao katika Halmashauri ya Kibiti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya jirani na ndugu yangu Mheshimiwa Ally Seif Ungando na ninampongeza sana kwa jitihada kubwa anazozifanya za kuhakikisha kwamba maendeleo yanakwenda kule nyumbani kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza juu ya watu wa Mwaseni na Ngorongo kuahidiwa kupata mabwawa. Nataka nimwambie na niwaambie ndugu zangu wa Kibiti, Rufiji, Mkuranga, Kisarawe na Watanzania wote kwa ujumla, Kata za Mwaseni, Ngorongo na kata nyingine katika Wilaya ya Rufiji zitakwenda kuwa wanufaikaji wakubwa sana wa mradi mkubwa wa uzalishaji wa umeme wa Stiegler’s Gorge, mradi ambao utakuwa na matokeo chanya pia kwa sababu kutakuwa na eneo la ekari 140,000 kwa ajili ya kilimo. Vilevile katika bwawa lile tutakuwa na uwezo wa kuzalisha samaki wasiopungua tani 12,000 mpaka 20,000 kwa mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itakwenda kuwa na faida kubwa pia hata katika utalii kwa maana ya kwamba wapo watu watakaokuwa wanakuja kufanya kazi ya kuangalia bwawa lile kwa shughuli za utalii. Hivyo, niwaambie wananchi wa Kata hizi ya kwamba watakwenda kunufaika juu ya miradi hii ya mabwawa.
Kwa upande wa Kata za pale Kibiti pia kesho tunasoma bajeti yetu, namwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira, asikilize mipango mikakati tuliyonayo katika suala zima la ufugaji wa samaki. (Makofi)
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwanza tunashukuru Kibiti tumechimbiwa visima 12 vikiwa katika Kijiji cha Mtunda, Nyamisati, Mahege, Mlanzi na Kivinja A. Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha miundombinu hiyo ili wananchi hawa wapate maji safi na salama?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwamba je, sasa Naibu Waziri yupo tayari kuongozana na mimi kwenda katika Wilaya Mpya ya Kibiti, ili kujionea adha ya wananchi wanayopata na ukizingatia sasa hivi Kibiti ni salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge binafsi, Mbunge anafanya kazi nzuri sana. Nataka nimhakikishie wananchi wa Kibiti kwamba Mbunge wao anatosha mpaka chenji inabaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge sisi Wizara yetu ya Maji tumeona haja ya kuusaidia Mji wa Kibiti na tumechimba visima 12. Kubwa sisi tunataka tukamilishe miundombinu ile, ili wananchi wale waweze kupata maji. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi jukumu letu katika kuhakikisha miradi ile tunaikamilisha kwa wakati, ili wananchi wake waweze kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu suala la mimi kwenda Kibiti. Nataka nimhakikishie kwa kuwa, sasahivi Kibiti ni salama, mimi kama Naibu Waziri niko tayari kwenda kuambatana naye kuzungumza na wananchi.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Swali langu la nyongeza. Sasa hivi Kibiti imekuwa Kibiti salama, je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha maslahi ya Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba, inaboresha maslahi na mazingira ya utendaji kazi wa vyombo vyetu vya Polisi hatua kwa hatua na kadiri ya uchumi wa nchi utakavyokuwa unaimarika.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya swali hilo, nina maswali mawili ya nyongeza.
(i) Wananchi wa Nyamisati walipisha ujenzi huo lakini sehemu waliyopelekwa miundombinu yao imekuwa siyo rafiki. Mfano hakuna choo, banda la abiria ni kifusi katika hilo gati la muda. Je, lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi huo?
(ii) Vijana wa maeneo hayo wamejiunga na vikundi vyao vya ujasiriamali kama mkombozi. Je, sasa Serikali ina mpango gani wa kuwapa kipaumbele katika ujenzi huo ili vijana hao wafaidike, wapate vibarua ukizingatia watu wa Pwani wanasema mgeni njoo mwenyeji apone? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Ungando kwa jinsi alivyofuatilia kwa muda mrefu sana ujenzi wa gati hili la Nyamisati. Ninakumbuka kuna kipindi fulani tuliwahi kwenda naye mpaka kufanya kikao na watu wa TPA kwa ajili ya kufuatilia kwa ukaribu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kujibu swali lake la kwanza, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, tayari TPA wanamtafuta mkandarasi kwa ajili ya kujenga choo cha umma pamoja na sehemu ya kupumzikia kwa maeneo ambako wananchi wamepisha ujenzi wa gati uendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira kidogo, tutakapopata mkandarasi hilo eneo litajengwa kwa ajili ya wananchi kupumzika vilevile kutakuwa na maeneo rafiki kwa ajili ya wananchi ambao watakuwa wanasubiri huduma za gati hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu la swali lake la pili, ninaielekeza TPA, ninajua kwamba kwenye mkataba ambao wameingia na hawa wakandarasi wawili kuna kipengele ambacho kinawataka wakandarasi wawachukue wazawa katika shughuli zile ambazo siyo za kitaalam kuweza kufanya kazi kama vibarua na vitu kama hivyo. Ninawaagiza TPA wahakikishe wanafanya kazi kama walivyoingia mkataba na wakandarasi kutumia wazawa katika shughuli ambazo siyo za kitaalam. Ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; wananchi wa Mtunda – Kikale -Myuyu bado wanapata shida kwani njia ile haipitiki kabisa kutokana na mvua nyingi zilizonyesha. Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati huo kwa haraka ili barabara hiyo iweze kutoa huduma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, barabara ya kutoka Bungu - Msolo nayo haipitiki kabisa, tena hatari zaidi kuna shimo kubwa pale Bungu ambalo linaweza likakata mawasiliano baina ya wananchi wa Bungu na Msolo. Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati barabara hiyo ili wananchi hawa sasa wapeleke mazao yao sokoni na wapate faida haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata fursa ya kutembelea Jimboni kwa Mheshimiwa Mbunge, nikafika mpaka Delta na changamoto anazozitaja nazifahamu. Naomba nitumie fursa hii kumwagiza Meneja wa TARURA aende site akatazame kilichopo ili aweze kutushauri nini kifanyike ili wananchi wa Jimbo analolisema Mheshimiwa Mbunge wasije wakapata adha ya kukosa usafiri ili mazao yao yaweze kufika sokoni. (Makofi)
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia Mto Rufiji kupeleka maji Ikwiriri, Bungu na Nyamisati?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa mjukuu wangu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imepata grant kutoka Serikali ya Korea na tumeanza feasibility study ambayo inakamilika Julai, 2018 kwa ajili ya kuchukua maji kutoka Mto Rufiji kuyaleta Dar es Salaam kupitia kwenye maeneo yote ikiwepo pamoja na eneo Mheshimiwa Mbunge.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza; Kituo cha Afya Kibiti kimezidiwa, je, ni lini Serikali itafanya ukarabati mkubwa ikizingatia pale hakuna X-ray, nyumba za wagonjwa na maabara ya uhakika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ungando, Mwenyekiti wa Wandengereko ambaye kwa mara ya kwanza amenipandisha boti nikaenda Delta, sehemu ambayo unaambiwa kwamba ikifika muda fulani maji yakikauka inabidi usibiri saa nne. Nimefika kule na naomba nimpongeze jinsi ambavyo anapigania wananchi wa Jimbo lake la Kibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri kazi ambayo tulienda kusimamia sasa inakwenda vizuri. Kuna mambo ya hovyo yalikuwa yanafanyika katika ujenzi wa kituo kile cha afya lakini hata jana nilikuwa naongea na Mwenyekiti wa CCM ambaye alikuwa Mbunge, Ndugu Jabir Marombwa amenihakikishia ujenzi unakwenda vizuri. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, eneo hilo ambalo hakuna X-ray tayari tumeshapeleka pesa MSD kwa ajili ya vifaa, kwa sababu tunataka vituo vya afya vikamilike kwa kuwa na vifaa pamoja na wataalam ili vitoe huduma iliyokusudiwa kwa wananchi. (Makofi)
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga machinjio ya kisasa ili kuwaletea tija wananchi wa kibiti ambao sasa hivi wana mifugo mingi katika maeneo ya Makima, Nyatanga, Mwambao, Nyambunda, Msala na Muyuyu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, Wizara sasa haioni ina kila sababu ya kukaa na wakulima na wafugaji ili kubaini changamoto zao kutatua kama ilivyofanya katika Wizara ya Madini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Ungando, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Mheshimiwa Ally Seif Ungando anataka kujua mkakati wa Serikali juu ya ujenzi wa machinjio ya kisasa kulingana na idadi ya mifugo iliyopo katika ukanda huu wa Wilaya ya Kibiti na jirani zake Mkuranga, Rufiji mpaka Kilwa. Jambo hili ni jema na Serikali imekuwa na mkakati huu ambapo baadhi ya maeneo katika Halmashauri mbalimbali nchini zimejengewa machinjio ya kisasa. Hivyo basi, ni wakati muafaka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kuibua mradi huu wa kimkakati na nina hakika Serikali itakuwa pamoja kulingana na ukweli kwamba maeneo haya niliyoyataja hivi sasa yana fursa hii kubwa na nzuri ya Uhamiaji wa mifugo kwa wingi ambapo itakwenda kusababisha upatikanaji wa uhakika wa ajira vilevile kuongeza kipato cha Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili Mheshimiwa Ungando amenihimiza na kututaka Wizara yetu kukaa na wadau hasa wa ufugaji na wakulima, sawa na walivyofanya wenzetu wa Wizara ya Madini. Ni wazo jema na ni zuri sana. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Ungando na Waheshimiwa Wabunge wote, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa na utaratibu huo. Mara nyingi tumekuwa tukikutana na wadau wetu na hata sasa ninavyozungumza wako wataalam wetu kwa maana ya timu maalum inayoshughulika na migogoro ya wakulima na wafugaji, timu ambayo imeundwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi inayojumuisha wataalam kutoka Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Ardhi na Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi inayokwenda kusikiliza wakulima, kuwasikiliza wafugaji vijijini kwa ajili ya kuweza kupata suluhu ya migogoro yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo ninavyozungumza, timu ile ya wataalam iko katika Wilaya ya Kibiti ikifanya mazungumzo na wafugaji na wakulima kwa ajili ya kutafuta suluhu ya kudumu ya matatizo ya migogoro ya wakulima na wafugaji.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Wananchi wa Bungu wanashida kubwa ya Kituo cha Afya na wenyewe walishaanza kujenga majengo. Je, Serikali ina mpango wa kuunga mkono Kata ile ya Bungu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata fursa ya kwenda Kibiti na tukaenda kutembelea mpaka Kituo cha Afya Mbwera, kituo cha afya ambacho kipo ndani kweli kweli unaenda delta kule, kama mtu anataka kuona jinsi ambavyo Serikali ya CCM inafanya kazi ni pamoja na kwenda maeneo kama delta, naomba nimhakikishie Mbunge na yeye mwenyewe ni shuhuda kazi nzuri ambayo inafanyika, hakika hata huko kituo cha afya ambacho hakijafanyiwa ukarabati kwa kadri fedha zitakazopatikana, tutaenda kukikarabati.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Kibiti wanategemea sana nishati yao ya mkaa na kuni, je, ni lini sasa wataunganishiwa hii gesi asilia katika Miji ya Kibiti, Bungu na Jaribu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali sasa inajenga mradi mkubwa wa umeme kule Mloka wa Stiegler’s, je wananchi wa Kibiti ambao kwa kiasi kikubwa wanategemea kukata kuni na mkaa wanaweza wakapatiwa upendeleo wa kupata vibarua?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuruku kwa kunipa nafasi ya kujibu swali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeza kwa kazi nzuri anayofanya katika Jimbo la Kibiti, hususan katika sekta hii ya nishati. Maswali yake ya nyongeza kwanza ameuliza ni lini sasa Serikali itasambaza gesi katika Wilaya hii ya Kibiti, katika jibu letu la msingi tumesema katika kipindi hiki cha muda wa kati kati ya mwaka 2010 mpaka 2020 tumekuwa tukutekeleza miradi ya muda wa kati na muda mfupi wa kusambaza gesi katika maeneo mbalimbali. Mpaka sasa Mheshimiwa Waziri wa Nishati wiki mbili zilizopita amezindua uunganishaji wa gesi nyumba mpya 26. Matarajio yetu mpaka ifikapo Septemba, 2019 kuunganisha nyumba kama 333 katika Mkoa wa Mtwara na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mkoa wa Lindi na Pwani, Serikali kupitia TPDC imekuja na mradi mkubwa kabambe wa kusambaza gesi asilia. Mradi huu utafanywa na mashirikiano baina ya sekta binafsi na Serikali na kwa sasa hatua ambao imefikia tumeshampata Mshauri Mwelekezi, anaandaa makabrasha na kufanya feasibility study ya mradi mzima, matarajio yetu mwezi wa Tano mwakani kuwapata wakandarasi wa sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri niwakaribishe sekta binafsi katika maeneo mbalimbali ili kujumuika na Serikali katika mradi mkubwa wa kusambaza gesi asilia kwa matumizi ya majumbani na viwandani na hususan katika Wilaya ya Kibiti kwa kuwa nayo imepitiwa na bomba la gesi hususan katika maeneo ambayo ameyataja Jaribu, Kibiti maeneo ya Nyamwimbe, Kata ya Mlanzi, maeneo ya Mangwi, Kata ya Mchukwi na maeneo mengine kama ambavyo anafahamu Mheshimiwa Mbunge, kwa hiyo nimwaidi hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza mradi wa Stiegler’s Gorge Rufiji Hydro Power unaotekelezwa katika Kata ya Mwaseni, Kijiji cha Mloka. Ni kweli mradi ule una matarajio makubwa ya kutoa ajira na kwa kuwa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, utekelezaji huu wa miradi hii mikubwa ya mikakati, lengo kubwa ni kuzalisha ajira na katika maeneo ambayo mradi unatekelezwa na kwa Watanzania wote kwa ujumla. Kwa hiyo nimwahidi na hata yeye anafahamu, hata zile kazi za awali za madereva zilizotangazwa, zimetangazwa kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibiti na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Rufiji na Wakuu wa Wilaya wa Mkoa wa Morogoro. Kwa hiyo ni wazi kabisa kipaumbele kwa watakaokuwa na sifa wanaostahili, lakini zipo kazi za kawaida za vibarua mbalimbali, watapata wananchi wa Kibiti na wananchi wa Wilaya ya Rufiji na wa maeneo ya Mkoa wa Morogoro. Kwa hiyo hilo kwa kweli halina mjadala, ndivyo ambavyo tumelipangilia. Ahsante sana.
MHE. ALLY SEIF UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, nina maswali mawili ya nyongeza, moja kwa kuwa sasa wananchi hawa wa Delta wamesubiri sana kwa muda mrefu umeme wa solar; Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwapelekea hata taa katika wakati huu mfupi ili waweze kujipatia huduma kwenye vituo vya afya na shule?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa wananchi wa Lungungu, Nyamatanga, Lwaluke, Kikale, Mtunda, kuna laini kubwa ambayo imepita na tayari kazi imekamilika. Je, lini umeme utakwenda kuwashwa kwenye maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Ungando hii ni mara ya tatu anawaulizia wananchi wa Visiwa vya Delta, kwa kuwa ni Mbunge wa Mkoa wa Pwani natambua Visiwa hivyo na nimefanya ziara kimoja hadi kimoja vyote pamoja naye Mheshimiwa Mbunge Ally Seif Ungando.

Mheshimiwa Naibu Spika, atakubaliana na mimi kwamba kwa kuwa Serikali yetu ina nia ya kufikisha umeme vijiji vyote nchini, na kwa kuzingatia yapo maeneo kama 89 hivi ambayo yako Visiwani na wao lakini wana haki ya kupata umeme. Ndiyo maana kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Serikali iliamua kufanya upembuzi yakinifu kuainisha mahitaji na kumpata mzabuni mkandarasi ambaye atafanya kazi hiyo na mchakato huo unakamilika tarehe 26 Juni, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ameainisha kwa kuwa huu muda wa mchakato mpaka mkandarasi, inawezekana ikachukua muda mrefu anauliza namna gani Serikali inaweza ikatumia mkakati wa muda mfupi wa kuwezesha hususan taasisi za umma ikiwemo kituo cha afya cha Mbwera. Tunaishukuru sana Serikali kwa mara ya kwanza kutupatia fedha za kujenga kituo cha afya Mbwera, kinapatiwa umeme mara baada ya kuanza shughuli zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge hilo tumelipokea na Wakala wa Nishati Vijijini katika maeneo ya Kiongoroni, Kiechuru, Kiasi na Mbwera itafanya kupeleka mfumo wa taa kwa ajili ya taasisi za umma ili zitoe huduma kabla mradi huu wa kupeleka nishati ya solar katika maeneo hayo kwa ajili ya matumizi ya wananchi na wa taasisi za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge ameyaulizia maeneo ya Lungungu, maeneo ya Rwaluke, maeneo ya Nyamatanga, maeneo ya Mtunda. Maeneo haya kulikuwa na mradi wa REA Awamu ya Pili na mkandarasi hakufanya vizuri lakini Serikali hii inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli iliamua kuanza tena mchakato na maeneo yale ambayo kazi haikukamilika ilipewa TANESCO na baada ya kupewa TANESCO wameendelea na kazi. Nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge ajiandae ili twende tukazindue kuwasha umeme kuanzia Jumatano wiki ijayo mara baada ya kuhitimisha bajeti yetu ya Serikali. Tutafanya sherehe kubwa sana katika maeneo haya kwa kuwa wamesubiri muda mrefu. Kwa hiyo, niwataarifu wakati wa Kibiti kwamba maeneo haya ambayo mmesubiri Serikali imefanya kazi na tutawasha umeme kwa kishindo. Ahsante sana.