Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rose Kamili Sukum (3 total)

MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ambayo kwa kweli hayatekelezeki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili lilipitisha Mpango wa Miaka Mitano 2011/2012 hadi 2015/2016 na swali langu ndiko lilikoelekea, lakini kitu cha kushangaza ni kwamba, tuliamua kwamba Bunge hili shilingi bilioni 100 ziwe zinatengwa na zinatolewa kila mwaka kwa ajili ya benki hiyo kama mtaji ambapo ni shilingi bilioni 60 tu zilizotolewa katika benki hiyo kwa miaka mitano. Je, shilingi bilioni 440 ambazo hazikutolewa na Serikali hii, ziko wapi? Tunataka kujua, kama hamna huo mtaji, hiyo Benki ya Mikopo itafanyaje kazi kwa Watanzania ambao ni wakulima 98%? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; nasikitika sana kuwadanganya Watanzania. Hii benki imeundwa kwa ajili ya kuinua uchumi wa wakulima wadogo wadogo. Wako wakulima zaidi ya 98% nchini. Leo tangu benki imeanzishwa imekwenda Iringa tu na kuwapa vikundi vinane tu shilingi bilioni moja: Je, kati ya zile shilingi bilioni 60, nyingine zilikwenda wapi kama ni shilingi bilioni moja tu zilitolewa kwa hao wakulima ambao ni wachache? Je, asilimia..
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kesho tunatarajia kwamba tutafanya negotiation na African Development Bank kwa ajili ya mkopo nafuu wa UA milioni 50 lakini pia UA milioni 25 ambao tunatarajia kwamba utakuwa ni mkopo nafuu ambao Serikali ita-own land TADB kwa ajili ya kuboresha mtaji wa benki hiyo iweze kuendelea kufanya kazi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya fedha zote hizo zile 50 za kwanza ni takriban shilingi bilioni 150 na hizi nyingine ni takriban shilingi bilioni 75. Kwa hiyo, Serikali inafanya jitihada ya dhati kabisa kuongeza mtaji wa TADB.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili; niseme tu kwamba, Benki hii imetoa mikopo kwa vikundi mbalimbali zaidi ya hivyo ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amevieleza, Mheshimiwa Rose Sukum naweza nikakupatia orodha ya vijiji ambavyo vimepatiwa jumla ya bilioni 5.9 kwa Mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga hadi hivi sasa na naweza nikatoa hii taarifa ya mikopo iliyotolewa hadi kufikia tarehe 31 Oktoba.
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, lakini nina maswai mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba Afisa Masuhuli anayetumia fedha bila idhini ya TAMISEMI au ya Hazina, hastahili kutumia hizo fedha. Je, ni kwa nini ofisi yake haikutekeleza wajibu huo kwa Maafisa Masuhuli ambao wametumia hizo fedha bila idhini yake au bila idhini ya Ofisi yake pamoja na Hazina? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe mwenyewe umekiri kwamba fedha endapo itabainika imeongezwa, lakini (b) yake umesema kwamba hakuna bajeti inayoidhinishwa ikazidi kupelekwa kwenye Halmashauri: sasa ni ipi tuipokee kutoka kwako endapo fedha zimeongezeka? Unasema kwamba haziongezeki, nami nina uhakika kwamba fedha zinaongezeka; sasa naomba kuuliza. Je, kwa wale ambao wameongezewa fedha na wale ambao wamepunguziwa wanafidiwaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri atupatie majibu ambayo yanastahili.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa kwamba kwa Afisa Masuhuli yeyote ambaye atakiuka utaratibu wa fedha, maana yake atachukuliwa hatua. Kwa sababu, Mheshimiwa Sukum hakunipa mfano halisi, lakini naomba nimhakikishie, kuna maamuzi mbalimbali ya kinidhamu tumeyachukua kwa Watendaji mbalimbali. Hata baadhi ya Wakurugenzi wengine ambao wameenda nje ya system sasa kutokuwa Wakurugenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni kwa sababu mwanzo katika njia moja ama nyingine walikiuka utaratibu wa fedha na kufanya ufisadi mkubwa katika fedha hizo na ndiyo maana Serikali ilichukua hatua. Ni kwa sababu hatuwezi ku-publicize hapa kwamba nani na nani, lakini tumechukua hatua mbalimbali kwa baadhi ya Wakurugenzi ambao ni Maafisa Masuhuli, walioko katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake lingine kwamba fedha sehemu nyingine zinaongezeka na nyingine zinapungua, nimezungumza wazi, hapa kila Mbunge akisimama anazungumza kwamba fedha haziji, fedha haziji. Ndiyo nimesema, kwa uzoefu tuliokuwa nao, mara nyingi sana fedha zile tunazozipanga, ndiyo maana hata Mheshimiwa Kawambwa hapa anaomba fedha za wodi yake hazijafika. Uzoefu uliokuwepo ni kwamba fedha zinazokwenda ni chache kuliko kile kilichopangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kunatokea na special
case kwamba kuna baadhi ya fedha zimeongezeka, ni lazima utaratibu ufuatwe kama nilivyoelekeza katika maelezo yangu ya awali, kwamba lazima atoe taarifa aidha Hazina au Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa Katibu Mkuu kwa ajili ya ufuatiliaji, fedha hizo zirudishwe katika Mfuko Mkuu wa Hazina.
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba unipe fursa niweze kumuelezea Mheshimiwa Waziri alivyodanganywa na waliomjibia maswali haya.
Mheshimiwa Spika, uchunguzi umeshafanyika Wilaya ya Hanang na uchunguzi huo umefanywa na timu ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara kwa ajili kujua ubadhirifu wa fedha hizo, sio tu fedha za chakula bali ni fedha nyingine pia zipo za shilingi bilioni moja.
Mheshimiwa Spika, nasikitika Mheshimiwa Waziri, nimekuletea document hizi za uchunguzi uliofanyika ndani ya ofisi yenu, leo unakuja kujibu kirahisi kiasi hiki ina maana kwamba wewe umedanganywa, haya si majibu yaliyotakiwa. Fedha hizi zimetumika, shilingi milioni 100 unazozisema hizo zimetumika ni fedha za SEDEP ziko kwenye uchunguzi hii na nitakukabidhi sasa hivi. Hizi za SEDEP zimetumika kwenda kununua magodoro na kadhalika kwenye hayo mabweni. Kwa hiyo ni kosa moja wapo lilitumika la kutumia fedha ambazo hazistahili kutumika.
Mheshimiwa Spika, la pili taarifa ya Mkaguzi wa Ndani imeeleza Aprili 15 zikisema matumizi mabovu ya hizi fedha, fedha hizi hazikutumiwa na halmashauri zimetumiwa na mtu mmoja au watu wachache ndani ya Halmashauri. Sasa iweje Halmashauri irudishe hizi fedha ili kuweza kulipia deni la mtu ambaye amekula hizo hela? Pia kwa taarifa uliyosema majibu ya Mkurugenzi kwamba amesimamishwa, Mkurugenzi yuko kazini anafanya kazi yuko ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, na hawa watumishi wengine wako Wilaya ya Hanang wanafanya kazi.
Mheshimiwa Spika, naomba unisaidie, ni kwa nini hawa watumishi hawakuchukuliwa hatua mpaka sasa hivi na taarifa hii iko ofisini kwako?
La pili, kama kweli inatakiwa ithibitike, utatumia hatua gani kuwezesha uchunguzi maalum ufanyike kwa ajili ya kujua ubadhilifu wa fedha za Wilaya ya Hanang? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza wizi ni wizi hakuna wizi mdogo hakuna wizi mkubwa; wizi ni wizi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Sukum kwamba japokuwa hapa tulikuwa tunaeleza ule mchakato wa zile fedha maalum lakini kilichokuwepo kutokana na specific questions ambazo umeuliza ni kwamba inaonekana Halmashauri ya Hanang si hiyo, kuna lidudu likubwa liko katika Halmashauri ya Hanang. Ndiyo maana nimesema wizi ni wizi hauna mjadala.
Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie, haya yote aliyosema Mheshimiwa Sukum kwamba tutafanyaje, nimesema hapa tumechukua hatua. Kama kuna ubabaishaji wa aina yoyote katika zile hatua tulizochukua naomba nikuhakikishie kwamba by this week ambapo leo Ijumaa, by next week ofisi yetu itatuma special investigation team. Lengo lake kubwa ni kwenda kujiridhisha ni kitu gani kimejificha ndani ya boksi; kwenda kutatuta tatizo la msingi la fedha ambazo inawezekana zimetumika kinyume cha taratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na hili naomba nimhakikishie Mheshimiwa Sukum; katika jambo hili Serikali ya Awamu ya Tano haitavumilia uzembe wa mtu yoyote wa aina yoyote. Hili naomba niseme kwamba kwa concern aliyozungumza Mheshimiwa Rose Kamil Sukum, tunaiagiza timu yetu ya investigation and follow up kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, si kutoka ofisi ya Mkoa, kutoka katika ofisi yetu; iende ikafanye uchunguzi wa haraka, by next week tuweze kupata majibu halisia. Lengo kubwa tulinde fedha za walipa kodi wa Tanzania na hatimaye ziweze kusaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuyajibu maswali yake kwa pamoja kwa muktadha wa namna hiyo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri Jafo, lakini concern iliyooneshwa na Mheshimiwa Mbunge ni kubwa na kwa sababu hiyo basi kwa kuwa pia taarifa zetu zinakuwa tofauti na alizonazo, nimuombe baada ya kipindi cha maswali aje ofisini kwetu tuweze kupata taarifa zaidi, kwa sababu jambo hili ni la muda mrefu na bahati mbaya yule Mkurugenzi aliyekuwa pale sasa hayuko pale, lakini kesi ipo na inaendelea. Pengine kwa hatua hii sasa tunahitaji kwenda kwa haraka zaidi kulingana na concern aliyoonesha Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ni kweli kwamba kumekuwa na maamuzi mabaya kwenye Halmashauri yenye lengo la kutaka kuzitafuna fedha fulani kama zipo ambayo chanzo chake huwa ni kubadilisha matumizi. Waheshimiwa Wabunge mimi napenda niwasihi sana, mabadiliko ya matumizi ya fedha za miradi zinazoletwa kwenye Halmashauri yanafanywa na Waheshimiwa Madiwani na vikao vile vinaridhia. Kupitia mwanya huo basi yanayotokea ni mambo ya ajabu. Kuna watu wamebadilisha hela ya mradi ambayo fedha inatolewa na World Bank wamekwenda kufanya yao, wamegawana posho, wamelipana vitu vya ajabu na wamepeana safari.
Mheshimiwa Spika, sasa kuanzia sasa uamuzi tulioufanya sisi kama Wizara ni kwamba mabadiliko ya matumizi ya fedha yoyote itabidi na Katibu Mkuu - TAMISEMI aridhie. Kwa sababu yanayofanywa huko ni mambo ya ajabu sana, kuna watu wanabadili fedha lakini kubadili huko ni kwa lengo la kwenda kutaka kuzitafuna. Kwa hiyo, sisi Serikali ya Awamu ya Tano hatutakubali jambo hilo liendelee kutokea. Niwasihi Waheshimiwa Wabunge mtusaidie kwa sababu na ninyi mnakuwepo kwenye vikao hivyo. (Makofi)