Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Sophia Hebron Mwakagenda (29 total)

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ni sehemu ya ghala la chakula la Taifa katika mikoa mitano (5) inayolima chakula kwa wingi nchini Tanzania; lakini kikwazo kikubwa ni usafirishaji wa mazao kufikia masoko ya nje ya Wilaya; Halmashauri imeomba ongezeko la bajeti ya barabara kufikia shilingi bilioni 7,969,000 ili kuweza kukarabati barabara zote muhimu na kuwezesha wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi na hatimaye kuongeza kipato cha Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe:-
Je, Serikali ipo tayari kukubali ombi la Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe la kuongeza fedha katika bajeti ya 2016/2017?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe iliandaa makisio ya bajeti ya shilingi bilioni 7.9 kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Hata hivyo, kutokana na ukomo wa bajeti, fedha zilizoidhinishwa ni shilingi milioni 920 ambazo zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara na ujenzi wa madaraja. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, Halmashauri hiyo ilitengewa shilingi milioni 870 na tayari Serikali imepeleka shilingi milioni 157.9.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za Mfuko wa Barabara katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ni shilingi bilioni 247.5 ambazo endapo zingegawanywa sawa kwa kila Halmashauri zote 181 zilizopo, kila Halmashauri ingeweza kupata bajeti ya shilingi bilioni 1.3 tu. Hivyo, mara zote mahitaji yamekuwa ni makubwa kuliko uwezo wa rasilimali fedha kukidhi mahitaji hayo, ndiyo maana tunaweka vipaumbele ili kutekeleza mambo machache kwanza kulingana na uwezo uliopo kibajeti. Serikali itaendelea kuongeza bajeti kwa ajili ya barabara kadri uwezo utakavyowezekana.
MHE. EDWARD F. MWALONGO (K.n.y. MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA) aliuliza:-
Shule ya Sekondari ya Ndembela Wilayani Rungwe awali ilijengwa kwa nguvu za wananchi na baadaye Kanisa la Waadventista Wasabato liliingia kama wabia na kuiendeleza na hatimaye kuiendesha shule hiyo ikiwa na majengo yaliyokamilika. Baada ya wananchi kuihitaji shule yao, Kanisa limekubali kuirejesha kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kwa fidia ya Sh.947,862,000/= Halmashauri imeomba Wizara ya Elimu isaidie kulipa fidia hiyo:-
Je, ni lini Serikali itasaidia kurejesha shule hiyo mikononi mwa wananchi kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, thamani halisi ya majengo ya Shule ya Sekondari Ndembela ni shilingi milioni 762 baada ya tathmini. Mwaka 2013, Kanisa la Waadventista Wasabato na Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe walikubaliana mbele ya Mahakama kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ilipe fidia ya shilingi milioni 762 ikiwa ni thamani halisi ya maendelezo yaliyofanyika ili shule iweze kurejeshwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imeidhinishiwa shilingi milioni 190 kwa ajili ya kulipa sehemu ya deni hilo. Aidha, Halmashauri imewasilisha maombi maalum ya shilingi milioni 947.8 katika Mamlaka ya Elimu Tanzania yaani TEA kwa ajili ya kulipa fidia na ukarabati wa miundombinu ya shule.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA Aliuliza:-
Wakulima wa chai wa Wilaya ya Rungwe wanauza majani ya chai kati ya shilingi 230 hadi 240 kwa kilo, wakati wakulima wa Njombe wanauza majani ya chai kwa shilingi 500 kwa kilo huku kukiwa na Bodi moja na ni nchi moja.
Je, kwa nini wakulima wa chai Wilaya ya Rungwe wanalazimishwa kuuza majani mabichi ya chai kwa bei ndogo kuliko wakulima wa chai wa Wilaya za Njombe na Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, bei dira ya majani mabichi ya chai hupangwa katika mkutano mkuu wa wadau wa chai ambao ni wa kisheria na hufanyika kila mwaka kabla ya msimu kuanza. Kwa mfano, mkutano wa wadau wa msimu 2016/2017 uliofanyika Njombe wadau walikubaliana bei dira
kuwa shilingi 230. Hata hivyo, kulingana na kifungu cha 49(2) katika kanuni za zao la chai za mwaka 2010, wakulima kupitia vyama vyao wamepewa uwezo wa kujadiliana bei na wenye viwanda ambayo itakuwa zaidi ya bei dira. Kutokana na makubaliano na wakulima Kampuni ya Chai ya Mufindi wanaomiliki viwanda vya Kibena, Luponde, Ikanga na Itona waliwalipa wakulima shilingi 250.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bei dira hupangwa na kukubaliwa na wadau wote, tofauti ya bei kati ya eneo moja na lingine hutokana na majadiliano kati ya wakulima na wenye viwanda kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za zao la chai. Majadiliano hayo ndiyo yaliyopelekea wakulima wa Wilaya za Mufindi na Njombe kulipwa shilingi 250 kwa kilo wakati wale wa Lushoto, Muheza, Korogwe na Kagera wanalipwa shilingi 230 ambayo ni bei elekezi. Kwa upande wa Wilaya ya Rungwe, bei ni kati ya shilingi 240 na 250 ambayo ni juu ya bei elekezi. Tofauti ya bei kwa maeneo hayo inatokana na malipo ya pili, kwa mfano katika mwaka 2015/2016 Kampuni ya Unilever inayomiliki viwanda vya Kibwele, Kilima na Lugoda, imelipa malipo ya pili kati ya shilingi 80 hadi 200 kwa kilo kutegemeana na ubora wa majani ya chai na hivyo kufanya malipo ya jumla kuwa kati ya shilingi 330hadi 400.
Mheshimiwa Spika, kiwanda cha Wakulima Tea Company cha Rungwe hulipa malipo ya kwanza shilingi 240 na ya pili shilingi 29 na kufanya jumla kuwa shilingi 259. Katika mwaka 2016/2017 Kiwanda cha Kibwele kinachomilikiwa na Unilever kinatoa malipo ya pili ya shilingi tatu na jumla kuwa shilingi 253 na Viwanda vya Kilima na Lugoda malipo yatakuwa kati ya shilingi 100 na 200 ingawa vinamilikiwa na kampuni hiyo hiyo. Kiwanda cha Dindira kilichopo Lushoto malipo ya kwanza yatakuwa shilingi 230 na ya pili shilingi saba na jumla kuwa shilingi 237.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya Kampuni ya Highland Estate Mbarali na wananchi wanaolizunguka shamba hilo kwa kuwa mwekezaji amekuwa akipora ardhi kwa wananchi na kusababisha uvunjifu wa amani kwa muda mrefu sasa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, shamba linalomilikiwa na Kampuni ya Highland Estate awali lilikuwa likimilikiwa na Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula kuanzia mwaka 1978. Baada ya upimaji kukamilika 1981, shamba hilo liliendelea kumilikuwa na NAFCO kwa Hati Na. 327–DLR. Tarehe 18 Agosti, 2008 shamba hili liliuzwa na Serikali kwa Kampuni ya Highland Estate Ltd.
Mheshimiwa Spika, mgogoro wa shamba la Highland Estate unahusu tafsiri ya mipaka baina ya shamba hilo na vijiji vya Mwanavala, Ibumila, Imalilo, Songwe, Urunda, Ubaruku, Utyego, Mbarali, Mpakani, Mkombwe, Mwakaganga, Ibohola na Nyelegete.
Mheshimiwa Spika, hatua za awali za utatuzi wa mgogoro huu zinahitaji kupata tafsiri sahihi ya mpaka wa shamba kulingana na ramani ya upimaji iliyoidhinishwa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na vijiji vinavyozunguka shamba hilo. Zoezi la kutafsiri mipaka baina ya shamba na vijiji husika limeshaanza kufanyiwa kazi na wataalam wa Ofisi ya Mkuu wa wa Mkoa wa Mbeya, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbarali pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kwa kushirikiana na wanakijiji husika isipokuwa wanakijiji wa kijiji cha Nyelegete ambao wamesusia zoezi hili.
Mheshimiwa Spika, juhudi za kutatua mgogoro huu bado zinaendelea kufanywa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kwa kuwahimiza kijiji cha Nyalegete kutoa ushirikiano kwenye utatuzi wa mgogoro huu ili uweze kumalizika.
Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kutoa ushirikiano kwa wataalam wa sekta ya ardhi katika maeneo yao ili kuharakisha utatuzi wa migogoro ya ardhi hususan inayohusiana na mipaka ya mashamba. Aidha, napongeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa utaratibu wake wa kusikiliza kero za wananchi ikiwemo kutatua migogoro ya ardhi mara mbili kwa kila mwezi.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-
(a) Ranchi ya NARCO Mbarali ilianzishwa kwa ajili ya mifugo; Je, ni kwa nini eneo hilo sasa linatumika kwa kilimo?
(b) Migogoro ya wakulima na wafugaji Mbarali imekuwa ni mingi; je, kwa nini Serikali isitoe eneo la Ranchi ya NARCO Mbarali ili litumike kwa ajili ya malisho ya mifugo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Ranchi ya NARCO iliyopo Mbarali inajulikana kwa jina la Ranchi ya Usangu na ina ukubwa wa hekta 43,727 ambazo zimegawanywa katika vitalu 16 vyenye ukubwa wa hekta kati ya 2,000 na 3,000. Kutokana na maelekezo ya Wakala wa Baraza la Mawaziri Namba (2) wa mwaka 2002, vitalu vya Ranchi ya Usangu vimekodishwa kwa mkataba maalum kwa wawekezaji wa Kitanzania kwa ajili ya kuendeleza ufugaji wa kisasa na kibiashara ili kuwa na ufugaji wenye tija. Kwa sasa vitalu vya wawekezaji hao vina jumla ya ng’ombe 2,722, mbuzi 1,145 na kondoo 500.
Mheshimiwa Spika, shughuli za uendelezaji mifugo zinaendana na kilimo cha malisho ya mifugo na mazao mengine ambayo mabaki yake hutumika kwa kulishia mifugo. Shughuli za uendeshaji wa nyanda za malisho ni kipengele muhimu kulingana na mkataba wa uwekezaji. Aidha, unenepeshaji wa mifugo hufanyika ndani ya vitalu vya wawekezaji ili kuvuna mifugo kwa muda mfupi na hivyo mabaki ya mazao hutumika kulisha mifugo kama sileji na hei.
Serikali kupitia NARCO inafanya tathmini ya vitalu hivyo na wale watakaobainika kukiuka makubaliano, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuvunja mikataba ya ukodishaji ili kuwapatia wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuwekeza kulingana na mikataba.
(b) Mheshimiwa Spika, kutokana na mkataba wa uwekezaji, Ranchi hiyo haiwezi kugawiwa kwa wananchi, kwa kuwa kuruhusu maeneo ya Ranchi kutumiwa na mifugo kwa ajili ya malisho itakuwa ni ukiukwaji wa sheria ya mkataba kati ya wawekezaji na NARCO. Aidha, kuruhusu uingizaji wa mifugo ndani ya Ranchi kutasababisha maambukizi ya magonjwa kwa mifugo ya wawekezaji.
MHE. AIDA J. KHENAN (k.n.y MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA) aliuliza
(a) Je, kuna sheria yoyote ya nchi inayomruhusu askari polisi kumkatamata mtuhumiwa, kumpiga na kumtesa kabla hajajua kosa lake na kabla ya kufikishwa katika Kituo cha Polisi?
(b) Je, Serikali inachukua hatua zipi za kuhakikisha kuwa askari wanaofanya vitendo kama hivyo wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi?
(c) Je, mpaka sasa ni askari wangapi wameshachukuliwa hatua za kisheria kutokana na makosa ya kujichukulia hatua mkononi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum lenye shemu (a),(b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 kifungu cha 11 kinaeleza namna ya ukamataji. Aidha, kifungu hiki mahsusi cha ukamataji hakimruhusu askari kumpiga na kumtesa raia wakati wowote anapokuwa kizuizini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Utendaji wa Jeshi la Polisi (PGO) askari yoyote anapobainika kufanya vitendo vya kupiga au kutesa raia huchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi na au hata kufikishwa mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha januari mpaka Desemba, 2017 jumla ya askari 105 waliotenda makosa mbalimbali walichukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-
Je, ni lini ujenzi unaoendelea katika Vituo vya Afya Ikuti, Wilayani Rungwe na Ipinda Wilayani Kyela utakamilika ili kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kupata huduma kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Ikuti kimekarabatiwa katika awamu ya kwanza ya ukarabati wa vituo vya afya 44 ulioanza tarehe 10 Oktoba, 2017 na kukamilika tarehe 31 Januari, 2018 kwa gharama ya shilingi milioni 500 ili kuongeza huduma za upasuaji wa dharura kwa mama wajawazito. Aidha, shilingi milioni 220 zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba vya upasuaji na samani. Kituo hicho kinaendelea kutoa huduma zote za matibabu isipokuwa huduma za upasuaji wa dharura. Ujenzi wa majengo ya Kituo cha Afya Ikuti umekamilika na kinachosubiriwa kwa sasa ni vifaatiba kutoka Bohari ya Dawa (MSD).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kituo cha afya cha Ipinda ulianza Oktoba, 2017 katika ujenzi huu jumla ya majengo mapya nane yamejengwa pamoja na ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje, uwekaji wa miundombinu ya maji safi na majitaka, kichomea taka na ujenzi wa njia zinazounganisha majengo (walk way). Jumla ya shilingi 625,899,806 zimetumika mpaka sasa katika mchanganuo ufuatao; Serikali Kuu shilingi 500,000,000, Halmashauri pamoja na wadau shilingi 90,100,975.40 na wananchi 35,798,830.60.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majengo hayo, Halmashauri ya Wilaya ya Kyela imepokea vifaatiba kutoka MSD vyenye thamani ya jumla ya shilingi 73,909,900 na vilivyosalia vinatarajiwa kupatikana mnamo mwezi huu wa nne. Vilevile Halmashauri imenunua vitanda 47, magodoro na mashuka vyenye thamani ya shilingi 27,066,500 ambavyo vimefungwa na vinatumika katika majengo hayo. Kituo cha Afya Ipinda kinaendelea na ujenzi wa miundombinu kwa gharama ya shilingi milioni 500 ambao unahusisha kupanua huduma za upasuaji wa dharura na shilingi milioni 220 zimetolewa kwa ajili ya vifaatiba vya upasuaji na samani. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-
Wakati ujenzi wa barabara muhimu ya Ipinda – Matema ukiendelea.
Je, ni lini wananchi, taasisi kama makanisa na ofisi za vijiji katika vijiji vya Matema, Katusyo, Mababu, Ngyekye, Katela na Ngeleka ambao hawajabomoa majengo yao kwa sababu hawajafidiwa fidia zao ambayo kimsingi ni haki yao na kupisha ujenzi unaoendelea wa barabara hii muhimu sana katika maendeleo na uchumi wa Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya zitalipwa fidia hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Kikusya – Ipinda – Matema yenye urefu wa kilometa 39.2 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ambapo ujenzi kwa kiwango cha lami unatekelezwa kwa sehemu ya Tenende hadi Matema (kilometa 34.7).
Mheshimiwa Spika, wakati wa utekelezaji wa mradi huu na kwa kuzingatia Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009, uthamini wa mali za wananchi na taasisi zilizoathiriwa na ujenzi wa barabara hii ulifanywa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa uthamini huo ambao ulifanywa na Mthamini kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, malipo yalifanyika kwa waliostahili tarehe 17 Septemba, 2017 katika vijiji vya Masebe, Mpunguti, Mpanga, Ipinda, Ngamanga, Bwato, Mpegele, Ngeleka, Katela, Mababu, Kilombero, Kisyosyo na Matema. Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ipinda walifungua mashtaka Mahakamani dhidi ya Serikali na hadi sasa hawajaondoa mali zao zilizo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya mchepuo ya Mlima Nyoka - Songwe yenye urefu wa kilometa 48.9 utaanza baada ya ya usanifu na upembuzi yakinifu kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa barababa ya mchepuo inayoanzia Uyole yaani Mlima Nyoka hadi Songwe kilomita 48.9 ni mahsusi kwa ajili ya kupunguza msongamano wa magari katika barabara kuu ya TANZAM katika Jiji la Mbeya.

Mheshimiwa Spika, upembuzi na usanifu wa kina wa barabara hii ulikamilika chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Hata hivyo, ilionekana kuwa ipo haja ya kufanya mapitio ya usanifu huo ambao katika mwaka wa fedha 2018/ 2019 kiasi cha shilingi milioni 2.6 kimetengwakwa ajili kupitia na kukamilisha usanifu huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi huu umeingizwa kwenye mradi wa ukarabati wa barabara kuu ya TANZAM kuanzia Igawa hadi Tunduma unaofandhiliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba ulisainiwa tarehe 18 Disemba, 2018 kati ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Mhandisi Mshauri Studio International ya Tunisia ikishirikiana na Global Professional Engineering Service ya Tanzania kwa ajili ya kazi ya mapitio ya usanifu wa kina wa barabara hii. Kazi hii inatarajiwa kukamilika tarehe 18 Februari, 2020. Hadi sasa Mhandisi Mshauri yupo eneo la mradi anaendelea na kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii itakapokamilika na Serikali kupata fedha, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami utaanza.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Kwa mujibu wa GN. No. 222 na 223 ya mwaka 1972 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2002, Wazee wa Mabaraza ya Mahakama wanateuliwa na vikao vya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Kamati za Maadili za Mahakimu zipo chini ya Uenyekiti wa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya:-

Je, ni lini Mahakama itaacha kuingiliwa na siasa?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Tanzania ni moja ya mihimili mitatu ya dola ambayo kwa mujibu wa Ibara ya 4 na 107(B) ya Katiba, Mahakama ni Mhimili huru na hauingiliwi na chombo chochote katika utekelezaji wa majukumu yake ya utoaji haki.

Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa majukumu yake, Mahakama imekuwa ikiwatumia Wazee wa Baraza katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo na Mahakama Kuu ambao hupatikana kwa mujibu wa Kanuni za Wazee wa Baraza katika Mahakama za Mwanzo
G.N. No. 222/223 za Mwaka 1972, ambao huteuliwa kulingana na sifa za umri na uzoefu walionao katika masuala mbalimbali hasa ya kijamii katika eneo husika.

Aidha, Wazee wa Baraza huwa na jukumu moja la kuishauri Mahakama na ushauri wao hauifungi Mahakama katika kutoa uamuzi inaouona unafaa. Hata hivyo, Wizara yangu imeanza mchakato wa kuboresha sekta ndogo ya mfumo wa haki, jinsia nchini ambao pamoja na mambo mengine inapitia Sheria za Kamati zote ambazo zimetungwa miaka mingi iliyopita ili ziendane na wakati.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya, Sheria ya Usimamizi wa Mahakama ya Mwaka 2011, imebainisha majukumu ya Kamati hizi kwa mujibu wa vifungu vya 50 na 51. Lengo la Kamati hii ni kushughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya utendaji wa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Mahakimu Wakazi katika kutimiza shabaha na kulingana na kusawazishana (checks and balances) katika utendaji wa Mihimili ya dola. Kamati hizi haziingilii uhuru wa Mahakama ambayo inatekeleza majukumu yake ya utoaji haki ambao unatajwa kwa mujibu wa Ibara ya 107 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, ninapenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, nchi yetu itaendelea kuheshimu misingi ya mgao wa madaraka baina ya mihimili ya Dola na kamwe Mahakama haiwezi na haiingiliwi na chombo kingine cha Dola katika utekelezaji wa majukumu yake.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Michezo mingi ikiwemo mpira wa miguu inapata ufadhili sana hapa nchini kupitia kampuni mbalimbali binafsi na za Kiserikali:-

Je, ni lini Serikali itahakikisha ufadhili unapatikana kwenye michezo inayohusu wanawake hususan michezo ya ngumi kwa wanawake?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nisahihishe dhana ya kwamba michezo inayowahusisha wanaume inapata “ufadhili sana” nikinukuu maneno aliyotumia Mheshimiwa Mbunge, kuliko inayowahusisha wanawake. Mfano hai ni Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu upande wa Wanaume kwa msimu wa 2018/2019 ambayo ilikosa udhamini na kusababisha matatizo makubwa ya maandalizi na usafiri kwa timu zote 20 zilizoshiriki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufadhili haushinikizwi na Serikali bali ni suala la hiari upande wa wafadhili ambao huchukua hatua hiyo wakishaziona fursa za kibiashara na kijamii upande wao. Wajibu wa Serikali ni kujenga mazingira rafiki ya ufadhili huo bila kujali jinsia. Hivi sasa Tanzania ina Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu kwa Wanawake ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Vinywaji ya Serengeti Breweries kupitia bia yake ya Serengeti Lite.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa riadha, Kampuni ya Multichoice imekuwa mstari wa mbele kudhamini wanariadha bora wanaojitokeza na kuandaa makambi ya mazoezi bila ubaguzi wa jinsia. Kampuni ya SportPesa pekee imejitokeza kumfadhili Mwanamasumbwi Mwakinyo aliyekuwa namba 174 kwa ubora Duniani katika uzito wake, baada ya kumtwanga Eggington wa Uingereza, wakati huo namba akiwa 8 kwa ubora duniani. Hakuna kigezo kingine kilichotumika na SportPesa kumfadhili Mwakinyo zaidi ya weledi aliouonesha katika mchezo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwaomba wadau wote wa michezo nchini wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, kusaidia kushawishi makampuni, taasisi na wadau wenye uwezo kifedha, kudhamini na kufadhili maendeleo ya michezo yote nchini ukiwemo mchezo wa ndondi upande wa wanawake.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018 Serikali iliondoa kodi kwenye taulo za kike (pads) jambo ambalo ni muhimu sana kwa maisha ya Wanawake na Wasichana mpaka sasa ni mwaka mmoja tangu kodi hizo ziondolewe lakini bei ya taulo za kike haijashuka licha ya kuondolewa kwa kodi hizo Nchi nzima.

Je, ni lini Serikali itasimamia kwa ukamilifu suala hilo ili bei za taulo za kike zishuke na kusaidia afya za Wanawake hususani Wasichana?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hatua ya kuondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye taulo za kike ililenga kupunguza sehemu ya gharama za uzalishaji wa bidhaa hiyo na mojawapo ya athari chanya iliyotegemewa ni kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo. Pamoja na Serikali kuchukua hatua ya kuondoa kodi imebainika kuwa hakuna mabadiliko ya bei ya bidhaa hiyo katika soko. Hii inatokana na ukweli kuwa, bei ya bidhaa katika soko inaamuliwa na nguvu ya soko pamoja na gharama nyingine za uzalishaji na uendeshaji kama vile gharama za malighafi, mishahara, uwekezaji, mifumo ya uzalishaji, teknolojia, ushindani katika soko, umeme, maji na majitaka, usambazaji, ubora wa bidhaa n.k. Hivyo basi kutokushuka kwa bei ya taulo za kike kunabainisha kwamba kodi inachangia sehemu ndogo sana katika kupanga bei ya bidhaa kama ambavyo Serikali imekuwa ikisisitiza na kutoa ufafanuzi mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa mfumo wetu wa uchumi ni mfumo wa soko huria, bei ya bidhaa huamuliwa na nguvu ya soko yaani ugavi na mahitaji ya soko. Fursa pekee iliyopo ni kuhamasisha uwekezaji mkubwa kwa kutumia teknolojia yenye gharama nafuu katika kutengeneza taulo za kike, kupunguza gharama nyingine sambamba na kuchochea ushindani wa bei katika soko na sio Serikali kuondoa kodi na kupanga bei ya bidhaa.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Katika kujenga Tanzania ya viwanda, Serikali imekuwa na mikakati ya muda mrefu.

Je, ule mkakati wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI wa kujenga viwanda 100 kwa kila Mkoa ni sehemu ya mkakati na umeainishwa kwenye waraka gani wa Serikali ili kuwapa wananchi rejea ya pamoja ya kitaifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa kujenga viuwanda 100 kila MKoa ni sehemu ya mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano kujenga uchumi wa viwanda uliofungamanishwa na maendeleo ya watu. Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeandaa mwongozo kubainisha majukumu Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika utekelezaji wa Sera ya viwanda. Lengo la mkakati huo ni kutoa hamasa kwa viongozi na wananchi kushiriki kikamilifu kuwezesha uwepo wa viwanda katika maeneo yao hivyo mkakati huo haupaswi kutenganishwa na mipango mingine ya Serikali inayohamasisha ujenzi wa viwanda nchini. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA Aliuliza:-

Serikali imezuia kampuni binafsi kununua kokoa katika Wilaya za Kyela na Rungwe kwa msimu huu na Vyama vya Ushirika havina uwezo wa kununua kokoa hizo kwa wananchi:-

Je, ni lini Serikali itaruhusu tena kampuni binafsi kuendelea kununua kokoa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijazuia kampuni binafsi kununua kokoa kwa wakulima bali imezuia mfumo wa ununuzi wa ulanguzi maarufu kama “njemke” ambao umekua ukimlalia mkulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia mfumo wa Vyama vya Ushirika imekuwa ikikusanya na kuuza mazao hayo kupitia minada ya wazi katika kusaidia kutambua bei za mazao hayo (price discovery). Kwa kutumia utaratibu wa ushirika wakulima waliouza kokoa kwa mfumo wa stakadhi za ghalani bei ya kokoa ilipanda kutoka Sh.3,000 mpaka kufika kiasi cha Sh.5,000 katika msimu wa 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mfumo huo wakulima hupeleka kokoa katika Vyama vya Msingi na kupata asilimia 60 ya bei ya soko. Baada ya mnada kufanyika hupewa kiasi kilichobaki ili kufikia bei ya mnada kwa kuzingatia gharama za usafiri, uhifadhi, ushirika na ushuru. Bei hii iko juu ukilinganisha na bei ya ununuzi binafsi kabla ya ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia faida inayopatikana kupitia kuuza mazao katika ushirika, Serikali haitoruhusu makampuni binafsi kununua kokoa kwa wakulima kwa kununua kuyafuata shambani. Aidha, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaendelea kuimarisha na kujenga uwezo wa Vyama vya Msingi ili viweze kukusanya, kununua kokoa yote kwa wakulima na kuwasaidia wakulima kupata pembejeo sambamba na kuwa na nguvu ya pamoja katika kusimamia bei.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka wakaguzi ili kuhakiki thamani ya fedha ya Shilingi bilioni 15 zilizotolewa na Serikali kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kwa ajili ya mradi wa maji wa Masukulu ambao unaonekana kujengwa chini ya kiwango?
NAIBU WAZIRI MAJI: Mheshimiwa Spika; kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda Mbunge wa Rungwe Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika; ni kweli Serikali kupitia Wizara ya Maji ilitekeleza mradi wa Maji wa Masukulu katika Wilaya ya Rungwe ambao ulitenga kuhudumia vijiji viwili vya Ijigha na Masukulu kwa gharama ya Shilingi milioni 335.6 na si shilingi bilioni 15 kama ilivyoelezwa na Mheshimiwa Mbunge. Mradi huo ulihusisha ujenzi wa chanzo, tanki lenye ujazo wa lita 90,000 na vituo 13 vya kuchotea maji vimekamilika na vinatoa huduma kwa wananchi wapatao 3,706.

Mheshimiwa Spika; katika kuhakikisha vijiji vya Ijigha na Masukulu vinapata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza; RUWASA Wilaya ya Rungwe inatumia chanzo cha maji cha Mto Mbaka ambacho kina cha maji kinatoa maji ya uhakika na tayari mradi huo umewekwa kwenye mpango wa bajeti ya RUWASA ya mwaka 2021/2022.
MHE. SOPHIA H. MWAKANGENDA aliuliza:-

Je, ni kwa nini wananchi wa Wilaya ya Rungwe wanalazimishwa kuuza chai na maziwa kwa mnunuzi mmoja hali inayosababisha mnunuzi kupanga bei kitu ambacho ni kinyume na Sera ya Ushindani wa Biashara?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Ushindani ya Mwaka 2003, uwepo wa mnunuzi mmoja katika soko siyo kosa, kosa ni endapo mnunuzi huyo atatumia nguvu ya hodhi ya soko aliyonayo katika kufupisha ushindani kwa kuzuia washindani wengine waliopo sokoni kufanya biashara. Kufifisha ushindani kwa kuwaondoa washindani wengine waliopo sokoni na kufifisha ushindani kwa kuzuia makampuni au watu wengine kuingia kwenye soko husika.

Mheshimiwa Spika, iwapo itathibitika kuwa kuna kosa la kupanga bei ya huduma au bidhaa Tume ya Ushindani kwa maana ya FCC kuchukua hatua kwa kutumia Kifungu Namba 9 cha Sheria ya Ushindani. Kwa mujibu wa Kifungu hiki ili kosa husika lifanyike ni lazima kuwe na washindani katika soko, ambapo washindani hawa hukutana na kupanga bei ya bidhaa au huduma wanayotoa au kupanga kiasi cha kuzalisha au kugoma kusambaza bidhaa na huduma husika au kupanga zabuni.

Mheshimiwa Spika, hivyo Wizara kupitia FCC inafanya uchunguzi wa suala hili ili kubaini uwezekano wa kuwepo kwa uvunjifu wa Sheria ya Ushindani. Katika hatua za awali za uchunguzi FCC imeshawasiliana na Bodi ya Chai Tanzania, Bodi ya Maziwa Tanzania na Ofisi ya Katibu Tawala, Mkoa wa Mbeya ili kupata taarifa muhimu kwa ajili ya kujiridhisha kuhusu changamoto hii katika soko la chai na maziwa Wilayani Rungwe. Ikiwa itabainika kuwa kuna uvunjifu wa sheria ya ushindani, hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya wahusika.

Mheshimiwa Spika, nipende kutumia fursa hii kuwajulisha wafanyabiashara wote nchini kuzingatia sheria zilizowekwa ili kuwa na ushindani wa haki katika soko.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Je, ni lini barabara ya Kiloba – Njugilo yenye urefu wa kilometa 7 itajengwa ili kurahisisha mawasiliano ya wananchi na wanafunzi wanaokwenda Kata ya Masukulu – Rungwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge Viti Maalum, kama Ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kiloba-Njugilo ni barabara inayounganisha Kata mbili za Bujela na Masukulu. Kwa kutambua umuhimu wake, barabara ya Kiloba-Njugilo ipo kwenye hatua za uhakiki ili iweze kuingizwa kwenye Mfumo wa Barabara za Wilaya kwa maana ya DROMAS ili iweze kupatiwa fedha za Mfuko wa Barabara kwa ajili ya matengenezo na ujenzi. Utaratibu wa kuingizwa kwenye mfumo wa barabara za Wilaya ukikamilika barabara hiyo itatengewa fedha kupitia fedha za Mfuko wa Barabara kwa maana ya Road Fund ili iweze kujengwa walau kwa kiwango cha changarawe na kuiwezesha kupitika katika majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imejenga Daraja la Kigange linalounganisha Vijiji vya Kiloba na Mwalisi kwa gharama ya shilingi milioni 46.8.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA Aliuliza: -

Je, ni lini mgodi wa makaa ya mawe Kiwira utapata Mwekezaji mpya na kulipa mafao ya waliokuwa wafanyakazi wa mgodi huo?
WAZIRI WA MADINI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Shirika limeamua kuchukua hatua za ndani za kuendesha mgodi wa Kiwira kwa kuchukua hatua mahsusi za kuendeleza mradi wa Kiwira kwa ajili ya uwekezaji mkubwa wa kuzalisha umeme wa MW 200 badala ya kutafuta mwekezaji mpya. Hatua hizo ni pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu ya mgodi, kuboresha barabara, kurejesha njia za reli katika mgodi wa chini (underground mine), mifumo ya hewa, maji na matengenezo ya mikanda ya kusafirishia makaa kuja nje ya mgodi.

Mheshimiwa Spika, hatua hii ni kuwezesha kuchimba makaa ya mawe kwa wingi kwa ajili ya kuzalisha umeme na matumizi mengine. Ukarabati wa miundombinu ya mgodi huu umefikia asilimia 98. Aidha, hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ni kuanzisha ushirikiano kati ya STAMICO na TANESCO. Katika ushirikiano huo, STAMICO itahusika na uzalishaji wa makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi kwenye kinu cha umeme (power plant) na TANESCO itahusika na ujenzi wa kinu cha kuzalisha umeme pamoja na miundombinu yake. Kadhalika, TANESCO watahusika na uzalishaji na usambazaji wa umeme kwa wananchi kwa kujenga njia ya umeme yenye urefu wa km 100 kutoka kwenye mgodi huo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa mgodi unaendelea na uchimbaji wa makaa ya mawe kwa matumizi ya viwanda katika eneo la Kabulo. Makaa hayo yanauzwa kwenye viwanda mbalimbali vya saruji nchini.

Mheshimiwa Spika, kuhusu malipo ya mafao ya waliokuwa wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira, Wizara ya Fedha na Mipango inayafanyia kazi kufuatia kukamilika kwa uhakiki wa madai hayo ambayo yanahusisha stahiki na mapunjo ya watumishi waliokuwa wafanyakazi wa Mgodi wa Kiwira baada ya Mgodi huo kusimamisha uzalishaji wake mwaka 2007. Aidha, katika kipindi hicho mgodi ulikuwa unaendeshwa na kampuni binafsi ya TANPOWER na mwaka 2013 mgodi huo ulikabidhiwa Serikalini kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Wapimaji wa Ardhi katika Mji wa Tukuyu Wilayani Rungwe ili kupunguza migogoro ya ardhi?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ina watalaam wa sekta ya ardhi ambao ni Maafisa Ardhi, Mpima Ardhi na Afisa Ramani ambao wanaendelea na utaratibu wa shughuli za ardhi katika Halmashauri hiyo ikiwemo kushughulikia mgogoro wa ardhi. Aidha, Mkoa wa Mbeya una timu ya wapima ardhi ambayo kukiwa na uhitaji wa kupima eneo katika Halmashauri za Mkoa wa Mbeya timu hiyo hushiriki katika kazi za kupima katika maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Mbeya itapeleka timu ya wataalam wa ardhi katika Wilaya ya Rungwe tarehe 26 Septemba, 2022 ili kushughulikia kero na mgogoro wa ardhi.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya kilimo kuwa kipaumbele cha kwanza cha Taifa kwa kupunguza bei ya mbolea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya kupanda kwa bei ya mbolea katika msimu wa mwaka 2020/2021. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, msimu wa mwaka 2022/2023 Serikali inatekeleza mpango wa utoaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima ili kuwaongezea uwezo wa kununua na kutumia mbolea. Hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2023 jumla ya tani 246,714 za mbolea zimenunuliwa na wakulima kwa bei ya ruzuku ikilinganishwa na tani 173,957 za mbolea ambazo zilinunuliwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Januari, 2021.
MHE. AIDA J. KHENANI K.n.y. MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaongeza fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa REA III katika Wilaya za Busokelo na Rungwe?
WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Mradi wa REA awamu ya tatu (REA III) awamu ya kwanza jumla ya Vijiji 47 vimepatiwa umeme katika Halmashauri ya Busokelo, na Vijiji 22 katika Halmashauri ya Rungwe. Aidha, katika utekelezaji wa Mradi wa REA III round two, Vijiji vyote 32 vilivyobaki bila umeme katika Halmashauri ya Rungwe na Kijiji kimoja kilichobaki bila umeme katika Halmashauri ya Busokelo vitapatiwa umeme.

Mheshimiwa Spika, Mkandarasi M/S Electrical Transmission and Distribution Construction and Maintenance Co. LTD aliyepewa kazi ya kutekeleza mradi katika Mkoa wa Mbeya anaendelea na kazi katika maeneo ya Vijiji vya Busokelo na Rungwe ambapo wateja wa awali 594 wataunganishwa kwa huduma ya umeme.

Mheshimiwa Spika, gharama ya mradi ni Shilingi Bilioni 5.133. Serikali itaendelea kuongeza fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kufikisha umeme katika maeneo yote ya vitongoji vya Halmashauri za Busokelo na Rungwe kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itabadili majina ya kigeni kuwa ya Kitanzania kwenye rasilimali za Taifa ikiwemo Mlima Livingstone na Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo baadhi ya Rasilimali za Taifa zenye majina na maeneo ambayo zilipewa tangu kipindi cha utawala wa ukoloni. Majina hayo yalitolewa kutokana na juhudi za waasisi katika ulinzi na uhifadhi wa rasilimali hizo. Majina na maeneo hayo yameendelea kufahamika kihistoria kutokana na kutangazwa na Taifa na kuandikwa kwenye nyaraka na vitabu mbalimbali na rasilimali hizo zimeendelea kuhifadhi historia ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa rasilimali hizo kwa historia ya nchi yetu na kuendelea kufahamika zaidi kitaifa na kimaitafa pasipokuwa na changamoto yoyote, Serikali haioni haja ya kubadili majina na maeneo hayo ambayo kwa sasa yana mchango mkubwa kiuchumi kwa Taifa letu. Aidha, Serikali kwa sasa inaendelea pia kuzingatia majina ya wazawa kwenye rasilimali mbalimbali za Taifa kadiri zinavyoanzishwa.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itahakikisha Watanzania wanaofanya kazi kwenye Kampuni za Kichina wanalipwa vizuri kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninaomba kujibu swali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria za Kazi ili kulinda haki za wafanyakazi. Aidha, katika kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa sekta binafsi, Serikali kupitia Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara cha Sekta Binafsi imefanya utafiti na kuboresha kima cha chini cha mishahara ya sekta binafsi, viwango hivyo vipya vya mishahara vilitangazwa kupitia Gazeti la Serikali Namba 687 la tarehe 25 Novemba, 2022 na utekelezaji wake umeanza rasmi tarehe 01 Januari, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazohusika na masuala ya kazi itaendelea kuhakikisha kuwa waajiri wanatekeleza ipasavyo viwango vya mishahara vilivyotangazwa kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara katika maeneo ya kazi na kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi ili uelewa wao katika kutekeleza Sheria za Kazi unafanyika. Aidha, ofisi imeendelea kuchukua hatua dhidi ya waajiri wanaobainika kukiuka Sheria za Kazi hususan ulipaji wa mishahara kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Aliuliza: -

Je, kwa nini kumekuwa na ugumu wa upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi waliosoma shule binafsi wanapojiunga na elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda kama ifuatavyo: -

Mheshimwa Spika, mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inawalenga vijana wenye sifa za kitaaluma za kujiunga na taasisi za elimu ya juu lakini hawana uwezo wa kumudu gharama za elimu.

Mheshimwa Spika, aidha, upangaji na utoaji mikopo unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo Sura 178 kwa kuzingatia sifa za msingi ambazo ni: awe Mtanzania; awe amepata udahili wa masomo ya shahada au stashahada katika taasisi inayotambuliwa na Serikali; asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake; na kwa wanaoendelea na masomo ya mwaka wa pili, watatu na kuendelea, wawe wamefaulu kuendelea na masomo yao katika mwaka unaofuata.

Mheshimwa Spika, Kila mwaka bodi huandaa mwongozo unaopaswa kuzingatiwa na waombaji na kuweka masharti ya utoaji mikopo kwa mwaka husika. Pamoja na vigezo vilivyotajwa, mwongozo hueleza taratibu za kufuata wakati wa kuomba mkopo pasipo kuangalia mwanafunzi kasoma shule ya binafsi au ya umma.

Mheshimiwa Spika, iwapo muomboji atafuata maelezo yote kama yalivyo katika mwongozo wa mwaka husika na akawa ana vigezo vyote, hatutegemei pawepo na ugumu wowote katika kupata mkopo hata kama alisoma shule binafsi. Nashukuru.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Je, kwa nini Serikali inaajiri kwa kigezo cha mwaka wa kumaliza chuo na kupitia mafunzo ya jeshi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kutoa ajira kwa kada mbalimbali zinazohitajika katika Utumishi wa Umma, Serikali imekuwa ikizingatia Sera ya Menejimenti ya Ajira na Utumishi wa Umma Toleo la 2 la mwaka 2008 aya ya 4.2 ambayo inataka zoezi la ajira katika Utumishi wa Umma liendeshwe kwa wazi na ushindani ili kuwezesha Serikali kupata watumishi wenye utaalam na sifa stahiki kwa kuzingatia uwezo, weledi na umahiri wa waombaji fursa za ajira.

Mheshimiwa Spika, ili kuleta ushindani katika soko la ajira, vigezo mbalimbali hutumika kuzingatia mazingira maalum au mazingira mahsusi ya waajiri. Katika vyombo vya Ulinzi na Usalama na Taasisi zilizoingia katika mfumo wa Jeshi USU kutokana masharti ya kazi hizo na mahitaji maalum au mahsusi ya vyombo husika, ajira zinazotolewa kwa kigezo cha ukomo wa umri na kigezo cha kupitia Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, kada nyingine katika Taasisi za Umma nje ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Taasisi zenye mfumo wa Jeshi USU kigezo cha Kupitia Mafunzo ya Jeshi hakitumiki. Hata hivyo, waombaji wa fursa za Ajira Serikalini kwa masharti ya kudumu Serikali wanatakiwa kuzingatia Kanuni ya D. 39 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 ambayo inawataka wasiwe na umri usiopungua miaka 18 na wasiozidi umri wa miaka 45 kwa lengo la kuwawezesha kuchangia katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii walau kwa miaka 15 ili kustahili kulipwa pensheni.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itashughulikia kuboresha ujira wa madereva wa magari ya IT?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua mchango wa sekta mbalimbali katika uchumi ikiwemo sekta ya usafirishaji, tayari imepanga kima cha chini cha mshahara kilichoboreshwa ambacho kimeanza kutumika tarehe 1 Januari, 2023. Hivyo mishahara na maslahi kwa madereva imeboreshwa kupitia amri ya kima cha chini cha mshahara kipya.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa kazi kwa madereva wanaoendesha magari ya IT unafanyika kwa kuingia makubaliano ya kazi kati ya mmiliki wa gari na dereva husika ambapo malipo hufanyika baada ya mhusika kufikisha gari linapokwenda. Kwa muktadha huo, mahusiano yaliyopo si ya ajira bali ni makubaliano/mikataba binafsi ya kibiashara (independent contractor) kwa ajili ya contract for service.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, natoa rai kwa madereva wa magari ya IT kuingia mikataba ya kazi ya kibiashara na pale ambapo atatokea mwajiri au kampuni ambayo itaajiri madereva kwa ajili ya kuendesha magari ya IT atapaswa kuzingatia Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ambayo inaelekeza ulipaji wa ujira kulingana na sekta hiyo, ahsante.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA K.n.y MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Je, Serikali ina kauli gani kuhusu mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa kuwa mfumo unawaacha nje vijana wengi kwa kukosa sifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 6 ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2018 pamoja na marekebisho yake inaelekeza sifa na vigezo vya kuzingatiwa kwenye utoaji mikopo kwa vijana.

Mheshimiwa Spika, vigezo na sifa hizo ni pamoja na kikundi kinachofanya shughuli za ujasiriamali au kinachotarajia kuanza shughuli hizo, Kikundi kiwe kimetambuliwa kama kikundi cha vijana; Wanakikundi wawe Watanzania wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35; Kikundi cha vijana kiwe na idadi ya wanakikundi kuanzia watano (5) na kuendelea; Kikundi kiwe na akaunti ya benki iliyofunguliwa kwa jina la kikundi kwa ajili ya matumizi ya kikundi; na Kikundi hakitajumuisha wajumbe wenye ajira rasmi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sifa hizo, katika mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya Vikundi 1,441 vya Vijana vilikopeshwa mikopo yenye thamani ya shillingi Bilioni 13.5 nchini kote.

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali ni kwamba, vijana wenye sifa tajwa waendelee kujiunga katika vikundi vya wajasiriamali na kuomba mikopo hiyo ili kuinua uchumi wao. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaharakisha na kumaliza upembuzi yakinifu kwa ajili ya mradi wa maji katika vijiji 46 Wilaya ya Rungwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Mbeya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 utekelezaji wa miradi ya maji unaendelea katika vijiji 15 na kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji kwa wastani wa asilimia 70. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 kazi za usanifu kwa vijiji 31 itakamilika na kuanza ujenzi wa miradi, matarajio ni kuhakikisha wananchi wa vijiji 155 Wilaya ya Rungwe wanapata maji kwa lengo la kufikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kuongeza bei ya chai Wilayani Rungwe kutoka shilingi 340 hadi shilingi 700 kwa kilo hasa ikizingatiwa kupanda kwa gharama za mbolea na madawa?
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mkulima wa chai anapata bei nzuri Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi imedhamiria kuanzisha mnada wa chai nchini ili kupunguza gharama za usafirishaji na uhifadhi wa chai kwenye maghala katika mnada wa Mombasa. Mnada utasaidia upatikanaji wa soko la uhakika kwa wakulima na kuimarisha bei ya chai nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia itaendelea kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya kuchanganya na kufunga chai nchini ili kupunguza utegemezi wa soko la nje. Hatua hii itaendelea kupanua soko la ndani na kuimarisha bei ya chai nchini.