Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Maryam Salum Msabaha (48 total)

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami naomba niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa huu Mradi wa REA umesambazwa sana vijijini na nguzo zimewekwa sana vijijini, lakini nguzo hizi zimeanza kuoza. Je, ni lini Serikali itahakikisha nguzo hizi zinawekwa na wananchi wa vijijini wanapata umeme? Ahsante sana.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza labda iwe ni miujiza, hizi nguzo kuharibika siyo chini ya miaka kumi. Kwa hiyo, kuoza kisayansi hatukubaliani na hilo, la kwanza hilo. (Makofi)
La pili, Waheshimiwa Wabunge, ni kwamba jumla Tanzania tuna vijiji 15,029. Vijiji ambavyo vimepata umeme hadi sasa ni 5,900, sawa na asilimia 33. Kwa hiyo, tukiingia REA Awamu ya Tatu, ya Nne na ya Tano, nadhani Tanzania itakuwa katika nchi pekee Barani Afrika kwamba umeme umetapakaa vijijini kote.
Mheshimiwa Mbunge, ndiyo maana ni wiki moja kutoka sasa tunafanya tathimini ya REA Awamu ya Pili, ili tuingie REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, nguzo haziozi na hazitaoza, umeme utapatikana. Ahsante.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu ya Waziri na amekuwa mfuatiliaji sana wakati nauliza maswali yanahusu Vikosi vya Ulinzi na Usalama. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka ya jeshi inalindwa na Wanajeshi wenyewe, je, ni kwa nini kuna vikosi ambavyo vinavaa nguo za jeshi na kulinda mipaka ya jeshi na kuchafua taswira ya Jeshi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Zanzibar, kipindi cha uchaguzi kumekuwa na vikosi vingi sana na vingine havina taaluma ya kutumia silaha na wamekuwa wakiwadhuru wananchi kwa silaha za moto na waliodhurika wengine ni wazee wakongwe wa miaka 60 na kuwapatia ulemavu wa kudumu. Je, Serikali ina mikakati gani kuunda Kamati Teule kukichunguza hiki kikosi cha Mazombe ili tutambue kwa mujibu wa sheria kimesajiliwa na Serikali ipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mipaka ya Vikosi vya Jeshi inalindwa na Wanajeshi wenyewe, hakuna kikosi tofauti kinacholinda mipaka ya Vikosi vya Jeshi. Kwa hiyo, hilo wala asipate tabu ya kudhani kwamba kuna watu wanavaa sare za kijeshi lakini sio Wanajeshi, hapana. Wanaolinda mipaka hiyo ni Wanajeshi wenyewe na hakuna tatizo kama hilo katika mipaka ya Vikosi vya Jeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la hicho anachokiita kikundi au kikosi cha Mazombe, sina taarifa ya kikosi hicho na kama jambo hilo linatokea Zanzibar, basi ingekuwa vyema swali lake alielekeze kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hicho kikosi mimi sikitambui. (Makofi)
MHE. MARYAM S. MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naona Mheshimiwa Naibu Waziri sijui alikuwa kalala, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kambi hii niliyoitaja hasa hii Mesi ya Ulinzi na Usalama ipo katika mazingira ambayo siyo rafiki sana na jamii iliyowazunguka, upande kuna Skuli ya SOS na upande kuna Msikiti, pia kunakuwa na vitendo ambavyo vinaendelea pale ambavyo siyo rafiki na jamii inayowazunguka. Je, ni lini Serikali itahakikisha inatenga fedha za kutosha ili kukarabati Kambi hii na hasa hii Mesi ya Jeshi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vikosi vingi vya Ulinzi na Usalama vinaishi uraiani na vinakuwa siyo rafiki sana na wananchi hasa wananchi ambao siyo waadilifu na nchi yao. Je, ni lini Serikali itahakikisha vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama vinajengewa makazi bora na yenye sifa kama vikosi vya Ulinzi na Usalama?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Maryam Msabaha kwamba maoni yake tutayazingatia katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao tutaangalia uwezekano wa kutilia maanani mapendekezo yake, hasa ukizingatia kwamba amezungumza changamoto ambazo ni za msingi kabisa .
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na nyumba, tayari kuna program ya ujenzi wa nyumba na hilo liko tayari katika mipango ya Serikali, nadhani muda siyo mrefu suala la nyumba litaanza kupunguzwa kadri ya uwezo wa nchi kifedha utakapokuwa unaruhusu.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimuulize Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa huu umeme wa REA wananchi wengi hawajapata elimu ya kusaidiana na Serikali katika kutoa maeneo ya kuweka huu umeme wa REA. Je, Serikali mna mpango gani kuhakikisha mnakwenda kijijini kutoa hii elimu ili wananchi watoe maeneo haya ya kupitisha umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa REA wanavyofanya kazi, elimu inayotolewa inatolewa kwa kiwango kidogo. Nichukue nafasi hii kutamka rasmi kwamba kuanzia tarehe 1 Julai, wafanyakazi wote wa REA pamoja na TANESCO watakuwa sasa wanawafuata wateja badala ya wao kufuatwa, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili tunawaelekeza sasa kutoa elimu sahihi kwa ajili ya taratibu za uunganishaji umeme pamoja na ada zinazotakiwa kulipwa. Kwa sasa wananchi wataelimishwa kwamba hawatakiwi kuweka mchango wowote kwenye maombi ya umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, wananchi wataeleweshwa kuhusu gharama za service levy kwamba zimeondolewa, kwamba huduma ya kuhudumiwa umeme sasa imeondolewa. Kwa hiyo, jitihada za Serikali za kuhakikisha kwamba wananchi wanapata elimu zitaendelea. Zilikuwa zikifanyika lakini sasa tutaongeza nguvu zaidi kwa kuwafanya watumishi wa TANESCO na REA kufanya kazi kibiashara kwa kuwafuata wateja na kuwapa elimu badala ya wao kufuatwa.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa watumishi hawa wanaohamishwa katika sekta ya afya wanacheleweshewa mafao yao huko wanakopelekwa. Je, Serikali itahakikishaje wanapata stahiki zao kwa wakati muafaka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la malipo ya watumishi, nadhani kama tulivyozungumza awali tutaendelea kuyashughulikia malipo haya hasa kulipa madeni ya watumishi, lakini siyo watumishi pekee hata madeni ya wazabuni mbalimbali ambao wanadai Halmashauri zetu, suala hili tutalifanya kwa pamoja. Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba tunalipa madeni yote ya watoa huduma aidha watumishi au wale wanaotoa huduma za zabuni katika hospitali zetu na center mbalimbali ili isije kufika muda tukawafunga mikono wakashindwa kufanya kazi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kuna jambo tulizungumzia katika maeneo mbalimbali kwamba kuna pesa ambazo zitakuwa zinatumika kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi. Hata hivyo, naomba kusema kwamba kama hakuna ulazima wa kuhamisha watumishi, tusifanye hivyo kwa sababu tutakuwa tunakuza madeni ya watumishi bila sababu ya msingi.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nimwulize Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza kutokana majibu yake kuwa marefu sana.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bandari bubu zipo mipakani; vyombo vya ulinzi na usalama huwa vinakutana na changamoto kwenye bandari hizi. Je, Serikali mnatambua kama vyombo hivi vinakutana na changamoto kubwa kudhibiti silaha na hata magendo? Mna mpango gani kuongezea vyombo vya ulinzi na usalama, stahiki zao na hata vifaa vya utendaji kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa majahazi ndiyo yanayotumika kufanya sana uhalifu, kubeba madawa ya kulevya na hata kutorosha bidhaa haramu kama pembe za ndovu: Je, Serikali mna mikakati gani kukagua majahazi na kudhibiti vyombo hivi vya majahazi ndani ya bahari na ukaguzi wa mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sheria na taratibu zinazotumika katika kulipa vyombo vya dola. Nimechukua wazo lake na tutawasiliana na Wizara mbalimbali ikiwa ni pamoja na Idara Kuu ya Utumishi pamoja na Wizara yenyewe ya Mambo ya Ndani ili tuangalie kwa pamoja uwezekano wa kuboresha kile ambacho sasa hivi kipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, limefanana na hili la kwanza ingawa limeulizwa kwa namna nyingine. Namhakikishia kwamba vyombo hivi vya ulinzi na usalama vinatekeleza wajibu wake kwa umakini sana na namhakikishia kwamba tutaendelea kudhibiti kama ambavyo sasa hivi tumekamilisha kudhibiti katika eneo hili la mwambao wa Bahari ya Hindi na tumeamua bandari hizo ambazo nimezielezea katika swali la msingi zirasimishwe na tutahusisha halmashauri husika katika kuendelea kudhibiti na kukusanya mapato.


NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyatoa, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kuongezea majibu hayo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba vyombo vya usalama vinakabiliwa na changamoto nyingi wakati wa kukabiliana na wahalifu hawa wa magendo pamoja na uhalifu mbalimbali wa madawa ya kulevya, biashara haramu, wahamiaji haramu na kadhalika. Miongoni mwa changamoto hizo si tu kwamba vitendea kazi ni changamoto lakini pia hali ya hewa na masafa marefu ya kuelekea kwenye kina cha maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hatua ambazo tumechukua mpaka sasa hivi, kwanza kabisa tunajaribu kupata taarifa za kiintelijensia ili kazi ya kuweza kufanya operation iwe rahisi pale ambapo taarifa za uhakika tumezipa. Hii tunashirikiana vizuri sana na wananchi pamoja na jamii za maeneo husika. Lingine ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuimarisha vitendea kazi hivi hasa speed boat kwa kadiri hali ya bajeti itakavyokuwa inaruhusu.
MHE. MARYAM S. MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na pole sana. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa rehma. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nchi za wenzetu kama kwa mfano nchi za jirani South Africa na nchi nyingine wametenga maeneo kwa ajili ya mama lishe, maeneo rafiki na wanauza vyakula vyao bila kubughudhiwa.
Je, Serikali mna mikakati gani kuhakikisha mnatenga maeneo maalum kwa ajili ya wajasiriamali wadogo wadogo hasa mama lishe?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, Jafo, kwa majibu mazuri ya swali la msingi.
Mheshimiwa Spika, lakini nikuhakikishie tu kwamba Serikali inatambua mchango mkubwa katika uchumi wa nchi yetu kutoka kwa wafanyabiashara wadogo wadogo.
Hata hivyo Serikali imeweka mkakati na tumetoa waraka maalum kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya, kusimamia Halmashauri kutenga maeneo mahususi, maalum kabisa kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo. Na ndiyo maana Mheshimiwa Rais katika agizo lake la kwamba, wafanyabiashara wadogo wadogo hawa, wamachinga, wasibughudhiwe bali wasaidiwe. Ni agizo ambalo tunalitekeleza na tumeanza kulipa mkakati wa namna ya kulitekeleza.
Mheshimiwa Spika, lakini niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, wao ni Wajumbe wa Mabaraza ya Madiwani na wao ni Madiwani. Hawa mgambo wameajiriwa na Halmashauri zetu, hawa mgambo si sawa na polisi, kwa hiyo, hawawezi wakapewa kazi kubwa ya kufanya operation hivi kwenye Halmashauri, maeneo ambayo sisi tunayasimamia bila maamuzi ya vikao, bila kusimamiwa na wataalam au hata na kamati fulani ya madiwani wakaanzisha tu operation hivi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunawapa madaraka makubwa ambayo hayastahili, sisi ndio wenye Halmashauri na hawa ni waajiriwa wa Halmashauri, lazima kila operation inayofanyika kwa nia nzuri ya kuwatoa watu ambao wanavunja mahususi ya Halmashauri, hakika ni lazima tuhakikishe kwamba tunasimamia zoezi hilo na si kuliacha likafanyika kiholela.
Mheshimiwa Spika, yanayofanyika mengi ni makosa ya sisi Halmashauri kuwaruhusu wale kuwa na mamlaka makubwa na kufanya operation bila kuwasimamia.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zama hizi tumeona askari wakifanya mazoezi katika barabara wakiwa na silaha za moto na kwa mujibu wa sheria vikosi vyote vya ulinzi na usalama wana maeneo yao maalum ya kufanyia mazoezi. Je, Serikali haioni kwamba wanawapa maadui nafasi kuona udhaifu wa askari wetu na kuingiza maadui kupambana na vyombo vya ulinzi na usalama? Ni kwa nini vyombo hivi visibaki sehemu zao za kufanyia mazoezi huko huko vilikopangiwa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza vikosi vya ulinzi na usalama kufanya mazoezi ni sehemu ya maisha yao…
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Na kila siku kwao ni mazoezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili alilosema kwamba kufanya mazoezi barabarani wanawafanya maadui wajue udhaifu wao, nimwambie tu mazoezi yale wanayofanyia barabarani ni ya viuongo na ni sehemu tu ndogo kati ya yale mazoezi makubwa wanayofanya ya kukabiliana na wahalifu. Na mimi niseme tu kwamba kwa mwananchi yeyote ambaye havunji sheria hana haja ya kushtuka anapoona askari wanafanya mazoezi. Wanafanya mazoezi hayo kwa ajili ya wahalifu, kwa hiyo, kama siyo mhalifu huna haja ya kuwa na mashaka.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Zanzibar kumekuwa na matukio ambayo yanaendeshwa na vikosi vya Janjaweed; na kama Kikosi cha Polisi mna taarifa hiyo, ni kwa nini kikosi hiki kimekuwa kikifanya matukio ya kuumiza wananchi na kuwasababishia ulemavu wa kuendelea na hata kutokujitafutia riziki kwa mahitaji yao ya kila siku?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali kipindi cha uchaguzi kunakuwa na matukio mengi sana ya kupiga wananchi ambao hawana silaha na mnapambana nao na kuwaachia ulemavu wa kudumu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Maryam Msabaha anataka kujua kwamba kuna Kikundi cha Janjaweed ambacho kinapiga watu. Niseme tu kwamba kikundi cha Janjaweed mimi sikielewi. Ninachoweza kusema ni kwamba, kama Mheshimiwa Mbunge ana taarifa za kikundi chochote ambacho kinavunja sheria za nchi, basi ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anashirikiana na nchi kufikisha taarifa hizo kwa Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Polisi kupiga watu wakati wa uchaguzi, Polisi imefanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba uchaguzi wetu unakwenda vizuri na sote ni mashahidi kwamba uchaguzi wa mwanzo na uchaguzi wa marudio Zanzibar ulikwenda kwa salama na amani na wananchi walitumia haki yao kidemokrasia vizuri kuchagua wale ambao wameamua wenyewe kuwachagua. Kwa hiyo, siyo sahihi kusema kwamba uchaguzi ulikwenda vibaya na Polisi wameshiriki katika kufanya uvunjifu wa sheria katika uchaguzi huo.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana. Nami naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, hili tatizo la matundu ya choo hasa shule ambazo ziko pembezoni, shule za vijijini siyo rafiki sana na watoto wa kike pamoja na wanafunzi kwa ujumla. Ni lini Serikali itahakikisha tatizo hili la matundu ya choo linakwisha mara moja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MTAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la dada yangu Maryam Msabaha Mwanajeshi kutoka kambi ya Bulombora kule Mkoani Kagera kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali kwamba mpango mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo la vyoo kama Mheshimiwa Molel alivyoanza na swali hili. Nilipopita maeneo mbalimbali kwa mfano takriban wiki moja na nusu nilikuwa katika Wilaya ya Kakonko, Buhigwe na maeneo mengine kule, nilipita katika maeneo hayo nikikagua hata baadhi ya miundombinu ya vyoo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna kila sababu, ndiyo maana tuna mpango mkakati mpana sana. Tumetenga fedha karibu bilioni 12, lengo kubwa ni investment katika kuondoa kero hii. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Serikali kwa umoja wake lakini vilevile na wadau mbalimbali niwashukuru sana, katika kipindi hiki tumeweza kushirikiana vema kwa sababu baada ya kuondoa ajenda ya tatizo la madawati, sasa hivi Serikali na wadau mbalimbali tumejielekeza katika vyoo na vyumba vya madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imani yangu ni kwamba ndani ya muda mfupi tutaona mazingira makubwa sana yamebadilika katika sekta ya elimu katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na tabia ya wananchi au vyombo vya ulinzi na usalama na wengine ambao wanakwenda kwenye mafunzo ambayo siyo halali kutesa raia wasiokuwa na hatia na kuwasababishia maumivu makali na hatimaye kupelekwa rumande bila kupatiwa huduma za kiafya. Je, Serikali hamuoni kama mnavunja haki za binadamu na utawala bora?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Maryam Msabaha liko too general, nadhani si sahihi kusema Polisi kazi yao ni kutesa raia. Polisi wamekuwa wakifanya kazi ya kulinda raia na kazi hii imefanyika kwa mafanikio makubwa sana na ndiyo maana mpaka leo nchi yetu iko salama. Ningemwomba Mheshimiwa Maryam Msabaha kama ana tukio specific ambalo linamhusisha Polisi kwa kufanya tendo lolote ambalo limekwenda kinyume na sheria basi aliwasilishe ili hatua zichukuliwe.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda na mimi nimuulize Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa hii michezo ya kamari imekuwa ikichezwa kwenye stendi kubwa na sehemu za starehe na kupelekea watu kufilisika na wengine kufikia hatua hata ya kujiua. Je, hamwoni sasa ni wakati muafaka wa kukataza michezo hii isichezwe na wale wanaochezesha michezo hii wachukuliwe hatua?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema michezo hii ipo kisheria, sisi kama Wizara hatuwezi kuisitisha. Tutafanya utafiti ili tuone kama inahitajika kuleta sheria mpya Bungeni ili tufanye hivyo. Hata hivyo, tusisahau kama nilivyosema michezo hii ni sawa na michezo mingine pale inaposimamiwa vizuri na sisi tuna uhakika inasimamiwa vizuri. Kwa mfano, kwa mwaka jana 2016 mchezo huu ulichangia zaidi ya shilingi bilioni 2.1 katika mapato yetu. Hivyo, niombe tu kama jamii na kama Taifa tuweze kuwasimamia vizuri vijana wetu ili yale madhara hasi yasiweze kupatikana.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, na mimi naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa wajasirimali wadogo wadogo hasa mama lishe na wamachinga na ambao wengine wana vipato vya chini wamekuwa wakikopa mikopo kwa ajili ya biashara zao na kutozwa riba kubwa na kushindwa kurejesha mikopo ile na kufilisiwa.
Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha inatafuta fedha kwa ajili ya Wajasiriamal wadogo wadogo na kuwatoza riba ambayo inaendana na biashara zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nilikumbushe Bunge lako tukufu kwamba tayari Serikali imeshatunga sera ya huduma ndogo za fedha za mwaka 2016 na sasa tupo katika hatua nzuri kuja na sheria katika Bunge lako tukufu ili kuwalinda wajasiriamali wadogo wanaokopeshwa kwa riba kubwa. Ni imani yangu sheria hii itakapokuwa imepitishwa watakopa katika viwango halisi ambavyo viko sokoni na sivyo ambavyo wanaonewa kwa sasa.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Nami naomba nimuulize Naibu Waziri swali
dogo la nyongeza. Kwa kuwa ongezeko la watoto wa
mitaani linachangiwa na akinababa kukataa mimba na
kukataa familia zao. Je, Serikali inaweza kusema mpaka sasa
hivi ni akinababa wangapi wameshatiwa hatiani na
kufunguliwa mashtaka ili kutunza familia zao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza hatuna takwimu sahihi za watu waliochukuliwa hatua kwa kukataa mimba. Hata hivyo, nimhakikishie tu kwamba tuko makini katika kufuatilia kesi za namna hiyo ili kuweza kuchukua hatua pindi inapojitokeza.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Watanzania wengi
wanategemea bandari na kumekuwa na ukiritimba wa kutozwa kodi mara kwa mara wafanyabiashara sasa hivi wanakwepa bandari zetu, je, Serikali ina mikakati gani kuweka utaratibu mzuri wa utozaji kodi katika mizigo ya wafanyabiashara ili biashara zipate kupita katika bandari zetu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi kwamba upangaji wa bei na hiki kitabu ambacho kinatumika na watu wa TPA wakati kinaandaliwa
kabla hakijapitishwa huwa kinashirikisha wadau wa bandari. Labda tu nimhakikishie kwamba tutakapofika muda wa kureview hizi rates tutahakikisha wadau tunawashirikisha tena,
inawezekana dynamics zimebadilika kwamba mazingira ya wakati bei hizi zinapangwa ni tofauti na mazingira ya sasa. Tutamshirikisha na nitaomba sana comments zako na wadau
waziweke ili tupate kitabu kipya ambacho kitazingatia hayo ambayo wewe umeyasema na Mheshimiwa aliyeuliza swali la msingi ameyasema.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi naomba nimwulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa kuna wananchi ambao wanakamatwa kwa uhalifu mbalimbali, aidha wa kubandikiziwa kesi na kupata kipigo kikali sana na kufanyiwa majeraha kwenye miili yao na kufikishwa kwenye vyombo vya mahabusu bila kupatiwa huduma za afya, hamuoni kama mnakiuka haki za binadamu?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kama jambo hilo limetokea Zanzibar, pia kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, vitendo hivyo ni vitendo vya kukiuka Katiba kama vimetokea. Kwa yule viliyemtokea kama vimemtokea; moja, anayo nafasi ya kuiambia Mahakama ameteswa au amefanywa hivyo na hatua kuchukuliwa. Pia kuchukua hatua hizo kuziarifu mamlaka nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ushahidi upo kama ilivyovyoelezwa, Serikali na vyombo vyake inao utaratibu wa kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo ambavyo Katiba yenyewe imevizuia, sheria imevizuia, lakini hiyo haina maana hakuna binadamu wanaofanya hayo. Tumepewa amri kumi na Mwenyezi Mungu, mara nyingi tunazihalifu, lakini haina maana kwamba hazipo. Kwa hiyo, yakitokea hayo, tuarifiwe.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba kumuuliza Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna migodi ambayo inakuwa imeshafungwa na inakuwa si salama kwa wachimbaji wadogowadogo na hawa wachimbaji wadogowadogo wamekuwa wakikiuka sheria na kuvamia migodi hii na kuhatarisha maisha yao. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha uvamizi huu wa wachimbaji wadogowadogo unakwisha na kuchukulia hatua za kisheria?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya 2010, hairuhusiwi kufanya uchimbaji wowote bila leseni na kwa hiyo uvamizi kwa hali ya kawaida hauruhusiwi. Hata hivyo, yapo mazingira ambapo wananchi wamekuwa wakivamia maeneo na hasa ambao wao wameanza kuchimba mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu na mkakati wa Serikali, kwanza ni kufanya mazungumzo na hao wachimbaji wadogo kuwaelewesha lakini hata wale wenye leseni ambao wameyashikilia bila kuyaendeleza nao kuzungumza nao. Tunachofanya sasa, maeneo ambayo yanachukuliwa na watafiti bila kuyaendeleza Serikali inayachukua na kuwagawia wachimbaji maalum wadogo kwa utaratibu wa kisheria ili kufanya uchimbaji huu uwe wa manufaa kwa wachimbaji wadogo pamoja na wachimbaji wakubwa.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sambamba na kuokoa tatizo la akina mama katika uzazi salama bado akina mama hao wamekuwa wamachinga wa kubeba vifaa mbalimbali wakati wa kwenda kujifungua. Je, kama Serikali mnatambua tatizo hili ni lini Serikali mnahakikisha mnatenga bajeti ya kutosha katika hospitali zote za akina mama na akina mama wakifika kule kujifungua wapate huduma salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba kwanza nimesema kwenye jibu la msingi kwamba kuanzia mwaka wa fedha unaoendelea sasa hivi tuliweka bajeti ya kununua delivery packs ambayo itakuwa ina vifaa vyote vya kujifungulia kuanzia mackintosh kuja catgut na vitu vingine vyote vinavyopaswa kujifungulia, nguo zile za kujifungulia, sterile gown kwa ajili ya kumsaidia mama wakati wa kujifungua, na tutawagawia akina mama laki tano. Lakini pia kwenye bajeti ya mwaka huu tunavyo vifaa vingine (delivery packs) milioni moja, kwa hivyo katika akina mama 1,900,000 ambao wanajifungua kila mwaka tutakuwa tuna vifaa vinavyokaribia 1,500,000, lakini sio wote ambao watahitaji vifaa hivyo. Kwa hiyo, tutavigawa kwa watu ambao wana mahitaji kwa hivyo ni jambo ambalo tumekwisha kulitazama.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Naibu Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imekuwa kisiwa cha amani, lakini kuna genge la wahuni ambalo hatujui wanapata wapi silaha za kijeshi na kushambulia raia wasiokuwa na hatia.
Je, Serikali haioni sasa imefika wakati muafaka kufanya doria katika sehemu zote za mipaka na barabarani na hata katika vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha genge hili halina nguvu kwa sababu linachafua taswira ya Tanzania katika medali za kitaifa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa bado silaha hizi zinaendelea kuuzwa sehemu za starehe kama vile minadani na sehemu mbalimbali na kuhatarisha amani ya ambao wanafika katika kupata huduma katika sehemu hizo.
Je, Serikali ina mikakati gani ya ziada kuhakikisha suala hili kuuza silaha holela linakomeshwa na wale wanaokamatwa wachukuliwe sheria kali ili suala hili likome mara moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni bahati mbaya sana Mheshimiwa Mbunge hajalitaja jina la kundi ambalo amelizungumza, lakini kimsingi nataka nimueleze tu kwa ufupi kwamba hali ya matumizi ya silaha kufanya uhalifu nchini imepungua, ndiyo maana hata ukiangalia takwimu tokea Juni, 2016 mpaka Agosti, 2017, hakuna matukio makubwa ya mauaji ya kutumia silaha za jadi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utaona ni kazi kubwa ambayo Serikali imefanya kupitia Jeshi la Polisi kuweza kudhibiti wahalifu na magenge mbalimbali ambayo yamekuwa yakitumia silaha hizo za jadi kwa ajili ya kufanya uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba mafaniko hayo yamepatikana kwa sababu gani? Kuna mikakati mingi ambayo imefanyika ili kuweza kufikia malengo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tumeendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusiana na makundi ambayo yamekuwa yakijitokeza, kwa mfano, maeneo ya Kanda ya Ziwa kuna watu walikuwa wanaitwa wakata mapanga, ukija huku Mbeya na kadhalika, wapo watu ambao walikuwa wanafanya mauaji kwa vikongwe kwa imani za kishirikina. Kwa hiyo, Jeshi la Polisi kwa kupitia utaratibu wake wa ulinzi shirikishi tumekuwa tukifanya jitihada kubwa sana za kutoa elimu kwa jamii ili kufahamu madhara ya matumizi ya silaha za jadi, hasa matumizi ya kujichukulia sheria mkononi kwa jamii, hilo moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, tumekuwa tukiendelea kufanya doria na ukaguzi barabarani kuweza kusimamisha magari na watu ambao wakipita na silaha hizo za jadi na kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria. Hii doria imekuwa ikiendelea na ndiyo maana mpaka sasa hivi tumeweza kufanikiwa kwa mujibu wa takwimu ambazo nimezieleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeendelea kuhakikisha kwamba huduma zetu za Jeshi la Polisi zinashuka katika ngazi ya Tarafa na Kata. Tuna Ofisi za Ukaguzi katika ngazi ya Tarafa na Kata ili kusogeza huduma ya Polisi karibu na wananchi kuweza kukabiliana na matukio mbalimbali ya uhalifu ya aina kama hii ambayo Mheshimiwa Mbunge amezungumza. Kwa hiyo, nikiri tu kwamba kwa jumla kazi kubwa imefanyika na mafanikio yake mpaka sasa hivi ndiyo haya ambayo nimeyaeleza, ni makubwa ya kuridhisha kwa kiasi fulani.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa vijana wengi wamekuwa wakijiajiri kwa kupitia uvuvi wa bahari kuu, lakini vijana hawa hawana mitaji ya kuendeleza sekta hii ya uvuvi.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha vijana hawa wanapatiwa angalau mikopo ya bei nafuu ili wapate kujiendeleza katika sekta hii ya uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vijana kufanya uvuvi katika bahari kuu, taarifa tulizonazo ni kwamba hakuna vijana wanaofanya uvuvi katika bahari kuu. Bahari kuu ni suala lingine, ni gumu kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na vijana wanaojishughulisha na uvuvi katika maji ya kawaida na maji ya Kitaifa tunafahamu. Zanzibar mradi wa Sawfish umetoa dola milioni 11 kwa ajili ya kuwezesha wananchi wajishughulishe na shughuli za uvuvi. Labda Mheshimiwa Mbunge tunaweza tukaonana tukitoka hapa leo nimhabarishe na nimpe taarifa vizuri zaidi ili aangalie namna ya kuwasaidia vijana wake wawekeze katika uvuvi.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika Ziwa Tanganyika kumekuwa na tatizo la wavuvi wengi kuvamiwa hasa kutoka nchi za jirani kama Congo, wale wavuvi wamekuwa wakipata shida sana. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha hawa wavuvi wanaotoka upande wa Kigoma nao angalau wanaridhika na rasilimali zao na kutokunyanyaswa na raia ambao wanatoka Congo na nchi jirani za Burundi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu mojawapo ya kufanya ukaguzi ni pamoja na kuvisajili vyombo hivyo ili vipate uraia kwa sababu mara nyingi vyombo hivi vinapotumika kwenye maji siyo rahisi kujua hapa umevuka mpaka au hapa uko ndani ya nchi yako. Kwa hiyo, usajili wa vyombo hivi ni muhimu sana na vikishasajiliwa vinatambulika kwamba hiki ni chombo cha Tanzania, hiki chombo cha Burundi, hiki chombo cha DRC tunapokutana katika maeneo yale ya Ziwa Tanganyika. Hiyo ndiyo silaha pekee ya kuiwezesha nchi yetu, kwanza wale maadui kutambua kwamba wanamgusa raia wa Tanzania na hivyo Serikali ya Tanzania inaweza kuwa tayari kumtetea mtu huyo. Kwa hiyo, njia mojawapo ya utetezi ni hiyo ya kuvisajili vyombo hivyo na tukiishavisajili tunafanya shughuli za doria mara kwa mara katika ziwa lile na nadhani Mheshimiwa Mbunge atakuwa amewahi kuona matokeo mazuri ya doria zinazofanywa katika Ziwa Tangayika katika kuhakikisha kwamba wavuvi wa Tanzania wanakuwa salama.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Na mimi naomba nimuulize Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Ziwa Tanganyika kulikuwa na uharamia, wale wavuvi walikuwa wakivamiwa na maharamia kutoka nchi za jirani na kuwapokonya nyavu zao na hata mitumbwi yao. Je, Serikali imedhibiti vipi maharamia hawa katika Ziwa Tanganyika?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba wavuvi wetu wa Ziwa Tanganyika na hata wavuvi katika Ziwa Victoria wamekuwa wakivamiwa na maharamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie kwamba Serikali imepata taarifa hizi na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimejipanga ipasavyo kuhakikisha wavuvi wetu wanalindwa ili waweze kufanya shughuli zao za uvuvi kama kawaida bila ya hofu yoyote.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi nipate kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kumekuwa na tatizo la watoto wa mitaani hasa kwenye miji mikubwa kwa mfano, Arusha, Mwanza, Dar es Salaam na kadhalika na watoto hawa wamekuwa wakitumiwa kwenye masuala ya uhalifu kama madawa ya kulevya na kadhalika. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha watoto hawa wanarudi shuleni na kupata angalau malezi bora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali tunakiri tumekuwa na tatizo hilo na moja ya jambo ambalo tumelifanya kwanza ni kubaini idadi ya watoto katika hii miji mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika takwimu tulizokuwa nazo sasa hivi katika Mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Iringa, Mbeya, Dodoma na Arusha tuliweza kubaini watoto 7,748 ambapo 6,365 walibainika kwamba wanashinda mitaani na kurudi nyumbani na watoto 1,383 hushinda na kulala mitaani. Pamoja na juhudi hizo, Serikali kati ya mwezi Julai, 2017 mpaka Novemba, 2017 tuliweza kuwaunganisha watoto 952 na kuwarejesha katika familia zao.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kuwa haya maswali tumekuwa mara kwa mara tunauliza na hakuna utekelezaji. Je, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri nusu mwaka wa fedha unakwishwa. Ni majengo mangapi yamekarabatiwa kwa upande wa Zanzibar na ni vituo vingapi vya kambi vya Kambi za Jeshi kwa upande wa Zanzibar vimekarabatiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa hivi vituo vya afya tunavyoviulizia ambavyo vipo kwenye makambi ya Jeshi havihudumii tu majeshi na familia zao, zinahudumia pia na jamii zilizowazunguka na hasa hichi kituo nilichokiulizia kiko sehemu ambapo ajali zinatokea mara kwa mara.
Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha vituo vyote vya majeshi vinapata dawa kwa wakati muafaka na sitahiki zinazofaa kwa wakati muafaka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilivyojibu katika majibu ya msingi kwamba kwa bajeti ya mwaka 2018/2019 Serikali imeazimia kuvifanyia ukarabati vituo vyote ikiwemo vya Zanzibar na kikiwemo hiki cha kwenye Brigedi ya Nyuki, Migombani. Kwa hiyo, mwaka wa fedha 2018/2019 bado haujaisha kadri ambavyo fedha kama ambavyo nimesema zitapatikana basi vituo hivi pamoja na hiki cha Migombani vitafanyiwa ukarabati. Sambamba na kuvipatia huduma nyingine muhimu kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa kwa hatua za awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ikumbukwe kwamba vituo hivi kwa kawaida vinatumika kwa ajili ya kutoa huduma za awali kabla ya kuweza kuwapeleka wagonjwa wenye matibabu makubwa katika Hospitali za Kikanda kwa upande wa Zanzibar ikiwemo Hospitali ya Jeshi ya Bububu.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, na mimi naomba kumuuliza Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya vituo vingi Zanzibar ni vibovu na majengo ni chakavu na askari hawana vitendea kazi wanapokamata wahalifu kama wino wa kuchapisha barua na mahitaji mengine muhimu na hata wahalifu wale hawapati hata mkate kwa sababu siyo wahalifu wote wana jamaa wa kwenda kuwaangalia kwenye vituo vya polisi wanapokuwa mahabusu.
Je, ni lini Serikali itahakikisha vituo vyote vinapatiwa huduma stahiki za kuendesha kazi zao kwa wakati muafaka.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pale ambapo Serikali itapata uwezo wa kifedha.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa vijana wetu wanaanza vipaji wakiwa mashuleni, je, Serikali ina mpango gani kuipa sekta ya michezo hasa mashuleni ili angalau vijana hao tuwakuze katika vipaji vya michezo ili tuweze kufikia kama nchi ya Brazil?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri ambalo ameuliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Wizara kupitia Serikali tuna mpango mzuri sana wa kuhakikisha kwamba vijana wetu waliopo shuleni wanashiriki katika michezo. Sasa hivi ninavyoongea tayari Wizara kwa kushirikiana na Serikali tumesharejesha ile michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA katika mashule yetu. Haya ni mashindano ambayo kwa kiasi kikubwa sana yanasaidia kuibua vipaji vya vijana. Tumeshuhudia kwamba michezo hiyo inakwenda vizuri na wanafunzi wengi wamekuwa wakishiriki na vipaji vingi vya vijana vimeendelea kujitokeza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikutoe hofu kwamba Wizara tuna mikakati mizuri na tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kwamba tunaedelea kuinua vipaji vya vijana wetu ambao wapo mashuleni, ahsante sana.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Mwenyezi Mungu akupe wepesi katika siku hii ya leo kwa sababu Wabunge umewafurahisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Waziri, kuna watu wanafanya makusudi kabisa kuambukiza wenzao ugonjwa huu. Mtu anajua kama ni muathirika wa UKIMWI lakini anambukiza watu kwa makusudi hata watoto wadogo ambao ni wanafunzi wa vyuo. Je, Serikali ina mikakati gani kwa hawa ambao wanafanya maambukizi ya makusudi kwa wanafunzi wa vyuo na hata kwa ambao hawajaambukizwa maradhi haya? Naomba tamko la Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Bunge lako Tukufu palitungwa sheria ambayo inatoa adhabu kwa watu ambao wataambukiza wengine Virusi vya UKIMWI kwa makusudi huku wakijua kwamba wana Virusi vya UKIMWI. Kwa hivyo, ili sheria hii iweze kufanya kazi ni watu kuripoti kwamba wameambukizwa Virusi vya UKIMWI kwa makusudi. Watakaporipoti, mkondo wa sheria utafuata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, kwanza watu wenyewe wapime, kwa mfano wewe unazungumzia mabinti, maana yake mabinti wapime wajue hali zao. Wakishajua hali zao hata ikitokea ameambukizwa na mtu ambaye hakupima naye anaweza akasema wewe ndiyo umeniambukiza kwa sababu mimi nilikuwa sina maambukizi. Kwa hivyo, wapime wajue hali zao na waweze kutumia kinga kama hawawezi kuacha kufanya ngono, lakini kama wanaenda kuoana basi wapime kila mtu ajue hali wakate wanaoana ili wasiambukizane bila kujua.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nipate kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa watumishi wengi wa Serikali wamehamishiwa Mkoa wa Dodoma, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha watumishi wote wa Serikali wanapata nyumba na waache kuhangaika hangaika mitaani kwa sababu nyumba za National Housing hazitoshi kwa watumishi wa Serikali waliohamishiwa Dodoma?
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mate wangu wa Bulombora dada yangu Mheshimiwa Maryam Msabaha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli, ni nia njema Serikali. Tumesema kwamba Serikali ya Awamu ya tano si mlimila dole, kwamba inatekeleza kile ilichokiahidi; imesema tunaamia Dodoma na tumehamia sasa hivi Dodoma. Naomba niwahakikishie kwamba Serikali imeweka mipango vizuri kupitia nyumba za TBA, National Housing na CDA. Mkiangalia kule kama mnapita Iringa Road zimekarabatiwa, lengo lake kubwa ni kwamba kuweza kuwa-accommodate watumishi wote wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunashukuru sana kwa suala hili zuri, Serikali imeweka mpango vizuri. Niwaahakikishie watumishi wote kwamba msiwe na hofu mtakapokuja Dodoma, Serikali inapanga mipango mizuri, na ndiyo maana hata National Housing sasa wanajenga huu mji mpya pale. Hii yote ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kwenye mchakato huu wa Mji Mkuu wa Serikali kuhamia Dodoma, Dodoma iweze ku-accommodate watumishi hawa wanaokuja hapa.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi naomba nimuulize Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Hospitali za Mikoa ya Dar es Salaam, kwenye wodi za akina mama kumekuwa na msongamano mkubwa sana wa mama wajawazito, wengine wanalala wawili na wengine wanalala chini.
Je, Serikali ina jitihada gani za maksudi kuhakikisha hizi wodi za akina mama zinakuwa na mpangilio maalum, mama mjamzito anavyofikishwa hospitalini apate kitanda cha peke yake, kwa sababu wako wawili na kulala watu wawili pia inachangia kuambukiza maradhi? Je, Serikali ina mkakati gani…
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaboresha mnyororo wa utoaji wa huduma za afya kwa kuboresha mifumo ya rufaa na moja ya mikakati ni hii ambayo tumeendelea kuisema na nimeigusia hapa kuboresha vituo vya afya, hospitali za Wilaya na hospitali za Rufaa za Mikoa ili ziweze kutoa huduma za uzazi salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema jana, kwangu siyo faraja sana kusikia kwamba wakina mama 100 wamezaa katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili. Tunachotaka kuona pale Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ni case zile ambazo zipo complicated, kesi nyingine zote sasa hivi tumejenga uwezo katika vituo vyetu vya afya, hospitali zetu za Wilaya na Hospitali za Rufaa za Mikoa ili ziweze kutoa huduma. Nitoe rai kwa wananchi kuzitumia hospitali zetu hizi. (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niulize swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri kumekuwa na malalamiko nafasi nyingi za Balozi Wazanzibari wengi wanapelekwa nchi za Kiarabu. Je, kama malalamiko haya ni kweli hamuoni kama sasa kuna umuhimu wa kufanya uwiano sawa ili Wazanzibari wengi wasipelekwe nchi za Kiarabu nao wapelekwe nchi hizi nyingine kama Marekani, Ulaya na kwingineko?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maryam Msabaha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, anasema kwa siku nyingi sana wamekuwa wakilalamika kwamba Watanzania ambao wanatoka Zanzibar wanapoteuliwa kuwa Mabalozi wanapelekwa kwenye nchi za Kiarabu zaidi. Naomba niweke taarifa hii sawa kwamba tunapowateua Mabalozi tunawateua kwa kigezo cha weledi, ufahamu wao na uwezo wao wa kushika nafasi hiyo ya kiubalozi. Tunapowateua kuwapeleka mahali popote iwe ni kwenye nchi za Kiarabu, Afrika, Ulaya au Latin America wako sawa kabisa kwa status.
Mheshimiwa Spika, nimwambie tu siyo tu kwamba katika hizi nchi za Kiarabu wako Watanzania ambao wanatoka Zanzibar yaani Mabolozi ambao wanatoka Zanzibar tu wapo pia wameteuliwa na wamekwenda huko wanatoka pia Tanzania Bara. Naomba hisia hizo za kusema kwamba tunawapeleka Mabalozi kwenye nchi za Kiarabu wale tu ambao wanaotoka Zanzibar zitolewe.
Mheshimiwa Spika, vilevile niseme tu kwamba sisi tunapowapeleka Mabalozi mahali popote iwe nchi za Kiarabu, tunaangalia pia additional value ambayo anaweza akaifanya. Sisi tunapowapima wale ambao pengine wanatoka Zanzibar au Bara tunajua kabisa kwamba kwa kufanya kazi kule watasimamia maslahi ya Taifa na maslahi wa nchi hii kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, wako Watanzania Mabalozi ambao wanatoka Tanzania Bara wameteuliwa hivi karibuni na wamekwenda kule. Nafasi hiyo itaendelea kufanywa hivyo na wale wanaotoka Zanzibar na wao ikifika wakati tunaweza tukawachukua tukawapeleka sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba hakuna upendeleo wala dharau kwamba wanapopelekwa kwenye nchi za Kiarabu maana yake kwamba tumewaonea na wanafanya kazi nzuri. (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba na mimi nimuulize Mheshimiwa Naibu swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyeiti, kwa kuwa machinjio ya Mazizini ni machafu sana na mazingira yake yako tete na yanahatarisha hata maisha ya watumiaji na Halmashauri pia haipati mapato kutokana na machinjio hayo. Je, Serikali ina mikakati gani kuboresha machinjio haya ya Mazizini ili na Halmashauri nayo ipate kipato?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba naomba tu nijibu kwa ujumla kwa sababu sijafahamu kwamba hayo machinjio ya Mazizini anazungumzia Halmashauri gani, lakini naomba nimhakikishie kwamba Wizara yetu imeendelea kuhakikisha kwamba machinjio yote yawe safi. Ndiyo maana sasa hivi tuna operation maalum ya ukaguzi ya kuhakikisha tunaweka utaratibu mzuri wa tasnia nzima ya mifugo ya nyama kuanzia katika machinjio na hata huko katika minada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tumekuwa tukilifanyia usimamizi wa karibu kabisa ili tuweze kupata ithibati ya nyama yetu kwa sababu biashara hii ya nyama haiishii kwetu sisi wenyewe, ni sheria za kimataifa zinazoongozwa na Shirika la Kimataifa la Mifugo (OIE). Kwa hiyo, tunasimamia vizuri na nataka nimhakikishie tutafika Mazizini na kuhakikisha ya kwamba machinjio yale yanakuwa ya viwango kwa maana ya usafi ili nyama yetu inayotoka pale iweze kuwa bora wa mlaji.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa hali ya utalii kwa sasa hivi imeshuka kutoka asilimia 12.9 na kufika asilimia 3.3 na Mji wa Bagamoyo wanategemea uvuvi na utalii na kuonekanika mahoteli mengi ya kitalii ya Bagamoyo kukosa wageni, je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha inatangaza vituo vya utalii vya Bagamoyo na kuangalia ni tatizo gani lililofanya kushuka kwa asilimia hii ya utalii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa majengo ya kale ya mji mkongwe wa Bagamoyo yamekuwa yanabomolewa na ramani za majengo yale yanatoweka ambapo yalikuwa ni kivutio sana kwa utalii, lakini ramani zile za kale zinapotea na kujengwa katika miundombinu mingine tofauti, je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha majengo yale yanaboreshwa kurudi katika hali ile ya mji mkongwe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya utalii kwamba imeshuka kutoka asilimia 12 hadi asilimia tatu katika eneo la Bagamoyo, hii kwa kweli inahitaji labda nipitie takwimu vizuri. Kilichojitokeza zaidi ni kwamba katika hoteli nyingi za kitalii zile za Bagamoyo zilikuwa zinategemea sana uendeshwaji wake wa mikutano, yaani utalii ule wa mikutano ambao ulikuwa unaendeshwa sana Bagamoyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi sasa mikutano mingi imepungua kutokana na mabadiliko ya hali ya uchumi. Hata hivyo, kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Wizara imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuamua kuchukua mashirika yetu yaliyoko chini ya Wizara ili yaweze kukabidhiwa hii dhamana ya kutangaza maeneo yote yaliyoko Bagamoyo ikiwemo na ile Hifadhi nyingine ya Saadan kusudi iweze kuvutia watalii zaidi waendelee kuwepo na kuongezeka kule Bagamoyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu majengo ambayo yamekuwa yakiharibiwa na kubomolewa ramani zao zile za awali, ni azma ya Serikali kuendelea kuwahamasisha wananchi wanayoyamiliki hayo majengo kuhakikisha kwamba wanafuata taratibu za kurudishia ujenzi uliokuwepo kabla. Kwa sababu katika eneo lile tunataka majengo yale yaendelee kuwa na ramani na sura iliyokuwa inaonekana toka awali ili iendelee kuwa kivutio kwa upande wa wageni.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Na mimi naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, sambamba na Mahakama nyingi kuwa chakavu na wale wazee wa Mahakama maslahi yao ni duni, ni lini Serikali itakarabati Mahakama zote na kuboresha stahiki za wazee wale?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, moja, Mahakama inatekeleza mpango wa miaka kumi wa ukarabati na ujenzi wa Mahakama zote. Baada ya Bunge leo anione ili niweze kumpa mpango wote wa miaka kumi, lakini tuonane hapa hapa Bungeni. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, pili, wazee wa Mahakama, tutaangalia maslahi yao ili yazidi kuboreshwa.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi naomba nimuulize Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa mashamba mengi ya mkonge yalikuwa wanamilikiwa na wakulima wale wahifadhi wa mikonge. Lakini mashamba yale yamekuwa Mashamba pori na wananchi wengi na hasa wa hususa wananchi wa Korogwe wanahangaika mashamba ya kulima na mashamba yale hayaendelezwi. Je, Serikali ina mpango gani kurudisha mashamba haya kwa wananchi wa Korogwe ili nao wapate kulima?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake anataka kujua ni lini pengine yale mashamba ambayo yamekuwa mashamba pori hayaendelezwi tuweze kuyarejesha pengine kwa wananchi waweze kuyatumia.
Napenda tu nilifahamishe Bunge lako suala la kutambua shamba hili ni shamba pori, halijaendelezwa na limekiuka taratibu jukumu hilo analo Afisa Ardhi Mteule katika Halmashauri husika. Kwa hiyo ni jukumu la Halmashauri husika kuanza kufanya zile hatua za awali za kuweza kuchukua taratibu zote za kisheria, kuweza kuona kwamba huyu mtu amekiuka taratibu zake basi utaratibu wa kumnyang’anya unafuata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niwaombe sana kwa sababu tulishasema, ni jukumu la Halmashauri sisi kama Wizara mkishakamilisha kazi yetu ni kumshauri Mheshimiwa Rais kuweza kuyafuta na yanarudi kupangiwa matumizi. Lakini pia kwa nafasi hii nitoe rai mashamba yote yale ambayo yanafutwa na Mheshimiwa Rais, yakirudishwa katika maeneo yetu msiyapangie matumizi ya makazi mashamba yote kwa sababu sasa hivi unajikutakwamba hata pale ambapo panahitaji kuendeleza kilimo watu wanagawana mashamba. Kinachotakiwa eneo lile likisharudishwa lazima pawekewe mpango mzuri wa matumizi. Kama linaendelea kuwa shamba basi tuweze kujua ni mwekezaji yupi atafanya kazi hiyo, au kama mnabadilisha matumizi kwa sababu mengine yanakuwa yameshavamiwa na wananchi basi pia tuwe na utaratibu wa kuwa na akiba ya ardhi kwa baadae, lakini tuwe pia na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji, ili tena tusije tukapata shida, Kwa sababu ardhi haiongezeki na watu wanaongezeka. Kwa hiyo ni jukumu la kila Halmashauri kuona namna bora ya kutumia Wizara tupo kwa ajili ya kutoa ushauri, kwa ajili kutoa Wataalam kuweza kufanikisha azma ya Halmashauri.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa na mimi fursa ya kuuliza swali la nyongeza:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vivuko vya Kigamboni vimekuwa vikiharibika mara kwa mara; je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha inavitengeneza vivuko hivi ili kuondosha maafa yasitokee kwa wananchi ambao wanavitumia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia TEMESA Serikali imeendelea kuvihudumia vivuko mbalimbali vilivyopo nchini kwetu kuhakikisha vinafanya kazi kama vinavyotakiwa.
Mimi nina taarifa kwamba hicho kivuko kilikuwa na hitilafu kidogo na ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kufuatilia baada ya muda, hata tukitoka nje tutawasiliana na watu wa TEMESA kuona kuna changamoto gani kwenye hicho kivuko ili ziweze kutatuliwa. Ahsante.
MHE. MARYAM S. MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kumuuliza Naibu Waziri suala dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna watu wazima ambao wana akili zao timamu na wana kazi zao, lakini wamekuwa wakikiuka maadili na kuwachukua hawa mabinti wakiwa katika umri mdogo na sana kuwazalisha watoto na kuongeza ongezeko la watoto wa mitaani. Je, Serikali ina mikakati gani kuchukua sheria na mikakati ili kuhakikisha tunakomesha vitendo hivi na hawa watoto wa kike kupata haki zao stahiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) : Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria imeeleza vyema ni katika mazingira gani mtoto wa kike anaweza kuolewa na kinyume chake maana yake ni kosa linatengenezwa. Kwa hiyo, kwa wale wote ambao wanafanya vitendo hivyo vya kukiuka sheria, sheria zetu zipo, watachukuliwa hatua na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria ili haki ionekane imetendeka kwa mtoto huyu ambaye anakuwa amekatishwa shughuli mbalimbali ikiwemo masomo.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Naibu Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, pamoja na Serikali kutoa elimu katika sekta hii ya vyuo vya utalii, lakini wamekuwa wakichukua wanafunzi ambao wamefeli au wanapata division four na kutofanya vizuri katika vyuo vingi na kusababisha hoteli nyingi za kitalii kuajiri wafanyakazi kutoka nje. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha vyuo vya utalii ili kuhakikisha wanachukua wale wanafunzi ambao wanafanya vizuri ili sekta hii iweze kufanya vizuri katika anga za kimataifa na hapa nchini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wenzetu Kenya, kwa mfano unatokea London unafika Airport ya Kenya, watalii wengi wanashuka sana Kenya na unaona ni namna gani wenzetu wamejitangaza katika sekta hii ya utalii na kupunguza tozo katika suala la utalii. Nauliza Serikali, je, haini sasa kuna umuhimu wa kupunguza kodi katika sekta hizi za utalii ili tuweze kufanya vizuri na kuingiza Pato la Taifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kumekuwa na upungufu wa wataalam katika Sekta hii ya Utalii na ndiyo maana kwa kuliona hilo, Serikali imechukua hatua ya kuhakikisha kwamba kwanza tunakiimarisha chuo chetu cha utalii ili kiweze kutoa mafunzo. Kwa hivi sasa kilikuwa kinatoa mafunzo katika ngazi ya stashahada na astashahada, lakini kuanzia mwaka 2019 kwa ushirikiano pamoja na chuo cha Canada (Vancouver) tumeamua kwamba sasa tuanzishe programme ya kutoa degree, degree hizo zitasaidia kuandaa wataalam mbalimbali ambao watashiriki katika sekta ya utalii. Baadhi ya degree ambazo tunategemea kuzianza ni hizi zifuatazo:-
(i) Digrii ya ukarimu (degree in hospitality operations) ;
(ii) Digrii ya Utalii (degree in travel and tourism management) na
(iii) Digrii ya Utaratibu wa Matukio (degree in events management)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika hizi degree tatu zitakapoanza ni imani yetu kwamba tutakuwa tunaweza kupata wataalam wale ambao sasa watakuwa wanatoka hapa hapa nchini na kuweza kuhudumia vizuri sekta hii ya utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo pia tunawahamasisha wawekezaji katika vyuo vingine vya binafsi waweze kuwekeza katika eneo hili kwa sababu sasa hivi mahitaji bado ni makubwa na wataalam bado ni wachache.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili la kwamba tunachukua wale waliofeli, si kweli. Kwa mujibu wa taratibu zilizopo katika nchi hii, watu wote waliomaliza hata kama yuko division four kama ana ‘D’ nne na kuendelea anaruhusiwa kujifunza na ngazi ya cheti (astashahada) na akifaulu anaendelea katika ngazi ya stashahada. Kwa hiyo, nadhani kwamba mkakati huu bado hatuchukui wale ambao ni failure, tunachukua wale ambao wana sifa za kujiunga na hivi vyuo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili kuhusu kupunguza kodi katika huduma mbalimbali za utalii; ni azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kwamba kodi hizi zinapunguzwa ili wawekezaji na watu mbalimbali waweze kushiriki katika hizi shughuli za utalii; na mmesikiliza katika hatua mbalimbali ambazo tumechukua. Hivi sasa bado tunaendelea kutazama ni aina gani za kodi ambazo zinaweza zikapunguzwa zaidi ili kusudi hii sekta iweze kuimarika zaidi nchini. (Makofi)

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nimependa niongeze majibu ya nyongeza kutokana na majibu mazuri aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada tunazofanya za kuongeza kozi ambazo zinatolewa kwenye Chuo chetu cha Utalii lakini pia tunatambua kwamba sekta ya utalii pamoja na kwamba inaajiri watu zaidi ya 1,500,000 Chuo chetu cha Utalii toka kimeanza kimetoa wahitimu wasiozidi 5,000. Kwa maana hiyo wanaofanya kazi kwenye hoteli si lazima kwamba wanatoka kwenye chuo chetu cha utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua hilo na kwa kutambua kwamba kuna wadau wengine ambao wanatoa taaluma ambazo zinatumika kutoa huduma kwenye sekta ya utalii kama VETA na vyuo vingine ambavyo vimesajiliwa na NACTE, tumeona tuanzishe mtihani wa Kitaifa ambao utaweka standard pamoja zote kwa usawa ili kila anayehitimu atoke kokote kule anakotoka afanye huo mtihani, aingie katika vigezo ambavyo vitakuwa vinatambulika kitaifa na sasa ndiyo aende kuajiriwa kwenye sekta ya utalii. Kwa sababu tunaamini, ili tuweze kupata watalii wengi, ni lazima tuongeze ubora wa huduma tunazotoa ili watalii wapate experience nzuri na wanapoenda kule kwao warudi tena kutalii lakini pia waseme maneno mazuri kwa watu wengine katika cycles of influence zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo pamoja na jitihada hizo, tumetunga kanuni za kufanya certification ya professionals wanaotaka kuajiriwa kwenye sekta ya utalii, lakini pia tunaanzisha mafunzo ya Uanagenzi katika hoteli na maeneo yote ya utalii ili ku-boost kidogo quality ya watoa huduma kwenye Sekta ya Utalii. (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba nimuulize Naibu Waziri swali ndogo la nyongeza. Kwa kuwa hizi barabara zimekuwa zikijengwa kwa gharama kubwa sana, halafu zinaharibika kwa muda mfupi, je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha wakandarasi wote wanaojenga barabara hizi wanachukuliwa hatua na kurudia ujenzi ili kuepusha kutumika tena gharama nyingine ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli kuna baadhi ya maeneo baada ya barabara kutengenezwa zinaharibika, lakini ni hali ya kawaida kwa sababu ziko sababu nyingi ambazo zinaweza kusababisha miundombinu hii kuharibika. Ndiyo maana baada ya ujenzi wa barabara katika kipindi cha maisha ya barabara tunatenga fedha kwa ajili ya kufanya rehabilitation na baada ya miaka 20 tunafanya matengenezo makubwa kwa maana kwamba ule muda wa maisha ya barabara unakuwa umekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali…
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wachimbaji wadogo wadogo wanachangia sana pato la Taifa kwa kulipa kodi na Wizara ya Madini kwa kuongeza kukusanya maduhuli. Je, Serikali ina mikakati gani kurudisha maduhuli haya katika Wizara ya Madini ili kutatua changamoto hasa hizi za wachimbaji wadogo wadogo kupata zana za kisasa za uchimbaji ili waweze kuliingizia tena Serikali pato la Taifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wale ambao walikopeshwa ruzuku kwenye sekta ya madini kama mikopo na wakaitumia sivyo. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha wale waliochukua mikopo ile wanachukuliwa hatua na mikopo ile kurudishwa tena kwa wachimbaji wale wadogo wadogo ili waweze kuendeleza sekta hizo za madini za wachimbaji wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Msabaha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wachimbaji wadogo tunawategemea sana katika kukusanya maduhuli. Wachimbaji wakubwa walikuwa wanachangia zaidi ya asilimia 95 za michango yote ambayo ilikuwa inakwenda Serikalini na wachimbaji wadogo walikuwa wanachangia asilimia 4 mpaka 5. Sisi kama Serikali tunatambua umuhimu wa wachimbaji wadogo, tukiwawezesha tutapata maduhuli mengi ya kutosha. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tulikuta katika Wizara ya Madini walikuwa tayari wachimbaji wadogo wanapewa ruzuku kutoka Serikalini. Ruzuku ile walipewa wanaostahili na wasiostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara ya Madini tumewafuatilia wale maafisa wote waliokuwa wanawawezesha wachimbaji wadogo wasiostahili kupata ruzuku zile. Tumeshawafuatilia na wengine tumeshawaondoa katika nafasi zao za kazi. Vilevile kwa wale wachimbaji wa madini waliopewa fedha kinyume na taratibu na hawana sifa ya kupewa fedha hizo tumewafikisha katika vyombo vya sheria na sasa hivi kuna kesi zinaendelea ziko chini ya PCCB na zingine zimepelekwa Mahakamani. Tunachotaka ni kwamba warudishe fedha hizo na tuangalie namna bora ya kuwawezesha wachimbaji wadogo. Nia yetu kama Serikali tunataka wachimbaji wadogo tuwawezeshe, wawe wengi kwa sababu tunatambua kabisa kwamba tukiwawezesha tutaweza kupata kipato kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais tarehe 22 alikaa na wachimbaji wadogo na walizungumza changamoto zao. Changamoto nyingine ilikuwa ni za kodi ambazo tunawatoza katika uchimbaji huo. Kwa hiyo, hatua tunachukua kuangalia namna ya kuwasaidia wachimbaji hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili ni kwamba changamoto za wachimbaji zipo na sisi kama Serikali tunaendelea kutoa elimu kuhakikisha kwamba wachimbaji hao wadogo wanapata elimu ya kutosha katika uchimbaji huo na wanatunza kumbukumbu ili wawe na sifa za kupata mikopo katika benki na vyombo mbalimbali ambavyo vinakopesha (financial institutions) na sisi kama Serikali tutashawishi vyombo hivyo kuwakopesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais watumishi wengi wanakaimu.

Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha watumishi hawa sasa, wale wanaokaimu wanapandishwa madaraja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru. Nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Serikali ina dhamira ya dhati kabisa kuhakikisha maeneo yote ambayo watumishi wanakaimu waweze kufanya kazi yao kwa ukamilifu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tayari ofisi yetu imeshafanya utaratibu wa kuomba kibali kwa ajili ya kuhakikisha watumishi wote wale au maeneo yote, position zote ambazo zinakaimiwa ziweze kupata watalaam ambao wako kamili. Ahsante.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ili nami niweze kufafanua swali la Mheshimiwa Mbunge, Maryam Msabaha. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba nifafanue kidogo juu ya suala zima la kuhusu watumishi kukaimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli watumishi wamekuwa wakikaimu kwa muda mrefu sana na nimekuwa nikilizungumza hili kwamba, hii ni kutokana na watumishi wengi wamekuwa wakikaimishwa na waajiri wao kienyeji na nafasi za kukaimu ni kukaimu tu sio kwamba, ni nafasi ya kuthibitishwa au ni kwamba, umeshapewa ile kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi nafasi za kukaimu ziko katika uwezo wa madaraka kwa maana ya superlative substantive post. Kwa maana hiyo, sisi kama Serikali, tumetoa waraka kwamba, kukaimu mwisho miezi sita. Kwa maana hiyo waajiri wote nchini wanapaswa kuomba kibali na kama unataka mtumishi aendelee kukaimu basi tuandikie tena barua. Kukaimu lazima iwe kulingana na level ya ile nafasi ambayo unastahili kukaimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, askari wa usalama barabarani wamekuwa na matukio ya kujificha vichochoroni, wanajificha vichakani sasa magari yanakuwa yanakwenda kwa speed na wanasimamisha gari kwa ghafla na huku nyuma kuna msururu wa magari. Hili Morogoro imeshawahi kutokea na Tukuyu imeshawahi kutokea kutokana na Askari wa Usalama Barabarani.

Je, Serikali ina mikakati gani kuwapitia askari wote ambao wanakaa kwenye vituo vya Usalama Barabarani kuhakiki hii tabia ya kujifichaficha vichochoroni kwani hakuna mbinu mbadala ya kusimamisha magari mpaka mtu utoke vuup na kusimaisha gari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa matrafiki wa barabarani uweledi wao wakufanya kazi baadhi yao ni changamoto hasa kwa barabarani. Je, Serikali ina mikakati gani kuwapeleke matrafiki wote kuwapa mafunzo ya mbinu mbadala na zile tochi kuzitumia kwa sababu zile tochi wananchi wamekuwa wakizilalamikia sana, wanaweza kusema unapigwa tochi wanasema inakwenda speed, lakini ile speed haifanani na ile tochi? Naomba majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili kwa pamoja ya Mheshimiwa Maryam Msabaha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu swali langu la msingi kwamba tumefanikiwa kupunguza ajali kwa asilimia 43 na hususan ambazo zinasababishwa na magari ya abiria, mafanikio hayo pamoja na mambo mengine yalisababishwa kutokana na mbinu na uweledi wa askari wetu katika kubaini mbinu na njama ambazo zinatumika na madereva wasiokuwa waaminifu kuweza kukiuka sharia. Kwa hiyo hili suala ambalo amelizungumza kwa askari kukaa barabarani kuweza kujificha na mengine yote, malengo yalikuwa ni ya nia njema, lakini kama kutakuwa na upungufu katika utekelezaji wa hayo kwa baadhi ya askari basi tunachukua kama ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge afahamu kwamba dhamira ya Jeshi letu la Polisi kupitia Vikosi vya Usalama Barabarani si kuburuza wananchi, lakini kusaidia wananchi kuokoa maisha yao hususan kwa wale madereva ambao hawafuati sheria.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, katika tafiti nilizozifanya kuna makundi manne, kuna kundi la hawa watoto wanaofanya kazi majumbani, akina mama ambao wanajiuza na wanafunzi. Swali linakuja hivi, kuna akina baba ambao wana akili zao timamu na wengine ni watu wa Serikali wamekuwa wakiyalaghai makundi haya niliyoyataja na kuwapa ujauzito na wakati wanawafuata labda wanataka huduma za kijamii wanawatosa na wengine kuwatishia na bunduki. Naomba kujua ni nini kauli ya Serikali kwa wale wanaobainika kuhusika na matukio haya? Watu hawa wanapopelekwa kwenye Vituo vya Polisi au Serikali za Mitaa wachukuliwe hatua za kinidhamu na sheria kali ili iwe fundisho kwa wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa majiji makubwa Mwanza, Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Mbeya, yamekuwa na ongezeko la wanawake ambao wanafanya biashara za kujiuza (biashara za ngono). Je, Serikali ina mikakati gani hasa katika Jiji la Dodoma ambalo ni Makao Makuu ya Serikali kudhibiti hali hii ili kupunguza ongezeko la kutupa watoto majalalani? Naomba kauli ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, hakuna kitu chochote ambacho kinaweza kuhalalisha juu ya hatua yoyote ambayo atachukua mama kumtupa mtoto wake. Pili, wale ambao wanahusika kuwapa ujauzito mabinti hawa wadogo ambapo wengine ni wanafunzi na wale ambao amewataja, imeelezwa wazi katika sheria kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kwamba kuna Sheria ya Mtoto lakini pia Kanuni ya Adhabu ambazo zinaelezea wajibu wa mtu ambaye ameamua kuzaa mtoto kwa hiari yake ama amejitolea kuwa mlezi wa mtoto yule na jinsi ambavyo sheria inazungumza kwa wale ambao watashindwa kutekeleza wajibu huo. Kwa hiyo, sheria iko wazi na adhabu inaeleza kwamba kwa mtu ambaye atashindwa kuhudumia mtoto wake kutimiza wajibu huo anaweza kufungwa kifungo kisichopungua miaka mitano. Kwa hiyo, sheria iko wazi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hoja yake ya pili kuhusu madada wanaojiuza, sina hakika kama utafiti wake aliouzungumza una usahihi kiasi gani kuhusu mahusiano ya akina mama ambao wanatupa watoto na wale madada wanaojiuza. Hata hivyo, niseme tu kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likifanya jitihada mbalimbali kukabiliana na aina ya watu ambao wanafanya biashara haramu ikiwemo biashara za ngono.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito kwa wananchi wote kwa ujumla ikiwemo na akina baba kujiepusha kuwa wateja wa biashara hizo. Kwa hiyo, hapa ni shilingi inaangaliwa pande zote mbili, kwa hawa akina dada ambao wanafanya biashara hizi lakini mpaka wanunuzi wa biashara hizi. Kwa hiyo, wote wawili wanafanya makosa na pale ambapo watabainika basi sheria itachukua mkondo wake.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, shirika limekuwa likipata tenda kutoka ndani ya Serikali na limekuwa likifanya kazi hizi kwa weledi mkubwa sana. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha shirika linalipwa kwa wakati ili hata zile changamoto ndogondogo wanapopata zile hela kwa wakati wapate kuzitatua wenyewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; miundombinu ya haya mashirika, hiki Kikosi cha Mizinga kwenye makambi mengi ni chakavu na si rafiki sana na ni siku nyingi. Sasa Serikali ina mikakati gani ya kutenga fedha na kuangalia hiki kitengo kwa sababu hiki kitengo ni kwa kazi maalum na kinafanya kazi kwa ujasiri na kwa weledi mkubwa. Je, Serikali na Wizara ya Fedha ina mkakati gani kuhakikisha kwamba kile kinachotengwa kwa ajili ya kitengo hiki kinapelekwa ili kutoa hizi changamoto ambazo zipo katika Kikosi hiki cha Mizinga katika hili Shirika la Mzinga? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Msabaha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu malipo kwa kazi ambazo shirika linafanya za Serikali naweza nikamueleza Mheshimiwa Mbunge kwamba malipo hayo yanafanyika. Hivi karibuni Shirika la Ujenzi la Mzinga limepata kazi kadhaa ikiwemo ujenzi wa ofisi za Serikali hapa Dodoma, lakini katika baadhi ya halmashauri pia wamekuwa wakipata kazi. Kwa taarifa nilizokuwa nazo ni kwamba malipo yanafanyika na fedha hizo zinawasaidia kuboresha mambo madogomadogo katika shirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miundombinu ya shirika lenyewe; ni kweli kwamba kwa kiwango kikubwa miundombinu pale katika Shirika la Mzinga imechakaa, ni ya muda mrefu na ndiyo maana kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba sasa wametengeneza mpango mkakati ambao kwa kiwango kikubwa ukipata fedha utaweza kushughulikia yote haya ikiwemo kuboresha miundombinu, lakini kuleta wataalam waliobobea katika fani hizo na kuwa na mtaji wa kuweza kuendeleza shirika hili. Ni matumaini yetu kwamba mpango mkakati huo utapitishwa na Serikali ili shirika liweze kupata fedha na kuweza kuboresha miundombinu yake.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa vyanzo vingi vya mapato vya Halmashauri vinaenda Mfuko Mkuu: Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha vyanzo vile vya Halmashauri vinarudi kwa wakati muafaka ili changamoto ambazo zinakabili Halmashauri zipate kutatuliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SRIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Juzi nilikuwa najibu swali hapa katika Bunge lako Tukufu ambalo liliuliza namna ambavyo Serikali imejipanga kuwezesha Halmashauri. Tukasema kwamba fedha hizi ambazo zimekusanywa kutoka maeneo ya Halmashauri yale, kuna Halmashauri kulingana na mapato yao walikuwa wanapata fedha nyingi zaidi kuliko Halmashauri nyingine na matokeo yake kuna baadhi ya maeneo mengi ya nchi yalikuwa hayawezi kupata miradi ya maendeleo hasa miradi ile mikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejiandaa na imetoa maelekezo kwa Halmashauri zote nchini kwamba ziko fedha ambazo zitasimamiwa na Hazina, tumewaambia wataalam wetu katika Halmashauri zetu waandae miradi ya kimkakati kama ni stendi au soko kadri watakavyoona wenyewe katika maeneo yao fursa ni ipi, wakiandika andiko linakuja TAMISEMI, linapitiwa na wataalam wa TAMISEMI, linapitiwa pia na wataalam pia wa Wizara ya Fedha kupitia Hazina na baadaye wanaridhia kuanzisha mradi huo mkubwa. Mradi huo ukianzishwa ukakamilika watakuwa watakura wanarejesha lakini pia watapata fedha ambayo ina uhakika, changamoto zingine zote katika maeneo yao zitamalizika kwa sababu wana fedha ya uhakika. Tunataka wakipata fedha hizo wapange miradi ya maendeleo ili waweze kuitekeleza kwa fedha ambazo wenyewe wanazisimamia na zinapatikana kwa wakati. Ahsante.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumuuliza Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa ma-DAS na Wakuu wa Mikoa na wateuliwa wa Rais wengi wao wengine hawataki kufuata taratibu kusikiliza kero za wananchi na hata pale wananchi wengine wanapodhulumiwa haki zao hawatatui kwa wakati, mpaka wanasubiri msafara wa Rais na kwenda kulalamika mbele ya Rais wale wananchi ambao wamedhulumiwa haki zao. Je, Serikali ina mkakati gani hawa ma-DAS na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wasiowajibika katika nafasi mbalimbali walizoteuliwa ili kuwahakiki na kuchukuliwa hatua za kisheria?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MIAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Maryam Msabaha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, kuna baadhi ya maeneo kumekuwa na malalamiko, lakini Mheshimiwa Rais alipokuwa anahutubia katika eneo la Mbarali, Mkoani Mbeya alitoa maelekezo mahususi kwamba, kila Mkuu wa Mkoa, kila Mkuu wa Wilaya, kila mteule wa Serikali na mamlaka yake mpaka ngazi ya chini waweke ratiba ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua. Zile ambazo zitakuwa zimeshindikana kwenye ngazi yao wapeleke ngazi ya juu, lakini tumeenda hatua mbele zaidi tunafuatilia, Mheshimiwa Maryam na Wabunge wengine kama kuna maeneo ambayo Mheshimiwa Rais ataenda au viongozi wengine watu wananyanyua mabango kulalamikia kero ambazo zipo ndani ya uwezo wa viongozi wale, hao watu ndio wanapaswa kimsingi kuondolewa katika nafasi hiyo kwa sababu, wameshindwa kutimiza wajibu wao. Ahsante.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo wanafunzi wengi wa kike wamekuwa wakipata mimba katika mazingira magumu.

Je, Serikali ina mikakati gani kujenga hostel za watoto wa kike ili wapate kujistiri waondokane na vishawishi vya barabarani?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ndio maana azma ya Serikali juzi juzi mwezi wa tatu Serikali imetoa takribani shilingi bilioni 54.6 ambayo katika hili lengo lake ni kujenga madarasa takribani 988 lakini mabweni mapya 210 kwa hiyo ni commitment ya Serikali kuhakikisha jinsi gani mabweni haya yanjengwa.

Kwa hiyo, Mheshimiwa dada yangu naomba nikuhakikishie kwamba tutafanya kila liwezekano tutaangalia nini tufanye licha tunaanza kujenga mabweni 210 katika maeneo mbalimbali lakini juhudi ya Serikali itaendelea kuhakikisha vijana hawa wa kike tunawaondoa katika hali hatalishi zaidi hasa kwa watu ambao wana nia mbaya kuhakikisha wanaharibu future ya watoto wa kike. Kwa hiyo, tunaendelea kulichukua kwa ajili ya Serikali kulifanyia kazi.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nianze na hapa kwenye huu Mkoa wako wa Dodoma. Niko maeneo ya katikati hapo Mjini, baa hizi zimekuwa kero kwa wananchi ambao wamejenga maeneo karibu na hizi bar.

Mheshimiwa Spika, isitoshe, wamekuwa wanatoka wanawake mbalimbali, wengine wanatoka Dar es Salaam, wanatoka Morogoro, wanatoka mikoa mbalimbali wanakuja hapa kwenye Jiji hili la Dodoma kwa sababu ni Makao Makuu ya Serikali. Tatizo kubwa bar hizi zinapiga miziki na matusi makubwa sana kwa jamii, imekuwa ni kero kubwa sana kwa jamii.

Je, ni lini Serikali itahakikisha inafanya msako maalum kwa Mkoa huu wa Dodoma, hasa ukichangia maeneo ya Mjini niliyoyataja Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuna hawa akinamama ambao hawataki kufanya kazi wanajiingiza kwenye haya masuala yasiyokuwa ya stahiki za kijamii yaani kama tukisema kama Marekani wao wana tozwa kodi, Uholanzi wanatozwa kodi, sasa hawa wanawake askari wa Dodoma wamekuwa mara kwa mara askari kanzu wamekuwa wakiwachukua mara kwa mara lakini wanarudi tena kwenye maeneo haya haya wanakuwa wanafanya matukio ambayo hayaendani na jamii ya Kitanzania na maadili.

Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha inawachukua wanawake wote hawa ambao wanafanya biashara haramu ambazo hazina stahiki na kuangalia hata wanawapeleka kwenye mashamba ya JKT wakafanye kazi? Naomba jibu la Serikali.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Msabaha, meti wangu wa kambi yetu ya Bulombola kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kilio hiki cha Dodoma kikubwa zaidi nini mkakati wa Serikali? Nimuelekeze Mkuu wa Mkoa kwa sababu akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Mkoa, na Mkuu wake wa Wilaya kuhakikisha kwamba vile vitendo vya hovyo vyote ambavyo vinakiuka utaratibu waweze kuvisimamia kwa sababu Jeshi la Polisi hapa lipo waangalie nini kinachofanyika kuhakikisha hadhi ya Jiji la Dodoma linabakia kama lilivyo badala ya kuchafuliwa.

Mheshimiwa Spika, mkakati hawa watu ambao hii kauli nyingine uliyoizungumza ya watu inawezekana wanafanya biashara zisizo sawasawa, ndiyo maana Serikali mnakumbuka mwaka jana hapa tulipitisha sheria asilimia 10 iende katika vikundi ya vijana, akinamama na walemavu. Imani yetu ni kwamba kwa vile ukiangalia Dodoma pato lao ni kubwa mpaka juzi juzi wamekusanya zaidi ya shilingi bilioni 55 own source collection. Kwa hiyo ukichukua hapo asilimia nne yake maana yake ni fedha nyingi sana, kwa hiyo vikundi hivi ninaimani kwamba viongozi wetu watendaji wetu hasa maafisa maendeleo ya jamii chini ya Mkurugenzi wakiweka utaratibu mzuri wa kuwawezesha hawa akinamama tutawatoa katika suala zima hatarishi walilokuwepo nalo kwa wao kwamba kujiingiza katika shughuli halali za kiuchumi za Taifa letu hili.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, utakubaliana na mimi kwa sababu na wewe pia ni mdau wa Zanzibar, unalea chama chako kwa upande wa Kaskazini na upande wa Kusini na mara nyingi unatumia usafiri wa bandari, hutumii usafiri wa ndege na unakutana na wapigakura.

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo bandarini ni kuwa hata kilokumi zinakuwa charged na imekuwa ni malalamiko sana kwa wananchi. Ni vigezo gani ambavyo vinatumika kwa mizigo ya biashara na mizigo binafsi kwa hawa wasafiri? Naomba Serikali ifafanue kwa sababu mtu anapita na kilo 20 za mchele anakuwa charged. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukilalamika mara kwa mara abiria wanaokwenda Zanzibar. Kuna hizi boti za Bakhresa wana nauli zao kwenye mizigo, lakini sasa pale kwenye bandari imekuwa mara kwa mara inarudiana. Naomba kauli ya Serikali, hizi kauli zinazotolewa humu Bungeni ni lini zitafanyiwa kazi kwa vitendo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, vigezo vinavyotumika nimevitaja na vinapatikana kwenye tariff book. Labda hata baadae Mheshimiwa Mbunge naweza pia nikamuelekeza kwa sababu pia tariff book iko kwenye website ya Mamlaka ya Bandari ili kuweza kuongeza ufahamu na atusaidie kupunguza pia usumbufu.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hapa inaonekana kwamba ni uelewa na mimi nitumie tu nafasi hii kutoa maelekezo kwa Mamlaka ya Bandari ili kwamba tuweze kuweka ufafanuzi wa kutosha kwa abiria wanaotumia bandari hii kwenda Zanzibar ili waweze kuweka mabango yanayoonekana kuonesha vigezo vinavyotakiwa huu uzito wa kilo 21 na kwenda mbele ndiyo wanatakiwa kutozwa. Lakini pia waweze kutoa ufafanuzi na kutoa maelekezo na mimi ntalifuatilia hili ili kuona kwamba hili tunalitekeleza kupunguza usumbufu kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo nia ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuona wananchi wake wanateseka.

Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo ndiyo maana nasema nitafuatilia ili kuona kwamba usumbufu unaondoka, uelewa unaongezeka kwa wananchi wanaotumia bandari. Wakati mwingine wanaingia kwenye kutozwa kutokana na kutokuelewa.

Mheshimiwa Spika, lakini msisitizo mkubwa niseme tu kwamba wale wanaofanya biashara wapitie kwenye eneo maalum kama nilivyosema, ambalo ni kwa ajili ya biashara, wakijichanganya na abiria wengine inaongeza usumbufu ambao Mheshimiwa Mbunge ameutaja.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, amezungumza kwamba kuna usumbufu kwenye usafiri wa boti ya Bakhresa, na wiki iliyopita tu kulikuwa na swali lilijibiwa hapa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Serikali tutaendelea kuchukua hatua na tutafuatilia vizuri ili menejimenti ya mamlaka iweke usimamizi madhubuti ili wananchi hawa wasiendelee kupata shida na sisi kama viongozi upande wa Wizara tutalisimamia hili ili usumbufu tuweze kuupunguza na hatimaye tuumalize kabisa.