Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mbaraka Kitwana Dau (37 total)

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Kwa kuwa tatizo la kivuko cha Kitunda, Lindi linafanana sana na tatizo la kivuko baina ya Kilindoni na Nyamisati katika Wilaya ya Rufiji; na kwa kuwa, wananchi wa Mafia kupitia Mbunge wao, tuliiomba Wizara itupatie iliokuwa MV Dar es Salaam, ambayo kwa sasa imepaki pale Navy, Dar es Salaam ili ije itusaidie Mafia kuunganisha baina ya Kilindoni na Nyamisati. Je, ni lini Wizara itaridhia ombi hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Dau kwamba, dhamira yetu ya kuhakikisha kivuko kinakuwepo kati ya Kilindoni na Nyamisati ni ya dhati na tutahakikisha inatekelezwa. Kikubwa nimwahidi kwamba hii meli anayoingolea MV Dar es Salaam, tumeshaeleza katika Bunge hili kwamba, meli hii bado hatujaipokea kutoka kwa supplier kutokana na hitilafu chache zilizokuwa zimeonekana na tumemtaka supplier arekebishe hizo hitilafu kabla haijatumika ilivyokusudiwa kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Dau kwamba, kama wahusika wataona kwamba ni busara kwa sababu aina hii ya kivuko siyo ya kuipeleka mwendo mrefu sana. Kila kivuko kina design yake na kina capacity yake ya distance ya kutembea. Wataalam watakapotushauri kwamba, hili eneo nalo linaweza likatumika kwa MV Dar es Salaam, nimhakikishie hatutakuwa na sababu ya kusita kuhakikisha MV Dar es Salaam inahudumia kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo na Dar es Salaam hadi Mafia.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii.
Kwa kuwa, tatizo la Nyamagana la nyumba za makazi ya Polisi linafanana sana na tatizo la makazi kwa Polisi wa Kisiwa cha Mafia. Je, Mheshimiwa Naibu waziri anaweza kulitolea maelezo gani tatizo la makazi kwa Polisi wa Kisiwa cha Mafia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli lipo tatizo la makazi ya Polisi pia katika Jimbo la Mafia. Nataka tu nimpe taarifa Mheshimiwa Dau kwamba katika ujenzi wa hizi nyumba ambazo tunataka kujenga, kwa upande wa Pwani tunatarajia kujenga nyumba 150. Mpaka sasa hivi, bado mchanganuo wa ujenzi kwa kila Wilaya ama kila Jimbo haujakamilika. Kwa kuwa, Mheshimiwa Mbunge amelizungumza hilo tatizo la Mafia basi tutalichukua tuone katika ujenzi wa hizo nyumba 150 kwa upande wa Pwani tuone uwezekano wa kuweza kuhakikisha kwamba naamini kabisa Mafia itakuwa imo katika mpango huu, lakini siwezi kuzungumza ni nyumba ngapi kwa upande wa Mafia, hilo tunaweza tukafanya kazi kwa kushirikiana mimi na yeye baadaye.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa. Kwa kuwa gati ya Bukondo linafanana sana na kesi iliyopo kwenye gati la Nyamisati na la Kilindoni kule Mafia.
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Gati la Nyamisati, na lini Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo la abiria kwa Gati la Kilindoni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa yako, mimi naitwa Bwana Nyamisati. Kila ninapokutana na Mheshimiwa Dau, ndivyo anavyoniita Mr. Nyamisati, kwa sababu ameniambia nisipokamilisha hili ana namna, mimi sijui ana namna gani ya kuhakikisha sirudi hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia tena Mheshimiwa Dau na Waheshimiwa Wabunge wengine waliokuwa wanafuatilia masuala hayo mawili pamoja na ile meli ya kutoa huduma kati Mafia na Dar es Salaam, naomba kuwahakikishieni wote, kwamba kile ambacho tumewaambia tuliwaambia tukiwa na dhamira njema. Tutahakikisha Nyamisati ambayo tayari imeshapangiwa bajeti kwa mwaka huu na mmeshaipitisha inatekelezwa. Na vilevile Kilindoni, kwa sababu tunajua Kilindoni na Nyamisati ndiyo tunakamilisha mawasiliano kati ya Mafia na upande huu wa Bara. Naomba nikuhakikishie nisingependa kuahidi kwamba tutaanza dakika hii au tutamaliza dakika hii, mimi nikuhakikishie kazi hii tutaisimamia mpaka ikamilike.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwanza Naibu Waziri anakiri kwamba barabara ile imejengwa chini ya kiwango;
lakini Naibu Waziri atakubaliana na mimi, alipotembelea Mafia tuliikagua barabara hii mimi na yeye. Barabara hii si ya kufanyiwa matengenezo makubwa, ni ya kurudiwa upya.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, ng’ombe akikatisha kwenye barabara anaacha mashimo, barabara ya lami! Gari likipata
puncture ukipiga jeki, jeki inakwenda chini kama unapiga jeki kwenye tope, kule Mafia wanaiita barabara ya big G
(chewing gum).
Mheshimiwa Spika, sasa nina maswali mawili. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali inakiri kwamba mkandarasi
huyu ameijenga chini ya kiwango, ni hatua gani za kimkataba na za kisheria zimechukuliwa dhidi ya huyu
mkandarasi aliyeisababishia Serikali hasara? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wananchi wa maeneo ya Kilindoni, Kiegeyani na Utende ambao wahanga wa kubomolewa nyumba zao, wengine walikuwa ni wahanga wa kubomolewa nyumba zao, wengine wamekatiwa minazi yao na mikorosho yao na mazao yao mbalimbali, mpaka leo wengi wao hawajalipwa fidia kutokana na ujenzi wa barabara ile, ningependa nisikie kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, nini hatma ya waathirika hawa wa fidia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba
nilikuwa Mafia na Mheshimiwa Dau na tuliikagua hiyo barabara. Lakini namuomba tu asiongeze utani sana ndani
ya Bunge, maeneo machafu ni machache ambayo yameshaainishwa na kwa mujibu wa mkataba tumeshachukua hatua ya kumlazimisha mkandarasi kurudia maeneo hayo kwa gharama zake.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu fidia; nimuombe Mheshimiwa Kitwana Dau, kwamba yale tuliyoongea Mafia
ayazingatie. Nikuhakikishie yeyote mwenye haki ya kulipwa fidia atalipwa. Sehemu ya wengi tunaowaongelea pale ni
wale ambao waliifuata barabara.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa Wilaya ya Mafia imezungukwa na bahari na hakuna Police Marine na kuna matishio ya Maharamia wa Kisomali. Je, ni lini sasa Serikali itafikiria uwezekano wa kuleta doria ya Police Marine katika Kisiwa cha Mafia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mafia ni kati ya maeneo ambayo tumeyawekea kipaumbele katika kuimarisha usalama katika maeneo ya bahari. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalitambua hilo; na pale ambapo hali ya bajeti itakaporuhusu, tutalifanyia kazi.(Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kumuuliza swali moja Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa Taasisi ya Hifadhi ya Bahari Mafia, imeshindwa kazi yake ya msingi ya kuzuia uvuvi haramu na uhifadhi na hivi sasa inauza visiwa na maeneo Wilaya Mafia. Je, Sasa Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuondoa uongozi wa juu pale na kubadilisha kuleta uongozi mwingine?Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tulielezea kwamba hakuna visiwa ambavyo vimeuzwa Mafia isipokuwa sheria tu zimefuatwa kukodisha Kisiwa cha Shungimbili kwa miaka 20 kwa Mwekezaji wa Hoteli. Vile vile kama kuna ushahidi wowote ule ambao utaonesha kwamba, maafisa anaowazungumzia wameshindwa kufanya kazi yao au wamejihusisha na vitendo ambavyo ni kinyume na sheria, lakini vile vile na maadili ya kazi yao, naomba Mheshimiwa Mbunge atuletee na sisi bila kusita tutachukua hatua.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo la Songea Mjini linafanana sana na tatizo lililopo katika Wilaya ya Mafia. Wilaya nzima ya Mafia haina hata Kituo kimoja cha Afya. Ukizingatia kwamba alipokuja Waziri Mkuu tulimwomba suala hili na mchakato tumeshauanza katika ngazi ya Wilaya. Je, ni lini sasa Serikali itatupatia Kituo cha Afya angalau kimoja pale Kilongwe kwa kuongeza hadhi ile zahanati iliyopo pale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tulipofika Mafia tulienda katika hicho Kituo cha Afya na nikatoa mapendekezo kadhaa likiwemo suala zima la makazi ya watu katika maeneo yale, lakini tulikubaliana kwamba wafanye mchakato na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Dau, kwa sababu Mafia jiografia yake lazima tuboreshe huduma ya afya na nilitoa maelekezo pale mbele ya DC na mbele ya Mkurugenzi nini kifanyike kituo kile kiweze kuboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Mheshimiwa Dau kwamba Serikali imechukua ile, tutafanya kila liwezekanalo hasa eneo la Mafia katika kile Kituo cha Afya ambacho nimekitembelea mwenyewe, tutafanya uboreshaji mkubwa katika kipindi kinachokuja.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru pia ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii sio ahadi tu ya Rais Mstaafu na kwenye Ilani ya Uchaguzi bali pia ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipotembelea Wilaya ya Mafia mwezi Septemba, 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mafia kwa kuwa ni kisiwa, hali ya upatikanaji wa udongo ni ndogo sana. Udongo unapatikana katika kijiji kimoja cha Bweni na wataalam wanasema baada ya miaka miwili udongo huo utakuwa umekwisha kabisa. Kwa hiyo, mtakapokuwa tayari kuja kujenga barabara ya lami, udongo Mafia utakuwa umekwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, sasa kwa kuwa Ilani ya CCM inasema mwaka huu mtaanza na usanifu na katika majibu yako hujasema hata kama usanifu utafanyika, swali la kwanza; kwa nini usanifu usifanyike mwaka huu ili ujenzi ufanyike mwakani?
La pili; ni kwanini sasaSerikali isitilie maanani hili suala la ukosefu wa udongo na kuharakisha ujenzi huu ifikapo mwakani? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau kwa namna anavyofuatilia masuala ya miundombinu katika Kisiwa cha Mafia na kwa kweli aliponipeleka Mafia mimi nimebadilika kabisa. Naomba nimhakikishie yale ambayo tuliyaongea tutayafuatilia ili kuhakikisha ahadi hii ambayo kama alivyosema sio ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne peke yake bali ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015; lakini vilevile Waziri Mkuu alipokwenda pale ambapo yeye alitangulia kabla yangu naye alirudia kuahidi kutokana na mazingira yalivyo pale Mafia.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba nikuhakikishie kwamba tutawasiliana ndani ya Wizara kama ambavyo tulikwambia awali ili tuone uwezekano wa kuanza feasibility study and detailed design ya barabara ile mwaka huu kwa kadri ambavyo Mwenyezi Mungu atatujaalia na mimi naamini Mwenyezi Mungu yupo upande wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dau kwa swali lako la pili naomba tukutane na Mheshimiwa Waziri wangu na kwa sababu leo ni siku ya mwisho ya Bunge na Waziri wangu yupo jana ulikutana nae lakini naomba tukutane nae tena ili tulikamilishe hili kama ambavyo uliambiwa na Waziri wangu jana.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya vituo vya reli yanafanana sana na matatizo ya vituo vya boti vinavyomilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari - TPA. Kituo cha boti cha Nyamisati hakina vyoo, maji na migahawa. Je, ni lini Naibu Waziri ataielekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari - TPA wakajenge vyoo, maji, umeme pamoja na masuala mengine ya kijamii? Ahsante sana.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukulia aliyoyasema ni mapendekezo, tumepokea mapendekezo yake na kwa sababu anajua kile kituo cha Nyamisati hivi sasa ndiyo kinaanza kufanyiwa kazi ya kujengwa basi watakapokuja katika hatua za ujenzi watu wa TPA wafikirie vilevile mapendekezo ambayo Mheshimiwa Dau ameyatoa ili yaweze kushughulikiwa.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mafia ina vivutio vingi sana akiwemo huyu samaki wa ajabu anayeitwa Potwe au whale shark. Vile vile Mafia kuna maeneo mazuri sana ya scuba diving, sports fishing na kuna fukwe tulivu. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mafia kama Wilaya mpaka leo haina Afisa wa Utalii. Sasa swali la kwanza, ni lini Serikali itatupatia Afisa wa Utalii katika Wilaya ya Mafia?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini Serikali itaruhusu
au itaifungulia ile hoteli ambayo Mheshimiwa Simbachawene alikuja akaifunga ya Chole Mjini, ambapo wananchi wanapata pale ajira, Serikali inapata kodi na wale wawekezaji pale walikuwa wanasomesha vijana wengi katika kisiwa cha Chole, sasa ni nini tamko la Serikali juu ya kuondoa tofauti zilizokuwepo ili ile hoteli iendelee kufanya kazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza nakubaliana na yeye na Serikali inatambua kwamba, Mafia ni Kisiwa tajiri cha vivutio vya utalii; na kwa kweli Mafia ni mojawapo ya maeneo nchini ambayo yataiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya ku-diversify, kutanua wigo wa aina ya vivutio, lakini pia kutanua wigo wa kufanya utalii maeneo mengi zaidi nchini kuliko maeneo machache ambayo yanaendelea hivi sasa. Kwa hiyo, ule umuhimu wa Mafia tayari Serikali inaufahamu na inaufanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na hoja yake ambayo ni ya msingi kabisa ya kwamba ili tuweze kufikia malengo katika hayo ni vema tukawa na Afisa Utalii kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, nakubaliana naye. Hata hivyo, nimshauri tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili ni vema akaenda kulipeleka kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ili waweze kuangalia kwa namna gani wanaweza kuingiza kwenye ikama nafasi hiyo ya Afisa Utalii.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la hoteli aliyoitaja, hoteli ya Chole pale Mjini Mafia, licha ya faida zote alizozitaja ni kweli Serikali inafahamu kulikuwa na fursa za ajira za wananchi na faida nyingine kama ambavyo ameweza kuzigusia, lakini kulikuwa na changamoto za kimsingi ambazo ni za kisheria na ndiyo maana Mheshimiwa Waziri alipokwenda kule Mheshimiwa Simbachawene alichukua hatua aliyoichukua na kuweza kusimamisha uendeshaji wa hoteli ile.
Mheshimiwa Spika, lakini ametoa maoni ambayo nayapokea na hivyo ndivyo ambayo tunafanya hivi sasa kufanya mawasiliano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya TAMISEMI. Mawaziri wawili hawa wanaendelea kulijadili na kulitazama ili hifadhi za malikale ziweze kutumika kwa mujibu wa sheria inayotakiwa, lakini pia shughuli za utalii zifanyike kwa mujibu wa sheria tulizojiwekea.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa fursa hii.
Tatizo la mgogoro wa shamba la Madaba linafanana sana na tatizo la shamba la Kigomani na Utumaini lililopo Wilayani Mafia.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuja Mafia kukaa na wadau wa Halmashauri pamoja na Viongozi wengine kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge na lile deni letu tumeshatoa shilingi milioni 50 tumemaliza kituo cha afya, hongera sana Mheshimiwa Mbunge kwa ujenzi wa theatre. Hata hivyo, katika jambo hili mimi naomba nilichukue, lakini kabla mimi sijaja kule nimuagize Mkuu wa Wilaya ya Mafia kwanza aende akalishughulikie jambo hili na ikiwezekana tupate taarifa amelishughulikia vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakapopata hiyo taarifa jinsi gani limeshughulikiwa jambo hili na mgogoro huo haukuisha, na mimi nitaona jinsi gani ya kufanya, lakini kwamba nitatumia vyombo vyangu vya chini kule kwanza, Mkuu wa Wilaya ya Mafia aanze kuifanya kazi hiyo harka iwezekanavyo kumaliza hilo tatizo na ofisi yetu ipate taarifa ndani ya mwezi mmoja, jinsi gani mgogoro huo umeshughulikiwa kwa kadiri iwezekanavyo. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Kwa kuwa Serikali imepiga marufuku uvuvi wa majongoo bahari Kisiwani Mafia; wakati huo huo majongoo bahari yanavunwa kule Zanzibar upande wa pili wa Muungano.
Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka kuruhusu uvuvi wa majongoo bahari kuendelea Mafia?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema kwamba uvuvi wa majongoo bahari umepigwa marufuku Mafia, kwa sababu kimsingi kwa namna ulivyokuwa unaendelea ulikuwa unaharibu sana matumbawe. Kwa sababu kuvua majongoo bahari inabidi uzame ndani uende kwenye mazalia ya samaki na ni lazima uingie kwenye miamba ndiyo uweze kuvua majongoo bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar wao wanaendelea kufanya, lakini nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la uvuvi katika maji yale ya kawaida siyo suala la Muungano. Kwa hiyo, Zanzibar wanakuwa na sheria zao na sisi tuna sheria zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri anachosema Mheshimiwa Mbunge ni kwamba ni vizuri katika kujenga ule ushirikiano tuwe na maamuzi ambayo yanaweza yakafanana na hasa yale ambayo yanasaidia pande zote mbili kuendelea kuimarisha na kulinda rasilimali za uvuvi.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Tatizo la viboko lililopo katika Jimbo la Ulanga linafanana sana na tatizo la viboko lililopo Kisiwani Mafia. Wananchi wa kata za Ndagoni, Baleni na Kirongwe wameharibiwa mazao yao na ng’ombe wao wameuwawa na viboko waharibifu. Kutokana na ongezeko kubwa sana la viboko hawa na Kisiwa cha Mafia ni eneo dogo, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutoa ruhusa tuanze kuwavuna viboko hawa kwa sababu kule ni kitoweo pia? Ahsante. (Kicheko)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpa pole sana Mheshimiwa Dau na wananchi wake wa Mafia kwa kadhia hii ambayo imewakumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ambayo tutachukua ni pamoja kutuma wataalamu waende wakafanye sensa ili tujue kwamba kuna viboko wangapi katika eneo hilo na tuweze kuangalia kama kuna uwezekano wa kuweza kuwavuna hao viboko ili kupunguza madhara yake kwa wananchi wa eneo la Mafia.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii. Pamoja na majibu mazuri na yenye kutia matumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisiwa cha Jibondo kimejengeka kutokana na mawe na miamba mikubwa, huwezi ukachimba kisima pale ukapata maji. Wananchi wa Jibondo wamekuwa kwenye kadhia ya ukosefu wa maji toka dunia hii iumbwe, wanapata maji ya bahari na mara chache maji ya mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kwamba usanifu pamoja na ujenzi utaanza mwaka ujao wa fedha.
Nilikuwa naomba aliahakikishie Bunge lako, ujenzi huu utaanza lini? Kwa sababu usanifu na ujenzi vyote vimewekwa pamoja, utaanza lini na utachukua muda gani ili nikitoka hapa niende nikawaambie wananchi wa Jibondo kwamba tarehe fulani maji yataanza kutoka Jibondo? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuingia katika vitabu vya historia na kuwa Waziri wa pili kufanya ziara katika Kisiwa cha Jibondo toka Mzee Malecela alipofanya hivyo miaka ya 1970 akiambatana na mimi Mbunge wa Jimbo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameuliza ujenzi utaanza lini? Kama nilivyosema kwamba usanifu umekamilika na wanakamilisha nyaraka za zabuni, tutatangaza tender. Kwenye ule mchakato wa tender ndiyo tutapata tarehe kamili kwamba mkandarasi ataanza lini na atakamilisha lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi ni kwamba kazi hiyo itafanyika katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, Mheshimiwa Mbunge tutahakikisha tunafanya kazi hiyo na tunakamilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema kwamba Kisiwa cha Jibondo kimejaa mawe, ni kweli na ndiyo maana tumechimba kisima eneo lingine la Kiegeani na bomba lile litapita chini ya bahari mpaka liende kwenye Kisiwa cha Jibondo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeniomba nitembelee pamoja na wewe, Mheshimiwa Mbunge, nipo tayari. Baada ya kumaliza bajeti hii, basi tutazungumza na tutatengeneza ratiba ili twende mpaka Kisiwa cha Jibondo nikawahakikishie wananchi kwamba wanapata maji. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri hapa kwamba kutokana na jiografia yake kisiwa cha Mafia, kiwanja cha ndege ni muhimu sana katika kukuza uchumi. Lakini mimi nataka nimuongezee, kuna ziada pia masuala ya jamii. Hivi ukiwa Mafia ikifika saa kumi na mbili na ukapata dharura ya ugonjwa huna namna ya kutoka kwenda katika Hospitali ya Rufaa kwa sababu kiwanja hakina taa.
Sasa kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kwamba usanifu na upembuzi ulishafanyika toka mwaka 2009 na leo ni miaka minane kwa hesabu za haraka bado unakuja kutuambia kwamba pesa hazija patikana?
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini hizi pesa zitapatikana ili ujenzi wa kuweka taa katika uwanja wa Mafia na jengo la abiria ufanyike?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya kurukia na kutua yani runway ya kiwanja cha Mafia ina mita kama 800 hivi, hivyo ndege kubwa haziwezi kutua na unasema kuna fursa za kitalii pale.
Je, ni lini sasa Serikali itaongeza urefu wa uwanja ule kwenda mpaka kilometa mbili ili kuruhusu ndege kubwa zitue moja kwa moja kutoka Ulaya na kuleta watalii Mafia? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ninapenda nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dau mjukuu wangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada anazozifanya ili kuhakikisha kwamba kisiwa cha Mafia kinachangia pia katika ukuaji wa uchumi Taifa, kwa maana ya kuleta maendeleo katika kisiwa cha Mafia.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi kwamba upembuzi yakinifu na kazi ya ukarabati wa uwanja baada ya usanifu ilishaanza, kwa sababu kazi iliyofanyika ya kupanua kiwanja na kukarabati ilikuwa ni awamu ya kwanza. Kwa hiyo, kuna awamu ya pili ambayo itafanyika kwa ajili ya kuhakikisha kwamba uwanja huu sasa unafanana na kwamba unatoa pia huduma. Kwa sababu Serikali tunapanua viwanja vikubwa kwa mfano Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa KIA, kwa maana hiyo na viwanja vingine vya Mikoani tunavyovifanyia upanuzi sasa vitakuwa na tija kwa kutoa huduma katika viwanja hivi vikubwa.
Mheshimiwa Spika, ni nia ya Serikali kufanya upanuzi, na mimi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Mafia kwamba kwenye awamu ya pili tutazingatia ushauri wake kwamba tuone namna ya kuvipanua vile viungio ili huduma ziweze kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, mimi nitahakikisha kwamba kwenye bajeti zinazokuja awamu hii ya pili tutaiwekea fedha ili huu uwanja wa Mafia uweze kufanana na hali ilivyo na kwamba tuweze kukuza utalii, lakini pia uweze pia kuweza ku-feed viwanja vikubwa ambavyo tunavipanua.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Dau mjukuu wangu usiwe na wasiwasi tutakuja Mafia na mimi nitahakikisha kwamba jambo linakwenda vizuri. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya wavuvi wadogo katika Ziwa Tanganyika yanafanana sana na matatizo ya wavuvi wadogo katika Kisiwa cha Mafia. Taasisi ya Hifadhi ya Bahari Mafia imekuwa ikiwanyanyasa na kuwabambikia kesi wavuvi wadogo wa Mafia na kuwanyang’anya nyavu zao. Je, Mheshimiwa Waziri utakuwa tayari kufanya ziara Mafia na kutukutanisha sote ili kupata ufumbuzi wa tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie kaka yangu, Mheshimiwa Mbaraka Dau, Mbunge jirani wa Mafia ya kwamba nipo tayari kwenda nyumbani Mafia kwa ajili ya…
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri sambamba na Waziri mwenye dhamana wamekuwa mara kadhaa wakijibu maswali hapa na kuahidi kwamba, visiwa vidogo vyote nchi nzima vitapatiwa umeme wa solar. Sasa ningependa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, ni lini umeme wa solar utakwenda katika Visiwa vya Jibondo, Chole, Juani na Bwejuu? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Dau, Mbunge wa Mafia kwa swali lake zuri na tunatambua Mafia nako ni Wilaya ambayo ina visiwa vingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nisisitize kwamba, hii miradi tunayosema, huu mradi kabambe wa REA awamu ya tatu tunaoutekeleza, vijiji ambavyo vimetamkwa 7,873 vinahusisha pia na vijiji ambavyo tunaviita off grid. Kwa hiyo, nimthibitishie mchakato wa kuwapata Wakandarasi wanaopeleka umeme katika maeneo ambayo si rahisi kufika miundombinu ya kawaida unaendelea. Kwa mfano, Mkuranga kuna visiwa ambavyo tulipeleka umeme kupitia REA hii na utaratibu unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo niseme siyo Mafia tu, lakini katika maeneo mbalimbali ambayo ni magumu kufikika kwa miundombinu ya kawaida, mradi huu wa REA Awamu ya Tatu ambapo vipindi vyake ni hii 2017/2018, 2018/2019 na 2019/2020 vijiji hivyo vitapatiwa. Hakuna kijiji ambacho kitaachwa kwa sababu tu ya mazingira yake. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya usafiri wa baharini ya Bumbwini yanafanana sana na matatizo ya usafiri baina ya Bandari ya Kilindoni, Mafia na Bandari ya Nyamisati, Kibiti. Wananchi wa Mafia wamekuwa wakisafiri katika maboti ya mbao ambayo si salama na hayana bima.
Je, ni lini Serikali itainunulia Wilaya ya Mafia boti ya kisasa kuondokana na tatizo la usafiri baina ya Bandari ya Nyamisati na Kilindoni ili kuepusha maafa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbaraka Dau anafahamu kwamba Serikali ina mikakati maalum ya kuhakikisha inatatua tatizo la usafiri Mafia. Tukianzia kuhakikisha kwamba magati yanayotumika ni ya kisasa na yako salama. Kwa vyovyote vile magati haya yakishakaa salama tutavutia wawekezaji wa kuleta meli na kama ikitokea kwamba hakutakuwa na meli zitakazofika, pamoja na kuimarisha gati kwa maana ya gati iliyoko tayari pale Mafia, lakini vilevile hili linalopokea upande wa Bara, tukishakamilisha hizo kama hatutakuwa na wawekezaji binafsi watakaovutika kutoa huduma za usafiri nikuhakikishie Mheshimiwa Dau tutakaa pamoja tuangalie tufanyeje pamoja na Serikali tuone namna ya kutatua usafiri wa eneo hili la Mafia. (Makofi
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, hali ya usalama wa abiria na mizigo katika bandari ya Kilindoni kwa zaidi ya miezi mitatu sasa iko mashakani kufuatia kukatika kwa ngazi katika gati la Kilindoni. Abiria wanalazimika kupanda kwa kutumia mitumbwi na viboti vidogo vidogo kwenda kupanda boti kubwa hali ambayo ni hatari sana kwa usalama wao.
Sasa je, Mheshimiwa Waziri anaweza akatuhakikishia Wananchi Mafia kwamba atawaelekeza watu wa Mamlaka ya Bandari waje watengeneze warekebishe gati lile ili lianze kutumika? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ninafahamu umuhimu wa usafiri wa majini kwa ndugu zetu wa Mafia, ni njia kuu kwa wale ambao hawana uwezo wa kutumia ndege na kwa sababu hiyo nawaagiza TPA wafanye haraka sana kwenda Mafia pale Kilindoni ili lile daraja ambalo limekatika liweze kurekebishika na hatimaye ile gati iweze kuanza kutumika kwa kutoa usafiri kwa ndugu zetu wa Mafia.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Tatizo la kutoanza ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo linafanana sana na tatizo la kutokuanza ujenzi wa Bandari ya Nyamisati katika Wilaya ya Kibiti. Bandari ya Nyamisati ni Bandari ambayo ni kiungo baina ya wananchi wa Mafia wanapokuja Dar es salaam. Mkandarasi ameshapatikana toka mwaka jana mpaka leo hajafika site, ni nini kauli ya Serikali kuhusu Mkandarasi huyu? Nakushuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua na Mheshimiwa Dau hapa amekuwa akipiga kelele kweli, uko ule utaratibu wa kujenga Bandari ya Nyamisati unaendelea. Nimwombe tu asiwahishe shughuli hata wakati wa bajeti ataona tumependekeza fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa Bandari hii ya Nyamisati. Kwa hiyo kama atataka taarifa za ziada basi naomba tuonane ili angalau nimwoneshe mpango madhubuti uliopo kwa ajili ya kuokoa wananchi wa Mafia na Watanzania wengine ambao watakuwa wakisafiri kwenda Mafia.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya uvuvi haramu katika maeneo ya Lindi yanafanana sana na matatizo ya uvuvi haramu katika Kisiwa cha Mafia. Taasisi iliyopewa mamlaka ya kushughulika na uvuvi haramu Mafia imejitwika majukumu mengi zaidi ya uhifadhi kwa maana ya wanauza maeneo ya vivutio na kukusanya mapato. Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba Taasisi ya Hifadhi ya Bahari ya Mafia wanabaki na kazi ya uhifadhi peke yake badala ya kujishughulisha na kukusanya mapato? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Hifadhi ya Bahari kwa Kiingereza tunaiita kwa kifupi MPRU ipo kwa mujibu wa sheria za nchi. Miongozo ya kuanzishwa kwake MPRU kwa maana ya hifadhi ya bahari inawaelekeza kufanya kazi kadha wa kadha.
Moja ya kazi hizo ni uhifadhi lakini mbili ni kusimamia masuala yanayohusu wanaokuja katika maeneo yale ya hifadhi ikiwa ni pamoja na kuwatoza ushuru ambao kwa pamoja unarudishwa katika vijiji na Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa mfumo wa asilimia 30. Asilimia 10 inakwenda katika halmashauri ya wilaya na asilimia 20 inakwenda moja kwa moja katika vijiji vinavyohusika na uhifadhi ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Mbunge ni lini sasa MPRU itajielekeza katika kusimamia uhifadhi tu badala ya kukusanya ushuru. Masuala haya ni ya kisheria na kikanuni tunamkaribisha Mheshimiwa Dau kwa hoja hiyo mahsusi kabisa ya kutaka kwamba MPRU ijielekeze na uhifadhi tu badala ya kufanya shughuli zingine ikiwemo hiyo ya kukusanya mapato. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Gati la Kilindoni lilipo Wilayani Mafia lipo katika hali mbaya sana. Mbao zake zimechakaa, ngazi imekatika na lile tishali ambalo abiria pale wanapandia limekaa vibaya kiasi kwamba wakati wowote inaweza ikatokea ajali. Sasa Mheshimiwa Waziri ningependa atufafanulie, kwamba imekuwaje, ni lini Serikali itafanya ukarabati mkubwa wa gati la Kilindoni ukizingatia kwamba ile boti ya DMY itaanza kazi mwezi wa 10? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba gati la Kilindoni lipo katika hali isiyoridhisha kwa matumizi ya abira. Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania pamoja na wataalam kutoka TEMESA na DMY wameshatumwa maeneo yale kwa ajili ya kwenda kufanya ukaguzi na kuleta gharama ambazo zitatumika kutengeneza BOQ kwa ajili ya kufanya marekebisho makubwa ambayo tunakiri yanahitajika katika eneo hilo. Ahsante.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa, barabara ya Rasimkumbi mpaka Kilindoni kilometa 55 katika kisiwa cha Mafia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na imo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Lakini mpaka sasa hata usanifu haujaanza.
Swali, je, ni lini Mheshimiwa Waziri barabara hii usanifu utaanza na hatimaye kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Dau, Mbunge wa Mafia kwamba barabara ya Rasimkumbi hadi Kilindoni upembuzi yakinifu tayari umekwishaanza, tukishapata taarifa ya upembuzi yakinifu tutakwenda kufanya usanifu wa kina kwa ajili sasa ya kutafuta pesa kwa ajili ya kujenga eneo hilo. Kwa hiyo, tunaomba avute subira kazi zinaendelea tumekwisha jipanga kwa ajili ya kutekeleza.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, moja ya matishio ya samaki aina hii ni anapoingia katika mitego ya wavuvi huwa anajeruhiwa kwa sababu wao wanakuwa hawamli lakini anapata majeraha katika kumnasua kwenye zile nyavu. Matokeo yake kwa kuwa ngozi yake iko very delicate, akipata michubuko anakufa. Sasa kwa kuwa samaki huyu ni wa season anapatikana kuanzia miezi ya mwanzo ya Septemba mpaka Machi, je, Serikali haioni sasa ipo haja ya kutengeneza quota system ambapo msimu wa potwe maeneo ya Kilindoni anapopatikana papigwe marufuku ya kuvua samaki wengine ili kumnusuru samaki huyu kwa sababu huenda akaondoka Mafia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, utalii katika Kisiwa cha Mafia una gharama kubwa sana. Kila mtalii anayeingia eneo la hifadhi ya bahari analazimika kulipa dola 24 kwa siku moja. Kutokana na ughali huu, inalazimisha baadhi ya watalii kuanza kushindwa kuja Mafia. Je, Serikali sasa ina mpango gani kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupunguza kiwango hiki cha entrance fees za kuingia maeneo ya marine park ili kuweza kuvutia watalii wengi kuja Kisiwani Mafia? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya kaka yangu Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Utalii Mheshimiwa Hasunga kwa majibu mazuri ya msingi hasa pale aliposema anaitaka jamii iweze kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa samaki hawa au papa huyu anayeitwa papa potwe ama pia ninachukua pongezi nyingi sana kwa kaka yangu Dau kwa kuwa mshirika mzuri wa kulinda rasilimali zetu za Taifa ambazo zimekuwa ni kivutio kikubwa cha watalii katika visiwa vyetu hivi vya Mafia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala alilolisema la kuweka utaratibu maalum Wizara yetu tunalichukua ili kusudi sasa tuwe na wakati wa uvuvi katika eneo la Kilindoni na kuna wakati ambapo tutazuia ili kuwapisha papa potwe waweze kustawi. Bila ya kufanya hivyo, papa potwe watahama Mafia na tutasababisha utalii wa papa potwe uweze kutoweka katika eneo hili la Mafia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili juu ya tozo mbalimbali ambzo zinachukuliwa na Wizara yetu kupitia kitengo chetu cha MPRU kwa maana ya hifadhi ya bahari na zile zinazokwenda Wizara ya Utalii, mimi naomba nimhakikishie kwamba sisi Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Maliasili na Utalii tutakaa kwa pamoja na kufanya review ya hizi tozo na kodi hizi zinazohusika katiak utalii huu ili kusudi tuweze kuhakikisha kwamba watalii waweze kuvutika kwa wengi zaidi. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo la kukatika kwa umeme Mkoani Mtwara linafanana sana na tatizo la kukatika kwa umeme katika Kisiwa cha Mafia. Kisiwa cha Mafia kinapata umeme kutoka kwenye majenereta manne makubwa ya dizeli. Kwa kuwa Mheshimiwa naibu Waziri amesema Mkoa wa Mtwara una majenereta 11 yakiwemo mawili mapya; je, haoni sasa ni muhimu tuchukue yale majenereta mawili mapya ya Mtwara na kuyapeleka mafia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa shahidi, Mheshimiwa Mbaraka Dau ameshauliza maswali zaidi ya mawili kwa tatizo la umeme la Mafia. Naomba nimthibitishie kwamba Serikali kama ambavyo imepata kumjibu ndani ya Bunge, tunalishughulikia kwa karibu tatizo la upatikanaji wa umeme katika Wilaya ya Mafia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hilo swali alilosema kwamba tupeleke mashine mbili, naomba nimwombe kaka yangu, nami pia ni Mbunge wa maeneo hayo kwamba hili suala aje Ofisini tulizungumze, lakini kwa sasa zile mashine lazima zitumike Mtwara na Mafia tutafanya utaratibu mwingine. Ahsante sana.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukweli kwamba mkandarasi yupo site, lakini kasi ya mobilization na vifaa duni anavyovitumia vinatia mashaka sana kama mkandarasi anaweza akamaliza kazi hii katika muda uliotajwa.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari baada ya kikao hiki cha bajeti, mimi, Mheshimiwa Ungando, Mbunge wa Kibiti na mama yetu Mheshimiwa Salma Kikwete ambaye ni mdau mkubwa sana wa Gati la Nyamisati, tufanye ziara ya pamoja ili kuhakikisha kwamba gati hili linakwisha kwa muda uliopangwa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba kati ya Wabunge ambao wamekuwa wakifuatilia suala la Gati hili la Nyamisati ni pamoja na Mheshimiwa Dau na Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, wote kwa pamoja wamekuwa wakifuatilia na wakitaka kujua hatua mbalimbali ambazo zinaendelea katika ujenzi wa gati hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vifaa wakandarasi wanavyo, bado wanaendelea kukusanya, kama nilivyozungumza kwenye majibu ya awali kwamba wako kwenye mobilization kwa hiyo vifaa bado vinaendelea kuletwa na wana vifaa vya kutosha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo, ndiyo maana tumeweka deadline, huu mradi utakabidhiwa mwezi mapema Machi mwakani. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba vifaa vitafika kwa wakati na nipo tayari kwenda nao Waheshimiwa Wabunge wote kwa ajili ya kwenda kuukagua mradi huo.(Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Faida zote zinazopatikana katika michikichi zinapatikana pia katika zao la minazi. Je, Serikali ina mikakati gani ya kufufua zao la minazi ambalo linalimwa zaidi katika Mikoa ya Ukanda wa Pwani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Dau swali lake moja dogo la nyongeza kuhusu minazi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunaelewa kwamba minazi nayo ni zao muhimu sana kwa kilimo katika nchi hii. Kama nilivyosema ni kwamba kupitia Bodi yetu ya Mazao Mchanganyiko ambayo Bunge lako Tukufu limepitisha bajeti hapa, minazi nayo ipo chini ya Bodi yetu ya Mazao na Nafaka Mchanganyiko. Kama Serikali tuko tayari kuhakikisha kwamba tunaimarisha zao la minazi ili nalo liweze kuwa ni zao la kibiashara na chakula kama kiungo. Ahsante.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri anasema mshauri elekezi ataanza kazi mwezi Julai na itachukua kama miezi saba. Sasa nataka atuhakikishie watu wa Mafia, baada ya miezi saba ya mshauri kumaliza kazi, je, ujenzi rasmi wa hizi hybrid utaanza lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa sasa hivi kuna tatizo kubwa sana Mafia la kukatikakatika umeme na vyanzo ni vya mafuta, hivyo vimekuwa havitoshelezi na kwa kuwa Mikoa ya Lindi na Mtwara imeshaingizwa kwenye Gridi ya Taifa na kuna majenereta pale kama manane hivi ya two megawatts, je, Mheshimiwa Naibu Waziri haoni sasa kwa kipindi hiki cha mpito wakati tukisubiri hizo jitihada nyingine kuwa tayari, tupatiwe angalau majenereta mawili yale ya Lindi na Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Mheshimiwa Mbaraka Dau, swali lake la kwanza ameuliza baada ya upembuzi yakinifu kuanza na kukamilika, nimthibitishie kwamba ni kweli mradi huo utaanza ndani ya hiyo miezi saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumweleza Mheshimiwa Dau kwamba kwa mujibu wa swali langu la msingi tumesema kabisa kwamba Benki ya Maendeleo ya Ufaransa imeonesha nia ya kufadhili mradi huu na kinachosubiriwa ni upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa eneo tumelipata na kazi itaanza mwezi wa saba, naomba nimthibitishie kwamba kwa kudra za Mwenyezi Mungu kwa kipindi cha miezi saba hiyo na kwa kuwa tunayo benki tayari imeonesha nia, kazi hiyo itaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ameuliza kwamba sasa baada ya mafanikio makubwa ya kuunganisha Mikoa ya Mtwara na Lindi kwenye Gridi ya Taifa, amewasilisha ombi kwa niaba ya wananchi wake na naomba nimpongeze, ni lini kwamba tunaweza tukapeleka yale majenereta?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kama Serikali tumelipokea hilo jambo lake na linazungumzika, lakini kwa sasa tunajaribu kwa sababu uzinduzi wenyewe wa kuunganisha umeme wa gridi umefanyika tu juzi, tunajaribu kuangalia upatikaji wa umeme baada ya kuunganisha mikoa hii kwenye gridi, lakini hapo baadaye tutakapoona umeme umetulia unapatikana kwa ukamilifu, basi nalo linazungumzika na tutalipokea. Ahsante. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa. Kufuatia operesheni ya kijeshi iliyoendelea pale Mafia na kupelekea madhila na hasara kubwa sana kwa wavuvi ambao walinyang’anywa zana zao halali za kuvulia, wengine mashine zao za boti zimezuiwa; wengine compressors zao, wangine magenereta yao yamezuiwa na hifadhi ya bahari. Mheshimiwa Waziri alitoa taarifa hapa kwamba vitu vyote hivi viachiwe. Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana atakuwa tayari kufuatana nami twende Mafia, Jibondo, Tumbuju na Kilimnoni akaonane na wavuvi ili awaelezee kiuhalisia zoezi hili lilivyokwenda?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Dau, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari kwenda na nimeshamkubalia Mheshimiwa Mbunge, tukimaliza tu Bunge hapa kuanzia Jumapili, nitakuwa ukanda huo kutembelea maeneo hayo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kukiweka sawa ni kwamba saa nyingine tunapozungumzia wananchi wetu, wanaweza kuwa wako sahihi kulingana na malalamiko yao, lakini wanaweza kuwa wahalifu. Sasa ni vizuri pia tukawa makini na hilo kwa sababu kama ni wahalifu halafu wanazungmziwa kupata unafuu hapa Bungeni, nadhani itakuwa ni utaratibu ambao haukubaliliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka niseme, mimi niko tayari. Waheshimiwa Wabunge, hakuna hata sababu kwa mfano mhalifu mmoja wa kumzungumzia hapa Bungeni. Sisi tuko hapa kama ofisi, kama kuna mtu yoyote ameonewa mahali popote, lete tushughulikie, hakuna hata sababu ya kuhangaika kuuliza swali hapa. Kwa sababu wengine ni wahalifu. Sasa Bunge likigeuka kuwa linazungumzia wahalifu kila siku, litakuwa linapoteza muda wake mwingi. Saa nyingine wengine wanataka huruma ya Mheshimiwa Waziri, sasa huwezi kuipata huruma kwa kuvunja sheria halafu unataka utetewe na Bunge.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa. Mradi wa Maji kati ya Kisiwa cha Jibondo ambao una thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili, Mkandarasi ameshaujenga na sasa amefikia asilimia zaidi ya 70. Mradi unatakiwa ukabidhiwe mwezi Machi mwaka huu. Mpaka sasa Mkandarasi hajalipwa hata senti tano na certificate zipo Wizaran. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza akatuhakikishia ni lini sasa Mkandarasi huyo atalipwa ili aweze kumaliza mradi ule?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nampongeza Mheshimiwa Dau kwa kazi nzuri sana anayofanya kwa wananchi wake wa Mafia na pamoja na Jibondo. Tunatambua kabisa wananchi wa Jibondo wamekuwa na changamoto kubwa sana katika suala zima la maji na hata chanzo cha maji kukosekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tumeona haja sasa ya kutekeleza mradi mkubwa na tunatambua kazi nzuri aliyoifanya Mkandarasi. Nataka nimhakikishie, katika mgao wa mwezi huu Mheshimiwa Mbarawa ameshatenga fedha zaidi ya shilingi milioni 200 katika kuhakikisha tunamlipa Mkandarasi yule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwaagiza Mhandisi wa Maji wa Mafia, fedha zile zitakapofika ahakikishe anamlipa Mkandarasi haraka ili asimkwamishe katika suala zima la utekelezaji na wananchi waweze kupata maji. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Wananchi wa Mafia kwa kushirikiana na Mbunge wao wamejenga chuo cha kisasa kabisa cha VETA na kukamilisha taratibu zote, lakini mpaka leo Wizara haijatoa usajili. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri sasa atakuwa tayari kutoa usajili kwa ajili ya VETA ya Mafia?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dau amekuwa akifuatilia sana suala la VETA ya Mafia. Kwa kweli, kuna wakati hata mimi na yeye kidogo tulitofautiana kwa sababu, aliona kwamba, hatufanyi kazi kwa kasi ambayo anaitaka kwa hiyo, nampongeza sana kwa sababu, amekuwa akifuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, VETA ya Mafia imekuwa na changamoto mbili kubwa ambayo ni changamoto ya vifaa, hasa kwenye fani za ushonaji, lakini vilevile Walimu ambao wana viwango vinavyohitajika, ili VETA iweze kusajiliwa. Nimemwahidi Mheshimiwa Mbunge na ninaendelea vilevile kumwahidi kupitia Bunge lako Tukufu kwamba, Wizara yangu iko tayari kusaidiana na yeye pamoja na wananchi wake wa Mafia ili changamoto hizo tuweze kuziondoa na tuweze kutoa usajili mapema kwa ajili ya chuo chake.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja namajibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza,kwa kuwa hizi bilioni sita alizozisema zimekokotolewa kutoka kwenye net revenue, baada ya kuondoa gharama na kwa kuwa hifadhi ya bahari wanaweka gharama za mafuta, gharama za likizo, gharama za uendeshaji wa hifadhi, mpaka kupelekea gharama zinakuwa ni kubwa lakini net revenue inakuwa ni ndogo ambayo halmashauri ya Mafia inatakiwa ipate asilimia 30.

Sasa swali, je, Mheshimiwa Naibu Waziri, haoni sasa umefika wakati gharama za kukusanya mapato peke yake ndiyo zitolewe, waachane na gharama za uendeshaji wa hifadhi ya bahari kwa sababu gharama zinakuwa ni kubwa na kipato kinakuwa ni kidogo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwamoja ya vikwazo vya Wilaya ya Kisiwa cha Mafia kupata watalii wachache, kwa mwakatunapata pale watalii kama elfu sita, ukilinganisha na Kisiwa cha Zanzibar, moja ya vikwazo ni hii entrance fees ya dola 24 kwa kila mtalii. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri haoni sasa umefika wakati wa kuangalia uwezekano wa kupunguza kiwango hiki cha entrance fees ili kuweza kuvutia watalii wengi kuja katika Kisiwa cha Mafia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya kaka yangu Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Daukama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza anataka na kutushauri Serikali kuona umuhimu wa kupunguza gharama za uendeshaji ili kusudi ile faida inayopatikana na shughuli nzima za uhifadhi na utalii ziweze kwenda moja kwa moja katika jamii ya Mafia pia. Naomba nimhakikishie kuwa wazo lake hili tunalibeba naSerikalitumelichukua. Kwa kuwa ni jambo la kimchakato, tutakwenda kulitazama na kuona ni namna gani tunavyoweza kuendana na mawazo hayo ya wananchi wa Mafia.

Mheshimiwa Spika,jambo la pili, ni juu yakuona umuhimu wa kupunguza fee ya kuingilia katika maeneo haya ya hifadhi, ili kusudi kupata watalii wengi zaidi. Ni lengo la Serikali la kuhakikisha kuwa watalii wanaongezeka katika maeneo yetu ya utalii na hivyo, kama moja ya kikwazo ni entrance fee, nataka nimhakikishie pia Mheshimiwa Mbunge kwamba, hili nalo ni wazo ambalo tutalichukua, tutakwenda kulikokotoa na kuona umuhimu wake ili kuweza kufikia lengo letu la kuongeza idadi ya watalii nchini.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini Serikali sasa itahakikisha kwamba bandari ya uvuvi inajengwa ili fursa ya uvuvi wa bahari kuu iweze kutumika vizuri sana? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la ndugu yangu Mbunge wa Mafia, jirani yangu, Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni lini bandari itajengwa. Hivi sasa tuko katika kumalizia mchakato wa upembuzi yakinifu wa eneo itakapokwenda kujengwa bandari ya uvuvi. Tayari mkandarasi huyu kupitia pesa zetu wenyewe, pesa za ndani tumeshamlipa na anamalizia kazi ya kutuelekeza mahali gani katika ukanda wetu wa pwani tutakwenda kujenga bandari ya uvuvi.

Mheshimiwa Spika, habari njema zaidi, nadhani wote tumemsikia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipokuwa katika Mei Mosi pale Mbeya ameeleza juu ya nia njema ya nchi rafiki ya Korea ambapo wameonesha nia ya kutaka kushirikiana nasi katika kwenda kujenga bandari hii ya uvuvi.

Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania kwa ujumla kwamba nia yetu hii itakwenda kutimia na hatimaye kuweza kupata faida ya uvuvi katika eneo la bahari kuu.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kivuko cha Nyamisati, Kilindoni mpaka leo bado hakijakamilika. Ningependa kusikia kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini kivuko hiki kitakamilika?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHATA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetoka kumwambia Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ukerewe ni kwamba hivi vivuko viwili manunuzi yamekamilika na sasa hivi mkandarasi ameanza kazi na tunanunua engine haraka ili baada ya matengenezo sasa vivuko hivyo vianze kufanya kazi. Tulikuwa hatuna kivuko ambacho kilikuwa kinaenda Nyamisati na Mafia, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge pamoja na wapiga kura wake ni kwamba, Serikali imeshachukua hatua, tunajenga kivuko kipya ambacho kita-operate kati ya Nyamisati na Mafia.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Matatizo ya wavuvi wa Ukerewe yanafanana sana na matatizo ya wavuvi wa Kisiwa cha Mafia. Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana mezani kwake kuna barua kutoka kwangu na kwa wavuvi wangu tukiomba ruzuku ya msaada wa zile mashine.

Je, ni lini majibu yake yatatoka?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake hili la nyongeza akiulizia suala la zile mashine za ruzuku, tukitoka hapa Bungeni aje pale ofisini kwa ajili ya utaratibu wa kupata zile mashine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala hili la vijana na wavuvi wetu kuhakikisha wanaheshimika katika mabenki na mahali popote pale, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa Uvuvi Database ambapo ndiyo kilikuwa kipengele kikubwa sana kilichokuwa kinawafanya wavuvi wetu wasiaminike kwenye mabenki kwa sababu ya shughuli zao za kuhamahama na kila mtu mwenye benki anakuwa na mashaka juu ya fedha zake atakapozipeleka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipoanzisha Uvuvi Database sasa hivi benki yotote ile ikitaka kumkopesha mvuvi ambaye yupo Buchosa, Ukerewe, Mafia na maeneo mengine watamuona mpaka na kazi zake anazozifanya. Hii inaenda kuongeza imani kubwa kwa wavuvi wa nchi yetu na ile dharau iliyozoeleka ya kwamba wavuvi hawakopesheki sasa itakuwa mwisho. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nilikuwa na swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kwamba Kisiwa cha Mafia ni maarufu na ni eneo zuri sana kwa ajili ya snorkelling, scuba diving na aina nyingine za uzamiaji:-

Je, Serikali itakuwa tayari sasa kuleta hicho chuo ikakiweka Mafia ili wananchi wa Mafia wanufaike nacho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dau, Mbunge wa Mafia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye majibu ya nyongeza ya Mheshimiwa Yusuph; baada ya wataalam hao kurejea; na kwa sababu wataalam hao wametumwa na Serikali kwenda kuchukua masomo hayo maalum kupitia vyuo ambavyo vipo; ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba katika maeneo ambayo tutayapa kipaumbele ni pamoja na Kisiwa cha Mafia.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Matatizo haya ya Mto Msimbazi yanafanana sana na matatizo yaliyopo maeneo ya Hananasifu. Sasa je, Mheshimiwa Waziri kwa kuwa World Bank wako tayari kutupatia fedha kwa ajili ya kuondoa matatizo haya ya mafuriko katika mto ule: Je, ni lini sasa Serikali itaridhia hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, utayari wa Benki ya Dunia ni jambo moja, lakini uhalisia wa gharama pia ni jambo jingine, kwa hiyo kama Serikali siyo kwamba ni Serikali inayopokea pokea offers tu ni lazima tuangalie kwamba tunachokipokea kina tija na je gharama yake ni sahihi? Kwa hiyo, nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kama Serikali tuna nia ya kutekeleza mradi na andiko liko tayari na kwa kweli wadau wanaojitokeza siyo World Bank tu wako na wengine wanaojitokeza wengi lakini lazima tutafakari na kuangalia uhalisia wa gharama, Hivyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itafanya uwekezaji lakini kwa kuangalia uwezo wa uchumi wa nchi yetu lakini pia na aina ya msaada tunaoupokea.