Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Risala Said Kabongo (5 total)

MHE. RISALA S. KABONGO aliuliza:-
Hifadhi za Mikoa ya Kusini za Mikoa ya Kusini za Ruaha, Kitulo, Udzungwa, Mikumi na Katavi na maeneo mengine ya kihistoria husifika sana kwa vivutio vyake, lakini kutembelewa na idadi ndogo sana ya watalii na hivyo kuwa na mapato madogo na kuwa tegemezi kwa Hifadhi za Mikoa ya Kaskazini:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi na mrefu wa kuongeza idadi ya wageni katika hifadhi hizo?
(b) Je, Serikali ina mikakati gani ya kuboresha miundombinu ya barabara, malazi na viwanja vya ndege katika hifadhi hizo kwa matumizi ya watalii?
(c) Je, kwa nini Serikali isishirikiane na wawekezaji binafsi ili kuwekeza katika maeneo ya utalii kwenye Hifadhi hizo za Mikoa ya kusini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Risala Saidi Kabongo, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa na Shirika la USAID, ilifanya upembuzi yakinifu na kuandaa mikakati ya kuendeleza na kutangaza utalii kwenye eneo la Kusini mwa Tanzania mwaka 2015. Ili kutekeleza mikakati hiyo, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia itatekeleza mradi utakaojulikana kama Tanzanian Resilient Natural Resources Management for Growth. Mradi huu ambao utatekelezwa kwa miaka sita, umepangwa kuanza kutekelezwa Januari, 2017 na utagharimu takribani Dola za Kimarekani milioni 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zitakazotekelezwa na mradi huo ni pamoja na kuimarisha uhifadhi wa mazingira, kuendeleza utalii na kuwezesha wananchi kunufaika na utalii. Mradi huu utahusisha pamoja na mambo mengine, uimarishaji wa miundombinu ya utalii hasa barabara, viwanja vya ndege na huduma za malazi. Vilevile kutengeneza circuit ya utalii kwa upande wa Kusini ili mgeni aweze kutembea au kutembelea eneo au hifadhi zaidi ya moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada mbalimbali zimefanywa na zinaendelea kufanywa ili kuboresha shughuli za utalii Kusini na Magharibi mwa Tanzania. Jitihada hizo ni pamoja na kuimarisha barabara toka Tunduma kwenda Mpanda kupitia Sumbawanga kwa kiwango cha lami ambayo itaziwezesha hifadhi za Katavi na Mahale kufikika kwa urahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika, ujenzi wa barabara ya Sumbawanga hadi Kasanga kwa kiwango cha lami ambayo itapanua wigo wa wataalii kutembelea Ziwa Tanganyika pamoja na vivutio vingine nje ya hifadhi kama vile maporomoko ya Kalambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada nyingine ni kuimarisha na kuboresha viwanja vya ndege vya Songwe, Kigoma na Mpanda ambavyo vitasaidia kufikika kwa maeneo ya vivutio yaliyotajwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ukarabati wa barabara itokayo Kigoma kuelekea Kusini hadi Kaliya, Namwese ambayo itaunganisha Mkoa wa Katavi, hivyo kuwezesha watalii kufika Mahale kwa urahisi zaidi. Shirika la Hifadhi za Taifa litaunganisha Hifadhi ya Mikumi na Pori la Akiba la Selous kwa barabara itakayopitika mwaka mzima ili kuwezesha watalii wengi wanaofika Selous kufika Mikumi, kutembelea maeneo hayo kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, vivutio vya Utalii Kusini mwa nchi vitaendelea kutangazwa na taasisi zilizo chini ya Wizara na kuimarisha Ofisi ya Kanda ya Iringa Mjini.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuvutia wawekezaji binafsi kutoa huduma mbalimbali za watalii ikiwemo malazi, ambapo vibali 11 vimetolewa kuwekeza kwenye huduma za malazi katika Hifadhi za Ruaha, Mikumi, Katavi na Mahale. Uwekezaji huo ambao upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji utaongeza jumla ya vitanda 544.
MHE. RISALA S. KABONGO aliuliza:-
Vijiji vya Ngiresi, Sokoni II na Oldadai Kata ya Sokoni II Jimbo la Arumeru Magharibi vinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji ya bomba, kwa muda mrefu licha ya kwamba vijiji hivyo kuna vyanzo vingi vya maji na mabomba yanayopeleka maji Arusha Mjini:-
(a) Je, Mamlaka ya Maji Jiji la Arusha inashindwa kutekeleza maombi ya wananchi wa vijiji hivyo ya kupatiwa maji kutoka kwenye mabomba kwa utaratibu wa kulipia?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza na kuboresha vyanzo vya maji katika Jiji la Arusha na Halmashauri zake kutokana na ongezeko kubwa la wakazi wake?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Risala Saidi Kabomgo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika kuondoa tatizo la maji Jiji la Arusha, imepata mkopo wa dola za Kimarekani milioni 210.96 kutoka Benki ya Maendeo ya Afrika (AfDB) ili kutekeleza mradi wa upanuzi wa mtandao maji safi na maji taka sambamba na kuboresha vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu mkubwa utawezesha Jiji la Arusha pamoja na viunga vyake, ikiwa ni pamoja na vijiji vyote vilivyopo umbali wa kilometa 12 kando kando ya bomba kuu, vikiwemo vijiji vya Ngilesi, Sokoni II na Oldadai ili kupata huduma ya majisafi na majitaka. Jumla ya gharama za ujenzi ni dola za Marekani milioni 233.92 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 476.44.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba wa mkopo huu nafuu umesainiwa na Mamlaka ya Maji Arusha, kwa sasa inaendelea na taratibu za kupata Mhandisi Mshauri wa kusimamia mradi pamoja na Wakandarasi wa Ujenzi. Ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017 na kukamilika mwaka 2019/2020. Mradi huu ukikamilika utaboresha vyanzo vya maji na utaongeza upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Arusha na Halmashauri zake ambazo zimekumbwa na ongezeko kubwa la wakazi.
MEH. RISALA S. KABONGO aliuliza:-
Utekelezaji wa Tangazo rasmi la Serikali la Mwaka 2008 juu ya mpaka mpya wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha katika Bonde la Usangu umeshindikana, hivyo kufanya upanuzi holela wa maeneo ya kilimo, uvamizi wa mifugo mingi na matumizi holela ya maji katika kilimo, jambo ambalo limesababisha uharibifu wa mazingira, Mto Ruaha Mkuu kuendelea kukauka kila mwaka na kuathiri uzalishaji umeme katika Bwawa la Mtera na Kidatu na shughuli zingine na matumizi ya maji ya Mto Ruaha Mkuu:-
(a) Sababu zipi za msingi zilizosababisha utekelezaji wa Tangazo hilo kushindwa kwa takribani miaka nane sasa?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani za haraka ili kunusuru na kusitisha uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea katika Bonde la Usangu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Risala Said Kabogo, Mbunge wa Viti Maalumu, lenye Sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inampongeza Mheshimiwa Risala Kabongo kwa kutambua na kuthamini jitihada za Serikali na kuona umuhimu wa uhifadhi katika Taifa, hususan uhifadhi katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha katika Bonde la Usangu, ambako shughuli za kilimo, uingizaji, uchungaji na ulishaji mifugo na matumizi ya maji yasiyo endelevu katika kilimo zimesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, unaosababisha pamoja na athari nyingine kukauka kila mwaka kwa Mto Ruaha Mkuu na hatimaye kuathirika shughuli za uzalishaji umeme kutokana na kukosekana kwa kiasi cha maji kinachohitajika katika mabwawa ya Mtera na Kidatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu nilioainisha hapo juu Serikali ilikamilisha taratibu zote husika na kutoa Tangazo la Serikali Namba 28 la mwaka 2008, ambalo msingi wake ni Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura ya 282, hususan Kifungu cha tatu (3) na cha nne (4) cha sheria hiyo ili eneo la Bonde la Usangu lijumuishwe ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa Tangazo la Serikali Namba 28 la mwaka 2008 haujashindikana na badala yake matakwa ya Tangazo hilo yameanza kwa kuhakiki mipaka na kuweka alama za kudumu beacons kwa baadhi ya maeneo yaliyoongezwa. Kutoa elimu na kuhamasisha wananchi waliotakiwa kuhama ili kupisha hifadhi, kufanya tathmini na kulipa fidia ya ardhi na mali zisizohamishika kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 na Na. 5 za mwaka 1999. Aidha, Serikali inaendelea na utekelezaji wa matakwa ya Tangazo la Serikali Namba 28 la mwaka 2008, ambapo baada ya changamoto zilizojitokeza kutatuliwa, wananchi walioko katika eneo husika pamoja na mali zao zinazohamishika wataondoka kupisha shughuli za uhifadhi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu yangu ya swali Namba 53 lililouliza na Mheshimiwa Haroon Mulla Pirmohamed, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, katika Kikao cha Sita cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja kilichofanyika tarehe 27/4/2016, nilisisitiza kuhusu umuhimu wa kuhifadhi eneo la Bonde la Usangu kwa maslahi mapana ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu hayo nilieleza kuhusu kuwepo kwa timu ya Wataalam iliyopitia changamoto za utekelezaji wa Tangazo la Serikali, ikiwa ni pamoja na kutafsiri mpaka, kuweka alama na kukamilisha malipo ya fidia kwa mujibu wa sheria katika kipindi cha mwezi mmoja, hatua ambayo itawezesha Serikali kuendelea na hatua muhimu na za haraka ili kudhibiti uharibifu wa mazingira katika Bonde la Usangu.
MHE. RISALA S. KABONGO aliuliza:-
Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Mto Ruaha Mkuu unatiririsha maji yake katika Bwawa la Mtera na Kidatu kwa mwaka mzima kama ilivyokuwa miaka iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Risala Saidi Kabongo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mto Ruaha Mkuu ni kati ya mito mikuu minne inayounda Bonde la Rufiji ambayo ni Mto Kilombero, Mto Luwegu, Mto Ruaha Mkuu na Mto Rufiji wenyewe. Maji ya Mto Ruaha Mkuu hutokana na mito inayotiririka kutoka safu za Milima ya Livingstone kule Mbeya. Mito hiyo huingiza maji yake kwenye eneo oevu la Usangu (Ihefu) ambalo likishajaa maji hutoka hapo kama Mto Ruaha Mkuu.
Mheshimiwa Spika, upungufu wa maji kwenye mto huu kwa kiasi kikubwa unachangiwa na shughuli za kijamii na kiuchumi ambazo zinasababishwa na ongezeko la watu. Shughuli hizo ni pamoja na kupanuka kwa kilimo cha umwagiliaji ambapo miundombinu yake haijasanifiwa na kuboreshwa. Vilevile uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji miti, kilimo kisichokuwa bora, ongezeko la mifugo na mabadiliko ya tabia nchi vinachangia upungufu huo wa maji.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na hali hii, Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika Bonde la Rufiji imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kwa lengo la kuongeza mtiririko wa maji kwenye mto huo. Jitihada hizo ni pamoja na mpango wa ujenzi wa Bwawa la Lugoda katika Mto Ndembela ambapo lengo kuu la mradi ni kuongeza mtiririko wa maji wakati wa kiangazi katika Mto Ruaha Mkuu unaopita katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yakiwemo Mabwawa ya Mtera na Kidatu.
MHE. RISALA S. KABONGO aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Vwawa ambayo inatoa huduma kwa Halmashauri nne za Mbozi, Ileje, Songwe na Momba inakabiliwa na upungufu wa vifaatiba, wodi, watumishi pamoja na Madaktari Bingwa.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupandisha hadhi Hospitali ya Vwawa kuwa Hospitali ya Mkoa ili iweze kutengewa bajeti ya kutosha kukabiliana na changamoto zilizopo sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Risala Said Kabongo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilituma timu ya wataalam kutoka Idara mbalimbali na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo ilifanya ukaguzi wa siku kumi kuanzia tarehe 25 Agosti, 2017 hadi 5 Septemba, 2017 katika Hospitali ya Vwawa iliyopo Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe ili kufanya tathmini kuona kama hospitali hiyo inaweza kutumika kama Hospitali ya Mkoa na hatimaye kuwasilisha matokeo ya tathmini hiyo kwa Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri aliridhia Hospitali ya Wilaya ya Mbozi yaani Vwawa itumike kwa muda kama Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe wakati Mkoa unaendelea na taratibu za kujenga Hospitali ya Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha huduma katika hospitali hii, Serikali ilipeleka watumishi tisa akiwemo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akina mama pamoja na kufunguliwa akaunti Bohari ya Dawa (MSD) yenye namba MB 310004 yenye kutoa mgao wa dawa ngazi ya mkoa ili kuweza kutoa huduma kama Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshatoa kiasi cha shilingi milioni 767 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe ambapo eneo lenye ukubwa wa hekari 23 lililopo Hasamba katika Mji Mdogo wa Vwawa limeshatengwa na taratibu za kuanza ujenzi wa Hospitali hiyo kwa awamu ya kwanza zimeshaanza ikiwemo uandaaji wa michoro ya usanifu inayofanywa na Wakala wa Majengo Tanzania. Inatarajiwa Wakala wa Majengo ndiye atasimamia ujenzi wa hospitali hiyo. (Makofi)