Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Susan Anselm Jerome Lyimo (84 total)

MHE. SUZAN A. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni wazi kwamba Tanzania imeathirika sana na mabadiliko ya tabianchi, lakini vilevile sababu kubwa pamoja na kwamba kuna sababu za nje, lakini kuna sababu za ndani ambayo kubwa ni ukataji hovyo wa miti, lakini Serikali kwa muda mrefu imekuwa na kaulimbiu ya kusema kwamba kata mti panda miti.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nilikuwa nasikiliza au naangalia vyombo vya habari hapa Dodoma ambapo ni kati kati ya nchi na Makao Makuu, Mkuu wa Mkoa alikuwa anapanda miti na ikatolewa taarifa kwamba katika miti milioni mbili na laki tatu iliyopandwa ni miti mia tisa tu imeota, sawa na asilimia 0.039. Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba wanafuatilia ili miti inapopandwa iweze kuota ili kuondoa tatizo la mabadiliko ya tabianchi?
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ukataji miti na suala la kupanda miti isiote. Sasa hivi tunaandaa mkakati wa pamoja, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, pamoja na Maliasili na Utalii na wadau wengine kuhusu mkakati wa Taifa hili katika kuhakikisha kwamba tunapanda miti ya kutosha nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, tunawashirikisha kwa karibu sana wataalam wetu wa Chuo cha SUA ili kuweza kujua ni miti gani au ya aina gani inaweza kuzalishwa katika mazingira ya mkoa gani ikastawi kwa uzuri zaidi.Katika kufanya hivyo tayari report ya kwanza tumekwishaipata na tutahakikisha kwamba tunawashauri mikoa mbalimbali namna ya upandaji miti kulingana na mazingira waliyonayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nichukue wito huu kuwahamasisha Watanzania wote, tumeshaagiza kila Halmashauri kupanda miti 1,500,000 kila Wilaya kwa mwaka. Zoezi hili lifanyike na tutahakikisha kwamba wataalam wetu wanawasaidia katika kuhakikisha kwamba mbegu zinapatikana, zinazokubalika kulingana na mazingira hayo na wananchi wapande miti yenye faida na wao miti ya matunda na miti ya mbao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema pia hata suala ambalo lilizungumzwa jana na Mheshimiwa hapa kwamba, unapanda miti lakini mwisho wa siku viwanda vyetu vya juice vinakosa matunda ambayo yanastahili kwa ajili ya juice hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huu tunafanya utafiti pia wa kutosha kuona kwamba, miti inayopandwa, inatuletea na inatupatia matunda ambayo yatakuwa ni chanzo cha raw material kwa ajili ya viwanda vyetu vinavyojengwa hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, najua kwamba vyanzo vya kipindupindu hasa ni uchafu na hasa katika maeneo ya mikusanyiko kama vile kwenye masoko. Kwenye haya masoko huwa watu wanalipa kodi, lakini Serikali inashindwa kufanya usafi au kuzoa takataka. Je, Serikali sasa haioni kwamba yenyewe ndiyo chanzo cha kipindupindu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa sasa hivi kuna tahadhari kubwa sana ya ugonjwa wa homa ya zika ambayo homa hii sasa hivi iko kule Marekani ya Kusini, lakini Tanzania siyo kisiwa na wote tunajua kwamba zika ilianzia Uganda kwenye Milima ya Zika miaka hiyo ya 1920 au 1930 huko. Kwa hiyo, bado jana nimemsikia mtendaji mkuu wa World Health Organization akisema kwamba, kuwe na tahadhari.
Je, Tanzania kama nchi imejiandaaje hasa ukizingatia kwamba, wakati ugojwa wa ebola umetokea zile specimen zilipelekwa Nairobi, je, sasa hivi ukitokea hapa Tanzania tumejiandaje kama Serikali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Serikali yenyewe ndiyo chanzo cha kipindupindu si kweli na naomba niseme tu jukumu la usafi, ni jukumu la kila mtu, kuanzia usafi wa mwili wake, usafi wa nyumba yake, usafi wa mahali pake pa kazi,ni jukumu la kila mtu na si jukumu la Serikali. Serikali ni mratibu kwenye uteketezaji wa taka ambayo ni hatua ya mwisho ya usafi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu ugonjwa wa zika Serikali imejiandaaje? Serikali imekwishachukua hatua za awali za kufanya matayarisho ya kujikinga na ugonjwa huu. Kwanza, nitumie nafasi hii kuwatoa hofu Watanzania wote kwamba ugonjwa huu bado haujaingia kwenye nchi yetu wala kwenye nchi za jirani. Tahadhari kubwa ambayo tumechukua ni kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwanza kutoa tamko la uwepo wa ugonjwa huu kwenye nchi nyingine. Hiyo ni hatua ya kwanza ya kiepidemolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili, ni kutoa taarifa za ukweli kuhusu ugonjwa yaani fact sheet, ambayo tayari Waziri wa Afya kwa mamlaka yake amekwishatoa taarifa sahihi zinazohusu ugonjwa wa homa ya zika na zimetawanywa nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ni kuweka mikakati ya kuripoti mtu yeyote yule ambaye atafika kwenye vituo vya kutolea huduma na ikaonekana ana dalili zinazofanana na ugonjwa wa homa ya zika kuleta taarifa hizo centre ili tuweze kuangalia kama anaweza akawa ameambukizwa na ugonjwa huu ama la.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ndio taratibu za kiepidemolojia za kufanya udhibiti wa ugonjwa wa mlipuko katika hatua ya awali ambapo ugonjwa bado haujangia nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuwatoa hofu Watanzania kwamba ugonjwa huu sio hatari katika viwango vya ugonjwa kama wa ebola, denge, ama West Nile fever kwa sababu ugonjwa huu unasababisha tu homa ndogo ndogo lakini una madhara makubwa kwa akinamama wajawazito walio kwenye first trimester, wenye mimba changa, kwamba wanaweza wakazaa watoto wenye vichwa vidogo. Nakushukuru.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 20 Oktoba, 2015 aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne alipokea magari ya washawasha 399 kati ya magari 777. Kati ya magari hayo ni magari 50 tu yalitumika. Nime-google bei ya gari moja ni sawa kabisa na kipimo cha MRI na Scanner kwa maana ya kwamba gari moja ni kama dola 400 na hiyo mashine bei yake ni hiyohiyo.
MWENYEKITI: Dola 400?
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Dola 400,000. Je, ni kwa nini sasa Serikali haioni kwamba huo ni upotevu mkubwa wa fedha na kutokuwajali wananchi na kwamba fedha hizo zingetosha kununua Scanner na MRI kwa nchi nzima kwenye Hospitali zote za Rufaa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSI, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba magari ya washawasha yamenunuliwa na hayana tija. Magari ya washawasha yamenunuliwa ikiwa ni miongoni mwa ile programu ya kununua magari 777 kwa ajili ya matumizi ya Askari. Kwa hiyo, magari haya yamesaidia sana na bado mengine yatafika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kipolisi. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, ninataka kujua hii Hospitali ya Wilaya ambayo inajengwa hapo Kivule inagharimu kiasi gani kwa sababu mpaka sasa hivi anasema zimeshatoka shilingi milioni 1.9?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla una idadi kubwa sana ya wananchi na hospitali nyingi zimepandishwa hadhi. Kwa mfano, Hospitali ya Amana - Ilala ambapo wananchi wa Kivule wanakwenda pale, lakini mpaka leo huduma za afya bado ni mbovu sana.
Je, sasa Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba hospitali hizi zinazopandishwa hadhi ikiwemo na hii inayojengwa, inakidhi mahitaji ili wananchi waweze kupata huduma ya afya ambayo ni haki yao ya msingi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kama alivyosema ni kweli sehemu ya Kivule ina changamoto kubwa sana, ndiyo maana tumeamua ujenzi wa ile hospitali ya Wilaya na kwa miundombinu yote mpaka inakamilika, hospitali ya Wilaya inagharimu takriban bilioni 24, lakini katika zoezi la kwanza ambapo katika bajeti niliyosema kwamba kumetengwa shilingi milioni 900 ya kwanza, na mkandarasai yuko site na ameshaanza stage ya foundation. Mkataba uliosainiwa na Skol Building Contractors Limited utagharimu karibu shilingi bilioni moja na milioni 19.
Mheshimiwa Spika, huu ujenzi maana yake utafanikisha sasa angalau sehemu ya OPD ianze kukamilika, katika sehemu ya pili ni kwamba Hospitali ya Amana imepandishwa hadhi ni kweli, lakini ukiangalia Manispaa ya Ilala ni eneo lina changamoto kubwa sana na ndiyo maana tunajenga Hospitali ya Kivule. Sambamba na hilo kwa sababu Jimbo la Ilala ni pana, kulikuwa na harakati ya kujenga sehemu maalum ya akina mama na watoto katika eneo la Chanika katika kituo cha afya cha Chanika.
Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Wizara ya Afya na Serikali kwa ujumla kwamba ni nini kimefanya katika maeneo hayo ni kupandisha vituo viwili vya Pugu pamoja na Chanika, sambamba na hilo maana yake jambo linalofanyika maeneo ya kati ya Ilala ambayo imetanuka kuna zahanati nyingi ambazo nimezisema pale awali ambazo zinafanyiwa ukarabati na zingingine kuhakikisha kwamba vituo vyake vya afya vinafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Spika, kwa nini sasa hii hospitali ikipandishwa hadhi itaweza kufanyakazi vizuri, ndiyo maana katika bajeti ya mchakato wa mwaka huu mtaona kwamba bajeti ya Wizara ya Afya itakuwa imejielekeza kwa kiwango kikubwa kuhakikisha kwamba bajeti ya dawa inaongezeka kwa kiwango kikubwa kukidhi hili ongezeko la watu na ongezeko la mahitaji ya wananchi katika sekta ya afya.
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi, lakini lazima ni-admit kwamba nimefedheheshwa sana na majibu ya Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba elimu imeporomoka kama ambavyo amekiri lakini hajatupa mikakati. Katika majibu yake ya msingi anasema kwamba Walimu wamekuwa na morali, ni wazi kwamba Serikali labda haijui maana ya motivation theories na hawa Walimu wanapata motive gani. Ni wazi hilo suala la umeme miaka ya 60, 70 hapakuwa na umeme lakini nyumba za Walimu zilionekana. Sasa hivi mtoto anaona aibu kusema yeye ni mtoto wa Mwalimu, anaona afadhali hata aseme ni mtoto wa Mmachinga.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunavyoongea Walimu...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Susan, naomba uende kwenye swali tafadhali.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye swali, nataka kujua kama tuna tatizo kubwa la Walimu, Walimu wame-graduate toka mwaka jana mwezi wa tano mpaka leo tunapoongea hawajaajiriwa, hiyo ndiyo motisha? Kwa hiyo, naomba kujua ni lini Walimu waliomaliza masomo yao wanapata ajira zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, moja ya mikakati ni kuhakikisha kwamba Walimu wanapata mafunzo, lakini ukisoma ripoti ya CAG inaonesha Walimu hawajakwenda mafunzo, ni asilimia 11 ya Walimu wa sekondari ndiyo tu wanapata in-service program na Walimu wa primary ni asilimia 30. Ni lini Walimu hawa watapata in service training ili waweze kuendana na mazingira halisi ya ualimu na hasa kuhakikisha kwamba elimu yetu haiporomoki?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli tulivyoeleza kwamba Walimu wameanza kupata motisha kwa sura mbalimbali hasa za mazingira wezeshi na ni jambo endelevu. Hata hivyo, katika suala la ajira huwezi kuajiri mtu kabla hujamwekea bajeti yake. Katika mwezi huu unaoanza mpaka mwishoni kuna mpango wa kuajiri Walimu. Kwa misingi hiyo, mimi nafahamu kwamba kumaliza ni namba moja na kuajiriwa ni namba mbili, lakini kwa taratibu ambapo lazima uwe umeshamwandalia stahiki zake zote ili kupunguza malalamiko yasiyo ya lazima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusu Walimu kutopewa mafunzo ya ziada kama ambavyo imeelezwa katika taarifa ya Mkaguzi Mkuu, niseme tu kwamba, hili suala ni endelevu, hata hivi tunavyoongea sasa hivi kuna mafunzo yanayoendelea huko Mwanza na wiki iliyopita kuna mafunzo yalikuwa Iringa. Kwa hiyo, suala hilo haliwezi kukamilika kwa siku moja lakini kimsingi Wizara imedhamiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachosema ni kwamba, fedha inayotengwa kwenye bajeti haendi katika Wizara ya Elimu peke yake, inaenda katika Wizara mbalimbali na kila Wizara kama tulivyojionea ina umuhimu wake. Kwa hiyo, tutakwenda hivyo hivyo kutokana na kiasi kile kinachopatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kuna msemo wa Kiswahili unaosema samaki mkunje angali mbichi. Ujenzi wa kituo hicho hautakuwa na maana kama hatujawekeza huku chini. Tunatambua kwamba wakati Serikali inapanua elimu walihakikisha kabisa viwanja katika shule zetu za msingi havipo kwa maana kwamba walijenga shule za pili. Je, Serikali inasema nini kuhakikisha kwamba shule zetu za msingi zina viwanja ili watoto waanze kucheza riadha au michezo mingine ili sasa hivi vituo wanavyovijenga huku juu viwe na maana?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza siyo kweli kwamba Serikali ilihakikisha kwamba shule hizi hazina viwanja. Bahati mbaya iliyotokea yako baadhi ya maeneo ambapo suala la kutenga viwanja vya kutosha halikuzingatiwa wakati wanapanga mipango na maeneo mengine viwanja vilichukuliwa vikabadilishwa matumizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeendelea kusisitiza kwanza katika kila mpango wa ardhi kuhakikisha tunatenga maeneo ya michezo siyo tu kwenye shule, lakini maeneo ya michezo yatengwe kwenye makazi ya watu ili kurahisisha watu kushiriki michezo kwenye maeneo yao ya makazi. Pili, tumeendelea kukagua na kurudisha maeneo ambayo yamevamiwa na kubadilishwa matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Waheshimiwa Wabunge ninyi ni Madiwani tusaidieni mambo mawili. La kwanza, hakikisheni hakuna mipango ya matumizi ya ardhi inapitishwa wakati hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo.
Pili, shule hizi zinaendeshwa na kumilikiwa na halmashauri zetu. Sisi Waheshimiwa Wabunge ambao ni Madiwani tukiwa wakali kwenye kubadilisha matumizi ya maeneo yetu bila shaka viwanja vitapatikana na michezo yetu itaendelea. Nakubaliana na wewe michezo ili iendelee lazima ianze ngazi ya chini, habari ya kuanzia ngazi ya juu tutapoteza muda wetu bure.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niulize swali moja dogo la nyongeza. Ukiangalia katika majibu amesema kwamba, mabadiliko haya yanafanywa baada ya utafiti, baada ya wataalam kuleta taarifa mbalimbali. Naomba kujua GPA imetumika kuanzia mwaka 2013 na sasa 2015 tayari imebadilika imekuwa madaraja, yaani ilikuwa madaraja ikaja GPA within a year, sasa naomba kujua huo utafiti ulifanywa lini hasa ikizingatiwa wataalam walioko Baraza la Mitihani ni wale wale kuanzia Mtendaji Mkuu? Kwa hiyo, naomba kujua huo utafiti umefanywa wapi na mazingira ya jamii ni watu gani walitaka hasa wabadilishwe kutoka madaraja kwenda GPA na kurudi tena kwenye madaraja?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kimsingi wakati huu mfumo wa GPA unaanza kutumika ulikuwa pia uanze katika misingi ya majaribio. Lengo lilikuwa ni kufanya kwamba, toka mwanafunzi anapokuwa katika hatua za awali yaani katika sekondari na kuendelea aweze kuwa na mfumo mmoja unaokwenda mpaka vyuo vikuu. Kwa sababu unakuta vyuo vikuu tunatumia GPA, lakini huku chini tulikuwa tunatumia division na kwa kweli lilikuwa ni jambo jema tu, lakini kukawa na maneno tena ya malalamiko mbalimbali kupitia vyombo, kama jana ulivyoona Mheshimiwa Susan Lyimo ulisema kwamba hata magazeti na yenyewe pia ni nyaraka sahihi kutumika katika Bunge letu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maneno haya yamekuwa yakitoka katika pressure mbalimbali na hata hivyo baada ya kupitisha huu mfumo wa division hii juzi, nafahamu kuna magazeti mengi hata Waheshimiwa Wabunge walipongeza. Sasa mjue tu kwamba ni hayo mawazo yetu tunayoyatoa na Serikali ni wajibu wake kufanyia kazi. Ahsante sana.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri ametoa ufafanuzi mzuri, ningependa tu kuongezea pale alipojibu Mheshimiwa Naibu Waziri, kwamba kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri hata huu mfumo wa GPA ulitokana na maoni ya wadau. Hata hivyo, baada ya Serikali kutekeleza, wadau tena wakawa wameleta malalamiko, kwa hiyo, lazima Serikali tuweze kuyafanyia kazi kadri mahitaji yanavyojitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwasihi Watanzania tunapopewa nafasi ya kutoa maoni, tuitumie nafasi hiyo kutoa maoni ya dhati kabisa. Kwa sababu tunatoa maoni, Serikali inapotekeleza halafu tena kuna kuwa na malalamiko kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amesema. Vilevile ningependa pia kuchukua nafasi hii kumwambia Mheshimiwa Ndugu yangu Mwita Waitara kwamba hii Sheria ya Baraza la Mitihani akisoma kifungu cha nne, kinatoa fursa kwa wananchi kutoa maoni kwa Baraza la Mitihani kuhusiana na masuala ya uendeshaji mitihani na maoni yao yanazingatiwa. (Makofi)
Kwa hiyo, siyo kwamba tu imempa mamlaka Waziri wa Elimu, lakini vilevile imetoa fursa kwa maoni kutolewa na naomba kama kuna maoni yoyote ambayo yana tija, basi wahakikishe na yatafanyiwa kazi.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, ni kweli sijaridhikia kwa sababu ukiangalia kwa miaka takribani kumi toka wameanza kujenga hivi vipande vidogo vidogo wamejenga kilometa 19 tu, ina maana hizi kilometa 96 labda zitatumia miaka mingine 30.
Swali, kwa kuwa barabara hii sasa ilianza kujengwa kwa vipande vya lami toka mwaka 2008 ambapo lami zile ziliziba kabisa makalavati hali inayopelekea wananchi wa Ndungu na Maore ama kufariki au mazao yao kuharibika kutokana na mvua au maji yale yanayotuama.
Je, ni lini sasa mtahakikisha kwamba makalavati yale yanajengwa ili watani zangu kule wasipate matatizo pamoja na vifo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naelekea kwangu sasa, kwa kuwa barabara ya Kawawa hadi Marangu Mtoni ilijengwa kwa lami mpaka kiasi cha nusu, lakini cha ajabu barabara hiyo imejengwa kiwango cha lami madaraja yote hayajajengwa hali ambayo inapelekea magari kuanguka na watu wameshafariki, ni lini madaraja katika barabara hiyo yatajengwa hasa ukizingatia land scape ya Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwa upande wa barabara hiyo ambayo umeisema haina lami na ni barabara pekee isiyo na lami..
SPIKA: Ni katika barabara za TANROADS za Mkoa.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kama tulivyosema katika jibu la msingi kwamba sasa tumedhamiria kuijenga barabara hiyo yote kwa lami na tutaanzia na upembuzi yakinifu pamoja na usanifu wa kina ambao unafanyika katika mwaka huu ujao wa 2016/2017 wa fedha na ninaamini Waheshimiwa Wabunge mtaipitisha bajeti yetu ili tuweze kuifanya hiyo kazi tuweze kutekeleza ahadi za viongozi wetu wawili waliopita kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wa maeneo hayo wanapenda.
Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili nimejulishwa na CEO wa TANROADS kwamba amelisikia na tutakuja kulitolea jibu wakati wa bajeti ya Wizara.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipatia nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo wote tunajua kuna tatizo kubwa sana la madawati na Halmashauri nyingi sasa hivi zinatengeneza madawati. Swali langu la msingi ni kwamba, je, ni nani anayedhibiti ubora wa madawati hayo? Kwa sababu yawezekana kabisa mbao hizo wakati mwingine zinaweza zikawa hazijakauka vizuri na maana yake ni kwamba hayo madawati hayatadumu. Swali langu ni nani anayedhibiti kuhakikisha kwamba mbao zinazotengeneza madawati hayo ni bora na zimekauka ili isiwe tunafanya kazi ya zimamoto? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la quality control (ubora wa madawati) ndiyo maana Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imegawanyika katika Halmashauri na Mikoa na huko tuna watu tunaita wahandisi au mainjinia ambao jukumu lao kubwa kwa kila kitu kinachotengenezwa sio madawati peke yake hata majengo, kuhakikisha wanazingatia viwango vya ubora ili tupate vitu katika ubora unaokusudiwa. Kwa hiyo, tuliowapa dhamana hii ni Wahandisi wa Halmashauri wetu kuhakikisha kwanza madawati hayo yanakidhi vigezo siyo kwa ajili ya uvyevunyevu peke yake hata mbao ya aina gani inatumika ili tupate madawati siyo ya kutumika mwaka mmoja bali ya muda mrefu.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumzia suala la uhaba wa bajeti lakini naomba kuuliza; Benjamin Mkapa Foundation wamejenga vituo vya afya kule mkoa wa Rukwa ambako kuna matatizo makubwa sana; kwa mfano kuna Zahanati ya Kala - Nkasi, Milepa – Sumbawanga, Ngorotwa – Kalambo pamoja na ile ya Kishapu na wamekabidhi kwa Halmashauri toka Juni 2014, lakini mpaka leo havijatumika wakati kuna matatizo makubwa sana, ni kwa nini Serikali haijaweza kuvitumia vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Pamoja na majibu mazuri naomba nimsaidie Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu kwamba suala hili ni kwa nini, ni kwa sababu taratibu za makabidhiano bado zinaendelea. Pindi taratibu hizo zitakapokamilika tutakabidhi majengo hayo kwa Halmashauri.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, disability is not inability. Kwa muda mrefu tumepiga kelele sana kwamba majengo hasa madarasa yawe disabaility friendly ili watoto wenye ulemavu waweze kusoma, lakini mpaka leo tunashuhudia madarasa yanajengwa hayana ngazi za kuwasaidia au ramps ili hawa watoto waweze kusoma kama wenzao na kwa kufanya hivyo suala la kwamba waongezewe muda wa kustaafu halitakuwepo. Serikali inatoa kauli gani kuhakikisha kwamba majengo yote ya Serikali yanakuwa disability friendly ili watoto waweze kuingia madarasani toka wakiwa na umri mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme tu wazi kwamba dhana ya elimu shirikishi au dhana ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za jamii kwa watu wenye ulemavu inaendana kabisa na kubadilisha mazingira ili kumfanya mtu mwenye ulemavu afike pale anapotaka bila vikwazo vyovyote vile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Ofisi ya Waziri Mkuu ilishatoa maagizo kwa Halmashauri mbalimbali ambazo zinahusika na ujenzi wa miundombinu mbalimbali kuhakikisha kwamba majengo yanayojengwa hasa ya shule yanakuwa ni shirikishi, yana hali ya kumfanya mtu mwenye ulemavu afike bila matatizo yoyote darasani. Siyo tu kwamba yalikuwa maagizo bali hilo ni takwa la Sheria Na. 9 ya mwaka 2010. Kwa hiyo, niseme tu kilichobakia ni kufuatilia utekelezaji wa sheria hiyo.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na sababu ambazo Mheshimiwa Waziri amezizungumza, naamini kabisa baadhi ya ajali, tena ajali nyingi sana zinatokea kwa sababu ya kutokuwa na alama barabarani pamoja na matuta makubwa sana. Tulishasema hapa Bungeni matuta yawe na standards. Ni lini Serikali itafanya matuta nchi nzima yawe ya standard ili kuepusha ajali ambazo siyo za lazima?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kudhibiti ajali barabarani ni suala ambalo ni mtambuka linahusisha taasisi mbalimbali. Kwa mfano, suala ambalo Mheshimiwa Suzan Lyimo amelizungumza ni la msingi, ambalo kwa upande wa Serikali linahusisha Wizara ya Ujenzi na ndiyo maana tukawa na mkakati kabambe wa kushirikisha wadau wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda muafaka utakapofika tunaweza tukauanika mpango huu, tupo katika hatua nzuri ambapo tuna ushirikiano mzuri na SUMATRA, Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS, TBS na shule za udereva pamoja na Polisi, tunakaa pamoja ili tuweze kuwa na utatuzi wa kudumu wa matatizo ya ajali kwa kuunganisha nguvu kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe tu wasiwasi kwamba mambo hayo tunayafanyia kazi na wakati muafaka utakapofika basi tutauweka hadharani.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tatizo la shule hasa Kidato cha Tano na cha Sita ni la Kitaifa na hii inatokana na azma ya Serikali ya kuongeza Shule za Kata ambazo zilianzia Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne. Nimeshangaa sana Naibu Waziri alipozugumzia kwamba hizi Shule za Kidato cha Tano na cha Sita ni za Kitaifa lakini hapo hapo anazungumzia habari ya Halmashauri kuendelea kujenga shule hizi. Je, anaweza akatuambia baada ya shule hizi za Kata, kuanzia Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne, Serikali imeshajenga shule ngapi za Kidato cha Tano na cha Sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwalimu Suzan Lyimo anafahamu, unapozungumzia Minaki, Tabora, Ilboru, Mzumbe zote ni Shule za Kitaifa hizo. Kwa hiyo, nilikuwa na maana kwamba huo ni msingi wa Shule za Kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tulielezea, kwa sababu tulikuwa na mchango mkubwa sana katika ujenzi wa shule za Kata na kila Halmashauri ilielekezwa kwa sababu watoto wengi watafaulu katika elimu ya Form Four, lakini idadi yetu ya shule zitakuwa ni chache kuwa-accommodate hao wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana kila Halmashauri imeelekezwa kufanya kila liwezekanalo miongoni mwa shule zao kubainisha miongoni mwa shule nyingine ziweze kuchukua advanced level, Form Five na Form Six. Hata hivyo, haikatazi, japokuwa wamekuza; mfano Shule ya Mchinga itakapokuwa Form Five na Form Six haitakataza mtoto kutoka Wanging‟ombe kwenda kule Mchinga, maana yake itakuwa ni room hiyo, watu kwenda maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ajenda yetu kubwa ni nini? Ni watu kupata elimu kadri iwezekanavyo. Amesema idadi ya takwimu, hata ukiangalia katika kanuni, nitampa takwimu, idadi halisi ya jinsi gani mchakato umekwenda. Sitaki kukupa jibu ambalo halitakuwa sawasawa hapa.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Tatizo la uhaba wa umeme ni kubwa sana nchi nzima, na hili linatokana na gharama kubwa ya nguzo. Nilikuwa naomba kujua ni lini Serikali itachukua ushauri kwamba nguzo ziwe ni gharama za Serikali lakini zile gharama nyingine ziwe ni za watu binafsi kama ilivyokuwa kwenye masuala mazima ya simu, kwamba nguzo za simu zilikuwa bure, ni kwa nini Serikali isifanye utaratibu huo ili wananchi wengi waweze kupata umeme?
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kukatikatika kwa umeme pia kunachangiwa na uharibifu wa nguzo. Lakini nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwamba kuanzia mwezi Januari mwaka huu TANESCO sasa inaanza kutengeneza nguzo zinazoitwa concrete pole, nguzo ambazo ni za concrete, ambazo zitakuwa haziozi. Nguzo hizo sasa zitahakikisha kwamba nguzo zitakuwa hazianguki na kukatikakatika kwa umeme kutakoma mara moja.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaitwa Susan Lyimo. Nashukuru kwa majibu mafupi sana ambayo hayana uelekeo; nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Kamati ya UKIMWI ilipotembelea MSD, pamoja na mambo mengine ilipata taarifa kwamba kuna shehena kubwa sana ya dawa za UKIMWI ambayo ilikwama bandarini kwa sababu ya kutokulipa VAT, nataka kujua kama dawa zile tayari yameshaondoka bandarini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; natambua kwamba wafadhili wengi walisema watajitoa na hivyo Serikali ikaanzisha Mfuko wa UKIMWI, nataka kujua mpaka sasa hivi mfuko huo una kiasi gani cha fedha hasa ikizingatiwa kwamba wagonjwa hawa au waathirika hawa wakishaanza kutumia madawa wanapaswa kuendelea kuyanywa mpaka mwisho wa maisha yao. Nataka kujua mfuko huo toka umeanzishwa mpaka leo una kiasi gani cha fedha na tusipewe ahadi za uongo kama ambavyo tumesikia?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumtoa hofu kwamba Serikali haishindwi kuwahudumia wagonjwa wa UKIMWI katika nchi hii, lakini ni utaratibu wa kawaida tu wa kujenga mahusiano mema na marafiki ambao wanajitokeza kutusaidia kubeba mzigo mzito wa kutoa huduma za afya kwa watu wetu. Na huu ni utamaduni wa nchi zote duniani na haitarajiwi hata mara moja kwamba itafika siku wataamua ghafla kusitisha misaada hii ambayo wanaitoa kwa wagonjwa wa UKIMWI, lakini kama tutafika huko tayari tumeandaa fall back position kwa kuanzisha Mfuko wa UKIMWI anaouzungumzia, na mfuko huo tumeanza kuuwekea bajeti kwenye bajeti hii iliyopita na tumeanza kwa kiwango kidogo cha shilingi bilioni sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo waweze kuchangia fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye mfuko huu. Na nitoe rai kwake Mheshimiwa Mbunge na kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla tujitolee kuchangia Mfuko wetu wa UKIMWI kadri tutakavyoweza na pia hata kuvutia marafiki wawekeze kwenye mfuko huo ili iwe fall back position ambayo ina uwezo wa kutosha huko mbeleni kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisahau kuhusu shehena ya dawa, hakuna shehena ya dawa mpaka hivi sasa ambayo imekwama popote pale na kwamba dawa zinapatikana nchini kwa asilimia mia moja. Kwa sababu taarifa za dawa za UKIMWI na miradi misonge yote tunazipata kila wiki, kwa update niliyonayo kufikia Ijumaa iliyopita hakukuwa na shehena ya dawa iliyokwama bandarini, lakini dawa zote zipo kwenye bohari zetu za mikoa na bohari za kanda kwa kiwango cha asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nizungumzie jambo la kitaalam, tukisema kuna availability ya dawa kwa asilimia mia moja, tunamaanisha kwenye Bohari ya Taifa kuna dawa zinazojitosheleza kutumika kwa miezi sita mbele na kwenye bohari za mikoa tuna dawa za kujitosheleza kwa matumizi ya miezi mitatu mbele na kwenye bohari za wilaya tuna dawa za kujitosheleza kwa mwezi mmoja mbele hiyo ndiyo availability tunayoizungumzia ya asilimia mia moja, sasa kwenye dawa zote za miradi misonge zikiwemo dawa za UKIMWI tuna availabaility a hundred percent.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Ni wazi kwamba suala la Palliative Care yaani Tiba Shufaa hapa nchini halijaeleweka kabisa, naamini hata wewe labda huelewi na vilevile Wabunge wengi sana hawaelewi. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri sasa yuko tayari, kutoa semina kwa Wabunge wote ili wapate uelewa wa maana ya Palliative Care? Vilevile, elimu hii pia itolewe kwa wananchi wote ili waweze kulielewa na waweze kuwasaidia wagonjwa wetu ambao wanakufa katika mazingira magumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kwamba tuna tatizo kubwa la wahudumu wa afya, ambao pia hawana huo uelewa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba, kuna haja kubwa sasa ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na curriculum ya Palliative Care katika courses za undergraduate kama wanavyofanya wenzetu wa Kenya na Uganda ili sasa tuwe na wataalam wa kutosha kwa hii huduma, hasa tukizingatia sasa kwamba kuna magonjwa mengi ya kusendeka (chronic diseases) ambayo yako nyingi na kwa maana hiyo, wagonjwa ni wengi na hawapati huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali la kwanza, Waziri alikuwa ananinong’oneza hapa, uzuri Waziri wangu anakaa nyuma ya kiti cha kujibia maswali, kwamba yuko tayari kuleta semina kwa Wabunge wote kwa ajili ya kutoa elimu ya Tiba Shufaa (Palliative Care).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi Palliative Care ni nini? Kwenye mfumo wa afya, Palliative Care ni huduma ambayo inatolewa kwa wagonjwa ambao ni terminally ill, yaani wagonjwa ambao wanaumwa magonjwa ambayo sasa imefika wakati sayansi ya tiba haiwezi kuyatibu. Kinachofanyika sasa ni kutoa huduma ya kupunguza maumivu, lakini pia huduma ya ushauri nasaha na huduma ya kiroho (Spiritual Services). Kimsingi ni kumtibu mgonjwa holistically kwa kumtazama kwa ujumla wake, mgonjwa kama mgonjwa kama binadamu na sio kutazama ugonjwa ambao mgonjwa anaumwa.
Mheshimiwa Niabu Spika, swali lake la pili, kuhusu curriculum naomba kwanza nieleze jitihada za Serikali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tuna Sera ya Taifa, ambayo inatoa mwongozo kwenye huduma za tiba shufaa, ambayo mwezi Juni, 2016 imeanza kutumika. Sera hii inaelekeza sasa kuanzia mwaka huu vyuo vyote vinavyofundisha masomo ya Udaktari, Uuguzi, Ufamasia na Kada nyingine za afya waweke mtaala kwenye courses zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie jukwaa hili la kwako, kuwaagiza watu wote wanaoendesha vyuo vinavyotoa taaluma mbalimbali za kwenye sekta ya afya, kufuata mtaala ambao tayari umeandaliwa na Wizara yetu na waanze kuutumia kwenye masomo yanayoanza mwaka huu. Kwa hiyo, mtaala tunao tayari na nimeshaagiza sasa wautumie kufundishia.
MHE. SUSAN J. A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Katika siku hizi za karibuni, Tanzania tumepata sifa kubwa sana ya kuwa na chuo kikubwa sana Afrika Mashariki na Kati, Chuo Kikuu cha Dodoma; na chuo hiki kinaweza kuchukua takribani wanafunzi 40,000. Kwa mshangao mkubwa sana, leo Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeamua kufanya Chuo Kikuu cha Dodoma kuwa sehemu ya majengo ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, Serikali kwa kuleta utaratibu wa kubadili au wa kuchanganya wanafunzi na majengo ya Serikali (Wizara), maana yake ni kwamba tunachukua wanafunzi wetu kuwapekeleka kwenye simba. Nataka kujua huu ndiyo utaratibu wa kuhamia Dodoma kwa maana ya kubadilisha miundombinu ya elimu kuwa Ofisi za Serikali? Naomba majibu.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumfahamisha Mheshimiwa Suzan Lyimo kwamba pamoja na hayo aliyoyazungumza, ukweli ni kwamba chuo maana yake siyo majengo peke yake. Chuo maana yake ni majengo, Walimu pamoja na vitendea kazi vingine vya kufundisha na kufundishia. Kwa hali hiyo Chuo cha UDOM kilipojengwa kilijiwekea utaratibu wa namna gani kitakuwa kinakua sambamba na majengo. Kwa hiyo, kwa taasisi au Wizara kuhamia katika majengo haya ni kwa vile ni suala la muda mfupi na kwa sababu majengo hayo yalitokana na…
Kulingana na utaratibu na mipango yake ya kukua yalikuwa kwa sasa hayatumiki. Wizara zinatafutiwa maeneo yake ya kujenga, CDA wakishakamilisha kuleta viwanja hivyo, kila Wizara itakuwa na majengo yake katika eneo lake.
Kwa hiyo, niwaombe tu kwamba suala la kuhamia Dodoma, sisi kwetu tunaona ni suala lenye tija na litaongeza ufanisi mkubwa hasa kwa wananchi wetu kwa sababu sasa watakuwa wanapata huduma kiurahisi zaidi, ikizingatiwa kwamba Dodoma hata foleni hakuna na ni Makao Makuu ya nchi. Kwa hiyo, sisi Wizara tumejipanga na tutahakikisha kwamba tutahamia kwenye maeneo yetu muda ukifika.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa hapa ndani ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba nia ya Serikali katika kukiendeleza Chuo cha Dodoma ilijidhihirisha kutokana na nia njema ya Chama cha Mapinduzi kutoa ukumbi wake na kubadilisha matumizi kutoka kwenye matumizi ya Chama kuwa Chuo Kikuu cha Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hatua hiyo hiyo ya nia njema ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi, tunaendelea na mpango wa Taifa wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya kuhamishia Serikali Dodoma. Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge Majengo yatakayotumika na Serikali ni majengo ambayo Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilishayajenga na yakawa mengi. Kwa sababu majengo yale ni mengi na yamejengwa na Serikali hii, badala ya kuyaacha yaharibike bila kutumika, yatatumika na baadhi ya Wizara za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, majengo yale hayaingiliani na shughuli zozote za elimu pale UDOM. Nawahakikishia Watanzania wote, nazipongeza Wizara hizo kwa kuyalinda kwa kuyatumia majengo hayo.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa suala hili linahusu Jumuiya ya Afrika Mashariki, nilitaka kujua je, wastaafu wa Afrika Mashariki wa nchi nyingine walishalipwa lakini Tanzania imekuwa inasuasua na kuna sintofahamu wakati ambapo wengine wanasema wameshalipwa, bado tunatambua kuna wastaafu wengi wa Tanzania hawajalipwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka tamko la Serikali, je, wastaafu hao ni kweli wamelipwa wote na kama bado kuna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wastaafu wao au warithi wao wanapata fedha zao? Ahsante.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wastaafu hao wamelipwa na kama kuna madai zaidi wayawasilishe Serikalini tutayashughulikia kwa mujibu wa taratibu.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na majibu ya Serikali hususan Wizara ya Fedha kwamba wastaafu wote wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki walishalipwa mafao yao. Hapa nina check ya mzee mmoja ambaye anaitwa Mzee Malembeka na Mheshimiwa Naibu Waziri unamfahamu, katika madai yake alikuwa anadai shilingi milioni 15 Serikali imemlipa shilingi milioni tano tu. Sasa na hapa ni wazee wengi sana, naomba kauli ya Serikali.
Je, ni kweli kwamba wazee wastaafu wote wa Afrika Mashariki wamelipwa fedha zao na kwamba hawaidai Serikali? Atoe tu tamko ili tujue hili jambo limekwisha au bado wazee hawa wanaidai Serikali.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lako Tukufu linajua ilishatolewa kauli ya Serikali ndani ya Bunge hili kuhusu malipo ya wastaafu wa Afrika Mashariki kwamba wastaafu wote walishalipwa. Kama nilivyosema hiyo ndiyo kauli ya Serikali iliyotolewa ndani ya Bunge hili, tulishafungua milango mtu ambaye anaona hajalipwa ana udhibitisho Wizara ipo tayari kumpokea na tuweze kuhakiki na kumlipa malipo yake.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Naomba nirudie hapo hapo aliposema Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Waziri, tarehe 08/07/2016 Majaji wawili; Jaji Lila na Jaji Munisi walitoa hukumu in favour ya Rebecca Gyumi kuhusiana na suala la vifungu vya 13 na 17 kwenye suala la Sheria ya Ndoa. Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza agizo la Mahakama Kuu ili kufuta vifungu vya 13 na 17?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maamuzi yale Serikali imekata rufaa. Kwa mujibu wa sheria ya Basic Rights and Duties Enforcement Act, kama ni kesi ya kikatiba, unapowasilisha notice ya kukata rufaa inasimamisha utekelezaji moja kwa moja wa maamuzi ya Mahakama. Kesi ile haikuwa na mambo haya ya ndoa tu, kuna mambo mengi yalijitokeza na hayo yote lazima tupate mwongozo wa Mahakama ya Rufaa. Kwa hiyo, naomba kuwasihi Waheshimiwa Wabunge wawe na subira hadi hapo Mahakama itakapotoa maamuzi.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali, lakini ni wazi kwamba siku za nyuma kulikuwa na mgogoro kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Bwana Siro kuhusiana na suala hili. Naomba kujua wakati ambapo Polisi walisema hakuna, lakini Mkuu wa Mkoa alikuwa anasema zipo. Je, huu mgogoro umeishia wapi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba hakukuwa na mgogoro wowote kati ya Kamanda wa Kanda Maalum na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni viongozi wanaofanya kazi kwa pamoja na mara zote maelekezo ya Kamati ya Ulinzi na Usalama imekuwa ikielekezwa kwenye utekelezaji na shughuli hiyo imeendelea kufanyika na kama nilivyosema Mheshimiwa Waziri Mkuu alishaelekeza na Mikoa yote imeitikia na sisi kama Wizara tunawaelekeza wote wanaokuwa field kuhakikisha kwamba maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yanafanyiwa kazi bila kupunguza hata nukta.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Pamoja na upungufu huu, kuna tatizo kubwa sana la mgawanyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua, ni kwa nini Wizara ya TAMISEMI inapanga moja kwa moja badala ya kuhakikisha kwamba Halmashauri ndiyo zinakuwa na huo utaratibu kwa sababu wao ndio wanajua upungufu wa Walimu? Kwa hiyo, nataka kujua na kazi za Maafisa Elimu sasa itakuwa nini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kama ni wa sekta ya afya, basi Wizara ya Afya inaweza ikatoa tangazo na ikawaingiza kwenye ajira ya Serikali na baadaye taratibu nyingine za kiutumishi kufanywa na Wizara ya Utumishi na baadaye wale watumishi wanakabidhiwa TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma kulitokea matatizo kwamba tukiwapeleka huko hawafiki na ndiyo maana sisi TAMISEMI tukaamua kuwapangia mpaka na vituo vyao, lakini hatufanyi hivyo bila consultation na mamlaka husika, wanakuwa wanatuambia upungufu uko wapi na wapi na sisi tunaangalia kwa kuangalia ikama za shule husika au ikama za hospitali husika au zahanati au vituo vya afya husika ndiyo tunawapeleka. Ukiwaachia kule kinachotokea ni kitu cha ajabu kabisa cha tofauti sana na wengine hata hawafiki kule, ndio maana tulifanya hatua hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, endelea kutuamini tu kwa sababu bado tumefanya vizuri sana mpaka hao walimu wa sayansi ambao tumewapata, tulipowapangia, hawana option, wamekwenda mpaka kuripoti kwenye shule hizo. Ahsante sana.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikitishwa sana na majibu ya Wizara. Suala kwamba tuna wataalam wachache wa sayansi, sikubaliani nalo kwa sababu hivi karibuni tu Mheshimiwa Rais alikuwa ameishatoa kibali madaktari wetu 500 kwenda kufanya kazi nchini Kenya. Vilevile tunatumbua kwamba kuna manesi wengi wako mitaani hawajaajiriwa kwa sababu ya kukosa vibali.
Mheshimiwa Naib Spika, kwa hiyo, swali langu la msingi ninataka kuuliza ni kwamba ni kweli kwamba Mheshimiwa Waziri alitoa tamko na mimi nashukuru kwamba umesema waraka bado haujatoa na ninajua kwamba government moves with papers. Kwa kuwa masomo ya sayansi najua ni muhimu sana na kwa kuwa kwa bajeti ya mwaka huu ukiangalia tuna upungufu wa maabara nyingi sana, vilevile ili kumfanya mtoto asome sayansi inabidi kuwe na madarasa mazuri. Kwa mwaka huu tuna upungufu wa madarasa 158,000 na Serikali imesema inaweza ikajenga madarasa 2,000, hii ina maana itachukua miaka 79 kuweza kukamilisha hayo madarasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama lengo la Serikali ni kufanya watoto wetu wasome sayansi, nini mpango mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wanajenga mazingira mazuri na sio tu kutoa matamko wanafunzi wasome sayansi?
Swali la pili, kwa kuwa tunatambua kwamba nchi hii haihitaji tu wanasayansi bali pia inahitaji wengine, kwa mfano mameneja wanahitajika watu waliosoma, lawyers kama Mheshimiwa Naibu Spika na wengine, ni kwa nini sasa Serikali isihamasishe pia wanafunzi wasome masomo mengine kwa bidii?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Waziri Kivuli wa Wizara yetu Mheshimiwa Susan Lyimo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ieleweke bajeti zote za Wizara zinapitishwa na Bunge lako Tukufu na Bunge hili linao uwezo mkubwa sana wa kusema jambo hili lipewe kipaumbele au jambo hili lisubiri kidogo, kama ambavyo tumeona kwenye Wizara ya Maji wote kwa pamoja tumesema iongezewe fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imekuwa ikijitahidi sana kuhakikisha inatafuta wafadhili kila kona ya dunia kuhakikisha kwamba tunapunguza tatizo hilo. Mfano ni madarasa ambayo yamejengwa mwaka huu zaidi ya madarasa 2,000, vyoo tulivyojenga na hali hiyo itaendelea kufanyika hivyo. Pamoja na kwamba kwa upande wako Mheshinimwa Waziri Kivuli unaona hakuna upungufu wa wanasayansi, nataka nikuhakikishie kutokana na mikakati ya Serikali ya kutaka uchumi uwe uchumi wa viwanda, uchumi wa viwanda unaendeshwa na sekta tofauti tofauti, kwenye kiwanda utahitaji watu wa afya, kwenye kiwanda utahitaji watu wa ujuzi wa ufundi, kwenye kiwanda utahitaji mambo mengi, lakini hali kadhalika kwenye sehemu zetu za kuhudumia afya zinahitaji wataalam wa aina hiyo. Kwa hiyo, ukiangalia kwa mapana yake huwezi ku-plan kwa kuangalia leo unaangalia kwa mapana, sisi tunaona iko haja kubwa sana ya wanafunzi wetu kuchukua masomo ya sayansi kwa wingi zaidi ili kukidhi maeneo ambayo bado yana upungufu.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni pamoja na hiyo ya kusema kwamba tunatamka tamka, niseme tu kwamba suala siyo kutamka, unapohamasisha lugha unayotumia ni yoyote inayowezeshwa kutoa hamasa kwa wale vijana na wakafanya maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, samahani swali la pili la nyongeza yako naomba limenitoka kidogo, kama unaweza ukarudia.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba labda awe pia anaandika wakati mtu anauliza ili isimletee shida. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili niliuliza kwamba kwa sababu nchi hii nadhani pia ameshalijibu amechanganya kwamba kwa sababu tunahitaji wataalamu mbalimbali ni kwa nini pia Serikali isihamasishe masomo mengine, kwa sababu hatuhitaji tu wanasayansi tunahitaji variety ya watu.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi mbali ya hayo niliyomjibu ninayo ya kumuongezea na nilikuwa nataka nijue kama na wewe bado unakumbuka swali lako vizuri. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wanafunzi katika maeneo mengine Wizara yetu haijajikita kwenye sayansi peke yake. Kwa mfano sasa hivi tunaendelea kuona namna ambavyo tunaweza hata tukaingiza somo la kuwezesha wanafunzi katika masuala ya moyo (mindset). Unakuta mtu anao uwezo wa kufanya jambo lakini kwa sababu tu kimoyo hajawa tayari anashindwa hata kusoma. Kwa hiyo, kuna masomo mengi pamoja na hilo, lakini haya ya sayansi tumeyapa kipaumbele kutokana na uhaba wake mkubwa.(Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipatia nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo linatusikitisha ni kwamba pamoja na kupandishwa madaraja walimu hawa hawalipwi pesa zao suala ambalo linapelekea kila mwaka walimu hao kudai takribani shilingi bilioni 21. Je, Serikali haioni kutokuwapandisha madaraja na kutokuwalipa kunasababisha kulimbikiza madeni yao na ndiyo sababu inafanya walimu kutokuwa na motisha wa kazi? Ni lini sasa Serikali itawalipa fedha zao wanapopandishwa madaraja?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, unafahamu tumekuwa tukitoa taarifa mbalimbali ya madeni ya walimu ambayo tumekuwa tukiyalipa na tulisimama kwa ajili ya zoezi la uhakiki. Kwa hili naomba niwaambie, tumezungumza na hapa nilisema katika eneo langu la kwanza kwamba suala la malipo haya yote mwaka huu wa fedha unapokuja kila mtu atapata stahiki yake.
Serikali hii ya Awamu ya Tano lengo lake kubwa ni kuondoa hizi changamoto ndogo ndogo tulizokuwa nazo kwani tunataka tupate wafanyakazi wenye ari ya kutosha. Sisi ambao ni beneficiaries wa utekelezaji wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi lazima tuitekeleze, naomba nimhakikishie jambo hilo halina mashaka tutalitekeleza.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na nashukuru kwamba Serikali imetambua umuhimu wa Hospitali ya KCMC, na niseme tu kwamba hospitali hii ni ya rufaa na inahudumia zaidi ya watu milioni moja wa Kanda ya Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa masikitiko makubwa sana hospitali hii iliomba Serikali zaidi ya shilingi bilioni nne mwaka jana kwa ajili ya huduma za cancer ambazo hospitali ile inaanza kuzitoa, lakini mpaka tunafika Machi bado Serikali ilikuwa haijatoa na Mheshimiwa Naibu Waziri mimi kama Mjumbe wa Kamati nalitambua hilo. Lakini je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha hizo ili hospitali ile iweze kuwahudumia wananchi wa Kanda ya Kaskazini kutoka Singida mpaka Arusha na Tanga?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba mnafanya kazi na TAMISEMI ili kuhakikisha kwamba zile Hospitali za Rufaa za Mikoa kama vile Mawenzi na Mount Meru ziweze kutoa huduma ili kupunguza idadi kubwa ya watu wanaoenda Hospitali ya KCMC, lakini hapa ninavyoongea Hospitali ya Mawenzi Mkoa wa Kilimanjaro na Hospitali ya Mount Meru ziko katika hali mbaya sana, jamboambalo linafanya wagonjwa katika hospitali hizo waendelee kwenda KCMC hospitali ambayo pia Wizara bado imeshindwa kuipatia vifaa tiba kamaambavyo wameomba. Je, sasa mna mpango gani kuhakikisha kwamba hospitali hizi za Mikoa ya Mawenzi na Mount Meru zinakarabatiwa majengo yake na kutoa vifaa tiba pamoja na kuweka watumishi hasa ikizingatiwa kwamba watumishi wengi wa afya…
Mheshimiwa Spika, watumishi wengi wa afya wamekumbwa na tatizo la vyeti fake na kwa maana hiyo wameondolewa, je, Serikali ina mkakati gani sasa? ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpe pole na nimtie moyo kwamba asisikitike sana kuhusiana na hali ya Hospitali ya KCMC, mimi binafsi toka nimeteuliwa nimeshafika pale takribani mara tatu na hivyo ninafahamu vizuri sana namna ambavyo hospitali ile inatoa huduma zake na ina madaktari mahiri sana vijana wakiwemo marafiki zangu kina Kajiru, kina Urassa ambao ni mabingwa waliobobea. Tumewapeleka pale sisi kutoka Wizara ya Afya na wamekubali kukaa pale kwenye Kanda yetu ya Kaskazini kutoa huduma kwa Watanzania wenzetu wa eneo lile na nadhani angepongeza kwa jitihada hizo ambazo tumezifanya.
Mheshimiwa Spika, pili, kwamba lini tutapeleka fedha. Tutapeleka fedha pindi ambapo uwezo wa Serikali wa kufanya hivyo utakapohimili, lakini kwa sasa naomba atambue tu azma yetu ya kutenga shilingi milioni 500 ili kuchangia katika kukamilisha mradi wa kujenga bankers kwa ajili ya kufunga mashine za mionzi na naomba nimfahamishe kwambamradi ule wa kujenga bankers kwa ajili ya kutoa tiba ya mionzi sio wa Serikali peke yake wala sio wa KCMC peke yake tunaufanyakwa ubia na wadau wa maendeleo ambao tayari wamashajitolea baadhi ya vifaa kwa ajili ya kutekeleza mradi ule. Kwa hiyo, sisi kama Serikali lakini wenzetu wa KCMC tutashirikiana na huyo mdau kuhakikisha mradi ule unakamilika na sisi mchango wetu ni hizo shilingi milioni 500 ambazo tumeziweka kwenye bajeti.
Swali la pili, kwamba hospitali ya Mawenzi na Mount Meru ziko katika hali mbaya sana, si kweli ninaomba tuwe tunatumia maneno ambayo yanatia moyo wananchi kwa sababu hospitali hizi nimezitembelea zaidi ya mara mbili zote hizi na ninafahamu miradi mikubwa inayofanyika katika hospitali hizi. Na niwapongeze wenzetu wa TAMISEMI na wadau wa maendeleo ambao wametoa misaada mikubwa katika kuboresha eneo la maabara na eneo la huduma za mionzi na kwa kweli kwa pale Mawenzi kuna theatre nzuri sana ya kimataifa, zipo theatre karibu nne pale ndani na zote zinafanya kazi na ni za kisasa kabisa na ninadhani labda Mheshimiwa Mbunge uende ukatembelee maabara ya Mawenzi pamoja na theatre ili uone jinsi hospitali ile ilivyo katika hali nzuri kuliko unavyosema wewe. Nitoe rai kwa wananchi waendelee kuamini huduma bora zinazotolewa na hospitali zetu za Mawenzi, Mount Meru na hospitali ya KCMC.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa sababu nilikuwa nimefikiri atazungumzia wanawake tu kwa kuwa hii biashara ni ya watu wawili. Hata hivyo, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, pamoja na kwamba kunakuwa na biashara hiyo ya wanawake na wanaume, lakini pia sasa hivi kuna biashara ya homosexuals, wanaume peke yao au lesbians; je, hawa wanachukuliwa hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hiyohiyo niliyoisema wakati natoa majibu ya msingi hapa inakataza pia vitendo vya watu wa jinsia moja kufanya mapenzi kinyume cha maumbile. Pia inakataza hata, kwa mfano kwa mwanaume kufanya vitendo ambavyo vinaashiria kwamba ni vya jinsia ya kike, yaani kufanya mambo ya kike wakati wewe ni mwanaume. Sheria hiyo inakataza na inayajinaisha na kuna adhabu kali ambayo inatolewa na sheria hiyo, ni zaidi ya miaka 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tumekuwa tukipambana kwa nguvu zetu zote na makundi haya ambayo yamekuwa yakishiriki kwenye vitendo vya mapenzi ya jinsia moja ama kuyahamasisha ama kuyahalalisha ama kuyafanya yaonekane ni vitu vya kawaida kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu tuliendesha operesheni kubwa ya kudhibiti vitendo hivi lakini pia hata taasisi ambazo zilionekana zina mwelekeo wa kutekeleza afua mbalimbali za kinga kwenye sekta yetu ya afya tumezifuta, tumezibadilisha. Hata miongozo ambayo iliruhusu baadhi ya afua zinazohusiana na kupunguza maambukizi kutoka kwa watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja nayo tumeibadilisha, kwa hiyo tuko vizuri. Watakaofanya hivyo watakamatwa na Jeshi letu la Polisi na watachukuliwa hatua za kisheria.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, kwa maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri anasema takribani Wilaya 84 hazipati usikivu. Swali langu, ni kwa nini sasa ile kauli mbiu ya TBC ya Ukweli na Uhakika msiifute na muwe na kauli mpya?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, hatuwezi kufuta hiyo kauli mbiu kwa sababu tunatoa taarifa za ukweli na za uhakika, haihusiani kabisa na usikivu. Ahsante. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Tatizo la maji salama na maji safi katika nchi hii ni kubwa sana na Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI na Naibu Waziri wa Maji hivi majuzi walikuwa kwenye semina maalum ya programu ya maji inayoitwa “Uko Tayari?” Takwimu zinaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa katika hospitali wanaugua magonjwa yanayotokana na maji machafu. Je, Serikali kupitia Wizara zote (TAMISEMI na Maji) zina mkakati gani kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji safi na salama hasa katika Awamu hii ya Tano?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yake amedai kwamba kuna magonjwa mengi mahospitalini ambayo yanatokana na kutokuwepo kwa maji safi na salama. Kuanzia bajeti ya mwaka 2006/2007 tulianzisha Programu ya Utekelezaji wa Miradi ya Maji ambayo ilikwenda kwa muda wa miaka mitano, imekwisha Juni, 2016 sasa hivi tumeingia programu ya pili. Malengo yetu ni kuhakikisha kwamba tunaweka fedha ya kutosha na miradi mingi sasa inatekelezwa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji safi na salama na kwa karibu zaidi.
Kwa hiyo, tumeshaanzisha na tumelenga kwamba itakapofika mwaka 2020 vijijini tuwe tumeshakwenda zaidi ya asilimia 85 na mijini twende asilimia 95. Kwa hiyo, tupo na tumeshaanza siyo kwamba tumekaa, tunaendelea na tutahakikisha kwamba wananchi hawapati shida ya magonjwa yanayotokana na maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi ya hapo, sasa hivi tume-centralize kuhusiana na ununuzi wa dawa za kutibu maji. Utaratibu uliokuwepo ni kila Mamlaka inanunua dawa hizo kivyake sasa tutanunua kutoka center moja kwamba Serikali sasa itakuwa inafanya bulk purchase ya dawa za kutibu maji ili tuhakikishe kwamba maeneo yote tunakuwa na maji safi na salama. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii na nimpongeze Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba swali la msingi linahusu huduma za kuwapatia watu wenye albinism vifaa vyao lakini utakubaliana nami kwamba watu hawa wenye albinism wanaishi katika maisha hatarishi na Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikifuatilia lakini bado watu wenye albinism wamekuwa wakiuawa hasa kwa sababu ya masuala mazima ya ushirikina. Je, Serikali ina utaratibu gani kuhakikisha masuala haya yanakwisha ili hata hivi vifaa vinavyoletwa basi viweze kuwahudumia hasa hawa watu wenye albinism? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU) Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hizi imani za kishirikina, Serikali imepiga marufuku utolewaji wa vibali kwa waganga wanaopiga ramli chonganishi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lyimo hilo ndilo jibu langu la msingi na ndiyo jibu la Serikali kwamba tayari imeshapiga marufuku utoaji wa vibali kwa waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi.Pamoja na Serikali kuendelea kujenga vyuo katika Mikoa na Wilaya, tuna tatizo kubwa sana la Walimu wa Vyuo vya VETA, kwa sababu tuna chuo kimoja tu cha Morogoro ambacho ndicho kinachotoa Walimu. Je, Serikali inatusaidiaje kuhakikisha kwamba Vyuo hivi vya VETA vinavyojengwa na vilivyopo ambavyo vina tatizo kubwa sana la Walimu vinakuwa na Chuo kingine cha Walimu ili kuweza kutatua tatizo la wanafunzi, watoke pale wakiwa wamekamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema kwamba kuna changamoto ya kuwapata Walimu wa Vyuo vya VETA. Nimhakikishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mkakati wa kuhakikisha kwamba elimu ya ufundi inapatikana nchini kwa wingi na ubora zaidi ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunakuwa na Walimu wa kutosha. Kwa hiyo, katika mikakati ya Wizara kuna mkakati wa kuhakikisha kwamba Walimu pia wanapatikana.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sambamba na vipodozi hivyo, pia kumekuwepo na wimbi la baadhi ya akina dada na akina mama kutumia sindano za kuongeza sehemu za maumbile yao kama vile makalio na maziwa. Je, nyongeza hizi za maumbile yao zina athari yoyote kiafya na kama zinayo Serikali inatoa tamko gani? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu alituumba kila mtu kwa aina yake, kwa rangi yake na maumbile yake. Nyongeza hizi kitaalam zina madhara kama vilivyo vipodozi haramu. Ngozi ina matumizi yake, Mwenyezi Mungu hakuiweka pale kwa makosa, inatusaidia sisi kwanza kujikinga na mionzi na magonjwa. Kwa hiyo, matumizi ya vipodozi moja, yanaleta madhara katika ngozi lakini pili yanaweza kupelekea mtu kupata saratani sambamba na hizi sindano na dawa nyingine za kuongeza maumbile zina madhara makubwa kwenye mwili. Kauli yangu kwa wananchi, tuache kutumia vipodozi na madawa haya, Mwenyezi Mungu alituumba na makusudio yake tuendelee kuishi kwa maumbile na rangi zetu. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na jitihada za kudhibiti ubora wa elimu hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuanzia shule ya awali mpaka vyuo vikuu, naishukuru Serikali kwa juhudi hizo kwa sababu siku zote Upinzani tumekuwa tukizungumzia suala la ubora wa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kujua ni nini hatma ya wanafunzi katika vyuo vile ambavyo vimefutiwa usajili wakiwa tayari wanaendelea na masomo? Kwa mfano, unakuta vijana hao tayari walishalipa ada lakini na muda wao. Je, Serikali inatuambia nini au inawaambia nini wanafunzi ambao tayari walikuwa kwenye masomo lakini wakaondolewa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kweli kwamba huu ukaguzi ni mzuri sana lakini kumekuwa na ubaguzi mkubwa kwenye ukaguzi kwa maana ya shule za msingi za Serikali na zile za private, hali inayopelekea kuwa na double standard, kwa sababu wanafunzi wa shule za private kila mwanafunzi anatakiwa alipe shilingi 5000 kwa ajili ya ukaguzi, lakini wanafunzi wa shule za Serikali ni bure. Hamuoni kwamba kwa ubaguzi huu ndiyo inayopelekea kuporomoka kwa elimu hasa kwenye shule za Serikali na ndio sababu kunakuwa na matokeo mabaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwezekano wa wanafunzi wanaondelea na vyuo kuathirika na hatua ambazo tunachukua wakati wa kuhakikisha kwamba kuna ubora katika vyuo vyetu.
Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kila wakati tunapochukua hatua tunahakikisha kwamba wanafunzi hawataathirika lakini ifahamike kwamba kwa sababu tokea awali vyuo hivyo vinafahamu kuhusu utaratibu ambao wanatakiwa wafuate, pale tatizo linapotokea maana yake wenyewe watatakiwa kurejesha gharama hizo kwa wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusiana na tofauti aliyotaja ya ada ya ukaguzi kati ya shule za Serikali na zile za watu binafsi, Serikali haioni kwamba tofauti hiyo ina athari zozote zile katika ubora wa elimu. Ni utaratibu tu ambao umewekwa wa kuhakikisha kwamba hiyo ada inalipwa lakini hatuoni kwamba shilingi 5000 kulipa kwa shule binafsi kwamba ina athari katika ubora wa elimu.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana kwa nafasi na nasikitika sana kwa majibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyoruhusu kufanya elimu kuwa commodity, kuwa biashara. Pia ni Serikali hii hii inayoleta ada elekezi na kwamba utafiti umefanyika na wamebaini kwamba shule zinatofautiana. Hapakuwa na haja ya utafiti kwa sababu inajulikana shule hizi zinatofautiana. Sasa swali langu ni kwamba wanipe sababu ni kwa nini wanataka shule hizi za binafsi ziwe na ada elekezi huku wakijua kabisa kwamba shule hizi zinatofautiana ubora na ni wazi hata katika matokeo ya mitihani kwa muda wa miaka 10 mfululizo shule hizi zinaongoza? Watupe sababu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka kujua Serikali haioni kwamba shule hizi ada inakuwa kubwa kwa sababu kubwa moja tu, kwamba kuna tozo nyingi, kwa mfano wanalipa property tax, lakini vilevile kwenye suala la ukaguzi, wakati shule za Serikali wanalipa chini ya shilingi 3,000, hawa kila mwanafunzi anapaswa kulipa shilingi 5,000 ya ukaguzi. Je, ni lini Serikali itaondoa tozo kwenye shule hizi ili ada yao iweze kuwa kidogo na ili wazazi waweze lakini pia kwa nini msiboreshe shule zenu za Serikali ili wazazi waweze kuwapeleka kwenye shule za Serikali kwa sababu hakuna mwananchi yeyote asiyependa bure?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kusema, pamoja na kwamba elimu imekuwa ikitolewa kwa kushirikiana na taasisi binafsi na pamoja na kwamba kumekuwa na element ya biashara, lakini lazima tuzingatie kwamba elimu siyo biashara per se, elimu ni haki ya kila Mtanzania na si mwenye uwezo tu wa fedha ndiyo anayestahili kupata elimu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na dhana hiyo, kumekuwa na wazazi wengi ambao wangetamani kupeleka watoto wao katika shule mbalimbali, lakini wakati huo huo kumekuwa na ada za aina tofauti tofauti wakati mwingine si halisia kulinganisha na uwekezaji uliofanyika.
Hata hivyo, dhana kubwa ya uwekezaji ni pamoja na mwekezaji kuja na mtaji na si tu kuwekeza kwa kutegemea mtaji ule unaokusanywa kutokana na ada za wanafunzi kwa wakati huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, kutokana pia na kilio kutoka kwa wananchi wengi na hilo si tu kwamba litakuwa linafanyika kwa mara ya kwanza kwa Wizara yetu ya Elimu, bali pia limekuwa likifanyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo mafuta kwa mfano EWURA, wamekuwa wakipanga bei kutegemeana na uhalisia ili bei zinazotozwa zilingane na uhalisia. Kwa misingi hiyo ndiyo maana tumeona kuna umuhimu wa kushirikisha wadau wengi ili kupata bei ambayo haitaathiri utoaji wa huduma, lakini wakati huo kuwawezesha wananchi wengi zaidi kufaidika na sera hii nzuri ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, pamoja na jitihada kubwa inayofanywa na Serikali ya kuhakikisha kwamba shule zake za Serikali zinaboreshwa, ikiwemo shukrani kubwa kwa Bunge kupeleka Shilingi bilioni sita kwa ajili ya Madawati, hiyo ni sehemu ya kuboresha elimu katika shule za msingi, napenda tu niseme kwamba, sehemu za tozo ambazo zimekuwa zikitozwa zinaendana na uhalisia. Kwa misingi hiyo, niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge kukaa katika viatu vya wananchi ambao wapo na tunawawakilisha kuona kwamba kila jambo tunalolifanya, kila biashara inayofanyika, inaendana na uhalisia na si kuwa ni sehemu ya unyonyaji.
MHE. SUSAN J. A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Naibu Waziri, amekiri kwamba sasa hivi kuna magonjwa mengi ya akili na sasa hivi linaongezeka hili la vyuma kukaza watu wamekuwa na stress sana. Pamoja na kwamba Hospitali ya Mirembe ndiyo Hospitali ya Kuu na inafanyiwa maboresho na tunakubaliana kwamba magonjwa haya yamekuwa mengi na kwa maana hiyo jamii nzima ina haya magonjwa. Je, wana utaratibu gani kuhakikisha kwamba kwenye vituo huko mikoani, wilayani, wanaviboresha ili kuweza kuwasaidia hawa watu wenye matatizo ya magonjwa ya afya ya akili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Magonjwa ya akili yanasababishwa na mambo mengi ikiwa ni pamoja na kurithi kijenetiki lakini vilevile matumizi ya vilevi mbalimbali, changamoto na stress za maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ambazo Serikali inazifanya; moja ni kama tulivyosema tumeboresha huduma katika hospitali yetu ya Rufaa ya Mirembe. Sambamba na hilo tumeendelea kujenga uwezo katika hospitali zetu za Rufaa za Kanda na tumesema tutakwenda mbali zaidi na kwenda kuboresha katika hospitali zetu za Rufaa za Mikoa, sambamba na hilo kuweka mifumo mizuri ya Rufaa kutokea ngazi ya dispensari hadi katika hospitali yetu ya Mirembe. (Makofi)
MHE. SUZAN J. A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pia nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini tutambue kwamba sisi sote ni Wazee watarajiwa na kwa maana hiyo tunapaswa kuweka miundombinu imara ya kuweza kusaidia wazee hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hapa umesema kwamba Awamu ya Tano imedhamiria kuboresha na ukaelezea Ilani ya CCM, ninavyoelewa hii ni Ilani ya Kumi na Mbili ya CCM toka tumepata Uhuru au Ilani ya Nane kuanzia mwaka 1977 lakini bado tuna tatizo kubwa sana la masuala ya wazee; Ni miujiza gani Awamu hii ya Tano ya Hapa Kazi Tu mtafanya kuhakikisha kwamba hawa wazee wanaboreshewa maslahi yao na mahitaji yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa toka mwaka 1999 Serikali iliamua kwa dhati kuwa na Sera ya Wazee, Sera ambayo ilitengenezwa mwaka 2003. Mpaka leo hakuna sheria iliyoletwa, hawajaleta Muswada hapa Bungeni na Mheshimiwa Waziri wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Mheshimiwa Ummy, aliahidi na ameendelea kuahidi akaja Kigwangalla akaahidi na leo sasa Mheshimiwa Naibu Waziri Ndungulile, wanaiambia nini nchi hii. Je, ni kwa nini hawaleti Muswada ambao utatatua matatizo yote ya wazee katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO; Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Awamu ya Tano sasa hivi takribani inaingia mwaka wa tatu na nimeainisha katika jibu langu la msingi hatua ambazo tayari tumeanza kuzichukua katika kuboresha makazi ya wazee, sambamba na hilo kuhakikisha kwamba Wazee wale wanapata huduma ya chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tutenga bilioni mia nne tisini na tisa. Mpaka sasa hivi tumeshaweza kutoa milioni mia tatu hamsini na tatu elfu kwa ajili ya vyakula katika kambi hizi 17 za Wazee. Changamoto ambayo ipo na niendelee kusisitiza ni kwamba jukumu la kwanza la kutunza wazee ni la familia, baada ya hapo inafika ndugu na baada hapo ni jamii. Serikali inakuja mwishoni. Kwa hiyo, nataka niliwekee msisitizo hili ili nasi kama wanajamii tuweze kulitambua hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ameulizia ni lini Serikali italeta sheria, Sera ambayo ameiongelea Mheshimiwa Mbunge ni ya mwaka 2003 imepitwa na wakati. Sasa hivi tuko katika mapitio mapya ya sera ili sasa tuhuishe mahitaji ya wazee kwa sasa na baada ya hapo tutaelekea kutunga sheria. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba uchumi wa nchi yetu ungekua zaidi kama tungewekeza kwenye kilimo, lakini tunaona kwamba kilimo chetu kinaendelea kuporomoka. Huko nyuma kilikuwa kinaingiza asilimia nne, lakini sasa hivi kimeshuka mpaka asilimia 1.7. Sasa nilikuwa naomba kujua Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba, vijana hawa wanajiajiri kwenye mashamba ili kuweza kukuza uchumi wetu? Kwa sababu vijana wapo wamezagaa, lakini mapori, mashamba yako makubwa, lakini hakuna chochote kinachoendelea. Je, Serikali kupitia ofisi yako ina mkakati gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu tumeandaa mpango mkakati wa Kitaifa, it is a national strategy ya kuwaingiza vijana katika kilimo. Katika mpango huu malengo makubwa ni kuyatumia yale mashamba makubwa ya Serikali ambayo hayatumiki kwa ajili ya shughuli za kilimo kwa vijana.
Kwa hiyo, tunaamini kabisa katika mpango huu kwa muungano huu kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo, tutafanya kazi pamoja ili maeneo haya sasa tuweze kuwapatia vijana wa nchi hii wakafanye shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisema, narudia mara nyingine tena leo ya kwamba moja kati ya kazi ambayo tunaanza nayo mapema kabisa tumeamua katika eneo la Mkulazi na Mbigili pale Morogoro ambako Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF wanakwenda kujenga Kiwanda cha Sukari tutawafanya vijana wa nchi hii kuwa ndio out growers ambao watasaidia kulima miwa kwa ajili ya kukilisha kiwanda. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwa kupitia mkakati huu vijana wengi zaidi watapata ajira na waweze kujiajiri.(Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa swali la msingi linahusiana na kutokuwa na usawa katika suala la mitihani naomba niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa na huku Bara kuna tatizo kubwa sana kwamba kuna wanafunzi wa sayansi wana maabara nzuri sana lakini wengine hawana maabara lakini mitihani inakuja sawa. Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuhakikisha kwamba shule zote zinakuwa na maabara ili wanapotungiwa mtihani wawe sasa wana usawa katika mitihani hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli pale inapokuwa kwamba wengine wana fursa za kujifunzia zilizo kamili tofauti na wenzao na wakapata mtihani unaofanana si jambo jema ndiyo maana marekebisho yanafanyika. Jambo hilo kwa kweli haliko katika elimu tu, na hata katika masuala ya maji nimesikia Waheshimiwa Wabunge wakisema kwamba vijijini hakuna maji, mjini kuna maji na vitu kama hivyo. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba inatoa fursa na usawa katika maeneo yote kulingana na mahitaji ya wananchi wake. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ambayo yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu ningependa pia kutoa ufafanuzi kwamba utaratibu ulioko kwa sasa kwa shule ambazo hazina maabara lakini kuna wanafunzi wanafanya masomo ya sayansi, wanakuwa na mtihani tofauti na hawalazimishwi kufanya practical. Kwa hiyo kuna kitu ambacho kinaitwa alternative to practical.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mpango wa Serikali kama ambavyo tumekwisha eleza katika swali ambalo lilikuwa limeulizwa hapo awali ni kwamba tunataka kuhakikisha kwamba shule zote zina maabara na zinakuwa na vifaa ili hatimaye hii alternative to practical ambayo imekuwa ikitolewa isiendelee kuwepo. Ahsante.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mweyekiti, nakushukuru, pamoja na Serikali kuamua kuondoa tozo hizo tayari Halmashauri zilishaweka kwenye bajeti zao. Je, Serikali inatoa tamko gani ama wata-review hizo bajeti au itakuwaje? Hiyo ndiyo shida yangu ahsante na shida kwenye Halmashauri zetu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hii ni hofu ya Wabunge wengi humu ndani, na hata juzi Wabunge wengi walikuwa wananiuliza kule kwamba jinsi gani tunavyokuja. Na ndiyo maana naomba niwaambie kuwa Serikali itakachokifanya sasa hivi ndiyo maana nimesema tukifika katika Finance Bill tutaona jinsi gani mchanganuo utakavyokwenda. Lengo kubwa kwa sababu Halmashauri zimeshatenga bajeti yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia bajeti ya Halmashauri ilivyotengwa kuna tofauti sasa na kama ambavyo vingine viliwekwa kama ni vyanzo vya mapato katika Halmashauri hiyo. Ndiyo maana Wizara ya Fedha itakapohitimisha mijadala hii tutaona ni jinsi gani mafungu hayo yatawekwa vizuri. Lengo kubwa bajeti ya Halmashauri kama property tax ilivyowekwa katika suala la majumba, kwa hiyo, msihofu katika hili.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wote tunajua kwamba maambukizi ya virusi vya UKIMWI au UKIMWI yanatokana na sababu kubwa ya kuwa na sexual partners wengi; lakini kwa hapa Tanzania na duniani kote inaonekana wanawake ndio wanakuwa wengi kuliko wanaume. Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia sababu hasa ni nini? Kwa nini wanawake wanakuwa na maambukizi kuliko wanaume? Je, tatizo ni kwamba wanaume ndio wanawaambukiza zaidi au wanawake wanakosa maadili? Tusaidie kwa hilo.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nitazingatia muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba wanawake wanaambukizwa zaidi kuliko wanaume; uwiano hauko mbali sana, tofauti ni ndogo, lakini ni kweli kwamba maumbile ya kibaiolojia ya wanawake ni tofauti sana na maumbile ya wanaume. Pia tabia za wanawake kuhusiana na ngono ni tofauti sana na tabia za wanaume kuhusiana na ngono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaume wengi wana tabia ya kuchepuka sana na mara nyingi wanaweza wakavitoa virusi nje wakavileta kwenye ndoa zao kwa wanawake ambao wametulia; hilo halibishaniwi. Kwa hiyo, nitoe rai kwa wanaume wenzangu kujipanga sana kwenye eneo hili la kuchepuka, kuachana na michepuko, lakini pia kupima afya zetu, kupima hali zetu lakini pia kupima hali za wenza wetu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale Waislamu wenzangu, tunapewa fursa ya kuoa wake hadi wanne; kuliko kuchepuka na watu usiowajua, unawakuta mtaani huko, ni bora ukapima na ukajiridhisha kwamba unayekwenda kumuoa yuko salama, ukatulia na wake zako wanne. (Makofi)
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Katika Kamati yetu ya huduma za jamii ni wazi kwamba tuna upungufu wa watumishi wa afya takribani 48%. Katika zoezi hili la uhakiki vituo vingi vya afya vimefungwa, hali inayosababisha akinamama wengi wajawazito kuendelea kufariki na hata takwimu zinaonesha kwamba wanaokufa ilikuwa 400 na zaidi kati ya vizazi 100,000 leo tunaongelea zaidi ya wanawake 500 na zaidi katika vizazi 100,000.
Mheshimiwa Spika, ni kwa nini sasa Serikali haiajiri wakati Madaktari wako kibao na watumishi hao wako nje ya ajira? Ni kwa nini Serikali haiajiri wakati watu wetu wanaendelea kufariki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) :
Mheshimiwa Spika, tumekiri juu ya upungufu wa wataalam wa afya lakini pia ni ukweli usiopingika kwamba unapoajiri implication yake ni suala la bajeti. Naamini kabisa kwa upungufu huu tulionao na idadi ya watumishi katika kibali ambacho kimetoka wanaoenda kuajiriwa ni pamoja na Madaktari. Naomba tuvute subira tupitishe bajeti hii wengi wa wale wanaoenda kuajiriwa itakuwa ni Madaktari ili kupunguza tatizo hili kubwa tulilonalo.
MHE. SUSAN A.LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba kuna tatizo kubwa la upungufu wa Walimu hawa, lakini nina taarifa kwamba tuna Walimu wengi sana waliosoma katika vyuo kwa mfano Chuo cha Tabora cha Viziwi, wamesomea kufundisha watoto hawa, lakini wapo mitaani na wana resources.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni kwa nini Serikali isiwachukue Walimu hawa ambao wamesomea kwa miaka mitatu degree zao na kuendelea kuchukua Walimu ambao wamepata kozi za juu juu tu za mafunzo kazini wakati tunajua tuna tatizo kubwa sana la Walimu kwa ajili ya watoto hawa wenye ulemavu mbalimbali pamoja na viziwi na hawa wengine wa usonji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Susan Lyimo kwa sababu kwanza amekuwa ananiletea maswali mengi hata kwenye karatasi, vi-note na nimekuwa nikimpa maelezo ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili namuahidi katika Walimu ambao tutawaajiri hivi karibuni, kipaumbele kitakuwa ni kwa hawa ambao wana taaluma ya elimu maalum ambao hawajaajiriwa ili waajiriwe haraka waweze kutusaidia katika shughuli zetu.
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wizara ya Afya haijaanza jana wala juzi. Nimesikitika sana kusikia Mheshimiwa Waziri akisema sasa ndiyo wanafanya tathmini ya kujua Madaktari Bingwa ni wangapi ili waweze kuwapanga. Swali langu, hawaoni huu ni uzembe mkubwa kwamba walipaswa kuwa na kanzidata au database ya Madaktari Bingwa ili kusiwe na tatizo hili kwa sababu kila siku tunauliza na tunaambiwa kuna tatizo? Hawaoni huo ni uzembe kwamba walipaswa kuwa nayo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Lyimo ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambao nao wanasimamia sekta hii ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa maana ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekabidhiwa hospitali hizi za rufaa za mikoa mwishoni mwa mwaka jana wakati wa uzinduzi wa Hospitali ya Mloganzila. Tunatambua idadi ya Madaktari tuliokuwa nao na tunakuwa na mikakati ya kuhakikisha kwamba tunapata watumishi wa afya wa kutosha. Kwa hiyo, si uzembe, kila kitu ni mikakati ambayo Serikali tumeendelea kujiwekea na tutaendelea kuzihudumia na kuwapatia watumishi wa kutosha kadri uwezo wa Serikali unavyoruhusu.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Majibu ya Mheshimiwa Waziri yamekuwa ni hayo hayo kwa muda mrefu, na maswali yalikuwa ni kwa nini sasa wanafunzi wote wanaomaliza kidato cha sita wasiende JKT kwa sababu lengo la JKT kama ulivyosema mwenyewe ni suala la uzalendo na maadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila leo wanasema wanaboresha, wanaongeza lakini sisi tunachotaka ni kwamba wote Watanzania vijana hawa tunataka wote wawe in uniform waweze kutekeleza suala zima la uzalendo na maadili ili nchi yetu maadili yasiendelee kuporomoka, sasa ni lini watahakikisha hilo linafanyika?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema jitihada zimefanyika na zimeonekana. Wakati tunarudisha tena utaratibu wa JKT baada ya kuwa tumeuacha kwa miaka mingi kuanzia mwaka 1994, idadi tuliyokuwa tunaweza kuchukua ilikuwa ndogo sana si zaidi ya vijana 5000; leo tunavyozungumza tayari tumefikia 20,000 na kambi mpya nimezitaja tunazozifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo si maneno tu ya kurudia hii ni mkakati uliopo. Kila mwaka tunaendelea kufungua kambi mpya tunaboresha za zamani na idadi imeendelea kuongezeka. Leo tunavyozungumza kama tunachukua vijana 20,000, bila shaka ndani ya miaka michache ijayo tutaweza kukidhi mahitaji ya vijana 60,000 au 80,000 ambao watakuwa wanahitimu.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Ukiangalia kwenye majibu ya msingi ya swali langu Waziri anakiri kabisa kwamba bado mpaka sasa hivi wanasambaza vitabu vya darasa la nne na kimsingi darasa la nne wamefanya mtihani. Kwa hiyo ina maana kuna wanafunzi wamekosa vitabu na wamefanya mitihani na hawa watoto pia wanafanya mitihani ya kufanana. Je, Serikali haioni hili ni tatizo kubwa na kwamba ni lazima sasa watoto wapate vitabu kwa wakati kwa sababu tunajua Walimu nao wana matatizo yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; mwaka 2016 Taasisi ya Elimu ilitayarisha vitabu na vitabu hivyo vikaondolewa kwa sababu vilikuwa vibovu sana, lakini mwaka 2018 wametengeneza tena vitabu na baadhi ya vitabu vina matatizo. Je, Serikali haioni kwamba Taasisi ya Elimu imeshindwa kazi yake kwa sababu vile vitabu vilikuwa zaidi ya bilioni 100 tulivyoambiwa na kwamba sasa Serikali haioni kuna haja ya kuwa na ushindani na Sekta Binafsi ili vipatikane vitabu ambavyo vitakuwa bora ili watoto wetu waweze kupata elimu bora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwepo na changamoto ya kuhakikisha kwamba vijana wetu wa darasa la nne wanapata vitabu kwa wakati. Hata hivyo, kama nilivyoeleza sasa tunaelekea kukamilisha zoezi la kusambaza vitabu hivyo nchi nzima. Kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba changamoto hiyo sasa tuko mbioni kuachana nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili la vitabu anavyosema vina makosa tulishatoa rai kwamba kama kuna yeyote mwenye kitabu kati ya vitabu hivi ambavyo tumechapisha ambaye ameona au anahisi vina makosa atuletee kwa sababu sisi ka Wizara na kama Serikali. Mchakato ambao tumeutumia kuja na vitabu vipya umetuhakikishia kwamba kuna ubora mkubwa sana katika vitabu vipya ambavyo vimetoka kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Mbunge na wengine wote ambao wao wana vitabu ambavyo wanafikiri vina makosa wavilete kwetu na tutaviangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu tayari kulikuwa na vikaragosi vinazungushwa mtaani kumbe vilikuwa ni vikaragosi vya vitabu vya Kenya. Kuna watu wengi ambao wanajaribu kuichafua Serikali na kuchafua mfumo wetu wa elimu. Kwa hiyo, naombeni mwenye chochote kile ambacho anafikiri ni makosa alete tuangalie kwa sababu sisi tunajiridhisha kuwa vitabu havina makosa.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa mwenyekiti, nakushukuru sana pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nilitaka kujua tu kwamba sasahivi wananchi wengi wameshaelimika kuhusiana na masuala ya UKIMWI. Lakini nilitaka Serikali ituambie ni kwa nini hawaruhusu watu wajipime wenyewe kwa rapid ya HIV test kwa sababu wakienda vituo vya afya usiku vinakuwa vimefungwa na kuna watu wanapenda kufanya hilo jambo kwa chap chap.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini wasiruhusiwe wapate hivi vipimo waweze kujipima ili waende kwenye hiyo shughuli wakijua wako salama au hawako salama?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya UKIMWI, upimaji unafanyika katika kituo cha afya. Lakini tumeanza mchakato ndani ya Serikali ya kufanya mabadiliko ya Sheria ya UKIMWI ili sasa watu waweze kujipima wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka kumeibuka mjadala kuna wengine wanasema mtu akijipima mwenyewe atakuwa frustrated ataenda kuambukiza wengine. Kwa hiyo, tunaweka kwamba tutaanza ajipime mwenyewe mbele ya mtoa huduma za afya. Hayo ndiyo mapendekezo ambayo tumeyatoa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na tutakuja Bungeni tuwaombe Waheshimiwa Wabunge watuunge mkono, ahsante sana.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nina amini swali la msingi lilikuwa linahusu watoto kunyimwa haki yao ya kwenda shule kutokana na mila na destruri. Pamoja na mila na desturi sasa hivi au kwa muda mrefu kumezuka tabia ya wazazi hususani wanawake wakitembea na watoto yaani wakiwa na watoto wao wadogo au watoto wa kukodi kwa ajili ya kuombaomba, hali inayopelekea watoto hawa wasiende shule kwa sababu wakiwa na wale watoto maana yake wananchi watawahurumia na kuwapa msaada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali inajua kwamba kuna hili jambo na kama inajua ina mkakati gani kuhakikisha kwamba wazazi hao hawatumii watoto wao kama chambo cha kupata misaada na watoto hawa waweze kwenda shule kwa sababu bila hivyo watoto hawa wataendelea kuwa nyumbani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Susan Lyimo ameuliza swali zuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haki za msingi za mtoto ni pamoja na kuendelezwa, kulindwa, kutunzwa na kutotumikishwa kazi nzito. Swali hili ambalo ameliuliza katika maudhuhi yake yote haya haki zote hizi za msingi za mtoto zinavunjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niwaombe na tumeshatoa maelekezo kwa wataalam wetu ndani ya Wizara, kwanza tumefanya katika haya majiji makubwa sensa ya kubaini watoto wote ambao wanaishi katika mazingira hatarishi na tumebaini kama watoto karibu 7,000. Mpaka sasa hivi tumeweza tuwarudisha watoto zaidi ya 1,000 majumbani kwao kutegemea na nature ya matatizo ambayo tumekutana nao, lakini tunajua database ya watoto ambao tunao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuwasisitiza Maafisa wetu wa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii hususani katika haya majiji makubwa kuhakikisha kwamba hawa wakina mama ambao wana tabia kama hizo ambao watoto hawaendi shule na watoto wanatumikishwa kazi nzito tunaweza kuwabaini na kuchukua hatua za msingi ili kukomesha kabisa matatizo kama haya. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nashukuru kwa majibu ya Serikali, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sehemu ya mwisho ya jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kwamba sekta binafsi wanaruhusiwa hata kuongeza kile kiwango ili kuwapa motisha na tunaelewa kwamba motisha ndiyo kila kitu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri unaweza ukatuambia ni kwa nini Serikali mpaka leo haijawalipa watumishi wake annual increment ambayo ipo kisheria (statutory) na unakiri kwamba hii inasaidia sana motisha na sisi tunajua motisha ndiyo inaweza kusaidia maendeleo ya nchi hii. Je, unaweza kutupa hiyo ni kwa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia sekta binafsi pamoja na kwamba wana viwango vya juu lakini pia wana viwango vya chini sana na wale wafanyakzi wa chini wanapata hata pungufu ya shilingi laki moja. Je, Serikali inasema nini kuhusu hili hasa ikizingatia kwamba shilingi laki moja kwa sasa hivi haiwezi kitu chochote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watumishi wa umma na nyongeza ya mshahara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limekuwa likisemwa mara kwa mara hapa Bungeni ya kwamba Serikali si kwamba haitambui kwamba kuna umuhimu wa kufanya annual increment kwa watumishi wa umma, kilichotokea ni kwamba baada ya zoezi lile la uhakiki kuhakikisha kwamba tunatengeneza kanzi data ya wafanyakazi ambao wapo hawana changamoto zile za kwenye masuala ya uhakiki na maelekezo yameshatoka kwamba kuanzia hapo sasa Serikali itaona namna bora ya kuweza kulitimiza takwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi sasa shughuli hii ilikwama kwa sababu mtakumbuka kwa mwaka 2016/2017 zoezi la uhakiki liliendelea na kanzi data hiyo ikishatengenezwa vizuri naamini kabisa kwamba jambo hilo litatimizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusiana na suala la kima cha chini katika sekta binafsi. Kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya mwaka 2004 kifungu cha 37 kimetoa mamlaka kwa Bodi ya Mishahara iliyoanzishwa kufanya uchunguzi wa kina na utafiti kuhusiana na ongezeko la mishahara ya sekta binafsi na baadaye kumshauri waziri mwenye dhamana ili aweze kutangaza kutokana na hali halisi ya wakati huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nilitangazie Bunge lako kwamba tayari bodi hii imeshaundwa na muda siyo mrefu inaanza kazi yake kuhakikisha kwamba jambo hili wanalifanyia kazi kwa utafiti na baadaye kumshauri Mheshimiwa Waziri ili sasa kuja na viwango vya kima cha mshahara kutokana na hali halisi ya wakati huo. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wanasayansi wamefanya utafiti na wanasema kwamba vyombo vya plastiki vikikutana na joto kali vinasababisha madhara makubwa sana kwa afya ya binadamu kwa sababu yanatoa kemikali fulani inayoitwa BPA. Je, Serikali inalitambua hili na kama inalitambua inachukua hatua gani kuwasaidia wakulima hawa wa alizeti ambao wanauza mafuta yao barabarani na yanapigwa jua kali sana? Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanahifadhi mafuta hayo ipasavyo ili wananchi wetu wasipate madhara hasa ya kansa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli bidhaa za plastiki kuwekea vyakula hasa vya moto kuna madhara yake lakini kwa haya ya baridi bado tunafanyia utafiti katika Serikali na tumeshaagiza taasisi zetu za utafiti wafanye utafiti kujua madhara yanayopatikana kwa mafuta kuwekwa kwenye vyombo vya plastiki ili wakituletea majibu tutakuja kumpa Mheshimiwa Mbunge.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna tatizo kubwa sana la watoto njiti lakini vile vile na watoto wanaozaliwa kwa maumbile. Tofauti hii ni kwa sababu labda wakina mama hawaendi hospitali kwa wakati. Hivi karibuni majuzi majuzi tu hapa kule Kyaka kuna watoto wamezaliwa wameungana.
Sasa nilikuwa naomba kujua kama Serikali ina taarifa hii na kama inayo wanachukua hatua gani ili kuwasaidia waweze kufanyiwa labda matibabu ya haraka ili isije ikatokea kama Ndugu zetu Marehemu Consolata na Maria? Ahsante.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Susan Lyimo kwa swali lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tayari Serikali kupitia Wizara ya Afya inayo taarifa ya kuzaliwa kwa watoto wapacha ambao wameungana na tayari tumeshatoa maelekezo kwa Mganga Mkuu wa Serikali kufanya mawasiliano na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha watoto wale wanafikishwa Muhimbili haraka iwezekanavyo ili tuweze kufanya taratibu za kuwatenganisha kadri madaktari watakavyoshauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri angejibu swali hili, lakini nimesimama hapa kutoa rai kwa Watanzania wote, pale ambapo anazaliwa mtoto mwenye maumbile angalau labda ni tofauti na ilivyozoeleka, wawalete Hospitali yetu ya Taifa Muhimbili haraka iwezekanavyo ili tuweze sasa kuhakikisha Madaktari wetu Bingwa wanawapa msaada ikiwemo kuwatenganisha.
Kwa hiyo, tunaangalia kama tutawatenganisha ndani ya nchi au tutawapeleka nje ya nchi. Kwa hiyo nimesimama hapa kutoa rai tusiwafiche watoto hawa, tuwapate mapema. Mtoto yeyote ambaye tunamuona yuko na maumbile tofauti wawasiliane na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ili tuhakikishe tunaokoa maisha ya watoto wetu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kama alivyosema Naibu Waziri kwamba mvua za mwaka huu na miaka mingine zimekuwa zikileta adha kubwa sana kwa Jiji la Dar es Salaam.
Nataka Serikali ituambie, wana utaratibu gani sasa kuhakikisha kwamba miundombinu hasa ile ya mwendokasi pale walipoweka Makao Makuu pale Jangwani, inahamishwa ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Dar es Salaam wanapata usafiri bora, hasa ikizingatiwa kwamba Serikali iliwaondoa watu Jangwani lakini imejenga kituo kikubwa cha mwendokasi; ni lini mtakiondoa kituo kile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimetangulia kutoa majibu yangu, mvua za safari hii zimekuwa nyingi ukilinganisha na miaka ya nyuma. Katika swali lake anaongelea juu ya suala zima la kuondoa ile stand au tuite garage ya mabasi yaendayo kasi kwa maana ya pale Jangwani, lakini issue siyo kuiondoa bali kuhakikisha kwamba miundombinu ipi inakuwepo ili hata kama mvua zikinyesha pale pasiweze kuathirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna mpango mahsusi kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam wa kuhakikisha kwamba Bonde la Msimbazi linakuwa na miundombinu ambapo maji ambayo yatakuwa yanatoka kule juu yanaenda baharini kama ambavyo mkondo unaelekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa avute subira tarehe 20 Julai, kandarasi inafunguliwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miundombinu ile inakuwa na ukarabati ambao utakuwa ya uhakika kabisa. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa. Moja ya jukumu kubwa walilopewa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula lakini kubwa zaidi ni kuchangamkia fursa za upatikanaji wa masoko ya bidhaa za kilimo nje ya nchi. Nataka kujua benki hii imeshafanya juhudi hizo kwa kiasi gani?
NAIBU WAZIRI, VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani anaendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya hivi karibuni siku anazindua mradi wa ASDP kwamba benki hii imefanya kazi lakini ifanye kazi zaidi. Kwa sasa tunachosema ni kwamba isaidie zaidi katika suala la kuhakikisha kwamba pembejeo na nyenzo za kilimo zinawafikia wakulima wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo Wizara yetu tayari katika tractors ambazo tayari tumeshaziunganisha zaidi ya 148, Benki ya Kilimo (TAB) tayari tupo nao pamoja katika kuhakikisha kwamba tunawawezesha wakulima na wale ambao watahitaji kukopa trekta hizo. Kwa hiyo, niseme tu kwamba Mheshimiwa Mbunge ameunga mkono kwa kuuliza swali lakini tunataka Benki hiyo ifanye zaidi na zaidi.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ni kweli ule msemo ukishangaa ya Musa utaona ya firauni, ukishangaa ya Musa utaona ya CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaweza kutuambia kwamba ilitudanganya kwa sera hii kwa sababu ilisema elimu msingi ni darasa la kwanza mpaka la sita. Leo wanasema elimu ya msingi ni darasa la kwanza mpaka la saba kwa sheria ya mwaka 1978. Sasa wako tayari kuwaambia wananchi kwamba sasa wanafunzi watakuwa wanasoma darasa la kwanza mpaka la saba na kwamba ile sera ilikuwa ya kutudanganya? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa sasa wamekiri kwamba elimu msingi kwa maana ya elimu ya awali mpaka kidato cha nne haiwezekaniki, tena na sasa ni elimu ya msingi ya darasa la kwanza mpaka la saba.
Sasa nataka kujua hiyo, mitaala ambayo tayari walishaihuisha ya kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la sita kwa maana ya kwamba la saba lilikuwa halipo, wataenda tena kukaa na kutunga mingine au watafanyaje? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba Serikali imedanganya kwa kubadilisha elimu msingi kuwa miaka saba badala ya ile sita iliyokuwa imesemekana katika sera ya elimu ya mwaka 2014, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna kosa lililofanyika kwa sababu sera ni njozi, ni vitu ambavyo unatarajia kufanya katika kipindi cha muda mrefu, kwa hiyo, hakuna ulazima wa kufuata sera kwa asilimia 100. Kitu ambacho ni lazima kufuata ni sheria na Sheria yetu ya Elimu ya mwaka 1978 mpaka leo hii ndio sheria ambayo inatuongoza na ndio inatutaka tufuate elimu msingi ya miaka saba bila kukosa.
Kwa hiyo, kama tunataka tuhakikishe ile miaka sita inakuwa kisheria hatuna budi kubadilisha sheria na ndio kazi hasa ya Bunge hili. Kwa hiyo, kama yeye anaona kwamba ni lazima kufanya hivyo aje na mapendekezo na sisi hatuna shida.
Lakini niseme vilevile kwamba waingereza wanasema don’t fix that which is not broken, hatujaona shida na elimu ya miaka saba katika shule ya msingi. Waheshimiwa wote mlioko huku wote mmesoma katika mfumo huo. Kuhusu kwamba tulishapendekeza busara ikikujia nyingine wakati wowote ili mradi ni kitu kizuri haina shida, hakuna kosa lililofanyika na tutaendelea kwa miaka saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la mitalaa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kurekebisha mitaala yetu ili tuendane na maamuzi yoyote ambayo tutakuwa tumechukua kwa wakati huo. Nashukuru sana.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Hospitali au Kituo cha Afya cha Sinza maarufu kama Hospitali ya Palestina ilipandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya lakini bado iko katika mazingira madogo sana yaani eneo lake ni dogo sana na hata bajeti yake inakwenda kwenye masuala ya kituo cha afya. Je, ni lini sasa Serikali itatoa bajeti ya kutosha lakini vilevile kupanua mazingira yake ili wananchi wa Sinza na Ubungo kwa ujumla waweze kupata huduma stahiki? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la dada na mama yangu Mheshimiwa Susan Lyimo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, anachokisema Mheshimiwa Susan ni kweli. Wiki tatu zilizopita nilikuwa katika Kituo hicho cha Palestina, nilikwenda kukagua ujenzi, hasa miundombinu. Pale kulikuwa na ukarabati unafanyika lakini ukarabati ule nilipata mashaka kama value for money ipo? Nimekwenda kuangalia pale na population niliyoikuta pale ilikuwa ni kubwa sana. Ndiyo maana mpango wa Serikali kwa Wilaya ya Ubungo, kwanza yenyewe haina Hospitali ya Wilaya. Kile Kituo cha Afya hata ukiangalia mazingira yake siyo rafiki zaidi kupandishwa kuwa hospitali ya wilaya. Ndiyo maana mwaka huu sasa katika Jiji la Dar es Salaam tunakwenda kujenga hospitali tatu kuanzia Kigamboni, Ilala maeneo ya Kivule pamoja na Ubungo lakini wenyewe wata-decide wapi hospitali hizo zitakwenda kujengwa. Kwa hiyo, ni jukumu letu kuboresha huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nimemweleza pale Mkurugenzi kwamba ukusanyaji wa mapato sikuridhika nao. Leo hii Kituo kile cha Palestina, thamani ya fedha inayokusanywa hailingani na idadi ya watu. Kwa hiyo, maana yake kuna mianya mikubwa ya upotevu wa mapato. Kwa hiyo, nilitoa maagizo, imani yangu kubwa ni kwamba eneo lile marekebisho yatafanyika kwa maslahi mapana ya wakazi wa Ubungo.
MHE. SUSAN A. LYMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa mwaka 1994 Serikali ilifuta ile kwenda jeshini watoto wanaomaliza kidato cha sita kwa lazima na moja ya sababu hiyo ilikuwa ni pamoja na ukosefu wa fedha. Sasa hivi nchi yetu ina fedha na nikikukumbuka maneno ya Mheshimiwa Profesa Kabudi alisema nyumba yenye fedha ndio inaingiliwa na wezi. Sasa je, Serikali haioni kwa kuwa sasa tuna fedha nyingi, fedha hizo zitumike kupeleka wanafunzi wote wanaomaliza kidato cha sita kwenda jeshini ili kuwajengea ujasiri, ukakamavu na uzalendo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo aliloliuliza Mheshimiwa Mbunge hata sasa linafanyika mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sharia yalisharejeshwa na hivi ambavyo yanafanyika kufuatana na utaratibu wa kwenye makambi ambayo yanaendesha mafunzo hayo. Kutokana na bajeti zilivyotengwa idadi ya wanafunzi na wale wanaoenda kwa mujibu pamoja na wale wanaoenda kujitolea itaendelea kuongezea mwaka hadi mwaka. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Utakubaliana nami kwamba hakuna kada inayonyanyasika hapa nchini kama walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Serikali ilipunguza baadhi ya walimu wa sekondari kwenda shule za msingi kutokana na upungufu wa walimu na ikadai kwamba ina fedha za kuwalipa. Leo tunavyozungumza, baadhi ya Wakurugenzi wamewaambia wale walimu warudi kwenye shule za sekondari. Kwa hiyo, ina maana Serikali ilikuwa haijajipanga. Je, ni lini Serikali itawalipa walimu hao fedha kama ambavyo walidai kwamba watawalipa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Susan Lyimo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uamuzi ule wa kuhamisha walimu wa sanaa waliozidi katika shule za sekondari kuwapeleka kwenye shule za msingi ulikuwa ni sahihi. Kilichosisitizwa ni kwamba mtumishi yeyote anastahili apate haki zake kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni zetu za Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tangazo la Mheshimiwa Rais limetoka mwezi Februari kwamba mtumishi asihamishwe mpaka alipwe, wale ambao walikuwa wameshahamishwa watalipwa madeni yao halali, wala hakuna tatizo. Wale ambao walikuwa bado, wasubiri, watahamishwa baada ya fedha kupatikana. Wale ambao wamerudishwa ni kwa muda tu. Kwa hiyo, naomba hili liwe clear wala halina matatizo yoyote.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ahadi ni deni na kwa vyovyote vile Ilani hutekelezwa ndani ya miaka mitano, imekuwa ni kawaida kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi mara nyingi haitekelezwi siyo tu kwenye masuala ya afya ni pamoja na barabara na elimu. Nataka kupata kauli ya Serikali, je, hizi ahadi zao hasa za Marais zinakuwa ni za kuwadanganya watu? Pia ni lini sasa ahadi zote kuanzia zile za Mheshimiwa Mkapa…
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili ambalo linaulizwa leo halina tofauti kabisa na ambalo aliuliza Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kuhusiana na ahadi za wagombea Urais na utekelezaji wa Ilani ya CCM. Katika majibu yangu ambayo nilitoa siku ile nilieleza kwamba ahadi zimekuwa zikitekelezwa na Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa wakishukuru jinsi ambavyo ahadi zinatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ahadi za wagombea Urais ndiyo mkataba wao na wananchi na wananchi wamekuwa wakiwapigia kura kwa ku-base kwenye hizo ahadi ambazo zinatolewa na Ilani ya CCM inatekelezwa ndani ya miaka mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru kwa sababu amekuwa anafuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM na yeye mwenyewe anaamini kwamba tunatekeleza. Sasa amesema haitekelezwi, nadhani hapo atakuwa amepitiwa. Akatazame yale tuliyoahidi mangapi tumetekeleza, suala zima la afya yeye mwenyewe ni shuhuda na juzi tulikuwa tunaongea naye kuhusiana na barabara ya kule kwake na kazi imeshaanza kufanyika, kwa hiyo tunatekeleza. (Makofi)
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Barabara ya Kimara - Bahama Mama - Msewe kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilijengwa ili kuondoa msongamano katika Barabara ya Morogoro. Sasa magari haya yanapita Chuo Kikuu na Chuo Kikuu barabara imeharibika sana. Je, ni lini Serikali itajenga barabara ile ya Chuo Kikuu kutoka Msewe kuelekea jengo la Utawala ili kufanya mandhari ya Chuo Kikuu iwe nzuri kwa sababu kwa kweli barabara hiyo imeharibu sana barabara za Chuo Kikuu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara aliyoitaja ni muhimu sana katika kupunguza msongamano wa magari katika Barabara ya Morogoro hasa kwa watu wanaokwenda maeneo ya City Centre. Hata hivyo, barabara ile ina changamoto ya ufinyu wake. Kama inatakiwa kutengenezwa vizuri basi inatakiwa fidia kubwa sana ilipwe kwa wananchi ambao wamejenga mpaka karibu na barabara, hasa kuanzia Kimara kuja kupita maeneo ya milima ya Golani, kuja kuteremsha chini kwenye daraja hapo kuna uvamizi mkubwa sana ambao ulifanywa na wananchi, barabara ile ni finyu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo matengenezo yake yanahitaji tathimini ya kina ambayo itaishauri Serikali namna ya kuiendeleza hiyo barabara. Naomba sana kwa sasa hivi matengenezo madogo madogo ambayo yanafanyika wananchi watuvumilie yaendelee hiyo hivyo mpaka ambapo tathmini ya kina itakapokamilika.
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Mheshimiwa Naibu Waziri amesema na mimi najua kwamba ugonjwa wa kisukari ndiyo unaoongoza katika magonjwa yasiyoambukiza na mimi mwenyewe ni muathirika. Wataalam wanasema ugonjwa huu hauna dawa hasa Diabetic 1 lakini wataalam wengine hasa wa tiba mbadala wamekuwa wakidai kwamba ugonjwa huu unatibika. Ndiyo maana wengi wamekuwa wakienda huko ama wanatibiwa kweli au hawatibiwi. Naomba kujua Serikali inasema nini kuhusiana na hizi tiba asilia ambazo kimsingi naona kama zinapotosha. Nilikuwa naomba kauli ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeza kwa kuwa ni mfuatiliaji mzuri sana masuala ya magonjwa yasiyoambukiza hususan ugonjwa huu wa kisukari. Hoja yake ya msingi amegusia suala la tiba asili ya magonjwa ya kisukari. Naomba nitoe kauli kwamba hadi hivi sasa hatuna dawa yoyote ya tiba asili ambayo sisi kama Serikali tumeithibitisha kwamba inatibu ugonjwa wa kisukari. Nitumie nafasi hii kuwaambia watoa tiba za asili kwamba tunawahitaji na tunawataka wajisajili kama watoa huduma lakini kama kuna mtu ambaye anadhani ana tiba/dawa inayoweza kusaidia katika magonjwa yoyote yale kuna utaratibu wa kuhakikisha dawa hiyo inafanyiwa utafiti na inasajiliwa kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, nimalizie kwa kusema kwamba mpaka sasa hatuna dawa ambayo inatibu ugonjwa wa kisukari.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Kwa kuwa swali la msingi linahusu matatizo yanayowapata Watanzania wakiwa nchi za nje; na ni kweli kwamba kwa muda mrefu kumekuwa na matatizo makubwa, Watanzania wanakufa nje ya nchi, lakini unakuta wanaleta picha kwa mfano kutoka Marekani, watu wamekufa, watafutwe ndugu zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kujua Serikali ina kanzidata (database) ya Watanzania wanaoishi nje ili angalau pale wanapopata matatizo iwe rahisi kufuatilia? Vilevile hii itasaidia pia remittance ya kujua ni watu wangapi wanaishi nchi za nje?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Susan kwamba sisi katika Balozi zetu zote na sasa hivi zinafikia 40 kwa zile 35 za mwanzo, tumeweka mkakati wa kuhakikisha kwamba kila Balozi anahamasisha wale diaspora wanaoishi katika nchi husika kuanzisha jumuiya ambazo zinatupa record za Watanzania wangapi wako huko na wanafanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutumia hiyo diaspora tunaweza kujua kwamba huyu mtu yuko wapi na ni nani? Pale ambapo labda pengine Mtanzania ambaye yuko huku hajaweza kutoa taarifa zake kwenye Ubalozi ndipo tunapopata tatizo. Kule ambako tumeanzisha jumuiya na Watanzania ambao wamekwenda kutoa taarifa kwenye Ubalozi, tunakuwa tuna data zao.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Manispaa ya Moshi Mjini tayari imekidhi vigezo vyote na kikubwa zaidi ina Mlima Kilimanjaro ambayo ni highest pick in Africa. Nataka kujua process inaendelea vipi mpaka sasa hivi bado hatujapata majibu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, sijamwelewa vizuri Mheshimiwa Susan Lyimo kwa sababu Moshi tayari ni Manispaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, okay kuipandisha kuwa jiji. Pamoja na alivyosema kwamba imekidhi vigezo lakini bado hatujapata maombi rasmi kutoka kwenye vikao vinavyohusika kwa hivi karibuni….
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kama anazungumzia maombi ya zamani lakini ya hivi karibuni hatujapata.
MHE SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na nashukuru kwamba Serikali inatambua kwamba kuna changamoto nyingi za watoto wao kushindwa kwenda shule.
Mimi nilikuwa mmoja wa Wajumbe katika Kamati iliyozunguka nchi nzima kuangalia ni jinsi gani watoto hawa wanaweza kurudi shuleni na Serikali kama mtakumbuka mwaka 2017 Naibu Waziri alisema tayari wameshaandaa mwongozo wa jinsi gani ya kuwarudisha watoto hawa shule. Lakini ghafla bin vuu mtu mmoja tu Mheshimiwa Rais akatoa hilo katazo.
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu, ninaomba kujua kwamba Serikali imeshafanya tathimini ya kuona kuna athali gani za kijamii, kiuchumi na kisaikolojia kwa watoto hawa wa kike pamoja na watoto wanaozaliwa ni athari zipi hasa zinaweza kuwapata hasa ikizingatiwa kwamba hii sheria baba wa watoto hao nao atakuwa amefungwa miaka 30 hawaoni kwamba kutakuwa na athari kubwa sana?
Mheshimiwa Spika, swali la pili nchi nyingi pamoja na Zanzibar wanafunzi wanaopata ujauzito wanaendelea na shule, sasa hili jibu kwamba kuna elimu ya watu wazima. Serikali haioni kwamba hawa watoto wanaopata ujauzito wa miaka 12 mpaka 15, 16 ni watoto wadogo sana kiasi kwamba wakienda kwenye hiyo elimu ya watu wazima wanaenda kukutana na watu wazima. Lakini vilevile elimu hiyo ya watu wazima haiku coordinated hata kidogo na kwa maana hiyo wanawapelekea watoto hawa kufanya pia, mapenzi hawa watu wazima kwa vyovyote vile watawapa washawishi.
Serikali haioni kweli kuna kila sababu ya kuwapatia watoto hawa special education…
...ili waweze kuendelea na masomo yao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Lyimo ni mwalimu tena mzoefu na ni Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo na Huduma za Jamii. Kwa hiyo, haya masuala anayafahamu sana lakini ameamua kuleta mjadala. Lakini naomba maswali yake kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu kwamba katizo la wanafunzi wanaopata ujauzito kurudi mashuleni limetolewa na Mheshimiwa Rais naomba nimsahihishe kwamba katazo hilo limekuwepo toka mwaka 2002 kwa mujibu wa kanuni inayoitwa The Expulsion and Exclusion of Students from School Regulation 2002 iliyoanzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 60(o) ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978. Kwa hiyo, alichofanya Mheshimiwa Rais ni kusisitiza kitu ambacho kilishaamuliwa toka siku nyingi.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuhusiana na swali lake la pili kwamba elimu ya watu wazima haiwafai wale wanafunzi kwa sababu bado ni wadogo.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema yeye ni mwalimu Serikali imeamua kuchukua uamuzi huo kwa sababu ya kumlinda mtoto.
Mtoto ambaye anapata ujauzito mara nyingi akirudi shuleni anakuwa ananyanyapaliwa na wenzake. Kwa hiyo, hata yeye mwenyewe ata ukimruhusu aendelee na shule bado hawezi kuwa katika mazingira mazuri kisaikolojia. Lakini vilevile ni kwa sababu tunataka tuweke wazi kwamba hatutegemei wanafunzi wetu katika umri mdogo waendelee kufanya mapenzi wakiwa shuleni kwa sababu inawaathiri katika masomo yao. Kwa hiyo, ni suala la kuchagua na sisi tumechagua kwamba hatutaki tuchanganye mapenzi na elimu katika huo umri mdogo.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba SUMATRA imefanya maboresho na inatoa leseni kwa waendesha bodaboda, nataka kujua ni kwa nini kumekuwa na restriction kwa bodaboda kuingiza bodaboda zao katikati ya Jiji la Dar es Salaam, lakini vilevile ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hairuhusiwi? Naomba majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Susan Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Mkoa wa Dar es Salaam uongozi wa mkoa uliweka utaratibu wa namna vyombo hivi vya usafiri vitakavyoingia katikati ya mji kutokana na changamoto ambazo zilijitokeza awali likiwemo suala la msongamano pamoja na usalama. Tayari kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wameanza kuratibu zoezi hili katika umakini mkubwa ili kuona namna bora ambavyo wafanyabiashara hawa pia watafanya biashara zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika maeneo mengine zipo sababu za kimsingi za kwa nini yametokea masuala hayo lakini kubwa limekuwa ni suala la kiusalama. Ndiyo maana Serikali hivi sasa imeanza kuyatambua maeneo rasmi ya maegesho na kuwapatia vitambulisho ili likitokea jambo lolote la kiusalama tuweze kujua ni wapi limetokea na tuweze ku-trace ili kuondokana na dhana hii kwamba boaboda ni wahalifu.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu. Mabweni haya yana ghorofa nne nne na ni majengo 20. Bei hii ilileta maneno mengi sana na tukaomba CAG afanyie special audit. Nataka kujua ni jengo gani la ghorofa nne yenye kuchukua wanafunzi takriban 3,840 kwa majengo yote inaweza ghorofa moja kugharimu shilingi milioni 500 tu?

Mheshimiwa Spika, la pili, nataka kujua baada ya TBA kuyajenga majengo yale ndani ya miezi minne yalikuwa na nyufa nyingi, maarufu kama expansion joint ambazo sisi tunavyojua ni lazima jengo liwe nalo, lakini expansion joint
hizo zilienda mpaka kwenye floor na mpaka kwenye madirisha. Nataka kujua ni kwa sababu gani mabweni hayo yalimomonyoka na ni je ni gharama kiasi gani imetumika sasa kuweza kurekebisha hasa ikizingatiwa kwamba TBA hivi majuzi tu Mheshimiwa Rais aliwafukuza kwenye kazi mbalimbali. Je hili jengo ambalo sasa hivi limetengewa bilioni moja ni hao hao TBA pale kwenye hayo Magufuli Hostel watajenga au wamepata mkandarasi mwingine?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:

Mheshimiwa Spika, kuhusu hitilafu alizosema zimetokea na hususan zile zinazohusishwa na expansion joint naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba expansion joint sio hitilafu, expansion joint imekusudiwa kuwekwa kwenye maghorofa yale ili kuweza kuhimili changamoto ambazo zinaweza zikatokea, ni kazi ya kitaalamu na wala sio upungufu na tayari tulishatoa maelezo marefu sana kuhusu hili.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na upungufu mwingine mdogo mdogo uliotokea, hii ni kawaida ambayo inatokea katika ujenzi na tayari ilisharekebishwa na kwa sababu tayari mkandarasi aliyepewa kazi bado alikuwa katika kipindi cha liability alirekebisha yeye mwenyewe na tayari ilishakwisha na hakukuwa na fedha za ziada ambazo zilitumika kurekebisha changamoto hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu gharama naomba nimhakikishie Mheshimiwa Susan Lyimo kwamba jengo hilo limegharimu shilingi bilioni 10. Sasa kama yeye anatilia shaka kuhusu ukweli huo ambao namweleza labda yeye atuletee mahesabu yake ya kuonesha kwamba imegharimu zaidi, lakini hizi ni fedha za umma, zimelipwa kwa mujibu wa taratibu, taarifa rasmi ambayo naileta Bungeni ni kwamba imetumia shilingi bilioni 10 na hakuna fedha nyingine yoyote iliyotumika ukiacha fedha ambazo zimetumika kwa ajili ya kufanya masuala mengine ambayo ni nje ya scope ya kazi ile ambayo walipewa TBA.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri anapojibu anaelezea suala zima la kujenga vyuo kila wilaya na mkoa, lakini hawajazungumzia changamoto kubwa ya tatizo kubwa la Walimu wa ufundi stadi. Je, wanapojenga hivi vyuo kila mkoa na kila wilaya wana Walimu kwa sababu, wana Chuo kimoja tu cha Ualimu wa Ufundi Stadi kule Morogoro, ni lini wataongeza au waapanua chuo kile au kujenga chuo kingine, ili tupate Walimu bora ambao wataweza kuhimili au kwenda kwenye hivi vyuo ambavyo vinajengwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Lyimo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, kuna upungufu huo na Serikali inatambua na tumeanza hatua za makusudi kuhakikisha kwamba, tunaongeza upatikanaji wa Walimu katika vyuo vyetu vya ufundi.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri na mikakati yote ya Serikali bado idadi (ratio) ya wasichana kwa wavulana katika vyuo vyety vya elimu ya juu ni ndogo sana katika masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba baadhi ya vyuo, kwa mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siku za nyuma kilikuwa na programu ambayo ilikuwa inawasaidia wasichana ambao wamepata point chache wanakuja kwenye hiyo programU walau miezi miwili ili waweze sasa kujiunga na vyuo lakini programU hiyo sasa haipo na bado tunahitaji sana wasichana kuendelea na masomo. Swali la kwanza, je, ni lini programu kama hizo zitarudishwa ili kusaidia wasichana kwa kuwa tunatambua mazingira magumu wanayowapata wasichana huku chini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pamoja na kwamba wanajenga mabweni au hosteli katika vyuo na shule zetu lakini bado tuna tatizo kubwa sana la uhaba wa mabweni ambayo yangewasaidia wasichana hawa kuweza kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kuweza kuweka uwiano wa kijinsia siyo tu katika vyuo lakini hata katika masuala mazima ya siasa maana tunapata wanawake wachache kwa sababu hiyo. Ni lini mtatekeleza hilo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Susan Lyimo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siku za nyuma kilikuwa na mpango ambao ulifanikiwa sana wa kuwasaidia wanafunzi wengi wa kike kuweza kujiunga na masomo ya sayansi. Mpango ule muda wake ulishaisha lakini kwa sasa tayari kuna majadiliano ya kurudisha au kuanzisha programu inauhusiana na suala hilo na katika hali ambayo itawahusisha watoto wa kike wengi zaidi katika vyuo vingine, kwa hiyo, majadiliano yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi kama Serikali tunachofanya ni kuboresha elimu kwa ujumla wake pamoja na kutoa hamasa na kuomba wananchi na wadau wote washirikiane katika kuondoa mila na fikra potofu ambazo zinafanya watoto wa kike waogope kwenda kuchukua masomo ya sayansi. Nashukuru kwamba leo tumetembelewa na wanafunzi wa kike wa sekondari. Naomba nitumie nafasi hii kuwaeleza kwamba sayansi na hisabati ni ya kila mtu na siyo kwa ajili ya wanaume tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili kuhusiana na ujenzi wa mabweni na hosteli, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara yangu mwezi Januari ilipeleka katika shule na vyuo tofauti 560 shilingi bilioni 56 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kujenga miundombinu katika shule na vyuo vyetu na kati ya fedha hizo, nyingi zimeenda vilevile katika kujenga hosteli na mabweni. Yeye mwenyewe anajua baadhi ya vyuo kwa mfano Chuo cha Ardhi na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere tunajenga hosteli kwa ajili ya wanafunzi lakini maarufu kwa utetezi wake wa Hall 2 na Hall 5 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa sasa vimetengewa shilingi bilioni nne. Kwa kweli katika vyuo vyetu tunajitahidi kujenga mabweni na hosteli za wanafunzi.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Sekta ya afya kwa ujumla wake ina tatizo kubwa sana la watumishi, takribani asilimia 48 hakuna watumishi na hii imeathiri zaidi kwa sababu ya zoezi zima la uhakiki wa vyetii feki, ambapo tuliambiwa baadhi ya vituo ya afya vilifungwa. Nataka kujua nini mkakati wa Serikali
pamoja na kwamba wanajenga vituo, wana mkakati gani wa kuhakikisha kwamba vituo hivi vya afya vyote vinapata wataalam ili lipunguze tatizo kubwa la akinamama na watoto ambao wanafariki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lyimo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba mahali popote ambapo vituo vya afya vinajengwa vinakamilika, zahanati zinajengwa zinakamilika, hayabaki yakawa majengo ambayo tunayatazama, tutahakikisha kwamba vifaa vinapelekwa na wataalam wanapelekwa. Mheshimiwa Lyimo ni shahidi, siku tukiwa ndani ya Bunge hili Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Mkuchika alisema kama yupo Mbunge yeyote ambaye eneo lake zahanati imefungwa au kituo cha afya hakina wataalam kabisa apeleke orodha, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba huduma zinatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie, kuna kipindi ambacho tulitangaza nafasi especially kwa ajili ya Madaktari tuliweza kufanya mopping, hakuna Daktari hata mmoja ambaye alikuwa ame-qualify akabaki bila kuajiriwa. Ikafikia mahali ambapo Madaktari wote wameajiriwa na wengine hawajaripoti. Kwa hiyo pia tuna tatizo juu ya wataalam wenyewe kuwepo maana na demand nayo ni kubwa si kwa Tanzania peke yake, wengine wanaenda kutafuta green pastures outside this country.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na wimbi kubwa la wanaume na vijana kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume, sasa hivi kuna baadhi wanatumia dawa za kukuza maumbile ya kiume, nataka kujua nini madhara yake na ni kwa nini wanafanya hivi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Susan Lyimo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na taarifa nyingi za dawa zinazoweza kukuza maumbile na wito wangu ni kwamba, watu waendelee kuhakikisha kwamba hawatumii dawa yoyote ambayo haijasajiliwa, haijathibitishwa kitaalamu kwa sababu inaweza ikasababisha madhara na wale ambao wanatoa taarifa hizi bila ya uthibitisho kwa kweli wanafanya kosa na wanatakiwa wachukuliwe hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa nilizokuwa nazo ni kwamba hakuna dawa yoyote ambayo kitaalam imethibitishwa na imepewa kibali kwa ajili ya matumizi kama hayo. Kwa hivyo nawaomba Watanzania wawe makini wanapotaka kununua dawa kama hizi kwa sababu zinaweza zikawa zina madhara. Tungependa wananchi watoe taarifa endapo wamewahi kutumia na wamepata madhara yoyote ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Hapa Tanzania takriban watoto 213000 njiti huzaliwa kila mwaka na kati ya hao zaidi ya 9000 huwa wanafariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa natambua kwamba, tarehe 17 Novemba, kila mwaka ni siku ya watoto njiti duniani. Nilitaka Waziri atuambie kwa hapa Tanzania wanaadhimishaje siku hiyo kwa sababu, nadhani hata Wabunge hatuna taarifa; mnaadhimishaje siku hiyo kuhakikisha kwamba, tatizo hili sasa linapungua na wananchi wanalielewa vizuri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Susan Lyimo, Mbunge Viti Maalum, kwa ufuatiliaji mkubwa na kuwa mdau wa masuala haya. Niseme tu kwamba, siku hii ya tarehe 17 Novemba, ni fursa kwetu kama Wizara kutoa elimu kwa jamii kwa njia mbalimbali kuhakikisha kwamba, na mara nyingi tunakuwa na kauli mbiu mbalimbali kuhusiana na kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na suala hili, visababishi vyake ni nini, huduma zake ni zipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi kama Serikali sasa hivi tunahimiza sana hili suala la Kangaroo Motherhood. Kinamama kuwalea watoto wao njiti kwa kupitia kupeana joto la mwili kwa mwili, ili kuhakikisha kwamba, wale watoto ambao mara nyingi wanakuwa na matatizo ya mapafu na kutunza joto basi waweze kupata joto pasipokutumia incubators.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tatizo kubwa la misongamano katika hospitali zetu ni tabia ya Serikali kupandisha hadhi vituo vya afya kwenda hospitali ya wilaya, hospitali ya wilaya kuwa hospitali ya mkoa, hospitali ya mkoa kuwa hospitali ya rufaa. Kwa mfano Hospitali ya Mwananyamala ilianza kama clinic lakini leo ni hospitali ya rufaa kwa hiyo wale watu waliokuwa wanatibia pale wanaenda wapi? Kwa hiyo, nilitaka kujua ni lini Serikali itaacha tabia hii mbaya ya kupandisha vituo kuwa hospitali badala yake kama wanataka kujenga hospitali wajenge hospitali na vituo vya afya vibaki kama vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kutoa ufafanuzi Serikali haina tabia mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba idadi ya watu inazidi kuongezeka miji inazidi kukuwa na ndio maana na huduma zinazidi kuhitajika kwa wingi zaidi. Inawezekana tulianza kama zahanati ikaja kituo cha afya, hospitali za wilaya na zitakwenda mpaka ngazi ya rufaa. Lakini sisi kama Serikali tumeliona hilo na bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge tulikuwa naye na ni mjumbe wa kamati yetu anajua kuna maboresho makubwa sana hata lile jengo ambalo tulikuwa limesuasua la jengo la uzazi hilo Serikali imeshapata fedha na tuko katika hatua sasa hivi za kutaka kulikamilisha lile jengo kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma katika hospitali ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambasamba na hilo Serikali imeendelea kuweka mikakati moja ya changamoto ambayo inaleta misongamano katika hospitali hizi nyingi za rufaa za mikoa especially pale katika Jiji la Dar es Salaam ni mfumo mzima wa rufaa. Kwa hiyo, uboreshaji wa hivi vituo vya afya ambavyo tunavyovijenga ujenzi wa hospitali hizi za wilaya naami nazo zitasaidia sana kupunguza ule mzigo mkubwa ambao unaonekana katika hospitali zetu nyingi za rufaa za mikoa. Kwa hiyo, nimtoe tu wasiwasi Mheshimiwa Mbunge hili tumeliona na tumelifanyia kazi kwa kuimarisha sasa mifumo ya afya ya msingi ili sasa hospitali za rufaa za mikoa ziweze kutoa huduma zake za msingi kama hospitali za rufaa za mikoa.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ni wazi kwamba kwa nchi nzima tuna matatizo makubwa sana ya upungufu wa madarasa. Sasa nilitaka kujua Serikali ina mpango mkakati gani wa kuhakikisha kwamba walau kwa kila mwaka wanajenga madarasa kadhaa wakati wanajua kabisa kwamba projection ya idadi ya watoto wanaijua. Sasa nilitaka kujua wana mkakati gani mahsusi wa kuhakikisha kwamba hili tatizo walau kila mwaka watakuwa wanajenga madarasa kadhaa kwa kila mkoa na wilaya.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tumeona hiyo changamoto wakati ambapo watoto wanaenda kuingia kidato cha kwanza, darasa la awali na darasa la kwanza ilionekana kuna upungufu mkubwa wa madarasa. Tumeshawaelekeza wakurugenzi wanafahamu, mwaka huu projection darasa la saba wanamaliza wangapi, kwa hiyo vacancy itakuwa ni kiasi gani, form four wanamaliza wangapi, vivo hivyo kidato cha sita, wafanye hiyo kazi na kila halmashauri, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wameelekezwa lakini sisi kwenye bajeti tumetenga zaidi ya bilioni 90 kwa ajili ya kazi hiyo, ahsante.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu ya Serikali, kilio kikubwa cha wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ni pamoja na tozo ya asilimia moja kwa ajili ya administrative costs za bodi. Nilitaka kujua, Serikali haioni kwamba huku ni kuwaibia wanafunzi? Kwa sababu tunajua tuna bodi nyingi ambazo hazitegemei makato ama ya watumishi au ya wafanyakazi wake, ni kwa nini Bodi ya Mikopo unawatoza wanufaika asilimia moja kwa ajili ya administrative costs za bodi!
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, Serikali inatoza tozo ya asilimia moja kama management costs kwa ajili ya mkopo unaotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu, lakini ifahamike kwamba, kazi ya kuweza kufuatilia na kutoa mikopo ile ina gharama kubwa na ni kawaida katika utoaji wa mikopo, kwamba mkopo ule vilevile uweze kugharamia uendeshaji wake, vinginevyo inahitaji utafute fedha za ziada ili kuendesha ule mkopo.

Mheshimiwa Spika, asilimia moja anayosema Mheshimiwa Mbunge, inatozwa mara moja, haitozwi kwa mwaka. Kwa hiyo, ni one off payment na ukiangalia, ukilinganisha sisi tunachotoza na nchi zingine, sisi tunatoza asilimia ndogo sana, hata kwenye tozo zingine kwa ujumla wake. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba utoaji wa mkopo unafanyika kwa ufasaha zaidi.

Mheshimiwa Spika, na nimhakikishie tu kwamba, asilimia hiyo moja, imetuwezesha katika hii miaka minne kuongeza marejesho ya mikopo kutoka shilingi bilioni 23 toka mwaka 2015/2016 mpaka sasa kufikia bilioni 183 mwaka huu. Ile fedha inatusaidia kufuatilia kwa sababu watu ambao hawataki kutoa ni wengi, ina gharama. Kwa hiyo, naomba ajue tu kwamba lengo letu siyo kuwaumiza wanafunzi wala wazazi lakini ni kuhakikisha kwamba mikopo ile inarejeshwa na inatolewa kwa utaratibu ambao ni mzuri na yeye mwenyewe ni shahidi, yeye mwenyewe ameshatusifu mara nyingi kwamba tumefanikiwa sana kwenye elimu ya mikopo ya elimu ya juu.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, suala hili la upungufu wa madarasa limekuwa likijirudia mara kwa mara na Waziri anasema wana takwimu. Mwaka juzi wanafunzi 133,000 walifaulu lakini wakashindwa kuchanguliwa kwa sababu ya madarasa, lakini mwaka huu tena zaidi ya wanafunzi 58,000 wamefaulu darasa la saba lakini wamekosa madarasa.

Mheshimiwa Spika, swali langu, ni kwa sababu gani Serikali kama ina projection na inajua ni wanafunzi wangapi wanaweza kufaulu na wako darasa la saba, ni kwa sababu gani hawana mpango mahususi kuhakikisha kwamba kila mwaka wanatenga fedha kwa ajili ya madarasa ili angalau kwa miaka mitano tuhakikishe kwamba tatizo hili sugu limekwisha na wanafunzi wetu wanapomaliza darasa la saba wanakwenda shuleni kama wengine. Kwa sababu tunavyozungumza leo kuna Wanafunzi Dar es Salaam na Mikoa mingine wamefaulu darasa la saba lakini watakwenda kuanza mwezi wa tano, haoni kwamba hili ni tatizo? Ahsante sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimshukuru dada yangu Mheshimiwa Susan Lyimo kwa sababu amekuwa na mchango mkubwa sana katika elimu.

Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya kila liwezekanalo na kwa mfano, mwaka huu tulikuwa na wanafunzi takribani 759,000 waliofaulu na hii inaonekana kutokana na juhudi kubwa ndiyo maana mwaka huu ufaulu umepanda kwa wastani wa asilimia 3.7 ambayo ni mafanikio makubwa sana yaliyowahi kutokea.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana licha ya ufaulu huo ulikuwa mkubwa lakini zaidi ya asilimia 92 na wanafunzi wote tuliowachangua katika awamu ya kwanza tulibakisha wanafunzi 58,000 ambao hata hivyo wanafunzi wote hivi sasa tumeshawachangua na hivi sasa kuna shughuli kubwa sana ya umaliziaji baadhi ya madarasa 1,080 ambayo naomba niwahakikishie Watanzania kwamba ukiona juhudi wanafunzi wanafaulu ni impact kubwa ya Serikali ya uwekezaji iliyosababisha mpaka wanafunzi waweze kufaulu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tushikamane kwa pamoja kuona ufaulu mkubwa kwetu sisi iwe ni mafanikio makubwa kwamba Tanzania inasonga mbele katika suala zima la kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu. Ahsante.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na niseme tu kwamba majibu ya Waziri hayajaniridhisha hata kidogo kwa sababu swali langu lilihoji matatizo makubwa yaliyopo lakini na kama tuna haja ya kuleta Sheria ndani Bunge lakini bado hajajibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, ukiangalia hata jibu lake ni kweli kwamba bado kuna tatizo kubwa ndiyo sababu wanasema wanaendelea kuboresha, lakini baada ya nyongeza ya asilimia 15 takwimu zinaonyesha toka mwaka 1994 wakati Bodi ya Mikopo imeanzishwa au Sheria hii imeanzishwa kati ya Wanufaika takribani 500,000 ni wanufaika 11,000 tu wameweza kurejesha Mikopo mpaka mwaka jana kwa maana ya kwamba ni asilimia 2.3 tu na hapo bado Sheria ilikuwa haijaongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu, Waziri au Serikali haioni kwamba nyongeza hii kubwa ya makato yatapelekea sasa Wanafunzi badala ya kulipa ndani ya miaka 4 au 10 ambayo anasema Mheshimiwa Naibu Waziri sasa hivi itaenda mpaka miaka 30 kiasi kwamba wanafunzi hawa wanufaika watakuwa ama wameshafariki au wamestaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali za Wanafunzi zimekuwa ndiyo daraja kati ya Serikali na Serikali Kuu kwa maana ya Wizara pamoja na wanafunzi wenyewe na kwa muda mrefu na mimi kama Mshauri wa Wanafunzi nilivyokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Viongozi hawa wa Wanafunzi wamekuwa wakipata madhara makubwa sana ikiwa ni pamoja na kufukuzwa wakati wanadai madai ya Wanafunzi kwa sababu wote tunajua kwamba Wanafunzi wa Elimu ya Juu wanahitaji Mikopo. (Makofi)

SPIKA: Tatizo unahutubia sasa Mheshimiwa Susan.

MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nilitaka nimalizie.

SPIKA: Eeh malizia kwa kuuliza swali.

MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Spika, wanahitaji mikopo kwa ajili ya kusoma lakini Wanafunzi hao wanakaa zaidi mwezi mmoja bila kupata Mikopo hii, wanapodai wanafukuzwa wakati matatizo makubwa ni kwa Wizara yenyewe pamoja na Vyuo kutopeleka majina.

SPIKA: Basi sasa inatosha. (Makofi)

Mheshimiwa ...

MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Spika, sasa nilitaka kujua…

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri majibu na Profesa alitaka aongezee anasema matatizo ni wewe mwenyewe Wizara. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Waziri majibu tafadhali.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kuhusu kwamba inachukua muda mrefu sana kwa Wanafunzi hao wanaodaiwa Mikopo kurejesha Mikopo uzoefu wetu Wizarani unaonyesha kwamba tatizo halipo kwa sababu ya value retention fee ipo kwa sababu ya watu kutotaka kurejesha Mkopo.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 tulipoingia Madarakani urejeshwaji ulikuwa ni shilingi bilioni 23 kwa mwaka lakini baada ya kuweka jitihada napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mwaka huu tunategemea urejeshwaji utakuwa shilingi bilioni 200 kwa mwaka, mwaka jana ilikuwa bilioni 183.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, shida haipo katika fedha ile, tozo ya kulinda thamani ipo katika watu wenyewe kuhamasika kurejesha Mkopo. Kwa hiyo, kwa sababu tumeweka jitihada kubwa katika urejeshwaji wa Mkopo tumeanza kuona kwamba warejeshwaji wengi wanaanza kurejesha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kuhusu kama tuna mpango wa kuleta Marekebisho ya Sheria uzoefu wetu unatuonyesha kwamba Sheria ya sasa na hasa kama ilivyorekebishwa na Bunge hili mwaka 2016 bado inakidhi mahitaji ya utoaji wa Mikopo nchini, lakini pia kama Mheshimiwa Mbunge anaona kwamba kuna haja ya kuleta Marekebisho ya Sheria hiyo ndiyo kazi ya Bunge. Lakini angalau sisi kama Serikali tunaridhika na Sheria ya sasa haijatupa shida yoyote tunachoendelea kusema tu ni kwamba wale waliokopeshwa warejeshe Mikopo kwa sababu usiporejesha kwa wakati ndiyo deni lile linaongezeka na inakuwa ni vigumu kulipa.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili la kuhusu Serikali za Wanafunzi, nafurahi sana kwamba nimesikia swali hili kutoka kwake kwa sababu ni kweli kwamba Mheshimiwa Susan Lyimo kwa muda mrefu alikuwa ni anafanya kazi kwenye Ofisi ya Mshauri wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kipindi kile ambacho migomo ilikuwa ni mingi sana. Lakini tunachosema ni kwamba kilichotokea hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilikuwa ni kuturudisha nyuma, tulishaondoka kule hatupo tena kwenye enzi ya kuanza kuvutana na Wanafunzi kuhusiana na Mikopo.

Mheshimiwa Spika, Mikopo siku hizi, fedha za Mikopo zinatolewa na Serikali angalau miezi miwili kabla ya Vyuo kufunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachotokea hili ninaweza nikawahakikishia kwa sababu niko Wizarani kwa zaidi ya miaka miwili, na tena Mheshimiwa Rais mwenyewe anafuatilia kila, tatizo sasa hivi siyo fedha hazitoki Serikalini inakuwa ni changamoto ya michakato ya ndani ya Vyuo na hata kilichotokea kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilikuwa ni sehemu ndogo sana ya wanafunzi ambao bado taarifa zao zilikuwa hazijakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, hatutakaa tukubali wanafunzi ambao sisi ndiyo tunawapa Mikopo kama Serikali kuitishia Serikali kwamba msipotoa fedha katika masaa sabini na mbili wataandamana. Sio tu kwamba inapingana na Sheria na taratibu za kuendesha Vyuo Vikuu lakini hata katika maadili ya kawaida ya Kitanzania mtoto hawezi kumpa mzazi ultimatum kwamba Baba usipoleta karo nakuja nyumbani na utaniona, kwa hiyo, tunaendelea kuwachukua hatua kwa mujibu wa Sheria zilizopo. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niongezee majibu mazuri ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyasema, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Susan Lyimo Waziri mwenzangu wa Elimu yeye akiwa ni Waziri Kivuli na swali lake kuhusiana na Serikali za Wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuwahakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Serikali za Wanafunzi na inatambua kwamba Serikali za Wanafunzi ni daraja muhimu kati ya Wanafunzi na Uongozi wa Chuo lakini pia kati ya Wanafunzi na Serikali kwa ujumla pale ambapo kunakuwa na changamoto za Wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningeomba tu hizi Serikali za Wanafunzi ambazo tunazitambua na kuthamini michango yao watumie njia ambazo ni taratibu zinazotambulika katika kuwasilisha changamoto zao.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la kuchelewesha ulipaji wa fedha kwa ajili ya Wanafunzi, nirudie kusema jambo ambalo Mheshimiwa Naibu wangu amelisema Serikali imekuwa ikitoa fedha miezi miwili kabla ya Chuo kufunguliwa.

Mheshimiwa Spika, kinachotokea na kilichotokea mwaka huu kwa baadhi ya Wanafunzi wapo Wanafunzi ambao anasaini fedha yake ya kutumia ile boom ya chakula na malazi lakini anakuwa hasaini kwenye sehemu ya ada za Chuo kwa sababu ile hela haiendi kwake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kilichofanyika Vyuo vimeangalia kuna Wanafunzi ambao walikuwa wamefika mwaka wa tatu lakini alikuwa hajasaini fedha ya malipo ya Chuo kwa mwaka wa pili na kwa mwaka wa kwanza na kinachotokea asiposaini zile hela Bodi ya Mikopo inazirejesha kwa hiyo, Wanafunzi walikuwa ni wanufaika wa Bodi ya Mikopo lakini walikuwa wanaonekana wanadaiwa kwa sababu hawakuwa wamesaini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kuwasihi Wanafunzi kuhakikisha wanakamilisha taratibu zote ambazo zimewekwa ili waweze kupata fedha zao kwa wakati kwa sababu fedha za Mikopo zipo na Serikali hii inakuwa inazitoa kwa wakati. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ukiangalia matukio yote haya yanatokana na sababu kwamba wananchi wengi hawajapata elimu. Hapa Mheshimiwa Naibu Waziri anazungumzia suala la mpango mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, lakini sisi kama wadau wakubwa hatujapata hata semina wala hatujui huo mpango. Nataka kujua, Serikali italeta lini mpango huo ili sisi kama Wabunge tuujue na tuweze kuupeleka katika maeneo yetu. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali baada ya kubaini ukubwa wa tatizo hili, tulikuja na mpango unaitwa MTAKUWA ambao ni Mpango Mkakati wa Serikali wa Kutokomeza au Kudhibiti Ukatili wa Kijinsia wa Wanawake na Watoto. Ndani ya Mpango huu kuna mambo mbalimbali mbayo tumeyaainisha, moja ni kuanzisha Kamati za Ulinzi za Wanawake na Watoto, kuanzisha huduma za mkono kwa mkono na masuala ya kutoa elimu mbalimbali katika nyanja mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge naye ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Wabunge, wote kwa ujumla tutafanya utaratibu wa kuhakikisha tunatoa elimu kuhusiana na mpango mkakati huu. Tunawaomba sana Waheshimiwa Wabunge nanyi muwe mabalozi wa mpango huu wa MTAKUWA kwenda kukemea masuala haya ya ukatili wa kijinsia katika sehemu ambazo mnatoka.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake japo hayaridhishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Sera ya Afya inazungumzia suala la uchangiaji, lakini vilevile Serikali itakubaliana nami kwamba Tanzania bado watu wengi ni maskini lakini kubwa zaidi maiti inapaswa kupata heshima yake na ndiyo sababu inahifadhiwa na uhalisia unaonesha wazi, kwamba watu wengi wameshindwa kutoa maiti hizo na matokeo yake tumeona hata hivi majuzi pale Muhimbili Mheshimiwa Rais akitoa takribani 5,000,000 kwa yule Mama kwa ajili hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza Mheshimiwa Rais ataenda kila mahali kutoa hizo fedha. Nilitaka kujua sasa Serikali ina utaratibu gani wa muda mfupi na muda mrefu kuhakikisha kwamba wale wenye matatizo makubwa ambao wanashindwa kabisa wanakabidhiwa maiti zao kwa wakati? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Mheshimiwa Waziri amesema kweli watu wajiunge kwenye Bima ya Afya nami nakubaliana naye, lakini Serikali hii mpaka leo tunapoongea ni asilimia takribani 33 tu ya watu waliojiunga kwenye Bima ya Afya. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba hiyo asilimia 66 nayo inajiunga kwenye Bima ya Afya ili tuondokane kabisa siyo tu na tatizo la kutoa maiti hospitalini, vilevile wananchi wapate afya kama haki yao ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anapokwenda kupata matibabu kuna matokeo mawili anaweza akapona au akapoteza maisha. Nami naomba niseme tu kwamba hakuna maiti ambayo imezuiliwa moja kwa moja au tumezishikilia moja kwa moja kutokana na kwamba mtu ameshindwa kutoa gharama za matibabu. Serikali mimi pamoja na Waziri wangu na Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa wanatufuata, nitumie fursa hii kuwaomba wananchi katika ambao wanapata huduma katika hospitali zetu kubwa na hii tumekuwa tunaipata changamoto katika Hospitali ya Mloganzila, Hospitali ya Muhimbili na maeneo mengine kufika ofisi ya Ustawi wa Jamii katika hospitali husika, pale watapewa malekezo sahihi ya utaratibu wa kufanya na utaratibu wa kulipa, wanaweza wakapewa maelekezo ya kulipa taratibu. Siyo jukumu na nasi kama Serikali hatuzuii ile miili lengo ni kuhakikisha kwamba tunaweka utaratibu mzuri zaidi kuhakikisha kwamba yale madeni yanalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano kwa Mheshimiwa Mbunge hospitali ya Temeke kati ya Juni na Agosti mwaka huu ambao tunakaa tunaongelea wagonjwa wa msamaha kwa mwezi Juni, Temeke yake walikuwa ni wagonjwa 4,949, Julai wagonjwa 4, 816, mwezi Agosti wagonjwa 4, 809, na jumla yote ukikaa ukipigia hesabu ni takribani zaidi ya milioni 500.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo suala la kuwa na mgonjwa amefariki haiondoi jukumu la ndugu na jamaa wa yule mgonjwa kuhakikisha kwamba wanalipia zile gharama. Kama nilivyosema utaratibu tumeweka wa Serikali kupitia Idara za Ustawi wa Jamii katika hospitali husika mgonjwa ama ndugu wanapaswa kwenda pale na watapewa utaratibu sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lako la pili umeongelea kwamba asilimia 33 tu ya wananchi wako katika Bima ya Afya hii ni kweli tumeliona hilo, kusudio la Serikali ni kuleta Muswada wa Bima ya Afya ndani ya Bunge hili na huu mchakato umefikia hatua nzuri tunategemea kwamba ikifika Bunge la Novemba, Muswada huu tutauleta ndani ya Bunge lako Tukufu. Lakini katika kipindi cha mpito tumeona umuhimu na haja na uhitaji wa wananchi, tunataka sasa tufanye uzinduzi wa vifurushi ambavyo vitakuwa ni rafiki zaidi wananchi wa kawaida wanaweza wakavimudu kwa lengo kuhakikisha kwamba hii changamoto ambayo tunaipata wakati Serikali tumeboresha sana Sekta ya Afya, lakini uwezo wa wananchi kugharamia huduma za afya umekuwa ni changamoto ili wananchi sasa na kwa sababu wananchi tayari wameshahamasika tunaamini tutakapokuja na hivi vifurushi mbadala ambavyo tunategemea tutavizindua hivi karibuni itaongeza wigo mkubwa sana wananchi kuweza kujiunga nje ya wale ambao wamekuwa ni Watumishi wa Umma.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri ni kweli kwamba kwa Jiji la Dar es Salaam tunajua kwamba population ni kubwa sana lakini National Housing wamechukua maeneo na hasa eneo la Kawe ambalo ni Satellite City na walishaanza ujenzi pamoja na pale Morocco Square. Nataka kujua, ni kwa nini ujenzi huo umesimama na ni lini wataendeleza ili wananchi wa Dar es Salaam waweze kupata makazi salama? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Susan Lyimo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli miradi ile ilianza na ikawa imesimama na ilisimama tu sio pengine kwamba National Housing wameshindwa kuendeleza, lakini kulikuwa na taratibu za kisheria ambazo zilikuwa zinafuatwa ili kuweza kukamilisha. Napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kuanzia sasa ataona miradi ile inaendelea tukianza na Morocco Square kwa kutumia mapato ya ndani ya National Housing wanakwenda kujenga majengo yale na kukamilisha, kwa hiyo hatutakuwa na viporo tena. Tunamaliza Morocco Square then tunaenda kule seven eleven ya Kawe. Hayo yote yako kwenye Mpango na Bodi mpya ambayo inafanya kazi hiyo imeweka Mpango Kazi wa kuhakikisha miradi viporo yote ya National Housing inakamilika kutokana na schedule walivyojipangia. Kwa hiyo niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge, miradi hiyo yote inakwenda kuanza kukamilishwa.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi. Ilikuwa ni kilio cha muda mrefu kwamba kwa kuwa Sera ya Wazee ipo toka mwaka 2003, lakini sheria hamna ndiyo maana wazee wanaendelea kunyanyasika. Hata hivyo, kuna Sheria ya Watoto ambapo mzazi asipomlea mtoto au asipompa matunzo, anashtakiwa.

Mheshimiwa Spika, ni kwa nini basi kusiwe na sheria ambayo italazimisha mtoto au kijana, mtu mzima aweze kumlea mzazi wake kwa sababu tunajua kwamba wazee hawa kwa kweli wamefanya kazi kubwa, wamewasomesha watoto, lakini watoto wamewatelekeza. Ni kwa nini kama kuna Sheria ya Watoto, kusiwe na Sheria ya Wazee ambayo itarahisisha sana maisha ya wazee hapa Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, changamoto ya wazee tutazidi kuiona ikiongezeka na hii ni kwa sababu ya maendeleo makubwa ambayo tumeyapiga katika huduma zetu za jamii. Sasa hivi wastani wa Mtanzania kuishi miaka 64. Kwa hiyo, tunatengemea tutakuwa na idadi kubwa sana ya watu ambao wanaitwa wazee, kwa sababu vifo vimepungua na hali ya afya nayo imeboreka sana.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Sera ya Afya ni ya mwaka 2003 na sasa hivi tumeiona kwamba imepitwa na wakati. Tupo katika marejeo ya kuipitia hii Sera mpya ya Afya. Tukapoikamilisha, tuangalia sasa uwezekano kwa kuja na sheria mpya ambayo sasa itakuwa inaweka haki za wazee katika msingi mizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, hili ambalo analisema Mheshimiwa Susan Lyimo ni moja ya jambo ambalo tunaweza tukalizingatia.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu japo hayajajitosheleza Kilimo cha Umwagiliaji ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kwamba tunapata chakula cha uhakika, au mavuno kwa uhakika, lakini ukiangalia katika Magereza yote tuliyonayo nasema kwamba ni Gereza la Idete pekee ndiyo wenye Kilimo hicho cha Umwagiliaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata Bajeti ya mwaka huu, ya maendeleo bado Wizara hii imeendelea kutenga shilingi Bilioni tatu kwa ajili ya Kilimo, jambo ambalo bado litaendelea na utegemezi. Je, Wizara haioni sasa kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba wanaendeleza Kilimo cha Umwagiliaji ili Magereza wetu na Mahabusu waweze kupata chakula? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa takwimu zinaonyesha kwamba mahabusu ni wengi kuliko wafungwa na kwa maana hiyo ndiyo sababu chakula hakitoshi, Je, Serikali haioni sasa kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba mahabusu hasa wale wenye kesi za madai, kwa mfano kesi ya kuiba kuku nakadhalika nakadhalika, hawakai ndani ya Magereza kwa muda mrefu na kupewa shughuli nyingine ili wale wafungwa ambao ndiyo wanapaswa kufanya kazi, kwa sababu tunajua kwamba mahabusu hawaruhusiwi kufanya kazi yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isihakikishe kwamba wale mahabusu ambao ndiyo wengi kuliko wafungwa wanaondoka kwenye Magereza na kupata kazi nyingine za nje, ili sasa Magereza wetu au wafungwa waweze kufanya kazi na waweze kujitosheleza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimuhakikishie kwamba mawazo yake aliyoyatoa ni mawazo ya Serikali, na ndiyo maana katika Bajeti yetu ya mwaka huu tumeongeza kwa kutenga fedha hizo kwa ajili ya specifically kwenye eneo la Umwagiliaji, kwa Magereza kwa Kitengule na Isopilo, kwa hiyo siyo Idete peke yake, kuna Magereza mengine. Hata juzi juzi tu nilikwenda kwenye Gereza la Songwe na niliwasisitiza juu ya umuhimu wa kufikia malengo na tukakubaliana malengo hayo yatafikiwa kwa kuhakikisha kwamba wanatumia utaratibu wa umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hii hoja ya Umwagiliaji ni hoja ambayo ni ya msingi kama ulivyozungumza na sisi kama Serikali kupitia Jeshi la Magereza tumeiona na tunaifanyia kazi. Kuhusu suala la pili, kuhusu mahabusu ni kweli hatufurahishwi na msongamano wa mahabusu katika magereza yetu. Kama ambavyo nimejibu kwa kina wakati nikichangia bajeti hapa kwamba Serikali inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba tunapunguza idadi ya mahabusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini moja katika jambo ambalo ni la msingi ambalo nadhani hili wananchi watusaidie pamoja na wewe Mheshimiwa Mbunge ni kuhakikisha kwamba tunajitahidi kadri inavyowezekana kupunguza kufanya makosa. Tutakapopunguza kufanya makosa basi nadhani hata idadi ya mahabusu na wafungwa itapungua wakati ambapo Serikali inaendelea na jitihada nyingine mbalimbali ikiwemo kuharakisha ksi hizi ziweze kusikilizwa haraka. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi, ugonjwa wa Kansa unakuwa kwa kasi kubwa sana na Hospitali ya Rufaa ya KCMC imekuwa ikihudumia wagonjwa hao lakini tatizo kubwa sana na kilio kikubwa cha watu wa pale KCMC ni banker kwa ajili ya kuweka mashine ya Radiotherapy kwa ajili ya mionzi ya watu wenye matatizo ya kansa. Je, ni lini sasa Serikali itatatua tatizo hilo hasa ikizingatiwa hata katika bajeti ya maendeleo mwaka huu fedha hizo hazijatengwa?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Suzan Lyimo kwa swali lake la nyongeza na kwa kweli amekuwa akifuatilia suala hili la upatikanaji wa bankers kwa ajili ya utoaji wa matibabu ya mionzi, radiotherapy katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC. Ni lini watu wa Kanda ya Ziwa ni mashahidi tunaenda hatua kwa hatua. Tumeanza kuweka huduma za mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bungando na sasa hivi karibia asilimia 95 ya wagonjwa wa Kanda ya Ziwa wanapata huduma za matibabu ya saratani chemotherapy na radiotherapy katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lini tunaenda hatua kwa hatua tunahitaji takribani bilioni 9 na juzi nilikaa na timu yangu nikawaeleza tunaenda vizuri kwa upande wa Hospitali za Rufaa za Kanda na changamoto kubwa ya kanda ya KCMC kwa kweli nakubaliana na wewe ni bankers. Tukiweka bankers tutakuwa tumekamilisha kweli bajeti ya mwaka huu hatujaweka lakini kama unavyofahamu tunapata fedha kutoka vyanzo vingine mwenyewe pia ni mdau wa kanda ya Kaskazini. Kwa hiyo, tutahakikisha, Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kama najipendelea lakini tutahakikisha kwamba tunaweka bankers katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, pamoja na juhudi za Serikali kuhakikisha kwamba wanajenga mabweni, utakubaliana nami kwamba baadhi ya mabweni hayo yamekuwa yakiungua mara kwa mara na hivi karibuni shule ya Ashira mabweni yake mawili ya wasichana yameungua.

Je, Serikali mna utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba kunakuwa na ulinzi katika shule hizo ili hii rasilimali kubwa ambayo imeshatumika ya fedha kujenga mabweni hayo iweze kulindwa?

Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Dada yangu Susan.

Mheshimiwa Spika, ni kweli na niwape pole Wananchi wote wa Tanzania kwa sababu watoto wale, juzi nilikuwepo Ashira ile shule wkeli imeungua lakini ukija kuangalia taarifa ya awali inaonyesha kwamba ni hujuma tu kwa sababu yale mabweni mawili hayaungani na siyo kwamba kulikuwa na short ya umeme.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni kweli inawezekana maeneo mengine kuna hujuma na nawaomba niwaeleze Serikali juzi nilisha-deploy timu yangu ya Mainjinia iko pale tokea jana inafanyakazi na leo hii haraka iwezekanavyo ndani ya wiki mbili, tatu tuanze ukarabati wa yale majengo kwa sababu siyo muda mrefu vijana wa form five wengine tutawaingiza katika maeneo yale. Kwa hiyo, tutafanya ukarabati wa shule ile yote kwa ujumla wake kuhakikisha inarudi Ashira katika hali yake ya kawaida.

Mheshimiwa Spika, lakini hata hivyo ni maelekezo yetu sasa kipaumbele suala zima la walinzi na hasa kuangalia usalama wa shule zetu nini kifanyike kwa sababu tunatumia fedha nyingi sana, haiwezekani watu wenye nia mbaya wakahujumu juhudi hii kubwa ya Serikali na Wananchi wake kwa ujumla.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya Tarime ni matatizo ya nchi nzima. Na utakubaliana nami kutokana na matatizo maabara ndio maana wanafunzi wengi wanapofika kidato cha pili majority wana-opt kwenda masomo ya Arts kutokana na upungufu mkubwa wa maabara lakini vile vile upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri anapojibu hapo anasema kwamba wametenga takribani bilioni 59 mara nyingi fedha hizo tunatambua zinaenda walau nusu. Sasa nilitaka kujua Serikali ina mkakati gani mahususi katika miaka hii inayobakia mpaka tunapoenda kwenye Bunge la mwisho kuhakikisha kwamba wanatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maabara ili wanafunzi wetu wa opit kwenda masomo ya sayansi ili waendane na Tanzania ya viwanda.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, labda nitoe taarfa kwamba hapa tulipo sasa hivi tumepata shilingi bilioni 16.6 na tumeshaomba taarifa labda hili nisema inawezekana kuna tatizo la mawasiliano tukiomba maabara ambazo zimekamilika tunaomba kwa maafisa wetu wa elimu kuhamia mikoa na wilaya. Tumeshapata taarifa mbalimbali za halmashauri zote nchini. Mchakato unaendelea kupeleka vifaa tulitaja juzi hapa kwenye bajeti zaidi ya maabara 2500 nchi hii watapata vifaa vya maabara mpya.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini fedha inayozungumzwa hapa kwenye bajeti hii inazungumzia 2019/ 2020 ndio inayozungumzwa hapa. Lakini tunazingatia maeneo lakini tumeeomba taarifa kama kuna maabara zimekamilika tupate taarifa zao. Lakini kuna halmashauri zinatofautiana kutoka moja kwenda nyingine na tunaanza kama tunapeleka vifaa au wataalamu wa maabara au walimu wa sayansi tunapeleka mahali ambapo kuna changamoto kubwa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukipata taarifa zile labda niwaelekeze Waheshimiwa Wakurugenzi tunapoomba Taarifa kupitia Maafisa Elimu wa Mikoa, Msingi na Sekondari na Walimu, ni lazima wale watoe taarifa lakini pia na Waheshimiwa Wabunge mshirikishwe, maana yake tumepata kweli taarifa hapa hata ya maboma, ikaonekana tunapata taarifa ambazo ni old fashion Mbunge ana taarifa zake, na Mkurugenzi ameleta taarifa hapa zinatofautiana, ndiyo picha. Lakini, tukiomba taarifa ya Elimu au ya Afya au huduma nyingine kwenye halmashauri zetu, basi Wakurugenzi na Makatibu Tawala kabla ya kuleta taarifa kwenye Ofisi Kuu za Serikali wawasiliane na Waheshimiwa Wabunge ili wote tuwe kwenye line moja na tuweze kuzungumza lugha moja. Ahsante. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, wote tunatambua lengo kubwa la vyuo hivi ni pamoja na kuondoa ujinga lakini vilevile kufanya watu waweze kujiajiri wenyewe na lengo kubwa nilikuwa na mimi nashangaa ni kwa sababu gani what is the uniqueness ya hiki chuo mpaka hiki kiwe chini ya Wizara ya TAMISEMI wakati tunajua vyuo vyote vya maendeleo vilikuwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na vyote vikapelekwa Wizara ya Elimu.

Sasa nataka kujua what is uniqueness yaani nini upekee wa chuo hiki kuwa chini ya TAMISEMI wakati tunajua Wizara ya Elimu ndiyo ingeweza zaidi kuhakikisha kwamba vinajengewa labda hata hizi changamoto zisingekuwepo? Nilitaka kujua hilo.
WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, TAMISEMI kwa majibu yake mazuri kuhusiana na swali hili.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Lyimo kama ifuatavyo; ni kweli kwamba vyuo vyote vya maendeleo ya wananchi viko chini ya Wizara yangu na Wizara imekuwa ikivifanyia ukarabati vyote 54 ambavyo viko chini ya Wizara na hapa katika majibu ya msingi Mheshimiwa Naibu Waziri ameelezea historia ya hicho chuo. Lakini historia inaweza ikabadilika, naomba kama Serikali tulipokee hilo wazo tuangalie ni namna gani hiki chuo kinaweza tukakifanyia utaratibu ili kiweze kupata huduma vizuri zaidi kama ambavyo vyuo vingine 54 vinapata huduma. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka pia kujua, kwa kuwa nchi yetu tuna watumishi wa umma na watumishi katika sekta binafsi na siku zote tumekuwa tukihamasisha PPP, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba kama kuna hilo tatizo waajiri wawasiliane na Katibu Mkuu Utumishi.

Je, wale wafanyakazi au watumishi wanawake wenye matatizo hayohayo lakini wanafanya kwenye sekta binafsi, wao watasaidiwaje kwa sababu nchi ni moja? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa niaba ya Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma kwa majibu mazuri aliyoyatoa.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004, kifungu cha 33 kimeweka masharti ya kuhakikisha kwamba huduma bora kwa akina mama wote wajawazito, wanaojifungua na wanaume kwa maana ya waume wa akina mama hao kwenye private sector na wao wanapewa haki sawa na stahili katika kuhakikisha kwamba suala la uzazi linapewa kipaumbele pia kwa watumishi wa sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa wito kwa waajiri wote nchini kuhakikisha wanatekeleza matakwa hayo ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2014 na hivyo kuwafanya wanawake wote wa Tanzania waweze kuthaminiwa katika suala hili muhimu sana la kukuza uhai katika dunia hii. Ahsante.